Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, December 6, 2017

MKUKI KWA NGURUWE-35


 Nilitembea kwa haraka kama nataka kufanya jambo ...hadi nafika kwa huyo jamaa sikujua nitafanya nini, ili akilini, nilitaka nifanye jambo...nikafika pale aliposimama huyo jamaa,...nilipomkaribia tu,nikasikia mume wangu akiita huku nyuma;

‘Mke wangu unataka kufanya nini…’akasema mume wangu, lakini mimi sikumjali tena, kwani sasa nilikuwa nimesimama kwa huyo jamaa tunaangaliana uso kwa uso.

 Tatizo yeye, alikuwa kavaa hayo mawani, mkwe usinione, nilitamani niitoe, nione anahisi nini, …lakini mkono ukawa mnzito kufanya hivyo, nilitamani, nifanye jambo, mkono unawasha, lakini mkono ukawa mnzito kuinuka,, lakini kwa haraka mkono wangu ukaenda kwenye mikono ya jamaa, nikamshika mkono na kumvuta tutoke nje, lakini hakusogea, nilipoona hivyo nikasema;

‘Naomba tutoke nje, kama wewe mwanaume kweli...'nikasema hivyo

'Mhh...' jamaa akaguna tu, na hakusogea

'Sikiliza wewe mtu, mim nataka  tukaongelee haya mambo nje, maana hapa sio mahali pazuri pa kuongea, tutavunja taratibu za hospitali, na pia eeh…tunaweza kuleta matatizo kwa mume wangu..’ nikamwambia, na yeye kwa haraka ajaibu kwa kusema;

‘Kwa leo mimi siwezi kuongea na wewe chochote, kwa maana  mimi nimekuja hapa kwa ajili ya kuongea na mume wako,...'akasema

'Nafahamu hilo, ...nimeona kuwa umekuja kwa ajili yake, lakini nataka kukuambia jambo la msingi sana....'nikasema

'Hapana, siwezi kufanya hivyo, kabla sijaongea na mume wako,...'akasema

'Unataka nitumie nguvu...'nikasema

'Hapana usifanye hivyo, kwani haitasaidia kitu...mume wako kanipigia simu anataka kuongea na mimi...kiukweli tulishaongea mambo fulani fulani,...sasa  nimekuja kuna mambo mawili matatu ya kumalizana...'akasema

'Ina maana hunielewi, kwani mimi ni nani kwa huyo mgonjwa

'Ni mume wako...'akasema

'Kwahiyo hayo unayotaka kuongea naye mimi hayanihusu...?' nikauliza

'Nitajua nikimalizana kuongea na yeye, natii alichoniomba mteja wangu...'akasema

'Mteja wako...?'! nikauliza

'Ndio....'akasema na muda huo yeye alikuwa akinijibu kwa sauti, kama vile anataka kila mtu asikie wakati mimi nilikuwa nikimuuliza kwa sauti ndogo

‘Mliongea nini na mume wangu, mpaka akuitie huku hospitalini..au  ni ule utapeli wako wa kurubuni watu, …bado unataka kumfanyia tena mume wangu, mimi..nitakuitia polisi sasa hivi…’nikasema

‘Kwanza nikuambie jambo, mimi sio tapeli..na kuja kwangu hapa sio kwa kujitakia, ni mume wako kaniita..na tuliyoongea mimi na yeye, hayawezi kusemwa mpaka nimalizane na yeye, kama anataka ndio nitakuelezea, kwanini inakuwa vigumu kuelewa….’akasema

‘Kwangu mimi siwezi kukuelewa, japokuwa nakuelewa ulivyo,..na hilo unalotaka kuongea na mume wangu lazima nilichuje kwanza, kwasababu mume wangu ni dhamana yangu, lolote likitokea nitaulizwa...'nikasema, nikimuangalia moja kwa moja usoni

‘Ni kweli,…lakini kwa hivi sasa hata mimi sijajua kikamilifu kaniitia nini, kwasababu kwenye simu hajaniamba, zaidi ya kusema nifike hapa hospitalini, ni muhimu sana, ..kwahiyo mpaka niongee naye ndio nitakuwa na uhakika huo,,..'akasema

‘Lakini mlishaongea jambo kabla, wewe na yeye…?’ nikauliza

‘Kifupi, Ndio...'akasema

'Mliongea nini...?' nikauliza

'Mambo mengi, yakiwemo ya afya yake, familia, kazini, na mikataba ...'akasema

'Mikataba gani....?' nikauliza

'Mimi naomba ukamuulize mume wako, maana yeye ndiye kaniita hapa, labda anataka nimfanyie kazi yake..’akasema

‘Kazi gani sasa…?’ nikamuuliza nikitarajia jibu hilo.

‘Oh, mimi nilijua nyie wawili mumeshaongea na kukubaliana, sasa kama hamjaongea kwanini ameniita,..basi huenda kaniita kwa jambo jingine, ndio maana naomba npate muda wa kuongea naye kwanza ili nijue ni kitu gani, tafadhali...’akasema.

‘Huwezi kuongea naye mpaka nijua ni jambo gani, ili niwe na usalama moyoni, je mkiongea jambo likamkwanza..tafadhali...’ nikasema.

‘Madamu,…siwezi kusema kitu, nitakuambia nini sasa, mimi sijui kaniitia nini, huenda ni maswala mengine,...tafadhali nielewe hapo, tutalumbana hapa bure na sitaweza kukuambia kitu…’akasema

‘Sasa naona unataka na mimi nifanye kazi yangu,… hebu sikiliza, huyu mume wangu anaumwa, na mara kadhaa amekuwa akipoteza fahamu kwasababu ya shinikizo la damu..na madocta wakashauri  tusiwe tunamshinikiza kwenye mambo ya kumfikirisha sana,…sasa wewe eeh,…, hivi nikuulize..kama tukiongea hapa nisipokubaliana na nyie,akashikwa na hasira akadondoka, ....huoni kuwa utajiweka kubaya...’nikasema.

‘Haiwezi kutokea hivyo madamu..nakuhakikishia hilo…halafu nikuambie kitu, mimi sijafika hapa kwa ugomvi na wewe kwanini tusielewane...eeh,..na ama kwa huyo mumeo yeye ni rafiki yangu toka siku nyingi, wewe tu ndiye uliyeingilia urafiki wetu, na kunipiga marufuku nisiwe naonana na yeye, sawa mimi nilitii...'akatulia

'Sasa umefuata nini tena, nilishakupiga marufuku...'nikasema

'Mumeo anaumwa, na nirafiki yangu, mimi ni binadamu, kuumwa ni kitu kingine, unanisikia sana..sitaweza kuwa na amani, bila kuja kumjuliahali..kwa hapo nilivunja agizo lako samahani sana..’akasema

‘Kwahiyo kumbe ulikuwa unakutana naye mara kwa mara au sio kwa kujifanya wewe ni mwema, au sio…’nikasema

‘Madamu ni wewe tu hunifahamu, mimi ni mtu mwema sana…sina ubaya na watu, mimi ni mtu wa watu hasa wale wanaotaka huduma zangu…na kwa huyo mume wako, yeye tumeshibana sana, lakini tunaheshimu tu maagizo yako…kiufupi, wewe usiwe na wasiwasi kabisa na mimi, ni wewe tu madamu....’akasema.

‘Tatizo ni hivi..kauli yako na nafsi yako ni vitu viwili tofauti, mimi nakufahamu sana wewe ulivyo, upo tayari kufanya kazi yoyote inayohusiana na taaluma yako kwa ajili y pesa bila kujali kuwa ni kinyume na maadili yako...pesa kwako wewe ni kila kitu....na kwahiyo siwezi kukuamini kwa lolote lile utakaloongea na mume wangu, la sivyo, liwe halinihusu mimi, unanisikia..’nikasema

‘Hamna shida, ni wewe madamu…’akasema

‘Ila nakuonya, kama utafanya jambo la kumweka mume wangu kubaya, ..kama kuna njama za kumrubuni mume wangu kwa minajili ya kuchuma pesa kwa kutumia mgongo wake..., mimi na wewe tutapambana, kwanza nikitoka hapa nakwenda kutoa taarifa polisi…’nikasema

‘Mimi hayo siyafahamu…nijuavyo mimi ni kuwa katika kumsaidia mume wako, nitakuwa nimechangia kwa kiasi kikubwa, kumaliza matatizo yake ya kiafya, hilo nina imani nalo, kwa kiasi kikubwa nitakuwa nimemaliza jambo linalomsumbua sana mume wako,…je huo nao ni utapeli,..’akasema

‘Wewe ni docta au mganga wa kienyeji...?' nikauliza

'Mimi ni wakili, wakili wa kujitegemea...'akasema

'Hivi wewe hukumbuki kuwa polisi bado wanakuchunguza kwa tabia yako hiyo ya utapeli,..au unataka kufanya nini tena, unafahamu bado kesi yako ipo polisi au nikawaite polisi waje wakuchukue?’ nikamuuliza.

‘Hahaha, madamu, tafadhali, ...mimi sio tapeli,....polisi, nilishamalizana nao, hakuna kesi yoyote dhidi yangu, kawaulize ...., na hilo la kuwaita, usiogope kufanya hivyo, kama unaona ni njia sahihi ya kumsaidia mume wako haya, karibu, lakini nakuhakikishia mimi nitaweza kumsaidia mume wako kwa kiasi kikubwa sana…’akasema akitikisa kichwa kidogo.

'Sitaki huo msaada wako, siku zote nahangaika naye, leo umeona kapata nafuu, unataka kumpandisha tena shinikio la damu, ngoja nikaongea na docta wakutoe humu ndani...'nikasema

‘Nikuambie kitu madamu, labda kwa taarifa tu, kipindi uliponishitakia, nilikwenda polisi, nikawaambia waniambie kosa langu ni nini, na kama nina kosa wanifikishe mahakamani, mbona hawajafanya hivyo hadi leo…, kwahiyo hili la kusingiziwa utapeli, achana nalo, halina nguvu kabisa, mimi najiamini, ninafanya kazi zangu kisheria, na wanaobisha twende mahakamani.....’akasema na kutulia.

‘Sawa safari hii hilo litafanyika, nakuahidi hivyo…’nikasema

'Sawa ...unasema unataka kumuita docta anitoe, sawa, muite tu..usijali madamu, kama itasaidi....'akasema na mimi hapo nikasita kidogo, nikageuka kule walipo mume wangu.

**********

  Baada ya kuongea na huyo mtu,  nikageuka kumwangalia mume wangu, nilimuona akituangalia tu, hakuonyesha dalili ya kuingilia maongezi yetu, alikuwa katulia, huku macho yake yakipepesa pepesa, kama vile anajisikia vibaya, hapo nikaona nisije nikaleta hali nyingine mbaya, nikageuka kumwangalia huyu mtu na kusema;
.
‘Mimi nimekuelezea niliyotaka kukuelezea na mimi nimenawa mikono, na naona hunielewi, sawa, mimi naona ni bora niondoke, ili kuepusha shari, maana mimi nina uchungu wa mume , wewe hutojali chochote kikitokea…’nikasema

‘Ni wasi wasi wako tu madamu…’akasema

‘Ndio lazima niwe na wasiwasi huo,…ngoja nikuachie huyo mtu uendelee kumdanganya na utapeli wako, lakini kwa masharti, kama kuna lolote litatokea,mume wangu akizidiwa, au kama kuna lolote baya, kati yako na yeye,....mimi  sitasubiria polisi, wala nani, nitahakikisha nikapasua kichwa chako kwa risasi...hilo ninakuahidi...’nikasema na yule mtu akabenua mdomo kwa dharau na kusema;

‘Mbona mimi sina neno madamu…, mbona hunielewi, kwanini hayo yote huongei na mume wako tu kukuthibitishia kuwa mimi sina maana yoyote mbaya, ni kwa masilahi ya mume wako, sio zaidi ya hilo, umesema unakwenda kumuita docta anitoe, mbona hufanyi hivyo, tunapoteza muda bure, tutafukuzwa hapa na mume wako atakuwa hana amani, unajua ni nini kitatokea, ni nani atalaumiwa kwa hilo, mimi au wewe....’akasema

‘Sawa, nimekuelewa…’nikasema

‘Madam,..usiwe na wasiwasi na mimi, dada yangu, sina nia mbaya kabisa, mimi nimetii wito kutoka kwa mume wako, kama kuna cha kulaumu, basi mlaumu mume wako, na...nakuahidi nikitoka hapa mume wako atakuwa salama, salamini…’akasema

‘Sawa …sasa nimekuelewa, hamna shida…’nikasema.

‘Madamu sikiliza  nikuambie wazi, wewe ndiye unayesababisha mume wako asipone kwa haraka, jaribu kumsikiliza mume wako ni nini anakitaka, uone kama hatapona, ni ushauri wamgu wa bure tu, hapo alipo anajikakamua tu, lakini kupona vyema ni wewe tu…shauri lako....’akasema

Aliposema hivyo, nikaona nisiendelee kulumbana naye, maana kwa huyu mtu ni mjanja sana, ukimtaka kwa maneno mtalumbana mpaka kesho;

‘Kwahiyo kwa kifupi, mume wangu anakutakia nini wewe…?’ nikamuuluza

‘Kwa ufupi, anataka mimi niwe wakili wake….’akasema

‘Wakili wake kwa kesi gani…?’ nikamuuliza

‘Sio kesi, ila ananihitajia mimi kuwa wakili wake wa kifamilia na hata mambo ya kazini kwake, ila hatujafikiana muafaka, labda leo ndio kaniita tumalizane, sina uhakika na hilo, madamu....’akasema

‘Lakini  mbona tunaye wakili tayari, wa kifamilia na mambo ya kikasi, na unalifahamu hilo…’nikasema

‘Ukamuulize yeye mwenyewe, ila sijajua alichoniitia hapa hii leo, naomba usininakili vibaya...'akasema

'Ni lazima atakuwa kakuambia ni kwanini anahitajia wakili mwingine au sio...?' nikauliza kwa upole

'Ndio kasema wakili huyo hawakilishi matakwa yake, na ana wasiwasi kupona kwake kunaweza kuwa ni mwanzo wa tatizo jingine,..kwahiyo ameniita mimi kuja kumsaidia, na zaidi ni kutokana na ushauri wa docta, kuwa ajitahidi kuondoa yale yote yanayomsumbua akilini...ni hayo tu ninayoweza kukuelezea, siwezi kueleza zaidi ya hapo...’akasema

‘Wewe uwe wakili wake, ….hahaha, labda niwe maiti…’ nikasema.

‘Madamu, kwanini unasema hivyo, mimi ni wakili au sio…sasa kuna tatizo gani nikifanya kazi za mumeo, ....cheti changu kinatambulikana kimataifa, japokuwa fitina zimepita nyingi tu..,’akasema

‘Fitina au ndivyo ulivyo..’nikasema

‘Hao hao watu wanaoleta fitina wakikwama chini kwa chini, wanakuja kwangu kutaka niwakwamue, na ndivyo ninavyotaka kufanya kwa mume wako...kumsaidia rafiki yangu…kwenye matatizo yake.’akasema.

‘Mume wangu hana matatizo, kachanganyikiwa tu,na wewe unachukulia mwanya huo kumghilibu…’nikasema nikigeuka kumwangalia mume wangu, na wakati huo, alikuwa akiteta jambo na rafiki yake.

‘Docta kanithibitishia kuwa hali yake ipo shwari, na wala hajachanganyikiwa, na nikimsaidia nitakuwa nimechangia kwa kiasi kikubwa kumtibia,na nimemuhakikishia docta kuwa mimi nitamsaidia rafiki yangu apone kwa haraka..kama unabisha, kamuuliza docta wake…’akasema

‘Kwa hili tutapambana..’nikasema

‘Hebu kwanza, maana naona vitisho vyako vinazidi, unaonaje… , naomba dakika kumi tu,niongee na mteja wangu, nikimalizana naye mtaongea naye, na kama atataka kuwaambia lolote,atawaambia yeye, ila baada ya mimi kuongea naye leo,kama kuna lolote la kumshutumu yeye, naomba mliwasilishe kwangu mimi kama  wakili wake...’akasema.

‘Tapeli mkubwa wewe...sikia nikuambie...’nikasema hivyo na kugeukia kule alipo mume wangu, walikuwa bado wnaongea rafiki yake, na walionekana kama wakibishana jambo fulani, na rafiki yake…baadae niliona docta kama ananyosha mikono juu kusalimi amri,akasogea pembeni kama kukata tamaa.

Mume wangu aligeuka kuniangalia, na mimi nikitabasamu ile ya kebehi, na yeye alipoona hivyo,akainamisha kichwa chini, na ilionekana hakuwa na furaha , sijui waliongea nini na rafiki yake,mgeukia huyu mtu na kusema;

‘Nitahakikisha nayafahamu haya yote, na unanifahamu nilivyo...mimi naondoka, lakini kama kuna lolote baya linaloendelea dhidi ya mume wangu, au dhidi yangu mimi, tutapambana, ....tutaona mwisho wake, na safari hii, nitahakikisha hurudii tena...’nikasema huku najifanya natabasamu, na huyo jamaa akisema.

‘Usijali dada yangu, umeshaniambia hilo mara nyingi tu, usipoteze pumzi yako, kwa kurudia rudia, kitu kisichotekelezeka,…na sioni kwa nini usiniamini,...utakuja kunipa mkono wa ahsante, lakini nilijua na wewe unatakiwa kuwepo ....’akasema na kuangalia saa yake.

‘Siwezi kukaa kusikiliza utapeli wako…’nikasema

 Kwa muda ule nikageuka tena kumwangalia mume wangu, na mara docta akaingia, na sasa akawa anaongea na mume wangu, na dakitari akawa anaandika kitu kwenye kumbukumbu zake, halafu akageuka kuniangalia mimi na kusema;

‘Kuna lolote jamani maana muda umekwiisha wa kuwaona wagonjwa, kama kuna lolote jingine basi niwapa dakika kadhaa..au kama kuna kitu cha kuulizaniulizeni, vinginevyo dakika zilizobakia ni z huyu mgeni wa mgonjwa, au sio…’akasema akimuangalia mume wangu

‘Sawa kabisa docta, …na mke wangu,…’akasema


‘Hapana…nahisi ni bora mkaongea na huyu mtu wako hatutaki aina yoyote ya malumbano, unasikia, bado upo kwenye masharti, vinginevyo, usibiria mpaka hali iwe sawa, kwa vipimo vyako, bado kidogo…’akasema docta.

Mimi nilimwangalia mume wangu, yeye alibenua mdomo kama kulazimisha kutabasamu, lakini kwa undani zaidi machoni, niliona kama ana huzuni, nahisi mume wangu yupo kwenye matatizo makubwa..

‘Huyu mtu ana nini, kwanini amchukue huyu tapeli, sio bure, kuna tatizo hapa…’nikasema kimoyo moyo

Hapo sikutaka kupoteza muda, au kusikia kile alichosema mume wangu kuwa na mimi natakiwa niwepo,..., nikageuka, na kuanza kutoka nje,...na kabla sijafika mbali nikasikia mtu akiniita nyuma yangu, sikutaka kugeuka kwani sikutaka kuongea naye, lakini huyo mtu hakukata tamaa, alinikimbilia na kunishika bega.

‘Kwa hali ilivyo , nakushauri, acha wafanye wanavyotaka, ili kuepusha shari...naona kuna kitu kinaendelea , usipokuwa makini, utaumia, na unaweza ukampoteza mume wako…’alikuwa na docta rafiki

‘Wacha itokee hivyo, mim sijali tena…’nikasema

‘Lazima ujali huyo ni mume wako…na kwanini hukusubiria ukasikia wanataka kuongea nini, hasira zako zinakufanya ukose maana…’akasema

‘Acha nikose hadi hapo najua nimesimama na nani, na ni nani adui yangu, ila kwa mume wangu najua kuna mtego, kategewa na huyo mtu, huyo mtu ni tapeli, sio bure,..mume wangu anafanya kwa nguvu za….’hapo sikumalizia

‘Hahaha, sio kweli, mume wako anafanya hivyo kujihami, anajua akipona hapo, utaweza kumshitakia kwa wazazi wako, hiyo ni moja ya sababu  lakini pia pia kuna huo mkataba wenu, mimi sijui unahusu nini,  unaweza ukawa ni sababu nyingine kubwa sana…au..ni ..nakumbuka kuna kipindi ulipokuwa unasomea sheria ulisema ungelipenda kitu kama hicho…’akatulia akitaka mimi nisema neno, lakini sikusema kitu

‘Basi kama mlifanya hivyo, mkawa na mkataba kama huo…ndio unamueweka pabaya, yategemea mumekubalinana nini, maana naona hicho ndicho mume wako anakihofia sana, hasa akitaja mkataba…’akasema

‘Wala hilo kwangu sio tatizo kubwa, kama kakosea, akiri kosa, na mimi ni binadamu, tunaweza kuvumiliana kutegemeana na hilo kosa, lakini kwa jinsi nimjuavyo,…haweze kukiri kosa, atajibaragua na kutafuta uchochoro wa kujitetea, sasa hilo sitaweza kulivumilia, bora mkataba ufanye kazi yake nijue moja tu…’nikasema

‘Kutegemeana na kosa,…nakunukuu, je kama  kosa ni hilo la kuwa katembea na rafiki yako, na sasa kazaa naye,utalichukuliaje hilo…’akasema docta

‘Weeeh, mungu wangu, na rafiki yangu, hapana..ingelikuwa na mtu mwingine baki, hata hivyo, kwenye mkataba hilo ni kosa kubwa, halina msamaha…haaah, hapana, hawezi akafanya hivyo, maana anafahamu madhara yake…’nikasema

‘Mhh…sasa hilo, nahisi ndilo linamtesa, na huko kuhangaika kwake yawezekaan ikawa ndio sababu, ..lakini sioni ni kwanini amtafute wakili, hapo ndio nakuwa na mashaka,…ina maana kweli, huwezi kumsamehe..?’ akauliza

‘Kama mtu akivunja masharti ya ndoa, kama hivyo, akazini nje, ..na ushahidi ukawepo, basi kakiuka mkataba, na adhabu yake ipo wazi, hatuwezi kuchezea kiapo, tuliapa na kukubaliana, je kama ingelikuwa ni mimi angelifanyeje, mkuki usiwe kwa nguruwe, sasa akiri tuone, nita…haaaa…..’hapo sikumalizia, kwani simu ya docta iliita, na kwa haraka akaipokea, na akawa anasikiliza kwa muda, na alipomaliza, akaniangalia na kusema

‘Rafiki yako ameshafika,alikuwa akikuulizia, anasema kajaribu kukupigia kwenye simu yako lakini ulikuwa hupatikani....’akasema na mimi hapo ilikuwa kama mshtuko mwingine tena kama mtu kanipiga kibao cha kushtukizia usoni..nilishtuka kweli, na muda huo nilikuwa nimeshikilia mlango wa gari, ukiwa nusu wazi,.. nikajikuta naufunga huo mlango badala ya kuufungua.

‘Ka…ka…ooh, ….’nikashika kichwa na kutulia kidogo

Kwakweli pale nilihisi moyo ukinienda mbio, kama vile hasira, au…kutaka kufanya jambo. Nilibakia vile kwa muda, baadae docta akanisogelea akitaka kunishika, lakini kwa haraka nikaweka mkono kama kinga, asinisogelee, halafu nikauliza.

‘Yupo nyumbani kwake?’ nikawa nimeinamisha kichwa chini sikumuangalia docta.

‘Ndio, yupo nyumbani kwake…’akasema

‘Na mtoto wake hajambo…?’ nikauliza

‘Atakuwa hajambo, lakini hakuongelea lolote kuhusu mtoto wake na mimi sikumuulizia hilo....’akasema.

‘Sawa bosi…’nikasema hivyo

‘Hahaha mpendwa,  nimekua bosi tena, sikiliza ex-wangu,...napenda nikushauri jambo la kutoka moyoni…’akasema

‘Sihitajii ushauri wako…, hivi sasa sitaki kumuamini mtu zaidi ya wazazi wangu tu, nimeona wazazi wangu …ndio wa kuamini, waliyonishauri nikawapinga sasa ndio naona matokeo yake, nayaona, lakini sitakubali…’nikasema

‘Sikiliza tu… ninachopenda kukuambia ni kuwa kwa jinsi haya mambo yanavyokwenda, unanihitajia sana kuwa na mtu wa karibu sana wa kukusaidia, mtu anayeaminika, kwasababu nakuona upo katikati ya watu ambao unahisi ni marafiki zako kumbe pembeni wanakutendea visivyo…’akasema

‘Na mmojawapo akiwa ni wewe…’nikasema

‘Sawa kama utaamini hivyo…ila ukweli ndio huo, hao unao-ona ni marafiki zako, hao hao wanaweza kugeuka kuwa ni maadui zako wakubwa.....hebu fungua macho na masikio yako unisikilize angalau kidogo....’akasema.

‘Ni kweli unayoyasema, naanza kuamini hivyo,..na hao wanaojifanya ni marafiki zangu kumbe ni maadui zangu nimeshaanza kuwaona,  akiwemo wewe mwenyewe, siwezi kukuficha hilo,..’nikasema

‘Sio kweli, mimi sitaweza kuwa adui yako hata siku moja, nilishaapa kuwa nitakusaidia, na itakuwa hivyo mpaka mungu aichukue roho yangu…’akasema na mimi hapo nikageuka kumuangalia.

‘Hahaha.., usijifanye kuwa wewe haupo kwenye hilo kundi, maana wewe unauma na kupulizia,...upande mmoja unajifanya rafiki upande mwingine, unajificha kwenye maadui zangu, nimeshakufahamu kuwa wewe una ajenda ya siri,..’nikasema

‘Sio kweli….’akasema na kabla hajaendelea nikasema

‘Hata hivyo nawaambia hivi… mimi naamini sana watu, lakini nikija kugeuka, hutaweza kuamini kuwa mimi ndio yule mtu…na kwa hili nitapambana nanyi, mmoja baada ya mwingine....hilo nawathibitishia...’nikasema nikionyesha kidole cha kuapa.

‘Mhh, haya bhana, sina la kusema, lakini ipo siku utagundua huo ukweli niliokuambia,....ila, nakupa angalizo kama mtu anayekujali, usijidanganye sana na kujiaminisha kuwa utaweza kupambana na hao wtu kirahisi hivyo, muhimu tafuta muda, tuliza kichwa,… usiyachukulie haya mambo juu kwa juu, utaumia vibaya sana.....’akasema

‘Hilo sio la kunishauri mimi…, nimeshajua mwenyewe, na hujui nilivyo, nimekuwa na subira sana, sijachukulia haya mambo kwa pupa, kama ningelifanya hivyo, sasa hivi tungelikuwa hatuongei…nimeonekana mjinga nisiyeona au kusikia, unajua ni kwanini…’nikasema kama nauliza na huyo docta akaongea kama vile hakunisikia

‘Huyo wakili,…sio mtu wa mchezo mchezo kama unavyomfikiria wewe, ana uzoefu na kazi yake…, na huko polisi anajuana na kila mtu,…hap hapo polisi wanamtum,ia kwa mambo yao,…huyo jamaa ni mtu hatari sana...usije ukalogwa kupambana naye peke yako...’akasema na aliposema hivyo mimi nikafungua mlango wa gari na kuingia ndani ya gari langu, nikashusha kiyoo ili niweze kumuaga docta.

'Kama ni mtu hatari basi kakutana na mtu hatari zaidi yake, mimi namfahamu sana, nimeshapambana naye mara mbili na zote kalilia pua...wewe hunijui tu…subiria uone vumbi langu, kwaheri, nisalimie mkeo…..'nikasema huku nikikanyaga mafuta.

Niliendesha gari, kwa muda..na nilipofika mbele, nikachukua simu yangu na kumpigia mtu wangu.

'Sikiliza..kama nilivyokuambia, kuna mtu yupo hospitali na mume wangu, mfuatilie, hatua kwa hatua, nataka kila kitu anachokifanya..hata ukiweza kufahamu walichoongea…, na ujue wapi atakapokwenda akitoka hapo hospitalini, unasikia, hilo ni muhimu sana..kazi njema, ..'nikasema na kukata simu.


NB: Haya hiyo ya moto moto….


WAZO LA LEO: Sio wote wanaoitwa marafiki ni marafiki wa kweli kwako, sio wote wanakuchekea, wana nia njema na wewe, cha muhimu, ni kujaribu kutimiza wajibu lakini pia kuwa kuwa na tahadhari, kwa kutokutoa siri zako, kwa kile unayemuona ni rafiki yako. Kumbuka adui na rafiki yako ni huyo huyo anayekufahamu sana.

Ni mimi: emu-three
Ni mimi: emu-three

No comments :