Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, December 11, 2017

MKUKI KWA NGURUWE-38



 ‘Ndio …nataka niwahi uwanja wa ndege…najua sasa hivi hakutakuwa na foleni, anaondoka saa tatu na mimi ni lazima nionane naye, sasa hivi saa ngapi…’nikasema

‘Kufuata nini huko, ina maana hujanielewa nilichokuambia..?’ akauliza akiniangalia kwa uso uliotahayari.

‘Pamoja na yote uliyoniambia, ni lazima nihakiki baadhi ya habari, kwanza sina uhakika kuhusu rafiki yangu, kiubinadamu natakiwa nifanye jambo, kwa vile kaniambia yupo matatani…..je kama ni kweli, unafikiri mimi nitaelewekaje, ni lazima nifanye jambo au sio..?’nikasema

‘Una watu wako watume, na foleni zilivyo huwezi kufika huko kwa wakati, utakuwa unapoteza muda wako bure, na hata hivyo, kiusalama sio vyema, unanielewa hapo…?’ akasema kana ananiuliza

‘Hili sio tatizo lako,  mimi ni vyanzo vyangu vya habari, naondoka, …japokuwa hujanimalizia kuhusu hiyo kashafa ni ipi hasa ambayo hata baba yangu anaogopa itamuharibia sifa yake..,?’ nikauliza

‘Sikiliza,…ok, muda umekwisha, lakini kitu muhimu ni kuwa kila jambo linatumiwa kama silaha, sisi tutatumia hilo tukio kama silaha yetu, ni mambo ya kuwhiana, atakaye muwahi mwenzake atashinda, na …., kama wameamua kuwachukua watu wako wa karibu kama watu wao, tunaweza kuwatumia hao hao kama njia ya kufanikisha mambo yetu…’akasema

‘Sitakuelewa…saa ngapi…?’ nikauliza

‘Ngoja nikuulize kitu…’akasema

‘Uliza nataka kuondoka..najua unapoteza muda, ili nisiweze kufanya kazi yangu..’nikasema

‘Ni kweli, lengo moja wapo ni hilo, licha ya kuwa , nilitakiwa kukuelezea hayo niliyokuelezea, lakini pia kukutoa mbali na hatari iliyopangwa kutokea kwako, ukibisha hilo, ukifika nyumbani kwako muulize mlinzi wako, kulitokea nini..nani alikuja nyumbani, utaambiwa,…’akasema

‘Unataka kusema nini, uliza mimi nataka kuondoka..?’ nikauliza

‘Ni hivi kuhusu huyo wakili , unajua pamoja na kusomea uwakili jamaa huyo kasomea taaluma za nyota…kumsoma mtu, na kosomea nje, watu wanajiuliza ni kwanini alisomea mambo hayo…’akasema

‘Hayo ni ya kweli jamani au mnataka kumpakazia kila ubaya…?’ nikauliza

‘Hata vyeti anavyo, ndio maana nakuambia huyo mtu sio kama unavyomfikiria wewe, kuwa unaweza kumshinda kirahisi, kasomea taaluma nyingi mojawapo nyingine ni uaskari kanzu, na watu wengine wanamuhis kuwa ni usalama wa taifa, lakini sio kweli…’akasema

‘Umejuaje kuwa sio kweli..?’ nikauliza

‘Siwezi kukuambia hilo, lakini kiukweli hayupo huko,…’akasema akiangalia saa yake na mara kuna ujumbe uliingia kwenye simu yake akausoma, halafu akaniangalia.

‘Sawa nafahamu, sasa kitu kinachowashangaza wengi, ni jinis gani anavyoweza kuwalaghai watu, wakamuamini, na kumpa kazi, jinsi anavyoweza kumuingiza mtu katika anga zake, na mwisho wa siku mtu huyo analizwa, na bado jamaa huyu hapatikani na makosa.....’akasema.

‘Ni utapeli tu, mimi sizani kama anashindikana kukamatika kama kweli ana makosa…’nikasema

‘Mimi nilipoona huyo jamaa kaingia kwa mume wako,....ikabid nianze kumfahamu vyema kwa  haraka nilikimbilia kwa jamaa yangu mmoja, ofisa upelelezi, na nikamuelezea hayo niliyoyaona na hisia zangu....’akasema, hapo nikamkatisha na kusema;

‘Kwahiyo ulikwenda kunielezea matatizo yangu polisi bila kuniambia..?’ nikamuuliza

‘Sio kuelezea mambo yako, nia ni kupata ushahidi na taarifa za huyu jamaa, na ni kwanini hawajaweza kumchukulia hatua huyu mtu…’akasema

‘Najua hayo yote unayafanya kwa kivuli cha wazazi wangu, kweli si kweli…?’ nikauliza

‘Na kwa taarifa yako wazazi wako, walishakuacha, hawataki kuingilia mambo yako tena, wakijua wewe sio mtoto tena, unaweza kujimudu, walikupima wakaona unaweza kujimudu, ila kwa hili hawawezi kukuacha,ni kweli wazazi wako waliniomba mimi niwe nakusaidia saidia, kuhakikisha hupotoki, na kukuonya kuhusu maadui zako , lakini bado walikuwa na mashaka na mume wako,..na ndio maana nalifanya hili…’akasema

‘Nashukuru..’nikasema sasa nikawa nasimama kutaka kuondoka

‘Kwahiyo unataka kwenda nyumbani sio……’akasema

‘Ndio…’nikasema kumdanganya, lakini akilini mwangu nilikuwa sijawa na uhakika.

‘Jana niliitwa na baba yako, akanielezea mambo mengi waliyoyagundua, ..mengi tu ambayo hata wewe huyafahamu…wamesema wao wanasubiria kuona ni nini wewe utakifanya baada ya hili tukio, ambao limefunikwa na mambo ambayo yanaonekana kuwa ndivyo lakini sivyo…’akasema

‘Wazazi wako wanazidi kusisitiza kuwa hawataki kashfa, hilo alilolifanya mume wako ni nzito…halivumiliki, lakini je wewe utachukua hatua gani..wamekupa nafasi ya kukupima, kuona ukomavu wako katika mambo haya ya biashara..’akasema, na ilionekana alikuwa akinipotezea muda tu.

‘Kwahiyo kuniita kwako kote na kuzunguka kwako kote kuhusu wakili na maelezo yake kumbe mwisho wake ni kuwa wewe umetumwa na wazazi wangu kunionya au sio, japokuwa awali ulikataa hilo, sasa umekubali mwenyewe, sawa nimekuelewa..?’ nikauliza na kusema.

‘Ina maana hayo niliyokuelezea hayana maana…wewe subiria uone huo ushahidi, utakuja kugundua kuwa huyo wakili sio mtu wa mchezo, usiamue kupamba naye wewe mwenyewe, huko nyuma, alikuachia tu, kwa vile muda ulikuwa haujafika, usifikiri ulimshinda, kama ulivyoona, unajua kuwa alipanga kukushitaki kwa kumuharibia jina lake…’akasema

‘Sawa nashukuru kwa hiyo taaarifa, kwanini hakufanya hivyo basi kama kweli ndivyo alivyo, …’nikasema kama kuuliza

‘Nilipoongea na mpelelezi, alisema, hakuendelea kufungua mashitaka baada ya kuombwa asifanye hivyo na watu wake wa karibu, inaonekana ni sehemu ya mikakati yao, kujionyesha kuwa wao sio watu wa ugomvi...’akasema

‘Sawa… mimi naondoka…’sasa nikawa nachukua mkoba wangu

‘Wao bado wanamfuatilia, wanasubiria muda muafaka, maana ana watu wake wakubwa wanamlinda, lakini watu hao na wao hawana muda, wameshamulikwa, na awali hii ya utawala haina mchezo, wewe utakuja kusikia tu…’akasema.

‘Hilo la kusema kuwa eti ana mtu mkubwa anamlinda siliafiki, ....hamsini zake hazijafika, na kama kaingilia anga zangu tena, mimi sitajali huyo mtu wake, sizani kama kuna mtu ana uwezo juu ya sheria, sitaki kukuambia mengi, lakini ngoja nione nitakachokifanya, najua mnanidharau, lakini ngoje muone....’nikasema kwa kujiamini.

‘Wote wanasema hivyo, hata huyo mpelelezi anasema hivyo hivyo, lakini tujue kuwa hata huyo jamaa mwenyewe anajua hilo, na ndio maana anakuwa makini kwa kila analolifanya, huyo jamaa alivyo mjanja, hajipeleki kwa mtu ovyo ovyo, mambo yake ni kimiya kimiya, taratibu, kama tai anavyomvizia adui yake. 

‘Ukiona anafanya kazi fulani ujue, keshapitia kila njia, na huwezi kumuona akijipeleka ovyo ovyo tu, ... mara nyingi wateja wake, ndio wanamuita....na kila anayemuita, anahakikisha anafuata taratibu zinazokubalika kisheria, ..yupo makini sana kwa hilo...’akasema.

‘Umakini gani wa kufoji mikataba ya watu, kuibadili, na kuiba nyaraka kwenye maofisi ya watu...’nikasema

‘Unasema nini, kaiba nyaraka,...una uhakika na hilo…usikurupuke….usije ukalisema hilo kwake,…huna ushahidi, au unao….liache kama lilivyo…’akasema

 ‘Sina uhakika wa moja kwa moja na hilo, ..lakini kwa mtizamo wa haraka haraka, atakuwa ndio yeye tu, na sitalala mpaka nihakikishe nimemuweka ndani, na kama analindwa, basi mimi nitajua jinsi gani ya kumfanya mlinz wake asalimu amri...’nikasema.

‘Kuwa makini na kauli zako, kauli zako zinaweza kukufunga...na usije ukatamka maneno kama hayo kwake,...nilikuona ulivyokuwa ukiongea naye pale hospitalini, na kwa vile nilikuwa sijamjua, sikuweza kuingilia mazungumzo yenu, lakini kauli kama zile,...usizitamke tena kwa huyo jamaa,..tamka kitu kama una ushahidi nacho...yeye anajihami, na kwenye ule mkoba wake, ana vifaa vya kurekodi, mazungumzo’akasema

‘Kwani nimesema nini kibaya hapa...ndivyo ilivyo..’nikasema

‘Mimi ninachokushauri ni kuwa ujue unapambana na watu walio makini kisheria,wao wanasubiria kosa dogo, wanakunasa,  huyo mtu tuachie sisi, tumeshamfuatilia, na tunajua jinsi gani ya kumnasa, kwasasa hivi wewe hangaika na afya ya  mume wako tu na ujifanye hujui lolote, timiza wajibu wako, ili kusitokee sababu...’akasema.

‘Nitahangaika vipi na mume wangu, wakati huyo jamaa keshasema ni wakili wake, halafu wanaponiacha hoi, na pale anaposema kuwa, hata mimi siwezi kuongea na mume wangu mambo muhimu, yenye mlengo wa kisheria, mpaka huyo jamaa awepo, hapo, ina maana gani, ni kuwa mume wangu na mimi sasa ni kama watu wawili tofauti...’nikasema.

‘Ndio maana ya ule utangulizi wangu wa mwanzo, sasa hivi mume wako anaanza kuyaonyesha makucha yake, maana anahisi kile alichokuwa akikitaka kwako, kitapotea....na akirudi mitaani, ataadhirika, ...sasa afanye nini, ndio maana kaamua kujiunga na rafiki yake huyo....sina nia mbaya na rafiki yangu huyo, lakini ndivyo ilivyo, ....mimi nakujali wewe zaidi....’akasema.

‘Nimeshakuambia kuwa mimi sihitaji msaada wa yoyote yule, usijiingize kwenye maswala yangu, ukafikiria kuwa nitakuunga mkono, sitaki kuja kumbebesha mtu lawama, niachieni hayo ni mambo yangu, msije mkaanza kusema, `ooh, tulikuambia....’nikasema.

‘Usilichukulie hili swala juu juu, ...wewe unaliona kama ni swala dogo, lakini ujue hata watu mashuhuri wameshindwa kumkamata huyu mtu, unafikiri wao ni wajinga, ya kuwa hawana njia ya kumnasa, wanasubiria muda muafaka, na utafika hivi karibuni,.....’akasema.

‘Sawa tutaona...hao watu waliopo juu ya sheria..’nikasema.

‘Kama nilivyokuambia hawa watu ni wajanja sana, wameliweka hilo jambo lionekane hivyo linavyoonekana, wameanzia mbali sana,...lilianza kuonekana ni swala la mapenzi, …lakini kuna kitu kiliwashinda, ni huo mkataba wenu..’akasema

‘Mkataba wangu uliwashinda nini, wakati wameugushi..’nikasema

‘Ndio, hilo linafanyiwa kazi, usijali, kila jambo ni silaha kwetu, kama ilivyo kwao, tukinasa ushahidi, hapo jamaa hatoki, ..kaharibu meza yake mwenyewe, lakini hilo hakulifanya yeye, hutaamini hilo…’akasema

‘Nani kafanya sasa..?’ nikauliza

‘Yeye mkataba uliofika mezani kwake ndio huo wa kugushi, huo wa awali hajawahi kuuona, …mtu aliyefanikisha kugushi huo mkataba ni mtu mbali kabisa na yeye, na huyo mtu kwa hivi sasa hayupo hapa nchini, alishaondoka,…sio mzaliwa wa hapa, karudi kwao…’akasema


‘Ok, nimekuelewa, sasa unataka mimi nifanye nini?’ nikamuuliza.

‘Kunielewa haitoshi, muhimu ni kukubali tulifanye hili jambo kwa pamoja bila ya kujionyesha kwa watu kuwa mimi na wewe tuna shikirikiana , na pia na muhimu sana, usimwamini mtu yoyote kwa hivi sasa, hata hao watu wako, na huyo rafiki yako kuanzia sasa achana naye...hilo ni muhimu sana...’akasema

‘Nafahamu sana, kuanzia sasa simuamini mtu tena, sina rafiki tena, kama wapo sitawaamini tena,.....’nikasema.

‘Unaweza kusema hivyo, ila kwa hili, mtu pekee unayetakiwa kumwamini, kwa sasa ni mimi,...upende usipende ...mwenyewe utaona...’akasema.

‘Sifanyi makosa hayo tena…’nikasema

‘Sasa sikiliza, wakati tupo hospitalini, huyo wakili wa mume wako, alionekana akiongea na rafiki yako nje ya jengo,..unalifahamu hilo,...?’ akaniuliza.

‘Rafiki yangu, huyu huyu anayesafiri…?’ nikauliza

‘Huyo huyo ..ndio maana nakuambia uwe makini…’akasema

‘Mhh…kwahiyo hilo la kuwa mtoto wake katekwa na nini..ni hadithi ya kutungwa..’nikasema

‘Hilo bado tunalifanyia kazi, siwezi kukujibu kwa sasa, ila jiulize alikuja kuweka sahihi ya mikataba gani , na tumefuatilia, ndio kweli visa yake na mikataba yake ya kusoma huko nje ilikuwa na kasoro, akahisi ni wewe umefanya hivyo, ndio maana akaamua kutafuta mdhamini mpya, kwahiyo kuja kwake hapa imechukuliwa hivyo..’akasema

‘Ina maana unalifahamu hilo..?’ nikauliza

‘Ndio maana nakuambia utulie, mimi nina vyanzo vyangu, vitakusaidia, na kama unataka tuwe timu moja utaona jinsi gani tutaliharibu hili kundi, sasa ni hivi, kilichofanyika ni mbinu, ili ionekane hivyo, na kuna watu wamecheza na udhamini wake, na sasa wamemuweka mtu wao, unafahamu ni nani huyo….’akasema na kuuliza

‘Mimi sijui…’nikasema

‘Ni adui ya baba yako..yeye huwa anasomesha wanafunzi nje…au watu wasiojiweza, kwahiyo rafiki yako yupo kwenye orodha yao, na inasemakana kuna ajenda kuwa wewe ulimtelekeza ndio maana akatafuta mdhamini mwingine, hilo limefichwa…’akasema

‘Mhh..ina maana gani hiyo yote..?’ nikauliza

‘Sasa nikuambie kitu, huyo rafiki yako alipofika hapo hospitalini, hakuteremka kwenye gari,alifika na gari la kukodi,lisiloonyesha ndani, magari haya ya bei mbaya, jiulize kwanini alikodi gari hilo la bei mbaya…’akasema

‘Na alipofika hapo hospitalini, hakuteremka, alihakikisha kuwa hakuna mtu anayefahamu kuwa ni yeye, aliyekuja kuongea naye ni huyo wakili wa mume wako, na huyo wakili wa mume wako, …alijifanya anakwenda kwenye gari lake akasimama kama analikagua, huku anaongea na rafiki yako…’akasema

‘Walipomaliza kuongea, rafiki yako huyo akarudi ndani kuongea na mume wako, na rafiki yako akaondoka bila kuteremka kwenye gari, hebu jiuliza hapo kuna nini...na kwanini hakuenda kumuona mgonjwa moja kwa moja, wakati aliaga kuwa anakwenda kumuona mgonjwa.....!’akasema.

‘Vijana wangu wakamfuatilia, awali hawakufahamu kuwa ni yeye, si umafahamu rafiki yako alivyo, anaweza kujibadili usifahamu kabisa kuwa ni yeye, vijana wakataka kuhakiki

‘Hilo gari liliendeshwa hadi mjini, kwenye hoteli za kitalii, mdada akateremka kama kaja kutafuta chumba, akaingia ndani, na huko akaongea na watu wake, akabadili nguo, akatoka akiwa mtu mwingine kabisa, akachukua usafiri wa taksi za kawaida, uliompeleka hadi sehemu , na akateremka na kuingia kwenye daladala, iliyomfikisha hapo anapoishi, watu wangu walimfuatilia, na wakamgundua kuwa ni yeye....’akasema.

‘Mhh, nafahamu kuwa alifika hospitalini, aliniambia mwenyewe..’nikasema japokuwa sikuwa nina habari zote hizo.

‘Lazima angekuambia hivyo, ili kuficha ukweli zaidi,... sawa hakuna shida, ila ninachotaka kukuambia hapo ni kuwa huyo wakili, ana kitu kinachowaunganisha, rafiki yako na mume wako, kwahiyo wakili huyo anaongea na mume wako, halafu huyo wakili anapeleka taarifa kwa rafiki yako...mume wako na rafiki yako wameamua kuwa mbali mbali, na hawatakubalia lolote linalohusiana na wao wawili…’akasema.

**********
Kiukweli hapo niliona kuna mambo ambayo mimi sijaweza kuyapata na wenzangu wameshayapata, japokuwa kuna mambo mimi nayafahamu na nina uhakika wao hawayafahamu, lakini sikutaka kuongea nao lolote, akili ya kumuamini mtu ilishaanza kunitoka, …


‘Kwa vile hukuwahi kufika uwanja wa ndege, kuna watu walitumwa nyumbani kwako kufanya lolote, hatuna uhakika nia yao ni kufanya nini, maana hawakukuta,..tatizo lao, hawakulifikira hilo mapema....kiujumla, upo kwenye hatari, sasa ni wajibu wangu kufanya kila jitihada kukulinda…kwa hivi sasa njia ipo salama unaweza kwenda…’akasema

‘Je mna uhakika gani kuwa mume wangu ndiye aliyetembea na rafiki yangu,..?’ nikauliza

‘Hilo lisikutie shaka…ukweli upo wazi, ila kuna ajenda ya siri ambayo siwezi kukuambia kwa sasa…ninachokuomba ni wewe kuendelea kujifanye hivyo hivyo..unavyofanya, hujaamini kuwa tendo limefanyika hivyo watu wanavyosema, nia ni kuja kunasa jambo ambalo litakuwa ushahidi…kuna DNA, imetoka, lakin hatuna uhakika nayo bado,hawataki kuionyesha mpaka sasa…’akasema

‘DNA, ya huyo mtoto, mliwezaje kuipata, …niambie inasemaje…?’ nikauliza kwa hamasa

‘DNA, imefichwa, na kuna tetesi kua huenda hiyo DNA, inasema kuwa huyo mtoto, sio wa mume wako…’akasema

‘Mnasema, 'huenda, kwanini msiende kuulizia hapo ilipotolewa, kwani walipimia wapi.....mimi bado nina mashaka na hilo,...lakini .., mumeona sasa, na hakuna mtu anayeweza kugushi kitu kama hicho, kwahiyo ni kweli, sio mtoto wa mume wangu…’nikasema

‘Usijali, hilo linafanyiwa kazi…jiandae kwa lolote lile, na hata ikihakikiswa, wala usichukue maamuzii ya haraka maana mkataba huo mpya, utakufanya usifanye lolote, kuna maswali mengi bila majibu, kama ni hivyo, kuwa DNA kama yaonyesha kuwa, rafiki yako hajazaa na mume wako, hiyo mikataba ni ya nini, je labda alitarajia jambo sasa limekuwa kinyume chake, je hayo yanayoendelea ni kwa masilahi ya nani…’akasema

‘Hapo sijui…nahisi kuna jambo jingine sio kwa sababu ya huyo mtoto…’nikasema

‘Hizo ni silaha zetu zitatumika kwa wakati muafaka, wewe vuta subira, sasa unaweza kwenda, na nenda moja kwa moja nyumbani kwako, kupo salama, usije kwenda kinyuma na makubaliano yetu, sawa…’akasema, na kabla sijaondoka, akaniuliza swali

‘Hivi wewe unafahamu wapi Makabrasha anaishi?’ akaniuliza

‘Huyu mtu sijui anaishi wapi , ni mtu wa kuhama hama, na nijuavyo mimi ofisi yake ipo mikononi, popote ni ofisi yake,..wakati mwingi ukitaka kumpata, nenda ofisi za wanasheria, alikuwa anapenda sana kukaa hapo, lakini baadaye akawa anatumia hoteli, leo hii kesho ile,..kwa ujumla anahama hama, hana sehemu maalumu, ila ana nyumba kama tano hivi,, hutaamini hata mke wake, hayupo hapoa Dar...’nikasema.

‘Ndivyo unavyomfahamu hivyo, au sio…hahaha….’akasema na kucheka

‘Kwani sio kweli…?’ nikauliza kwa mshangao.

‘Huyu mtu anaishi maeneo ya uwanja wa ndege...kuna nyumba mpya ipo karibu na majumba sita, ina ghorofa hivi...inasadikiwa kuwa Makabrasha ana hisa nayo...ndipo ofisi zake zipo humo ndani,  …makazi yake ndio hayo ya kuhama hama, kwa vile ana nyumba nyingi, leo yupo hapa kesho yupo kwingine, anajihami kila mara…’akasema

‘Eti nini...unasema ofisi zake zipo uwanja wa ndege…una uhakika na hilo?’ nikauliza huku nikisimama

‘Sasa unataka kwenda wapi..?’ akaniuliza huku akinishangaa

‘Kuna kitu ….ina maana basi huyo rafiki yangu alikuwa kwa Makabrasha au sio...’nikasema

‘Ndio maana tukakuzuia usifike huko, haya yote yanafanyiwa kazi, kwa usalama wako...’akasema.

Nikakumbuka jinsi rafiki yangu huyo, alivyokuwa akiongea kwenye simu, na sauti yake ilikuwa sio ya usalama,kama vile anakwazwa kuongea kwa sauti, ilikuwa kama ya kunong’ona,simu ikakatika, kama vile kuna mtu alimnyang’anya...

Hapo akili yangu ikaniambia kuwa huenda rafiki yangu huyo ananificha jambo, au alikuwa hatarini, lakini hakuweza kuniambia, yote mawili yanawezekana, ..lakini kwa namna nyingine huenda rafiki yangu kaamua kunisaliti..sikutaka kumwambia lolote docta kuhusu mawazo yangu hayo mapya, nilitaka nikitoka hapo niwaulize watu wangu, ambao nilishawatuma huko.

‘Tutaongea siku nyingine naona muda umekwenda...’nikasema.

‘Umesikia nilipokuambia, uende moja kwa moja nyumbani kwako,, sawa tumeelewana hilo..’akasema

‘Sawa hamna shida...’nikasema

‘Haya ukijifanya mkaidi usije kunilaumu…’akasema akiangalia saa yake

‘Huyu rafiki yangu anajifanya mjanja,..kumbe walikuwa na huyu wakili wakati anaongea nami kwenye simu, na nina uhakika ndipo alikuwa muda wote huo.., ila sina uhakika maana aliniambia yupo kwa shangazi yake,..je hilo la kutekwa mtoto wake ni kweli, au alikuwa akinidanganya..? ’nikasema kumuuliza

‘Kuna kitu unatakiwa ukijue, huo mkataba aliolazimishwa rafiki yako kuweka sahihi ni wa nini, na  kwa masilahi ya nani, ndio ni kwa ajili ya mtoto, kama alivyodai, au kama alivyoambiwa, sasa ni kwa baba yupi…kwanini huo mkataba haujawekwa wazi mpaka sasa, ina maana unasubiria jambo fulani, unaona hapo…?’ akaniuliza

‘Hilo siwezi kujua, maana hata mimi sijauona huo mkataba, watu wangu wanafuatilia, lakini haujapatikana, labda haujatolewa bado na kufikishwa sehemu husika, lakini tutajua tu,…’nikasema na kuanza kuondoka

‘Sawa, ila nakuahidi mpaka kesho utakuwa umepatikana, mimi nimepanga kuonana na makabrasha nataka kuongea naye, tumakubaliana kesho, kwahiyo usiwe na haraka na hilo, sawa wewe …ukitoka hapa rudi nyumbani kwako….’akasema

‘Nimekuelewa, sawa..,’nikasema

Usiku ulikuwa umetanda, giza, na mihangaiko ya watu wakirejea makazini na wengine kwenda kwenye starehe, mimi sikuwajali hao..akili ilikuwa ina mengi ya kufanya, niliona nje barabarani kupo shwari nikaangalia saa…

'DNA, inasema huenda mtoto sio wa mume wako...kama sio mtoto wa mume wangu ni wa nani, basi atakuwa wa mdogo wa mume wangu...je ni kweli hili au ....hapana ni lazima nipate uhakika, kabla huyu mtu hajaondoka...na kama hivyo, basi rafiki yangu atakuwa kweli matatani...ni nani huyo yupo nyuma ya hili jambo...' nikawa nawaza sana, baadae nikaangalia saa.

Nikawapigia simu watu wangu na walichoniambia kikanifanya nizidi kuwa na hamasa:

‘Ni kweli madam, mtoto wa rafiki yako alichukuliwa na watu, na amekuwa akihangaika kumkomboa, …'wakaniambia

'Keshaingia uwnja wa ndege...?' nikauliza

'Bado, hajulikani wapi alipo mpaka sasa..tumejaribu kumtafuta hajaonekana, alitupotea wakati anahangaika kumalizana na hao watu waliokuwa na mtoto wake...'wakasema

'Je hamjasikia lolote kuhusu DNA, nasikia wamepima hicho kipimo..?' nikauliza

'Bado madamu, tutafuatilia tutakufahamisha, hilo ni jambo dogo tu...'wakasema

'Sawa endeleeni kumtafuta huyo mtu mjue kama keshaingia uwanja wa ndege au la...'nikasema

Nikaangalia saa yangu tena....

‘Huu muda naweza kuwahi, ninaweza kumuwahi rafiki yangu , ni lazima niongee naye, uso kwa uso, nijue ukweli. hiyo DNA, inasemaje,..ni lazima nilifahamu hilo kabla hajaondoka, ni lazima .…’nikasema hivyo.

Hapo hapo, nikageuza gari kulia...na sasa nikawa naendesha gari kuelekea uwanja wa ndege, akili ilishaamua hivyo, ni lazima nifike huko, ....

Nikakanyaga mafuta, huko moyoni najipa matumaini

'Nitawahi tu....'


WAZO LA LEO: Maisha ya ujanja ujanja, na kujiona una akili zaidi ya wengine, ukawa unafanya mambo ya dhuluma, na bahati ukawa unafanikiwa, sawa utafanikiwa leo…na ukajipa matumaini kuwa hakuna anayekuwea. Lakini nafsini hutaweza kuwa na amani. Dhuluma inamfanya mtu aishi kwa wasiwasi, hata kama atajificha vipi, au hata kama atakuwa na walinzi wa kimataifa. Tusisahau kuwa wanaodhulimiwa wapo wanamlilia mola wao, na ipo siku kilio chao kitajibiwa, kama sio leo, basi muda baadae kidogo.

Ni mimi: emu-three

No comments :