Mwenyekiti aliniangalia, akitaka ushauri wangu, kuwa tuendelee na kikao au kikao kiahirishwe hadi kesho, lakini kesho ni siku ya mapumziko huenda kila mtu ana ratiba yake , lakini hata hivyo, muda ulikuwa umekwenda sana, na watu walikuwa wamechoka, pamoja na hayo kikao kilitakiwa kimalize kila kitu kwa siku hiyo, ikizingatia kuwa kuna watu walitakiwa kusafiri, kesho yake, nilipoona mwenyekiti ananiangalia mimi nikasema;
‘Mwenyekiti mimi naona tuendelee na kikao kwa vile tumeamua kulifanya hili jambo, basi ni vyema tukalimaliza kabisa, mimi hapa nilipo sizani kama nitaweza kuliweka moyoni tena, nataka liishe tujue moja.
Na pia tuna bahati kuwa kesho ni siku ya mapumziko ya juma, basi tufanye hili jambo, tukitajia kuwa kesho tunapumzika, samahani kwa wale ambao tumewaharibia siku yao, lakini nafikiri ni kwa masilahi yetu sote, kwani sote tunahusika kwa namna moja au nyingine....’nikasema nikiwaangalia rafiki ya mume wangu na mkewe.
‘Labda ingelikuwa vyema, tukafahamu , huenda kuna mtu mwenye dharura, kama kuna mtu ambaye anaona tuahirishe aseme, ili tuone tutafanya nini, tunaweza kuahirisha hadi kesho, kama ikibidi, lakini tuhakikishe kuwa hawo wasafiri wa kuondoka kesho, wawe wanaondoka wakijua kuna makubaliano yenye muafaka juu yao, mfano huyo binti...’nikasema.na kumwangalia yule mfanyakazi wangu wa zamani.
‘Mimi naona tuendelee tu na kikao, tuyamalize, haya, ama kwa huyo binti, mimi sioni kwamba kuna jambo ambalo halijakubaliwa juu yake, kwani mtoto keshajulikana ni nani baba yake, na baba yake ni lazima awajibike juu yake, hilo halina mjadala , nafikiri rafiki yangu hawezi kukwepa hilo jukumu, ,...’akasema rafiki wa mume wangu, huku akimwangalia rafiki yake, na mume wangu hakusema neno, alionekana kuwa mbali kimawazao, na mwenyekiti alipoona watu wapo kimiya akasema;
‘Jamani naona tuendelee na kikao, ni muhimu tumalizane na hili jambo ili maisha yaendelee kama kawaida, na kama kuna mengine yakufuatilia, yafautiliwe, na kama kuna kuwajibika, watu wajue ni nini wanahitajika kuwajibika nacho, naona tulimalize hili ikiwezekana leo,...’akasema mwenyekiti huku akifungua makabrasha yake.
‘Kwahiyo kwa sasa muongeaji wetu anaweza kuendelea na sehemu yake ya pili, kama alivyoiita yeye mwenyemwe, ila hapo nina angalizo kidogo, kwenye utangulizi wake, kasema sehemu hiyo ya pili, pia itamgusa marehemu, hapo mimi nachelea kidogo, je wanasheria wetu mnasemaje kwa hilo,...?’akauliza mwenyekiti, akiwaangalia mawakili wetu.
‘Kwasababu ni maongezi tu, hakuna jambo linaloweza kuharibu mambo ya kisheria, sizani kama hayo atakayoongelea yataharibu mambo ya polisi na upelelezi wao, naona yeye aongee , akizingatia hayo, kuwa hilo swala lipo kwenye mikono ya polisi, mimi namfahamu muongeaji, yeye anafahamu wajibu wake, anafahamu mipaka ya jambo kama hilo...’akasema mwanasheria wa familia yangu, na mwenzake akakubaliana naye.
Mara akasimama,mke wa rafiki yangu , na kusema; ‘Mwenyekiti, samahani kidogo, kabla huyo muongeaji hajaongea nilikuwa nataka kuongea jambo moja, au niongee mimi kwanza, kwani hata mimi kesho natakiwa kuondoka, kurudi kijijini, nataka nikajiandae,...’akasema mke wa rafiki wa mume wangu, na mume wake, akawa kama anamzuia, na wakawa wanateta na mume wake, na baadaye, akasema;
‘Basi aendelee tu,...’akasema na mwenyekiti akasema;
‘Tunashukuru kwa kutuelewa, kwasababu mwenzako alishaanza, itakuwa sio vizuri,tukiwa tunakatisha katisha, tutashindwa kuyaweka haya mambo sawa, kama unavyoona hapa tuna wanasheria, yote haya wanayaweka kisheria, sio kwamba tunaongea tu, na kuishia hapa hapa, hapana, haya yote yanawekwa kwenye kumbukubu zetu, na kama kuna mambo ya kisheria ya kufuatilia, basi yatafanyiwa kazi..’akasema mwenyekiti.
‘Sawa mwenyekiti, nimekubali kusubiria, lakini akimaliza yeye, naomba sana niongee mimi, ni muhimu sana ...’akasema huku akigeuka kumuangalia mume wake, ambaye alikuwa akimwangalia kwa macho ya kumshangaa.
Mimi nilimwangalia huyo mwanamke nikahisi ana jambo kubwa sana la kuongea, na kama alivyoonekana toka awali, alikuwa kama hayupo kwenye kikao, na hicho alichotaka kukiongea inaonekana kakifikiria sana, na ameona ni lazima akiongee, nikakumbuka jinsi mume wake alivyosema kuwa mke wake anaonekana kuwa mawazo sana, kama vile ana matatizo makubwa, lakini hayataki kuyaongea hayo matatizo yake ni nini.
Nilitamani mwenyekiti amruhusu aongee, kwani huenda huyo mama akaghairi baadaye, hasa nilipoona mume wake, akiwa kama anamzuia aiongee hilo alilotaka kuongea.
‘Samahani mwenyekiti, huenda mwenzetu huyu ana jambo muhimu sana,kwanini tusimuachie akaongea,labda tumsikilize kwanza...’nikasema
‘Hapana, mimi naona, rafiki yako aendelee tu, sio muhimu sana...’akasema mume wake, na mke wake, akawa katulia, na alionekana kama kukerwa na maamuzi ya mume wake, akatizama chini, bila kusema neno. Na mwenye kiti akasema;
‘Basi mimi naona aliyekuwa akiongea aendelee, tusipoteze muda, haya tuelezee sehemu yako ya pili, na sehemu hiyo kama ulivyokwisha kuonywa, isije ikagusa mambo ya kipolisi na uchunguzi wao, sisi tunahitajika kufuata sheria, kwani hata kama hawapo hapa, lakini wanafuatlia kwa karibu, ni nini kinachoendelea kwenye hiki kikao, uwe makini nayo, kwani hatutaki kuja kuharibu sifa ya familia yetu, ongea yale yanastahili kuongewa hapa..natumai unaelewa, kwani wewe ni mjuvi wa mambo hayo...’akasema mwenyekiti.
‘Nashukuru sana, ndugu mwenyekiti, msiwe na wasiwasi na hilo, mimi nafahamu sana utaratibu huo, ninayotaka kuyaongea hapa ni mambo yanayoigusa familia yenu, na kwa vile hata mimi nimehusika kwa namna moja au nyingine, na hata kutambuliakana kama mwanafamilia, nitajitahidi nisiharibu jina la familia yenu, ni muhimu sana niyaweka haya wazi, ili wanafamilia wawe na maamuzi yaliyo sahihi...huenda mengi yamepotoshwa kwa masilahi fulani, lakini mimi kama mpelelezi, nimeyafanyia kazi...’akasema
‘Sehemu yangu hii ya pili, ambayo naona itakuwa hitimishi, la kila kitu kinachonihusu mimi, na walengwa, itahusu pale nilipojifungua...’akasema na kuniangalia mimi kidogo, halafu akamwangalia mume wangu, na akatabasamu kidogo.
‘Mengi yalisemwa, hasa baada ya kujifungua kwangu, na wengi, walitaak kujua ni nani aliyenipa mimba, kama nilivyosema awali, haya yaliyotokea hadi kupata mtoto, ni kutokana na ushauri wa rafiki yangu, ameshanishauri mengi, na nimekuwa muadilifu kwake, kama rafiki, kama mfanyakazi wake, na pia kama mtu ninayemuheshimu yeye kama dada yangu....’hapo akatabasamu kidogo aliposema kama dada yangu.
‘Nafahamu kuwa rafiki yangu atanilaumu sana, na hapo alipo hataman hata kuniona, ni kweli, ilivyo, na inavyoonekana kwa sasa nimekuwa kama msaliti kwake, kwa vile niliyafanya hayo niliyoyafanya, kinyume na alivyotaka yeye nimeshaelezea awali ni kwanini nilifanya hivyo..
Nilipojifungua, rafiki yangu alifika, na akagundua kuwa mtoto wangu anafanana sana na watoto wake, na kwa mtizamo wa haraka, kama angelikuwa hamuamini sana mume wake, angelijua moja kwa moja aliyefanya hayo ni mume wake, lakini akili yake ilifungwa kabisa, na hata alifikiria kuwa huenda ni mdogo wa mume wake, aliyefanya hivyo...’akasema na kuinama kidogo.
‘Mimi sio mtoto mdogo wa kutembea na huyo kijana, kwanini nifanye hivyo, ili nipate mtoto, halafu nije kumuita nani,hapana huyo ni mdogo wangu, nisingeliweza kujizalilisha kwake,.., sio yeye, na kama ilitokea nikaonyesha dalili kama hizo kuwa huenda yeye ndiye baba wa mtoto, basi nilifanya hayo kupoteza muda, ...mtoto huyo ni matokea ya yale tuliyofanya mimi na mume wa familia, samhani kwa mke wafmilia kwa kulisema hilo tena, nafahamu linamuumiza sana...
‘Nafahamu baada ya kujifungua, aliniuliza sana, kutaka kufahamu ni nani baba wa mtoto, na nilimkatalia kumwambia, na hata kumkatalia kuwa mume wake, sio baba wa mtoto wangu, nilifanya hivyo ni kwasababu ya kuogopa mabadiliko niliyoyaona kwa rafiki yangu ambayo kama ningelimwambia wakati ule, huenda kungelitokea mabaya zaidi. Sikutarajia kabisa kuwa rafiki yangu ataumia kiasi hicho, sikutarajia kuwa hilo nililolifanya ni kosa, ikizingatiwa kuwa ni yeye aliyenishauri nifanye hivyo...
‘Wakati nilipoonja asali, na ukijua asali huwezi kuionja mara moja, ..baada ya kuona kuwa kumbe kutembea na mume wa mtu sio tatizo sana, nikawa sasa nakutana na mume wa familia bila kuogopa, na hilo lilikuwa kosa kumbe kulikuwa na maadui wananifuatilia kwa karibu, mimi bila kuwa amkini kwa hilo,tukawa tunakutana na mume wa familia sehemu tiofauti, na kuna siku nyingine, nilikuwa naenda naye kwa ndugu yangu , hapo ninapoishi kwa sasa, na ikawa ndio sehemu yetu ya siri ya kukutana, kumbe hapo kulikuwa na ndoana ya kutunasa,..
Siku moja, baada ya kujifungua, alikuja mume wa familia, kipindi hicho nipo kwenye sehemu yangu ya kwanza niliyopanga, akaniambia kuwa kuna tatizo kubwa limetokea, nikamuuliza tatizo gani, mara akatoa picha na kunionyesha, ...oh...shabashi,....’akatulia kama anaziangalai hizo picha kwa hisia.
‘Zilikuwa chafu, zilikuwa picha zikionyesha jinsi gani tulivyokuwa tumejisahau mimi na huyo mume wa familia, maana ilionyesha ushahidi dhahiri ...bila kuficha kile tulichokuwa tukikifanya, picha ambayo haikufaa kuonyeshwa kwa watu..’akakunja uso kuonyesha uchungu au hisia ya kukasirika.
Nilishituka sana, sikutarajia kitu kama hicho, kwanza nikaziangalia, na kwa haraka nikazichana, na kuhakikisha hakuna kitu kinachoonekana na yeye, yaani mume wa familia, akaniambia;
‘Hata mimi nilipoonyeshwa hizo picha nilifanya hivyo hivyo, lakini kila siku nikawa naletewe picha kama hizo na nyingine mbaya zaidi ya hizo,...’akasema
‘Alikuwa akikuleta nani hizo pichai?’ nikamuuliza kwa hasira
‘Sijui,...ila mwishoni hapa, kuna simu nimepigiwa na mtu nisiyemfahamu, mtu huyo anasema anataka kuongea na mimi, nikamuuliza unataka kuongea na mimi kuhusu nini, akaniambia kuhusu mzigo niliokuwa nikiupokea mara kwa mara, nikamuuliza mzigo gani, akasema picha, ndio maana nimekuja kukuona wewe kwanza...’akasema
‘Ina maana huyo mtu aliyekuwa akikuletea hizo picha, mlikuwa hamuonani, naye, ulikuwa unazipata vipi, na hayo ya kupata hizi picha yalianzia lini nii siku nyingi, mbona hukuwahi kuniambia kabla, na kwanini sasai umeamua kunionyesha, au kwa vile kakuambia muonane ndio maana unakuja kunionyesha, ..?’ nikamuuliza
‘Ni kweli,picha hizi nilishazipata kabla,mapema tu, na sikutaka kukuonyesha mambo haya, kipindi ukiwa mja mzito, nilisubiria ujifungue kwanza, niliogopa usije ukaharibu mimba, ...’akasema
‘Unahisi huyu mtu ni nani?’ nikamuuliza kabla hajaendelea zaidi
‘Kwakweli nimefikiria sana, nikakumbuka kuwa mtu anayenisumbua sana, kwa mambo mengi, yanayofanana na hili, ni mtu wangu wa karibu, lakini sikutarajia kuwa anaweza kufikia hatua hii, nashindwa hata kuamini, na kwa namna ninavyomfahamu anaweza kufanya hivyo, lakini yeye asingelista kuja kuniambia moja kwa moja ni nini dhumuni lake, hili la sasa huenda kukawa na mtu mwingine nyuma yake...’akasema
‘Ni nani huyo rafiki yako na anataka nini kwako,?’ nikamuuliza
‘Huyu mtu anataka mambo mengi makubwa,sina uhakika kuwa ni rafiki yangu, ila kwa ujumbe wa kwanza, huyo mtu alianza kudai pesa, kwa kuogopa, nikampa, kwa kupitia kwa mtu mwingine, nafahamu kuwa huyo mtu mwingine asingeliweza kuomba kiasi kikubwa hivyo cha pesa, nikawa nafanya uchunguzi, lakini sikuweza kumtambua ni nani
‘Nikaona nimuuliza rafiki yangu huyo, lakini yeye alianiambia hajui, na kama simuamini, hajali,...’akasema
‘Hebu niambia kuhusu huyo rafiki yako..’nikamwambia
‘Rafiki yangu huyo, tunafahamiana tangu tukiwa huko kijijini alikuwa na ndoto nyingi za utajiri wa kutumia mambo kama hyo, lakini alitaka kutumia akili, na elimu aliyoitaak kuipata, akisema unaweza ukapata mali, kwa kutumia akili, bila kuvuja jasho, bila kutumia silaha,...’akasema...’akasema.
‘Mimi kwa kipindi hicho, nilikuwa napenda sana hayo maongezi yake, na akawa ananifundisha mbinu mbali mbali,...’akatulia, na mimi kwa jinsi alivyokuwa akiongea, nikaona kama anapoteza muda nikamwambia;
‘Ongea kwa haraka, maana nina mambo ya kufanya?’ nikamwambia nikiwa sitaki hata kuyasikiliza zaidi, kwani nilishajua ni nini kitafuata baadaye, lakini japokuwa yalinigusa moyoni,lakini kwa muda ule niliyachukulia kama vitisho tu, ....hata hivyo kwenye akili yangu, nikikumbuak jisni picha inavyoonyesha, nikawa nahisi mwili ukisisimukwa kwa woga, hasa nilipokumbuka kauli ya rafiki yangu ambaye kwa kipindi hicho,nilishaongea naye akatoa vitisho kuwa yoyote atakayetembea na mume wake, atamfanya kitu kibaya,...hofu ikaanza taratibu kuingia kwenye ubongo wangu..’akasema
‘Nikikumbua yale aliyokuwa akinisimulia, naishia kusema kuwa huenda huyo mtu, ni rafiki yangu, na naona sasa kaaamua kutumia njia hii baada ya kuwa namkatalia kila analonishauri, na sijapongea naye, baada ya kunikatalia mara ya kwanza kuwa hahusiki na uchaf huo, kama alivyouita uchafu.
‘Baada ya kupata ujumbe kuwa huyo mtu aliyenitumia picha anataak kuongea na mimi, nikampigia simu rafiki yangu ili nijue ni yeye au ni mtu mwingine, ...lakini kama ni yeye, mpiga simu sio mwanaume, ni mwanamke, ...anaweza akamtumia mfanyakazi wake, anipe huo ujumbe, inawezekana iwe hivyo pia,lakini jambo kama hili sizani kama atakuwa anamshirikisha mtu mwingine..’akatulia
‘Kwanini rafiki yako umuhisi kihivyo, mlikuwa na mipango gani naye, au alikuwa na mipango gani na wewei,?’ nikamuuliza
‘Yeye alitaka nimpe kazi kwenye kampuni yangu, lakini mimi nisingeleweza kumuajiri mtu kwenye nafasi hiyo bila kupata kibali kutoka kwa mke wangu...’akasema
‘Kwanini usingelimwambia mke wako, kama ana sifa zinazofaa?’ nikamuuliza
‘Ukimjua huyo mtu utafahamu kwanini mke wangu hamtaki, na hata wewe usingelimkubalia rafiki yako amuajiri mtu kama huyo...’akasema
‘Kwani ni nani huyo mtu...?’ nikamuuliza
‘Ni Makabrasha...’akasema na alipotamka hilo jina, nikahisi kama mtu akanigonga na yundo a chuma kichwani mwangu, nikajikuta nikisema kwa hali ya kuchanganyikiwa;
‘Eti nani, my, God, Ma..ma...oh, ni huyu mtu, sasa tumekwisha, ...hapana, sio yeye ...mtu yule nimehamsiki asifa zake, kuwa ana mambo kama hayo, na ....niliwahi kuongea naye siku moja, kama walivyo wanaume wengine, akaniomba urafiki nikamtolea nje, akaniambia bila kuogopa, kuwa ipo siku nitaingia kwenye anga zake, na nitamkubalia tu...’nikasema.
‘Ndio zake hizo, na akitaka jambo mpaka alipate,ana kila mbinu,..’akaniambia.
‘Oh, ina maana ndio kaamua kutumia njia hii, ....mh, sio rahisi kihivyo, ndio kanipata kwa namna moja au nyingine, ,naona nimeishaingia kwenye mtego wake,kwa namna moja au nyingine, lakini,nitapambana naye, kama kweli ni yeye, sikubali...’nikajikuta nikiongea , na mume wa familia akasema;
‘Mimi naona tusipaniki, cha muhimu ni kujipanga, ikishindikana, inabidi tufuate anavyotaka yeye, kwasababu huyu mtu ni hatari, na akitaka jambo lake ni lazima, litafanyika, namfahamu sana toka huko kijijini...’akasema
‘Inaonyesha hili jambo mumelipanga pamoja, kwa kauli yako hiyo,ninakuhisi vibaya, nakuambia hivi, kama na wewe unahusika kwa hili, nikifanya uchunguzi nikagundua hivyo, sitazama peke yangu kwenye hilo shimo, kama ni kuangamia tutaangamia sote, na ujue, mimi sitapoteza sana kama utakavyopoteza wewe.ukumbuke hilo kuwa wewe ni mume wa mtu, na umeolewa...’nikamwambia nikikazania neo `umeolewa, sio kaoa..’ nikiwa na maana yangu.
‘Nalifahamu hilo, ndio maana nimekuja kwako, na nakufahamu wewe ni askari, unaweza kupambana na mtu kama huyu, kwa mbinu zako za uchunguzi na mimi nitatumia kila hali, pesa , na kila njia, ili tuweze kupata mwanya wa kumshinda huyu mtu na mambo mengine yakaenda kama kawaida,...’akaniambia
‘Hili sio swala la uaskari, huu hapa ni utapeli, wa kishenzi, na mbinu kama hizi mwisho wake ni mbaya, sipendi kabisa kujiingiza huko, najua ni nini kitatokea baadaye, ...tamaa ya namna hiyo inaweza kugharimu maisha ya watu, na ukiingia huko, ukanasa kwenye mitegi yao, kuja kujinasua itakuwa vigumu sana, ..haya hebu niambie mlipanaga nini na huyo jamaa yako?’ nikamuuliza
‘Mimi sijapanga kitu na yeye, na ukumbuke kuwa mimi namuhisi tu, lakini sina uhakika kwa ndio yeye,...’akasema
‘Usinifanye mimi ni mtoto mdogo, huwezi kuja na picha kama hii uniambie kuwa wewe hujui ni nini kinachoendelea, ni kitu gani mnataka kutoka kwangu, niambie, moja kwa moja zitaki kuzunguka ..mimi sina utajiro wowote, mnataka nini kutoka kwangu?.’nikamuuliza.
‘Nafikiri hunielewi na huniamini, ngoja nikakutanae na huyo mtu, baada ya hapo nitajua ni kitu gani anakihitajia,...kama ni yeye nitafahamu tu , hata kama anamtumia mtu mwingine, kwa hivi sasa sijui lolote’ akasema
‘Umesema kuwa uliwahi kufanyiwa hivyo, ukatoa pesa nyingi, na nani, ni huyo huyo ?’ nikamuuliza
‘Nikuambie ukweli, yaani sasa nachanagnyikiwa, kwani siku za nyuma, kama miezi tisa iliyopita, nilitakiwa kumlipa binti mmoja pesa nyingi tu, baada ya vitisho vinavyofanana na hivi, sikuweza kufahamu ni nani, ila huyo binti aliniambia kuwa huyo anayeshirikiana naye ni mtu wa usalama wa taifa...’akasema
‘Mtu wa usalama wa taifa!, hapana wewe, ulijueja kuwa ni mtu wa usalama wa taifa?’ nikamuuliza
‘Ndivyo alivyoniambia huyo binti...’akasema
‘Usiwe mjinga, inawezekana ni huyo huyo mtu wako keshaonja asali sasa anataka kuchonga mzinga, naona hapo kuna jambo, nahisi wewe unafahamu zaidi ya hayo...je huyo binti ni nani?’ nikamuuliza
‘Mhh, ni binti mmoja muhuni tu, haina haja kumfahamu...’akaniambia
‘Au ni yule binti wenu wa ndani mliyesema katoroka?’ nikamuuliza na yeye akageuak pembeni,na kukaa kimiya.
‘Sikiliza, kama unataka kushirikiana na mimi kwa hili, unabidi uniambia kila kitu, niambia ukweli, huyo binti ni yule binti wenu wa ndani, na kwanini alitoroka?’ nikamuuliza.
‘Achana na yule binti, yule aliondoka kwa sababu aliiba pesa, na pesa hizo nilikuwa nazo mimi, na sikupenda mke wangu alifahamu hilo, achana naye...’akasema
‘Ina maana huyo binti aibe pesa, na bado ushutumiwe wewe, na uje utoe pesa nyingine, hiyo sio kweli, niamie ukweli, huyo binti aliondoka kwa makosa gani, nahisi kuna kitu ulimfanya huyo binti, na huenda ni uzinzi wako, na ndio maana ukalipa hizo pesa, ...kama ni hiyo tabia, naona wewe hustahili kuwa karibu na mimi...’nikamwambia.
‘Kama huniamini basi,..ndivyo ilivyokuwa, na ngoja nikionana na huyo mtu nitakuambia, vinginevyo, kama unaona huwezi kunisaidia niachie mwenyewe, nitajua ni nini cha kufanya...’akasema
‘Mpaka nifanye uchunguzi, siwezi kukubali upuuzi kama huo, mimi sio kama unavyonifikiria, na ole wenu nikiwagundua, .....mimi nitakubali hata hizo picha zifike kwa mkeo lakini nitahakikisha sikosi peke yangu, sitazalilika peke yangu, nyie mtakosa zaidi na mtaishia jela....’nikamwambia.
‘Ukinitisha mimi utajisumbua bure, sijui lolote...ninakuambia ukweli, sijui lolote hapa nilipo nimechanganyikiwa, nilikuja kwako nikitegemea ushauri na ushirikiano, sasa wewe uanzidi kunichanganya’akasema
‘Niambie huyo Makabrasha mlijuana naye kivipi, ndio umesema mlikuwa wote kijijini, je ilitokeaje mpaka mkawa na usuhuba wa karibu?’ nikamuuliza
‘Yeye mwenzangu alitangulia kidunia na kimaisha, ni mkubwa kuliko mimi, na aliwahi kufika mjini muda mrefu tu, na kutokana na kisomo chake, alikuwa akifahamu mengi, na mjanja sana...nilipenda sana tabia yake ya kujua kila kitu, akawa kama mwalimu wangu...akija kule kijijini, ananismulia mengi, na alipenda sana kusoma vitabu, na moja ya mambo aliyokuwa akinisimulia ni kama hayo...’akasema
‘Hayo yapi?’ nikamuuliza
‘Yakupata pesa kwa matajiri kwa njia hii, ya kuchukua picha mbaya na kuwatishia matajiri, na wanatoa pesa ili siri zao zisivuje...
‘Kwahiyo akakufundisha jisni gani ya kufanya?’ nikamuuliza
‘Hapana, alikuwa kinihadithia hivyo, visa, mimi nilikuwa nikimsikiliza tu, ikatokea nikamuoa mke wangu, na akalifahamu hilo kuwa nimemuoa mke mwenye uwezo, na hakusita kuja kwangu, kuniambia ndoto zake za kupata pesa kwa njia hiyo ya udanganyifu, mimi nikamwambia hilo siwezi kulifanya kwa mke wangu
Aliniambia mimi ni mjinga, nikiichia hiyo bahati sitapata tena bahati kama hiyo..
‘Wewe kwanza umemuoa huyo binti na kumuacha mpenzi wako wa siku nyingi, mnayependana sana, nafahamu kuwa umemuoa kwasababu ya pesa zake, hakuna mapenzi hapo...’akaniambia
‘Hilo unajua wewe, kuna mtu anaweza asimpende huyu binti, wewe unamuonaje mzuri, msomi ana pesa?’ nikamuuliza
‘Niambie ukweli kuhusuhuyo na mpenzi wako wa siku nyingi, ni nani na kweli unampenda sana?’ akaniuliza
‘Mpenzi wangu wa siku nyingi nampenda sana, na yeye anafahamu hilo, lakini huyu ana kitu cha ziada, na mapenzi ya moyoni tu, hayana cha zaidi, mkiingia ndani mtaishia kulumbana, pesa hakuna, kuna raha gani hapo, kwanini nimng’ang’anie mpenzi wa siku nyingi, ambaye ni mlalahoi kama mimi, itafika siku atampata mwenye pesa, atanitosa, tulikaa tukaongea ,tukakubaliana, ni vigumu, lakini tuliona ni bora iwe hivyo...’akaniambia hivyo
Basi kwa upande wa mpenzi wangu tulimalizana hivyo, na aliyekuja kunighasi, na huyo rafiki yangu wa huko kijijini, alipokuwa, akaja na sera zake zile zile, akawa haachi kunisihi nifanya anavyotaka yeye, na mimi sikumkubalia, kabisa, siku moja akaniambia,....
‘Sikiliza nikuambia wewe masikini wa akili, hawo matajiri wanakutumia tu, ipo siku itatokea tatizo, watakufukuza kama hawakujui, kwanza wewe umeolewa,m hujaolewa, kwahiyo wao wameshika mpini, ili ujue hilo, hebu niambie wazazi wake wanakukubali, wamekupokea kwa mikono miwili?’ akaniuliza
‘Nafahamu, lakini ilimradi mimi na mke wangu tunapendana, mimi sioni kwanini kuharibike jambo, wao wana maisha yao na mimi nina maisha yangu, nafahamu kabisa, hawanikubali kutokana na hali yangu, wananichukia mimi na familia yangu kwa umasikini wetu, lakini nina uhakika kuwa mke wangu ananipenda sana, ndio maana sitaki kumuangusha...’akamwambia huyo rafiki yake mshawishi.
‘Basi nikuambie ukweli, hiyo ndoa yako ipo hewan ipo siku itaanguka na kupasuka, ni ikapusuka, huponi, watahakikisha wanakuzamisha kabisa ardhini, wewe huwajui matajiri walivyo, cha muhimu ni kuitumia nafais uliyo nayo ipasavyo vinginevyo, utakuja kunikumbuka, huwenda wakati huo sipo duniani tena ...’akaambiwa na Marehemu, kama alikuwa akimbashiria kifo chake.
‘Mume wa familia aliniambia kuwa yeye hamkujali sana rafiki yake huyo kwa vile anamfahamu tabia yake ya tamaa, hata hivyo jamaa huyo hakuchoka kumshawishi, na kila akipata mwanya, anakuja na habari mpya mpya, na kizushi, kuna wakati anasema aliambiwa kuwa mke wake, anatembea na rafiki yake, amewaona wakiwa wawili wakiingia chumba cha wageni, mimi sikumjali japokuwa iliniuma sana,...’akaniambia hivyo
‘Hebu nikuulize huyo mpenzi wako wa zamani, alikukubalia umuoe huyo binti tajiri?’ nikamuuliza mume wa familia
‘Alikubali, kwa shingo upande, tulikuwa hatuna jinsi, lakini alifanya hivyo, kwa vile, alishampata mwanaume mwenye mwenye nazo, kwahiyo tukaona tukubali ili na sisi tuyajue maisha ya kitajiri, mimi nikamuoa binti mwenye hali nzuri, na yeye akaolewa na mume mwenye nafasi yake, na maisha yakaendelea nikijua kuwa pesa ni kila kitu...’akaendelea kunisimulia mume wa familia.
‘Kwahiyo kwa kauli hiyo inaonyesha kuwa huna raha na mke wako?’ nikamuuliza
‘Ningekuwa nayo ningekuja kwako, ..hilo nalo ni la kuuliza, ..sio kuwa sina kila kitu,kila kitu ninacho lakini sio raha ya kimapenzi,...hilo naona..oh, ndio hivyo, kila mtu na uwalakini wake, ...unafahamu mke wangu hajali kuangalia hisia za wenzake, ndio tatizo lake, yeye anaona utajiri ndio mapenzi yake,...’akaniambia
‘Nikuulize kitu, ina maana wewe na mpenzi wako wa zamani, huwa, mnakutana, mnaonana, au ulipoona na yeye kuolewa, hamuonani tena,ili kulinda heshima zenu, ili msije mkagundulikana kuwa mlikuwa wapenzi na bado mnapendana?’ nikamuuliza
‘Hili swali gani, hilo siwezi kulijibu, maana huko unakokwenda una nia ya kunichimba,huko unapokwenda hakuna maana usiniulize maswali ambayo hayatatusaidia kitu, sanasana ni kukuumiza moyo wako, na kuniumiza mimi pia, mengi yamepita na haya yaliyopo mbele yangu,yataharibu kila kitu,sema utanisaidia au niondoke, .?’akaniuliza
‘Mimi ninakuuliza hilo swali nikiwa na maana yangu muhimu, inawezekana huyo jamaa anashirikiana na mpenzi wako wa zamani, atakuwa anakufanyia hivyo kwasababu maalumu, ’nikawambia.
‘Hiyo hoja yako haina mshiko, yeye anifanyie hivyo ili iweje, ...ili nikose, nimuache mke wangu, nikikosa yeye atapa nini, au ili apate mali niliya nayo mimi, ..na mali aliyo nayo yeye iende wapi, hapo umakosea, hiyo hija yako haina mshiko...’akasema
‘Binadamu anaweza kukutwa na jambo, au kushawishika, au hata mume wake anaweza kumtumia kwa masilahi fulani, huwezi jua, ufahamu wewe upo kwenye sehemu ambayo kila mtu anaimezea mate, na kwa ajili hiyo, utegemee maadui wa nje na ndani...’nikamwambia lakini yeye akatingisha kichwa kutokukubaliana na mimi.
‘Hapana yule hawezi kunifanyia hivyo hata siku moja, ananipenda sana, hawezi kuniumiza, tumeamua iwe hivi, kwa vile tunafahamu wapi tulipotoka, kila mmoja ana mipango yake ya kimaisha na mwenza wake,tulishawekeana ahadi kuwa tusiingliane...’akasema mume wa familia.
‘Ina maana ulivyoniambia mimi kuwa unanipenda ulikuwa unanidanganya, ok, sawa nimekuelewa, ndio zenu wanaume, nimeshakuelewa, kuwa nia yako ni kunitumia, na kuutumia mwili wangu, ...na kwahiyo sasa kazi yako imekwisha, naomba tusijuane, au kwasababu ya hili ndio umekuja kwangu?’ nikamuuliza
‘Sio kwamba sikupendi, mimi nakupenda, lakini kila mmoja nampenda kwa nafasi yake, mke wangu nampenda kwa nafasi yake, na ni mtu muhimu sana kwangu, ndio maana sitaki nimkose kwa hali na mali, na wewe nakupenda kwa nafasi yake, lakini mpenzi wangu wa zamani penzi lake ni la asili, huwezi kulilinganisha na kitu chochote, na kama ikiwezekana, kama ikiwezekana...mmh, lakini najua hiyo imeshatoka,..tuyaache hayo..kama yalivyo’akaniambia na mimi nikafahamu kuwa huyu mtu anampenda sana huyo mpenzi wake wa zamani, na huenda mapenzi yao bado yanaendelea kwa siri, nikapania kumjua huyo mtu ni nani....
‘Ni nani huyo mpenzi wako huyo wa zamani?’ nikamuuliza.
NB: Ni nani huyo mpenzi wake wa zamani, tukutane sehemu ijayo mungu akipenda tuombeane uzima na changamoto za kimaisha.
WAZO LA LEO: Wapo wana ndoa wapo kwenye ndoa kwasababu ya mali, lakini kisiri wana wapenzi wao wa nje, hilo ni kosa kubwa sana, huko ni kumsaliti mwenza wako, tukumbuke kuwa mapenzi ya kweli yanatoka moyoni, tukijidanganya kuwa tunapenda eti kwasababu ya pesa, au mali, ipo siku hivyo vitu vyote vitakwisha, je ndio mwisho wa mapenzi yenu. Kama mumeamua kuoana kwasababu ya mali, au sababu fulani, basi jifunzeni kupendana kiukweli. Mungu atawasaidia na mapenzi yenu yatakuwa na baraka.
Ni mimi:
emu-three
2 comments :
Wapendwa X mass Njema na M3 ucsahau kutupostia mkuki kwa nguruwe..
Hi miram heri ya xmas na mwaka mpya sio siri hii simulizi inabamba sana yani wee acha tu pia nakupongeza kwa kutupa muendelezo kila kukicha hujawa mvivuu Mungu aendelee kukutia nguvu diary izidi kutufunza kwa visa na mikasa ya maisha
Post a Comment