Mtoto wa marehemu alionekana
mtu mwema, na alikuwa tayari kuniambia mengi ambayo huenda yangelifanikisha
malengo yangu, ya kutaka kujua ni kitu gani kinachoendelea, kitu gani
kilichoweza kumbadilisha mume kiasi hicho,lakini yeye akatoa ombi , kabla
hajasema yale mambo muhimu ninayoyataka;
‘Nataka umsikilize
mume wako..mkubaliane naye..mkisha kubaliana naye , mkawa kitu kimoja,basi sisi
tutajitoa kabisa kwenye huo mkataba ulioandaliwa, mkataba huo ulionyesha kuwa
baba ana hisa kwenye kampuni zako, ...’ Nilijiuliza huyu mtu kawekeza lini
kwenye kampuni yangu.
Nikaendelea
kumsikiliza huyu jamaa, akisema;
‘Pia baba ana zaidi ya
nusu ya hisa kwenye kampuni ya mume wako, ina maana yenye ndiye mwenye usemi
kwenye kampuni hiyo...’ hili lilinifanya nimuone mume wangu hana maana,
utakubali vipi kumpa mtu mamlaka kwenye kampuni yako mwenyewe, kuna tatizo
gani, kampuni inajiendesha haina amdni, iweje umpe mtu hivi hivi, hapo nikahisi
kuna tatizo.
‘Yule jamaa aliendelea
kuesema kuwa, yeye kachelewa kuondoka kwasababu ya kuhakikisha kuwa maagizo
aliyoyaacha baba yake yanatekelezwa,
inaonekana baba yake alishajua yupo kwenye hatari, na ndio maana aliacah hu
usia.
‘Wao kama familia
walisema hawataki kujihusisha na mambo aliyokuwa akiyafanya bba yao, na hata
yale aliyoyaacha kwao waliyaona ni machafu, sio halali,...ila wanachotaka wao ,
baba yao mdogo, kama walivyomtambua, yaani mume wangu, asije akapata taabu
kutokana na hayo yaliyotokea nyuma,kwani kwao ni mtu aliyewatendea wema, na wao
ni nafasi kwako kulipa fadhila, wakisisitiza kuwa, wema wake aliowatendea kwao
ni mkubwa sana...’
Mimi niliposikia
hivyo, nikahisi kuna kitu kimejificha hapo, au kuna jambo linapikwa, na
nisipokuwa makini, ninaweza kukubali matakwa yao, nikajikuta kwenye matatizo
mengine, lakini hata hivyo, sikuwa tayari kukubaliana na ombo lao kama
walivyotaka, ila nilitaka kupata mengo zaidi, ambayo huenda yakafichua hayo
yaliyojificha, ndio nikamuomba huyo jamaa amlete mama yake niongee naye..
Nikamwambia;
‘Naweza kuonana na
mama yako.....?’
Endelea na kisa chetu.......
‘Unataka kuongea na mama, nashukuru sana, kama unataka
kuongea naye, kwani hata yeye alikuwa na hamu sana ya kuonana na wewe, ...’akasema.
‘Na yeye alikuwa na haja gani na mimi?’ nikamuuliza
‘Pamoja na hayo yaliyotokea, yeye alishasikia sifa zako, za
uchapa kazi, na kwa vile yeye ni mjasiriamali, alikuwa na hamu akuone, ajifunze
mengi kutoka kwako...’akasema.
‘Kwani mama yako huko kijijini anafanya nini?’ nikamuuliza
‘Amejiajiri, ana miradi yake, ni mmoja wa viongozi wa akina
mama, na tunataka awekeze hapa Dar, lakini hiyo ni mipango ya baadaye...’akasema.
‘Mnataka kufanya hivyo kwa urithi wa baba yenu, maana
nasikia ana nyumba zaidi ya tano, .....?’nikauliza.
‘Nyumba zote tumepiga mnada, kwa ajili ya kulipa watu,
waliopata madhara kutokana na mambo yake, ...hutaki chochote kutoka kwake,ila
tulitaka kulisafisha jina lake ili mungu amsamehe, na hilo tumajitahidi kwa
kuhakikisha kile alichokichuma, ndicho kinachofuta madhambi yake...’akasema.
‘Mnaonekana hamtaki ubaya wa baba yenu uwangilie na nyie?’
nikauliza
‘Ndivyo tunavyotaka, lakini watu wengine wanaonekana
kutokutuamini, hata hivyo, hata kama hawatatuamini sisi tutafanya yale
tunayoona ni sahihi, tukimaliza hayo, basi wale wenye nia njema na sisi
watatuamini....’akasema
‘Mimi sina ubaya na nyie, kama kweli mna nia hiyo njema, ila
sitaki mtu kuniingilia kwenye mambo yangu, ....baba yenu alianza hivyo,
akajitahidi, na nilimkanay sana, bado hakuchoka, akatafuta mbinu mpaka akaweza
kuingia kwenye mambo yangu hata bila ya mimi kufahamu..’nikamwambia.
‘Kwahiyo, ili kweli niwaone kuwa hampo nyuma yake, na hamna
nia njema, nawataka kwanza, nipate mkataba wangu, ambao yeye aliubadili....’nikasema
na yeye akanikatiza na kusema;
‘Sisi hatujui lolote kuhusu mkataba wenu, sisi mkataba
tulioupata ambao hata wakili wetu anaufanyia akzi ndio huo, unaoonyesha kuwepo kwa hisa za baba kwenye kampuni zenu,
na ndio maana kwanza tulitaka kulithibitisha hilo, na mume wako, amethibitisha
hilo...ila alisema kuwa hiyo ya umiliki wa hisa zaidi ya nusu, ya hisa, hakuwa
na hiari, ..ilikuwa kama shinikizo kwake, alikubali tu ili mambo yaishe..’akasema.
‘Aliwaambia ni kutokana na shinikizo gani?’ nikamuuliza
‘Hakutaka kusema ni shinikizo gani, lakini kwa vile
tunamfahamu baba, kuwa akiwa anatafuta kitu, hasa mali, hajali aliyepo mbele
yake, hatukutegemea kuwa watafikia hatua ya kushinikizana kiasi hicho, kwani haiingii
akilini, mume wako akubali kumpa nusu ya hisa baba..ni lazima kuna kitu kipo
nyuma yake...’akasema.
‘Wewe hukugundua ni kitu gani?’ nikamuuliza.
‘Naona niliyotaka kukuambia kwa sasa yanatosha, na kwa vile
unataka kuongea na mama, ngoja nikamuite, muongee naye, nitamsubiria kwenye
gari...’akasema
‘Ina maana mumekuja naye!?’ nikamuuliza kwa mshangao.
‘Tulikuwa naye, alikuwa na mambo yake, nikamwambia napitia
kwako kwanza kujaribu kama utakubali kuongea na mimi, ...yupo nje kwenye
gari....’akasema
‘Sawa nitafurahi nikiongea naye, na samahani sana, kwa
kutokukubali ombi lenu mapema, unafahamu hali halisi, mambo yametokea mengi
kiasi kwamba huwezi kumwamini mtu tena...’nikasema.
‘Hamna shaka, ..nimefurahi sana kuongea na wewe nah ii iwe
ni mwanzo tu wa mazunguzmo yetu, na nina imani tutashirikiana kulimaliza hili
jambo..’akasema na kusimama, tukashikana mkono, na akaondoka na kuniacha nikiwa
nimesimama nikimwangalia anavyoondoka.
**********
Mke wa marehemu alikuwa wale akina mama wahangaikaji, wake
wa shoka, hata jinsi alivyokuwa akitembea kuja pale nilipokaa alionekana ,mama
mchapakazi,...hajibaragui, au kutembea kimikogo, anatembea kama mwanajeshi,
alifika pale niliposimama, kwanza akaniangalia kama ananikagua, halafu
akanisogelea tukakumbatiana, na kusalimiana.
‘Siamini kama ni wewe..’akasema
‘Kwa vipi dada...?’ nikamuuliza
‘Unafahamu, nimeziona picha zako kwenye magazeti tu, kwenye majirida
mbali mbali, ..lakini unavyoonekana kwenye picha, sio sawa na nilivyokuona leo,
ukiwa katika hali yako halisi...’akasema
‘Kwani leo nipo vipi na huko kwenye magazeti naonekana vipi?’
nikamuuliza.
‘Tuyaache hayo, maana sisi akina mama tukikutana mengi tutakayoanza
kuzungumzia,ni mavazi, muonekano , sura,
hata tutasahau jambo muhimu, na majukumu ya kila siku, mimi siku hizi sitaki
kupoteza muda tena, na tangu nije hapa Dar, naona napoteza muda wangu bure...’akasema
huku akikaa kwenye kiti.
‘Haya niambie kulikonI, mna matatizo gani na mume wako?’
akakimbilia kuniuliza hilo swali.
‘Kwanza nikupe pole za msiba wa mumeo, japokuwa siku ile
nilifika kukupa pole,lakini hatukuweza kuongea vizuri, nahisi bado kulikuwa na
hisia kuwa huenda mimi ndiye niliyemuua mume wako..’nikasema.
‘Ni kweli kibinadamu,ni lazima iwe hivyo, japokuwa mimi na
mume wangu tulikuwa mbali sana, lakini ni mume wangu,sikuwezi kumkataa,
japokuwa yeye, kwa kauli yake, alishanifanya kama sio mke wake....na huoni sasa
naitwa mjane, maana nilikuwa mke wake, akubali asikubali.. ..sina budi
kulikubali hilo, na yote ni mapenzi ya mungu..’akasema akionyesha huzuni.
‘Je wewe ulikuwa ukimpenda mume wako?’ nikamuuliza.
‘Sana tu...huwezi amini, mimi nilikuwa nampenda sana mume
wangu, na nikuambie ukweli, mimi ndiye niliyemtaka mume wangu..awe mpenzi
wangu, japokuwa ndoa ilikuwa kama ay kulazimishana...’akasema na kunifanya
niingiwe na hamu ya kuyafahamu maisha yao.
‘Hebu niambie ina maana wewe ndiye uliyemtongoza mume wako? ‘nikamuuliza
kiutani
‘Haswaa, mimi ndiye niliyemtongoza mume wangu, sio kwamba
alikuwa hanipendi, kihivyo, hapana, kipindi hicho tulikuwa kwenye ushindani wa
kumpata yeye, ..tulikuwa wanawake watatu,,kila mmoja anataka yeye ndiye ampate
huyo mwanaume, kipindi hicho yeye ni kijana, sisi ni mabinti wadogo sana,...ilikuwa
hapatoshi, lakini mwisho wa siku nikasimama mimi kidedea, ..tukawa wapenzi,
japokuwa upenzi wa kijijini ulikuja kulete matatizo tu...’akasema.
‘Hongera, ...’nikasema
‘Unafahamu, mimi tangu nikiwa mtoto, nililelewa kwa shida,
sikuwahi kupata raha, ...wazazi wangu hawakunidekeza, hawakuwa na kitu, kwahiyo
ilikuwa ni maisha ya suluba, ..kula na kulala kwa shida, ..unajua maisha tena
ya kijijini..basi ikatokea nikamfahamu mume wangu, kiajabu ajabu tu,yeye
alikuwa msomi, na tena msoni kweli, ....kila mara humuoni hivi hivi, anakitabu,
ana karatasi, anaandika..’akasema huku akitabsamu.
‘Yeye nakumbuka tangu nimfahamu, alikuwa ni mtu wa kusoma vitabu
tu...hata alipokimbilia mjini, na baaadaye akawa anafika fika, alikuwa muda
mwingi ukimuona kashikilia kitabu, hivi
vitabu vya hadithi, alikuwa anapenda sana kusoma vitabu vya kizungu, nakumbuka
kuna vitabu vyake, aliwahi kunionyesha, hata mimi baadaye nilipojiendeleza
nimekuwa nikivisoma, hivi vinaitwa, eeh, Jemsi Hadley Chase, na Peri
Masoni,
nahisi ndio maana akajikita kwenye uanasheria...’akasema.
‘Siku ya kwanza kukutana kwetu, ilikuwa kama vile
wanavyoonyesha kwenye sinema, maana ilikuwa ni kwenye shughuli, mimi nilikuwa
kasichana, na bahati mbaya mwili wangu ulikuwa haraka, ni baadhi ya wasichana
kijijini kwetu tuliokuwa kimwili haraka, ...ilikuwa siku hiyo nafanya usafi
kuwaandalia wageni, mara wakati nawapelekea watu maji ya kunywa, nikagongana
naye, ..akadondosha kitabu chake, kikalowana maji...maana kulikuwa na maji maji
sakafuni, mimi nikakiokota na kukifuta kwa kitambaa change cha kichwani.
Nilipomaliza nikamkabidhi kitabu chake, kumbe mwenzangu
wakati wote huo nahangaika kukifuta kile kitabu, alikuwa akinitizama, na hata
namkabidhi hicho kitabu, bado alikuwa akinitizama tu machoni....hapo bado
mbichi nasoma...urafiki ukaanza, ooh, sijui ilikuwaje, nikabebeshwa
mimba,....balaa likazuka...siunajua tena enzi hizo...nikafukuzwa nyumbani...’akasema.
‘Nilikwenda kuishi kwa bibi, mpaka nikajifungua...hebu
fikiria, darasa la sita enzi hizo, unabebeshwa mimba,hata darasa la saba
sikumaliza, ingawaje baadaye nikijisomesha, usinione hivi , nilijisomesha hadi
sekondari, kiaina aina.
‘Basi aliponipa mimba, wazazi wangu wakafahamu, palikuwa
hapatoshi jamaa huyo akakimbilia mjini,....’akasema
‘Lakini umesema wewe ndiye uliyemtongoza, naona hapo
inaonyesha yeye alikupenda pendo la awali,...au sio, lile pendo watu mnaonana
hapo hapo, kunajengeka hisia za kupenda...’nikasema.
‘Baada ya pale, siunajau tena mambo ya shule, nikawahadithia
wenzangu, basi, marafiki zangu kila mmoja akataka amjue, na walipomfahamu ikawa
ndio kila mmoja anajinadi kuwa huyo ni rafiki yake, mimi ikaniuma sana, ina
maana kuwaelezea wenzangu ndio imekuwa nongwa..basi nikaona nisilaze damu, ...’akasema.
‘Nilipoona wenzangu wanambana sana huyo kijana, kila mara
wapo naye, nikaamua kumwambia ukweli, ilikuwa ni kazi nzito, lakini mwisho wa
siku alikubali kuwa hata yeye ananipenda sana tangu siku ile kwenye shughuli,
basi...mambo yakaanzia hapo, ikawa mimi na yeye, nikawa nachapwa nyumbani kwa
ajili yake, sikusikia,...haniambii mtu...na asiyesikia la mkuu huvunjika mguu...ikatokea
kama mchezo tu, ...’akatulia.
‘Pamoja na urafiki wetu huo, hatukuwa na mambo ya kisasa,
haya ya kimjini mjini, hapana...ilikuwa ni kukaa pamoja kuongea, kutaniana,
kukimbizana,...ila siku hiyo sikumbuki ni kitu gani kilitokea, na tukajikuta tumefanya
jambo ambalo ndilo lilimleta huyu mtoto wangu duniani....’akatulia kidogo.
‘Nilitenda hilo mara moja, na ikawa nio tiketi ya shida, ...shida
kweli...na nikuambie ukweli, mtoto huyo niliteseka kwenye mimba yake, nikamlea
kwa shida sana, huwezi amini. Siwezi hata kukusimulia, ....na mungu hakunitupa,
pamoja na kumlea kwa shida, sikupenda awe mtoto wa ovyo ovyo, nilijitahidi
kumlea kihali niliyoona ni njema kwake..’akasema.
‘Ina maana ulipomzaa huyo mtoto, hukupata msaada kutoka kwa
mume wako?’ nikamuuliza.
‘Msaada gani, angelipata wapi pesa za kunisaidia wakati yeye
mwenyewe alikuwa kula kulala..hana mbele wala nyuma, na aliponipa mimba
akakimbilia mjini kujificha, hakuonekana, hadi nilipojifungua na alifika kwa
mara ya kwanza mtoto anatembea,hamjui ,.....na sikutaka hata kuongea naye..’akasema.
‘Ikawaje sasa mpaka mkafunga ndoa?’ nikamuuliza
‘Wazazi wangu waliweka shinikizo..kuwa ni lazima
anioe...huoni , hata nikiwa naye naonekana mimi ni mkubwa kuliko yeye, lakini
ni kwasababu ya maisha, na mwanamke mara nyingi anaonekana mkubwa, kama mkiwa
umri sawa..sisi wanawake tunakuwa haraka haraka, na ukizaa ndio basi tena...’akasema.
‘Basi ikabidi kweli anioe, japokuwa hakutaka, alishaniona
sifai tena..japokuwa mimi nilikuwa nampenda kweli kweli,...hata tulipoona
hatukuwa sawa, ilionekana kama ndoa ya lazima, akawa ananinyanyasa, ...yaani
sikuwa na raha na yeye, na hakutaka hata kutembea na mimi, yaani tutembee kama
mke na mume, haikuwahi kutokea....aliniona simfai, mwanamke wa kijijini,
mshamba, asiyejua kujiremba...na yeye
keshakulia mjini, anawafahamu warembo wa mjini, eeh..’akasema akibenua mdomo
kwa dharau.
‘Basi bwana, ..mimi nikawa mama wa kijijini, sikujali, bado
nilimtambua yeye kama mume wangu, yeye akawa anishi mjini , mimi kijijini,
sikujali, nikawa napigika kijijini, maisha ya shida, ..hanitumii pesa, akibahatisha
ni mara moja kwa miezi mitatu, ni pesa yenyewe pesa basi, nikawa nahangaika
kivyangu kumlea mwanangu, sikujali na wala sikukata tamaa, na wala sikuwahi
kumsaliti mume wangu...’akasema.
‘Nikawa naletewa taarifa za ajabu ajabu kutoka huko mjini,
kuwa mume wangu ana wanawake, sio mwanamke, ana wanawake, anawabadili kama
nguo...ikafika mahali nikamuuliza, na kumshitaki kwa wazee, nilivyosikia,
hutaamini kibao kiligeukia kwangu, kuwa nasikiliza majungu, ni wapi nilimuona
na hawo wanawake,...iliniuma sana, kwani mmoja wa wanawake zake, namfahamu,
alikuja kuniambia yeye mwenyewe, kuwa mimi nitabakia hukukijijini yeye atakuwa
akistarehe na mume wangu mjini...’akasema.
Mwanzoni nilipata shida sana, na ikafikia hatua nikaamua
kumwenda huko mjini, ili nikapate huo ushahidi wanaoutaka wazee, najuta kwanini
nilifanya hivyo, maana nilizalilika,....sitasahau, kwani siku hiyo nikiwa
nimevalia zile nguo zetu, kwetu kijijini niliziona za maana , gauni
refu...mikono mirefu, kitambaa kichwani,...nikaingia dar, ilikuwa ni mara ya
tatu, nilishawahi kufika kabla.
‘Nilikuwa nafahamu wapi mume wangu huyo anaishi, nikafika
bila hata ya yeye kufahamu, ilikuwa saa kumi kumi hivi, nikafika nyumbani
kwake, ...kulikuwa na mvua mvua inaanza kunyesha, nikafike eneo alikopanga
chumba, alikuwa na chumba kimoja, maisha muda huo hayajamnyookea,nikagonga
mlango , mara akatokea mwanamke na khanga moja kiunoni, akafungua mlango, huku
akisema kwa nyodo.
‘Hivi nani hawa wanaharibuu starehe za wenzao, ni Malaya gani
wewe...’akasema huku akinifungulia mlango, na kuniona mimi, akashikwa na
butwaa, maana ananifahamu, alikuwa mmoja wa mabinti ninaowafahamu kutoka huko
huko kijijini,, binti huyo alikuwa mdogo sana kwangu .
‘Ni wewe....?’ akauliza kwanza kwa aibu lakini baadaye
akabadilika na kugeuka kuangalia ndani, na kusema kwa sauti iliyojaa dharau;
‘Haya wewe bwana, kuna mgeni wako nje..’akasema na kuingia
ndani, na mimi nikaingia na kumkuta mume wangu akiwa na kichupi, kakaa kwenye
sofa, akageuka na kuniona, hakuonyesha ile dalili ya kushituka akasema;
‘Wewe mwanamke ni nani kakuambia uje bila taarifa, bila ya
kibali changu, nataka nikiinuka hapa haupo ..rudi huko ulipotoka..’akasema huku
haniangalii machoni...’
‘Mume wangu niende wapi, ..wakati nimekuja kwako, ..nitapata
wapi basi muda kama huu?’ nikamuuliza
‘Utajua mwenyewe....kwani ni nani alikuambia uje,
nilishakuambia kuwa sikutaki...unang’ang’ania tu kuwa wewe ni mke wangu, hebu
jiangalie, hivi wewe ni shepu ya kuwa mke wangu, ...huoni aibu, eti kusema
`mume wangu’, sikiliza rudi huko huko ulipotoka,unasikia...’akasema na
kusimama, bila kujali kuwa kavaa kichupi tu, akanisukumia nje, huku yule
mwanamke wake, akiniangalia kwa nyodo kashikilia kiuno...sikuona taabu,
nikatoka nje..nilikaa pale nje, kibarazani hadi walipomaliza mambo yao, ...’akasema
huku akitabasamu tu.
‘Ina maana hawakujali, na bado walikuwa wakiendelea na
starehe zao?’ nikamuuliza.
‘Yaani tena kwa karaha, maana walijua nipo hapo nje, na mvua
inanyesha..lakini kila kilichokuwa kikifanyiak ndani, nilikuwa nakisikia, kwa
dharau..ili kunionyesha kuwa mimi sina maana..’nililowana, maana kibaraza
kilikuwa hakina sehemu nzuri ya kujificha, na walipomaliza starehe zako,
wakatoka wakaenda bafuni kuoga, wakavalia, wakaondoka, sijui walipokwenda,
nikabakia hapo nje,sijui niende wapi.
‘Bahati nzuri jirani yao, akanikaribisha ndani, akanipa nguo
nikabadili, akanipikia tukala, japokuwa chakula hakishuki, huyo huyo
akanisaidia nauli, kesho yake asubuhi nikaondoka nikarudi nilikotoka,...hebu
ona huo unyama, hata nauli hakunipa...nimesaidiwa na majirani ambao waliniambia
mume wangu kila siku anakuja ni mke mwingine...na sijui kwa vipi hakupata
ukimwi...’akasema huku akikunja uso.
‘Niliporudi kijijini, nikamsimulia mama yangu hayo
nailiyoyaona, akasema, hayo ndio yo niliyoyataka, waliniambia sikusikia, ni
kweli , walinisema sana, kipindi hicho, wakanichapa, lakini sikuwasikia, na niliona
kweli ni dhambi zangu ndizo zinaniandama ngoja nipatilizwe, ...
‘Niliishi kijijini kwa shida, hadi nilipokutana na huyo mume
wako....’akasema
‘Mlikutana na mume wangu eeh?’ nikauliza
‘Ndio mume wako, namuona kama mdogo kwangu, lakini alinionea
huruma sana, kwani alikuwa akiniona ninavyoteseka, yeye alikuwa akihangaika na
shughuli zake anapita kwetu ananiachia chochote,, huwa alikuwa akiniita
shemeji....basi ndivyo tulivyozoeana. Hakuwahi kupita hapo bila kuniacha kitu.
‘Kuna kipindi niliumwa sana...karibu ya kufa, hatukuwa na
hata senti nyumbani, sina pesa ya kununua dawa, kwani nikwenda hospitalini na
kuandikiwa dawa za kununua, ...hatuna pesa, na tatizo hilo lilikuwa kubwa, hadi
nikaambiwa nikafanyiwe upasuaji, ..nipelekwe mjini, hakuna pesa , na mume wangu
alipoambiwa hakujali..alitaka nife tu...’akatulia.
‘Namshukuru sana mume wako, nafahamu kipindi hicho, alikuwa hajaku-oa...kama
sikosei, akauza mbuzi wake, akapata pesa, na kuzileta nyumbani, hatukuamini,
akasema amekuja kunisaidia ili nikatibiwe...na kweli nikapelekwa mjini
nikafanyiwa upasuaji, nikatibiwa nikapona..sitamsahau mume wako...’akasema.
‘Je alifanya hivyo kwa sababu gani hasa?’ nikamuuliza
‘Yeye, alisema alifanya hivyo, kwa vile mume wangu ni rafiki
yake ,mume wangu alikuwa akimfundisha
fundisha ufundi wa magari, ..udereva,..unafahamu mambo ya kijijini, basi
wakaivana, sijui zaidi ya hapo ilitokeaje wakaivana kiasi hicho, kwahiyo yeye
alinitambua kama shemeji , mke wa rafiki yake, akanijali kihivyo.....na ujirani
mwema tu...’akasema.
‘Kwahiyo kwetu sisi , kama familia, tunamthamini sana mume
wako, ni mtu mwema sana, na alipenda kuwasaidia sana watu,..sio mimi tu, ..yeye
alikuwa na tabia yake ya kupenda kusaidia watu, japokuwa familia yao ina tabia
ambayo wengi wanaiona sio nzuri, baba yale ni mlevi kupindukia, na mama yake
akawa hivyo hivyo....basi ni familia ya shida, lakini yeye akawa anajibidisha
na maisha yake, kuhangaika kivyake..hadi hapo mlipokutana naye...’akasema.
‘Mhh, kweli umenifungua masikio, hayo yaliyokukuta ni
makubwa, mimi niliona nipo kwenye mitihani, lakini wewe ilikuwa zaidi, sasa
ikawaje?’ nikamuuliza.
....NB: Ikawaje kwa mama huyu, tutaona sehemu ijayo, ili
tujifunze kutoka kwa mama huyu, je ilikuwaje mapaka akaweza kuishi maisha ya
kujitegemea, je yeye na mume wake, walikuja kuafikiana baada ya yote hayo?
WAZO LA LEO: Maisha yana mitihani yake, ukiona kwako ni
kugumu, ujue kuwa kuna wenzako kwao ni kugumu mara mbili yako, ukipatwa na
mitihani ka hiyo...usikate tamaa, pambana, ukijua kuwa wewe sio wa kwanza
kupata mitihani kama hiyo, wapo waliopata mitihani hiyo na wakaishinda, kwanini
wewe usiweze...kumbuka baada ya dhiki, mara nyingi ni faraja.
Ni mimi:
emu-three
3 comments :
kazi nzuri ndugu yangu ..kumbuka tupo pamoja ila tu majukumu mengiiii,,Nimependa wazo la leo....mno.
Jirani mimi nilipita kuomba maji ya kunywa tuu na kuacha zangu salaamu, maana ni kitambo kweli.Jumamosi yako na iwe njema jirani yangu wa ukweli.
Nakushukuru sana ndugu wangu,@Yasinta Tupo pamoja, na jirani yangu, kweli ni muda kweli, hatujatembeleana, lakini yote maisha, tupo pamoja.
Post a Comment