Kikao cha hitimisho hakikufanyika siku ya pili kama ilivyopangwa,
kwani siku ile ya hicho kikao cha mwanzo tulipomaliza tu,polisi walifika kabla
watu hawajatawanyika, na kuwakamata mume wa familia, mpenzi wake wa asili, na
mdogo wa mume wangu ambaye walishamkamta mapema. Polisi walisema sababu za
kukamatwa kwao ni kuisaidia poilisi kutokana na kifo cha Makabrasha.
Kesho yake, mimi na Docta, tulikwenda kituo cha polisi
waliposhikiliwa watuhumiwa hao. Tulipofika hapo tukaambiwa mke wa docta hayupo
kwenye kituo hicho, kapelekwa kituo kingine kwa sababu za kiusalam, kwahiyo
docta akaondoka kuelekea huko alipo mkewe.
Hata hivyo docta alitaka kuongea na rafiki yake kabla hajaondoka.
Polisi walikuwa wagumu kuturuhus kuongea na huyo mtu hata pale alipofika
wakili, ambaye alitakiwa kushughulikia dhamana ya huyo mshukiwa.
‘Mume ambiwa hao watu wameshikiliwa kuisaidia polis,….’akasema
polisi
‘Lakini mumemshikilia huyo mtu zaidi ya masaa 24, tuna haki ya
kudai huyu mtu aachiliwe au mtuambie kashikiliwa kwa kosa gani ili tufanye
taratibu za dhamana…’ikawa ni mabishano ya polis na wakili.
Kiukweli masaa mengi
yalipita, tukiendelea kupigwa danadana, kila tuliyemuuliza alisema yeye
hahusiki, mpaka ikabidi sasa kuomba kuonana na mkuu wa kituo hicho, ambaye
alisema;
‘Hawa watu tumewakamata kwa ajili ya kuisaidia polisi, hatujawakamata
kama wa halifu, tuna maana yetu kubwa kufanya hivyo, kwahiyo hamuhitajiki
kuwawekea dhamana...tafadhali mtuelewe hivyo..’akasema huyo mkuu.
‘Lakini dhamana ni haki ya mtu yoyote...’nilijitetea, sikufika na
wakili wetu kwa vile mume wangu alishamkataa, wakili tuliyekuwa naye ni yule
aliyekubalika na mume wangu.
‘Sikiliza niwaambie, hawo watu wapo hatarini, kuna tetesi, na sio
tetesi, ni kweli, kuwa kuna watu wanataka kuwauwa jamaa zenu hao, kwa
vile wanafahamu mengi kuhusu kifo cha Makabrasha, ....hivyo ndivyo ninavyoweza
kuwalezea, na kama mna akili ya kulifikiri hilo, na kama mnawajali wenzenu hao
mtaondoka na kusubiria…’akasema huyo mkuu .
‘Kama ni hivyo, basi mnaweza kuweka ulinzi nyumbani kwa hawo watu,
sio kuwaweka rumande hamuoni kuwa sehemu hiyo mliyowaweka sio nzuri,
kiafya...’akasema docta.
‘Ni kwa muda tu,…pamoja na hayo tulikuwa na maswali machache
tumewauliza, tatizo hawajataka kutoa ushirikiano, ni kwa usalama wao, na
wakitujibu vyema, ili tuweze kuyabaini mengine, hata leo wataondoka…’akasema
‘Kwahiyo kumbe sio kwa usalama wao, si ndio umesema hivyo awali…’nikasema
‘Ni kwa usalama wao, na hayo maswali ni katika kutuwezesha kujua
mambo mengine zaidi ya kuwezesha kuwabaini hao watu walio na nia mbaya ya
kuhatarisha usalama wa raia…’akasema.
Baadae baada ya kusihi
sana, ndio tukapata muda wa kuongea na mume wangu, na mdogo wake, wote walikuwa
kwenye kituo hicho, hutaamini, mume wangu hakutaka kuongea na mimi kabisa, akidai
kuwa mimi nimetumia mbinu ili tuachane naye, sikujali sana, kwahiyo akawa
anaongea na docta tu, na hata nilipomsalimia hakuitikia. Walipomaliza kuongea
na docta, nikamwambia;
‘Hamna shida, tutaonana ukitoka, nina imani tutayamaliza haya
mambo kwa amani, ..’nikasema
Na yeye hakusema chochote zaidi ya kuniangalia kwa hasira.
Na tulipotoka hapo tukaelekea kumuona mke wa docta,na Mke wa docta
hakuonekena na wasiwasi au kuonyesha kinyongo chochote, zaidi ya kujiona
yeye ni mkosaji,mbele ya mume wake, na tuliongea kwa pamoja na tulipomaliza
kuongea haya na yale, muda ulikwisha,na wakati tunataka kuondoka, mke wa docta
akamshika mume mkonona kusema;
‘Samahani sana docta,...utanisamehe sana, ...'hakutumia neno ‘
mume wangu’, nikajiuliza kwanini, lakini sikutaka kuyaingilia kwa undani.
'Nafahamu sana, mpendwa, jinsi gani nilivyokuumiza, lakini natumai
umenielewa, nataka uanze kuizoea hii hali, ya kuwa mbali na mimi,maana nikitoka
hapa, nataka nikaanza maisha yangu mengine, sitaki kitu kinachoitwa
mume..’akasema na kuniacha mimi njia panda, kumbe wao wameshafikia hapo...
‘Hayo sio muhimu, kwa sasa , cha muhimu ni wewe kumalizana na hili
hapa, na mimi nipo pamoja na wewe, hadi mwisho wa hili, na tutaongea vyema haya
yakiisha, ...’akasema docta.
‘Hili sio kubwa sana ,na hakuna cha kuongea na wewe,
tumeshayamaliza, mimi kinachonikwaza ni haya yaliyotokea huko nyuma, na sitaki
kuja kumuumiza mtu mwingine tena, nataka
kuanza maisha yangu nikiwa huru...’akasema.
Hapo nikamwangalia mdada huyu kwa makini, nikimuona kama mmoja wa
watu walioniharibia ndoa yangu, lakini sikuwa na kinyongo naye, kwani kwa
upande mwingine nilimuona ni mdada jasiri,…
Na wakati tunatoka tutakutana na rafki yangu, kaja kumtembelea mke
wa docta, akanisalimia, na mimi nikamuitikia kwa mkato, sikutaka kuongea naye
sana.
‘Bosi hujanijibu barua yangu, sijui kama natakiwa kazini au
mkataba wangu mimi na wewe umeshakwisha ....’akaniuliza.
‘Yote hayo tutayajua siku ya kikao cha familia, kwa hivi sasa
siwezi kukujibu lolote, endelea na shughuli zako binafsi tu, …maana ajira
kwangu ilikuwa ni kwa pale ni kikuhitajia, au sio, kwa hivi sasa sina kazi ya
kukuhitajia wewe...’nikasema na sikutaka kuongea naye, nikamuacha akiwa kaduwaa.
Docta akaja, kwani nilimuacha akiongea na mke wake na alipokutana
na rafiki yangu wakawa wanaongea na mimi nikatangulia kwenye gari, kwani
tulikuja kwa kutumia gari lake, na alipokuja, akaniambia;
‘Rafiki yako anasema nimsaidie kumuombea msamaha, hasa kwa hayo
aliyokutendea,...na mimi natimiza wajibu, nakuomba sana, umsamehe rafiki yako,
kwani aliyoyafanya aliyafanya kwa vile ulimshauri afanye hivyo…’akasema
‘Una uhakika na kauli hiyo…?’ nikamuuliza
‘Ndivyo alivyoniambia…yeye kasema kama alivyosema kwenye kikao,
yeye hakujua kuwa itakuja kuwa hivyo, anakuomba sana umsamehe mrejee urafiki
wenu kama zamani, kwani wewe unakuona kama dada yake mlezi, na kukukosa wewe ni
kama kumkosa mlezi wake katika maisha..’akasema
‘Hiyo kauli ndio itanifanya hata nisiongee naye, mimi nilimshauri
akazini na mume wangu, ina maana mimi sina akili..achana naye, na sitaki kabisa
kusikia neno rafiki yangu, sio rafiki yangu tena..’nikasema.
‘Ina maana hata mume wako hutamsamehe...?’ akaniuliza.
‘Nikuulize na wewe swali hilo, je na wewe utaweza kumsamehe mke
wako kwa hayo aliyokufanyia maana sote tupo njia moja..nashangaa kauli zenu,
ina maana mumeshaachana tayari?’ nikamuuliza.
‘Mke wangu kachukua maamuzi yake yeye mwenyewe, sikuwa
nimeshafikia maamuzi ya kuachana naye, japokuwa kitendo alichonitendea,
nisingeliweza kuishi naye kwa amani…’akatulia
‘Kumbe…’nikasema hivyo kabla sijaendelea kuongea, yeye akawa
anaendelea kuongea kwa kusema
‘Hata hivyo nilishamsamehe, na yeye mwenyewe akasema hataweza
kuishi na mimi tena, akaniomba na sio kuniomba , akasema tupeane talaka, haraka
iwezekanavyo, na hataki hilo tuliongelee kwenye kikao, yeye mwenyewe ataliongea
kama ikibidi,...’akasema.
‘Na wewe ukakubali kirahisi,…kwa kukubali kwako kirahidi hivyo,
inaonyesha kuwa moyoni mwako ilikuwa hujamsamehe, hukutaka kuonyesha dhahiri
kama mimi ninavyoonyesha,…au sio..?’ nikamuuliza.
‘Nilijaribu kumshawishi, na kumwambia kuwa mimi kama docta
nafahamu udhaifu huo, nipo tayari kumsamehe, na tutajaribu kuona kama maisha
yanaweza kuendelea, na hata kama ni kuachana tusifanye haraka hivyo,…..lakini
kakataa kata kata, nikaona ni bora iwe hivyo, ….’akasema
‘Je na wewe una umauizi gani juu ya mume wako...?’akaniuliza.
‘Mimi maamuzi yangu yatasikiwa kwenye kikao, kwa hivi sasa sina la
kusema, na leo natakiwa kukutana na wazazi wangu,...sijui wameniitia
nini...nahisi ni kuniuliza swali kama hilo, na kwa hali ilivyo, nahitaji muda
wa kufikiri sana, hasa nikiwaangalia watoto, watoto kwa ujumla....’nikasema
nikikumbuka kuwa wazazi wangu walinitaka niwe na kikao nao, wakasisitiza kuwa
ni muhimu sana.
‘Ni kweli katika maamuzi yako fikiria sana watoto, sio kwamba
nataka ufanye hivyo, kwa ajili yule ni rafiki yangu, hapana, na siwezi kuchukua
hiyo hali nikakushinikiza uachane na mume wako, ili turejeane…’akasema
‘Turejeane…!!’ nikasema kwa mshangao
‘Nasemea hivyo kihisia…unajua sisi sasa hivi ni watu wazima,
maamuzi yetu yanatakiwa yawe kiyoo cha watoto wetu,….’akasema
‘Ni kweli ndio maana , nataka maamuzi yangu nitakayofikia,
yasikiwe na kila mtu, sitaki kuyaongea pembeni, …’nikasema
‘Sawa ila kwa vyovyote iwavyo, ukumbuke mimi nipo na wewe… na
kiukweli mimi nakiri moyoni kuwa hatujachelewa bado….mimi nakuomba sana, kama
inawezekana turejeshe urafiki wetu wa zamani...’akasema na kunifanya nishituke
na kumgeukia.
‘Urafiki upo, mimi sizani kama tulikuwa maadui…’nikasema
‘Mhh…sio wa kihivyo, nataka ule wa kuelekea kwema, hata ikibidi
tumalizie pale tulipooshia….’akasema
‘Hahaha,...wewe una akili kweli, ina maana wewe bado kwenye akili
yako unaniwazia mimi, acha mzaha huo, hayo yalikuwa zilipendwa na kama
utaachana na mke wako nakushauri, tafuta mwanadada, ambaye anakustahili, mimi
tena, ni mama watoto, sikufai…nahitajia kukaa na watoto wngu tu…’nikamwambia.
‘Kwangu mimi wewe ni mwandada, mrembo, ....hata kama itakuwaje,
...naweza kusema mimi na wewe tuna pendo la asili, kama alilolisema mume wangu
na mke wako, kumbe hata sisi ni hivyo hivyo...’akasema.
‘Hapana, ..nakuomba sana, usije ukafanya makosa hayo, tafuta
msichana mrembo umuoe, hilo kwangu halipo nafsini kabisa, na wala usipoteze
muda wako, tafadhali unielewe, tutaendelea kuwa marafiki hivi hivi na huyo
utakayemuoa, atakuwa wifi yangu...’nikamwambia.
‘Kwanini nimtafute msichana wakati mimi sio kijana mdogo,...mimi
ni mtu mzima, ni vyema nioe mwanamke anayeendana na mimi, na wewe ndiye chaguo
langu...’aliposema hivyo
Nikageuka kuangalia pembeni, sikutaka mazungumzo kama hayo, nilikuwa
na mambo mengi kichwani ya kufikiri, nikamwambia;
‘Tuyaache hayo mazungumzo kabisa, na nakuomba tukikutana tuongee
mambo mengine sio hayo,hapa nilipo ninamawazo ya familia yangu,nina mawazo ya
maamuzi ya busara kwa hili lililotokea na sitaki nichukue maamuzi kwa
kishawishi kingine, nataka nichukue maamuzi kwa utashi wangu, na kwa manufaa ya
familia...’nikasema.
‘Hamna shida, uamuzi wowote utakaochukua nipo pamoja na wewe, mimi
ni rafiki yako wa ukweli...’akasema na tukawa tumefika nyumbani, mimi nikaingia
kwangu na kujiandaa kukutana na wazazi wangu.
***********
‘Hebu tuambie binti yetu umefikia maamuzi gani, ..?’ lilikuwa
swali la kwanza kutoka kwa baba
‘Baba siwezi kuwajibu hilo swali kwa sasa, ingelikuwa ni uwezo
wangu , na maamuzi yangu mwenyewe, ningekuwa na jibu la moja kwa moja, lakini
kuna mambo mengi natakiwa kuyafikiri, hasa watoto....’nikasema.
‘Swala la watoto, tulishakuambia, sisi tupo nao, na hata wakija
hapa hawakumbuki kabisa maswala ya baba, ndio maana tumewazoesha kila wakitoka
shule waje huku, wewe hufahamu ni kwanini tulianzisha utaratibu huo...’akasema
mama.
‘Mama, ni rahisi kusema hivyo, ....lakini, mkumbuke yule alikuwa
mwanandoa mwenzangu, na nisije nikachukua maamuzi ya haraka, hata nyie mkaja
kunilaumu, naombeni muda, na maamuzi yangu nitakuja kuwapa kwenye
kikao,...’nikasema.
‘Hicho kikao si mpaka huyo mumeo atoke huko jela, je ikionekana
kuwa kweli ndiye aliyemuua, ...kwahiyo mpaka amalize kifungo ndio utaweza kutoa
hayo maamuzi yako...?’ akauliza mama, nilimuona mama akishabikia sana nitoe
maamuzi yangu, ambayo sikutaka nichukulie haraka, nikasema;
‘Wazazi wangu nawaombeni sana, mvute subira, mimi nipo tayari
kumsubiria hata afungwe miaka kumi, huo ndio msimamo wangu....’nikasema na baba
akasema;
‘Unajua hata mimi nimelifikiria sana hilo, nimeliangalia katika
upande mwingine, nikawaza je ingelikuwa mimi nipo kwenye nafasi hiyo
ningelifanya nini…’akasema baba
‘Ungelifanya nini…?’ akauliza mkewe
‘Sio sahihi wawili hawa kuachana kwa kwasasa…’akasema, na mkewe
akabakia mdomo wazi,..
‘Leo hii unasema hivyo, unanigeuka tena…’akasema mkewe
‘Kiukweli, sio sahihi kumshawishi binti yatu afanye hivyo, hasa
baada ya kumuona mume wake pale kwenye kikao akifanya juhudi kuitetea familia
yake, hii ni konyesha kuwa kabadilika, na keshajifunza, na kwa hayo aliyokutana
nayo keshabadilika na sasa atakuwa mume mwema....’akasema baba na kunifanya
nimuangalia mara mbili, sikutegemea yeye kutoa ushauri kama huo.
‘Eti nini, hivi kweli, baba nanihii, unamshauri mtoto wako hivyo,
amrudie huyo mtu baada ya yote hayo yaliyotokea, kwanza ulimsikia mwenyewe,
huyo mume wake akitamka mbele ya watu kuwa bado anampenda mpenzi wake wa asili,…’akasema
mama
‘Ndio nilimsikia sana , lakini ile kauli haina nguvu mbele ya mke…’akasema
babaa
‘Mhh kwa hiyo hata kama watayasawazisha hayo yaliyotokea na binti
yetu akafanya makosa ya kumsamehe mwenzake, ajue kuwa anaishi na gogo, ni sawa
na gogo, maana mtu upo naye, lakini mawazo yake yapo kwa mwingine, huyo mume
wake ataendelea kuiba nje tu, wataendelea kuwa na mapenzi yao ya siri na mpenzi
wake wa asili , na ndoa yao itakuwa haina raha...’akasema mama.
‘Haitaweza kutokea tena hivyo, huyo mume atakuwa kama mtu
aliyeumwa na nyoka, hataweza kuyarudia tena hayo makosa, hilo nawahakikishia,
ila hayo nayasema kama mimi, kama nionavyo mimi,hata hivyo, binti yetu..’akasema
baba
‘Hata hivyo sio kwamba nimesema hivyo kukushauri ufanye nitakavyo
mimi, hapana, maamuzi ya hatima yako, yapo mikononi mwako,
tunakuachia wewe mke wa familia,uamue mwenyewe, mimi nimeshakuona kuwa
unaweza kufanya maamuzi yenye busara kwa manufaa yako na ya familia yako,
unaweza, na sio busara sisi tukikuingilia ....’akasema baba.
Mimi nikawaangalia wazazi wangu kila mmoja kwa nafasi yake,
nikaona kweli sasa wazazi wangu wamenielewa, na wapo tayari kunipa nafasi ya
kufanya kile ambacho nimekuwa nikikiwaza, na hapo nikasema;
‘Wazazi wangu nimewaelewa, sana, ndio maana nahitaji muda wa kwa
peke yangu kulitafakari sana hilo jambo, nisingelipenda kuchukua maamuzi ya
haraka haraka, nafahamu kabisa mume wangu na mwenzake , huyo mpenzi wake wa
asili wanapendana sana
‘Lakini pia huyo ni mume wa ngu wa ndoa,..japokuwa ukichunguza kwa
makini ndoa ni kama haipo, sijaulizia upande wa dini, maana ndoa yetu
imesimikwa kwenye imani ya dini, je imani ya dini inasemaje..
‘Hata hivyo pamoja na hayo, mimi sitaki kuja kuwanyima watu haki
zao,…kwa hayo na mengine , nahitaji muda sana wa kutafakari kwaa mapana
yake,..kama alivyosema baba, huyu mtu anaweza kujirudi na kuona makosa yake, na
akawa mume mwema, lakini kuna maswala mengine, ya familia na maisha yao ya
baadaye, nini watoto watajifunza kutoka kwake, na vitu kama hivyo ....mimi
mwenyewe nahitaji kulihakiki hilo...’hapo nikatulia.
‘Pengine katika maamuzi yako unaweza ukawa na wasiwasi kuwa watoto
hawatakua katika maisha ya raha, kisaikolojia wakimkosa baba yao wa kuwazaa, au
una wasiwasi gani binti yetu, mimi nataka nikusaidie katika maamuzi yako?’
akauliza mama.
‘Mama hilo ni moja ya jambo linalonipa shida, lakini..mmmh, ngoja
nawaulize wazazi wangu, kwa uzoefu wenu, tabia za wazazi kwa watoto wao,
zinaweza kurithiwa?’ nikauliza.
‘Hilo ndilo tulilokuitia, kabla ya kulizungumzia hilo tulitaka
tusikie kama una maamuzi yoyote, ...sasa ngoja tukupe shule kidogo ya mambo
hayo, unafahamu, ni muhimu sana, kama wazazi, ni muhimu sana kwa wale wanaotaka
kuoa, au kuolewa kuangalia maswala haya kizalia…akasema baba
‘Hatutaki kurejea nyuma kuwa tulikukanya nk…lakini kwa hili wengi
hawalijali kwa sasa, wanaona watu wakioana litajipanga lenyewe kutokana na
jinsi mtakavyoishi...kwani sasa hivi jamii zinaitwa zimestaarabika, watuy
wanakutana wanabadilika kutokana na mazingira,…’akasema baba na kumwangalia mke
wake, na mke wake, akasema;
‘Mueleweshe binti yako aelewe vyema hapo..., lakini sio kumshauri
amrejee huyo muhuni, mlevi na muongo, hizo sio tabia nzuri, zinaweza kuwarejea
watoto....watoto wenu wanaweza kuziiga hizo tabia mbaya, watarithi machafu ya
wazazi wao, ni muhimu sana hilo...’akasema mama.
‘Ina maana watoto wangu watakuwa na tabia kama ya baba yao?’
nikauliza
‘Tutakujibu hilo kwa mfano hai, angalia watoto waMarehemu
Makabrasha, chukua watoto wake hao wawili kutoka kwa mama wawili tofauti, wenye
tabia mbili tofauti, huyo mmoja mkubwa, aliyetelekezwa na baba yake, ....mama
akawa anaishi kijijini, angalia tabia zake zilivyokuwa, yeye kwa vile aliishi
muda wote na mama yake, na familia ya mama yake, akawa kachukua tabia kutoka
kwa mama yake, na wazazi wa mama yake ....’akasema baba.
‘Mimi nawafahamu sana wazazi wa mama yake huyo , familia ile sio
mchezo, wanajua kulea watoto, angalia, mtoto wao alivyokuja kubadilika, na
hakutaka kabisa kuwa karibu na baba yake alipojifunza, na kufahamu ubaya wa
baba yake na hayo anayoyafanya, akajengeka na kuwa kijana mwema kabisa..
‘Sasa angalia huyo mtoto mwingine, wa mama mwingine, wanyewe
mnaiita nyumba ndogo, mtoto yule pia alilelewa na mama yake kwa kiasi kikubwa,
lakini hebu angalia tabia ya mama yake huyo na familia ya mama yake huyo, wengi
tunaifahamu,...mama yake ni mama wa mjini, na ana tabia zisizo faa,ndio akawa
anaishi na mtoto wake huyo, hataki mtoto wake aguswe,...kwa ujumla, mtoto wao
huyo hakupata matunzo mema, na baba yake akamchukua, aishi naye akamsomesha,
mtoto yule akawa kama baba yake ....’akasema baba.
‘Kwahiyo mnataka kuniambia nini hapo hicho ndio kizalia au ni
malezi ya kutegemea na ulezi, na mazingira..?’ nikauliza nilioona maelezo yanazidi
kuwa marefu.
‘Ni kuwa usione kuwa tulikuwa tunaingilia ndoa yenu,sisi kama
wazazi, tunafahamu mengi , kwa yakini, hatukuangalii wewe tu kama wewe,
tunaangalia na matunda yenu, mke mwema na mume mwema, huzaa matunda mema,
...matunda mema,ndio kizazi, ndio jamii, ambayo inaweza kuleta amani na upendo
baadaye, au pia ndiyo inayoweza kuleta matatizo baadaye...’akasema baba.
‘Sisi tulifahamu kuwa haya yaliyotokea yatakuja kutokea, kwani
tunamfahamu mume wako na chimbuko lake, ..tulikushauri sana hilo, lakini kwa
vile nyie ni watoto wa taifa la leo, tukashindwa, lakini sasa umejionea
mwenyewe, sasa ni wakati wa wewe kukaa chini na kutathimini matokeo ya
juhudi zako, ya kile ulichoona ni bora kwako,...labda sisi wazazi tumepitwa na
wakati, nyie mnaona ya kisasa zaidi...’akasema baba.
‘Nikuambie kitu, mimi na mama yako, hatukuwa tunapenda
kuweka wafanyakazi wa ndani, uliona mwenyewe maisha tuliyoishi,sio kwamba
hatukuwa na uwezo huo, hali zetu zilituruhusu, tulikuwa na wafanyakazi wa
kawaida, lakini sio wa kulea watoto, watoto wetu, nyie…tuliwalea sisi wenyewe...wewe
umelelewa na mama yako na sana sana, alikulea bibi na shangazi yako...kweli si
kweli..?’akasema baba.
‘Unafikiri ni kwanini tulifanya hivyo, ..?’ akauliza baba, na mimi
nikawa kimiya sikujua niwajibu nini.
‘Mtoto anaiga na kuwa na tabia kutoka kwa yule anayemlea,...kuna
tabia za kurithi, na kuna tabia za kujijenga! Tabia za kurithi, ni zile za
asili kutoka kwa wazazi, kama baba au mama walikuwa na tabia hizo..
Kuna tabia kama za ukali kupindukia, upole, kuongea, uvivu,
uchapakazi au tabia za namna fulanifulani za kimaumbile, utaona na watoto
wanakuwa hivyo hivyo, na tabia hizo zinaweza kufifia kutokana na tabia za
kujijenga, au kujengwa, na yule mlezi, sio zote, lakini zile za matendo, nyingi
zinafifia kipindi hicho....’akamwangalia mama
‘Wazee wetu waliliona hilo, ndio maana walijenga tabia ya kulea
watoto wao wenyewe au kulelewa na ndugu zao wa karibu, siku hizi mnalelewa na
wafanyakazi wa ndani, ...ndio maendelea kwasababu baba na mama wote ni
wanafanya kazi, au sio
‘Lakini watu hawa wana ndugu zao kijijini, hawataki kuwachukua
ndugu zao hawo toka kijijini, waje wawalelee watoto wao, kwasababu gani…hawaoni
wanavunja udugu badala ya kuendeleza…umetuelewa hapo?’ akawa kama anauliza
tena.
‘Kwasababu mke hataki ndugu wa mume wajazane nyumbani
kwake...ubinafasi unaanzia hapo, kwa vile mke yule sio mke mwema, hajui kujenga
nasaba,....’akaendelea kuongea baba.
‘Lakini pia ndugu wengine wa mume wana tabia mbaya...hilo nalo
mume wangu uliangalie…usiangalie upande mmoja’akasema mama.
‘Sikatai hilo...nazungumzia wazazi wale waliojengwa na mke na mume
mwema, wanaotoa kizazi bora, watoto wao wanakuja kulea watoto wa wenzao, na
kizazi hicho kinakua, na maadili safi...hawa wanaifahamu vyema nasaba yao, na
wanajua nini maana ya familia bora sizungumzii vizazi vyenye maadili mabaya...’akasema
baba.
‘Angalia watoto hawa wanaolelewa sasa na wafanyakazi wa nyumbani,
wanakua je, baba na mama wanakutana na watoto wao jioni, na watoto hawa wanakua
hivyo hivyo, hadi wanafikia muda wa kwenda shule za awali, ...mtoto huyu
anakwenda kukutana na mwalimu....ni sawa sikatai ni maendeleo, kwani kwa
mwalimu sina shaka nako,...
‘Nasema kwa mwalimu sina shaka nako sana, kwani mwalimu kajifunza
jinsi ya kulea mtoto,...lakini mwalimu huyu atamlea, na kumfunza kitaaluma, sio
kiasili ya wazazi, kuna mambo muhimu hapo atayakosa, hatajua mila nzuri na
desturi za wazazi hao, tabia ya asili ya baba na mama inakuwa imesahaulika
kabisa, ....’akatulia kidogo.
‘Wakati mwingine ni vizuri,hasa kwa ajili ya kusafisha tabia mbaya
za kurithi, lakini wakati mwingine ni vibaya,kwani kuna vitu kama lugha,
na tamaduni muhimu kwa watoto hawa, hivyo vyote vinapotea, kwani hapa, walimu
wanachojua ni taaluma, na sio asilia,na mara nyingi, watakachofundishwa hapo ni
taamduni za nje, tunalioan hilo kila siku, hata shikamoo kwa mzazi inakuwa
shida ...’akatulia.
‘Mimi nimekaa na watoto wako hapa, na kwanza kabisa ulisema
tuwapeleke watoto shule za awali, mimi nikakukatalia, ukaona labda tunataka
kuwapoteza watoto wako, lakini uliona tulivyokushauri, kuwa kwanza watoto hawa
waende shule za maadili ya dini, unafikiri ni kwanini tulikushauri hivyo...?’
akawa kama anauliza.
‘Ni kwasababu maadili ya dini, humjenga mtoto awe na hulka ya
imani ya kutenda mema na kukataa mabaya, imani inayomweka mtoto afahamu
kuwa yeye ni kiumbe tu, na wazazi wake ni watu muhimu sana, na hatakiwi kufanya
mabaya, kwahiyo anajengeka kimaadili mema…
‘ Mtoto huyu akikutana na mwalimu anayejua vyema kazi yake, ile
hulka ya asili, ila tabia mbaya ya asili, inaondoka kabisa, na hataweza kufanya
makosa kwani muda wote anafahamu kuwa mungu yupo pamoja naye.
‘Mtoto kama huyu anfahamu kuwa nikiiba, nikisema uwongo ni makosa,
mungu ananiona wakati wote...leo hii hiyo ipo wapi, watoto wanakimbilia kujua
masomo ya taaluma tu lakini maadili ya imani ya moyoni, yanakuwa hayapo.
‘Na wenzetu kwa malengo yao wakaanzisha kinachoitwa haki za
watoto, ni sawa hatuzikatai, lakini haki zipi basi, haki za kumtukana mzazi
ukae kimia, eeh..je hizo haki zinamjengaje huyo mtoto, je ni maadili mema,....wao
wanasema mtoto hatakiwi kuchapwa, wala kukaripiwa, alelewe kama yai, aamue
anavyotaka yeye, hivi kweli sisi tungefanyiwa hivyo dunia hii
mngeikutaje....’hapo baba katikisa kichwa kwa masikitiko.
‘Mimi ningelikuwa kiongozi wa wizara ya elimu,ningesisitiza kuwa
elimu za awali, ziwe za mfumo wa dini, walimu wa dini ndio wapew hizo kazi, ili
ziambatane na maadili mema,, watoto wasomeshwe wajue jinsi gani ya kujiweka
mbali na uchafu, madhambi, wiz ink….somo la dini liwe ni lazima, kwa shule za
awali.Natambua kuwa Serikali haina dini, lakini dini ni muhimu kwa ajili ya
kuleta amani na upendo, ...’
‘Nikuambie ukweli binti yangu, maadili mema hujengeka vyema,
kwenye dini....hilo binti yangu nakushauri sana, uwe nalo akilini, usije
ukatekwa na propaganda potofu, maana dini sasa zinaonekana kama ni sehemu ya
kunyima watu uhuru wao, angalia dunia inapokwenda sasa, kwa ajili ya kuiga
tamaduni za watu
Hebu angalia hili tatizo baya linalotaka kuenezwa duniani, watu wa
jinsia moja wanaoana…hivi hawa ni watu ni wanyama, ..hivi kweli viongozi kama
hawa wanataka dunia ije kuwa vipi, halafu wanajifanya ni wacha mungu, huo ni
unafiki tu.....
‘Kwanini tunakuambia haya yote,...ni kwasababu tunataka
ukitoa maamuzi yako, uwe na yakini, uwe na uwoni wa mbali, kuwa msije
mkajibidisha tu kwenye kazi zenu, mkasahau mstakabali mzima wa malezi bora ya
watoto wenu, mkawa mnategemea wafanyakazi wenu wa ndani na walimu wa chekechea
kuwalelea watoto wenu, msikwepe majukumu, ..malezi mema ya watoto wenu hutoka
kwa wazazi, sasa hivi ni kila mzazi achunge familia yake, dunia
imeharibika....’akamwangalia binti yake halafu mama yake.
‘Ilivyo sasa, baba akitoka kazini anapitia kuweka moja moto moja
baridi na marafiki zake, mama anapewa kazi za maalumu ofisini, ...wote
wanachelewa kurudi, ...wakikutana nyumbani, baba kalewa, mama naye kachokeshwa,
ni nani hapo ana habari na watoto, sana sana baba na mama hawa wengine huishia
kugombana au kuzozana mbele ya watoto wao,watoto wanayaona hayo, wanajengeka
hivyo, kisaikolojia wanaathirika, na mwisho wake, na wao wanaona
hayo ndiyo maisha ya kawaida.
‘Jamii kimaadili inaanza kuharibika kutoka kwa wazazi wao, chanzo
kikubwa kimeanzia ndani ya familia, kwa baba na mama ambao hawakutimiza wajibu
wao,...mnawaachia watoto waangalia mapicha mabaya kwenye runinga na sasa kwenye
simu, simu mlizonunua kwa pesa zenu, mtoto huyu anakua akijua kuwa ugomvi
ni jadi, ulevi ni kawaida, bangi, vita ni mambo ya kawaida tu,..jamii ndivyo
inavyoanza kuharibiwa hivyo...
‘Angalia siku hizi, hizo haki zinazopigiwa debe, nyingine ni nzuri
sikatai, lakini pale mtoto aliyelelewa kama yai anapoadhibiwa na mwalimu na
wewe mzazi ukaja juu, mwalimu akijaribu kutimiza wajibu wake, kwa kumuadhibu,
wazazi wanakuja juu..hapa tunazidi kuiharibu jamii...,
Ndio wapo walimu wanakomoa, au wanaadhibu bila kipimo, anaumiza
badala ya kujenga huyu ni mpuuzi tu, nazungumzia walimu kwa ujumla, wanaojua
kazi yao,…ambao wanahakikisha mtoto anakulia kwenye maadili mema,
Kwahiyo kwa kifupi mtoto aliyekulia kwenye maadili mema, kuanzia
kwa wazazi hadi shuleni, huyu akipata kazi ofisini atakuwa mtendani mnzuri,
lakini kinyume chake ndio hapo tunapata viongozi mafisadi, wala rushwa, nk,
kwani watoto hawa wamedekezwa wamezoea kufanya wapendavyo, hawatajua umuhimu wa
kutii sheria, inafika mahali tunasema
asiyefunzwa na wazazi wake, dunia itamfunza, sasa hilo ni kosa....tuweni makini
wazazi, makosa tunayaaanza sisi wenyewe, tusije tukakimbilia kuilaumu
serikali...’akasema baba.
‘Sisi tutaishi na watoto wako hapa, kwasababu tunahitajia kizazi
chako kiwe na msingi mwema kama ule tuliokulelea wewe, kwahiyo usiwe na
wasiwasi kabisa kuhusu mstakabali mzima wa watoto wako,....
Ila kaa chini,fikiria na sahau kidogo kuhusu watoto, fikiria maisha
yako ya baadaye, ila kumbuka malezi ya watoto ya awali ni wajibu wa wazazi...na
cha msingi usije ukatekwa na ushauri wa watu wengine usiowafahamu vyema,
...hayo ndio tuliyokuitia, kama una swali uliza...’akamaliza baba. Mimi
nikainama chini na kuzama kwenye mawazo na mama ndiye alinishitua, akauliza;
‘Kwani huko polisi wamesema nini, kuhusu mume wako na
wengineo,.....?’ akauliza mama.
‘Hawo hawataachiwa mapema, mpaka wakubali kumtaja muuaji, mpaka
wasema yale wanayohitaji polisi..’akasema baba.
‘Kwani wao wanamfahamu muuaji ni nani?’ akauliza mama.
‘Kutokana na uchunguzi wa polisi wamegundua kuwa hawa watu
wanafahamu mengi yatakayowasaidia polisi kumpata huyo muuaji, lakini watu wetu
hawa hawataki kusema ukweli wote, kwasababu zao mbali mbali,...polisi sio malaika
kuwa watajua ni nini kimetokea, kama sisi raia hatutaoa ushirikiani, ukificha
ukweli unawapa shida polisi, ndio maana wakati mwingine wanaamua kutumia nguvu,
...
'Ina maana inawezekana muuaji anaweza kuwa miongoni mwa hao
waliokamatwa....'akauliza mama kumkatisha mume wake.
'Kwa uchunguzi wao polisi, wanahisi hivyo, kuwa huenda miongoni
mwao yupo huyu muuaji...ndio hapo polisi wakaja na wazo hilo, kuwakamata wote,
na huko wanajua mbinu zao,...watawafinya kidogo, watasema yote..., kwahiyo
wakitoka hapo ni mahakamani....’akasema baba.
‘Kwa namna hiyo, ina maana kikao hicho cha maamuzi na hukumu
hakitaweza kufanyika karibuni au hakitafanyika kabisa, ni maamuzi tu...?’
akauliza mama.
‘Kikao kitafanyika , cha muhimu ni bintio yetu awe na maamuzi huru, afahamu kuwa
maamuzi yake ndiyo msimamo wa ndoa yake ijayo au maisha yake yajayo… na ni
muhimu, akae stulize kichwa, atoe maamuzi yenye muafaka, lakini hata hivyo, kwa
vile bado hakuna mabadiliko mengine, yeye bado ni mke wa mtu, anahitajika
kumsaidia mume wake...’akasema baba.
‘Mimi hapo ndio sikuelewi mume wangu, huoni kama unamchanganya
mtoto, mwambie moja kwa moja, kuwa ajipange kuwa sasa kuwa hana mume,huyo mume
wake hamfai tena, kwanini tumzungushe mtoto..’akasema mama na baba aktikisa
kichwa kukataa.
‘Mbona hata wewe unanichanganya,….wewe ulianza vyema kuwa yeye,
anahitajiwa kuwa na mume mwema, lakini huyo mume aliyempata sio mume
mwema,anahitajika kuachana naye....sio ndio hivyo, sasa ukimchanganya mtoto
atashindwa kukuelewa,..jamani kuna ugumu gani kusema hivyo?’ mama akasema
akimwangalia mume wake.
‘Mke wangu sisi ni wazazi, jukumu na lengo letu ni kumshauri binti
yetu..., na kama ushauri wetu haukuwa na maana toka awali, unafikiri sasa
utakuwa na maana...’akawa kama anauliza akimgeukia mkewe, halafu akaongea kwa
kusema;
‘Sisi kama wazazi sio jukumu letu kuwatenganisha wanandoa,
awe binti yetu au mwanetu...., bali sisi kama wazazi jukumu letu, ni
kuwasuluhisha, kuwashauri na kuwajenga, ili wajaribu kuwa na ndoa
njema...’akasema baba huku mama akitikisa kama vile anapingana na maneno yake,
lakini baba akendelea kuongea kwa kusema;
‘Mke wangu, ukumbuke kuwa hawa wameshaoana, hivi sasa bado wao ni
mume na mke, tulijitahidi awali binti yetu ampate mume bora haikufanikiwa,yeye
akasema keshampata mume anayemuona anamfaa, hivyo basi mume aliye naye ndiye chaguo
lake, hana ujanja hapo, mpaka kuwe na maamuzi mengine, na hayo maamuzi mengine
sisi hatuwezi kuyaingilia, ..anachohitajika kwa sasa ni kumsaidia mume
wake,kipindi kama hiki, ...huo ndio ushauri wetu,...’akasema baba.
‘Mhhh, hapana mume wangu, bado binti yetu hajachelewa, na bado ana
nafasi ya kumpata mume bora...’mama kabla hajaendelea mara simu ya baba ikaita,
na ikabidi anyamaze na kukatiza kile alichokuwa akikielezea.
Na mara simu yake ikalia, akaishika mkononi kwa kuangalia mpigaji,
na alipoona ni nani akasema;
‘Mhh, naona kuna jambo ...rafiki yangu huyu, mtu wa usalama,
anayenipa habari za ndani, ...nahisi kuna jambo kubwa huwa hanipigii mpaka kuwa
na jambo muhimu kwangu, ngoja niongee naye nisikia anasemaje..
Akasimama na kusogea pembeni, huku akiweka simu yake skioni, akawa
anasikiliza kwa muda, halafu akauliza;
‘Kwahiyo humjamkamata japokuwa mumethibitisha kuwa anaweza kuwa ni
yeye. ......ohoo, kuna ushahidi wa kutosha, sawa kabisa, hapo naona mumemaliza
kazi, hongereni sana, ..tupo pamoja....’akasema na kukata simu, halafu
akatugeukia na kusema;
‘Hatimaye muuaji yupo mbioni kupatikana.....
NB: Hatimaye muuaji yupo mbioni kupatikana, ni nani...na je ni
maamuzi gani atakayoyachukua mke wa familia, tukutane mwisho wa kisa hiki.
WAZO LA LEO:Asili
ya jamii, ni kutoka kwa wanandoa, ndio maana tunaona ni muhimu kwa yule
anayetaka kuoa au kuolewa kumtafuta mwenza mwema. Wanandoa hawa ndio
watakaopata watoto, na kama ni mume mwema na mke mwema, basi watajua umuhimu wa
malezi kwa watoto, watoto ambao wanakuja kuwekeza kwenye jamii. Ni muhimu sana,
kwa wazazi na serikali, kuwaangalia watoto kwa macho mawili, hawa ndio chanzo
cha amani au vurugu.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment