Nilizindukana na kujikuta nipo hospitalini, na pembeni yangu
alikuwa kakaa mume wangu, huku kajiinamia, nikajaribu kuinuka, lakini nikahisi
maumivu ya kichwa, nikashikilia kichwa, na mume wangu akanisogelea na kujaribu
kunisaidia, nikainuka na kukaa vizuri,
‘Pole sana mke wangu unajisikiaje...’akasema kwa
unyenyekevu.
‘Kumetokea nini?’ nikauliza
‘Inaonekana kuna watu walitaka kukuumiza huko jela...’akasema
‘Kuniumiza kwasababu gani, nimewafanyia nini kibaya, na hawo
watu ni akina nani?’ nikawa nauliza maswali kwa mfululizo.
‘Hayo maswali kwasasa hayana msingi, cha muhimu ni kuwa upo
salama, na hilo limesaidia kupatikana kwa dhamana yako haraka, kwani kuna watu
walishaiwekea pingamizi...’akasema.
‘Oh, kumbe....’nikasema huku nikishika kichwa, sehemu ambayo
nilifungwa bandejii na mume wangu akaniangalia kwa mashaka na kuuliza
‘Kwani unajisikiaje?’ akaniuliza huku akiweka mkono sehemu
ile iliyowekwa bandeji na mimi nikawa najihami asije akanitonesha, na akaondoa
mkono wake, na kuniangalia machoni.
‘Maumivu ya kichwa kwa mbali, lakini sio sana, haya niambie
na wewe unaendeleaje, maana mgonjwa anamuuguza mgonjwa...?’ nikamuuliza
‘Mimi kwasasa sijambo, sina wasiwasi kabisa, nipo tayari
kupambana na yaliyopo mbele yangu, ...’akasema huku akijiweka vyema, kama vile
anajiandaa kuongea.
‘Una maana gani kusema kuwa unajiandaa na kupambana na
yaliyopo mbele yako, ...?’ nikamuuliza
‘Dunia hii ilivyo, maisha yetu wanadamu yalivyo, kila siku
ni mapambano, au sio, huwezi kulala tu, ukafanikiwa, ni lazima upambane, na
mimi nimejifunza jambo ..’akatulia kidogo, nikawa na wasiwasi nisije
nikamkwaza, nikaona nibadili maongezi, nikasema , kama kuuliza.
‘Hivi huyu wakili wangu yupo wapi...maana nataka kujua mambo
yanaendeleaje...’ nikawa kama nauliza huku nikitafuta simu yangu, sikujua ipo
wapi.
‘Wameondoka muda mfupi uliopita, watarudi, kuna mambo
wanafuatulia....unatafuta simu yako, nahisi ipo kwenye mkoba wako, nikuletee?’akaniuliza
huku akiinuka na kuchukua mkoba wangu uliokuwa umewekwa kwenye meza, sijui ni
nani alinichukulia, sikutaka hata kuuliza. Akanipa simu yangu, nikaiwasha kwani
ilikuwa imezimika, nikawa nimeishikilia mkononi.
‘Oh, hamna shida, ..hivi leo tarehe ngapi, ...’nikasema huku
nikiangalia simu, akaniambia tarehe na saa, nikasema;
‘Ahsante sana mume wangu,..nikamtaaj jina lake, na yeye
akatabasau na kusema
‘Ahsante mke wangu, na kunitaja jina langu...’nikatabasamu,
halafu nikasema;
‘Kama dhamana imepatikana basi iliyobakia ni kuangalia kesi
hiyo itakwenda vipi, na huyo muuaji ajulikane ni nani, ili niwe huru....’nikasema
na kutulia, nikamwangalia mume wangu, nilimuona kabadilika, kakonda, na
inaonyesha kuwa ana mawazo sana, nikawa naogopa kumuuliza maswali, lakini yeye
akaanza kuongea;
‘Mke wangu, kuuwawa kwa Makabrasha kumenishitua sana,sikutegemea
kabisa, ni kama namuona , yaani jana tu mtu mlikuwa naye, leo hayupo,
keshatoweka duniani, hatutamuona tena, hii inaonyesha kuwa sisi wanadamu si chochote...na
wengine wanajiona wana nguvu wana kila kitu wanaweza kufanya wapendavyo, kuua
kwako ni rahisi tu, kama wao hawatakufa’akasema.
