Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Showing posts with label Jamii na mahusiano-Wazee. Show all posts
Showing posts with label Jamii na mahusiano-Wazee. Show all posts

Friday, December 30, 2016

KISA CHA BINTI YATIMA-4


 Baba alifariki akiwa kawaacha mama na bibi hawana kitu, ni kama vile alikufa baada ya kuhakikisha kile alichowahi kukichuma kwa mikono yake, kiwe hakipo tena duniani,…hata umaarufu wake ulishapotea, ilibakia historia ya kufaninishwa na mabaya yake tu.

Na ndio maana hata baba alipofariki, mazishi yake..licha ya kuwa aliwahi kuwa kiongozi mwenye nyadhifa, yalikuwa ni ya kawaida tu, walihudhuria watu wachache…hakuna viongozi wanaomfahamu waliwahi kufika….

Sasa maajabu ya walimwengu, yalitokea siku ya kutangaza mirathi,….

Tuendelee na kisa chetu…

*********

 Wakati baba anaumwa, watu hawakuonekana, lakini cha ajabu baba alipozikwa, ikawa na siku ya kutangaza mirathi, watu walipotokea huamini, kumbe baba alikuwa na watoto wa nje, hawakujulikana, walijulikana siku hiyo, na wao wanataka mirathi!

Watu wakaanza kupigana…maana walitarajia baba, kaacha mali nyingi, wanandugu wakaanza kupigana wenyewe kwa wenyewe, ….baadaye wakamgeukia mama, na kuanza kumsakama kuwa eti kapeleka mali kwao, au kauza..yaani ikawa ni fujo mtindo mmoja..mama atasema nini, yeye analia tu!

Kwa bahati kulikuwa na baadhi ya maeneo yalibakia, viwanja na mashamba, hivyo ikabidi wanandugu waanze  kunyang’anyana, kila mmoja akidai apate sehemu, hapo hawakujali kuwa kuna mjane, au watoto hao wa nje…hawakuli kuwa mama mjane ana mtoto mchanga,…wakati huo mimi ni mtoto mchanga,, hayo alikuwa akinisimulia bibi ilivyokuwa,…bibi anasema mimi hata mwaka bado.

Basi wao bila hata kujali hayo wakaanza kugawana mali mashamba yote wakachukua, hata hicho kibanda, walichokuwa wakiishi bibi na mama walitaka kukichukua, lakini mzee wao mmoja akaingilia kati na kukataza, wao walisema wanawapa muda mama na bibi watafute sehemu, siku yoyote watakuja kuwafukuza….na waliokuwa wakiongoza hayo yote ni wanaume….usione ni kwanini nasema nawachukia…

Mama aliambiwa wazi wazi kuwa hana chake…maana yeye ndiye kamuua mumewe…akishirikiana na bibi,…shutuma zikaanzia hapo…maneno yakakuzwa, na mama akaanza kunyoshewa kidole,…, ilibidi hilo nalo wazee wengine na wakuu wa dini, waliingilie kati maana ilishafikia wakati mgumu, na mama na bibi wakabakia hapo kwenye kibanda wakiishi kwa mashaka, na..unafikiri kibanda chenyewe ni kibanda hasa..we acha tu. Baba alikuwa kauza nyumba zote nzuri.

Siku moja mama akiwa shambani , ..walikuwa na sehemu nyingine ya shamba, ilikuwa sio ya familia, mama alipewa tu na jamaa zake, wanandugu wakawa wakimfuatilia mama,…na siku hiyo walipogundua mama yupo peke yake shambani,  wanandugu wa mume wakamfuata huko huko shambani,..wakaanzisha fujo,, waanza kumpiga mama, walimpiga wee, mpaka hamu yao ikaisha, na mama akapoteza fahamu.

Bibi yeye siku hiyo alibakia nyumbani, alikuwa hajisikii vyema, ikafika jioni hamuoni mama akirudi, ikabidi aanze kufuatilia, ilishafika usiku sasa, bibi anaumwa, lakini mwanae haonekani atafanya nini, mimi kanibeba mgongoni,….akaanza kazi ya kumtafuta mama, akaelekea huko shambani,…na alipofika hakumuona mama, kumbe walimtupa kwenye bonde.

Wakati bibi kakata tamaa, mara akasikia mbwa akibweka,…ndio akafuatilia, na hapo akamkuta mama kalala, hajitambui, akapiga ukelele, watu wasamaria mwema wakafika,…ilikuwa ni bahati tu….vinginevyo mama angeliwa na fisi, kwani walishaanza kumsogelea.

Walimbeba hadi nyumbani akiwa hajitambui, bibi akawa anaomba watu wamsaidie wamfikishe hospitalini. Watu, walishajengewa fitina, hakuna aliyekubali, waondoka zao , bibi afanye nini, mgongoni ana mtoto, mwanae anaumwa, kumbeba hawezi, akabakia kulia.

Kwasabbabu ilikuwa usiku tena, bibi akatafuta majani ya miti shamba anayoyafahamu akamkanda kanda mwane, hadi asubuhi, na asubuhi na mapema, bibi akaenda kwa mjumbe, ili apate msaada, na hapo akapata msaada mama akapelekwa hospitalini. Huko akapimwa akaonekana kavunjika mbavu.

Haya matibabu yanahitajia pesa, bibi hana kitu...bibi hana pesa..., ikawa dana dana, mara inahitajika damu, na ni nani wa kutoa damu....Bibi akawa anatembea huku na kule kuomba, ..ni nani atamsikiliza, mama akawa anateseka tu, hakuna cha maana kinachofanyika,…

Siku zikawa zinakwenda mama  hali yake ikazidi kuwa mbaya, bibi anapita mitaani akiomba, akilia kama mtoto, na alikwua radhi hata kuuza hicho kibanda, ni nani atakinunua,,…basi tena, hapo apo hospitali, wakamtibia walivyoweza, lakini hali ya mama ikazidi kuwa mbaya, akawa sasa hata kuinuka kitandani hawazi…

Baadaye sana, hapo hospitalini wakashauri mama apelekwe hospiali kubwa zaidi..ikawa haina jinsi , na wao wenyewe walikuwa na gari la bosi wao, siku hiyo hiyo alikuwa akienda huko mjini, ndio wakamchukua na mama...sasa, huko ndio wakagundua makubwa,  kumbe mama pamoja na matatizo hayo pia alikuwa kaathirika…

‘Unaona..yote ni haya ni sababu ya nani…..ni baba, kumbe baba alimuachia mama ugonjwa huo...baba hakuwahi kusema,… na ilipogundulikana kuwa mama ameathirika, kibao kikageuzwa kuwa mama ndiye alimuambukiza baba,….’ akatikisa kichwa.

‘Nyie wanaume nyie,….’akasema msimuliaji.

‘Watu walisahau kabisa tabia aliyokuwa nayo baba…kuwa baba alikuwa hakimpiti, aliwabadilisha wanawake kama nguo, …na kumbe alikuwa keshapima, akajijua kuwa anao! Lakini hakuwahi kumwambia mtu, ilikuwa ni siri yake...

Sasa mama alipopimwa na kugundulikana kuwa kaathirika, mzigo wote anatupiwa yeye, sasa yeye ndiye anasingiziwa kuwa ndiye alimuambukiza baba..na haikuishia hapo watu wakaendelea na maneno yao ya fitina kuwa wao ndio walimloga baba, wakishirikiana na bibi....yote hayo ya ugonjwa ni njia tu…

'Huo ugonjwa ni visingizio tu...' wakawa wanasema.

Basi ikawa na shutuma nzito, fitina, uzushi...ukasambazwa hapo kijiji, mpaka watu wakaanza kuamini hivyo, na ikafikia hatua mama na bibi wakatengwa, hakuna mtu anayekuja kuwaona, na bibi akitoka kwenda sokoni, au dukani,  kununua kitu, wauzaji wengine wanakataa kumuuzia, inabidi waende mbali zaidi,…

Na hali ya mama ikawa inazidi kuwa mbaya sana, bibi anasema mama alikonda sana, wanasema alikuwa kama fito,..madonda yakawa yanamtokea mwilini,... akabadilika sura kabisa, na kila aliyefika akamuona kwa bahati mbaya, hawamuangalii mara mbili, muuguzaji wake ni bibi, nani kama mama, na walimwengu wanazidi kujenga fitina, wakisema,…

'Huyo anateseka kwasababu ya dhambi zake, si alimuua mumewe, ngoja na yeye aipate....'

Basi siku ya mama nayo ikafika, akafariki dunia…na siku hiyo anafariki bibi alikuwa kaenda kumtafutia dawa, ilikuwa dawa ya bei mbaya, bibi alitumia kila alivyoweza kuipata hiyo dawa, ndio anafika hospitalini, akiwa na hiyo dawa , anajua sasa mtoto wake atapona,...

Ile anafika kitandani anakuta kweupe...

'Binti yangu yupo wapi...?' akauliza

Ilibidi madocta watumie hekima kumwambia....na palikuwa hapatishi, bibi hakuamini, akawa anataka kumuona mwanae, ndio akapelekwa chumba cha maiti, akaonyeshwa....

Bibi alilia mpaka akazimia,...japokuwa mama alikuwa kaisha sana, ..lakini bibi alikuwa na matumaini ipo siku mwanae atapona, hakuwa amekata tamaa, na alisema  kuwepo kwa binti yake japokuwa anaumwa, lakini ilikuwa ni faraja, ...sasa ndio huyo bintii yake keshaondoka, kamuachia mtoto mdogo, hapo nilishafikisha miaka miwili hivi...

Ni ni nani wa kuja kumliwaza bibi...bibi anasema mimi japokuwa nilikuwa mdogo, lakini ndiye nilikuwa nikimliwaza,...najua nini hapo,...wakati mwingine namuuliza bibi unalia, nini...hapo bibi ndio anazidi kulia,..

 Haya msiba umekwisha….bibi hana mbele wa nyuma..shamba lile walilokuwa wakilima, mazao kumbe walikuja wakachoma moto...kulikuwa na migomba na mihogo, yote ikateketezwa...

Haikuishia hapo watu wakaanza kutoa vitisho kuwa ni lazima na bibi aiage dunia...

'Huyo ni mwanga lazima aondoke, ni lazima amalizwe....'vijana wakawa wanapita mitaani wakisema

Sasa bibi akawa anaishi kwa mashaka, anaogopa hata kutoka nje, watu wanamnyoshea kidole,..mwanga mwanga.... Haijapita muda, kukasikika minong'ono kuwa watu wamejipanga usiku huo kuja hapo nyumbani kuchoma nyumba moto…wamuangamize na bibi,

'Mungu wangu sasa nitafanya nini na hiki kiumba cha watu...'bibi akawa anahangaika, na wazo likamjia, bora ahame hapo usiku huo na mapema, Bibi alisema;

'Isingelikuwa ni wewe mjukuu wangu, nilikuwa radhi nibakie hapo wanieu tu, kwani nina thamani gani tena, lakini niliogopa watakuja kutuangamiza wote wawili, na mimi nilipata kuja kukulea hadi sikuyangu ya mwisho....ndio maana usiku huo nikaamua kuhama hicho kijiji na kwenda kuishi kijiji cha mbali...lakini haikuwa kazi rahisi...

 Bibi anasema wakati tunatoka huo usiku,.. kumbe kuna vijana walikuwa wakipita pita, walituona, wakaenda kutoa taarifa kwa hicho kikundi kilichokuwa kimejipanga kuja kutuangamiza na usiku huo wakaitana kwa haraka...

NB: Ngoja tuishie hapo kwa leo, ilikuwa nawashitua kidogo, kuwa kisa hiki bado kipo.

WAZO LA LEO: Fitina ni mbaya sana… na fitina hutokana na ulimi, watu hujenga hoja zisizokuwa na ukweli, nia ni kuangamiza wenzao. Ole wao, wanautumia ulimi wao mbaya, maana siku hiyo ya mwisho, kiwili wili hicho kitakuwa ni shahidi.

Tumuombe mola atusaidie, awasaidie wazee wetu wanaoteseka huko vijijini, wengine wanateseka kwasababu ya fitina mbaya tu…wengine wanateseka kwasababu ya hali mbaya za kiuchumi, au maradhi nk…yote hii ni mitihani. Tunakuomba uwasaidie wazee wetu hao, maana uzee nao ni mateso, hasa ukiwa huna msaada wowote.
Pia tunakuomba uwajalia makazi mema peponi wazee wetu na wale wote waliotangulia mbele za haki . AMYNI.


NB: Ni kutokana na maombi ya wengi, inabidi tukiendeleze kisa hiki, sio kirefu sana, tuwe pamoja.

Ni mimi: emu-three

Monday, December 5, 2016

MISSION TO HELL-tangulizi

                 

                         MISSION TO HELL( MIKAKATI YA KUFA AU KUPONA)


UTANGULIZI:

Ni kisa cha mstaafu mmoja wa jeshi, aliyestaafu akiwa na cheo cha ukapteni, na wakawa wanamuita Kapteni, na ni kweli alikuwa captain wa ukweli, kiutendaji na umahiri wa kipaji lichojaliwa nacho hasa cha shabaha na upangaji wa mikakati. Aliwahi kupewa nishani maalumu ya ‘shabaha na mikakati’ ni nishani ya aina yake.

 Tatizo la mstafu huyu jeshi lilikuwa kwenye damu,  kila kitu chake kilikuwa ni jeshi kutembea, kuongea…, hakujua kabisa maisha mengine ya uraiani, kula kulala jeshini,.., aliwahi kusema damu na hata nyama yake imegeuka kuwa jeshi. Na kwa bahati nzuri kutokana na cheo chake enzi hizo aliwahi hata kupewa nyumba ya jeshini, nje kidogo ya eneo la jeshi lakini nyumba hiyo  ilikuwa ni mali ya jeshi…baadae alinyang’anywa!

Tatizo umri,..na ile hali ya kujiona yeye ni mwanajeshi , ilimfanya asiwe na wazo la kuwa ipo siku atarejea uraiani, atakuja kustaafu, atakuwa mzee…hili ni tatizo la wengi wetu, hasa tukiwa makazini….na kwa vile alijengwa hivyo mtu wa kupokea amri na kutekeleza, hakuwahi kufikiria namna nyingine ya maisha.

Muda umeisha, taratibu zimebadilika, utawala umebadilika, sheria inafuatwa hakuna nafasi tena ya kuwaacha wazee wakati vijana wapo..ikabidi mzee mzima apewe barua yake ya kustaafu, …hakuamini siku hiyo…, alijua ataongezewa angalau hata muda kidogo ili ajipange,  kutokana na ustadi wake, alijua atabakia kambini  awe angalau mwalimu,

Lakini hata akiongezewa muda, hata miaka miwili, atafanya nini tena keshaonekana mzee kwenye makaratasi,..ukumbuke, anachojua yeye ni kuitumia silaha, na fani za kijeshi, na zaidi ni kupanga mikakati ya kivita,…kupewa amri na kutekeleza, akilini hakujua kitu kingine cha maisha ya uraiani...

‘Kwa mujibu wa sheria, unahitajika kukabidhi kila kitu ikiwemo nyumba ya jeshi, na unapewa muda wa mwenzi mmoja, uwe umekamilisha taratibu zote zikiwemo hizo za makabidhiano, na taratibu nyingine za malipo yako ya kustaafu, yatakwenda kwa mujibu wa sheria za nchi…’ yalikuwa maelezo ambayo aliwahi kuyaona wakiandikiwa wenzake, hakujua kuwa ipo siku na yeye yatamkuta.

Siku alipopewa hiyo barua,….alitoka ofisini muda wa kazi akaenda kunywa, hajawahi kufanya hivyo kabla, akavunja sheria kwa mara ya kwanza,....hakuwa na tabia ya kunywa sana, kwani alijua kunywa sana kunakupotezea focus, malengo na msimamo..siku hiyo aliivunja hiyo ahadi,…

Alikunywa mpaka akachelewa kurudi nyumbani, na alipofika nyumbani akaanza kugombana na mkewe aliyempenda sana, hajawahi kufanya hivyo kabla.., na akawa tena kavunja ahadi yake ya kuwa mtawala bora, ya kuwa mtawala bora huanzia kwenye familia yake…na kesho yake akachelewa kuamuka, akavunja sheria nyingine ya kuwa ili uwe askari bora ujali muda…alifika ofisini kichwa kinauma, na hakuweza hata kufuatilia majukumu yake,…akavunja nyingine na nyingine..!

Siku kabla hajakabidhi nyumba, akaja rafiki yake mmoja  wa zamani..rafiki  yake huyu kwenye hiki kisa ndiye aliyemshawishi kutoroka nyumbani kwao na kuja kuishi dar kama chokoraa….kuna matukio mengi alikutana nayo hapa kutoka kuteswa, hadi kwenda uchokoraa,…na  wakiwa mitaani ndio wakaja kuunda kikundi cha sarakasi,…..wakiwa kwenye kikundi hicho ndio kiongozi mmoja wa jeshi akawaona, na kuwatafutia nafasi jeshini kwenye kikundi cha utamaduni .

  Historia ya mstaafu huyu akiwa mdogo, alikuwa na vipaji  vingi vya kuzaliwa navyo, japo hakusoma… kwa vile alikuwa yatima, hana baba wala mama, hakuweza kufuatilia vyema maswala ya shule, matokea ya mtihani yakaja akiwa amefeli na kwa elimu yetu ya msingi isiyojali vipaji akawa hana namna,…akawa mitaani, akaishi na baba mdogo, akaanza kuteswa na mama wa kambo….ndio akakimbia nyumbani.

Sasa walipokuwa huku mjini, ndio vipaji vyake viikaanza kuonekana kumbe huyu mtoto alikuwa na kipaji cha , sarakasi, na  mwili wake ulikuwa mwepesi wa kupenya sehemu isiyopenyeka,…kusoma kifaa na kukifungua akakirudishia kama kilivyo....pia alikuwa na akili ya kushika mambo kwa haraka,…hata darasani waliliona hilo, ila matokea ya mtihani akaonekana kafeli,..

Na alipofika jeshini akagundulikana kuwa pia ana kipaji cha kulenga shabaha…kwa ustadi huo ikawa wepesi kwake, kuajiriwa na kuwa askari wa jeshi.

Alipanda vyeo kwa shida,… private , koplo….maana hakuwa na elimu , zaidi ya kuishia darasa la saba, kwahiyo kilichomsaidia ni ule ustadi wake wa kukariri vitu kwa haraka,..aliifahamu silah kama kiganja chake cha mkono…aliweza kuifungua na kurejesha akiwa kafunga macho…. Na zaidi baadaye  aliwahi kwenda vitani, huko akaja kupanda cheo hadi akafikia ‘Uluteni’,..na aliporudi nchini, akapata mafunzo ya uongozi , na kuja kufikia cheo cha ‘ukapteni’..ndicho alichobakia nacho hadi kustaafu.

**********

‘Rafiki yangu ,utaona labda  huu sasa ndio mwisho wa maisha yako,..lakini kwa vile bado upo hai, unapumua, lazima akili ifanye kazi…., tatizo lakekwasasa  ni kuwa maisha ya kutegemea kukinga kutoka serikalini hilo halipo tena, ule umri wa kusubiria mwisho  wa mwezi  huo haupo tena, ule umri wa kupewa kila kitu, hadi nguo za jeshi  sasa huo haupo tena…sasa ni umri wa wewe kutumia akili yako, uishi au ufe…ukilala imekula kwako,..hebu niambie ...sasa utafanyaje,…’rafiki akamueleza.

‘Hata sijui nifanyeje,..nasubiria amri ya mungu…’akasema mstaaafu.

‘Hilo ndilo tatizo lako, kila kitu amri..mungu hapa anasubiria pia juhudi yako….mkono utoao ndio upewao.. jibidishe utapata, riziki ipo, lakini itafute kwanza  au sio…Mimi ningekuhitajia, kama unataka,..’akaambiwa na jamaa , rafiki yake, mwenzake alishawekeza, ana gari ana nyumba, miradi kadhaa..

‘Unakaribishwa uraioani,..ukumbuke haya ni maisha mengine tofauti,  kiukweli  nilikuwa na jambo moja, unajua mimi nina mbinu zangu za maisha kuna zakuonekana na nyingine hakuna anyezifahamu,..wananita kinyonga…..najua hutanielewa kutokana na jinsi ulivyolelewa huko jeshini…, wewe umekuwa mtu wa kufuata sheria za nchi..lakini sheria hizo zimekusaidia nini hadi hii leo, hebu niambie…sheria hizo ndio zinakutupa mitaani, huna mbele wa nyumba…’akaambiwa.

‘Sasa ulitaka mimi nifanye nini..muda  umefika, lazima sheria ichukue mkondo wake, siwezi kuwalaumu kwa hilo..najilaumu mwenyewe tu, kujisahau,..’akasema jamaa kwa shingo upande.

‘Hebu rafiki yangu niambie, nani na nani, si unawafahamu,…hao umewaona walivyowekeza, mlikuwa nao hapa jeshini,…wakaondoka mapema tu, kabla hata ya muda wa kustaafu, jiulize ni kwanini, chukua hatua kabla hujakongoloka..,..acha hao, hawa wengine,..ambao walikuwa wakitumia mgongo wako, kukupa amri, sasa hivi wana mehakalu, miradi..hawana shida, wengine wamekuwa wakuu wa mikoa, nani sijui….wewe umepata nini…na leo wanakutupa nje, bila hata kujali maisha yako ya baadae…’ akaambiwa

‘ Ni kweli inaniuma sana…’akasema kwa masikitiko.

‘Mimi sitaki kukuharibu, maana nyie ni waadilifu wa nchi..hongereni sana.., ni sawa, sote twatakiwa tuwe hivyo, lakini je uadilifu unajenga,..unaweza kuwa kama akina nanihii kweli…kweli, hebu chunguza hili,..mimi nilifuatilia nyendo za kila mmojawapo, nimegundua mengi sana..asikudanganye mtu,…ili ufikie kule, inabidi wakati mwingine uruke ngazi, uruke ukuta…na ufanye hata yale yasiyofaa….sasa akili kichwani mwako, kama wahitajia msaada wangu, nifuate, kama hutaki subiria ufe na kihoro… kama akina nanihii…’akaambiwa.

‘Lakini wewe ndiye rafiki yangu, nisaidie kwa hili…’akasema.

‘Mimi nina misheni..najua wa kuifanikisha ni wewe…inaitwa misheni ya mafanikio, lakini ni mawili kupata au kukosa,,….najua nikiwa na wewe tutafanikiwa tu, hatuwezi kukosa, ila ukikosa, ndio to hell, hamna jinsi, lazima ukutane na Izraili hilo sikufichi…..maana ukibakia duniani itakuwa ni tatizo,..ila nina uhakika misheni hiyo itafanikiwa,..sijawahi kufeli kabla..labda nianzie kwako….siwezi kukuambia kila kitu kwa sasa…’akaambiwa.

‘Mhh, sijakuelewa, una maana gani , unataka nifanye nini…?’ hapo akashituka.

`It’s a mission to hell…’unanisikia, mimi nilibahatika kusoma nilipoacha jeshi, lakini wewe kama mtaalamu wa mipango ya kivita nk…. utanielewa nina maana gani.  Ina maana kubwa ya kucheza karata yako ya mwisho ya maisha, ukifanikiwa, umeula…utayasahau haya yote, lakini ukifeli,…it’s a hell, man…you ar going to die,…sizani kama utapenda kwenda jela,…na hata huko sizani kama utaishi, huko wapo watu wangu huko.., vichaa….’  Akaambiwa.

‘Unajua rafiki yangu mimi sijakuelewa, mimi ninachotaka ni shughuli ya kuniingizia kipato, halali..sijali ni kazi gani, lakini unavyoongea yaonekana unataka niwe jambazi..au sio..mimi siwezi hivyo…’akasema.

‘Ipo siku utakuja kunielewa….huna namna wewe..ushakwisha,..tumia kipaji chako ulichojaliwa na mungu wako kwa mara ya mwisho, cheza na karata yako uliyobakia nayo, utakufa  utafaidi wapi hilo…'akaambiwa.

'Kipaji gani, na uzee huu....?' akauliza

'Wewe unajua kupanga mikakati, hicho hakizeeki, na sasa unaweza kupanga vyema kihekima,,..lakini sasa ni mkakati ya vipi, sio  ya kivita tena, sasa upo uraiani utaipanga wapi hiyo mikakati.., hebu niambie….'akaambiwa

'Sasa uniambie wewe....'akasema

'Sikiza ndugu yangu, kila kitu kina shemu mbili nyuma na mbele...sasa hivi upo uwanja mwingine wa maisha ya duniani,..uraiani,…mimi nayajua yote hayo....siwezi kukuambia kila kitu, kwa hivi sasa..muda utafika,.., njoo kwangu utajirike, kama hutaki, sikulazimishi…wewe ni mpiganaji kufa sio tatizo au sio..but kifo cha uraiani ni tofauti na jeshini, ...ni kigumu, utateseka kitandani weee, mpaka watu wakuchoke,….'akaambiwa.

‘Mmhh…siamini…’akasema

‘Utakuja kuamini siku yake ikifika, ...., bado hujasota , ipo siku utanitafuta…’akaambiwa, na rafiki yake huyo akaondoka

*************

 Mazungumzo hayo alikuja kuyakumbuka baada ya kusota sana..muda huo hana mbele wala nyumba, kaibiwa kila kitu, kaumwa sana,. Kutokana na kuumizwa na hao majambazi, walikuja kumuibia mafao yake,...wakamkata mkono..akaponea chupu chupu kuwa kilema, muda huo anayawaza hayo, yupo ndani kwenye kibanda chake cha mbavu za mbwa…anaumwa…hana hata senti moja, mstaafu wa jeshi, kapteni…!

‘Hiki ni kisa cha aina yake, kinaingia ndani ya Nyanja za watu,….sipendi, lakini utafanya nini, wote ni hawa ni abira wetu,…hiki kisa kinamtoa mstaafu mmoja ambaye sasa yupo kitandani anahesabu masiku, tunampa moyo kuwa ipo siku, asikate tamaa ilimradi anapumua,...

Swali ni , je lifikaje hapo alipo....

Ni kisa cha ujasiri, masikitiko, kukata tamaaa, ujambazi  na kila aina ya ushenzi wa hii dunia..….

‘It’s a mission to hell,…’.hebu emuthree, ufanye vitu vyako kidogo,  watu wamechoka kusubiria, ni kama kile cha ‘dunia yangu’ lakini kivingine kihalisia zaidi..,..

Tuweni pamoja, tuone namna nyingine ya maisha, ya wajasiri , wastaafu, mashujaa wetu wazee wetu wastaafu, lakini wamesahaulika masikini…ni kwanini lakini, …na madhara yake ni yapi…mwenye kovu usione kapoa..tuweni makini na hawa watu, tuwasaidie, tusiwatupe…

Ni mikakati mingine ya  ‘mission to hell..’..

WAZO LA LEO: Katika kustaafu kuna kitu kinaitwa kiunua mgongo, bima za maisha na kadhalika, ..bima hizi zinawekezwa kwenye miradi mbali mbali, kutokana na michango ya watu. Nasikia eti kuna fadia inakuja kurejeshwa kwenye michango hiyo, na nyingine hawarejeshewi, eti kutokana na jinsi ulivyoijaza hiyo fomu ya makubaliano, japokuwa michango hiyo inatumika kuzalishia, ni jasho la mtu hilo..

Sasa tuchukulie huyu mtu anachanga elifu kumi kwa mwezi, kuanzia kaajiriwa, enzi anachanga hiyo hela, inaweza kununua kitu, ..na wakati anafikia kustafu  miaka labda thelathini mbeleni, pesa hiyo haiwezi kununua hata shati….thamani yetu ya pesa hubadilika haraka sana…, lakini kwa wakati huo imeweza kuwekezwa kwenye miradi yenye maendeleo, ni jasho la mtu hilo..
Pesa hizo hizo zinakopwa na wakubwa, uaambiwa ukifa zitasaidia maziko yako, hivi ulikopa ili uje uzikwe nazo…sielewi hapo..…

Hivi hakuna namna nyingine ya kuwafikiria hawa wastaafu. Basi hizoo pesa zao zihesabike kama share..mtaji,..ili wakistaafu waweze kuwa wawekezaji ndani ya hivyo vitega uchumi..vinginevyo, mimi naona kama tunawadhulumu watu kwa michango yao,..ni mawazo tu, ijui wengine mnasemaje… !
Ni mimi: emu-three

Friday, September 9, 2016

KISA CHA BINTI YATIMA-`KWANINI MIMI...'- 2


‘Mimi sipendagi kusimulia maisha yangu maana kila nikianza kusimulia ninaishia kulia tu, najikumbusha machungu mengi yaliyonisibu, maisha yangu yamekuwa ni kidonda kisichopona ambacho kila siku kinatoneshwa na watu…..’akasema huyu bint

Kisa kilianzia pale nilipomkuta binti mmoja akiuza mihogo, na mgongoni kabeba mtoto mdogo, na mtoto huyo akawa analia sana,..hali ya yule mtoto akiwa kabebwa mgongoni ilisikitisha, nguo alizovyaa, ...na hali ilikuwa nayo, na hali ya hewaa ilikuwa ni ya ubaridi..nikashikwa na huruma , nikamsogelea huyo binti, kujua zaidi, nia hasa ilikuwa kumshauri amuonee huruma huyo mtoto..lakini majibu niliyokutana nayo, yalinifanya niingiwe na hamasa zaidi ya kumfahamu huyo binti..

Wakati nikiwa kwenye hamasa hiyo mara linazuka jingine kubwa.....

Hiki ni kisa cha binti yatima, hebu tuenddee nacho...


***************  2***********



‘Sasa utasaidiwaje, maana shida ni kila mtu anazo, na hakuna anayewez
a kusema mimi nimejitosheleza, nahitaji mtu wa kumsaidia, kila mtu hata tajiri anaona maisha kwa ke ni magumu, hajatosheka…sasa ili watu waweze kuvitika na matatizo yako ni wewe mwenye shida ujieleze…’nikasama na yeye akawa kainamisha kichwa chini akilia.

‘Haya…, ndio maisha yetu yalivyo, …, huruma haipo karibu kwenye nafsi zetu, ni mpaka ifukuliwe…unaonaeeh,. Na mwenye kukuhurumia zaidi ni yule aliyewahi kupatwa na shida, na shida zipo kwetu sisi watu wa chini,….sasa,… ukiongea watu wakakusikia wakaona shida zako wenye huruma za karibu wanaweza kukusaidia…au sio, masikini tunasaidia wenyewe kwa wenyewe…’nikasema.

‘Hakuna mwenye huruma dunia hii…nimeteseka sana, watu wananiona hivi hivi,….wanajua kabisa mimi sina baba wala mama, mimi ni yatima, au yatima anatakiwa aweje,….mimi ni yatima aliyepitiliza, sina baba wala mama, wala mjomba aau shaangazi, dunia imenitekeleza….’akasema

‘Katika maisha kama hayo ukiwa mdogo wa mwaka, ..utakuwaje,…ufe, au…..sasa aliyejitolea kunisaidia ndio huyo amefariki,….wangapi waliniona na zaidi ya msaada wao ulikuwa ni masimango na kunyanyapaliwa na hata kuzaliliswa…Namshukuru sana bibi yangu, bila yeye, labda ningelishakufa zamani… oh, na ndio huyo ameshafariki, na hata bila ya watu kumuelewa…binadamu, jamani binadam..’akasema

‘Mhh…pole sana…’

‘Na sasa ndio huyo amefariki bibi yangu masikini, nitakuwa mgeni wa nani…sina ndugu sina jamaa…na na.., kinachoniuma ni kuwa amefariki hata sijapata muda wa kulipa fadhila zake, alinilea nikiwa mdogo kwa shida…., akanitibu nikiumwa,..akiwa hana mbele wala nyuma,.. akataabika kwa ajili yangu, na…za zaidi nikamuongezea  ugumu wa maisha kwasababu ya tamaa zangu za kimwili….mungu wangu kwanini, kwanini…..’akawa analia.

‘Pole sana, yote maisha….’nikisema

‘Yote maisha ehe..mnasema tu….’akainua uso uliojaa chuki.

‘Maisha…hahaha, maisha…,  mengine yanauma….yanauma ukizingatiwa kuwa mengi ya madhila hayo waliosababisha ni wanadamu wenzetu…na ni ndugu kabisa, unajua ndugu...damu moja kabisa, tena wanaume, ….’akaninyoshea kidole, huku akisema

‘Wanaume kama wewe…., eti wanajita wanaume, hahaha, kama ni wanaume kweli ni kwanini wasihangaike kivyao, kwanini kama ni wanaume mbona wanadhulumu,..nawachukia sana wanaume... unajua kuchukia,…masikini bibi yangu…’akawa analia.

‘Kwani bibi yako kafariki lini…?’ nikamuuliza baada ya kupita kitambo kidogo.

‘Ndio nimepewa taarifa leo nikiwa nahangaika kuuza mihogo…lakini sijui kama kazikwa au la..maana hakuna mawasiliano huko kijijini,na huenda wamemtelekeza kwenye kibanda chake, baada ya kumfukuza kwenye nyumba yake ya urithi……na ndugu niliotegemea waniambie nini kinachoendelea ndio hao hao  aaah, bibi yangu masikini….’akawa analia.

‘Pole sana….’nikasema

‘Oh…bibi yangu masikini, hivi mzee kama yule kawakosea nini jamani, nyie walimwengu mna nini jamani, bibi, kizee, hakina nguvu kabisa, masikini , hohe hahe…wana..wana…ole wao, nasema ole wao..…nilijua tu... nilijua mwisho wa siku watamuua tu…’akasema

‘Ina maana wamemuua…?’ nikauliza

‘Kifo chake kitakuwa kimesababishwa na vipigo na mfadhaiko alioupata…sijui kwanini watu hawana huruma, hivi kama wana miguvu kwanini wasiende kupigana wakapata pesa, eti…yaani wanakwenda kumpiga kizee wa watu,…ni kwanini lakini…’akasema.

‘Kipigo…!, mfadhaiko..!…hebu anza hatua kwa hatua, kwanini bibi yako alipata kipigo..?’ nikamuuliza.

‘Eti wanasema bibi ni mchawi..’akasema na watu waliokuwa wasikiliza wakaguna,

‘Ndio wanavyosema na hilo lilimuumiza sana bibi…hakujua hata ajitetee vipi,akawa analia tu, akimuomba mungu amsaidia, hakuwa na jamaa wakumsaidia, ikabakia kila siku akilia, akimuomba mungu siku ifike aondoke hapa duniani, kuliko kupata adha hiyo…lakini aliomba kwanza anilee nifikie hatia fulani…..’akatulia

                         ***********

‘Mchawi,…..?’ watu wakaguna na kuuliza

‘Lakini wazee wengine vigagula….,. Yawezekana bibi yako kweli alikuwa mchawi kweli….’watu wakazidi kuongea..

‘Ndio zenu hizo,…..mna uhakika gani na hilo…kama na nyie sio wachawi…wanafiki wakubwa nyie…hakuna aliyemfahamu bibi, hakuna..zaidi ya uzushi huo….’akasema akiwaangalia watu kwa hasira na hapo kukazuka zogo, kila mtu akiongea lake

Kulizuka mabishano ya watu kila mmoja akisema lake, wengine walifikia kusema huenda kweli huyo bibi alikuwa ni mchawi, lakini huyo binti hakujua tu, au hata huyo bintu anajua lakini anamtetea tu bibi yake…..wengine wakasema ni imani haba tu….yaani kila mtu akawa anasema lake, …nilitaka hayo mabishano yaishe ili niweze kumsikiliza huyo binti…kwani atakeyeweza kuelezea ukweli wote ni huyo binti!

‘Hebu nikuulize kwanini walisema bibi yako ni mchawi , alikuwaje mpaka wakamuhisi hivyo, maana wewe ulikuwa unaishi naye au sio, kwahiyo unamfahamu alivyokuwa, unajua lolote kuhusu bibi yako…?’ nikauliza.

‘Hata sijui hayo ya bibi mchawi yalianzaje,…’akasema.

‘Ukituelezea maisha ya bibi yako, itakuwa rahisi kwetu kuyafahamu hayo….’nikasema
‘Mimi bibi yangu ndiye aliyenilea, baada ya wazazi wangu kufariki,..hata siwajui wazazi wangu wanafananaje,…maana hata picha hakuna,…wazazi wangu walifariki nikiwa mdogo sana, bibi anasema nilikuwa na mwaka mmoja tu, unaona…sasa kama angelikuwa ni mchawi angenichukua mimi, angenilea mimi,…’akaanza kuelezea.

‘Si ili urithi uchawi wake…’akaropoka mtu mmoja.

‘Hujui unachokisema, kwasababu humfahamu bibi yangu…’akasema

‘Wazazi wako walikufa wote wawili kwa pamoja?’ nikauliza, nikitaka kudodosa ili kujua ukweli halisi wa binti huyo, kuliko kuchukulia juu, juu tu..

‘Alianza kufariki baba…..nilivyoambiwa na bibi, ..baba aliumwa sana, lakini chanzo cha ugonjwa wake ni kuwa alikuwa hajatulia, mlevi, mnzizi….ndio maana nasema siwapendi wanaume…kwasababu kutokana na tabia yake hiyo ya ulevi na umalaya, ndio alimuambukiza mama yangu, mama alikuwa mpole sana mcha mungu, lakini kutokana na baba, aah, nyie wanaume….’akasema akitikisa kichwa.

‘Oh…unasema baba yako ndiye alimuambukiza mama yako, una uhakika gani na hilo…?’akauliza jamaa mmoja.

‘Ndio nina uhakika..japokuwa sikuwepo, sikuwahi kuyaona maisha ya baba kwa macho yangu, lakini mengi niliyasikia kuhusu maisha yake, na sio mtu mmoja tu, wengi,….na hata waliowahi kutembea naye wamathibitisha hayo…wengi ni marehemu, waliopo hai walielezea kwenye…haya mambo ya ukimwi na matumaini…’akasema

‘Kwahiyo maisha ya baba yako unayafahamu kwa kupitia mazungumzo ya watu au sio…., je unaweza kutusimulia kidogo jinsi ulivyosikia kwa watu…, kwa faida ya watu wengine ili wajifunze, ..kama hutojali lakini…’nikasema

‘Siogopi kuyasimulia, …maana maisha yake yamekuwa ni funzo pale kijijini, kila mmoja amekuwa akitolea mfano kwake, hasa mzazi anapomuona mtoto wake anapotea, anakuwa mlevi, Malaya..ana uchu wa madaraka, hamtunzi mkewe….watu wamekuwa wakitoa mifano kwa kupitia maisha ya baba..kwahiyo hata nisipoongea mimi leo…, yameshaongelewa sana…mungu amsamehe tu baba yangu…’akasema

‘Kwani baba yako alikuwaje, maisha yake yalikuwaje ulivyosikia kwa watu...?’ nikamuuliza

NB: Haya haya…huyu baba mtu alikuwaje, kwani alikuwa kiongozi, mzazi…na mwenye uwezo kifedha, je hayo yalikuwaje mtihani kwake, na kwa jamii…, ni sehemu muhimu yenye mafunzo itafuata baadaye

WAZO LA LEO: Wazazi tunatakiwa tuwe kiyoo cha familia zetu, matendo yetu, tabia zetu huwa zinaaksi maisha ya watoto wetu, kwahiyo tuweni makini sana. Sisi wazazi ndio chanzo cha misingi mema ya watoto wetu,..huwezi ukamfunza mtoto adabu wakati wewe mwenyewe ni mtomvu wa nidhamu, unapigana na mkeo, mnazozana mbele ya watoto…hutunzi vyema familia yako..haya na mengine mengi huathiri sana maisha ya baadaye ya mtoto wetu. Na kama unatenda madhambi kwa watoto wa wenzako ujue na wewe madhambi hayo yatahamia kwa watoto wako. Uone jinsi gani mzazi ulivyo na dhamana kwa familia yako.

Tumuombe mungu tuwe wazazi wema, tutimize wajibu wetu, hata kama maisha ni magumu lakini hivyo hivyo tu, kwa matendo yetu mema, tabia njema… tunaweza kuwafanya watoto wetu wakawa nguzo imara ya vizazi vyetu.
Ni mimi: emu-three

Friday, November 27, 2015

RADHI YA WAZAZI-57





Kwanini nyie mumenifanyia hivi, lini mlisikia mtoto anamnyanyulia mzazi  mkono wake, haijawahi kutokea, mimi na umri wangu huu, kama ikitokea kuzozana mzazi na mwanae , mtoto akawa mkaidi, akamkosea mzazi wake, wazee wenzangu mnafahamu nini kinafanyika,...eti  wazee wenzangu,....?’ akauliza na wazee wakakaa kimia

‘Huu si mkosi jamani, ..... halafu eti mimi ndio nikae na huyo muhuni meza moja tuongee. Eti mimi mzazi ndio,  nijishushe, haitatokea hilo kwangu kamwe....’akasema mshitkiwa akitikisa kichwa

Wale wazee nao wakawa wanatikisa kichwa na mmoja akataka kuongea lakini wakili mtetezi akawamuwahi na kusema;

‘Kwa hali ilivyo, na kesi ilivyo inabidi , kwani sisi ndio tunaomba....kama nilivyosema awali, wenye kuomba inabidi wao wanyenyekee,  na ni muhimu mzee ukajua kuwa hili halitaingilia mila na desturi zenu, baada ya kukamilika hili, basi mtafaya taratibu zenu, au sio wakili mtetezi, au sio Profesa..’akasema msaidizi wa wakili na kumuangalia wakili mtetezi ambaye alikubali kwa kichwa, halafu akamuangalia profesa na Profesa akageuka kumuangalia kaka yake...

Mshitakiwa akiwa anatikisa kichwa kama kukataa akasema;

‘Na mbaya zaidi, mdogo wangu mwenyewe ananiendea kinyume, anafanya mambo anavyotaka yeye mwenyewe, ...kilichompata huko Ulaya keshasahau, hajui kuwa yote haya yalitokea kwa vile alidharau mila na desturi zetu za malezi, na dini zinasisitiza sana hayo, malezi bora kwa vijana wetu, na mtoto hata siku moja hawezi kuwa juu ya mzazi....’akatulia

‘Ni sawa kabisa....’akasema wakili

‘Mdogo wangu kwa vile kaishi na wazugu, basi anajifanya kalisahau hilo, na kutokana na kikiuka hayo, amejikuta kwenye mitihani na mateso mengi, hadi katimuliwa huko, wakijua keshakufa....mimi nashangaa, kuwa bado tena anarudia makosa yale yale,...hivi unataka yakupate yapi ndio ukiri kuwa umekosea....’akasema akimuangalia ndugu yake

Wote wakageuka  kumuangalia Profesa ambaye alionekana kutaka kumzuia kaka yake asiendelee kuongea lakini kaka yake akaendelea kuongea kwa kusema;

‘Sasa huyu....unataka na mimi yanipate .....hahaaah, sio mimi, kamwe mimi sitageuka jiwe, acha niende jela, kama ikifanya hivyo ni makosa, na nasema tena mnisikie , acha nihukumiwe, lakini sitakwenda kinyume na mila na desturi zetu za jinsi ya kulea na taratibu za kifamilia,...’akasema

‘Bro....’Profesa akataka kumkatisha kaka yake,lakini kaka yake akamuashiria kuwa anyamaze

‘Acha niongee,...nikuembie hili mlisikia wote, kama mimi kwa kufanya hivyo itatoklea  ikahukumiwa kwenda jela, kwasababu ya kutimiza wajibu wangu kama mzazi, na ikawa ni kutokana na huyo mtoto,.....nyie mtakuwa mashahidi, yatakayomkuta  huyo mtoto, ....sipenndi na wala sio mimi,....’akawageukia wazee na kusema

‘Wazee mnayafahamu hayo, lakini sijui, ...labda iwe kweli,yeye hakutokana na damu yangu, labda kama anavyodai yeye sio kweli mtoto wa kutokana na mimi....’akasema na kufanya kama ananawa mikono....

Tuendelee na kisa chetu

            *****************

‘Lakini mzee mwenzetu  hayo tutakuja kuyamaliza kinyumbani,tutahitajika kuyasafisha na kijana aelekezwe la kufanya ...hapa kama unavyoona, ni sheria inahitajika, na wao wamejaribu kuliona hilo, na wakajua kama hali itakwenda kisheria zaidi wewe utakwenda jela, je itasaidia..’akasema mzee

‘Kwahiyo, hebu kwanza, tuyasikilize hayo ya kisheria yanavyotaka kwanza, na tukirudi nyumbani, tutaendelea na taratibu zetu kabla hatujachelewa,,....muhimu huyo kijana apate mtu amuelekeze, lakini kwa hivi sasa tukubaliane na hili,..’akasema huyo mzee mwingine.

‘Hahaha wazee wenzangu, kwanini mnifanyie hivyo, mnasema tutayaongea....kweli mnasema hivyo, tuache mimi nivuliwe nguo,halafu ....ndio tuje tukae tuyaongee,  wakati mimi nimesha-aibika, nimeshakiuka miiko yetu,...hamjui wanachotaka mimi nifanye,...hebu niambieni wazee wenzangu tunamzihaki nani hapo...?’ akawa kama anauliza

Wazee wakawa kimia, na yeye akaendelea kuongea

‘Huu wazee wenzangu ni utoto, ....natamka hivi kwani mnafahamu hivyo, huo ni utoto, eti tufanye hivi,tukimalize tujifaye yale tuliyofanya sio, tulikosea wakati huo tunafahamu tulikosea haya tunayotaka kuyafanya, hivi kweli inakuja akilini,..?’ akawaangalia wazee wenzake, ambao walikuwa kimia wameagalia chini.

‘Najua hili ni langu, najua .....huu ni mkosi, umeingia kwenye familia yangu, na chanzo ni huyu mdogo wangu, kwa kujifanya yeye ni msomi, kaishi na wazungu..kaiga mambo yao, na nakuambia, ....wewe, toka awali nililiona hili, sasa sio mimi. Ni wewe ...utabeba huo mzigo mwenyewe....’akasema akimuangalia mdogo huku akimnyoshea kidole.

Mdogo mtu akawa kainamisha kichwa chini, akionekana mwingi wa mawazo, kabla hajajitetea, wakili mtetezi akasema;

‘Mzee, mimi nakuelewa sana, sio kwamba siyaelewi hayo,....mimi ni mzaliwa wa huko na pamoja na kusomea sheria, lakini pia nimejitahidi kujifunza mila na desturi zetu, na mila za ulezi ni kila mahali hata huko ulaya zipo, sema wenzetu wana yao ...sipendi kuyaongelea zaidi,...na hata hakimu anaelewa hayoo ndio maana akatumia hekima badala ya kusimamia kwenye sheria tu...akaona hekima itumike......’akasema wakili mtetezi

‘Kama ni hivyo, huoni.....’akataka kusema mshitakiwa na wakili mtetezi akamkatisha kwa kusema;

‘Huenda utasema nisingeliongea hilo mahakamani, sasa angalia kwa upande mwingine kama nisigelifanya hivyo, ingetokea nini,...’

‘Ungelifungwa,....’akadakia msaidizi wake, na wakili mtetezi akatikisa kichwa kukubali

‘Ni kweli hukumu ingeweza kuwa mbaya kihivyo, na baadaye ungelifahamu kuwa aliyekufunga ni mwanao, wakati huo hali imeshafikia huko, haingeliwezekana kabisa kuwa na suluhu, haya niliyawazia na mwisho wake nikaona ni heri nifanye hicho nilichofanya,...’akasema wakili akimuangalia mshitakiwa

‘Hapana, hamkunitendea yanayostahiki,.....’akasema mashitakiwa na Profesa akadakia kwa kusema

‘Bro, mimi naona kwanza tumsikilize wakili, ....na mimi sioni kwamba vibaya, hajafaya vibaya kabisa ni wewe tu hutaki kuelewa, kafaya jambo ambalo limezuia ubaya zaidi ...sasa tusipoze muda, kwa maswala hayo ya kimila na desturi, hayo yanaweza kusubiria, lakini kuna hili swala la sheria, wakili kapewa kazi na hakimu, tusipoteze muda,...’akasema Profesa

‘We bwana mdaogo unazarau tu...nakuelewa sana....’akasema kaka mtu

‘Ama hilo la kunilaumu mimi, nafahamu sana kosa langu,najua kama ingelitokea vinginevyo kijana akarudi vingine akawakubali, na hali nzuri, msingelisema haya, lakini hayo tuyaache hayo ..’akasema Profesa

‘Usijitetee makosa, huwezi kufuga nyoka wa sumu useme angesaidia baadaye, wakati keshaanza kuumiza watu..nyoka uliyemfuga huko sasa anatugeuka....ukaona ukae kimia, wengine nao wakione cha moto.....’akasema kaka mtu

‘Bro,...nina maana kubwa kwa mimi kukaa kimia kukuambia hili,  nitakuja kukuambia ni kwanini nilifanya hivyo, kwa hapa siwezi kukuambia, sipendi kulizungumza hili hapa, litaharibu kila kitu....’akasema Profesa

‘Unajua wewe bwana mdogo nakufahamu sana toka utotoni, wewe ni mbinafasi, inapofikia kwenye jambo la kuamua kwanza unaangalia ubinafsi wako, hujali wengine, hili ndilo limetufikisha hapa, na tabia yako umemuambukiza na huyo mtoto,hupendi kuambiwa ukweli, hupendi kuelekezwa, wataka kujiamulia utakavyo....’akasema

‘Bro....’akataka kujitetea

‘Sasa huyo nyoka,...natumia neno hilo, mnielewe, huyo mtoto, ni wako, na mimi kama ni kwenda kufungwa sawa, si na mimi natakiwa nikione cha moto,...lakini .....’akasema

‘Nani kakuambia utafungwa...’akasema wakili mtetezi

‘Unafahamu nyie hamnifahamu mimi vyema, ....haya yote mimi nilishayaona kwenye njozi, na kuna makubwa yanakuja,....kosa lilianzia mbali, sitaki kusema hapa, nikaoa, yakatokea haya, ya kutokea baadaye nikawa sina jinsi, sasa cha moto nakiona.....’akasema akiwa anatikisa kichwa, na wakili akawa anamuangalia huyo mzee kwa macho ya kutafakari.....

‘Lakini hayo yalishapita, nilishaosha mkono na kutubu dhambi zangu,...kumbe ..kumbe...kumbe...mambo bado, maana naishi na watu wasielewa, hawa watu hawa ndio wnaharibu jamii....’akasema akimnyoshea kidole profesa

‘Lakini hata hivyo mimi sitakubali, ..yanayokuja mimi sitakuwepo, wewe bwana mdogo utapambana nayo, ...si ndivyo ,mnavyotaka, utajiri au sio, haya utaupata, lakini hutapata raha....hilo nakuambia,.....’akatulia

‘Bro ....’akataka kukatisha lakini wakili akamtuliza, na mshitakiwa naye akanyamaza kimia

Kukapita ukimia kidogo kama vile kila mmoja aliyekuwepo hapo alikuwa akiliwazia hilo jambo na wakili mtetezi akaanza kuongea;

                                                  *************

‘Naona tusipoteze muda, ni muhimu nikawaelezea tukakamilisha hayo ninayotakiwa kuwaambia, utekelezaji wake, kama alivyopendekeza muheshimiwa hakimu , tukiyafanya hayo,tunaweza kumshawishi muheshimiwa hakimu...’akaanza kusema

‘Nafahamu sana mila na desturi zetu za malezi ndani ya jamii zetu, nafahamu sana mitihani ya ulezi hasa kizazi hiki cha sasa ambacho kunakumbana na mitihani mingi inayotakana na utanndawazi, ...’

‘Tunaweza kuwalaumu sana vijana wetu, lakini wakati ndio umetufikisha hapa, sio wao tu,...ni mabadiliko ya maisha duniani nzima kizuri kina changamoto zake,..utandawazi ni mnzuri, lakini changamoto zake ni nyingi...., na inapofikia kwenye ulezi, kwenye watoto wetu kila mwenye hekima litamgusa hili,....’akatulia

‘Usione mwenzako limetokea hili ukahisi wewe upo salama, labda wewe uwe una kijiji chako, una dunia yako, ambayo watoto wako wanaishi peke yao, na usiwe na aina yoyote ya mawasiliano, kitu ambacho hakiwezekani....hili ni letu sote  kwani mwenzako akinyolewa, na wewe tia maji, hili...

‘Mzee, hilo sio swala lako tu, wengi kila mmoja wetu hapa linamgusa kama sio kihivyo, ni kivile,....na kwingine ni kubaya zaidi kuliko hata hili lako, ni kwa vile tu halijawekwa hadharani....’akasema na kila mtu akawa anatikisa kichwa kukubali

‘Sasa ndugu zanguni, hili sasa limetokea tulione kama swala latu sisi wazazi..,ilitakiwa iwe hivyo, wazazi wote tungetakiwa tuwe kitu kimoja, likitokea jambo sio la kawaida, wazazi tukutane tuone tutalirekebisha vipi, kabla halijasambaa,  lakini sasa hivi ulezi ni kila mtu na watoto wake,....’akasema wakili

‘Siku hizi mtoto wa mwenzako akikosea, ukajaribu kumuadhibu, acha kumuadhibu, ile kumkemea tu, utazua ugomvi,...na ukiwa ndio mzee itazua balaa, mzee mwanga mzee mchawi,  na maneno ya kukatisha tamaa na hata kuvunja undugu au ujirani, utasikia wewe ulinisaidia kuzaa, ulinisaidia kulea wewe....hayo na mengine mengi, na matokea yake ndio haya....’akasema wakili

‘Sasa tusikimbilie kulaumu kama wapo wenye uoni wa mbali, basi tujaribu kulitatua lile linalowezekana, na hili letu liwe kama mfano, tusiadianeni, kabla hijafika mbali....’akasema wakili

‘Wazee wenzangu, nimeamua tusaidiane hili, na nimefaya hili kwa kujitolea, ni kwelii mimi kama ningetaka pesa , nisingelifuatilia hili jambo,hadi hatua hii,  ..lakini aliposimulia huyu rafiki yangu Profesa, nilihisi mwili mnzima ukinicheza, nikiwazia watoto wangu, nikiwazia watoto wa watoto wangu, huko tunapokweda ni kubaya,....’akasema wakili akiwaangalia wazee wale waliokuwepo

‘Huu ni mtihani, na ....hata kama sheria zitawekwa, adhabu zikatolewa, haitasaidia kitu, kwani chanzo kipo pale pale.....na kinazidi kuota mapembe, kiajitanua siku hadi siku, huko mbeleni yatazuka mabaya zaidi.....’akasema wakili

‘Sasa wazee , tulifikiria hili kama njia ya kuonyesha njia ili wegine wafuate, najua sio kazi rahisi, lakini sisi tutakuwa tumetimiza wajibu wetu, mimi nimeamua kutokuagalia masilahi, nimeamua kujitolea, ni kwanini, najua kujitolea siku hizi ni gharama, lakini najua ni faida mbele ya mungu....’akasema

‘Baada ya kusema haya, tusipoteze muda, najua mnahitajika kurudi kijijini, lakini nimeona ni bora tulifanye hili , tuanze utekelezaji mapema, ili mkirudi tena hapa mahakamani tukakuja kulimaliza hili kabisa,...’akasema

‘Sasa kuna mambo ya kufanya, naomba haya myasikilize kwa makini ili mimi niweze kulifanikisha hili, msiposhirikiana nami, itafika sehemu nitashindwa...’akasema

‘Hii ni kesi ya aina yake mtoto kumshitakia baba yake, na wakati huo wawili hawa hawafahamiani, ....’akasema

‘Haya sasa wamefahamiana iweje, na wamefahamiana wakati kesi inaendelea,...ila 
tuelewe tatizo sio kwa vile ni kesi ya baba na mtoto, hilo laweza kutokea, mtoto akamshitakia baba yake, na baba akamshitaki mtoto, na sheria ikafuata mkondo....’akasema wakili

‘Mimi nilimuelezea muheshimiwa hakimu hali halisi, kwa kadri alivyonielezea Profesa, na hakimu alishangaa sana kwanini hali hiyo ikawepo,  Profesa ilitakiwa uwepo kujibu maswali mengi , ya kwanini ilitokea hivyo,....mimi  nikatumia uzoefu wangu kumfahamishana hakimu, na ni kwanini tunaomba hii kesi iwe hivyo, ndipo hakimu akataka muda kulitafakari ombi letu...’akasema

‘Alitumia maneno hayo, apewe muda kulitafakari ombi letu, lakini akitia maagizo ya mambo yanayotakiwa sisi tufanye .....’akasema

‘Kwahiyo kuahirishwa huko ni kwa manufaa yetu, lakini kama tutafanya hayo aliyoagiza hakimu, ili yaweze kumshawishi hakimu, kuwa hili lilitokea kwa bahati mbaya , ....’akasema wakili

‘Tafadhali hapo kidogo.....’alikuwa mshitakiwa aliyetaka kuongea lakini Profesa akamzuia

‘Bro mengine tutaongea nyumbani najua unataka kuongea kitu gani.........’akasema na wakili akamuangalia mshitakiwa halafu Profesa, na baadaye akaendelea kuongea:

‘Sasa ni hivi, japokuwa hakimu kaahirisha hii kesi, lakini kesi yetu bado ni ngumu, kutokana na utata wake,...ni kesi ya jinai, na lengo letu ilikuwa kuirejesha hii kesi kuwa kesi ya madai, na.....zaidi tuliomba ikiwezekana ikaongelewe nje ya mahakama,....inakuwa ngumu sana kwa hakimu kuamua hivyo, lakini pamoja na sheria hekima nayo ni muhimu sana, nimefurahishwa sana na huyu hakimu...’akasema

‘Sasa kuna mambo muhimu sana tunahitajika kuyafanya ...’akasema na wote sasa wakatulia kumsikiliza wakili

‘Ili ombi letu liwe na uzito, inabidi sisi wenyewe kukaa kikao na waliotendewa hilo kosa tuwe na kitu cha maridhiano, na pande zote zikubaliane na hilo, hii ina maana waliotendewa hilo kosa, wakiri kuwa wameshasamehe na wapo tayari, kama wanahitaji fidia au itategemea na wao watakuja na hoja gani....’akasema wakili sasa akijaribu kumuangalia kila mtu kwa muda wake kuona kama hilo limeeleweka...na alipofika kwa mshitakiwa, ...

‘Tafadhali ngoja kwanza, ,,,..’akasema mshitakiwa

‘Bro tutaongea hayo yako tukifika nyumbanii,  subiria wakili aeleze kilichoongelewa na hakimu ili tukifika huko nyumbani tujue tunaanzia wapi, hii ni kwa manufaa ya hii kesi...’akaambiwa.

‘Mimi nataka niliweka hili wazi  mbele yenu, mkisema niache akaongea tu, wakati mimi sijakubaliana, itasaidia nini, ....mimi sijakubaliana na hilo ombi, kwasababu kwa mila na desturi zetu hicho hakipo....’akasema

‘Lakini hapa hatupo kimila, tupo kisheria...’akasema msaidizi wa wakili mtetezi

‘Sasa kama mpo kisheria, nasema hivi, mimi mzee Makunjazi, kamwe sitaweza kukaa na huyo muhuni, eti mimi mzazi nimuombe mtoto msamaha, na pia eti nimbembelezi kuwa mimi ni baba yake, nimuombe afute kesi,....yeye kama nani,...?’ akatulia

‘Eti  wazee wenzangu mbona hamnisaidii kwa hili, mnafahamu mila zilivyo, au kwa vile sio mtoto wenu, hahahaa basi sio mimi....kamwe....’akasema mshitakiwa

‘Bro, sikiliza kwanza, anachoongea wakili...tumsikilize wewe unang’ang’ania, hapa hatuongei maswala ya mila,tunaangalia sheria itatusaidiaje ili hii kesi iishe kwa amani, hapa hujashitakiwa na mila,...uelewe hilo,....’akasema Profesa

‘Haina haja ya kusikiliza zaidi basi, mimi nimeshaelewa, nia na lengo lenu ni kumvimbisha kichwa huyo mhuni, vijana wa namna hiyo ukiwapa nafasi wanazidi kuharibika, na kuona alichokifanya ni sahihi ...., ‘akasema kwa hasira

‘Kwa hivi sasa tutajifanya hivyo, ...’akasema msaidizi wa wakili

‘Kweli dunia imekwisha, mtoto anizalilishe mimi hivi, mtoto anipige, mtoto anivunje mbavu, kisa ni nini, halafu bado sisi tumbembeleze, hapana mimi sikubaliani nanyi kabisa...’akasema mshitakiwa

‘Lakini hayo ya kukufanyia hivyo, sio kosa lake, alikuwa hajui kuwa wewe ni baba yake,  mzee mwenzetu....’alikuwa mzee mmojawapo aliyesema

‘Kwahiyo kama mtu mzima sio baba yake afanye hivyo, ampige kama mwizi, bila kujua ni nini kilitokea kisa kafika nyumbani kwake akakosa kuelewana na mlinzi..hakutaka kujua kisa ni nini, mlinzi kaumia na kujigonga alipodondoka.....aaah, hata haina haja ya kuwaelezea zaidi...’akasema akitikisa kichwa

‘Hayo sasa tutayaongea nyumbani tusubirie, tunaomba  wakili uendelee kutoa maelezo yako...’akasema Profesa na kaka mtu akatulia akiwa kakaangalia pembeni kama vile hataki kusikiliza, na wakili akaendelea kuongea;

‘Sasa ndugu zanguni, hili nii ombi , tumeomba sisi, kwa muheshimiwa hakimu, na ombi letu lipo mikononi mwake, hakimu anataka kutumia busara zake,na kuacha vipengele vya kisheria,  fujo imefanyika, na ukikwaji wa sheria upo wazi, lakini kwa mustakabali wa kifamilia, muheshimiwa anaweza kufumba macho...’akasema wakili akiongea kwa sauti ya chini kama vile hataki watu wengine wasikie.

‘Japokuwa katika utetezi wangu, hakimu aliona kuwa kuna namna ya shahidi kuwa muongo, kutokana na jinsi nilivyombana, lakini bado haikuwa na tija,....mtu kaumizwa, na matendo hayo yametokea kwenye makazi ya mtu...hilo ni kosa....’akasema wakili kwa sauti ya chini

‘Hilo ni jambo moja lakini kuna hili jambo jingine kuwa tunahitajika tuwe na vielelezo vya kuthibitsha kuwa kweli huyo mtoto ni mtoto wako kweli,  mshitakiwa...’akasema

‘Vielelezo gani...?’ akauliza mshitakiwa

‘Vipimo vya kitaalamu kuwa kweli huyo ni mtoto wako..’akasema wakili

‘Mimi sina haja ya kuthibitisha hilo kama yeye kakana na kusema mbele ya mahakama kuwa mimi si baba yake, basi, kuna haja gani ya hilo, vipimo vya nini, nataka kuthibitisha nini, kumbembeleza kuwa mimi ni baba yake, hapana hili tuachane nalo.....’akasema

‘Sio kwamba ni hiari,....mimi nimeshalitamka hilo mahakamani na hakimu anahitaji ushahidi wa kitaalamu, ili kuweka  uzito wa madai yetu, ni taratibu na ni muhimu zifuatwe, na sisi ndio wenye shida, ..’akasema na kuwaangalia mshitakiwa na mdogo wake, na hakutaka kuwapa nafasi ya kuongea akasema;

‘Ujue sisi ndio tuliofanya kosa, na kosa ni kosa na mtendaji wa kosa hata akiwa nani  kamtendea nani sheria ipo pale pale, ukifanya kosa utahukumiwa tu,haijalishi kuwa wewe ni baba yake, hilo tulielewe kwanza ....lakini kutoka na hali ilivyo, hakimu kwa busara zake kaliona  hilo,kaamua kutumia busara zake ......’akasema

‘Kwahiyo ili tuwe na mshiko wa maombi yetu, inabidi wewe mshitakiwa na mtoto mkae kikao kilichoratibiwa, mbele ya wanasheria yawezekana ikawa mimi au yoyote mtakayemchagua, kulithibitisha hilo....’akasema wakili na kumuangalia mzee

‘Hahahaha, unajua wewe unaongea kirahisi sana, ...mimi ni mzazi, ndio natakiwa nimnyenyekee mtoto, si ndio maana yake, yaani, nikae na huyo mtoto muhuni asiye na adabu,  nianze kumbembeleza.... hivi nyinyi mnalionaje hili, au kwa vile haliwahusu saana, .....?’ akauliza mshitakiwa akimuangalia wakili na baadaye akawaangalia wazee wenzake.

‘Kukaa kikao ndivyo inatakiwa, lakini hilo la kumbembeleza,....hapana, yeye ataongea na muendesha mashitaka ataelekezwa la kufanya, akikubalia, sizani kama kuna maswala ya kubembelezana mzee, sizani kama atakuwa na ujeuri huo mbele ya mzazi wake....’akasema wakili

‘Pamoja na hilo kunahitajika vielelezo vya kulithibitisha hilo kitaalamu kuwa wewe kweli ni baba yake, ni utaratibu tu, kwa ajili ya kumbukumbu, na muhimu vielelezo hivyo viwepo ....’akasema

‘Una maana gani kuthibitisha....?’ akauliza

‘Ni hivi, wewe ni baba yake, kihalisia, lakini kimaandishi tutathibitisha vipi, ...kimaandishi tunahitajika kuwa na vielelezo, tunahitajika tupate vipimo vya kitaalamu, na siku hizi kuna vipimo ambavyo havina mashaka, ambavyo ukipimwa kweli inathibitisha kuwa wewe kweli ni baba yake halisi, vipimo hivyo vinaitwa DNA, ...’akasema

‘Hapo mzee kama ulibambikiwa itathibitika.....’akasema msaidizi wa wakili mtetezi akionyesha utani, ...

‘Kwa minajili hiyo mshitakiwa na mtoto tutahitajika twende hospitali za serikali, mtoe damu zenu, zipimwe, na majibu yake yataambatishwa kwenye maombi yetu...’akasema wakili

‘Lakini itakuwa na haja gani, hata kama vipimo hivyo vitathibtisha hivyo, lakini moyoni mwa huyo kijana haipo hivyo, hakubali, mtoto keshakana, na kasema hata kama itakuwaje, yeye hayupo tayari kunikubali mimi kuwa ni mzazi wake, mlisikia wenyewe akisema...’akasema mzee

‘Hayo aliongea tu, kwa hasira, lakini atakaa chini na atajirudi, haya hutokea kwa vijana kama yeye, lakini akipata muongoza hujirudi....’akasema msaidiazi wa wakili

‘Na jingine kwa hali ilivyo, Mzee tukubali kuwa sisi ndio tuatakiwa tuwe wampole, kwani yote hayo yanafanyika ili kukusaidia ombi letu likubaliwe, na ukiangalia zaidi mtoto au kijana yeye ni shahidi tu, japokuwa ni shahidi mkuu ambaye anaweza kukufunga, kwa hayo yaliyotokea, .....’akasema jamaa aliyekuwepo

‘Kwahiyo nyie mnataka mimi nifanyeje nini....ehee, siamini hayo?’ akaulizwa mzee akimuangalia wakili mtetezi

‘La kufanya ni kushirikiana na kile anachohitajia wakili,...yeye kajitolea kwa ajli yako, kwa mfano kuna hilo la kupata ushahidi wa kitaalamu unatakiwa kwenda hospitalini kutoa damu ili ikapimwe...., hilo sizani kama utakuwa na pingamizi nalo, nina uhakika mtoto huyo ni wako, ....’akaambiwa

‘Labda yeye anamfahamu baba yake mwingine, ....’akasema mshitakiwa

‘Ni kiburi tu, si unajua tena vijana wa siku hizi, lakini hilo tutalifankisha kwa njia zozote, hata kama kijana atalipingahilo, kuna njia nyingi tu za kulifanikisha hilo, lakini kuna hilo jingine umeambiwa,...’akasema jamaa ambaye anamsaidia wakili mtetezi

‘Lipi ...?’ akauliza mshitakiwa

‘Hilo la wewe kukaa meza moja na kijana wako ili mridhiane, wewe ukubali ni baba yake na yeye akubali kuwa wewe ni mzazi wake, mumekoseana, kwa bahati mbaya,...yapite yaliyopita tugange yajayo, sisi sote ni binadamu na mwanadamu ni mwingi wa kiburi,kujisahau, kukosea na hata kutakabari...hasa pale anapojiona unacho...’akasema

‘Na wewe ni mtu mzima, kwa busara zako tunajua utaliona hilo kihekima zaidi, unajua yote haya tunayafanya tukiangalia kuwa yanahitajika maandishi kuwa kweli mumekubalina na hilo, kuwa mtoto wako amekubali na yupo tayari kulifuta shitaka hilo, na ....anaweza kufidiwa kwa hasara uliyompatia.....au sio wakili....’akasema huyo jamaa

‘Ndio hivyo.....’akasema wakili

‘Fidia ....ya nini, nimempa hasara gani, mimi kaniumiza, ni nani atanifidia, hili hamulioni..?’ akauliza mshitakiwa akiwa kakunja uso.....na kabla wakili hajajibu au kuelekezea, Profesa akasema;

‘Lakini je kijana yupo tayari kwa hilo....huo ndio wasiwasi wangu mkubwa maana  mhh.....?’ akauliza Profesa na kukatisha maneno yake.

‘Wewe ndiye unayetakiwa utusaidie kwa hilo, maana wewe ndiye uliyeishi naye au sio.....?’ akasema huyo msaidizi wa wakili mtetezi na  wakili mtetezi akasema;

‘Ni kweli, wewe ndiye unayetakiwa ufanye juhudi hiyo kuhakikisha wawili hawa wanaelewana, na tukuulize wewe uliyewahi kuishi naye, je ikiwa vielelezo vyote vitathibitisha hilo, kuwa huyu mzee ni baba yake bado anaweza kuendelea kukataa ?’ akaulizwa Profesa

‘Tangu awali alishajenga hiyo hisia kuwa hana wazazi, japokuwa wakati naishi naye nilijaribu kumuelezea kilichotokea hadi yeye ikafikia kuwa hivyo, lakini.....sijui kwanini, yeye hakutaka kukubali, , kama ujuavyo, wenzetu huko juu, watoto wana haki zao, hawatakiwi kulazimishwa,kwahiyo sikuwa na la kufanya.....’akasema Profesa

‘Unaona ulivyomuharibu huyo mtoto, na madhara yetu yanaturudia sisi wenyewe...’akasema mshitakiwa

‘Sasa Profesa huu ni mpira wako, hatutaki kusikia kuwa wewe hutaki kuongea na huyo mtu hivi sasa, hili ni kwa manufaa ya familia yenu, ni kwa ajili ya kusaidia hii kesi imalizike na nyie kama familia mkae pamoja muelewane.....huyo ni kijana wenu’akasema wakili

‘Tatizo sio mimi, ....kama akikubali, tutakaa naye,,,,lakini sio rahisi kama mnavyofikiria nyie, huyo kijana, aliwahi kutoa ushahidi wa kunifunga mimi, kuonyesha jinsi gani asivyoikubali hii familia,...hebu fikiria, hakujali kuwa mimi ndiye niliyemfanikisha akafika hapo alipo....akawasikiliza wakwe zake , .....sasa ukiniambia mimi nikakae naye eti sijui nimshawishi..sijui ....kama ikibidi kufanya hivyo nitafanya, japo, apende asipende atakuja kukaa na mimi meza moja, hili likiisha,....’akasema Profesa

‘Unasema aliwahi kutoa ushahidi kama huo,.....mkiwa wapi, huko nje,...mmmh  kumbe ndio tabia yake...oh, dio hivyo, vijana wengine hubadilika kutegemeana na mazigira waliyokulia, lakini bado, msikate tamaa, mtu hujirudi, ....’akasema msaidizi wa wakili kwa mshangao.

‘Ila mimi ninachotaka ni kaka alielewe hili akubali, kwani mpaka sasa sijui kama yupo pamoja na sisi, ...’Profesa akasema akimuangalia kaka yake.

‘Ni wewe utafanya yote hayo, sio mimi....’akasema kaka yake

‘Unasikia bro, wewe usiwe ni kikwazo kwa hili, jaribu kulichukulia hili kama namna ya kumsaidia kijana ili ajirudi, najua mimi nitalaumiwa sana, lakinii nia yangu kwa kipindi hicho ilikuwa njema kumsaidia kijana  ili apate nafasi hiyoo ya kusoma nje, nafasi hiyo ilitolewa kwa watoto wenye mazingira magumu, nikaona nitumie huo mwanya ....sasa siwezi kuyasema hayo yote mahakamani, nielewe hivyo.....’akasema Profesa akimwangalia kaka yake aliyekuwa kainamisha kichwa chini huku akiwa kakishikilia akionekana kuwa na mawazo.

‘Kwani mimi nimesema nini, kwa vile wewe uamfahamu, mliishi naye basi endeleeni hivyo hivyo,mtakaa naye, mkubaliane, kama kuna maswala ya hati, wewe uwe ni kila kitu,....lakini sio mimi....’akasema kaka mtu

‘Bro huyo ni mwanao..mtoto wako,...usiharibu tena, tumeshakubaliana hilo....’akasema Profesa akizidi kumwangalia kaka yake

 ‘Lakini yote hayo ni kutokana na malezi, nyie  wazazi mnayo sehemu yenu ya lawama, japokuwa hilo kwa hivi sasa hatuna nafasi nalo, tukianza kulaumiana hapa tutapoteza muda...’akasema msaidizi wa wakili

‘Wakulaumiwa ni huyu, aliyemlea,....’akasema kaka mtu akimnyooshea ,kidole Profesa

‘Mwambieni yeye, kwanii yeye ndiye aliyemchukua na kumharibu huyo mtoto ...., ndio maana mimi sitaki kukaa meza moja na huyo muhuni, atakaa na huyu  baba yake mlezi,  wayamalize , yeye na mtoto wake, ,,,.’akasema kaka mtu akimuangalia profesa

‘Lakini mzee, kwenye maongezi ya maridhiano ni lazima wewe uwepo, ndivyo inavyotakiwa, ili mkataba wa makubaliano hayo ukamilike, ili hata hakimu aweze kushawishika na kuweza kutumia busara zake kukubaliana na maombi yetu, mtambue hiii ni michakato ya kumshawishi hakimu, ni kwa manfufaa ya hii kesi,.....’akasema wakili, na mshitakiwa akatikisa kichwa kuashiria kukataa akisema;

‘Mimi, labda kama yupo mzazi wake mwingine atalifanya hilo,...mimi sitaweza kukaa na huyo muhuni, huo ndio msimamo wangu, ....kama nilivyosema ,.huyu ndiye baba yake, atakaa naye watakubaliana, kama mama yake angelikuwepo hapa, basi angejumuika naye, lakini sio.....’kabla hajamaliza mara nyuma yako sauti ikatokea ikisema

‘Mimi mama yake nipo nitakaa naye meza moja nitaongea naye, ....’na wote wakageuka kuangalia sauti ilipotokea

NB: Kwa leo ndio hivyo, wewe wasemaje,.. Je ni kwanini pamoja na elimu kubwa wanayopata vijana wetu  mbona bado elimu hiyo, haiwasaidiii kimaadili....?


WAZO LA LEO: Katika swala la malezi kila mtu ana nafasi yake, hata kama mtoto muhusika hujamzaa wewe, lakini pindi unapoona kuwa mtoto huyo kapotoka una wajibu wa kumuelekeza kama mzazi, kama vile ungelifanya kwa mtoto wako wa kumzaa,....tukumbuke, wito huu, ‘’Tenda kwa mtoto wa mwenzako ukijua na wewe ni mzazi pia,’’

Ni mimi: emu-three