Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, February 8, 2010

Tutafakari

 Ulishawahi kufika Muhimbili, jana nilifika huko kumwangalia ndugu yangu, Umati nilioukuta pale Muhimbili utadhani Dar nzima ilihamia hapo, kila mmoja alikuwa na shauku saa ifike akamuangalie mgonjwa wake. Mara tukasikia sauti ya adhana, nikaangalia huko na huku kama nitawaona angalau robo ya waliopo hapo watainuka kwenda kuitikia wito wa adhana hiyo, lakini sikuona mtu, nikadhani huenda wengi wa waliopo hapo ni wa imani ya dini nyingine.


Eneo kama hili ni sehemu ambayo kiimani inamkurubisha mtu na mola wake kwani hapa ni kitovu cha matibabu ni eneo ambalo utaona ugonjwa wa kila namna, na kweli kila mara tuliona magari ya wagonjwa ya kutoka sehemu nyingine za hospitali yakipita kuonyesha kuwa kuna wagonjwa walioshindikana walikuwa wakiletwa hapo. Lakini mbona vitendo na hisisa hiyo haviendani, kwasababu mtu akitoka eneo hilo keshasahau kuwa leo au kesho anaweza naye akawa miongoni mwa wanaoletwa hapo kuhudumia, basi muda wa ibada ukifika inuka haraka ukamuombe mola wako, ili akuepushie na kila lenye kuepukika na awajalie wagonjwa wetu wapone!

Wakati nimefika kwenye nyumba ya ibada,tukiwa tunasubiri muda nikagundua kuwa kuna mtu ananitazama sana, kiasi kwamba hata nikigeuka kumtizama habandui macho kuniangalia mimi. Ikafika hatua nikaanza kuogopa , na hapa nikakumbuka hadithi ya babu yangu ambaye hakuchoka kutupa hadithi za kutufanya tuwe karibu ni mola, tuwe na imani thabiti. Kisa hicho kilikuwa cha jamaa mmoja ambaye pamoja na kupewa utajiri wa mali pia alijaliwa kuwa tabibu, na aliweza pia kutabiri na kujua nini kitafuata baadaye. Pia aliweza kutafsiri ndoto na kila akiota ndoto zake huwa kweli..

Kwasababu ya utajiri wake alikuwa na walinzi ambao walikuwa wakimlinda , kwani ukiwa tajiri na maadui huwa wengi. Walinzi hawa wakati anafanya ibada huwa wanakuwa pembeni mwake na nje wanakuwepo wengine. Kwa ujumla hakuna adui aliyeweza kumsogelea, alikuwa kama mfalme. Pamoja utajiri wake hakuacha kufanya ibada.

Siku moja jamaa huyu akiwa kwenye ibada akamuona mtu asiye mtambua, mtu huyu mgeni kwake muda wote alikuwa akimtazama na hakubandua macho kwake kiasi kwamba kilimpa uwoga huyu tajiri, akawaangalia walinzi wake na kuwaona wapo karibu naye akapunguza uwoga.Hamu ya kutaka kuinuka ili aende kumuuliza huyu jamaa kulikoni ikamjia na kabla hajafanya hivyo ghafla akashikwa na kitu kama kausingizi, na kupoteza fahamu kwa muda.

Wakati akiwa nje ya fahamu zake alimuona Yule jamaa akiinuka na kumjia , na alipomkaraibia alimwambia, `ndugu yangu mimi ndiye yule mgeni asiyependeka, lakini ni wajibu wangu kumtembelea kila mtu siku yake ikifika. Sasa nakuomba kwa vile wewe ni mja mwema, na muda wako haujafika nikupe taarifa kuwa baada ya nusu saa nitarudi kwako kuchukua ile dhamana ya mola wako aliyokukabidhi, na mara fahamu zikamrejea kabla hajaambiwa mengi.

Hebu fikiria mtu kama wewe upewe taarifa kama hiyo ungefanya nini. Lazima ungeshikwa na kihoro na huenda ungekimbila kufanya lile la mwisho ambalo ulikuwa hujalifanya kama ungekuwa na moyo huo. Mola ni mjuzi wa yote na katika kitu ambacho alitupa ni mtihani wa umauti. Kama kila mtu angejua siku yake ya kufa sijui dunia ingelikuwaje. Na labda tungekuwa tunapewa muda wa kutafakari kwa waja wema wangeutumia kutubia na kurejesha madeni ya watu kama yapo, hata kuandika usia lakini wapi, hiyo ni siri ya Manani.

Basi jamaa Yule alipozindukana cha kwanza nikuwaangalia walinzi wake, ambao walishahisi hali isiyo ya kawaida ya bosi wao, wakamuuliza vipi yupo safi. Akawajibu kwa sauti ya kukwaruza kuwa yupo safi na macho yake yakaangalia kwa Yule jamaa, na akakuta bado yupo pale nab ado kamtizama kama kwanza. Akawauliza walinzi wake kuwa Yule jamaa anayemuangalia aliwahi kuinuka pale alipokaa, na walinzi wake wakashangaa, kwani hakuna hata mtu mmoja aliyesogea pale walipokuwepo kwa muda wote huo.

Yule jamaa akaanza kuogopa, akainuka na kuelekea chooni, huko akatafakari kuwa ile ni ndoto au nikweli, na tafsiri yake ya haraka ni kuwa muda wake wa kuishi hapa duniani umeisha. Hili halikukaa kichwani, hakukubalina nalo moja kwa moja. Akaona arudi awaambia walinzi wake wamkamate Yule mtu, alipofika pale Yule jamaa akawa bado anamumuangalia kwa mtindo ule ule, lakini akaogopa kuwaamrisha walinzi wake wafanye kile alichotaka. Aliinuka na harakaharaka akatoka kupitia mlango wa chooni, nia yake ni kukimbia ili amkwepe Yule jamaa kama ndiye mtoa roho.

Alipofika nje, akawa anamtafuta dereva wake na alipoangalia saa yake akaona imebaki dakika mbili tu, na alichofanya ni kukimbilia gari lake alilokuwa amaligesha upande mwingine wa barabara. Katika kuvuka barabara kwa pupa hakuangalia vyema upande mwingine mwa barabara, kumbe kuna gari lililokuwa likija kasi likamzoa juu, juu na laipotua chini, akawa kapoteza fahamu na hali yake ilikuwa mbaya kabisa. Mara kwa mbali akamuona Yule jamaa akitoka nje ya ule msikiti akawa anamjia. Alijaribu kupiga kelele ili walinzi wake waje wamuokoe lakini wapi.

Jamaa akamjia na kumwambia, `hivi wewe hukunielewa, sasa muda umefika, na watakaonisaidia kuichukua dhamana na watu ni walinzi wako..’ Jamaa akashangaa, na kujitahidi kupapatika, na kweli waliokuwa wamemshika vizuri walikuwa walinzi wake, wao walikuwa wakijaribu kumsaidia ili asijiumize zaidi, kumbe wanamsaidia jamaa mtoa roho amalize kazi yake, na muda ulipofika akawa ameaga dunia!

Naombeni tutafakari, hasa tuliojaliwa, tunapopata mali isiwe ndio kuwa tumefika, tukumbuke kuwa yupo mfalme wa wafamle ambaye katukabidhi dhamana yake, ipo siku atafika popote na kuichukua dhamana yake. Ni vyema tukazitumia mali zetu vyema ili ziwe msaada wa baadaye. Hili ni kwa kila mtu kuwa, ugonjwa ni moja ya mitihani ya kutukumbusha kuwa sie hapa duniani ni wapiti njia tu, yupo mwenye milki yake na ndiye wakutegemewa.



From miram3

No comments :