‘Ni kweli, ndio maana umri wetu mdogo tuliopewa tunatakiwa
kuutumie vyema, ukikosea na kuutumia vibaya, unaweza hata usipate muda wa
kujitetea, utarudi kwa udongo, na siku ya mwisho unaamukia kwenye hukumu ya
mungu...’nikasema.
‘Ni kweli,..hilo nimeliona na nimekuwa nikiliwazia sana, ...’akasema
‘Unawaza nini cha zaidi?’ nikamuuliza huku nikimwangalia
usoni.
‘Hasa haya yaliyotokea kwetu, yananipa shida kweli kweli,
ndio maana hata nilipokuwa hospitalini, nilikuwa nikihangaika kuweka mambo
sawa, na nikitafuta njia ya kuyasawazisha, lakini mwili ulikuwa haukubali,..nilikuwa
kwenye mtihani mkubwa sana...lakini sasa naona kila kitu kipo sahihi , ni swala
tu la kukubaliana...’akasema.
‘Mhh, usijali, hayo yatakwisha, na maisha yataendelea, cha
muhimu ni kama ulivyosema, kukubaliana, na kingine cha muhimu, ni kuwa kuna
makosa yamefanyika, na kama yapo, mkosaji anahitajika kukubali kosa na kulikiri
kosa lake...ili tujua jinsi gani ya kuliweka sawa, kama kuna mengine, ...basi
tutakaa na kuyajadili, ..ila mimi ninachotaka, na ni muhimu sana kuambiwa ukweli...’nikasema.
‘Unataka kuambiwa ukweli, ukweli upi tena,..mmh, sawa hilo
halina shida, ila ukweli mara nyingi unauma....’akasema
‘Mhh, kwanini ukweli uume, ..labda kama una mashaka,
...lakini kama una nia thabiti,ya kujua na kukubali kwa nia njema sizani kama
utaumiza,...tatizo ni kuwa watu wengi hawataki kusema ukweli, wakichelea
yatakayotokea baada ya ukweli . Lakini ni vyema tukajifunza kuwa wakweli, bila
hivyo , hatutafika,...’nikasema nikimwangalia, na yeye akawa akiangalia
pembeni, nikamuuliza
‘Vipi hali yako kwa ujumla, umepona vyema, maana tusije
kuongea hapa likazuka jingine,..?’ nikamuuliza.
‘Mimi nimepona, nilifuata masharti yao,kama walivyotaka,
japokuwa ilikuwa kazi nzito, maana nilikuwa kama mfungwa, lakini kiukweli ilinisaidia
sana, na waliponipima kwa mara ya mwisho waliniambia nimepona kabisa, walisema kila
kitu kipo safi, hakuna matatizo tena, usiwe na wasiwasi na mimi mke wangu....’akasema.
‘Kwahiyo upo tayari kusema yote yaliyotokea, , ....?’nikamuuliza.
‘Hilo ndilo nataka tuliongelee, lakini wewe unaumwa,
tusubiri, kwanza, japokuwa nilikuwa na mambo muhimu, ya kujadili, na wewe...ni
kweli kuna mengi yametokea, na kuna yetu wenyewe, na kuna ambayo nilisaidiwa na
marehemu kidogo, kiushauri, ....hayo nayo yana nafasi yake, japokuwa yapo
kwenye maandishi,....’akatulia kidogo.
‘Yapi hayo yaliyopo kwenye maandishi?’ nikamuuliza
‘Ninaongea kuhusu mkataba...’akasema
‘Unaongea kuhusu mkataba upi, maana mkataba wetu wa hiari
umetoweka, na sasa upo mkataba wa kugushi, wewe hapa unazungumzia mkataba upi?’
nikauliza.
‘Mkataba wa kugushi!?’ akawa kama anauliza na kushangaa.
‘Kwani hujui, na wakati wewe na Makabrsaha ndio mliofanya
hayo!’nikamwambia huku nikimwangalia nikiwa na mashaka nisija nikazua balaa,
lakini sikuona mabadiliko,, yeye kwanza akainamisha kichwa chini, na baadaye
akasema;
‘Mke wangu nakupenda sana, ..na nisingeliweza kukubali
tuachane...mimi kama mume wako niliona ni heri nifanye jambo, kuilinda ndoa
yetu, ... nilifahamu fika kama mkataba ule ungelifika kwa wazazi wako, basi
mimi na wewe ingelikuwa ndio mwisho wetu ...wangeliuchukua ule kama kigezo, cha
kuvunja ndoa yetu, kutokana na hayo yaliyotokea, ...nikaona nifaye yaliyo
sahihi kama mume, ..nikamuona mwansheria, yeye akasema hilo kwake ni kazi ndogo
tu...’akaanza kuongea.
‘Kwahiyo kumbe wewe ndiye uliyeonana na marehemu ukamwambia
wazo hilo, kuwa mgushi mkataab wetu, na mtengeneze mambi yenu mtakavyo,na yeye
akakubali na kulifanyia kazi?’ nikamuuliza
‘Mke wangu kuna mengi yametokea kabla ya hilo, hilo lilikuwa
ni kama hitimisho la mambo mengi yaliyokuwa yamejificha, huenda hata mimi
sikuwa na mawazo hayo kabla,...sipendi kumuongelea vibaya marehemu, ..kwa vile
hayupo na hakuna wa kumtetea, lakini yule alikuwa rafiki yangu mkubwa sana, na
mengi alikuwa kanishauri kabla, na sikuwa na mtilia maanani, na ilipotokea
tatizo, nikaanza kumkumbuka yeye....’akatulia
‘Tatizo gani lililotokea hadi kukimbilia kwake?’
nikamuuliza.
‘Hilo nitakuja kukuambia kwa wakati muafaka,....’akasema
‘Kwahiyo sasa hivi unataka tuongelee nini?’ nikamuuliza
‘Kuna mambo kidogo, tunahitajika kukubaliana...tuyaongee,
ili ukibali, na tukakubaliana basi kinachofuata ni utekelezaji tu...’akasema,
na mimi kwa vile sikujua anataka
kuongelea jambo gani, nikasema;
‘Mhh, kama upo tayari kuyaongea hayo uliyoyaoanga kuyaongea
sasa hivi, mimi nakusikiliza...’nikasema
‘Nipo tayari, labda wewe mgonjwa, kama haupo tayari,
tusubiri, ..kwani muda upo, na mimi nimeahidi kuwa nitakuambia kila kitu, ..ila
kwa masharti kwamba, tuyaongee kwanza wawili, na tukubaliana wawili, kama
hakuna tatizo, basi,tusiwahusishe wengine, ...kwani hapa yalipofikia nahisi
haya mambo yanatupeleka pabaya, kama imefikia sehemu ya kuuana, ..mimi naanza
kuogopa...’akasema.
‘Unaposema ku-uana, una maana gani,?’ nikamuuliza
‘Kwanini Makabrasha ameuwawa,..?’ akaniuliza
‘Mimi sijui, ....na nimejikuta katikati ya mambo haya, na
hata kushutumiwa kuwa mimi ndiye niliyemuua, wakati sijui kabisa mambo haya, na
ninaona mambo mengi yanatokea bila hata kujua ni kwanini, siambiwi ukweli,...inanipa
mashaka sana ...na inafikia mahali nashindwa haat kuwaamini watu, hasa marafiki
wangu wa akribu, naona kama wananizunguka....’nikasema.
‘Kwahiyo kama huwaamini, hata wakikuambia ukweli, nahisi hutaweza
kuwasamehe, ....?’ akaniuliza.
‘Ukweli ndio utaoamua,...maana sijaambiwa ukweli, ...’nikasema.
‘Mimi ni mume wako, niakuambai ukweli...’akasema.
‘Ni bora fanye hivyo, maana nilishaahidi kuutafuta ukweli
mwenyewe, na kama ikifikia hapo, nikautafuta mwenyewe, huo ukweli nikaugundua ,
nikaona una nia mbaya na mimi, sitavumilia tena...’nikasema.
‘Ni kweli,...inahitajika kufikia hapo, na mimi nimeliona
hilo, kuwa kinachotakiwa hapa ni ukweli, mimi sina wasiwasi na hilo maana
nimeshajiandaa kwa upande wangu, mwanzoni nilikuwa naogopa sana, lakini
sasa,...hata kama nitauwawa, ..kuna nini kimebakia, kama mtu aliyekuwa
akijiamini kupita kiasi kauwawa, sembese mimi...’akasema.
‘Kwahiyo wewe unataka kusema nini?’ nikamuuliza.
‘Mimi nakusikiliza wewe kwanza...’akasema kwa kujiamini.
‘Sikiliza mume wangu, usije ukajidanganya na huo mkataba wa
kugushi, ukajiona kuwa upo salama, huo mkataba wa kugushi, ni ukiukwaji wa
sheria, na hilo tunaweza kulithibistiha
kisheria, kuwa huo mkataab wa sasa ni wa kugushi...hata kama kila mbinu
zimetumika, kuubadili, lakini kila kosa lina udhaifu wake, ..’nikasema.
‘Hakuna kosa kwenye huo mkataba wetu, na sijui kwanini
unauita wa kugushi...’akasema.
‘Huo mkataba mpya mimi siukubali, maana
sikushirikishwa,..kwanza ni mkataba wa nani na nani, ...nasema hivi na unielewa
kuwa mimi sitakubaliana na ujinga huo, nahitaji ule mkataba wa mwanzo kwanza,
na kama una marekebisho ni juu yangu mimi na wewe kuyafanyia kazi, na sio mtu
mwingine...’nikasema.
‘Na mimi narudia tena kukuambia mke wangu, mimi sijui kama
kuna mkataba uliogushiwa, upi huo uliogushiwa....!’akasema.
‘Mume wangu acha hayo maneno...kwa kauli yako ulisema uliona
kuwa kuna vipengele ambavyo vingebakia wakaona wazazi wetu, ndoa ingelivunjika,
je hivyo vipengele vipo au havipo...na sasa unakuaj na kauli nyingine, ambayo
nahisi inanionyesha kuwa kweli una malengo yasiyofaa, ambayo mimi
sitayakubali....’nikasema.
‘Mke wangu, mimi sijui mambo ya kugushi mkataba,...mimi sio
mwanasheria, nitagushi vipi kataba, na mkataba huandikwa na wanasheria, mimi ninachofahamu
ni kuwa upo mkataba wetu wa hiari, na huo ndio utakaoweka mambo yetu bayana,...’akasema.
‘Una uhakika na hayo unayoyasema?’ nikamuuliza na yey e
kwanza akaniangalia, halafu akaangalia chini na kusema;
‘Mke wangu, kwanini niswe na uhakika na hilo, nimeshakuambia
kuwa mimi nakupenda sana, na hayo yaliyofanyika, yalifanyika kwa nia njema tu,
ya kulinda ndoa yetu, na nakuhakikishia
kuwa mkataba wetu upo, na una ammbo mazuri tu, ya kuwezesha mimi na wewe
tuendelee kuishi kwa amani na upendo , na mimi nitakuwa mume mwenye mamlaka kama
mwanaume, sio mwanaume jina...’akasema
‘Una maana gani kusema hivyo?’ nikamuuliza.
‘Mkataba ndio unasema hivyo...kuwa mimi kama mume nitakuwa
na mamlaka ya uongozi wa familia, nitaweza kupitisha maamuzi, kama ninaona ni
sahihi kwa masilahi ya familia....wewe utakuwa msaidizi wangu, na hiyo ndio
kawaida,..mume unakuwa na nguvu ya kuongea, kwa vile una mamlaka, kwani hapo kuna makosa...’akasema.
‘Haya unayoyaongea yapo kwenye huo mkataba, na yalipitishwa
na kukubaliawa na nani?’ nikamuuliza
‘Mimi na wewe..na wakili wetu..’akasema.
‘Tatizo lako, Makabrasha alikuingiza kwenye anga zake za
ulaghai, na umesahau kuwa wewe sio mwanasheria, huyo mtetezi wako hayupo tena
duniani, kuna mambo ya kisheria huyafahamu,...na hayo yatakupeleka
pabaya,...mkataba uliokubalika kisheria
ni ule tuliokaa mimi na wewe tukakubalina sio huo uliokaa wewe na mwanasheria
wako, ....’nikasema.
‘Ndio huo huo, hakuna mkataba mwingine...kila kitu kipo
sawa, kuna sahihi yako, kuna sahihi ya mwanasheria...’akasema.
‘Mwanasheria gani?’ nikamuuliza.
‘Mwanasheria wetu wa familia, ..ngoja nikuonyeshe mkataba
wetu..hakuna kitu kilichobadilika, ni mambo madogo madogo tu ulikuwa huyajui,
....na yote ni kwa masilahi yetu...’akasema huku akiutoa huo mkataba, na
mlangoni, niliona mtu kasimama kwa nje, nahisi alikuwa akisikiliza tunachoongea,
sikuweza kumtambua ni nani,...nikataka kumpa ishara mume wangu, lakini hakuwa
makini na yeye akawa ananionyesha sehemu zile za sahihi akasema;
‘Huu ndio mkataba wetu,..unaona hii hapa ni sahihi yangu,
hii ni ya kwako, hii ni sahihi ya mwanasheria wetu wa familia,...hakuna
kilichobadilika, ...unaonaeeh...’akasema huku akifungua fungua huo mkataba, na
mimi nikamwangalia kwa makini na kusema;
‘Mume wangu usitake tufikishane huko..huko unapokwenda ni
kubaya, usikubali hayo mambo aliyokudanganya Makabrasha, ..huyo jamaa
anajulikana sana kwa hadaa an ulaghai, hata watu wana usalama wanalitambua hilo..sasa
na wewe usiwe mshirika wake, tunachotakiwa kwasasa ni kusahihisha yale makosa
yaliyotokea, ili tuanze pale tulipoishia, ...tusilazimishe migogoro isiyo na
msingi, na tusitake kulazimisha chuki na uhasama, wakati kuna njia nzuri ya
haki, yenye kuleta mariziano na maafikiano,...hebu nikuulize hivi wewe unachotaka
hasa ni nini?’ nikamuuliza mwishoni.
‘Nakupenda sana mke wangu , sitaki mimi na wewe tuachane...’akasema
‘Ni nani kasema hatutapendana na tunataka kuachana?’
nikamuuliza.
‘Hayo yaliyotokea yangeliweza kufanya tuka....kosana, huoni
ilishaanza fitina, na tulikuwa tunakwenda kubaya, nilikuwa sina kauli, ni kama
mume bwege,...na hayo yalitokana na vipengele visivyo na msingi kwenye mkataba
wetu, nilikuwa naogopa kuwa vipo, kumba hakuna,kumbe kuna mambo mazuri tu,
....ndio maana sasa najiamini, napigania upendo wangu kwako, na pigania ndoa
yangu....’akasema.
‘Unapigania ndoa yako au unapigania mali?’ nikamuuliza na
hapo akashituka na kuniangalia machoni.
‘Mke wangu nimesema kuwa nakupenda sana....sipiganii mali, kwanza
kwanini niipiganie mali wakati ipo , mali
ninayo,....huwezi kupigania kitu chako, eti mke wangu, mbona sikuelewi...’akasema.
Hapo akaanza kunichefua, nikaona mwenzangu kadhamiria kweli,
na ile subira ya kumuonea huruma kuwa ni mgonjwa, ikaniishia, nikaona sasa
nipambane na mtu ambaye hataki kuelewa, nikasema ;
‘Kwahiyo umedhamiria hayo mliyokuwa mumepanga na marehemu?’
nikamuuliza
‘Sijapanga kitu na marehemu, yeye alinishauri tu kama
mwanasheria wangu, alipitia mkataba wetu, akausoma, na kuniambia upo safi
kabisa, akanionyesha hivyo vipengele muhimu kuwa nisiogope maana mimi kama mume
nina mamlaka ya kufanya yale ninayoona ni sahihi kwa masilahi ya familia...’akasema.
‘Kwahiyo ndio ukafanya ulivyoona kuwa ni sahihi,..hata kama
mimi sijaurizia, ?’ nikamuuliza
‘Nimefuata mkataba unavyosema, ...sijakiuka kitu, kama
ilitokea kwa bahati mbaya, basi Katina inanipa nafasi ya kujirudi, ndio maana
nipo haap mbele yako kukuomba msamaha kwa hayo yaliyotokea, ili tusonge
mbele..katiba inasema hivyo, sisi kama wana ndoa wakati mwingine tunakosea kama
wanadamu, kosa likishagundulika, na sote tukalikubali ni kosa, basi mkosaji
anatakiwa kutubu, na kuomba msamaha, na sote tunakubaliana na kushikana mkono,
ndio ndoa ilivyo ...’akasema
‘Basi nashukuru, nakuomba uondoke, nataka kupumzika, naona
hatutaelewana kwa sasa....’nikasema
‘Lakini mke wangu kuna mambo nataka tuyaongee, ...kuna mtu
anasubiri, maamuzi yangu mimi na wewe’akasema
Nani anasubiri hayo maamuzi yangu mimi na wewe, na hapa
tulikuwa tunaongea tu, hakuna maamuzi yoyote yamepita hapa, ..hatujakubaliana
lolote hapa.mimi siutambui huko mkataba wenu, .’nikasema.
‘Mtoto wa marehemu, anahitajia maamuzi yetu, ...’akasema
‘Nimeshakuambia hakuna maamuzi yoyote yaliyopitishwa hapa,
kama una lako jambo endelea kivyako, na kama umezamiria hayo uliyokusudia, basi
tutapambana,sheria ipo, haki ipo ..maana nakuona hutaki kunielewa, tukakubaliana,
na nakuasa,uwe makini, usihadaike na tamaa za watu wengine, kumbuka
ulipotoka,...kumbuka kuwa ndoa hujengwa na mume na mke, na wengine wote ni
wapambe tu, ...ukiwafuta wapambe, mkafarakana wanandoa, hawo hawo wapembe,
waliokuhadaa, watakuja kukucheka.
‘Nimekuelewa mke wangu...usijali, mimi kama mume wako
sitakubali hilo litokee...’akasema huku akiinuka kuondoka, nilishangaa sana, ni
kitu gani kimempata mume wangu awe hivyo..kabadilika, kawa sio yule mume
ninayemfahamu...
‘Umenielewa vipi?’ nikamuuliza kabala hajatoka
‘Umesema niondoke,unataka kupumzika, au?’ akaniuliza huku
akigeuka kuniangalia.
‘Sawa ...tukikutana tena nataka uwe umejiandaa, ...kusema
ukweli, wa kwako, na sio wa shinikizo, nataka ule mkataba wa awali uwepo, ili
tulinganisha na huo mkataba wenu mpya,
vinginevyo hatutaelewana...’nikasema.
‘Hamna shida mke wangu, ...mimi nipo, tutaongea tu, na
tutayamaliza bila wasiwasi, mimi ni mume wako, na nina haki zote kisheria, na
nafanya hayo kama tulivyoainisha kwenye mkataba wetu..’akasema kwa kujiamini.
Na mara mlango ukafunguliwa,kwa nje, niliona watu wawili, na
mmoja, anafanana sana na marehemu nahisi ndio mtoto wake, alikuwa akitaka
kuingia ndani, na mume wangu akawa anamzuia,nikasikia wakisema;
‘Huyu ndiye yule wakili wangu niliyekuambia, atachukua
nafasi ya baba...
‘Tutaongea huko mbele,...’akasema mume wangu mlango
ukafungwa, na mimi nikampigia simu wakili wangu, nikijua sasa ni mapambano,
hakuna kulala.
‘Sikiliza hayo ndiyo mazungumzo yangu na mume wangu...’nikasema
nikiiweka simu hewani
NB: Doa la tamaa limeshagusa mtima, ibilisi hachezi mbali
hapo,...je itakuwaje, Kwa leo inatosha.
WAZO LA LEO:
Maisha ya kiujanja ujanja, dhuluma ,kugushi, hayana amani,...kwa vyovyote
utakavyofanya ili kufanikisha dhuluma, ili kupata kipato kisicho halali, ili
kuhalalisha uwongo wako, ujue hilo ni deni kwako, na aina hiyo ya
maisha,inaondoa baraka, inaondoa amani, na upendo. Hata kama utafanikiiwa na
kupata hiyo dhuluma na hata kuwa tajiri, lakini utajiri wako utakuwa hauna
heri, hauna amani hauna baraka, na mwisho wake ni dhiki, kujuta na kuzalilika.
Wangapi wangapi walifanya hivyo, na sasa
hawapo dunia tena, tukumbuke dunia hii ni mapito tu, chuma
chumo la halali, ili maisha ayko yawe na amani, baraka na furaha..
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment