Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, July 12, 2019

IMANI HUTOKA MOYONI


IMANI YA KWELI HUTOKA MOYONI , NA SIRI HIYO AIJUE NI MOLA PEKEE.

Hiki sio kisa ni ukweli,

Katika maisha yangu… niliwahi kuajiriwa kwenye kampuni moja, nilipofika hapo nikazoeana na msichana mmoja,…nilimzoea kwa vile yeye ndiye alinikaribisha, na kunionyesha mazingira ya hapo kazini, ufanyeje, uende wapi kiutawala na sehemu ya kula, ofsini ipi ni ipo, vitu kama hivyo.

Basi kila nikihitajia kitu namuuliza yeye, na kiukweli hakuwa na hiyana, aliweza kunielekeza vyema tu, na kuna muda watu wakaanza kutuangalia kwa macho ya kujiuliza, huenda tumekuwa marafiki, lakini moyoni mwangu sikuwa na mawazo hayo kabisa.

Siku zikapita, na ule ukaribu wetu na huyo mdada ukapungua, maana sikuwa na cha kumuuliza tena, mimi nipo idara nyingine na yeye yupo idara nyingine, …sasa katika mazungumzo, nikaja kujua kuwa huyo msichana ni wale wenye msimamo mkali…mtakuwa marafiki lakini sio kwenye tendo la ndoa.

‘Huyu dada ni bikira bwana,…’watu wakawa wanamtania.

‘Labda bikira wa sehemu nyingine, mimi sidanganyiki  ‘mmoja akasema.

‘Kwanini, na wewe unamfahamu, tokea tuajiriwe hapa ulishawahi kumuona na mvulana, ..maana hapa hakuna siri, na hata huko nyumbani kwake si unakufahamu, uliwahi kumuona akiwa na mvulana..?’ akaulizwa.

‘Siri ya mtu anaijua yeye mwenyewe..ila mimi siamini kwa umri ule, atakuwa bado bikira, ni lazima atakuwa na mtu wa siri..’akasema huyo jamaa, na wengi hawakumshabikia, waliona ni wale wasiopenda maendeleo yaw engine.

Ikawa ni utani tu, wengi wakawa wanamtania huyo mdada kwa kumuita ‘sister bikira..’ akawa anaitwa hivyo.

Kiukweli mimi sikuweza kumuuliza huyo mdada kama hayo maneno na utani yana ukweli ndani yake,..niliamini kuwa yawezekana,…mtu ukiamua unaweza ukaishii hivyo,, na kwa vile ule ukaribiu wetu wa kumuuliza hiki na kile ulishakwisha, nikawa sikupata muda wa kuwa naye karibu tena, kila mtu kwenye idara yake na maisha yakaendelea.\

 Ila mimi niliamini waliyosema watu kuwa huyo mdada ni mgumu, sivyo kama walivyokuwa wanadada wengine, huyo mdada hakuwahi kuwa na rafiki wa kiume, niliyewahi kumuona au kuambiwa …kama ilitokea kukutana naye hasa kwenye chakula maana tulikuwa na mgawahawa wafanyakazi wote hukutana humo, huyo mdada..alionekana kivyake vyake tu..na ole mvulana ajaribu kumgusa, hata kiutani, ataambulia matusi,…

Hapo kazini karibu kila mmoja alijulikana ni nani na mwenzake wa jinsia tofauti ni nani, na wengine wakatokea hata kuoana kabisa,…lakini kwa miaka kadhaa niliyofanya hapo, sikuweza kumgundua rafiki wa huyo msichana…moyoni nikasema,..basi huyo ni ‘sister bikira kweli’.

Miaka kama miwili ikapita…nikaja kufikiria kama mimi nina tabia yangu kuwa  msichana wangu wa kwanza kukutana naye nikutane naye ndani ya ndoa, sasa kwanini nisifanye urafiki na huyo mdada, ambaye naye anaonekana ana msimamo huo..lilikuwa wazo katika kuhangaika kumpata mwenza wa maisha, ilikuwa wazo, na nikawa na mikakati hiyo, lakini siweza kulifanikisha, maana kiukweli moyoni sikuweza kuvutika na mdada huyo kimapenzi. Nafsi hupenda kile kinachomvutia mtu.

Bahati mbaya, nikahama hiyo kampuni…

Baada ya miaka kadhaa, nikasikia, kuwa yule msichana kafariki,

‘Kafariki!!!... ilikuwaje jamani…?’ nikauliza kwa mshangao na masikitiko.

‘Alianza kuumwa, umwa..akawa anapungua, baadae akazidiwa, anatibiwa, anapona hali inarejea, anaanza kuumwa tena,..baadae..akapelekwa kwao…yaani binadamu hubadilika haraka sana, unamfahamu jinsi alivyokuwa mrembo,...watu waliomuoana kipindi kazidiwa, wanasema ule urembo ulikwisha akawa kama mzee, alikuja kubadilika akawa…mweusi….’akasema jamaa,

‘Mhh...kwasababu ya huko kuumwa au, , kwani alikuwa anaumwa nini…?’ nikauliza moyo sasa ukinienda mbio. 

Unajua kipindi cha nyuma, watu wakiumwa sana, na kukonda, na kubadilika mwili, moja kwa moja unajau ni ugonjwa gani,..kipindi hiho kulikuwa hakuna dawa za kusaidia kuongeza nguvu, kwahiyo watu wengi waliougua ugonjwa huo, waliteseka sana kabla ya umri wao kuisha. Kwa vyovyote iwavayo kila mtu ana umri wake.

‘Unauliza jibu bwana, mdada alipatwa na maambukizi, na ..huwezi amini, ..hata ndugu zake hawakuamini wakasema kalogwa, lakini hakuna siri, aliyemuambukiza aligundulikana, kwani naye kwa kipindi hicho alikuwa akiugua ugonjwa huo huo..na alipoulizwa, yeye alidai huyo mdada ndiye kamuambukiza, lakini uchunguzi zaidi ulionyesha kuwa huyo mvulana alikuwa hajatulia, yeye ndiye alimuambukiza huyo msichana.

‘Mhh..lakini si mlisema huyo mdada ni bikira.

‘Hahaha, tulijua hivyo, kiukweli hata mimi niliamini hivyo…hadi msichana huyo anafikia kuumwa, sote tuliamini hivyo….’akasema.

‘Haiwezekani…japokuwa kila kifo lazima kiwe na sababu..nahis aiumwa maradhi mengine tu..hata hivyo....’nikasema na jamaa akanikatisha kwa kusema.

‘Iliwezekana sasa, na alitembea na cha pombe fulani, wakati yeye alikuwa akituzarau pale kazini kuwa hatuna maana, walevi, eeh..si unakumbuka, alivyokuwa,akitudharau, ...wewe uliondoka, sasa ilifikia mahali hamgusi mtu....anasema yeye ana bwana wake yupo Ulaya...sasa kumbe alikuwa na mvulana cha pombe tu..hakuwa na hadhi kwa yule mdada,…sijui ilikuwaje..masikini mungu amsamahe tu...’akasema huyo jamaa.

‘Kwani hamkujua ilikuwaje..?’ nikauliza.

‘Aaah. ilikuwa kujulikana dunia hii ina siri,na kwa vile alikuwa akiringa, jamaa zake walikuja kuvujisha siri..tukajua kila kitu, ikawa kufuatilia kuhakiki tu....unajua msijifanmye mna imani sana ya dini, aheri muwe kama sisi...unajua imani. ya.kweli ya mtu aijue ni mungu pekee, ujidanganya ipo sisku imani hiyo inataisha kidogo kidogo kama mshumaa unavyokwisha halafu utakuja kuumbuka, ila niliumia sana, yule mdada nilimpenda, nilitamani nimuoe, akanikataa,…’akasema huyo jamaa akionyesha kusikitika.

'Mhh..lakini kweli wewe ukizi  kulewa, nani angekubali umuoe....'nikasema kwa utani.

'A wapi mimi nilikuwa nakunywa kistaarabu, sema, ndio hivyo kila kitu kwa wakati wake, ni kweli kuna muda nilizidisha, nikaumwa karibu ya kufa...kifua ikawa TB,...aisee, nilijua nakufa...nilipopona nikabadilika, ...hapo nikaona umuhimu wa kuoa...sasa huyo mdada alitolea nje kabisa, ..'akasema

'Labda alikuwa na mtu wake kweli...'nikasema

'Ndio yupo jamaa mmoja yupo Ulaya kweli, lakini jamaa huyo akaja kumuoa mzungu, na ndio maana huyo mdada akachanganyikiwa akaanza kulewa...japo hakujionyesha,...nasikia ndio hapo akaja kukumbana na cha pombe..lakini kwa siri kubwa...hayo ni mambo ya ndani, ...'akasema

'Oh, siku zake zilishafika...'nikasema

 Ni kweli kwa taarifa za kifamilia, japo ilikuwa siri, msichana huyo alifariki kwa HIV, kutokana na dalili, na hata vipimo,  kiukweli mimi sikuamini, wengi hawakuamini..japo kwa hivi sasa HIV, unaweza kuipata kwa njia nyingine ila kwa huyo mdada ilikuja kuthibistishwa..aliipata kwa namna gani

Watu katika kuchunguza sana, kumbe, huyo mdada alikuwa akitembea na mvulana kwa siri sana kwa vile alikuwa ni jirani yake..ilikuwa ni kwa siri sana…wanasema alifanya hivyo kwa siri, na hakufanya kwa vile anampenda huyo mvulana, maana kiukweli hawakuwa wanaendana..ila kulikuwa na sababu za kuchanganyikiwa....

Ilivyoonekana, alifanya hivyo, pale anapozidiwa, mawazo na mengine yaliyokuja kusemwa baadae msichana huyo akatokea kuwa mpweke, alikuwa hana rafiki tena, akawa anawachukia wanaume, kila mwanume kwake ni sawa na huyo aliyemuacha solemba, swali likawa ilikuwaje huyo cha pombe amuone sio sawa na wanaume wengine.

Tatizo huyo msichana hakupenbda kuwa muwazi, na .maumbile ya kibinadamu hufikia sehemu utashindwa kuvumilia hasa ukiwa unatumia kilevi..kiukweli yasemakana, siku katika masiku ubinadamu ulimzidi, akakwaana na huyo mvulana, ilikuwa kwa bahati mbaya tu kama alivyokuja kusema..

'Hiyo bahati mbaya, ikaja kuwa mazoea hasa akizidiwa, 'alijitetea.

'Ilikuwa nawaza sana, ..mpaka nataka kujiua,...sasa huyo mvulana akawa ndiye mtu wangu wa karibu wa kuniliwaza,,,akawa anakuja kwangu, usiku wa manane maana nilikuwa naishi naye nyumba moja sema ni chumba tofauti, wote ni wapangaji'

Kiukweli huyo msichana  hakutaka kabisa watu wajue, na kiukweli hakumpenda kabisa huyo mvulana,..na yeye alitaka watu wajue kuwa yupo hivyo, ..bikira. Ila kilichoharibu ni kwa sababu ya huyo mchumba wake kumtelekeza.

Na zaidi ya hapo huyo mdada ndoto zake, zilikuwa  yeye aje kuolewa na watu wenye uwezo kwasababu wapo wengi walimtaka tena kindoa akawakataa.

‘Mimi siwezi kuolewa na mtu kama huyo…hana nyumba wala gari….mmh, mimi siwezi kuolewa na mtu kama huyo hajasoma,..ikawa zake ndio hivyo, siku zikaenda, hadi mauti yanamkuta,
Sasa ilikuwaje aje kutembea na huyo mvulana, ambaye hata kazi ya maana hana,..msikuma mkokoteni, na akipata peza zke ni kulewa tu,..siri ikaja kuvuja,!

**********

Inatokea, kiubinadamu,..tunahitajia umaarufu Fulani, lakini umaarufu huo, uwe wa kweli  , utoke moyoni. Usiwe wa kuwaonyesha wanadamu tu....na hasa umaarufu wa imani. 

Umaarufu wa imani haudanganyiki, utawadanganya wanadamu wenzao, lakini sio muumba wetu,…mola wetu anatufahamu zaidi tunavyojifahamu wenyewe, yeye anajua imani ya mja wake ni ipi ya kweli. Kiukweli  wapo wanajitahidi lakini nafsini mwao, kuna mambo mengi ya tamaa, husuda chuki, nk...na, wapo wanafanya mengi mabaya kwa hisia..nafsi zao zina siri kubwa sana.

Cha muhimu ni kumuomba mole wetu atusaidie tuweze kufikia malengo yetu..yale tunayotamani yawe, yale ya haki, yaweze kuwa hivyo,..na atusaidie kuziondoa tamaa mbaya nafsini mwetu, atujalie tuweze kuwapata wenza wema katika maisha yetu.


Ni mimi: emu-three

Saturday, July 6, 2019

HUJAFA HUJAUMBIKA...'Hivi kwanini mimi,...., nimemkosea nini mwenyezimungu...'nilisikia suti hiyo ya huzuni na kunifanya nisimame ghafla, na kunifanya nisite kuendekea na safari yangu, nilihisi mwili ukinisisimuka...'nimemkosea ni mwenyezimungu...' kauli hiyo ilinifanya nigeuze kichwa kuangalia kule nilipohisi sauti hiyo imetokea.

'Oh Mungu, nimekosa nini mimi jamani mpaka nipitie majaribu yote haya, ..mungu wangu naomba unionyeshe tu njia...'maneno ya huzuni yaliendelea wakati huo nimeshageuza kichwa kuangalia sauti hiyo inatokea kwa nani.

Kwa sauti tu,nilihisi ni sauti ya mwanadada, lakini macho yangu yalipotua kwa huyo ninayehisi kuwa ndiye aliyekuwa wakiongea, niligwaya.

Alikuwa binti mdogo sana, tofauti na nilivyodhania.

Kwanza kwa tahadhari nilitembeza macho huku na kule..maana dunia hii imegauka sivyo ndivyo, ya walimwengu ni mengi... kuna mitego mingi ya wahalifu inafanyika hivyo, unajitoa kwa wema unaangukia kwenye mitego ya hao watu, wanakudhuru au kukunyanganya kila na kukuacha uchi. Ila kilichonitia matumaini ni kuwa eneo hilo lina nyumba za watu, na nyumba nyingi ni kubwa zenye ukuta, na wengi wameweka nyaya za ulinzi, kuashiria kuwa wanaoishii humo ni watu wenye uwezo wao.

Niliangalia eneo lile alipokuwa huyo binti..nyumba hiyo kama nyingine ilikuwa na ukuta mkubwa tu na, ..juu yake ilionyesha kuna ulinzi wa kitaalam, ..nikajiuliza huyo binti anafanya nini kwenye eneo hilo, ..hajui kuwa nyumba hiyo ina ulinzi, na wenye nyumba hiyo hawatakubali watu kukaa eneo hilo kiusalama...na kwanini kakaa hapo, na anamlilia nani..

Nilipoona nazidi kutingwa na maswali, ....nikaamua jambo, nikavuta hatua moja, mbili....kabla sijafika pale alipo huyo binti,...na ukumbuke kwa muda huo, bado alikuwa akiongea kwa kulalamika kuhusu masahibu anayokumbana nayo...

Mwili uliendelea kunisisimuka, na hii ni kuashiria kuwa kuna hatari,...mimi nina hisia hizo, mwili ukinisisimuka, ujue kuna jambo la hatari ...lakini nafsi haikunipa uwoga, nafsi ilinipa ujasiri, kuwa nahitajia kujua, nikijua nitajua la kufanya...nikawa sasa navuta hatua, ...

'Ewe mola wangu, nionyeshe kosa langu, hadi nitaabike hivi...nimekuwa mtumwa wa walimwengu, wananichezea kama mpira wa karatasi, naadhirika, na hata wale niliowategemea kuwa watakuwa msaada kwangu wanageuka kunidha....dha...lilisha...'hapo kwikwi ya kilio.

Hapo na mimi nikasita mguu ukawa mnzito kuendelea ...nikatulia kwanza, akilini nikichanganua, je haya ni yangu, ..yasije yakawa maji mazito kwangu, ..aah, nikajipa moyo, ..ngoja nikasikia kwa kulikono,...nikaendelea kutembea...na sikuvuta hatua mbili, mara nikasikia...

'Mimi  ...siwezi tena..bora nife ..bora nijiue.'

Mungu wangu, bora nijiue...

Hapo sikuweza kusubiria, nikahisi nina dhamana, hii ni dhamana maana ni kwanini mola akanifanya niweze kuyasikia hayo, na ni kwanini, niache kiumbe kama huyu ..binti mdogo tu, aje kufanya, hilo alolodhamiria,na ni mashahibu gani yamemkuta hadi kufikia kudhamiria hivyo. Nafsi ikaingiwa na mshawashwa,..ikatamani kujua,...

Nikamsogelea,,,,.

Hata pale niliposegea hadi kumkaribia, bado alikuwa hajafahamu kuwa kuna mtu alikuwa bado hajafahamu kuwa mimi nipo hapo karibu yake, na hata kabla sijaweza kutoa sauti ya kumsalimia huyo binti , nikasikia sauti kali ikitokea ndani mwa hiyo nyumba, ambapo huyo binti kajiegemeza ukutani mwake.

'Huyu mshenzi kaenda wapi....we Taabu, ...we Taabu,...' sauti hiyo ilimfanya yule binti akaurupuke, na kusimama, hapo akaniona, akashika mkono kuziba mdomoni, lakini ...

'Usigope mimi sio mtu mbaya
'Ina maana umesikia nilichokuwa nikiongea
'Hapana...sijui uliongea nini...'nikasema
'Mungu wangu ..'akasema hivyo tu na haraka akakimbilia ndani

Kesho yake nilipita eneo hilo tena, nia ni kukutana na huyo binti, nijue ni nini kinachoendelea kwenye hiyo nyumba, nilipofika hapo nilikuwa watu wamejikusanya
'Kuna nini jamani...?' nikauliza
'Kuna binti kataka kujiua,...'akasema
'Kwanini
'Hata sisi tumebakia kujiuliza tu, na wenye nyumba hawataki kuelezea ukweli, wanasema hata wao hawajui
 Mara nikaona gari la wagonjwa likitoka, ..nikajua watakuwa wamemuwahi, ...
'Akipona ashukuru mungu...'ilikuwa kauli ya askari mmoja aliyetoka kwenye hiyo nyumba
'Kwanini unasema hivyo?'
'Sumu aliyokunywa ni kali sana...na walichelewa kutoa taarifa...'akasema askari

Kiukweli niliumia sana, ni kwanini sikufanya jitihada za ziada kukutana na huyo binti, nikasema na hata hivyo sikukata tamaa, nikafanya utafiti kujua huyo binti kapelekwa hospitalini gani, na wakati nauliza uliza ndio nikakutana na mama mmoja aliyesema anamfahamu huyo binti tokea akiwa mdogo.

'Sasa kwanini kakimbilia kutaka kujiua...?' nikauliza

'Mhh...we acha tu, hujafa hujaumbika, usilolijua ni sawa na kiza cha totoro...yule binti kapitia masahibu mengi, na huwezi amini huyo anayeishi naye ni mama wa kambo, mama yake alishafariki....

NB: Bado tupo kwenye maajribio, ili tuweze kurudi tena.

Ni mimi: emu-three

Tuesday, March 5, 2019

LA KUVUNDA HALINA UBANI...


 Ni wakati nipo msibani macho yangu, yalitua kwa mtoto mmoja aliyekuwa akilia sana, cha ajabu kilichonishangaza mimi,  hakuna hata mtu mmoja aliyemjali, …nilijiuliza ni kwanini, kiukweli hali yake hasa kimavazi haikuonekana njema, nguo zilikuwa chafu, na kuukuu. Hata hali yake ya kiafya yaonekana ni dhoofu…lakini naye ni muombolezaji, naye ana uchungu,….na…
Nahisi huo msiba umemgusa,…na sijui….

Nikageuka huku na kule, nikiwaangalia watu wengine,  watu hapo kwa ujumla  walikuwa kwenye majonzi makubwa,  wengi walikuwa wakilia, wengine wakionyesha nyuso za huzuni,…ilimradi kila mmoja alikuwa kaguzwa na huo, masiba.

Kuna wengine walilia hadi kupoteza fahamu…na watu kama hao, walikuwa na jamaa zao wa akaribu wa kuwaliwaza,..lakini huyu …mtoto, niliyemuona awali, hana…hana hata wa kumkaribia, kila aliyemuona alimtupia jicho moja, na kujifanya hajamuona…, swali akilini mwangu likawa linajiuliza, ni sawa, wengi wameguswa na msiba huo, hata kama sio ndugu wa karibu wa marehemu kivile…na wengi wanalia,…je huyu naye analia kwasababu gani…ni ndugu wa karibu,….au ….

Hamasa ya kufahamu zaidi ikanivuta….

Nikaamua kufanya jambo, …hata hivyo, awali haikuwa rahisi,..maana kulikuwa na watu wengi  mbele yangu na kwa wingi wa watu, nisingeliweza kuwapita  kwa urahisi, nafasi ilikuwa ndogo, ukiondoka sehemu mwingine anakuja kukaa…aah, hata hivyo, hamasa ilizidi…
Niligeuka kumuangalia tena,….bado alikuwa akilia, …tena kwa kwa huzuni kubwa,…hata mimi, pale nilipo, nikavutwa na hisia za kulia,….

Msiba unauma jamani….

Kiukweli msiba unauma…na unauma zaidi kutegemeana na mtu huyo alikuwaje mbele ya jamii, na zaidi kutegemeana na waombolezaji , na je kaacha nini nyuma yake,…watoto, mke au jamaa waliokuwa wakimtegemea, na zaidi ….hata waombolezaji wenyewe, au wana habari, wanaweza kumfanya kila mtu aliyehudhuria msiba huo aweze kulia….

Kwa  jinsi ilivyo, huyu marehemu,  alikuwa mtu aliyegusa watu, kimatendo, kitabia,…ndio maana wengi walifika  kumsindikiza kwenye safari  yake ya mwisho, ambayo ndio safari ya kila mwanadamu, …kwakwe tumetoka, na kwake ndio marejea yetu…

Nilisia mshehereshaji akiongea mambo mazuri ya marehemu…

Kwa vyovyote iwavyo, mtu akifariki, yatubidi tumuongelee kwa mambo mazuri, maana hayo mambo yake mema,  ndiyo taa ya mja huyo huo endapo,…tukiyaongea, taa hii huzi kuwaka,, kamwe tusipende kuongelea mambo yasiyo mema, hata kama aliyafanya, ili tusififishe mwanga wa taa yake..hayo ni maneno mazuri  niliyoyakumbuka kutoka kwa watu wa imani.

Akili yangu ikarejea kwa yule mtoto…ni…kijana, ni kijana wa takiribani, miaka kumi na mbili hivi…….nikaamua kumsogelea, hadi pale alipochuchumaa, pembeni yake kulikuwa na mfuko wa Rambo, na ndani yake kulionekana nguo nguo hivi….kwa muda ule yule kijana, alikuwa kachuchumaa, naona sasa miguu imemuisha nguvu…hawezi kusimama tena, na bado hakuna mtu aliyemjali..

Hakuna hata aliyepoteza muda kumuangalia tena…, wengi walitekwa na matendo yanayoendelea mbele ya jukwaa…watu wanavyoomiongelea  marehemu…na mengineyo.
Mimi nikamsogelea yule mtoto….

‘Pole kijana…pole sana..yote ni kwa mapenzi ya mungu, …’nikasema nikimsogelea na kumshika begani.

Yule mtoto, ..ni kijana akainua uso na kuniangalia, uso ulikuwa umefunikwa na machozi….akatikisa kichwa…kama kusikitika. Akavuta pumzi, haalfu akasema;

‘Ni kweli yote ni kwa mapenzi ya mungu, lakini kwangu, …..kwa-kwa…ngu, ime-ime….kuwa ni….mengine yanauma kaka yangu,sijui nikuite kaka yangu, au baba, hata sikujui…..sijui niseme nini…inaniuma kwa-kwa –kwa -kwe….’akasema. akishindwa kumalizia maneno.

