Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Showing posts with label Ndani ya diari yangu-Riwaya. Show all posts
Showing posts with label Ndani ya diari yangu-Riwaya. Show all posts

Wednesday, October 30, 2019

CHUMA ULETE-6


 Hata sijui ni kwanini...

Mimi  sikuweza kumuamini huyu mtu wa jamii, kuwa ataweza kunisaidia kwenye hili janga, kwangu mimi, sana sana  niliona yeye anataka kutumia hili tukio, ili aweza kukamilisha utafiti wake tu..na hii kesi inahitajia pesa, inahitajia wakili mwenye ujuzi mkubwa,...mimi sina pesa, rafiki yangu halidhalika, na cha ajabu rafiki yangu kaenda kuniletea mtu ambaye, hana pesa., ...sio wakili kisheria,

‘Huyu mtu atanisaidia nini mimi..’ nilijikuta nawaza na kusema hivyo kwa sauti ndogo.


 Tulibakia wawili , mimi na mtu wa jamii, yeye akaniuliza maswali machache, muda wa kuongea na wageni ulishakwisha, yeye  akaondoka akisema anataka kuonana na mkuu wa hicho kituo, sijui waliongea nini....

Siku hiyo ikapita sikuchukuliwa kwenda Ukonga, niliona ajabu sana...,na hakuna aliyekuja kuniambia ni kwanini..lakini nilijua ni swala la muda, nitachukuliwa tu..

Kisa kinaendelea.....

**************


Kesho yake akaja shemeji, macho yamemuiva, na nilibahatika kuyaona hayo macho yake baada ya yeye kuvua miwani, aliyokuwa amevaa, nahisi aliivaa hiyo miwani kwa makusudi ya kuficha hayo macho yake, ni dhahiri kuwa anavuta bangi, japokuwa yeye, halikubali hilo.


'Shem, kwanini unaniuza..'akaanza kuniambia hivyo, hata bila ya salamu.


'Kwa vipi shem...?'nikamuuliza, nilishamzoea, maana kila tukikutana, mimi na yeye, tunaishia kwenye ugomvi tu, jamaa huyu ananichukia sana, ila kama dada yake yupo, jamaa huyu  anajifanya kuwa ni muungwana kwangu.

'Mimi nimejitolea muhanga kukusaidia wewe, ...unajua ni nini nilichokifanya, imeniuma sana, kukusaidia wewe na haki ya dada yangu ipotee....’akatikisa kichwa.

‘Unaja nikuambie ukweli, tukio hili  ilikuwa ndio wakati mnzuri wa kukumaliza kabisa...ulichokifanya, hakistahiki kusamehewa,..unahitajika kunyongwa,..lakini kwa upumbavu wangu, nikaogopa....niliogopa, nitaambiwa nimechukua sheria mikononi mwangu, na mimi sitaki kuingia kwenye mikono ya polisi...ndio hivyo tu...sasa wewe umeharibu..’akasema

‘Mimi nimeharibu kwa vipi shemu...?’ nikamuuliza

‘Wewe unawatangazia watu kuwa  mimi ndiye niliyekupiga kichwa....kweli si kweli...?’ akaniuliza sasa akinikazia macho, awali nilikuwa nikimuogopa sana huyu jamaa, lakini ikafikia mahali nikaanza kumzoea,..kwahiyo hapo sikujali, nikamkabili, japokuwa siwezi kupambana naye kimabavu.

'Nimemtangaza nani kuhusu hilo, wewe usiwe unasikiliza majungu watu,..ilivyo, hata taarifa ya polisi inasema dada yako ndiye aliniumiza...’nikasema, na jamaa akabenua mdomo kwa dharau.

'Sikiliza, najua wewe na mimi hatuivani kabisa..., na ukiona mimi nimefanya jambo la kukusaidia, ujue kuna gharama, na gharama yake ni kubwa sana...,’akasema na nilikuwa nalisubiria hilo.

'Natakiwa nikulipe shilingi ngapi..hata hivyo ukumbuke mimi ni shemeji yako....’nikasema

'Mjinga mkubwa wewe, wewe moyoni mwangu sio shemeji yangu, kabisa kabisa..., natamka hilo unielewe, na najua unanielewa hivyo...mengine ninafanya kwa heshima ya dada yangu...’akatulia akikunja uso , niliona kama ana sikitika.

‘Mimi  niliapa sitakutambua wewe kama shemeji yangu, kamwe,..nitafanya hivyo tu, pale dada akiwepo, kumridhisha yeye...sasa wewe unataka gharama si ndio hivyo,...haya, je nikikuambia nataka nyumba yako utasemaje..’akasema akitizama miwani yake aliyokuwa kashikilia mkononi.

'Shemeji, huko unapokwendsanaa ni mbali...’nikasema nikihis mwili ukinicheza cheza..nilijua tu, huyu jamaa kalenga jambo.

'Mimi eeh, nimekwenda mbali sio.., najua utakuwa mgumu kwa hilo......sasa kipi bora, nyumba yako ipigwe mnada kwa ajili ya milion chache ulizokopa au...nichukue mimi hiyo nyumba, halafu nipambane na huyo anayekudai,...na dada angelikuwepo, ningewachia muishi,humo, lakini kwa vile...’hapo akatulia.

'Siwezi kufanya ujinga huo, unajua thamani ya ile nyumba,...hahaha, eti ipigwe mnada, kwa deni gani hilo,....hata hivyo, mimi nitamlipa huyo jamaa pesa yake...’nikasema

'Hahaha, wewe mpuuzi, kweli kweli, sitamani hata kukuita shemeji, hebu niambie kwa hali yako, wewe utapatia wapi hizo  pesa, kapuku kama wewe , dada yangu mjinga kweli kweli, sijui alipumbazika na nini kukubali wewe uwe mke wake,..’akakohoa
 Mfululizo, nahisi mate yalimkoholeza.

‘Dada kuolewa na masikini kama wewe ni kosa kubwa sana... wewe hujui tu, ...wakati nyie mumeishiwa kabisa, mimi ndiye nilikuwa nawalisha, sikutaka dada yangu akuambie hilo ila leo nimekuambia ili uelewe kosa ulilolifanya...kiukweli mimi nampenda sana dada yangu, na sikutaka apate shida...’akatulia kidogo

‘Lakini sio kweli, angeliniambia ...’nikajitetea

‘Hivi wewe hukuwa unaona ajabu, ukirudi nyumbani unakuta  chakula kipo, wakati hujaacha hata senti moja, ulifikiri mke angelikula wapi, wakati hukutaka hata aende sokoni, eeh...usitake niseme mengi..’akasema hivyo

Kiukweli, kipindi nimekwamba kabisa, kuna wakati nikrudi nyumbani nikiwa sijaacha chochote, bado nakuta chakula, ...na kila nikitaka kufunua mdomo kumuuliza mke wangu najikuta nashikwa na kigugumizi,ungesema nini tena, huna kitu, nilijua ni jitahada za mke za hapa na pale, ...sikufikia kumdahani mke wangu vibaya...ila  nilishafikia wakati, nilitaka nimuulize...bahati mbaya ndio yakatokea haya ya kutokea.


‘Sasa shemu, nilitumai wewe umewahi kuja hapa jela, kwa nia ya  kunisaidia mimi nitoke hapa, hapa sio sehemu nzuri, na natakiwa kufuatilia maswala ya...ooh, hata sijui kinachoendelea,..sasa wewe kumbe  umekuja kuniongezea maumivu tu, huo ndio ubinadamu gani shemu,?’ nikauliza.

‘Hahaha, mimi nije kukusaidia wewe,...kama ningelipewa nafasi, ya kukufanya chochote,mimi ningekukata kata vipande niwe nameza nyama yako..na kuitema, mimi nakuchukia, unajua kuchukia, we acha tu, lakini siku zinahesabika ..utakuja kuona ..’akasema kwa sauti ya kibabe.

‘Lakini kosa langu ni....’ kabla sijamaliza, akaendelea kusema;

‘Na nikuambie ukweli... kama ingelifaa, mimi ninataka wewe wakufunge ufie huko huko jela,..hapo ndio moyo wangu utatulia, lakini kwanza, kabla hujaenda kuzimu..nataka unilipe..na malipo yangu, kama nilivyokuambia, ...’akatulia.

‘Kuwa ....’nikataka kuongea anakiniashiria kwa mkono ninyamaze kwanza

Nimeshakuambia...nataka nyumba , hilo sikutanii...mimi nitakuja na hati ya makubaliano, ..la sivyo, jamaa mwenye deni atakuja kwako...unamjua alivyo...na ukumbuke yeye anajua mengi kukuhusu wewe...si niliwahi kukugusia,...anakujua fika, kuwa wewe ni muuaji, ..lakini nilikudhamini mimi...’akasema.

‘Sasa kwanini wewe ulinidhamini...?’nikauliza sasa kwa mashaka, maana niliona kweli huyu mtu alinitega.

‘Hahaha, bwege mkubwa wewe..nilishakuambia, mimi siwezi kukufanya jambo kwako lenye manufaaa na wewe..., maana wewe ni nani kwangu, muuaji mkubwa wewe, usitake ni badilike hapa, ..’akanisogelea, nilijua kichwa kinakuja nikakwepa hewa.

‘Hahaha, unakwepa nini sasa, mimi sio mjinga,... hapa siwezi kukufanya hivyo, ila ujue jambo moja, wewe na mimi, ni kama mafuta na maji, eeh, na ,...utajuta kuzaliwa kwa ulichomfanyia dada eeh...sijaanza malipizo yake bado...’akasonya.

‘Lakini ..eeh ili twende sawa, niume na kupiliza...fanya nilivyokuambia,...na unaweza kuona utanivunga, au utasita kukubaliana na mimi...kwanza ukumbuke, mimi ndiye nilitoa kauli ya kukusaidia,..lakini ile ni kauli tata,....bado haina mshiko, kuwa, nilisema hivyo, kuwa dada yangu alikupiga,..hiyo haina mshiko saana, ...’akawa ananichoma choma ni kidole kifuani.

‘Mimi naweza kuitengua hiyo kauli wakati wowote..kumbuka jela kulivyo...eeh, uliponea tundu la sindani, unakumbuka, eeh...sasa kule ni cha mtoto, huko..Ukonga, kule wapo jamaa zangu wengi tu, tunajuana...usijali kwa vipi..., nilishawatipu, ukikanyaga tu pale Ukonga, wewe ni chakula chao, utashindwa hata kutembea..hahaha...’akasimama na kuanza kuondoka.

Nilibakia nimeduwaa...maana nimjuavyo huyu jamaa hana utani, akisema jambo, hatanii....nitafanya nini sasa, dada yake wa kunitetea ndio hivyo hayupo,..jamaa aliponiona nimeduwaa, akarudi na kuanza kunipiga piga begani kwa ngumi kama kunipa moyo, lakini upigaji wake  unahsi  maumivu...nikawa najaribu kuukwepa huo mkono.

‘Sikiliza hii ni dili, hati inakuja,..tena sio kesho leo...na jiulize ni kwanini hadi sasa hujapelekwa Ukonga, eeh...jibu unalo, si ndio hivyo, mimi natoka hapa, nakwenda kwa mwanasheria wangu, keshaikamilisha hiyo hati,..nikirudi tutaelewana, ..’akahema kidogo.

‘Shemu,....’nikataka kusema neon, jamaa akanitolea macho,...halafu akasema;

‘Hata hivyo, wewe una thamani gani..ulitakiwe ufe...nyumba ile ni yangu kwa hivi sasa,..na mimi nitamlipa huyo anayekudai, unasikia, mengine niachie mimi...natumaii umenielewa, mimi sitaki longo longo...unanijua nilivyo..’akaanza kuondoka.

 Kabla hajafika mlangoni, mlangoo ukagongwa, jamaa akavaa miwani yake kwa haraka, mlango ukafunguliwa, mtu wa jamii akaingia, nyuma yake yupo mtu wa dini. Nilifahamu huyo ni mtu wa dini kutokana na mavazi yake, ..moyoni nikasema, huyu mtu wa jamii hana la kunisaidia, yeye kaenda kunileta huyo mtu wa dini  ili aniombee..kuombewa kwa hivi sasa kutasaidia nini kwa hali kama hii.

‘Hapa ninakabiliwa na kesi ya mauaji...na huyu shemu sasa hivi tu, kaniletea janga jingine, anataka nyumba iwe yake kitapeli,..nitafanyaje sasa...nyumba ndio mali yangu pekee ya kujivunia, kiukweli ni nyumba nzuri, na niliijenga kwa gharama kubwa sana...’nikawa nawaza hivyo.

Shemu akasita kuondoka akawa kasimama, na mtu wa jamii, akamsalimia ..lakini shemu hakuitikia hiyo salamu, jamaa akawa kama kashikilia mlango, lakini akawa kasimama tu.

‘Nimekuja, ..kuanza kazi, ..na..huyu ni mtu wa dini, kuna mambo nataka atusaidie,..nikuulize jambo moja,.’akasema mtu wa jamii, kwanza akageuka kumuangalia shemu, shemu akajifanya kama anataka kufungua mlango, lakini hakufanya hivyo kwa haraka.

‘Umeshapata taarifa yoyote, ya kuhusu mkeo, ..je kuna taratibu zozote, maana nijuavyo mimi , nilivyosikia,..mwili wake umehifadhiwa, sehemu ambayo haitakiwi kuonekana...’akasema mtu wa jamii.

‘Mwili wake una maana gani kusema hivyo...?’ nikauliza sasa kwa mashaka, ujue kukweli kuna hisia mbili akilini mwangu, kuna hisia ambayo, bado inatamani kuwa mke wangu bado yupo hai, nyingine inahisi kuwa mimi nimemuua mke wangu.

‘Ina maana huna taarifa hizo, au...?’ akasema mtu wa jamii, sasa na yeye akionyesha wasiwasi Fulani hivi.

Sasa sauti ikatokea mlangoni...

‘Una unakika na unachokisema wewe, ni nani wewe kwanza, wa kumuongelea dada yangu, eeh..mwili, mwili, .....?’ ilkuwa sauti nzito ya shemu, na sasa alikuwa anakuja kukabiliana na mtu wa jamii, sote tukabakia kushangaa,  tukawa tunamuangalia tu..nilitaka kumuambia mtu wa jamii awe makini, maana huyo jamaa kichwa kinamtoka kama mshale..


WAZO LA LEO: Tuweni makini na mikataba tunayoandikishana, hasa ya madeni,na ikiwa ni lazima kuandikishana hivyo, tuhakikishe tumepata ushauri wa mawakili, kabla hatujaweka sahihi zetu,..kwani sio kile anayekuchekea, ana furaha na wewe.
Ni mimi: emu-three

Wednesday, October 23, 2019

CHUMA ULETE 2


‘Chuma ulete...!..’nikang’aka. Na msimuliaji wa hiki kisa akatabasamu japo uso ulionekana na huzuni, na alikaa kimia kwa muda.

‘Una maana gani au ndio hizo imani za watu kuwa,...’ nikamuuliza pale nilipoaana yupo kimia.

'Ndio,...chuma ulete... ndivyo alivyoniambia hivyo mke wangu, mke ambaye awali hakupenda kabisa imani hizo za kishirikina,...uchawi tuseme...kiukweli nilishangaa kidogo, kwani awali hakuwa akiamini mambo hayo..'akasema, na kutulia kidogo

'Nikajaribu kumuasa mke wangu kihekima na kiimani, unajua tena...eeh...kuwa uchawi upo sikatai, lakini ukimuamini mungu, ukamuomba yeye, bila kuweka nafsi ya shiriki, huwezi kushindwa jambo..’akasema.

‘Na nikaendelea  kumuasa...’

''Mke wangu, tusiamini sana hayo mambo maana ukiyaamini sana hayo mambo, mwisho wake utaingia kwenye shirki, na imani yetu haitaki hivyo, ...nikamwambia mke wangu’’.

Awali alijifanya kunielewa, lakini mambo hayakuendelea hivyo....’msimuliaji akaendelea kuongea, na alipofika hapo alitulia kidogo.

'Kwa vipi...kwani kulitokea nini tena zaidi...'nikauliza sasa nikiwa na shauku zaidi.

'Sikuacha kumnasihi, mke wangu, nikijua kuwa mimi ndio  mume wake, na mimi ndiye kichwa cha familia,  unasikia sana...’akasema.

‘Sawa kabisa...’

‘Lakini..eeh, ndugu yangu wee, kumlea mtu mnzima ni kazi sana..ni mpaka yeye mwenyewe akubaliane na wewe...moyoni nikadhamiria kutumia nguvu japo kidogo.., mimi najua wengi watanilaumu sana kwa hilo, unajua ni kwanini nilitaka kufanya hivyo, kwa akili yangu, niliona bila hivyo, hataweza kuachana na ushetani huo...sumu ya ushetani, ilishapenyezwa kwenye ubongo wake,..’akatulia.

‘Sijakuelewa...’nikasema.

‘Yule mke niliyemuamini...ambaye nilikuwa namuasa jambo, ananisikia kwa unyenyekevu. Yule mke mpole, mwelekevu, hakuwa yeye tena, najuta kwanini nilimpatia nafasi hiyo ya kujichanganya...nahisi tamaa za nafsi na ushawishi wa mashoga, vilishamteka nafsi yake...’hapo akahema kwa nguvu.

‘Ndugu yangu makosa yaliendelea kujirudia, kidogo kidogo,akawa sasa haambiliki,hata kauli zake zikawa za kijeuri jeuri hivi, japo sio kwa moja kwa moja...kila hatua akawa ananipandisha presha...'akaendelea.

Niliumia sana..ilifika mahali naanza kukata tamaa, nilimpenda sana mke wangu, sikupenda abadilike, sikupenda, nije nianze kutumia nguvu, maana naogopa...naogopa sana kupiga,...naogopa sana, najijua nilivyo, nikianza..sirudi nyuma, nina hasira za mbali lakini zikipanda, ooh, ndugu yangu...sitaki kuua tena...’akasema na kushtuka, nahisi hakupenda kutamka hivyo.

‘Kuua tena, ina maana uliwahi kuua...?’ nikauliza kwa mshangao.

‘We acha tu, hayo yalishapita....samahani kwa hilo, limetoka tu..sija-jawahi..ku-kua bwana...’akasema sasa kwa kusita sita.

***********

Kisa kikaendelea....

Haikupita muda, hali ikaanza kubadilika, maisha yakaanza kuwa magumu, biashara haziendi , pesa haikamatiki...sikufichi,...kuna wakati imani ikaanza kushuka, maana unaambiwa mengi,..wanakushauri wengi..fikiria kutoka maduka hadi...genge la nyanya mbili tatu, na...ikawa mbaya zaidi ya hapo, hata ingelikuwa ni wewe....ila,  hata hivyo, sikufikia hatua ya ...kuamini maneno ya mke wangu...’akatulia kama anawaza jambo.

‘Maneno gani...?’ nikauliza kama sijui.

'Umasikini ni mtihani ndugu yangu, ...tatizo sasa ikawa kwa  mwenzangu yeye anaendelea kudai matumizi tu, hata pale ninapomwambia sina kitu na wakati mwingine anafikia hata kunikasirikia,..na kuanza kutoa maneno ya kashfa...sikupenda hilo....maana alivuka mpaka...’akaendelea bila kujali swali langu.

'Mke wangu hali unaiona, na mitihani hii ni kawaida kwenye familia, awali ulikuwa unavumilia nakueleza kitu unanielewa,... hivi nimekosea nini mke wangu, kosa langu mimi ni kukupatia uhuru, au...?’ nikamuuliza.

‘Hapana mume wangu, nahisi kosa ni la kwangu mimi....kukuambia ukweli...’akasema

‘Ukweli upi...?’ nikamuuliza.

‘Aaah..sitaki tena kuongea...maana wewe ndio mume...nitasema nini tena mbele yako, nina nini tena mtoto yatima,...wewe ndio baba, wewe ndio mama yangu...’akasema.

‘Nahitajia ushauri wenye tija, sio imani haba na mambo ya kuambiwa..’nikasema.

‘Nikushauri nini tena mume wangu, ushauri wangu nilishakuambia,..kwanza nilikuambia tujiunga na michezo ya kupeana, hukukubali, ..na..na hali hii ambayo nimeshaiona, wewe hutaki kuniamini..mume wangu tatizo lipo humu ndani...’akaniambia na kabla sijamkatisha akaniambia

‘Najua unanidharau, kwa vile ni mwanamke,..sio vibaya,...lakini ..mmh,...mimi  kuna mambo nayaona, ila wewe hutaki kuniamini....utakuja kunikumbuka kwa hili...’akasema kwa sauti ya unyonge.

‘Una maana gani...?’ nikauliza sasa nikimuangalia kwa mashaka mashaka.

‘Mume wangu, u-meingiliwa na chuma ulete...fanya haraka kabla hali haijawa mbaya...’akasema sasa akishika kichwa na kuangalia huku na huku kama ana wasiwasi ...na ile hali ya kukuna kuna kichwa, kama kinamuwasha ikanipa mashaka.

‘Nini.....’nikang’aka hivyo, nikimuangalia kwa kumkagua akijikuna kuna kichwani.
Kiukweli hadi hapo mimi  nilishaamini, mke wangu sio mwaminifu tena...nilimuona kama anajifanyiza tu, kunivunga mimi.

  Unakumbuka nilivyokuambia awali, huko nilipomtoa mke wangu, sifa yake kubwa ni uaminifu...hadi hapo niliona ni uwongo, labda ...walinidanganya...... awali ilikuwa hivyo sio sasa..na hebu niambie, hata kama ingelikuwa ni wewe..ungefanya nini hapo, maana sio mara moja, au mbili...imekuwa ni kawaida,..’akasema akiniangalia mimi usoni.

Hapo sikuwa na jibu la kumuambia, nikasubiria aendelee...

**********
Unajua tena, katika kuishi na watu unaweza ukawa na marafiki, na kati ya hao, ikatokea mmoja au hata wawili ukawaamini, japo mimi nina hulka yangu, sio rahisi kumuamini mtu,...hasa kwenye maswala ya imani, msimamo wangu ni thabiti.....kuna rafiki yangu mmoja, muungwana, ana busara sana, siku moja nikaongea naye nikitaka ushauri kwake.

‘Ndugu yangu kabla hujaanza kuingia huko, kwenye hasira, mkaja kukosana wewe na mke wako, hebu fanya uchunguzi wako wa kina..yawezekana tatizo lipo humo humo ndani, au...majirani,..siwezi kukupinga, au kupinga mawazo ya mkeo, maana hayo mambo yapo....’akanishauri.

‘Yawezekana tatizo lipo humo humo ndani kwa vipi...?’ nikauliza hivyo.

‘Yaani...yawezekana...ila...uchunguzi kwanza, usiwe na papara...’akasema.

‘Unajua ndugu yangu, mimi nimefanya kila uchunguzi, sijawahi kuona dalili ya kumshuku mtu baki, na nikuambie ukweli nyumbani kwangu watu hawaingii mara kwa mara, wananiogopa...’nikasema.

‘Sawa....lakini ...’nikamkatisha.

‘Ninasema hivyo kwasababu..mke wangu nilishamkanya,..sitaki majirani waingie ndani, mimi naafahamu sana majirani wangu...kwahiyo, kama ni kukutana na hao watu watakuwa wanakutana huko huko nje hasa  hao mashoga , waliomuharibu akili yake...mimi sina mfanyakazi wa ndani au ndugu ninayeishi naye, ni mimi na mke wangu tu...’nikasema.

‘Kwahiyo shaka yako kubwa ..ni kwa mke wako..si ndio hivyo..?’ akaniuliza.

‘Siwezi mshuku mtu wa nje..sijui unanielewa hapo...shuku itakwendaje nje kwanza, eeh... pesa ipotee humo humo ndani...na nipo mimi na mke wangu, nitamshukuje mtu wa nje kwa vipi, mlango haujavunjwa,...sijui unanielewa hapo....’nikasema kumuamboa huyo rafiki yangu.

‘Basi...vuta subira..ngoja nilifanyie hilo kazi rafiki yangu..’akaniambia huyo rafiki yangu. Kwa pale, sikuelewa, atalifanyiaje kazi, hata hivyo sikutaka kumdadisi, nikaachana naye...maana akili ilikuwa na mikakati mingine ya kibiashara.

***********

Siku moja  nikarudi nyumbani mapema....nilikuwa na pesa nimekopa mahali..., kwa ajili yakuanzisha biashara tena.., niliona nianze mtindo huo wa kukopa na kurejesha, labda nitafanikiwa, japo nianze kidogo kidogo.

Nilishapanga bajeti yangu vyema, iliyobaki ni kununua vifaa na kuingia sokoni,..kiukweli nilishapanga nitoke, kihivyo, ...na ndoto nyingi za Alinicha ziliuteka ubongo wangu, si unajua tena, ukikwama, na ukaja kuzishika pesa, ...mmh, akili inakuwa na mengi sana.

Pamoja  na shauku ya biashara,...bado  mwili ulikuwa hauna nguvu, sijui kwanini siku ile ilikuwa hivyo, na hali ile..ilinianza pale nilipozishika hizo pesa, nahisi hivyo.....maana hata kula sasa kulikuwa kwa shida, mawazo mengi kupitiliza.

Nikafika nyumbani...sikumkuta mke wangu, nikajua katoka kidogo, nikavua koti langu, nikatundika kwenye kabati la nguo...sikuwa na shaka, kwenye lile koti ndio niliweka pesa, nikajilaza kitandani...sijui usingizi ulitoka wapi, ...mwili ukalegea,...sijui nielezeje, nikashikwa na usinginzi mnzito ajabu,...nashtuka nasikia mke wangu anaongea nje...anaagana na mtu.

‘Kwaheri ...’

‘Kwaheri...’

Mimi kwa haraka  nikashtuka nikikumbuka natakiwa kwenda kununua bidhaa muda umeshapita, hata sijui kama nitakuta maduka ya jumla yapo wazi..sikukata tamaa, na sikupenda nilale na hizo pesa ndani, nikiogopa hayo yanayoendelea, hapo ilishafika jioni kama saa kumi na moja hivi.

Nikachukua koti langu,..nikavaa, wakati navaa,  mke wangu akaingia, aliponiona akashtuka, na kusema;

‘Oh, la azizi wangu umerudi mapema leo....,vipi kuna tatizo, sikujua kaam upo humu ndani.. kumbuka kauli hiyo,...’

‘Ndio mke wangu,...ume-rudi saa ngapi...?’ nikauliza, na kbla hajanijibu nikasikia mtu anagonga mlango.

‘Ni nani tena, kwanza sikiliza ,maana nimechelewa, nataka kutoka, nikirudi tutaongea vizuri..’nikasema,

Mke wangu akatulia akinisikiliza huku mtu anayegonga mlango anaendelea.

‘Sasa sikiliza....chukua pesa hii ufanye fanye mambo, japo ni pesa ya kukopa, lakini aheri, ntoe kidogo, tule chakula kizuri leo japo kidogo...au sio mke wangu’nikasema sasa naingiza mkono mfukoni kutoa pesa,..mkono ukazunguka kwenye mfuko wa koti...moyo ukaanza kunienda mbio, siamini.....


WAZO LA LEO: Tusiwe na tabia ya kuzania dhana mbaya, kabla hatujafanya uchunguzi wa kutosha,..dhana mbaya, hupunguza imani moyoni.
Ni mimi: emu-three

Saturday, July 6, 2019

HUJAFA HUJAUMBIKA...



'Hivi kwanini mimi,...., nimemkosea nini mwenyezimungu...'nilisikia suti hiyo ya huzuni na kunifanya nisimame ghafla, na kunifanya nisite kuendekea na safari yangu, nilihisi mwili ukinisisimuka...'nimemkosea ni mwenyezimungu...' kauli hiyo ilinifanya nigeuze kichwa kuangalia kule nilipohisi sauti hiyo imetokea.

'Oh Mungu, nimekosa nini mimi jamani mpaka nipitie majaribu yote haya, ..mungu wangu naomba unionyeshe tu njia...'maneno ya huzuni yaliendelea wakati huo nimeshageuza kichwa kuangalia sauti hiyo inatokea kwa nani.

Kwa sauti tu,nilihisi ni sauti ya mwanadada, lakini macho yangu yalipotua kwa huyo ninayehisi kuwa ndiye aliyekuwa wakiongea, niligwaya.

Alikuwa binti mdogo sana, tofauti na nilivyodhania.

Kwanza kwa tahadhari nilitembeza macho huku na kule..maana dunia hii imegauka sivyo ndivyo, ya walimwengu ni mengi... kuna mitego mingi ya wahalifu inafanyika hivyo, unajitoa kwa wema unaangukia kwenye mitego ya hao watu, wanakudhuru au kukunyanganya kila na kukuacha uchi. Ila kilichonitia matumaini ni kuwa eneo hilo lina nyumba za watu, na nyumba nyingi ni kubwa zenye ukuta, na wengi wameweka nyaya za ulinzi, kuashiria kuwa wanaoishii humo ni watu wenye uwezo wao.

Niliangalia eneo lile alipokuwa huyo binti..nyumba hiyo kama nyingine ilikuwa na ukuta mkubwa tu na, ..juu yake ilionyesha kuna ulinzi wa kitaalam, ..nikajiuliza huyo binti anafanya nini kwenye eneo hilo, ..hajui kuwa nyumba hiyo ina ulinzi, na wenye nyumba hiyo hawatakubali watu kukaa eneo hilo kiusalama...na kwanini kakaa hapo, na anamlilia nani..

Nilipoona nazidi kutingwa na maswali, ....nikaamua jambo, nikavuta hatua moja, mbili....kabla sijafika pale alipo huyo binti,...na ukumbuke kwa muda huo, bado alikuwa akiongea kwa kulalamika kuhusu masahibu anayokumbana nayo...

Mwili uliendelea kunisisimuka, na hii ni kuashiria kuwa kuna hatari,...mimi nina hisia hizo, mwili ukinisisimuka, ujue kuna jambo la hatari ...lakini nafsi haikunipa uwoga, nafsi ilinipa ujasiri, kuwa nahitajia kujua, nikijua nitajua la kufanya...nikawa sasa navuta hatua, ...

'Ewe mola wangu, nionyeshe kosa langu, hadi nitaabike hivi...nimekuwa mtumwa wa walimwengu, wananichezea kama mpira wa karatasi, naadhirika, na hata wale niliowategemea kuwa watakuwa msaada kwangu wanageuka kunidha....dha...lilisha...'hapo kwikwi ya kilio.

Hapo na mimi nikasita mguu ukawa mnzito kuendelea ...nikatulia kwanza, akilini nikichanganua, je haya ni yangu, ..yasije yakawa maji mazito kwangu, ..aah, nikajipa moyo, ..ngoja nikasikia kwa kulikono,...nikaendelea kutembea...na sikuvuta hatua mbili, mara nikasikia...

'Mimi  ...siwezi tena..bora nife ..bora nijiue.'

Mungu wangu, bora nijiue...

Hapo sikuweza kusubiria, nikahisi nina dhamana, hii ni dhamana maana ni kwanini mola akanifanya niweze kuyasikia hayo, na ni kwanini, niache kiumbe kama huyu ..binti mdogo tu, aje kufanya, hilo alolodhamiria,na ni mashahibu gani yamemkuta hadi kufikia kudhamiria hivyo. Nafsi ikaingiwa na mshawashwa,..ikatamani kujua,...

Nikamsogelea,,,,.

Hata pale niliposegea hadi kumkaribia, bado alikuwa hajafahamu kuwa kuna mtu alikuwa bado hajafahamu kuwa mimi nipo hapo karibu yake, na hata kabla sijaweza kutoa sauti ya kumsalimia huyo binti , nikasikia sauti kali ikitokea ndani mwa hiyo nyumba, ambapo huyo binti kajiegemeza ukutani mwake.

'Huyu mshenzi kaenda wapi....we Taabu, ...we Taabu,...' sauti hiyo ilimfanya yule binti akaurupuke, na kusimama, hapo akaniona, akashika mkono kuziba mdomoni, lakini ...

'Usigope mimi sio mtu mbaya
'Ina maana umesikia nilichokuwa nikiongea
'Hapana...sijui uliongea nini...'nikasema
'Mungu wangu ..'akasema hivyo tu na haraka akakimbilia ndani

Kesho yake nilipita eneo hilo tena, nia ni kukutana na huyo binti, nijue ni nini kinachoendelea kwenye hiyo nyumba, nilipofika hapo nilikuwa watu wamejikusanya
'Kuna nini jamani...?' nikauliza
'Kuna binti kataka kujiua,...'akasema
'Kwanini
'Hata sisi tumebakia kujiuliza tu, na wenye nyumba hawataki kuelezea ukweli, wanasema hata wao hawajui
 Mara nikaona gari la wagonjwa likitoka, ..nikajua watakuwa wamemuwahi, ...
'Akipona ashukuru mungu...'ilikuwa kauli ya askari mmoja aliyetoka kwenye hiyo nyumba
'Kwanini unasema hivyo?'
'Sumu aliyokunywa ni kali sana...na walichelewa kutoa taarifa...'akasema askari

Kiukweli niliumia sana, ni kwanini sikufanya jitihada za ziada kukutana na huyo binti, nikasema na hata hivyo sikukata tamaa, nikafanya utafiti kujua huyo binti kapelekwa hospitalini gani, na wakati nauliza uliza ndio nikakutana na mama mmoja aliyesema anamfahamu huyo binti tokea akiwa mdogo.

'Sasa kwanini kakimbilia kutaka kujiua...?' nikauliza

'Mhh...we acha tu, hujafa hujaumbika, usilolijua ni sawa na kiza cha totoro...yule binti kapitia masahibu mengi, na huwezi amini huyo anayeishi naye ni mama wa kambo, mama yake alishafariki....

NB: Bado tupo kwenye maajribio, ili tuweze kurudi tena.

Ni mimi: emu-three

Thursday, October 11, 2018

CHOZI LA KUTOKA MOYONI-2


‘Ndugu yangu liogope chozi la kutoka moyoni…hili ni chozi la huzuni, chozi la majuto, chozi la kukosewa, chozi la kulalamika…huwezi kulitafsiri, maana linakuja tu..na huja kwa jambo maalumu sio hivi hivi tu..kwa aliyezoea kulia, …hili sio chozi lake..’aliendelea kunihadhithia rafiki yangu.

Hiki ni kisa cha kweli kilichonitokea mimi na familia yangu...’akasema huyo rafiki yangu anayenisimulia kisa hiki....

‘Unajua mimi sikupenda kuyahadithia haya, lakini nataka mlione chozi la namna hii linavyofanya kazi yake maana sio chozi la kawaida,…na  nakuhadithia hiki kisa, sio kwa nia ya kuwalaumu hao walionitelekeza, huenda walifanya hivyo kwa nia ya jinsi walivyoona ni sahihi kwao, ila maamuzi hayo yalitoka kipindi ambacho niliwahitajia sana…maana nilitarajia mengi  baada ya kuwafanyia kazi zao kwa kujitoa kwa moyo wangu wote, na nini walikuja kunilipa sasa,…

'Malipo yangu ndio hayo kuwa mimi sihitajiki tena....'akasema

'Pole sana...'nikamwambia 

‘Yote namuachia mungu…’akasema na kutulia.

'Hebu sasa niambie kwa kirefu, ilikuwaje kwenye hiyo kampuni hadi ikafikia hapo...?' nikamuuliza

Tuendelee na kisa chetu...

*************

 Kwa kuhadithia tu, mimi nilianza kufanya kazi kwenye kampuni hiyo, ikiwa na mapungufu mengi tu, na waliniita hapo kwa vile walisikia kuwa mimi ni mtaalamu kwenye hiyo idara ...ni kweli na nilipofika hapo na kuyaona hayo mapungufu, nikaamua kutumia ujuzi wangu na uzoefu wangu kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa…na nilifanya hivyo nikijua huenda huko mbele kutakuwa na neema. Hayo ndio yalikuwa matarajio yangu.

Katika kuwajibika huko, niliweza kuokoa mamilioni ya pesa, pesa hizo hazikuwa zimejulikana, kutokana na mahesabu yao  na kumbukumbu zao, kutokuwa sawasawa, na bosi aliposikia hivyo alifurahi sana, nikajua labda tutapewa kifuta jasho (bonasi,..lakini haikutokea, sikukata tamaa, nikajua ipo siku.

Kazi zikaendelea, lakini kutokana na hali halisi ya mabadiliko, ya kinchi, nisema hivyo... ambayo sio kwa kampuni hiyo peke yake tu,…biashara haikuwa nzuri sana, kwahiyo kukawa sasa na tetesi kuwa huenda watu wakapunguzwa, mimi sikuwa na wasiwasi na hilo..., maana kama niliweza kuokoa mamilioni ya pesa, kwanini kampuni inipunguze mimi.

Ndio maana baada ya kupata taarifa hiyo, niliumia sana, niliumia kwa vile nilishafika mahali nikawa napanga maisha, nakopa huku na kule ili watoto wasome,..najua mwisho wa mwezi nitapata fungu langu, japokuwa lilikuwa lapatikana kwa nusu nusu...lakini unakuwa na uhakika hata ukikopa utakuja kulipa.. Sikujali, nilijua ndio hali halisi…

 Sasa kilichoniuma zaidi ni pale nilipopigiwa mahesabu ya nini nilipwe,..hapo ndio unaweza kuona jinsi gani haya makampuni ya watu binafasi yalivyo na dhuluma...

‘Wewe mwenyewe unaifahamu hali halisi, kwanza nilikuwa sijakuajiri, kweli si kweli... ulikuwa kama kibarua tu,…kwahiyo kutokana na hali halisi,...sipendi, unaonaee..nifaneje sasa, na sitaki uondoke mikono mitupu, etu usubiria mpaka nikijaliwa, lini sasa..kwahiyo mimi nimeona hivi.. tutapiga mahesabu yako ya mwezi huu…umefanya siku ngapi vile…’akajifanya kama hajui. Mimi nikabakia kimia.

‘Eeeh mwezi uliopita umelipwa pesa yako yote…?’ akauliza kama vile hajui hilo

‘Bado, …nimelipwa nusu mwezi…’nikasema kwa sauti ya unyonge, nimeshavunjika nguvu, nilikua kwa juhudi zangu nilizofanya, angalau...ningelipewa hata asante

‘Ok, sasa..tutachukua hiyo nusu mwezi ilibakia na tutaongeza na siku hizi za mwezi huu ulizofanya, tutakulipa,…nitahakikishe umelipwa hizo pesa zako, sitaki uondoke mikono mitupu…’akasema

‘Ina maana, ndio malipo hayo ya  mwisho…?’ nikauliza

‘Wewe mwenyewe si unaona hali halisi, nitakulipa nini, shukuru kuwa mimi nitafanya juhudi upate hizo…nusu mshahara uliobakia, na siku hizi za mwezi huu ulizowahi kufanya..na..kiukweli sikutegemea kuwa kazii hii itachukua muda wote huu, mimi nilitarajia utafanya miezi mitatu, ..tumalizane…’akasema

Sikutaka kusema lolote kuwa kama ningefanya hivyo anavyodai yeye, asingeliweza kuyapata hayo mamilioni ya pesa, nikabakia kimia, nikiumia kimoyo moyo..

‘Nitamwambia mshika pesa wangu akupigia mehesabu yako, na akulipe, lakini hakikisha kazi zako zote ulizotakiwa kufanya umemaliza…najua sina shaka na wewe, lakini kwa kukumbushia tu, sitaki mtu aondoke hapa kabla hajamaliza kazi zake,..na nitakulipa baada ya kukaguliwa kuwa kweli umemaliza kazi zako…’akasema

Sikuamini hayo maneno, ina maana kafikia sehemu ya kutokuniamini tena…moyoni nilitaka kumuambia, kama ungelinijua nilivyo, usingelisema maneno hayo, hata kama unaniondoa mimi nitafanya kazi yako yote…kimujibu wa taaluma yangu, ..ndivyo nilivyo, sina haja ya kuwa na kisasi na yeye.

Yaliyofuata hapo baadae huwezi amini, nilioanza kuonekana kama mtu ambaye naweza kuharibu kazi, naweza kuiba, naweza kufanya jambo na kukimbia,…sikuamini…

Haya ngoja turudi siku ile…ambayo, nilitakiwa nirejee nyumbani, nikutane na muuza duka,..siku ya kulipa ada..siku ya…mke wangu anategemea nitakuja na mkopo, ili aweze hata kuanzisha duka,…siku ambayo nilipewa hiyo taarifa kuwa kazi sasa basi.

*************
Siku ile naikumbuka sana, kwani ni siku ambayo….nilianza hata kuumwa maradhi ya moyo…

Wakati naondoka kazini, nilipanga nisipitie njia ile ya dukani, kama nitawahi kufika, kama nitafika maduka yamefungwa itakwua ahueni kwangu…na hata hivyo huko kwa dukani nikipita salama, nitakwenda kusema nini kwa familia yangu…kiukweli nilikuwa na wakati mgumu sana.

 Siku ile…, pamoja ya kutoka kazini kwa muda ule ule wa saa kumi na moja, cha ajabu siku ile usafiri ukawa ni rahisi,…hakukuwa na wingi wa abiria, nikapata gari, japo la kusimama, mwili hauna nguvu, lakini utafanya nini..tumbo halina kitu, ningelikula nini, wakati bajeti imebana.

 Cha ajabu siku hiyo nikafika nyumbani mapema sana, tofauti na siku nyingine…akilini nawaza nikifika nitaanzaje kumwambia mke wangu…mawazo hayo yakawa sasa ndio yameuteka ubongo wangu…unajua mkiwa mnaishi pamoja, unajau ni kitu gani uongee na mwenzako kwa wakati gani,…nilimpenda mke wangu na familia yangu sikupenda kabisa ije kuumia, nipo tayari kufa kwa ajili ya famili yangu.

Kwa jinsi nilivyotekwa na mawazo hayo ..ya jinsi gani ya kufikisha ujumbe huo kwa familia yangu,…, nilisahau kabisa lile wazo la kupitia sehemu nyingine kumkwepa mwenye duka, maana njia ya kufika nyumbani ni lazima upitie kwenye hilo duka, lakini kuna njia nyingine ya kuzunguka…wakati natoka kazini, nilipanga nipitie njia ya kuzunguka…lengo ku mkwepa huyo muuza duka.

Ndugu yangu, sio kwamba mimi ni muoga kiasi hicho, ila kiukweli huyo jamaa sifa zake za ukatili, zinajulikana sana, kwanza alikuwa jambazi, na…sio kwamba natania, ipo siku moja alishikwa mwizi, ..kwa macho yangu nilimuona jamaa huyu akionyesha unyama wake kwa huyo mwizi, aliyetaka kuvunja duka lake ili aweze kuiba, ilikuwa alifajiri mimi nawahi kazini

Walikuwa wawili mmoja akaweza kuponyoka na kukimbia, sasa huyu aliyeshikwa, ambaye alijiona ni mbabe, ndiye alikutana uso kwa uso na huyu muuza duka,…mwizi alikuwa mtu kashiba, ana miraba minne, na akaamza kukabiliana na huyu muuza duka, lakini hakuweza.

‘Huyu niachieni mimi mwenyewe, nataka niwaonyeshe kuwa mimi siibiwi..na hakuna atakyefanya hivi hapa tena….sitaki utani mbele ya mali yangu…’akasema, kwanza alikuwa na kisu akakurusha pembeni.

Mwizi kuona hivyo, akajua huyo muuza duka ni rahisi kwake, ,…wakaanza kutupiana ngumi na huyu mwizi kwanza mwizi alionekana kumzidi muuza duka, lakini hakuna aliyeingilia,..watu walikuwa wamesimama  pembeni.

‘Ukinishinda, umepona, ..nikikushinda umekufa….’akasema huyo muuza duka, kifua wazi, na bukuta la kulalia…bukta lake lina sehemu ya kuhifadhia kisu –ala.

Ikawa kila mwizi akipatwa na konde moja usoni, anabwagika chini,…anajizoa hara haraka, kawa sasa kama kalewa… watu wakawa wanacheka…mwizi gani kila ngumi anakwenda chini…lakini mwizi akawa anapmbana akijua ndio kupona kwake, kufa au kupona…

 Ikatokea wakati mwizi akarusha ngumi, mkono ukadakwa na huyo muiza duka, kwa jinsi alivyoshikwa tulisikia mlio wa kooo….mkono ukavunjwa na hapo hapo, huyo mwizi akarushwa hewani, alizungushwa hewani kama mzigo tu, na kubamizwa chini, na watu walishangaa huyu mtu ana nguvu gani ya kuweza kumbinua huyu mwizi hewani, mwizi ambaye kiumbile anamzidi huyo muuza duka…ilibakia historia.

‘Mimi sina huruma na pesa yangu,…pesa yangu ina thamani ya utu, ukinichukulia pesa yangu, umevunja utu wangu na mimi sitakuwa na huruma na utu wako..nitakumaliza tu…hilo nimeapa, sasa wewe  mwizi utakuwa fundisho hapa mtaani, nitakuonyesha kile ambacho watu hawakijui kunihusu mimi…’akasema

Huyo mwizi anagugumia mkono umevunjwa, muuza duka akawa bado hajaridhika,…akasogea pale alipoweka kisu chake, akakichukua mwizi hata hawezi kuinuka, kukimbia, ..muuza duka akamrejea na kumshika huyo mwizi sikio akalikata sikio…

‘Hiyo kwanza ndio alama yako kuwa wewe ni mwizi, mimi nilikuwa jambazi, na jaambazi ukikamatwa ujue ni kifo, sasa mimi nimeacha, sitaki kuibiwa tena, wewe wataka nirejee kwenye wizi…’akasema

Na hapo hapo akakitumbukiza kile kipande cha sikio mdomoni akakitafuna..sasa sijui atakimeza au la,… kwa haraka ageuka kwa kasi ya ajabu, kile kisu, kikapita kooni kwa huyo mwizi, damu zikaruka,…

‘Aaah…’ mwizi akapiga ukelele.

Tukajua koromeo limekatika…bahati mbaya kisu hicho kilkwepa koromeo, kikakata sehemu ya koo … lakini kilifanya kazi yake ..mwizi yule akalala chini, anakoroma kama mtu anayekata roho.

‘Hufwi eeh,..umechafua kisu changu halafu hujafa… ngoja nikuone kama hutakufa…’jamaa akaingia dukani, na kuchukua chupa ya mafuta ya taa…mimi hapo  sikuweza kuvumilia tena…huyo, nikaondoka zangu kuwahi kazini..

 Nilipokumbuka hayo, nikajua huyu mtu hana mzaha kweli kwenye pesa yake, na kweli kwa maana kwa yoyote eliyewahi kumkopa akachelewa kumlipa pesa yake cha moto alikiona.., kwanza akija kwako utapokea  kipigo, na kipigo hicho yeye mwenyewe anakuruhusu upigane naye, halafu anachukua kitu chochote ambacho kinaweza kulipa deni lake,..

Sasa sijui mimi yatanikuta hayo au….kwahiyo sio kwamba niliingiwa na wasiwasi huo bure… jamaa huyo ana visa vingi, akipigana na mtu,..ngumi yake ikikupata lazima utaenda chini, yeye anadai, alishaambiwa asitumie mkono wake kupiga mtu, hasa wa kushoto..alishawahi kumvunja kaka yake mkubwa wake taya, kwenye ugomvi ugomvi

*********

Sasa ghafla bin vuu,..nikawa nipo maeneo  ya duka…nilishasahau, kuwa nilipanaga nitumie njia nyingine ili kumkwepa huyo muuza duka, ..mawazo ni kitu kingine kabisa, na ilipangwa tu , lazima nipitie hapo dukaniu.
.
 Nilipofika hapo , nikawa sina jinsi, nikasema moyoni potelea mbali, mungu atanilinda, nikasogea pale dukani, …sikumuona huyo jamaa, yupo kijana wake, ajabu mara nyingi huyu jamaa hamuamini mtu, nikajua labda yupo chooni, ..hata hivyo nikasema  afadhali.

Nilisema afadhali, ..sio kuwa nitakuwa namkwepa hivyo kila siku, nilikuwa na maana nahitajia kwanza nifike nyumbani,…, nipate muda wa kujipanga, jinsi gani ya kukabiliana naye,..najua ni lazima nionane naye ..hata hivyo akili ilikuwa imechoka sana..nilihitajia nikalale kidogo hadi kesho .

'Bosi wako yupo wapi…?’ nikamuuliza hapo kwa kujiamini kidogo.

'Katoka hapa sasa hivi…, anasema anawafuatilia wadeni wake, kakasirika kweli kweli…’akasema huyo kijana wake.

'Mungu wangu...'nikasema hivyo tu kuondoka pale dukani kwa haraka…, nikikimbilia nyumbani kwangu sio mbali sana na hapo dukani,…na hisia zangu, ni kuwa huenda familia yangu ipo chini ya ulinzi ya huyo jamaa au keshawafanyia kitu kibaya. Pamoja na kumuogopa hivyo, kama atakuwa kaifanyia kitu kibaya familia yangu, tutapambana…

Nafika eneo la nyumba yangu, nasikia sauti ya jamaa akifoka huko ndani, nikajua sasa..kumekucha, sasa naingia vitani, japokuwa nafahamu fika kupambana na huyo mtu siwezi lakini nitajitahidi …

Na kwa namna nyingine nikaona labda kuepusha shari, ni bora nirudi nilipotoka, nikakae sehemu hadi usiku ndio nirudi, lakini je hapo alipo hajafanya chochote kibaya, ikawa ndio wasiwasi wangu huo..

Nikawa sasa natamani nigeuke nirudi nilipotoka, na kabla sijafanya lolote la maamuzi yangu, mara mlango ukafunguliwa,  jamaa huyo katoka. Akaniona, au sijui hakuniona maana kilichofuata baadae ilikuwa ndio jibu halisi…

 Alipojitokeza pale malngoni, uso umebadilika kawa mweusi, …jicho limemtoka nikajua sasa napambana na simba…kurudi nyuma siwezi, kusogea mbele siwezi nikawa nimeganda, nasubiria kitakachofanyika

Jamaa huyu anakuja usawa wangu, nikawa nimejiandaa, huku moyoni nasema, kiukweli ilibidi iwe hivyo, kumuomba mungu, maana sikupenda iwe shari..,…

‘Mungu wangu nisaidie kwa hili, haya yote sio kwa kusudio langu. Je mimi sikutimiza wajibu wangu kazini,.., je mimi nimefanya dhambi gani hadi niondolewe kazini, nimefanya kosa gani hadi nije kuzalilika hivi…najua kabisa ningelikuwa kazini, haya yasingelitokea…naomba msaada wako, ewe mola wangu…’nilijikuta nasema hivyo tu, kwa hisia za ndani,..sijui ila nahisi ilikuja hali ya chozi kama lile la ofisini

Nilishangaa….mimi sina kawaida ya kutoa machozi…na niliona ajabu tukio hilo liniathiri kiasi hicho,…najiona nipo kwenye mabadiliko mengine makubwa.

Basi kwa muda jamaa alishafika usawa wangu…nikitarajia kipigo, najua nitajitetea, lakini najua kiundani siwezi kupambana na mtu kama huyo…

Ajabu kabisa jamaa akanipita kama hanioni,…upepo tu, nikayumba… sikuamini hilo…karibu anipige kikumbo, huyooo kwa haraka akawa anaondoka…

Mimi ilinijia kwa mshangao, sikumini kabisa kama jamaa huyo angeliliweza kunipita bila kufanya jambo, bila hata kunifokea…kwa vile sikuamini, taratibu  nikageuka kwa mashaka, kumuangalia kama kweli ndio anaondoka,...

Ile nageuka, kumbe naye sijui alikuwa akiwaza nini, naye kumbe akagauke, tukawa tumeangaliana, lakini kwa umbeli, alishanipita na kwa vile alikuwa akitembea kwa haraka ilikuwa ni umbali wa hatua kadhaa,..hapo ndio sijui, alikuwa hajaniona au..na kwanini alipogeuka alikuwa akainiangalia kama kushangaa vile…na alipogeuka tulikutanisha macho.
.
Hakusimama na wala hakurudi nyuma…

Ilipita dakika mbili hivi bado nimesimama, na akili iliporejea kwenye msimamo wake, ndio nikakumbuka kuingia ndani kuiona familia yangu…nikatembea kwa hatua za haraka haraka, kawaida nikifika nyumbani nagonga mlango kupiga hodi..

Sikufanya hivyo….nikasita kufanya hivyo, nikajikuta nasita hata kushika kitasa…nahisi mwili ukinisisimuka, …ni hali ngeni kwangu..hata hivyo, nikashika kitasa na kuzungusha , mlango ukawa wazi..

Ile natupa macho ndani, naangalia sakafuni, namuona mke wangu…na mtoto kasimam akiwa kainamisha kichwa…

NB….ILIKUWAJE…Ndugu zangu, nahis kama nisipopata kitendea kazi, kisa hiki na hicho kingine kitechelewa kidogo maana sehemu niliyoitegemea , nilipokuwa nimejishikiza sitakuwepo tena…mniombee tu, nipate sehemu nyingine.


WAZO LA LEO: Yakikukuta matatizo, shida , mitihani, kamwe usikate tamaa, wewe elekeza imani yako kwa mwenyezimungu, kwani yeye anatosha kukuongoza na kukusaidia kwenye hatua nyingine.
Ni mimi: emu-three