‘Ndugu wajumbe hiki ni kikao cha hitimisho cha kikao kilichopita,
kama mnakumbuka vyema, kikao kilichopita tulikikatisha kutokana na muda, na pia
wajumbe walishachoka, na pia tukaomba wale wajumbe waliotarajia kusafiri
waahirishe safari zao, lakini kutokana na mambo yaliyokuwa juu ya uwezo wetu,
mengi hayakufanyika kwa wakati, kama mlivyoona wenyewe,...sintofahamu
iliyotokea na baadhi ya wajumbe wa kikao hiki wakakamatwa.....’Mwenyekiti
akaanza kuongea.
‘Poleni sana kwa mkasa huo, kama wanafamilia sote lilitugusa, ndio
maana tulikuwa bega kwa bega kuwaombea dhamana wale waliokamatwa, lakini
tulikataliwa kutokana na pingamizi za wanausalama hao...’akaendelea
mwenyekiti.
‘Wakati mwingine tunaweza kuwalaumu polisi kwa jitihada zao,
tukaona kuwa wanatusumbua, wanatumia mabavu nk, lakini wakati mwingine inakuwa
haina jinsi, kwani raia ambao walitakiwa kutoa ushirikiano, wanakuwa
wagumu, wanaficha ukweli kwasababu zao binafsi, na hapo ndipo polisi wanapoamua
kutumia nguvu...na wakati mwingine wanafanikiwa, au sio..'akasema mwenyekiti, na wajumbe wakikuwa kimia.
‘Siwezi kuwalaumu sana wale mliofanya hivyo, lakini kuna mambo
ambayo nataka kuyaweka wazi kama wanafamilia, huenda wengine hawatanielewa,
lakini ni vyema nikaeleza sera na taratibu za familia hii, mimi bado ni
mwenyekiti wake, na kama bado mnanitambua hivyo, ni lazima nisimamie yale
mamlaka ya kifamilia yetu hii kuu...’akatulia.
‘Katika familia hii, tumejitahidi sana kuwa mbali na kashifa,...na
hili nimekuwa nikilirudia mara kwa mara katika kila kikao, na kile anayekuja
kuoa kwetu, au tukimleta muolewaji hapa, ninajaribu kuwaasa kuhusu hili, lakini
hali inazidi kubadilika, ...sijui kwanini, labda ndio karne hii ilivyo.
Kiukweli hili lililotokea limetutia doa kubwa, na sijui
tutafanyaje ili tutaweza kujiisafisha, japokuwa tumesalimika kihivyo...mimi sitaacha kulisema hili...sikufurahia na kitendo hiki kabisa,, nawaonya tena, hili
lisijirudie. Hatutaki kashfa kwenye hii familia, mnasikia…
'Ndioooh..'wajumbe wakasema
‘Hebu niwauliza ni nani anayependa kukaa jela, hivi jela ni
kuzuri,....hivi ni nani anapenda kukaa na wasiwasi, akakosa raha na amani akawa
anaishi kwa mashaka-mashaka, hakuna anayependa kuwa hivyo, sasa kama hatupendi
kuwa hivyo, kwanini tujiingize kwenye yale mambo ambayo tunayaona
yanaleta kashfa, yanatuweka katika hali ya kukosa amani na usingizi,
kwanini....?’ akawa kama anauliza.
‘Ndio maana katika familia hii tunalipinga sana hilo..., na wale
wanao-olewa au kuoa ndani ya familia hii, nimewaonya na nitendelea kuwaonya
tena na tena, hatutaki kashifa, na kama una dalili na mienendoo hiyo mibovu,...tutakusakama, mpaka ubadilike, au uondoke wewe mwenyewe maana hutufai.
‘Sasa basi, tunaanza kikao chetu, na ajenda moja kubwa, ni hitimisho
ya ajenda muhimu ya matatizo ya familia husika…tunaweza kuiita ni ajenda ya
hukumu.
Lakini kabla ya hukumu, ningelipenda tuliweke wazi tukio zima
lilivyokuwa, najua kila mmoja ana dukuduku la kufahamu ni nini kilitokea, ni nani hasa muuaji wa Makabrasha, huyu mmuaji kapatikana au bado.
Tunashukuru mungu kuwa wajumbe mpoo,..nani hayupo, maana kama kuna mtu hayupo ujue bado yupo na wenyewe polisi...
Sasa bila kupoteza muda,...nimeona hili ni muhimu, na niliongea na watu wa usalama, wakasema haina shida, tunaweza kuliongea tu,...kuwa mwenzetu mmoja hapa ambaye
alishirikiana na polisi hadi kufanikisha juhudi za watu wa usalama, na tunavyoongea hapa, muuaji anaweza kuwa mbaroni, ...
