Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, November 19, 2013

Mkuki ni kwa Nguruwe-31


Ilikuwa siku maalumu ya kupokea taarifakutoka kwa watu wangu, nilikuwa nimewapa kazi maaumu hawo watu wangu ninaowaamini, na nilitarajia kupata matunda mazuri, kwani wote nawafahamu walishawahi kunifanyia kazi zangu nyingi, kwa uhakika zaidi. Na aliyekuwa wa kwanza kuja kutoa taarifa ni yule niliyempa kazi ya kuchunguza jinsi gani mIkataba yangu ulivyopotea hasa ule kwa kule ofisini.

‘Kutokana na uchunguzi wangu, mtu aliyechukua huo mkataba atakuwa ni mtu wa humo humo ndani, hakuna mtu tofauti aliyeonekana kuingia ofisini kwako, au mtu kati ya watu tunaowashuku aliyeonekana akikaribia hiyo ofisi yako,...kwahiyo huyo aliyefanya hiyo kazi atakuwa ni mtu wa ndani...’akasema

‘Hakuna mtu yoyote ambaye ninayefahamiana naye, aliyeweza kuonekana maeneo ya ofisini, siku zote nilizokuwa likizo?’ nikamuuliza

‘Rafiki wa mume wako, alionekana mara kwa mara, lakini alikuwa kafika kwa shughuli zake maalumu, na mara nyingi, aliishia mapokezi, na hufika mara kwa mara kwa ajili ya kufuatilia malipo yake, au kaitwa kwasababu ya mgonjwa, hakuonekana kabisa kukaribia ofisi yako....’akasema

‘Na mwingine aliyeonekana, ni....rafii yako, kipindi alichofika toka huko alipokuwa akisoma, lakini hata hivyo, hakuingia kabisa ndani ya ofisi kuu, alikuja kuulizia tu kama upo, alipoambiwa haupo, akaondoka....’akasema

‘Kwahiyo hakuna mtu yoyoye mwingine ambaye tunayemshuku, aliyeonakana akiongoea na mfanyakazi wangu wa usafi, na kutunza fungua?’ nikamuuliza

‘Tatizo ni kuwa huyo mfanyakazi wako anaongea na watu wengi sana, sasa sio rahisi kuhisi yupo ni yupi, hata nilipotumia mbinu za ziadi kupata taarifa kwake, ilionekana kama tunamshutumu mtu ambaye hajafanya jambo kama hilo, nina uhakika kama ni mtu aliingia, yeye atakuwa hajui kabisa..’akasema.

‘Sasa kwa uchunguzi wako, hakuna  yoyote uliyemuhisi, ambaye anaweza kufanya hivyo?’ nikamuuliza

‘Mwanzoni nilimuhisi katibu wako muhutasi, lakini nilipofuatilia nyendo zake, niliona hahusiki, hata kukanyaga ofisini mwako hakuwahi...kipindi upo likizo na yeye alikuwa likizo, kama unakumbuka vyema, kwahiyo, yeye nikamuondoa kwenye watu niliokuwa nikiwahisi ....sasa sijui atakuwa ni nani..nimeshindwa kabisa kumgundua..’akasema

‘Ahsante....’nikaona hana jambo la ziada, akaondoka.
Wa pili alikuwa mtu ambaye nilimpa kazi ya kuchunguza nyendo za mume wangu kipindi hicho, kabla hajapata ajali, huyu alikuja na mambo ambayo yalizidi kunichanganya, akasema;

‘Siku mume wako alipopata ajali, anaonekana kutokea maeneo ya rafiki yako,kwahiyo huenda alipita hapo,au alitokea hapo kwa rafiki yako ...na ilionekana alikuwa akiwahi jambo, na.....hakuwa amelewa kabisa,..’akasema

‘Lakini mimi nilikuwa huko kwa rafiki yangu, .kama alikuja huko siku hiyo ningelimuona.’nikasema

‘Inawezekana hakuwa kwa rafiki yako, lakini alitokea maeneo ya huko, ...na alipofika kweny e hiyo kona, akashindwa kukata, nahisi breki zilikataa, ndio ikapatikana na hiyo ajali...., na kilichomuokoa ni kwa vile alifunga mkanda,...alitoka haraka, akiwa na mkoba, .....alionekana kabisa hakutaka kabisa kuachana nao....kwani alionekana kuubeba kwa shida,...’akasema.

‘Na alipofika mlangoni mwa nyumba yenu, alionena kupiga simu,..ndio akaja jirani yenu, rafiki yake, ndiye alyemsaidia...’akasema.

‘Mlipochunguza nyendo zake za , mligundua nini?’ nikamuuliza.

‘Mara nyingi alikuwa akienda kunywa na rafiki yake, yule docta, na wakati mwingine akiwa peke yake, alionekana mpweke, ahkupenda kukaa na makundi ya watu, na kwa upande wa mwanamke, hakuna mwanamke aliyeonekana kuwa naye karibu kirafiki,....japokuwa kwenye maeneo kama hayo huwezi kusema hakuwahi kunywa na mtu wa aina hiyo, ila sio kwa urafiki wa kimapenzi, mara nyingi mwanamke aliyeonekana kuwa naye ni yule rafiki yako, mfanyakazi wako...hata hivyo, kila walipomaliza, waliondoka, na kila mmoja alielekea njia yake...’akasema.

‘Je mume wangu hakuwahi kumsindikiza rafiki yangu huyo hadi kwake,, na hata kuingia kwake, na hata kukaa kwa muda mrefu wa kutilia mashaka, au japokuwa kwa muda mfupi?’ akaulizwa.

‘Hilo katika uchunguzi wetu, hatukuliona, alionekana kumpeleka, na walipofika kwake,waliondoka, na mara nyingi, walikuwa hawatoki kwenye gari,anatoka, rafiki yako peke yake, kama wanatumia gari moja.....’akasema

‘Kwahiyo, hakuna dalili zozote za mahusiano ya kimapenzi kati ya rafiki yangu, na mume wangu, au rafiki yangu na rafiki ya mume wangu, au rafiki yangu na mdogo wa mume wangu?’ nikamuuliza.

‘Kwa uchunguzi wetu, hizo dalili hazikuwahi kuonekana, na kama ilitokea hivyo, basi itakuwa ni siku ambayo haikuwahi kuonekana na watu wangu waliowahi kumuona...na huyo mdogo wa mume wako, alionekana kuwa mbali kabisa, na rafiki yako, ...inaonekana anamuheshimu sana, yeye huwezi kabisa kumuhisi hivyo....’akasema

‘Haiwezekani, ina maana mume wangu hakuwa na rafiki mwingine wa kike.....sasa huyo mtoto ninayesikia anaye ni kutoka kwa mwanamke gani?’ nikauliza

‘Kwa uchunguzi wetu, ....hilo halikuweza kuonekana, kwani kama ulivyotaka, ni kuwa tuchunguze bila kuweka tetesi, tuwe na uhakika na hicho tulichokifanya, na sisi hatukuona au kugundua mwanamke mwenye mahusiano na mume wako..na hatukuwahi kuona mwanamke aliyedai kuwa ana mtoto wa mume wako, wale wote ambao kwa namna moja au nyingine walionekana na mume wako, hawana watoto, na kama wanao, ni watoto wa waume wengine, sio mume wako.’akasema

‘Je katika uchunguzi wenu huko hospitalini hakumgundua lolote, kuwa kulikuwa na mtoto aliyezaliwa ambaye mnahisi mume wangu alionekana kuwa karibu naye..?’ nikauliza

‘Hakuna, mume wako san sana, alionekana kwenda kumuona rafiki yako, alipojifungua, kitu ambacho ni kawaida, maana yule ni mtu wenu wa karibu, kwahiyo vyanzo vyetu , havikuona ajabu kwa hilo...’akasema.

‘Je vyanzo vyenu viliwahi kumuona mtoto wa rafiki yangu, kisura,..anafananaje?’ akaulizwa

‘Ni kitu ambacho wengi wetu waliona ni ajabu, kwani mtoto huyo amekuwa akifichwa sana, hajawahi kuonekana sura yake na mtu yoyote....’akasema

‘Haiwezekani, ina maana na ujanja wenu wote hamkuweza kuiona sura ya huyo mtoto wake, hajawahi kupiga picha, ?’ nikawauliza

‘Unamfahamu sana rafiki yako huyo, kazi za uchunguzi, ulinzi na usalama anazifahamu sana, na akiamua kufanya jambo, analifanya kwa makini sana, nahisi hakupenda kabisa mtu kuiona sura ya mtoto wake, kwahiyo alimvalisha vitu ambavyo huwezi kabisa kumgundua sura yake ya asili, nahisi alikuwa akimvalisha nywela za bandia hata sura za bandia, kwani wengine, wanasema ana sura ya kizungu, wengine kihindi...’akasema.

‘Unahisi kwanini amefanya hivyo....?.’nikawauliza

‘Huenda hataki baba wa mtoto huyo ajulikane...’akasema

‘Kwanini?’ nikamuuliza

‘Huenda yeye au wamanume aliyezaa naye anaogopa kashifa, huenda huyo baba wa mtoto hakutaka itokee hivyo, au vinginevyo.  Au yeye mwenyewe rafiki yako hataki baba wa mtoto huyo afahamu kuwa ni mtoto wake....’akasema.

`Nashukuru, huenda nikakuhitajia tena, endelea na uchunguzi....’

*******

Baadaye alikuja mtu ambaye nilimpa kazi ya kuchunguza kifo cha Makabrasha, yeye aliwahi kufanyia kazi za upelelezi, lakini kwasababu za kiafya akaacha kazi, ..na hata alipopona hakutaka tena kuirudia hiyo kazi, akawa anafanya kazi hiyo binafsi, na y eye akatoa taarifa yake.

‘Kifo cha Makabrasha, kimefunikwa kiaina, nahisi hata polisi walishachoka na tabia ya huyo mtu, na waliona kufa kwake, ni neema kwako, japokuwa walifanya juhudi ya kumtafuta muuaji, lakini hawakufika popote, wakahitimisha walivyoona wao....’akasema

‘Kwanini unasema hivyo?’

‘Kwasababu ya matendo ya marehemu,  kwani alifikia hatua ya kuwawekea hata hao polisi mitego, akawanasa kwenye mambo yanayoenda kinyume na taratibu zao, akawa anazitumia kuwatishia, kuwa ukifanya lolote na mimi nakulipua, kwahiyo hata wao, wakawa hawana jinsi, ila kufuata anavyotaka yeye....unaona eeh..’akasema

‘Kwahiyo unataka kusema nini?’ nikamuuliza

‘Ninachotaka kukuambia ni kuwa ukweli wa kifo cha Makabrasha hautaweza kugundulikana, kwani kufa kwake, imekuwa faraja kwa wale waliokuwa wahanga wake, ikiwemo hao hao, watu wa usalama...’akasema

‘J e inawezekana hata wao wamehusika kwenye kifo chake?’ nikamuuliza

‘Inawezekana pia, lakini aliyefanya hayo mauaji, ni mtu ambaye alijua ni nini anakifanya, na alijiandaa kwa muda mrefu, huenda alikuwa kwenye hilo jengo, siku mbili kabla akimvizia, ni mtu anayefahamu mfumo wa mawasiliano na jinsi ofisi ile ilivyokuwa...kwahiyo anaweza pia kuwa ni mmoja aliyehusika kwenye ujenzi wa hilo jengo...’akasema.

‘Lakini Mjenzi sianajulikana,...unahisi ndio yeye aliyefanya hivyo?’ nikamuuliza

‘Anaweza asiwe yeye , maana tulimfanyia uchunguzi, na siku zote hizo hakuwepo hapa Dar, na vijana wake ambao alikuwa akifanya nao, halikadhalika hawapo hapa Dar, wapo mikoani, kuna ujenzi wanafanya huko, lakini wanaweza kuuza siri za mjengo huo,..huyo mtu aliyefanya hayo mauaji sio wa kawaida, ni mtaalamu wa majengo.....kwani kwa jinsi alivyoingia, na kwajinsi alivyoweza kusoma mfumo wa mawasiliano, na mtandao uliokuwa umewekwa humo ndani,, ...sio mtu wa kawaida....’akasema

‘Haya niambie kutokana na uchunguzi wenu Makabrasha aliuwawa kivipi, na kwanini?’ nikamuuliza

‘Huyo mtu inawezekana alikuwepo humo ndani kwa siku mbili kabla, kama nilivyosema, na silaha aliyoitumia, itakuwa ililetwa usiku wake, na ikaingizwa kwa kupitia nyuma ya ukuta....kwasababu kama ingelipitia kwenye njia ya kawaida, kupitia mlangoni, ...kungelitokea milio ya kuashiria hivyo.....kuna mfumo mle ndani, wa kugundua kuwa mtu kabeba kitu cha hatari, kuna mfumo wa kuchukua kumbukumbu za matukio, ina maana kila anayeingia ataonekana,..lakini cha ajabu siku hiyo ya tukio, hayo yote hayakuonekana kwenye mtandao uliowekwa humo ndani...’akasema.

‘Ili uingie kwenye jengo hilo kuna njia moja tu, na ukishaingia kwenye jengo, ili upande juu, kuna njia moja tu, na huko kote waliweka vinasa matukio na sauti,..hebu fikiri, kote huko hakukuonekana hilo tukio, kumefutwa kabisa..ina maana huyo mtu hakutaka kabisa kuonekana chochote siku hiyo..

‘Na ina maana basi hata kama huyo mtu aliingia na silaha, ...labda akamuhonga mlinzi, lakini angelipita wapi na hiyo silaha,  kwasababu mawasiliano ya kudhibiti hiyo hali ipo sehemu ya siri, huko juu, ...inawezekana basi walinzi wawe wamekula njama,...lakini hilo tulichunguza hakuna kitu kama hicho,...mtu akipita silaha, kuna kelele za kuashiria hatari, na hizo kelele, zingelijulikana kwa watu wote, pale huwezi kuingia na silaha,....’akasema.

‘Hiyo silaha itakuwa ilipitishwa nyuma ya jengo, na walichofanya ni kutengeneza kamba ndefu, iliyoshuka hadi chini, na mtu aliyekuwa chini, akaifunga ile silaha kwenye hiyo kamba, na huyo aliyekuwa juu, akavuta hadi juu, na kuhakikisha, haipiti sehemu zenye kuhisi au kugundua kitu cha hatari..na huenda kwa muda huo, huyo mtu alikuwa keshazima viwambo vya hatari vya ndani....’akasema.

‘Mtu huyo asingeliweza kuzima viwambo hivyo kwa jengo zima, walinzi wa chini wangeliona hilo, na wangeliweka kwenye taarifa zao, hakuna taarifa kama hiyo, na hata tulipojaribu kufanya uchunguzi kwa watu hao, haukukuwa na dalili zozote kama hizo siku hiyo...’akasema

‘Kwahiyo muuaji, atakuwa alikuwa ndani, na muda ulipofika, akafanya kazi yake kirahisi, akaondoka..na cha ajabu basi hata tukio lenyewe,hilo la mauaji halipo...polisi wanadai kuwa walioona baadhi ya sehemu ya tukio hilo, lakini sio kweli..hakuna  kitu kama hicho,...kuna mtu aliyekuja kuondoa kila kitu...cha siku hiyo, na huyo mtu alifahamu ni nini anakifanya , ...’akasema.

‘Kwahiyo hamkuweza kugundua lolote, kwa njia zenu, kuwa huenda mtu fulani anaweza kuhusika?’ nikamuuliza.

‘Huyo aliyefanya hivyo ni mtaalamu, kweli..hatukuweza, na kwa vile polisi wenyewe wamesalimu amri na kuona kuwa ni kifo cha kulipiza kisasi, mimi naona haina haja ya kuhangaika sana..ila kuna kitu ninachoshangaaa,...’akasema

‘Kitu gani....?’ nikauliza

‘Siku ile ya tukio, kuna watu wanasema kuna mtu, japokuwa alijibadili, lakini anafanana na mume wako kimaumbile’akasema

‘Unataka kusema nini hapo?’ nikamuuliza

‘Mume wako alikuwepo kwenye hilo jengo, wakati tukio hilo linafanyika, na polisi hawakuligundua hilo, ..kama wangeligundua hilo, nina imani kuwa mume wako angelikuwa hatarini, wangemshika....mimi nilijaribu kufanya uchunguzi wangu, na hata kuongea na mume wako, lakini hakutaka kutoa ushirikiano...je kuna njia yoyote naweza kuongea naye,...?’ akaniuliza.

‘Hapana, haina haja, inatosha....’nikasema.

‘Lakini nina uhakika sio yeye aliyefanya hayo mauaji....’akasema

‘Kwanini unasema hivyo?’ nikamuuliza

‘Mume wako sio mtaalamu sana wa kutumia silaha, huyo muuaji, anafahamu kutumia silaha, na alifahamu wapi pa kulenga,...ni mtaalamu kweli kweli....na ndio maana nawahisi sana watu wa usalama..mtu aliyefanya hayo mauaji, ni mtu anayejua ni nini anakifanya.’akasema

‘Nashukuru kwa taarifa yako....

**********

Walipoondoka, nilibakia peke yangu, sikuwa na jinsi gani nyingine ya kupata kile nilichokitaka, nikaona kazi iliyobakia niifanye mwenyewe, nikatoka mle ndani na kwenda kwa rafiki ya mume wangu,na nilipofika nilimkuta akiwa kapumzika, na mkewe alikuwa hayupo.

‘Samahani kwa kukusumbua ila nataka kukuuliza maswali machache...’nikasema

‘Uliza, lakini ukumbuke tulishakubaliana, kuwa mimi sihitajiki tena kwenye mambo yako na mume wako’akasema.

‘Ninachotaka kusikia kwako ni ukweli, ukiniambia ukweli, sina shida na wewe,...’nikasema

‘Ukweli gani unautaka kutoka kwangu?’ akaniuliza.

‘Nataka kufahamu kuwa kweli mume wangu ana mtoto nje au sio kweli,...?’ nikamuuliza

‘Unarudi kule kule...nilishakuambia kuwa mume wako, alikuwa kabadilika, na huenda alikuwa na mahusiano na mwanamke wa nje, na mwanzoni nilihisi huenda alikuwa ni urafiki wa siri na rafiki yako, lakini baadaye, nilipochunguza sana, nikaona kama hakuna ukweli ndani yake, huenda, kama waliwahi kufanya hivyo, basi ilikuwa ni bahati mbaya tu...’akasema

‘Kwanini unasema ni bahati mbaya, ina maana unafahamu kuwa kuna bahati mbaya ilitokea, ?’ nikamuuliza

‘Nimekuambia kama iliwahi kutokea hivyo, mimi sikuwahi kuona, na kama ilitokea, basi ni siku mimi sikuwepo, na kama ilitokea, labda ni kwasababu ya ulevi, maana ukilewa unaweza kufanya lolote, kwahiyo labda, ..kitu ambacho sinakithibitisha,..labda...na hiyo labda ndio naiita bahati mbaya.....’nikamkatisha.

‘Kwahiyo zile tetesi zako za awali, sio za kweli, na je kwanini kila mara nilipokuwa nikitaka kuongea na mume wangu, na akawa yupo tayari kuongea ukweli, wewe ulikuwa ukionekana kumzuia asiniambia huo ukweli?’ nikamuuliza

‘Kwa kipindi kama kile, mimi kama dakitari, pia mimi kama rafiki yenu mkubwa, nilijitahidi kuzuia madhara..., sikupenda kuje kutoka tatizo ambalo hata mimi ningekuja kujilaumu, ..hata hivyo, hata mimi nilikuwa nimeshajenga hisia mbaya, kwa rafiki yangu na rafiki yako...lakini nimekuja kufanya uchunguzi nikaona hilo halipo, na kama lipo, lilifanyika kwa siri kubwa sana, nimeongea na rafiki yangu, nikamuomba aniambia ukweli...lakini inaonekana kama upo ukweli zaidi, basi kaamua kuuficha kwenye nafsi yake...na mimi siwezi kumlazimisha mtu aongee kitu ambacho hakitaki kukiongea,....’akasema.

‘Swali langu ni hili, Je ni kweli mume wangu ana mtoto nje?’ nikamuuliza

‘Yeye anahisi hivyo, lakini sio kweli...’akasema

‘Unaposema yeye anahisi hivyo, ina maana gani, si ina maana kuwa alikuwa na mahusiano nje, alikuwa na mwanamke mwingine?’ nikamuuliza.

‘Kwa hali ilie mliyokuwa mkienda nayo, na kwa tabia yake ile ya kulewa, kupitiliza, hilo siwezi kuona ni ajabu....kama nilivyokuambia awali, ....wakati nipo na yeye, nilijitahidi sana kumdhibiti, na asingeliweza kufanya lolote mbele yangu, na mwanamke ambaye tuliweza kumkaribisha na kuwa naye karibu ni rafiki yako, na huyo nilimwamini, asingeliweza kukusaliti, japokuwa kuna muda nilifikia hatua ya kumshuku, lakini baada ya uchunguzi wa kina nimeona sio sahihi...’akasema.

‘Umesema yeye anahisi hivyo...mume wangu anahisi hivyo, kuwa ana mtoto nje, kwahiyo, kuna mwanamke mwingine...anaweza asiwe rafiki yangu, je zaidi ya rafiki yangu amabye alikuwa naye, kuna mwanamke gani mwingine ambaye mlizoeana, akawa anakuaj mnakunywa weote, ....kwasababu inaonekana kweli alikuwa na mahusiano nje, kwanini ahisi kuwa ana mtoto nje,...?’ nikamuuliza huku nikiwa nimeshaanza kukasirika.

‘Kutokana na ulevi wake, huenda siku ambayo sikuwepo, aliwahi kwenda na mwanamke mwingine,..hilo nililifanyia kazi, lakini sikuweza kumgundua huyo mwanamke, hata mdogo wake, alithibitisha hilo, kuwa kama yake hajawahi kutoka na mwanamke mwingine....’akasema

‘Sasa hapo unataka kusema nini, maana kama hakuna mwanamke mwingine, basi anayebakia ni rafiki yangu, huoni kuwa kutokana na ulevi lolote liliwezekana huenda walijikuta wakifanya jambo hilo bila kutarajia...’nikasema.

‘Hilo sina uhakika nalo, kama ingelitokea hivyo, mdogo wako angalifahamu,kwani wakizidiwa ulevi, anayefanya kazi ya zaida ni mdogo wako....na sizani kama angeliweza kunificha....sizani,...’akasema

‘Kwahiyo hata wewe huajweza kugundua ni nani baba wa mtoto wa rafiki yangu ?’ nikamuuliza.

‘Hiyo imekuwa ni siri ya hali ya juu, na hata nilipokwenda kumuuliza dakitari aliyehusika naye siku ile sikuweza kupata lolote, hilo limekuwa siri kubwa sana, ana maana yake na mimi kwasasa sitaki tena kuumiza kichwa changu, kwanini usimuulize mwenyewe, na wewe uliwahi kumuona huyo mtoto, hukugundua lolote , sura yake ipoje,....?’ akaniuliza.

‘Hapo kuna utata....na kwa jinsi ilivyo, nashindwa hata kuhitimisha, ...iliyobakia ni ukweli kutoka kwa mume wangu...nahitajia kauli yake mwenyewe, yeye na rafiki yangu, ’nikasema.

‘Mimi nakushauri hivi, kwa vile mume wako kajirudi, ..achana na mambo hayo, ya kumchunguza chunguza, sana, unaweza kujikuta unaumia zaidi, na huenda ukafanya jambo ambalo utakuja kujilaumu baadaye, achana naye kwasasa, kafanya kosa, , na kufanya kosa sio kosa , kosa ni pale unapolirudi ahilo kosa, ....’akasema na mimi sikujali maelezo yake nikamuuliza swali jingine.

‘Je wewe uliwahi kuongea na wazazi wangu hivi karibuni?’ nikamuulzia

‘Jana tu, nilikuwa na wazazi wako..’akasema

‘Wanasema nini juu ya hili tukio...?’ nikamuuliza

‘Wao wameamua kukuachia mambo yako, ila wanachoogopa ni kuwa mume wako anaweza kukuingiza kwenye kashifa kubwa, wanahisi hiyo iliyotokea ni ndogo, lakini baadaye kunaweza kukazuka mambo ambayo hata wao hawatataka kuyasikia....’akasema

‘Kwahiyo wao wanashauri nini?’ nikamuuliza

‘Unafahamu msimamo wa wazazi wako toka awali, msimamo wao ni ule ule, hawana imani na mume wako...wanasema wamegundua kuwa mume wako sio mkweli, na ana tamaa, na anaweza akaharibu maisha yako ya baadaye, kwahiyo waliniomba niingilia kati, ikibidi, ....ooh, sipendi huo ushauri wao’akasema

‘Ikibidi nini..?’ nikauliza

‘Wao, wanazidi kusema ndoa yako na mume wako haifai, kwahiyo wanasema ikibidi nikushawishi, muivunje hiyo ndoa,...’akasema.

‘Hivi nyie mnaona kuwa hilo jambo ni rahisi sana...yule ni baba wa watoto wangu, ...hamuoni kuwa nikifanya hivyo, nitawaumiza waoto, angalia wale watoto, wanavyofanana na baba yao, na baba yao anawapenda sana, ni kweli hata mimi imefikia hatua natamani nifanye hivyo..lakini kila nikiwaangalia  watoto wangu, nakosa amani...nashindwa kuchukua huo uamuzi...’akasema

‘Hata mimi, nimeliona hilo,..ndio maana nimekuwa nikipingana na ushauri wa wazazi wako, kama 
ningelikuwa sijaoa, ningelifanya juhudi ya ziada , na ningafanya hivyo,...hata hivyo,  mwisho wa yote ni wewe mwenyewe, kama kosa limetokea, na una uhakika halitajirudia tena basi msamehe mume wako, sio lazima mtu awe kama watu wanavyohisi, yeye kama binadamu anaweza kujirudi na akabadilika....’akasema.

‘Tatizo mume wangu hajakubali kuwa mkweli, na ili kuficha uwongo wake, kazua mambo mengine makubwa, na makubwa zaidi, ambayo sitaweza kuyavumilia, na nahisi kutokana na hayo mambo makubwa, yatazuka mengine makubwa, na amani kwenye familia itakuwa haipo tena...’nikasema.

‘Ni kuhusu huo mkataba?’ akauliza

‘Kuhusu huo mkataba, na kuhusu huyo mtoto wan je..asiyejulikana.’nikasema.

‘Hata wazazi wako wanahisi hivyo hivyo’akasema

‘Ina maana wazazi wangu wanafahamu kuwa mume wangu ana mtoto nje?’ nikamuuliza.

‘Huwezi kuwaficha wazazi wako kitu, wazazi wako wana macho ya kuona mbali, wana masikio yakusikia kila kinachotokea kwenye ardhi, ukuhusu wewe, japokuwa hawataki kuthibitisha hilo, lakini nahisi wameshaliona hilo, na hilo ndilo linalowafanya wasimwamini mume wako, ....wanasema anaweza kukuletea matatizo bila hata ya yeye kujua, mfano ni hilo la marehemu, sasa je huyo mtoto ni wa mwanamke gani, je huyo mwanamke ana nini kakipanga juu yake....’akasema.

‘Je wao wanataka mimi nifanye nini?’ nikauliza

‘Wanasema waliwahi kugundua kuwa wewe una mkataba ambao ukiutumia utaweza kumaliza kila kitu, lakini cha ajabu mkataba waliokuja kuuona wao, hauna manufaa kwao, na walikuja kugundua kuwa ule wa awali umebadilishwa,...sasa .’

‘Ni nani aliwaambia atakuwa ni wakili wangu nini?’ nikauliza

‘Hapana, ni wakili wao....’akasema

‘Kwahiyo wakili wao anafahamu mengi kuhusu hiyo mikataba?’ nikauliza

‘Sina uhakika na hilo, kwani yule ni mtu wa wazazi wako hawezi kuongea zaidi, yeye anaongea yale wazazi wako wanayotaka aongee, hasa inapofikia maswala ya kifamilia...’akasema.

‘Je nitawezaje kuupata mkataba huo wa awali....?’ nikawa nauliza

‘Je ukiupata unaweza kufanya nini?’ akaniuliza

‘Mkataba wenyewe utaongea, na safari hii sirudi nyuma, mkataba wenyewe utasema ni nini cha kufanya, kwakeli nimechoka, ....naona sasa basi....na kama ni kweli kuna mtoto nje, ..nitahakikisha nafanya lile nililoliahidi, sitavunja ahadi yangu kamwe...’nikasema

‘Uwe makini, usije ukafanya jambo ukaja kujilaumu...’akasema.

‘Huwezi kubeba mtu asiyebebeka, ...wema wangu usiniponze, ...siwezi kutengeneza maadui kutoka ndani kwa marafiki zangu, ni lazima,nijue ukweli, na kama ukweli ndio huo, basi, ni bora nibakie bila marafiki kuliko kuwa na marafiki maadui....’nikasema na kuondoka zangu.

Nilipofika nyumbani, niliona gari la mume wangu, anatumia gari jingine, la kampuni yake, nikajua yupo ndani, nikaingiza gari langu na haraka nikaingia ndani, nilitaka leo niongee naye nijue moja, ....sikutaka tena kzungushana, kama hataki itabidi nichukuea hatua kubwa zaidi, ikibidi niende mahakamani kwa kugushi mkataba, kwa kuvunja kiapo cha ndoa, kwani kwasasa nina ushahidi wa kutosha, na nina mashahidi..

Nikaingia ndani, hadi chumbani, sikumuona nikajua yupo maktaba, nikafungua mlango wa makitaba, hakufunga kwa ndani kwani mara nyingi, kama hutaki kusumbuliwa, huwa unajifungia kwa ndani, nikafungua mlango taratibu na kuingia ndani.

Mume wangu alikuwa kachuchumaa kwenye kabati langu, ...huwa mara nyingi nalitumia mwenyewe, na akitaka kitu huwa nakwenda kukichukua mwenyewe, na hapo ndipo niliweka ule mkataba, na bastola,...sasa kabati  limefunguliwa, kapata wapi ufungua, alikuwa hajanigundua kuwa nimeingia, alikuwa kainama akiwa anapekuapekua , ..katoa vitu vingi nje, kuna kitu anatafuta, ...

‘Unafanya nini kwenye kabati langu...’nikamshitua...

NB: Mambo yanaanza kujitokeza, wewe unahisi nini hapo?


WAZO LA HEKIMA: Mnapo-oana,na mkafikia kwenye msigishano ambao unaweza kuleta madhara ya ndoa, mujaribu kuangalia  hatima ya watoto wenu, je tatizo hilo ni kubwa sana la hata kuvunjika kwa ndoa yenu, inawezekana ikafikia hapo,na hakuna njia nyingine, kama ni hivyo basi ni bora mkapata ushauri wa kitaalamu ni jinsi gani  mnawezaje kuwasaidia watoto wenu, ili wasije kuathirika kisaikolojia....msiwajengee watoto wenu chuki, kwa mama au baba kuwapandikiza watoto chuki kuwa  wamchukie baba au mama. 

Ni mimi: emu-three

No comments :