‘Chuma ulete...!..’nikang’aka. Na
msimuliaji wa hiki kisa akatabasamu japo uso ulionekana na huzuni, na alikaa
kimia kwa muda.
‘Una maana gani au ndio hizo
imani za watu kuwa,...’ nikamuuliza pale nilipoaana yupo kimia.
'Ndio,...chuma ulete... ndivyo alivyoniambia hivyo mke
wangu, mke ambaye awali hakupenda kabisa imani hizo za kishirikina,...uchawi
tuseme...kiukweli nilishangaa kidogo, kwani awali hakuwa akiamini mambo
hayo..'akasema, na kutulia kidogo
'Nikajaribu kumuasa mke wangu kihekima na kiimani, unajua
tena...eeh...kuwa uchawi upo sikatai, lakini ukimuamini mungu, ukamuomba yeye,
bila kuweka nafsi ya shiriki, huwezi kushindwa jambo..’akasema.
‘Na nikaendelea kumuasa...’
''Mke wangu, tusiamini sana hayo mambo maana ukiyaamini sana
hayo mambo, mwisho wake utaingia kwenye shirki, na imani yetu haitaki hivyo, ...nikamwambia
mke wangu’’.
Awali alijifanya kunielewa, lakini mambo hayakuendelea
hivyo....’msimuliaji akaendelea kuongea, na alipofika hapo alitulia kidogo.
'Kwa vipi...kwani kulitokea nini tena zaidi...'nikauliza
sasa nikiwa na shauku zaidi.
'Sikuacha kumnasihi, mke wangu, nikijua kuwa mimi ndio mume
wake, na mimi ndiye kichwa cha familia, unasikia
sana...’akasema.
‘Sawa kabisa...’
‘Lakini..eeh, ndugu yangu wee, kumlea mtu mnzima ni kazi sana..ni mpaka yeye mwenyewe akubaliane na wewe...moyoni nikadhamiria kutumia nguvu japo kidogo.., mimi najua
wengi watanilaumu sana kwa hilo, unajua ni kwanini nilitaka kufanya hivyo, kwa akili yangu, niliona bila hivyo, hataweza kuachana na ushetani huo...sumu ya ushetani, ilishapenyezwa kwenye ubongo wake,..’akatulia.
‘Sijakuelewa...’nikasema.
‘Yule mke niliyemuamini...ambaye nilikuwa namuasa jambo, ananisikia
kwa unyenyekevu. Yule mke mpole, mwelekevu, hakuwa yeye tena, najuta kwanini
nilimpatia nafasi hiyo ya kujichanganya...nahisi tamaa za nafsi na ushawishi wa
mashoga, vilishamteka nafsi yake...’hapo akahema kwa nguvu.
‘Ndugu yangu makosa yaliendelea kujirudia, kidogo kidogo,akawa
sasa haambiliki,hata kauli zake zikawa za kijeuri jeuri hivi, japo sio kwa moja
kwa moja...kila hatua akawa ananipandisha presha...'akaendelea.
Niliumia sana..ilifika mahali naanza kukata tamaa,
nilimpenda sana mke wangu, sikupenda abadilike, sikupenda, nije nianze kutumia
nguvu, maana naogopa...naogopa sana kupiga,...naogopa sana, najijua nilivyo,
nikianza..sirudi nyuma, nina hasira za mbali lakini zikipanda, ooh, ndugu yangu...sitaki
kuua tena...’akasema na kushtuka, nahisi hakupenda kutamka hivyo.
‘Kuua tena, ina maana uliwahi kuua...?’ nikauliza kwa
mshangao.
‘We acha tu, hayo yalishapita....samahani kwa hilo, limetoka
tu..sija-jawahi..ku-kua bwana...’akasema sasa kwa kusita sita.
***********
Kisa kikaendelea....
Haikupita muda, hali ikaanza kubadilika, maisha yakaanza
kuwa magumu, biashara haziendi , pesa haikamatiki...sikufichi,...kuna wakati
imani ikaanza kushuka, maana unaambiwa mengi,..wanakushauri wengi..fikiria
kutoka maduka hadi...genge la nyanya mbili tatu, na...ikawa mbaya zaidi ya hapo,
hata ingelikuwa ni wewe....ila, hata
hivyo, sikufikia hatua ya ...kuamini maneno ya mke wangu...’akatulia kama
anawaza jambo.
‘Maneno gani...?’ nikauliza kama sijui.
'Umasikini ni mtihani ndugu yangu, ...tatizo sasa ikawa
kwa mwenzangu yeye anaendelea kudai
matumizi tu, hata pale ninapomwambia sina kitu na wakati mwingine anafikia hata
kunikasirikia,..na kuanza kutoa maneno ya kashfa...sikupenda hilo....maana
alivuka mpaka...’akaendelea bila kujali swali langu.
'Mke wangu hali unaiona, na mitihani hii ni kawaida kwenye
familia, awali ulikuwa unavumilia nakueleza kitu unanielewa,... hivi nimekosea
nini mke wangu, kosa langu mimi ni kukupatia uhuru, au...?’ nikamuuliza.
‘Hapana mume wangu, nahisi kosa ni la kwangu
mimi....kukuambia ukweli...’akasema
‘Ukweli upi...?’ nikamuuliza.
‘Aaah..sitaki tena kuongea...maana wewe ndio mume...nitasema
nini tena mbele yako, nina nini tena mtoto yatima,...wewe ndio baba, wewe ndio
mama yangu...’akasema.
‘Nahitajia ushauri wenye tija, sio imani haba na mambo ya
kuambiwa..’nikasema.
‘Nikushauri nini tena mume wangu, ushauri wangu
nilishakuambia,..kwanza nilikuambia tujiunga na michezo ya kupeana, hukukubali,
..na..na hali hii ambayo nimeshaiona, wewe hutaki kuniamini..mume wangu tatizo
lipo humu ndani...’akaniambia na kabla sijamkatisha akaniambia
‘Najua unanidharau, kwa vile ni mwanamke,..sio
vibaya,...lakini ..mmh,...mimi kuna
mambo nayaona, ila wewe hutaki kuniamini....utakuja kunikumbuka kwa hili...’akasema
kwa sauti ya unyonge.
‘Una maana gani...?’ nikauliza sasa nikimuangalia kwa
mashaka mashaka.
‘Mume wangu, u-meingiliwa na chuma ulete...fanya haraka
kabla hali haijawa mbaya...’akasema sasa akishika kichwa na kuangalia huku na
huku kama ana wasiwasi ...na ile hali ya kukuna kuna kichwa, kama kinamuwasha
ikanipa mashaka.
‘Nini.....’nikang’aka hivyo, nikimuangalia kwa kumkagua
akijikuna kuna kichwani.
Kiukweli hadi hapo mimi nilishaamini, mke wangu sio mwaminifu
tena...nilimuona kama anajifanyiza tu, kunivunga mimi.
Unakumbuka
nilivyokuambia awali, huko nilipomtoa mke wangu, sifa yake kubwa ni uaminifu...hadi
hapo niliona ni uwongo, labda ...walinidanganya...... awali ilikuwa hivyo sio
sasa..na hebu niambie, hata kama ingelikuwa ni wewe..ungefanya nini hapo, maana
sio mara moja, au mbili...imekuwa ni kawaida,..’akasema akiniangalia mimi
usoni.
Hapo sikuwa na jibu la kumuambia, nikasubiria aendelee...
**********
Unajua tena, katika kuishi na watu unaweza ukawa na
marafiki, na kati ya hao, ikatokea mmoja au hata wawili ukawaamini, japo mimi
nina hulka yangu, sio rahisi kumuamini mtu,...hasa kwenye maswala ya imani,
msimamo wangu ni thabiti.....kuna rafiki yangu mmoja, muungwana, ana busara
sana, siku moja nikaongea naye nikitaka ushauri kwake.
‘Ndugu yangu kabla hujaanza kuingia huko, kwenye hasira,
mkaja kukosana wewe na mke wako, hebu fanya uchunguzi wako wa kina..yawezekana tatizo lipo humo humo ndani,
au...majirani,..siwezi kukupinga, au kupinga mawazo ya mkeo, maana hayo mambo
yapo....’akanishauri.
‘Yawezekana tatizo lipo humo humo ndani kwa vipi...?’
nikauliza hivyo.
‘Yaani...yawezekana...ila...uchunguzi kwanza, usiwe na papara...’akasema.
‘Unajua ndugu yangu, mimi nimefanya kila uchunguzi, sijawahi
kuona dalili ya kumshuku mtu baki, na nikuambie ukweli nyumbani kwangu watu
hawaingii mara kwa mara, wananiogopa...’nikasema.
‘Sawa....lakini ...’nikamkatisha.
‘Ninasema hivyo kwasababu..mke wangu nilishamkanya,..sitaki
majirani waingie ndani, mimi naafahamu sana majirani wangu...kwahiyo, kama ni
kukutana na hao watu watakuwa wanakutana huko huko nje hasa hao mashoga , waliomuharibu akili yake...mimi
sina mfanyakazi wa ndani au ndugu ninayeishi naye, ni mimi na mke wangu tu...’nikasema.
‘Kwahiyo shaka yako kubwa ..ni kwa mke wako..si ndio hivyo..?’
akaniuliza.
‘Siwezi mshuku mtu wa nje..sijui unanielewa hapo...shuku
itakwendaje nje kwanza, eeh... pesa ipotee humo humo ndani...na nipo mimi na
mke wangu, nitamshukuje mtu wa nje kwa vipi, mlango haujavunjwa,...sijui
unanielewa hapo....’nikasema kumuamboa huyo rafiki yangu.
‘Basi...vuta subira..ngoja nilifanyie hilo kazi rafiki yangu..’akaniambia
huyo rafiki yangu. Kwa pale, sikuelewa, atalifanyiaje kazi, hata hivyo sikutaka
kumdadisi, nikaachana naye...maana akili ilikuwa na mikakati mingine ya
kibiashara.
***********
Siku moja nikarudi
nyumbani mapema....nilikuwa na pesa nimekopa mahali..., kwa ajili yakuanzisha
biashara tena.., niliona nianze mtindo huo wa kukopa na kurejesha, labda
nitafanikiwa, japo nianze kidogo kidogo.
Nilishapanga bajeti yangu vyema, iliyobaki ni kununua vifaa
na kuingia sokoni,..kiukweli nilishapanga nitoke, kihivyo, ...na ndoto nyingi za
Alinicha ziliuteka ubongo wangu, si unajua tena, ukikwama, na ukaja kuzishika
pesa, ...mmh, akili inakuwa na mengi sana.
Pamoja na shauku ya
biashara,...bado mwili ulikuwa hauna
nguvu, sijui kwanini siku ile ilikuwa hivyo, na hali ile..ilinianza pale
nilipozishika hizo pesa, nahisi hivyo.....maana hata kula sasa kulikuwa kwa
shida, mawazo mengi kupitiliza.
Nikafika nyumbani...sikumkuta mke wangu, nikajua katoka
kidogo, nikavua koti langu, nikatundika kwenye kabati la nguo...sikuwa na
shaka, kwenye lile koti ndio niliweka pesa, nikajilaza kitandani...sijui
usingizi ulitoka wapi, ...mwili ukalegea,...sijui nielezeje, nikashikwa na
usinginzi mnzito ajabu,...nashtuka nasikia mke wangu anaongea nje...anaagana na
mtu.
‘Kwaheri ...’
‘Kwaheri...’
Mimi kwa haraka nikashtuka
nikikumbuka natakiwa kwenda kununua bidhaa muda umeshapita, hata sijui kama
nitakuta maduka ya jumla yapo wazi..sikukata tamaa, na sikupenda nilale na hizo
pesa ndani, nikiogopa hayo yanayoendelea, hapo ilishafika jioni kama saa kumi
na moja hivi.
Nikachukua koti langu,..nikavaa, wakati navaa, mke wangu akaingia, aliponiona akashtuka, na
kusema;
‘Oh, la azizi wangu umerudi mapema leo....,vipi kuna tatizo,
sikujua kaam upo humu ndani.. kumbuka kauli hiyo,...’
‘Ndio mke wangu,...ume-rudi saa ngapi...?’ nikauliza, na
kbla hajanijibu nikasikia mtu anagonga mlango.
‘Ni nani tena, kwanza sikiliza ,maana nimechelewa, nataka
kutoka, nikirudi tutaongea vizuri..’nikasema,
Mke wangu akatulia akinisikiliza huku mtu anayegonga mlango
anaendelea.
‘Sasa sikiliza....chukua pesa hii ufanye fanye mambo, japo
ni pesa ya kukopa, lakini aheri, ntoe kidogo, tule chakula kizuri leo japo kidogo...au
sio mke wangu’nikasema sasa naingiza mkono mfukoni kutoa pesa,..mkono
ukazunguka kwenye mfuko wa koti...moyo ukaanza kunienda mbio, siamini.....
WAZO LA LEO: Tusiwe
na tabia ya kuzania dhana mbaya, kabla hatujafanya uchunguzi wa kutosha,..dhana
mbaya, hupunguza imani moyoni.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment