Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Showing posts with label mila na desturi. Show all posts
Showing posts with label mila na desturi. Show all posts

Friday, July 12, 2019

IMANI HUTOKA MOYONI


IMANI YA KWELI HUTOKA MOYONI , NA SIRI HIYO AIJUE NI MOLA PEKEE.

Hiki sio kisa ni ukweli,

Katika maisha yangu… niliwahi kuajiriwa kwenye kampuni moja, nilipofika hapo nikazoeana na msichana mmoja,…nilimzoea kwa vile yeye ndiye alinikaribisha, na kunionyesha mazingira ya hapo kazini, ufanyeje, uende wapi kiutawala na sehemu ya kula, ofsini ipi ni ipo, vitu kama hivyo.

Basi kila nikihitajia kitu namuuliza yeye, na kiukweli hakuwa na hiyana, aliweza kunielekeza vyema tu, na kuna muda watu wakaanza kutuangalia kwa macho ya kujiuliza, huenda tumekuwa marafiki, lakini moyoni mwangu sikuwa na mawazo hayo kabisa.

Siku zikapita, na ule ukaribu wetu na huyo mdada ukapungua, maana sikuwa na cha kumuuliza tena, mimi nipo idara nyingine na yeye yupo idara nyingine, …sasa katika mazungumzo, nikaja kujua kuwa huyo msichana ni wale wenye msimamo mkali…mtakuwa marafiki lakini sio kwenye tendo la ndoa.

‘Huyu dada ni bikira bwana,…’watu wakawa wanamtania.

‘Labda bikira wa sehemu nyingine, mimi sidanganyiki  ‘mmoja akasema.

‘Kwanini, na wewe unamfahamu, tokea tuajiriwe hapa ulishawahi kumuona na mvulana, ..maana hapa hakuna siri, na hata huko nyumbani kwake si unakufahamu, uliwahi kumuona akiwa na mvulana..?’ akaulizwa.

‘Siri ya mtu anaijua yeye mwenyewe..ila mimi siamini kwa umri ule, atakuwa bado bikira, ni lazima atakuwa na mtu wa siri..’akasema huyo jamaa, na wengi hawakumshabikia, waliona ni wale wasiopenda maendeleo yaw engine.

Ikawa ni utani tu, wengi wakawa wanamtania huyo mdada kwa kumuita ‘sister bikira..’ akawa anaitwa hivyo.

Kiukweli mimi sikuweza kumuuliza huyo mdada kama hayo maneno na utani yana ukweli ndani yake,..niliamini kuwa yawezekana,…mtu ukiamua unaweza ukaishii hivyo,, na kwa vile ule ukaribiu wetu wa kumuuliza hiki na kile ulishakwisha, nikawa sikupata muda wa kuwa naye karibu tena, kila mtu kwenye idara yake na maisha yakaendelea.\

 Ila mimi niliamini waliyosema watu kuwa huyo mdada ni mgumu, sivyo kama walivyokuwa wanadada wengine, huyo mdada hakuwahi kuwa na rafiki wa kiume, niliyewahi kumuona au kuambiwa …kama ilitokea kukutana naye hasa kwenye chakula maana tulikuwa na mgawahawa wafanyakazi wote hukutana humo, huyo mdada..alionekana kivyake vyake tu..na ole mvulana ajaribu kumgusa, hata kiutani, ataambulia matusi,…

Hapo kazini karibu kila mmoja alijulikana ni nani na mwenzake wa jinsia tofauti ni nani, na wengine wakatokea hata kuoana kabisa,…lakini kwa miaka kadhaa niliyofanya hapo, sikuweza kumgundua rafiki wa huyo msichana…moyoni nikasema,..basi huyo ni ‘sister bikira kweli’.

Miaka kama miwili ikapita…nikaja kufikiria kama mimi nina tabia yangu kuwa  msichana wangu wa kwanza kukutana naye nikutane naye ndani ya ndoa, sasa kwanini nisifanye urafiki na huyo mdada, ambaye naye anaonekana ana msimamo huo..lilikuwa wazo katika kuhangaika kumpata mwenza wa maisha, ilikuwa wazo, na nikawa na mikakati hiyo, lakini siweza kulifanikisha, maana kiukweli moyoni sikuweza kuvutika na mdada huyo kimapenzi. Nafsi hupenda kile kinachomvutia mtu.

Bahati mbaya, nikahama hiyo kampuni…

Baada ya miaka kadhaa, nikasikia, kuwa yule msichana kafariki,

‘Kafariki!!!... ilikuwaje jamani…?’ nikauliza kwa mshangao na masikitiko.

‘Alianza kuumwa, umwa..akawa anapungua, baadae akazidiwa, anatibiwa, anapona hali inarejea, anaanza kuumwa tena,..baadae..akapelekwa kwao…yaani binadamu hubadilika haraka sana, unamfahamu jinsi alivyokuwa mrembo,...watu waliomuoana kipindi kazidiwa, wanasema ule urembo ulikwisha akawa kama mzee, alikuja kubadilika akawa…mweusi….’akasema jamaa,

‘Mhh...kwasababu ya huko kuumwa au, , kwani alikuwa anaumwa nini…?’ nikauliza moyo sasa ukinienda mbio. 

Unajua kipindi cha nyuma, watu wakiumwa sana, na kukonda, na kubadilika mwili, moja kwa moja unajau ni ugonjwa gani,..kipindi hiho kulikuwa hakuna dawa za kusaidia kuongeza nguvu, kwahiyo watu wengi waliougua ugonjwa huo, waliteseka sana kabla ya umri wao kuisha. Kwa vyovyote iwavayo kila mtu ana umri wake.

‘Unauliza jibu bwana, mdada alipatwa na maambukizi, na ..huwezi amini, ..hata ndugu zake hawakuamini wakasema kalogwa, lakini hakuna siri, aliyemuambukiza aligundulikana, kwani naye kwa kipindi hicho alikuwa akiugua ugonjwa huo huo..na alipoulizwa, yeye alidai huyo mdada ndiye kamuambukiza, lakini uchunguzi zaidi ulionyesha kuwa huyo mvulana alikuwa hajatulia, yeye ndiye alimuambukiza huyo msichana.

‘Mhh..lakini si mlisema huyo mdada ni bikira.

‘Hahaha, tulijua hivyo, kiukweli hata mimi niliamini hivyo…hadi msichana huyo anafikia kuumwa, sote tuliamini hivyo….’akasema.

‘Haiwezekani…japokuwa kila kifo lazima kiwe na sababu..nahis aiumwa maradhi mengine tu..hata hivyo....’nikasema na jamaa akanikatisha kwa kusema.

‘Iliwezekana sasa, na alitembea na cha pombe fulani, wakati yeye alikuwa akituzarau pale kazini kuwa hatuna maana, walevi, eeh..si unakumbuka, alivyokuwa,akitudharau, ...wewe uliondoka, sasa ilifikia mahali hamgusi mtu....anasema yeye ana bwana wake yupo Ulaya...sasa kumbe alikuwa na mvulana cha pombe tu..hakuwa na hadhi kwa yule mdada,…sijui ilikuwaje..masikini mungu amsamahe tu...’akasema huyo jamaa.

‘Kwani hamkujua ilikuwaje..?’ nikauliza.

‘Aaah. ilikuwa kujulikana dunia hii ina siri,na kwa vile alikuwa akiringa, jamaa zake walikuja kuvujisha siri..tukajua kila kitu, ikawa kufuatilia kuhakiki tu....unajua msijifanmye mna imani sana ya dini, aheri muwe kama sisi...unajua imani. ya.kweli ya mtu aijue ni mungu pekee, ujidanganya ipo sisku imani hiyo inataisha kidogo kidogo kama mshumaa unavyokwisha halafu utakuja kuumbuka, ila niliumia sana, yule mdada nilimpenda, nilitamani nimuoe, akanikataa,…’akasema huyo jamaa akionyesha kusikitika.

'Mhh..lakini kweli wewe ukizi  kulewa, nani angekubali umuoe....'nikasema kwa utani.

'A wapi mimi nilikuwa nakunywa kistaarabu, sema, ndio hivyo kila kitu kwa wakati wake, ni kweli kuna muda nilizidisha, nikaumwa karibu ya kufa...kifua ikawa TB,...aisee, nilijua nakufa...nilipopona nikabadilika, ...hapo nikaona umuhimu wa kuoa...sasa huyo mdada alitolea nje kabisa, ..'akasema

'Labda alikuwa na mtu wake kweli...'nikasema

'Ndio yupo jamaa mmoja yupo Ulaya kweli, lakini jamaa huyo akaja kumuoa mzungu, na ndio maana huyo mdada akachanganyikiwa akaanza kulewa...japo hakujionyesha,...nasikia ndio hapo akaja kukumbana na cha pombe..lakini kwa siri kubwa...hayo ni mambo ya ndani, ...'akasema

'Oh, siku zake zilishafika...'nikasema

 Ni kweli kwa taarifa za kifamilia, japo ilikuwa siri, msichana huyo alifariki kwa HIV, kutokana na dalili, na hata vipimo,  kiukweli mimi sikuamini, wengi hawakuamini..japo kwa hivi sasa HIV, unaweza kuipata kwa njia nyingine ila kwa huyo mdada ilikuja kuthibistishwa..aliipata kwa namna gani

Watu katika kuchunguza sana, kumbe, huyo mdada alikuwa akitembea na mvulana kwa siri sana kwa vile alikuwa ni jirani yake..ilikuwa ni kwa siri sana…wanasema alifanya hivyo kwa siri, na hakufanya kwa vile anampenda huyo mvulana, maana kiukweli hawakuwa wanaendana..ila kulikuwa na sababu za kuchanganyikiwa....

Ilivyoonekana, alifanya hivyo, pale anapozidiwa, mawazo na mengine yaliyokuja kusemwa baadae msichana huyo akatokea kuwa mpweke, alikuwa hana rafiki tena, akawa anawachukia wanaume, kila mwanume kwake ni sawa na huyo aliyemuacha solemba, swali likawa ilikuwaje huyo cha pombe amuone sio sawa na wanaume wengine.

Tatizo huyo msichana hakupenbda kuwa muwazi, na .maumbile ya kibinadamu hufikia sehemu utashindwa kuvumilia hasa ukiwa unatumia kilevi..kiukweli yasemakana, siku katika masiku ubinadamu ulimzidi, akakwaana na huyo mvulana, ilikuwa kwa bahati mbaya tu kama alivyokuja kusema..

'Hiyo bahati mbaya, ikaja kuwa mazoea hasa akizidiwa, 'alijitetea.

'Ilikuwa nawaza sana, ..mpaka nataka kujiua,...sasa huyo mvulana akawa ndiye mtu wangu wa karibu wa kuniliwaza,,,akawa anakuja kwangu, usiku wa manane maana nilikuwa naishi naye nyumba moja sema ni chumba tofauti, wote ni wapangaji'

Kiukweli huyo msichana  hakutaka kabisa watu wajue, na kiukweli hakumpenda kabisa huyo mvulana,..na yeye alitaka watu wajue kuwa yupo hivyo, ..bikira. Ila kilichoharibu ni kwa sababu ya huyo mchumba wake kumtelekeza.

Na zaidi ya hapo huyo mdada ndoto zake, zilikuwa  yeye aje kuolewa na watu wenye uwezo kwasababu wapo wengi walimtaka tena kindoa akawakataa.

‘Mimi siwezi kuolewa na mtu kama huyo…hana nyumba wala gari….mmh, mimi siwezi kuolewa na mtu kama huyo hajasoma,..ikawa zake ndio hivyo, siku zikaenda, hadi mauti yanamkuta,
Sasa ilikuwaje aje kutembea na huyo mvulana, ambaye hata kazi ya maana hana,..msikuma mkokoteni, na akipata peza zke ni kulewa tu,..siri ikaja kuvuja,!

**********

Inatokea, kiubinadamu,..tunahitajia umaarufu Fulani, lakini umaarufu huo, uwe wa kweli  , utoke moyoni. Usiwe wa kuwaonyesha wanadamu tu....na hasa umaarufu wa imani. 

Umaarufu wa imani haudanganyiki, utawadanganya wanadamu wenzao, lakini sio muumba wetu,…mola wetu anatufahamu zaidi tunavyojifahamu wenyewe, yeye anajua imani ya mja wake ni ipi ya kweli. Kiukweli  wapo wanajitahidi lakini nafsini mwao, kuna mambo mengi ya tamaa, husuda chuki, nk...na, wapo wanafanya mengi mabaya kwa hisia..nafsi zao zina siri kubwa sana.

Cha muhimu ni kumuomba mole wetu atusaidie tuweze kufikia malengo yetu..yale tunayotamani yawe, yale ya haki, yaweze kuwa hivyo,..na atusaidie kuziondoa tamaa mbaya nafsini mwetu, atujalie tuweze kuwapata wenza wema katika maisha yetu.


Ni mimi: emu-three

Saturday, July 6, 2019

HUJAFA HUJAUMBIKA...



'Hivi kwanini mimi,...., nimemkosea nini mwenyezimungu...'nilisikia suti hiyo ya huzuni na kunifanya nisimame ghafla, na kunifanya nisite kuendekea na safari yangu, nilihisi mwili ukinisisimuka...'nimemkosea ni mwenyezimungu...' kauli hiyo ilinifanya nigeuze kichwa kuangalia kule nilipohisi sauti hiyo imetokea.

'Oh Mungu, nimekosa nini mimi jamani mpaka nipitie majaribu yote haya, ..mungu wangu naomba unionyeshe tu njia...'maneno ya huzuni yaliendelea wakati huo nimeshageuza kichwa kuangalia sauti hiyo inatokea kwa nani.

Kwa sauti tu,nilihisi ni sauti ya mwanadada, lakini macho yangu yalipotua kwa huyo ninayehisi kuwa ndiye aliyekuwa wakiongea, niligwaya.

Alikuwa binti mdogo sana, tofauti na nilivyodhania.

Kwanza kwa tahadhari nilitembeza macho huku na kule..maana dunia hii imegauka sivyo ndivyo, ya walimwengu ni mengi... kuna mitego mingi ya wahalifu inafanyika hivyo, unajitoa kwa wema unaangukia kwenye mitego ya hao watu, wanakudhuru au kukunyanganya kila na kukuacha uchi. Ila kilichonitia matumaini ni kuwa eneo hilo lina nyumba za watu, na nyumba nyingi ni kubwa zenye ukuta, na wengi wameweka nyaya za ulinzi, kuashiria kuwa wanaoishii humo ni watu wenye uwezo wao.

Niliangalia eneo lile alipokuwa huyo binti..nyumba hiyo kama nyingine ilikuwa na ukuta mkubwa tu na, ..juu yake ilionyesha kuna ulinzi wa kitaalam, ..nikajiuliza huyo binti anafanya nini kwenye eneo hilo, ..hajui kuwa nyumba hiyo ina ulinzi, na wenye nyumba hiyo hawatakubali watu kukaa eneo hilo kiusalama...na kwanini kakaa hapo, na anamlilia nani..

Nilipoona nazidi kutingwa na maswali, ....nikaamua jambo, nikavuta hatua moja, mbili....kabla sijafika pale alipo huyo binti,...na ukumbuke kwa muda huo, bado alikuwa akiongea kwa kulalamika kuhusu masahibu anayokumbana nayo...

Mwili uliendelea kunisisimuka, na hii ni kuashiria kuwa kuna hatari,...mimi nina hisia hizo, mwili ukinisisimuka, ujue kuna jambo la hatari ...lakini nafsi haikunipa uwoga, nafsi ilinipa ujasiri, kuwa nahitajia kujua, nikijua nitajua la kufanya...nikawa sasa navuta hatua, ...

'Ewe mola wangu, nionyeshe kosa langu, hadi nitaabike hivi...nimekuwa mtumwa wa walimwengu, wananichezea kama mpira wa karatasi, naadhirika, na hata wale niliowategemea kuwa watakuwa msaada kwangu wanageuka kunidha....dha...lilisha...'hapo kwikwi ya kilio.

Hapo na mimi nikasita mguu ukawa mnzito kuendelea ...nikatulia kwanza, akilini nikichanganua, je haya ni yangu, ..yasije yakawa maji mazito kwangu, ..aah, nikajipa moyo, ..ngoja nikasikia kwa kulikono,...nikaendelea kutembea...na sikuvuta hatua mbili, mara nikasikia...

'Mimi  ...siwezi tena..bora nife ..bora nijiue.'

Mungu wangu, bora nijiue...

Hapo sikuweza kusubiria, nikahisi nina dhamana, hii ni dhamana maana ni kwanini mola akanifanya niweze kuyasikia hayo, na ni kwanini, niache kiumbe kama huyu ..binti mdogo tu, aje kufanya, hilo alolodhamiria,na ni mashahibu gani yamemkuta hadi kufikia kudhamiria hivyo. Nafsi ikaingiwa na mshawashwa,..ikatamani kujua,...

Nikamsogelea,,,,.

Hata pale niliposegea hadi kumkaribia, bado alikuwa hajafahamu kuwa kuna mtu alikuwa bado hajafahamu kuwa mimi nipo hapo karibu yake, na hata kabla sijaweza kutoa sauti ya kumsalimia huyo binti , nikasikia sauti kali ikitokea ndani mwa hiyo nyumba, ambapo huyo binti kajiegemeza ukutani mwake.

'Huyu mshenzi kaenda wapi....we Taabu, ...we Taabu,...' sauti hiyo ilimfanya yule binti akaurupuke, na kusimama, hapo akaniona, akashika mkono kuziba mdomoni, lakini ...

'Usigope mimi sio mtu mbaya
'Ina maana umesikia nilichokuwa nikiongea
'Hapana...sijui uliongea nini...'nikasema
'Mungu wangu ..'akasema hivyo tu na haraka akakimbilia ndani

Kesho yake nilipita eneo hilo tena, nia ni kukutana na huyo binti, nijue ni nini kinachoendelea kwenye hiyo nyumba, nilipofika hapo nilikuwa watu wamejikusanya
'Kuna nini jamani...?' nikauliza
'Kuna binti kataka kujiua,...'akasema
'Kwanini
'Hata sisi tumebakia kujiuliza tu, na wenye nyumba hawataki kuelezea ukweli, wanasema hata wao hawajui
 Mara nikaona gari la wagonjwa likitoka, ..nikajua watakuwa wamemuwahi, ...
'Akipona ashukuru mungu...'ilikuwa kauli ya askari mmoja aliyetoka kwenye hiyo nyumba
'Kwanini unasema hivyo?'
'Sumu aliyokunywa ni kali sana...na walichelewa kutoa taarifa...'akasema askari

Kiukweli niliumia sana, ni kwanini sikufanya jitihada za ziada kukutana na huyo binti, nikasema na hata hivyo sikukata tamaa, nikafanya utafiti kujua huyo binti kapelekwa hospitalini gani, na wakati nauliza uliza ndio nikakutana na mama mmoja aliyesema anamfahamu huyo binti tokea akiwa mdogo.

'Sasa kwanini kakimbilia kutaka kujiua...?' nikauliza

'Mhh...we acha tu, hujafa hujaumbika, usilolijua ni sawa na kiza cha totoro...yule binti kapitia masahibu mengi, na huwezi amini huyo anayeishi naye ni mama wa kambo, mama yake alishafariki....

NB: Bado tupo kwenye maajribio, ili tuweze kurudi tena.

Ni mimi: emu-three

Monday, October 8, 2018

TUSHUKURU NA WALA TUSIKUFURU


 JE NI ZIPI NEEMA ZA MOLA WETU TWAWEZA KUZIKANUSHA…

Nikiwa kwenye dala dala, niliwaona mabinti wawili, wakiwasiliana…awali kwa fikira za haraka nilhisi ni majigambo,…maana wanaongea kwa vitendo zaidi ya kutumia midomo yao,..au ni katika namna ya  kuhimizana jambo fulani, lakini nilipochunguza  kwa makini nikagundua, …sio kuongea kwa kuhimizana..

Nikasogea karibu, nikijua wanahizana jambo fulani...

Nikagundua kitu,..hawa watu wanaongea kwa ishara, wakitumia vidole na mikono...walikuwa wakiwasaliana hivyo, na walikuwa wakielewana kabisa,..

 Baada ya kuligundua hilo hisia zangu zilinifanya nihisi kama kutoa machozi!!...ni likwenda mbali zaidi kimawazo…hawa wanaweza kuongea wakafurahi, lakini sisi hatuwezi kujua wanaongea nini labda ukisie tu..

Katika hisia hizo, nikakumbuka maneno matakatifu yanayosema ‘…basi ni ipi katika neema za mola wenu mlezi  mnayoikanusha…’ kwa mwenye imani ya kuelewa, ukisikia hayo maneno, utatafakari sana, na unaweza kutamani hata kulia.

Kiukweli, sisi kama wanadamu tuna neema nyingi tu mola katujalia, hata kama utaikosa mojawapo ya hizo neema, una macho, una masikio, una kiwili wili, na unaweza kupumua,..kuacha hayo, kuna mambo mengi ya ajabu, yote ni neema za yule aliyetuumba…! Nilipofikia kuliwaza hilo, nikainua kichwa na kuwaangalia wawili wale.

Niliwaangalia sasa kwa hamasa zaidi, sio mimi peke yangu, wengi, walizamisha mawazo yao na kuyaelekeza kwa mabinti hao wawili wakiwa wanaendelea kuongea kwa furaha kwa kuonyesha ishara ile ya vidole na kiganja cha mkono,,..walikuwa wamevalia vyema kimaadili, na mkononi mmojawapo alikuwa kashikilia simu.

Ilionekana mabinti hawa wawili walikuwa wakienda sehemu , na wakawa wanawasiliana na jamaa zao kwa simu..sasa hapo utajiuliza walikuwa wanawasilianaje na hao jamaa zao huko, na mimi niligunduaje hilo,  kuwa wao walikuwa wakiwasiliana na jamaa zao hao, wakati wanatumia ishara tu...

Mimi nilivutika nao sana, ..nikajitahidi , nikasogea hadi nikafika pale waliposimama, nikajitahidi hadi nikaona ile simu, vidole ndivyo vilikuwa vinafanya kazi, kumbe huyo mmoja alikuwa akiandika ujumbe wa maneno kwa jamaa zao hao..

Swali likawa anaadika nini...?

Kiukweli nilitarajia, atakuwa anaandika kiishara shara kama vile anavyowasiliana na huyo mwingine...hapana, kwenye simu niliona akiandika, kwa lugha sahihi ya Kiswahili na kiingereza.

Ndio sasa nikawa na uhakika , kuwa kumbe ni wenzetu hawa wenye ulemavu wa kuongea, na kusikia, kwa lugha isiyo rasimu, watu wanawaita ‘mabubu na viziwi’.

Wakati huo…watu wengi mle ndani ya gari,wakawa sasa wanawaangalia kwa hamasa, maana mabinti hawa walikuwa wakiwasiliana huku wakicheka, kuashiria wanaongea jambo la furaha na kuelewana vyema kabisa, ni kama mimi na wewe tunavyoweza kuongea kwa mdomo na kwa sauti.

‘Je ni ipi neema ya mola wetu mlezi unayoweza kuikanusha…’ hapo nikawa najiuliza mimi mwenyewe, nikitafakari na jibu likawa  ‘hakuna…’.

Wewe ukijiona huna hiki, au kile, ujue una hiki au kile ambacho mwingine hana, na huenda kina thamani kubwa zaidi ya kile unachoona huna, sema wewe hujui tu…mara nyingi, tunakimbilia kulalamika, na kujisikia vibaya na hata kusema kwanini mimi

Je hawa...je yule mwenye mapungufu hayo asema nini..ni kweli katika maisha yetu ya kawaida, hao,  …tunaokimbilia kuwaita wana mapungufu fulani, tukaona hawawezi kufanya jambo, kumbe kwa kadara za mola, kawajalia mambo ambayo hata wewe na ukalifu wako huwezi kuyafanya…

Nikawaangalia mabinti wale tena, moyoni nikasema kumbe wenzetu hawa wanacho zaidi ya kile tulicho nacho sisi, kwa vipi…!! Utalishangaa hili,…

Sisi twaweza kuongea kwa mdomo kwa lugha tuliyo nayo, lakini je kama huwezi kuongea kiingereza unaweza kuwasiliana na muingereza,  mkaelewana,..au kama unaweza Kiswahili hujui kuongea kichina, unaweza kuwasiliana na mchini mkaelewana, kwa vipi sasa , labda upate mkalimani

Lakini kumbe kuna lugha ya ishara...sasa kwa ukamilifu wetu wa kuweza kuongea na mdomo, na kusikia, lugha hiyo ya mawasiliano hatuiwezil, lakini wenzetu hawa kwa lugha yao hiyo ya ishara ..wanaweza kuwasiliana na mtu yoyote duniani…je hii si neema kwao, je ni ipi neema ya mola wako waweza kuikanusha....

Hapo nikamshukuru mungu, kuwa yeye ni muweza wa kila kitu, yeye, kakadria kila kitu  kwa namna yake, kampa kila mtu kwa namna ainayo yeye ni sahihi kwa huyo mtu au kiumbe hicho..sisi hatuwezi kulifahamu hilo.

Katika dunia hii kila mtu ana matatizo yake, ..kila mtu ukimtafiti ana matatizo yake, mengi tu, sizani kama kila mtu kakipata kila kitu anachokitaka yeye mwenyewe...tunaweza kuhisi kuwa matajiri hawana shida, si wana pesa bwana.

Lakini ndugu yangu, ... tajiri, na utajiri wake wote ana matatizo yake lukuki, sema yeye kutokana na utajiri wake anaweza kuyafukia matatizo yake kwa pazia,..wangapi, wana mali, hawana watoto, wangapi wana mali, lakini hawana raha ya ndoa,..wengine wana maradhi yanawatesa, hata kuitumia mali yake kwa raha hawezi tena wengine wana maradhi ya kisukari, wana presha, hawatakiwi kula vyakula fulani fulani hata kama wanavitamani.

Wapo wengine na utajiri wao huo, walitegemea watoto wao waje kuwasaidia, waishi nao kwa furaha,, lakini watoto hao hao wanageuka kuwa mtihani kwao,..watoto wengine hawasikii, wavuta unga, au wana matatizo haya na yake…lakini mapesa wanayo. Je hizo sio shida kwao...

Ina maana ya kuwa, hata kama una matatizo, au una mapungufu fulani bado kuna neema umepewa na mola wako ambazo, watakiwa ushukuru kwa kuwa nazo...na huenda ukiweza kuzitumia vyema hizo neema, unaweza ukayashinda hayo matatizo uliyonayo, ...

Ndio, unaweza kuishinda hiyo mitihani, hata kama sio kwa kuiondoa, lakini yale matatizo yakazidiwa na hizo neema ulizo nazo, na wewe kwa imani ukaziona, ukujiona una vitu mola wako kakupatia, ukajawa na imani hiyo ya kushukuru, zile shida nyingine zitafifia tu...muhimu kumbuka jambo moja, hizo neema  kakubariki mola wako, bure tu,..je haitoshi wewe kumshukuru kwa hizo neema.

Wakati bado nipo kwenye hiyo safari yangu, nilipita sehemu na kukuta watu wapo kwenye harusi, na pembeni yake mbele kidogo tu, kuna msiba..watu wanalia, ..wamepoteza mwenza wao,..na mtaa wa pili yake karibu na hizo nyumba nikawakuta wakina mama wakipiga vigelele, wamajaliwa mtoto mchanga,..

Je hizo si neema,

Ajabu kabisa..leo kule nimewakuta wati wanalia, mwenza wao safari yake imeshafika, hapa anazaliwa mwingine, mtu mwingine mpya anakaribishwa kwenye hii dunia ya mitihani…na wakati huo huo kule nilipita harusi, wanatayarishwa wengine, kwa maandalizi ya kuleta baraka ya kizazi kipya, ..je hizo zote ni nini, ni neema, na ni nani kazileta , japokuwa nyingine zinaumiza moyoni…

Ni ipi kati ya hizo neema alizotupatia mola wetu twaweza kuzikanusha, hebu niambie wewe

Kweli ukikosa hiki, utalalamika...kwa vile mwenzako anacho au sio..lakini huenda ungelikuwa nacho, huenda ingelikuwa mengine, hayo hatuwezi kuyaelewa kwa utashi wetu mdogo wa ufahamu.

Sasa ni wakati, hicho ulicho nacho, ..shukuru sana, kama una macho, una masikio, umekamilika kwa kila kitu, shukuru sana..na ujue wenzako wasio nacho wanakitamani, japokuwa kwa kutokuwa nacho, mola kawatunuku neema nyingine zaidi ya hivyo ulivyo navyo..tusikimbilie kulalamika, au kuhuzunika tukakufuru.

Hata hivyo kuna wengine ambao mola kawajalia lakini kujaliwa kwao huko, wao badala ya kutumia vyema, wanatumia kwa isirafu,… wapo hao, wanaagiza sahani hotelini, anagusa tu, anaacha, kinaenda kumwagwa...au ndani kwake, kajaza zaidi ya hata ya uwezo wake, huku anamuona jirani yake hana..hataki kumpa, ni bora kiharibike ndani, jamani …wapo wenzetu hata huo mlo mmoja wa siku hawauwezi, na sio kosa lao, ni shida,….inasikitisha....sana

Hii ni nasaha kwangu na kwako pia, ,…tuzishukuru neema za mola wetu mlezi  na wala tusikufuru…


Ni ujumbe wetu sote kwa leo...niwatakie jumatatu njema , jumatatu yangu ya kumbukumbu, ....


Ni mimi: emu-three

Friday, October 5, 2018

NGUMI MKONONI-athari za ulimi



NGUMI MKONONI-athari za ulimi.


'Jamani watauana hao watu, mbona mpo watu wazima hapa mnawaachia watu hao, wanapigana na kuumizana hivyo, waamulieni jamani...'ilikuwa sauti ya mwanamama.

Ni nani atamsikiliza, watu ndio wanainua simu zao juu kuchukua picha za video, na wengine wanashangalia…..ni ajabu kabisa dunia ya leo.

Kwa muda ule, mmoja alishatoa ndutu kichwani, kavimba…na mwingine jicho limevimba, na bado kila mmoja ana hasira na mwingine….

’nitakuua, nitakumaliza…’linafuta tusi, ndio lugha iliyosikika kutoka kwa vinywa vya mabondia hao wasio na kibali, ..ni wakubwa, yawezekana miaka thelathini hivi.

Akatokea askari mmmoja kupita eneo hilo..ndio ikawa salama, wapiganaji hao, wakaachana utafikiri refa kawaambia ‘stop’…sasa damu zinawavuja…wamevimba hoi bin taabani..

‘Ehee, endeleeni sasa…’akawatania mmoja wa wapambe waliokuwa pembeni na simu yake mkononi.

Yule mtu wa usalama akafika, na kuuliza ni nini kinachoendelea hapo…, watu kimia wengine haoo, wanaondoka mdogo mdogo, na bahati nzuri yule mtu wa usalama akawaona  hao wanandondi  wawili wakijaribu kujiweka sawa, lakini mwili haujifichi , ushahidi upo, utamficha nani hapo;
.
'Haya nyie wawili, tuambieni, kisa cha  nini cha kuumiza dhamana ya mungu aliyowapa, hamjui huo mwili ni dhamana kwenu, hapa duniani ni dhamana kwa jamuhuri, na huko kwa mungu, mtakuja kuulizwa, kwanini mliuumiza huo mwili uliopewa kama dhamana,...'akasema mtu wa usalama, jamaa kimia.

'Haya mumeumizana mumepata faida gani, nikawafunge  sasa hivi, nina mamlaka hayo, nifanye kazi yangu eeh, niambieni sasa mnapigania nini....?' akauliza yule mtu wa usalama ,, wanandondi wale wakawa wanajitetea

 'Hivi mwili ni dhamana kwa jamuhuri...'akasema jamaa aliyekuwa nyuma yangu, na mwingine akasema

'Wewe hujui hilo, ...jinyonge upone uone utafanywa nini...'akasema huyo mwingine..huku watu wakianza kutawanyika , kuendelea na shughuli zao. Na wengine wakiogopa ushahidi…ndio maisha yetu hayo…

 Nilisikia wale jamaa wakiendelea kuhojiwa..
.
'Huyu jamaa kazoea kunitukana, matusi mabaya, leo sikukubali, nimetaka kumfundisha adabu...'akasema mmojawapo.

'Wewe je..hujanitukana mimi. ..na pia umezoea kunidokolea bidhaa zangu za sokoni, ndio tabia yako hiyo mwizi mkubwa wewe…’akasema

‘Wewe umeniona ni kikuibia, ..wewe ni hisia zako tu…wivu tu, maana kila mara mimi nauza wewe huuzi,…’akasema mwingine

‘Kakutukana kasema nini…?’ akaulizwa

‘Yeye, kila kauli unayotoa ni tusi, tena ananitukania mzazi wangu, mama yangu...'akasema mwingine.

'Mimi sijamtukana mama yake nimemtukana yeye mwenyewe, kwasababu kazoea kuniibia , yeye ndio tabia yake hiyo chafu, kazoea,…wizi…’akasema mwingine.

Ilionekana ni jaziba za ujana, lakini kweli matusi yalitoka, kila mmoja alitumia ulimi wake akatoa matusi, kauli chafu, na mbaya zaidi matusi yalielekezwa kwa wazazi, wazazi ambao hata hapo hawapo, wazazi wanatukanwa , wazazi waliwafanya wawepo hapo, leo hii wana minguvu, wanawatukana wazazi wao...si laana hii .

‘Hivi nyie watu mnafahamu athari za kutumia ndimi zeni vibaya,..na shetani anapenda sana kupitia njia hiyo, keshajua madhaifiu yenu yapo huko kwenye ndimi zenu…na kwanini muwatukane wazazi waliowazaa, wakawalea..?' wakauliza wakabakia kimia

'Haya niambieni, ni….nani mshindi, au bado hamjamalizana,.. tuwaachie mpigane tena, haya piganeni…’akasema huyo mtu wa usalama....jamaa wakawa wamenywea nahisi muda huo ndio wanaanza kuhisi maumivu.

Mimi sikuwa na muda wa kujua hatima yao, akilini mwangu, nikawa najiuliza tu;

‘Iweje watu watukanane, na ni nani wanamtukana hapo, kama mtu anamtukana mzazi wa mwenzie ina maana gani hapo, sio kajitukania mzazi wake pia....haya sasa matusi yamezaa ugomvi, ugomvi umefikia kupigana, ni nini athari za kupigana, kuumizana,..kuna faidi gani wameipata hapo, je tusi linaweza kumgeuza mtu akawa hilo tusi..mimi hapo sijui…?’ nikajiuliza tu..

'Kumbe ni ‘ulimi…kumbe ni mtihani wa ndimi zetu..' nikajikuta nimesema hivyo kwa sauti.

Ulimi umekuwa ni mtihani kwetu, na kutokana na ulimi, wengi wetu, tutaingia motoni, tusipopata muda wa kutubia, kabla mlango wa toba haujafungwa…na nikizungumzia ulimi , sio ulimi tu…ni pamoja utumiaji wa  ‘kalamu’ ..na kalamu hapa nina maana ya matumizi yote ya kuandika, …hasa huku mtandaoni, kwenye simu zetu..hapa..tuna kesi kubwa ya kujibu mbele ya mungu.

Enyi mliopewa nafasi hiyo ya kutumia ulimi, kutumia kalamu,…kwenye mitandao , simu , tv, redio nk…tuweni makini sana kwa kile tunachokiandika, au kuongea, wengine wanaandika ‘matusi’ kabisa kama wanavyoyatamka kwenye ndimi zao, wengine imekuwa ni biashara, ukipata wanachama wengi, unapata ingizo, wengine ndio hao wanatunga hadithi za mambo yanayoathiri hisia za vijana,..

Ni nani anajiuliza athari za kuhamasisha ‘ngono’…watu wanajiandikia tu…huishii kwa hao wanaosoma leo, watakuja kusoma wajukuu zako, watoto wako, je hao waliosoma , wakahamasika, kufanya hayo maasi kutokana na hisia ulizowajengea,..hujui kisa ni wewe, je hujui kuwa wewe ndio umewalogeza 'uasherati'..na yote ni kutokana na kalamu yako…ndugu yangu unayefanya hivyo, una kesi ya kujibu…

Ukumbuke jambo moja,…..ushahidi wa kuandika haufutiki, unachoandika leo mtandaoni hakitafutika miele…usijidanganye kuwa utafuta kwenye simu yako, kwenye komputa yako, nk..hayo hayafutiki kama yameshaenda hewani. Ni halikadhalika, ulichoongea leo na ulimi wako, ukazua ghadhabu, ugomvi,...nk...hakifutiki, ulimi utakuja kukielezea mbele ya mungu, na kama watu waliumizana, mwili utatoa ushaidi, kisa ni nani,..je uliwahi kuliwazia hilo kwa mapana yake

Ndugu yangu…andika jambo la hekima ili iwe sadaka yako ya baadae, ..

 ‘Ulimi..’, sasa umekuwa ni tatizo. Hatujui jinsi gani ya kuuchunga ‘ulimi wetu..’ tukikaa wawili ni kutetana tu,..achilia mbali hayo matusi,…kusengenya imekuwa ni donda ndugu..unajua kusengenya ni sawa na kumla mtu nyama yake….sijui kama tunalifahamu hilo...umekula nyama za watu wangapi...

 Haya labda ndio huko kutafuta ‘kiki..’, sawa utapata wafuasi wengi, na wengine ni biashara kwasasa, lakini ukumbuke ulichoandika atakuja kuulizwa nacho..na wapo waliondika zamani sasa ni viongozi, wamekuja kuonyeshwa walichoandika kipindi hicho, imekua ni aibu kwao..sasa hayo ni ya hapa duniani, je huko mbele ahera ambapo kila la siri litawekwa wazi, kila ulilofanya ukiwa umejifungia chumbani, litabainika,...kila mtu ataliona,..yabidi tulie sana kwenye toba...

 Tunaambiwa na watu wa imani, haya  ya ulimi, hayaishii hapa hapa duniani,Ulimi utakuwa ndio shahidi, siku hiyo ya kiama, kila kiungo kitatoa ushahidi wake, kwa jinsi nafsi yako ilivyokituma,…huna cha kukwepa hapo,..ulimi utasema ulichoongea kwa kupitia wewe, mkono, macho, na kila kiungo chako…ni siku ngumu sana jamani,.

 Labda kwa wale watakaojiwa na imani wakatubia, wakapata muda huo wa kutubu madhambi yao, lakini sasa muda huo tunao, na kama tuliwatukana wazazi wa wenzetu, na ndio tabia yetu, tutawezaje kutubia hilo, maana toba ya kweli hapo ni uende kwa kila mzazi uliyemtukana umuombe msamaha..tutaweza hilo.

Yawezekana kabisa matatizo tuliyo nayo , mitihani tuliyo nayo ya maisha, na mabalaa mengi yanatokana na ndimi zetu, hulka na tabia zetu, hatujaweza kujichuja ,  tunachukulia kila jambo kwa jaziba,…kila jambo tunakimbilia kulalamika tu…kulaumu tu, mwisho tunachukiana, tunanyonyosheana vidole,...tunashikana mashati, tunaumizana…kila mtu anawaona, je hayo tunayoyafanya kwa siri tukijifanya hatuonekani, usiku tunawanga, hayo yote yatakuja kubainika siku hiyo ya hukumu…tutakuja kusema nini.

Ndugu yangu,  toba ya kweli ndio dawa ya maradhi haya ya ulimi..tutubu na tuache kabisa madhambi hayo…, na toba nyingine ni kukithirisha kutenda mema, mambo mema hufuta maovu yetu,…

Tumuombe mwenyezimungu atusaidie maana haya sasa ni zaidi ya uwezo wetu, bila neema yake yule aliyetuumba,  tutaangamia, ulimi, kalamu, mitandao..itatuangamiza,..leo twapigana makonde, kesho yaweza kuwa silaha…wengine walianza hivyo, hivyo… kikao kidogo ngumi, uchaguzi mdogo ngumi, …kidogo kidogo, uchaguzi mkubwa je…

Tumuombe mungu atuepushie hayo na chuki zilizojaa mafundoni mwetu ziyeyuke na kuwa upendo na amani…

Ila kwa wazo la leo, tukumbuke jambo moja tu…
.
'Maovu, hufutwa kwa wema, , tutende wema tufute maovu yetu..tutende wema, tuwezeshe wenye maovu, waone aibu ya kuendelea kutenda maovu yao, ili na wao waje kutenda mema,.., na tusizidishe maovu kwa kupigana na kuumizana, tutazidi kuifukuza Baraka, na neema.

 Hilo ndilo Wazo la leo, nawatakia ijumaa njema.


Ni mimi: emu-three

Thursday, September 27, 2018

YOTE NI KWA MAPENZI YA MUNGU-52


'Ndugu muheshimiwa hakimu, nawakilisha ushahidi huo…unao-onyesha sahihi za ndugu yetu Dalali, sahihi ambazo zinafanana...ile ya kwenye malipo inafanana na sahihi ya kitambulisho cha Dalali,..na sahihi hiyo ipo kwenye malipo yaliyofanyika benki kwa ajili ya mkopo, ulitolewa kwa jina la marehemu…’akasema wakili akipeleka ushahid ule mbele ya hakimi.
'Na pia inafanana na sahihi iliyopo kwenye mkataba...'akaongezea wakili huyo
Hakimu akawa anakagua…na kuwaonyesha wenzake, na wote wakawa wanatikisa kichwa kukubaliana na hilo, kuwa kweli sahihi hizo zinafanana..hakimu akauliza.
‘Dalali…hiyo sahihi kwenye malipo sio yako…?’ akaulizwa Dalali.
‘Si-sio ya kwangu muheshimiwa ha-ha-kimu…..’akasema na hakimu akarejea kuchunguza ile sahihi, na aliporidhika akasema.
‘Tutawaomba wataalamu wa maandishi waje kututhibitishia hilo, na kama ni ya kwako, ujue umeidanganya mahakama…’akaambiwa Dalali..
‘Lakini muheshimiwa kabla ya kulifanya hilo, ninaomba..muda, sijui ilivyotokea, nasema ukweli muheshimiwa, sio mimi…sijui ilikuwaje, sina uhakika muheshimiwa…..’akasema akihangaika kwenye kiti.
Mimi nikamsogelea Dalali, na kusema…
‘Dalali tuambie ukweli..kwanini sahihi yako inafanana na hii hapa ya kwenye malipo ya huo mkopo,…?’ akaulizwa Dalali sasa akiwa katulia.
Dalali akabakia kimia.
Mimi nikachukua zile nakala za ushahidi nikamuonyesha Dalali,..
‘Unaona hapa Dalali, chunguza mwenyewe kwa makini…hapa kwenye mkataba pia,..sahihi hii hapa ni ya kwako,..au tusema, inafanana naya kwako…wewe si umesema sio wewe uliyeweka sahihi yako, ..labda kwa niaba ya marehemu…iweje sasa sahihi hii hapa, ifanane ya kwako… eeh…?’ Dalali akaulizwa sasa yeye akawa anaangalia tu ile sehemu ya sahihi, hajibu kitu.
Hakimu akawa anawaangalia watu hao kwa uso wa kujiuliza, hakutaka kuingilia kati, aliacha mazungumzo hayo ya maswali na majibu yaendelee tu..
‘Dalali bora tu ukiri kosa, tuone haki ikitendeka, kukiri kosa ni uwajibikaji wa muungwana,…hakuna kilichobakia sasa, ukweli sasa upo bayana, ni muda muafaka wa kukiri kosa, utuambie tu ilikuwaje,…au unaoenewa .. je hii hapa sio sahihi yako…?’ nikamuuliza akabakia kimia;
‘Au labda eeh… utuambie kitu, labda, useme… sahihi zenu wewe na marehemu zinafanana ndio hivyo au…?’ nikamuuliza, na hapo Dalali naye akachungulia tena zile sahihi, halafu kwa sauti ya mashaka akasema;
‘Ni kweli sahihi zetu zinafanana,…’akasema na watu wakacheka.
‘Sahihi zenu zinafanana, sasa hivi unasema hivyo, ok…haya tuambie kwa vipi…?’ akaulizwa. Na watu wakacheka na kukatokea mngurumo wa mnong’ono, watu wengi wakinong’ona inakuwa ni mngurumo…Hakimu akagonga rungu lake , kukawa kimia
Dalali akasema akiwaangalia watu…
‘Ni kweli msicheke,…unajua nilishikwa na butwaa baada ya kuona hivyo…na sijui kwanini sikuweza kulisema hili mapema,..ni kweli kuwa sahihi zetu zinafanana, hata mwandiko, mimi nilikuwa napenda kumfuatisha sana kaka yangu huyo kila anachofanya tokea utotoni, nikawa naiga hata mwandiko wake,…na ikaja hata kwenye kuweka sahihi…sasa kwenye sahihi, tofauti yangu na bro,..bro yeye...’watu wakaguna.
‘Ni kweli jamani…bro yeye huwa anaweka nukta hapa mbele…’akasema, akionyeshea sehemu nukta inapowekwa…
‘Inua juu watu waone unachoongea…nahisi ungelikuwa na kalamu ungeiweka hiyo nukata,…au sio…lakini umeshachelewa Dalali…kubali tu yaishe…’akaambiwa na wakili, Dalali akainua ile nakala ya mlipo akionyesha wapi nukata inapowekwa.
Wakati anafanya hivyo mimi nikachukua karatasi nyingine ya malipo, ambayo ilionyesha malipo yaliyofanywa na kusainiwa na kaka yake…nikasema;
‘Kama hii hapa, au sio…hii ndio sahihi kamili ya kaka yako au sio…?’ nikamuonyesha na yeye akaangalia, halafu akasema.
‘Ndio kama hiyo hapo muheshimiwa, hiyo ni sahihi ya kaka …haina shaka…’akasema kwa sauti yenye kuparuza…koo limekauka ghafla;
‘Sasa kama ni hivyo, kwenye hii stakabadhi ya malipo, au kwenye huu mkataba,… wewe usema tu,…ulisahau kuweka hiyo nukta ili ionekane kuwa kaka yako ndiye kachukua hizo pesa, umeliona hilo kosa ulilolifanya eeh…, au ni yeye alisahau kuweka hiyo nukta,..?’ nikamuuliza na Dalali akabakia kimia.
‘Dalali, Dalali… tuambie ukweli Dalali, muda unakwenda, au tumuachie hakimu yeye mwenyewe atajua jinsi gani ya kufanya, ila muhimu hadi hapa, hili deni sio la marehemu, hili deni ni la kwako, ..japokuwa huku juu limewekwa jina la mlipwaji ni l;a kaka yako, lakini huku kwenye sahihi sio ya kwake..kwanini, ..sasa utuambie wewe....’nikasema
Dalali, sasa akawa anahema tu…, kiti akakiona hakimtoshi,..jasho linamtoka, akawa anazichungulia zile stakabadahi za malipo, nikamsogelea na kumshika mkono..
‘Naona nikusaidie usimame, ..utoke kwenye hicho, kiti maana kinakubana, au sio..?’ nikasema na watu wakacheka.
Dalali hakujali hilo, sasa akasema;
‘Lakini mimi sijui lolote kuhusu hilo, kwangu imekuwa mshtuko, na hapa nilipo kweli naanza kukubali kuwa huenda kweli hilo deni sio la marehemu….naanza kuliona hilo….’akasema
‘Ehee..tuambie ukweli ni la nani, …?’ akaulizwa
‘Hapa inabidi tuwaulize vyema watu wa benki…’akasema
‘Kwanini wakati sahihi ni yako, ukumbuke wewe unawaamini sana watu wa benki, wao wana utaratibu wao mnzuri tu..si umelisema hilo tena na tena, au…kwanini sasa unaanza kuwatilia mashaka…?’ nikamuuliza
‘Kiukweli muheshimiwa,..ndugu yangu…hili….linanifanya niwe kwenye mshtuko, je ina maana mizimu,…ina maana benki, ..haiwezekani…siamini hiki, kuwa ni mimi niliweka hiyo sahihi…hapana lazima kuna mtu….’watu wakacheka.
‘Mizimu ndio iliweka sahihi, hiyo au una maana gani hapo…?’ nikauliza na watu wakazidi kucheka.
‘Msicheke jamani, hapa…mnacheza na maisha ya watu, ..huu ni uonevu, mimi sijawahi kuweka hiyo sahihim mkicheka mnanifanya mimi ni mjinga, mimi sio mjinga hapa naongea ukweli, na huo ukweli utakuja kuwasuta mwisho wa siku, ukweli ukija kubainika, kuwa mimi sihusiki na lolote hilo…nasema hivi, mimi sikumbuki kufanya hivyo, hata sijui,…mimi nasema ukweli kabisa, muheshimiwa hakimu…’akasema
Watu sasa wakabakia kimia,..na hakimu akawa anatuangalia tu…
‘Labda kwa kumbukumbu zako,…Je wewe uliwahi kuweka sahihi kwenye kitu kama hiki, au kwenye mkataba wowote huko benki kwasababu fulani nyingine,…?’ nikamuuliza
Dalali akawa kama anawaza halafu akasema;
‘Haa-ha-hapana..sio mimi niliyeweka bwana…’akasema hivyo, na watu wakacheka na hakimu akagonga rungu lake watu watulie.
‘Naona upo mbali sana…nauliza hivi, Ina maana wewe hujawahi kuweka sahihi…kwenye mkataba,… labda ulipewa tu huko benki na labda kwa bahati mbaya,… hukuwahi kuusoma kuwa ni mkataba,…labda…, kwa haraka zako wewe ukaweka sahihi yako tu, labda…eeh. Hebu kumbuka..?’ akaulizwa
‘Hata sikumbuki…..’akasema na watu wakacheka.
‘Dalali…kumbuka vyema ndugu yangu, hili sasa ni lako…sio la kaka yako tena, huu mkopo sasa ni wa kwako…’akasema wakili
‘Kwanini uwe ni mkopo wangu, mimi sijachukua huo mkopo,…siwezi kukubaliana na hilo kamwe….’akasema
‘Sasa Dalali, sisi tutakusaidiaje….hebu tusema hivi…, labda katika mabadiliko ya kibenki, ..eeh huko benki, si kulitokea mabadiliko …hilo si unalijua, au sio, maana wewe ulikuwa unafuatilia sana hilo….labda kipindi hicho, wewe…ulipewa nasema kwa mfano, maana haa hivyo haiji…au sio…’nikasema
‘Sijakuelewa muheshimiwa…?’ akaniuliza
‘Nasema hivi, jaribu kuvuta kumbukumbu zako, ukumbuke vyeka, kuwa labda ulitakiwa wewe uweke sahihi yako kwa niaba ya kaka yako…maana hapa kweli. hakuna nukta, kuashiria kuwa hayo malipo hakuweka sahihi marehemu , au siowewe ndiye uliweka hiyo sahihi,…?’ akaulizwa na akaendelea kuzitizama zile karatasi.
‘Dalali, hiyo sio sahihi yako……?’ akaulizwa
‘Inaonekana kama ya kwangu….’akasema
‘Lakini sio sahihi yako…?’ akaulizwa
‘Mimi siwezi kuwa na uhakika….’akasema
‘Kwanini…?’ akaulizwa
‘Ni kweli, kuna …kipindi nimeshawahi kuweka sahihi kwenye stakabadhi za benki kwa niaba ya kaka….na..na ..hata kwenye malipo…lakini aliniambia yeye mwenyewe kutokana na ya kwua alikuwa mbali, na alihitajia pesa kwa haraka….’akasema
‘Dalaliii….ujanja wako upo wapi, unakumbuka awali ulisemaje, kuwa kama ni malipo ya benki, wewe hujawahi kuweka sahihi, kaka yako ndiye alikuwa akifanya hivyo, wewe hukuwahi kuweka sahihi yako kwenye malipo,…hukusema hivyo awali…?’ akauliza na hapo akabakia kimia
‘Dalali,Dalali ....tuamini lipo sasa ndugu yangu, kauli ya kwanza au hii ya pili…?’ nikamuuliza
‘Awali nilisema nikimaanisha malipo, ndio…bro mara nyingi kwenye malipo alikuwa akiandika yeye na kuweka sahihi yeye, na ananipa mimi nikalipe au kuchukua pesa, ..lakini ilitokea dharura kama hiyo, ..ni mara moja au mbili hivi tu…’akasema na watu wakacheka,.
‘Ni mara moja au mara mbili hivi ti…, na huenda ya tatu na ya nne, au zaidi ya hapo, ndio ikawa hii ya kusaini malipo ya mkopo na mkataba, au sio…?’ nikamwambia kama kumuuliza, na yeye akakunja uso kama kukerwa, halafu akasema
‘Sio kweli muheshimiwa, mimi sijaweka sahihi kwenye huo mkopo, siwezi ku-ku-jua hilo lilitokeaje,..naombeni muda wa kufikiria tafadhali…’akasema
‘Unahitajia muda gani hivi wa kufikiri, maana tupo mahakamani, na muda ni muhimu sana, eeh, tuambie unahitajia muda gani wa kufikiri…?’ akauliza na hapo akabakia kimia…na alipoona anasubiria yeye kujibu akasema;
‘Nasema hivi,…kwenye malipo ilitokea hiyo dharura, nikafanya hivyo, lakini sio kwa huo mkopo, huo mkopo mimi sijui..na kiukweli kuna mambo mengine ambayo sio ya malipo, bro, alikuwa akisema niweke sahihi kwa niaba yake…’akasema
‘Kwahiyo ile kauli yako ya mwanzo unaikana…?’ akaulizwa, na kukaa kimia
‘Sijaikana,…mnielewe jamani…kuna utaratibu na dharura…kikawaida utaratibu wa bro ilikuwa hivyo,..lakini ikatokea dharura…’akajitetea hivyo.
‘Na je kwenye mkataba wa benki ilikuwaje maana ni sahihi yako pia…unaiona ilivyo,…, haina nukta mbele, hebu ikague vizuri, usije kusema imefutwa na nukta ya kaka yako, inakolea sana, nimepitia malipo yote aliyoweka sahihi…ni hivyo hivyo, angalia, hii nah ii na hii hapa, nukta imekolea sio y akugusa…naona alihakikisha hiyo nukta inaonekana vyema…’akaambiwa
‘Ni kweli, yeye alihakikisha kwenye sahihi zake zote hiyo nukta inaonekana vyema, aliwahi kuniambia kwenye sahihi, kila kitu kwake ni muhimu, na …hiyo nukta ikawa …ni kama nembo yake, kwenye sahihi yake kutofautisha na sahihi yangu…’akasema Dalali.
‘Hapo umetusaidia sana..sasa tuambie…eeh au, bado unahitajia muda wa kufikiria zaidi…?’ akauliza na akabakia kimia
‘Au bwana Dalali…, labda tukusaidie hivi..…labda uliambiwa uweke sahihi hiyo na benki bila yaw ewe kujua,…mhh, au danganya danganya hivi, kujitetea..labda kuna mtu alikuhadaa, …kijana wako labda,…?’ akauliza na bado akabakia kimia
‘Au…labda, ….yeye huyu huyo, alikuambia kuna mambo ya kibenki,…akakuhadaa hivyo, na wewe ukaweka sahihi …ukijua ni ni mambo ya kibenki, ukiweka kwa niaba ya kaka yako hukujua kama ni mkopo, au…?’ akaulizwa.
‘Mhhh….lakini sio mkataba…ilikuwa kitu kingine, mimi mkataba nakuwa nao makini sana, kiukweli,..nimechanganyikiwa…’akasema
‘Haya hicho kitu kingine ni kipi labda…?’ akaulizwa
‘Kiukweli mimi sikumbuki jamani… mimi kiukweli, nikiambiwa kitu ‘m-ka-ta-ba’ ninakuwa makini sana na kilichoandikwa, ..na hii inatokana na kazi yangu ilivyo,…sasa hili hata sielewi, ilikuwaje, kiukweli mimi nisikumbuki, na kiukweli sijui lolote kuhusu hilo deni, kuwa ni mimi niliweka hiyo sahihi…sikumbuki, …ngoja nifikirie..’akasema sasa akishika kichwa
‘Haya chukua muda wa kufikiria, tunakusubiria …’akaambiwa, na hakimu akasema;
‘Kwa vile tumeongea sana, natoa dakika chache za mapumziko, huku shahid naye akipata muda wa kukumbuka,….’akasema hakimu, na mimi pake nikamuangalia Dalali, halafu nikageuka kwenda sehemu yangu ya kukaa..
Kabla sijatulia vyema nikaguswa bega na mtu, nikageuka kuangalia ni ndani, nikapewa karatasi, imeandikwa.
‘Naomba niongee na wewe…’ mama mjane.
Nikgeuka upande ule alipokaa mama mjane, sikumuona, nikageuka upande wa pembeni, nikamuona kasimama, huku akiangalia upande huo tulipokaa, nikajua ananisubiria mimi, akilini nikawa najiuliza huyu mama kagundua nini
Nikamuelezea wakili kuwa natoka kidogo.
‘Unataka kwenda wapi, huyo mtu ni wa kwako…’akasema akimaanisha Dalali.
‘Nipo,..siende mbali…’nikasema na kuanza kutoka ile sehemu kuelekea upande wa kuelelea mlango wa chooni, ndio nikamkuta mama mjane ananisubiria.
‘Vipi dada, kuna nini….maana unajua mimi ndio natakiwa kumuhoji shemeji yako…?’ nikamuuliza
‘Ndio maana nikakuhitajia, ni kuhusu hilo hilo, kumuhusu Dalali…’akasema
‘Ehee..ongea kwa haraka kidogo, …ana nini…?’ nikamuuliza
‘Dalali anasema kweli, kuwa hilo deni halitambui…’akasema na kunifanya nimuangalia mara mbili tatu, nikajikuta nimesema hivi
‘Shemu…ooh, dada wewe na Dalali, mna nini…unajua nimegundua kitu, wewe unapenda kumtetea sana..je huoni kuwa tayari keshaingia kwenye hali ya kukubali, kuwa hilo deni sio la kaka yake, bado kidogo tu ataongea kila kitu…’nikasema
‘Kaka, pamoja na hayo, sema ukweli wako, je unaamini kuwa kweli Dalali anaweza kulifanya hilo kwa kaka yake…?’ akaniuliza
‘Ndio maana nimetaka nimuhoji mimi…nitakuja kumweka mahali atasema ukweli wote…..inawezekana katumiwa, lakini anaogopa kumsema huyo mtu aliyemtumia,…’nikasema
‘Dalali…hajui lolote,….sio kwamba nasema haya kwa kumtetea, au kama unavyofikiria wewe..hapana, mimi namfahamu sana shemeji yangu, akisema jambo la uwongo, ukimuuliza mara mbili tatu, …atakubali tu, na kuna dalili usoni, y akumtambua kuwa anasema ukweli au uwongo, hajui, kudanganya kwa muda mrefu…’akasema mama mjane
‘Kwahiyo unatakaje…maana kama sio yeye, basi ni mume wako…’nikasema
‘Mume wako hahusiki na hilo deni, na pia Dalali, atakuwa hajui…nakuomba usimshinikize kwenye jambo ambali hajalifanya…’akasema mama mjane
‘Mhh…sawa …je wewe unahisi ni nani basi…maana unaongea kama vile unamfahamu mtu mwingine…au wewe kuna kitu unakifahamu kutokana na hilo deni…?’ nikamuuliza
‘Kiukweli hapa nilipo …kwanza nina furaha kuwa hilo deni sasa linatambulikana kuwa sio la marehemu..lakini bado sijawa na amani, ni nani alilifanya hilo, kiukweli sina mtu ninayemuwazia…na..ni nani alifanya mpaka akapata ajali…’akasema kwa sauti ya huzuni.
‘Sawa nimekuelewa shemeji, ngoja tukaendelee maana hakimu huyo kaingia…’nikasema na kuachana na huyo mama mjane…wakati naondoka nikageuka kumuangalia, nilimuona akiuta machozi.
Hakimu akasema kesi iendelee…na mimi nikamsogelea Dalali, na kumuuliza.
‘Bwana Dalali, natumai umepata muda wa kutosha, kufikiria, je sasa umekumbuka,…?’ nikamuuliza na Dalali, kwanza akatulia kidogo, baadae akasema;
‘Oooh…nimekumbuka, ….sasa nimekumbuka,…’akasema akijaribu kama kusimama, halafu akajiweka vyema
‘Unataka kusimama…?’ nikamuuliza na yeye akatikisa kichwa kukataa..
‘Basi ongea…tukusikie…’nikasema
‘Yah…nimekumbuka….sijui kwanini nililisahau hilo…kunaah. Eeh…. kipindi kulikuwa na mabadiliko pale benk, kwenye hiyo benki kulitokea kitu kama mageuzi, kiongozi yule wa zamani wa hiyo benki, aliachishwa, akaletwa mwingine, kabla ya …hayo mageuzi, nakumbuka kulitokea mabadiliko, tukaambiwa wenye akaunti, wanatakiwa kupeleka kumbukumbu zao upya……ndio ndio..…sasa nimekumbuka…’akaniangalia na mimi nikawa kimia tu.
‘Inaonekana wewe unalifahamu hili, ndio maana unanisaidia nikumbuke na kunisihi sana nikumbuke....’akasema akiniangalia mimi.
‘Mimi sijui kitu, nataka wewe ukumbuke tu, maana wewe ndio ulikuwepo…’nikasema
‘Ndio…nashukuru sana kwa hilo,…umesaidia kukumbuka…, lakini eeh…sina uhakika saana…, kuna muhasibu mmoja alinisainisha, kitu kama hicho…’akasema na kukaa kimia kidogo.
‘Ile siku ilikuwa na shughuli nyingi pale benki…na mimi mwenyewe nilitngwa na shughuli nyingi sana…na hata bro, alikuwa na kazi zake za kibiashara alitakiwa kusafiri, kwahiyo …nilipomuambia hilo, kuwa kuna kumbukumbu zinahitajika, yeye alisema kila kitu chake kipo benki,..hawezi kupoteza muda kwa hilo…akaniagiza pesa kidogo…’akatulia
‘Nilipofika, nikaambiwa mpaka niwasilishe hizo kumbukumbu..nikampigia bro simu…akaniambia basi, kama haiwezekani kwa leo, basi, niache tu…sasa wakati nataka kuondoka,…maana kulikuwa na pilika pilika nyingi sana,.., akaunti nyingi zilikuwa zinarekebishwa, watu wanataka pesa…na ndio muhasibu akaniita…’akatulia
‘Kwa ile hali…na..nakumbuka nilikuwa na mnada wa kufanya, wenzangu walishanipigia simu kuwa nachelewa,…sasa kwa hiyo hali,..nahitajika huko, huku benki muhasibu ananiambia kaniita, ..na anajua hawezi kuniita kwa jambo lisilo la muhimu…nikamuendea
‘Aliniambia akaunti ya kaka yangu haina shida ila mwenye akaunti anahitajika kuweka sahihi zake na inatakiwa siku hiyo hiyo…, ndio maana tulitangaziwa…na kama isipofanyika hivyo, itabidi afuate taratibu zote kama kufungua akaunti upya…
Unajua kitu kikipangwa kimepangwa,…nikamwambia huyo muhasibu..
‘Kwani nikimuwekea sahihi kwa niaba yake…haina shida,….unaona sahihi yangu na yake zinafanana kabisa,na hata kama nitakosea yeye mwenyewe....baadae bro, atakuja kuliweka sawa, hatuna muda wa kufungua tena akaunti, inasumbua…’nikasema
‘Haiwezekani, anatakiwa yeye mwenyewe aweke sahihi…’akaniambia na mimi pale nikampigia simu Bro, akawa hapatikani…nilichofanya nikuchukua zile eeh, kwa pale mimi niliona kuwa ni..kumbukumbu za kibenki za kuweka sawa akaunti za watu..juu ilionyesha hivyo, …sasa mimi sijui kwa ndani, sikusoma…kwa haraka nikatafuta sehemu ya sahihi nikaweka,….’akasema
‘Mhh…umefikria sana, kubuni hadithi hiyo…’nikasema
‘Ni kweli muheshimiwa,..na kwa vile nilimuamini sana yule muhasibu,…nikafanya haraka kuweka sahihi nikamrejeshea, akaniuliza je keshaweka sahihi, nikamwambia ndio..’
‘Na dole gumba, ..’akasema na mimi nikamwambia
‘Jamani ataweka dole guma mara ngapi…juzi tu ulinipatia zile…karatasi nimpelekee akaweka dole gumba, na sahihi yake sasa ya nini tena…?’ nikamuuliza
‘Ok…ok, nimekumbuka,..kumbe ..basi hilo halina shida…’akasema hivyo..
‘Sasa kiukweli mimi sikupata nafasi ya kusoma maelezo yote, nilisoma tu pale juu…huo ndio uzembe wangu…’akasema.
‘Kwahiyo huo ni mkataba, je kwenye kuweka sahihi ya mkopo wenyewe, maana huu hapa unaonekana, kiasi, jina la mkopaji, ..inajieleza hapa haijifichi kitu, uliwekaje hii sahihi hapa…?’ nikamuuliza
‘Siku ile ile nakumbuka …eeh, ndio yule muhasibu, alisainisha kitu…alisema kwa vile kuna kuhamishwa,…pesa kutoka akaunti ya zamani,..anahitajika kuweka sahihi kwenye karatasi ya malipo…mimi niliangalia nikaona jina la bro..ni jina lake…nikafanya vile nikatoka nje, na baadae nikarejesha,…ilikuwa kitendo cha haraka…’akasema.
‘Hukusoma kabisa kilichoandikwa…?’ nikamuuliza.
‘Kiukweli kwa siku ile ni mara yangu ya kwanza kufanya uzembe huo, sikuweza kusoma….’akasema
‘Huyo muhasibu ndio nani…?’ akaulizwa
‘Alikuwa muhasibu wa benki kipindi hicho…’akasema
‘Yupo wapi huyo mtu kwa hivi sasa…, bado yupo benki au alishaacha kazi…?’ akaulizwa
‘Ni marehemu…’Dalali akasema na hapo watu wakacheka…kicheko kile kilimfanya Dalali, awageukie watu, na kusema;
‘Mnacheka nini sasa..ni kweli ninayoongea, ..msione kuwa ni mzaha huu…hili lilifanyika, waulizeni watu wa benki kama tendo hilo halikutokea,…aliniita huyo muhasibu, tatizo huyo muhasibu hayupo tena duniani…’akasema
‘Alifariki lini…?’ akaulizwa
‘Nahisi ni kipindi kile kile…baada ya hilo tukio, niliwahi kufika pale banki nikamuulizia, nikaambiwa huyo muhasibu hayupo tena duniani…kiukweli iliniuma sana, maana alikuwa mhasibu aliyependa kusaidia watu…’akasema
‘Unauhakika …?’ akaulizwa
‘Uhakika gani sasa, huyo muhasibu ni marehemu, kaulizeni huko benki…au huyo wakili hapo, anaweza kunisaidia kwa hilo…’akasema akimuangalia wakili wa benki ambaye alikuwa kama hana habari na maelezo yake.
‘Wakili wa benki anamfahamu sio,..kuwa huyo muhasibu ni marehemu, naona wakili hata hana habari na maelezo yako anaona unadanganya…?’ akaulizwa
‘Huyo wakili anaweza kunisaidia kulifuatilia hilo, kama mnataka , huyo muhasibu ni marehemu, alikuwa anaitwa nani…mmh, jina lake..…’akasema akawa kama anatafakari
‘Sasa kama huyo mtu ni marehemu, atakusaidiaje kwenye maelezoo yako, na hata jina lake hulikumbuki, na wewe kiuzoefu huwa husau mambo, iweje leo…?’ akaulizwa, na hapo akabakia kimia
‘Huyo ndio shahidi wako wa kukutetea,..lakini atakuteteaje kama alifanya hivyo kwa nia ya kukubebesha huo mkopo, na kwanini afanye hivyo…?’ akaulizwa.
‘Ndio hapo….hata mimi sijui…ila nazungumzia hivyo, kama ulivyosema nikumbuke, ni kweli nilisainishwa kitu kama hicho,…na sio kusainishwa, niliweka sahihi mimi mwenyewe, nilijua sahihi ya ngu na bro, hazitofautiani, …ama wa hiyo nukta mara nyingi nasahau….na kwa kipindi kile mimi nilijua ni kwa ajili ya utaratibu wa kibenki..na..sikuwa na ..sikuwa makini, kuwa huo ni mkataba wa kibenki…’akasema
‘Dalali anasema …sasa anasema hivyo, kuwa yeye alisainishwa au aliamua kuweka sahihi kwenye kitu asichokijua,,…awali alisema yeye yupo makini sana kwenye vitu kama mkataba kutokana na uzoefu wa kazi yake…
Sasa anadai kuwa aliyemfanyia hivyo hadi akaweka sahihi, ila hana uhakika ilikuwa ni kitu gani,..aliyefanikisha hilo …ni marehemu…jamani,…mnamuelewa huyu mtu…’nikauliza nikiangalia watu.
Watu wakacheka kidogo.
Na mara sauti kubwa ikasikika kwa nyuma ikisema;
‘Huyo muhasibu sio marehemu, yupo hai….’…
Watu wote wakageuka kuangalia wapi sauti ilipotokea, …na hakimu naye akawa anaaangalia usawa wa watu, kuitafuta hiyo sauti ilipotokea,…na ile sauti ikarudia tena..
‘Huyo muhasibu yupo hai…samahani kwa kuingilia ila mimi ninao ushahidi kuwa huyo muhasibu hajafa, na kama Dalali kasema hivyo kwa nia ya kufiria kuwa huyo muhasibu hayupo duniani, kiukweli…huyo muhasibu bado yupo hai …’sauti ikasema
Sasa ile sauti ikajulikana inatokea wapi…
‘Wewe ni nani hebu pita huku mbele…’kasema hakimu…, na watu wakawa wanampisha huyo mtu…safari hii ni tofauti na ilivyokuwa awali, mtu akitaka kupita mbele ni mpaka itokee kusukumana…
Huyo mtu akasogea hadi mbele, …..
NB: Raha si raha…nakatiza kwa muda….

WAZO LA LEO: Kila mtu anapenda kupata,..kila mtu anapenda yeye aonekane zaidi, au ajulikane zaidi, (umaarufu), na watu kama hao, wanapenda mambo yao yapewe kipaumbele na yasipofanyiwa hivyo, inakuwa ni taabu kwao…. Watu kama hao, hata kama wanacho, bado watakuwa wanataka zaidi,(hawatosheki) .Huo ndio ubinafsi wa kibinadamu, ukiendelea hivyo, ndio dhuluma inakuja kuchukua nafasi, hakuna kujaliana tena hapo.

emu-three