Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, August 28, 2009

MFADHAIKO

Katika shida hii ya usafiri, ambayo wakati mweingine hukulazimisha kusimama kwamguu mmoja (mithili ya hadithi za shetani tunazozisikia kuwa anasimama kwa mguu mmoja), unakutana ni vituko vya ajabu ambavyo huwezi kuamini kuwa vipo. Ambavyo vingi unavisoma kwenye magazeti au mitandaoni na kuishia kusema `hizo ni hadithi tu’ lakini lisemwalo lipo, na ukikukutana nalo, ndipo unapoweza kuamini!
Jioni ya siku ile ilikuwa na foleni kubwa ajabu,licha ya foleni watu tulibananishwa kama magunia ya mchanga. Kila kwenye mataa ilibidi tukae zaidi ya saa,kiasi kwamba wale wenye mioyo dhaifu walianza kumuota iziraili. Nami angalau nilikuwa kwenye kiupenyo karibu na dirisha, ingawaje nilisimama na kujifanya nachukua zoezi la kusimama na mguu chamoto nilikiona.
Ukiwa katika hali kama hii mawazo hukurudisha nyuma nakuwaza wenzako watakuwa wapi saa hizi, wengine watakuwa kwenye viti virefu, wengine wanalea na wengine wanaangalia runinga, lakini sio wa Gongo la mbali bado tulikuwa tunaota ndoto za lini nitafika nyumbani.
Katika hali isiyo ya kawaida macho yangu yalimuangalia dada mmoja, kibonge, kweli alikuwa na mvuto, kimaumbile na hata kisura, lakini kilichowavutia wengi ni ile nguo aliyovaa, ilikuwa kama ya hariri na laini,kiasi kwamba maumbile ya ndani ungeweza kuyachora bila kugandamizia.
Mwanadada yule naye kama wengine alikuwa ameminywa katikati ya watu wa aina tofauti, hamna aliyejali kuwa huyu ni dada,mama au kaka, kilammoja alikuwa akiinua kichwa juu kutafuta hewa kama samaki wafanyavyo baharini, au kwenye maji. Haya ndio maisha mazuri kwa kila Mtanzania,kama hupendi nenda kakodi taksi.
Jicho bwana halina pazia na ajabu ya jicho,likiona kitu kibaya, ndio linataka lione zaidi, hivi kweli yaleni `mavi’ ashakumsi matusi lakini ndio mfano wa maana. Jicho langu likaona na moyo ukalipuka kamavile umeshikwana shoti ya Umeme. Sikuamini kile nilichokiona. Lahaula, huyu kweli ni binadamu, lahaula , lahaula.
`Jamani, jamani , umanifanya nini jamani..’kilio cha ajabu kilitanda ndani ya gari,na hapo vichwa vilivyoangalia juu kwa shinda viliinama kutafuta kulikoni. Na mara kishindo cha kusukamana kilijongea upande ule niliopo. Jamaa njema lilikuwa limekwidwa kisawasawa, na sio kukwidwa shingoni,lahasha, lilikuwa limekamatwa sehemu nyeti huko jicho limemtoka kwa machungu na aibu.
`Jamani nini kulikoni..’ watu wengi waliuliza. Mmmh,kile nilichokiona kwa macho kimetoka hadharani, nami ndipo nikaamini kuwanikweli, kwani mwanzoni nilidhani ni ndoto hutaamini hata mimi niliona aibu kama vile nimehusika. Alituabisha jamaa, nilisema na kauli hiyo ilipokewa na wengi. Jamaa ametuaibisha.
`Kwanini umenifanya hivi, kwanini umenichafua, wewe mnyama, mkubwa, nitaikata hii ndude yako..’ alikuwa yule mrembo akilalama huku kamshikilia jamaa, ambaye alihangaika kujitoa kimasomaso’,lakini ilikuwa kazi bure kwasababu ya kule kubanana!
Huu ni mfadhaiko, na jamaa alipobanwa alisema ukweli na kukiri kuwa kutokana na msongamano,na hali ya yule dada alivyovaa, na ulaini wa mwili na akaongezea kusema na vile hajawahi kukutana na mwanamke sasa ni mwaka wa tano uzalendo ulimshinda, akafanya alichokifanya. Alipata raha gani hatujui, lakini ilikuwa zinga la soo!
From miram3.com

Thursday, August 27, 2009

SHIDA YA USAFIRI NA FOLENI DAR

Leo tarehe 27-08-2009, niliona niitoe kero yangu katika tovuti ya http://www.wananchi.go.tz/
Tunawashukuru sana kwa kutoa Tovuti hii, na nivyema wananchi tukaitumia vyema kwa kutoa kero zetu, kutoa maoni au pongezi. Nami kwa kuanzia ningependa kutoa dukuduku langu kuhusiana na tatizo la usafiri hasa kwa wakazi wale tunaishi nje ya mji kama vile Majohe,Kipunguni nk, ambapo hakuna magari ya moja kwa moja kuelekea sehemu kama vile Msasani, Kawe, au Kunduchi nk ,na fikiria unatakiwa ufike ofisini saa mbili, bila hivyo kazi huna.

Maoni yangu ni kuwa kuna haja ya wahusika wa usafiri kuruhusu magari ya kutoka maeneo kama hayo ya moja kwa moja kwa kutoa nauli yenye unafuu, kuliko hili la kupanda magari mawili au matatu na mojawapo unalipa nauli ya masafwa marefu(sh 450/-). Na hii ina mana kuwa kwa siku unatakiwa kulipia nauli si chini ya sh 1400/- kama umebahatisha kupanda magari mawili, lakini mara nyingi haiwi hivyo kwasababu inakubidi ulipie nauli ya kugeuza nalo,ili angalau upate kiti au uweze kuingia ndani ya gari bila kudandia (Huwa asubuhi au jioni kama hujui kudandia huwezi kuingia ndani, magari haya hayasimami kituoni kwa kukwepa wanafunzi.) kwahiyo kutumia nauli zaidi ya sh 1900/-kwasiku.
Kero hii inatukwaza sana sisi watu wa maeneo haya kwasababu, sio tu kwa swala la nauli, lakini pia inatubidi tuamuke saa kumi za alifajiri kila siku ya kazi , ili kukwepa foleni ambayo huanzia saa kumi na mbili, na hutaamini kama utakutana nahii foleni unaweza ukatumia zaidi ya masaa matatu kutoka Msasani hadi Gongolamboto bado hujatafuta usafiri wa kwenda Majohe au Kipinguni unapoishi. Kwa minajili hii familia yako unaiacha ikiwa imelalana huenda ukarudi ukaikuta imeshalala pia.
Kwa maoni yangu kuhusiana na tatizo la foleni ndefu, kama inawezekana ni kuanzisha barabara za moja kwa moja, yaani magari yakienda yasirudie njia ileile, nafikiri inawezekana kwasababu zipo njia za mkato kutoka Gongolamboto hadi Ubungo, au Gongolamboto hadi Mbagala, na ndani kwa ndani zipo barabara za mikato ambazo tumeyaona magari ya daladala yakipitia kukwepa foleni, hizi zote zikiwekwa vizuri itapunguza foleni kwa kiasi kikubwa. Na kama inawezekana usafiri wa treni kwa maeneo haya ungefaa pia!
Na pia wakati mataa hayafanyi kazi,matrafiki hutumia muda mrefu kuita sehemu moja tu, sijui hufanya hivi kwasababu gani,kwanini wasitumie `stop-watch’ ili kutowaumiza abiria ambao hujazwa ndani ya daladala kama magunia. Nimeshuhudia abiria wakizimia ndani ya magari haya kwasababu ya kusimama muda mrefu na kukosa hewa!
Natumai wahusika wanalifanyia kazi tatizo hili,lakini ni sie waathirika inabidi tutoe sauti zetu ili mjue kweli tunaumia, kwani tusiposema mtajuaje shida zetu

Ahsanteni na poleni sana kwa majukumu haya mazito.
NB. mfadhaiko nilioushuhudia ndani ya daladala nitautoa kesho Mungu akipenda.

From miram3.com

Wednesday, August 26, 2009

MAWAZO YANGU

HAYA NI MAWAZO YANGU, JE WEWE
Wakati napita katikati ya mji, nilimkuta mama mmoja mwenye matatizo ya Akili, mama huyu alikuwa na mtoto wake pembeni. Nilishangaa kidogo,kwani mama huyu ana matatizo haya kwa siku nyingi. Nilijiuliza ilikuwaje akapata huu ujauzito. Kwa hisia za harakaharaka nilikisia kuwa huenda jamaa walimbaka.
Hapa mawazo yangu yalinikumbusha jamaa mmoja aliyekuwa na matatizo kama hayo maeneo ya Kariakoo, huyu alikuwa mwanaume, na akimuona mwanamke aliyempenda hutaka kumshika kwa nguvu, kwahiyo wanawake wanapomuona hukimbia.
Wenzetu hawa wapo dunia ya aina yao, kwani wakati mwingine utawakuta wanaongea, wanaimba, wanacheza na hata kufanya mambo ya ajabu-ajabu ambayo wakiwa na Akili zao wasingediriki kufanya vitendo hivyo. Haya ni matatizo na ni ugonjwa ambao huenda ukapona au usipone kutegemeana na kiini chake.
Kuna wale waliozaliwa na tatizo hilo,au tatizo limetokana na kurithi,lakini kuna wale waliopata matatizo haya kutokana na maisha kwa ujumla. Kuna waliopata kwasababu walidhulumu, wapo waliopata balaa hili kwa kuwatendea wazazi wao isivyotakiwa. Na wapo waliopata matatizo haya kwa kutendewa na binadamu wenzao, na hapa nikajiuliza kwa vipi binadamu aamue kumtesa mwenzake na kumzalilisha kiasi hiki.
Wakati natafakari hivi nikawakumbuka wavuta unga, na waathirika na madawa ya kulevya,ambao hawana tofauti sana na hawa wenye matatizo ya akili,ingawaje hawa wa madawa wanaweza wakajizuia na hubadilika tu pale wanapobwia hayo madawa au kujidunga hayo madawa.
Tarehe ya leo 26-08-2009, nikaona niliweke hili hapa nikijaribu kutafuta mawazo kwa wenzangu kuwa kwanini kizazi chetu kinateketea na madawa haya. Na tufanyeje ili tusipate wagonjwa wa akili wa kujitakia. Huenda tukabuni njia mbadala, mfano kuanzisha kijiji cha vijana ambao wameshaingia katika kundi hili. Kijiji hiki kikawa kama sehemu ya mafunzo, wawepo wataalamu wa kuwahudumia kisaikolojia, wawepo wataalamu wa kazi mbalimbali ili kuvumbua vipaji vyao walivyonavyo. Nafikiri kwa kufanya hivyo tutakuwa tumeliokoa taifa na kuyaokoa maisha ya hawa ambao wameanza au wameshatumbukia katika balaahili.
Haya ni mawazo yangu tu,kwa leo.
From miram3.com

Monday, August 24, 2009

MGENI WETU MTUKUFU

Ramadhani mosi (22-08-2009)
Muumini aliwaita wanae kwenye chumba cha siri, na mara nyingi akiwaita kwenye chumba hiki anakuwa na habari muhimu yakuwaeleza,
`Natumai nyote mumeshamuona mgeni wetu mtukufu ambaye tumekuwa tukimsubiri kwahamu, natumai nyote mnafahamu nini cha kumkirimu mgeni wetu huyu,natumai kwa ajili ya aliyotuletea nyote mnahitaji awakilishe makisio mema ya utendaji wetu bora, na kufaulu kwema, kwa kusamehewa kila ovu tulilofanya ,ili kwa fadhila hizo tuweze kurehemewa na kusamehewa mbele ya mola wetu.
`Hivyo basi kwa kukumbushana mgeni wetu hataki kukirimiwa kwa chakula mchana,si chakula tu ila kila kinachoweza kupenya kwenye matundu yetu yanayojulikana, na sio tu kila kinachoweza kupenya kwenye matundu hayo bali pia tunatakiwa tusiseme yale yasiyofaa, tusisengenye mbele yake, tupendane, tusaidiane nk. Na hivyo basi sisi wenyeji wake kama alivyotuusia muumba wetu tunatakiwa tuwe mfano kwake, kama hali nasi hatutakiwi kula,kama hanywi na sie hatutakiwi kunywa na kila ambalo halitaki mgeni wetu kwa muda wamchana basi na nasisi pia tuwe mfano kwake’
Muumini aliwatizama watoto wake ili kujua kuwa wameelewa au la, alipoona kimya kingi akajua kuwa ama wameelewa au hawajui kabisa nini anachowaeleza. Akachukua moja ya boksi aliloleta mgeni. Akalifungua na kutoa zawadi ambayo ilingara kama dhahabu, ikiwa imepambwa na rangi za kila namna juu yake.

Kila mmoja mle ndani aliwaza kivyake, huenda ile zawadi ni alimisi, dhahabu,lulu, pesa au kila kizuri ambacho mwanadamu anachokipenda,angependa akipate . Mhhh, zawadi jamani zawadi, zawadi gani hiyo.

`Hii ndio zawadi aliyotuletea mgeni wetu, zawadi hii inatakiwa tuitumia kila mara, zawadi hii inaelekeza jinsi gani ya kuishi na mageni wetu, leo akiwepo na hata kiondoka, jinsi gani ya kuishi sisi wenyewe na jinsi gani tufanye, kama walivyofanya waliopita, na inatuongoza ili tuifikie ile njia iliyonyooka kwa kutenda mema na kukatazana mabaya, zawadi hii tunayo kila siku,lakini kila muda kama huu huzidi thamani yake. Na muda kama huu ndio wakati wakujipima,kuomba na kutubu na ni-nini ulichofanya na je afanyeje zaidi ili apate kurehemewa, na kupata msamaha wa mola wako’’

Zawadi hii nawakabidhi ili pakipambuzuka mbele ya mgeni wetu tuanze kuifanyia kazi zawadi yetu kwa vitendo.

Pale watoto wakatabasamu na kila mmoja akaipokea ile zawadi akiwa na hamu ya kujua nini kilichomo ndani yake na je ataifanyia nini zawadi hiyo ambayo thamani yake imezidi zawadi zote unazoweza kuzifikiria duniani.
Ni nani asiye mjua huyu mgeni wetu,?

Ni nani asiyejua zawadi aliyotuletea huyu mgeni wetu?, Kama hutujui basi sisi sio watoto wa `muumini’
Na huyu muumini ni nani kwetu?
Tuendelee kutafakari !!!
From miram3.com

Friday, August 21, 2009

VITENDO NI BORA KULIKO MANENO

Katika utendaji wa kazi kuna sehemu mbili, kufanya kazi na kazi ijieleze yenyewe, au kufanyakazi na wewe uielezee ile kazi, ama kwa mkubwa wako au kwa jamii. Hii sehemu ya pili wengi ndipo walipo, mtu hawezi kufanya kitu bila kujisifia, bila kujitangaza, bila kujionyesha kuwa ndiye aliyefanya au anajua, na wengi wa watu hawa wapo kwenye siasa.
Mimi sio mwanasiasa,ila ninaikumbuka hadithi ya babu yangu kuhusu milki moja ya majigambo. Mkuu wa nchi ile alikuwa na washauri wake wawili, hawa walikuwa wakipewa kazi mara kwa mara za kufuatilia mambo ya utendaji na mwisho wa siku huleta taarifa.
Watendaji wake wawili hawa walikuwa wajuzi kila mmoja kwa nafasi yake. Mpole alikuwa akifuatilia na kufanya kazi yake kimya kimya, na mwisho wa siku hupeleka taarifa na kumkabidhi bosi wake,ama kwa kupitia katibu muhtasi wa bosi au wakati mwingine kupitia kwa mwenzake ambaye alikuwa Chakaram kwani Chakaramu anajua kuielezea kazi kama alikuwepo.
Chakaramu alikuwa mjanja, yeye huitumia nafasi ya wengine kufanya kazi yake na kwa uchakaramu wake aliweza kupeleka taarifa nyingi kwa bosi wake kuliko Mpole,kwahiyo bosi wake alikuwa akimtumia sana katika kupata taarifa. Watu kama hawa ndio wamejaa maofisni kibao, maneno mengi, lugha utafikiri kazaliwa huko,lakini…ok ngoja tuendelee.
Likatokea lakutokea,kuna mtu kauliwa, na taarifa zikafika kwa bosi, Chakaram na Mpole wakambiwa wafuatilie, Mpole kama kawaida yake akaifanya ile kazi kwa umakini zaidi akijua ule ni uhai wa mtu na kugundua ukweli,na ukweli huo ulimuumiza sana na akaona ni heri aufiche kwanza ili kwanza awe na uhakika nao. Kwa minajili hiyo akajenga hoja ya kuwa huenda aliyekufa alijiua mwenyewe. Na hii akainasa Chakaramu, akaitenhenezea hoja yenye ushahidi kabambe mwisho wa siku akaipeleka kwa bosi wake.
Bosi wake akaisikiliza,na ushahidi alioletewa, kiasi kwamba aliridhika, na kumsifia sana jamaa, kimoyoni akasema duu jamaa huyu ni mkali, huyu ndiye ananifaauyu ninayemuamini kaniletea ushahidi huu basi sina wasiwasi,jamaa atakuwa kajiua.
Bosi akataka kujua kutoka kwa mshauri wake Mpole. Mople alipofika,kama kawaida yake,akafika kwa katibu muhutasi na kumwambia kuwakesi hiyo ina utata, na anahitaji muda wa kuifanyia kazi. Kitendo hiki kilimuudhi bosi,kwasababu muda ulishatolewa na kwanini mwenzake aweze kuleta matokea yeye ashindwe. Jamaa akafukuzwa kazi.
Licha ya kufukuzwa kazi alifilisiwa na akawa katika maisha magumu. Hatimaye siku ya mwisho aliyoomba apewe kutoa taarifa yake ilifika. Aliomba siku hiyo wawepo wazee wa baraza, na hakimu wa-nchi.
`Ndugu Mheshimiwa, nilisita sana kutoa taarifa yangu kwasababu mdomo kutamka ni rahisi,lakini kile unachokitamka sio rahisi kujielezea,lakini kama utaacha kile ulichokitamka kijielezee ni bora zaidi, hakuna haja hata ya kuinua mdomo. Bosi najua unajua muuaji ni nani, labda tumiite shahidi yangu wa kwanza ambaye ni Mheshimiwa mkeo. …’’ Watu pale wakashangaa,iweje. Na mke wa raisi inasadikiwa kapotea kimijiuza.
Ni kesi ndefu kidogo, nitaielezea kwa undani baadaye. Lakini alichotaka kunieleza babu yangu ni kuwa wakati wote, hakikisha kazi na majukumu yako uliyopewa unayatenda kwa vitendo na ukiyatenda ipasavyo yatajieleza yenyewe, usipende mara kwa mara kutumia mdomo kuielezea kazi yako,iache kazi ijielezee yenyewe, akiwa na maana kuwa vitendo huwakilisha ukweli kuliko maneno. Huu ni ujumbe wangu wa leo tarehe 21-08-2009 Je w ewe mwenzangu wasemaje?
From miram3.com

Thursday, August 20, 2009

MUJIBU WA SHERIA

Nimesikia kuwa enzi ya `mujibu wa sheria’ zinarudi tena, enzi hizo, ukibahatika kumaliza vidato au chuo ulitakiwa kulitumikia taifa kwa kwenda kwanza `kuhenya’ miezi sita na miezi sita ya mwisho kutoa huduma ndani ya JKT. Wengi waliobahatika wana hadithi nyingi kuhusiana na uwanja huu wa mujibu wa sheria.Nani anazikumbuka?
Narejea miaka ile ya 80’s mimi nilibahatika kutimiza sheria hii kule Mafinga na enzi hizo alikuwepo CO mmoja, mkali kwelikweli-Mlai. Huyu alikuwa akisimama smart-area akasema `heyii’ si kuruta, si green kwanja, kuku au..’ wote wanapotolea popote penye kujificha. Alikuwa akiogopewa kama jitu fulani kubwa, au kitu cha kutisha unachoweza kukifananisha nacho, hutaamini ukikutana naye, ni mfupi, mdogomdogo tu na mcheshi, lakini akiwa kazini popote pale yeye alikuwa kama simba aliyejeruhiwa. Walikuwepo afande `nusu-mungu’ alinyofolewa pete zake kwa ukali wake, yeye wakati anatukaribisha tuliambiwa kuwa yeye huanza kwa kusoma barua toka kwa mama yake ikimlalamikia kuwa awamu iliopita aliua kuruta wawili tu, hii imemvunja nguvu sana mama yake, na kama safari hii hataongeza mara kumi zaidi yake atamuachia laana.
Vituko vya JKT ni vingi na maelezo yake ni mengi na mengine huaanzia pale unapopewa taarifa kuwa unaenda kujiunga, wengi wanakuambia kuwa huko maji utayasikia kwenye bomba, kiasi kwamba chawa ni rafiki yako, wanajaa kwenye bukuta yako au kwenye `green vest yako ya njano’, na ili uwaue inabidi uiweke kwenye jiwe kubwa halafu uchukue jiwe jingine uanze kuwagonga-gonga,kwani ni wengi ajabu na ole wako uonekane ukiwaua, hairuhusiwi kwani ni sehemu yako, kuwaua ni makosa.
Nakumbuka siku tupo makao makuu ya JKT tunasubiri `bogi’ lakutupeleka kambini, tuliambiwa ukifika uwanja wa maeneo ya mafunzo, mizigo yako unatakiwa uruke nayo kichura, mfano kama umbali wa kutoka ulipopokelewa ni maili kadha basi wewe utaruka na mizigo yako, au utakimbia nayo hadi eneo lako la kufikia. Na mengi mengineyo, kama vile muda wa kula ni mchache na unapewa uji wamoto sana unawekewa kwenye `mistini’(bakuli au kikombe cha bati) na unatakiwa unywe kwa muda mfupi, dawa hapa ni kuongeza maji ili angalau kama utafanikiwa unywe kidogo.
Mimi nilipoingia mafinga kila kilichoelezewa nilikuta baadhi yake ni kinyume chake. Hutaamini, siku tuliyokaribishwa tulikaribishwa kwenye moto, kwani Mafinga kuna baridi ile mbaya, na kwa vile ilikuwa saa saba za usiku, tulilala pembeni ya huo moto hadi asubuhi. Na kesho yake tukasindikizwa na OC, hadi bwenini kwetu tukasajiliwa na kukabidhiwa kitanda. Muda wa kula ulikuwepo ila, mwanawane ilifika muda chakula unachopewa haushibi, hii sikudanganyi, na sio kuwa ni kichache, laa, huko kama unataka nitakusimulia baadaye. Kitanda tulipewa lakini kilikuwa kinaonekana kigeni, sababu gani niulize siku nyingine nitakuhadithia.
Ndugu zanguni, hakuna sehemu nzuri na yenye mafunzo ya ukakamavu kama JKT, ikirudishwa itapunguza mengi na nafikiri hata hawa vijana wanaovuta unga kama ingewezekana wakapelekwa huko, kwani baada ya muda wa mafunzo kuisha kama ni mwaka, au miezi sita,adabu na nidhamu ni asilimia mia.
Wale waliobahatika wenye hizi kumbukumbu naomba mziwakilishe ili ziwavutie kizazi cha sasa,ili na wao waone umuhimu wake.

From miram3.com

Wednesday, August 19, 2009

Dunia ni duara

Leo tarehe 19-08-2009, nilikumbuka tukio moja lilitokea tarehe 25-3-2008, tukio lenyewe lilikuwa hivi:

Dunia hii ni duara, na watu kama tulivyo, kukutana ni wajibu, tofauti na milima. Katika kukutana ndipo tunapojenga urafiki, udugu na hata uchumba, ndio ni kweli hata uadui pia. Lakini tusisahau kuwa kama binadamu tulivyo, kukoseana na hata kujengeana uadui kupo, lakini hili ni nadra, na linapotokea huwa lina sababu, kwani ibilisi huja na visa vyake ili viwe fundisho kwetu.

Diana baada ya kukaa kwenye kampuni moja kwa muda mrefu, alipata bahati ya kuomba sehemu nyingine. Alifanya hivi ili kupata sehemu itakayokidhi mahitaji yake, lakini pia alishachoka kufanya kazi na meneja wake ambaye kila siku waliishia kugombana. Siku alipopewa barua ya ajira sehemu nyingine, ambayo ilimuahidi kipato kikubwa, alitamani dunia yote ijue kuwa yeye sasa hivi, sio yule Diana waliyemjua ni Diana mwingine. Kwa raha aliyokuwa nayo, aliingia ofisisni kwa taksi, na akiwa amechelewa.

Alipofika asubuhi ofisini, aliwasabahi wale waliokuwa karibu naye huku akiwapa mkono wa kwaheri. Alimwendea bosi wake ambaye walikuwa hawaivani, na alipoulizwa kwanini kachelewa alijibu kwa dharau, `tatizo la usafiri,’ Bosi alipotaka kuja juu akaona huo ndio muda muafaka wa kumpa bosi vipande vyake, na kweli alimpa bosi vipande vyake, na kumwambia sasa hivi yeye na kampuni yake basi.Bosi wake Mr. JeuriMbaya ambaye licha ya ukali wake katika kazi, kitu ambacho wengi walimuona ana roho mbaya, alikuwa muungwana pale panapohitajika, alichofanya ni kumtakia kila-laheri, na kumwambia kama katika utendaji wake wakazi walikwazana, basi anaomba msamaha, kwani yeye alikuwa akitimiza wajibu wake tu. Diana alimwangalia kwa jicho la dharau, akageuka na kuelekea kwenye meza yake, huku moyoni akisema, bosi wa namna yako hastahili kufanya kazi na mimi.

Hapo mezani alitumia muda mwingi kuwajulisha marafiki zake kuwa yeye sasa atakuwa katika ofisi za Kampuni kubwa ya Kimarekani, ambapo pia ameahidiwa kupekwa masomoni.Ilipofika jioni, Diana alichukuliwa na taksi, ya mshikaji wake na moja kwa moja walielekea Kaunta. Huko alikunywa kama amesingiziwa. Waliondoka maeneo hayo usiku akiwa hajitambui. Njiani kwa vile walikuwa wamelewa chakari, wakapata ajali mbaya, ajali hiyo ilimvunja Diana mguu na kujikuta anapelekwa Muhimbili.

Kwa vile Kampuni yake mpya ilishaingia mkataba naye, ilimsaidia na kumhakikishia kuwa ajira yake bado ipo ingawaje alikuwa hajaanza kazi. Hii ilimpa faraja sana Diana, na akaendelea na matibabu yake huku akijua hawezi kumrudia meneja JeuriMbaya.. Hapo Muhimbili alikaa miezi miwili. Alipotoka, alipewa mapumziko ya mwezi mzima nyumbani.

Siku ikafika, na hali ya mguu wake ilisharejea vyema, ikabidi aripoti ofisini kwake, kwenye ofisi mpya. Alikariribishwa kwa bashasha na kila mmoja akimpa pole kwa huruma na upendo. Hali hii hakuizoea huko alikotoka. Alifurahi moyoni, na kusema `hapa ndipo nilipokuwa nikapataka…

`Diana tuna bahati kubwa sana, kwani tumepata meneja utawala mpya, ambaye utakuwa katibu muhtasi wake, naye kaajiriwa karibuni, kwahiyo twende ofisini kwake ukatambulishwe’ Aliambiwa na Ofisa utawala.

Akiwa na bashasha ya kumuona meneja wake mpya, ambaye alihisi atakuwa Mzungu, alitabasamu akamtafadhali Ofisa Utawala na kuchepuka kwanza chooni ili aweze kujikwatua. Hii ilikuwa sehemu ya mambo ambayo alifundishwa kuwa anatakiwa apendeze ili kumvutia bosi wake pamoja wageni.

Aliongozana na ofisa utawala, mama wa makamo, mama ambaye aliijua kazi yake vilivyo. Na kwa uzoefu wa siku nyingi, aliona amuelekeze yule binti wake mambo kadhaa kabla hajampeleka kwa bosi wake mpya. Diana alijisikia vibaya, hakupenda kukosolewa, lakini alijikaza akijua kuwa anabembeleza ajira.Kabla ya kuingia kwa meneja huyo ilibidi wapitie kwa meneja wengine mbalimbali, na kila sehemu alipokelewa vizuri na kukaribishwa ofisi mpya.

Mwishowe walifika kwenye ofisi iliyoandikwa `Meneja utawala’ Waligonga mlango wa Meneja Utawala na kukaribishwa ndani.Walipoingia walimkuta meneja Utawala akiwa ameinama na kugeukia upande mwingine, kwahiyo sura yake ilikuwa haionekani vizuri.‘Karibuni tafadhali, natafuta faili moja hapa, la huyu katibu wangu Mhtasi, unasema anaitwa nani vile…’

Aliwakaribisha huku akitaka kulifunua lile faili, bila kuwaangalia.‘Tafadhali bosi hatutaki kuchukua muda wako mwingi, yeye kwa vile mtakuwa naye karibu atajitambulisha kwako vizuri, kama unavyojua alikuwa anaumwa, kabla hata hajaanza kazi hapa….’ Aliongea ofisa utawala.

‘Oooh, karibuni sana,..’ aligeuka akiwa amenyosha mkono.Mshangao alioupata Diana ulimfanya aishiwe na nguvu, na kama asingekuwa ameegemea meza angejikuta kadondoka chini. Hakuamini macho yake…

‘Ahsante, sh-shi-kamoooo bosi’ Alijikuta akitoa salama ambayo hajawahi kumsalimia bosi wake kabla.Aliyekuwa amesimama mbele yake si mwingine ila ni bosi wake wa zamani, ambaye waliachana naye kwa mizengwe, sasa ni bosi wake mpya, Mr.Jeuri Mbaya.JE KAMA WEWE UNGEKUWA NI DIANA UNGEFANYAJE


From miram3.com

Tuesday, August 18, 2009

MWANGALIE ALIYECHINI YAKO

Mwisho wa wiki hii nilienda hospitali, mke wangu alikuwa anaumwa na hali tuliyomchukua nayo nyumbani ilikuwa sio nzuri, kiasi kwamba tuliona tukifika tu tusikae foleni,tuingie moja kwa moja kumuona dakitari.
Wakati tunasubiri kuingia kwa dakitari,kwani tulikuta ana mgonjwa , ghafula wakawa wanaletwa wagonjwa aina kwa aina, na hali zao zilikuwa taabani, ilibidi tuwapishe wamuone dakitari kwanza, licha ya hali ya mke wangu ilivyokuwa, lakini kwa kipindi kile alionekana hajambo ukilinganisha na hao wagonjwa walioletwa.
`Vipi unajisikiaje mke wangu’ Nilimuuliza akiwa ameniegemea
`Najisikia sijambo’ alisema, lakini sauti yake ilionyesha udhaifu kuwa sio kweli hajambo ila alivyowaona wenzake walivyo alijiona yeye hajambo.
Ni ukweli usiopingika kuwa ukitaka kujipima na matatizo yako ni vyema ukaangalia yule aliye chini yako, na ukitaka kujipima kiuchumi kimaendelea ni vyema ukaangalia aliye juu yako. Lakini wengi wetu tunapenda kuangalia juu,kiasi kwamba vichwa vimeganda kuelekea juu, na hii ni hatari.
Dunia ya sasa hivi ni ya papa mkubwa kuwameza samaki wadogo, hakuna cha huruma wala mapenzi. Wale wenye uwezo wanatamani wapate zaidi na hata kama hawakihitaji, kwasababu alieye nacho anazidi kuongezewa na hali yule asiye nacho anazidi kunyang’anywa hata kile kidogo alicho nacho. Jifikirie wewe uliyejaliwa ni mara ngapi umemwaga chakula jalalani, ni mara ngapi umechoma nguo kwasababu haziendani na wakati !
Ushauri wangu wa leo tarehe 18-08-2009 ni kuwa tujitahidi sana kuwaangalia wale walio chini yetu, ili tuwakwamue waje sawa au karibu sawa na sisi kwa kufanya hivyo, hatutasikia vilio vya njaa, hatutasikia vilio vya mwiziii, na kitakachotawala ni upendo, na amani kwani hata yule aliyezidiwa itafika muda atasema `aah, mimi sasa sijambo’

From miram3.com

Monday, August 17, 2009

Mikataba ya ajira kulikoni

Mkono ukiwa shavuni ukiwa umeshikilia kichwa kilichobeba lukuki la matatizo,na huenda hayo matatizo yangelijazwa kwenye magunia huo mkono ulioshikilia shavu usingelihimili. Hii ilikuwa jumatatu nyingine ya tarehe 17-08-2009, nikikumbuka jamaa yangu nilyemkuta upenuni mwa nyumba anayoishi huku kashikilia shavu.
`Ndugu yangu aheri nimekuona,manake watoto wamefukuzwa shule sijalipa ada sasa mihula mitatu, jana nimepokea barua kuwa mwisho wa mwezi huu mkataba unakwisha na hawana haja ya kunichukua tena. Baba yangu anaumwa na mke wangu ndio huyu hauchihauchi kunakucha sina hela ya kumtibia, je nina thamani gani katika hii dunia, hebu niambie rafiki yangu?' alinielezea huku machozi yakimlengalenga.
Rafiki yangu huyu alimaliza diploma yake vizuri akapata kazi katika kampuni moja ya watu binafsi, aliitumikia kampuni hiyo kwa zaidi ya miaka 15, kwa uaminifu na uchapajikazi bora, kiasi kwamba mwajiri wake alimpenda sana, lakini kwa mdomo, hakuwahi kuongezwa mshahara na walioajiriwa baadaye ambao wangi walikuwa watoto wa wakubwa au wageni toka nchi nyingine walipewa mishahara minono . Alidai haki yake ili naye afikiriwe, na huko kudai kukamtokea nyongo, mwajiri akabadili kibao na mkataba ulipoisha akaambiwa katafute sehemu watakaokulipa mshahara unaotaka, na barua hiyo alipewa jioni wakati muda wa kazi unaishia.
Katika mkataba wake wa ajira alitakiwa alipwe mshahara wa mwezi mmoja tu kama zawadi, na kwa vile alikuwa na madeni hela yote aliyotakiwa kulipwa ilikatwa kufidia sehemu ya deni lake.
Hadithi ni ndefu, na unaweza ukasema yote maisha, lakini dukuduku langu ni huu utaratibu wa nchi, wa kutowalinda raia zake katika sehemu za kazi. Hawa wenye makampuni wanawatega wafanyakazi wao kwa mikataba ambayo hatimayake ni mbaya. Nafikiri kungekuwa na mkataba wa ujumla kuwa kila anayeajiriwa anatakiwa kupata haki hii na alindwe vipi na mikataba hiyo. Makampuni mengi ya watu binafsi hayataki vyama vya wafanyakazi, je serikali inajua hili? Au mimi ndio sijui , naomba tujadiliane hili.
From miram3.com

Friday, August 14, 2009

Adha ya Usafiri na diari yangu

Diary yangu inanikumbusha siku ile ya kashehe 30-09-2008, ambako simu yangu ilizimka kwahiyo sikuweza kuamushwa na `alarm’ Niligutuka kutoka kwenye ndoto ya kutisha ya kuumwa na nyoka. Cha ajabu hata kama upo usingizini ukimuota huyu mdudu, utazinduka tu. Kwa imani za watu wengine, ukiota ndoto kama hii, inaashiria kukumbana na wanga. Nashukuru, sikudhurika na nyoka huyo, kwani alitokea jamaa kwenye ndoto akanitibu jeraha, na kuniambia niko safi.
Nilizinduka na kuangalia nje `kweupeee’. Ilikuwa saa kumi na mbili na dakika chache, na saa kama hizo nilitakiwa niwe maeneo ya TAZARA. Ilikuwa bado na kigizagiza, ingawaje mionzi ya kupambazuka ilishapenya madirishani.
Nilivaa haraka na kukimbilia kituoni, cha ajabu nilikuta umati wa watu kituoni, kuonyesha kuwa hata wale waliowahi walikuwa hawajaondoka. Nini kilichoajiri siku ya leo ilikuwa swali la kila mtu, je madereva wamegoma, au kuna nini cha ajabu.
Kituo hiki cha Moshi Bar, kimejaza magari mabovu, magari ya vituo vyote utayakuta hapa, si Mwenge, Kimara, Kigogo,Temeke,na kila kituo unachokijua wewe utayakuta magari yenye nembo za maeneo hayo, lakini mwisho wake ni Mombasa.
`Kimvua hiki kidogo tu kimefanya magari yote yashindwe kufanya kazi, hawa wenye madaladala sijui wanaishi kibiashara kweli’ mmoja wa abiria alilalamika.
Ni kweli kwa vile usiku kulinyesha magari mengi yanaogopa maji na kunasa kwa tope, kwani barabara hii ya Moshi Bar hadi Mombasa inasifika kwa tope, makorono na vumbi kipindi cha jua kali.
Gari moja lilikuja kwa kasi utafikiri lipo kwenye mashindano likijifanya linapitiliza, na lilipofika umbali fulani likageuza ghafla na hamadi liligeuzia pale niliposimama na kunifanya niwe wa kwanza kuingia ndani ya gari. Nilishukuru Mungu kimoyomoyo.
Nikiwa nawashangaa watu wanavyogombea kuingia macho yangu yalikagua viatu nilivyovaa. Ilikuwa Bahati ya ajabu, sijui ingekuwaje kama nisingegundua makosa haya mapema.
Sikuamini macho yangu, sijui ni kwa sababu ya ile harakaharaka ya kuwahi au ni kwasababu ya tatizo la umeme, kwani asubuhi hii umeme ulikuwa umegoma. Hapa bongo kila kitu kina mgomo wake, bila hivyo hakueleweki kitu. Nilikagua tena viatu vyangu na nilipohakikisha kweli nimevaa viatu viwili tofauti, nilijicheka na kujiandaa kushuka ndani ya gari.
‘Vipi mzee unaenda wapi’ konda aliuliza akiwa tayari ameamurisha gari liondoke.
‘Nimesahau nauli..’ nilijibu haraharaka huku naruka nje ya gari. Kidogo nidondokee magoti, kwani gari gari lilishaanza mwendo.
Nilirejea kituoni baada ya kubadilisha viatu na umati ulikuwa umeanza kupungua nafikiri wengi wa abiria waliamua kutembea kwa mguu. Nami wazo hilo lilinijia na kuanza kutembea mwendo mdogo mdogo.
Nilipofika relini, gari moja lilokuwa linatengenezwa lilianza kusukumwa, nami nikajiunga kulisukuma na ikawa ndio ahueni yangu. Tulipofika Mazizini gari likasimama, na kuzima. Ilikuwa saa kumi na mbili na nusu. Saa kama hizo mara nyingi ninakuwa maeneo ya Msasani au Magomeni.
Hali ilivyokuwa ilibidi abiria wote tutoke tusukume gari, na ndivyo ilivyokuwa, lakini gari halikuwaka, ikabidi tuanze mwendo wa mguu. Kwasababu tulikuwa wengi, mwendo ulikuwa wa haraharaka na tukawasili Mombasa kiasi cha saa moja na dakika kadhaa.
Sheria za kazini ni kuwa saa mbili kazi zimeanza, na ukichelewa utakuta daftari la mahudhurio limepelekwa kwa meneja utawala, na huenda ukaishia kupewa onyo kali. Lakini baya zaidi kampuni ilikuwa katika mchakato wa kupnguzwa wafanyakazi kwahiyo mchelewaji ananafasi kubwa ya kupewa barua hiyo.
Kijasho chembamba, kilinitoka licha ya kile cha kutembea mwendo mrefu, umati nilioukuta hapo Mombasa utafikiri watu wote waishio maeneo ya huku waliamua kusafiri siku hiyo. Niliamua kusubiri magari yatokayo mjini, ili niende nayo hadi Gongolamboto halafu nirudi nayo, manake nilipe nauli mara mbili. Na hii iliniashiria kuwa inabidi niamua kutokula mchana ili nipate nauli ya kurudia nyumbani jioni.
Wakati tunageuza kichwa huko na kule utafikiri tunaamurishwa na mjamaa fulani aliyejificha, macho yetu yalishuhudia mama akikoswakoswa na magurudumu ya basi moja la Msasani-Gongolamboto. Magari haya yanamtindo wa kuchukua abiria juu kwa juu. Yaani huku linatembea huku wanapakiza abiria. Yule mama alipoinuka pale, bado hakukubali alilikimbilia lila gari na bahari nzuri akafanikiwa kudandia. Ni hatari lakini atafanyaje?
Nilibahatisha basi lakini lilijaza kupita kiasi. Nilipokanyaga nilikuwa nimesimamia vidole, na kila nilipojaribu kushusha unyayo chini, nilisikia abiria akilalamika, `unanikanyaga, unaniumiza’ Kwahiyo ilibidi nisimame kwa mtindo huo hadi pale abiria walipoanza kupungua.
Nilifika ofisini saa tatu kasoro hivi, na hapo iliashiria kuchelewa kupita kiasi, na maana yake niende kwa meneja utawala kujieleza. Sipendi kabisa hii hali lakini ningefanyaje? Nilijiuliza bila majibu.
Niliwakuta wenzangu wanaoishi maeneo ya majirani wameshafika, na kila mmoja aliniangalia kwa jicho la huruma. Nilianza kunywea kwanini wananiangalia kwa jicho la huruma, kuna nini cha ajabu kimetokea.
Tutaendela baadaye.
NB. Jamani kutokana na tukio hili nikaamua kutunga kitabu cha `YOTE MAISHA’ Mungu akijalia nitakiweka hewani.
Na siku za nyuma niliandika maelezo mazuri kuhusiana na tatizo la Usafikiri njia ya kuelekea Gongolamboto na kuiepeleka kwa michuzi ikiwa na kichwa cha habari kero ya usafiri Gongolamboto.

From miram3.com

Thursday, August 13, 2009

Tusaidie wenye ulemavu

Leo tarehe 13-08-2009, nikiwa ndani ya daladala kulikuwa na watoto wenye ulemavu wa kusikia, walikuwa wkienda shule. Ndani ya gari hilo wengi walikuwa wanawatazama jinsi wanavyoongea kwa ishara kwa kutumia mikono yao. Mimi mawazo yangu yalienda mbali zaidi ya kuwaangalia, nilijaribu kuwafikiria watoto kama hao ambao wapo vijijini, hawana hili wala lile, kwasababu wamezaliwa na upungufu huo wao wanakosa hudumamuhimu kama hii ya kusoma.
NGO, nyingi zinaanzishwa lakini ni chache zinazopenya vijijini. Ombi langu kwa wenye uwezo wasaidie kuanzishwa shule kama hizi vijijini kwani kati ya hawa wapo wenye vipaji vikubwa, wataalamu na viongozi wa baadaye. Inabidi na wamanchi waelimishwe kuwa kuwa kilema sio mkosi, bali ni sehemu ya maumbile tu ya kibinadamu.

Wednesday, August 12, 2009

Mtoto wa mwenzako ni wako pia

Ni asubuhi nyingine ya tarehe 12-08-2009, kama kawaida nilidamka asubuhi nakuwahi kituoni, ilikuwa saa kumi na moja alifajiri. Nilipata basi la kwanza kirahisi, nilipofika Mombasa nilikuta umati wa watu ukisubiri gari, na magari ya kwenda Msasani ni juu kwa juu,yaani hayasimami, na kama hujui kudandia basi utalala hapo kituoni.
Katika kukuru kakara hiyo mtoto mmoja wa shule ya msingi alidandia, na wakati huo gari linaongeza mwendo na yule konda, au mpiga debe akawa anamsukumia nje. Ilikuwa ni hatari kwasababu kama yule mtoto angeishiwa nguvu na kuachia vile alivyong'ang'ania ule mlango wa gari angedondoka na kuumia. Baadhi ya wazazi mle ndani wakaanza kumshambulia yule konda kwa maneno kuwa amuachie yule mtoto aingie ndani.
Hatimaye yule mtoto alipenya kwa shida akaingia ndani ya daladala. Niliwaza sana ni nikijua kuwa hata mimi watoto wangu watakuwa wanafanyiwa hivyo. Hii ni kujisahau na kutizama yale matamanio yetu ya muda ule. Namshukuru sana mke wa raisi wetu alipotoa kauli kuwa `mtoto wa mwenzio na mtoto wako pia.
Kama usipomjali mtoto wa mwenzio ujue hata wakwako atakuwa hajiliwi pia, ukimtenda ubaya ujue na wakawao atatendewa ubaya pia, hata kama una uwezo ipo siku na wewe au yeye atakumbana na maswahiba hayo.
Ombi langu tusipende kutendea ubaya wenzetu, kwani na sisi yatatukuta kwa namna moja au nyingine, kama sio kwako ni katika uzazi wako, na muumba anatuona kwa hayo tunayo tenda kwani yeye ni mwingi wa hekima.

Tuesday, August 11, 2009

Ubinadamu unatokomea

Siku ya leo tarehe 11-08-2009, niliwaza sana jinsi gani watu wanavyogeuka kuwa wanyama. Ubinadamu unatokomea. Nilisikia kuwa kuna maiti ya mtoto imeokotwa ikiwa imetupwa ndani ya mifuko ya plastiki. Jaribu kufikiria huyu mtu ndani ya roho yake yukoje, na kwanini aamue kufanya jambo hilo la kinyama.

Je ipo sababu kweli kubwa ya kufanya kitendo hicho?

Kuna wengine walidai, alipopewa mimba aliyempa alimsaliti, lakini je hicho kiumbe kina kosa gani, kwani kusalitiana ni kati yao wawili, na hicho kiumbe hakikuwepo kwenye makubaliano yao. Hii yote ni kujisahau nakujiona tuna maamuzi na utawala wetu binafsi. Tunajisahau kuwa kuna leo na kesho, na yupo muumba mwenye mamlaka na wewe zaidi ya unavyofikiria.
Kwa ushauri wangu binafsi, kila tunalofanya tujaribu kuangalia kulikoni, je ikitokea hivi itakuwaje? Na pili je kama na mimi ningefanyiwa hivi ingekuwaje?
Tushauriane kwa hili