‘Kwa muda huu, hakuna cha kusema iliyobaki ni kumshukuru mungu, kwani yeye ndiye mwenye mamlaka ya haya yote…, kwake tumetoka na kwake ndio marejeo yetu, ndio kauli sahihi,..’nikasema

‘Ni sawa…lakini mwenyewe si umeona..mimi kama mimi nitakuwa mgeni wa nani,…nimetoka mbali nikijua nimeshafika kwa…..lakini sasa,..ooh,.. ‘akaanza kulia.

‘Umetokea wapi…?’ nikamuuliza.

‘Yaani,..nilijua,…nikifika nitamkuta…nitaongea naye, nita…..sasa nakutana na haya….niende wapi mie…’akasema.

‘Oh, ina maana…’nikatakla kuongea kuhusu hisia zangu, lakini yeye akaendelea kuongea.

‘Hebu niangalie…mimi kama mimi nitamuendea nani sasa , hebu niambie kaka yangu…ni nani atakayeniamini, mtoto wa majalalani…niangalia nilivyo, ni nani, ata……kwa hivi sasa sina mama, na sasa sina….ooh…’akaanza kulia,…kiukweli hata mimi nikalia.
Baadae nikamwambia…

‘Oh..usijali yote ni mapenzi ya mungu, yey e ndiye atajua uta…’hapo sikuweza kuendelea yule mtoto, au yule kijana  akalala chini, na kunyooka,…alionekana kupoteza fahamu.
Hapo sasa baadhi ya watu wakafika na kuanza kumsaidia.

‘Huyu ni nani…?’ akauliza mmoja wa jamaa aliyefika pale.

‘Mhh..hata simjui…’akasema mwingine

‘Sio jamaa au mtoto wa marehemu…’nikasema

‘Hapana,….mtoto wa marehemu awe hivi..wewe vipi bwana….’akasema jamaa aliyeonekana kuwa ni mtu au jamaa wa  marehemu.

‘Lakini…..’nikataka kuyarudia yale maneno ya yule mtoto, lakini huyo aliyesema…hapana, akiwa na uhaklika kuwa huyo mtoto sio jamaa ya marehemu akaondoka, .
Kwa muda ule huduma za kwanza za huyo mtoto zilikuwa zikiendelea, baadae akazindukana, na alichosema kwa haraka,,,

‘Najua hawataniamini, ..najua…kwa vile mimi sasa ni yatima, lakini, nasema hivi…haya ni kizalia,, leo kwangu kesho itakuwa kwa mwingine…’aliposema maneno hayo, akapoteza fahamu tena.


WAZO LA LEO: Diary yangu, inatoa pole kwa msiba wa mpendwa wa wengi, …RIP Ruge, ..hatuna cha kuongeza, zaidi ya kukuombea makazi mema peponi, na kuwaombea wazazi na ndugu subira njema, …kwani yote hayo ni kwa mapenzi ya mola.

Ni mimi: emu-three

Thursday, October 11, 2018

CHOZI LA KUTOKA MOYONI-2


‘Ndugu yangu liogope chozi la kutoka moyoni…hili ni chozi la huzuni, chozi la majuto, chozi la kukosewa, chozi la kulalamika…huwezi kulitafsiri, maana linakuja tu..na huja kwa jambo maalumu sio hivi hivi tu..kwa aliyezoea kulia, …hili sio chozi lake..’aliendelea kunihadhithia rafiki yangu.

Hiki ni kisa cha kweli kilichonitokea mimi na familia yangu...’akasema huyo rafiki yangu anayenisimulia kisa hiki....

‘Unajua mimi sikupenda kuyahadithia haya, lakini nataka mlione chozi la namna hii linavyofanya kazi yake maana sio chozi la kawaida,…na  nakuhadithia hiki kisa, sio kwa nia ya kuwalaumu hao walionitelekeza, huenda walifanya hivyo kwa nia ya jinsi walivyoona ni sahihi kwao, ila maamuzi hayo yalitoka kipindi ambacho niliwahitajia sana…maana nilitarajia mengi  baada ya kuwafanyia kazi zao kwa kujitoa kwa moyo wangu wote, na nini walikuja kunilipa sasa,…

'Malipo yangu ndio hayo kuwa mimi sihitajiki tena....'akasema

'Pole sana...'nikamwambia 

‘Yote namuachia mungu…’akasema na kutulia.

'Hebu sasa niambie kwa kirefu, ilikuwaje kwenye hiyo kampuni hadi ikafikia hapo...?' nikamuuliza

Tuendelee na kisa chetu...

*************

 Kwa kuhadithia tu, mimi nilianza kufanya kazi kwenye kampuni hiyo, ikiwa na mapungufu mengi tu, na waliniita hapo kwa vile walisikia kuwa mimi ni mtaalamu kwenye hiyo idara ...ni kweli na nilipofika hapo na kuyaona hayo mapungufu, nikaamua kutumia ujuzi wangu na uzoefu wangu kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa…na nilifanya hivyo nikijua huenda huko mbele kutakuwa na neema. Hayo ndio yalikuwa matarajio yangu.

Katika kuwajibika huko, niliweza kuokoa mamilioni ya pesa, pesa hizo hazikuwa zimejulikana, kutokana na mahesabu yao  na kumbukumbu zao, kutokuwa sawasawa, na bosi aliposikia hivyo alifurahi sana, nikajua labda tutapewa kifuta jasho (bonasi,..lakini haikutokea, sikukata tamaa, nikajua ipo siku.

Kazi zikaendelea, lakini kutokana na hali halisi ya mabadiliko, ya kinchi, nisema hivyo... ambayo sio kwa kampuni hiyo peke yake tu,…biashara haikuwa nzuri sana, kwahiyo kukawa sasa na tetesi kuwa huenda watu wakapunguzwa, mimi sikuwa na wasiwasi na hilo..., maana kama niliweza kuokoa mamilioni ya pesa, kwanini kampuni inipunguze mimi.

Ndio maana baada ya kupata taarifa hiyo, niliumia sana, niliumia kwa vile nilishafika mahali nikawa napanga maisha, nakopa huku na kule ili watoto wasome,..najua mwisho wa mwezi nitapata fungu langu, japokuwa lilikuwa lapatikana kwa nusu nusu...lakini unakuwa na uhakika hata ukikopa utakuja kulipa.. Sikujali, nilijua ndio hali halisi…

 Sasa kilichoniuma zaidi ni pale nilipopigiwa mahesabu ya nini nilipwe,..hapo ndio unaweza kuona jinsi gani haya makampuni ya watu binafasi yalivyo na dhuluma...

‘Wewe mwenyewe unaifahamu hali halisi, kwanza nilikuwa sijakuajiri, kweli si kweli... ulikuwa kama kibarua tu,…kwahiyo kutokana na hali halisi,...sipendi, unaonaee..nifaneje sasa, na sitaki uondoke mikono mitupu, etu usubiria mpaka nikijaliwa, lini sasa..kwahiyo mimi nimeona hivi.. tutapiga mahesabu yako ya mwezi huu…umefanya siku ngapi vile…’akajifanya kama hajui. Mimi nikabakia kimia.

‘Eeeh mwezi uliopita umelipwa pesa yako yote…?’ akauliza kama vile hajui hilo

‘Bado, …nimelipwa nusu mwezi…’nikasema kwa sauti ya unyonge, nimeshavunjika nguvu, nilikua kwa juhudi zangu nilizofanya, angalau...ningelipewa hata asante

‘Ok, sasa..tutachukua hiyo nusu mwezi ilibakia na tutaongeza na siku hizi za mwezi huu ulizofanya, tutakulipa,…nitahakikishe umelipwa hizo pesa zako, sitaki uondoke mikono mitupu…’akasema

‘Ina maana, ndio malipo hayo ya  mwisho…?’ nikauliza

‘Wewe mwenyewe si unaona hali halisi, nitakulipa nini, shukuru kuwa mimi nitafanya juhudi upate hizo…nusu mshahara uliobakia, na siku hizi za mwezi huu ulizowahi kufanya..na..kiukweli sikutegemea kuwa kazii hii itachukua muda wote huu, mimi nilitarajia utafanya miezi mitatu, ..tumalizane…’akasema

Sikutaka kusema lolote kuwa kama ningefanya hivyo anavyodai yeye, asingeliweza kuyapata hayo mamilioni ya pesa, nikabakia kimia, nikiumia kimoyo moyo..

‘Nitamwambia mshika pesa wangu akupigia mehesabu yako, na akulipe, lakini hakikisha kazi zako zote ulizotakiwa kufanya umemaliza…najua sina shaka na wewe, lakini kwa kukumbushia tu, sitaki mtu aondoke hapa kabla hajamaliza kazi zake,..na nitakulipa baada ya kukaguliwa kuwa kweli umemaliza kazi zako…’akasema

Sikuamini hayo maneno, ina maana kafikia sehemu ya kutokuniamini tena…moyoni nilitaka kumuambia, kama ungelinijua nilivyo, usingelisema maneno hayo, hata kama unaniondoa mimi nitafanya kazi yako yote…kimujibu wa taaluma yangu, ..ndivyo nilivyo, sina haja ya kuwa na kisasi na yeye.

Yaliyofuata hapo baadae huwezi amini, nilioanza kuonekana kama mtu ambaye naweza kuharibu kazi, naweza kuiba, naweza kufanya jambo na kukimbia,…sikuamini…

Haya ngoja turudi siku ile…ambayo, nilitakiwa nirejee nyumbani, nikutane na muuza duka,..siku ya kulipa ada..siku ya…mke wangu anategemea nitakuja na mkopo, ili aweze hata kuanzisha duka,…siku ambayo nilipewa hiyo taarifa kuwa kazi sasa basi.

*************
Siku ile naikumbuka sana, kwani ni siku ambayo….nilianza hata kuumwa maradhi ya moyo…

Wakati naondoka kazini, nilipanga nisipitie njia ile ya dukani, kama nitawahi kufika, kama nitafika maduka yamefungwa itakwua ahueni kwangu…na hata hivyo huko kwa dukani nikipita salama, nitakwenda kusema nini kwa familia yangu…kiukweli nilikuwa na wakati mgumu sana.

 Siku ile…, pamoja ya kutoka kazini kwa muda ule ule wa saa kumi na moja, cha ajabu siku ile usafiri ukawa ni rahisi,…hakukuwa na wingi wa abiria, nikapata gari, japo la kusimama, mwili hauna nguvu, lakini utafanya nini..tumbo halina kitu, ningelikula nini, wakati bajeti imebana.

 Cha ajabu siku hiyo nikafika nyumbani mapema sana, tofauti na siku nyingine…akilini nawaza nikifika nitaanzaje kumwambia mke wangu…mawazo hayo yakawa sasa ndio yameuteka ubongo wangu…unajua mkiwa mnaishi pamoja, unajau ni kitu gani uongee na mwenzako kwa wakati gani,…nilimpenda mke wangu na familia yangu sikupenda kabisa ije kuumia, nipo tayari kufa kwa ajili ya famili yangu.

Kwa jinsi nilivyotekwa na mawazo hayo ..ya jinsi gani ya kufikisha ujumbe huo kwa familia yangu,…, nilisahau kabisa lile wazo la kupitia sehemu nyingine kumkwepa mwenye duka, maana njia ya kufika nyumbani ni lazima upitie kwenye hilo duka, lakini kuna njia nyingine ya kuzunguka…wakati natoka kazini, nilipanga nipitie njia ya kuzunguka…lengo ku mkwepa huyo muuza duka.

Ndugu yangu, sio kwamba mimi ni muoga kiasi hicho, ila kiukweli huyo jamaa sifa zake za ukatili, zinajulikana sana, kwanza alikuwa jambazi, na…sio kwamba natania, ipo siku moja alishikwa mwizi, ..kwa macho yangu nilimuona jamaa huyu akionyesha unyama wake kwa huyo mwizi, aliyetaka kuvunja duka lake ili aweze kuiba, ilikuwa alifajiri mimi nawahi kazini

Walikuwa wawili mmoja akaweza kuponyoka na kukimbia, sasa huyu aliyeshikwa, ambaye alijiona ni mbabe, ndiye alikutana uso kwa uso na huyu muuza duka,…mwizi alikuwa mtu kashiba, ana miraba minne, na akaamza kukabiliana na huyu muuza duka, lakini hakuweza.

‘Huyu niachieni mimi mwenyewe, nataka niwaonyeshe kuwa mimi siibiwi..na hakuna atakyefanya hivi hapa tena….sitaki utani mbele ya mali yangu…’akasema, kwanza alikuwa na kisu akakurusha pembeni.

Mwizi kuona hivyo, akajua huyo muuza duka ni rahisi kwake, ,…wakaanza kutupiana ngumi na huyu mwizi kwanza mwizi alionekana kumzidi muuza duka, lakini hakuna aliyeingilia,..watu walikuwa wamesimama  pembeni.

‘Ukinishinda, umepona, ..nikikushinda umekufa….’akasema huyo muuza duka, kifua wazi, na bukuta la kulalia…bukta lake lina sehemu ya kuhifadhia kisu –ala.

Ikawa kila mwizi akipatwa na konde moja usoni, anabwagika chini,…anajizoa hara haraka, kawa sasa kama kalewa… watu wakawa wanacheka…mwizi gani kila ngumi anakwenda chini…lakini mwizi akawa anapmbana akijua ndio kupona kwake, kufa au kupona…

 Ikatokea wakati mwizi akarusha ngumi, mkono ukadakwa na huyo muiza duka, kwa jinsi alivyoshikwa tulisikia mlio wa kooo….mkono ukavunjwa na hapo hapo, huyo mwizi akarushwa hewani, alizungushwa hewani kama mzigo tu, na kubamizwa chini, na watu walishangaa huyu mtu ana nguvu gani ya kuweza kumbinua huyu mwizi hewani, mwizi ambaye kiumbile anamzidi huyo muuza duka…ilibakia historia.

‘Mimi sina huruma na pesa yangu,…pesa yangu ina thamani ya utu, ukinichukulia pesa yangu, umevunja utu wangu na mimi sitakuwa na huruma na utu wako..nitakumaliza tu…hilo nimeapa, sasa wewe  mwizi utakuwa fundisho hapa mtaani, nitakuonyesha kile ambacho watu hawakijui kunihusu mimi…’akasema

Huyo mwizi anagugumia mkono umevunjwa, muuza duka akawa bado hajaridhika,…akasogea pale alipoweka kisu chake, akakichukua mwizi hata hawezi kuinuka, kukimbia, ..muuza duka akamrejea na kumshika huyo mwizi sikio akalikata sikio…

‘Hiyo kwanza ndio alama yako kuwa wewe ni mwizi, mimi nilikuwa jambazi, na jaambazi ukikamatwa ujue ni kifo, sasa mimi nimeacha, sitaki kuibiwa tena, wewe wataka nirejee kwenye wizi…’akasema

Na hapo hapo akakitumbukiza kile kipande cha sikio mdomoni akakitafuna..sasa sijui atakimeza au la,… kwa haraka ageuka kwa kasi ya ajabu, kile kisu, kikapita kooni kwa huyo mwizi, damu zikaruka,…

‘Aaah…’ mwizi akapiga ukelele.

Tukajua koromeo limekatika…bahati mbaya kisu hicho kilkwepa koromeo, kikakata sehemu ya koo … lakini kilifanya kazi yake ..mwizi yule akalala chini, anakoroma kama mtu anayekata roho.

‘Hufwi eeh,..umechafua kisu changu halafu hujafa… ngoja nikuone kama hutakufa…’jamaa akaingia dukani, na kuchukua chupa ya mafuta ya taa…mimi hapo  sikuweza kuvumilia tena…huyo, nikaondoka zangu kuwahi kazini..

 Nilipokumbuka hayo, nikajua huyu mtu hana mzaha kweli kwenye pesa yake, na kweli kwa maana kwa yoyote eliyewahi kumkopa akachelewa kumlipa pesa yake cha moto alikiona.., kwanza akija kwako utapokea  kipigo, na kipigo hicho yeye mwenyewe anakuruhusu upigane naye, halafu anachukua kitu chochote ambacho kinaweza kulipa deni lake,..

Sasa sijui mimi yatanikuta hayo au….kwahiyo sio kwamba niliingiwa na wasiwasi huo bure… jamaa huyo ana visa vingi, akipigana na mtu,..ngumi yake ikikupata lazima utaenda chini, yeye anadai, alishaambiwa asitumie mkono wake kupiga mtu, hasa wa kushoto..alishawahi kumvunja kaka yake mkubwa wake taya, kwenye ugomvi ugomvi

*********

Sasa ghafla bin vuu,..nikawa nipo maeneo  ya duka…nilishasahau, kuwa nilipanaga nitumie njia nyingine ili kumkwepa huyo muuza duka, ..mawazo ni kitu kingine kabisa, na ilipangwa tu , lazima nipitie hapo dukaniu.
.
 Nilipofika hapo , nikawa sina jinsi, nikasema moyoni potelea mbali, mungu atanilinda, nikasogea pale dukani, …sikumuona huyo jamaa, yupo kijana wake, ajabu mara nyingi huyu jamaa hamuamini mtu, nikajua labda yupo chooni, ..hata hivyo nikasema  afadhali.

Nilisema afadhali, ..sio kuwa nitakuwa namkwepa hivyo kila siku, nilikuwa na maana nahitajia kwanza nifike nyumbani,…, nipate muda wa kujipanga, jinsi gani ya kukabiliana naye,..najua ni lazima nionane naye ..hata hivyo akili ilikuwa imechoka sana..nilihitajia nikalale kidogo hadi kesho .

'Bosi wako yupo wapi…?’ nikamuuliza hapo kwa kujiamini kidogo.

'Katoka hapa sasa hivi…, anasema anawafuatilia wadeni wake, kakasirika kweli kweli…’akasema huyo kijana wake.

'Mungu wangu...'nikasema hivyo tu kuondoka pale dukani kwa haraka…, nikikimbilia nyumbani kwangu sio mbali sana na hapo dukani,…na hisia zangu, ni kuwa huenda familia yangu ipo chini ya ulinzi ya huyo jamaa au keshawafanyia kitu kibaya. Pamoja na kumuogopa hivyo, kama atakuwa kaifanyia kitu kibaya familia yangu, tutapambana…

Nafika eneo la nyumba yangu, nasikia sauti ya jamaa akifoka huko ndani, nikajua sasa..kumekucha, sasa naingia vitani, japokuwa nafahamu fika kupambana na huyo mtu siwezi lakini nitajitahidi …

Na kwa namna nyingine nikaona labda kuepusha shari, ni bora nirudi nilipotoka, nikakae sehemu hadi usiku ndio nirudi, lakini je hapo alipo hajafanya chochote kibaya, ikawa ndio wasiwasi wangu huo..

Nikawa sasa natamani nigeuke nirudi nilipotoka, na kabla sijafanya lolote la maamuzi yangu, mara mlango ukafunguliwa,  jamaa huyo katoka. Akaniona, au sijui hakuniona maana kilichofuata baadae ilikuwa ndio jibu halisi…

 Alipojitokeza pale malngoni, uso umebadilika kawa mweusi, …jicho limemtoka nikajua sasa napambana na simba…kurudi nyuma siwezi, kusogea mbele siwezi nikawa nimeganda, nasubiria kitakachofanyika

Jamaa huyu anakuja usawa wangu, nikawa nimejiandaa, huku moyoni nasema, kiukweli ilibidi iwe hivyo, kumuomba mungu, maana sikupenda iwe shari..,…

‘Mungu wangu nisaidie kwa hili, haya yote sio kwa kusudio langu. Je mimi sikutimiza wajibu wangu kazini,.., je mimi nimefanya dhambi gani hadi niondolewe kazini, nimefanya kosa gani hadi nije kuzalilika hivi…najua kabisa ningelikuwa kazini, haya yasingelitokea…naomba msaada wako, ewe mola wangu…’nilijikuta nasema hivyo tu, kwa hisia za ndani,..sijui ila nahisi ilikuja hali ya chozi kama lile la ofisini

Nilishangaa….mimi sina kawaida ya kutoa machozi…na niliona ajabu tukio hilo liniathiri kiasi hicho,…najiona nipo kwenye mabadiliko mengine makubwa.

Basi kwa muda jamaa alishafika usawa wangu…nikitarajia kipigo, najua nitajitetea, lakini najua kiundani siwezi kupambana na mtu kama huyo…

Ajabu kabisa jamaa akanipita kama hanioni,…upepo tu, nikayumba… sikuamini hilo…karibu anipige kikumbo, huyooo kwa haraka akawa anaondoka…

Mimi ilinijia kwa mshangao, sikumini kabisa kama jamaa huyo angeliliweza kunipita bila kufanya jambo, bila hata kunifokea…kwa vile sikuamini, taratibu  nikageuka kwa mashaka, kumuangalia kama kweli ndio anaondoka,...

Ile nageuka, kumbe naye sijui alikuwa akiwaza nini, naye kumbe akagauke, tukawa tumeangaliana, lakini kwa umbeli, alishanipita na kwa vile alikuwa akitembea kwa haraka ilikuwa ni umbali wa hatua kadhaa,..hapo ndio sijui, alikuwa hajaniona au..na kwanini alipogeuka alikuwa akainiangalia kama kushangaa vile…na alipogeuka tulikutanisha macho.
.
Hakusimama na wala hakurudi nyuma…

Ilipita dakika mbili hivi bado nimesimama, na akili iliporejea kwenye msimamo wake, ndio nikakumbuka kuingia ndani kuiona familia yangu…nikatembea kwa hatua za haraka haraka, kawaida nikifika nyumbani nagonga mlango kupiga hodi..

Sikufanya hivyo….nikasita kufanya hivyo, nikajikuta nasita hata kushika kitasa…nahisi mwili ukinisisimuka, …ni hali ngeni kwangu..hata hivyo, nikashika kitasa na kuzungusha , mlango ukawa wazi..

Ile natupa macho ndani, naangalia sakafuni, namuona mke wangu…na mtoto kasimam akiwa kainamisha kichwa…

NB….ILIKUWAJE…Ndugu zangu, nahis kama nisipopata kitendea kazi, kisa hiki na hicho kingine kitechelewa kidogo maana sehemu niliyoitegemea , nilipokuwa nimejishikiza sitakuwepo tena…mniombee tu, nipate sehemu nyingine.


WAZO LA LEO: Yakikukuta matatizo, shida , mitihani, kamwe usikate tamaa, wewe elekeza imani yako kwa mwenyezimungu, kwani yeye anatosha kukuongoza na kukusaidia kwenye hatua nyingine.
Ni mimi: emu-three

Wednesday, October 10, 2018

CHOZI KUTOKA MOYONI
CHOZI KUTOKA MOYONI…

                        UTANGULIZI

Nilifika ofisini asubuh kama kawaida yangu, nikafanya shughuli zangu kwa haraka, nikijua leo bosi akija cha kwanza tu nafika ofisini kwake nimpa ripoti yangu ya wiki, ya kazi zangu nilizofanya , ndivyo tunavyofanya, … halafu namkabidhi barua ya mkopo...lengo la mkopo, kulipa ada za watoto, mengine ni siri yangu..

Moyoni nikawa namuona mke wangu akifurahi, ..kama vile nimeshaupata huo mkopo na sasa namkabidhi sehemu ya fungu anampeleka mtoto hospitali na nyingine atafanyia biashara..na mawazo hayo yalikatishwa na mawingu ya sauti zenye kunitia mashaka …sauti za kumbukumbu…

'Kama usipolipa ada yako mwezi huu… watoto wako wasije tena hapa shuleni..'barua ya shule ilisema hivyo, na ujumbe wa simu, kwenye simu yangu..


Hawa walimu bwana...hivi hawajui hali halisi,...ngoja nipate pesa, mimi  nitawalipa pesa yao yote, niwe huru, watoto wangu na wao wasome kwa amani, najua elimu ni bure lakini nimeona niwalete huku angalau wasome kama watoto wa bosi, japokuwa shule yenyewe sio sawa na ile ya bosi,..angalau lakini..nikawaza moyoni,

‘Lakini wapi pa kuzipata hizo  pesa…’nikasema moyoni

‘Mhh, hizi sasa. ni ndoto za Alinacha…’nikazidi kujisemea.

Mara nikasikia sauti nyingine akilini hii ni ya kutisha kabisa…hadi mwili ukazizima kwa uwoga.


'Unasikia, kama usiponilipa hilo deni,...nitakachokifanya usije kunilaumu...'hiyo ilikuwa sauti ya muuza duka. Huyu muuza duka wanasema awali alikuwa ni jambazi mkubwa, na pesa alizoanzishia hilo duka ni za uporaji, na wanasema yeye kwake kuua ni kazi ndogo tu, askari wameshindwa kumpata kwa vile hajawahi kukamatwa, na ushahidi.


'Nitakulipa ndugu yangu...kesho nikifika kazini nitaomba mkopo, najua bosi atanipatia tu...huwa najituma sana kazini..'nikasema nikiwazia wazo la mke wangu.


'Mkopo ulipe mkopo, hahaha, unanishangaza sana wewe mtu, sawa, ila niamini, sitaki mzaha kwenye pesa yangu...'akasema muuza duka


'Wewe hujui maisha...ndivyo tunavyoishi, wewe subiria pesa yako, na kama nisipokulipa,...njoo, kachukue chochote nyumbani...'nikasema kwa kujiamini


'Hahaha haya bwana,...wewe hutaamini nitakachokifanya...'akasema , ni kweli muuza duka huyu ni rahisi kukukopesha, lakini muda ukipita, wewe sikilizia vumbi lake, wengi wanamfahamu wakikipa haraka hurudi kumlipe deni lake, kwahiyo wengi wanakopa wakiwa na uhakika wa kuja kumlipa, hana wasiwasi kukupa kitu.


Mimi nilikuwa na imani nitapata pesa, maana nimekuwa nikijtuma sana kazini, wakati mwingine nafanya kazi hadi usiku, bila hata malipo ya ziada,..,..na sijawahi kuomba mkopa kwenye hiyo ofisi kwa vile naifahamu ilivyo, huyo bosi kutoa mkopo ni nadra sana


Na tokea awali sikuwa na wazo kabisa la kukopa ofisini hapo, kwa jinsi nimjuavyo huyp bosi na hali halisi ya ilivyo, lakini hadi kufikia uamuzi huo, ni kutokana na ushawishi wa mke wangu ndiye alinishauri,


'Mume wangu waonaje kutokana na hii hali, ukakope kiasi fulani ili nikifanyie biashara,..na kiasi kingine tulipie ada, watoto wasifukuzwe wapo mwaka wa mwisho...na kufukuzwa fukuzwa kuna wavunja nguvu..na nyingine tumtibie huyu mtoto wetu anayeumwa, unajua tunazarau hali yake, inaweza kutuletea matatiz baadae…tukaja kulaumiwa na madocta..'akasema mke wangu.


'Mhh, mke wangu, ..ungelijua...ofisini kwetu, mpaka bosi akupe mkopo labda, itokee miujiza...bosi wetu hajali kabisa masilahi ya mfanyakazi zaidi ya mshahara wako,.na imefikia hata mshahara analipa tarehe 35 au 40….na hata hivyo hali ya kiofisi ni mbaya,biashara hakuna, na  pesa hakuna kampuni ina hali mbaya sana..'nikasema


'Wewe nenda kajaribu tu, huwezi jua, muelezee hali halisi yeye kama mzazi ataelewa, si yeye ana watoto pia, anasomesha kama sisi, anauguliwa kama sisi, wewe mjaribu tu.....usijitwike mzigo kabla haujatua kichwani mwako...'akasema mke wangu .


'Mhh...haya...'nikasema hivyo.


Hapo ndio na mimi niliingiwa na wazo hilo la kukopa kazini…, nikajipanga, nikiona kweli kwasasa ina haja ya kufanya hivyo,.utaenda wapi sasa, muajiri wako ndiye wa kukufaa wa wakati wa dhiki…nimefanya mengi ya kuiaidia kampuni, kwanini mimi wasinisaidie na mimi..

‘Nikipata huo mkopo, sehemu yake nitamlipa yule muuza duka deni lake, maana mhh…asija kunkata kichwa, …sura hata macho yake yanatisha..na hilo deni hata mke wangu halifahamu..’nikajisemea hivyo.


**************
Japokuwa nilikuwa nawajibika sana kazini, lakini siku hiyo moyoni mwangu nilihisi wasiwasi,…ni kama vile unahisi kitu kibaya chaweza kukutokea, labda ni mawazo ya maisha, na nikakumbuka labda….


Nikahisi labda ni ile taarifa niliyoisikia wiki iliyopita, kutoka kwa wafanyakazi wawili wakiongea,...ni mazungumzo ya kawaida tu ambayo yanaongelewa kila siku.


'Nasikia bosi kapanga kupunguza baadhi ya wafanyakazi...'nilisikia mfanyakazi mmoja akisema.

'Acha afanye hivyo bwana..’akasema huyo mwingine

‘Yaani wewe unaona ni sawa tu..’akasema mwingine

‘Ndio hata mimi ..namuunga mkono bosi…, maana wanaajiriwa wafanyakazi wapya , eti wasomi, halafu wanalipwa mishahara mikubwa zaidi yetu sisi. Hebu wewe angalia, sisi tupo hapa kwa muda gani, tokea kampuni hii inaanzishwa, hatuongezwi kitu, tunakuwa wasindikizaji tu, mimi nitafurahi wakiondolewa tu....'akasema mwingine.

'Wewe una uhakika gani kuwa hutaondolewa hapa kazini?'akaulizwa.


'Mimi najua tu, siwezi kuondolewa, mshahara wangu ni mdogo sana, hauwezi kuitia kampuni hasara, …nakuambia kitu,…wote wamekuja na wote wataondolewa, wewe niamini hilo…’akasema

‘Mhh…unajiamini …’akasema mwenzake.

‘Mimi nakuambia..hao, wataondolewa wote..wametukuta, na watatuacha na kampuni yetu,.."akasema kwa kujiamini na kucheka, sikujua kwanini huyo mfanyakazi anajiamini hivyo.


'Ni kweli, uzuri wake sisi bosi tumeshamjulia, hawa wageni wakija , wanajifanya wanajua kuliko hata bosi,..hawamjui huyu bosi wetu alivyo, anakupenda akiwa na shida na wewe, shinda yake ikiisha, hajali, atakuondoa tu...'akasema mwingine.
Wafanyakazi hao kazi yao ndio hiyo, wakifika ofisini asubuhi, asilimia kubwa ni kuteta, magumzo vibarazani, hawafanyi kazi mpaka wamuone bosi..


Bosi akiingia hutaamini,...wanajituma utafikiria sio wale waliokuwa wamekaa , wakiongea, kusoma magazeti…au kupiga gumzo la mipira au siasa..lakini ngoja bosi afike, huwezi amini, watakavyowajibika,..na bosi akiwepo, kweli wanawajibika,...na wanahakikisha bosi anaona kile wanachokifanya....kiukweli wanajua kuigiza. na wanampatia sana huyo bosi


'Ukitaka bosi huyu akupende iwe hivi, na jingine eeh…usije kumuomba pesa, anaipenda pesa zaidi ya benki…na jingine usije kumlalamikia shida zako, hapendi kusikiliza shida za mtu, kwake yeye umuonyeshe kazi, uongee naye kuhusu kazi zake, atakuwa rafiki yako,…ole wako uende kulalamika mambo ya mshahara hautoshi, umechelewa,…hahaha, utaniambia..'aliniambia mmoja wa wafanyakazi siku nilipomuuliza kwanini wanafanya hivyo.


'Kiukweli mimi hivyo siwezi, nitafanya kazi kwa mujibu wa taaluma yangu, akiwepo au asipokuwepo, na akija kama sina zaidi, nimemaliza kazi nahitaji kupumzika kidogo nitafanya hivyo, ilimradi nimetimiza wajibu wangu…mimi sio mtumwa wa kuigiza...'nikasema


'Hahahaha haya, na kwa jinsi anavyowalipa, moyoni hafurahii kabisa, ipo siku wewe utaniambia wewe jitume tu...'akasema jamaa huyo.


Pamoja na kujituma kwangu, kuwajibika kwa mujibu wa kazi yangu, niliona kama wafanyakazi hao walikuwa hawaniangalii kwa jicho jema, mimi sikuwajali nikijua udhaifu wa binadamu ulivyo, husuda na chuki ni hulka zetu.


**************

Basi mara nikasikia bosi mwenye kampuni kafika, kwa haraka nikaweka barua yangu vyema na kuhakikisha kila kazi niliyotakiwa kuifanya nimeikamilisha, nikatengeneza taarifa ya kazi yangu ya wiki ili iwe chambo cha kuanzia, sikutaka matatizo


Wakati ndio nataka niende ofisi kwa bosi, mara nikasikia nikiitwa.


Nilihisi moyo ukinilipuka, phaa...sijui kwanini,.. hata hivyo sikujali sana, nikajua labda bosi leo kanianza mimi, anahitajia kujua nilichofanya wiki nzima iliyopita.


'Hamna shida sasa nimepata wapi pa kuanzia...'nikasema nafsini mwangu.


Kwa haraka nikakusanya makabrasha yangu, na laptop, ili niwe kamili kamili,...sikutaka uzembe kwenye kazi zangu, kwa haraka nikaelekea huko.


Sasa wakati natembea kuelekea kwenye hiyo ofisi, nikakutana na wafanyakazi wale wawili, , wakaonyesha tabasamu, kama la kujali na kunipa moyo na nilipogeuka kuangalia ninapokwenda, wao wakaangaliana na mimi nikawa nimegauka kwa haraka kuwaangalia


Niliwaona wakionyesheana ishara ya dole gumba...mimi sikuwajali, haraka nikaingia ofisi ya mkubwa wa kampuni.


'Habari za asubuh bosi...'nikasalimia kwa heshima na bosi kwanza akahema kwa nguvu, halafu akasema.

'Nzuri tu,...hebu kaa hapo, nina mazungumzo na wewe..' akasema hivyo. Hapo, nikaanza kukata tamaa, maana nilitaka aanze kuniulizia hali za familia, ili niweze kuchomeka matatizo yangu halafu, phaa...namkabidhi barua ya mkopo.


'Bosi mimi ripoti yangu ipo tayari kama ndio uliyoniitia...'nikasema


'Sio kuhusu ripoti, nimekuitia,jambo jingine tu, wewe kaa hapo, na weka pembeni kazi zako. ...'akasema na kutulia kidogo, hapo nikaanza kuwaza mengine, kaniitia jambo jingine kuhusu nini...binadamu unaweza kuwaza mambo mengi kwa sekunde chache tu.


' Kiukweli, mimi nimefurahishwa na utendaji wako wa kazi, hata kwenye vikao vyetu, huwa tunakupongeza sana...'akaanza kusema hivyo.


Hapo moyoni kidogo nikaanza kuingiwa na tumaini jema,..nikajua labda natakiwa kuongezwa mshahara, japokuwa katika hiyo kampuni kuongezwa mshahara haijawahi kutokea.


Jingine lilinitia mashaka kidogo, niliona bosi kama anakwepa kuniangalia machoni...sio kawaida yake , yeye huwa akikuita ofisini kwake akianza kuongea na wewe anahakikisha anakuangalia moja kwa moja machoni.


'Nashukuru bosi...'niliposema hivyo, akainua uso sasa kunitizama machoni.


'Lakini kwa hali ya kampuni, nashindwa hata kuelezea, hata wewe mwenyewe umeiona au sio, kama tumefikia hatua hatuwezi kulipana mshahara kwa wakati...eeh,...na hata tukilipana twalipana nusu.mishahara, ni jambo mimi sipendi kabisa..'Hapoi nikahisi moyo ukinienda mbio.


'Wewe ni mmoja wa wafanyakazi tunaowalipa vizuri, na nilipenda niendelee kufanya hivyo...ndio kwanini nisikulipe hivyo wakati, elimu yako inaruhusu, achilia mbali utendaji wako...'akasema


'Ahsante bosi najitahidi tu..bado, sijafanya kile ninachokitaka...'nikasema


'Inatosha,..umefanya vyema tu...'akasema hivyo, halafu kama vile hataki niongee zaidi akasema


'Kiukweli, umekuwa ukinipa moyo,..uliyoyafanya ni makubwa sana...ndio maana nilipowaza,..eeh kutokana na hali ya kampuni ilivyo ngumu, niliona labda niwapunguze mshahara, ili tuweze kumudu hali halisi...kwako wewe niliona sio sahihi...'akatulia


'Kutokana na hali halisi ilivyo, ...hili nimeamua mwenyewe, usije kusema ni ushawishi wa mtu,...mimi nimeona tukupatie nafasi, ili utafute kazi sehem nyingine...'hapo akaangalia pembeni.


'Bosi mbona sijakuelewa...'nikasema


'Kiukweli sina uwezo wa kuendelea kukulipa, ...nimejitahidi kila mwezi, hata kukopa huku na kule, lakini uwezo wangu umefika mwisho...na naanzia kwako, pengine hata nikiona naweza kufunga kampuni....'akasema


'Oh...bos lakini...nilikuwa na matatizo...ndio nilitaka nikuelezee...'nikasema


'Matatizo ...hasa yanayohusu pesa, sitayaweza tena, mimi nakuomba ufanya jambo moja..muda wa mwezi huu, jitahidi kutafuta sehemu nyingine ukipata, basi...lakini baada ya mwezi huu,...sitaweza kukulipa tena mshahara...'akasema


Hapo, nikanywea,...akili ikaganda...nguvu zote zikaisha...kila nikitaka kumuangalia huyo bosi nashindwa, macho yameshakuwa mazito...


'Ndio zaidi ya hayo, ningeliomba uanze kumzowesha yule mwenzako kazi zake...najua utapata kazi sehemu nyingine wewe ni mchapa kazi mnzuri sana..na ukipata mimi mwenyewe nitakudhamini, maana nakufahamu sana...'akasema sasa akiweka mambo yake vyema mezani kuwa niondoke.


Taratibu nikasimama, na kuanza kutoka, sasa mwili hauna nguvu, akili ikaenda mbali,...watoto shule tena basi, nilijaribu kuwatoa kwenye shule za awali walizokuwa wakisoma ili wasome kwenye shule za kulipia, angalau wawe japo sio sana na watoto wa mabosi,…sasa haitawezekana tena.. na itakuwaje, kwa yule muuza duka, asiponiona leo, familia yanagu inaweza kuwa hatarini, na nikimuendea, kwa hasira alizo nao anaweza kunikata kichwa,…lakini la zaidi ...mtoto anaumwa anataka matibabu nifanyaje.


Niliwaza hivyo hata sijui nilifikaje mezani kwangu, ...nilipofika nikainamisha kichwa, nikawaza, na kuwazua, sijui ilikuwaje, chozi likanitoka, ...sijui chozi la nini, na sijui namlilia nani sasa mie mtoto wa kiume,..kiukweli lilikuwa chozi lenye hisia kali....'CHOZI KUTOKA MOYONI..


'NB: hiki ni kisa kifupi cha rafiki yangu, kanitumia,..kwa yaliyomkuta....nashindwa kukiendeleza kwa hivi sasa maana na mimi nipo kwenye mitihani hiyo ya maisha…ila kwa faraja nimeona nikitume siku isipite bure.


WAZO LA LEO: Baada ya dhiki huja faraja, baada ya magumu fulani mwisho wake huja mafanikio, je inapotokea umefanya jitihada zote, umepitia ,magumu mengi sana, na inafika muda wa kutegemea faraja, bahati mbaya, ikaja kutokea machungu utafanyaje...

‘litakutoka chozi …’ 
Ni mimi: emu-three