Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha
Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..
Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.
MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.
TUPO PAMOJA DAIMA
Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;
https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:
https://www.facebook.com/diaryyangu/
`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;
Friday, February 26, 2010
Mama wa kambo-3
Ili uelewe vizuri soma sehemu ya pili kwanza
Kisa cha msamaria mwema kilikuwa bado kinaelea kichwani mwangu, nikitafakari yaliyotokea yasije yakanikuta na mimi, kwahiyo niliona nitumie busara kumshawishi Yule mama, nikamwambia; ‘Mama yangu dunia hii ina mengi, sisi tungependa ulale humu kama ulivyoomba, na kesho uondoke, lakini usiku ni mrefu, na hatujui nini mola kapanga, wema unaweza ukageuka kuwa shubiri mama yangu…’
‘Aaah, jamani, usiku mmoja tu,msiwe na wasiwasi na mimi, nimepita kote nikaona nije hapa kwenu, unafikiri kwanini…hili mlizingatie, ninachoomba nikulala kwasababu huu ni usiku nitaenda wapi, na kama mkikataa, basi mimi nitalala hapa hapa nje, au hata chooni…najua kama ningezaa nisingepata matatizo yote haya…nashangaa hata nyinyi mumejazwa uongo mnakubaliana na huyu mtoto wa mke mwenza, muwongo na ana chuki na mimi tu’ akasema huku anatoa machozi
‘Sio hivyo mama, sheria itatufunga pia, licha ya kukosana na huyo jirani yetu, kuwa tumekulaza bila ridhaa yao. Sasa mama unaonaje kama tukienda kwa mjumbe ili atusaidie kwa hili, huwezi jua ya mungu mengi..’
‘Kwa mumbe, kwani mimi mwizi, na swla la kutoke nini kwani mimi nina kifafa, mimi siumwi siwezi kufa, kama ni wasiwasi wenu au mnaogopa nini, kama hamtaki basi ngoja niondoke, na kama nikikutwa kesho nimekufa barabarani, nyie mtawajibika, nimewaomba msaada wa kujistiri angalau usiku mmoja mumekataa, mnafikiri nyie hayatawakuta kama mimi, au kwa vile sina watoto…haya naondoka lakini… ‘ Yule mama akachukua begi lake akaanza kuondoka. Huruma ikanishika, nikataka kumsimamisha lakini mdomo ukashikwa na kigugumizi. Niliwaza kile kisa cha msamaria mwema, nini kilichomsibu baadaye. Hebu tuendelee nacho:-
Mjumbe alipoitwa pembeni na wasamaria wema akawaambia`Huu sio muda wa kuficha kitu, ila busara inahitajika sana, kwanza ngoja nikaongee naye nje, nyie endeleeni kufungua huo mlango, najua kwenye wengi hapaharibi neno, huenda mgeni wenu huyo kazidiwa na usingizi, lakini kama kuna baya, tutajua nini cha kufanya. Mjumbe akachepuka nje na jamaa wengine wakawa wanaendelea kuufungua ule mlango. Mama msamaria mwema akawa anajenga hisia nyingi, zakujiuliza kama huyu mgeni kazidiwa, huenda alikuwa anaumwa, au baya zaidi kama kafa..hapana hajafa, mungui wangu kama kafa…hapana Mungu atuepushie hilo!
‘Mume wangu kama huyu mama kafa tutafanyeje, si tutaishia jela, ina maana wema utatuponza. Unakumbuka yaliyomsibu yula baba mwenye nyumba tuliokuwa tukiishi zamani. Unakikumbuka kile kisa vizuri, si aliishia jela, kwa kisa kama hikihiki. Mungu wangu, mbona hatukukumbuka pale jana tukampeleka kwa mjumbe kwanza.’ Yule mke mtu akaanza kubwabwaja huku anapigapiga miguu chini. Mume mtu ilibidi afiche hisia zake na kumtoa wasiwasi mkewe, kuwa hakuna kitu kama hicho, wao wametenda wema, na kwa vile walichofanya ni ubinadamu haki itawalinda, hata hivyo kwanini wafikiri kitu ambacho hakipo. Kichwani mume msamaria mwema naye akakikumbuka kisa cha mwenye nyumba wao, na kweli kilikuwa sawa na tukio hili.
Baba mwenye nyumba wao, alijiwa na mke wa mpangaji wake, ilikuwa usiku , mke na mumewe waligombana, na ilikuwa ndio kawaida yao!. Yule mke alipoona kazidiwa akakimbilia kwa baba mwenye nyumba, kwani mumewe alimwambia siku hiyo lazima amuue, na nyumba ya mwenye nyuma ilikuwa pembeni kidogo mwa nyumba ya wapangaji. Bila ajizi baba mwenye nyumba akaamua huyo mama alale kwake hadi asubuhi, kwenye chumba cha wageni. Kumbe kila kipigo kilikuwa kikali, Yule mama akafiriki usiku.
Mume mtu akaamuka asubuhu kwenda kazini, akiwa bado na hasiria. Baadaye akapewa taarifa kuwa mke hajiwezi aje haraka nyumbani. Alipofika akaambiwa aende kwa baba mwenye nyumba, ndipo mkewe alipo!
‘Nini, yupo kwa baba mwenye nyumba, mtaniambia vizuri, kwanza nilishamuhisi mke wangu anatembea na mtu mwingine, nahisi ni huyu baba mwenye nyumba, kwanini akimbilie huko asiende kwao au kwa ndugu zangu…ngoja’ akaingia ndani akachukua panga. Watu wakamsihi, lakini hali ikawa ngumu jamaa, kawa mbogo, hadi kwa baba mweny nyuma. Huko alipofika polisi walishafika, kwani taarifa zilishapelekwa mapema na muda huo walikuwa wakimhoji baba maweny nyumba, jamaa hakujali cha polisi akalirusha panga, badala ya kumpiga baba mwenye nyumba, polisi aliyekuwepo karibu aliliona na kujaribu kumuokoa baba mwenye nyumba, na bahati mbaya likashukia kwake.
Polisi wengine wakaja kusaidia, na kilichosaidia ni pale mmoja aliposema, `wewe badala ya kusikiliza nini kimetokea unapigana, unataka utuletee misiba mingine, mkeo kafa nawe unataka kuua, nini unafanya..’
‘Mke wangu kafa, unasema nini, hata mtanieleza, vizuri, wewe baba mwenye nyuma…aaah, hapana mke wangu kafa..’ ikawa nguvu zimemuishia jamaa, na pingu zikatinga mikononi, yeye na baba mwenye nyumba wakapelekwa polisi. Kesi ikawa ndefu ajabu, baba mwenye nyumba akatiwa hatiani kwa kutokufuata sheri na mume mtu kwa kujeruhi na kusababisha kifo cha mkewe na pia kushambulia kwa silaha na kumjeruhi polisi.
Baba msamaria mwema alipofika mwisho wa kisa hiki cha baba mwenye nyumba wake aliinua mkono juu na kuomba , aliomba yasije yakamkuta makubwa, aliomba akijua kesi kama hii itamgharimu sana, naye yupo katika hali ngumu ya kimaisha, mtoto wao anaumwa anahitaji matibabu, walikuwa wanajadili wapi wakapate msaada saa lizuke kubwa kama hilo itakuwaje. `Ewe mola tuukoe na janga hili’
‘Mke wangu tusubiri mlango ufunguliwe, najua rafiki yetu atatuelewa, kama alimtimua kwake alitegemea akalale wapi, polisi au wapi..’ akasema mume mtu.
From miram3
Imekula kwetu
Nilijaribu kupitisha macho yangu huku na huko nikiwaangalia watu mbalimbali waliokuwemo humo ndani, wengi walikuwa wamechoka, na kuchakaa. Kuchoka huko na kuchakaa sio kwasababu ya umri, yawezekana ikawa hivyo kwa baadhi yao, lakini dhahiri,ilionyesha kuwa ni sababu ya hali ngumu za kimaisha. Wewe fikiria kwa mfano kesi yetu inakaribia miaka kumi inapigwa tarehe, na mtu kama huyo awe anasota na maisha ya mitaani, akihangaika na hili au lile bila ajira maalumu, atakuwa katika hali gani! Fikiria hela gani aliyolipwa na muajiri ambayo angeanzishia hata kigenge cha nyanya, hela hiyo ni kama tiketi ya kumsaidia kurahisisha kifo chake. Ni lazima atachakaa hata kabla ya umri wake.
‘Kesi namba kadhaa, ya mwajiri(jina) na mfanyakazi (marehemu mwenyekiti wetu)akiwakilisha wafanyakazi wenzake 33..’ alianza hakimu, pamoja na mengine alisoma vipengele kadhaa, na kusema yeye atakachofanya ni kusoma hukumu, na sio kusoma mapitio yote ya kesi. Lakini kwa vipengele alivyovisoma ilionyesha wazi kuwa hakuna kitu. Nikatafakari na kuwaza juu ya wote waliokuwepo hapo nini hatima yao. Ukumbuke kuwa kila mmoja hapo amebeba sio familia yake tu, bali wapo tegemezi kibao, na huenda walichokuwa wakitegemea kama tonge la mwisho la maisha yao ni kupata chochote kwenye kesi hiyo, kwasababu kesi ilishaenda vizuri mwanzoni.
‘Hoja Ya wafanyakazi kuwa wamechelewesha kufikisha maombi yao ya kusikilizwa upya kesi ndani ya wakati haina miguu, kwa sababu wao wanauzoefu kwa vile kesi yao imeshasikilizwa mara nyingi, kwahiyo jopo la majaji limetuplia mbali maombi ya kesi hiyo…’ akasema hakimu na mengineyo. Wote tukaguna na kuinamisha kichwa chini, nahisi kwa muwakilishi wa muajiri aliyekuwepo pale mbele atakuwa akitabasamu, na kusema `imekula kwao hao, walie tu’
Kweli `imekula kwetu’ hatuna jinsi, tulijisemea kimoyomoyo na kuinuka kwenye yale mabenchi, na baadaye tuliamua kumwendea katibu wa chama cha wafanyakazi. Yeye alisikitika na kusema hata yeye ameona ajabu kwanini katika siku 45, wakili wetu wakati huo hakuweza kupeleka maombi yetu mahakamani! Nakupunguka kipindi hicho wakili huyo alikuwa akidai kuwa kabanwa na kazi nyingi, mara kasafiri na hatimaye siku zikapita! Je tumlaumu nani, na baya zaidi wakili huyo hatupo naye duniani. Chakusema kwasasa ni kuwa kesi imekula kwetu.
Wakati tunatoka kuelekea kwa katibu nikamkumbuka mwenyekiti wetu, kuwa kwa muda kama huu tungelikuwa naye, lakini sasa ni marehemu.Nilimkumbuka jinsi gani alivyokuwa akihangaika na kujituma kuifuatilia hii kesi yetu. Hadi hatua za mwisho, akiwa amechoka, amekonda na maisha yakiwa magumu kwake na kwetu, lakini aliweza kuja kwetu kutupa moyo. Huyu ndiye kiongozi shujaa, kiongozi aliyejali matakwa ya wenzake, hata kama yeye alikuwa akiumia, Alijua wazi kuwa hakuwa akiwatetea wafanyakazi wenzake tu, bali alikuwa akiwatetea wao na walio nyuma yao. Mungu amlaze mahala pema peponi , na wengine waliotangulia mbele za haki, kwani sio yeye tu, wapo wafanyakazi wengine wameshafariki, na kushindwa kabisa kuipata haki yao ambayo imeshaota mbawa.
Kwa muajiri kwake ni kicheko, kwani nakumbuka siku wanatugaia barua zetu, wakati tumegoma kukubaliana na matakwa yao, yenye masharti ya kututega, alituaga kwa kebehi kuwa, hata kama tutashitaki, lakini hatutamuweza. Alisema kesi kama hiyo kwa uzoefu wake itachukua muda mrefu na hiyo ni faida kwao, kwani hata kama tungeshinda, hiyo hela itakuwa imeshazalisha na kufidia hiyo ‘hasara’, lakini aliendelea kusema kuwa `Kwa uzoefu wake ni nadra kwa wafanyakazi kushinda. Simtaona, fikiria mkikaa zaidi ya mika mitano nyumbani mtapata wapi hela za kumlipa wakili, mtakuwa mumeshaishiwa…kwaherini ‘ alisema.
Swala la kujiuliza je ili wafanyakazi waweze kupata haki zao vyema ifanyike nini? Je mikataba ya ajira, ambayo baaaye huja kuvunjwa na waajiri, ina maana gani, kwani hatima ya siku kwao hubakia kicheko cha dharau! Ni nani wa kuwalinda wafanyakazi wan chi ambao kila siku huangukia pua kwa kukubali mikataba yenye mitego, inayotungwa na waajiri. Rejea maelezo yetu ya utumwa wa nguvu kazi
Vipo vyama vya wafanyakazi, lakini nguvu zao huwa pale mkiwa bado waajiriwa, mnapokuwa nje ya kazi, nguvu yao huwa ndogo, ingawaje bado wana haki ya kuwatetea, lakini asiyekuwepo na lake halipo. Tukumbuke pia wao kama vyama vya kutetea wafanyakazi wana matatizo mengi ya wafanyakazi na sheria za ajira hazipo wazi, kwani wa-ajiri, na wenye makampuni mara nyingi huwa hawakubaliani na vyama vya wafanyakazi, na wengine huvipinga waziwazi. Hata wakikubaliana navyo bado yeye kama muajiri ana nguvu ya ziada, pesa. Pesa huongea na pesa inarahisisha mambo ya kufuatilia. Hata kama una haki kama huna pesa, utaipata haki yako kweli? Kuna gharama za usafiri, gharama za makabrasha, nk.
Kwa ujumla, kama muajiri akikutema, iwe ni kwa haki au kwa batili ujue wewe mfanyakazi huna chako, utaambulia mshahara mmoja, na kusubiri `enisisiefu' yako, na ukijitia unajua sana ukafungua kesi hatima yake,ndiyo hiyo `imekula kwako'.
From miram3
Thursday, February 25, 2010
Mama wa kambo-2
Ili uelewe vyema soma sehemu ya kwanza, halafu endelea:-
Wakati natafakari kisa cha msamaria mwema, huyu mama aliyekuja kwangu usiku kuomba hifadhi alikuwa akituhadithia maisha yake na hawa watoto waliomfukuza. Yeye alipoolewa alikaa muda mrefu bila kupata mtoto, baadaye ikadhihiri kuwa ni mgumba kwahiyo mume wake aka-ona aoe mke wa pili. Mke wa pili akabahatika kuzaa watoto watatu, mmojawapo ni huyu wa kike aliyeolewa na kuja kuishi jirani nasisi. Mume wa wao alifariki mapema, lakini kipindi watoto wameshakuwa wakubwa, na wanajitegemea, baadaye Mama wa hawa watoto naye akafiriki. Kwahiyo familia hiyo ikabaki na mama huyu wa kambo.
Siunajua tena mambo ya uke wenza kuna chuki zilijijenga kuwa huyu mama wa kambo amehusika katika kufariki kwa mumewe na baadaye pia akasababisha kufariki kwa mama wa hawa watoto! Zilikuwa hisia, sisizo na ushaihidi wowote. Chuki hizo zilianza kwa mke mwenza , zikaja kupandikizwa kwa watoto. Watoto wakawa wanamchukia mama yao wa kambo, kiasi kwamba hata akipika chakula watoto hawa wanasusa kula. Haya ni kwa mujibu wa huyu mama.
Huyu jirani yetu, yaani binti wa mama huyu aliyetugongea usiku alikuwa mja mzito na baadaye akajifungua , na mumewe akamshauri mkewe wamchukue mama yao wa kambo aje awasadie katika huduma za ulezi. Mara nyingi katika mila za kiafrika, mama huchukuliwa kuwasaidia watoto wao wanapojifungua hasa katika mimba za mwanzo. Hii husaidia katika kuelekezana, na kumkanda mama aliyejifungua. Mke akakubali ingawaje ile hali ya kutompenda huyo mama ilikuwa bado kwenye damu.
Tatizo la mama yao wa kambo alikuwa mnywaji wa pombe , hatujui ni kwasababu ya hali halisi ya kimaisha, kuwa yeye ni mgumba au ni kutokana na mkandamizo wa kunyanyaswa au ndio kawaida ya kabila lao, ambalo pombe kwao ni kama chai. Hali hii ya kunywa ilikuwa haiwapendezi watoto, na popote alipokuwa akienda kuishi, kulikuwa na kutokuelewana kati ya mama huyu na watoto, naye kama mtu mzima hakupenda kupangiwa maisha , na matokeo yake ni kufukuzwa. Lakini yeye hakukata tama, akijua kuwa hawo ni wanae tu. Hii ni kutokana na maelezo niliyopata kutoka kwa huyu mama na mtoto huyo wa kike aliyemfukuza mama huyo.
Nilipomuuliza huyo mama kuhusu mambo ya ulevi alikataa akasema hilo sio tatizo kwao kwani wote wanakunywa, wao wanamfukuza kwasababu ya chuki zilizojijenga kabla na kwa vila hana watoto wanamsakama kila anapokwenda kuwasalimia. Na hata hivyo, yeye kuja kwake hapa Dar, hakupenda ila wao ndio waliomuita inakuwaje sasa wamfukuze na kumzalilisha kiasi hiki, je kama ingekuwa mama yao aliyewazaa wangemfanyia hivyo, au ni kwasababu yeye hana watoto…
Huyu mama alipokuwa akituhadithia hii habari ya maisha yake wote tulijawa na majonzi. Kumbe ni kwasababu yeye hakuwahi kuza, kumbe ni kwasababu ya visa vya uke wenza ndio vimejenga hii chuki. Tukajiuliza mara mbili, tatu je tumwamini nani; huyu mama au mtoto wake ambaye amekataa kata kata kumuhifadhi mama yake?
‘Kwanza muulizeni usiku wote huu ametoka wapi, si ametoka kulewa, hamsikii harufu ya pombe? Na ni vyema akarudi huko alikotoka, nahisi alikwenda kwa dada yangu akafukuzwa kwa kulewa kwake, hii ndio tabia yake, hata huko nyumbani’ alisema mtoto wa huyu mama. Lakini mama huyo alijitetea kuwa ndio alitoka kwa mtoto wao huyo mwingine lakini hakufukuzwa huko, yeye alikuja hapo kwa nia ya kuchukua baadhi ya nguo zake, na usafiri ulikuwa wa shida ndio maana akafika hapo akiwa amechelewa.’
‘Mimi simlazi hapa kwangu , nyie mfukuzeni atajua wapi pa kulala, na mtajua wenyewe lakumfanya, sisi hatuhusiki’ akasema yule mtoto wa kike wa Yule mama.
Kauli hii ilinishitua kidogo, ina maana tutawajibika kama litatokea la kutokea, nikaogopa kama nitaamua kuwa msamaria mwema huenda yakawa yale ya hiki kisa nitakachoendelea kukuhadithia na huenda nikifanya usamaria wema mwisho wa siku nitaingia matatani. Je nimuhifadhi au nichukue hatua gani, nikajiuliza huku nikikikumbuka hiki kisa cha msamaria mwema:
Yule mume-mtu kwenye kisa chetu cha msamaria mwema alipoona watu wkadhaa wapo kwa rafiki yake akaamua aulizie kumetokea nini. Wale watu, wasiopitwa na kitu wakamwambia kuwa wao wamesikia kuwa kuna mtu kahifadhiwa humo, lakini chumba hakifunguki, na inavyoonyesha mhifadhiwa kalewa sana au anaumwa au vinginevyo kakata roho, huwezi jua, ndio maana mjumbe kaitwa ili atoe ushauri, kwani chumba kimefungwa kwa ndani, si msala huo…!
‘Hawa watu bwana sasa inakuwaje wamuhifadhi mtu hivihivi tu, kama ni jambazi je, au hata kama sio jambazi , anaweza akawa na ugonjwa, akifa si tatizo hilo?. Kama ni ndugu yangu au wako kafanyiwa hivyo, utasahau usamaria wema na kuangalia janga lilitokea, na unafikiri kutaeleweka kitu hapo. Lakini kwa vile ni rafiki yangu ngoja nikamsaidie kwa mawazo wasije wakamfunga rafiki yangu bure kwa usamaria wema wake’ Yule mume mtu akasema huku akigonga mlango.
Kule ndani walikuwa katika harakati za ku-ufungua ule mlango kwa kutoa kitasa cha mlango, ilibidi fundi aitwe ili mlango ubomolewe kitaalamu kuliko kuvunjwa. Na wakiwa katika pilikapilika hizo za kuuvunja ule mlango , mara wakasikia sauti ya huyu mume-mtu akiongea huko nje, na hapo wasiwasi ukawatinga mama na baba msamaria wema. Uwoga ukawatanda, wakatamani wasimkaribishe huyo rafiki yao, lakini kwa kigezo gani, na je huenda ameshajua kuwa mkewe ndiye aliyepo humo ndani, sasa wafanyeje ikabidi wamuite mjumbe pembeni ili atoe ushauri.
Tukutane baadaye
-Je mjumbe alitoa ushauri gani? From miram3
Leo kwake kesho kwako
‘Jamani kufiwa, usikie kwa mwenzako, hakuna jinsi kwasababu ni jambo lipo nje ya uwezo wa kibinadamu, lakini ni mtihani..’ alisema Yule mama ingawaje tuliona kama anataka kuanza kulia.
‘Ni kweli, hilo ni la kumshukuru mola kwani yote hupanga yeye, nafikiri hujapata manyanyaso yoyote mapaka sasa.
‘Kwaweli sijaanza, ila kama wasengekuja watu wa dini na kuyaweka mambo sawa, ningeishia kubaya. Kwanza yaliletwa mambo ya kimila, eti nijengewe kajijumba ka kinamna, humo nilale hata bila mkeka, chini, hakuna cha neti wala shuka…nilitamani hata mimi nijifie nimfuate mume wangu. Nashukuru mlvyokuja kututemblea siku ila na wale watu wa dini na kuyakataza hayo mambo kuwa ni mambo ya kimila, dini inayakataza kabisa. Mtu umefiwa, una majonzi, bado uzidi kuteswa, hayo yametoka wapi?’
Wakati anaongea hayo nikakumbuka jinsi gani mtu akifiwa anavyoteseka, sio kwa majonzi tu, ila gharama zake! Mimi karibuni nimefiwa na ndugu zangu , baba mdogo na mama mdogo. Misiba hii ilifululiza, kiasi kwamba tulibaki tukijiuliza nini kulikoni. Yote tulijua ni mapenzi ya muumba, ila kilichotuweka katika kuwaza zaidi ni hizi taratibu zinazotungwa sasa hivi na jamii. Si za kidini ila inakuwa ni taratibu zinazichipuka, na huishia kumuumiza mfiwa badala ya kumsaidia.
Siku hizi mtu ukifiwa, ujiandae kama unaandaa harusi, hata harusi inanafuu zake kwasababu kunapita kamati watu wanachangishana, lakini sasa hivi ukifiwa inabidi mkope , inabidi mchangishane wanandugu ili muweze kuwalisha wanakuja kuwapa pole. Nimejionea nilivyofiwa, kwani misiba iliongazana, kwahiyo hali ilikuwa tete kiuwezo. Ilifika wale waliokuja kutupa pole kuanza kulalamika kuwa mbona mnatupikia maharage, sie hatuli hiki tunataka hiki, tunataka nyama..huu sio utani, ila kweli watu wanadhamiria kuwa kwenye misiba siku hizi ni sehemu ya kupunguzia bajeti.
‘Kuna msiba kwa jirani, naona siku tatu tutahamishia bajeti yetu kwa jirani, mji huu usipojua kuishi utakufa njaa’ nilimsikia jamaa mmoja akisema. Nilimuangalia bila kummaliza. Kweli unahamishia bajeti yako huko, changia basi kiasi angalau nusu ya hiyo bajeti yako, lakini ukifika hapa hutoi chochote na kama ukitoa ni kiasi ambacho hata robo kilo hainunui. Huko tunakoenda ni kubaya….
Nilimugeukia Yule mama ili nisikie nini anachosema, nilimuonea huruma sana, kwani anasema hata rambirambi alizopewa kutoka huko mwanaume wake anapofanyia shughuli zake ameambiwa zitolewe ili zifanyiwe hitimisho la msiba. Hili hitimisho nalo ni sherehe siku hizi. Watu wameacha taratibi za kidini wanafanya yao. Hapo kunahitajika maandalizi ya hali ya juu watu wale na kunywa mpaka sare zinashonwa, picha za video zinachukuliwa ili ziwekwe kumbukumbu. Ni sawa, lakini hayo yafanywe na michango yetu sio kuwakamua wale wafiwa.
Mama huyu analalamika kuwa sasa hivi hana hata hela ya kula kwani hizo hela za rambirambi zilishachukuliwa muda, na alitegemea kuwa angalau angeanzishia kibiashara, kwasababu kipindi mume wake anafariki alikuwa ndio kachishwa kazi, na kunzisha kijibiashara kidogo kwahiyo hata akiba walikuwa hawana. Siunajua tena makapuni kama wamekulipa sana ni mshahara mmoja, zaidi ni kile kiinua mgongo chako.
Nafikiri ipo haja kwa viongozi wa dini kulikemea hili, kwani linavyoachiwa linaendelea kukua na kuwa kitu kingine kabisa. Itafika mtu akifiwa badala ya kulia uchungu na huzuni ya kufiwa, atalia ukata na jinsi gani atakavyowahudumiwa wanaokuja kumpa pole. Tumuogope mungu na tuwe na huruma na wafiwa, ni bora tujenge taratibu njema kuwa mfiwa akifiwa taratibu zote ziwe nje ya mfuko wake. Tumsaidie huyu kwasababu ana majonzi, ana pengo, na huenda kama ni mjane anajukumu la kuihudumia familia aliyoachiwa. Tumuogope mungu jamani, kwani leo kwake kesho kwako!
From miram3
Tuesday, February 23, 2010
Mama wa Kambo
Tukio hili linanikumbusha ile hadithi ya nani kama mama, ipo siku tutaimalizia;-
Ilikuwa saa tano za usiku, wakati tunajiandaa kulala, mara tukasikia hodi nje! Kwa muda kama huo hodi inaashiria mawili jema au baya. Ingawaje sauti ya huyo mtu aliyepiga hodi haikuwa ngeni kwangu, ilikuwa sauti ya kike, na ili tuwe na uhakika vyema, tukauliza `ni nani wewe?’
‘Mimi jamani, mama nani hii huielewi sauti yangu’ Nikamuangalia mwenzangu kuwa kweli ana uhakika na mpiga hodi. Mama nanihii akamtambua na kuelekea huko nje. Maongezi yao yalichukua muda mrefu mpaka nikaingiwa na wasiwas,i huenda huyo mgeni ana masahibu makubwa na alihitaji msaada wetu! Nikaona nami nitoke nje nikasikie mwenyewe. Nilipotaka kutoka nje, mara mama nanihii akaniita toka dirishani, nikabaki nimeduwaa, vipi tena ya kuongelewa dirishani, tena upande mwingine wa nyumba, ina maana haya mazungumzo hayakutakiwa huyo mgeni ayasikie?
‘Hapa kuna mtihani, huyu mama anasema ndugu zake wamemfukuza, na hana pa kulala, sasa mimi naona nikaongee na hao ndugu zake, kwasababu hao ndugu zake ni jirani zetu, tukimlaza huyu mama hapa watatuelewaje, Na ya Mungu Mengi, huwezi jua la kutokea’ Nikaduwaa kusikia hivyo, mtoto anamfukuza mama yake!
Baada ya muda mama nanihii akarejea kuwa mtoto wa huyu mama hataki kusikia kuhusu huyo mama.Mimi nkaona niende mwenyewe kuonana na huyo mtoto wa huyu mama na hadithi ikawa ile ile, na mengi waliyosema, yaani binti wa huyu mama na mumewe yalinitia wasiwasi, kuwa huyu mama anapenda kunywa, na akinywa ni mkorofi na isitoshe yeye ana ndugu zake wengine kwanini ang’ang’anie hapo. Nikawauliza sasa mimi nifanyeje kwasababu kaja kwangu na anahitaji msaada wa kujistiri huu usiku,na sio ubinadmu kumfukuza, yeye ataenda kulala wapi saa hizi. Jibu likawa nimfukuze atajua pa kulala!
Niliporejea na kuongea na mwezangu tukaona si jambo jema kumlaza huyu mama hapa kwetu bila taratibu za msingi. Wakati nawaza haya nikaikumbuka kisa kimoja cha msamaria mwema, jamaa iliyeamua kutenda wema kwa kumuhifadhi mke wa mtu ambaye aligombana na mumewe. Na katika ugomvi huo, mume mtu akamfukuza mkewe, usiku wa manane. Mke huyu ikabidi akimbilie kwa jirani kuomba hifadhi.
Jirani aliyegongewa, akashindwa afanyeje usiku kama huo na kwa mjumbe ni mbali kidogo, wakaona, huyo mke-wa- mtu alale hapo hadi asubuhi, na mapema waende kwa mjumbe. Wakampa huduma zote chumba na kupata chochote na baadaye wakaagana kuwa kesho asubuhi wadamkie kwa mjumbe ili kuondoa shari, na pili kusuluhisha hilo tatizo kwani kama huyu mume mtu atagundua kuwa wao wamemuhifadhi hapo itazua mtafaruku mwingine!
Asubuhi na mapema baba mtu akawahi kwa mjumba na kumwambia mkewe amuamushe mke- wa -mtu, ili ajiandae vyema, na waje huko kwa mjumbe. Mkewe akakubali akijua kuwa wanawake wanahitaji maandalizi ya asubuhi sio kama wanaume. Na mumewe alipoondoka, mkewe akamgongea mwenzake ili aamuke na kujiandaa, akaona kimya. Akagonga kiasi cha muda, na kudhani huenda huyo mgeni kwasababu ya uchomvu, kalala sana, kimya…!Akaona ampe muda kidogo huku yeye akijiandaa na kufanya kazi ndogondogo.Baadaye akagonga tena kimya...!
Kule kwa mjumbe baba mtu alifanya kazi ya ziada kumwamsha mjumbe, siunajua tena asubuhi na mapema, na kazi za ujumbe ni wito, pamoja ya kuchoka na shughuli za mchana kutwa ilibidi mjumbe aamuke tu huku akilalamika lakini kwa vile amekubali majukumu ikabidi amsikilize mtu wa shina lake. Baada ya maelezo ikabidi mjumbe amuendee msaidizi wake na wazee wengine , halafu mmoja akatumwa nyumbani kwa mume-wa- mtu ili aje naye kwa mashauri ya usuluhishi!
Huku nyuma mama-msamaria mwema akawa kachanganyikiwa kwanini mgeni wao haamuki licha ya kugonga kote huko. Mwishowe, akaamua ampigie simu mumewe kumueleza kuwa mgeni wao bado kalala, na licha ya kugonga kote haamuki. Ikabidi mjumbe aambiwe na wote wakaamua wafuatane hadi kwa msamaria mwema. Walipofika hali ikawa ile ile. Mjumbe na wazee wakashauri mlango uvunjwe, kwasababu ulikuwa umefungwa kwa ndani.
Kumbuka kuwa mume-wa- mtu alishaitwa kwa mjumbe na alishangaa alipofika kwa mjumbe anaambiwa asubiri kwani mjumbe katoka kidogo na kumbuka kuwa walioleta shauri hili walitaka isijulikane kuwa huyo mke-mtu kalala kwao. Yule mume-wa- mtu alisubiri kiasi cha kukata tamaa na akaamua arudi nyumnani kwake. Njiani akaamua apitie njia ya kwa rafiki yake ambapo mkewe alihifadhiwa,lakini alikuwa hajui kuwa kahifadhiwa hapo. Aliona kuwa ndio njia ya mkato ili afike kwake haraka. Alipofika karibu na nyumba ya huyu rafiki yake akakuta watu kadhaa wamesimama nje, akashangaa , akasema moyoni huenda jirani kapatwa na matatizo ni heri afike aulize kwani ujirani ni kusaidiana.
***********
Naona muda niliolipia intenet café umeisha, tutaendelea siku nyingine. Tubakie na kujiuliza maswali haya yafutayo:
-Je mimi nilikubali huyu mama alale kwangu, na kama nilikubali ilitokeaje
-Je ni masahibu gani yaliyowakuta wasamaria wema kwa kumhifadhi huyo mke wa mtu. Kuna mafundisho ndani ya kisa hiki naomba tuwe pamoja kama hutajali
From miram3
Mwoga huogapa kivuli chake
Ilikuwa zamu yetu ya sungusungu, na kundi letu lilijaa waongeaji, kila mmoja alijifanya anajua hii kazi na ya kuwa aliwahi kupitia jeshini, au mgambo. Wengine walijiita makomandoo, wengine mti mkavu nk. Ilimradi kila aliyepanua mdomo alijitapa kwa namna alivyowea. Hamna aliyebisha kwani wote waliokuwepo kwenye kundi letu walionekana ni wale waliokulia kipindi cha Nyerere. Kama ulimaliza vidato ulistahili kwenda mujibu wa sheria. Na ni wazi kabisa kama ulipitia enzi hizo utasimulia mengi yaliyokukuta na uwongo uliokithiri.
‘Taarifa kutoka kituo kidogo cha polisi inasema kuna majambazi yameoneka yakija kuelekea usawa wetu na polisi wanawafuatilia kwa nyuma, tunachotakiwa wakija tusijaribu kupambana nao kwani wana silaha kali’ alisema kiongozi wa kundi letu. Niliwageukia wenangu hasa yule aliyekuwa akisema sana, nikamuona mdomo upo wazi kwa woga. Nikamwambia ‘muda umefika wa wewe kuonyesha ujasiri wako..’ Akanigeukia na kuniangalia kwa woga akasema; ‘wewe hebu acha utani, hichi sasa ni kifo cha kujitakia, tutapambanaje na majambazi walibeba bunduki, kwanini tusirejee majumbani mwetu tuwaachie polisi..’
Mara gari lilioneka kwa mbali likija kwa kasi, nilichosikia ni mchakato wa miguu, ikipambana na nyasi, na nilipogeuka nyuma sikumuona yule rafiki yangu au wale waliojiita makomandoo wakati wa mujibu wa sheria. Nilishangaa, na kwa mbele nilimuona kiongozi wetu wa sungusungu akihangaika kutafuta mawasailiano na polisi. Nilimsogelea na kumuuliza wenzetu wapo wapi. Aligeuka nyuma nakujikuta anashangaa ‘ina maana hawakunielewa hawa watu, sasa wamekimbia, huko wanakokimbilia kuna usalama, wanaweza wakakutana na hao wamjambazi, watu wengine bwana..’ alisema Yule kiongozi.
Baada ya muda polisi walifika na kuanza kuwafuatilia hao majambazi, na baadaye tulianza kuwatafuta wenzetu walikokimbilia, na wengi wao walishafika majumbani mwao na kujifungia hakuna aliyekubali kuendelea kulinda. Na mmoja aliyetoka nje alisema kuna kundi moja lilikuata na majambazi siku zilizopita na wale majambazi waliawaamrisha sungusungu wote wavue nguo, na kuzalilishwa, ndio maana akakimbia. Ilikuwa hadithi ya uwoga wote tukabakia kumcheka.
Katika maisha yetu yakila siku, wengu tunapenda kuongea sana kuliko vitendo, wapo ambao kwa kuongea wanaweza wakamshinda hata mchezaji wa kombe la dunia, na kwa mdomo anaweza akaishinda timu yoyote, ngoja mtu kama huyu umpeleke uwanjani, utaishia kicheko, kwani badala ya kuupiga mpira vyema utaishia ugokoni! Wapo ambao wanajua kupigana kwa mdomo akikutana na mwenzake atamtambia kuwa yeye ni Tyson, lakini yote ni maneno matupu, kwasababu mdomo ni mwepesi kunena kuliko vitendo.
Tunashuhudia viongozi wetu wanavyotumia midomo yao kutafuta kura zetu, na kipindi chao kinafika. Tujiandae kusikia lugha nzuri za kisiasa, na sisi ambao ni wepesi kudanganyika tutaishia kupokea vijizawadi. Tuweni makini kwa hili, kwani hawa tunaowachagua ndio majemedari wa vita, na zamu yao ya sungusunu ikifika isije ikawa ile hadithi ya mwoga aliyeshia kukimbia kivuli chake mwenyewe na matokeo yake akaanguka kwenye korongo. Isije ikawa wale tuliochaguliwa kulinda sungusungu na majambazi walipokuja tukasingizia hatuna silaha!
From miram3
Friday, February 12, 2010
Mtenda akitendewa (2)
''Mimi na mke wangu tunapendana sana na nikuhakikishie kuwa sijawahi kutoka nje au kushawishika na mwanamke yoyote Yule na kutenda tendo la kuvunja ndoa yangu. Hili lilivyotokea ninahisi kuna mpango ulipangwa si bure. Lakini kama upo mpango basi umeniumiza vibaya sana, na sidhani kama nisipopata utatuzi wa mke wangu , sidhani kama nitaweza kuishi tena kwa raha.
''Hivi ninavyoongea mke wangu yupo jela kwa kosa la kutaka kuua bila kukusudia. Na baya zaidi alikiri mbele ya mahakama kuwa alifanya alichokifanya, kwahiyo mahakama iamue yenyewe. Nakumbuka alivyosema, au kuwauliza wazee mahakama. Aliwauliza hivi
‘Kama mume akimfumania mke wake anampa talaka na kama haitatoka talaka kitatoka kipigo na kudhalilishwa, je kama imetokea kinyume chake mke afanyeje, ikizingatiwa kuwa mali na watoto ilikuwa jasho la wote wawili , hakuna mali ya urithi au ndugui wa pande nyingine?’
Wazee wale walimwangalia kama mke aliyepagawa, na hakimu alichukua rungu lake la dola na kusema Pamoja na kuwa kosa limefanyika, haijalishi kuwa ni ni nani, sheria ndio ingetakiwa ifuate mkondo wake na sio kujichukulia sheria mkononi, kwahiyo mahakama inatoa adhanu kali iwe kama fundisho kwa wengine. Hutamini, mke wangu alinigeukia na kutabasamu, akisema ''haki imetendeka, ukitaka mfuate huyo kimada wako au nisubiri nikitoka nitahakikisha kuwa haki yangu ninaipata''. Na baadaye alianza kulia na sikuweza kuvumilia na mimi nikajikuta ninalia''. Alipofika hapa kweli alianza kulia, ikabidi nifanye kazi ya kumliwaza.
''Ushahidi ulionyesha dhahiri kuwa mke wangu aliporudi toka kwenye ile shughuli alinikuta nikiwa uchi na huyo mwanamke ambaye simjui na ilikuwa mara yangu ya kwanza kukutana naye. Niliambiwa baadaye kuwa alikuwa rafiki mkubwa wa mke wangu.
''Alipofika hakuamini macho yake alitoka mbio hadi jikoni na huko alikuwa panga. Aliporudi akamkuta Yule mwanamke akitaka kukimbia akamsukumizia kitandani na hapo likafuata pigo la panga, moja baada ya jingine. Kumbuka na muda huo mke wangu alikuwa kalewa. Mahakama yote hayo ilifikiria lakini ikatoa hiyo hukumu na nimemuona wakilimmoja ili anisaidie ili nimkomboe mke wangu. Na kama itashindikana ni heri na mimi niende jela , na ninahakikisha nitaenda jela kwa kmtafuta huyu mwanamke aliyenitega kiasi hiki, nasikia hakupata majeraha mengi...''
Nilibaki mimeduwaa nikitafuta ushauri mwema kwa jamaa yangu huyu ambaye ninamjua kuwa ni miongoni mwa waadilifu, na kama limetokea lililotokea ni ushawishi wa pombe. Pombe ni kishawishi kikubwa cha kutenda usiyoyategemea, ni vyema tukawa waangalifu na hili. Sasa nimshauri nini huyu ndugu yangu, ili kwanza amuokoe mke wake atoke jela, na je ipo sheria ya kumuokoa mtu kama huyu aliyekiri mbele ya mahakama kuwa ametenda alilotenda. Na pili ni jinsi ya kumuokoa rafiki yangu huyu ambaye nia yake ianweza ikampeleka pabaya, anayofikiria ni mabaya zaidi.
Hebu tuchangie kabla sijasema nilichomshauri !
From miram3
Tatizo ni kufaulu mitihani?
Wakati nawasikiliza hawa vijana waliojaa mle ndani kwa shauku, nilijaribu kujiuliza lengo hasa la mitihani hii ni nini, na je linakidhi haja ya watoto wetu? Nilicheka pale nilipotamani kumuuliza mzazi mmoja aliyekuwa akimgombeza mtoto wake kuwa amemuabisha kwa kupata chini ya kiwango.
‘Nimepoteza hela zangu nyingi kwa tuisheni, na kila kitu nilikupa sasa ndio nini hiki umefanya’ alilalamika Yule mzazi. Pembeni yake alikuwepo mama mmoja aliyejaa furaha kuona mtoto wake amefaulu vizuri, na hakusita kumshauri mwenzake kuwa kufeli sio kwamba mtoto wake alikuwa hana akili, lakini mitihani wakati mwingine inaweza ikaja kinyume na mtoto alivyojiandaa! Nikashangaa kidogo kusikia kuwa `kuna jinsi mtoto anavyotakiwa kujiandaa’
Hebu tujiulize kama wazazi mfano mtoto wako kipindi chote cha miaka mine aliyokaa shule hakuwa akifanya vizuri katika masomo na ghafla katika matokleo yake haya ya mwisho akawa amefaulu vizuri , wewe kama mzazi utasemaje? Na pia tuchukulie wewe mtoto wako alikuwa akifanya vizuri katika masomo yake, na kila mara anakuwa wa kwanza darasani, lakini mtihani huu wa mwisho akawa amefanya vibaya, wewe kama mzazi utasemaje, nahisi unaweza hata ukalaumu kuwa kuna jambo limefanyika kumfanya mtoto wako asifaulu na hata kukata rufaa!
Mimi nahisi kuwa ni bora tukawa tumewaandaa watoto wetu vyema, ili hata kabla ya mtihani watoto wetu wawe wameshafulu. Watoto kama hawa sidhani mtihani wao wa mwisho utakuwa ni tatizo, hata kunagalia matokeo itakuwa ni wajibu tu. Hawa ndio watakuwa wataalamu wetu, kwani maandalizi yalishafanyika mapema, nini alichofundishwa kilishafanyiwa kazi, na mtihani wa mwisho inakuwa kama marejeo ya kupima kile alichojifunza.
Wapo watoto waliokuwa wakienda shule kwasababu wanalazimishwa na hawakujua nini umuhimu wa elimu kwao, wengine walikwenda kwasababu baba zao wana uwezo na wakawa wakionyesha nini wazazi wao walicho nacho, bila kujali juhudi za wazazi wao. Hawa walifikia hata kuwadanganya wenzao ili wajiunge nao katika pilikapilika za starehe, na masomo kwao ilikuwa kama kupoteza muda. N hawa wanahamu ya kuangalia matokeao yao , na furaha yao ni kufaulu. Sasa fikiria mtoto kama huyu akiwa amefaulu, nini taifa letu litaraji baadaye!
Elimu ni muhimu sana, na kama ingefaa ilihitajika kila mtoto asome hadi chuo kikuu, ili aweze kuonyesha nini anachokijua. Nina imani kila mmoja ana uwezo Fulani, kama sio wa fani hii itakuw ya fani fulani ambayo ianweza ikaleta tija kwa taifa na kwa maisha yake mwenyewe, sasa ni bora elimu zikalenga taaluma. Ni bora vijana wakapimwa bado wakiwa wadogo nini wanakijua zaidi ili waweze kukisoma na kukifanyia kazi na tusiwaburuze watoto katika kukariri tu.
Nikiwa bado natafakari nikasikia mzazi mmoja akijisifia kuwa mtoto wake amefaulu vizuri , na anajua kuongea kiingereza kama mzungu. Nilimuuliza hesabu na Sayansi amepata ngapi, akasema katika masomo haya hakufaulu kwa kiwango kikubwa lakini kwa ujumla amefaulu.`Ukiongea naye utafikiri unaongea na mzungu’ akamalizia Yule mama. Mimi nilimpa hongera sana
From miram3
Thursday, February 11, 2010
Nifanyeje jamani...
‘Mama nanihii unahitaji mfanyakazi wa ndani?’ Yule mama alimuuliza mama watoto wangu, niliguna moyoni, nikijua nini jibu atakalopata.
‘Kwa hivi sasa sihitaji, inagwaje kweli ni muhimu ningekuwa naye, kwasababu, nashindwa kufanya shughuli nyingine au kutoka, kwa vile sina mtu wa kumkabidhi majukumu’ mama watoto alimijibu.
‘Sawa, lakini huyo ni mtoto mzuri kitabia, ingawaje hawa watoto wa nyumbani unaweza ukawaamini sana lakini wakafanya jambo ambalo hutazamii. Yaani mimi hapa nilipo natamani duniani inimeze kwa tukio lililotokea kwangu, kisa cha mfanyakazi wa nyumbani’ Huyo mama akaamua kukaa kwenye ngazi za nyumba yangu ili aweze kumhadithia mke wangu. Nilikuwa dirishani kwahiyo maongezi yao nilikuwa nkiyasikia vizuri, na kwa vile Yule mama hakujua kuwa nipo aliongea kiundani mambo yake , kama unavyowajua akina mama wakiamua kuongelea swala Fulani kwa mtu anayemwamini.
‘Ndiye unayetaka kuniletea mama nanihii?’ mke wangu aling’aka
‘Hapana sio huyo, huyo wangu namuandaa aende kwao kalikoroga mwenyewe’ Yule mama alisema , na kabla mke wangu hajamuuliza vizuri alianza kuhadithia kisa ambacho kilinifanya nishituke na kuamua kukiweka hapa ili wale wenye nia njema wachangie, na huenda iwe fundisho kwa wenye wafanyakazi wa nyumbani.
Binti huyu niliye naye nilimchukua akiwa mdogo, alipomaliza darasa la saba. Tulikaa naye kama binti yangu, na kwa vile alikuwa na adabu , mchapakazi mzuri niliamua kumsomesha sekondari hadi kidato cha nne. Hakufaulu, lakini tulikuwa na malengo ya kumsomesha zaidi. Lengo hilo lilikwama kwasababu mume wangu kibarua chake kiliota majani, ikawa mimi ndiye mhudumiaji wa familia. Kama unavyojua kipato changu ni kidogo nisingweza kumsomesha na kuilisha familia, kwahiyo tukapanda asubiri hadi mume wangu atakapopata kazi.
Siunajua maeneo ya huku kwetu kama unafanyakazi ili uwahi kazini inabidi uondoke saa kumi na moja alifajiri na kurudi nyumbani ni kuanzia saa mbili za usiku. Hili halikuwa tatizo kwasababu mume wangu alikuwa katika mkumbo huo kabla hawajampunguza kazini kwao. Na pia yupo huyo binti ambaye tulimchukua kama mfanyakazi wa nyumbani nab ado tunaendelea kumlipa, licha ya kujitolea kumsomesha na kumpa huduma zote kama mtoto wetu. Lakini kama walivyosema wahenga, kuku wa kienyeji hafugiki, na kweli kwa hili sidhani kama nitahitaji mfanyakazi wa nyumbani tena.
Mama nanihii, wakati mwingine nawashangaa sana hawa waume zetu, sijui akili zao zipoje. Unajua ninakuhadithia hili sio kwasababu niminga wa kutoa siri za mume wangu nje. Hapana, lakini lilotokea inabidi nimhadithie mtu ninayemuamini ili anipe ushauri. Naujua ushauri, na hasa ushauri nasaha kwani nimeshaupitia, lakini huu sasa ni mkali zaidi.
Wiki kama mbili zilizopita nimepata kalikizo kadogo nikaona nishirikiane na familia kujifanyia miradi midogo midogo, na hapo ndipo nilipogundua kubwa kuliko. Niligundua kuwa mfanyakazi wangu huyu wa nyumbani ni mja mzito. Na nilipombana sana anitajie ni nani aliyempa alikataa katakata, hadi nilipomwambia namrejesha kwao kijijini. Nitamrejesha ingawaje hataki lakini kwa hali ilivyo sitaweza kusihi naye tena.
Unajua tangu aliponitamkia mtu aliyempa ujauzito ule nilishikwa na kitui ambacho hadi sasa siamini na kwa vile hata aliyempa ujazito huo kakataa kabisa nashindwa kuamini kuwa ni kweli, hili linawezekana . Simini, naombeni msaada wenu kwenye janga hili’
‘Ni nani aliyempa uja-uzito huo?’ mama watoto akauliza kwa shauku.
Unajua mama nanihii, kama isingekuwa hili tatizo nililonalo na mume wangu, ningefungasha virago niondoke nimuachie huyu mume nafasi , manake kaniona sifai, lakini tatizo tulilonalo ni kubwa tunahitajiana sana, na hasa kumlea mwanetu ambaye naye pia waligundua kuwa anatatizo kama hilo. Na tuligundua kipindi mtoto wetu anaumwa mara kwa mara. Alipopimwa akaonekana ana virusi vya ukimwi. Ilibidi na sisi tukapime, na wote tukaonekana tunavyo!
Najua wote mnajua hili, sio siri kuwa mimi na mume wangu na mtoto tumeathirika, sasa sikutegemea kuwa mwenzangu anaweza kukosa imani na kudiriki kutembea na mfanyakazi wetu ilihali anajua kuwa anamtataizo haya. Hili mimi siamini kwani mume wangu kakataa katakata, na kusema huyu binti kaumua kumpakazia ili asiondoke hapa nyumbani. Je nifanyeje ili kuupata ukweli na mume wangu namuamini sana, na tangu tuoane naye hajawahi kunisaliti au kunidanganya. Sasa mimi nachanganyikiwa. Nisidieni ushauri, nifanyeje?
‘Fuata sheria mama nanihii, mshitaki na kwnye sheria utapata ukweli’ mke wangu alimshauri kwa harakaharaka hivyo, na ushauri huo ulimfanya Yule mama ainuke na kwa hasira akaaga huku akisema
‘Nini, nimshitaki mume wangu…kwaheri...'
From miram3
Mtenda akitendewa..(1)
‘Kwanini unaniuliza swali kama hili, kwani mimi nalichukulia kama maswali yenye muonekano hasi, yaani swali la kujitabiria ubaya, wakati ni vyema wakati wote tukajitabiria uzuri, mimi..’ nilijaribu kumpa ushauri nasaha lakini akanikatisha.
‘Wewe nijibu kama vile imekutokea kwa vyovyote vile, huenda ikawa bahati mbaya au kutegewa, na hamadi mkeo huyu kakufumania, ungefanyaje?’ aliniuliza huku kanikazia macho
‘Jibu liko wazi, ni kiasi cha kujiuliza, kama wewe umemfumania mkeo ungechukua hatua gani’ nikamuelezea nikijua kuwa kuna jambo zito jamaa anataka kunihadithia.
''Ni sawa, kwa wanaume ni rahisi kwasababu sisi ndio wenye uamuzi mkubwa, na kwa yoyote angesema kuwa talaka ingetoka bila kusubiri usuluhishi, lakini imetokea kinyume, na ujue kuwa mke kama ataamua kama mume, ina maana atakosa haki zake nyingi, nay eye atakuwa kwenye hasara kuliko mume. Naomba utafakari hili swali kwani sio natania, hili ni tatizo kwangu ndio maana nimekuja kwako, umesaidia wengi kwa ushauri, na nahisi utanisaidia kwa hili. Sikiliza kisa kilichonitokea mimi mwenyewe ndio utaweza kunipa jibu la uhakika.
''Ilikuwa siku ya sherehe ya kutimiza nusu karne, na iliandaliwa na mke wangu, sikupenda sherehe hasa zinazohusiana na ulevi ndani yake, lakini kwa vile mke wangu mpenzi ndiye aliyeandaa nikakubali na sikuwa na haja ya kukubali au kukataa kwani ilivyofanyika sikujua nilishanga nimepigiwa simu, nikiwa kazini kuwa kuna tatizo limetokea kwenye ukumbi wa jirani yetu. Jirani yangu ana ukumbi mkubwa wa sherehe na ni mtu ninayemheshimu sana, kwahiyo nilivyosikia kuwa ana tatizo sikuhitaji kuuliza tatizo gani nikaaga ofisini na kwa vile ilikuwa Jumamosi hapakuwa na kikwazo chochote.
''Nilifika kwenye ukumbi huo, na nilikuta mlango umefungwa, na pale ,langoni kumewekwa karatasi kubwa kuwa kuna ajali na watu hawaruhusiwi kuingia. Hutaamini, nilitumia mabavu kuingia, kwani huyo rafiki yangu alivyonipigia simu alisema kuwa mke wangu alikuwepo humo. Simu ilisema, rafiki yangu njoo hapa kwangu kuna tatizo kubwa na mkeo yumo, akakata simu. Sasa nakuta karatsi kuwa kuna ajali usiingie humu, sikukubaliana na hilo kwa muda huo nikawasukuma walinzi na kujitosa ndani mara nikakutana na kelele za `happy birth to you…
''Nilibaki nimeduwaa na mbele yangu alikuja mrembo kuliko wote duniani, alivyojipamba, alivyonivutia, nilitamani nimkumbatie hapohapo, lakini nikashikwa na kigugumizi kwani pembeni yake walikuwepo wazazi wake. Nikatabasamu nakumsogelea, na wote tukaelekea kwenye meza niliyoandaliwa , au tuliyoandaliwa. Nikalitaka kukasirika, lakini sikuweza, nilitaka kusema nina kazi nyingi nimeziacha ofisini lakini ikashindikana, kwani msemaji mkuu alikuwa akitoa burudani ya kila namna iliyonifanya niwe nikitabasamu na kuwaza nini kitafuata baadaye.
''Mara vinywaji vikaletwa, nilitaka kukataa nikijua udhaifu wangu, lakini aliyenisogezea kinywaji kikali ni mke wangu, nikanywa, nikanywa, nikanywa,…kila nikimaliza naongezewa. Mwisho nikamwambia mke wangu basi, naomba twende nyumbani, kwasababu namtamani. Pombe ilishakolewa kichwani. Mke wangu akasema mambo bado subiri.
''Nilitoka kama kwenda kujisaidia, nilipofika njia panda ya kwenda kwa wanawake nikamkukuta binti mmoja, na taswira ikanifananisha na mke wangu. Sijui ilikuwaje nikaanza kumtania, na utani uakazaa mengine nilishangaa tupo kwangu, kwenye kitanda change, na yaliyofuata hapo sitamanai hata kuyakumbuka. Na mara usingizi ukanishika. Niliposhituka ni asubuhi, nilizinduka nikijaribu kukuimbuka yaliyotokea jana, nikafumbua macho taratibu, na mara nikajikuta nimeshika kitu kama maji,…nikashituka na kuamuka haraka, mungu wangu, nilichokiona kilinifanya niamuke kutimua mbio, lakini nikaishia mikononi mwa asikari...''
Hebu fikiria ni nini kilitokea?
From miram3
Miadi ya kumuona bosi
Nilipofika kwenye hiyo ofisi, nilianza kukwamishwa na walinzi, kuwa nionyeshe kitambulisho na ni nani ninayekwenda kumuona. Nilijaza maelezo yangu kwenye daftari la wageni na kuelekea kwenye jengo la ofisi , sijui kuwa jengo lote hilo ni ofisi moja au kuna ofisi nyingi , nikajisemea moyoni nitajkua hukohuko. Hutaamini Tanzania yetu hii sio ile ya jana, majengo , maofisi yamewekwa kiutalaamu zaidi. Nilitamani name niwe ndani ya jengo hilo nakuitwa mfanyakazi wa kampuni hiyo.
Nilipofika maulizo nilimkuta dada mmoja ambaye kuongea kwake inaonyesha sio Mtanzania, ingawaje baadaye niliambiwa ni Mtanzania ila ni zile mbwembwe za kuongea Kiingreza mara kwa mara ndio maana hata akitamka maneno ya Kiswahili, inakuwa una-jua, you know…eeehe, tell… na vitu kama hivyo.
‘naomba kumuona Mr Mate(sio jina halisi)’ Nilimueleza Yule binti niliyemkuta pale mapokezi. Akaniangalia kwa dharau na baadaye akasema huku anainua simu nikijua kuwa anampigia huyo boso, kumbe anaongea na rafiki yake akimuombe amtoe chakula cha mchana. Alipomaliza akaniuliza nina ahadi naye
‘Kwakweli hapana, ila nilisoma naye na ukimwambia mimi ni nani hatahitaji hiyo miadi’ Nilimwambia
‘Sheria zetu za kazi hapa kama unataka kumuona huyu bosi mpaka uwe na ahadi naye, kwa ushauri andikisha hapa ili siku yako ikifika nitakuarifi kuwa uje umuone lini na saa ngapi, na ningeshauri iwe ni swala la kikazi’ akanisogezea karatasi iliandikwa `appointment to……
Nilitaka nisijaze , niondoke, lakini nikaona huo ni utaratibu, na kila ofisi ina taratibu zake. Lakini kumuona rafiki yangu ambaye tulipokuwa tulikuwa chumba kimoja kwenye sekondari ya bweni, na tulishibana sana. Nikaijaza ile fomu, lakini kabla sijaondoka, nikaamua nimpigie simu ambayo niliipata toka kwa mfanyakzi mmoja ambaye alinielekeza kuwa huyo jamaa siku hizi ni bosi hapo. Simu iliita mapaka ikakata, nikajisemea huenda yupo kwenye mikutano yao, siunajua tena mameneja kila mara ni mikutano.
Nilirejea nyumbani nikijutia nauli yangu niliyoipoteza na kukosa kumuona rafiki yangu huyu ambaye tangu tumalize shule pale , yeye akaenda mlimani mimi nikaelekea Mzumbe, hatukuwahi kuoanana naye tena. Nilikuwa na mengi ya kumuelezea, na huenda akanishika mkono, siunajau tena kazi siku hizi ni mkono kwa mkono, lakini wapi.`Ili umuone bosi lazima uwe na ahadi naye, na uapngiwe saa ngapi na nini cha kuongea..aaah,kweli tumekuwa wadhungu’
Siku ya pili nilimpigia jamaa aliyeniunganisha na huyu `bosi-mate’ akasema yeye alimuendea hado ofisini kwake, akiwa katika kazi zake za kiofisi, na hapo alimdokezea kuhusu mimi, na jibu alilopata hakuamini kuwa alikuwa rafiki yangu, tuliyesoma naye na kuishi chumba kimoja kwenye shule za bweni
`Achana na hawa Waswahili bwana, wakisikia upo ofisi Fulani, basi wao wanaleta ushule hapa. Nimesikia habari zake, sina cha kumsaidia najua kakwama..’ alisema huyo bosi huku anatizama katatasi za miadi, na alipoiona karatasi yangu akaiweka pembeni, ikimainisha haina umuhimu kwake.
Siku ya pili nikasikia gari likisimama nje ya nyumba yangu, nilipotizama dirishani sikuamini aliyekuwa akifungua mlango wa lile gari. Ni Yule Yule rafiki-mate wangu. Alikuwa sio Yule nilyemjua, kachana, suti na kitambi cha haja. Alitembea kwa mitao, huku akiangalia kwa dharau jengo ninaloishi.
Nilimwambia mke wangu huyo jamaa akija amuulize kuwa ana ahadi na mimi, na kama hana aandike kwenye kidaftari ili nitafute muda wa kuonana naye. Mke wangu akacheka na kusema hapa ni nyumbani wageni hawana cha ahadi. Lakini nikamukumbusha hii ni ofisi yangu, na mimi nina haki kama yeye akiwa ofisini kwake.
Nilimkaribisha rafikiyangu na alinitembelea kwasababu kasikia maeneo ninayoishi kuna viwanja vinauzwa kwahiyo anahitaji nimsaidia kuhakiki, asije akauziwa kanyaboya. Nilimkumbusha kuwa nina miadi niliyoiweka ofisni ya kukutana naye. Akacheka, na baadaye akapapasa mfukoni na kutoa elifu kumi. Nilishikwa na mshangao, na kumuuliza kuwa ina maana kila mwenye miadi na yeye anampa shilingi elifu kumi. Akacheka kwa dharau akasema hapana najua hali halisi hii ni kwa ajili ya chai kwa watoto. Nikaikataa,lakini akaipitishia kwa mke wangu, ambaye kiuungwana aliipokea.
Haya ndio maisha halisi, tunajifunza nini hapa. Tujadili hili kama linatugusa.
From miram3
Monday, February 8, 2010
Tutafakari
Eneo kama hili ni sehemu ambayo kiimani inamkurubisha mtu na mola wake kwani hapa ni kitovu cha matibabu ni eneo ambalo utaona ugonjwa wa kila namna, na kweli kila mara tuliona magari ya wagonjwa ya kutoka sehemu nyingine za hospitali yakipita kuonyesha kuwa kuna wagonjwa walioshindikana walikuwa wakiletwa hapo. Lakini mbona vitendo na hisisa hiyo haviendani, kwasababu mtu akitoka eneo hilo keshasahau kuwa leo au kesho anaweza naye akawa miongoni mwa wanaoletwa hapo kuhudumia, basi muda wa ibada ukifika inuka haraka ukamuombe mola wako, ili akuepushie na kila lenye kuepukika na awajalie wagonjwa wetu wapone!
Wakati nimefika kwenye nyumba ya ibada,tukiwa tunasubiri muda nikagundua kuwa kuna mtu ananitazama sana, kiasi kwamba hata nikigeuka kumtizama habandui macho kuniangalia mimi. Ikafika hatua nikaanza kuogopa , na hapa nikakumbuka hadithi ya babu yangu ambaye hakuchoka kutupa hadithi za kutufanya tuwe karibu ni mola, tuwe na imani thabiti. Kisa hicho kilikuwa cha jamaa mmoja ambaye pamoja na kupewa utajiri wa mali pia alijaliwa kuwa tabibu, na aliweza pia kutabiri na kujua nini kitafuata baadaye. Pia aliweza kutafsiri ndoto na kila akiota ndoto zake huwa kweli..
Kwasababu ya utajiri wake alikuwa na walinzi ambao walikuwa wakimlinda , kwani ukiwa tajiri na maadui huwa wengi. Walinzi hawa wakati anafanya ibada huwa wanakuwa pembeni mwake na nje wanakuwepo wengine. Kwa ujumla hakuna adui aliyeweza kumsogelea, alikuwa kama mfalme. Pamoja utajiri wake hakuacha kufanya ibada.
Siku moja jamaa huyu akiwa kwenye ibada akamuona mtu asiye mtambua, mtu huyu mgeni kwake muda wote alikuwa akimtazama na hakubandua macho kwake kiasi kwamba kilimpa uwoga huyu tajiri, akawaangalia walinzi wake na kuwaona wapo karibu naye akapunguza uwoga.Hamu ya kutaka kuinuka ili aende kumuuliza huyu jamaa kulikoni ikamjia na kabla hajafanya hivyo ghafla akashikwa na kitu kama kausingizi, na kupoteza fahamu kwa muda.
Wakati akiwa nje ya fahamu zake alimuona Yule jamaa akiinuka na kumjia , na alipomkaraibia alimwambia, `ndugu yangu mimi ndiye yule mgeni asiyependeka, lakini ni wajibu wangu kumtembelea kila mtu siku yake ikifika. Sasa nakuomba kwa vile wewe ni mja mwema, na muda wako haujafika nikupe taarifa kuwa baada ya nusu saa nitarudi kwako kuchukua ile dhamana ya mola wako aliyokukabidhi, na mara fahamu zikamrejea kabla hajaambiwa mengi.
Hebu fikiria mtu kama wewe upewe taarifa kama hiyo ungefanya nini. Lazima ungeshikwa na kihoro na huenda ungekimbila kufanya lile la mwisho ambalo ulikuwa hujalifanya kama ungekuwa na moyo huo. Mola ni mjuzi wa yote na katika kitu ambacho alitupa ni mtihani wa umauti. Kama kila mtu angejua siku yake ya kufa sijui dunia ingelikuwaje. Na labda tungekuwa tunapewa muda wa kutafakari kwa waja wema wangeutumia kutubia na kurejesha madeni ya watu kama yapo, hata kuandika usia lakini wapi, hiyo ni siri ya Manani.
Basi jamaa Yule alipozindukana cha kwanza nikuwaangalia walinzi wake, ambao walishahisi hali isiyo ya kawaida ya bosi wao, wakamuuliza vipi yupo safi. Akawajibu kwa sauti ya kukwaruza kuwa yupo safi na macho yake yakaangalia kwa Yule jamaa, na akakuta bado yupo pale nab ado kamtizama kama kwanza. Akawauliza walinzi wake kuwa Yule jamaa anayemuangalia aliwahi kuinuka pale alipokaa, na walinzi wake wakashangaa, kwani hakuna hata mtu mmoja aliyesogea pale walipokuwepo kwa muda wote huo.
Yule jamaa akaanza kuogopa, akainuka na kuelekea chooni, huko akatafakari kuwa ile ni ndoto au nikweli, na tafsiri yake ya haraka ni kuwa muda wake wa kuishi hapa duniani umeisha. Hili halikukaa kichwani, hakukubalina nalo moja kwa moja. Akaona arudi awaambia walinzi wake wamkamate Yule mtu, alipofika pale Yule jamaa akawa bado anamumuangalia kwa mtindo ule ule, lakini akaogopa kuwaamrisha walinzi wake wafanye kile alichotaka. Aliinuka na harakaharaka akatoka kupitia mlango wa chooni, nia yake ni kukimbia ili amkwepe Yule jamaa kama ndiye mtoa roho.
Alipofika nje, akawa anamtafuta dereva wake na alipoangalia saa yake akaona imebaki dakika mbili tu, na alichofanya ni kukimbilia gari lake alilokuwa amaligesha upande mwingine wa barabara. Katika kuvuka barabara kwa pupa hakuangalia vyema upande mwingine mwa barabara, kumbe kuna gari lililokuwa likija kasi likamzoa juu, juu na laipotua chini, akawa kapoteza fahamu na hali yake ilikuwa mbaya kabisa. Mara kwa mbali akamuona Yule jamaa akitoka nje ya ule msikiti akawa anamjia. Alijaribu kupiga kelele ili walinzi wake waje wamuokoe lakini wapi.
Jamaa akamjia na kumwambia, `hivi wewe hukunielewa, sasa muda umefika, na watakaonisaidia kuichukua dhamana na watu ni walinzi wako..’ Jamaa akashangaa, na kujitahidi kupapatika, na kweli waliokuwa wamemshika vizuri walikuwa walinzi wake, wao walikuwa wakijaribu kumsaidia ili asijiumize zaidi, kumbe wanamsaidia jamaa mtoa roho amalize kazi yake, na muda ulipofika akawa ameaga dunia!
Naombeni tutafakari, hasa tuliojaliwa, tunapopata mali isiwe ndio kuwa tumefika, tukumbuke kuwa yupo mfalme wa wafamle ambaye katukabidhi dhamana yake, ipo siku atafika popote na kuichukua dhamana yake. Ni vyema tukazitumia mali zetu vyema ili ziwe msaada wa baadaye. Hili ni kwa kila mtu kuwa, ugonjwa ni moja ya mitihani ya kutukumbusha kuwa sie hapa duniani ni wapiti njia tu, yupo mwenye milki yake na ndiye wakutegemewa.
From miram3
Ni mali asili yetu tu!
Njiani tulishuhudia mahindi yaliyositawi vizuri kuashiria kuwa huenda neema baada ya kipindi cha ukame inakaribia. Pia tulishuhudia maeneo mengi yaliyojaa rutuba, lakini hayajawahi kulimwa, na hapo ndipo mjadala ukazuka, wengi wakiuliza kwanini maeneo kama hayo yapo wazi muda mrefu, ina maana hayana watu wa kulima, au ni maeneo yaliyotengwa na serikali kuwa yasilimwe!
‘Mimi sikubaliani na hilo kuwa haya ni maeneo ya serikali ambayo hayaruhusiwi kulimwa, haya yapo miaka nenda rudi, ila nani atakuja kupambana na hizi mbuga, si hatari tupu, wanyama na huduma za kimsingi hazipo maeneo kama haya..’ alisema mmojawapo.
‘Mimi naona ipo siku serikali itamkabidhi muwekezaji mmoja toka nje, na itakuwa mwanzo wa migogoro kama ya akina Mgabe..’ akasema mmoja wa abiria.
`Lakini ina maana hata kilimo kinahitaji muwekezaji, kina utaalamu gani zaidi wa kumuita Mzungu, hili naona lipo ndani ya uwezo wetu, labda tuseme zana za kilimo kama matrekita, na pembejeo, na haya yanaweza kununuliwa’ akasema mwanamama mmoja.
‘Mimi inanishangaza kweli kila kitu muwekezaji toka nje, ina maana vyuo vyetu haviwezi kutoa wataalamu wakuweza kuyamudu haya, hawa mabwana shamba hawa wataalamu wa viwanda, mashine wanaomaliza wanakwenda wapi?’ Mmoja akauliza, akisubiri apatiwe jibu.
‘Mimi nauliza swali moja, kuna kitu gani ambacho tumekifanya kama waafrika, au tuseme kama Watanzania ambacho wazungu watakuja au wanatamani kuja kukiiga, kweli kipo kitu kama hicho?’
Swali hili ndilo lilozaa mjadala na kila mmoja alijaribu kutoa hoja zake, wengine waliishia uchekesha watu kuwa kitu pekee ambacho mzungu angependa kuja kuiga kwetu ni uchawi na utamaduni wa asili kama wa kimasai. Huyu alitoa mfan, kuwa maeneo mengi tunayopita ambayo wanaishi watu, lakini maendeleo yao ni duni, vijumba vya majani , mashamba madogo yote hayo yanasababishwa na ushirikina, watu wanaogopa kulogwa na hili wazungu hawana na huenda wanatamani walijue’ watu wakaangua kicheko,.
‘Mimi naona kitu pekee ambacho mzungu anakitamani kutoka kwetu ni maliasili yetu tu, hakuna kingine. Malisili iliyopo hapa nchini ni utajiri mkubwa na wazungu wakipita hewani wanautamani, na hili ndilo jambo ambalo wao kwao ni adimu na wanatamani waje , na ipo siku watakuja tu!’ akasema mzee mmoja. Ilibidi nigeuke nimwangalie mara mbili, kwani hoja yake ina maana kubwa kwa wenye kutafakari.
Ukiangalia maeneo yaliyopo wazi ni mengi lakini asilimia kubwa ya kila Mtanzania inauangalia mji wa Dar, au miji mingine, hata mambo muhimu na huduma za kibinadamu zote zinalenga mijini, na hapo sera zetu ni kilimo kwanza. Hivi hiki kilimo kwanza kitakujaje, kama vitu muhimu kama matrekita na huduma za jamii zitakuwa hazikupelekwa vijijini.
Mimi ningeonelea ile sera ya Mwalimu ya vijiji vya ujamaa, ingerejeshwa kitaalamu zaidi. Wakusanywe vijana, mashababi, wenye nia safi wakabidhiwe vifaa vya uzalishaji na huduma muhimu wapewe mapori, na huko vitu kama jeshi la kujenga taifa likapewa dhamana ya kusimamia. Kama ingefanyika hivi nahisi miji ingehamia vijijini muda si mrefu, na tusingekuwa na haja yawawekezaji wenye uchu wa uchumi wetu.
Na jambo jingine kwanini hawa wawekezaji wakija wanapewa viwanda vyetu ambavyo tulishaumia navyo, kwanii wasiunde vyao vipya ili vije vishindane na hivi vyetu? Kwa mfano wangekuja waanzishe Tanesco yao, Tazara yao , TRC, yao, na waanzishie vijijini…akaongezea Yule mzee.
Jamani mna chakuongezea, kwani mjadala huu ulitufikisha kwenye foleni za Dar, tulijikuta tumeshafika Ubungo, na kukaribishwa na adha ya foleni.
From miram3
Wednesday, February 3, 2010
Haya sio mapenzi
Nikiwa nimekata tama, mara nikasikia mngurumo wa gari ukija kuelekea kwenye lile geti, name nikasogea pembeni. Alieyekuwemo mle ndani alipiga honi mara tatu na mara geti likafunguliwa. Mlinzi akiwa na sare za kimgambo aliharakisha kuliweka geti vizuri na baada ya gari kupita akasogelea ule upande niliposimama, akaniuliza nina shida gani.
`Nilikuja kumuona mwenye nyumba hii, ni rafiki yangu sijui kama yupo?’ niliuliza. Na cha kushngaza yule mlinzi akaniangalia kutoka utosini hadi chini, akarudia mara mbili, halafu akageuka akaondoka kufunga lile geti. Nilishikwa na butwaa, lakini sikukata tama, nikaamua kutumia njia nyingine. Nilikuwa na simu ya huyo rafiki yangu nikampigia, akasema nisubiri anakuja, na mara geti likafunguliwa.
`Mna ulinzi mkali kweli, mnajihami nini hivi?’ nilimuuliza rafiki yangu ambaye aliishia kucheka, na kusema hayo ni mambo ya kawada. Na tulipofika ndani akanitambulisha kwa mkewe amabye alisema aliniona wakati anaingia lakini hakuja kuwa mimi ni rafiki wa mume wake.
‘Samahani sana shemeji , sikujua kuwa aunakuja kwetu, karibu jisikie nyumbani.
‘Mama, nataka maji ya kunywa’ Mtoto wa miaka saba hivi alimwambia mama yake, na mara mama akabonyeza kitufe fulana, akaja dada mmoja akaambiwa ampe mtoto maji. Na mtoto alipokunywa akawa amejimwagia na kuanza kulalamika kuwa nguo zimelowana. Mama yule akafanya kama mwanzo alipokuja yule binti akaambiwa ambadilishe yule mtot nguo. Na mara likatokea hili, na lile kuhusiana na mtoto ikawa kila mara anaitwa mtumishi wa nyumbani. Ilifikia hatua tukawa hatuongei, ni kumsikiliza yule mtoto, mapaka mimi mwenyewe subira ikaniishia.
‘Unajua rafiki yangu, siku moja tulikuwa nyumbani na babu yangu, tulikuwa tunategea kazi tuliyopewa ya kuchota maji. Maji hayo tulikuwa tukiyafuta mbali kidogo. Na kwa nje wakaoneka watoto wakipita na ndoo za maji. Watoto hawa baba yao anauwezo, kwenye kijiji kile alikuwa ni miongoni mwa waliojaliwa kuwa na hali nzuri, nyumba nzuri, umeme, na maji, lakini wakati mwingine maji yanakatika. Cha ajabu ambacho tulimuliza babu ni kwanini pamoja na uwezo wao wote, lakini watoto wa nyumba ile walifanya kazi kama mchwa. Hawakujali utajiri wa baba yao, walifuata majani ya ngombe kama sie, walichota maji wenyewe na wala hawakuwa na mtumishi ndani…’
‘Huo ni ubahili tu, kama wana uwezo kwanini wawatese watoto, inaonyesha hawana upendo kwa watoto’ alinikatiza shemeji yangu.
‘Babu yangu alisema, mtoto ni sawa na maji akiwa bado mtoto, lakini akiwa mkubwa ni sawa na plastiki inayovunjika. Alisema muda wa kumweka mtoto vizuri ni muda akiwa mdogo, na hapo ndipo anaweza kuijenga fikira yake kinamna utakavyomuelekeza. Ukakamavu wa akili, ujasiri heshima na adamu ni wakati mtoto akiwa mdogo. Babu yangu alituasa kuwa ukitaka kumpenda mtoto wako usimdekeze. Kumdekeza mtoto sio upendo, ni kumharibu na huyo mtoto akikua kama atapata matatizo kutokana na kudekezwa huko atakuwa akikulaumu wewe kuwa ndio chanzo. Na kumweka mtoto katika ujasiri wa kufanya kila kazi, hata kama mtoto atalalamika kwa muda ni tunu na ni akiba ya huyo mtoto pindi akiwa mkubwa.
‘Shemeji, ni sawa uongeayo, lakini yote hutegemea wakati, na uwezo, kama mna uwezo kwanini umtese mtoto. Mimi mwanangu sitamtesa kabisa kama bado nina uwezo’ alisema shemeji yangu, lakini rafiki yangu kila nililoongea aliniunga mkono, lakini ilionyesha wazi hana cha kusema mbele ya mkewe.
Baada ya maongezi niliaga, lakini nilimuonea huruma sana yule mtoto. Nilimuonea huruma kwasababu malezi yale hayakustahili hivyo, kwa umri kama ule, alihitajika kujituma baadhi ya kazi, inashangaza hata maji ya kunywa hajui ayapate vipi, chhoni mapaka apelekwe, anawishwe,… jamani wazazi tusihadaike na uwezo, tukawaharibu watoto wetu tukijifanya tunawapenda. Huo sio upendo kabisa, huko ni kumharibu mtoto.
From miram3
Ndoto ya ajabu
Nilihisi kuwa karibu na wenzangu ambao nao walikuwa katika hali kama yangu. Kwa mpangilio ule tulikuwa tukipangwa makundi ya watu kadhaa, wakiisha yanaletwa mengine, na kundi lililopo sasa lilikuwa kundi langu. Niliwaza jinsi ya kujinasua, lakini kila nilivyowaza nilijikuta nikikabiliwa na vikwazo, na ili kwenda kuchomoa moja ya mnyororoniliyofungwa nayo ilibidi niwavuke wenzangu waliopangwa karibu nami, na hawakubali uwavuke kwasababu ukiwavuka zamu yao itakuwa karibu na hata nikiwavuka kwa mbele kulionekana vitu kama ukuta wenye seng’enge zilizotegeshwa umeme, na kuwekwa vibao vyenye maneno fulani.
Seng’enge ya ukuta wa kwanza iliandikwa ngawila, nilihisi kuwa pale palihitajika pesa, ili upite, na si pesa ndogo, na hata kama ni ndogo inategemea uwezo wako wa kuzipata, sijui ilihitajika kiasi gani lakini niliona sifuri nyingi tu. Nikagwaya nakujiuliza ina maana wote waliokuwa wahanga wa lile bisu hawakuwa na hizo pesa. Labda kikwazo cha ukuta wa pili
Naomba hamsini...
Mtoto wa miaka tisa hivi alikuwa akiniangalia kwa macho ya huruma, alikuwa akisubiri niitikie shikamoo yake, na nilijua nini kitafuata baaada ya hapo. Nilisimama na kumsogelea Yule mtoto, sijui kwanini , ila nahisi kuna jambo lilinivuta ili nisikie nini mtoto yule anataka kusema zaidi ya kunisalimia.
`Marahaba, hujambo mtoto’ nilimuitikia
`Sijambo, naomba hamsini baba, naomba nipate nauli ya kufika mjini’aliatamka yule mtoto akinisogelea. Nahisi alishaambiwa mtu akikuitikia shikamoo yako ni mtumwema wengine watashia kukutukana, wakijua shikamoo yako ina nia ya kuomba.
`Mjini unaenda kufuata nini, nawewe sahizi ulitakiwa uwe shule’ nilimuuliza na moyoni nikajisemea kwanini na mimi asiniulize swali, wewe sahizi unafanya nini hapa wakatui ulitakiwa uwe ofisini au shambani au sehemu yako ya kazi.
‘Ninakwenda mjini kuomba pesa, baba anaumwa hana hela ya matibabu na yakutusaidia kuishi, mama alikufa zamani, sasa kila ninayemsalimia hataki kuitikia kwasababu wanajua nitawaomba pesa. Sio nia yangu kuomba pesa, lakini ninaogopa kuwa na baba naye anaweza akafa, kwasababu anaumwa TB, na hana ndugu wakumsaidia’ alisema yule mtoto huku machozi yakimtoka. Kwa hali kama ile hata kama una roho ngumu namna gani ungeitoa ile senti yako ya mwisho uliyoiweka kwa ajili ya nauli.
‘Wamezoea hao watoto kuombaomba, hawataki kwenda shule wanabakia kuombaomba baadae wanageuka kuwa vibaka’ Jamaa mmoja akapayuka akinipita kwa kasi. Nilimwangalia kwa makini nikajisemea, kama kweli angelisikia masahibu ya huyu mtoto hangelitamka maneno kama yale. Ni kweli wapo watoto ambao hugeuka ombaomba kwa kukaidi kwenda shule, ni sawa na watu wengine wazima wanageuka kuwa ombaomba kwa kujisingizia ugonjwa na kuwafanya wenye haki na wanaostahili msaada kukosa.
Nilimgeukia yule mtoto na kumuuliza kwanini asingeenda shule kwanza, jibu alilonipa ni kuwa hana hela ya sare za shule, hana hela ya madaftari na hata hivyo angewezaje kumuacha baba yake afe ndani na ili hali yeye ndiye anayetegemewa kutafuta pesa, ili wapate angalau pesa kidogo ya kununulia chakula.
‘Baba , wakati baba anafanya kazi tulikuwa tukisoma shule nzuri ya kulipia, lakini mama alivyoanza kuumwa baba akapunguzwa kazi, na hapo baba ilibidi auze baadhi ya vitu ili amtibie mama. Aliuza kila kitu nab ado mama hakupona na hatimaye akafariki. Nilibaki na baba ambaye alikuwa akifanya vijibarua hapa na pale na ghafula naye akaanza kuumwa, alipopimwa akaonekana ana TB. Alianza kukonda na kukosa nguvu ya kufanya vibarua sasa yupo nyumbani sijui kama atapona. Lakini ipo siku nitapata pesa nyingi nitamtibia baba yangu..’ ilikuwa kauli ya huzuni ya yule mtoto.
Nilitoa kilichokuwa mfukoni na kumpa yule mtoto , na alinishukuru hadi kunipigia magoti , na mara gari la mjini likaja akapanda akaondoka. Niliwaza na kuwazua nini dunia inapokwenda, ina maana huruma zimekwisha ndani ya mioyo ya wanadamu? Ina maana hakuna majirani wanaojua tatizo hilo la huyo baba anayeumwa? Ina maana kweli kizazi hiki cha watoto kama hawa kitaishije? Je hata hawo waajiri waliomfukuza au kumpunguza kazi huyu jamaa hawana watoto kama yeye? Labda wao hawatakutana na masihibu kama hayo, kwasababu wao ni matajiti lakini tukumbuke kuwa kuna leo na kesho.
Ombi langu kwa jamii ni kutafuta jinsi gani ya kuwasaidia hawa watoto ombaomba, huenda hadithi kama hii imo kwa wengi. Nina imani kuwa wapo wenye uwezo, na kama tukiamua kwa ukweli, kila tajiri mwenye uwezo akaamua kumsaidia mtoto mmoja mmoja, nina imani tutakuwa tumesadia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la watoto wa mitaani. Sidhani hamsini, au shilingi mia utakayompa itamsaidia sana zaidi ya kuwasaidia elimu kwa ajili ya maisha yao ya baadaye. Badala ya kuomba hamsini, tuwaambie waombe elimu.
From miram3
Mdharau Mwiba
‘Jirani vipi naona umejiinamia, unatunga sheria nini, au mama watoto kakupa mgongo’ nikamuuliza kwa kebehi, nikijua kuwa ni mtani wangu kwahiyo hata ni mtanie vipi siwezi kutupiwa mawe.
‘We mtani acha tu, kama ni mtihani wa maisha, basi mie niliopewa ni wa chuo kikuu wakati nipo chekechea. Hapa nilipo natamani aridhi ipasuke nizame mzimamzima, lakini mmh, maisha bado nayatamani ndio maana natafakari bila majibu’ akisema kwa kuchanganya na lafudhi ya kwao kuonyesha kuwa hali aliyonayo imemkwaza hadi kusahau kile Kiswahili cha visiwani, kwani wengi walizoea kumuiita mkisiwani badala hasa ya kabila lake kutokana na jinsi alivyopenda kuongea lafdhi ya Kiswahili cha watu wa kisiwani.
‘mtihani gani mtani wewe, usije ukawa umefumaniwa na mkeo kaambiwa na sasa …’ nilisema kiutani na hapohapo akanikatiza .
‘Sikiliza mtani, mie sina tabia hizo za kihuni, mimi nilikuaja hapa Dar kutafuta pesa, nikachuma nikajenga na kuwekeza kama unavyonijua, nikarudi kijijini, wazee wakanikazania nioe, sikupenda sana kuoa, niliona pesa ndio mke-wangu. Aaah, lakini nikaona kuna haja ya kuoa, ila sikupenda masharti ya wazee, wao walitaka nioe mke walionichagulia wao.’ Mtani akaanza kunipa kisa na kunionyesha kwa ishara kuwa nikae karibu naye.
‘Basi mtani, mimi kwasababu nina pesa, nina uwezo nikawaambia wazazi nitatafuta mke anayeendana na mimi, awe amesoma na awe mtoto wa mjini na sio wa huko kijijini. Wazee wakaniasa kuwa wao walinitafutia mke ambaye wanajua tabia na mienendo ya koo na sili yao, kwa ajili yangu na kizazi kitakachozaliwa. Mimi nikawaambia hayo ni mambo ya kizamani.
‘Nikamtafuta mke wa kwanza tukafunga hjarusi ya kukata na shoka, wazee wakaja Dar, wakala na kunywa hadi wakasahau kwao, baadaye wakaondoka. Haikupita mwezi mke yule akawa anaumwa ugonjwa wa ajabu. Kila mara anadondoka anatoa mapofu, anapoteza fahamu. Nilihangaika wee, paka nikakata tama, ikabidi mwenyewe asalimi amri arudi kwao, na hutaamini hali ilimwia mbaya hadi akapoteza maisha.
‘Nikaomboleza weee, baadaye nikasema hata lazima nitafute mke mwingine. Mke wa pili alikuwa chuma, lakini bwana we, akawa kila akibeba mimba inaporochoka, hee nikasema sasa inabidi nirejee nyumbani nikatambike manake imekuwa too much. Hutaamimi mimba ikajipanga vizuri inafikia miezi ya katiokati ikachomoka na mwenyewe akapoteza uhai. Je hali kama hii utasema ni nini hasa.
‘Sasa nimakaa nikawaendea wazazi wanieleze kwanini wananifanyia hivyo, kama ni laana, imeshanifunza kwanini wasiniachie maisha yangu. Nikawapa vidonge vyao, nikawaambia bado sijakoma, nitamuoa nimpendaye si wanaompenda wao. Nikatafuta wee, mwishowe nikampata chotara wa kisomali na kibantu, ndio huyo shemeji yako niliye naye sasa, ingawaje jana kaondoka kwenda kwao. Tatizo, likawa kila akizaa ikifikia miaka miwili mtoto anaumwa, damu inakwisha anapoteza maisha, sasa mtoto wa tatu tatizo linajirudia, nimepoteza pesa, kwa matibabu lakini hakuna kilichopatikana. Nikaenda kwa madakitari bingwa wakasema kuna mgongano wa viasilia. Yaani damu yangu na mke wangu haiendani, na ina maana kwa vyovyote kila tukizaa tatizo litakuwa pale pale. Sasa nimechanganyikiwa.
‘Unajua kwanini, wazee nilipoondoka mara ya mwisho niliwaudhi nikaawambia wasitegemee kuwa nitaenda kuwaomba msamaha na kumuoa binti wanaomtaka wao. Na wakasema asiyesikia la mkuu huvunjika guu. Ni wazee wangu wanafikia kusema kuwa mimi siwasikii, nisingewasikia ningewejengea hekalu kule mlimani….hata, sijui ni laana au ni huko kutokusikia, hebu nisaidie mtani.
Nilimshauri mtani wangu kuwa ni kweli tuendapo hakuna cha ukabila, hakuna cha ukoo upi ni bora na hakuna cha kuchambua undani wa nani ni nani kwasababu dunia sasa ni kijiji kimoja, lakini bado upo utaalamu wa kisayansi kuwa kabla hatujaamua kuwa wapenzi wa undani ni vyema tukaangalia afya zetu, na kama tuna uwezo basi kwanini tusiende mbali zaidi ya kuangalia vitu kama damu kama zinaendana. Sio lazima sana lakini ukiona umeumwa na nyoka lazima utashituka kila ukiguswa na unyasi. Basi ni heri ukatahdhari kabla ya hatari, pima vyote mjue afya zenu. Nilimuacha mtani akitafakari, nahisi huenda akarejea kwa wazee wake na hali ilivyo atarejea na binti wa kijijini kwao!
From miram3