Aliposema hivyo watu wakapiga makofi.
Sitaki mimi niongee hili mwenzenu ndiye ataongea hili, nasikia mahakama mahakama ilimpa onyo kwa kuingilia kazi za polis bila kibali, lakini kwa namna nyingine imemshukuru sana, na wamependekeza kama inafaa apate ajira huko huko, ni yeye mwenyewe tu.
Kwahiyo basi….tunakuomba, mke wa docta, uchukue nafasi hii utuliezee japokuwa kidogo, jinsi ilivyotokea
hadi mkafanikiwa kumpata Muuaji, sasa hivi hakuna kikikwazo, kuelezea hilo au sio, au badoi haturuhusiwi maana mimi sijapewa taarifa na nilipoomba kibali cha kikao, niliambiwa niendelee tu hakuna shida...’akasema
mwenyekiti,
Mke wa docta, akakohoa kidogo na kusema;
‘Mhh, naona hiyo mke wa docta, unaipenda sana mzee, hahaha, sawa sio shida, itaendelea kuwepo tu kama sifa..., japokuwa
imeshafika mwisho…hata hivyo, sio mbaya, ila yupo atakayekuwa hivyo, mungu
akipenda sio mimi tena....’akasema huyo msemaji, na mwenyekiti akadakia na kusema;
‘Samahani, unafahamu hilo halijawa wazi kwenye hiki kikao ndio
maana tunaendelea kukuita hivyo mke wa docta, mimi kama mwenyekiti sijapata taarifa kamili, na hata kikao hiki ambacho ni wanafamilia, na wao wanahitajia kulisikia hilo....’akasema mwenyekiti
‘Kwakweli mazoea yana taabu, hata mimi mwenyewe huwa ninajisahau
na kujiita mke wa docta, lakini ukweli ndio huo, na kuanzia leo ningelifurahia
mkisema, aliyekuwa mke wa docta,...’akasema huku akiinamisha kichwa chini.
‘Hili msishangae, nimeamua hivyo kwa hiari yangu mwenyewe, baada
ya kuona kuwa sitakuwa nimemtendea haki mwenzangu , kwa yale yaliyotokea mimi
nimeona niwajibike, na kuwajibika kwa muungwana ni kuachia ngazi zu sio…na pia
kutokana na kazi zangu mwenywe nimeona kuwa nahitaji kukaa mwenyewe ...maana
huwezi kulazimisha jambo kama moyo hautaki.
‘Ni ukweli usiopingika kuwa tumeshamaliza taratibu zote za talaka,
kisheria, na hivi mnavyoniona nipo mbioni kuelekea kijijini, huko
nimeshajipanga, nina miradi yangu na maisha yangu, na nitakaa kwa muda hadi
hapo nitakapoamua ni nini kingine cha kufanya, maana ukiingia kwenye hii fani,
muda wote unahitajika, ..ila kiukweli kutokana na haya yaliyotokea nisingelipenda
kufanya kazi za kutumwa-tumwa tena, inafikia sehemu unajizalilisha,...ndio kazi…,
lakini jamii haiwezi kukuelewa, sasa hivi nataka kujituma, na
kujiajiri....’akasema .
‘Kwanza kabisa nawaombeni sana radhi wajumbe wa kikao hiki na wanafamilia hii, kwa
hayo yaliyotokea, mimi kama binadamu nimkosaji, na mkosaji anastahili
kusamehewa, ...ni kweli nimekosa sana, hasa kwa mume wangu, yeye nimeshamuomba sana
masamaha, na japokuwa kanikubalia, lakini bado nahisi sijasamehewa, moyoni nahisi hivyo…., maana
kosa nililolifanya kwake ni kubwa sana,...’akasema huku akimgeukia docta.
Docta akatikisa kichwa kukubali tu...hakusema neno.
Naona nianze kutoa maelezo, japokuwa yameshapita, lakini kwa faida
ya wanafamilia, nitaelezea ilivyokuwa;
‘Kwa ujumla aliyemua Makabrasha ni mtalaamu wa hali ya juu, alifanya
hilo jambo kwa kuangalia nyakati, ..., na aliyapanga hayo mauaji kwa utaalamu
wa aina yake...ilikuwa vigumu sana kumnasa, kwanza alienda na muda na pili
akawa anatumia madhaifu ya watu, na kuyachanganya na matukio, kiasi kwamba
polisi walifikia kuhisi huyu au yule, bila kupata ushaidi kamili.
Hata mimi mwenyewe sikuwa na uhakika na kile nilichokuwa
nikikiwaza kwani hata yule niliyemuwaza kuwa ndiye, mwisho wa siku nilijikuta
nakosa ushahidi kamili, na hata nilipotoa wazo kwa polisi, wao walishia kuniona mimi ndiye muuaji.
Wao walishakusanya ushaidi wao wa kutosha kwa muuaji, kuwa ni mimi , nikishirikiana na mume wa familia, kwani mimi
ndiye niliyekuwepo kwenye hilo jengo, na silaha niliagiza mimi, na silaha iliyotumika nilikuwa nayo mimi,
na sababu za kumuua marehemu nilikuwa nazo mimi, na nilishawahi kutamka kuwa
nitafanya hivyo......
Mwishowe nikapewa mimi jukumu la kumpata huyo muuaji, kama sio mimi, kilichonisaidia ni kuwa humo ndani ya watu wao kuna watu wananifahamu japokuwa ni kwa siri kubwa, na wananiamini,..pia nafahamu sheria na jinsi ya
kujitetea, na kwahiyo hawakuwa na jinsi bali ni kunitumia mimi.
Kwa pamoja tukafanya jambo lililoshindikana.
**********
Kwanza niliwaambia ili kumpata huyo muuaji, kwanza tumchambue huyo
mtu, aliyefanya hayo mauji, anaweza kuwa na sifa gani,… kwani mimi nilikuwepo
humo ndani, na mazingira ya humo ndani nilishayasoma karibu yote.
'Humo ndani hawezi kuingia mtu akafanya mauaji kama hayafahamu mazingira ya humo..'nikawaambia
'Maana kuna vifaa vya hali ya juu vya kuhisi silaha...kuna walinzi wa seehmu ya kuingilia na walinzi wa nje wasiojulikana wapi walipo, wanatumia mitandao tu, kwahiyo ni lazima mtu huyu alifahamu hilo, pili awe,analifahamu hilo jengo vyema kiramani.., maana mauaji hayo
yalifanyika kwa muda mfupi, na kwa tahadhari ya hali ya juu, ...
Niliwaambia kuwa mtu huyo inaonekana kama alipita mlangoni ni mtu
nayefahamika, na hata walinzi hawakuwa na shaka naye, 'kama alipitia
mlangoni,..', na angelipitia wapi maana mlango ni mmoja na mlangoni hapo ndio utaruhusiwa kwenda juu au chini,..
Jengo hilo lina juu na chini, watu wengi hawafahamu hilo...na sehemu ya chini haitambulishwi kabisa, zaidi ya marehemu na watu wake maalumu.
Nikawaambia huyo muuaji, alipomaliza hiyo kazi atakuwa alikimbilia
vyumba vya chini na kukaa huko hadi hali ilipotulia, ...na ina maana huyu
muuaji ana chumba maalumu cha kujificha huko chini, sasa ni nani anayelifahamu
hilo jengo vyema, zaidi ya Makabrasha na mjenzi wake....hapo ikawa kazi
kumtafuta mtu anayejulikana kuwa analifahamu hilo jengo vyema, ..
‘Lakini pia mtu huyo awe anafahamu mtandao wa ulinzi wa lile
jengo, awe anaweza kuusimamia huo mtandao, bila watu kujua, na awe anaweza
kuona ni kitu gani kinafanyika ndani ya hilo jengo, ina maana basi kwasabbau
hii huyo mtu hawezi kuwa ni mmoja, ni lazima walishirikiana watu wawili....
‘Kwa hoja hizo, hakuna zaidi ya Makabrasha mwenyewe,..’wakasema
'Mimi nina tetesi na watu watatu, ...'nikasema
'Kwa uchunguzi wangu niliwachuja mpaka nikabakiwa na watu watatu, mjenzi wa hilo jengo, mtu wa karibu wa Makabrasha na mtoto wake Marehemu, kati ya watu hao nahisi mmoja atakuwa anahusika, au wawili walikula njama ya pamoja.lakini huyo wa tatu hana nguvu, …huyu
wa tatu namuondoa
'Mjenzi wa hilo jengo nilishamchunguza sana nikaona kuwa haweza kufanya kitu kama
hicho, tunabakiwa na watu wawili ninaowafahamu mimi …’nikasema
‘Tuambie ni nani na nani
‘Mmoja ni mtu aliyaminika sana na Makabrasha, na huyo ni mtu
mwanifu sana kwa Makabrsha, lakini huwezi kumuona akiwa karibu na Makabrasha, mtu huyu hajulikani sana machoni
mwa watu, maana hajionyeshi, kuwa ana mahusiano na marehemu.. Anayemfahamu huyo
mtu kuwa ana ukaribu na Marehemu ni mtoto wake, na mimi tu
‘Ni nani huyo mtu..?’ wakaniuliza.
‘Ni mlinzi wake wa karibu, ...lakini sio wa kukaa naye !..’ nikasema
'Kwa vipi...?' wakauliza
'Huyu anamlinda Makabrsha kwa mtandao,..na akiona shaka tu anawapigia walinzi wa karibu wa Makabrasha...yeye anavyoingia kwenye jengo, wengi hawafahamu, wakati mwingine wanamuita 'mzuka'...
'Ni nani huyo...?' wakauliza
'Basi nikawatajia huyo mtu ni nani na wapi anaishi, polisi hawakutaka
zaidi kwanza, wakaanza kumfanyia uchunguzi bila hata ya yeye mwenyewe kufahamu, ikaja
kugundulikana kuwa ni kweli siku hiyo ya mauaji huyo mlinzi kweli alikuwepo
sehemu yake.
**************
Lakini muda mchache baadae mtu huyo alipigiwa simu, mkewe alikuwa mjamnzito,
akawa anahitajika nyumbani kwake kwa haraka, kumbe mkewe alikuwa mbioni
kujifungua, kwahiyo akaondoka sehemu yake hiyo baada ya kuwasiliana na Marehemu
mwenyewe
Na ushahidi upo, muda mwingi, alikuwa hospitalini, na muda
aliotoka hapo hospitalini kurudi nyumbani ulikuwa muda ambao mauaji yalishafanyika, kwahiyo akawa hahusiki kwa upelelezi wa polisi..kwahiyo akaambiwa huyo mtoe
‘Haya tuambie huyo wa pili ni nani,....?’ wakaniuliza
‘Ni mtoto wa Makabrasha,...’ nikawaambia na wao wakaguna na
kuniambia, haya tuelezee toka lini mtoto akamuua baba yake...lakini ngoja tuone,
Wakachunguza nyendo za huyo mtu kwa siku hiyo, ikaonekana kweli siku hiyo hakuwahi kufika kwenye hilo jengo, hata mimi pamoja na kumweka kwenye orodha hiyo, sikuwa nimempa nafasi ya kuwa muuaji...maana haya mimi mwenyewe nafahamu kuwa siku ile muda wote hakuonekana
kwenye jengo, na kama angelionekana walinzi wangeliniambia,…’nikasema
‘Una uhakika gani kuwa walinzi walikuambia ukweli wote..?’
wakaniuliza
‘Kuna watu wangu humo humo wasingeliweza kunificha mimi,…kwahiyo
yeye haiwezekani kuwa aliingia humo, atakuwa alipitia wapi, na isitoshe yeye ni
mtoto wa marehemu, kwahiyo mimi siwezi kumshuku sana yeye.
‘Ni nani mwingine ambaye ana sifa hizo zote..?’ nikaulizwa
Hapo sasa nikawa sina la kusema, ina maana aliyebakia ni mimi,
....’
‘Na wa tatu ni wewe au sio....’wakasema polisi na hapo ndio walipasubiria
ili kuninasa mimi
‘Ni mimi…! Hapana…sijamuua Makabrasha…’nikajikuta nimesema hivyo,
na wao wakacheka,
‘Sasa nani mwingine..tuliyajua haya yote, tulitaka ujilete wewe
mwenyewe na hoja zako hizo sio kwamba tulikuwa hatujazifanyia kazi, tulishazifanyia kazi, lakini tulitaka tukuone labda mwenzetu una hoja za ziada, aliyebakia ni nani, kama sio wewe..’wakasema
‘Lakini mimi nisingeliweza
kumuua Makabrasha, kama ningelitaka kufanya hivyo, ningelishamuua siku nyingi
tu, na kwa namna nyingine kabisa, .....’nikajitetea.
‘Tuambie ukweli, maana wewe ulisema alikufanyia mambo mengi mabaya
na ulikuwa na hasira naye na sifa zote za huyo muuaji unazo wewe kama
ulivyozibainisha wewe mwenyewe.., kama sio wewe ni nani mwingine..?’ polisi
wakaniuliza.
‘Mimi nataka tusaidiane kwa hili, nina uhakika muuaji yupo, na
anatuchezea akili, ila sio mimi, ila yupo...ninachowaomba ni jambo moja, nipeni muda nitamtafuta huyo muuaji,wa halali…’nikasema
‘Jambo gani…?’ wakauliza
‘Kwanza…nataka ijulikane kuwa bado nipo humu rumande, muwe mnanipa
nafasi ya kutoka kila ninapohitaji kutoka, ili niendelee na uchunguzi wangu,
nina uhakika tutampata huyo muuaji, lakini kwa njia zangu nijuavyo mimi..nawaomba msiniingilia kabisa...’nikawaambia.
‘Hatuwezi kukuachia kwasababu sasa hivi wewe ni mshukiwa namba
moja,na pili kuna tetesi kuwa kuna watu wanataka kukuua, ni tetesi, na tetesi
hatuwezi kuzipuuzia,….sasa ni kwanini wanataka kukuua, ndio hapo tunamashaka...’wakaniambia.
‘Kwanini watake kuniua mimi…, kama sio kwamba wao ndio wauwaji, na
sasa wameona kuwa nilikuwa mbioni kuwafichua ndio maana wanataka kuniua,
kwanini hamjiulizi hilo, nipeni hiyo nafasi, nina uhakika tutampata huyo
muuaji halisi kuliko kuning'ang'ania mimi, niamini mimi, mimi sijamuua Makabrasha,..’nikawaambia polisi.
‘Hebu tuambie huo mpango wako wa kumpata muuaji,...?’ akaniuliza
mpelelezi wao, nikamuambia hii kazi nataka kushirikiana na mmoja wa wapelelezi
wao ninaowaaamini mimi…
‘Akina nani…?’ wakaniuliza na mimi nikawatajia, maana nawafahamu nimeshawahi kufanya kazi na watu hao, ni
wasiri wangu wa kubwa,...hata hivyo wakataka wafahamu mipangilio yangu ipoje.
‘Mimi nawaomba jambo moja, mimi nitaendelea kuwepo humu, ila muda
fulani fulani nipeni ruhusa ya kutoka, na nyuma yangu wawepo hao wapelelezi, kwa
kificho, wasijulikane kabisa,…’nikawaambia.
Na pili chombo cha kuvaa ambacho, nikikivaa mtaniona kila
ninapokwenda...’ wakaitana na kukaa kikao chao, wakajadiliana na baadaye
wakanikubalia, lakini ni baada ya mabishano yao marefu, kwani wao walitaka kila
hatua niwe pamoja nao, nikawaambia kwa njia hiyo hatufanikiwa. ..
‘Siku ya kwanza sikufanikiwa, na ya pili,….ikawa sasa kuna kukata
tamaa, yaonekana mimi najaribu kupoteza muda, …ujue hadi hapo bado na wao
walikuwa hawana ushahidi wa uhakika kuwa mimi ndiye muuaji...ni kwanini kuna watu wanataka kuniua mimi...ni kwanini....., vinginevyo
wasingelipatia hiyo nafasi.
Siku ya tatu, ndio mambo
yakajileta, na siku zote hizo nilikuwa nikienda kwenye hoteli moja ambayo jamaa
hawo ninaowashuku hupenda kwenda kustarehe hapo, na humo kuna seehmu maalumu marehemu aliweka vifaa vyake pia, ...vya kuangalia jengo lake kwa mbalia...humo kuna kila starehe, na nilijua
udhaifu wao, ni pombe na umalaya...
‘Mimi nikajiweka kinamna, nilipewa gari, la kifahari, na
pesa kidogo, nikajifanya kama binti wa geti kali, nilijibadili kabisa, na
ungeniona usingelinitambua kuwa ni mimi, huwa nikiwa kazini nabadilika
kabisa,....maumbile, mwendo, sauti...huwezi amini...
‘Wanaume kwa uroho wao, waliponiona ile siku ya kwanza, wakaanza
kunimezea mate, maana nilitokelezea, hata ingelikuwa ni nani, angenitaka.
Wakwanza nikamtolea nje, maana sikuwa na haja naye, akaja mwingine na mwingine,
hadi siku ya tatu alipokuja mtu wangu ninayemtaka....
‘Mtu niliyemlenga sana na huyu mlinzi wa karibu wa Marehemu, mimi huyu nilimweka kwenye shuku zangu...
Kwa kipindi hiki, sasa anafanya kazi kwa mtoto wa Makabrasha, huyu nilikuwa bado sijakata
tamaa naye, ..hisia zangu zilinituma kuwa huyu mtu atakuwa anahusika kwa namna mja au nyingine...na hasa nilipoona bado anaendelee kuwa karibu na mtoto wa Makabrasha, nikajua kuna kifo kingine kitakuja,...
Jingine hawa watu wawili, mtoto wa marehemu na huyu mlinzi walikuwa hawaivani kabisa, kipindi cha uhai wa marehemu,...walikuwa ni maadui, leo hii wanaelewana, hapa nikatilia shaka..ni kwanini....
‘Siku hiyo huyu jamaa akanijia,...nilikuwa nimekaa meza ya peke yanu nikionekana kumsubiria mtu...nashangaa mtu huyu.... na alionekana kuwa na pesa kweli,
nikahisi wana jambo wamelifanya, nikajibaragua na baadaye tukaelewana,
hakunitambua kabisa kuwa ni mimi, hata ingelikuwa nani, asingelitambua, ...
‘Tukaanza kuongea kidogo, moja likazaa jingine, tukawa marafiki wa
muda mfupi, mimi naifahamu sana hiyo kazi, nina uzoefu nayo, jinsi ya kuwanasa hawa viumbe waitwao wanaume,..sijisifii, lakini sijawahi kufanya makosa, najua madhaifu yao yapo wapi.....jamaa bila
kujijua akanasa kwenye anga zangu....sikumchelewesaha, wakati anakwenda
kujisaidia mimi nikaweka kitu kwenye kinywaji chake.
‘Kuna aina ya madawa ukimwekea mtu, analewa haraka, anakuwa kama
kapagawa hivi...lakini hapotezi fahamu, wanaitumia sana majasusi wanapotaka
kupata taarifa kwa mtu,...niliiomba kwa watu wa usalama, wakanigaia, na hiyo
ndiyo ilikuwa silaha yangu, sikutaka bastola hapo...
Aliporudii kutoka kujisaidia, nikaendelea kumelegezea, kwanza
alijaribu kuwa muangalifu,…unajua tena watu waliopitia uaskari walivyo,..lakini
hakunielewa, ikafika muda akajisahau na kuanza kunywa kile kinywaji,..nilimuona
kama anasita lakini huyo akanywa,..mara kaanza kulegea, na akili ikaanza
kumtoka, na mimi hapo hapo nikamwambia;
‘Mimi ni mchumba wa mtu, sitaki kuonekana onekana hadharani hivi,
nilikuja hapa tu kupotza mawazo,…nataka kuondoka,…’nikasema
‘Oooh, hapana, usiwe na wasiwasi, kuna sehemu tunaweza kwenda
hutaonekana kabisa, unasikia, unajua mimi nimevutiwa sana na wewe,…kiukweli
wewe nai maalumu, unsikia, sikilizaa…twende sehemu pesa sio shida…’akasema
‘Usinihadae,…nawafahamu sana nyie waume, nikiharibu kwangu utakuja
kunikimbia, na mimi sitakubali…’nikasema;
‘Kuna sehemu naifahamu, twende.....’ akasema, basi nikajifanya
nimekubali kwa shingo upande.
Nikamwambia atangulie nje…nitakuja…
‘Sikiliza wewe acha gari lako hapa, huyu mlinzi wa hapa namafahmu,
atakulindia kwa muda wowote unaoutaka, …au unasemaje, usijali kabisa..’akasema,
na alionekana kweli kazimia kwangu
Basi tukatoka hapo kwa kupitia mlango wa nyuma, yeye akaniambia
nibakie nyuma, ili yeye atangulia akaongee na mlinzi, basi akafanya hivyo,
baadae nikajitokeza na tukakutana kwenye gari lake, kabla sijaingia kwenye gari
lake ndio akaniuliza.
‘Huwa unafika hapa mara kwa mara..?’ akaniuliza
‘Ndio, lakini mara nyingi nafika na mchumba wangu, sema kasafiri,
lakini kwa vile ni sehemu nimeizoea, ..siachi kufika, lakini ni mtu ambaye
anaweza kuja ghafla,..si unajua tena…’nikasema
‘Ok..akija,…gari lipo, au sio, na sisi tukirudi nitahakikisha
unaingia mlango wa nyuma,…unaonaeeh, atajua ulitoka kidogo au sio…’akasema
‘Hata hivyo sura yao sio ngeni sana kwangu…’ akasema hapoo
nikashtuka ina maana keshanigundua nini..lakini nilikuwa na uhakika hawezi
kunifahamu, maana kuna utaalamu wa kubadili nyusi, na rangi za macho, na
nywele, sikuhitaji kuvaa ngozi bandia,...mimi katika kazi yangu hiii wanapenda
kuniita kinyonga, ....naweza tukawa pamoja sasa hivi nikaingia chumbani
nikitoka hunikumbuki tena....
Basi, yule jamaa akasema kwa vile naogopa, atanipelekea sehemu
ambayo anaiona ni salama zaidi ambayo sio mbali na hapo.., tukaingia kwenye
gari lake, na kuanza kuendesha, kama nilivyotarajia nikaona tunelekea uwanja wa
ndege, nikajua ni kule kule, na mtego umefanikiwa,
Tukafika karibu na jengo la Marehemu, jamaa huyo hakulipeleka moja
kwa moja kwenye maegesho ya mgari, akalipitisha kwa nyuma, hadi sehemu
nyingine, kunapohifadhiwa magari ya jengo la pili yake, akachukua ufungua na
kufungua geti, kulikuwa na geti dogo la jengo hilo la pili kwa nyuma....kulikuwa
hakuna walinzi.
‘Huku ni wapi? Nikamuuliza
‘Huku ni kwa rafiki yangu, ila nataka tuingie kwenye hilo jengo
hapo, ni la marehemu, kuna hoteli ya ndani kwa ndani, humo tutastarehe
tupendavyo, huyo mchumba wako hatakuona kabisa..’akasema kwa sauti ya kuonyesha
hayo dawa imemchukua na sikupenda hiyo dawa iishe nguvu kabla hatujaingia
ndani.
Tulipoingia kwenye hilo geti dogo, nikaona akifungua mfuniko, kama
ile mifuniko ya mashimo ya maji machafu, nikamuuliza;
‘Unafanya nini ...mbona unafungua mifuniko ya choo?’ nikamuuliza
‘Usijali hii ni njia muhimu ya kuingia ndani, hakuna anayeifahamu
zaidi yangu mimi na marehemu na mtoto wa marehemu....’akasema.
‘Huyo marehemu unayemtaja ni nani?’ nikamuuliza
‘Mhh, alikuwa akiitwa Makabrasha ameshafariki....’akasema
‘Mhh, yaani kafariki na kuliacha jengo nzuri hivyo, na wewe ni
mtoto wake?’ nikamuuliza
‘Hapana yupo mtoto wake, ndiye anayelimiki hilo jengo kwa
sasa..’akasema
‘Na huyo mtoto wake ni nani anaonekana ni tajiri sana....?’
nikamuuliza
‘Achana naye, akikuona wewe najua ataninyang’anya anapenda sana
kuninyanganya mawindo yangu...sio mtu mzuri, ...hana huruma, akikuambia utakuwa
chakula cha mchwa utakuwa kweli...haogopi, ...’akasema.
‘Una maana gani..?’ nikauliza
‘Usiwe na wasiwasi upo na mimi, …najua yeye ku-ua mtu sio tatizo….sio
mtu wa mchezo ila kwangu ananiheshimu, ukiwa nami hakuna shaka…hata hivyo mimi
ndiye ninayefahamu siri zake…’akasema na moyoni nikasema sawa kabisa.
‘Kumbe kuna njia hii ...’ hapo nikasema kimoyo moyo…nikatulia
kwanza, sikutaka kumuuliza sana, asije akanitilia mashaka, akafungua kile
kifuniko na kuninyoshea mkono kuwa nisogee pale, hakufahamu kuwa mimi ni mkakamavu
wa kijeshi.
‘Sasa tunaingia,…njia hii ni safi kabisa, kwa nje kunaonekana
hivyo, lakini ukiaanza kuingia ndani utazikuta ngazi, unateremka nazo..hizo
zinakwenda moja kwa moja hadi kwenye hilo jengo la marehemu, hii ni sehem yake
maalumu ya usalama, ni njia za dharura...’akasema.
‘Oh, kwanini awe na njia za namna hii, mnauza madawa ya kulevya
nini?’ nikamuuliza
‘Matajiri wengi wana mbinu zao za kuishi, wanajihami kwa kila
njia...’akasema.
‘Sasa kama ni hivyo huyo marehemu alikufa kwa ugonjwa au
aliuwawa?’ nikamuuliza
‘Walimua bwana,..alikuwa bosi wangu, nikiwa na shida, ananisaidia,
sasa nimebakia na huyu mnyama, ananifanya kama mtumwa wake, inabidi nitumie
mbinu za kumuibia, sina ujanja...kama jana nimemchomoa mamilioni ya pesa..bila
hata kufahamu, akabakia kusema kaibiwa na watu wa benki...’akasema.
‘Oh kumbe walimuua, jamaa wa watu, kwanini walimuua....?’
nikamuuliza
‘Mambo ya mali hayo, unafikiri, ukiwa na watoto waroho, wanawake
waroho, na una mali, ujue upo hatarini, na ikizingatiwa kuwa hata marehemu mwenyewe
alizipata mali hizo kwa dhuluma..kwahiy ndio hivyo maisha ya dhuluma mwisho
wake ndio huo.....’akasema na kutulia.
‘Na mara nyingi watu kama hao wanauliwa na watu wao wa karibu,
..hasa nyie mliokuwa mkifanya naye kazi karibu…’nikasema na kucheka, na yeye akasema
‘Hahaha…acha zako hizo,…keshaondoka basi …acha sisi tutumie,
japokuwa kiukweli nilikuwa na mpenda sana…’akasema
'Kwahiyo ina maana waliomuua ni mtoto wake, au mke wake, au
walishirikiana kumuua....au ni wewe ?' nikamuuliza, hapo akabakia kimia.
Akafungua mlango wa kuingia kwenye jengo, huku akiwa kimiya,
halafu akaniangalia na kusema;
'Tumeshafika...karibu hoteli ya maraha ya Marehemu, hapa usiwe na
wasiwasi kabisa....'akasema na mimi nikamuuliza
'Mhh, wasije kuniua na mimi, nimeshaanza kuogopa,…kama watu
wanafikia kumuua tajiri kama huyo sembuse mimi....'nikasema
‘Hahaha usijali , mimi nitakulinda usijali kabisa, ..’akasema
‘Mbona hukuweza kumlinda bosi wako…?’ nikamuuliza na hapo kidogo
akashtuka.
‘Mbona maswali yako yapo hivyo, usiwe na wasiwasi…’akasema
‘Hapana mimi sipendi maisha ya mashaka mashaka, …ndio maana
nakuhoji, ili nijue nipo sehemu kweli salama…’nikasema
‘Usijali…’akasema
‘Au nimekosea kukuuliza…’nikasema
‘Hapana wewe uliza tu…’akawa anaongea kilevi kilevi.
‘Mimi ukinambia jambo napenda kujiuliza uliza sana…ni nani alimuua
huyu mtu wa watu naogopa sana, mtu tajiri kama huyu anauliwa,…si alikuwa mtu
mwema, anasaidia watu au sio..?’ nikamuuliza,
‘Alikuwa mwema, wakati mwingine, wakti mwingine ndio hivyo
kutafuta, sasa kutafutwa na yeye akawahiwa, ndio maisha ajali kazini,…, unajua
ukimuongelea nakumbuka mbali sana, nilimpenda sana, lakini kazi ni kazi,
utafanyaje …’akasema
‘Kama ulimpenda kwanini hukusaidia polis wampate huyo muuaji wake,
..au muuaji unamfahamu au ni wewe?’ nikamuuliza na hapo akatabasamu, halafu
akatikisa kichwa na kusema;
‘We acha…ndio maana nakuambia ni ajali kazini, alikuwa sio mtu
rahisi kihivyo, mmh, sasa sikiliza tusiongee sana hayo, au…’akasema na kunywa,
alionekana kama dawa inaisha nguvu nilitaka nipate mwanya wa kumuongezea
nyingine,..na kweli ikapatikana kwenye gilasi yangu mwenyewe, ndio nikaweza, na
kujivunga kama nakunywa, aliporudi nikawa nimebadili zile gilasi kia-aina,
akanywa.
‘Mbona hujanijibu swali langu, mimi huwa nikiuliza swali mtu
asiponijibu nakuwa na mashaka naye…’nikasema
‘Swali gani mpenzi, uliza chochote mimi nitakujibu,..unasikia
chochote…’akasema
‘Ni nani alimuua huyu tajiri wa watu jamani…?’ nikamuuliza hapa,
akatikisa kichwa kusikitika, inaonekana kweli inamchukua hiyo hali ya
kumbukumbu, na anakuwa kama anawaza mbali, au kuogopa, vyote viwili,…nikasubiria
jibu
NB: Tuishie hapa kwa leo..naombeni maoni yenu maana kisa kinafikia ukingoni, je kuna kitu tumekisahau....
WAZO LA LEO:
Mali na watoto ni mtihani mkubwa kwa wazazi, ukiwa navyo ni ufahari,...lakini vyote hivi vina
mitihani yake. Mali ikiwa ni ya halali, inaweza isiwe ni tatizo, muhimu ni jinsi gani y kuitendea haki yake. Ama kwa watoto ujue jinsi gani ya kuwalea..wawe na elimu na maadili mema. Elimu pekee haitoshi. Elimu bila maadili mema inaweza kugeuka kuwa tatizo pia, wasomi wangapi wazuri lakini wanafanya mambo ya hatari kwenye jamii, kwa kutumia elimu yao, ukichunguza sana ni kutokana na ukosefu wa maadili mema,...
Tumuombe mola atupe mali za halali zenye tija, na watoto wema, wenye elimu na maadili mema. Aamin
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment