Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, December 23, 2013

Mkuki ni kwa Nguruwe-53


Mwenyekiti alituliza kikao baada ya kuona kuna majibishano makali kati ya rafiki yangu na mume wangu, kiasi kwamba kama asingeliingilia kati yangelizungumzwa mengi ambayo hata hayakustili kuzungumzwa kwenye hicho kikao. Wawili hawa walikuwa wakitupiana maneno makali, wakajisahau kabisa kuwa humo kwenye kikao wamo wazazi, watu wa kuheshimika, na kama hawo wazee wasingelikuwepo hapo, wengi  walitamani hawa watu wawili waachiwe wapashane mpaka hamu yao iwaishe.

Ilivyoonekana hayo yote yalitokana  na kutokukubaliana kuhusu mtoto.Wawili  hawa walishindwa kukubaliana hapo kabla hawajafika kwenye kikao, inaonekana walikutana kabla  li wakubaline kuhusu taratibu za mtoto, na moja ya jambo kubwa , ni jinai gani wangelificha ukweli, na ilitakiwa mama mtoto akane kabisa kuwa mtoto huyo hajazaa na mume wangu. Lakini hilo lilileta ushindani kwani wakikana hivyo, ina maana mtoto atakosa haki zake za msingi.

Mume akiwa anajua kuwa atashinda, kwa kutumia mkataba wa bandia, alitoa hoja kuwa mkataba unampa nafasi ya yeye kufanya atakavyo, kwahiyo hilo halitakuwa na tatizo,yeye kwenye kikao atakana kuwa hana mtoto, na baadaye atageuza hiyo kauli yake akitumia mkataba huo wa bandia. Rafiki yangu alisema kama ni kukana, iwe hivyo moja kwa moja, mtoto wake, asijulikane kabisa kuwa baba yake ni m ume wangu. Kila mmoja akawa na msimamo wake.....

Ndio maana hata mume wangu alipofika hapo kwenye kikao alikuja na kauli hiyo, ya kukana kuwa hana mtoto mwingine, kauli hiyo ingekuwa na uzito kama shahidi wa kwanza wa yule binti asingelikuwepo, lakini kuja kwake, kulisababisha hayo yalijificha yafichuke, na kuja kwake, kungempa mtoto wa huyo binti nafasi ya kutambulikana zaidi ya mwingine, na huenda kikao kingeamua kumpa haki zote huyo mtoto, mama wa huyo mtoto mwingine akashindwa kuvumilia.

Pili mume wangu alitaka , pamoja na kukana kwenye kikao kuwa huyo mtoto hajazaa na yeye, lakini kwa siri yao wawili na mkataba wao wa siri, wao waje kumtambua huyo mtoto, na haki zake ambazo zilikwisha andikwa kwenye mkataba  mwingine wa siri, na kwa vile wao walijua kuwa ule mkataba wao waliogushi unampa mamlaka mume ya kufanya apendavyo, baada kikao angeliweza kumtambulisha huyo mtoto kwangu na kuomba msamaha, na mimi niwajibike kumkubali na kumsamehe....

Lakini kutokana na mkataba wetu wa awali kuonekana, mkataba ambao ulikuwa ukimpa haki kila mmoja, mke na mume, hakuna aliyepewa  mamlaka ya zaidi ya kufanya apendavyo, kila jambo lilihitaji kukubaliana na kushauriana, na kama mmoja akikiuka masharti ya ndoa, hasa hayo makubwa ya kusaliti ndoa, basi huyo mkosaji, anawajibika, kukosa kila kitu, na ndoa inakuwa haipo tena. 

Rafiki yangu alipewa kibali cha kuongea na mwenyekiti, akawa anatoa maelezo yake, japokuwa mimi akili yangu ilikuwa mbali sana, lakini niliweza kumsikiliza, rafiki yangu alisema;

‘Nitatoa maelezo yangu katika sehemu kuu mbili, ya kwanza ni ukweli kabla sijapata mtoto na sehemu ya pili yenye ushahidi mnzito, ni ukweli baada ya mimi kjifungua, naomba muwe watulivu, ili niweze kuyasema yote niliyoyakusudia kuyaongea leo hii...’akasema na kuniangalia mimi.

‘Mimi ninaamini kwamba kila jambo huja kwa minajili fulani, na hili la kupata mtoto huenda na kweli limetokea ili iwe fundisho sio kwangu tu, na hata kwa wale wote lilowagusa kwa namna moja au nyingine. Ni changamoto, ambayo sitaweza kuisahau katika maisha yangu, ....’akasema

‘Mimi nilishajipangia kuwa huyu mtoto, nitamzaa na itakuwa siri yangu mimi mwenyewe,  na sikutaka awe na baba, japokuwa huwezi kuzaa mtoto bila baba. Kauli hii ya kuwa mtoto huyu hana baba niliwahi kumwambia huyu mwanaume aliyefanikiwa kunipa huu ujauzito, siku nilipopewa kibali kutoka kwa mshauri wangu, haya nitayaeleze kinamna, ..naomba mnielewe hivyo, sitayaeleza kwa undani sana, ili nispoteze muda.

Japokuwa nilipanga iwe hivyo, kuwa mtoto ni wangu, na hana baba, lakini mume wa familia alipogundua kuwa nimejifungua, akawa wa kwanza kufika hospitalini, na alipomuona tu, ilikuwa kama mtu aliyepagawa, akasema huyo ni mtoto wake, hakuna ubishi,...nikaharibu kila kitu, na nkajua sasa mambo yatakwenda kinyume na  matarajio yangu, na makubaliano yangu na mshauri wangu kuwa nikizaa hata mume aliyenipa mimba ikiwezekana asifahamu.

‘Mimi ninahisi kilichomfanya mume wa familia ang’ang’anie sana ni kwa vile nimepata mtoto wa kiume, na yeye kwa kauli yake mwenyewe, alikuwa akitaka mtoto wa kiume, maana watoto alio nao na mke wake , wote ni wa kike,...mimi sikuyajali hayo kwani mipanglio yangu ilikuwa nizae mtoto, na huyo mtoto awe ni wangu wote hata nikiandikisha jina lake kwenye cheti chake, lisomeke jina lake,na ubini wa baba yake, liwe ni jina langu kwa herufi yangu ya mwanzo, halafu jina la tatu liwe la baba yangu mzazi  ndio nilivyotaka  iwe hivyo

Lakini baadaye tulipokutana mimi na mwanasheria wao na mume wa familia, mume wa familia akasema hilo halikubali, mtoto huyo ni wake, kwani yeye ndiye mume aliyeweka mbegu, ana haki ya kufanya apendavyo kwa huyo mtoto,na hata kisheria yeye kama baba ana haki na huyo mtoto , na pia huyo mtoto aandikwe kwa ubini wake, ili atambulikane kuwa yeye ni baba yake, na hili atalifaya nipende au nisipende. Utaona mbinu gani walitumia baadaye akiwa na mshirika wake mkuu, kwenye ushahidi wangu wa pili,

Mpaka hapo mimi na mume wa familia tukawa hatukuelewana hadi muda wa kikao ukawa umeshafika, akaona yeye aje kwenye kikao, akisema akifika kwenye kikao atahakikisha uwezo wote wa kifamilia anao yeye, na alisema mkataba alionao yeye unampa hiyo nafasi, alinionyesha huo mkataba, lakini niliuona una utofauti, na jinsi nilivyokuwa nikifahamu mimi kutoka kwa rafiki yangu , sikuwahi kuusoma huo mkataba wao wote kabla, lakini kwa kauli ya rafiki yangu, mkatana wao, ulikuwa hauruhusu mume au mke, kujitwalia madaraka bila kumshirikisha mwenzake.

Na nakumbuka rafiki angu huyo aliniambia kuwa kama mmoja akimsaliti mwenzake, na ukapatikana ushahidi, ama wa kuona au kudhihiri, kwa mfano kupatike mtoto, ambaye ni ushahidi tosha, basi nijuavyo mimi, ni kuwa ndoa hiyo imeshavunjika, na muhusika hana chake, sasa niliona ajabu akiniambia kuwa yeye kwenye huo mkataba alio nao yeye ana mamlaka, ya kufanya apendavyo kama mume wa familia...

‘Kuhusu huo mkataba wao, sikuwa naufahamu kabla, kwani unaweza kusema kuwa nilifanya makusudi ili nipate mtoto na huyo mume, ili ndoa yao ivunjike, ili mimi nije kuchukua nafasi ya mke wa mume wa familia, na mali iwe imeshaandikiswha kwa mtoto wangu,..hapana...sikuwa na tamaa hiyo na hilo halikuwa ni lengo langu, naomba mniamini kwa hilo.

Mimi nilikuja kuufahamu huo mkataba wao, walio nao, kipindi waliponiita nije kwa dharura,...nikaonyeshwa na kuambiwa kuwa nikikubaliana nao, basi nitapata mafanikio mengi, ....ni nini nahitajika kukubaliana nayo, naona hayo nitayaelezea kwenye sehemu ya pili ya ukweli wangu. Mimi ninachokumbuka sana, ni kauli ya rafiki yangu ambaye alinielezea kuwa mume wake asingeliweza kusaliti ndoa yake, kwani anafahamu ugumu wa mkatba wao ulivyo. Akimaanisha mkataba wao wa awali, lakini mkataba niliokuja kuonyeshwa baadaye ulikuwa hauna vipengele hivyo vigumu.

Mume wa familia kwa kujiamini aliniambia kuwa akitoka huku kwenye kikao atakuwa kamaliza kazi, kila kitu kitakuwa kwenye miliki yake, kwahiyo kinachofuatia ni kumwandikisha mtoto kama mmoja wa warithi wake..na ikizewekana kama mimi nataka nitakuwa nyumba yake ndogo....uone jinsi alivyonizarau, eti mimi niwe nyumba yake ndogo. Mimi nilimwambia hilo halipo, yeye aende akapiganie ndoa yake huko kwenye kikao, na kama akifanikiwa basi menginE tutayamaliza kinamna ambayo mimi nitarizika nayo, lakini nilifahamu kabisa kuwa baada ya hicho kikao, huyo mume atakuwa hana chake....’akasema

‘Ni kweli kuwa mtoto ni lazima awe na baba yake, lakini kwa mazingira niliyompatia huyu mtoto sikutaka kuwe na mtu anayeitwa baba, ukumbuke kuwa mimba hii niliipata kutoka kwa mume wa mtu, na niliipata baaada ya kupata ushauri  kutoka kwa rafiki yangu mkubwa japokuwa badaye rafiki yangu huyo alinikana kuwa yeye hakunipa ushauri wa mimi kutembea na mume wake,...muone jinsi gani sisi wanadamu tulivyo, ...’akatikisa kichwa kama kusikitika.

‘Rafiki yangu kwa kauli yake mwenyewe alinishauri kuwa nipate mtoto kwa kila hali,hata ikibidi nitembee na mume wa mtu, leo hii ananiambia kuwa mume wake, sio mume wa mtu, yeye ushauri wake ulilenga kwa  waume wengine sio kwa mume wake, eti kwa vile mimi ni rafiki yake, na ni sawa na mdogo wake..lakini mimi hayo sikuyajua kabla..ndio mimi ni rafiki yake lakini haoni kuwa kwa kuniambia hata mume wa mtu, basi kwa urafiki wetu wa karibu, mume wange ingelikuwa ni bora zaidi, kusibitisha kuwa sisi ni marafiki wa kweli kweli,..sijui, ndivyo mawazo yangu yalivyokuwa hivyo...mnaweza kusema najitetea tu kwa vile imetokea hivyo..

‘Huenda nilifikia uamuzi huo kwa vile niliwapenda sana watoto wake, au huenda nilimpenda sana mume wake, lakini nguvu za ushawishi ambazo mimi nakiri moyoni,zilitokana na kauli yake, kauli kutoka kwa rafiki yangu, kuwa nitembee, hata na mume wa mtu..na pia ni kutokana na ushawishi wa mume wake mwenyewe, kunishurutisha kwa kila hila...sisi wanawake ni rahisi sana kudanganyika....

 Baada ya tukio hilo urafiki wetu wa mimi n a rafiki yangu huyo uligeuka na kuwa uadui na mimi nikaonekana mtu mbaya sana, na nilistahili nipewe adhabu ya kuzalilishwa na kuharibiwa na watoto wakihuni, na kweli siku niliyofika tu kutoka Ulaya, nikatumiwa hawo watoto wa kihuni, kwa lengo hilo, lakini walishindwa kufanya hivyo, baada ya mbinu zao kugundulikana na polisi, vijana hawo sasa wapo jela, na nitahakikisha wanaozea huko, kama mna nia njema na wao muende mukawatoe.wao wamechezea kusipochezewa, hawajui kiini cha yote hayo,wanachojali ni pesa, mimi sio kama wanavyofikiria wao....’akasema.

‘Watu mtajiuliza ni nani aliyenishauri hivyo, kuwa nikazae kwa vile umri wangu umeshapita, ambaye alinishauri kuwa nimtafute mwanaume yoyote nitembee naye ili nipate mtoto, hata kama huyo nitakayetembea naye ni mume wa mtu,...?’ akatulia, alikuwa kama anawauliza watu, na akageuka kuniangaiia mimi, na mimi nilikuwa namuangalia tu, sikusema neno.

‘Huyo aliyetoa ushauri huo  ni rafiki yangu mpenzi, mke wa familia , kama ni uwongo, mulizeni mwenyewe kama sio yeye aliyenishauri hivyo, ..hebu muulizeni mume wa mtu ni nani, au labda aseme kuwa kauli yake haikumaanisha mume wake,  kuwa hakutoa ufafanusi wa kutosha, kuwa aliposema mume wa mtu, hakumaanisha mume wake, mume wake, ana sifa ya ziada ya mume wa mtu, labda yeye sio mume wa mtu, ni mume wake...sijui kama ingelieleweka, hapo. Lakini angeliniambia hivyo mapema, kuwa nikisema mume wa mtu, usimguse mume wangu, ni dhahiri kuwa hata mimi nisingelikuwa karibu na mume wake, ningeliangalia hilo onyo zaidi....

Lakini hakuwahi kutoa hilo anagalizo, yeye akanishauri hivyo, kuwa nitembee hata na mume wa mtu ili nipate mtoto, sasa kumbe mwenzangu akitendewa kwa mume wake itauma kiasi hicho, mimi sina kosa, sikujua hivyo, nilichofanya ni kufuata ushauri wake, na mahali pema nlipopaona ni kwa mume wake, je kwanini nilipotembea na mume wake ikawa ni taabu, je hawo wengine sio waume , kama alivyo mume wake, wao ni nguruwe, maana wanasema mkuki ni kwa nguruwe tu...kwa nguruwe, haumi, lakni mkuki kwa binadamu ni mchungu, unauma eeh...pole sana rafiki yangu na samahanai sana kwa hayo yaliyotokea...’akasema rafiki yangu akiogopa kuniangalia mimi, hakufahamu jinsi gani nilivyokuwa nikiumia.

‘Ndio maana sikutaka hata mtoto huyu ajulikae kabisa, kama ingelikuwa ni uwezo wangu, ningelimlea huko Ulaya, mpaka awe mkubwa, nimsomeshe huko huko naa kiwa mkubwa nimsomeshe kiini cha yeye kutokuwa na baba mpaka anielewe , hilo kwa Ulaye angelinielewa, ni kwani  nilifanya hivyo, huko ni jambo la kawaida tu,

Mtu aliyemuona kwa ukaribu sana pale nilipojifungua ni mume wa familia, na mume wa familia moja kwa moja akatambua kuwa ni damu yake, na wa pili, aliyekuja kumuona ni mke wa familia...’hapoa akatulia kidogo. Uone mitizamo ya watu hawa wawili.

Cha ajabu kabisa mke wa familia japokuwa alimuona mtoto anafanana na watoto wake, watoto wake, wanaofanana na baba yao, yeye alishindwa kabisa kutokumshuku mume wake, kwa vile alikuwa akimuamii sana mume wake, hakujua kuwa mume wake, ni msaliti asiyethaminika, wakati  yeye anamuamini mume wake, mume wake alikuwa akimcheka kwa nyuma kuwa mke wake ni mjinga, hana akili ya kufikiri, ..hayo siyasemi kutoka mdomoni kwangu kwa nia ya uchochezi, ...nayanukuu kutoka kwa kauli ya mume wake, akiyatamka mbele yangu, alivyokuwa akiniambia

Aliniambia  kuwa mke wake anavyomuamini amekuwa kama mjinga fulani  asiyeweza kuona mbali kwahiyo tunaweza kufanya lolote tuwezavyo, na wala asishituke, na ndivyo ilivyokuwa baada ya kupewa kibali kile siku ya kwanza, siku ambayo ilifungua ukurasa mwingine ambao sikuwahi nao kabla, ukurasa wa kutembea na waume za watu. Mimi kwa ujumla sikuwa na tabia hiyo..

Siku aliponitamkia rafiki yangu kuwa nikatafute hata mume wa mtu nitembee naye ili nipata mtoto, ndio siku nilipoanza kuingiwa na wazo hilo la kufanya hivyo, kuwa kumbe waume za watu inawezekana, japokuwa kiujumal watu niliokuwa nikiawapenda walikuwa ni waume za watu, lakini nilikuwa naogapa sana kutembea nao, nikiwaogopa na kuwaheshimu wake zao, japokuwa ni wengi waliokuwa wakinitaka.

Rafiki yangu aliponishauri hivyo, nitafute yule ambaye nampenda na ninaweza kuzaa watoto, au mtoto nitayempenda, akili yangu ikadondokea kwa watoto wake, ..ni kweli bila kuficha watoto wake nawapenda sana, hata yeye mwenyewe analifahamu hilo,..

Je ningeliwezaje kutembea na mume wake, hilo lilikuwa swali gumu sana kwangu, na sikutarajia kuwa ningeliweza kufanikiwa kirahisi namna hiyo, na sio kwamba mimi ndiye niliyekwenda kumtongoza huyo mume, hapana, ..mume huyu alishaanza tabia hiyo ya kunitongoza siku nyingi, ila mimi nilikuwa namtolea nje, nikijua kuwa yeye ni mume wa rafiki yangu na nilikuwa namtambua kama shemeji yangu, ..ilikuwa vigumu sana kumkubalia ...lakini nahisi kama ilipangwa iwe hivyo, ili sote tupate fundisho.

Niwaambie ukweli, mke anapokuwa na mdogo wake ndani, au mume anapokuwa na mwanamke mwingine tofauti ndani, nafsi zao hujenga tamaa, na kama huyo mtu wa kike asipokuwa na ushujaa wa kujiamini, na kumkwepa huyo mume, basi, ni mtihani, ...wengi wanashindwa huo mtihani, na utaona wanaitana shemeji lakini mke akiondoka yanayotendeka huku nyuma ni mengine. Tujaribu sana kuwashibisha waume zetu, ili wasiwe na kisingizio,kama tuna wadogo zetu, au hata yoyote anayejulikana kama shemeji, na akawa na ukaribu na mume wako, uakuja kujuta, wakati huo umeshachelewa...nasema hili kwa uzoefu wangu mimi.

********

Turudi nyuma kidogo, siku nilipoanza mazoea na huyu bwana,maana msione anayatamka maneno hayo ya kashifa mkafikiri yeye ni mtakatifu, msimuone anatembea kichwa chini mkafikiri yeye ni kondoo, sio kweli, mimi namfahamu sana pengine hata mnavyomfahamu nyie.

Ofisi yangu ninapofanyia kazi ipo karibu sana na ofisini kwake, na katikati yetu, kuna hoteli kwahiyo nikitoka kwenda kula chakula cha mchana, ninapita kwenye ofsi yake, sasa bwana huyu alikuwa kama ananisubiria, kila nikipita hapo yeye anakuja kwa nyuma, au tunaongozana , hata kama hana njaa, atakuja kukaa karibu yangu, akiniongelesha, mimi kama mwanamke nilishamfahamu nia na lengo lake ni nini, lakini sikutaka kumzalilisha, na watu wanaonijua tabia yangu, ningelifanya hivyo, na asingeliweza kunifuata futa tena, lakini nilimstahi kwa vile ni shemeji yangu.

Alianza mapema tu kunitaka, akaanza kunielezea mengi ya nyumbani kwake, jinsi anavyoishi na mkewe, jinsi gani anavyopata taabu, hapati yale yaliyomuhimu kutoka kwa mke wake,kwahiyo, kama anavyodai yeye, ndicho kinamtuma afanye yale ambayo hakutakiwa kufanya,kama mume wa familia, kwa mfano, yeye kwa siri sana, alikuwa akitongoza wahudumu wa hiyo hoteli, wengi hawafahamu huenda hata rafiki yake mkubwa hafahamu hilo, lakini mimi nafahamu, kwa kinywa cha mume wafamilia, aliwahi kuniambia, na nikahakikisha kutoka kwa hawo wahudumu,...

Basi yeye akawa ananivuta kwa njia hiyo, na mwisho wake, akaniambia wazi wazi kuwa ananipenda, na mimi mwanzoni nilichukulia kuwa huko kupenda hakuna maana hasa ya kupenda, bali anataak kusema anautamani mwili wangu, si unafahamu tabia za wanaume, ....wana mbinu nyingi za kuwaingia wanawake, na huyo alifikia kuniambia kuwa toka aliponiona kwa mara ya kwanza, amekuwa akipata shida sana,akili yake haitulii kuniwaza,  ..

'Na alifikia kusema kuwa angelifurahi mimi nikachukua nafasi ya mkewe, ...hayo aliyatamka kwa kinywa chake mwenyewe, na usipokuwa na akili ya kutafakari, utafikiria ni kweli, lakini kauli kama hiyo, sio wewe peke yake unayeambiwa, huenda wewe ni wa kumi , au zaidi, ...kama mwanamke unatakiwa uyajue hayo, mimi nilijua ni maneno ya wanaume wakiwa na tamaa zao...nikajitahidi kumshinda kwa hoja, na kwa hekima.

Alipoona ameshindwa kwa mbinu hizo, na mara nyingi akiongea hivyo huwa nimetulia namsikiliza, akaanza kuja na maneno ya moja kwa moja kuwa ananitaka, nikaona sasa amekwenda mbali, nikampasha ukweli, kuwa asinione mimi nipo karibu naye, na asinione mimi namsikiliza tu akaniona mimi ni muhumi, nilimwambia wazi wazi kuwa mimi nawaheshimu sana waume za watu, na sitatembea na mume wa mtu abadan.

Kauli yangu hiyo ilimvunja nguvu, kwa kiasi fulani, na haikupita muda nikamuona akianza kulewa kupita kiasi, na nilipomuuliza kwanini anafanya hivyo, akaniambia anafanya hivyo kwa vile mimi nimemkatalia ombi lake na ananipenda kiasi kwamba hawezi kukaa mbali na mimi, na anapenda kila siku niwe naye, na zaidi anipate mimi, kimapenzi, na njia peke yake ya kuondoa mawazo ni kulewa..muulizeni mwenyewe hakuniambi hayo..’akasema rafiki yangu akimwangalia mume wangu ambaye alikuwa akicheka kwa dharau, utafikiri linaongewa jambo la maana sana kwake, hakufahamu jinsi gani nilivyokuwa naumia.

‘Basi akawa analewa kiukweli, mwanzoni nilijua ni mbinu zake, tu, lakini akawa analewa mpaka anakuwa ni mtu wa kubebwa, na wakati mwingine tunakuwa pamoja, mimi sinywi kihiyo, kwahiyo ikawa tunafanya kazi ya kumbeba mimi na ndugu yake, na akilewa ndio anabwabwaja ukweli, kuwa kulewa kote ni kwasababu yangu,....anasema siku nikimkubalia tu ombi lake ataacha kabisa kulewa.

‘Hali hiyo ikawa na mimi inanitesa, kwani kimoyoni kiukweli, nilitamani sana nifany e hayo anayoyayataka yeye, nilipenda sana, nimtimizie na ikiwezekana awe ni mpenzi wangu, nafahamu kuwa kumpata yeye kama mume wangu haiwezekani kwa vile yeye ni mume wa mtu lakini mimi ningeliweza kuwa mpenzi wake wa siri, au nyumba yake ndogo, kuna muda nilikuwa naingiwa na ibilisi wa kuwazia hivyo, unapokuwa huna mume, unaweza kufikiria mengi, na hizo ni ndoto za wwalio wengi, ambao hawajaolewa,kama mimi.

‘Nilijaribu sana kumfanya rafiki yangu anielewe kuwa mume wake yupo hivyo,kuwa ana njaa, ya haki yake ya ndoa, lakini kila nilipotumia lugha ya busara kwake, niliona kama ananiona mtoto mdogo nisiyejua mambo ya mke na mume kwahiyo nisubiri nikiolewa nitayafahamu, basi mimi nikaona niyaache yaendelee kama yalivyo, na nikajaribu kumkwepa mume wake, kwa kadiri ya uwezo wangu lakini ilikuwa ngumu.

Siku nilipoongea na rafiki yangu na kunitamkia yale maneno kuwa nitembee hata na mume wa mtu, niliona kanipa kibali, lakini mimi kama mwanamke nisingeliweza kumwambia moja kwa moja mume wa mtu kuwa mke wako kasema hivyo...ila ikatokea siku hiyo hiyo alipotamka hayo maneno, kukawa na sherehe, na mume wa familia kama kawaida yake akazinywa pombe kama anashindana, na mimi siku hiyo sijui ni kwanini na mimi nikanywa tofauti na siku nyingine....moja likazaa jingine, tulijikuta tupo kwangu,...na usije ukasema nilipanga mimi iwe hivyo, hapana, na wala sikujua kuwa itatokea hivyo, ..ilikuwa hivi

Baada ya kunywa kwenye hiyo sherehe na tukawa hata kutembea inakuwa shida, aliyefanya kazi ya ziada kutusaidia alikuwa mdogo wa mume wa familia, alituchukua hadi nyumbani kwangu, tulipofika kwa vile nimelewa, nikawa sijui ninachokifanya, tukanywa tena,na kilichofuata ni kutimiza yale ambayo niliyokuwa nikayapiga vita siku zote,..sikujijua hadi ilipofika usiku wa manane, nikatambua kuwa nimelala na mume wa mtu. Hapo moyo ukashituka, na kuanza kuogopa, ..

‘Nilitoka na kumuona mdogo wa mume wa familia akiwa kalala sebuleni, nikamuamusha na kumuomba afanye haraka amchukue ndugu yake waondoke, maana sitaki alake kwangu, ilikuwa kazi kumshawishi, lakini baadaye waliondoa, na hapo ikawa ndio mwanzo wa mahusiani yangu na huyu mume wa familia, nikawa siogopi tena, kama ilivyokuwa mwanzoni, na kwa vie nilikuwa nimesharuhusiwa kinamna na mshauri wangu, ikawa sasa kila tukipata mwanya nautumia ipasavyo, na ombi likatimia, nikapata hiyo mimba...’hapo akatulia na kumwangalia mwenyekiti ambaye alikuwa mara kwa mara akiandika kitu kwenye makabrasha yake kama vile ananukuu hayo yanayoongewa.

‘Kipindi cha ujauzito kilikuwa kigumu sana kwangu, nilijitahidi sana kujizuia, na kujificha ili watu wasifahamu kuwa nina mimba, ukizingatia kuwa mimi sina mume, nilichofanya ni kuvaa manguo mapana, na kutokuonekana kwenye kadamnasi za watu, nashukuru kuwa kipindi chote hicho, hakukuwa na kazi kubwa zilizonihusu mimi kwa bosi wangu, na kama zilitokea niliweza kuwapa wasaidizi wangu, wakazifanya na kwahiyo sikuweza kukutana na mshauri wangu ambaye pia alikuwa ni bosi wangu, kwahiyo sikuwa na wakati mgumu, wa kujieleza, na siku zikaenda na hauchi hauchi , miezi nane ikafika,

Nilizaa nikiwa na miezi nane, na mambo yakaanzia hapo, na pamoja na furaha ya kupata mtoto, lakini ilifikia mahali nikaanza kujuta, kuwa kumbe nilichukulia mambo hayo kwa haraka, huenda sikumuelewa rafiki yangu, lakini hata hivyo, nisingeliweza kuyafanya hayo kama isingelikuwa ni kutokana na shinikizo la huyo mume wa familia, najua wengi watasema mimi ni mtu mzima, ningeliweza kupima kila jambo kwa unagalifu, ni sawa....lakini tuangalie na upande mwingine wa shilingi’akaniangalia mimi na mimi nilikuwa nimemkazia macho.

‘Ni kweli kwa umri wangu huu,  mwanaume hawezi kunishika kwa nguvu, tungelipambana naye hadi hatua ya mwisho,lakini hata hivyo siweri kusema kuwa hayo niliyotenda niliyatenda kwa hiari yangu mwenyewe, kama ni hivyo kwanini sikuyafanya hayo kabla,hii inaonyesha kuwa kulikuwa na kichocheo, kilichonisukuma mpaka kuona kuwa nikitenda sio kosa, ...sio rahisi kuelewa hilo kwa sasa...’akasema na kuinama chini.

‘Hata hivyo, ukiangalia kwa namna nyingine, mwanaume ndiye kisababishi kikubwa, kwani hata kabla sijapata kibali cha kutembea naye, mume wa familia alishaanza kunitaka kwa kila hila,kuna wakati kweli akiwa amelewa huwa alikuw akaitumia nguvu, ningelifanya nini mimi, nashangaa mimi hapa kuitwa 
Malaya,..jamani mimi na yeye ni nani Malaya, huo ndio ukweli wangu wa kwanza,..

Huo ndio ukweli wangu wa kwanza kama nitaruhusiwa nipo tayari kuelezea ukweli wangu wa  pili, yale yaliyotokea  baada ya mimi kujifungua, ni mambo gani makubwa yaliyotokea, hadi kufikia kifo cha Makabrasha, nitawaeleza kila kitu, ili mjue ni nani mbaya wenu...’akasema na kumwangalia mwenyekiti, na mwenyekiti angaalia saa, na kuinua simu yake...

NB: Naona tushie hapa, tusubiri sehemu inayokuja, je ndio itakuwa hitimisho, au bado mambo yanaendelea..tuzidi kuwemo.


WAZO LA LEO: Ushauri tunaotoa kwa wenzetu, uwe wenye hekima, ukilenga yale ambayo hata wewe ungelishauriwa ungelifanya hivyo hivyo. Tusitoe ushauri ambao ukija kutendewa wewe hutakubali, tukumbuke sote ni binadamu, na sote tunahali sawa za kuumia, pale linapotokea  tatizo au kutendewa kile kisichofaa.

Ni mimi: emu-three

3 comments :

sonny said...

Ey there... miriam I presume thats your name. M sorry my Kiswahili is a bit rusty but your entries r just heavenly. I recently started reading your posts and I cant get enough. 1 question though isn't there a way or a link that will take me all the way to the beginning of ur first entry?

sonny said...

Ey there... k so 1st let me apologise because my Kiswahili its a bit rusty. With that being said, I think your diary entries are just heavenly. I recently started reading your posts and I can't get enough of them. 1 question though myb you can assist me, isn't there a link or somewhere that I can click to go to your 1st entry?

sonny said...

Ey there... miriam I presume thats your name. M sorry my Kiswahili is a bit rusty but your entries r just heavenly. I recently started reading your posts and I cant get enough. 1 question though isn't there a way or a link that will take me all the way to the beginning of ur first entry?