Mwenyekiti alituliza kikao baada ya kuona kuna majibishano
makali kati ya rafiki yangu na mume wangu, kiasi kwamba kama asingeliingilia
kati yangelizungumzwa mengi ambayo hata hayakustili kuzungumzwa kwenye hicho
kikao. Wawili hawa walikuwa wakitupiana maneno makali, wakajisahau kabisa kuwa
humo kwenye kikao wamo wazazi, watu wa kuheshimika, na kama hawo wazee
wasingelikuwepo hapo, wengi walitamani hawa
watu wawili waachiwe wapashane mpaka hamu yao iwaishe.
Ilivyoonekana hayo yote yalitokana na kutokukubaliana kuhusu mtoto.Wawili hawa walishindwa kukubaliana hapo kabla
hawajafika kwenye kikao, inaonekana walikutana kabla li wakubaline kuhusu taratibu za mtoto, na
moja ya jambo kubwa , ni jinai gani wangelificha ukweli, na ilitakiwa mama
mtoto akane kabisa kuwa mtoto huyo hajazaa na mume wangu. Lakini hilo lilileta
ushindani kwani wakikana hivyo, ina maana mtoto atakosa haki zake za msingi.
Mume akiwa anajua kuwa atashinda, kwa kutumia mkataba wa
bandia, alitoa hoja kuwa mkataba unampa nafasi ya yeye kufanya atakavyo,
kwahiyo hilo halitakuwa na tatizo,yeye kwenye kikao atakana kuwa hana mtoto, na
baadaye atageuza hiyo kauli yake akitumia mkataba huo wa bandia. Rafiki yangu
alisema kama ni kukana, iwe hivyo moja kwa moja, mtoto wake, asijulikane kabisa
kuwa baba yake ni m ume wangu. Kila mmoja akawa na msimamo wake.....
Ndio maana hata mume wangu alipofika hapo kwenye kikao
alikuja na kauli hiyo, ya kukana kuwa hana mtoto mwingine, kauli hiyo ingekuwa
na uzito kama shahidi wa kwanza wa yule binti asingelikuwepo, lakini kuja
kwake, kulisababisha hayo yalijificha yafichuke, na kuja kwake, kungempa mtoto
wa huyo binti nafasi ya kutambulikana zaidi ya mwingine, na huenda kikao
kingeamua kumpa haki zote huyo mtoto, mama wa huyo mtoto mwingine akashindwa
kuvumilia.
Pili mume wangu alitaka , pamoja na kukana kwenye kikao kuwa
huyo mtoto hajazaa na yeye, lakini kwa siri yao wawili na mkataba wao wa siri,
wao waje kumtambua huyo mtoto, na haki zake ambazo zilikwisha andikwa kwenye
mkataba mwingine wa siri, na kwa vile wao
walijua kuwa ule mkataba wao waliogushi unampa mamlaka mume ya kufanya
apendavyo, baada kikao angeliweza kumtambulisha huyo mtoto kwangu na kuomba
msamaha, na mimi niwajibike kumkubali na kumsamehe....
Lakini kutokana na mkataba wetu wa awali kuonekana, mkataba
ambao ulikuwa ukimpa haki kila mmoja, mke na mume, hakuna aliyepewa mamlaka ya zaidi ya kufanya apendavyo, kila
jambo lilihitaji kukubaliana na kushauriana, na kama mmoja akikiuka masharti ya
ndoa, hasa hayo makubwa ya kusaliti ndoa, basi huyo mkosaji, anawajibika,
kukosa kila kitu, na ndoa inakuwa haipo tena.
Rafiki yangu alipewa kibali cha kuongea na mwenyekiti, akawa
anatoa maelezo yake, japokuwa mimi akili yangu ilikuwa mbali sana, lakini
niliweza kumsikiliza, rafiki yangu alisema;
‘Nitatoa maelezo yangu katika sehemu kuu mbili, ya kwanza ni
ukweli kabla sijapata mtoto na sehemu ya pili yenye ushahidi mnzito, ni ukweli
baada ya mimi kjifungua, naomba muwe watulivu, ili niweze kuyasema yote
niliyoyakusudia kuyaongea leo hii...’akasema na kuniangalia mimi.
‘Mimi ninaamini kwamba kila jambo huja kwa minajili fulani,
na hili la kupata mtoto huenda na kweli limetokea ili iwe fundisho sio kwangu
tu, na hata kwa wale wote lilowagusa kwa namna moja au nyingine. Ni changamoto,
ambayo sitaweza kuisahau katika maisha yangu, ....’akasema
‘Mimi nilishajipangia kuwa huyu mtoto, nitamzaa na itakuwa
siri yangu mimi mwenyewe, na sikutaka
awe na baba, japokuwa huwezi kuzaa mtoto bila baba. Kauli hii ya kuwa mtoto
huyu hana baba niliwahi kumwambia huyu mwanaume aliyefanikiwa kunipa huu
ujauzito, siku nilipopewa kibali kutoka kwa mshauri wangu, haya nitayaeleze
kinamna, ..naomba mnielewe hivyo, sitayaeleza kwa undani sana, ili nispoteze
muda.
Japokuwa nilipanga iwe hivyo, kuwa mtoto ni wangu, na hana
baba, lakini mume wa familia alipogundua kuwa nimejifungua, akawa wa kwanza
kufika hospitalini, na alipomuona tu, ilikuwa kama mtu aliyepagawa, akasema
huyo ni mtoto wake, hakuna ubishi,...nikaharibu kila kitu, na nkajua sasa mambo
yatakwenda kinyume na matarajio yangu,
na makubaliano yangu na mshauri wangu kuwa nikizaa hata mume aliyenipa mimba
ikiwezekana asifahamu.
‘Mimi ninahisi kilichomfanya mume wa familia ang’ang’anie
sana ni kwa vile nimepata mtoto wa kiume, na yeye kwa kauli yake mwenyewe,
alikuwa akitaka mtoto wa kiume, maana watoto alio nao na mke wake , wote ni wa
kike,...mimi sikuyajali hayo kwani mipanglio yangu ilikuwa nizae mtoto, na huyo
mtoto awe ni wangu wote hata nikiandikisha jina lake kwenye cheti chake,
lisomeke jina lake,na ubini wa baba yake, liwe ni jina langu kwa herufi yangu
ya mwanzo, halafu jina la tatu liwe la baba yangu mzazi ndio nilivyotaka iwe hivyo
Lakini baadaye tulipokutana mimi na mwanasheria wao na mume
wa familia, mume wa familia akasema hilo halikubali, mtoto huyo ni wake, kwani
yeye ndiye mume aliyeweka mbegu, ana haki ya kufanya apendavyo kwa huyo mtoto,na
hata kisheria yeye kama baba ana haki na huyo mtoto , na pia huyo mtoto
aandikwe kwa ubini wake, ili atambulikane kuwa yeye ni baba yake, na hili
atalifaya nipende au nisipende. Utaona mbinu gani walitumia baadaye akiwa na
mshirika wake mkuu, kwenye ushahidi wangu wa pili,
Mpaka hapo mimi na mume wa familia tukawa hatukuelewana hadi
muda wa kikao ukawa umeshafika, akaona yeye aje kwenye kikao, akisema akifika
kwenye kikao atahakikisha uwezo wote wa kifamilia anao yeye, na alisema mkataba
alionao yeye unampa hiyo nafasi, alinionyesha huo mkataba, lakini niliuona una
utofauti, na jinsi nilivyokuwa nikifahamu mimi kutoka kwa rafiki yangu ,
sikuwahi kuusoma huo mkataba wao wote kabla, lakini kwa kauli ya rafiki yangu,
mkatana wao, ulikuwa hauruhusu mume au mke, kujitwalia madaraka bila
kumshirikisha mwenzake.
Na nakumbuka rafiki angu huyo aliniambia kuwa kama mmoja
akimsaliti mwenzake, na ukapatikana ushahidi, ama wa kuona au kudhihiri, kwa
mfano kupatike mtoto, ambaye ni ushahidi tosha, basi nijuavyo mimi, ni kuwa
ndoa hiyo imeshavunjika, na muhusika hana chake, sasa niliona ajabu akiniambia
kuwa yeye kwenye huo mkataba alio nao yeye ana mamlaka, ya kufanya apendavyo
kama mume wa familia...
‘Kuhusu huo mkataba wao, sikuwa naufahamu kabla, kwani
unaweza kusema kuwa nilifanya makusudi ili nipate mtoto na huyo mume, ili ndoa
yao ivunjike, ili mimi nije kuchukua nafasi ya mke wa mume wa familia, na mali
iwe imeshaandikiswha kwa mtoto wangu,..hapana...sikuwa na tamaa hiyo na hilo
halikuwa ni lengo langu, naomba mniamini kwa hilo.
Mimi nilikuja kuufahamu huo mkataba wao, walio nao, kipindi
waliponiita nije kwa dharura,...nikaonyeshwa na kuambiwa kuwa nikikubaliana
nao, basi nitapata mafanikio mengi, ....ni nini nahitajika kukubaliana nayo,
naona hayo nitayaelezea kwenye sehemu ya pili ya ukweli wangu. Mimi
ninachokumbuka sana, ni kauli ya rafiki yangu ambaye alinielezea kuwa mume wake
asingeliweza kusaliti ndoa yake, kwani anafahamu ugumu wa mkatba wao ulivyo.
Akimaanisha mkataba wao wa awali, lakini mkataba niliokuja kuonyeshwa baadaye
ulikuwa hauna vipengele hivyo vigumu.
Mume wa familia kwa kujiamini aliniambia kuwa akitoka huku
kwenye kikao atakuwa kamaliza kazi, kila kitu kitakuwa kwenye miliki yake,
kwahiyo kinachofuatia ni kumwandikisha mtoto kama mmoja wa warithi wake..na
ikizewekana kama mimi nataka nitakuwa nyumba yake ndogo....uone jinsi
alivyonizarau, eti mimi niwe nyumba yake ndogo. Mimi nilimwambia hilo halipo,
yeye aende akapiganie ndoa yake huko kwenye kikao, na kama akifanikiwa basi
menginE tutayamaliza kinamna ambayo mimi nitarizika nayo, lakini nilifahamu
kabisa kuwa baada ya hicho kikao, huyo mume atakuwa hana chake....’akasema
‘Ni kweli kuwa mtoto ni lazima awe na baba yake, lakini kwa mazingira
niliyompatia huyu mtoto sikutaka kuwe na mtu anayeitwa baba, ukumbuke kuwa
mimba hii niliipata kutoka kwa mume wa mtu, na niliipata baaada ya kupata
ushauri kutoka kwa rafiki yangu mkubwa japokuwa
badaye rafiki yangu huyo alinikana kuwa yeye hakunipa ushauri wa mimi kutembea
na mume wake,...muone jinsi gani sisi wanadamu tulivyo, ...’akatikisa kichwa
kama kusikitika.
‘Rafiki yangu kwa kauli yake mwenyewe alinishauri kuwa
nipate mtoto kwa kila hali,hata ikibidi nitembee na mume wa mtu, leo hii
ananiambia kuwa mume wake, sio mume wa mtu, yeye ushauri wake ulilenga kwa waume wengine sio kwa mume wake, eti kwa vile
mimi ni rafiki yake, na ni sawa na mdogo wake..lakini mimi hayo sikuyajua
kabla..ndio mimi ni rafiki yake lakini haoni kuwa kwa kuniambia hata mume wa
mtu, basi kwa urafiki wetu wa karibu, mume wange ingelikuwa ni bora zaidi,
kusibitisha kuwa sisi ni marafiki wa kweli kweli,..sijui, ndivyo mawazo yangu
yalivyokuwa hivyo...mnaweza kusema najitetea tu kwa vile imetokea hivyo..
‘Huenda nilifikia uamuzi huo kwa vile niliwapenda sana watoto
wake, au huenda nilimpenda sana mume wake, lakini nguvu za ushawishi ambazo
mimi nakiri moyoni,zilitokana na kauli yake, kauli kutoka kwa rafiki yangu, kuwa
nitembee, hata na mume wa mtu..na pia ni kutokana na ushawishi wa mume wake
mwenyewe, kunishurutisha kwa kila hila...sisi wanawake ni rahisi sana
kudanganyika....
Baada ya tukio hilo
urafiki wetu wa mimi n a rafiki yangu huyo uligeuka na kuwa uadui na mimi
nikaonekana mtu mbaya sana, na nilistahili nipewe adhabu ya kuzalilishwa na
kuharibiwa na watoto wakihuni, na kweli siku niliyofika tu kutoka Ulaya,
nikatumiwa hawo watoto wa kihuni, kwa lengo hilo, lakini walishindwa kufanya
hivyo, baada ya mbinu zao kugundulikana na polisi, vijana hawo sasa wapo jela,
na nitahakikisha wanaozea huko, kama mna nia njema na wao muende mukawatoe.wao wamechezea
kusipochezewa, hawajui kiini cha yote hayo,wanachojali ni pesa, mimi sio kama
wanavyofikiria wao....’akasema.
‘Watu mtajiuliza ni nani aliyenishauri hivyo, kuwa nikazae
kwa vile umri wangu umeshapita, ambaye alinishauri kuwa nimtafute mwanaume
yoyote nitembee naye ili nipate mtoto, hata kama huyo nitakayetembea naye ni
mume wa mtu,...?’ akatulia, alikuwa kama anawauliza watu, na akageuka
kuniangaiia mimi, na mimi nilikuwa namuangalia tu, sikusema neno.
‘Huyo aliyetoa ushauri huo ni rafiki yangu mpenzi, mke wa familia , kama
ni uwongo, mulizeni mwenyewe kama sio yeye aliyenishauri hivyo, ..hebu
muulizeni mume wa mtu ni nani, au labda aseme kuwa kauli yake haikumaanisha
mume wake, kuwa hakutoa ufafanusi wa
kutosha, kuwa aliposema mume wa mtu, hakumaanisha mume wake, mume wake, ana
sifa ya ziada ya mume wa mtu, labda yeye sio mume wa mtu, ni mume wake...sijui
kama ingelieleweka, hapo. Lakini angeliniambia hivyo mapema, kuwa nikisema mume
wa mtu, usimguse mume wangu, ni dhahiri kuwa hata mimi nisingelikuwa karibu na
mume wake, ningeliangalia hilo onyo zaidi....
Lakini hakuwahi kutoa hilo anagalizo, yeye akanishauri
hivyo, kuwa nitembee hata na mume wa mtu ili nipate mtoto, sasa kumbe mwenzangu
akitendewa kwa mume wake itauma kiasi hicho, mimi sina kosa, sikujua hivyo, nilichofanya
ni kufuata ushauri wake, na mahali pema nlipopaona ni kwa mume wake, je kwanini
nilipotembea na mume wake ikawa ni taabu, je hawo wengine sio waume , kama
alivyo mume wake, wao ni nguruwe, maana wanasema mkuki ni kwa nguruwe tu...kwa
nguruwe, haumi, lakni mkuki kwa binadamu ni mchungu, unauma eeh...pole sana
rafiki yangu na samahanai sana kwa hayo yaliyotokea...’akasema rafiki yangu akiogopa
kuniangalia mimi, hakufahamu jinsi gani nilivyokuwa nikiumia.
‘Ndio maana sikutaka hata mtoto huyu ajulikae kabisa, kama
ingelikuwa ni uwezo wangu, ningelimlea huko Ulaya, mpaka awe mkubwa, nimsomeshe
huko huko naa kiwa mkubwa nimsomeshe kiini cha yeye kutokuwa na baba mpaka anielewe
, hilo kwa Ulaye angelinielewa, ni kwani nilifanya hivyo, huko ni jambo la kawaida tu,
Mtu aliyemuona kwa ukaribu sana pale nilipojifungua ni mume
wa familia, na mume wa familia moja kwa moja akatambua kuwa ni damu yake, na wa
pili, aliyekuja kumuona ni mke wa familia...’hapoa akatulia kidogo. Uone
mitizamo ya watu hawa wawili.
Cha ajabu kabisa mke wa familia japokuwa alimuona mtoto
anafanana na watoto wake, watoto wake, wanaofanana na baba yao, yeye alishindwa
kabisa kutokumshuku mume wake, kwa vile alikuwa akimuamii sana mume wake,
hakujua kuwa mume wake, ni msaliti asiyethaminika, wakati yeye anamuamini mume wake, mume wake alikuwa
akimcheka kwa nyuma kuwa mke wake ni mjinga, hana akili ya kufikiri, ..hayo
siyasemi kutoka mdomoni kwangu kwa nia ya uchochezi, ...nayanukuu kutoka kwa
kauli ya mume wake, akiyatamka mbele yangu, alivyokuwa akiniambia
Aliniambia kuwa mke
wake anavyomuamini amekuwa kama mjinga fulani asiyeweza kuona mbali kwahiyo tunaweza kufanya
lolote tuwezavyo, na wala asishituke, na ndivyo ilivyokuwa baada ya kupewa
kibali kile siku ya kwanza, siku ambayo ilifungua ukurasa mwingine ambao
sikuwahi nao kabla, ukurasa wa kutembea na waume za watu. Mimi kwa ujumla
sikuwa na tabia hiyo..
Siku aliponitamkia rafiki yangu kuwa nikatafute hata mume wa
mtu nitembee naye ili nipata mtoto, ndio siku nilipoanza kuingiwa na wazo hilo
la kufanya hivyo, kuwa kumbe waume za watu inawezekana, japokuwa kiujumal watu
niliokuwa nikiawapenda walikuwa ni waume za watu, lakini nilikuwa naogapa sana
kutembea nao, nikiwaogopa na kuwaheshimu wake zao, japokuwa ni wengi waliokuwa
wakinitaka.
Rafiki yangu aliponishauri hivyo, nitafute yule ambaye
nampenda na ninaweza kuzaa watoto, au mtoto nitayempenda, akili yangu ikadondokea
kwa watoto wake, ..ni kweli bila kuficha watoto wake nawapenda sana, hata yeye
mwenyewe analifahamu hilo,..
Je ningeliwezaje kutembea na mume wake, hilo lilikuwa swali
gumu sana kwangu, na sikutarajia kuwa ningeliweza kufanikiwa kirahisi namna
hiyo, na sio kwamba mimi ndiye niliyekwenda kumtongoza huyo mume, hapana,
..mume huyu alishaanza tabia hiyo ya kunitongoza siku nyingi, ila mimi nilikuwa
namtolea nje, nikijua kuwa yeye ni mume wa rafiki yangu na nilikuwa namtambua
kama shemeji yangu, ..ilikuwa vigumu sana kumkubalia ...lakini nahisi kama
ilipangwa iwe hivyo, ili sote tupate fundisho.
Niwaambie ukweli, mke anapokuwa na mdogo wake ndani, au mume
anapokuwa na mwanamke mwingine tofauti ndani, nafsi zao hujenga tamaa, na kama
huyo mtu wa kike asipokuwa na ushujaa wa kujiamini, na kumkwepa huyo mume,
basi, ni mtihani, ...wengi wanashindwa huo mtihani, na utaona wanaitana shemeji
lakini mke akiondoka yanayotendeka huku nyuma ni mengine. Tujaribu sana
kuwashibisha waume zetu, ili wasiwe na kisingizio,kama tuna wadogo zetu, au
hata yoyote anayejulikana kama shemeji, na akawa na ukaribu na mume wako,
uakuja kujuta, wakati huo umeshachelewa...nasema hili kwa uzoefu wangu mimi.
********
Turudi nyuma kidogo, siku nilipoanza mazoea na huyu
bwana,maana msione anayatamka maneno hayo ya kashifa mkafikiri yeye ni
mtakatifu, msimuone anatembea kichwa chini mkafikiri yeye ni kondoo, sio kweli,
mimi namfahamu sana pengine hata mnavyomfahamu nyie.
Ofisi yangu ninapofanyia kazi ipo karibu sana na ofisini
kwake, na katikati yetu, kuna hoteli kwahiyo nikitoka kwenda kula chakula cha
mchana, ninapita kwenye ofsi yake, sasa bwana huyu alikuwa kama ananisubiria,
kila nikipita hapo yeye anakuja kwa nyuma, au tunaongozana , hata kama hana
njaa, atakuja kukaa karibu yangu, akiniongelesha, mimi kama mwanamke
nilishamfahamu nia na lengo lake ni nini, lakini sikutaka kumzalilisha, na watu
wanaonijua tabia yangu, ningelifanya hivyo, na asingeliweza kunifuata futa
tena, lakini nilimstahi kwa vile ni shemeji yangu.
Alianza mapema tu kunitaka, akaanza kunielezea mengi ya
nyumbani kwake, jinsi anavyoishi na mkewe, jinsi gani anavyopata taabu, hapati
yale yaliyomuhimu kutoka kwa mke wake,kwahiyo, kama anavyodai yeye, ndicho
kinamtuma afanye yale ambayo hakutakiwa kufanya,kama mume wa familia, kwa mfano,
yeye kwa siri sana, alikuwa akitongoza wahudumu wa hiyo hoteli, wengi
hawafahamu huenda hata rafiki yake mkubwa hafahamu hilo, lakini mimi nafahamu,
kwa kinywa cha mume wafamilia, aliwahi kuniambia, na nikahakikisha kutoka kwa
hawo wahudumu,...
Basi yeye akawa ananivuta kwa njia hiyo, na mwisho wake,
akaniambia wazi wazi kuwa ananipenda, na mimi mwanzoni nilichukulia kuwa huko
kupenda hakuna maana hasa ya kupenda, bali anataak kusema anautamani mwili
wangu, si unafahamu tabia za wanaume, ....wana mbinu nyingi za kuwaingia
wanawake, na huyo alifikia kuniambia kuwa toka aliponiona kwa mara ya kwanza,
amekuwa akipata shida sana,akili yake haitulii kuniwaza, ..
'Na alifikia kusema kuwa angelifurahi mimi nikachukua nafasi ya
mkewe, ...hayo aliyatamka kwa kinywa chake mwenyewe, na usipokuwa na akili ya
kutafakari, utafikiria ni kweli, lakini kauli kama hiyo, sio wewe peke yake
unayeambiwa, huenda wewe ni wa kumi , au zaidi, ...kama mwanamke unatakiwa
uyajue hayo, mimi nilijua ni maneno ya wanaume wakiwa na tamaa zao...nikajitahidi
kumshinda kwa hoja, na kwa hekima.
Alipoona ameshindwa kwa mbinu hizo, na mara nyingi akiongea
hivyo huwa nimetulia namsikiliza, akaanza kuja na maneno ya moja kwa moja kuwa
ananitaka, nikaona sasa amekwenda mbali, nikampasha ukweli, kuwa asinione mimi
nipo karibu naye, na asinione mimi namsikiliza tu akaniona mimi ni muhumi,
nilimwambia wazi wazi kuwa mimi nawaheshimu sana waume za watu, na sitatembea
na mume wa mtu abadan.
Kauli yangu hiyo ilimvunja nguvu, kwa kiasi fulani, na
haikupita muda nikamuona akianza kulewa kupita kiasi, na nilipomuuliza kwanini
anafanya hivyo, akaniambia anafanya hivyo kwa vile mimi nimemkatalia ombi lake
na ananipenda kiasi kwamba hawezi kukaa mbali na mimi, na anapenda kila siku
niwe naye, na zaidi anipate mimi, kimapenzi, na njia peke yake ya kuondoa
mawazo ni kulewa..muulizeni mwenyewe hakuniambi hayo..’akasema rafiki yangu
akimwangalia mume wangu ambaye alikuwa akicheka kwa dharau, utafikiri
linaongewa jambo la maana sana kwake, hakufahamu jinsi gani nilivyokuwa naumia.
‘Basi akawa analewa kiukweli, mwanzoni nilijua ni mbinu
zake, tu, lakini akawa analewa mpaka anakuwa ni mtu wa kubebwa, na wakati
mwingine tunakuwa pamoja, mimi sinywi kihiyo, kwahiyo ikawa tunafanya kazi ya
kumbeba mimi na ndugu yake, na akilewa ndio anabwabwaja ukweli, kuwa kulewa
kote ni kwasababu yangu,....anasema siku nikimkubalia tu ombi lake ataacha
kabisa kulewa.
‘Hali hiyo ikawa na mimi inanitesa, kwani kimoyoni kiukweli,
nilitamani sana nifany e hayo anayoyayataka yeye, nilipenda sana, nimtimizie na
ikiwezekana awe ni mpenzi wangu, nafahamu kuwa kumpata yeye kama mume wangu haiwezekani
kwa vile yeye ni mume wa mtu lakini mimi ningeliweza kuwa mpenzi wake wa siri,
au nyumba yake ndogo, kuna muda nilikuwa naingiwa na ibilisi wa kuwazia hivyo,
unapokuwa huna mume, unaweza kufikiria mengi, na hizo ni ndoto za wwalio wengi,
ambao hawajaolewa,kama mimi.
‘Nilijaribu sana kumfanya rafiki yangu anielewe kuwa mume
wake yupo hivyo,kuwa ana njaa, ya haki yake ya ndoa, lakini kila nilipotumia
lugha ya busara kwake, niliona kama ananiona mtoto mdogo nisiyejua mambo ya mke
na mume kwahiyo nisubiri nikiolewa nitayafahamu, basi mimi nikaona niyaache
yaendelee kama yalivyo, na nikajaribu kumkwepa mume wake, kwa kadiri ya uwezo
wangu lakini ilikuwa ngumu.
Siku nilipoongea na rafiki yangu na kunitamkia yale maneno
kuwa nitembee hata na mume wa mtu, niliona kanipa kibali, lakini mimi kama
mwanamke nisingeliweza kumwambia moja kwa moja mume wa mtu kuwa mke wako kasema
hivyo...ila ikatokea siku hiyo hiyo alipotamka hayo maneno, kukawa na sherehe,
na mume wa familia kama kawaida yake akazinywa pombe kama anashindana, na mimi
siku hiyo sijui ni kwanini na mimi nikanywa tofauti na siku nyingine....moja
likazaa jingine, tulijikuta tupo kwangu,...na usije ukasema nilipanga mimi iwe
hivyo, hapana, na wala sikujua kuwa itatokea hivyo, ..ilikuwa hivi
Baada ya kunywa kwenye hiyo sherehe na tukawa hata kutembea
inakuwa shida, aliyefanya kazi ya ziada kutusaidia alikuwa mdogo wa mume wa
familia, alituchukua hadi nyumbani kwangu, tulipofika kwa vile nimelewa, nikawa
sijui ninachokifanya, tukanywa tena,na kilichofuata ni kutimiza yale ambayo
niliyokuwa nikayapiga vita siku zote,..sikujijua hadi ilipofika usiku wa
manane, nikatambua kuwa nimelala na mume wa mtu. Hapo moyo ukashituka, na
kuanza kuogopa, ..
‘Nilitoka na kumuona mdogo wa mume wa familia akiwa kalala
sebuleni, nikamuamusha na kumuomba afanye haraka amchukue ndugu yake waondoke,
maana sitaki alake kwangu, ilikuwa kazi kumshawishi, lakini baadaye waliondoa,
na hapo ikawa ndio mwanzo wa mahusiani yangu na huyu mume wa familia, nikawa
siogopi tena, kama ilivyokuwa mwanzoni, na kwa vie nilikuwa nimesharuhusiwa
kinamna na mshauri wangu, ikawa sasa kila tukipata mwanya nautumia ipasavyo, na
ombi likatimia, nikapata hiyo mimba...’hapo akatulia na kumwangalia mwenyekiti
ambaye alikuwa mara kwa mara akiandika kitu kwenye makabrasha yake kama vile
ananukuu hayo yanayoongewa.
‘Kipindi cha ujauzito kilikuwa kigumu sana kwangu,
nilijitahidi sana kujizuia, na kujificha ili watu wasifahamu kuwa nina mimba,
ukizingatia kuwa mimi sina mume, nilichofanya ni kuvaa manguo mapana, na
kutokuonekana kwenye kadamnasi za watu, nashukuru kuwa kipindi chote hicho,
hakukuwa na kazi kubwa zilizonihusu mimi kwa bosi wangu, na kama zilitokea
niliweza kuwapa wasaidizi wangu, wakazifanya na kwahiyo sikuweza kukutana na
mshauri wangu ambaye pia alikuwa ni bosi wangu, kwahiyo sikuwa na wakati mgumu,
wa kujieleza, na siku zikaenda na hauchi hauchi , miezi nane ikafika,
Nilizaa nikiwa na miezi nane, na mambo yakaanzia hapo, na
pamoja na furaha ya kupata mtoto, lakini ilifikia mahali nikaanza kujuta, kuwa
kumbe nilichukulia mambo hayo kwa haraka, huenda sikumuelewa rafiki yangu, lakini
hata hivyo, nisingeliweza kuyafanya hayo kama isingelikuwa ni kutokana na
shinikizo la huyo mume wa familia, najua wengi watasema mimi ni mtu mzima, ningeliweza
kupima kila jambo kwa unagalifu, ni sawa....lakini tuangalie na upande mwingine
wa shilingi’akaniangalia mimi na mimi nilikuwa nimemkazia macho.
‘Ni kweli kwa umri wangu huu, mwanaume hawezi kunishika kwa nguvu,
tungelipambana naye hadi hatua ya mwisho,lakini hata hivyo siweri kusema kuwa hayo
niliyotenda niliyatenda kwa hiari yangu mwenyewe, kama ni hivyo kwanini sikuyafanya
hayo kabla,hii inaonyesha kuwa kulikuwa na kichocheo, kilichonisukuma mpaka
kuona kuwa nikitenda sio kosa, ...sio rahisi kuelewa hilo kwa sasa...’akasema
na kuinama chini.
‘Hata hivyo, ukiangalia kwa namna nyingine, mwanaume ndiye kisababishi
kikubwa, kwani hata kabla sijapata kibali cha kutembea naye, mume wa familia
alishaanza kunitaka kwa kila hila,kuna wakati kweli akiwa amelewa huwa alikuw
akaitumia nguvu, ningelifanya nini mimi, nashangaa mimi hapa kuitwa
Malaya,..jamani mimi na yeye ni nani Malaya, huo ndio ukweli wangu wa kwanza,..
Huo ndio ukweli wangu wa kwanza kama nitaruhusiwa nipo
tayari kuelezea ukweli wangu wa pili,
yale yaliyotokea baada ya mimi kujifungua,
ni mambo gani makubwa yaliyotokea, hadi kufikia kifo cha Makabrasha,
nitawaeleza kila kitu, ili mjue ni nani mbaya wenu...’akasema na kumwangalia
mwenyekiti, na mwenyekiti angaalia saa, na kuinua simu yake...
NB: Naona tushie hapa, tusubiri sehemu inayokuja, je ndio
itakuwa hitimisho, au bado mambo yanaendelea..tuzidi kuwemo.
WAZO LA LEO:
Ushauri tunaotoa kwa wenzetu, uwe wenye hekima, ukilenga yale ambayo hata wewe
ungelishauriwa ungelifanya hivyo hivyo. Tusitoe ushauri ambao ukija kutendewa
wewe hutakubali, tukumbuke sote ni binadamu, na sote tunahali sawa za kuumia,
pale linapotokea tatizo au kutendewa
kile kisichofaa.
Ni mimi:
emu-three
3 comments :
Ey there... miriam I presume thats your name. M sorry my Kiswahili is a bit rusty but your entries r just heavenly. I recently started reading your posts and I cant get enough. 1 question though isn't there a way or a link that will take me all the way to the beginning of ur first entry?
Ey there... k so 1st let me apologise because my Kiswahili its a bit rusty. With that being said, I think your diary entries are just heavenly. I recently started reading your posts and I can't get enough of them. 1 question though myb you can assist me, isn't there a link or somewhere that I can click to go to your 1st entry?
Ey there... miriam I presume thats your name. M sorry my Kiswahili is a bit rusty but your entries r just heavenly. I recently started reading your posts and I cant get enough. 1 question though isn't there a way or a link that will take me all the way to the beginning of ur first entry?
Post a Comment