Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Thursday, March 22, 2018

MKUKI KWA NGURUWE-99


Mume wa familia, akainamisha kichwa na alipoona watu wapo kimia, taratibu akainua kichwa na kumuangalia mwenyekiti,…alimuangalia kwa muda, halafu akatikisa kichwa kama kukataa, haikueleweka, kwanini anatikisa kichwa vile, anakataa kuongea ana anakataa nini, na zaidi akaendelea kubakia kimiya hakuongea, baadaye akainamisha kichwa chake kama ilivyokuwa awali, akatulia kimiya.

Mwenyekiti akabakia kaduwaa, akasema ….

‘Je mume wa familia hayo yaliyoongewa na mpenzi wako wa zamani ni kweli au na yeye kajitungia uzushi wake?’ akaulizwa mwenyekiti, sasa kwa sauti kubwa yenye mamlaka,

Mume wa familia aliendelea kubakia vile vile, kajiinamishia kichwa chake chini, kama vile hawezi kukuinua na kumwangalia mume wa familia, ambaye alikuwa bado katulia kimiya, na mwenyekiti akaongeza kuongea kwa kusema;

‘Huyo ni mtu wako, yupo kwenye moyo wako, kipenzi chako cha asili, ...asingeliweza kusema hayo aliyoyasema kama angelijua kuwa yatakuumiza, kajitosa kwa ajili yako, na kwa kuongea hivyo anatarajia mema kwako, japokuwa ni kwa kukuumiza au sio,…sasa je hayo aliyoyaongea yana ukweli, unayakubali, au ni kama yale yale ya rafiki wa mke wa familia,…?’ akauliza

Mume wa familia kimia…hata wakili wake ambaye alikuwa katulia akiangalia mbele sasa akawa anamuangalia yeye.

‘Na ujue..tunajitahidi sana kukupatia nafasi hizi, ili mwenzetu ujirudi, ujue makosa, yako utubu,…’akasema mwenyekiti.

‘Ilivyo ni kuwa kila kitu kimeshaongelewa, lakini una nafsi ya kuyathibitisha hayo au kuyakana, hasa hayo aliyoyangea mke wa docta…ya rafiki wa mke wa familia uliyapinga,  sasa je na haya aliyoyaongea ex- wako, unayapinga pia, ni uzushi, hayana ukweli, toa kauli yako kama mwanaume...’akasema mwenyekiti, na hapo mume wa familia akainua uso kidogo, lakini hakusema neno.

‘Kukaa kwako kimiya inaonyesha nini, ama ni kutuzarau, au ama ni kiburi, au tusemeje, au ndio wakili wako kakushauri hivyo,…?’ akauliza mwenyekiti, na mume wa familia akaendelea kukaa kimiya, na wakili akataka kuongea, lakini akasita na kukaa kimia

Mimi nilipoona hivyo, nikaona niingilie kati, nikasema;

‘Ndugu mwenyekiti, mimi naona tusipoteze muda, kuna mengi yamesemwa na yote ni ukweli mtupu, kwa mwenye hekima, ataelewa, na kukiri kosa, lakini kwa mtu mwenye tabia yake, ataona ni yale yale,tu, na ndivyo inavyoonekana, labda kaona tunamuonea, au labda, kasingiziwa, hatujui, lakini kwanini tupoteze muda...’ nikasema.

‘Mimi nataka aongee yeye mwenyewe…’akasema mwenyekiti, na mume wa familia, akageuza geuza kichwa halafu akainamisha kichwa hakusema neno

‘Unaona….’nikasema

‘Ndugu mwenyekiti naomba niendelee kuongea,…’nikasema na mwenyekiti hakuniambia niendelee kuongea mimi nikaendelea kuongea tu.

‘Ndugu mwenyekit tuyaangalie hayo mambo kwa mapana yake kihekima zaidi…,kama unavyoona mtu anaulizwa anakaa kimia, hapa sisi sio watoto wadogo, pili anayeuliza swali hilo ni kiongozi wetu, ….baba mkwe, mtu anazarau nna kukaa kimia,…lakini hilo tuliache labda kama ulivyosema mwenyekiti wameshauriana afanye hivyo…’nikasema

‘Lakini mimi nimejiuliza sana…kukaa kwangu kimia muda mrefu nimegundua jambo, kuwa haya yote yalikuwa na maana gani, ni nani alilengwa, kwa haraka nimegundua kuwa mimi ndiye mlengwa,..sasa najiuliza ni kwanini ni mimi, ….kwasababu ya mali,? Au kuna jingine, jibu lipo wazi ndio sababu ya mali,

‘Mali zimechukuliwa kama kigezo, mengine ni kuzunguka tu, lakini tujiulize mali ni ya nani,…ukilendeleza hivyo utakwenda kuwakuta wazazi wangu, sasa kumbe mimi nilichaguliwa kama njia ya kufika kwa wazazi wangu, ili iwe ni kashfa na baadae wafanikiwe…’ nikatulia

‘Sisemi haya kwa kujitukuza, lakini ndio ukweli ulivyo,…, mali zilizotoka kwa wazazi wangu, zimewavuta watu kufanya waliyoyafanya, maana hawafanyi bure, hayo waliyoyafanya yana gharama, au sio..

‘Ni kweli wazazi wangu, walifanya juhudi hadi tukafikiwa sisi hapo tulipo…na sisi tulitakiwa tupokee kijiti au sio,..ndio maana mimi nilijaribu kumshirikisha mwenzangu, ili ajifunze, ili tuwe sambamba,…na niwaambie ukweli, hili halikuwa jambo rahisi, ..kama mnalivyoona hivi,.. ilikuwa ni kazi kubwa, kumjenga mtu wa namna hiyo nilificha kila adha nilizozipata,…sikusikiliza ushauri wa wazazi wangu...’nikasema.

‘Wakati mwingine, ilibidi mimi nigeuka kuwa kama mume wa familia, kufoka, na …na..kiukweli haikupendeza kabisa maana baada ya hapo nakaa nakujuta kwanii nimefanya hivyo, kwanini nimemfokea mume wangu…unaona eeh,,..lakini nilifanya hivyo, kwa vile mimi nafahamu,…ni kwanini nafanya hivyo,…sio kazi rahisi kama watu wanavyofikiria ..’akatulia

‘Mimi nimekulia katika familia ya hali hiyo,…familia ya kazi,…familia ambayo haina muda wa kupoteza, starehe ni kwa nadra sana, maana bado tunachuma bado twawekeza…

Niwaambie ukweli,…. japokuwa wazazi wangu walikuwa wana uwezo wao, lakini sikudekezwa kabisa..mimi nilitakiwa niishi kama wengine, nijua hali ngumu ipoje ili nikue nayo, nijifunze…, kuna muda niliweza hata kukataliwa kula, chakula kipo, lakini kwa uzembe wangu, napewa adhabu ya kukosa kula,, ilifikia hata nachapwa viboko, wakati huo nimeshakuwa mkubwa.

Wazazi wangu walianzia mbali,…nakumbuka nikiwa mdogo, niliwaona wazazi wangu wakiamuka usiku kukanda, chapati, kutengeneza maandazi kwa ajili ya kuuza kesho yake, usiku kwao ilikuwa ni kazi hiyo, asubuhi, kubeba vikapu vilivyojazwa hayo maandazi na chapo kwenye hoteli za watu, baadae ndio wakaanisha hoteli yao wenyewe, na ndio mwanzo wa kuanza kuchipukia,…..kazi kwetu ilikuwa kipimo cha utu,…starehe ilikuwa sehemu ya ziada tu, hakuwa na nafasi kwenye nyumba ya wazazi wangu…’akatulia

‘Kwa….kifupi, kazi kwetu ni  jadi, hayo mnayoyaona, hizo mali, na utajiri kama mnavyouita, haukuja hivi hivi...nayasema haya ili watu waelewe wapi familia yetu ilipotokea....’nikamwangalia mume wa familia aliyekuwa bado kainama.

‘Nafahamu kabisa kusudio lao hawa wenzetu, ni kuwa kila tajiri, kila mwenye uwezo, kaupata utajiri huo kwa njia za kubumashi, kutepeli, kuiba, dhuluma… nk tukirejea zile kauli za marehemu....jamani sio kweli, ...wapo wengine, kama sisi, ..najivunia hilo, kwani mimi nimeishi na wazazi wangu, nimeona jinsi gani walivyokuwa wakijituma, mali na vitega uchumi hivyo vimetokana na jasho la wanafamilia.

‘Kiukweli inaniuma sana, nikukumbuka wapo wazazi wangu walipoanzia, halafu watu wengine wanakuja kusema sisi mali na vitega uchumi hivyo tumevipata kwa dhuluma….kiukweli inauma sana,…’ pale mke wa familia akawa anajizuia kulia.

‘Sisemi haya kwa vile…, ila nataka kuwaelezea wapi mali na vitega uchumi hivyo vilipotokea…, sio wote jamani…mnamkosea sana, mnaweka shuku zisizo na ukweli.., na kwanza sisi hatujafikia ngazi hiyo ya kuitwa matajiri, tunajitahidi tu, na mali hizo mnazoziona ni juhudu zetu, juhudi za wazazi wangu,…’akatulia kidogo

‘Kwahiyo kwa jinsi ilivyo, watu, eeh, kama mume wangu walitaka  mimi nilale, nibweteke, niwe mtu wa matumzi tu,…mali si zipo, mali za baba na mama zipo, nitumie tu,  je zikiisha…maana mtumie huku zinazalisha, lakini mnatumia uzalishaji duni, masoko hakuna, mnaandamwa na madeni, mtafika wapi hivyo…vizazi vyetu vitakuja kufaidika na nini…hilo hawajiulize, kwangu mimi nasema hilo haliwezekani...’nikatulia kidogo.

‘Ndio maana ilifika mahali, nikasahau kila kitu, nikasema sasa ni kazi, starehe baadaye, huenda kwa kufanya hivyo, nilimkwaza mwenzangu, akaona nadharau majukumu muhimu ya ndoa, eti mimi ni bakhili, aliwahi kuniambia hivyo, kuwa mimi ni bakhili..

Na…nimuulize tu kama nilisahau majukumu yangu ya ndoa…, hawo watoto wangelipatikana, awali nilimdekezea, si unajua kupenda, nikawa namuhenga henga, ili nimuone, mwisho wake…nikijua mwenzangu atakuja kuona umuhimu wake kama mume wa familia, nilikwenda naye hivyo,..biashara ikashuka tukaanza kuyumba,…’akatulia

‘Hali ikawa mbaya, ikanibidi niende kuongea na wazazi wangu, wakaja kutuinua tena, kwa mkopo, lakini huku wakituasa..

‘Jamani, tutainualiwa mpaka lini,..ndio  maana..ikafika mahali nikaona kuna umuhimu wa kujitosa ili kulikoa jahazi…, ikawa hakuna kulala, hakuna starehe tena
Angalau tufike mahali tusema sasa tunazalisha kwa faida,ndilo lilikuwa lengo langu, hapo kiukweli sikueleweka kivitendo….!

‘Nimejifunza mengi kwa hili, na kwa kauli ya haraka haraka , ninaweza kusema, imekuwa kama mtoto akililia, wembe muache, ukimkata atajifunza, lakini pia imekuwa changamoto kwangu, kwani yote haya yaliyotokea muathirika mkubwa ni nani, ni mimi na watoto wangu...,

Ni wazazi wangu pia, ambao walikuwa wamelengwa kisiasa, na hata kiuchumi…

 ‘Hebu angalieni huo mlolongo mzima, kumbe haya yalikuwa yamepangwa kutoka huko kijijini hata kabla ya ndoa yangu, na ndoa yangu ikawa kama kisingizio, na udhaifu wangu wa kibinadamu ukatumiwa kama ngazi ya kutekeleza hayo yaliyokwisha pangwa…

‘Nawashukuruni sana kwa hayo,nawashukuruni sana, wote, mliokuja kwangu na nikawapa kila kitu changu, ikiwemo nafsi yangu katika moyo, nikawaona kama ndugu, kama marafiki wema, kama mume mpenzi,...lakini hii ndio faida yake, mtoto akililia wembe muache, ukimkata atajifunza. Na mimi nimejifunza, japokuwa nakejeliwa kuwa mkuki sasa umenipata ndio maana napiga ukelele, sawa…nimekubali mkuki ni kwa nguruwe….

 ‘Kwa hivi sasa nina machungu mengi moyoni, huenda nikitoa uamuzi wangu, naweza kuharibu, nahitajia muda wa kulitafakari hili kwa undani, ...yaliyotokea yamenifungua macho na masikio, nimejua ni nini nahitajika kukifanya…’akamuangalia mwenyekiti

‘Naomba sana,…kama yawezekana kikao hiki kiahirishwe , ili mimi niweze kukaa na kulitafakari hili jambo vizuri..na ili nikija kusema neno la moyoni, liwe sahihi.

Nina mengi ya kuja kuyasema, sasa kama ni kesho au ije kupangwa siku nyingine nitashukuru sana, ndugu mwenyekiti…

Lakini hata hivyo, leo, kabla hatujaweza kuondoka hapa, mimi mwenyewe  ningelipenda kumuuliza mume wa familia, maswali machache, mbele yenu, na nataka ayajibu yeye mwenyewe kwa kinywa chake, ...bila kuficha, mwenyekiti kamuuliza kamzarau, sasa mimi kama mkewe na kama atakaa kimia hivyo basi, atakuwa kanizarau na mimi mkewe…na kwa maana hiyo, mimi nitaona sina mume, maana nini maana ya kikao hiki, ni kutatua mgogoro wa kifamilia ndani ya hii ndoa, au sio…sasa ewe mume wa familia, nataka unijibu hayo maswali....'nikasema na kumgeukia mume wa familia,

'Mimi ninayekuuliza haya ni mke wa familia nakuuliza wewe kama mume wa familia, nategemea wewe kama mume wa familia, utayajibu hayo bila kuniogopa, kama utaniogopa itakuwa ni ajabu, ...uanaume wako utatiliwa mashaka...’nikasema na watu wakacheka.

Na mume wangu hapo akaniangalia kwa macho yaliyojaa hasira, ni mimi sikujali macho yake, nikasema;

‘Swali langu la kwanza, ni swali la msingi na lenye hekima,  umeshaulizwa ukazarau na mimi kama mkeo nakuuliza swali hilo tena,… je hayo yaliyosemwa na wote hasa shahidi wa mwisho aliyekuja kuthibitisha…yeye alithibitisha, na kufafanua zaidi yale yale ya shahid wa kwanza,…, je hayo aliyoyathibitisha ni ya kweli au kajitungia yeye mwenyewe?’...nataka unijibu hilo swali, kwani majibu yake, yataweza kunipa mimi mwanga,ili tukirudi tena, niwe na kauli ya hekima,…’nikatulia

Mume wa familia sasa akaonekana kama ana uhai, akataka kusema neno, na mimi nikamkatili na kusema;

‘Na kauli yangu, ya hekima…haitakuwa mbali nay ale tuliyokubaliana, lakini mimi ni binadamu, wengi tunakosea, hatuna muamala wa kusema mimi ni mtakatifu, mimi…nimeshajikomboa sitafanya dhambi, kusema hivyo tunajidanganya sisi wenyewe…

Lakini sisi wawili tulikaa pamoja tukaona kuna haja ya kuweka misingi yetu ya jinsi ya kuishi, misingi hiyo itaweza kutulinda, ili tusije kukengauka, tukajidhulumu nafasi zetu na kuja kuwadhulumu wengine ndio nikaandika huo mkataba,..sasa kwanini tuje kuuharibu tena,….

‘Tunauharibu kwa kutokujiheshimu, na kutokuamini maamuzi yetu kama watu wazima,…sasa haya kama watu wazime tumajivua nguo, kwanini tusikimbilie kujisitiri, na kujisitiri, ni kutubu, kurejea ndani na kuvaa nguo zetu, au sio

‘Wakati tunaandika hiyo mikataba tulikuwa na akili zetu timami, na tuliandika tukisema sisi,… yoyote atakayekiuka huo mkataba…, atawajibika, au sio, sio mimi, au yule akifanya atawajibika, haukuwepo huo ubinafsi,… sasa iweje mkuki huo uje kuniumiza mimi mwenyewe....’nikamwangalia mume wa familia na yeye akaniangalia kwa macho yale yale yaliyojaa hasira;

‘Sasa nikuulize wewe mume wa familia, najua sasa umeshajitambua, je unaweza kunijibu hilo swali langu la kwanza au niendelee na maswali mengine?’ nikauliza

Hapo mume wa familia, akajiweka vyema, usoni alionekana kukerwa, na ilionekana akianza kuongea hapo anaweza kuongea maneno makali sana..lakini haikuwa hivyo,

Alipoanza kuongea, akaanza kwa sauti ya taratibu, …, akasema;

‘Nilijua kuwa mwisho wa yote ni nini kinatafutwa, nilifahamu kuwa ni  mtego wa panya, sawa…., nimekubali, na sina haja ya kung’ang’ania mali  zenu,...’akasema na watu wakaguna, mwenyekiti akasema

‘Tulieni…mpeni nafasi huu ndio wakati wake, huenda anasingizwa, sasa atuambie ukweli wake wa mooni,…’akasema mwenyekiti

************

‘Mimi ninachoweza kusema kwa hivi sasa na huenda ndiyo wengi wanavyotaka mimi niseme…

‘Mke wangu nakuomba unisamehe sana…na sio mara yangu ya kwanza kulisema hili, nikijua kuwa nimekosa…’akatulia

‘Ni kweli yaliyosemwa na waliotangulia mengine ya ukweli, siwezi kuyakataa, au kuyapinga…nitasema nini tena..ukiaka kumuua mbwa, ni lazima kwanza umuita majina mabaya…

‘Mimi,..sijali tena, maana hatua iliyofikia, nimeshajua ni nini kitafuta…nimekubali kushindwa, nimekiri nimekosa,...lakini mke wangu, katika maisha kuna kukosa, kuna kupanda an kushuka,..hayo ni majaribu tu na kama binadamu unaweza kuyapitia, na mimi sio wa kwanza, nilijaribu kwa njia hiyo, nia ni kwa ajili ya familia yangu, hilo hamlioni kabisa....’akasema na sasa akabadili uso wa hasira na kuwa uso wa huzuni.

‘Mke wangu, nakupenda sana...nilijitahidi kufanya hivyo, kukupenda..lakini huenda namna ya kukuonyesha kwangu sivyo ulivyokuwa ukitaka wewe..

‘Hata hivyo, vyovyote iwavyo, nakuomba sana, uwakumbuke watoto wetu, watoto hao wanawahitajia baba na mama yao,…ndio maana nilifanya kila niliwezalo nionekane na mimi ni baba wa familia, niwe mkali, niwe na mamlaka…’akatulia

‘Je mimi ningeendelea kuwa hivyo, hadi lini, baba asiye na meno, jamani hili hamlioni…, lakini juhudi zangu za kuleta mabadiliko katika familia, zikaja kuvurugwa na watu wengine, ....’akatulia

‘Mimi sitaki kuwatupia hao watu wengine lawama, nafahamu haitaeleweka vyema kwa hivi sasa, nimeshavuliwa nguo, nimesha…..sina maana tena,..hata hivyo kauli yangu ni kuwa, mimi ndiye baba wa familia, na hayo niliyoyafanya, nilitaka nieleweke hivyo, kama nimekosea nakubali na mimi nimekiri kosa...’akasema nahapo akatulia…na ilionekana kama keshamaliza.

Mke wa familia, akaanza kama kucheka, akasema….

‘Hahahaha, huko ndio kukiri kosa jamani….’nikasema

‘Mhh…haya jamani, hatimaye mume wa familia anakiri kosa, japokuwa kwa shingo upande, lakini sio kutoka moyoni, kasema yeye anakubali kwa vile ametegwa kama panya, jamani, hebu angalieni huo mlolongo wote, kuna kutegwa hapa…?’ akauliza mwenyekiti akiwaangalia wajumbe

‘Ndugu mwenyekiti niache mimi niendelee naye …mume wa familia, tuambie ukweli,…na nia yeti ni wewe utujibu, sio lazima uongee kwa maneno mengi sana kihivyo, sawa upo hiari kujitetea utakavyo, lakini swali letu lilikuwa wazi, je hayo aliyoyasema shahidi aliyepita ni kweli au ni uwongo, je kazua kama yule shaidi wa kwanza…?’ nimamuuliza sasa akabakia kimia.

‘Maana wewe una watoto wangapi vile…kuonyesha kuwa wewe ni nani kijogoo, anayeweza kupanda mitetea popote pale, leo huyu kesho yule..hivi kweli ni ubinadamu huo, ni utu huo, je hayo umesingiziwa, maana hapa nakuotolea mifanio iliyo halali, hilo umesingiziwa hao sio watoto wako, je hujatembea na hao watu…’nikamuuliza.

‘Unataka nijibu nini tena hapo, umeshaongea uliyotaka kuyaongea, umeshajirizisha, sasa hapo unataka niongee nini, …nizid kujitukana au…?’akasema mume wa familia

‘Mimi au kikao, kinahitajia jibu la moja kwa moja, kutoka kwako wewe mwanaume, kwanini unaogopa,…kwa jinsi ulivyojibu ni kuwa unasingiziwa, umetegwa kama ulivyosema, huko kutegwa kuna maana gani, hebu toa kauli ya kujiamini,…’nikasema na mume wa familia kwanza alitaka kuongea baadae akaghairi, hapo mwenyekiti akasema;

‘Tunakusubiria mume wa familia,…’akasema mwenyekiti

‘Mimi nimeshajibu mwenyekiti, naona kama mnanizalilisha sasa, hizo kauli zeni sizipendi, nafahamu kuwa nimekosea, na nimeshatoa kauli yangu, lakina hizo kauli zenu ni za kunifanya mimi mtoto mdogo…na si chochote, nafikiri ni zarau, kutokana na asili yetu, kuwa labda sisi tumekulia, na kulelewa kitabia mbaya, hatupendi kazi, tuna tamaa,na kitu kama hicho…’akatulia

‘Lakini mkumbuke yoyote anaweza kupitiwa, na shetani, akaghibilka na ni ibilisi, na .....ni nimeshawaambia kuwa sikuwa na nia mbaya, kwa hayo niliyoyatenda, na hamtaki kukubali ukweli kuwa  nilifanya hayo yoate kwa ajili ya kuilinda familia yangu, kwani kama nisingelifanya hivyo, hamjui ni kitu gani Makabrasha alinitishia nacho...’akasema

‘Haya sasa …mume wa familia anasema hayo aliyoyafanya sio kwa matakwa yake ni kutokana na vitisho kwa marehemu…’akasema mwenyekiti…

‘Tunataka tusikie hicho kitisho alichokutishia Makabrasha, maana kukutishia wewe ni kama alitishia familia yote hapa, je alikuambia nini, sisi tunavyojua ni kuwa Makabrasha alikutishia kuwa usipofanya anavyotaka yeye, atakuumbua kwa machafu yako uliyoyafanya, atakwenda kumwambia mke wako, na mkwe wako, au sio?’ akauliza mwenyekiti.

‘Pamoja na hayo, ...’akatulia na kutikisa kichwa kama kusikitika,

‘Hamkumjua Makabrasha nyie, hamkuwahi kuishi naye kwa karibu, yeye alisema, anaweza kuiumiza familia yangu, hasa watoto, atawateka nyara na kuwafanya wasionekane tena, ..hata wakionekana watakuwa mazezeta...hivi wewe kama mzazi ukisikia hivyo, utachukua hatua gani...’akasema

‘Hivi wewe kwa akili zako uliamini kuwa Makabrasha angeliweza kufanya hayo aliyokutishia, au alishakufahamu udhaifu wako kuwa wewe ni mwoga, ...au hebu tupe mifano hai, ambayo yeye aliwahi kuwafanyia watu wengine, ili tuamini kuwa vitisho vyake vilikuwa ni kweli...’akasema mwenyekiti.

‘Mimi nawapenda watoto wangu, nipenda familia yangu, siwezi kubahatisha kwenye familia yangu, iwe ni kweli au si kweli, iwe ni vitisho tu au ni kweli, mimi nilichotakiwa kufanya ni kile nilichoona ni sahihi, kwa ajili ya kuilinda familia yangu...’akasema.

‘Ina maana hata kutembea na wake za watu, mfanyakazi wako wa ndani inatokana na vitisho vya Makabrasha?’ akaulizwa na hapo akakaa kimiya.

‘Au labda tukuulize hili swali huenda nalo linaweza kuwa ni sababu ya Makabrasha, je ni kitu gani kilichokufanya uwe mnzizi na kuisaliti ndoa yako?’ akaulizwa

‘Ni hali iliyokuwa imenizunguka, nilikuwa nimechanganyikiwa na mambo mengi yalikuwa yakiniandama, ikiwemo hilo la mipango aliyoibuni Makabrasha, na hata hivyo, mke wangu alikuwa na kazi nyingi sana, na yeye alitakiwa awe karibu na mimi ili niweze kuyasahau yote hayo, lakini hata nilipojaribu kumvuta ili aniliwaze, niliona kama yeye ananisukumio huko...’akajitetea.

Mimi nikamwangalia kwa hasira na kusema; ‘Huo ndio utetezi wako, kuwa mimi sikuwa karibu nawewe, je uliwahi kuniambia hilo, kwa kinywa chako nikakukatalia au kukusukuma, ...?’ nikamuuliza

‘Kwa vitendo visivyo dhahiri, unaweza ukamkatalia mtu, kwa vitendo visivyo vya moja kwa moja, na mimi 
kama mtu mzima nililiona hilo, kuwa hukuwa karibu na mimi na niliposema kusukuma sio kwa kusukuma kwa mikono, ni kwa vitendo, visivyo moja kwa moja...’akasema

‘Kwa matendo hayo ina maana nilionyesha hivyo kwa vile sikupendi,au ni kwa vile nilikuwa nawajibika kwa ajili ya kujiendeleza, kwa ajili ya maisha yetu ya baadaye na familia?’ nikamuuliza

‘Hapana sijasema hivyo, kuwa hunipendi, na hujawahi kunitamkia hivyo, kuwa hunipendi…., kiukweli ulikuwa unanipenda na ulikuwa ukifanya hivyo kwa ajili ya kuinua kipato chetu zaidi na zaidi, hili siwezi kulipinga, …lakini hukufanya yale yanayostahili kuonyesha upendo wa mke na mume…, ulijali sana kazi hata muda usio wake...’akasema.

‘Ina maana wakati mke wako anahangaika na kazi hadi kusahau majukumu yake ya ndoa wewe ulikuwa huna kazi , unafikiria mambo ya mke na mume….au sio, hebu fafanua hapo kidogo,… huenda  kweli mke wako hakuwa na kazi kweli, alikuwa akijifanya ana kazi kwa mbinu za kukwepa majukumu yake ya ndoa, sema ukweli, jitetee?’ akaulizwa.

‘Hayo yapo wazi, kazi ni kazi, na majukumu ya ni majukumu ya ndoa, na mahali pale panajulikana, na muda wake muafaka unajulikana,...siwezi kusema alifanya hivyo kwa ajili ya kukwepa majukumu yake ya ndoa, hapana, ni kweli alikuwa akifanya kazi kiukweli, niliona kwa macho yangu, na siwezi kumlaumu sana kwa hilo…lakini kila siku, ..hata muda wa usiku, hapana….’akasema

‘Kama huwezi kumlaumu kwanini ukamsaliti, kwani  ukafikia hadi kutembea na mfanyakazi wako wa ndani, kwanini ukafikia hadi kutembea na mke wa mtu,...kwahiyo huko ndio kujitetea kwako kuwa ulifikia mahali ukazidiwa, kwa vile hukutendewa haki kwenye majukumu ya kindoa au sio, ?’ akaulizwa tena na mwenyekiti.

‘Nimeshasema ndio hivyo, mimi ni mtu mzima siwezi kusema kila kitu kiuwazi zaidi, mnataka nisema nini zaidi ya hapo,…sawa na nimeshakiri kosa, mbona mnatka kuvua nguo zaidi ..’akasema hapo kwa ukali.

Mimi nikamwangalia na nikasema ;

‘Ndugu mwenyekiti, mimi nimesharizika na jibu la swali hilo, ngoja nimuulize swali la pili...’nikasema na mwenyekiti akatabasamu na akamwangalia mume wa familia, halafu akasema;

‘Haya muulize maana ni mume wako unamfahamu sana kuliko sisi, ...’akasema mwenyekiti

Swali langu la pili, ni hili, ni muhimu sana , tena sana unijibu kutoka moyoni mwako, ...maana ukinidanganya tutajua,...hili swali ni kwa ajili yangu na wake wenzangu.’nikasema na kumwangalia na yeye akaniangalia kwa mashaka, akisubiri hilo swali.

‘Je unampenda mpenzi wako wa asili?’ nikamuuliza

Ilikuwa kama kashikwa na butwaa kwa swali hilo, …kwanza akahema kwa nguvu, na akaniangalia mimi moja kwa moja kwanza, ..halafu akatabasamu…ni lile tabasamu kama nimemuuliza swali la mzaha tu, halafu kwa haraka akageuka kumwangalia huyo mpenzi wake wa asili na baadaye akamwangalia rafiki yake, yaani docta, halafu akasema;

‘Kwanini mnaniuliza swali kama hilo, ...sioni umuhimu wake kwa sasa, hapa naona mnaendelea kunitega tu, hilo swali nafahmu kabisa lina ajenda ya siri, na mimi kama binadamu, siwezi kudanganyika, niliyoyafanya niliyafanya nikijua mimi ni mume wa familia, nilikuwa na mimi nawajibika, kwa manufaa ya familia yangu, mlitaka nikae tu,...’akawa katoa macho ya hasira akimwangalia mke wake.

‘Jibu swali kama mwanaume…’akasema mwenyekiti

‘Mzee, samahani sana baba yangu kama nitakosea, ni hivi kweli kuna mtu anaweza kuja pale kwako baba akakupangia jinsi gani ya kuishi,wewe umeshaoa  au sio, wewe una mke wako,halafu watu wengine waje na sera zao...au ni kwa vile mimi...’akasema

‘Una maana gani hapo…?’ akauliza mwenyekiti.

‘Nimekuuliza hivyo ili unielewe,…nimekuuliza hivi, baba ulipomuoa mama, familia ya mama waliwahi kuja kwako na kuwapangia  jinsi gani bora ya kuishi na familia yako...mbona hayo hamyafikirii, kwanini nyie mnakuja kutupangia sisi jinsi gani ya kuishi, wajumbe hivi hamuoni hawa watu walivyo eeh...’akasema huku akigeuka kumwangalia mama yangu.Na mama akawa anamwangalia tu.

Alipoona wajumbe wapo kimia

‘Kiukweli haya sio maswali ya kuniuliza hapa mbele ya kadamnasi, ni kunizalilisha tu,ni kunitega tu ,sitaki maswali ya namna hiyo, nooh, now its too much...naona sasa mnataka kunikalia puani, mumeshanizalilisha vya kutosha, sasa nasema basi, amueni mnalolitaka....’akasema kwa hasira huku akisimama na huku anamwangalia mwenyekiti akiwa ametoa macho.

‘Huna haja ya kukasirika hivyo, na hoja uliyotoa, au kama ni swali uliloniuliza, halina msingi, ni kuonyesha jinsi gani usivyokuwa makini na ndoa yako,...kwanini tumefikia hapa, ni kwasababu umekiuka sheria za ndoa...hatukuja kuingilia ndoa yako, tumekuja kusikiliza mashitaka ....usitake kuturudisha nyuma....'akasema mwenyekiti.

Mume wa familia akatulia na mwenyekiti akasema;

'Na hilo swali kauliza mke wako, anataka majibu, na ana maana yake kukuuliza hilo swali,kwa wenye hekima wanaelewa ni kwanini kakuuliza hivyo, hatumtetei, bali mimi kama mwenyekiti nimeona hekina ya hilo swali…’akasema mwenyekiti


‘Kwahiyo unataka mimi nijibu hilo swali…?’ akauliza mume wa familia

‘Ndio, jibu swali …baba, usikwepe mada kwa jaziba, jaziba hapa hazitakusaidia kitu,hilo swali  hata mimi naona lina umhimu wake, ili kubainisha ukweli wako ndani ya moyo wako....jibu kama ulivyoulizwa…je ni kweli unampenda mchumba wako wa asili, kwanini hujiamini…’akasema mwenyekiti, na mume wa familia akainama kidogo, na watu walifikiria hatajibu, lakini baadaye akainu akichwa na kusema;

 ‘Kwa hali iliyofikia naona kama mnanilazimisha niseme hata yale yasiyostahili, sawa mimi nitasema ili muweze kufanya mnayotaka, sitajali tena..nitajibu  kama ifuatavyo....,’akatulia

‘Kiukweli hakuna asiye-elewa jibu la swali hilo, japokuwa nafsi itatamani kusema vinginevyo, nakubali nimeshakubali kosa, nakubali kuwa na sisi kutokana na umasikini wetu, tulikuwa katika harakati za kutafuta maisha bora, na njia tuliyoona ni sahihi ni hiyo, kwa vile tulikuwa na mwalimu wetu na yeye kwa kipindi hicho tulimuamini, ..hatukuwa na njia nyingine...’akageuka kumwangalia docta.

‘Docta ataweza kunisaidia hilo, kuwa moyo wa binadamu unakuwa na kitu kikishanasa kwenye moyo, inakuwa vigumu kukiondoa, kutegemeana na mazingira,...tunaweza kujidanganya, tunaweza kujitahidi, lakini kama kitu hicho kipo, kinaonekana kila siku, ..hutaweza kukisahau,…’akatulia

‘Na huenda hilo ndilo kosa lililotokea,...kama mwenzangu angeliolewa mbali kabisa, tukawa hatuonani, huenda tungalisahauliana, lakini ukumbuke kuwa nyuma yetu alikuwepo Makabrasha, anataka tutimize ahadi zake,..na alifanya vitisho vya kila namna hilo hamuwezi kuliona kwasasa… ‘akatulia

‘Jamani mitihani yake ilikuwa mingi , lugha za hadaa, ili tu tuweze kuhadaika,…mtu aje kwako kila siku anakuelezea lugha za kukutamanisha, eeh,..wewe ni mwanaume wewe…ndio mimi kama mtu mzima nilitakiwa niyapime kwanza hayo.lakini nitawaambia nini ili mnielewe...ni vitu ambavyo kama hujakutana navyo huwezi kuelewa...’akasema na kutulia na mwenyekiti alipoona katulia akasema

‘Swali bado lipo pale pale...hujalijibu kama linavyotakiwa kujibiwa, je unampenda mpenzi wako wa asili, au tuulize hivi bado unampenda mpenzi wako wa asili au ulikuwa ukimtumia tu, ili upate yale uliyokuwa ukiyataka,....?’ akaulizwa na mwenyekiti.

‘Umeshasema mpenzi  au penzi la asili,...hilo kwa wengi, wanaolifahamu halifutikia,kuna watu walikuwa na wapenzi wao wa asili, lakini hawakuoana, wakaenda kuoa wengine, lakini moyoni bado ule upendo upo, ...siwezi kudanganya, nampenda, ...’akasema na kutulia kidogo.

‘Lakini nilishaoa…na mapenzi hayo yalikuwa ni  ujana, ni mapenzi ya asili tu, kama unavyosema,…mimi sasa nina mke, kwahiyo nafasi ya upendo wake kama mpenzi wa asili inafichika, unabakia upendo kwa mke wangu..

Sasa mimi siwezi kulikana hilo,…upendo wangu na mwenzangu niwa asili, upon a utendelea kuwepo,…lakini kwa nafasi yake, iliyojificha, nafasi iliyo wazi ni upendo wangu na mke wangu, nampenda sana mke wangu ...ndio maana nikamuoa,...’akasema.

‘Hujaulizwa kuhusu mke wako, kuwa unampenda au la, vitendo vyako vimeshajielezea,swali uliloulizwa ambalo ni muhimu kwako kulijibu ni je bado unampenda mpenzi wako wa asili, ...au hayupo tena moyoni kwako, ikiwa na maana ulikuwa unamtumia tu kukamilisha mambo yako....?’ akaulizwa swali hilo tena.

‘Nampenda, sijasema kuwa simpendi, sio kweli kuwa nilikuwa namtumia tu,upendo wetu haujafutika, ila ni kwa upendo huo wa kiasili, kwa hivi sasa nina mke, kwahiyo mpenzi huyo wa zamani hana nafasi sawa kama ilivyokuwa ....ninaweza kusema hivyo, sina zaidi....’akasema na kuinama chini.

Mwenyekiti, mimi nimeshapata jibu la swali hilo, naomba nieleweka hivyo,...’nikamwambia mwenyekiti na kumgeukia mume wa familia, nikasema;

‘Nashukuru kwa jibu lako hilo, nimekuelewa, kama binadamu hayo yapo...siwezi kuyapinga, lakini mlolongo mzima unajieleza, dhamira yenu, ipo wazi, ....

Mimi nimekuuliza maswali hayo kama nyongeza tu,  ili kusikia kauli yako kutoka kwenye kinywa chako mwenyewe, kwani wenzako walishatamka yao kutoka moyoni, wewe hukupenda kufanya hivyo kwa hiari yako mwenyewe, mpaka shinikizo la ushahidi, sawa, hiyo ndio hulka yako hatuwezi kuigeuza..., sio shida, nimeshakuelewa, ....’nikasema an kumgeukia mwenyekiti.

‘Ndugu mwenyekiti, mimi naona tufunge kikao, ili kila mtu aweza kuyafikiria haya yote yaliyoongelewa hapa, na wanasheria, wayafanye kazi zao kisheria,

Ila bado mimi nasisitiza, nyie kama watu wazima, wajumbe kama watu wazima walioenda shule, nawaomba hili jambo tukae nalo tulitafakarikwa kina, mtusaidie kwa hekima zenu…tusilichukulie kijaziba…’nikatulia

‘Nayasema haya kwa vile sote ni watu wazima,…tuna familia , tuna watoto, tunakuza, je haya yalitokea tufanyeje,..tusaidiane kwa hilo…kabla mimi sijaweza kuyasema ya kwangu,…tuziangalia familia zetu,…tuangalia maisha yetu, tuiangalia jamii, je haya yalitokea tufanye nini,..,...nafikiri tukikaa tukitafakari tutaweza kuja kwa majibu mazuri,…

Sasa kwa niabaya yangu nay a familia yangu, samahani sana kuwasumbua wazee wetu, majirani zetu, marafiki,… nafahamu mlihitajika kupumzika, lakini hili pia ni jukumu lenu, kama wazazi, naowaombeni tena mkae mtumie hekima zenu, ili muone tutalitatuaje hili tatizo…kwahiyo nawaombeni tukutane tena siku nyingine…’nikasema na mwenyekiti akawa sasa anaangalia saa yake..

‘Ila kiukweli, mimi napenda kusimamia kwenye haki na ukweli…na sijajua maamuzi yangu hadi hivi sasa, akili bado imeganda, sio jambo rahisi kama mnavyoliona nahitajika kutafakari kwa kina ….naombeni  mnielewe hapo....’nikageuka kumwangalia mume wangu.

Yeye sasa alikuwa akiniangalia mimi nikiongea kwa macho yanye kutoa huruma, lakini kwa muda huo sikuweza kuiona huruma yake zaidi ya kuona jambo jingine akilini mwangu.

Nikageuka kuwaangalia wanasheria wetu,..walikuwa wakiandika andika mambo yao, na baadae nikageuka kuwaangalia wale walioitwa marafiki zangu…huwezi amini kila niliyemuangalia nilikuwa simuoni yeye, naona taswira nyingine kila mmoja kwa uhalisi wa fikira zangu, halafu nikageuka kumwangalia mwenyekiti, na kuendelea kusema;

‘ Basi ndugu mwenyekiti, kwa ruhusa yako,…sijui kama tutaweza kuendelea na ajenda nyingine mimi siwezi kukuingilia, ila kwa hili letu naomba tupatiwe muda kwanza..’nikasema

‘Mnahitajia muda gani…?’ akauliza mwenyekiti akituangalia sisi wawili

‘Hata kesho tunaweza kuitisha kikao, kwa …nafasi za wajumbe, labda muda gani ni wao wasema..kiukweli mimi hapa, akili yangu hapa haifanyi kazi tena,tatizo ni kuwa kuna wale wa kusafiri,..na kama ulivyosema kuna watu wa usalama wapo nyuma yetu, sasa sijui.... ‘nikasema

‘Hilo la watu wa kusafiri na watu wa usalama niachie mimi…’akasema mwenyekiti.

‘Basi kama ni hivyo, sisi tutakusikiliza wewe, au wajumbe mnasemaje..?’ nikauliza

Wajumbe wakajielezea kila mtu kwa kauli yake, lakini ikaonekana kuwa wajumbe wapo tayari kwa hilo, ila muda ukawa ni tatizo.

 ‘Sawa mke wa familia, lakini nakuonya, usiniingilie uenyekiti wangu,...’akasema na kuangalia saa yake, halafu akageuka kuwangalia watu, akasema;

‘Ni kweli,  nikiaangalia saa muda umekwenda sana, na kuna watu wapo hapa, japokuwa wanahusika kwa namna moja au nyingine, lakini wanakazi zao, kuendelea kuwachosha hapa ni kuwatesa, yupo docta hapo, japokuwa kaniambia yupo mapumziko, lakini anahitajia kupumzika, wapo mawakili wetu, na kulikuwa na watu wa kusafiri kesho, tunaomba, ...kama ilivyoombwa, waahirishe safari zao...’akasema na kumwangalia mke wa docta, na mke wa docta akasema;

‘Kwangu haina shida, nitaangalia, na muelekeo ulivyo, kama nilivyokudokezea..’akasema na mwenyekiti 
akamwangalia kwa mashaka, halafu akageuka kuangalia wajumbe huku akisema;

‘Kwa upande wa binti yetu wa kufikia..oooh, hilo nitaongea na mwenzangu, tutangalia kama inawezekana kuahirisha hiyo safari yake, maana alishajiandaa kuondoka, hata hivyo kwa vile ni muhimu sana na inagusa hatima yake na mtoto wake, tutaliangalia hilo, na nitawajulisha kesho asubuhi na mapema kama kikao kipo au tupange siku nyingine

‘Hata hivyo wasi wasi wangu ni kwa watu wa usalama, nahitajia kupata kibali chao, hili tatizo sio la ndani ya familia tu, tatizo letu limegusa na maswala ya kijinai, ni muhimu sana mkalielewa hilo, kwahiyo kila tunalolifanya kama familia, tunahitajika kuwajulisha wenzetu wa usalama, ili tuweze kusaidiana nao, ndio jukumu letu kama raia wema,...kwahiyo kwa hili lipo nje ya uwezo wetu maamuzi yao yanaweza kuathiri muda wa kikao…hatujui…

‘Kwa hivi sasa tunavyoongea hapa, wao , watu wa usalama wapo kazini, wanahangaika kumtafuta muuaji wa Makabrasha, msifikiri kifo chake kimefukiwa na mchanga, hapana, wanawajibika, usifikiri umesalamika kama unahusika, kifo cha mtu kinamuandama mtendaji hadi siku anaingia kaburini,

‘Na kwa taarifa tu, wao wamesema wao tayari kumnasa muuaji halisi. Anaweza akawa miongoni mwetu, hatujui, kwani kafanya hilo tendo kwa ujanja wa hali ya juu....’akakatiza mazungumzo, kwani simu yake ilikuwa inalia, akaangalia mpigaji, akawaangalia wajumbe, halafu akasema;

‘Samahani subirini kidogo niongee na watu wa usalama, naona ndio hao wananipigia huenda kuna amri nyingine,...subirini kidogo msiondoke....’akasema  huku akipokea hiyo simu...

NB: Haya tunasubiri hukumu..


WAZO LE LEO:Jehivi kweli kuna kisingizio cha kuisaliti ndoa yako? Je unaposalitiwa au kusaliti ndoa yako kama mwanandoa unahitajika kufanya nini?. Ni maswali madogo lakini yenye mambo makubwa, wewe kama mwanandoa kama mwenzako kaislaiti ndoa yenu mtafanya nini..


Toa maoni yako hapa…

Ni mimi: emu-three

No comments :