Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, November 27, 2015

RADHI YA WAZAZI-57





Kwanini nyie mumenifanyia hivi, lini mlisikia mtoto anamnyanyulia mzazi  mkono wake, haijawahi kutokea, mimi na umri wangu huu, kama ikitokea kuzozana mzazi na mwanae , mtoto akawa mkaidi, akamkosea mzazi wake, wazee wenzangu mnafahamu nini kinafanyika,...eti  wazee wenzangu,....?’ akauliza na wazee wakakaa kimia

‘Huu si mkosi jamani, ..... halafu eti mimi ndio nikae na huyo muhuni meza moja tuongee. Eti mimi mzazi ndio,  nijishushe, haitatokea hilo kwangu kamwe....’akasema mshitkiwa akitikisa kichwa

Wale wazee nao wakawa wanatikisa kichwa na mmoja akataka kuongea lakini wakili mtetezi akawamuwahi na kusema;

‘Kwa hali ilivyo, na kesi ilivyo inabidi , kwani sisi ndio tunaomba....kama nilivyosema awali, wenye kuomba inabidi wao wanyenyekee,  na ni muhimu mzee ukajua kuwa hili halitaingilia mila na desturi zenu, baada ya kukamilika hili, basi mtafaya taratibu zenu, au sio wakili mtetezi, au sio Profesa..’akasema msaidizi wa wakili na kumuangalia wakili mtetezi ambaye alikubali kwa kichwa, halafu akamuangalia profesa na Profesa akageuka kumuangalia kaka yake...

Mshitakiwa akiwa anatikisa kichwa kama kukataa akasema;

‘Na mbaya zaidi, mdogo wangu mwenyewe ananiendea kinyume, anafanya mambo anavyotaka yeye mwenyewe, ...kilichompata huko Ulaya keshasahau, hajui kuwa yote haya yalitokea kwa vile alidharau mila na desturi zetu za malezi, na dini zinasisitiza sana hayo, malezi bora kwa vijana wetu, na mtoto hata siku moja hawezi kuwa juu ya mzazi....’akatulia

‘Ni sawa kabisa....’akasema wakili

‘Mdogo wangu kwa vile kaishi na wazugu, basi anajifanya kalisahau hilo, na kutokana na kikiuka hayo, amejikuta kwenye mitihani na mateso mengi, hadi katimuliwa huko, wakijua keshakufa....mimi nashangaa, kuwa bado tena anarudia makosa yale yale,...hivi unataka yakupate yapi ndio ukiri kuwa umekosea....’akasema akimuangalia ndugu yake

Wote wakageuka  kumuangalia Profesa ambaye alionekana kutaka kumzuia kaka yake asiendelee kuongea lakini kaka yake akaendelea kuongea kwa kusema;

‘Sasa huyu....unataka na mimi yanipate .....hahaaah, sio mimi, kamwe mimi sitageuka jiwe, acha niende jela, kama ikifanya hivyo ni makosa, na nasema tena mnisikie , acha nihukumiwe, lakini sitakwenda kinyume na mila na desturi zetu za jinsi ya kulea na taratibu za kifamilia,...’akasema

‘Bro....’Profesa akataka kumkatisha kaka yake,lakini kaka yake akamuashiria kuwa anyamaze

‘Acha niongee,...nikuembie hili mlisikia wote, kama mimi kwa kufanya hivyo itatoklea  ikahukumiwa kwenda jela, kwasababu ya kutimiza wajibu wangu kama mzazi, na ikawa ni kutokana na huyo mtoto,.....nyie mtakuwa mashahidi, yatakayomkuta  huyo mtoto, ....sipenndi na wala sio mimi,....’akawageukia wazee na kusema

‘Wazee mnayafahamu hayo, lakini sijui, ...labda iwe kweli,yeye hakutokana na damu yangu, labda kama anavyodai yeye sio kweli mtoto wa kutokana na mimi....’akasema na kufanya kama ananawa mikono....

Tuendelee na kisa chetu

            *****************

‘Lakini mzee mwenzetu  hayo tutakuja kuyamaliza kinyumbani,tutahitajika kuyasafisha na kijana aelekezwe la kufanya ...hapa kama unavyoona, ni sheria inahitajika, na wao wamejaribu kuliona hilo, na wakajua kama hali itakwenda kisheria zaidi wewe utakwenda jela, je itasaidia..’akasema mzee

‘Kwahiyo, hebu kwanza, tuyasikilize hayo ya kisheria yanavyotaka kwanza, na tukirudi nyumbani, tutaendelea na taratibu zetu kabla hatujachelewa,,....muhimu huyo kijana apate mtu amuelekeze, lakini kwa hivi sasa tukubaliane na hili,..’akasema huyo mzee mwingine.

‘Hahaha wazee wenzangu, kwanini mnifanyie hivyo, mnasema tutayaongea....kweli mnasema hivyo, tuache mimi nivuliwe nguo,halafu ....ndio tuje tukae tuyaongee,  wakati mimi nimesha-aibika, nimeshakiuka miiko yetu,...hamjui wanachotaka mimi nifanye,...hebu niambieni wazee wenzangu tunamzihaki nani hapo...?’ akawa kama anauliza

Wazee wakawa kimia, na yeye akaendelea kuongea

‘Huu wazee wenzangu ni utoto, ....natamka hivi kwani mnafahamu hivyo, huo ni utoto, eti tufanye hivi,tukimalize tujifaye yale tuliyofanya sio, tulikosea wakati huo tunafahamu tulikosea haya tunayotaka kuyafanya, hivi kweli inakuja akilini,..?’ akawaangalia wazee wenzake, ambao walikuwa kimia wameagalia chini.

‘Najua hili ni langu, najua .....huu ni mkosi, umeingia kwenye familia yangu, na chanzo ni huyu mdogo wangu, kwa kujifanya yeye ni msomi, kaishi na wazungu..kaiga mambo yao, na nakuambia, ....wewe, toka awali nililiona hili, sasa sio mimi. Ni wewe ...utabeba huo mzigo mwenyewe....’akasema akimuangalia mdogo huku akimnyoshea kidole.

Mdogo mtu akawa kainamisha kichwa chini, akionekana mwingi wa mawazo, kabla hajajitetea, wakili mtetezi akasema;

‘Mzee, mimi nakuelewa sana, sio kwamba siyaelewi hayo,....mimi ni mzaliwa wa huko na pamoja na kusomea sheria, lakini pia nimejitahidi kujifunza mila na desturi zetu, na mila za ulezi ni kila mahali hata huko ulaya zipo, sema wenzetu wana yao ...sipendi kuyaongelea zaidi,...na hata hakimu anaelewa hayoo ndio maana akatumia hekima badala ya kusimamia kwenye sheria tu...akaona hekima itumike......’akasema wakili mtetezi

‘Kama ni hivyo, huoni.....’akataka kusema mshitakiwa na wakili mtetezi akamkatisha kwa kusema;

‘Huenda utasema nisingeliongea hilo mahakamani, sasa angalia kwa upande mwingine kama nisigelifanya hivyo, ingetokea nini,...’

‘Ungelifungwa,....’akadakia msaidizi wake, na wakili mtetezi akatikisa kichwa kukubali

‘Ni kweli hukumu ingeweza kuwa mbaya kihivyo, na baadaye ungelifahamu kuwa aliyekufunga ni mwanao, wakati huo hali imeshafikia huko, haingeliwezekana kabisa kuwa na suluhu, haya niliyawazia na mwisho wake nikaona ni heri nifanye hicho nilichofanya,...’akasema wakili akimuangalia mshitakiwa

‘Hapana, hamkunitendea yanayostahiki,.....’akasema mashitakiwa na Profesa akadakia kwa kusema

‘Bro, mimi naona kwanza tumsikilize wakili, ....na mimi sioni kwamba vibaya, hajafaya vibaya kabisa ni wewe tu hutaki kuelewa, kafaya jambo ambalo limezuia ubaya zaidi ...sasa tusipoze muda, kwa maswala hayo ya kimila na desturi, hayo yanaweza kusubiria, lakini kuna hili swala la sheria, wakili kapewa kazi na hakimu, tusipoteze muda,...’akasema Profesa

‘We bwana mdaogo unazarau tu...nakuelewa sana....’akasema kaka mtu

‘Ama hilo la kunilaumu mimi, nafahamu sana kosa langu,najua kama ingelitokea vinginevyo kijana akarudi vingine akawakubali, na hali nzuri, msingelisema haya, lakini hayo tuyaache hayo ..’akasema Profesa

‘Usijitetee makosa, huwezi kufuga nyoka wa sumu useme angesaidia baadaye, wakati keshaanza kuumiza watu..nyoka uliyemfuga huko sasa anatugeuka....ukaona ukae kimia, wengine nao wakione cha moto.....’akasema kaka mtu

‘Bro,...nina maana kubwa kwa mimi kukaa kimia kukuambia hili,  nitakuja kukuambia ni kwanini nilifanya hivyo, kwa hapa siwezi kukuambia, sipendi kulizungumza hili hapa, litaharibu kila kitu....’akasema Profesa

‘Unajua wewe bwana mdogo nakufahamu sana toka utotoni, wewe ni mbinafasi, inapofikia kwenye jambo la kuamua kwanza unaangalia ubinafsi wako, hujali wengine, hili ndilo limetufikisha hapa, na tabia yako umemuambukiza na huyo mtoto,hupendi kuambiwa ukweli, hupendi kuelekezwa, wataka kujiamulia utakavyo....’akasema

‘Bro....’akataka kujitetea

‘Sasa huyo nyoka,...natumia neno hilo, mnielewe, huyo mtoto, ni wako, na mimi kama ni kwenda kufungwa sawa, si na mimi natakiwa nikione cha moto,...lakini .....’akasema

‘Nani kakuambia utafungwa...’akasema wakili mtetezi

‘Unafahamu nyie hamnifahamu mimi vyema, ....haya yote mimi nilishayaona kwenye njozi, na kuna makubwa yanakuja,....kosa lilianzia mbali, sitaki kusema hapa, nikaoa, yakatokea haya, ya kutokea baadaye nikawa sina jinsi, sasa cha moto nakiona.....’akasema akiwa anatikisa kichwa, na wakili akawa anamuangalia huyo mzee kwa macho ya kutafakari.....

‘Lakini hayo yalishapita, nilishaosha mkono na kutubu dhambi zangu,...kumbe ..kumbe...kumbe...mambo bado, maana naishi na watu wasielewa, hawa watu hawa ndio wnaharibu jamii....’akasema akimnyoshea kidole profesa

‘Lakini hata hivyo mimi sitakubali, ..yanayokuja mimi sitakuwepo, wewe bwana mdogo utapambana nayo, ...si ndivyo ,mnavyotaka, utajiri au sio, haya utaupata, lakini hutapata raha....hilo nakuambia,.....’akatulia

‘Bro ....’akataka kukatisha lakini wakili akamtuliza, na mshitakiwa naye akanyamaza kimia

Kukapita ukimia kidogo kama vile kila mmoja aliyekuwepo hapo alikuwa akiliwazia hilo jambo na wakili mtetezi akaanza kuongea;

                                                  *************

‘Naona tusipoteze muda, ni muhimu nikawaelezea tukakamilisha hayo ninayotakiwa kuwaambia, utekelezaji wake, kama alivyopendekeza muheshimiwa hakimu , tukiyafanya hayo,tunaweza kumshawishi muheshimiwa hakimu...’akaanza kusema

‘Nafahamu sana mila na desturi zetu za malezi ndani ya jamii zetu, nafahamu sana mitihani ya ulezi hasa kizazi hiki cha sasa ambacho kunakumbana na mitihani mingi inayotakana na utanndawazi, ...’

‘Tunaweza kuwalaumu sana vijana wetu, lakini wakati ndio umetufikisha hapa, sio wao tu,...ni mabadiliko ya maisha duniani nzima kizuri kina changamoto zake,..utandawazi ni mnzuri, lakini changamoto zake ni nyingi...., na inapofikia kwenye ulezi, kwenye watoto wetu kila mwenye hekima litamgusa hili,....’akatulia

‘Usione mwenzako limetokea hili ukahisi wewe upo salama, labda wewe uwe una kijiji chako, una dunia yako, ambayo watoto wako wanaishi peke yao, na usiwe na aina yoyote ya mawasiliano, kitu ambacho hakiwezekani....hili ni letu sote  kwani mwenzako akinyolewa, na wewe tia maji, hili...

‘Mzee, hilo sio swala lako tu, wengi kila mmoja wetu hapa linamgusa kama sio kihivyo, ni kivile,....na kwingine ni kubaya zaidi kuliko hata hili lako, ni kwa vile tu halijawekwa hadharani....’akasema na kila mtu akawa anatikisa kichwa kukubali

‘Sasa ndugu zanguni, hili sasa limetokea tulione kama swala latu sisi wazazi..,ilitakiwa iwe hivyo, wazazi wote tungetakiwa tuwe kitu kimoja, likitokea jambo sio la kawaida, wazazi tukutane tuone tutalirekebisha vipi, kabla halijasambaa,  lakini sasa hivi ulezi ni kila mtu na watoto wake,....’akasema wakili

‘Siku hizi mtoto wa mwenzako akikosea, ukajaribu kumuadhibu, acha kumuadhibu, ile kumkemea tu, utazua ugomvi,...na ukiwa ndio mzee itazua balaa, mzee mwanga mzee mchawi,  na maneno ya kukatisha tamaa na hata kuvunja undugu au ujirani, utasikia wewe ulinisaidia kuzaa, ulinisaidia kulea wewe....hayo na mengine mengi, na matokea yake ndio haya....’akasema wakili

‘Sasa tusikimbilie kulaumu kama wapo wenye uoni wa mbali, basi tujaribu kulitatua lile linalowezekana, na hili letu liwe kama mfano, tusiadianeni, kabla hijafika mbali....’akasema wakili

‘Wazee wenzangu, nimeamua tusaidiane hili, na nimefaya hili kwa kujitolea, ni kwelii mimi kama ningetaka pesa , nisingelifuatilia hili jambo,hadi hatua hii,  ..lakini aliposimulia huyu rafiki yangu Profesa, nilihisi mwili mnzima ukinicheza, nikiwazia watoto wangu, nikiwazia watoto wa watoto wangu, huko tunapokweda ni kubaya,....’akasema wakili akiwaangalia wazee wale waliokuwepo

‘Huu ni mtihani, na ....hata kama sheria zitawekwa, adhabu zikatolewa, haitasaidia kitu, kwani chanzo kipo pale pale.....na kinazidi kuota mapembe, kiajitanua siku hadi siku, huko mbeleni yatazuka mabaya zaidi.....’akasema wakili

‘Sasa wazee , tulifikiria hili kama njia ya kuonyesha njia ili wegine wafuate, najua sio kazi rahisi, lakini sisi tutakuwa tumetimiza wajibu wetu, mimi nimeamua kutokuagalia masilahi, nimeamua kujitolea, ni kwanini, najua kujitolea siku hizi ni gharama, lakini najua ni faida mbele ya mungu....’akasema

‘Baada ya kusema haya, tusipoteze muda, najua mnahitajika kurudi kijijini, lakini nimeona ni bora tulifanye hili , tuanze utekelezaji mapema, ili mkirudi tena hapa mahakamani tukakuja kulimaliza hili kabisa,...’akasema

‘Sasa kuna mambo ya kufanya, naomba haya myasikilize kwa makini ili mimi niweze kulifanikisha hili, msiposhirikiana nami, itafika sehemu nitashindwa...’akasema

‘Hii ni kesi ya aina yake mtoto kumshitakia baba yake, na wakati huo wawili hawa hawafahamiani, ....’akasema

‘Haya sasa wamefahamiana iweje, na wamefahamiana wakati kesi inaendelea,...ila 
tuelewe tatizo sio kwa vile ni kesi ya baba na mtoto, hilo laweza kutokea, mtoto akamshitakia baba yake, na baba akamshitaki mtoto, na sheria ikafuata mkondo....’akasema wakili

‘Mimi nilimuelezea muheshimiwa hakimu hali halisi, kwa kadri alivyonielezea Profesa, na hakimu alishangaa sana kwanini hali hiyo ikawepo,  Profesa ilitakiwa uwepo kujibu maswali mengi , ya kwanini ilitokea hivyo,....mimi  nikatumia uzoefu wangu kumfahamishana hakimu, na ni kwanini tunaomba hii kesi iwe hivyo, ndipo hakimu akataka muda kulitafakari ombi letu...’akasema

‘Alitumia maneno hayo, apewe muda kulitafakari ombi letu, lakini akitia maagizo ya mambo yanayotakiwa sisi tufanye .....’akasema

‘Kwahiyo kuahirishwa huko ni kwa manufaa yetu, lakini kama tutafanya hayo aliyoagiza hakimu, ili yaweze kumshawishi hakimu, kuwa hili lilitokea kwa bahati mbaya , ....’akasema wakili

‘Tafadhali hapo kidogo.....’alikuwa mshitakiwa aliyetaka kuongea lakini Profesa akamzuia

‘Bro mengine tutaongea nyumbani najua unataka kuongea kitu gani.........’akasema na wakili akamuangalia mshitakiwa halafu Profesa, na baadaye akaendelea kuongea:

‘Sasa ni hivi, japokuwa hakimu kaahirisha hii kesi, lakini kesi yetu bado ni ngumu, kutokana na utata wake,...ni kesi ya jinai, na lengo letu ilikuwa kuirejesha hii kesi kuwa kesi ya madai, na.....zaidi tuliomba ikiwezekana ikaongelewe nje ya mahakama,....inakuwa ngumu sana kwa hakimu kuamua hivyo, lakini pamoja na sheria hekima nayo ni muhimu sana, nimefurahishwa sana na huyu hakimu...’akasema

‘Sasa kuna mambo muhimu sana tunahitajika kuyafanya ...’akasema na wote sasa wakatulia kumsikiliza wakili

‘Ili ombi letu liwe na uzito, inabidi sisi wenyewe kukaa kikao na waliotendewa hilo kosa tuwe na kitu cha maridhiano, na pande zote zikubaliane na hilo, hii ina maana waliotendewa hilo kosa, wakiri kuwa wameshasamehe na wapo tayari, kama wanahitaji fidia au itategemea na wao watakuja na hoja gani....’akasema wakili sasa akijaribu kumuangalia kila mtu kwa muda wake kuona kama hilo limeeleweka...na alipofika kwa mshitakiwa, ...

‘Tafadhali ngoja kwanza, ,,,..’akasema mshitakiwa

‘Bro tutaongea hayo yako tukifika nyumbanii,  subiria wakili aeleze kilichoongelewa na hakimu ili tukifika huko nyumbani tujue tunaanzia wapi, hii ni kwa manufaa ya hii kesi...’akaambiwa.

‘Mimi nataka niliweka hili wazi  mbele yenu, mkisema niache akaongea tu, wakati mimi sijakubaliana, itasaidia nini, ....mimi sijakubaliana na hilo ombi, kwasababu kwa mila na desturi zetu hicho hakipo....’akasema

‘Lakini hapa hatupo kimila, tupo kisheria...’akasema msaidizi wa wakili mtetezi

‘Sasa kama mpo kisheria, nasema hivi, mimi mzee Makunjazi, kamwe sitaweza kukaa na huyo muhuni, eti mimi mzazi nimuombe mtoto msamaha, na pia eti nimbembelezi kuwa mimi ni baba yake, nimuombe afute kesi,....yeye kama nani,...?’ akatulia

‘Eti  wazee wenzangu mbona hamnisaidii kwa hili, mnafahamu mila zilivyo, au kwa vile sio mtoto wenu, hahahaa basi sio mimi....kamwe....’akasema mshitakiwa

‘Bro, sikiliza kwanza, anachoongea wakili...tumsikilize wewe unang’ang’ania, hapa hatuongei maswala ya mila,tunaangalia sheria itatusaidiaje ili hii kesi iishe kwa amani, hapa hujashitakiwa na mila,...uelewe hilo,....’akasema Profesa

‘Haina haja ya kusikiliza zaidi basi, mimi nimeshaelewa, nia na lengo lenu ni kumvimbisha kichwa huyo mhuni, vijana wa namna hiyo ukiwapa nafasi wanazidi kuharibika, na kuona alichokifanya ni sahihi ...., ‘akasema kwa hasira

‘Kwa hivi sasa tutajifanya hivyo, ...’akasema msaidizi wa wakili

‘Kweli dunia imekwisha, mtoto anizalilishe mimi hivi, mtoto anipige, mtoto anivunje mbavu, kisa ni nini, halafu bado sisi tumbembeleze, hapana mimi sikubaliani nanyi kabisa...’akasema mshitakiwa

‘Lakini hayo ya kukufanyia hivyo, sio kosa lake, alikuwa hajui kuwa wewe ni baba yake,  mzee mwenzetu....’alikuwa mzee mmojawapo aliyesema

‘Kwahiyo kama mtu mzima sio baba yake afanye hivyo, ampige kama mwizi, bila kujua ni nini kilitokea kisa kafika nyumbani kwake akakosa kuelewana na mlinzi..hakutaka kujua kisa ni nini, mlinzi kaumia na kujigonga alipodondoka.....aaah, hata haina haja ya kuwaelezea zaidi...’akasema akitikisa kichwa

‘Hayo sasa tutayaongea nyumbani tusubirie, tunaomba  wakili uendelee kutoa maelezo yako...’akasema Profesa na kaka mtu akatulia akiwa kakaangalia pembeni kama vile hataki kusikiliza, na wakili akaendelea kuongea;

‘Sasa ndugu zanguni, hili nii ombi , tumeomba sisi, kwa muheshimiwa hakimu, na ombi letu lipo mikononi mwake, hakimu anataka kutumia busara zake,na kuacha vipengele vya kisheria,  fujo imefanyika, na ukikwaji wa sheria upo wazi, lakini kwa mustakabali wa kifamilia, muheshimiwa anaweza kufumba macho...’akasema wakili akiongea kwa sauti ya chini kama vile hataki watu wengine wasikie.

‘Japokuwa katika utetezi wangu, hakimu aliona kuwa kuna namna ya shahidi kuwa muongo, kutokana na jinsi nilivyombana, lakini bado haikuwa na tija,....mtu kaumizwa, na matendo hayo yametokea kwenye makazi ya mtu...hilo ni kosa....’akasema wakili kwa sauti ya chini

‘Hilo ni jambo moja lakini kuna hili jambo jingine kuwa tunahitajika tuwe na vielelezo vya kuthibitsha kuwa kweli huyo mtoto ni mtoto wako kweli,  mshitakiwa...’akasema

‘Vielelezo gani...?’ akauliza mshitakiwa

‘Vipimo vya kitaalamu kuwa kweli huyo ni mtoto wako..’akasema wakili

‘Mimi sina haja ya kuthibitisha hilo kama yeye kakana na kusema mbele ya mahakama kuwa mimi si baba yake, basi, kuna haja gani ya hilo, vipimo vya nini, nataka kuthibitisha nini, kumbembeleza kuwa mimi ni baba yake, hapana hili tuachane nalo.....’akasema

‘Sio kwamba ni hiari,....mimi nimeshalitamka hilo mahakamani na hakimu anahitaji ushahidi wa kitaalamu, ili kuweka  uzito wa madai yetu, ni taratibu na ni muhimu zifuatwe, na sisi ndio wenye shida, ..’akasema na kuwaangalia mshitakiwa na mdogo wake, na hakutaka kuwapa nafasi ya kuongea akasema;

‘Ujue sisi ndio tuliofanya kosa, na kosa ni kosa na mtendaji wa kosa hata akiwa nani  kamtendea nani sheria ipo pale pale, ukifanya kosa utahukumiwa tu,haijalishi kuwa wewe ni baba yake, hilo tulielewe kwanza ....lakini kutoka na hali ilivyo, hakimu kwa busara zake kaliona  hilo,kaamua kutumia busara zake ......’akasema

‘Kwahiyo ili tuwe na mshiko wa maombi yetu, inabidi wewe mshitakiwa na mtoto mkae kikao kilichoratibiwa, mbele ya wanasheria yawezekana ikawa mimi au yoyote mtakayemchagua, kulithibitisha hilo....’akasema wakili na kumuangalia mzee

‘Hahahaha, unajua wewe unaongea kirahisi sana, ...mimi ni mzazi, ndio natakiwa nimnyenyekee mtoto, si ndio maana yake, yaani, nikae na huyo mtoto muhuni asiye na adabu,  nianze kumbembeleza.... hivi nyinyi mnalionaje hili, au kwa vile haliwahusu saana, .....?’ akauliza mshitakiwa akimuangalia wakili na baadaye akawaangalia wazee wenzake.

‘Kukaa kikao ndivyo inatakiwa, lakini hilo la kumbembeleza,....hapana, yeye ataongea na muendesha mashitaka ataelekezwa la kufanya, akikubalia, sizani kama kuna maswala ya kubembelezana mzee, sizani kama atakuwa na ujeuri huo mbele ya mzazi wake....’akasema wakili

‘Pamoja na hilo kunahitajika vielelezo vya kulithibitisha hilo kitaalamu kuwa wewe kweli ni baba yake, ni utaratibu tu, kwa ajili ya kumbukumbu, na muhimu vielelezo hivyo viwepo ....’akasema

‘Una maana gani kuthibitisha....?’ akauliza

‘Ni hivi, wewe ni baba yake, kihalisia, lakini kimaandishi tutathibitisha vipi, ...kimaandishi tunahitajika kuwa na vielelezo, tunahitajika tupate vipimo vya kitaalamu, na siku hizi kuna vipimo ambavyo havina mashaka, ambavyo ukipimwa kweli inathibitisha kuwa wewe kweli ni baba yake halisi, vipimo hivyo vinaitwa DNA, ...’akasema

‘Hapo mzee kama ulibambikiwa itathibitika.....’akasema msaidizi wa wakili mtetezi akionyesha utani, ...

‘Kwa minajili hiyo mshitakiwa na mtoto tutahitajika twende hospitali za serikali, mtoe damu zenu, zipimwe, na majibu yake yataambatishwa kwenye maombi yetu...’akasema wakili

‘Lakini itakuwa na haja gani, hata kama vipimo hivyo vitathibtisha hivyo, lakini moyoni mwa huyo kijana haipo hivyo, hakubali, mtoto keshakana, na kasema hata kama itakuwaje, yeye hayupo tayari kunikubali mimi kuwa ni mzazi wake, mlisikia wenyewe akisema...’akasema mzee

‘Hayo aliongea tu, kwa hasira, lakini atakaa chini na atajirudi, haya hutokea kwa vijana kama yeye, lakini akipata muongoza hujirudi....’akasema msaidiazi wa wakili

‘Na jingine kwa hali ilivyo, Mzee tukubali kuwa sisi ndio tuatakiwa tuwe wampole, kwani yote hayo yanafanyika ili kukusaidia ombi letu likubaliwe, na ukiangalia zaidi mtoto au kijana yeye ni shahidi tu, japokuwa ni shahidi mkuu ambaye anaweza kukufunga, kwa hayo yaliyotokea, .....’akasema jamaa aliyekuwepo

‘Kwahiyo nyie mnataka mimi nifanyeje nini....ehee, siamini hayo?’ akaulizwa mzee akimuangalia wakili mtetezi

‘La kufanya ni kushirikiana na kile anachohitajia wakili,...yeye kajitolea kwa ajli yako, kwa mfano kuna hilo la kupata ushahidi wa kitaalamu unatakiwa kwenda hospitalini kutoa damu ili ikapimwe...., hilo sizani kama utakuwa na pingamizi nalo, nina uhakika mtoto huyo ni wako, ....’akaambiwa

‘Labda yeye anamfahamu baba yake mwingine, ....’akasema mshitakiwa

‘Ni kiburi tu, si unajua tena vijana wa siku hizi, lakini hilo tutalifankisha kwa njia zozote, hata kama kijana atalipingahilo, kuna njia nyingi tu za kulifanikisha hilo, lakini kuna hilo jingine umeambiwa,...’akasema jamaa ambaye anamsaidia wakili mtetezi

‘Lipi ...?’ akauliza mshitakiwa

‘Hilo la wewe kukaa meza moja na kijana wako ili mridhiane, wewe ukubali ni baba yake na yeye akubali kuwa wewe ni mzazi wake, mumekoseana, kwa bahati mbaya,...yapite yaliyopita tugange yajayo, sisi sote ni binadamu na mwanadamu ni mwingi wa kiburi,kujisahau, kukosea na hata kutakabari...hasa pale anapojiona unacho...’akasema

‘Na wewe ni mtu mzima, kwa busara zako tunajua utaliona hilo kihekima zaidi, unajua yote haya tunayafanya tukiangalia kuwa yanahitajika maandishi kuwa kweli mumekubalina na hilo, kuwa mtoto wako amekubali na yupo tayari kulifuta shitaka hilo, na ....anaweza kufidiwa kwa hasara uliyompatia.....au sio wakili....’akasema huyo jamaa

‘Ndio hivyo.....’akasema wakili

‘Fidia ....ya nini, nimempa hasara gani, mimi kaniumiza, ni nani atanifidia, hili hamulioni..?’ akauliza mshitakiwa akiwa kakunja uso.....na kabla wakili hajajibu au kuelekezea, Profesa akasema;

‘Lakini je kijana yupo tayari kwa hilo....huo ndio wasiwasi wangu mkubwa maana  mhh.....?’ akauliza Profesa na kukatisha maneno yake.

‘Wewe ndiye unayetakiwa utusaidie kwa hilo, maana wewe ndiye uliyeishi naye au sio.....?’ akasema huyo msaidizi wa wakili mtetezi na  wakili mtetezi akasema;

‘Ni kweli, wewe ndiye unayetakiwa ufanye juhudi hiyo kuhakikisha wawili hawa wanaelewana, na tukuulize wewe uliyewahi kuishi naye, je ikiwa vielelezo vyote vitathibitisha hilo, kuwa huyu mzee ni baba yake bado anaweza kuendelea kukataa ?’ akaulizwa Profesa

‘Tangu awali alishajenga hiyo hisia kuwa hana wazazi, japokuwa wakati naishi naye nilijaribu kumuelezea kilichotokea hadi yeye ikafikia kuwa hivyo, lakini.....sijui kwanini, yeye hakutaka kukubali, , kama ujuavyo, wenzetu huko juu, watoto wana haki zao, hawatakiwi kulazimishwa,kwahiyo sikuwa na la kufanya.....’akasema Profesa

‘Unaona ulivyomuharibu huyo mtoto, na madhara yetu yanaturudia sisi wenyewe...’akasema mshitakiwa

‘Sasa Profesa huu ni mpira wako, hatutaki kusikia kuwa wewe hutaki kuongea na huyo mtu hivi sasa, hili ni kwa manufaa ya familia yenu, ni kwa ajili ya kusaidia hii kesi imalizike na nyie kama familia mkae pamoja muelewane.....huyo ni kijana wenu’akasema wakili

‘Tatizo sio mimi, ....kama akikubali, tutakaa naye,,,,lakini sio rahisi kama mnavyofikiria nyie, huyo kijana, aliwahi kutoa ushahidi wa kunifunga mimi, kuonyesha jinsi gani asivyoikubali hii familia,...hebu fikiria, hakujali kuwa mimi ndiye niliyemfanikisha akafika hapo alipo....akawasikiliza wakwe zake , .....sasa ukiniambia mimi nikakae naye eti sijui nimshawishi..sijui ....kama ikibidi kufanya hivyo nitafanya, japo, apende asipende atakuja kukaa na mimi meza moja, hili likiisha,....’akasema Profesa

‘Unasema aliwahi kutoa ushahidi kama huo,.....mkiwa wapi, huko nje,...mmmh  kumbe ndio tabia yake...oh, dio hivyo, vijana wengine hubadilika kutegemeana na mazigira waliyokulia, lakini bado, msikate tamaa, mtu hujirudi, ....’akasema msaidizi wa wakili kwa mshangao.

‘Ila mimi ninachotaka ni kaka alielewe hili akubali, kwani mpaka sasa sijui kama yupo pamoja na sisi, ...’Profesa akasema akimuangalia kaka yake.

‘Ni wewe utafanya yote hayo, sio mimi....’akasema kaka yake

‘Unasikia bro, wewe usiwe ni kikwazo kwa hili, jaribu kulichukulia hili kama namna ya kumsaidia kijana ili ajirudi, najua mimi nitalaumiwa sana, lakinii nia yangu kwa kipindi hicho ilikuwa njema kumsaidia kijana  ili apate nafasi hiyoo ya kusoma nje, nafasi hiyo ilitolewa kwa watoto wenye mazingira magumu, nikaona nitumie huo mwanya ....sasa siwezi kuyasema hayo yote mahakamani, nielewe hivyo.....’akasema Profesa akimwangalia kaka yake aliyekuwa kainamisha kichwa chini huku akiwa kakishikilia akionekana kuwa na mawazo.

‘Kwani mimi nimesema nini, kwa vile wewe uamfahamu, mliishi naye basi endeleeni hivyo hivyo,mtakaa naye, mkubaliane, kama kuna maswala ya hati, wewe uwe ni kila kitu,....lakini sio mimi....’akasema kaka mtu

‘Bro huyo ni mwanao..mtoto wako,...usiharibu tena, tumeshakubaliana hilo....’akasema Profesa akizidi kumwangalia kaka yake

 ‘Lakini yote hayo ni kutokana na malezi, nyie  wazazi mnayo sehemu yenu ya lawama, japokuwa hilo kwa hivi sasa hatuna nafasi nalo, tukianza kulaumiana hapa tutapoteza muda...’akasema msaidizi wa wakili

‘Wakulaumiwa ni huyu, aliyemlea,....’akasema kaka mtu akimnyooshea ,kidole Profesa

‘Mwambieni yeye, kwanii yeye ndiye aliyemchukua na kumharibu huyo mtoto ...., ndio maana mimi sitaki kukaa meza moja na huyo muhuni, atakaa na huyu  baba yake mlezi,  wayamalize , yeye na mtoto wake, ,,,.’akasema kaka mtu akimuangalia profesa

‘Lakini mzee, kwenye maongezi ya maridhiano ni lazima wewe uwepo, ndivyo inavyotakiwa, ili mkataba wa makubaliano hayo ukamilike, ili hata hakimu aweze kushawishika na kuweza kutumia busara zake kukubaliana na maombi yetu, mtambue hiii ni michakato ya kumshawishi hakimu, ni kwa manfufaa ya hii kesi,.....’akasema wakili, na mshitakiwa akatikisa kichwa kuashiria kukataa akisema;

‘Mimi, labda kama yupo mzazi wake mwingine atalifanya hilo,...mimi sitaweza kukaa na huyo muhuni, huo ndio msimamo wangu, ....kama nilivyosema ,.huyu ndiye baba yake, atakaa naye watakubaliana, kama mama yake angelikuwepo hapa, basi angejumuika naye, lakini sio.....’kabla hajamaliza mara nyuma yako sauti ikatokea ikisema

‘Mimi mama yake nipo nitakaa naye meza moja nitaongea naye, ....’na wote wakageuka kuangalia sauti ilipotokea

NB: Kwa leo ndio hivyo, wewe wasemaje,.. Je ni kwanini pamoja na elimu kubwa wanayopata vijana wetu  mbona bado elimu hiyo, haiwasaidiii kimaadili....?


WAZO LA LEO: Katika swala la malezi kila mtu ana nafasi yake, hata kama mtoto muhusika hujamzaa wewe, lakini pindi unapoona kuwa mtoto huyo kapotoka una wajibu wa kumuelekeza kama mzazi, kama vile ungelifanya kwa mtoto wako wa kumzaa,....tukumbuke, wito huu, ‘’Tenda kwa mtoto wa mwenzako ukijua na wewe ni mzazi pia,’’

Ni mimi: emu-three

No comments :