Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Thursday, September 27, 2018

YOTE NI KWA MAPENZI YA MUNGU-52


'Ndugu muheshimiwa hakimu, nawakilisha ushahidi huo…unao-onyesha sahihi za ndugu yetu Dalali, sahihi ambazo zinafanana...ile ya kwenye malipo inafanana na sahihi ya kitambulisho cha Dalali,..na sahihi hiyo ipo kwenye malipo yaliyofanyika benki kwa ajili ya mkopo, ulitolewa kwa jina la marehemu…’akasema wakili akipeleka ushahid ule mbele ya hakimi.
'Na pia inafanana na sahihi iliyopo kwenye mkataba...'akaongezea wakili huyo
Hakimu akawa anakagua…na kuwaonyesha wenzake, na wote wakawa wanatikisa kichwa kukubaliana na hilo, kuwa kweli sahihi hizo zinafanana..hakimu akauliza.
‘Dalali…hiyo sahihi kwenye malipo sio yako…?’ akaulizwa Dalali.
‘Si-sio ya kwangu muheshimiwa ha-ha-kimu…..’akasema na hakimu akarejea kuchunguza ile sahihi, na aliporidhika akasema.
‘Tutawaomba wataalamu wa maandishi waje kututhibitishia hilo, na kama ni ya kwako, ujue umeidanganya mahakama…’akaambiwa Dalali..
‘Lakini muheshimiwa kabla ya kulifanya hilo, ninaomba..muda, sijui ilivyotokea, nasema ukweli muheshimiwa, sio mimi…sijui ilikuwaje, sina uhakika muheshimiwa…..’akasema akihangaika kwenye kiti.
Mimi nikamsogelea Dalali, na kusema…
‘Dalali tuambie ukweli..kwanini sahihi yako inafanana na hii hapa ya kwenye malipo ya huo mkopo,…?’ akaulizwa Dalali sasa akiwa katulia.
Dalali akabakia kimia.
Mimi nikachukua zile nakala za ushahidi nikamuonyesha Dalali,..
‘Unaona hapa Dalali, chunguza mwenyewe kwa makini…hapa kwenye mkataba pia,..sahihi hii hapa ni ya kwako,..au tusema, inafanana naya kwako…wewe si umesema sio wewe uliyeweka sahihi yako, ..labda kwa niaba ya marehemu…iweje sasa sahihi hii hapa, ifanane ya kwako… eeh…?’ Dalali akaulizwa sasa yeye akawa anaangalia tu ile sehemu ya sahihi, hajibu kitu.
Hakimu akawa anawaangalia watu hao kwa uso wa kujiuliza, hakutaka kuingilia kati, aliacha mazungumzo hayo ya maswali na majibu yaendelee tu..
‘Dalali bora tu ukiri kosa, tuone haki ikitendeka, kukiri kosa ni uwajibikaji wa muungwana,…hakuna kilichobakia sasa, ukweli sasa upo bayana, ni muda muafaka wa kukiri kosa, utuambie tu ilikuwaje,…au unaoenewa .. je hii hapa sio sahihi yako…?’ nikamuuliza akabakia kimia;
‘Au labda eeh… utuambie kitu, labda, useme… sahihi zenu wewe na marehemu zinafanana ndio hivyo au…?’ nikamuuliza, na hapo Dalali naye akachungulia tena zile sahihi, halafu kwa sauti ya mashaka akasema;
‘Ni kweli sahihi zetu zinafanana,…’akasema na watu wakacheka.
‘Sahihi zenu zinafanana, sasa hivi unasema hivyo, ok…haya tuambie kwa vipi…?’ akaulizwa. Na watu wakacheka na kukatokea mngurumo wa mnong’ono, watu wengi wakinong’ona inakuwa ni mngurumo…Hakimu akagonga rungu lake , kukawa kimia
Dalali akasema akiwaangalia watu…
‘Ni kweli msicheke,…unajua nilishikwa na butwaa baada ya kuona hivyo…na sijui kwanini sikuweza kulisema hili mapema,..ni kweli kuwa sahihi zetu zinafanana, hata mwandiko, mimi nilikuwa napenda kumfuatisha sana kaka yangu huyo kila anachofanya tokea utotoni, nikawa naiga hata mwandiko wake,…na ikaja hata kwenye kuweka sahihi…sasa kwenye sahihi, tofauti yangu na bro,..bro yeye...’watu wakaguna.
‘Ni kweli jamani…bro yeye huwa anaweka nukta hapa mbele…’akasema, akionyeshea sehemu nukta inapowekwa…
‘Inua juu watu waone unachoongea…nahisi ungelikuwa na kalamu ungeiweka hiyo nukata,…au sio…lakini umeshachelewa Dalali…kubali tu yaishe…’akaambiwa na wakili, Dalali akainua ile nakala ya mlipo akionyesha wapi nukata inapowekwa.
Wakati anafanya hivyo mimi nikachukua karatasi nyingine ya malipo, ambayo ilionyesha malipo yaliyofanywa na kusainiwa na kaka yake…nikasema;
‘Kama hii hapa, au sio…hii ndio sahihi kamili ya kaka yako au sio…?’ nikamuonyesha na yeye akaangalia, halafu akasema.
‘Ndio kama hiyo hapo muheshimiwa, hiyo ni sahihi ya kaka …haina shaka…’akasema kwa sauti yenye kuparuza…koo limekauka ghafla;
‘Sasa kama ni hivyo, kwenye hii stakabadhi ya malipo, au kwenye huu mkataba,… wewe usema tu,…ulisahau kuweka hiyo nukta ili ionekane kuwa kaka yako ndiye kachukua hizo pesa, umeliona hilo kosa ulilolifanya eeh…, au ni yeye alisahau kuweka hiyo nukta,..?’ nikamuuliza na Dalali akabakia kimia.
‘Dalali, Dalali… tuambie ukweli Dalali, muda unakwenda, au tumuachie hakimu yeye mwenyewe atajua jinsi gani ya kufanya, ila muhimu hadi hapa, hili deni sio la marehemu, hili deni ni la kwako, ..japokuwa huku juu limewekwa jina la mlipwaji ni l;a kaka yako, lakini huku kwenye sahihi sio ya kwake..kwanini, ..sasa utuambie wewe....’nikasema
Dalali, sasa akawa anahema tu…, kiti akakiona hakimtoshi,..jasho linamtoka, akawa anazichungulia zile stakabadahi za malipo, nikamsogelea na kumshika mkono..
‘Naona nikusaidie usimame, ..utoke kwenye hicho, kiti maana kinakubana, au sio..?’ nikasema na watu wakacheka.
Dalali hakujali hilo, sasa akasema;
‘Lakini mimi sijui lolote kuhusu hilo, kwangu imekuwa mshtuko, na hapa nilipo kweli naanza kukubali kuwa huenda kweli hilo deni sio la marehemu….naanza kuliona hilo….’akasema
‘Ehee..tuambie ukweli ni la nani, …?’ akaulizwa
‘Hapa inabidi tuwaulize vyema watu wa benki…’akasema
‘Kwanini wakati sahihi ni yako, ukumbuke wewe unawaamini sana watu wa benki, wao wana utaratibu wao mnzuri tu..si umelisema hilo tena na tena, au…kwanini sasa unaanza kuwatilia mashaka…?’ nikamuuliza
‘Kiukweli muheshimiwa,..ndugu yangu…hili….linanifanya niwe kwenye mshtuko, je ina maana mizimu,…ina maana benki, ..haiwezekani…siamini hiki, kuwa ni mimi niliweka hiyo sahihi…hapana lazima kuna mtu….’watu wakacheka.
‘Mizimu ndio iliweka sahihi, hiyo au una maana gani hapo…?’ nikauliza na watu wakazidi kucheka.
‘Msicheke jamani, hapa…mnacheza na maisha ya watu, ..huu ni uonevu, mimi sijawahi kuweka hiyo sahihim mkicheka mnanifanya mimi ni mjinga, mimi sio mjinga hapa naongea ukweli, na huo ukweli utakuja kuwasuta mwisho wa siku, ukweli ukija kubainika, kuwa mimi sihusiki na lolote hilo…nasema hivi, mimi sikumbuki kufanya hivyo, hata sijui,…mimi nasema ukweli kabisa, muheshimiwa hakimu…’akasema
Watu sasa wakabakia kimia,..na hakimu akawa anatuangalia tu…
‘Labda kwa kumbukumbu zako,…Je wewe uliwahi kuweka sahihi kwenye kitu kama hiki, au kwenye mkataba wowote huko benki kwasababu fulani nyingine,…?’ nikamuuliza
Dalali akawa kama anawaza halafu akasema;
‘Haa-ha-hapana..sio mimi niliyeweka bwana…’akasema hivyo, na watu wakacheka na hakimu akagonga rungu lake watu watulie.
‘Naona upo mbali sana…nauliza hivi, Ina maana wewe hujawahi kuweka sahihi…kwenye mkataba,… labda ulipewa tu huko benki na labda kwa bahati mbaya,… hukuwahi kuusoma kuwa ni mkataba,…labda…, kwa haraka zako wewe ukaweka sahihi yako tu, labda…eeh. Hebu kumbuka..?’ akaulizwa
‘Hata sikumbuki…..’akasema na watu wakacheka.
‘Dalali…kumbuka vyema ndugu yangu, hili sasa ni lako…sio la kaka yako tena, huu mkopo sasa ni wa kwako…’akasema wakili
‘Kwanini uwe ni mkopo wangu, mimi sijachukua huo mkopo,…siwezi kukubaliana na hilo kamwe….’akasema
‘Sasa Dalali, sisi tutakusaidiaje….hebu tusema hivi…, labda katika mabadiliko ya kibenki, ..eeh huko benki, si kulitokea mabadiliko …hilo si unalijua, au sio, maana wewe ulikuwa unafuatilia sana hilo….labda kipindi hicho, wewe…ulipewa nasema kwa mfano, maana haa hivyo haiji…au sio…’nikasema
‘Sijakuelewa muheshimiwa…?’ akaniuliza
‘Nasema hivi, jaribu kuvuta kumbukumbu zako, ukumbuke vyeka, kuwa labda ulitakiwa wewe uweke sahihi yako kwa niaba ya kaka yako…maana hapa kweli. hakuna nukta, kuashiria kuwa hayo malipo hakuweka sahihi marehemu , au siowewe ndiye uliweka hiyo sahihi,…?’ akaulizwa na akaendelea kuzitizama zile karatasi.
‘Dalali, hiyo sio sahihi yako……?’ akaulizwa
‘Inaonekana kama ya kwangu….’akasema
‘Lakini sio sahihi yako…?’ akaulizwa
‘Mimi siwezi kuwa na uhakika….’akasema
‘Kwanini…?’ akaulizwa
‘Ni kweli, kuna …kipindi nimeshawahi kuweka sahihi kwenye stakabadhi za benki kwa niaba ya kaka….na..na ..hata kwenye malipo…lakini aliniambia yeye mwenyewe kutokana na ya kwua alikuwa mbali, na alihitajia pesa kwa haraka….’akasema
‘Dalaliii….ujanja wako upo wapi, unakumbuka awali ulisemaje, kuwa kama ni malipo ya benki, wewe hujawahi kuweka sahihi, kaka yako ndiye alikuwa akifanya hivyo, wewe hukuwahi kuweka sahihi yako kwenye malipo,…hukusema hivyo awali…?’ akauliza na hapo akabakia kimia
‘Dalali,Dalali ....tuamini lipo sasa ndugu yangu, kauli ya kwanza au hii ya pili…?’ nikamuuliza
‘Awali nilisema nikimaanisha malipo, ndio…bro mara nyingi kwenye malipo alikuwa akiandika yeye na kuweka sahihi yeye, na ananipa mimi nikalipe au kuchukua pesa, ..lakini ilitokea dharura kama hiyo, ..ni mara moja au mbili hivi tu…’akasema na watu wakacheka,.
‘Ni mara moja au mara mbili hivi ti…, na huenda ya tatu na ya nne, au zaidi ya hapo, ndio ikawa hii ya kusaini malipo ya mkopo na mkataba, au sio…?’ nikamwambia kama kumuuliza, na yeye akakunja uso kama kukerwa, halafu akasema
‘Sio kweli muheshimiwa, mimi sijaweka sahihi kwenye huo mkopo, siwezi ku-ku-jua hilo lilitokeaje,..naombeni muda wa kufikiria tafadhali…’akasema
‘Unahitajia muda gani hivi wa kufikiri, maana tupo mahakamani, na muda ni muhimu sana, eeh, tuambie unahitajia muda gani wa kufikiri…?’ akauliza na hapo akabakia kimia…na alipoona anasubiria yeye kujibu akasema;
‘Nasema hivi,…kwenye malipo ilitokea hiyo dharura, nikafanya hivyo, lakini sio kwa huo mkopo, huo mkopo mimi sijui..na kiukweli kuna mambo mengine ambayo sio ya malipo, bro, alikuwa akisema niweke sahihi kwa niaba yake…’akasema
‘Kwahiyo ile kauli yako ya mwanzo unaikana…?’ akaulizwa, na kukaa kimia
‘Sijaikana,…mnielewe jamani…kuna utaratibu na dharura…kikawaida utaratibu wa bro ilikuwa hivyo,..lakini ikatokea dharura…’akajitetea hivyo.
‘Na je kwenye mkataba wa benki ilikuwaje maana ni sahihi yako pia…unaiona ilivyo,…, haina nukta mbele, hebu ikague vizuri, usije kusema imefutwa na nukta ya kaka yako, inakolea sana, nimepitia malipo yote aliyoweka sahihi…ni hivyo hivyo, angalia, hii nah ii na hii hapa, nukta imekolea sio y akugusa…naona alihakikisha hiyo nukta inaonekana vyema…’akaambiwa
‘Ni kweli, yeye alihakikisha kwenye sahihi zake zote hiyo nukta inaonekana vyema, aliwahi kuniambia kwenye sahihi, kila kitu kwake ni muhimu, na …hiyo nukta ikawa …ni kama nembo yake, kwenye sahihi yake kutofautisha na sahihi yangu…’akasema Dalali.
‘Hapo umetusaidia sana..sasa tuambie…eeh au, bado unahitajia muda wa kufikiria zaidi…?’ akauliza na akabakia kimia
‘Au bwana Dalali…, labda tukusaidie hivi..…labda uliambiwa uweke sahihi hiyo na benki bila yaw ewe kujua,…mhh, au danganya danganya hivi, kujitetea..labda kuna mtu alikuhadaa, …kijana wako labda,…?’ akauliza na bado akabakia kimia
‘Au…labda, ….yeye huyu huyo, alikuambia kuna mambo ya kibenki,…akakuhadaa hivyo, na wewe ukaweka sahihi …ukijua ni ni mambo ya kibenki, ukiweka kwa niaba ya kaka yako hukujua kama ni mkopo, au…?’ akaulizwa.
‘Mhhh….lakini sio mkataba…ilikuwa kitu kingine, mimi mkataba nakuwa nao makini sana, kiukweli,..nimechanganyikiwa…’akasema
‘Haya hicho kitu kingine ni kipi labda…?’ akaulizwa
‘Kiukweli mimi sikumbuki jamani… mimi kiukweli, nikiambiwa kitu ‘m-ka-ta-ba’ ninakuwa makini sana na kilichoandikwa, ..na hii inatokana na kazi yangu ilivyo,…sasa hili hata sielewi, ilikuwaje, kiukweli mimi nisikumbuki, na kiukweli sijui lolote kuhusu hilo deni, kuwa ni mimi niliweka hiyo sahihi…sikumbuki, …ngoja nifikirie..’akasema sasa akishika kichwa
‘Haya chukua muda wa kufikiria, tunakusubiria …’akaambiwa, na hakimu akasema;
‘Kwa vile tumeongea sana, natoa dakika chache za mapumziko, huku shahid naye akipata muda wa kukumbuka,….’akasema hakimu, na mimi pake nikamuangalia Dalali, halafu nikageuka kwenda sehemu yangu ya kukaa..
Kabla sijatulia vyema nikaguswa bega na mtu, nikageuka kuangalia ni ndani, nikapewa karatasi, imeandikwa.
‘Naomba niongee na wewe…’ mama mjane.
Nikgeuka upande ule alipokaa mama mjane, sikumuona, nikageuka upande wa pembeni, nikamuona kasimama, huku akiangalia upande huo tulipokaa, nikajua ananisubiria mimi, akilini nikawa najiuliza huyu mama kagundua nini
Nikamuelezea wakili kuwa natoka kidogo.
‘Unataka kwenda wapi, huyo mtu ni wa kwako…’akasema akimaanisha Dalali.
‘Nipo,..siende mbali…’nikasema na kuanza kutoka ile sehemu kuelekea upande wa kuelelea mlango wa chooni, ndio nikamkuta mama mjane ananisubiria.
‘Vipi dada, kuna nini….maana unajua mimi ndio natakiwa kumuhoji shemeji yako…?’ nikamuuliza
‘Ndio maana nikakuhitajia, ni kuhusu hilo hilo, kumuhusu Dalali…’akasema
‘Ehee..ongea kwa haraka kidogo, …ana nini…?’ nikamuuliza
‘Dalali anasema kweli, kuwa hilo deni halitambui…’akasema na kunifanya nimuangalia mara mbili tatu, nikajikuta nimesema hivi
‘Shemu…ooh, dada wewe na Dalali, mna nini…unajua nimegundua kitu, wewe unapenda kumtetea sana..je huoni kuwa tayari keshaingia kwenye hali ya kukubali, kuwa hilo deni sio la kaka yake, bado kidogo tu ataongea kila kitu…’nikasema
‘Kaka, pamoja na hayo, sema ukweli wako, je unaamini kuwa kweli Dalali anaweza kulifanya hilo kwa kaka yake…?’ akaniuliza
‘Ndio maana nimetaka nimuhoji mimi…nitakuja kumweka mahali atasema ukweli wote…..inawezekana katumiwa, lakini anaogopa kumsema huyo mtu aliyemtumia,…’nikasema
‘Dalali…hajui lolote,….sio kwamba nasema haya kwa kumtetea, au kama unavyofikiria wewe..hapana, mimi namfahamu sana shemeji yangu, akisema jambo la uwongo, ukimuuliza mara mbili tatu, …atakubali tu, na kuna dalili usoni, y akumtambua kuwa anasema ukweli au uwongo, hajui, kudanganya kwa muda mrefu…’akasema mama mjane
‘Kwahiyo unatakaje…maana kama sio yeye, basi ni mume wako…’nikasema
‘Mume wako hahusiki na hilo deni, na pia Dalali, atakuwa hajui…nakuomba usimshinikize kwenye jambo ambali hajalifanya…’akasema mama mjane
‘Mhh…sawa …je wewe unahisi ni nani basi…maana unaongea kama vile unamfahamu mtu mwingine…au wewe kuna kitu unakifahamu kutokana na hilo deni…?’ nikamuuliza
‘Kiukweli hapa nilipo …kwanza nina furaha kuwa hilo deni sasa linatambulikana kuwa sio la marehemu..lakini bado sijawa na amani, ni nani alilifanya hilo, kiukweli sina mtu ninayemuwazia…na..ni nani alifanya mpaka akapata ajali…’akasema kwa sauti ya huzuni.
‘Sawa nimekuelewa shemeji, ngoja tukaendelee maana hakimu huyo kaingia…’nikasema na kuachana na huyo mama mjane…wakati naondoka nikageuka kumuangalia, nilimuona akiuta machozi.
Hakimu akasema kesi iendelee…na mimi nikamsogelea Dalali, na kumuuliza.
‘Bwana Dalali, natumai umepata muda wa kutosha, kufikiria, je sasa umekumbuka,…?’ nikamuuliza na Dalali, kwanza akatulia kidogo, baadae akasema;
‘Oooh…nimekumbuka, ….sasa nimekumbuka,…’akasema akijaribu kama kusimama, halafu akajiweka vyema
‘Unataka kusimama…?’ nikamuuliza na yeye akatikisa kichwa kukataa..
‘Basi ongea…tukusikie…’nikasema
‘Yah…nimekumbuka….sijui kwanini nililisahau hilo…kunaah. Eeh…. kipindi kulikuwa na mabadiliko pale benk, kwenye hiyo benki kulitokea kitu kama mageuzi, kiongozi yule wa zamani wa hiyo benki, aliachishwa, akaletwa mwingine, kabla ya …hayo mageuzi, nakumbuka kulitokea mabadiliko, tukaambiwa wenye akaunti, wanatakiwa kupeleka kumbukumbu zao upya……ndio ndio..…sasa nimekumbuka…’akaniangalia na mimi nikawa kimia tu.
‘Inaonekana wewe unalifahamu hili, ndio maana unanisaidia nikumbuke na kunisihi sana nikumbuke....’akasema akiniangalia mimi.
‘Mimi sijui kitu, nataka wewe ukumbuke tu, maana wewe ndio ulikuwepo…’nikasema
‘Ndio…nashukuru sana kwa hilo,…umesaidia kukumbuka…, lakini eeh…sina uhakika saana…, kuna muhasibu mmoja alinisainisha, kitu kama hicho…’akasema na kukaa kimia kidogo.
‘Ile siku ilikuwa na shughuli nyingi pale benki…na mimi mwenyewe nilitngwa na shughuli nyingi sana…na hata bro, alikuwa na kazi zake za kibiashara alitakiwa kusafiri, kwahiyo …nilipomuambia hilo, kuwa kuna kumbukumbu zinahitajika, yeye alisema kila kitu chake kipo benki,..hawezi kupoteza muda kwa hilo…akaniagiza pesa kidogo…’akatulia
‘Nilipofika, nikaambiwa mpaka niwasilishe hizo kumbukumbu..nikampigia bro simu…akaniambia basi, kama haiwezekani kwa leo, basi, niache tu…sasa wakati nataka kuondoka,…maana kulikuwa na pilika pilika nyingi sana,.., akaunti nyingi zilikuwa zinarekebishwa, watu wanataka pesa…na ndio muhasibu akaniita…’akatulia
‘Kwa ile hali…na..nakumbuka nilikuwa na mnada wa kufanya, wenzangu walishanipigia simu kuwa nachelewa,…sasa kwa hiyo hali,..nahitajika huko, huku benki muhasibu ananiambia kaniita, ..na anajua hawezi kuniita kwa jambo lisilo la muhimu…nikamuendea
‘Aliniambia akaunti ya kaka yangu haina shida ila mwenye akaunti anahitajika kuweka sahihi zake na inatakiwa siku hiyo hiyo…, ndio maana tulitangaziwa…na kama isipofanyika hivyo, itabidi afuate taratibu zote kama kufungua akaunti upya…
Unajua kitu kikipangwa kimepangwa,…nikamwambia huyo muhasibu..
‘Kwani nikimuwekea sahihi kwa niaba yake…haina shida,….unaona sahihi yangu na yake zinafanana kabisa,na hata kama nitakosea yeye mwenyewe....baadae bro, atakuja kuliweka sawa, hatuna muda wa kufungua tena akaunti, inasumbua…’nikasema
‘Haiwezekani, anatakiwa yeye mwenyewe aweke sahihi…’akaniambia na mimi pale nikampigia simu Bro, akawa hapatikani…nilichofanya nikuchukua zile eeh, kwa pale mimi niliona kuwa ni..kumbukumbu za kibenki za kuweka sawa akaunti za watu..juu ilionyesha hivyo, …sasa mimi sijui kwa ndani, sikusoma…kwa haraka nikatafuta sehemu ya sahihi nikaweka,….’akasema
‘Mhh…umefikria sana, kubuni hadithi hiyo…’nikasema
‘Ni kweli muheshimiwa,..na kwa vile nilimuamini sana yule muhasibu,…nikafanya haraka kuweka sahihi nikamrejeshea, akaniuliza je keshaweka sahihi, nikamwambia ndio..’
‘Na dole gumba, ..’akasema na mimi nikamwambia
‘Jamani ataweka dole guma mara ngapi…juzi tu ulinipatia zile…karatasi nimpelekee akaweka dole gumba, na sahihi yake sasa ya nini tena…?’ nikamuuliza
‘Ok…ok, nimekumbuka,..kumbe ..basi hilo halina shida…’akasema hivyo..
‘Sasa kiukweli mimi sikupata nafasi ya kusoma maelezo yote, nilisoma tu pale juu…huo ndio uzembe wangu…’akasema.
‘Kwahiyo huo ni mkataba, je kwenye kuweka sahihi ya mkopo wenyewe, maana huu hapa unaonekana, kiasi, jina la mkopaji, ..inajieleza hapa haijifichi kitu, uliwekaje hii sahihi hapa…?’ nikamuuliza
‘Siku ile ile nakumbuka …eeh, ndio yule muhasibu, alisainisha kitu…alisema kwa vile kuna kuhamishwa,…pesa kutoka akaunti ya zamani,..anahitajika kuweka sahihi kwenye karatasi ya malipo…mimi niliangalia nikaona jina la bro..ni jina lake…nikafanya vile nikatoka nje, na baadae nikarejesha,…ilikuwa kitendo cha haraka…’akasema.
‘Hukusoma kabisa kilichoandikwa…?’ nikamuuliza.
‘Kiukweli kwa siku ile ni mara yangu ya kwanza kufanya uzembe huo, sikuweza kusoma….’akasema
‘Huyo muhasibu ndio nani…?’ akaulizwa
‘Alikuwa muhasibu wa benki kipindi hicho…’akasema
‘Yupo wapi huyo mtu kwa hivi sasa…, bado yupo benki au alishaacha kazi…?’ akaulizwa
‘Ni marehemu…’Dalali akasema na hapo watu wakacheka…kicheko kile kilimfanya Dalali, awageukie watu, na kusema;
‘Mnacheka nini sasa..ni kweli ninayoongea, ..msione kuwa ni mzaha huu…hili lilifanyika, waulizeni watu wa benki kama tendo hilo halikutokea,…aliniita huyo muhasibu, tatizo huyo muhasibu hayupo tena duniani…’akasema
‘Alifariki lini…?’ akaulizwa
‘Nahisi ni kipindi kile kile…baada ya hilo tukio, niliwahi kufika pale banki nikamuulizia, nikaambiwa huyo muhasibu hayupo tena duniani…kiukweli iliniuma sana, maana alikuwa mhasibu aliyependa kusaidia watu…’akasema
‘Unauhakika …?’ akaulizwa
‘Uhakika gani sasa, huyo muhasibu ni marehemu, kaulizeni huko benki…au huyo wakili hapo, anaweza kunisaidia kwa hilo…’akasema akimuangalia wakili wa benki ambaye alikuwa kama hana habari na maelezo yake.
‘Wakili wa benki anamfahamu sio,..kuwa huyo muhasibu ni marehemu, naona wakili hata hana habari na maelezo yako anaona unadanganya…?’ akaulizwa
‘Huyo wakili anaweza kunisaidia kulifuatilia hilo, kama mnataka , huyo muhasibu ni marehemu, alikuwa anaitwa nani…mmh, jina lake..…’akasema akawa kama anatafakari
‘Sasa kama huyo mtu ni marehemu, atakusaidiaje kwenye maelezoo yako, na hata jina lake hulikumbuki, na wewe kiuzoefu huwa husau mambo, iweje leo…?’ akaulizwa, na hapo akabakia kimia
‘Huyo ndio shahidi wako wa kukutetea,..lakini atakuteteaje kama alifanya hivyo kwa nia ya kukubebesha huo mkopo, na kwanini afanye hivyo…?’ akaulizwa.
‘Ndio hapo….hata mimi sijui…ila nazungumzia hivyo, kama ulivyosema nikumbuke, ni kweli nilisainishwa kitu kama hicho,…na sio kusainishwa, niliweka sahihi mimi mwenyewe, nilijua sahihi ya ngu na bro, hazitofautiani, …ama wa hiyo nukta mara nyingi nasahau….na kwa kipindi kile mimi nilijua ni kwa ajili ya utaratibu wa kibenki..na..sikuwa na ..sikuwa makini, kuwa huo ni mkataba wa kibenki…’akasema
‘Dalali anasema …sasa anasema hivyo, kuwa yeye alisainishwa au aliamua kuweka sahihi kwenye kitu asichokijua,,…awali alisema yeye yupo makini sana kwenye vitu kama mkataba kutokana na uzoefu wa kazi yake…
Sasa anadai kuwa aliyemfanyia hivyo hadi akaweka sahihi, ila hana uhakika ilikuwa ni kitu gani,..aliyefanikisha hilo …ni marehemu…jamani,…mnamuelewa huyu mtu…’nikauliza nikiangalia watu.
Watu wakacheka kidogo.
Na mara sauti kubwa ikasikika kwa nyuma ikisema;
‘Huyo muhasibu sio marehemu, yupo hai….’…
Watu wote wakageuka kuangalia wapi sauti ilipotokea, …na hakimu naye akawa anaaangalia usawa wa watu, kuitafuta hiyo sauti ilipotokea,…na ile sauti ikarudia tena..
‘Huyo muhasibu yupo hai…samahani kwa kuingilia ila mimi ninao ushahidi kuwa huyo muhasibu hajafa, na kama Dalali kasema hivyo kwa nia ya kufiria kuwa huyo muhasibu hayupo duniani, kiukweli…huyo muhasibu bado yupo hai …’sauti ikasema
Sasa ile sauti ikajulikana inatokea wapi…
‘Wewe ni nani hebu pita huku mbele…’kasema hakimu…, na watu wakawa wanampisha huyo mtu…safari hii ni tofauti na ilivyokuwa awali, mtu akitaka kupita mbele ni mpaka itokee kusukumana…
Huyo mtu akasogea hadi mbele, …..
NB: Raha si raha…nakatiza kwa muda….

WAZO LA LEO: Kila mtu anapenda kupata,..kila mtu anapenda yeye aonekane zaidi, au ajulikane zaidi, (umaarufu), na watu kama hao, wanapenda mambo yao yapewe kipaumbele na yasipofanyiwa hivyo, inakuwa ni taabu kwao…. Watu kama hao, hata kama wanacho, bado watakuwa wanataka zaidi,(hawatosheki) .Huo ndio ubinafsi wa kibinadamu, ukiendelea hivyo, ndio dhuluma inakuja kuchukua nafasi, hakuna kujaliana tena hapo.

emu-three

No comments :