Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, October 5, 2018

NGUMI MKONONI-athari za ulimi



NGUMI MKONONI-athari za ulimi.


'Jamani watauana hao watu, mbona mpo watu wazima hapa mnawaachia watu hao, wanapigana na kuumizana hivyo, waamulieni jamani...'ilikuwa sauti ya mwanamama.

Ni nani atamsikiliza, watu ndio wanainua simu zao juu kuchukua picha za video, na wengine wanashangalia…..ni ajabu kabisa dunia ya leo.

Kwa muda ule, mmoja alishatoa ndutu kichwani, kavimba…na mwingine jicho limevimba, na bado kila mmoja ana hasira na mwingine….

’nitakuua, nitakumaliza…’linafuta tusi, ndio lugha iliyosikika kutoka kwa vinywa vya mabondia hao wasio na kibali, ..ni wakubwa, yawezekana miaka thelathini hivi.

Akatokea askari mmmoja kupita eneo hilo..ndio ikawa salama, wapiganaji hao, wakaachana utafikiri refa kawaambia ‘stop’…sasa damu zinawavuja…wamevimba hoi bin taabani..

‘Ehee, endeleeni sasa…’akawatania mmoja wa wapambe waliokuwa pembeni na simu yake mkononi.

Yule mtu wa usalama akafika, na kuuliza ni nini kinachoendelea hapo…, watu kimia wengine haoo, wanaondoka mdogo mdogo, na bahati nzuri yule mtu wa usalama akawaona  hao wanandondi  wawili wakijaribu kujiweka sawa, lakini mwili haujifichi , ushahidi upo, utamficha nani hapo;
.
'Haya nyie wawili, tuambieni, kisa cha  nini cha kuumiza dhamana ya mungu aliyowapa, hamjui huo mwili ni dhamana kwenu, hapa duniani ni dhamana kwa jamuhuri, na huko kwa mungu, mtakuja kuulizwa, kwanini mliuumiza huo mwili uliopewa kama dhamana,...'akasema mtu wa usalama, jamaa kimia.

'Haya mumeumizana mumepata faida gani, nikawafunge  sasa hivi, nina mamlaka hayo, nifanye kazi yangu eeh, niambieni sasa mnapigania nini....?' akauliza yule mtu wa usalama ,, wanandondi wale wakawa wanajitetea

 'Hivi mwili ni dhamana kwa jamuhuri...'akasema jamaa aliyekuwa nyuma yangu, na mwingine akasema

'Wewe hujui hilo, ...jinyonge upone uone utafanywa nini...'akasema huyo mwingine..huku watu wakianza kutawanyika , kuendelea na shughuli zao. Na wengine wakiogopa ushahidi…ndio maisha yetu hayo…

 Nilisikia wale jamaa wakiendelea kuhojiwa..
.
'Huyu jamaa kazoea kunitukana, matusi mabaya, leo sikukubali, nimetaka kumfundisha adabu...'akasema mmojawapo.

'Wewe je..hujanitukana mimi. ..na pia umezoea kunidokolea bidhaa zangu za sokoni, ndio tabia yako hiyo mwizi mkubwa wewe…’akasema

‘Wewe umeniona ni kikuibia, ..wewe ni hisia zako tu…wivu tu, maana kila mara mimi nauza wewe huuzi,…’akasema mwingine

‘Kakutukana kasema nini…?’ akaulizwa

‘Yeye, kila kauli unayotoa ni tusi, tena ananitukania mzazi wangu, mama yangu...'akasema mwingine.

'Mimi sijamtukana mama yake nimemtukana yeye mwenyewe, kwasababu kazoea kuniibia , yeye ndio tabia yake hiyo chafu, kazoea,…wizi…’akasema mwingine.

Ilionekana ni jaziba za ujana, lakini kweli matusi yalitoka, kila mmoja alitumia ulimi wake akatoa matusi, kauli chafu, na mbaya zaidi matusi yalielekezwa kwa wazazi, wazazi ambao hata hapo hawapo, wazazi wanatukanwa , wazazi waliwafanya wawepo hapo, leo hii wana minguvu, wanawatukana wazazi wao...si laana hii .

‘Hivi nyie watu mnafahamu athari za kutumia ndimi zeni vibaya,..na shetani anapenda sana kupitia njia hiyo, keshajua madhaifiu yenu yapo huko kwenye ndimi zenu…na kwanini muwatukane wazazi waliowazaa, wakawalea..?' wakauliza wakabakia kimia

'Haya niambieni, ni….nani mshindi, au bado hamjamalizana,.. tuwaachie mpigane tena, haya piganeni…’akasema huyo mtu wa usalama....jamaa wakawa wamenywea nahisi muda huo ndio wanaanza kuhisi maumivu.

Mimi sikuwa na muda wa kujua hatima yao, akilini mwangu, nikawa najiuliza tu;

‘Iweje watu watukanane, na ni nani wanamtukana hapo, kama mtu anamtukana mzazi wa mwenzie ina maana gani hapo, sio kajitukania mzazi wake pia....haya sasa matusi yamezaa ugomvi, ugomvi umefikia kupigana, ni nini athari za kupigana, kuumizana,..kuna faidi gani wameipata hapo, je tusi linaweza kumgeuza mtu akawa hilo tusi..mimi hapo sijui…?’ nikajiuliza tu..

'Kumbe ni ‘ulimi…kumbe ni mtihani wa ndimi zetu..' nikajikuta nimesema hivyo kwa sauti.

Ulimi umekuwa ni mtihani kwetu, na kutokana na ulimi, wengi wetu, tutaingia motoni, tusipopata muda wa kutubia, kabla mlango wa toba haujafungwa…na nikizungumzia ulimi , sio ulimi tu…ni pamoja utumiaji wa  ‘kalamu’ ..na kalamu hapa nina maana ya matumizi yote ya kuandika, …hasa huku mtandaoni, kwenye simu zetu..hapa..tuna kesi kubwa ya kujibu mbele ya mungu.

Enyi mliopewa nafasi hiyo ya kutumia ulimi, kutumia kalamu,…kwenye mitandao , simu , tv, redio nk…tuweni makini sana kwa kile tunachokiandika, au kuongea, wengine wanaandika ‘matusi’ kabisa kama wanavyoyatamka kwenye ndimi zao, wengine imekuwa ni biashara, ukipata wanachama wengi, unapata ingizo, wengine ndio hao wanatunga hadithi za mambo yanayoathiri hisia za vijana,..

Ni nani anajiuliza athari za kuhamasisha ‘ngono’…watu wanajiandikia tu…huishii kwa hao wanaosoma leo, watakuja kusoma wajukuu zako, watoto wako, je hao waliosoma , wakahamasika, kufanya hayo maasi kutokana na hisia ulizowajengea,..hujui kisa ni wewe, je hujui kuwa wewe ndio umewalogeza 'uasherati'..na yote ni kutokana na kalamu yako…ndugu yangu unayefanya hivyo, una kesi ya kujibu…

Ukumbuke jambo moja,…..ushahidi wa kuandika haufutiki, unachoandika leo mtandaoni hakitafutika miele…usijidanganye kuwa utafuta kwenye simu yako, kwenye komputa yako, nk..hayo hayafutiki kama yameshaenda hewani. Ni halikadhalika, ulichoongea leo na ulimi wako, ukazua ghadhabu, ugomvi,...nk...hakifutiki, ulimi utakuja kukielezea mbele ya mungu, na kama watu waliumizana, mwili utatoa ushaidi, kisa ni nani,..je uliwahi kuliwazia hilo kwa mapana yake

Ndugu yangu…andika jambo la hekima ili iwe sadaka yako ya baadae, ..

 ‘Ulimi..’, sasa umekuwa ni tatizo. Hatujui jinsi gani ya kuuchunga ‘ulimi wetu..’ tukikaa wawili ni kutetana tu,..achilia mbali hayo matusi,…kusengenya imekuwa ni donda ndugu..unajua kusengenya ni sawa na kumla mtu nyama yake….sijui kama tunalifahamu hilo...umekula nyama za watu wangapi...

 Haya labda ndio huko kutafuta ‘kiki..’, sawa utapata wafuasi wengi, na wengine ni biashara kwasasa, lakini ukumbuke ulichoandika atakuja kuulizwa nacho..na wapo waliondika zamani sasa ni viongozi, wamekuja kuonyeshwa walichoandika kipindi hicho, imekua ni aibu kwao..sasa hayo ni ya hapa duniani, je huko mbele ahera ambapo kila la siri litawekwa wazi, kila ulilofanya ukiwa umejifungia chumbani, litabainika,...kila mtu ataliona,..yabidi tulie sana kwenye toba...

 Tunaambiwa na watu wa imani, haya  ya ulimi, hayaishii hapa hapa duniani,Ulimi utakuwa ndio shahidi, siku hiyo ya kiama, kila kiungo kitatoa ushahidi wake, kwa jinsi nafsi yako ilivyokituma,…huna cha kukwepa hapo,..ulimi utasema ulichoongea kwa kupitia wewe, mkono, macho, na kila kiungo chako…ni siku ngumu sana jamani,.

 Labda kwa wale watakaojiwa na imani wakatubia, wakapata muda huo wa kutubu madhambi yao, lakini sasa muda huo tunao, na kama tuliwatukana wazazi wa wenzetu, na ndio tabia yetu, tutawezaje kutubia hilo, maana toba ya kweli hapo ni uende kwa kila mzazi uliyemtukana umuombe msamaha..tutaweza hilo.

Yawezekana kabisa matatizo tuliyo nayo , mitihani tuliyo nayo ya maisha, na mabalaa mengi yanatokana na ndimi zetu, hulka na tabia zetu, hatujaweza kujichuja ,  tunachukulia kila jambo kwa jaziba,…kila jambo tunakimbilia kulalamika tu…kulaumu tu, mwisho tunachukiana, tunanyonyosheana vidole,...tunashikana mashati, tunaumizana…kila mtu anawaona, je hayo tunayoyafanya kwa siri tukijifanya hatuonekani, usiku tunawanga, hayo yote yatakuja kubainika siku hiyo ya hukumu…tutakuja kusema nini.

Ndugu yangu,  toba ya kweli ndio dawa ya maradhi haya ya ulimi..tutubu na tuache kabisa madhambi hayo…, na toba nyingine ni kukithirisha kutenda mema, mambo mema hufuta maovu yetu,…

Tumuombe mwenyezimungu atusaidie maana haya sasa ni zaidi ya uwezo wetu, bila neema yake yule aliyetuumba,  tutaangamia, ulimi, kalamu, mitandao..itatuangamiza,..leo twapigana makonde, kesho yaweza kuwa silaha…wengine walianza hivyo, hivyo… kikao kidogo ngumi, uchaguzi mdogo ngumi, …kidogo kidogo, uchaguzi mkubwa je…

Tumuombe mungu atuepushie hayo na chuki zilizojaa mafundoni mwetu ziyeyuke na kuwa upendo na amani…

Ila kwa wazo la leo, tukumbuke jambo moja tu…
.
'Maovu, hufutwa kwa wema, , tutende wema tufute maovu yetu..tutende wema, tuwezeshe wenye maovu, waone aibu ya kuendelea kutenda maovu yao, ili na wao waje kutenda mema,.., na tusizidishe maovu kwa kupigana na kuumizana, tutazidi kuifukuza Baraka, na neema.

 Hilo ndilo Wazo la leo, nawatakia ijumaa njema.


Ni mimi: emu-three

No comments :