‘Ni mali zake mwenyewe ndizo chanzo cha kifo chake....’akasema
sasa akionekana kulewa anajiongelea tu…
‘Kwa vipi, mbona sikuelewi,....mbona unapenda kuongea
kimafumbo-mafumbo...maana mimi nijuavyo mali ni utajiri unaokufanya upate kile
unachokitaka, sasa ilikuwaje mali zake mwenyewe zimuue huyo marehemu...?’
nikamuuliza.
‘Kutokana na mali zake kulitokea kutokuelewana yeye na familia
yake ya pembeni…unaonaeeh….ndio hivyo watu wengine bwana..’akasema na
kubekuwa…akawa anakunywa tu.
‘Kumbe alikuwa na familia ya pembeni, mke au hawara tu..?’
nikauliza
‘Ufahamu huyu mtoto sio mtoto wa mke wake wa ndoa, japo anajifanya
karithi mali yote ya baba yake…ni mwizi tu huyu, …, yeye alizaliwa nje ya ndoa,
mama yake alikuwa hawara wa marehemu…kuna mtoto halali alitakiwa ndiye arithi,
lakini huyo mtoto haki mali ya dhuluma, kaacha kaondoka zake..’akasema kama
kumnyodoa bosi wake.
‘Nyie wanaume jamani…kwanini lakini’nikasema hivyo, na yeye
akaendelea kuongea.
‘Sasa huyo aliyekuwa hawara yake eeh…, akawa anamfunda mtoto wake,
kumfisidi baba yake, hebu fikiri mama anamfundisha mtoto wake kumuibia baba yake
na si kumuibia tu…unajua nikuambie kitu eeh...mwanzoni mtoto huyo alikuwa hataki,
maana namfahamu hata tukakosana kwa hilo…’akatulia
‘Nilimuambia achana na mawazo ya mama yako, weeh, ukitaka ukosane
na huyo jamaa mtaje mama yake, akanijia juu kweli, tukawa hatupatani tena mimi nay
eye, sikujali..lakini ukweli nilimpa…sasa wanaume nao bwana,…Marehemu alikuwa
kichwa lakini wakati mwingine namlaumu…’akatulia
‘Unajua walikuka kukosana baba na mtoto wake kwenye mambo ya …kuandikisha
mirathi, si ujinga huu jamani, utaandikishaje mirathi hujafa eeh,..hilo
lilimponza huyo jamaa…mtoto akaona, kwanza….eeh nimekumbuka, kwanza baba kwa
kupenda alimuandikisha mtoto..kuwa ndiye mrithi mkuu…’akatulia
‘Baadae baba kapata mawazo huku na kule akagundua kafanya makosa,
sijui madawa aliyowekewa yalishakwisha, akabadili mirathi,..hapo sasa ndio
mambo yakaharibika….mtoto akawa haivani na baba yake…mtoto akawa sasa anamfuata
mama yake kile anchotaka kumfisidi baba yake….’akafunguka hivyo
‘Mungu wangu kwahiyo mama akamtuma mwanae afanya mabaya,…ina maana
gani hapo…kuwa ndiye alimtuma akamuue baba yake au…?’ nikamuuliza
‘Wewewe…sijasema hivyo mimi…unajua uhuni ni mbaya sana, ukifanya
haya mambo kwa siri….haya eeh, hayaaah…nasema taratibu, haya…, ipo siku siri
hiyo itakuumbua, marehemu ana watoto wengine, lakini hawo wengine hawana
matatizo, tatizo lipo kwa huyo mtoto wake aliyemuona ni kichwa chake...’akasema
‘Kwahiyo alimpenda sanaa mtoto wake huyo…kwanini hakumlinda baba
yake asiuwawe..?’ nikauliza
‘Subiri nikuambie sasa…huyo mtoto na mama yake, wakawa sasa hiki….’
Akaonyeshea kwa kidole..
‘Umenielewa hapo…kitu kimoja, sasa wakawa na ajenda moja ya
siri,...huku wakijipendekeza kwa marehemu kuwa wanamjali wanampenda, siunajua
tena ile ya kujipendekeza.....mimi hilo nalifahamu sana….’akahema kidogo
‘Nahisi kama nimelewa haraka, sio kawaida yangu …lakini usijali…unajua
eeh, mimi nilijaribu kumuonya mzee, lakini …watu wengine mimi namshauri kwa nia
njema, anakuja kunigeuka kuwa mimi ndiye nawachonganisha,..mimi najali maisha
yake na uhai wake, leo hii naonekana mbaya, lakini, sawa maana mimi si kibarua
tu…hajui jinsi gani nilivyohangaika naye..’akasema akilegeza domo.
‘Kwahiyo unataka kusema nini, kuwa mtoto huyo huenda ndiye alimuua
baba yake au sio, na wewe uliona kwa vile alishakuudhi ukaachia tu, au njama
hizo na wewe ulihusika…?’ nikamuuliza lakini hakulijibu hilo swali moja kwa
moja.
‘Mimi na mzee tulihangaika naye sana kuweza kufikia hapo alipo, nilijitokea
nafsi yangu kumlinda, ndio maana mzee aliniweka karibu sana,…na nilijua mimi
nitakwua kama mtoto wake,…ile mirathi ya kwanza alinipa mali, lakini
alipobadili, sikuweza kuona jina langu,…watanificha nini wakati mimi naona kwa
kiona mbali, hakuniweka, iliniuma sana..unajua
kuumia, niliumia, nika-fikia kuapa, nitamkomesha, unajua tena…’akasema
‘Oh,…kwahiyo…ukapanga mbinu za kumuua huyo mzee, sasa
nimeshaelewa, kumbe, lakini kwanini ulisahau fadhila, au..?’ nikauliza
‘Unajua haya mambo yasikie tu….kuna watu wanajua kucheza na vichwa
vya watu, watu wanapanga mambo wakiangalia matukio…wakajua kuna mambo nikifanya
hivi watu wataegemea huku..unaona, …sasa mmh, mimi nahisi kulewa, kwanini leo
imekuwa hivi..’akashika kichwa.
‘Kumbe …wewe ni mtoto wa pombe…’ nikasema
‘Mimi…weeeh, hata nikikesha,…nipo imara kabia, na …tukienda
kustarehe, utakimbia…’akasema
‘Kustarehe..kupi tena…’nikasema
‘Hahaha, usijali…leo tunywe tu, wewe si rafiki yangu eeh,
nimeshakupenda, wewe utakuwa mke wangu..unasemaje…’akawa sasa anajiongelea
nikaona hapa nikichelewa gari linaweza kuzimika kabisa.
‘Tunywe huku tunaongea, au…?’ nikauliza
‘Ni wewe tu…mimi ni wako au sio…’akasema
‘Sasa hebu nikuulize maana hii hadithi, inafurahisha sana…’nikasema
‘Hadithi gani…?’ akauliza
‘Si ya marehemu na mali yake iliyomuua…’nikasema
‘Hahaha…ndio hivyo, ndio maana nasema mali yake mwenyewe ndiyo
ilimuua,…mali na watoto, unaona, na watoto wenyewe wa nje ambao, wanajali mali
tu…’akasema
‘Haiwezekani ina maana mtoto ndiye aliyemuua mzazi wake, kwasababu
ya mali, haiwezekani...ungelisema mke, hapo ningelikubaliana na wewe, maana
sisi wanawake, tukiamua jambo, tunaweza…’nikasema
‘Mhh, unaonaeeh,…hata huyo mtoto alibadilika kutokana na mama
yake, sio yeey..mwanzoni alikuwa mtu mnzuri tu… lakini, mama..maana mama alijua
mzee akiondoka atapatia wapi mali, kwahiyo cha muhimu ni kuwahi…akamfunda
mtoto, umeona hapo…’akasema
‘Kwahiyo..ikawaje..?’ nikauliza
‘Unajua… tuyaache hayo maana jamaa ana msikio, na tukiongea
kwenye hili jengo jamaa atakuwa anatuona, na kutusikia, kwahiyo, ngoja
....’akasema na mimi nikamkatisha na kusema;
‘Kama anatuona na kutusikia, mimi siwezi kukaa hapa, wewe
uliniambia hapa ni sehemu ya usalama, kumbe kuna watu wanatuona, hapana, wewe
hunitakii mema,mimi naondoka zangu...’nikajifanya kutoka kuondoka.
‘Hahaha…sikia bwana, humu ndani kawezeka vitu vya kuona matukio,
uliniona wakati naingia nilifanya nini…taaaa…nikazima ule mtambo, kwahiyo hapo
alipo seehmu hii hawezi kuona kitu, kesho atagomba, lakini..ndio hivyo…’akasema
‘Hili jengo ni la ajabu
sana…kuna vitu vingi eeh ina maana kuna mitambo ya matukio, kuna mitambo ya
ulinzi, …kwanini sasa marehemu akauwawa kirahisi hivyo…?’ nikauliza
‘Ni kweli mambo ya ulinzi yalikuwa mikononi mwangu, mimi najua
kila kitu kuhusu ulinzi wa humu ndani..unajua kuna kipindi marehemu alimchukua
binti mmoja, yule binti alikuja kuharibu mitambo yote…imechukua muda kuijenga
upya, lakini bado..na nafanya hivyo makusudi kumkomoa huyu bosi wangu mpya…’akasema
‘Juu kuna sehemu nyingine au sio…?’ nikauliza
‘Yah…ipo lakini imekodishiwa watu wengine sisi makao yetu ni huku,…huku
anamiliki mwenyewe bosi na mambo yake,…juu ni mradi wake wa kuingiza mapesa,..huko
juu hawajui kabisa kuhusu huku chini…’akasema
‘Ina maana ukiwa huko juu, huwezi kuteremka huku chini..?’
nikamuuliza
‘Kuna chumba kama store,…kimejengwa ovyo ovyo..ni mbinu tu,
ukifungua humo huwezi kujua siri yake, sasa humo ndio kuna ngazi za kushuka
chini, unafungua mlango…unateremka, watu hawajui, hizo ni mbinu nilimfundisha
mzee, zinatoka izraili…nilijifunza huko, hahaha…’akacheka sana.
‘Kwahiyo huku chini mnatumia kwa kazi gani…maana sioni watu wengi,
…?’ nikauliza
‘Starehe na biashara haramu…na umalaya tu , huyo mtoto ndio zake,
akitaka kufanya shughuli zake za haramu, ni huku..akitaka kumtesa adui yake ni
huku, akiteka watu watu ni huku …hakuingiliki ovyo…nimekuingiza wewe kwa vile
tu..nakupe-ndaaa…’akataka kunishika
‘Ohh, sory….’akasema nilipomkwepa.
Ilibid nibadili muelekeo wa kumuhoji kwanza, kwasababu kwa maelezo
yake hayo, huku kutakuwa na siri nyingi sana, ambazo zitasaidia kama ushahidi,
sikutaka kwanza kushinikiza kufahamu muuaji wa Makabrasha, nilijua hilo
litafikia muda wake.
‘Kwahiyo huku kuna siri nyingi sana za marehemu au sio…?’
nikauliza
‘Marehemu keshaondoka, sasa hivi ongelea siri za bosi mpya,…kuna
vyumba vingi tu, kila chumba kina mambo yake, ..mimi kila kitu
najua,..hanibabaishi mimi..’akasema
‘Sasa hebu niambie ni nani aliyemuua huyo jamaa wa watu, maana
naanza kuingiwa na hamasa ya kumtambua huyo marehemu na familia yake, wakati
mwingine unaweza kujifunza kutoka kwa familia za watu wengine au sio...?’
nikaanza kumchota tena kuhusu mauaji...
‘Hiyo familia achana nayo, ni familia ya laana, walichokitenda
hawataweza kuishi kwa amani, nikuambie ukweli, pamoja na utajiri wao wote, bado
wanaishi kwa majuto, na wakati mwingine nasikia huyo jamaa analia na hata
kupiga makeleke usiku...’akasema
‘Ni nani analia, ....?’ nikamuuliza
‘Si huyo mtoto wa marehemu, wewe unacheza na damu za watu...’akasema
‘Ina maana yeye ukimkosea tu anaku-ua, ..mbona unanitisha…?’
nikauliza
‘Upo na mimi,…mimi nilikuwa mlinzi hodari wa mzee, sasa wa kijana
wake, wananiamini, mimi sio mchezo, …’akasema akijipiga kifua
‘Kwanini anaweweseka usiku…kaua watu wengi au…?’ nikauliza
‘Laana ya watu waliowaua..na zaidi laana ya mzazi wake yeye
mwenyewe…’akasema hapo nikaona hajasema ninalotaka kulisikia.
‘Lakini huyu mtoto alimpenda sana baba yake au sio, sasa iweje
apate laana…?’ nikamuuliza
‘Hivi unafikiri mzazi ni mchezo…hata kama asipokutamkia,..kama
wewe umaimwaga damu yake, si lazima utapata laana yake…’akasema
‘Ni kweli kama alimuua baba yake ni lazima atapata laana yake …’nikasema
‘Ndio maana halali…anaweweseka….’akasema
‘Una uhakika gani kuwa yeye ndiye aliyemuua baba yake?’ nikamuuliza
huku akimimina kinywaji...
‘Uhakika sikuwa nao mwanzoni, lakini nilikuja kuangalia mkanda wa
matukio, niliouchukua pale ofisini kwa Makabrasha, yeye mwenyewe aliniambi siku
nikisikia kafa, nifungue sehemu moja ya siri, iliyokuwa chumbani kwake, nitoe
hicho kifaa cha kuhifadhi matukio ya hilo jengo, nimpe mtoto wake
mkubwa..’akaniambia.
‘Kwanini alikuambia hivyo, ina maana alishafahamu kuwa atakufa?’
nikamuuliza
‘Watu kana hawo, hujihami tu, ...na sijui kwanini, nahisi kama
alishatabiri kifo chake kwani siku ile ya mwisho aliniambia, niondoke, ila
nikisikia lolote limetokea, nisisahau kufanya kama alivyoniagiza, na mimi
nikamuitikia, na niliposikia kuwa amekufa cha kwanza kukifanya ni hicho,
nikafungua sehemu hiyo ya siri ma nikachukua hicho chombo, na alipofika huyo
mtoto wao mkubwa nikamkabidhi...
‘Ina maana huyo mtoto wao mkubwa anafahamu ni nani aliyemuua baba
yao?’ nikamuuliza.
‘Kile chombo kilikuwa kinachukua matukio ya mle ndani ya ofisi na
mazungumzo yake na watu mbali mbali, na muuaji, alijitokea mara moja akiwa
kavaa nguo za kuficha sura, kwahiyo sizani kama huyo mtoto wake anamfahamu huyo
muuaji...,mimi niliwahi kuchukua kile ambacho hakikuwa wazi, ambacho mitambo
yake ndio ipo huku chini,
‘Sasa wewe ulifahamu vipi kuwa muuaji ni nani?
‘Wewe unauliza sana maswali, kama polisi, tunywe, tustarehe,
tusahau machungu ya dunia, unasemaje...’akasema huku akinisogelea akitaka
kunibusu, nikawa natumia mbinu za kumweka mbali, ili niaweze kupata taarifa
muhimu, nikasema;
‘Kuongea pia ni sehemu ya starehe, niambie kwanza,una wasiwasi
gani, umeshasema huku hakuna mtu anayeweza kutuingilia, tuongee, ili tujuane
vyema, mimi sipendi mpenzi mwenye papara au ndio zenu za hit-and run...’nikamwambia.
‘Aaa, bwana, wewe umesema una mcumba, hata nikikufahamu vyema
itasaidia nini, leo ok, nimekuelewa, tutakuwa tukikutana hivi kwa siri au sio,
...’akasema.
‘Unajua mimi nina tatizo moja, ukiniambia jambo likanivutia,
natamani kulifahamu vyema, na mimi nimekupendea kwa jinsi unavyoweza kuchunguza
mambo na ujanja mwingi, …’nikasema
‘Hapa uemfika kila kitu najua…’akasema
‘Sasa wewe mwenyewe umenugusia maisha ya huyo marehemu yamenivutia
sana, niambie wewe ulimgunduaje huyo muaji wa marehemu kwasababu mimi
ulivyonieleza, naweza kukuhisi kuwa wewe huenda ndiye uliyemuaa huyo marehemu,
?’ nikamuuliza
‘Hapana mimi nisingemuua tajiri wangu, ili nipate nini, mimi siku
ile niliondoka mapema niliposikia mke wangu kashikwa na uchungu, na nikapigiwa
simu kuwa tajiri yangu kapigwa risasi, nikaja kwa haraka, na cha kwanza ni
kufanya kama alivyoniagiza mimi nifanye nikatimiza…’akasema,
‘Kwahiyo kumbe hata wewe humfahamu vyema huyo muuaji wa marehemu ,
unafanya kukisia tu, na ujanja wote huo, ulishindwa kumfahamu muuaji wa bosi
wake, au unaogopa kuniambia...?’ nikamuuliza
‘Kwakweli mwanzoni nilikuwa nachanganyikiwa hata mimi , kwa
asilimia kubwa nilikuwa nawatuhumu watu wawili, ...kuna jamaa mmoja,
alikuwa anafika fika sana na ni rafiki wa marehemu namfahamu sana, japokuwa
alikuwa mgonjwa,..siri zao nazifahamu…’akatulia
‘Nilishangaa mtu mgonjwa, anawezaje kufika hapo…nikachunguza
nikajua watu hawa wapo kitu kimoja..huyu mtu wakawa hawaelewani, unajua siku
ile mitambo ilizima kama isingelizima ningeligundua kila kitu..,..., hata siku
ile wakati naondoka, huyo jamaa alikuwa ameshafika....yeye nikamtuhumu sana,
polisi hawakufaamu kuwa mtu huyo aliwahi kufika hapo mimi nilikuwa najua...’akasema.
‘Mtu gani huyo wewe ulimgunduaje?’ nikauliza
‘Mimi na marehemu siri yetu ni moja, ....aah, achana nye huyo, ila
kulikuwa pia na dada mwingine, ni mtu wa karibu na huyo marehemu , nilimshuku
sana, nakumbuka hata wakati naondoka, niliongea na mtoto wa marehemu, huyo
mtoto wa marehemu akaniambia niwe makini sana na huyo dada, kwani kamshuku
anaweza kufanya jambo baya kwa baba yake....’akasema.
‘Mhh, kwahiyo....?’ nikataka kumuuliza swali, lakini akanikatiza
na kusema.
‘Hawo wawili niliwatilia mashaka sana, nikajua wao ndio
walishirikiana kumuua Bosi wangu mpendwa....’akasema
‘Kwanini uwatilia mashaka hawo watu wawili…?’ nikamuuliza.
‘Kuna mabishano ya mara kwa mara ya watu hawo, na kulikuwa na
mambo ya mikataba yao ya siri, walikuwa hawajaelewana, nikajua ni yale mambo ya
marehemu ya kuwabana watu ili apate pesa kutoka kwao, japokuwa nilikuwa
nawafahamu hao watu, lakini mambo mengine kama siri za mikataba yao alikuwa
haniambii, .....’akasema.
‘Kwahiyo ikawaje tena usiwashuku watu hawo?’ nikamuuliza.
‘Siku moja, nilifika nyumbani kwa huyo bosi, wakati nafika
mlangoni, nikawasikia,, ...mtoto alikuwa akiongea na mama yake,...hiyo
sehemu nimeirekodi, siunajua tena mitambo ipo wazi wakati
wote,hawakufahamu kuwa mimi nipo hapo mlangoni,, na wakawa wanaongea jinsi gani
wataweza kuisafisha damu ya marehemu, kwani mtoto alikuwa akisema alikuwa
akimuota baba yake akimjia mara kwa mara
‘Mimi nitakutafutia mtaalamu atakusaidia...lakini usije ukajiweka
roho juu, kuwa marehemu anakujia, hizo ni ndoto tu, unasikia mwanangu....’mama
akamwambia mtoto wake
‘Lakini naota ndoto za kutisha, najuta kwanini nilifuata ushauri
wako, mama sizani kama nitaweza kulisahau hili, nilikuwa nampenda sana baba...’akasema
huyo jamaa kumwambia mama yake
‘Kama usingelifanya hivyo, ungeliwezaje kumiliki hilo jengo na
mali za marehemu nishukuru sana mimi kwa kukushauri hivyo, ...;akasema huyo
mtoto.
‘Mama mimi sitaweza kulisahau hilo tukio,japokuwa tumelifanya kwa
makini na hakuna anayeweza kutushuku sisi, labda huyu mlinzi wetu , nina
wasiwasi kuwa atakuwa katuhisi, kwani nilipochelewa kumpa zile pesa zake, aliniambia
anafahamu kuwa sisi huenda tunahusika na kifo cha baba,.....’akasema.
‘Atafahamu vipi, kwani siulisema uliharibu kumbukumbu zote kwenye
ule mtambo wa kunasia matukio,..’mama akasema.
‘Kuna ule mtambo wa chumba cha baba, ….unajua ile ni siri ya baba,
niligundua kuwa pale pia panachukua matukio, na siku nilipofika sikukuta kitu,
ina maana kuna kitu kilichukuliwa, sasa nina wasiwasi na huyu mlinzi, ..kitu
ambacho kinanitia wasiwasi...’akasema
‘Kama ni hivyo, kwanini asimfuate huyo marehemu ....kwasababu
akibakia hai, hutakuwa na amani...’akasema mama.
‘Tukianza hivyo, tutaua wengi, kwasababu hata yule mwanadada
aliyekuwa akifanya kazi na mzee, pia na yeye anadai ana ushahidi huo huo , na
yule ni hatari zaidi ya huyu mlinzi wetu, huyu mlinzi wetu, ukimpa pesa
atanyamaza lakini yule mwanamke, hawezi kufanya hivyo, na amekuwa akihangaika
kumtafuta muaji, ...’akasema.
‘Kama ni hivyo unafikiri tutafanya nini, ....ni kuwamaliza mmoja
baada ya mwingine kwa mbinu zetu…, sio lazima kwa kifo cha hapo hapo, tunaweza
kutumia sumu,...na ajali za kawaida tu, hilo niachie mimi, wewe hakikisha huyo
mlinzi, unamweka sawa...’akasema mama.
‘Basi niliposikia hivyo, sikuwa na amani....cha kwanza
nilichofanya ni kwenda kuangalia kile kifaa nilichokichukua kwa marehemu,
....nilikuwa sijapata muda wa kukiangalia mwanzo hadi mwisho, ndipo nikagundua
ukweli...kumbe...ndio yeye aliyefanya hivyo...’akasema an kutulia.
‘Nikagundua kuwa kumbe nina ushahidi mzuri sana, nikawa nawaza
nifanye nini, niwaambie polisi, nikaona hapana muda bado wa kufanya hivyo...
‘Nikahakikisha ule ushidi nimeuweka sehemu ambayo hawataweza
kuupata, kwanza nilitaka niutumie kutajirika, baada ya hapo, kama watanizid
nguvu, nawakamatisha kwa polisi,..ndio sasa wameanza kunijali, nafahamu
wanatafuta mbinu kuupata huo ushahidi nilio nao, halafu waniue, lakini
nilimwambia huyo jamaa akiniua na yeye ajue anakamatwa...’akasema.
‘Kwa vipi sasa....akikuua, polisi hawajui kuwa unafahamu siri
zako..’nikamwambia.
‘Nimeziweka mahali ambapo, hawataziona, na nimeshatayarisha
taarifa yangu, nikaiweka mahali ambapo, nikifa tu, itasambaa...kuwepo kwangu
hai ndio naweza kuidhibiti isivuje…mimi ni mtaalamu usinione hivi..’akasema.
‘Sasa kwanini uishi maisha ya hatari kihivyo, waambie polisi,
utakuwa umejiokoa, kwasababu kwa hivi sasa unafanya makosa, polisi walifahamu
kuwa unamfahamu muuaji na una ushahidi umeuficha, utashikwa kama na wewe
ulihusika, waambie polisi, uoshe mikono yako....’nikamwambia.
‘Mpaka nihakikishe nimekipata ninachokitaka, wana mali nyingi
sana,na pia wameharibu, urithi wa baba yao, kwenye huo urithi, mimi nilitakiwa
kupewa sehemu ya mali, kwani mimi mzee yule alinithamini sana, sasa nimewaambia
ili hayo yaishe, wanijengee jumba la maana, na liwe na miradi, ili niweza kukaa
hapo na kusahau kila kitu...’akasema
‘Wameshalitimiza hilo?’ nikamuuliza
‘Wameanza, nimepata kiwanja, na tayari ujenzi umeanza, sina
wasiwasi, ndio unaniona na mimi nastarehe, kama alivyokuwa akifanya yule mzee,
yule, ..kwasababu mzee, alikuwa akinijali, wao wakajifanya wanaanza
kunisahau...’akasema.
‘Kwenye huo mtambo, hakuna ushahidi unaoweza kuwakamata hawa watu
kuachilia mbali huo ushahidi ulio nao wewe?’ nikamuuliza, nikamuona keshachoka
na maswali, akasema ...
‘Wewe sasa unauliza maswali mengi, ...hebu njoo hapa
nikuonyeshe..’akasema na tukatoka hapo akanipeleka kwenye hicho chumba chenye
mitambo ya usalama, mimi sikuwahi kukisia kuwa chumba hicho nacho kina mitambo
hiyo, kilikuwa chumba, kama stoo, lakini kwa ndani kuna chumba kingine, na humo
kuna mitambo kama ile ile ninayoifahamu mimi, usingeliweza kuligudua hilo.
‘Unaona hapa, hapa kuna mitambo, ambayo haijawahi kuzimwa, ile ya
juu, inazimwa mara kwa mara, lakini hii ipo wakati wote, na anayeusimamia huu
mtambo, ni huyo mtoto wa marehemu, akifika, anahifadhi kumbukumbu zote za siku,
na kusiweka, mahali pa usalama, kwahiyo hilo tukio analo yeye, na sizani kama
atakuwa hajaharibu hiyo sehemu.
‘Sasa wewe uliwezaje kuipata hiyo sehemu?’ nikamuuliza.
‘Si nimeshakuambia kuwa ,Marehemu alikuwa anafahamu hayo yote,
kwahiyo kule kwake, kuna mtambo mdogo, wenye mawasiliano na huku,..kila
akifika, anaangalia, anawasiliana na huu mtambo mkubwa, anajua ni kitu gani
kilitokea, hakuwa na haja ya kufika huku.
‘Kwahiyo wewe ulipofungua, kama alivyokuelekeza mzee, ukaona tukio
zima..hukumwambia mtoto wake mkubwa?’ nikamuuliza.
‘Nilipokichukua, sikuwa na haraka ya kuangalia kila kitu, nilikuja
kukiangalia baada ya kusikiliza hayo mazungumzo kati ya mtoto wa marehemu na
mama yake,siku ile...ndipo baadaye nikaenda kukiangalia kwa makini, ndio
nikaoana tukio lilivyokuwa...aliiingia kwa njia hiyo tuliyoingilia sisi pale
pale…umeona eeh…, akajibadili, akavaa kama mafundi, akajifunika uso mzima,
usingeliweza kumtambua...akaenda chumba cha yule mwanadada,akachukua bastola...
Hapo hapo….polisi mpoo….akilini nikawa nasema hivyo!
Tuendelee…
WAZO LA LEO: Hakuna siri hapa duniani…kila mtenda mema
atakumbukwa kwa wema wake, na kila mtenda maovu atakumbukwa kwa uovu wake,
usijifanye wewe ni mjanja sana wa maovu, ukafikiria siri zako hazitagundulikana….unajidanganya,…
uovu, dhuluma,ukatili unanuka kama mzoga, japokuwa hatuhisi harufu yake…lililojema
ni kutubu, kwa toba ya haki na kumrejea mola wako….
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment