Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, March 28, 2018

MKUKI KWA NGURUWE-103



 Nilipoichukua sikuwa na haraka ya kuiangalia,…lakini niliposikia wakiongea nikataka kuhakiki, sikuamini nilichosikia hadi pale nilipoangalia hiyo video ya matukio ya siku ile,….sikuamini, hadi leo nashindwa kuamini…we acha tu…

‘Niambie ukweli maana wewe si umesema hapa kuna ulinzi, kuna mitambo, iliwezekanaje mtu kuchukua silaha na kwenda kumuua bosi…bila hata kujulikana, kwahiyo hiyo mitambo iliisha chaji au..…?’ nikamuuliza kuonyesha sijui kitu

‘Hahaha, sio chaji…. kuna mtu alizima hiyo mitambi, ina maana ni mtu anayeifahamu, na mtu huyo ni huyo huyo…unaonaeeh, …’akatulia kidogo

‘Mimi niliona kila kitu kwenye hiyo video, nashukuru niliipata kabla haijafika mikononi mwa hao watu wake, au polisi, maana inaonyesha kila kitu hakuna kilichobakia, …inaonyesha kila kitu, …

‘Kama nilivyosema japokuwa mtu kazima mtambo mkubwa lakini huo mdogo ndani ya chumba kwa Marehemu bado uliendelea kuchukua taarifa, wenyewe hauzimiki haraka, Marehem alilijua hilo kuwa kunaweza kutokea tatizo mitambo ikazima, kwahiyo akaweka server……’akasema

‘Ok, sasa hiyo silaha ilifikaje…?’ nikauliza

‘Mhh..hapo hata mimi sijui..ila kilichoonekana silaha hiyo ilikuwa chumbani kwa mdada…’akasema

‘Wewe si mlinzi wa mbali, unamlinda mzee, ilikuwaje silaha ifike humo ndani wewe usione ..hapo ndio nakuwa na mashaka na ulinzi wako, au na wewe ulihusika…’nikasema

‘Mimi namlinda mzee, ..sio jengo, sio kila kitu kwenye jengo, unasikia, ulinzi wa jengo wapo watu wengine, na mkuu wao ni mtoto wa mzee, unasikia, kwahiyo jinsi silaha ilivyoingia sijui…mimi isingelikuwa hilo tatizo,…la mke wangu mzee asingeliuwawa…’akasema

‘Kwahiyo silaha ilikuwa chumbani kwa mdada, huyu jamaa alijuaje kuwa ipo huko…?’ nikauliza

‘Unataka kutunga kitabu…?’ akauliza huku akicheka

‘Au usije ukawa ni shushushu…nitakuua….’akasema na kucheka

‘Hahahaha, hapana….ni hadithi au tukio la kuvutia….’nikasema

‘Sio hadithi, hilo ni tukio la kweli, upo ushahidi…silaha ilikuwepo kwa huyo mdada, swali ilifikaje, kama huyo mdada naye hakuwa na nia mbaya na bosi, ndio maana awali nilijua yeye ndiye kamuua…’akasema

‘Endelea,..very interesting story…’akasema

****************

Jamaa akaingia chumbani kwa mdada, akaichukua hiyo silaha, maana huyo mdada hakuwepo hapo chumbani kwake alikuwa kwenye ofisi yake…usingelimuona awali, usingelijua ni yeye, alivyojivika hayo manguo, kuonyesha kweli huyo jamaa ni jasusi..

Ili kuwa ni kitendo cha haraka sana…wakati huo marehemu alikuwa akiongea na yule jamaa yake, walikuwa hawaelewani,…walikuwa wanabishana sana, unajua kama isingelikuwa ni huo ushahid , pia ungelisema huyo jamaa yake ndiye alimuua, maana ilifikia mahali, huyo jamaa yake anasema kwa sauti.

‘Ipo siku nitakuua kwa hili….’

‘Nani alisema hivyo…?’ nikamuuliza

‘Huyo jamaa yake waliyekuwa wakiongea naye…’akasema

‘Unamfahamu huyo jamaa…?’ nikauliza

‘Unajua…awali, sikuweza kumfahamu maana alikuwa kajibadili…lakini nikaja kugundua kuwa ni jamaa gani,...ni jamaa mmoja bwege-bwege fulani, yeye hakujua tu, alikuwa kitumiwa kwa masilahi ya wengine……’akasema na kutulia

‘Ulikuja kumgunduaje kuwa ni yeye…?’ nikauliza

‘Mtandao..unaweka picha, …inakuambia huyo mtu ni mtu fulani, kajibadili…siku hizi mambo ya kisasa…haikuwa kazi kwangu kumgundua,…mimi ni mtaalamu usinione hivi..mzee alikuwa akinifahamu ndio maana akaniamini.

‘Ok, sawa endelea…’nikasema nikijifanya kuangalia saa.

 Ikaonekana jamaa katoka na silaha…lakini wakati anatoka alikuwa kaifutika kwenye koti…, nilishangaa kwanini mlio wa hatari haukulia, kwani yeye alikuwa na silaha, nikagundua kuwa yeye kwa vile ni mtaalamu aliweza kuzima sehemu ya mlio wa hatari....

‘Alikuwa yeye peke yake…?’ nikauliza

‘Peke yake….ila alionekana kama anawasilana na watu…kwenye simu kabla na baada ya tukio…’akasema

‘Ok endelea…’nikasema

‘Basi akafika kwenye ile ofisi, ..akasimama, kama anasita kufanya anachotaka kukifanya, ghafla akasukuma mlango.

‘Ile video inazunguka, kwahiyo ilikuwa kama ..imekata, halafu ikaonekana sasa anamlenga baba yake, hiyo inaonyesha wazi, hakuna kuremba, bila chenga, risasi inatoka inakwenda kutua kifuani kwa mzee..…nahisi baba yake alimuona….ila huenda baba yake hakufahamu ni nani.

‘Akawa sasa anataka kummaliza huyo jamaa mwingine, ile bastola ikawa imeishiwa risasi, kwa ujinga wake, aliichukua ile bastola, bila kuhakikisha kuwa ina risasi za kutosha, kwa mshituko wa kile alichokifanya, akairusha kwa ndani...nahisi alifanya hivyo makusudi ili watu wengine, hasa huyo jamaa aliyekuwepo humo ndani ashukiwe kama muuaji,...

‘Kwahiyo una uhakika kuwa huyu mtu ndiye huyo mtoto wa mzee,…maana hapa ni muhimu…?’ nikauliza

‘Uhakika gani sasa..ukiangalia hiyo video ya matukio utaona kila kitu…..’akasema

‘Oh….inatisha, mtoto kumuua baba yake…haiwezekani…’nikasema

‘Ndio maana nakuambia hata mimi siamini….ukiangalia hiyo video, utafikiri ya kuigiza, lakini ndio tukio lenyewe,…sasa hebu niambia mtu kama huyo utaweza kuishi naye bila kuwa na mashaka…’akasema
‘Halafu ikawaje…?’ nikamuuliza sasa nikiwa sina hamu na mengine ni kupoteza muda sasa…

‘Baadaye  sasa, akaonekana mwanadada mwingine akiingia, huyo ndiye waliyekuja kum-kamata kama mshukiwa,…’akasema

‘Huyu mwanadada ni nani…?’ nikauliza

‘Yaani huwezi amini, huyo mwanadada ni mke wa huyu jamaa aliyekuwa akiongea na marehemu…’akasema kwa sauti ya chini..

‘Oh…alikuja kufanya nini…?’ nikauliza

‘Nahisi alikuwa na yake,…na marehemu, ..si unajua marehemu ana wateja wengi, na mambo yake ni mengi tu…’ akasema

‘Kwahiyo wakazidi kuchelewa, kumpata muuaji halisi,…na ushahidi mwingi ukawa unapotea bure, ila halisi ya matukio, ikawa imechakachuliwa, lakini ya kwangu ilibakia kama ilivyo, kila kitu kipo...’akasema kwa haraka haraka, nilimpata kwa vile nilishajua mengine...

‘Sasa nikuulize kumbe wewe ulikuwa na ushahidi wote huo, kwanini hukuwafahamisha wanafamilia, yaani mtoto mkubwa wa marehemu?’ nikamuuliza

‘Sikufanya haraka hivyo, hata hivyo, wao yaani yeye na mama yake hawakutaka kuingilia yote hayo, japokuwa walihisi kuwa kuna mtu anahusika, wao walirizika na taarifa ya polisi kuwa huenda muuaji ni miongoni mwa maadui zake.

‘Mhh..wewe ulilionaje hilo…?’ nikauliza
‘Sikuona cha ajabu,…hawakuwa karibu sana na mzee, kabisa, walifanya tu kutumiza wajibu,, wewe huoni ajabu kuwa hawakutaka mali ya marehemu kabisa, urithi ulikuwepo kwa ajili yao, mtoto na mama yake, lakini hawakuutaka kabisa....’akatulia kidogo.

‘Sina uhakika na hilo, ila nakala halali ya nani arithi, ilipatikana,..ikionyesha kuwa kaka mkubwa ndiye msimamizi wa kila kitu, na msaidizi wake ndio huyo mtoto mwingine …aliyemuua baba yake…ile ya kwako waliyogushi ikachelewa kupatikana,kukawa na mkanganyiko hapo.

‘Maana hadi kufanya hayo mauaji ni ili …mirathi yao waliyotengeneza wao, iwe halali na hiyo ya mzee ipotezewe, ikawa kinyuma chake, mtoto na mama walihaha, kilichowafanya wasifanye jambo, ni pale walipoona wenzao hawana tamaa na mali, hawataki chochote kutoka kwa marehemu.

‘Sasa kibaya zaidi ni pale wenzao walipoanza kugawa mali,..hilo lilifanya kuzuke mgongano, lakini wenzao walikuwa wastaarabu, wakasema wao hawatagusa mali kubwa kubwa, wao, wanataka mali zile ambazo zinaondosheka, wauze, kulipia madeni, ..na kuwalipa wale waliodhulimuwa, japokuwa hazikutosha.

‘Mambo yakawa yanachelewa..huyu mtoto mkubwa, akaona bora aondoke na iliyobakia ikawa chini ya huyu msaidizi wake,..alipoondoka tu, huyo mdogo mtu akacheza, akahakikisha ile mirathi yake ndio inatambulikana, hadi sasa utaona hivyo…

‘Kwa vipi sasa, wakili wao si yupo…wakili aliyekabidhiwa hayo mambo na mzee…?’ akaulizwa

‘Wakili hahaha…tuyaache tu hayo…nikuambie kitu.., huyu sio sawa na Makabrasha, akikutisha anakutisha kweli…wakili akafyata mkia, akawa sasa anafuata anachotaka bosi mpya…’akaangalia saa nahisi alinihofia mimi nachelewa kuondoka, akili za kunijali bado zilikuwepo.

‘Unafikiri kwanini huyu mtoto mkubwa na mama yake hawakutaka kuchunguza kwa undani kifo cha Makabrasha, hapo bado mimi najiuliza, isije ikawa na wao wapo nyuma na jambo fulani….?’ nikamuuliza

 ‘Hapo hata mimi sijui,...sijui kwanini hawakutaka kufanya uchunguzi wao wa kina...ila mimi nilitaka kumwambia huyo mtoto wa mzee yale niliyokuwa nayafahamu kwa wakati huo, lakini huyo mtoto wake, aliniambia niachane kabisa na maisha ya baba yake, kwani yeye hataki kabisa kuyaingilia na wala hataki mali yake, alishajitoa kwake, yeye amefika kwasababu ni baba yake na niwajibu wake kumzika, mengine kama ninayo ni mwambie huyo mdogo wake….yeye keshamaliza kilichomleta na kama nina ushahid wa kutosha wa muuaji, niwaone polisi….

‘Aliponiambia hivyo nikaona basi haina haja...nitautumia huo ushahidi nilionao nionavyo mimi,..siunaona, imanisaidia na mimi, japokuwa nahisi nipo kwenye hatari, hata hivyo, hatari imekuwa ndio maisha yangu,...huwezi jua, kifo changu kinaweza kuwa kama cha marehemu..’akasema.

‘Mimi nakushauri kitu, ongea na polisi, jisalimishe, ili uwe na maisha ya usalama, maana hujui wenzako wamejipanga vipi, kwanza kama ulivyosema kwenye mirathi halali ya marehemu alikutaja kama mmoja wa warithi wake, huoni utafaidika kihalali ukifanya hivyo...?’nikamwambia.

‘Mhh, ni rahisi kusema hivyo,… lakini huwajui hawa watu, ...mimi siwaamini, na wala siamini kuwa polisi watawaweza kunisaidia kwa hili jambo, nahisi likifika mikononi mwao, hata kile kidogo nilichotarajia kukipata sitakipata tena,…’akasema

‘Unajua huyu …mtoto wa marehemu , kama alivyokuwa baba yake, hata yeye kuna wanamtumia wenye pesa, japokuwa hakuna ushahidi wa moja kwa moja kuwa wanahusika kwenye hayo mauaji,…ni wajanja sana…’akasema

‘Wewe unao ushahidi wa kuonyesha kuwa hao watu wanahusika…?’ nikamuuliza

‘Unajua nikuambie kitu…hawa watu walishafikia sehemu wamemchukia Makabrasha…kuna video inaonyesha hivyo…ninayo…, kwani Marehemu alipoona kafanikiwa mambo yake, akavunja mahusiano na hao wafadhili, …sio moja kwa moja y akukatisha mkataba nao, hapana, alikuwa kama hawajali-jali fulani hivi…, na kazi aliyopewa akawa anaifanya kwa masilahi yake…’akatulia

‘Ehe…’nikasema

‘Kwahiyo kwa hali hiyo, huenda..huyu mtoto wake pamoja na mawazo ya mama yake, pia yawezekana aliahidiwa donge nono, kumbuka kutokana na madeni yaliyobakia ya mzee, jengo lilitakiwa kupigwa mnada, yeye akaligomboa, akalipa madeni yote,…sasa huyu jamaa pesa alipatia wapi, walichunguza hilo watagundua mengi…’akasema

‘Mhh..hapo yawezekana, lakini hata hivyo hakuna ushahidi kuwa hao watu walihusika kwenye hayo mauaji,  huo uhakika haupo, au sio..’nikasema

‘Mimi nilivyoona ni hivyo…, sikutaka kuingia huko sana, maana huko sio pa kuingilia, huko waachie wenyewe…’akasema

‘Mimi ninachojiuliza ni kwanini,  toka marehemu afariki hadi leo, wewe unao ushahidi,  kwanini hukuwaambia polisi, unajitia matatani bure…’nikasema

‘Wao wamefanya nini muda wote huo, kazi kuwakamata watu wasiohusika, kwanini wanawasikiliza wanasiasa, kwanini hawafanyi kazi yao ....mimi naona wengi wao, ni wale wale tu…mimi ndio maana nimeamua nifanye nionavyo mimi, kwa masilahi yangu kwanza, hapo nitakaposhindiwa basi nitajua la kufanya...’akasema.

‘Je na huyu mtoto wa marehemu akikugundua huoni utakuwa ndio mwisho wako?’ nikamuuliza.

‘Kunigundua kwa vipi sasa, wao wanafahamu kuwa nina siri hizo,…wao wanachojitahidi ni kutafuta wapi siri hizo zipo…lakini hawataweza kugundua ng’ooo…mimi sio mjinga…’akasema

‘Wao kila wanachokifanya ninakiona, kwanza mimi mwenyewe ni mtaalamu , na pia...mzee wao alinifundisha mambo mengi, ndio maana aliniamini, ...unaona nilivyo mjanja,  pale nyumbani kwako, napaona kila siku, ...wakiongea , wakipanga, mimi napata taarifa, ni kwa usalama wao, lakini pia mimi nachunguza zaidi ya hayo...’akasema.

‘Kwahiyo wao kwa sasa, wapo wapi, wapo hapa nchini au wamewekeza huko nchi za nje… ?’ nikamuuliza, maana mama na mtoto wake, hawajaonekana hapa jijini kwa siku ya tatu sasa, nikaona niulize hilo swali ili watu wa usalama wasikie na wajue jinsi gani ya kufanya.

‘Hao wamekwenda hapo jirani tu,- Kenya, kuna miradi yao wanaifuatilia, ilikuwa miradi ya marehemu, ilikuwa haijakamlika wakati wa uhai wake kwahiyo wao wanataka kuhamisha umiliki kutoka kwa baba kwenda kwa huyo mtoto…’akasema

‘Mhh, ni mradi mkubwa sana…?’ nikauliza

‘Ndio, kama wakifanikiwa, basi wao sio wenzetu tena, na jiulize pesa za kuendeleza mradi huo wamezipatia wapi, ni zawadi kutoka kwa maadui wa marehemu au kuna nini nyuma ya pazia,…aah, mimi huko sipo, ila nitakula nao….’akasema

‘Huenda wakija watakupatia angalau hisa kidogo..?’ nikauliza

‘Hapo ndipo naumia kwanini wachukue kila kitu, kwanini mimi wasinipe haki yangu, ndio maana nimelifanya hili, …kuwakomoa kwanza,…kwa hivi sasa kila kitu wameniachia mimi mpaka wakirudi, wakirudi tu, nawabana, vitisho vyangu ni vile vile...’akasema

‘Kumbe sasa wewe ni bosi...’nikasema.

‘Hahaha, kwa hivi sasa eeh, nimeachiwa usukani,..ila wakirudi wanaweza kuja na ajenda ya siri, lakini mimi nitaigundua tu, ..hawaniwezi...’akasema.

‘Inakuwaje mtu afahamu siri za watu wengine, hicho chombo alichokuachia marehemu kipoje...naona dunia ina mambo mengi, mimi mambo mengi siyajui, naona kama miujiza tu...?’ nikamuuliza

‘Unafikiri ni chombo kikubwa sana wewe…’akasema akionyesha kuchoka.

‘Ni kitu kidogo tu…kama simu tu, unatembea nayo, ukitaka kuangalia mahali fulani ulipoweka vitu vyako, unabonyeza namba, unavuta ule mnara wake, basi unatafuta muelekeo wa namba, unawaona, ...

‘Sasa kama unataka kukihamisha hicho kidude kwenye komputa unakiweka, ...hapo unaweza kuangalia, kama unavyoangalia picha za kawaida, wanawasanifu watu kweli kweli, lakini mpaka upandikize chombo fulani hapo unapotaka kupata taarifa ....mimi ni mtaalamu bwana..’akasema kwa sauti ya kilevi.

‘Sasa wewe una uhakika gani kuwa mwenzako huyo naye hakufanyii kama unavyo mfanyia yeye,huenda huko alipo anakuona..huenda hata nyumbani kwako unapoishi kapandikiza kitu kama hicho?’ nikamuuliza.

‘Kuna kifaa kingine cha kugundua hivyo vitu vya kupandakiza, mimi kama mlinzi ninacho, kama kuna kitu kimepandikizwa kwako kinakuashiria, lakini sijawahi kumuonyesha huyo mtoto wa marehemu, aliwahi kukipandikiza kwangu, nikakigundua, kwahiyo mimi nipo mbele zaidi yake....’akasema.

‘Wao wanarudi lini?’ nikamuuliza

‘Kesho, ila kila siku nawasiliana nao, wanaweza wakaja hata leo, kwa usalama mara nyingi hawasemi lini wanafika, ndio maisha ya watu kama hawo, kama alivyokuwa marehemu, ila mimi nafahamu ni kesho.....’akasema.

Mara simu yake ikalia, akaiangalia, na kusema, ...
*****************

‘Bosi,...naona keshafika, huenda wapo hapo uwanja wa ndege,...sasa mimi kwa hali niliyo nayo,sijui kama nitaweza kuwafuata, inabidi nimwambia mtu akawachukue, ngoja niongee naye kwanza, maana nahisi nimelewa sitaweza kuongea nao katika hali hii, au unasemaje mpenzi,....’akasema.

‘Kweli...’mimi nikasema huku nikijua sasa kazi imekwisha, nikahakikisha namsogelea ili kusikia anachoongea, sikuweza kusikia huyo bosi wao anaongea nini, lakini alivyokuwa akijibiwa nilisikia, jamaa akawa anajiuma uma,..mimi kwa haraka nikawasiliana na watu wangu kwa ujumbe wa simu, na wao wakanijibu kuwa wananifuatilia kwa karibu,nisiwe na wasiwasi.

‘Haloo bosi, mnasemaje?’ akawa anaongea kwa kujitahidi kuficha kuwa kalewa, huku pia akijaribu kunikwepa ili nisiwe karibu naye, lakini sikumpa nafasi hiyo nikamsogelea, akawa sasa anaongea na simu, akasema;

‘Unasema mumeshafika, mpo nyumbani, mbona hamkuniambia nije kuwapokea hapo uwanja wa ndege, nipo hapa karibu kabisa...!’akasema kwa akionyesha mshangao.

‘Ohoo, ndio nilizima kidogo, maana nina mtoto, nastarehe kidogo, siunajua leo ni mapumziko bosi...sasa sikutaka mambo yangu yaonekane huko, nitawasha,...nikimaliza..nipe nusu saa,...sasa hivi, kwanini bosi, mbona unaniharibia starehe zangu, unasema kuna nini..hapana bosi, mimi nina uhakika hakuna kitu kama hicho...una uhakika,...’akasema na nilimuona akiwa na wasiwasi.

Baadaye alinigeukia, na kusema;

‘Mhh, naona mambo yameharibika, kitumbua kimeingia mchanga....’akasema akionyesha wasiwasi.

‘Kuna nini kimetokea....? nikamuuliza

‘Jamaa anasema kafika tu ,polisi wamemvamia, ananihisi eti mimi ndiye nimemuuza, polisi wameshafika kwa bosi, haapo kajiiba ,kusogea pembeni, kunipa tahadhari, nihakikishe hawafiki huku,  sasa naona mambo yangu yameharibika, sijui nifanye nini, ..kwanini polisi wamefanya haraka kiasi hiki hata ujenzi haujakamilika...’akasema, na mimi nikamwambia.

‘Wewe usijali, ..cha muhimu ni kutoa ushirikiano na polisi, maana inavyoonekana polisi wameshafahamu ni nani muuaji, sasa ukijificha, na wewe utashikwa kama mshirika wao..mimi naona hapa hakuna usalama tena nataka kuondoka....’nikamwambia na yeye akawa kama anafikiria jambo.

‘Sasa bosi  kasema niharibu kila kitu, ....’akasema

‘Wewe, usije ukafanya hilo kosa, unaharibu vidhibiti vya polisi, huoni kuwa wewe utaonekana  mshirika wa hayo mauaji..’nikamwambia.

‘Ok, nimekuelewa, lakini kwanini huyu bosi anasema hata sasa hapa nilipo, nipo na watu wa usalama, mimi simuelewi kabisa... ngoja nikawashe hiyo mitambo niliyokuwa nimeizima, tuondoke zetu, wameniharibia starehe yangu,....nisubiri...’akasema na mimi nikamuuliza

‘Tutatokea wapi?’ nikamuuliza nikimchelewesha na yeye akaniangalia halafu akaingalia kule tulipoingilia, na kusema

‘Hukohuko tulipoingilia....’akasema, na kabla hajamaliza  mara tukasikia mlango ukigongwa, akawa anangalia huku akionyesha wasiwasi, akaniashiria kwa mkono, nitoke, kwa kupitia ule mlango tulioingilia, huku yeye akianza kuelekea kwenye kile chumba cha ile mitambo, lakini kabla hajaufikia huo mlango, mara mlango ukafunguliwa.

Wa kwanza kuingia alikuwa askari, mwenye sare, na baadaye wakaingia wengine, wakiwa wamevalia kiraia, wote hawo nawafahamu,...

‘Sisi ni askari usalama, mpo chini ya ulinzi, hakuna kusogea au kugusa kitu chochote..’akasema huyo mwenyesare, lakini hakuwa na silaha yoyote zaidi ya rungu, ...nikajua kwanini, wasingeliweza kuingia na silaha kwa kupitia upande wa juu, mlio wa hatari ungelitushitua, na huyu jamaa angelikimbia, ...lakini na mara tukasikia sauti kutoka kule tulipoingilia wakaingia askari wengine, hawa walikuwa na silaha, na hapo hapo mlio wa hatari ukaanza kulia...

‘Kwanini mnanivamia nimefanya kosa gani?’ akauliza na wao wakamshika na kumfunga pingu, na kumweka chini ya ulinzi, mimi taratibu nikatoka,nikijua nimetimiza wajibu wangu ...kazi nyingine yote waliimalizia wao, kila kitu kikawa wazi, muuaji akajulikana, na ushahidi wote ukapatikana,mtoto na mama yake, ndio waliomuua Makabrasha,...’akasema huku akimwangalia mwenyekiti.

‘Inatosha, tunakushukuru sana, mengine yote, tunayafahamu kwa wale waliokuwa wakifuatilia hiyo kesi na kuhudhuria mahakamani, kuwa wahalifu hawo, wanatumikia jela zao, haki imtendwa, iliyobakia ni sisi kama familia, tutimize yale yanatuhusu, na kusuluhisha tatizo la familia hii, kama wazazi ni lazima tutimize na sisi wajibu wetu,..’akasema mwenyekiti.

‘Sasa ni ajenda yetu ya mwisho kama nilivyosema…, ajenda hii ni hukumu, au mstakabali wa ndoa ya mke na mume wa familia ....na hapa mimi sitaingilia sana, maana wanandoa waliosababisha hiki kikao wapo hapa, na walishapata muda wa kukaa pamoja na kulijadili hili, nasikia bado kuna mvutano, ...sasa mimi kama mwenyekiti, nahitajika kutumia rungu langu la uenyekiti...kulimaliza hili tatizo,..., 

NB: Naona tuishie hapa kwanza.


WAZO LA LEO: Ubaya na matendo mabaya, sio sifa ya kujinadi mbele ya wenzako, kuwa mimi ni mjuzi wa ubaya fulani, watu hawaniwezi, nk....kwanini tusijisifu kwa matendo mema, tuangalie wenzetu waliobuni , na kugundua mambo ambayo mpaka leo yapo, yanatumika kwa manufaa ya jamii, ina maana watu hawo, ni kama vile bado wapo hai, ...hizo ndio sifa njema,..., 
Ni mimi: emu-three

Tuesday, March 27, 2018

MKUKI KWA NGURUWE-102



‘Ni mali zake mwenyewe ndizo chanzo cha kifo chake....’akasema sasa akionekana kulewa anajiongelea tu…

‘Kwa vipi, mbona sikuelewi,....mbona unapenda kuongea kimafumbo-mafumbo...maana mimi nijuavyo mali ni utajiri unaokufanya upate kile unachokitaka, sasa ilikuwaje mali zake mwenyewe zimuue huyo marehemu...?’ nikamuuliza.

‘Kutokana na mali zake kulitokea kutokuelewana yeye na familia yake ya pembeni…unaonaeeh….ndio hivyo watu wengine bwana..’akasema na kubekuwa…akawa anakunywa tu.

‘Kumbe alikuwa na familia ya pembeni, mke au hawara tu..?’ nikauliza

‘Ufahamu huyu mtoto sio mtoto wa mke wake wa ndoa, japo anajifanya karithi mali yote ya baba yake…ni mwizi tu huyu, …, yeye alizaliwa nje ya ndoa, mama yake alikuwa hawara wa marehemu…kuna mtoto halali alitakiwa ndiye arithi, lakini huyo mtoto haki mali ya dhuluma, kaacha kaondoka zake..’akasema kama kumnyodoa bosi wake.

‘Nyie wanaume jamani…kwanini lakini’nikasema hivyo, na yeye akaendelea kuongea.

‘Sasa huyo aliyekuwa hawara yake eeh…, akawa anamfunda mtoto wake, kumfisidi baba yake, hebu fikiri mama anamfundisha mtoto wake kumuibia baba yake na si kumuibia tu…unajua nikuambie kitu eeh...mwanzoni mtoto huyo alikuwa hataki, maana namfahamu hata tukakosana kwa hilo…’akatulia

‘Nilimuambia achana na mawazo ya mama yako, weeh, ukitaka ukosane na huyo jamaa mtaje mama yake, akanijia juu kweli, tukawa hatupatani tena mimi nay eye, sikujali..lakini ukweli nilimpa…sasa wanaume nao bwana,…Marehemu alikuwa kichwa lakini wakati mwingine namlaumu…’akatulia

‘Unajua walikuka kukosana baba na mtoto wake kwenye mambo ya …kuandikisha mirathi, si ujinga huu jamani, utaandikishaje mirathi hujafa eeh,..hilo lilimponza huyo jamaa…mtoto akaona, kwanza….eeh nimekumbuka, kwanza baba kwa kupenda alimuandikisha mtoto..kuwa ndiye mrithi mkuu…’akatulia

‘Baadae baba kapata mawazo huku na kule akagundua kafanya makosa, sijui madawa aliyowekewa yalishakwisha, akabadili mirathi,..hapo sasa ndio mambo yakaharibika….mtoto akawa haivani na baba yake…mtoto akawa sasa anamfuata mama yake kile anchotaka kumfisidi baba yake….’akafunguka hivyo

‘Mungu wangu kwahiyo mama akamtuma mwanae afanya mabaya,…ina maana gani hapo…kuwa ndiye alimtuma akamuue baba yake au…?’ nikamuuliza

‘Wewewe…sijasema hivyo mimi…unajua uhuni ni mbaya sana, ukifanya haya mambo kwa siri….haya eeh, hayaaah…nasema taratibu, haya…, ipo siku siri hiyo itakuumbua, marehemu ana watoto wengine, lakini hawo wengine hawana matatizo, tatizo lipo kwa huyo mtoto wake aliyemuona ni kichwa chake...’akasema

‘Kwahiyo alimpenda sanaa mtoto wake huyo…kwanini hakumlinda baba yake asiuwawe..?’ nikauliza

‘Subiri nikuambie sasa…huyo mtoto na mama yake, wakawa sasa hiki….’ Akaonyeshea kwa kidole..

‘Umenielewa hapo…kitu kimoja, sasa wakawa na ajenda moja ya siri,...huku wakijipendekeza kwa marehemu kuwa wanamjali wanampenda, siunajua tena ile ya kujipendekeza.....mimi hilo nalifahamu sana….’akahema kidogo

‘Nahisi kama nimelewa haraka, sio kawaida yangu …lakini usijali…unajua eeh, mimi nilijaribu kumuonya mzee, lakini …watu wengine mimi namshauri kwa nia njema, anakuja kunigeuka kuwa mimi ndiye nawachonganisha,..mimi najali maisha yake na uhai wake, leo hii naonekana mbaya, lakini, sawa maana mimi si kibarua tu…hajui jinsi gani nilivyohangaika naye..’akasema akilegeza domo.

‘Kwahiyo unataka kusema nini, kuwa mtoto huyo huenda ndiye alimuua baba yake au sio, na wewe uliona kwa vile alishakuudhi ukaachia tu, au njama hizo na wewe ulihusika…?’ nikamuuliza lakini hakulijibu hilo swali moja kwa moja.

‘Mimi na mzee tulihangaika naye sana kuweza kufikia hapo alipo, nilijitokea nafsi yangu kumlinda, ndio maana mzee aliniweka karibu sana,…na nilijua mimi nitakwua kama mtoto wake,…ile mirathi ya kwanza alinipa mali, lakini alipobadili, sikuweza kuona jina langu,…watanificha nini wakati mimi naona kwa kiona mbali,  hakuniweka, iliniuma sana..unajua kuumia, niliumia, nika-fikia kuapa, nitamkomesha, unajua tena…’akasema

‘Oh,…kwahiyo…ukapanga mbinu za kumuua huyo mzee, sasa nimeshaelewa, kumbe, lakini kwanini ulisahau fadhila,  au..?’ nikauliza

‘Unajua haya mambo yasikie tu….kuna watu wanajua kucheza na vichwa vya watu, watu wanapanga mambo wakiangalia matukio…wakajua kuna mambo nikifanya hivi watu wataegemea huku..unaona, …sasa mmh, mimi nahisi kulewa, kwanini leo imekuwa hivi..’akashika kichwa.

‘Kumbe …wewe ni mtoto wa pombe…’ nikasema

‘Mimi…weeeh, hata nikikesha,…nipo imara kabia, na …tukienda kustarehe, utakimbia…’akasema

‘Kustarehe..kupi tena…’nikasema

‘Hahaha, usijali…leo tunywe tu, wewe si rafiki yangu eeh, nimeshakupenda, wewe utakuwa mke wangu..unasemaje…’akawa sasa anajiongelea nikaona hapa nikichelewa gari linaweza kuzimika kabisa.

‘Tunywe huku tunaongea, au…?’ nikauliza

‘Ni wewe tu…mimi ni wako au sio…’akasema

‘Sasa hebu nikuulize maana hii hadithi, inafurahisha sana…’nikasema

‘Hadithi gani…?’ akauliza

‘Si ya marehemu na mali yake iliyomuua…’nikasema

‘Hahaha…ndio hivyo, ndio maana nasema mali yake mwenyewe ndiyo ilimuua,…mali na watoto, unaona, na watoto wenyewe wa nje ambao, wanajali mali tu…’akasema

‘Haiwezekani ina maana mtoto ndiye aliyemuua mzazi wake, kwasababu ya mali, haiwezekani...ungelisema mke, hapo ningelikubaliana na wewe, maana sisi wanawake, tukiamua jambo, tunaweza…’nikasema

‘Mhh, unaonaeeh,…hata huyo mtoto alibadilika kutokana na mama yake, sio yeey..mwanzoni alikuwa mtu mnzuri tu… lakini, mama..maana mama alijua mzee akiondoka atapatia wapi mali, kwahiyo cha muhimu ni kuwahi…akamfunda mtoto, umeona hapo…’akasema

‘Kwahiyo..ikawaje..?’ nikauliza

‘Unajua…  tuyaache hayo maana jamaa ana msikio, na tukiongea kwenye hili jengo jamaa atakuwa anatuona, na kutusikia, kwahiyo, ngoja ....’akasema na mimi nikamkatisha na kusema;

‘Kama anatuona na kutusikia, mimi siwezi kukaa hapa, wewe uliniambia hapa ni sehemu ya usalama, kumbe kuna watu wanatuona, hapana, wewe hunitakii mema,mimi naondoka zangu...’nikajifanya kutoka kuondoka.

‘Hahaha…sikia bwana, humu ndani kawezeka vitu vya kuona matukio, uliniona wakati naingia nilifanya nini…taaaa…nikazima ule mtambo, kwahiyo hapo alipo seehmu hii hawezi kuona kitu, kesho atagomba, lakini..ndio hivyo…’akasema

 ‘Hili jengo ni la ajabu sana…kuna vitu vingi eeh ina maana kuna mitambo ya matukio, kuna mitambo ya ulinzi, …kwanini sasa marehemu akauwawa kirahisi hivyo…?’ nikauliza

‘Ni kweli mambo ya ulinzi yalikuwa mikononi mwangu, mimi najua kila kitu kuhusu ulinzi wa humu ndani..unajua kuna kipindi marehemu alimchukua binti mmoja, yule binti alikuja kuharibu mitambo yote…imechukua muda kuijenga upya, lakini bado..na nafanya hivyo makusudi kumkomoa huyu bosi wangu mpya…’akasema

‘Juu kuna sehemu nyingine au sio…?’ nikauliza

‘Yah…ipo lakini imekodishiwa watu wengine sisi makao yetu ni huku,…huku anamiliki mwenyewe bosi na mambo yake,…juu ni mradi wake wa kuingiza mapesa,..huko juu hawajui kabisa kuhusu huku chini…’akasema

‘Ina maana ukiwa huko juu, huwezi kuteremka huku chini..?’ nikamuuliza

‘Kuna chumba kama store,…kimejengwa ovyo ovyo..ni mbinu tu, ukifungua humo huwezi kujua siri yake, sasa humo ndio kuna ngazi za kushuka chini, unafungua mlango…unateremka, watu hawajui, hizo ni mbinu nilimfundisha mzee, zinatoka izraili…nilijifunza huko, hahaha…’akacheka sana.

‘Kwahiyo huku chini mnatumia kwa kazi gani…maana sioni watu wengi, …?’ nikauliza

‘Starehe na biashara haramu…na umalaya tu , huyo mtoto ndio zake, akitaka kufanya shughuli zake za haramu, ni huku..akitaka kumtesa adui yake ni huku, akiteka watu watu ni huku …hakuingiliki ovyo…nimekuingiza wewe kwa vile tu..nakupe-ndaaa…’akataka kunishika
‘Ohh, sory….’akasema nilipomkwepa.

Ilibid nibadili muelekeo wa kumuhoji kwanza, kwasababu kwa maelezo yake hayo, huku kutakuwa na siri nyingi sana, ambazo zitasaidia kama ushahidi, sikutaka kwanza kushinikiza kufahamu muuaji wa Makabrasha, nilijua hilo litafikia muda wake.

‘Kwahiyo huku kuna siri nyingi sana za marehemu au sio…?’ nikauliza

‘Marehemu keshaondoka, sasa hivi ongelea siri za bosi mpya,…kuna vyumba vingi tu, kila chumba kina mambo yake, ..mimi kila kitu najua,..hanibabaishi mimi..’akasema

‘Sasa hebu niambie ni nani aliyemuua huyo jamaa wa watu, maana naanza kuingiwa na hamasa ya kumtambua huyo marehemu na familia yake, wakati mwingine unaweza kujifunza kutoka kwa familia za watu wengine au sio...?’ nikaanza kumchota tena kuhusu mauaji...

‘Hiyo familia achana nayo, ni familia ya laana, walichokitenda hawataweza kuishi kwa amani, nikuambie ukweli, pamoja na utajiri wao wote, bado wanaishi kwa majuto, na wakati mwingine nasikia huyo jamaa analia na  hata kupiga makeleke usiku...’akasema

‘Ni nani analia, ....?’ nikamuuliza

‘Si huyo mtoto wa marehemu, wewe unacheza na damu za watu...’akasema

‘Ina maana yeye ukimkosea tu anaku-ua, ..mbona unanitisha…?’ nikauliza

‘Upo na mimi,…mimi nilikuwa mlinzi hodari wa mzee, sasa wa kijana wake, wananiamini, mimi sio mchezo, …’akasema akijipiga kifua

‘Kwanini anaweweseka usiku…kaua watu wengi au…?’ nikauliza

‘Laana ya watu waliowaua..na zaidi laana ya mzazi wake yeye mwenyewe…’akasema hapo nikaona hajasema ninalotaka kulisikia.

‘Lakini huyu mtoto alimpenda sana baba yake au sio, sasa iweje apate laana…?’ nikamuuliza

‘Hivi unafikiri mzazi ni mchezo…hata kama asipokutamkia,..kama wewe umaimwaga damu yake, si lazima utapata laana yake…’akasema
‘Ni kweli kama alimuua baba yake ni lazima atapata laana yake …’nikasema

‘Ndio maana halali…anaweweseka….’akasema

‘Una uhakika gani kuwa yeye ndiye aliyemuua baba yake?’ nikamuuliza huku akimimina kinywaji...

‘Uhakika sikuwa nao mwanzoni, lakini nilikuja kuangalia mkanda wa matukio, niliouchukua pale ofisini kwa Makabrasha, yeye mwenyewe aliniambi siku nikisikia kafa, nifungue sehemu moja ya siri, iliyokuwa chumbani kwake, nitoe hicho kifaa cha kuhifadhi matukio ya hilo jengo, nimpe mtoto wake mkubwa..’akaniambia.

‘Kwanini alikuambia hivyo, ina maana alishafahamu kuwa atakufa?’ nikamuuliza

‘Watu kana hawo, hujihami tu, ...na sijui kwanini, nahisi kama alishatabiri kifo chake kwani siku ile ya mwisho aliniambia, niondoke, ila nikisikia lolote limetokea, nisisahau kufanya kama alivyoniagiza, na mimi nikamuitikia, na niliposikia kuwa amekufa cha kwanza kukifanya ni hicho, nikafungua sehemu hiyo ya siri ma nikachukua hicho chombo, na alipofika huyo mtoto wao mkubwa nikamkabidhi...

‘Ina maana huyo mtoto wao mkubwa anafahamu ni nani aliyemuua baba yao?’ nikamuuliza.

‘Kile chombo kilikuwa kinachukua matukio ya mle ndani ya ofisi na mazungumzo yake na watu mbali mbali, na muuaji, alijitokea mara moja akiwa kavaa nguo za kuficha sura, kwahiyo sizani kama huyo mtoto wake anamfahamu huyo muuaji...,mimi niliwahi kuchukua kile ambacho hakikuwa wazi, ambacho mitambo yake ndio ipo huku chini,

‘Sasa wewe ulifahamu vipi kuwa muuaji ni nani?

‘Wewe unauliza sana maswali, kama polisi, tunywe, tustarehe, tusahau machungu ya dunia, unasemaje...’akasema huku akinisogelea akitaka kunibusu, nikawa natumia mbinu za kumweka mbali, ili niaweze kupata taarifa muhimu, nikasema;

‘Kuongea pia ni sehemu ya starehe, niambie kwanza,una wasiwasi gani, umeshasema huku hakuna mtu anayeweza kutuingilia, tuongee, ili tujuane vyema, mimi sipendi mpenzi mwenye papara au ndio zenu za hit-and run...’nikamwambia.

‘Aaa, bwana, wewe umesema una mcumba, hata nikikufahamu vyema itasaidia nini, leo ok, nimekuelewa, tutakuwa tukikutana hivi kwa siri au sio, ...’akasema.

‘Unajua mimi nina tatizo moja, ukiniambia jambo likanivutia, natamani kulifahamu vyema, na mimi nimekupendea kwa jinsi unavyoweza kuchunguza mambo na ujanja mwingi, …’nikasema

‘Hapa uemfika kila kitu najua…’akasema

‘Sasa wewe mwenyewe umenugusia maisha ya huyo marehemu yamenivutia sana, niambie wewe ulimgunduaje huyo muaji wa marehemu kwasababu mimi ulivyonieleza, naweza kukuhisi kuwa wewe huenda ndiye uliyemuaa huyo marehemu, ?’ nikamuuliza

‘Hapana mimi nisingemuua tajiri wangu, ili nipate nini, mimi siku ile niliondoka mapema niliposikia mke wangu kashikwa na uchungu, na nikapigiwa simu kuwa tajiri yangu kapigwa risasi, nikaja kwa haraka, na cha kwanza ni kufanya kama alivyoniagiza mimi nifanye nikatimiza…’akasema,

‘Kwahiyo kumbe hata wewe humfahamu vyema huyo muuaji wa marehemu , unafanya kukisia tu, na ujanja wote huo, ulishindwa kumfahamu muuaji wa bosi wake, au unaogopa kuniambia...?’ nikamuuliza

‘Kwakweli mwanzoni nilikuwa nachanganyikiwa hata mimi , kwa asilimia kubwa nilikuwa nawatuhumu  watu wawili, ...kuna jamaa mmoja, alikuwa anafika fika sana na ni rafiki wa marehemu namfahamu sana, japokuwa alikuwa mgonjwa,..siri zao nazifahamu…’akatulia

‘Nilishangaa mtu mgonjwa, anawezaje kufika hapo…nikachunguza nikajua watu hawa wapo kitu kimoja..huyu mtu wakawa hawaelewani, unajua siku ile mitambo ilizima kama isingelizima ningeligundua kila kitu..,..., hata siku ile wakati naondoka, huyo jamaa alikuwa ameshafika....yeye nikamtuhumu sana, polisi hawakufaamu kuwa mtu huyo aliwahi kufika hapo mimi nilikuwa najua...’akasema.

‘Mtu gani huyo wewe ulimgunduaje?’ nikauliza

‘Mimi na marehemu siri yetu ni moja, ....aah, achana nye huyo, ila kulikuwa pia na dada mwingine, ni mtu wa karibu na huyo marehemu , nilimshuku sana, nakumbuka hata wakati naondoka, niliongea na mtoto wa marehemu, huyo mtoto wa marehemu akaniambia niwe makini sana na huyo dada, kwani kamshuku anaweza kufanya jambo baya kwa baba yake....’akasema.

‘Mhh, kwahiyo....?’ nikataka kumuuliza swali, lakini akanikatiza na kusema.

‘Hawo wawili niliwatilia mashaka sana, nikajua wao ndio walishirikiana kumuua Bosi wangu mpendwa....’akasema

‘Kwanini uwatilia mashaka hawo watu wawili…?’ nikamuuliza.

‘Kuna mabishano ya mara kwa mara ya watu hawo, na kulikuwa na mambo ya mikataba yao ya siri, walikuwa hawajaelewana, nikajua ni yale mambo ya marehemu ya kuwabana watu ili apate pesa kutoka kwao, japokuwa nilikuwa nawafahamu hao watu, lakini mambo mengine kama siri za mikataba yao alikuwa haniambii, .....’akasema.

‘Kwahiyo ikawaje tena usiwashuku watu hawo?’ nikamuuliza.

‘Siku moja, nilifika nyumbani kwa huyo bosi, wakati nafika mlangoni,  nikawasikia,, ...mtoto alikuwa akiongea na mama yake,...hiyo sehemu nimeirekodi,  siunajua tena mitambo ipo wazi wakati wote,hawakufahamu kuwa mimi nipo hapo mlangoni,, na wakawa wanaongea jinsi gani wataweza kuisafisha damu ya marehemu, kwani mtoto alikuwa akisema alikuwa akimuota baba yake akimjia mara kwa mara

‘Mimi nitakutafutia mtaalamu atakusaidia...lakini usije ukajiweka roho juu, kuwa marehemu anakujia, hizo ni ndoto tu, unasikia mwanangu....’mama akamwambia mtoto wake

‘Lakini naota ndoto za kutisha, najuta kwanini nilifuata ushauri wako, mama sizani kama nitaweza kulisahau hili, nilikuwa nampenda sana baba...’akasema huyo jamaa kumwambia mama yake

‘Kama usingelifanya hivyo, ungeliwezaje kumiliki hilo jengo na mali za marehemu nishukuru sana mimi kwa kukushauri hivyo, ...;akasema huyo mtoto.

‘Mama mimi sitaweza kulisahau hilo tukio,japokuwa tumelifanya kwa makini na hakuna anayeweza kutushuku sisi, labda huyu mlinzi wetu , nina wasiwasi kuwa atakuwa katuhisi, kwani nilipochelewa kumpa zile pesa zake, aliniambia anafahamu kuwa sisi huenda tunahusika na kifo cha baba,.....’akasema.

‘Atafahamu vipi, kwani siulisema uliharibu kumbukumbu zote kwenye ule mtambo wa kunasia matukio,..’mama akasema.

‘Kuna ule mtambo wa chumba cha baba, ….unajua ile ni siri ya baba, niligundua kuwa pale pia panachukua matukio, na siku nilipofika sikukuta kitu, ina maana kuna kitu kilichukuliwa, sasa nina wasiwasi na huyu mlinzi, ..kitu ambacho kinanitia wasiwasi...’akasema

‘Kama ni hivyo, kwanini asimfuate huyo marehemu ....kwasababu akibakia hai, hutakuwa na amani...’akasema mama.

‘Tukianza hivyo, tutaua wengi, kwasababu hata yule mwanadada aliyekuwa akifanya kazi na mzee, pia na yeye anadai ana ushahidi huo huo , na yule ni hatari zaidi ya huyu mlinzi wetu, huyu mlinzi wetu, ukimpa pesa atanyamaza lakini yule mwanamke, hawezi kufanya hivyo, na amekuwa akihangaika kumtafuta muaji, ...’akasema.

‘Kama ni hivyo unafikiri tutafanya nini, ....ni kuwamaliza mmoja baada ya mwingine kwa mbinu zetu…, sio lazima kwa kifo cha hapo hapo, tunaweza kutumia sumu,...na ajali za kawaida tu, hilo niachie mimi, wewe hakikisha huyo mlinzi, unamweka sawa...’akasema mama.

‘Basi niliposikia hivyo, sikuwa na amani....cha kwanza nilichofanya ni kwenda kuangalia kile kifaa nilichokichukua kwa marehemu, ....nilikuwa sijapata muda wa kukiangalia mwanzo hadi mwisho, ndipo nikagundua ukweli...kumbe...ndio yeye aliyefanya hivyo...’akasema an kutulia.

‘Nikagundua kuwa kumbe nina ushahidi mzuri sana, nikawa nawaza nifanye nini, niwaambie polisi, nikaona hapana muda bado wa kufanya hivyo...

‘Nikahakikisha ule ushidi nimeuweka sehemu ambayo hawataweza kuupata, kwanza nilitaka niutumie kutajirika, baada ya hapo, kama watanizid nguvu, nawakamatisha kwa polisi,..ndio sasa wameanza kunijali, nafahamu wanatafuta mbinu kuupata huo ushahidi nilio nao, halafu waniue, lakini nilimwambia huyo jamaa akiniua na yeye ajue anakamatwa...’akasema.

‘Kwa vipi sasa....akikuua, polisi hawajui kuwa unafahamu siri zako..’nikamwambia.

‘Nimeziweka mahali ambapo, hawataziona, na nimeshatayarisha taarifa yangu, nikaiweka mahali ambapo, nikifa tu, itasambaa...kuwepo kwangu hai ndio naweza kuidhibiti isivuje…mimi ni mtaalamu usinione hivi..’akasema.

‘Sasa kwanini uishi maisha ya hatari kihivyo, waambie polisi, utakuwa umejiokoa, kwasababu kwa hivi sasa unafanya makosa, polisi walifahamu kuwa unamfahamu muuaji na una ushahidi umeuficha, utashikwa kama na wewe ulihusika, waambie polisi, uoshe mikono yako....’nikamwambia.

‘Mpaka nihakikishe nimekipata ninachokitaka, wana mali nyingi sana,na pia wameharibu, urithi wa baba yao, kwenye huo urithi, mimi nilitakiwa kupewa sehemu ya mali, kwani mimi mzee yule alinithamini sana, sasa nimewaambia ili hayo yaishe, wanijengee jumba la maana, na liwe na miradi, ili niweza kukaa hapo na kusahau kila kitu...’akasema

‘Wameshalitimiza hilo?’ nikamuuliza

‘Wameanza, nimepata kiwanja, na tayari ujenzi umeanza, sina wasiwasi, ndio unaniona na mimi nastarehe, kama alivyokuwa akifanya yule mzee, yule, ..kwasababu mzee, alikuwa akinijali, wao wakajifanya wanaanza kunisahau...’akasema.

‘Kwenye huo mtambo, hakuna ushahidi unaoweza kuwakamata hawa watu kuachilia mbali huo ushahidi ulio nao wewe?’ nikamuuliza, nikamuona keshachoka na maswali, akasema ...

‘Wewe sasa unauliza maswali mengi, ...hebu njoo hapa nikuonyeshe..’akasema na tukatoka hapo akanipeleka kwenye hicho chumba chenye mitambo ya usalama, mimi sikuwahi kukisia kuwa chumba hicho nacho kina mitambo hiyo, kilikuwa chumba, kama stoo, lakini kwa ndani kuna chumba kingine, na humo kuna mitambo kama ile ile ninayoifahamu mimi, usingeliweza kuligudua hilo.

‘Unaona hapa, hapa kuna mitambo, ambayo haijawahi kuzimwa, ile ya juu, inazimwa mara kwa mara, lakini hii ipo wakati wote, na anayeusimamia huu mtambo, ni huyo mtoto wa marehemu, akifika, anahifadhi kumbukumbu zote za siku, na kusiweka, mahali pa usalama, kwahiyo hilo tukio analo yeye, na sizani kama atakuwa hajaharibu hiyo sehemu.

‘Sasa wewe uliwezaje kuipata hiyo sehemu?’ nikamuuliza.

‘Si nimeshakuambia kuwa ,Marehemu alikuwa anafahamu hayo yote, kwahiyo kule kwake, kuna mtambo mdogo, wenye mawasiliano na huku,..kila akifika, anaangalia, anawasiliana na huu mtambo mkubwa, anajua ni kitu gani kilitokea, hakuwa na haja ya kufika huku.

‘Kwahiyo wewe ulipofungua, kama alivyokuelekeza mzee, ukaona tukio zima..hukumwambia mtoto wake mkubwa?’ nikamuuliza.

‘Nilipokichukua, sikuwa na haraka ya kuangalia kila kitu, nilikuja kukiangalia baada ya kusikiliza hayo mazungumzo kati ya mtoto wa marehemu na mama yake,siku ile...ndipo baadaye nikaenda kukiangalia kwa makini, ndio nikaoana tukio lilivyokuwa...aliiingia kwa njia hiyo tuliyoingilia sisi pale pale…umeona eeh…, akajibadili, akavaa kama mafundi, akajifunika uso mzima, usingeliweza kumtambua...akaenda chumba cha yule mwanadada,akachukua bastola...

Hapo hapo….polisi mpoo….akilini nikawa nasema hivyo!

Tuendelee…

WAZO LA LEO: Hakuna siri hapa duniani…kila mtenda mema atakumbukwa kwa wema wake, na kila mtenda maovu atakumbukwa kwa uovu wake, usijifanye wewe ni mjanja sana wa maovu, ukafikiria siri zako hazitagundulikana….unajidanganya,… uovu, dhuluma,ukatili unanuka kama mzoga, japokuwa hatuhisi harufu yake…lililojema ni kutubu, kwa toba ya haki na kumrejea mola wako….



Ni mimi: emu-three

Monday, March 26, 2018

MKUKI KWA NGURUWE-101


‘Ndugu wajumbe hiki ni kikao cha hitimisho cha kikao kilichopita, kama mnakumbuka vyema, kikao kilichopita tulikikatisha kutokana na muda, na pia wajumbe walishachoka, na pia tukaomba wale wajumbe waliotarajia kusafiri waahirishe safari zao, lakini kutokana na mambo yaliyokuwa juu ya uwezo wetu, mengi hayakufanyika kwa wakati, kama mlivyoona wenyewe,...sintofahamu iliyotokea na baadhi ya wajumbe wa kikao hiki wakakamatwa.....’Mwenyekiti akaanza kuongea.

‘Poleni sana kwa mkasa huo, kama wanafamilia sote lilitugusa, ndio maana tulikuwa bega kwa bega kuwaombea dhamana wale waliokamatwa, lakini tulikataliwa kutokana na pingamizi za wanausalama hao...’akaendelea mwenyekiti.

‘Wakati mwingine tunaweza kuwalaumu polisi kwa jitihada zao, tukaona kuwa wanatusumbua, wanatumia mabavu nk, lakini wakati mwingine inakuwa haina jinsi, kwani  raia ambao walitakiwa kutoa ushirikiano, wanakuwa wagumu, wanaficha ukweli kwasababu zao binafsi, na hapo ndipo polisi wanapoamua kutumia nguvu...na wakati mwingine wanafanikiwa, au sio..'akasema mwenyekiti, na wajumbe wakikuwa kimia.

‘Siwezi kuwalaumu sana wale mliofanya hivyo, lakini kuna mambo ambayo nataka kuyaweka wazi kama wanafamilia, huenda wengine hawatanielewa, lakini ni vyema nikaeleza sera na taratibu za familia hii, mimi bado ni mwenyekiti wake, na kama bado mnanitambua hivyo, ni lazima nisimamie yale mamlaka ya kifamilia yetu hii kuu...’akatulia.

‘Katika familia hii, tumejitahidi sana kuwa mbali na kashifa,...na hili nimekuwa nikilirudia mara kwa mara katika kila kikao, na kile anayekuja kuoa kwetu, au tukimleta muolewaji hapa, ninajaribu kuwaasa kuhusu hili, lakini hali inazidi kubadilika, ...sijui kwanini, labda ndio karne hii ilivyo.

Kiukweli hili lililotokea limetutia doa kubwa, na sijui tutafanyaje ili tutaweza kujiisafisha, japokuwa tumesalimika kihivyo...mimi sitaacha kulisema hili...sikufurahia na kitendo hiki kabisa,, nawaonya tena, hili lisijirudie. Hatutaki kashfa kwenye hii familia, mnasikia…

'Ndioooh..'wajumbe wakasema

‘Hebu niwauliza ni nani anayependa kukaa jela, hivi jela ni kuzuri,....hivi ni nani anapenda kukaa na wasiwasi, akakosa raha na amani akawa anaishi kwa mashaka-mashaka, hakuna anayependa kuwa hivyo, sasa kama hatupendi  kuwa hivyo, kwanini tujiingize kwenye yale mambo ambayo tunayaona yanaleta kashfa, yanatuweka katika hali ya kukosa amani na usingizi, kwanini....?’ akawa kama anauliza.

‘Ndio maana katika familia hii tunalipinga sana hilo..., na wale wanao-olewa au kuoa ndani ya familia hii, nimewaonya na nitendelea kuwaonya tena na tena, hatutaki kashifa, na kama una dalili na mienendoo hiyo mibovu,...tutakusakama, mpaka ubadilike, au uondoke wewe mwenyewe maana hutufai.

‘Sasa basi, tunaanza kikao chetu, na ajenda moja kubwa, ni hitimisho ya ajenda muhimu ya matatizo ya familia husika…tunaweza kuiita ni ajenda ya hukumu. 

Lakini kabla ya hukumu, ningelipenda tuliweke wazi tukio zima lilivyokuwa, najua kila mmoja ana dukuduku la kufahamu ni nini kilitokea, ni nani hasa muuaji wa Makabrasha, huyu mmuaji kapatikana au bado.

Tunashukuru mungu kuwa wajumbe mpoo,..nani hayupo, maana kama kuna mtu hayupo ujue bado yupo na wenyewe polisi...

Sasa bila kupoteza muda,...nimeona hili ni muhimu, na niliongea na watu wa usalama, wakasema haina shida, tunaweza kuliongea tu,...kuwa mwenzetu mmoja hapa ambaye alishirikiana na polisi hadi kufanikisha juhudi za watu wa usalama, na tunavyoongea hapa, muuaji anaweza kuwa mbaroni, ...

Aliposema hivyo watu wakapiga makofi.

Sitaki mimi niongee hili mwenzenu ndiye ataongea hili, nasikia mahakama mahakama ilimpa onyo kwa kuingilia kazi za polis bila kibali, lakini kwa namna nyingine imemshukuru sana, na wamependekeza kama inafaa apate ajira huko huko, ni yeye mwenyewe tu.

Kwahiyo basi….tunakuomba, mke wa docta, uchukue nafasi hii utuliezee japokuwa kidogo, jinsi ilivyotokea hadi mkafanikiwa kumpata Muuaji, sasa hivi hakuna kikikwazo, kuelezea hilo au sio, au badoi haturuhusiwi maana mimi sijapewa taarifa na nilipoomba kibali cha kikao, niliambiwa niendelee tu hakuna shida...’akasema mwenyekiti,

Mke wa docta, akakohoa kidogo na kusema;

‘Mhh, naona hiyo mke wa docta, unaipenda sana mzee, hahaha, sawa sio shida, itaendelea kuwepo tu kama sifa..., japokuwa imeshafika mwisho…hata hivyo, sio mbaya, ila yupo atakayekuwa hivyo, mungu akipenda sio mimi tena....’akasema huyo msemaji, na mwenyekiti akadakia na kusema;

‘Samahani, unafahamu hilo halijawa wazi kwenye hiki kikao ndio maana tunaendelea kukuita hivyo mke wa docta, mimi kama mwenyekiti sijapata taarifa kamili, na hata kikao hiki ambacho ni wanafamilia, na wao wanahitajia kulisikia hilo....’akasema mwenyekiti

‘Kwakweli mazoea yana taabu, hata mimi mwenyewe huwa ninajisahau na kujiita mke wa docta, lakini ukweli ndio huo, na kuanzia leo ningelifurahia mkisema, aliyekuwa mke wa docta,...’akasema huku akiinamisha kichwa chini.

‘Hili msishangae, nimeamua hivyo kwa hiari yangu mwenyewe, baada ya kuona kuwa sitakuwa nimemtendea haki mwenzangu , kwa yale yaliyotokea mimi nimeona niwajibike, na kuwajibika kwa muungwana ni kuachia ngazi zu sio…na pia kutokana na kazi zangu mwenywe nimeona kuwa nahitaji kukaa mwenyewe ...maana huwezi kulazimisha jambo kama moyo hautaki.

‘Ni ukweli usiopingika kuwa tumeshamaliza taratibu zote za talaka, kisheria, na hivi mnavyoniona nipo mbioni kuelekea kijijini, huko nimeshajipanga, nina miradi yangu na maisha yangu, na nitakaa kwa muda hadi hapo nitakapoamua ni nini kingine cha kufanya, maana ukiingia kwenye hii fani, muda wote unahitajika, ..ila kiukweli kutokana na haya yaliyotokea nisingelipenda kufanya kazi za kutumwa-tumwa tena, inafikia sehemu unajizalilisha,...ndio kazi…, lakini jamii haiwezi kukuelewa, sasa hivi nataka kujituma, na kujiajiri....’akasema .

‘Kwanza kabisa nawaombeni sana radhi wajumbe wa kikao hiki na wanafamilia hii, kwa hayo yaliyotokea, mimi kama binadamu nimkosaji, na mkosaji anastahili kusamehewa, ...ni kweli nimekosa sana, hasa kwa mume wangu, yeye nimeshamuomba sana masamaha, na japokuwa kanikubalia, lakini bado nahisi sijasamehewa, moyoni nahisi hivyo…., maana kosa nililolifanya kwake ni kubwa sana,...’akasema huku akimgeukia docta.

Docta akatikisa kichwa kukubali tu...hakusema neno.

Naona nianze kutoa maelezo, japokuwa yameshapita, lakini kwa faida ya wanafamilia, nitaelezea ilivyokuwa;

‘Kwa ujumla aliyemua Makabrasha ni mtalaamu wa hali ya juu, alifanya hilo jambo kwa kuangalia nyakati, ..., na aliyapanga hayo mauaji kwa utaalamu wa aina yake...ilikuwa vigumu sana kumnasa, kwanza alienda na muda na pili akawa anatumia madhaifu ya watu, na kuyachanganya na matukio, kiasi kwamba polisi walifikia kuhisi huyu au yule, bila kupata ushaidi kamili.

Hata mimi mwenyewe sikuwa na uhakika na kile nilichokuwa nikikiwaza kwani hata yule niliyemuwaza kuwa ndiye, mwisho wa siku nilijikuta nakosa ushahidi kamili, na hata nilipotoa wazo kwa polisi, wao walishia kuniona mimi ndiye muuaji.

Wao walishakusanya ushaidi wao wa kutosha kwa muuaji, kuwa ni mimi , nikishirikiana na mume wa familia, kwani mimi ndiye niliyekuwepo kwenye hilo jengo, na silaha niliagiza mimi, na silaha iliyotumika nilikuwa nayo mimi, na sababu za kumuua marehemu nilikuwa nazo mimi, na nilishawahi kutamka kuwa nitafanya hivyo......

Mwishowe nikapewa mimi jukumu la kumpata huyo muuaji, kama sio mimi, kilichonisaidia ni kuwa humo ndani ya watu wao kuna watu wananifahamu japokuwa ni kwa siri kubwa, na wananiamini,..pia  nafahamu sheria na jinsi ya kujitetea, na kwahiyo hawakuwa na jinsi bali ni kunitumia mimi.

Kwa pamoja tukafanya jambo lililoshindikana.

**********

Kwanza niliwaambia ili kumpata huyo muuaji, kwanza tumchambue huyo mtu, aliyefanya hayo mauji, anaweza kuwa na sifa gani,… kwani mimi nilikuwepo humo ndani, na mazingira ya humo ndani nilishayasoma karibu yote.

'Humo ndani hawezi kuingia mtu akafanya mauaji kama hayafahamu mazingira ya humo..'nikawaambia

'Maana kuna vifaa vya hali ya juu vya kuhisi silaha...kuna walinzi wa seehmu ya kuingilia na walinzi wa nje wasiojulikana wapi walipo, wanatumia mitandao tu, kwahiyo ni lazima mtu huyu alifahamu hilo, pili awe,analifahamu hilo jengo vyema kiramani.., maana mauaji hayo yalifanyika kwa muda mfupi, na kwa tahadhari ya hali ya juu, ...

Niliwaambia kuwa mtu huyo inaonekana kama alipita mlangoni ni mtu nayefahamika, na hata walinzi hawakuwa na shaka naye, 'kama alipitia mlangoni,..', na angelipitia wapi maana mlango ni mmoja na mlangoni hapo ndio utaruhusiwa kwenda juu au chini,..

Jengo hilo lina juu na chini, watu wengi hawafahamu hilo...na sehemu ya chini haitambulishwi kabisa, zaidi ya marehemu na watu wake maalumu.


Nikawaambia huyo muuaji, alipomaliza hiyo kazi atakuwa alikimbilia vyumba vya chini na kukaa huko hadi hali ilipotulia, ...na ina maana huyu muuaji ana chumba maalumu cha kujificha huko chini, sasa ni nani anayelifahamu hilo jengo vyema, zaidi ya Makabrasha na mjenzi wake....hapo ikawa kazi kumtafuta mtu anayejulikana kuwa analifahamu hilo jengo vyema, ..

‘Lakini pia mtu huyo awe anafahamu mtandao wa ulinzi wa lile jengo, awe anaweza kuusimamia huo mtandao, bila watu kujua, na awe anaweza kuona ni kitu gani kinafanyika ndani ya hilo jengo, ina maana basi kwasabbau hii huyo mtu hawezi kuwa ni mmoja, ni lazima walishirikiana watu wawili....

‘Kwa hoja hizo, hakuna zaidi ya Makabrasha mwenyewe,..’wakasema

'Mimi nina tetesi na watu watatu, ...'nikasema

'Kwa uchunguzi wangu niliwachuja mpaka nikabakiwa na watu watatu, mjenzi wa hilo jengo, mtu wa karibu wa Makabrasha na mtoto wake Marehemu, kati ya watu hao nahisi mmoja atakuwa anahusika, au wawili walikula njama ya pamoja.lakini huyo wa tatu hana nguvu, …huyu wa tatu namuondoa

'Mjenzi wa hilo jengo nilishamchunguza sana nikaona kuwa haweza kufanya kitu kama hicho, tunabakiwa na watu wawili ninaowafahamu mimi …’nikasema

‘Tuambie ni nani na nani

‘Mmoja ni mtu aliyaminika sana na Makabrasha, na huyo ni mtu mwanifu sana kwa Makabrsha, lakini huwezi kumuona akiwa karibu na Makabrasha, mtu huyu  hajulikani sana machoni mwa watu, maana hajionyeshi, kuwa ana mahusiano na marehemu.. Anayemfahamu huyo mtu kuwa ana ukaribu na Marehemu ni mtoto wake, na mimi tu

‘Ni nani huyo mtu..?’ wakaniuliza.

‘Ni mlinzi wake wa karibu, ...lakini sio wa kukaa naye !..’ nikasema

'Kwa vipi...?' wakauliza

'Huyu anamlinda Makabrsha kwa mtandao,..na akiona shaka tu anawapigia walinzi wa karibu wa Makabrasha...yeye anavyoingia kwenye jengo, wengi hawafahamu, wakati mwingine wanamuita 'mzuka'...

'Ni nani huyo...?' wakauliza

'Basi nikawatajia huyo mtu ni nani na wapi anaishi, polisi hawakutaka zaidi kwanza, wakaanza kumfanyia uchunguzi bila hata ya yeye mwenyewe kufahamu, ikaja kugundulikana kuwa ni kweli siku hiyo ya mauaji huyo mlinzi kweli alikuwepo sehemu yake.

**************

Lakini muda mchache baadae mtu huyo alipigiwa simu, mkewe alikuwa mjamnzito, akawa anahitajika nyumbani kwake kwa haraka, kumbe mkewe alikuwa mbioni kujifungua, kwahiyo akaondoka sehemu yake hiyo baada ya kuwasiliana na Marehemu mwenyewe

Na ushahidi upo, muda mwingi, alikuwa hospitalini, na muda aliotoka hapo hospitalini kurudi nyumbani ulikuwa muda ambao mauaji yalishafanyika, kwahiyo akawa hahusiki kwa upelelezi wa polisi..kwahiyo akaambiwa huyo mtoe

‘Haya tuambie huyo wa pili ni nani,....?’ wakaniuliza

‘Ni mtoto wa Makabrasha,...’ nikawaambia na wao wakaguna na kuniambia, haya tuelezee toka lini mtoto akamuua baba yake...lakini ngoja tuone,

Wakachunguza nyendo za huyo mtu kwa siku hiyo, ikaonekana kweli siku hiyo hakuwahi kufika kwenye hilo jengo, hata mimi pamoja na kumweka kwenye orodha hiyo, sikuwa nimempa nafasi ya kuwa muuaji...maana haya mimi mwenyewe nafahamu kuwa siku ile muda wote hakuonekana kwenye jengo, na kama angelionekana walinzi wangeliniambia,…’nikasema

‘Una uhakika gani kuwa walinzi walikuambia ukweli wote..?’ wakaniuliza

‘Kuna watu wangu humo humo wasingeliweza kunificha mimi,…kwahiyo yeye haiwezekani kuwa aliingia humo, atakuwa alipitia wapi, na isitoshe yeye ni mtoto wa marehemu, kwahiyo mimi siwezi kumshuku sana yeye.

‘Ni nani mwingine ambaye ana sifa hizo zote..?’ nikaulizwa

Hapo sasa nikawa sina la kusema, ina maana aliyebakia ni mimi, ....’

‘Na wa tatu ni wewe au sio....’wakasema polisi na hapo ndio walipasubiria ili kuninasa mimi

‘Ni mimi…! Hapana…sijamuua Makabrasha…’nikajikuta nimesema hivyo, na wao wakacheka,

‘Sasa nani mwingine..tuliyajua haya yote, tulitaka ujilete wewe mwenyewe na hoja zako hizo sio kwamba tulikuwa hatujazifanyia kazi, tulishazifanyia kazi, lakini tulitaka tukuone labda mwenzetu una hoja za ziada, aliyebakia ni nani, kama sio wewe..’wakasema

‘Lakini  mimi nisingeliweza kumuua Makabrasha, kama ningelitaka kufanya hivyo, ningelishamuua siku nyingi tu, na kwa namna nyingine kabisa, .....’nikajitetea.

‘Tuambie ukweli, maana wewe ulisema alikufanyia mambo mengi mabaya na ulikuwa na hasira naye na sifa zote za huyo muuaji unazo wewe kama ulivyozibainisha wewe mwenyewe.., kama sio wewe ni nani mwingine..?’ polisi wakaniuliza.

‘Mimi nataka tusaidiane kwa hili, nina uhakika muuaji yupo, na anatuchezea akili, ila sio mimi, ila yupo...ninachowaomba ni jambo moja, nipeni muda nitamtafuta huyo muuaji,wa halali…’nikasema

‘Jambo gani…?’ wakauliza

‘Kwanza…nataka ijulikane kuwa bado nipo humu rumande, muwe mnanipa nafasi ya kutoka kila ninapohitaji kutoka, ili niendelee na uchunguzi wangu, nina uhakika tutampata huyo muuaji, lakini kwa njia zangu nijuavyo mimi..nawaomba msiniingilia kabisa...’nikawaambia.

‘Hatuwezi kukuachia kwasababu sasa hivi wewe ni mshukiwa namba moja,na pili kuna tetesi kuwa kuna watu wanataka kukuua, ni tetesi, na tetesi hatuwezi kuzipuuzia,….sasa ni kwanini wanataka kukuua, ndio hapo tunamashaka...’wakaniambia.

‘Kwanini watake kuniua mimi…, kama sio kwamba wao ndio wauwaji, na sasa wameona  kuwa nilikuwa mbioni kuwafichua ndio maana wanataka kuniua, kwanini hamjiulizi hilo, nipeni hiyo nafasi, nina uhakika tutampata huyo muuaji halisi kuliko kuning'ang'ania mimi, niamini mimi, mimi sijamuua Makabrasha,..’nikawaambia polisi.

‘Hebu tuambie huo mpango wako wa kumpata muuaji,...?’ akaniuliza mpelelezi wao, nikamuambia hii kazi nataka kushirikiana na mmoja wa wapelelezi wao ninaowaaamini mimi…

‘Akina nani…?’ wakaniuliza na mimi nikawatajia, maana nawafahamu  nimeshawahi kufanya kazi na watu hao, ni wasiri wangu wa kubwa,...hata hivyo wakataka wafahamu mipangilio yangu ipoje.

‘Mimi nawaomba jambo moja, mimi nitaendelea kuwepo humu, ila muda fulani fulani nipeni ruhusa ya kutoka, na nyuma yangu wawepo hao wapelelezi, kwa kificho, wasijulikane kabisa,…’nikawaambia.

Na pili  chombo cha kuvaa ambacho, nikikivaa mtaniona kila ninapokwenda...’ wakaitana na kukaa kikao chao, wakajadiliana na baadaye wakanikubalia, lakini ni baada ya mabishano yao marefu, kwani wao walitaka kila hatua niwe pamoja nao, nikawaambia kwa njia hiyo hatufanikiwa. ..

‘Siku ya kwanza sikufanikiwa, na ya pili,….ikawa sasa kuna kukata tamaa, yaonekana mimi najaribu kupoteza muda, …ujue hadi hapo bado na wao walikuwa hawana ushahidi wa uhakika kuwa mimi ndiye muuaji...ni kwanini kuna watu wanataka kuniua mimi...ni kwanini....., vinginevyo wasingelipatia hiyo nafasi.

 Siku ya tatu, ndio mambo yakajileta, na siku zote hizo nilikuwa nikienda kwenye hoteli moja ambayo jamaa hawo ninaowashuku hupenda kwenda kustarehe hapo, na humo kuna seehmu maalumu marehemu aliweka vifaa vyake pia, ...vya kuangalia jengo lake kwa mbalia...humo kuna kila starehe, na nilijua udhaifu wao, ni pombe na umalaya...

 ‘Mimi nikajiweka kinamna, nilipewa gari, la kifahari, na pesa kidogo, nikajifanya kama binti wa geti kali, nilijibadili kabisa, na ungeniona usingelinitambua kuwa ni mimi, huwa nikiwa kazini nabadilika kabisa,....maumbile, mwendo, sauti...huwezi amini...

‘Wanaume kwa uroho wao, waliponiona ile siku ya kwanza, wakaanza kunimezea mate, maana nilitokelezea, hata ingelikuwa ni nani, angenitaka. Wakwanza nikamtolea nje, maana sikuwa na haja naye, akaja mwingine na mwingine, hadi siku ya tatu alipokuja mtu wangu ninayemtaka....

‘Mtu niliyemlenga sana na huyu mlinzi wa karibu wa Marehemu, mimi huyu nilimweka kwenye shuku zangu...

Kwa kipindi hiki, sasa anafanya kazi kwa mtoto wa Makabrasha, huyu nilikuwa bado sijakata tamaa naye, ..hisia zangu zilinituma kuwa huyu mtu atakuwa anahusika kwa namna mja au nyingine...na hasa nilipoona bado anaendelee kuwa karibu na mtoto wa Makabrasha, nikajua kuna kifo kingine kitakuja,...

Jingine hawa watu wawili, mtoto wa marehemu na huyu mlinzi walikuwa hawaivani kabisa, kipindi cha uhai wa marehemu,...walikuwa ni maadui, leo hii wanaelewana, hapa nikatilia shaka..ni kwanini....

‘Siku hiyo huyu jamaa akanijia,...nilikuwa nimekaa meza ya peke yanu nikionekana kumsubiria mtu...nashangaa mtu huyu.... na alionekana kuwa na pesa kweli, nikahisi wana jambo wamelifanya, nikajibaragua na baadaye tukaelewana, hakunitambua kabisa kuwa ni mimi, hata ingelikuwa nani, asingelitambua, ...

‘Tukaanza kuongea kidogo, moja likazaa jingine, tukawa marafiki wa muda mfupi, mimi naifahamu sana hiyo kazi, nina uzoefu nayo, jinsi ya kuwanasa hawa viumbe waitwao wanaume,..sijisifii, lakini sijawahi kufanya makosa, najua madhaifu yao yapo wapi.....jamaa bila kujijua akanasa kwenye anga zangu....sikumchelewesaha, wakati anakwenda kujisaidia mimi nikaweka kitu kwenye kinywaji chake.

‘Kuna aina ya madawa ukimwekea mtu, analewa haraka, anakuwa kama kapagawa hivi...lakini hapotezi fahamu, wanaitumia sana majasusi wanapotaka kupata taarifa kwa mtu,...niliiomba kwa watu wa usalama, wakanigaia, na hiyo ndiyo ilikuwa silaha yangu, sikutaka bastola hapo...

Aliporudii kutoka kujisaidia, nikaendelea kumelegezea, kwanza alijaribu kuwa muangalifu,…unajua tena watu waliopitia uaskari walivyo,..lakini hakunielewa, ikafika muda akajisahau na kuanza kunywa kile kinywaji,..nilimuona kama anasita lakini huyo akanywa,..mara kaanza kulegea, na akili ikaanza kumtoka, na mimi hapo hapo nikamwambia;

‘Mimi ni mchumba wa mtu, sitaki kuonekana onekana hadharani hivi, nilikuja hapa tu kupotza mawazo,…nataka kuondoka,…’nikasema

‘Oooh, hapana, usiwe na wasiwasi, kuna sehemu tunaweza kwenda hutaonekana kabisa, unasikia, unajua mimi nimevutiwa sana na wewe,…kiukweli wewe nai maalumu, unsikia, sikilizaa…twende sehemu pesa sio shida…’akasema

‘Usinihadae,…nawafahamu sana nyie waume, nikiharibu kwangu utakuja kunikimbia, na mimi sitakubali…’nikasema;

‘Kuna sehemu naifahamu, twende.....’ akasema, basi nikajifanya nimekubali kwa shingo upande.

Nikamwambia atangulie nje…nitakuja…

‘Sikiliza wewe acha gari lako hapa, huyu mlinzi wa hapa namafahmu, atakulindia kwa muda wowote unaoutaka, …au unasemaje, usijali kabisa..’akasema, na alionekana kweli kazimia kwangu

Basi tukatoka hapo kwa kupitia mlango wa nyuma, yeye akaniambia nibakie nyuma, ili yeye atangulia akaongee na mlinzi, basi akafanya hivyo, baadae nikajitokeza na tukakutana kwenye gari lake, kabla sijaingia kwenye gari lake ndio akaniuliza.

‘Huwa unafika hapa mara kwa mara..?’ akaniuliza

‘Ndio, lakini mara nyingi nafika na mchumba wangu, sema kasafiri, lakini kwa vile ni sehemu nimeizoea, ..siachi kufika, lakini ni mtu ambaye anaweza kuja ghafla,..si unajua tena…’nikasema

‘Ok..akija,…gari lipo, au sio, na sisi tukirudi nitahakikisha unaingia mlango wa nyuma,…unaonaeeh, atajua ulitoka kidogo au sio…’akasema

‘Hata hivyo sura yao sio ngeni sana kwangu…’ akasema hapoo nikashtuka ina maana keshanigundua nini..lakini nilikuwa na uhakika hawezi kunifahamu, maana kuna utaalamu wa kubadili nyusi, na rangi za macho, na nywele, sikuhitaji kuvaa ngozi bandia,...mimi katika kazi yangu hiii wanapenda kuniita kinyonga, ....naweza tukawa pamoja sasa hivi nikaingia chumbani nikitoka hunikumbuki tena....

Basi, yule jamaa akasema kwa vile naogopa, atanipelekea sehemu ambayo anaiona ni salama zaidi ambayo sio mbali na hapo.., tukaingia kwenye gari lake, na kuanza kuendesha, kama nilivyotarajia nikaona tunelekea uwanja wa ndege, nikajua ni kule kule, na mtego umefanikiwa,

Tukafika karibu na jengo la Marehemu, jamaa huyo hakulipeleka moja kwa moja kwenye maegesho ya mgari, akalipitisha kwa nyuma, hadi sehemu nyingine, kunapohifadhiwa magari ya jengo la pili yake, akachukua ufungua na kufungua geti, kulikuwa na geti dogo la jengo hilo la pili kwa nyuma....kulikuwa hakuna walinzi.

‘Huku ni wapi? Nikamuuliza

‘Huku ni kwa rafiki yangu, ila nataka tuingie kwenye hilo jengo hapo, ni la marehemu, kuna hoteli ya ndani kwa ndani, humo tutastarehe tupendavyo, huyo mchumba wako hatakuona kabisa..’akasema kwa sauti ya kuonyesha hayo dawa imemchukua na sikupenda hiyo dawa iishe nguvu kabla hatujaingia ndani.

Tulipoingia kwenye hilo geti dogo, nikaona akifungua mfuniko, kama ile mifuniko ya mashimo ya maji machafu, nikamuuliza;

‘Unafanya nini ...mbona unafungua mifuniko ya choo?’ nikamuuliza

‘Usijali hii ni njia muhimu ya kuingia ndani, hakuna anayeifahamu zaidi yangu mimi na marehemu na mtoto wa marehemu....’akasema.

‘Huyo marehemu unayemtaja ni nani?’ nikamuuliza

‘Mhh, alikuwa akiitwa Makabrasha ameshafariki....’akasema

‘Mhh, yaani kafariki na kuliacha jengo nzuri hivyo, na wewe ni mtoto wake?’ nikamuuliza

‘Hapana yupo mtoto wake, ndiye anayelimiki hilo jengo kwa sasa..’akasema

‘Na huyo mtoto wake ni nani anaonekana ni tajiri sana....?’ nikamuuliza

‘Achana naye, akikuona wewe najua ataninyang’anya anapenda sana kuninyanganya mawindo yangu...sio mtu mzuri, ...hana huruma, akikuambia utakuwa chakula cha mchwa utakuwa kweli...haogopi, ...’akasema.

‘Una maana gani..?’ nikauliza

‘Usiwe na wasiwasi upo na mimi, …najua yeye ku-ua mtu sio tatizo….sio mtu wa mchezo ila kwangu ananiheshimu, ukiwa nami hakuna shaka…hata hivyo mimi ndiye ninayefahamu siri zake…’akasema na moyoni nikasema sawa kabisa.

‘Kumbe kuna njia hii ...’ hapo nikasema kimoyo moyo…nikatulia kwanza, sikutaka kumuuliza sana, asije akanitilia mashaka, akafungua kile kifuniko na kuninyoshea mkono kuwa nisogee pale, hakufahamu kuwa mimi ni mkakamavu wa kijeshi.

‘Sasa tunaingia,…njia hii ni safi kabisa, kwa nje kunaonekana hivyo, lakini ukiaanza kuingia ndani utazikuta ngazi, unateremka nazo..hizo zinakwenda moja kwa moja hadi kwenye hilo jengo la marehemu, hii ni sehem yake maalumu ya usalama, ni njia za dharura...’akasema.

‘Oh, kwanini awe na njia za namna hii, mnauza madawa ya kulevya nini?’ nikamuuliza

‘Matajiri wengi wana mbinu zao za kuishi, wanajihami kwa kila njia...’akasema.

‘Sasa kama ni hivyo huyo marehemu alikufa kwa ugonjwa au aliuwawa?’ nikamuuliza

‘Walimua bwana,..alikuwa bosi wangu, nikiwa na shida, ananisaidia, sasa nimebakia na huyu mnyama, ananifanya kama mtumwa wake, inabidi nitumie mbinu za kumuibia, sina ujanja...kama jana nimemchomoa mamilioni ya pesa..bila hata kufahamu, akabakia kusema kaibiwa na watu wa benki...’akasema.

‘Oh kumbe walimuua, jamaa wa watu, kwanini walimuua....?’ nikamuuliza

‘Mambo ya mali hayo, unafikiri, ukiwa na watoto waroho, wanawake waroho, na una mali, ujue upo hatarini, na ikizingatiwa kuwa hata marehemu mwenyewe alizipata mali hizo kwa dhuluma..kwahiy ndio hivyo maisha ya dhuluma mwisho wake ndio huo.....’akasema na kutulia.

‘Na mara nyingi watu kama hao wanauliwa na watu wao wa karibu, ..hasa nyie mliokuwa mkifanya naye kazi karibu…’nikasema na kucheka,  na yeye akasema

‘Hahaha…acha zako hizo,…keshaondoka basi …acha sisi tutumie, japokuwa kiukweli nilikuwa na mpenda sana…’akasema

'Kwahiyo ina maana waliomuua ni mtoto wake, au mke wake, au walishirikiana kumuua....au ni wewe ?' nikamuuliza, hapo akabakia kimia.

Akafungua mlango wa kuingia kwenye jengo, huku akiwa kimiya, halafu akaniangalia na kusema;

'Tumeshafika...karibu hoteli ya maraha ya Marehemu, hapa usiwe na wasiwasi kabisa....'akasema na mimi nikamuuliza

'Mhh, wasije kuniua na mimi, nimeshaanza kuogopa,…kama watu wanafikia kumuua tajiri kama huyo sembuse mimi....'nikasema

‘Hahaha usijali , mimi nitakulinda usijali kabisa, ..’akasema

‘Mbona hukuweza kumlinda bosi wako…?’ nikamuuliza na hapo kidogo akashtuka.

‘Mbona maswali yako yapo hivyo, usiwe na wasiwasi…’akasema

‘Hapana mimi sipendi maisha ya mashaka mashaka, …ndio maana nakuhoji, ili nijue nipo sehemu kweli salama…’nikasema

‘Usijali…’akasema

‘Au nimekosea kukuuliza…’nikasema

‘Hapana wewe uliza tu…’akawa anaongea kilevi kilevi.

‘Mimi ukinambia jambo napenda kujiuliza uliza sana…ni nani alimuua huyu mtu wa watu naogopa sana, mtu tajiri kama huyu anauliwa,…si alikuwa mtu mwema, anasaidia watu au sio..?’ nikamuuliza,

‘Alikuwa mwema, wakati mwingine, wakti mwingine ndio hivyo kutafuta, sasa kutafutwa na yeye akawahiwa, ndio maisha ajali kazini,…, unajua ukimuongelea nakumbuka mbali sana, nilimpenda sana, lakini kazi ni kazi, utafanyaje …’akasema

‘Kama ulimpenda kwanini hukusaidia polis wampate huyo muuaji wake, ..au muuaji unamfahamu au ni wewe?’ nikamuuliza na hapo akatabasamu, halafu akatikisa kichwa na kusema;

‘We acha…ndio maana nakuambia ni ajali kazini, alikuwa sio mtu rahisi kihivyo, mmh, sasa sikiliza tusiongee sana hayo, au…’akasema na kunywa, alionekana kama dawa inaisha nguvu nilitaka nipate mwanya wa kumuongezea nyingine,..na kweli ikapatikana kwenye gilasi yangu mwenyewe, ndio nikaweza, na kujivunga kama nakunywa, aliporudi nikawa nimebadili zile gilasi kia-aina, akanywa.

‘Mbona hujanijibu swali langu, mimi huwa nikiuliza swali mtu asiponijibu nakuwa na mashaka naye…’nikasema

‘Swali gani mpenzi, uliza chochote mimi nitakujibu,..unasikia chochote…’akasema

‘Ni nani alimuua huyu tajiri wa watu jamani…?’ nikamuuliza hapa, akatikisa kichwa kusikitika, inaonekana kweli inamchukua hiyo hali ya kumbukumbu, na anakuwa kama anawaza mbali, au kuogopa, vyote viwili,…nikasubiria jibu

NB: Tuishie hapa kwa leo..naombeni maoni yenu maana kisa kinafikia ukingoni, je kuna kitu tumekisahau....



WAZO LA LEO: Mali na watoto ni mtihani mkubwa kwa wazazi, ukiwa navyo ni ufahari,...lakini vyote hivi vina mitihani yake.  Mali ikiwa ni ya halali, inaweza isiwe ni tatizo, muhimu ni jinsi gani y kuitendea haki yake. Ama kwa watoto ujue jinsi gani ya kuwalea..wawe na elimu na maadili mema. Elimu pekee haitoshi. Elimu bila maadili mema inaweza kugeuka kuwa tatizo pia, wasomi wangapi wazuri lakini wanafanya mambo ya hatari kwenye jamii, kwa kutumia elimu yao, ukichunguza sana ni kutokana na ukosefu wa maadili mema,...

Tumuombe mola atupe mali za halali zenye tija, na watoto wema, wenye elimu na maadili mema. Aamin

Ni mimi: emu-three