Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha (diaries), ikiwemo visa , matukio, mijadala na yale yote unayopenda kuwemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA

Tushirikiane ,tupendane, tusaidiane, tutafika tu

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/likes

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, September 19, 2016

KISA CHA BINTI YATIMA-'KWANINI MIMI...'-3


‘Siogopi kuyasimulia maisha ya baba yangu, …maana maisha yake yamekuwa ni funzo pale kijijini kwetu..alipewa majina mengi, mzee tupa tupa…mzee wa matumizi, havinipiti…nk…, kila mmoja amekuwa akiyatolea mfano hayo maisha yake…, hasa pale mzazi anapomuona mtoto wake anapotea, anakuwa mlevi, Malaya..au ana uchu wa madaraka, au kama hamtunzi mkewe, basi watu hutolea mfano kwa maisha hayo ya baba..kwahiyo hata nisipoongea mimi leo…, yameshaongelewa sana…mungu amsamehe tu baba yangu huko alipo…’akasema

Aliposema hivyo huyo binti, niliingia na hamu sana ya kujua maisha ya baba yake yalikuwaje japokuwa nia yangu ilikuwa ni kujua mambo yanayomuhusu huyu binti…kwani na muda nao ulikuwa hautoshi..

‘Kwani maisha ya baba yako yalikuwaje,...?’ nikamuuliza

‘Baba…mmh…we acha tu nyie wanaume ….sijui kama nitakuja kuwasamehe…’akasema

‘Usijali yote maisha…’nikasema

‘Yote maisha …hahaha..haya ya binti yatima yalizidi kiasi….maana ni kizalia…we acha tu…’akasema

‘Sawa hebu tugusie kidogo kuhusu huyo baba yako,…alikuwa chama gani vile…hahaha, hayo ya chama yaache, usije kuleta sintofahamu….hebu tuelezee alivyokuwa, ili tumfahamu, maana yaonekana chuki zako zimeanzia huko…’akasema jamaa mmoja.

********** tuendelee na kisa chetu*******

Kwanza binti aliinama chini kama anawaza jambo, halafu akainua kichwa na kuanza kuongea, alikuwa akiongea kwa haraka haraka, kama mtu aliyekaririshwa hayo maneno, na ilikuwa kama anaivuta hiyo habari kichani mwake, na kuiona mbele yake…

 ‘Baba yangu alikuwa mtu mkubwa sana enzi hizo, nikiwa na maana pale kwetu kijijini… unajua baba alianzia kuanzia kufanya kazi kwenye wizara..akiwa mkuruguenzi fulani.., akaja kugombea ubunge, akapata, baadaye akawa mkuu wa mkoa sijui akawa nani tena, kusoma raha…na ukiwa mjanja kwenye kuongea mdomoni, kushawishi watu baba alikuwa hajambo….

Lakini pamoja na hayo, watu wengi walimfahamu, kutokana na tabia yake, ya kujiona, na hata kunata kuwa, ana pesa, na ni kiongozi, amesoma, mtoaji imla, fanya, ni lazima ufanye, hata kama kuna sababu za msingi za kutokufanyika….ni kweli alisoma, maana niliwahi kuiona vyeti vyake,….alisomea hiki akamaliza , akaja kusomea hiki, yaani alikuwa kasomea nyanja tofauto tofauti….kiasi kwamba ilishindikana awekwe wapi…

Tatizo ni hilo, tamaa, kupenda ukubwa, na kutaka afanye apendavyo..kwasababu yeye si kasoma bwana, anajua zaidi.., na ikafikia sasa anatumia  mali ya umma kama yake…, unajua tena….lakini cha zaidi ambacho ilikuwa ni sifa yake, ilikuwa ni hiyo tabia ya kubadili wanawake kama nguo, madaraka yana mitihani yake…’akasema.

Hakujali kuwa ana mke,..na mama alikuwa mke mremboo tu, alikuwa na Tabia njema, mtulivu…kila mmoja alimsifia kwa tabia yake hiyo, na wengi walimsikitikia kwanini aliolewa na baba, wengine wakamzihaki kuwa kakubali kuolewa kwa ajili ya pesa…ndio hivyo…mama alishinikizwa na wazazi hakupenda,…na hakuwa na jinsi….’akasema

‘Sasa kwanini mama yako alikubali, au alilazimishwa…?’ akaulizwa

‘Hivi hamkunielewa,…..sirudii tena….’akasema kwa hasira

‘ok….sawa endelea…hakuwa na jinsi, …tunmekuelewa…’nikasema

‘Kwa tabia hiyo ya baba, mama hakutulia, alijaribu kumkanya baba kila awezavyo, lakini baba hakusikia,..na hata alifikia kumpigwa mama mara kwa mara, na akaambiwa kama hataki kuishi naye, njia ipo nyeupe aondoke kwao.

Unajua tena maisha ya kijijini, ukishaolewa, umeolewa,…mama ilibidi avumilie tu, lakini ikafika muda, mama akaamua kuondoka na kuachana na baba,…sijui kwanini mama hakuweza kusimamia kwenye uamuzi wake huo,…’hapo akatulia kidogo.

‘Angewezaje, …wazazi wa mama ndio akina mie..hawakuwa na uwezo ukilinganisha na familia ya akina baba, …baba yake naye ndio hao wazee wanaopenda kuwafanya watoto wao kama mtaji, kila kitu sawa bwana mkubwa, …na babu kila akiwa na shida, akitaka pesa za kulewea anamuendea mkwewe, hapo mama angefanya nini….lakini ikafikia muda mama naye yakamfika shingoni, akachukua furushi la nguo zake akaondoka.

‘Kwenda wapi…?’ akauliza mtu mmoja

‘Kwenda wapi…tatizo lenu nyie wanaume mkio, mnahisi kuwa mke hana pa kwenda, ukishamuoa ni mtumwa wako…. mama alikuwa na kwao, sema tu….ndio mfumo dume…mwanamke anachukuliwa kama hana kwao tena, yeye ni mtumwa kwako si ndio hivyo....nyie watu nyie…’akasema

‘Ndio maana huolewi, ukiwa na imani hiyo…’akaropoka mtu mmoja, na mdada akageuka kumuangalia, na mimi nikasema;

‘Wewe endelea usimsikilize huyo…..’ nikasema

‘Nyie acheni tu…..’akatulia kidogo

Kufika nyumbani anakuta ugomvi wa baba na mama…mama analia kivyake, babu anarudi kila siku mlevi, akirudi ni kipigo kwa bibi….mama akasimama mlangoni, akijiuliza afanye nini, arudi alipotoka au …..

‘Na wewe umefuata nini…’ilikuwa kauli ya babu akiwa bwiiii…

 Mama akajaribu kujieleza, lakini nani angemsikiliza, hata kama bibi alimuelewa mama…, lakini ni nani mwenye usemi hapo nyumbani, ni babu, na babu ndio huyo, mtumwa wa baba’ngu, baba yangu ndiye alikuwa mfadhili wa babu, kwahiyo kila alichosema mama hakikusikilizwa, mama akaonekana hana maana, akafukuzwa usiku huo huo arudi kwa mumewe.

‘Mama yako akarudi, mama yake hakumtetea…?’ akaulizwa

 ‘Bibi…hahaha hivi nyie mnawafahamu wazee wa zamani …waume kwao ni ….ni kama afande, amri moja,….bibi alijitahidi lkini wapi,…. mama akabidi arudi kwa mumewe…, ….angefanya nini, na aliporudi akakuta mlango umefungwa ikabidi alale nje, hadi mume wake aliporudi na hawara wake,…maana baba alijua mama hayupo, mama siku hiyo alilala chumba cha wageni, na baba alipogundua mama yupo akajivunga, akamrudisha huyo hawara wake wakaenda kulala , walipolala…uone ni kwanini nikukuambia nawachukia nyie watu msione nawaonea….’akatulia.

‘Bibi anasema mama alikuwa kama mtumwa, baba akirudi amelewa, anatapika ovyo, wakati mwingine anapitiwa na haja..si unajua tena walevi..basi mama kazi yake kumfulia nguo…yaani bibi akikuhadithia , utatamani ulie…lakini mama alivumulia, si mume wake bwana, na keshaambiwa na wazazi wake hakuna kurudi nyumbani ….’akatulia.

‘Sasa ilikuwaje bibi yako huyo, akaja kuishi kwa mama yako….?’ Nikamuuliza

‘Nitakuelezea ni kwanini…..’akasema

‘Basi mama akawa anaishi na baba hivyo hivyo, ikafikia hatua , baba anawaleta wanawake hadi nyumbani, haogopi tena…mama akaona imezidi akaenda kushitaki kwa wazazi wa mume…wewewe…ndio alijichongea,..huko ndio kukawa kubaya zaidi aheri hata kwao…kwanza alianza kuambiwa yeye ni nuksi, yeye ndiye kamuharibu mume wake, ikafikia hatua kuambiwa yeye ni mchawi…..’akatulia akitikisa kichwa.

‘Bibi yangu alikuja kuishi na wazazi wangu, baada ya babu yangu kufariki, babu alipofariki, bibi akafukuzwa kwenye makazi ya hiyo familia,..akawa hana pa kwenda, basi mama akamchukua waishi naye, baba hakupinga …na huyu bibi ndiye aliyekuja kuwasaidia sana wazazi wangu hasa kipindi baba anaumwa, yeye na mama wakawa wanahangaika huko na kule, hata kutafuta riziki…maana ndugu wa mume walipoona baba hana kazi tena, anaumwa, hawamkujali tena..’akatulia.

Bibi anasema baba enzi zake, alikuwa hawajali ndugu zake, ndio maana na wao walikuwa kama wametenga kifulani hivi…walisema baba ana majivuno,na zarau…na hakupenda kuwasaidia ndugu zake, hata hivyo, walimuheshimukipindi hicho  kwasababu ya pesa, na alikuwa kiongozi, …

‘Bibi anasema baba alianza kuumwa siku alipofukuzwa kazi….kwani kulipita uchunguzi wa wakaguzi hapo kazini, wakagundua kuwa kuna ufujaji wa mali na pesa kupotea, na mwisho wa siku wakasema baba ndiye aliyefanya yote hayo, akasimamishwa kazi.

 Siku baba alipopokea taarifa hiyo, akapoteza fahamu..na tatizo likaanzia hapo, sio kwamba hakuwa anaumwa kabla, alishaanza kuumwa umwa, magonjwa mengi tu, na alikuja kujijua tatizo nini…., lakini hakusema kwa mtu, akawa anaendelea na tabia yake ya kuwaharibu mabinti wa wenzake, lakini mungu hamfichi mnafiki

Siku ikafika,…muda mungu aliouweka wa mwanadamu ni mfupi tu… alipopokea taarifa hiyo kuwa kasimamishwa alikuwa na kimada…walikuwa kwenye hoteli,wameshatumia vya kutosha, na hawajalipa….anatarajia akifika kazini achote, taarifa inakuja, hana kazi, na haruhusiwi kuingia ofisini,..ilikuwa ‘surprise..’

Alidondoka….akapoteza fahamu , na tatizo likazua tatizo jingine….utajiri, cheo ..majigambo yakaishia hapo, ..
Akiwa nyumbani hana kazi, ..ana madeni kila kona..ikafiki mahali magari yakapigwa mnada…nyumba, maana alikuwa na zaidi ya nyumba tano hivi……wakabakiwa na kibanda tu,..kile walichoanzia maisha ya mama, hutaamini ilifikia muda wakageuka kuwa omba omba….waliishiwa kabisa...ikawa inahitajika tiba ya baba, hakuna pesa wafanyeje, kazi ikawa kuomba, na kazi hiyo waliifanya bibi na mama yangu….baadaye siku yake ikafika, akafa akiwa hana thamani….mungu amsamehe tu..lkn nyie waume mlio hai siwapendi, …


WAZO LA LEO: Ukiwa na cheo, ukawa na uwezo wako, usijivike kilemba cha majigambo, ukajitanda nguo ya dharau, ukavaa joho la kiburi...ukumbuke hayo yote ni mapambo ya dunia tu, yana mwisho wake, wapo walikuwa navyo na sasa hawapo tena duniani,…na wapo walikuwa navyo, vikageuka kuwa sumu …muhimu, tumshukuru mungu kwa neema hizo kwa kuwajali wenzetu, tuwasaidie kuwainua, tujenge jina nzuri la wema, maana hata tukifa bado majina yetu yataendelee kuwa hai kwa matendo hayo mema.

Ni mimi: emu-three

Friday, September 9, 2016

KISA CHA BINTI YATIMA-`KWANINI MIMI...'- 2


‘Mimi sipendagi kusimulia maisha yangu maana kila nikianza kusimulia ninaishia kulia tu, najikumbusha machungu mengi yaliyonisibu, maisha yangu yamekuwa ni kidonda kisichopona ambacho kila siku kinatoneshwa na watu…..’akasema huyu bint

Kisa kilianzia pale nilipomkuta binti mmoja akiuza mihogo, na mgongoni kabeba mtoto mdogo, na mtoto huyo akawa analia sana,..hali ya yule mtoto akiwa kabebwa mgongoni ilisikitisha, nguo alizovyaa, ...na hali ilikuwa nayo, na hali ya hewaa ilikuwa ni ya ubaridi..nikashikwa na huruma , nikamsogelea huyo binti, kujua zaidi, nia hasa ilikuwa kumshauri amuonee huruma huyo mtoto..lakini majibu niliyokutana nayo, yalinifanya niingiwe na hamasa zaidi ya kumfahamu huyo binti..

Wakati nikiwa kwenye hamasa hiyo mara linazuka jingine kubwa.....

Hiki ni kisa cha binti yatima, hebu tuenddee nacho...


***************  2***********‘Sasa utasaidiwaje, maana shida ni kila mtu anazo, na hakuna anayewez
a kusema mimi nimejitosheleza, nahitaji mtu wa kumsaidia, kila mtu hata tajiri anaona maisha kwa ke ni magumu, hajatosheka…sasa ili watu waweze kuvitika na matatizo yako ni wewe mwenye shida ujieleze…’nikasama na yeye akawa kainamisha kichwa chini akilia.

‘Haya…, ndio maisha yetu yalivyo, …, huruma haipo karibu kwenye nafsi zetu, ni mpaka ifukuliwe…unaonaeeh,. Na mwenye kukuhurumia zaidi ni yule aliyewahi kupatwa na shida, na shida zipo kwetu sisi watu wa chini,….sasa,… ukiongea watu wakakusikia wakaona shida zako wenye huruma za karibu wanaweza kukusaidia…au sio, masikini tunasaidia wenyewe kwa wenyewe…’nikasema.

‘Hakuna mwenye huruma dunia hii…nimeteseka sana, watu wananiona hivi hivi,….wanajua kabisa mimi sina baba wala mama, mimi ni yatima, au yatima anatakiwa aweje,….mimi ni yatima aliyepitiliza, sina baba wala mama, wala mjomba aau shaangazi, dunia imenitekeleza….’akasema

‘Katika maisha kama hayo ukiwa mdogo wa mwaka, ..utakuwaje,…ufe, au…..sasa aliyejitolea kunisaidia ndio huyo amefariki,….wangapi waliniona na zaidi ya msaada wao ulikuwa ni masimango na kunyanyapaliwa na hata kuzaliliswa…Namshukuru sana bibi yangu, bila yeye, labda ningelishakufa zamani… oh, na ndio huyo ameshafariki, na hata bila ya watu kumuelewa…binadamu, jamani binadam..’akasema

‘Mhh…pole sana…’

‘Na sasa ndio huyo amefariki bibi yangu masikini, nitakuwa mgeni wa nani…sina ndugu sina jamaa…na na.., kinachoniuma ni kuwa amefariki hata sijapata muda wa kulipa fadhila zake, alinilea nikiwa mdogo kwa shida…., akanitibu nikiumwa,..akiwa hana mbele wala nyuma,.. akataabika kwa ajili yangu, na…za zaidi nikamuongezea  ugumu wa maisha kwasababu ya tamaa zangu za kimwili….mungu wangu kwanini, kwanini…..’akawa analia.

‘Pole sana, yote maisha….’nikisema

‘Yote maisha ehe..mnasema tu….’akainua uso uliojaa chuki.

‘Maisha…hahaha, maisha…,  mengine yanauma….yanauma ukizingatiwa kuwa mengi ya madhila hayo waliosababisha ni wanadamu wenzetu…na ni ndugu kabisa, unajua ndugu...damu moja kabisa, tena wanaume, ….’akaninyoshea kidole, huku akisema

‘Wanaume kama wewe…., eti wanajita wanaume, hahaha, kama ni wanaume kweli ni kwanini wasihangaike kivyao, kwanini kama ni wanaume mbona wanadhulumu,..nawachukia sana wanaume... unajua kuchukia,…masikini bibi yangu…’akawa analia.

‘Kwani bibi yako kafariki lini…?’ nikamuuliza baada ya kupita kitambo kidogo.

‘Ndio nimepewa taarifa leo nikiwa nahangaika kuuza mihogo…lakini sijui kama kazikwa au la..maana hakuna mawasiliano huko kijijini,na huenda wamemtelekeza kwenye kibanda chake, baada ya kumfukuza kwenye nyumba yake ya urithi……na ndugu niliotegemea waniambie nini kinachoendelea ndio hao hao  aaah, bibi yangu masikini….’akawa analia.

‘Pole sana….’nikasema

‘Oh…bibi yangu masikini, hivi mzee kama yule kawakosea nini jamani, nyie walimwengu mna nini jamani, bibi, kizee, hakina nguvu kabisa, masikini , hohe hahe…wana..wana…ole wao, nasema ole wao..…nilijua tu... nilijua mwisho wa siku watamuua tu…’akasema

‘Ina maana wamemuua…?’ nikauliza

‘Kifo chake kitakuwa kimesababishwa na vipigo na mfadhaiko alioupata…sijui kwanini watu hawana huruma, hivi kama wana miguvu kwanini wasiende kupigana wakapata pesa, eti…yaani wanakwenda kumpiga kizee wa watu,…ni kwanini lakini…’akasema.

‘Kipigo…!, mfadhaiko..!…hebu anza hatua kwa hatua, kwanini bibi yako alipata kipigo..?’ nikamuuliza.

‘Eti wanasema bibi ni mchawi..’akasema na watu waliokuwa wasikiliza wakaguna,

‘Ndio wanavyosema na hilo lilimuumiza sana bibi…hakujua hata ajitetee vipi,akawa analia tu, akimuomba mungu amsaidia, hakuwa na jamaa wakumsaidia, ikabakia kila siku akilia, akimuomba mungu siku ifike aondoke hapa duniani, kuliko kupata adha hiyo…lakini aliomba kwanza anilee nifikie hatia fulani…..’akatulia

                         ***********

‘Mchawi,…..?’ watu wakaguna na kuuliza

‘Lakini wazee wengine vigagula….,. Yawezekana bibi yako kweli alikuwa mchawi kweli….’watu wakazidi kuongea..

‘Ndio zenu hizo,…..mna uhakika gani na hilo…kama na nyie sio wachawi…wanafiki wakubwa nyie…hakuna aliyemfahamu bibi, hakuna..zaidi ya uzushi huo….’akasema akiwaangalia watu kwa hasira na hapo kukazuka zogo, kila mtu akiongea lake

Kulizuka mabishano ya watu kila mmoja akisema lake, wengine walifikia kusema huenda kweli huyo bibi alikuwa ni mchawi, lakini huyo binti hakujua tu, au hata huyo bintu anajua lakini anamtetea tu bibi yake…..wengine wakasema ni imani haba tu….yaani kila mtu akawa anasema lake, …nilitaka hayo mabishano yaishe ili niweze kumsikiliza huyo binti…kwani atakeyeweza kuelezea ukweli wote ni huyo binti!

‘Hebu nikuulize kwanini walisema bibi yako ni mchawi , alikuwaje mpaka wakamuhisi hivyo, maana wewe ulikuwa unaishi naye au sio, kwahiyo unamfahamu alivyokuwa, unajua lolote kuhusu bibi yako…?’ nikauliza.

‘Hata sijui hayo ya bibi mchawi yalianzaje,…’akasema.

‘Ukituelezea maisha ya bibi yako, itakuwa rahisi kwetu kuyafahamu hayo….’nikasema
‘Mimi bibi yangu ndiye aliyenilea, baada ya wazazi wangu kufariki,..hata siwajui wazazi wangu wanafananaje,…maana hata picha hakuna,…wazazi wangu walifariki nikiwa mdogo sana, bibi anasema nilikuwa na mwaka mmoja tu, unaona…sasa kama angelikuwa ni mchawi angenichukua mimi, angenilea mimi,…’akaanza kuelezea.

‘Si ili urithi uchawi wake…’akaropoka mtu mmoja.

‘Hujui unachokisema, kwasababu humfahamu bibi yangu…’akasema

‘Wazazi wako walikufa wote wawili kwa pamoja?’ nikauliza, nikitaka kudodosa ili kujua ukweli halisi wa binti huyo, kuliko kuchukulia juu, juu tu..

‘Alianza kufariki baba…..nilivyoambiwa na bibi, ..baba aliumwa sana, lakini chanzo cha ugonjwa wake ni kuwa alikuwa hajatulia, mlevi, mnzizi….ndio maana nasema siwapendi wanaume…kwasababu kutokana na tabia yake hiyo ya ulevi na umalaya, ndio alimuambukiza mama yangu, mama alikuwa mpole sana mcha mungu, lakini kutokana na baba, aah, nyie wanaume….’akasema akitikisa kichwa.

‘Oh…unasema baba yako ndiye alimuambukiza mama yako, una uhakika gani na hilo…?’akauliza jamaa mmoja.

‘Ndio nina uhakika..japokuwa sikuwepo, sikuwahi kuyaona maisha ya baba kwa macho yangu, lakini mengi niliyasikia kuhusu maisha yake, na sio mtu mmoja tu, wengi,….na hata waliowahi kutembea naye wamathibitisha hayo…wengi ni marehemu, waliopo hai walielezea kwenye…haya mambo ya ukimwi na matumaini…’akasema

‘Kwahiyo maisha ya baba yako unayafahamu kwa kupitia mazungumzo ya watu au sio…., je unaweza kutusimulia kidogo jinsi ulivyosikia kwa watu…, kwa faida ya watu wengine ili wajifunze, ..kama hutojali lakini…’nikasema

‘Siogopi kuyasimulia, …maana maisha yake yamekuwa ni funzo pale kijijini, kila mmoja amekuwa akitolea mfano kwake, hasa mzazi anapomuona mtoto wake anapotea, anakuwa mlevi, Malaya..ana uchu wa madaraka, hamtunzi mkewe….watu wamekuwa wakitoa mifano kwa kupitia maisha ya baba..kwahiyo hata nisipoongea mimi leo…, yameshaongelewa sana…mungu amsamehe tu baba yangu…’akasema

‘Kwani baba yako alikuwaje, maisha yake yalikuwaje ulivyosikia kwa watu...?’ nikamuuliza

NB: Haya haya…huyu baba mtu alikuwaje, kwani alikuwa kiongozi, mzazi…na mwenye uwezo kifedha, je hayo yalikuwaje mtihani kwake, na kwa jamii…, ni sehemu muhimu yenye mafunzo itafuata baadaye

WAZO LA LEO: Wazazi tunatakiwa tuwe kiyoo cha familia zetu, matendo yetu, tabia zetu huwa zinaaksi maisha ya watoto wetu, kwahiyo tuweni makini sana. Sisi wazazi ndio chanzo cha misingi mema ya watoto wetu,..huwezi ukamfunza mtoto adabu wakati wewe mwenyewe ni mtomvu wa nidhamu, unapigana na mkeo, mnazozana mbele ya watoto…hutunzi vyema familia yako..haya na mengine mengi huathiri sana maisha ya baadaye ya mtoto wetu. Na kama unatenda madhambi kwa watoto wa wenzako ujue na wewe madhambi hayo yatahamia kwa watoto wako. Uone jinsi gani mzazi ulivyo na dhamana kwa familia yako.

Tumuombe mungu tuwe wazazi wema, tutimize wajibu wetu, hata kama maisha ni magumu lakini hivyo hivyo tu, kwa matendo yetu mema, tabia njema… tunaweza kuwafanya watoto wetu wakawa nguzo imara ya vizazi vyetu.
Ni mimi: emu-three

Wednesday, September 7, 2016

Wakati ukuta...


 Wakati napita barabarani, kwenye vimtaa vinavyoingia kwenye ofisi mbalimbali, nikavutiwa na bustani zilizopembezoni mwa barabara hizo, ambazo zimetengenezwa na wenye maofisi hayo. Macho yangu yalivutiwa na ua-waridi, lilikuwa ndio kwanza linaanza kufunuka na ule uzuri wake ulikuwa ukianza kuonekana, nikatabasamu na moyoni nikasema, ama kweli ua waridi ni mrembo wa maua. Basi ikawa kila nikipita hapo nalichungulia lile ua, mpaka likachanua vyema na kudhihiri ule uzuri wake, wa kuitwa ua waridi, na wengi walikuwa wakilitupia jicho, kwa tamaa za kulichuma.


Nilikaa siku kadhaa bila kupita njia hiyo, kwasababu mbalimbali na jana nikaona nipitie hapo, nikakumbuka lile ua waridi, nikalichungulia kwa hamasa nikaongeza mwendo ili nifike maeneo yale. Nilipofika hapo nilitamani kulia, kwani lile ua-waridi lilikuwa limeanza kunyauka, na yale mabawa yake ya pembeni , yanayoliremba kwa rangi yalikwa yamelegea karibu kudondoka chini. Nikalisogelea na kujaribu kuyainua yale maua yake ili yakae vyema, lakini haikuwezekana, kwa yakini lilikuwa limeisha muda wake, na mbegu zake zilidhihiri, nikatabasamu na kusema angalau mbegu hizo zitadondoka na kuzalisha miti ya maua waridi mengine mengi.

Wakati nahangaika na lile ua mara likapita gari la mwanadada mmoja, kwa umri wake sasa huwezi kumuita mwanadada, ingawaje hajabahatika kupata mtoto, na kama angebahatika kupata mtoto na mtoto wa kike labda angelikuwa na wajukuu! Nikamtizama akipita na hilo gari huku kumbukumbu za akili zangu zikinipeleka enzi hizo ambapo nilikuwa bado nasoma, na huyu mwanadada alikuwa keshaanza kazi, na sie kama wanafunzi wa sekondari damu moto, tukawa tukimuona tunatamani kuongea nayeye. Na yeye alikuwa mkali sana, akituasa kuwa tusome tusiwe na tamaa na watu wakubwa. `Naombeni mniheshimu mimi ni dada yenu..’ alikuwa akisema hivyo!

Dada huyu namkumbuka sana, kwani tulipokuwa wanafunzi, wengi tulikuwa tukimuona akipita na magari ya matajiri, na kila mmoja wetu alitamani ampate mrembo kama yule. Ni kweli alikuwa mrembo, na kama angeliamua kugombea huo urembo wa dunia, angelikuwa miongoni mwa washindi. Lakini siku moja tulimsikia akisema, `nigombee urembo ili iweje, mwenyewe najiamini kuwa mrembo, halafu nitafute watu wanilinganishe na wengine…na kama ni pesa ninazo za kutosha kwanini nihangaike…

’Kweli mungu alimjalia, toka sura hadi maumbile ya mwili, ila kasoro tu tabia ilikuwa haiwafurahishi wengi. Labda ni kutokana na urembo wake ndio maana aliringa sana, na hata kuwadharau wenzake na hasa wale wa hali ya chini. …labda!

‘Mwenye kisu kikali ndiye anayekula nyama..’ huu ulikuwa mmoja wa msemo wake, pale alipokuwa akigombewa na matajiri mbalimbali, kila mmoja akitaka kummiliki yeye na hata kumtaka awe mpenzi wake. Lakini kwa kunata kwake , alihakikisha anawatoa majaso hawa wanaume na mwisho wa siku midume yenye uroho waliambulia kutoa zawadi kibao na bado akawa hataki kumilikiwa na yoyote katii yao..., kama mpenzi wa kudumu.

‘Mimi sitaki rafiki wa kudumu, kwani sijafikia umri wa kuolewa, kwahiyo anayetaka urafiki na mimi, ajiandae kwa `part- time’ tu..’ aliwaambia hawo wanaume waliokuwa wakijigonga gonga kwake. Na kweli ungelimkuta muda wa chakula cha machana utakuta yupo na mwanaume huyu, chakula cha usiku mwanaume huyu, hatujui kama usiku alikuwa na rafiki mwingine, lakini yeye alisema waziwazi kuwa urafiki na waume hawo mwisho wake ni geti la nyumba kwao, hana mpenzi wa kuchezea mwili wake!

Ni heri kwake kama msimamo huo ulikuwa wa kweli, na watu wakamsifia kuwa kama ana msimamo huo wa kuwa `hataki watu wa kuchezea mwili wake’ basi atakuwa na mawazo ya maana sana. Lakini tukasikia kipindi fulani kuwa kapachikwa mimba, na mtu aliyempachika mimba ni njemba fulani, na njemba huyo ni wale ambao sura hazina mvuto.

 Kilichotokea ni kuwa njemba huyo kwa vile alikuwa na pesa aliamua kumtoa huyo dada kwa chakula cha usiku na kumbe ulikuwa mpango rasimi wa kumkomoa huyo mwana dada, kwenye kinywaji akawa kaweka dawa ya kulevya, na dada alipoishiwa nguvu, akachaguliwa bega!

Katika skendo hiyo , huyo dada ndipo alipobebea mimba,na kitendo hiki kilimsononesha sana huyu mwanadada, kwani alisema hataki azae mapema, na hata akizaa hataki kuzaa watoto wenye sura mbaya, alitamani sana kuzaa watoto wenye sura za kizungu-kizungu , …alipenda sana wazungu na ndoto yake ilikuwa kuolewa na mzungu. Alipogundua kuwa kapachikwa mimba na huyu jamaa, ilikuwa imeshapita miezi miwili. Mwenyewe alidaii kuwa siku zake zinaweza kuchelewa hata miezi miwili, lakini kutokana na mabadiliko fulani mwilini alijihisi kuwa ana mimba, akaenda kupimwa na kukutwa kweli ana ujauzito.

Kwa hakika alijua kuwa nani kampachika hiyo mimba, ila sisi wa mitaani tukawa tunajiuliza itakuwa mimba ya tajiri gani, au mzungu gani kama mwenyewe alivyotaka, na kwanini mimba hiyo ikaja mapema. Penye wengi hapafichiki kitu, licha ya kuwa yeye mwenyewe alifanya siri, lakini uvumi ulienea mitaani na kila mtu akajua. Swali lilikuwa ni uja-uzito wa nani,…!

‘Siwezi kuzaa mtoto mwenye sura mbaya kama njemba ile, lazima nikaitoe hiyo mimba…’ akasema na yule njemba aliposikia hivyo, akajitahidi kumbembeleza huyo mwanadada asiitoe kwani yupo tayari kumuoa, lakini huyu mwanadada aksema wazi kama ni lazima kuolewa na mtu kama yeye, labda aoe mwili wake ukiwa mfu! …kufuru!

Basi mwanadada huyo akafanya mpango akakutana na mtaalamu wa kuporochoa viumbe vya watu visivyokuwa na hatia. Na mungu kwa uwezo wake akataka kumpa mitihani huyo mwanadada, kwani wakati anaitoa hiyo mimba kukatokea matatizo, ambayo yalipelekea mwanadada huyo kupata matatizo ya ndani kwa ndani. Mimba ilikuwa haikutoka vyema, ikawa imeleta mdhara ndani ya kizazi. Na matokeo yake ikahitajika dada huyoo kufanyiwa upasuaji na kusafisha kizazi, na kilichotokea ni kuharibika kabisa kwa kizazi chake,…!

‘Eti nini ina maana sitazaa tena?’ akamuuliza docta

‘Nasikitika sana ndio hivyo, kwani ulivyotoa hiyo mimba imeleta athari kubwa sana kwenye nyumba ya uzazi , na bahati yako ndiyo hiyo kuwa kizazi kimesafishwa vyema na kuondoa balaa ambalo lingekugharimu maisha yako…’ akamwambia docta

‘Sawa, hata hivyo watoto wa nini…’ akajisema huyo dada na kuondoka zake

Miaka ikaenda na umri wa yule dada ukawa umesogea, akabahatika kuolewa na mwanaume mmoja, lakini hawakudumu naye, wakaachana, …haikuchukua muda akaolewa tena, ikawa ndio hivyo akiolewa anakaa na mume mwaka au miaka mwili anaachika, kwasababu ya tabia yake ya kutaka anasa au kugundulika kuwa hazai. Na hili likamfikisha hapo alipo, umri umekwenda mbele sasa hana mume wala mtoto.

Umri haujifichi katika maisha ni kama kifo, ambacho hakikwepeki, umri hauna dawa kama kama kilivyo kifo, ufanye ufanyalo umri huwa unasogea mbele, na maumbile ya kibinadamu hubadilika siku zinavyokwenda. Uzuri wa ujanani haudumu, una muda wake, na sura ile ya mvuto hubadilika na kuwa sura ya makunjazi,…sura ya utu uzima na hapo tena inabakia kusimulia, `enzi zangu bwana…’

Dada yetu huyu ambaye yupo kwenye umri wa akina mama ambao walitakiwa kuwa na wajukuu, hadi leo hana mume wala mtoto, na uzuri ule aliokuwa akiringia nao umetoweka, sio `mrembo tena wa kimataifa’ bali `ni aliyekuwa ..’ .

Huyu mwanadada alisahau kabisa kuwa wakati ni ukuta, huwezi kushindana nao, ukishindana nao utaumia mwenyewe. Kwani kwa bahati mbaya hana kizazi ambacho kingeendeleza ule uzuri wake. Ni heri ya lile ua waridi ambalo kesho au kesho kutwa litadondosha mbegu na kuendeleza kizazi chake. Si sawa na huyu mwanadada, au mwanamama. Ambaye sasa anatamani hata mume asiye na pesa lakini hampati! Bahati mbaya hiyo!

Haya ndiyo maisha yetu, tunapokuwa katika `chati’ tukawa maarufu tunasahau kuwa kuna kitu muda, na muda huendana na `umri’ umri katu hautongoji, muda ukienda na umri unakwenda na maisha ya mtu yanapungua, na sura halikadhalika inasawajika. Ni dhahiri kuwa, umri unakwenda na wakati na mabadiliko ya wakati huwezi kuyaona mara moja, …labda joto, baridi nk,…ila siku zinavyokwenda mabadiliko ya kimaumbile yatajionesha waziwazi. Ulikuwa ukiitwa mtoto, ukaitwa msichana au mvulana, baadaye dada, mrembo, kaka mtanashaji na sasa mama au baba, na hatimaye bibi au babu…hiyo ndiyo hali halisi.

Upende usipende utazeeka, kwani hakuna dawa ya kuondoa uzee, msijidanganye kwa kujichubua…eti ule umri wa ujanani utarudi…tusijidanganye kabisa .Cha muhimu ni kuwekeza, kiafya, kimaadili, kiuchumi kwa manufaa ya baadaye .

Muhimu wenzangu, tujenge tabia ya kuwekeza kwenye wema, ambao hata uzee ukija utakuwa unakulinda. Wapo waliozeeka, lakini kila mtu anatamani awe naye kama mume wake au mke wake, kwasabau ya tabia njema afya yake nk….Tabia njema, nidhamu , na uadilifu hujenga mwili kuwa `imara’ wakati wote. Hata ukifa jina lako halitasahaulika kwenye kumbukumbu za watu wema.Thursday, September 1, 2016

KISA CHA BINTI YATIMA-UTANGULIZI


Kilio cha mtoto kilinifanya nisimame,..kwangu mimi mtoto akilia, nahisi moyo ukiumia, maana najua mtoto mdogo kama huyo akilia anataka kutoa ujumbe wake umfikie mtu..hawezi kuongea kwa umri huo, kilio chake ndio ishara yake ya maongezi.

Kwa haraka nikamgeukia Yule mama, aliyekuwa kambeba huyo mtoto…Alikuwa ni hawa akina mama wanaouza mihogo mibichi barabarani, na kwa muda ule alikuwa na sinia lilipangwa mihogo mibichi, kichwani mwake, na mkono mwingine kashika muhogo ulibakia nusu, na mwingine kashikilia kisu. Ni hawa wajasiriamali wa barabarani, ukitaka muhogo mbichi anakukatia kipande kutegemeana na pesa yako. Anapata riziki yake halali…

Nilisogea hadi kwa Yule mama, kwa muda huo alikuwa akihangaika kuulizia wateja, abiria waliokuwa kwenye daladala, kama kuna mtu anayetaka muhogo, mimi nikawa sasa nipo nyuma yake karibu sana na yeye,  nikawa najaribu kumchekesha Yule mtoto ili aache kulia…

‘Toto nyamazaee…’nikasema na sauti hiyo ikamfanya huyo mama ageuke, na kuniangalia

‘Nikukatie wa shilingi ngapi…?’ akaniuliza

‘Mtoto analia…na kwa jinsi ulivyombeba , na nguo ulizomvalisha na kwa hali hii ya hewa utamuathiri kiafya…’nikasema..ni kweli mtoto alibebwa kwa kitenge kilichochanika na kama kafungwa mgongoni, na asilimia kubwa ya mtoto yupo uchi.

‘Nikukatia wa shilingi ngapi…?’ akaniuliza sasa akiwa anataka kuanza kukata kipande.

‘Mia mbili…’nikasema na kwa haraka aka-kata kipande kidogo, kiukweli  sikuwa na haja ya muhogo, huruma yangu ilikuwa kwa Yule mtoto. Alipomaliza kukata kile  kipande akaanza kukimenya.

‘Mtoto analia sana, muonee huruma…’nikasema , yeye wakati huo anasubiria nimkabidhi pesa.

‘Nikimuonea huruma atakula nini….acha alie akichoka atanyamaza, kwani kulia kaanza leo… au wewe unajua maisha ya huyu mtoto….kwani wengine wanaumwa huko wananitegemea…’akasema huku akiniangalia kwa macho yaliyojaa chuki. Uso umeumbwa kwa aina yake, uso unaweza ukaelezea kile kichomo moyoni mwa mtu.

‘Kwanini unaonekana una chuki hivyo, mimi ni mteja wako watakiwa uninyenyekee au sio..?’ nikasema

‘Kwasababu nawachukua sana wanaume…’akasema hapo hata wale wanaume waliokuwepo pembeni waligeuka kumuangalia, na mmoja akasema

‘Ukiwachukia wanaume ujue unamchukua hata baba yako mzazi…’wakasema

‘Kauli yangu ni hiyo hiyo, nawachukia sana wanaume, habari ndio hiyo, wewe nipe pesa yangu…’akasema na mimi nikatoa noti ya elifu moja nikampa, akanitupia jicho kama kutaka kusema , kwanini nanunua kipande kidogo, kumsumbua kutafuta chenji.

‘Usijali hiyo chenji ni ya mtoto…’nikasema , hapo akanitupia jicho tena, na mmoja wa watu akasema,;

‘Haya huyo ni mwanaume …kataa hiyo pesa anyokupatia…’sauti ikasema

‘Siwezi kukataa maana haya madhila yote ninayoyapata kisa ni wanaume..unamuona huyu mtoto, baba yake alimkataa, wakati yeye ndiye aliyeni…..’akasita, halafu akaendelea kusema

‘Anadai kuwa huyu mtoto sio wa kwake, wakati anafanana na huyo mwanaume kwa kila kitu, na mimi sikuwahi kumjua mwanaume mwingine zaidi yake,…yeye ndiye aliyenifanya nifukuzwe shule…akiniahidi atanioa….’akawa anabadili sauti kama anataka kulia.

‘Sasa hilo utamlaumu nani, kwanini ulikubali , si kwa ujinga wako, kwani alikubaka, wewe si uliona ni peremende, …kwanza wewe yaonekana ulikuwa mapepe, mtoto wa shule unatembea na wanaume wakubwa….’mmoja wa wauza vitu barabarani akasema.

‘Nilikuwa mapepe mimi hebu uliza..huyo mwanaume alikuwa mwalimu wangu…, hebu fikiria mwalimu wa shule… na mimi nilikuwa mwanafunzi wake, msitake niongee ambayo sikutaka kuyaongea. …’akasema, na kuanza kuondoka.

Mimi niliingiwa na hamu sana ya kutaka kujua ni masahibu gani yaliyompata huyo mdada, nikaahidi kumtafuta.

Hutaamini jioni wakati narudi toka kwenye mishughuliko yangu, nikakutana na huyo mdada kwenye treni, bila ajizi nikajitambulisha kwake na kumuuliza, maisha yake ya nyuma, …mdada Yule alikuwa katulia,..niliona kama macho yamevimba..alikuwa analia, na nilipomuuliza kulikoni, ikawa kama nimejichongea, akaanza kulia kwa kwikwi, nikabakia nimeshangaa.

‘Mbona unalia..?’ nikamuuliza

‘Bibi yangu amefariki..bibi ambaye ndiye alikuwa baba na mama yangu, na juhudi zote za kuuza mihogo, ni kuhakikisha napata pesa ya kwenda kumtibia, sasa amekufa…….siwezi kuamini, ..kwanini dunia hii inanieleleza, sasa sina baba, sina mama, sina hata mlezi,….nitaishi na nani…nitakwendaje kumzika bibi yangu, wakati hata pesa kidogo niliyokusanya leo wameniibia…’akasema akilia

‘Wamekuibiaje…?’ mmoja akauliza

‘Nilijua tu…kuna tatizo, ..’akasema akitikisa kichwa
Haya jamani sijui bado mnahitajia visa vyangu, hiki kingina kinaitwa kisa cha ….
‘Kisa cha binti yatima….’


  Hiki ni moja ya kisa cha haraka nilichokipata jana, na sikupenda kukilaza, nikakiingiza kwenye shajara yangu, japokuwa kwakweli kinasikitisha,…nilijaribu kukiandika kwenye simu, lakini sikuweza kuendelea, simu iliisha mfuta, chaji , sikukata tamaa!Lakini huo ndio utangulizi wake, na tukijaliwa tutakiendeleza

Ni mimi: emu-three

Wednesday, August 24, 2016

Tenda wema uende zako

‘Leo nimepata Bahati kubwa kweli’ jamaa mmoja alikuwa akimhadithia mwenzake kijiweni kwa zile walizoziita habari za leoleo.

‘Bahati gani hiyo hebu nipe za `live’ mwenzake akamsogelea huku akishika shikio kuonyesha kuwa sikio liko wazi kumsikiliza

‘Nimepanda daladala la kwanza, konda hakunidai nauli, la pili hakunigusa kabisa, na ajabu abiria mmoja niliyekaa naye kwenye gari la kwanza alipoteremka akawa amedondosha mkono, elifu kumi kavu kabisa, nikaisweka mahala pake! Siunajua tena bongo, bajeti ikawa imekubali’ aliinua juu mkono kwa kujipongeza.

‘Rafiki yangu hapana, mimi mimi sikuungi mkono kwa hilo, ni kwanini hukumrejeshea huyu abiria aliyedondosha pesa yake..au ungempa konda ili aitangaze hapo ungekuwa umetenda uadilifu. Nasema hivyo kwasababu, abiria mwenzako ni sawa na wewe ipo siku na wewe utadondosha na kama ungefanya usamaria mwema kwake na wewe ungefanyiwa hivyohivyo…’ akasema mwenzake

‘Wewe , sirudii ujinga huo tena, niliwahi kukuhadithia kisa kilichonipata huko kijijini. Siku moja nilikuwa nalimia bustani zangu, ilikuwa karibu na barabara. Mara likapita gari la mhindi mmoja, ilikuwa siku ya mvua, kwahiyo magari mengi yalikuwa yakikwama kwama....

Basi siku hiyo mara likapita gari la mhindi lilikuwa landrover, unajua tena magari ya aina hiyo hayakwami kwami kwenye matope, Lilipofika pale nilipo, likawa kama linataka kudondoka, na ajabu kukadondoka bahasha kubwa toka ndani, ya hiyo gari..sijui ilidondakaje. Nikaisogelea na kuikagua, na ndani kuliswekwa mabulungutu ya manoti. Fikiria maisha yangu yote sijawahi kuona pesa za kiasi kikubwa hivyo, hasa kwa maisha yetu kule kijijini.

Nilifikiri kwa muda nikasema, Hapana huu sio uungwana, mimi nimelelewa vyema na wazazi wangu... nikaamua kuwakimbilia ili niwaopatie pesa yao.

Na kwasababu kulikuwa na utelezi, na barabara ilikuwa mbovu, ilikuwa ni rahisi kulifikia lile gari kwa kupitia njia za mkato. Nikalikuta limesimama. Wenyewe walikuwa wakibishana kuwa ile bahasha wameisahau huko walipotoka kwahiyo ni vyema warudi.

Mara pale mimi nikatokea, nikiwa na ile bahasha mkononi,
'Samahani wandugu wakati mnapita pale kwenye shamba langu mlidondosha hii bahasha...'nikawaambia

Jamaa walinitolea macho ya mshangao.

Yule Mhindi aliniangalia kwa muda, halafu kwa mshangao akanizaba kibao. Kibao cha haja, hadi vidole vikaonekana shavuni kwangu. Na baadaye akatoa bulungutu moja kati ya yale mabulungutu yaliyokuwemo humo ndani na kunipatia, halafu akaniambia

‘Weye afrika gani, ..., utakufa masikini…’ Akacheka sana na wenzake wakaungana naye kwenye kucheka, na bila kusema zaidi  wakaingia kwenye gari lao na kuondoka...

'Niliiumia sana moyo wangu, nilitamani niwakimbilie niwatukane, lakini lile bulungutu nililopewa lilimaliza yote. Nikapiga mahesabu kuwa pale hazipungui milioni kadhaa. Na kweli ilikuwa milioni tano. Hivi fikiria pesa yote hiyo enzi hizo milioni tano ilikuwa pesa nyingi sana kwangu, Pesa hiyo niliweza kujenga banda langu na kufungua duka, na hapo dukani nikaandika `tenda wema uende zako..’

'Na tangu siku hiyo, sifanyi makosa hayo tena..nikiokota ni bahati yangu.....'

Mimi sikupenda kuendelea kuwasikiliza, kwani hitimisho lake sikulipenda, na huo usemi unaashiria enzi nyingine ya ajabu, enzi iliyotabiriwa , enzi ya kukaribia mwisho wa dunia, enzi hii uaminifu hautakuwepo tena, enzi ya watu kunyang'anyana,  mdogo hamuheshimi mkubwa, matusi ni lugha ya kawaida, matendo yasiyofaa kuenea....

Je hii hali hatuioni..? Ndio hii hali iliyopo sasa, mwenye nacho hamjali asiyekuwa nacho na asiyekuwa nacho anatafuta kupata kwa njia yoyote ile, hata ile isiyo ya halali..Angalia sasa hivi ukidondasha kitu kwa bahati mbaya akiokota mwenzako ni chake, sio chako tena...mtu huyo , hawezi kukushitua na kukuambia samahani umedondosha kitu chako..., hasa pesa.

 Enzi hii ya ajabu imefikia hatua watu wanaogopana , kama ni usiku unaombea mungu usikutane na mwanadamu mwenzake , ni heri ukutane na mnyama, maana mnyama anaweza akakuogopa akakumbia lakini sio binadamu mwenzako, ....huyo binadamu mwenzako anaweza akawa ni jambazi, ambaye hatosheki na kukuibia tu,...anaishia na kukuua, ili usije kumtaja..hivi sasa huruma, upendo na kuaminiana imekuwa ni misemo tu,..na huenda ikawa misemo adimu.

Tumuombe mungu atuepushia na hii hali, kwani kutokana na kazi zetu kuna watu wanarudi usiku au tunatoka majumbani asubuhi sana, je tutaishije, tutawahije kwenye sehemu zetu za kutafuta riziki. Na tatizo hili linazidi kwasababu watu hawazithamini tena dini, watu hawamjui mungu.... Dini zimekuwa ni sehemu tu ya kukamilisha maisha yetu, ..kufunga ndoa, nk

Tujiulize ni kwanini hii hali inazidi...na tufanye nini....

Ni mimi: emu-three

Search This Blog

Loading...