Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, March 28, 2018

MKUKI KWA NGURUWE-103



 Nilipoichukua sikuwa na haraka ya kuiangalia,…lakini niliposikia wakiongea nikataka kuhakiki, sikuamini nilichosikia hadi pale nilipoangalia hiyo video ya matukio ya siku ile,….sikuamini, hadi leo nashindwa kuamini…we acha tu…

‘Niambie ukweli maana wewe si umesema hapa kuna ulinzi, kuna mitambo, iliwezekanaje mtu kuchukua silaha na kwenda kumuua bosi…bila hata kujulikana, kwahiyo hiyo mitambo iliisha chaji au..…?’ nikamuuliza kuonyesha sijui kitu

‘Hahaha, sio chaji…. kuna mtu alizima hiyo mitambi, ina maana ni mtu anayeifahamu, na mtu huyo ni huyo huyo…unaonaeeh, …’akatulia kidogo

‘Mimi niliona kila kitu kwenye hiyo video, nashukuru niliipata kabla haijafika mikononi mwa hao watu wake, au polisi, maana inaonyesha kila kitu hakuna kilichobakia, …inaonyesha kila kitu, …

‘Kama nilivyosema japokuwa mtu kazima mtambo mkubwa lakini huo mdogo ndani ya chumba kwa Marehemu bado uliendelea kuchukua taarifa, wenyewe hauzimiki haraka, Marehem alilijua hilo kuwa kunaweza kutokea tatizo mitambo ikazima, kwahiyo akaweka server……’akasema

‘Ok, sasa hiyo silaha ilifikaje…?’ nikauliza

‘Mhh..hapo hata mimi sijui..ila kilichoonekana silaha hiyo ilikuwa chumbani kwa mdada…’akasema

‘Wewe si mlinzi wa mbali, unamlinda mzee, ilikuwaje silaha ifike humo ndani wewe usione ..hapo ndio nakuwa na mashaka na ulinzi wako, au na wewe ulihusika…’nikasema

‘Mimi namlinda mzee, ..sio jengo, sio kila kitu kwenye jengo, unasikia, ulinzi wa jengo wapo watu wengine, na mkuu wao ni mtoto wa mzee, unasikia, kwahiyo jinsi silaha ilivyoingia sijui…mimi isingelikuwa hilo tatizo,…la mke wangu mzee asingeliuwawa…’akasema

‘Kwahiyo silaha ilikuwa chumbani kwa mdada, huyu jamaa alijuaje kuwa ipo huko…?’ nikauliza

‘Unataka kutunga kitabu…?’ akauliza huku akicheka

‘Au usije ukawa ni shushushu…nitakuua….’akasema na kucheka

‘Hahahaha, hapana….ni hadithi au tukio la kuvutia….’nikasema

‘Sio hadithi, hilo ni tukio la kweli, upo ushahidi…silaha ilikuwepo kwa huyo mdada, swali ilifikaje, kama huyo mdada naye hakuwa na nia mbaya na bosi, ndio maana awali nilijua yeye ndiye kamuua…’akasema

‘Endelea,..very interesting story…’akasema

****************

Jamaa akaingia chumbani kwa mdada, akaichukua hiyo silaha, maana huyo mdada hakuwepo hapo chumbani kwake alikuwa kwenye ofisi yake…usingelimuona awali, usingelijua ni yeye, alivyojivika hayo manguo, kuonyesha kweli huyo jamaa ni jasusi..

Ili kuwa ni kitendo cha haraka sana…wakati huo marehemu alikuwa akiongea na yule jamaa yake, walikuwa hawaelewani,…walikuwa wanabishana sana, unajua kama isingelikuwa ni huo ushahid , pia ungelisema huyo jamaa yake ndiye alimuua, maana ilifikia mahali, huyo jamaa yake anasema kwa sauti.

‘Ipo siku nitakuua kwa hili….’

‘Nani alisema hivyo…?’ nikamuuliza

‘Huyo jamaa yake waliyekuwa wakiongea naye…’akasema

‘Unamfahamu huyo jamaa…?’ nikauliza

‘Unajua…awali, sikuweza kumfahamu maana alikuwa kajibadili…lakini nikaja kugundua kuwa ni jamaa gani,...ni jamaa mmoja bwege-bwege fulani, yeye hakujua tu, alikuwa kitumiwa kwa masilahi ya wengine……’akasema na kutulia

‘Ulikuja kumgunduaje kuwa ni yeye…?’ nikauliza

‘Mtandao..unaweka picha, …inakuambia huyo mtu ni mtu fulani, kajibadili…siku hizi mambo ya kisasa…haikuwa kazi kwangu kumgundua,…mimi ni mtaalamu usinione hivi..mzee alikuwa akinifahamu ndio maana akaniamini.

‘Ok, sawa endelea…’nikasema nikijifanya kuangalia saa.

 Ikaonekana jamaa katoka na silaha…lakini wakati anatoka alikuwa kaifutika kwenye koti…, nilishangaa kwanini mlio wa hatari haukulia, kwani yeye alikuwa na silaha, nikagundua kuwa yeye kwa vile ni mtaalamu aliweza kuzima sehemu ya mlio wa hatari....

‘Alikuwa yeye peke yake…?’ nikauliza

‘Peke yake….ila alionekana kama anawasilana na watu…kwenye simu kabla na baada ya tukio…’akasema

‘Ok endelea…’nikasema

‘Basi akafika kwenye ile ofisi, ..akasimama, kama anasita kufanya anachotaka kukifanya, ghafla akasukuma mlango.

‘Ile video inazunguka, kwahiyo ilikuwa kama ..imekata, halafu ikaonekana sasa anamlenga baba yake, hiyo inaonyesha wazi, hakuna kuremba, bila chenga, risasi inatoka inakwenda kutua kifuani kwa mzee..…nahisi baba yake alimuona….ila huenda baba yake hakufahamu ni nani.

‘Akawa sasa anataka kummaliza huyo jamaa mwingine, ile bastola ikawa imeishiwa risasi, kwa ujinga wake, aliichukua ile bastola, bila kuhakikisha kuwa ina risasi za kutosha, kwa mshituko wa kile alichokifanya, akairusha kwa ndani...nahisi alifanya hivyo makusudi ili watu wengine, hasa huyo jamaa aliyekuwepo humo ndani ashukiwe kama muuaji,...

‘Kwahiyo una uhakika kuwa huyu mtu ndiye huyo mtoto wa mzee,…maana hapa ni muhimu…?’ nikauliza

‘Uhakika gani sasa..ukiangalia hiyo video ya matukio utaona kila kitu…..’akasema

‘Oh….inatisha, mtoto kumuua baba yake…haiwezekani…’nikasema

‘Ndio maana nakuambia hata mimi siamini….ukiangalia hiyo video, utafikiri ya kuigiza, lakini ndio tukio lenyewe,…sasa hebu niambia mtu kama huyo utaweza kuishi naye bila kuwa na mashaka…’akasema
‘Halafu ikawaje…?’ nikamuuliza sasa nikiwa sina hamu na mengine ni kupoteza muda sasa…

‘Baadaye  sasa, akaonekana mwanadada mwingine akiingia, huyo ndiye waliyekuja kum-kamata kama mshukiwa,…’akasema

‘Huyu mwanadada ni nani…?’ nikauliza

‘Yaani huwezi amini, huyo mwanadada ni mke wa huyu jamaa aliyekuwa akiongea na marehemu…’akasema kwa sauti ya chini..

‘Oh…alikuja kufanya nini…?’ nikauliza

‘Nahisi alikuwa na yake,…na marehemu, ..si unajua marehemu ana wateja wengi, na mambo yake ni mengi tu…’ akasema

‘Kwahiyo wakazidi kuchelewa, kumpata muuaji halisi,…na ushahidi mwingi ukawa unapotea bure, ila halisi ya matukio, ikawa imechakachuliwa, lakini ya kwangu ilibakia kama ilivyo, kila kitu kipo...’akasema kwa haraka haraka, nilimpata kwa vile nilishajua mengine...

‘Sasa nikuulize kumbe wewe ulikuwa na ushahidi wote huo, kwanini hukuwafahamisha wanafamilia, yaani mtoto mkubwa wa marehemu?’ nikamuuliza

‘Sikufanya haraka hivyo, hata hivyo, wao yaani yeye na mama yake hawakutaka kuingilia yote hayo, japokuwa walihisi kuwa kuna mtu anahusika, wao walirizika na taarifa ya polisi kuwa huenda muuaji ni miongoni mwa maadui zake.

‘Mhh..wewe ulilionaje hilo…?’ nikauliza
‘Sikuona cha ajabu,…hawakuwa karibu sana na mzee, kabisa, walifanya tu kutumiza wajibu,, wewe huoni ajabu kuwa hawakutaka mali ya marehemu kabisa, urithi ulikuwepo kwa ajili yao, mtoto na mama yake, lakini hawakuutaka kabisa....’akatulia kidogo.

‘Sina uhakika na hilo, ila nakala halali ya nani arithi, ilipatikana,..ikionyesha kuwa kaka mkubwa ndiye msimamizi wa kila kitu, na msaidizi wake ndio huyo mtoto mwingine …aliyemuua baba yake…ile ya kwako waliyogushi ikachelewa kupatikana,kukawa na mkanganyiko hapo.

‘Maana hadi kufanya hayo mauaji ni ili …mirathi yao waliyotengeneza wao, iwe halali na hiyo ya mzee ipotezewe, ikawa kinyuma chake, mtoto na mama walihaha, kilichowafanya wasifanye jambo, ni pale walipoona wenzao hawana tamaa na mali, hawataki chochote kutoka kwa marehemu.

‘Sasa kibaya zaidi ni pale wenzao walipoanza kugawa mali,..hilo lilifanya kuzuke mgongano, lakini wenzao walikuwa wastaarabu, wakasema wao hawatagusa mali kubwa kubwa, wao, wanataka mali zile ambazo zinaondosheka, wauze, kulipia madeni, ..na kuwalipa wale waliodhulimuwa, japokuwa hazikutosha.

‘Mambo yakawa yanachelewa..huyu mtoto mkubwa, akaona bora aondoke na iliyobakia ikawa chini ya huyu msaidizi wake,..alipoondoka tu, huyo mdogo mtu akacheza, akahakikisha ile mirathi yake ndio inatambulikana, hadi sasa utaona hivyo…

‘Kwa vipi sasa, wakili wao si yupo…wakili aliyekabidhiwa hayo mambo na mzee…?’ akaulizwa

‘Wakili hahaha…tuyaache tu hayo…nikuambie kitu.., huyu sio sawa na Makabrasha, akikutisha anakutisha kweli…wakili akafyata mkia, akawa sasa anafuata anachotaka bosi mpya…’akaangalia saa nahisi alinihofia mimi nachelewa kuondoka, akili za kunijali bado zilikuwepo.

‘Unafikiri kwanini huyu mtoto mkubwa na mama yake hawakutaka kuchunguza kwa undani kifo cha Makabrasha, hapo bado mimi najiuliza, isije ikawa na wao wapo nyuma na jambo fulani….?’ nikamuuliza

 ‘Hapo hata mimi sijui,...sijui kwanini hawakutaka kufanya uchunguzi wao wa kina...ila mimi nilitaka kumwambia huyo mtoto wa mzee yale niliyokuwa nayafahamu kwa wakati huo, lakini huyo mtoto wake, aliniambia niachane kabisa na maisha ya baba yake, kwani yeye hataki kabisa kuyaingilia na wala hataki mali yake, alishajitoa kwake, yeye amefika kwasababu ni baba yake na niwajibu wake kumzika, mengine kama ninayo ni mwambie huyo mdogo wake….yeye keshamaliza kilichomleta na kama nina ushahid wa kutosha wa muuaji, niwaone polisi….

‘Aliponiambia hivyo nikaona basi haina haja...nitautumia huo ushahidi nilionao nionavyo mimi,..siunaona, imanisaidia na mimi, japokuwa nahisi nipo kwenye hatari, hata hivyo, hatari imekuwa ndio maisha yangu,...huwezi jua, kifo changu kinaweza kuwa kama cha marehemu..’akasema.

‘Mimi nakushauri kitu, ongea na polisi, jisalimishe, ili uwe na maisha ya usalama, maana hujui wenzako wamejipanga vipi, kwanza kama ulivyosema kwenye mirathi halali ya marehemu alikutaja kama mmoja wa warithi wake, huoni utafaidika kihalali ukifanya hivyo...?’nikamwambia.

‘Mhh, ni rahisi kusema hivyo,… lakini huwajui hawa watu, ...mimi siwaamini, na wala siamini kuwa polisi watawaweza kunisaidia kwa hili jambo, nahisi likifika mikononi mwao, hata kile kidogo nilichotarajia kukipata sitakipata tena,…’akasema

‘Unajua huyu …mtoto wa marehemu , kama alivyokuwa baba yake, hata yeye kuna wanamtumia wenye pesa, japokuwa hakuna ushahidi wa moja kwa moja kuwa wanahusika kwenye hayo mauaji,…ni wajanja sana…’akasema

‘Wewe unao ushahidi wa kuonyesha kuwa hao watu wanahusika…?’ nikamuuliza

‘Unajua nikuambie kitu…hawa watu walishafikia sehemu wamemchukia Makabrasha…kuna video inaonyesha hivyo…ninayo…, kwani Marehemu alipoona kafanikiwa mambo yake, akavunja mahusiano na hao wafadhili, …sio moja kwa moja y akukatisha mkataba nao, hapana, alikuwa kama hawajali-jali fulani hivi…, na kazi aliyopewa akawa anaifanya kwa masilahi yake…’akatulia

‘Ehe…’nikasema

‘Kwahiyo kwa hali hiyo, huenda..huyu mtoto wake pamoja na mawazo ya mama yake, pia yawezekana aliahidiwa donge nono, kumbuka kutokana na madeni yaliyobakia ya mzee, jengo lilitakiwa kupigwa mnada, yeye akaligomboa, akalipa madeni yote,…sasa huyu jamaa pesa alipatia wapi, walichunguza hilo watagundua mengi…’akasema

‘Mhh..hapo yawezekana, lakini hata hivyo hakuna ushahidi kuwa hao watu walihusika kwenye hayo mauaji,  huo uhakika haupo, au sio..’nikasema

‘Mimi nilivyoona ni hivyo…, sikutaka kuingia huko sana, maana huko sio pa kuingilia, huko waachie wenyewe…’akasema

‘Mimi ninachojiuliza ni kwanini,  toka marehemu afariki hadi leo, wewe unao ushahidi,  kwanini hukuwaambia polisi, unajitia matatani bure…’nikasema

‘Wao wamefanya nini muda wote huo, kazi kuwakamata watu wasiohusika, kwanini wanawasikiliza wanasiasa, kwanini hawafanyi kazi yao ....mimi naona wengi wao, ni wale wale tu…mimi ndio maana nimeamua nifanye nionavyo mimi, kwa masilahi yangu kwanza, hapo nitakaposhindiwa basi nitajua la kufanya...’akasema.

‘Je na huyu mtoto wa marehemu akikugundua huoni utakuwa ndio mwisho wako?’ nikamuuliza.

‘Kunigundua kwa vipi sasa, wao wanafahamu kuwa nina siri hizo,…wao wanachojitahidi ni kutafuta wapi siri hizo zipo…lakini hawataweza kugundua ng’ooo…mimi sio mjinga…’akasema

‘Wao kila wanachokifanya ninakiona, kwanza mimi mwenyewe ni mtaalamu , na pia...mzee wao alinifundisha mambo mengi, ndio maana aliniamini, ...unaona nilivyo mjanja,  pale nyumbani kwako, napaona kila siku, ...wakiongea , wakipanga, mimi napata taarifa, ni kwa usalama wao, lakini pia mimi nachunguza zaidi ya hayo...’akasema.

‘Kwahiyo wao kwa sasa, wapo wapi, wapo hapa nchini au wamewekeza huko nchi za nje… ?’ nikamuuliza, maana mama na mtoto wake, hawajaonekana hapa jijini kwa siku ya tatu sasa, nikaona niulize hilo swali ili watu wa usalama wasikie na wajue jinsi gani ya kufanya.

‘Hao wamekwenda hapo jirani tu,- Kenya, kuna miradi yao wanaifuatilia, ilikuwa miradi ya marehemu, ilikuwa haijakamlika wakati wa uhai wake kwahiyo wao wanataka kuhamisha umiliki kutoka kwa baba kwenda kwa huyo mtoto…’akasema

‘Mhh, ni mradi mkubwa sana…?’ nikauliza

‘Ndio, kama wakifanikiwa, basi wao sio wenzetu tena, na jiulize pesa za kuendeleza mradi huo wamezipatia wapi, ni zawadi kutoka kwa maadui wa marehemu au kuna nini nyuma ya pazia,…aah, mimi huko sipo, ila nitakula nao….’akasema

‘Huenda wakija watakupatia angalau hisa kidogo..?’ nikauliza

‘Hapo ndipo naumia kwanini wachukue kila kitu, kwanini mimi wasinipe haki yangu, ndio maana nimelifanya hili, …kuwakomoa kwanza,…kwa hivi sasa kila kitu wameniachia mimi mpaka wakirudi, wakirudi tu, nawabana, vitisho vyangu ni vile vile...’akasema

‘Kumbe sasa wewe ni bosi...’nikasema.

‘Hahaha, kwa hivi sasa eeh, nimeachiwa usukani,..ila wakirudi wanaweza kuja na ajenda ya siri, lakini mimi nitaigundua tu, ..hawaniwezi...’akasema.

‘Inakuwaje mtu afahamu siri za watu wengine, hicho chombo alichokuachia marehemu kipoje...naona dunia ina mambo mengi, mimi mambo mengi siyajui, naona kama miujiza tu...?’ nikamuuliza

‘Unafikiri ni chombo kikubwa sana wewe…’akasema akionyesha kuchoka.

‘Ni kitu kidogo tu…kama simu tu, unatembea nayo, ukitaka kuangalia mahali fulani ulipoweka vitu vyako, unabonyeza namba, unavuta ule mnara wake, basi unatafuta muelekeo wa namba, unawaona, ...

‘Sasa kama unataka kukihamisha hicho kidude kwenye komputa unakiweka, ...hapo unaweza kuangalia, kama unavyoangalia picha za kawaida, wanawasanifu watu kweli kweli, lakini mpaka upandikize chombo fulani hapo unapotaka kupata taarifa ....mimi ni mtaalamu bwana..’akasema kwa sauti ya kilevi.

‘Sasa wewe una uhakika gani kuwa mwenzako huyo naye hakufanyii kama unavyo mfanyia yeye,huenda huko alipo anakuona..huenda hata nyumbani kwako unapoishi kapandikiza kitu kama hicho?’ nikamuuliza.

‘Kuna kifaa kingine cha kugundua hivyo vitu vya kupandakiza, mimi kama mlinzi ninacho, kama kuna kitu kimepandikizwa kwako kinakuashiria, lakini sijawahi kumuonyesha huyo mtoto wa marehemu, aliwahi kukipandikiza kwangu, nikakigundua, kwahiyo mimi nipo mbele zaidi yake....’akasema.

‘Wao wanarudi lini?’ nikamuuliza

‘Kesho, ila kila siku nawasiliana nao, wanaweza wakaja hata leo, kwa usalama mara nyingi hawasemi lini wanafika, ndio maisha ya watu kama hawo, kama alivyokuwa marehemu, ila mimi nafahamu ni kesho.....’akasema.

Mara simu yake ikalia, akaiangalia, na kusema, ...
*****************

‘Bosi,...naona keshafika, huenda wapo hapo uwanja wa ndege,...sasa mimi kwa hali niliyo nayo,sijui kama nitaweza kuwafuata, inabidi nimwambia mtu akawachukue, ngoja niongee naye kwanza, maana nahisi nimelewa sitaweza kuongea nao katika hali hii, au unasemaje mpenzi,....’akasema.

‘Kweli...’mimi nikasema huku nikijua sasa kazi imekwisha, nikahakikisha namsogelea ili kusikia anachoongea, sikuweza kusikia huyo bosi wao anaongea nini, lakini alivyokuwa akijibiwa nilisikia, jamaa akawa anajiuma uma,..mimi kwa haraka nikawasiliana na watu wangu kwa ujumbe wa simu, na wao wakanijibu kuwa wananifuatilia kwa karibu,nisiwe na wasiwasi.

‘Haloo bosi, mnasemaje?’ akawa anaongea kwa kujitahidi kuficha kuwa kalewa, huku pia akijaribu kunikwepa ili nisiwe karibu naye, lakini sikumpa nafasi hiyo nikamsogelea, akawa sasa anaongea na simu, akasema;

‘Unasema mumeshafika, mpo nyumbani, mbona hamkuniambia nije kuwapokea hapo uwanja wa ndege, nipo hapa karibu kabisa...!’akasema kwa akionyesha mshangao.

‘Ohoo, ndio nilizima kidogo, maana nina mtoto, nastarehe kidogo, siunajua leo ni mapumziko bosi...sasa sikutaka mambo yangu yaonekane huko, nitawasha,...nikimaliza..nipe nusu saa,...sasa hivi, kwanini bosi, mbona unaniharibia starehe zangu, unasema kuna nini..hapana bosi, mimi nina uhakika hakuna kitu kama hicho...una uhakika,...’akasema na nilimuona akiwa na wasiwasi.

Baadaye alinigeukia, na kusema;

‘Mhh, naona mambo yameharibika, kitumbua kimeingia mchanga....’akasema akionyesha wasiwasi.

‘Kuna nini kimetokea....? nikamuuliza

‘Jamaa anasema kafika tu ,polisi wamemvamia, ananihisi eti mimi ndiye nimemuuza, polisi wameshafika kwa bosi, haapo kajiiba ,kusogea pembeni, kunipa tahadhari, nihakikishe hawafiki huku,  sasa naona mambo yangu yameharibika, sijui nifanye nini, ..kwanini polisi wamefanya haraka kiasi hiki hata ujenzi haujakamilika...’akasema, na mimi nikamwambia.

‘Wewe usijali, ..cha muhimu ni kutoa ushirikiano na polisi, maana inavyoonekana polisi wameshafahamu ni nani muuaji, sasa ukijificha, na wewe utashikwa kama mshirika wao..mimi naona hapa hakuna usalama tena nataka kuondoka....’nikamwambia na yeye akawa kama anafikiria jambo.

‘Sasa bosi  kasema niharibu kila kitu, ....’akasema

‘Wewe, usije ukafanya hilo kosa, unaharibu vidhibiti vya polisi, huoni kuwa wewe utaonekana  mshirika wa hayo mauaji..’nikamwambia.

‘Ok, nimekuelewa, lakini kwanini huyu bosi anasema hata sasa hapa nilipo, nipo na watu wa usalama, mimi simuelewi kabisa... ngoja nikawashe hiyo mitambo niliyokuwa nimeizima, tuondoke zetu, wameniharibia starehe yangu,....nisubiri...’akasema na mimi nikamuuliza

‘Tutatokea wapi?’ nikamuuliza nikimchelewesha na yeye akaniangalia halafu akaingalia kule tulipoingilia, na kusema

‘Hukohuko tulipoingilia....’akasema, na kabla hajamaliza  mara tukasikia mlango ukigongwa, akawa anangalia huku akionyesha wasiwasi, akaniashiria kwa mkono, nitoke, kwa kupitia ule mlango tulioingilia, huku yeye akianza kuelekea kwenye kile chumba cha ile mitambo, lakini kabla hajaufikia huo mlango, mara mlango ukafunguliwa.

Wa kwanza kuingia alikuwa askari, mwenye sare, na baadaye wakaingia wengine, wakiwa wamevalia kiraia, wote hawo nawafahamu,...

‘Sisi ni askari usalama, mpo chini ya ulinzi, hakuna kusogea au kugusa kitu chochote..’akasema huyo mwenyesare, lakini hakuwa na silaha yoyote zaidi ya rungu, ...nikajua kwanini, wasingeliweza kuingia na silaha kwa kupitia upande wa juu, mlio wa hatari ungelitushitua, na huyu jamaa angelikimbia, ...lakini na mara tukasikia sauti kutoka kule tulipoingilia wakaingia askari wengine, hawa walikuwa na silaha, na hapo hapo mlio wa hatari ukaanza kulia...

‘Kwanini mnanivamia nimefanya kosa gani?’ akauliza na wao wakamshika na kumfunga pingu, na kumweka chini ya ulinzi, mimi taratibu nikatoka,nikijua nimetimiza wajibu wangu ...kazi nyingine yote waliimalizia wao, kila kitu kikawa wazi, muuaji akajulikana, na ushahidi wote ukapatikana,mtoto na mama yake, ndio waliomuua Makabrasha,...’akasema huku akimwangalia mwenyekiti.

‘Inatosha, tunakushukuru sana, mengine yote, tunayafahamu kwa wale waliokuwa wakifuatilia hiyo kesi na kuhudhuria mahakamani, kuwa wahalifu hawo, wanatumikia jela zao, haki imtendwa, iliyobakia ni sisi kama familia, tutimize yale yanatuhusu, na kusuluhisha tatizo la familia hii, kama wazazi ni lazima tutimize na sisi wajibu wetu,..’akasema mwenyekiti.

‘Sasa ni ajenda yetu ya mwisho kama nilivyosema…, ajenda hii ni hukumu, au mstakabali wa ndoa ya mke na mume wa familia ....na hapa mimi sitaingilia sana, maana wanandoa waliosababisha hiki kikao wapo hapa, na walishapata muda wa kukaa pamoja na kulijadili hili, nasikia bado kuna mvutano, ...sasa mimi kama mwenyekiti, nahitajika kutumia rungu langu la uenyekiti...kulimaliza hili tatizo,..., 

NB: Naona tuishie hapa kwanza.


WAZO LA LEO: Ubaya na matendo mabaya, sio sifa ya kujinadi mbele ya wenzako, kuwa mimi ni mjuzi wa ubaya fulani, watu hawaniwezi, nk....kwanini tusijisifu kwa matendo mema, tuangalie wenzetu waliobuni , na kugundua mambo ambayo mpaka leo yapo, yanatumika kwa manufaa ya jamii, ina maana watu hawo, ni kama vile bado wapo hai, ...hizo ndio sifa njema,..., 
Ni mimi: emu-three

No comments :