Wakati nipo nje kwa dhamana, baada ya kushukiwa kuwa eti
mimi ndiye niliyemuua Makabrasha kwa kutumia watu, kwa vile nilionekana kwenye
ofisi ya marehemu huyo. Ili kuondoakana na kashifa hiyo, nikaona ni bora na
mimi nifanye uchunguzi wangu wa kina, kubaini ni nini kinachoendelea ndani ya
familia yangu, hadi kufikia hatua hiyo.
Niliona nianze na ndoa yangu mwenyewe, kwa kumchunguza mume
wangu, kutokana na mabadiliko yake, ambayo mimi nahisi kuna kitu kimetokea na
kumbadili mume wangu, kwani hakuwa hivyo kabla, japokuwa wazazi wangu waliniasa
kuwa huyo ni kunguru hafugiki, ....sikukubaliana na hilo, eti kutokana na
historia ya familia yake, ndio maana mambo yote hayo yanatokea.
Sikukata tamaa, mimi niliona nijaribu kila iwezekanavyo ili
mume wangu arudi kwenye mstari, na ili nifanikiwe hilo, kwanza nilianza kwa
kunyenyekea, kumuomba na kumsihi, lakini nilipoona hilo halifanikiwi, basi
nikaona nitumie ule uwezo wangu mungu
alinionijalia nao, japokuwa sikupenda kufikia huko. Nilijaribu kuongea naye
mara kwa mara, ili aniambie ukweli, lakini mazungumzo yetu hayakufika kokote,
yeye aling’ang’ania kuwa anachofuata ni taratibu tulizokubaliana ambazo zipo
kwenye mkataba , kila kitu anafuata mkataba, kila kitu anafuata mkataba...
‘Mume wangu nimeshakuambia mkataba huo unaoufuata wewe
haukubaliki, ...na ukiendelea na tabia hiyo, mimi nitachukua hatua nyingine,
...’nikasema.
‘Hatua gani tena mke wangu,...mimi ni mume wako, na
ninalofanya jesha ni kwa masilahi yetu sote, mimi na wewe na familia yetu, na
watoto wetu,...sifanyi kwa kujinufaisha sisi, huoni siku hizi nimeacha kunywa
kabisa....’akasema.
‘Umeacha kwasababu ya mipango yako ambayo unahisi
imekamilika, ...’nikasema.
‘Mipango gani mke wangu...kwani mkataba wetu unasemaje,
..mbona hutaki kuukubali, kuna tatizo gani pale...’akarudio huko huko kwenye
mkataba.
‘Kama unataka tuelewane, rejesha ule mkataba wa awali, hapo
tutakaa meza moja kama mke na mume, lakini kama utaendelea na mkataba wenu huo
wa kugushi, basi, nitakuacha uendelee na maisha yako na mimi nitaendelea na
maisha yangu...’nikasema.
‘Hapana, siwezi kukubali hilo, mimi ni mume wako na mimi
ndiye kiongozi wa familia, na natakiwa kuhakikisha familia yangu ipo pamoja,
...nataka watoto wetu watuone tuna upendo na mshikamano,..’akasema.
‘Wewe ndiye uliyesababisha haya yote, kashifa imeingia
kwenye familia , tumeanza kwenye ulevi,
ndoa isiyo na masikilizano, ..kuzaa nje, imekwenda hasi kushutumiwa kuua,
kugushi, ulaghai, hivi hayo ni maisha geni unayoyataka wewe, mimi sijakulia
kwenye maisha ya namna hiyo, familia yangu ni safi....’nikasema
‘Ina maana unaninyanyapaa kuwa familia yangu ni chafu, ndio
maana haya yote yanatokea?’ akauliza
‘Usiongelee kuhusu familia yako ongea kuhusu wewe
mwenyewe,...kwasababu wewe una uwezo wa kujibadili na kuwa mtu mwema,
mwaminifu, mkweli ....unaweza kabisa, lakini kama unataka kuishi kwa ujanja
ujanja...hutafika mbali...’nikasema.
‘Mke wangu mimi kama mume wako, naomba kauli hiyo, ya
kuiniona mimi mchafu, tapeli mlaghai,..iishie, ..’akasema huku akinitolea
macho, na mimi nikatabasamu na kusema;
‘Itaisha pale utakapoleta mkataba wetu wa awali,
tuliokubalina kwa rizaa moja,....’nikasema.
‘Mkataba ni mmoja tu, hakuna mkataba mwingine, mkataba ni
ule ule,...ila wewe unataka kunipanda kichwani, ili nisiwe na sauti kama
mume..hili mimi siliafiki,...na nakuomba mke wangu, jaribu kuniangalia na mimi,
unielewe na mimi...kwani nimefanya nini kibaya’akasema kwa sauti ya upole.
‘Wewe sio mkweli, ...’nikasema
‘Kwa vipi, mbona nimekuambia ukweli, kuhusu mkataba wetu,
...sijaukiuka, ..kuna jingine mke wangu,
hakuna, nimejaribu kuwa mume mwema, silewi tena, hilo huliungi mkono, unataka
nianze kuelewa tena...’akasema.
‘Usibadili mada, mkataba wetu wa zamani upo wapi,..pili huyo
mtoto uliyezaa nje ni nani, na umezaa nani, nijibu hayo maswali, na hayo
ukiyaweka wazi, tutakubaliana, ...’nikasema.
‘Mkataba hauna shida, mkataba ndio huo, mimi sijui mkataba
mwingine, mtoto niliyezaa nje, ilikuwa ni bahati mbaya, na ilitokea kutokana na
wewe..’akasema
‘Kutokana na mimi, mimi ndiye niliyekutuma ukazini nje...’nikasema.
‘Matendo yako ndiyo yaliyonisukuma hadi nikafika huko,
sikuwa na raha kama mume, wewe muda wote upo na kazi zako, sikuwa na raha kama
mume, sikuwa na sauti kama mume, nilikuwa nipo nipo tu,....nikawa natafuta njia
ya kijiliwaza,...nikaona pombe atakuwa mpenzi wangu, kumbe pombe ina mitihani
yake...’akasema huku natamani kumzaba kibao, nilimuona kama mtoto mdogo vile.
‘Hivi wewe hujitambui hayo unayoyaongea, unaongea kama mtoto
mdogo, ..ulewe kwasababu ya kujiliwaza, ....sikuelewi, ulienda kulewa kwasababu
ya starehe zako, mimi muda wote nilikuwa hapa ndani, kwanini hukuniambia
unachokitaka wewe...?’ nikamuuliza.
‘Hivi kulikuwa na raha gani, ....wewe hukutaka hata
nikuguse, ..unakumbuka, au umesahau, ..tuyaache hayo, kwangu yamekwisha,
nakuomba mke wangu tuishi kama mke na mume, tupendane kama zamani, tugange
yajayo....’akasema.
‘Hujanijibu huyo mtoto uliyezaa nje, ni nani na ulizaa na
nani?’ nikamuliza.
‘Hilo nitakuambia pale utakapokubaliana na mkataba wetu,
maana kila kitu kipo wazi, na huyo anatambulikana kama mtoto wetu,...ana haki
zote ndani ya familia hii....’akasema.
‘Una kichaa kweli...uzae ovyo mitaani, uniletee watoto, eti
wana haki, ina maana gani ya ndoa...je na mimi nikizaa nje, nikaleta mtoto hapa
utamtambua?’ nikamuuliza.
‘Kama io kwenye mkataba nitamtambua....’akasema.
‘Unanichefua,...nashindwa hata kukuelewa, sikiliza, mimi
ninakupa wiki moja, nataka mkataba wa zamani uje, kama hautapatikana basi,
...tutaita mawakili wetu, tutaangalia haki ilipo, na ikibidi tutafikishana
mbali,...nisingelipenda kuwashirikisha wazazi wangu kwa sasa...ila baada ya
wiki moja hiyo kwisha, kama utaendelea na ujinga wako huo....hutaamini kuwa ni
mimi...’nikasema.
‘Mke wangu, kwanini unakasirika,...kwanini yote hayo, mbona
mimi nakupenda, na nafanya haya yote kwa mapenzi ya dhati...jaribu kunielewa na
mimi....mbona hutaki angalau kuusoma huo mkataba ukaoana mambo yake, hakuna
ubaya kabisa, ....mimi sitakubali kamwe ndoa yetu ivunjike, ....nakuhakikishia
hilo....’akasema
Mimi sikutaka kuongea naye siku hiyo, nikaondoka kuendelea
na shughuli zangu nyingine
***********
Kwa hali kama hiyo niligundua kuwa mume wangu anahusika na
hayo yaliyotokea, lakini sikuwa na uhakika wa moja kwa moja kuwa alifanya hayo
kwa dhamira yake au kulikuwa na shinikizo kutoka kwa marehemu.Na je nay eye anahusika
na kifo cha rafiki yake. Hilo la kifo cha rafiki yake hata polisi walifika
sehemu wakashindwa kumbaini muuaji ni nani, na kusema kuwa jamaa huyo aliuliwa
na mmoja wa maadui zake, ambao walikuwa na kisasi naye, na uchunguzi bado
unaendelea.
Siku zikawa zinakwenda, na mimi nikaendelea na msimamo wangu
wa kutokuutambua mkataba huo waliotayarisha wao, sikutaka kulifuatilia kisheria
zaidi, hata wakili wangu aliyetaka kulifuatilia kisheria, nilimwambia anipe
muda kwanza nijaribu kivyangu, ikishindikana, itabidi tuingie kisheria.
Ikafika mahali mimi na mume wangu hatuongeai, sikutaka hata
kuonana naye, mimi niliweka agizo langu kuwa nitakaa meza moja na yeye pale tu
huo mkataba wa zamani utakapopatikana. Nikaanza kumwekea shinikizo, kwanza
nikakata mawasiliano ya kuongea naye, na kutokushirikiana naye kwenye shughuli
zozote alizozifanya kimkataba. Hata hundi za benki ambazo nilihitajia mimi
kupitsha nikazizua, kwahiyo akawa hana uwezo wa kipesa zaidi ya kiasi kile
alichoruhusiwa kukutoa kwenye kampuni yake, kwani kiasi kikzidi sana ilitakiwa
sahihi yangu na yake, kutokana na kumbukumbu za kibenki.
Hali ilivyozid kuwa mbaya, akaona amtumie rafiki yake, ili
aonge na mimi na ikibidi tukae tuyaonee kama mke na mume, lakini sikutaka
maongezi yoyote na huyo rafiki yake, nikishinikiza kuwa mkataba wa awali uwepo
kwanza.....halafu tutakaa na kuyamaliza.
‘Sasa kazi zitasimama, na kampuni zinaweza kuyumba...’akasema
huyo rafiki wa mume wangu.
‘Kama analiona hilo ni wajibu wake, kuleta huo mkataba wa
awali, na kama anajiona kuwa anauwezo wa kufanya anavyotaka basi aendelee, na
siku nitakapo kamilisha uchunguzi wangu na kuwa na ushahidi kuwa yeye
alishirikiana na marehemu kufanya hayo yaliyotokea, nitampeleka
mahakamani....’nikasema.
‘Lakini mambo ya kampuni msiyaingize kwenye mambo yenu ya
kifamilia’akashauri.
‘Sisi tulikuwa na utaratibu wetu zuri tu, yote hayo ya
kikampuni , ya kifamilia, tulikuwa tumekubaliana, ili kulinda mali za familia,
...kama tusingelifanya hivyo, kampuni hizo zisinelikuwepo, angalia sasa
anavyofanya yeye, ana mtoto nje, na kama ana mtoto nje, ina maana ana kimada
nje, ni nini kitaendelea hapo, kama sio kuanza kugawa mali halali, zilizotokana
na jasho letu kwa watu wasio jua kabisa zimetoka vipi...’nikasema.
‘Sitaki nikukumbushe ..lakini inabidi nikuambie, hayo
umeyataka wewe mwenyewe...nilikuambia mwanzoni jaribu kuwa akribu na mume wako,
jaribu kuangalia ana shida gani anataka nini, ujue kuwa binadamu wote sio sawa,
kuna utofauti wa kuwaza, unavyowaza wewe, na kutathimini mambo sio sawa na
ataakvyowaza mwingine...’akasema.
‘Nakufahamu sana, huenda hayo mliyapanga pamoja, ili
kujionyesha kuwa nyie ni wanaume, mnaweza kufanya mpendavyo, au sio...mlewe ,
mtembee ovyo na wanawake , mzao ovyo, si ndio,...?’ nikamuuliza.
‘Sina maana hiyo..ila maisha ya ndoa,msipovumiliana, mkaweza
kukaa pamoja, mkajaribu kuziangalia zile tofauti zenu za kifikira, mkazitafutia
suluhu, siku mambo yakiharibika inaweza ikaleta shida sana kujirudi, kwasababu
muda huo kila mmoja atakiona yupo sahihi...kama mngelikaa na kujuana, na
kuangalia mwenzangu anataka nini, mgeliweza kulizuia hilo....’akasema.
‘Mwambie rafiki yako, kama anataka tukae tukubaliane, aulete
mkataba wetu wa awali, kwasababu siwezi kukubali huo mkataba wa kugushi,
wamekaa na mwenzake, marehemu, wakatunga mambo yao, mimi sikuwepo, na humo
wameweka ammbo ambayo mume wangu atajifanyia apendavyo, bila hata kibali changu....huoni
kuwa ni hatari, kutokana na hilo, nasikia kuna mkataba mwingine, ambao, yeye
kama mume, kutokana na mkataba huu, ana hiari ya kuuza hisa kwa mtu mwingine...’nikasema.
‘Mhh, una uhakika na hilo?’ akaniuliza.
‘Ndio maana sitakubali huu mkataba wao, ..kamwe, kwani
nikikubali tu, kampuni yake, hatakuwa na hiari nayo, kwani marehemu
alishachukua zaidi ya nusu ya hisa, na kampunu yangu hii, marehemu ana hisa,
...ni nani alipitisha hilo, ....hebu niambie, mimi nikubali tu, ...ina maana
gani kuhangaika, kutokulala, usiku na mchana tulihangaika, leo matunda
yamepatikana, yachukuliwe na watu wengine kirahis rahisi tu....na kakubali
mwenyewe ana mtoto nje, na huyo mtoto, mzazi wake, wana haki, na watachukua
sehemu ya mali,...hivi nyie watu mnaniona mimi ni mjinga kiasi hicho...’nikasema.
‘mimi hayo siyajui, maana ulishanipiga marufuku kufuatilia
mambo ya ndoa yako, nilishakuambia kama unanihitajia ni kusaidie,nipo
tayari,...sasa nawashangaa, kesi yenu haijaisha, bado mpo kwenye migogoro ya
kifamilia hamuoni kuwa mnaweza kukosa yote?’ akaniuliza.
‘Kama nilivyokuambia toka awali, wewe endelea na familia
yako,mimi hili nitalimazia mwenyewe, yupo wakili wangu, nikishindwa
nitamkabidhi, na hapo itakuwa ndio mwisho...’nikasema
‘Upo tayari kuvunja ndoa yako kwasababu ya hilo?’ akaniuliza
‘Wewe unaliona ni dogo eeh, ikifikia hapo, hutaamini, kwanza
huo mkataba wa zamani ukipatikana tu,...kama tulivyoahidiana, hatua kwa hatua,
tutatekeleza, na huyo mwanamke wake waliyezaa naye, mimi nitamuonyesha kuwa ni
nani...huwa nikiahidi kitu sirudi nyuma,....’nikasema.
‘Ndio maana mume wako anaogopa kuulea mkataba wenu wa
zamani...’akasema.
‘Huo ni uwoga,...yeye kama ni mwanaume, anatakiwa aingie
uwanjani, apambane kiume, na asipofanya hivyo, akaegemea mawazo ya wenzake, atakosa yote....hajui mimi
ninawaza nini, hajui nina mipango gani kichwani, ..hajui...kwani nimetoka naye
wapi,...hakumbuki hilo,...’nikasema.
‘Haya mimi sitaki tena kuingilia mambo yenu, nitakuja tu
pale mtakaponihitajia, kama ulivyowaambia wazazi wako, wasiingilie, mambo yenu,
sisi tunawaangalia lakini kama mkikwama, sisi tupo tayari kuwasaidia..’akasema
na kuondoka.
************
Siku moja wakati nipo nyumbani nimepumzika, nikaambiwa kuna mgeni
anataka kuongea na mimi, nilikuwa sitaki kuongea na mtu, lakini nikaona ni
vyema kumsikiliza huyo mgeni, kibusara, nikauliza;
‘Ni mgeni gani huyo?’ nikauliza.
‘Ni mtoto wa marehemu Makabrasha..’akasema msaidizi wanguu
wa ndani.
‘Huyu mtu, nilishampiga marufu....’nikaanza kufoka, lakini
akili yangu ikanituma niongee naye tu, nilikuwa nimekataa kata kata kuongea
naye, nikiwa kwenye shinikizo lile lile la kupata mkataba wa zamani, lakini
siku hiyo sijui kilinijia kitu gani, nikasema wamkaribishe bustanini, sikutaka
kuongea naye ndani.
Walimkaribisha bustanini, nikaenda na nilipofika tu, nikamsalimia
kama ada, sikutaak kumuonyesha jinsi gani nilivyochukia, maana moyoni niliona
kuwa wao, kutokana na bba yao, watakuwa wamepanga jambo la kuifisidi familia
yangu. Nilipokaa nikasema;
‘Haya niambie una shida gani na mimi?’ nikamuuliza huku
nikimwangalia moja kwa moja usoni, maana tulikaa tukawa tunaangaliana na kati
kati yetu kulikuwa na meza. Nilitaka nimuone usoni, kwani mtu unaweza kumpima
ukweli wake, au ujasiri wake, kwa kumwangalia usoni.
‘Samahani sana kwa usumbufu wangu, wa kutaka kuongea na wewe...maana
nimejaribu mara nyingi bila mafanikio, na leo nilipanga, kama ikishindikana
basi nitaondoka,...siku zangu za likizo zimeisha, natakiwa kurudi
kazini...Ulaya...’akasema.
‘Sawa pole sana, ehe, unasemaje..?’ nikauliza.
‘Mimi sina nia mbaya kama unavyofikiria wewe,..huenda
ungelisikiliza toka awali tungelishamalizana, na kila mtu akashika hamsini
zake. Hapa nilipo nakwama kuondoka maana mambo bado hayajakaa sawa, na mimi
nimeachiwa majukumu mengi na marehemu baba....’akasema.
‘Hayo majukumu uliyoachiwa, yananihusu nini mimi?’ nikauliza
na yeye bila kujali swali langu akaendelea kuongea.
‘Mimi nilipofika hapa Dar kutoka nje kutokana na kifo cha
baba...nilitarajia mengi, maana mimi namfahamu
sana baba. Kwani nilitaka kujua
ukweli wa kifo cha baba, na nilipewa taarifa yote kutokana na uchunguzi wa
polisi. Na nilihisi nyie mnaweza mkahusika, ...na kiukweli kama mngelikuwa
mnahusika, ningesimama kidete kuhakikisha haki inapatikana,..lakini kutokana na
taarifa ya uchunguzi wa polisi, ikaonekana hauhusiki, na kwa kujirizisha,
nikafanya uchunguzi wangu binafsi, na kuhakiki taarifa niliyopewa, nikagundua
kuwa mambo ni yale yale....’akasema.
‘Mimi ninamfahamu sana marehemu baba yangu, nafahamu sana
mbinu zake za kupata mali, ..ndio yeye alikuwa ni wakili, lakini kazi hiyo,
aliitumia kama kivuli, nilikuwa nafahamu kuwa kuna mambo alikuwa akiyafanya
ambayo sio sahihi, na hilo nilikuwa napingana nalo sana.....’akasema.
‘Kifo chake hakikunishitua sana, maana ukiishi kwa kazi kama
hiyo aliyokuwa akiifanya yeye, ujue kifo kipo pembeni yako, mimi naishi nje, na
nimeona watu wa aina hiyo wanavyouwawa...blackmail,ni
kazi ya hatari sana, sio mchezo, kumghilibu mtu, na kupata kile alichokihangaikia
kwa jasho lake kwa shida, wewe uje ukichukue kilaini, ..na unapoanza kwa tabia
hiyo, hukomi, utataka leo, kesho na kesho kutwa, inafikia huyo mtu anaona ni
bora akuue tu,..nilimkanya sana baba yangu, lakini hakunielewa...’akaendelea
kusema.
‘Mimi nilikuwa sielewani
na baba tangu niwe na fahamu naye, japokuwa sikuwa ninaishi naye, maisha
yangu, nililelewa na babu na bibi, maana mama alikuwa akiishi huko ,....na hata
nilipokuwa nasoma hapa mjini ambapo nilikuja kukaa naye, hatukuwa tunaelewana,
damu zetu haikufanana,....mimi nia na lengo langu ni kusoma, na kutokumtegemea
baba, na kweli juhudi zangu na dua zangu zikakubaliwa, nikafaulu mitihani, na
nikapata nafasi ya kwenda kusoma nje ..kwenda kwangu nje, hakukuwa na mkono
wake, nilihangaika kivyangu, nikafanikiwa, na huko nikasoma kwa shida sana, na
aliposikia nasoma kwa shida, akanitumia pesa...nilizikataa
kabisa...nikamrudishia, hutaamini.
Hapo nikamuuliza;
‘Kwanini ulifanya hivyo?’ nikamuuliza nikimwangalia machoni,
huyu mtu huwezi kumhisia vyovyote, hajionyeshi tabia yake usoni,..ni watu
wachache wenye tabia hii.
‘Kwasababu nilijua pesa zake ni chafu na mimi sitaki pesa
chafu, ndio maisha yangu nilivyoamua yawe hivyo, wewe hujiulizi kwanini baba
alikuwa hakai na mama, ..mama alifahamu tabia ya baba, akaona ajitenge naye, na
mimi nimerithi tabia ya mama...nataka niishi kwa jasho langu, sio kama
alivyokuwa akiishi baba...’akasema.
‘Kifo cha baba, kikatufanya tukutane kama familia, nashukuru
sana kuwa wanafamilia wote walikuwa wakimfahamu baba, hakuna aliyetaka
kuingilia mambo yake, kila mmoja aliona kuwa akigusa huko huenda damu za watu,
walioumia zitamuandama. Mimi nikapewa jukumu la kusafisha jina la baba, maana
keshakufa, na maisha yanahitajika kuendelea, ..je tutaendelea kukumbatia hiyo
hali, hapana, ni lazina jambo lifanyika..’akatulia.
‘Kazi yangu kubwa, ilikuwa kufuatilia kwa kile aliyeumia
kutokana na baba...wapo wanaojulikana, na tulitanagaza kama kuna mtu kwa namna
moja au nyingine alipata athari, kutokana na utendaji wa baba akitokeze,..watu
waliona kama ni utani,..mimi nikafanya kazi ya zaida kuwafuta, na kujaribu
kutafuta suluhu...na ili hayo yafanikiwe, tulimtafuta mwanasheria ambaye alisaidia
kisheria....’akasema.
‘Tatizo likaja, kuna huo mkataba ...ambao hatukuwa na uelewi
sana nao, unaonyesha ni wa karibuni, ndio tukaanza kuufuatilia, na hapo
nikakutana na mume wako....namfahamu sana mume wako , maana mimi namtambua kama
baba mdogo, kwa jinsi familia yao na yetu zilivyokuwa karibu, na baba yangu na
mume wako walikuwa marafiki sana japokuwa baba yangu alikuwa mkubwa kwa mume wako.
‘Huu mkataba kama
tungelikuwa ni watu wa tamaa, basi tungeliutumia, kiukweli kama tungeliamua
kuutumia, tungeliweza na kuhakikisha kuwa tunarithi hayo aliyoyaacha baba,
ikiwemo kumiliki kampuni zako,....’akasema
‘Huo mkataba upo wapi?’ nikamuuliza
‘Huo mkataba ninao, ....’akasema
‘Nataka kuuona,...’nikamwambia.
‘Bado anao mwanasheria wetu, ....’akasema
‘Anao kwa ajili gani?’ nikamuuliza
‘Kuna mambo bado hayajakaa sawa, na hili linatokana na mume
wako, kama mume wako angelikubaliana na sisi, basi
tungelishamalizana,...’akasema
‘Mambo gani hayo mume wangu hajakubaliana na nyie?’
nikamuuliza
‘Kuna vipengele vingi vipo humo, vikionyesha kuwa mume wako
ndiye anamiliki kampuni yake na yako kwa asilimia fulani za hisa, lakini katika
mkatana aliouacha baba , kuna kipengele walishindwa kukubaliana, ...’akasema
‘Kipengele gani hicho?’ nikauliza
‘Baba alitaka kumiliki zaidi ya aslimia hamsini ya hiza za
kampuni ya jina la mume wako, na alitaka
jina hilo libadilishwe....na hapo kukatokea sintofahamu, nahisi hata kifo cha
baba kilitokea siku walipokuwa wakibishana kuhusu hilo...’akasema
‘Wewe umejuaje hayo, na wakati hukuwepo....?’ nikamuuliza
‘Baba alikuwa na kawaida ya kuhifadhi kumbukumbu za matukio
yote, ..tulichokuja kuona ni ajabu ni kuwa mle ndani kwenye hicho chumba
kulikuwa na kifaa cha kunasa matukio, lakini sehemu hiyo ya kifo cha baba
haikuwepo, ina maana huyo muuaji, alirudi na kufuta sehemu hiyo.
Mimi ni mtaalamu sana wa komputa, nikafanya mambo yangu, nikagundua sehemu ndogo inayoonyesha jinsi
gani kifo cha baba kilivyokuwa, ndio nikagundua kuwa aliuwawa na watu wake
waliokuwa hawaelewani naye...’akasema
‘Ni watu gani hao?’ nikauliza
‘Imeshindikana kuwagundua ni akina nani, huyo muuaji
hakuonekana sura, ...na alitokeza kiogo tu, huku kiasi cha kuweza kulenga
shabaha..na hakuweza kuonekana sura, alikuwa kaziba kabisa uso wake, na kuacha
macho tu,hata polisi hawanafahamu sehemu hiyo, mimi nafahamu ilivyokuwa
kutokana na kumbukumbu hizo,, na kwa vile niligundua kuwa huyo muuaji hataweza
kugundulikana, nikaona haina haja ya kuwapa polisi hiyo taarifa...’akasema
‘Kwanini?’ nikauliza.
‘Kwasababu sehemu kubwa inamuonyesha mume wako, na polisi
wangeliona sehemu hiyo mume wako angelikuwa kwenye hatia,...’akasema
‘Mimi sikuelewi hapo mume wangu alikuwa anaumwa,
inaonyeshaje kuwa alihusika?’ nikauliza
‘Siku huyo mume wako alikwenda kumuona baba, marehemu baba, ndivyo
inavyoonyesha, na walikuwa akibishana kuhusu huo mkataba na kiasi cha hisa baba
anachokihitajia....’akasema.
‘Hebu samahani kidogo, kwanini baba yako alihiaji kiasi
kikubwa cha hisa?’ nikamuuliza.
‘Kutokana na hayo mazungumzo, wazo, na mambo mengi kuhusu
kampuni ya mume wako yalitokana na marehemu baba, alivyokuwa akielezea ni kuwa
kumbe japokuwa baba hakuwa moja kwa moja kwenye hiyo kampuni, lakini yeye
alichangia mambo mengi,...kuna mambo yalikuwepo humo, yalifanywa ba marehemu
baba....’akasema.
‘Hapo sizani kama ninaweza kuelewa, anyway, endelea....’nikasema.
‘Siku ile mume wako, alifika kwa baba, ...haya ninayokuambia
hata mume wako hajui kuwa ninayafahamu,...sijamwambia, ila alifika wakaanza
kuongea, na siku hiyo walipanga kuhitimisha makubaliano yao,...na ikafika
sehemu mume wako akakubali na kuweka saini, walipomaliza, na wakati wanapena mikono ya kuagana, mara
mlango ulifunguliwa na mtu aliyekuwa kajifunika sehemu zote za usoni, usingeliweza kuiona sura yake,
akampiga baba risasi, kifuani kwenye moyo, na kufa hapo hapo..’akatulia kidogo.
‘Na wakati anataka kumpiga mume wako, ikasikika sauti ya mtu
akiita kwa nje, kwahiyo huyo mtu akashindwa kumpiga risasi mume wako,, akageuka
kukimbia, lakini akaiacha hiyo bastola pale ilipokuwa...kama inavyoonekana
kwenye huo mkanda...’akasema
‘Ukiangalia hiyo sehemu utaona vyema jinsi gani mume wako
alivyochanganyikiwa, kuonyesha kuwa hakuwa anafahamu ...maana ungelisema ni mtu
wake, aliyempanga kuja kufanya hivyo, alishituka, na kuweka mikono usoni, kama
vile mtu anavyoogopa kupigwa ...akainama na huyo muuaji alipoondoka, akikimbia
, mume wako akafunua mikono, na alipoona baba keshafariki, akawa anahangaika,
akishindwa afanye nini...baadaye, sijui alijiwa na wazo gani, akafungua mlango,
na kutoka, ...huwezi kuona kitu nje ya chumba...na sehemu hiyo iliondolewa.
‘Kwahiyo sura ya huyo muuaji haikuonekana, na huyo mtu
alitaka kumuua pia mume wangu?’ nikauliza
‘Ndivyo ilivyokuwa inaonyesha, kwani baadaye mume wako alionekana
akiuliza;
‘Wewe nani....’akatoka na hakuonekana kurudi tena...
‘Sasa kwanini usiwaonyeshe polisi, maana ingewasaidia kujua
zaidi?’ nikamuuliza.
‘Tunafuata maagizo ya baba, licha ya kuwa sikuwa na
mahusiano mema na yeye, lakini nakumbuka jinsi alivyokuwa akiniambia kuwa mume
wako nimuheshimu kama baba yangu mdogo, kwani amewahi kumsaidia sana..hata mimi
alinisaidia sana nikiwa mdogo..na alimsaidia sana mama, kipindi mama alikuwa
anaumwa sana, hana pesa, yeye alijitolea kuuza mbuzi wake, aliyekuwa naye,
mmoja, kwa ajili ya kumtibia mama,...mimi nilimwahidi baba kuwa mume wako
atakuwa baba yangu mdogo, na sitaweza kumvunjia heshima.
‘Sijakuelewa hapo, hata kama ni mhalfu, utamtetea tu, na huenda
akahusika na kifo cha baba yako?’ nikamuuliza.
‘Mume wako hahusiki na kifo cha baba yangu, hilo nina
uhakika nalo...usuhuba wao ni wahali ya juu, kifo cha baba kimemuumiza sana
mume wako, ..wewe hujui tu, yeye ndiye aliyekuwa kichwa chake, kila uliloliona
mume wako akilitenda, mara nyingi, alikuwa akifuata ushauri wa baba...’akasema.
‘Hata kuzaa nje ya ndoa?’ nikamuuliza
‘Hiyo ni sehemu ambayo nitakusimulia kama utakubaliana na
maombi yangu...’akasema
‘Maombi gani?’ nikamuuliza
‘Umsikilize mume wako..mkubaliane naye..mkisha kubaliana
naye , mkawa kitu kimoja,basi sisi tutajitoa kabisa kwenye huo mkataba
ulioandaliwa kuwa baba alikuwa na hisa, ...maana nyie bila kukubaliana bado
tutakuwa hatujafanya lolote, na sisi hatutaki kujihusisha na mambo yake,
hatutaki kupata mali isiyo halali,...lakini tunahitajika kumsaidia mume wako,
kwani ...wema wake kwetu ni mkubwa sana...’akasema.
Mimi nikatabasamu na kumwangalia huyo jamaa kabla sijamjibu,
nikasema;
‘Naweza kuonana na mama yako.....?’
NB: Inatosha kwa leo
WAZO LA LEO: Urafiki
ni mzuri, unajenga mahusiano mema, lakini tujaribu kuangalia aina ya marafiki wetu,kuna
marafiki wengine wana tabia mbaya, kazi zao sio nzuri, ni za dhuluma, marafiki
hao hawafai , na ikiwezekana tengana nao kabisa, kwani ukiungana nao, hata kama
hutafanya wanachokifanya wao, lakini ubaya wao unaweza kukuleta matatizo kwani
ukikaa na muuza uturi, utanukia uturi....
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment