MUDA HAUSUBIRI MTU..
Leo nilikuwa na miadi ya
kwenda,kulipa ada za watoto benki, nikadamuka kama kawaida yangu, alfajir na mapema nikijua nitakuwa wa kwanza
nimalize shughuli zangu niwahi kibaruani…ni Kariakoo tu hapo..nafika benki,
maandishi,…kazi kuanzia saa mbili na nusu…nilishasahau tena, nikijua sasa ni
mwendo wa viwanda, kazi masaa 24…
‘Utaratibu mzee, uje saa mbili na nusu….’akasema mlinzi,
nikaangalia saa saa kumi na mbili na nusu…nikageuka kuondoka, hakuna jinsi..
Ni kweli kwa utaratibu wa benki ao maofis mengi ya serikalini au
hata makampuni ya watu binafsi, ukitaka huduma ni kuanzia saa mbili…tena saa
mbili na nusu ndio wanafungua na kupata huduma labda kuanzia saa tatu…kwa wale
wenzangu na mimi.
Nilijutia kupoteza muda
wangu, labda ningelipitia kazini kwangu kwanza,…lakini nisingeliweza kufika
kazini na kutoka, kutokana na utaratibu wa kazi zangu,..na hata ukipanga ratiba
kuwa ufike kazini, uombe saa moja la kutoka haitawezekana, kwa shida za usafir,
wa Dar, na foleni hasa asubuhi…kwa ujumla kwa jiji letu hili,, huwezi kupanga
ratiba ya wapi utakuwa kwa muda gani.
'Sasa nifanye nini,..?’
nikajiuliza, sasa nikiona muda unakwenda taratibu, tofauti na nilivyokuwa
kwenye daladala, niliona gari linanichelewesha…kumbe nilikuwa nawahi buree.
Basi, kuliko kukaa bure, nikaona nifurahishe macho, nikatembelea
sehemu nilizokuwa nikipendelea kufika, ya kwanza, nikaona nipitie msikiti mmoja unaitwa ‘Kwa mtoro’ kama ulifika
enzi hizo ukawa mgeni wa Dar, ukirudi sasa hivi unaweza kupotea…, sasa msikiti
huu umezungukwa na magorofa, marefu kuliko msikiti wenyewe …watu wanataka
kufika mbinguni kwa majengo, sio kwa imani…maendeleo haya.
Akilini nikakumbuka miaka ya elifu mbili mbili hivi… haikuwa
hivi. Nikakumbuka enzi hizo nafika kununua cassette za dini, nikiwa na redio
yangu unayoweza kucheza hizo cassette…nilipenda sana kununua caste na
alimuruhumu Nassoro Bachu.
Kiukweli kwa Dar.., kuna mabadiliko makubwa ya kimajengo, na
nilijaribu kuwatafuta wafanyabiashara niliokuwa nikiwafahamu, wengine
walishahama,..hawapo tena, na niliowakuta niliwatambua kwa sura, lakini
kichwani bati jeupe limeshaezekwa, sura zile za ujana hazipo tena….umri
haumsubiri mtu.
Maisha na umri havimngoji mtu hata siku moja… Nashangaa sisi
bado mambo mengi ni ya kusubiria, ukiwa na shughuli za kibenki au serikalini
kwenye ofisi zao,..hata makapuni ya watu binafsi, usubirie saa mbili na
kuendelea…ndio taratibu zetu..KUSUBIRI.
Kwa maana hiyo hata kama mimi ninashida, au ni msafiri, basi,
siwezi kuipata huduma hiyo kama nilitarajia kuipata siku hiyo, na ukiwa mtu wa
ofisini,..uwe umeshaomba ruhusu jana yake la sivyo, kwa wenzetu, wasio na
simile, siku imekatwa…na usemi juu, mshika mawili, moja hufanya nini vile...
Je kwa hali hii, tutaweza kukimbizana na muda kweli,…kama
wanavyofanya wenzetu. Wenzetu sasa hivi, hata ule muda wa dakika moja ya kusalimiana
hawana. Mkikutana mkiwa huko makwao, ni mwendo wa Hai,hai…kila mtu mbio-mbio,
anawahi kazini au kwenye majukumu fulani, kila kitu kimeshakadiriwa muda wake…wanaweza
kwasababu hata usafiri wao sio wa huku kwetu…wa KUSUBIRIA…wa FOLENI.
Hata hivyo sisi wenyewe swala la muda bado sio ajenda muhimu
kwetu, tunaweza kupoteza siku nzima kwa ajili ya kikao cha harusi..mnasubiriana
na hata kikao kikianza, porojo nyingi, nje ya ajenda kuu na wakati mwingine kikao
kinaweza kuchukua mambo mengine ambayo sio ajenda kuu, na muda huo hauna hauna
marejesho…
‘Ni upendo wa kifamilia,ndivyo tunavyoona hivyo…. Ndio maana
tunaweza kusalimiana nusu saa nzima
ukikutana na rafiki yako zilipendwa, ni nini mnaongea, utesi, na yaliyopita,
ambayo hayarudi tena, na ole wako ujifanye una haraka, utaambiwa unaringa…lakini cha ajabu mtu huyu mwambia
aingie nyumba ya ibada nusu saa tu ataiona nyingi…ataondoka na kusema yupo
bize,…yupo bize kwa maswala ya kumshukuru yule aliyempa dhamana hiyo ya muda..,
Haya… achilia mbali masaa kadhaa tunayoyapoteza vijiweni,
ushabiki wa mpira na,mambo ya kisiasa, ndio hapo mtu hakumbuki muda, muda haumtoshi,….
Leo waitwa kijana, kesho baba, au kwa msemo wao dingi, au dadi, usishangae
ukitwa babu...babu wakiwa na maana umeshapitwa na wakati, haupo kwenye wakati
wa ujana, kwenye kuvaa, kimuonekano, na
sura…
Mbona hatujiuliza hili,
hivi umri umekwenda wapi, je umekwenda na nini, kwa faida au hasara,..tukumbuke
jambo moja, umri huu, nijuavyo mimi ni dhamana kwetu, aliyetupatia huo umri, atakuja
kutuulizia, tuliufanyia nini, tuulifanya nini,… achilia mbali tu,…huko kuja
kuwajibika uzeeni, wakati tukitwa babuuu….
Haya ngoja nisubiria hiyo saa mbili na nusu, wenye mamlaka ya
ajira, wenye nafasi za kuamua, ni muda gani tuanze kazi, ..ndio maisha huenda
hata mimi ningelikuwepo hapo ningalifanya hivyo,
Ni wazo tu la leo…ndani ya diary yangu.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment