Hata sijui ni kwanini...
Mimi sikuweza kumuamini huyu mtu wa jamii, kuwa
ataweza kunisaidia kwenye hili janga, kwangu mimi, sana sana niliona yeye anataka kutumia hili tukio, ili
aweza kukamilisha utafiti wake tu..na hii kesi inahitajia pesa, inahitajia
wakili mwenye ujuzi mkubwa,...mimi sina pesa, rafiki yangu halidhalika, na cha
ajabu rafiki yangu kaenda kuniletea mtu ambaye, hana pesa., ...sio wakili
kisheria,
‘Huyu mtu atanisaidia nini mimi..’
nilijikuta nawaza na kusema hivyo kwa sauti ndogo.
Tulibakia wawili , mimi na mtu wa jamii, yeye
akaniuliza maswali machache, muda wa kuongea na wageni ulishakwisha, yeye akaondoka akisema anataka kuonana na mkuu wa
hicho kituo, sijui waliongea nini....
Siku hiyo ikapita sikuchukuliwa
kwenda Ukonga, niliona ajabu sana...,na hakuna aliyekuja kuniambia ni
kwanini..lakini nilijua ni swala la muda, nitachukuliwa tu..
Kisa kinaendelea.....
**************
Kesho yake akaja shemeji, macho
yamemuiva, na nilibahatika kuyaona hayo macho yake baada ya yeye kuvua miwani, aliyokuwa
amevaa, nahisi aliivaa hiyo miwani kwa makusudi ya kuficha hayo macho yake, ni
dhahiri kuwa anavuta bangi, japokuwa yeye, halikubali hilo.
'Shem, kwanini unaniuza..'akaanza
kuniambia hivyo, hata bila ya salamu.
'Kwa vipi shem...?'nikamuuliza,
nilishamzoea, maana kila tukikutana, mimi na yeye, tunaishia kwenye ugomvi tu,
jamaa huyu ananichukia sana, ila kama dada yake yupo, jamaa huyu anajifanya kuwa ni muungwana kwangu.
'Mimi nimejitolea muhanga kukusaidia
wewe, ...unajua ni nini nilichokifanya, imeniuma sana, kukusaidia wewe na haki
ya dada yangu ipotee....’akatikisa kichwa.
‘Unaja nikuambie ukweli, tukio hili ilikuwa ndio wakati mnzuri wa kukumaliza
kabisa...ulichokifanya, hakistahiki kusamehewa,..unahitajika kunyongwa,..lakini
kwa upumbavu wangu, nikaogopa....niliogopa, nitaambiwa nimechukua sheria
mikononi mwangu, na mimi sitaki kuingia kwenye mikono ya polisi...ndio hivyo
tu...sasa wewe umeharibu..’akasema
‘Mimi nimeharibu kwa vipi shemu...?’
nikamuuliza
‘Wewe unawatangazia watu kuwa mimi ndiye niliyekupiga kichwa....kweli si
kweli...?’ akaniuliza sasa akinikazia macho, awali nilikuwa nikimuogopa sana
huyu jamaa, lakini ikafikia mahali nikaanza kumzoea,..kwahiyo hapo sikujali,
nikamkabili, japokuwa siwezi kupambana naye kimabavu.
'Nimemtangaza nani kuhusu hilo, wewe
usiwe unasikiliza majungu watu,..ilivyo, hata taarifa ya polisi inasema dada
yako ndiye aliniumiza...’nikasema, na jamaa akabenua mdomo kwa dharau.
'Sikiliza, najua wewe na mimi
hatuivani kabisa..., na ukiona mimi nimefanya jambo la kukusaidia, ujue kuna gharama,
na gharama yake ni kubwa sana...,’akasema na nilikuwa nalisubiria hilo.
'Natakiwa nikulipe shilingi ngapi..hata
hivyo ukumbuke mimi ni shemeji yako....’nikasema
'Mjinga mkubwa wewe, wewe moyoni
mwangu sio shemeji yangu, kabisa kabisa..., natamka hilo unielewe, na najua
unanielewa hivyo...mengine ninafanya kwa heshima ya dada yangu...’akatulia
akikunja uso , niliona kama ana sikitika.
‘Mimi niliapa sitakutambua wewe kama shemeji yangu,
kamwe,..nitafanya hivyo tu, pale dada akiwepo, kumridhisha yeye...sasa wewe
unataka gharama si ndio hivyo,...haya, je nikikuambia nataka nyumba yako
utasemaje..’akasema akitizama miwani yake aliyokuwa kashikilia mkononi.
'Shemeji, huko unapokwendsanaa ni mbali...’nikasema
nikihis mwili ukinicheza cheza..nilijua tu, huyu jamaa kalenga jambo.
'Mimi eeh, nimekwenda mbali sio..,
najua utakuwa mgumu kwa hilo......sasa kipi bora, nyumba yako ipigwe mnada kwa
ajili ya milion chache ulizokopa au...nichukue mimi hiyo nyumba, halafu
nipambane na huyo anayekudai,...na dada angelikuwepo, ningewachia muishi,humo,
lakini kwa vile...’hapo akatulia.
'Siwezi kufanya ujinga huo, unajua
thamani ya ile nyumba,...hahaha, eti ipigwe mnada, kwa deni gani hilo,....hata
hivyo, mimi nitamlipa huyo jamaa pesa yake...’nikasema
'Hahaha, wewe mpuuzi, kweli kweli,
sitamani hata kukuita shemeji, hebu niambie kwa hali yako, wewe utapatia wapi hizo
pesa, kapuku kama wewe , dada yangu
mjinga kweli kweli, sijui alipumbazika na nini kukubali wewe uwe mke wake,..’akakohoa
Mfululizo, nahisi mate yalimkoholeza.
‘Dada kuolewa na masikini kama wewe
ni kosa kubwa sana... wewe hujui tu, ...wakati nyie mumeishiwa kabisa, mimi
ndiye nilikuwa nawalisha, sikutaka dada yangu akuambie hilo ila leo nimekuambia
ili uelewe kosa ulilolifanya...kiukweli mimi nampenda sana dada yangu, na
sikutaka apate shida...’akatulia kidogo
‘Lakini sio kweli, angeliniambia ...’nikajitetea
‘Hivi wewe hukuwa unaona ajabu,
ukirudi nyumbani unakuta chakula kipo,
wakati hujaacha hata senti moja, ulifikiri mke angelikula wapi, wakati hukutaka
hata aende sokoni, eeh...usitake niseme mengi..’akasema hivyo
Kiukweli, kipindi nimekwamba kabisa,
kuna wakati nikrudi nyumbani nikiwa sijaacha chochote, bado nakuta chakula,
...na kila nikitaka kufunua mdomo kumuuliza mke wangu najikuta nashikwa na
kigugumizi,ungesema nini tena, huna kitu, nilijua ni jitahada za mke za hapa na
pale, ...sikufikia kumdahani mke wangu vibaya...ila nilishafikia wakati, nilitaka nimuulize...bahati
mbaya ndio yakatokea haya ya kutokea.
‘Sasa shemu, nilitumai wewe umewahi
kuja hapa jela, kwa nia ya kunisaidia
mimi nitoke hapa, hapa sio sehemu nzuri, na natakiwa kufuatilia maswala
ya...ooh, hata sijui kinachoendelea,..sasa wewe kumbe umekuja kuniongezea maumivu tu, huo ndio
ubinadamu gani shemu,?’ nikauliza.
‘Hahaha, mimi nije kukusaidia
wewe,...kama ningelipewa nafasi, ya kukufanya chochote,mimi ningekukata kata
vipande niwe nameza nyama yako..na kuitema, mimi nakuchukia, unajua kuchukia,
we acha tu, lakini siku zinahesabika ..utakuja kuona ..’akasema kwa sauti ya
kibabe.
‘Lakini kosa langu ni....’ kabla
sijamaliza, akaendelea kusema;
‘Na nikuambie ukweli... kama
ingelifaa, mimi ninataka wewe wakufunge ufie huko huko jela,..hapo ndio moyo
wangu utatulia, lakini kwanza, kabla hujaenda kuzimu..nataka unilipe..na malipo
yangu, kama nilivyokuambia, ...’akatulia.
‘Kuwa ....’nikataka kuongea
anakiniashiria kwa mkono ninyamaze kwanza
Nimeshakuambia...nataka nyumba , hilo
sikutanii...mimi nitakuja na hati ya makubaliano, ..la sivyo, jamaa mwenye deni
atakuja kwako...unamjua alivyo...na ukumbuke yeye anajua mengi kukuhusu
wewe...si niliwahi kukugusia,...anakujua fika, kuwa wewe ni muuaji, ..lakini
nilikudhamini mimi...’akasema.
‘Sasa kwanini wewe ulinidhamini...?’nikauliza
sasa kwa mashaka, maana niliona kweli huyu mtu alinitega.
‘Hahaha, bwege mkubwa
wewe..nilishakuambia, mimi siwezi kukufanya jambo kwako lenye manufaaa na wewe...,
maana wewe ni nani kwangu, muuaji mkubwa wewe, usitake ni badilike hapa, ..’akanisogelea,
nilijua kichwa kinakuja nikakwepa hewa.
‘Hahaha, unakwepa nini sasa, mimi sio
mjinga,... hapa siwezi kukufanya hivyo, ila ujue jambo moja, wewe na mimi, ni
kama mafuta na maji, eeh, na ,...utajuta kuzaliwa kwa ulichomfanyia dada
eeh...sijaanza malipizo yake bado...’akasonya.
‘Lakini ..eeh ili twende sawa, niume
na kupiliza...fanya nilivyokuambia,...na unaweza kuona utanivunga, au utasita
kukubaliana na mimi...kwanza ukumbuke, mimi ndiye nilitoa kauli ya
kukusaidia,..lakini ile ni kauli tata,....bado haina mshiko, kuwa, nilisema
hivyo, kuwa dada yangu alikupiga,..hiyo haina mshiko saana, ...’akawa ananichoma
choma ni kidole kifuani.
‘Mimi naweza kuitengua hiyo kauli wakati
wowote..kumbuka jela kulivyo...eeh, uliponea tundu la sindani, unakumbuka,
eeh...sasa kule ni cha mtoto, huko..Ukonga, kule wapo jamaa zangu wengi tu,
tunajuana...usijali kwa vipi..., nilishawatipu, ukikanyaga tu pale Ukonga, wewe
ni chakula chao, utashindwa hata kutembea..hahaha...’akasimama na kuanza kuondoka.
Nilibakia nimeduwaa...maana nimjuavyo
huyu jamaa hana utani, akisema jambo, hatanii....nitafanya nini sasa, dada yake
wa kunitetea ndio hivyo hayupo,..jamaa aliponiona nimeduwaa, akarudi na kuanza
kunipiga piga begani kwa ngumi kama kunipa moyo, lakini upigaji wake unahsi maumivu...nikawa najaribu kuukwepa huo mkono.
‘Sikiliza hii ni dili, hati
inakuja,..tena sio kesho leo...na jiulize ni kwanini hadi sasa hujapelekwa
Ukonga, eeh...jibu unalo, si ndio hivyo, mimi natoka hapa, nakwenda kwa
mwanasheria wangu, keshaikamilisha hiyo hati,..nikirudi tutaelewana, ..’akahema
kidogo.
‘Shemu,....’nikataka kusema neon,
jamaa akanitolea macho,...halafu akasema;
‘Hata hivyo, wewe una thamani
gani..ulitakiwe ufe...nyumba ile ni yangu kwa hivi sasa,..na mimi nitamlipa
huyo anayekudai, unasikia, mengine niachie mimi...natumaii umenielewa, mimi
sitaki longo longo...unanijua nilivyo..’akaanza kuondoka.
Kabla hajafika mlangoni, mlangoo ukagongwa,
jamaa akavaa miwani yake kwa haraka, mlango ukafunguliwa, mtu wa jamii
akaingia, nyuma yake yupo mtu wa dini. Nilifahamu huyo ni mtu wa dini kutokana
na mavazi yake, ..moyoni nikasema, huyu mtu wa jamii hana la kunisaidia, yeye
kaenda kunileta huyo mtu wa dini ili
aniombee..kuombewa kwa hivi sasa kutasaidia nini kwa hali kama hii.
‘Hapa ninakabiliwa na kesi ya
mauaji...na huyu shemu sasa hivi tu, kaniletea janga jingine, anataka nyumba
iwe yake kitapeli,..nitafanyaje sasa...nyumba ndio mali yangu pekee ya
kujivunia, kiukweli ni nyumba nzuri, na niliijenga kwa gharama kubwa sana...’nikawa
nawaza hivyo.
Shemu akasita kuondoka akawa
kasimama, na mtu wa jamii, akamsalimia ..lakini shemu hakuitikia hiyo salamu,
jamaa akawa kama kashikilia mlango, lakini akawa kasimama tu.
‘Nimekuja, ..kuanza kazi, ..na..huyu
ni mtu wa dini, kuna mambo nataka atusaidie,..nikuulize jambo moja,.’akasema
mtu wa jamii, kwanza akageuka kumuangalia shemu, shemu akajifanya kama anataka
kufungua mlango, lakini hakufanya hivyo kwa haraka.
‘Umeshapata taarifa yoyote, ya kuhusu
mkeo, ..je kuna taratibu zozote, maana nijuavyo mimi , nilivyosikia,..mwili
wake umehifadhiwa, sehemu ambayo haitakiwi kuonekana...’akasema mtu wa jamii.
‘Mwili wake una maana gani kusema
hivyo...?’ nikauliza sasa kwa mashaka, ujue kukweli kuna hisia mbili akilini
mwangu, kuna hisia ambayo, bado inatamani kuwa mke wangu bado yupo hai,
nyingine inahisi kuwa mimi nimemuua mke wangu.
‘Ina maana huna taarifa hizo, au...?’
akasema mtu wa jamii, sasa na yeye akionyesha wasiwasi Fulani hivi.
Sasa sauti ikatokea mlangoni...
‘Una unakika na unachokisema wewe, ni
nani wewe kwanza, wa kumuongelea dada yangu, eeh..mwili, mwili, .....?’ ilkuwa
sauti nzito ya shemu, na sasa alikuwa anakuja kukabiliana na mtu wa jamii, sote
tukabakia kushangaa, tukawa
tunamuangalia tu..nilitaka kumuambia mtu wa jamii awe makini, maana huyo jamaa
kichwa kinamtoka kama mshale..
WAZO LA LEO: Tuweni makini na mikataba
tunayoandikishana, hasa ya madeni,na ikiwa ni lazima kuandikishana hivyo,
tuhakikishe tumepata ushauri wa mawakili, kabla hatujaweka sahihi zetu,..kwani
sio kile anayekuchekea, ana furaha na wewe.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment