Kwa vile kila mmoja
alikuwa na kampuni yake, na utokana na taratibu zetu za kikazi, hata nyumbani kulikuwa na baadhi ya vitu,
ambavyo kila mmoja aliweka mahali pake, ili kusitokee mkanganyiko, na hata
kwenye maktaba yetu, kulikuwa na makabati mawili , moja la kwangu na jingine ni
la mume wangu.
Hakuna aliyekuwa
akihangaika na kabati la mwenzake, labda uamua kumtuma mwenzako, kuwa nisaidie
kunichukulia kitu fulani, na kwa vile humo tulikuwa tukiweza vile vitu muhimu,
ambavyo havitakiwi kupotea, ilibidi kila mmoja awe na funguo zake, kwahiyo, hakuna
liyekuwa akihangaika na kabati la mwenzake.
Kupotea kwa mkataba
wangu, ambao niliuweka kwenye kabati langu, na mimi mwenyewe ndiye mwenye
ufungua, kuliniweka kwenye njia panda, sikutaka hata siku moja kumshuku mume
wangu kwa baya lolote, moyoni nilikuwa namuamini sana, na hii imekuwa ni tabia
yangu, kuwa ukiwa kwenye nafasi yakuitwa rafiki yangu, basi huwa ninakuamini
moja kwa moja, ....sasa mkataba wangu umepotea, na mtu ambaye anayeweza
kuuchukua ni mume wangu, swali lilikuja kwa kutumia ufungua gani, na mimi
ufungua za kabati langu ninao mimi mwenyewe.
Leo hii ninafika
nyumbani ninamkuta mume wangu akiwa kwenye kabati langu, likiwa limefunguliwa,
sikuamini, nina uhakika ufungua wangu ninao, upo kwenye mkoba wangu, kwa muda
huo sikutaka kuhakikisha, ila nilisogea taratibu hadi pale alipochuchumaa mume
wangu, na hakuonekana kushituka, ina maana akili yote ilikuwa kwenye hicho kitu
alichokuwa akikitafuta, na alikuwa katoa vitu vyangu vingi na kuvisambaza
sakafuni, kitu ambacho hakikunifurahisha, huwa nathamini sana hivyo vitu vyangu
na kuvitunza katika usafi wa hali ya juu, leo vimesambazwa sakafuni.
‘Unafanya nini kwenye
kabati langu...’nikamshitua...
Endelea na kisa chetu..............
Mume wangu aliposikia sauti yangu, alishituka, hadi ile karatasi
aliyokuwa kashika mkononi ikamdondoka, kwanza alitulia na baadaye akajifanya
kutokujali, na kuikota ile karatasi, halafu akainua kichwa chake na kuniangalia
usoni, akasema;
‘Afadhali mke wangu umekuja, maana hapa akili yote
imevurugika, nimetafuta pale nilipokuwa nimeweka ule mkataba, wangu wa zamani,
nakala ya zamani, kwenye kabati langu, sijauona, sasa nikafikiria huenda upo
hapa kwako...’akasema.
‘Hujanijibu swali langu, unafanya nini kwenye kabati langu,
toka lini tukawa tunachangiana makabati, kila mmoja ana kabati lake na kila
mmoja ana vitu vyake na humu naweka vitu vynagu vya kikazi, angalia jinsi gani
ulivyoviweka ovyo sakafuni, ...huoni kuwa unataka kuniweka mimi mahala pabaya..vikiharibika,
vikipotea, huoni....’nikasema.
‘Usijali mke wangu hakitaharibika kitu hapa, niamini mimi,
mimi ni mume wako, nitahakikisha hakiharbiki kitu hapa, hata hivyo, akili yangu
inanasa kila kitu ninachokifanya, yaani siku hizi mke wangu naona ajabu sana,
nina akili ya ajabu sana, nitakirudisha kila kitu mahali pake...sisahau hata
kidogo...’akasema.
‘Unatafuta nini kwenye kabati langu?’ nikamuuliza kwa
hasira.
‘Mkataba...ulisema unahitaji ile nakala yangu ya zamani, pale nilipokuwa nimeiweka, kule kwenye kabati langu, siioni, siku hizi akili
yangu inanituma mambo mengi, na nikiweka kitu sisahau pale nilipokiweka, sasa
siuoni, imekuwaje tena...nilifikiria huenda umeuchukua wewe...au umeuchukuwa
wewe nini, huenda umeuchukua, na kuuweka sehemu nyingine?’ akaniuliza huku
akiendelea kupekua kwenye mafaili yangu.
‘Sikiliza mume wangu, ..sijapendezewa kabisa na hiki
ulichokifanya, ..na sio tabia yako, imekuwaje ...kuna nini unanitafuta?’
nikamuuliza huku nikiendelea kumwangalia.
‘Kwa vipi mke wangu, mimi ni mume wangu, ina maana sina haki
ya kuangalia kwenye vitu vyako, ...mke wangu, tuaminiane, mimi kama mume wako
nina haki ya kuangalia chochote kwenye mali zetu, ...au nimekosea?’ akaniuliza
na safari hii alianza kurudisha vitu kwenye kabati, nikawa namwangalia tu.
Hutaamini baada ya dakika moja, alikuwa karudisha kila kitu
kama kilivyokuwa...na akachukua ufungua akafunga , nikagundua ule ufungua
aliotumia ni wa kuchongesha, aaaah, kumbe, ...
‘Huo ufungua uliupatia wapi?’ nikamuuliza.
‘Mbona ninao siku nyingi,...niliamua kuwa na nakala ya
ufungua zote, maana wewe na mimi ni binadamu tu, unaweza kupoteza ufunguo zako,
na mimi kama mume wa familia natakiwa kuwa makini kwa hilo ni muhimu kuhakikisha
mambo yanakwenda vyema, ukipoteza ufunguo wako ninao wa akiba...kuna ubaya hapo
?’akasema akiwa kama ananiuliza, yaani anavyoongea, anavyoigiza sio yule mume
ninayemfahamu.
‘Sio kwamba uliamua kuchongesha ili uweze kuja kuiba mkataba
wangu, ili mkabadili na kuhakikisha nakala zote mumeziharibu, na pia ukaja
ukachukua bastola yangu, nakumbuka wewe ulikuwa hutaki hata kuishika hiyo
bastola,....imekuwaje sasa, uje uichukue na hiyo ndio imeafanya mauaji, ...na
ole wako polisi wakifahamu hilo...’nikasema
‘Unasema, nilichongesha ili nije kuiba,.... kwa nini niibe,
kuna mtu anaiba kitu chake, mbona mke wangu unaniangusha,...usisahau kuwa mimi
ni mume wako, sio mtu mwingine yoyote,...’akasema,
Moyoni, akilini, na mwili mzima, nilikwua nimejawa na
hasira, kama angelikuwa ni mtoto mdogo, ningemshika na kumchapa viboko, lakini
huyu ni mtu mzima na ni mume wangu, nikabakia kukunja uso, na aliponiangalia
usoni jinsi nilivyobadilika, alisimama,
na haraka akatoka nje ya hiyo makitaba.
Nilichukua mkoba wangu na kuutafuta ufungua wangu, ulikuwepo
kwenye moja ya fungua zangu ninazotembea nazo, nikafungua lile kabati na kila
kitu kilikuwa kwenye nafasi yake, na ule mkataba, ule waliotengeneza wao
ulikuwa pale pale...’nikafunga lile kabati, na akilini mwangu nikapanga
nikitoka hapo nabadili kila kitu, nitamwambia fundi abadili na kuweka kifaa cha
ufungua kingine unachofungua kwa namba za siri.
Nilitoka mle makitaba na kuingia kwenye chumba chetu cha
kulala, mume wangu hakuwepo humo, nikabadili nguo, na kuelekea sebuleni, chumba
cha maongezi, na hapo nilimkuta mume wangu akiwa kakaa huku kashikilia mkataba,
..mwanzoni nilifikiria ni ule mkataba wa zamani, lakini ulikuwa ule ule
waliougushi wao.
Nilimsogelea na kumwangalia, alikuwa katulia, na alionekana
alikuwa akisoma sehemu hiyo kwa makini, na alipohisi nimesimama karibu yake,
akauweka pembeni na kuniangalia, akatabasamu na kabla hajasema neno, nikasema;
‘Haya hebu niambie ukweli, ni kitu gani kinaendelea hapa
kwenye nyumba yetu?’ nikamuuliza
‘Mhh, mke wangu, kwani kuna nini kibaya kimetokea, mimi
sioni kama kuna kitu kibaya, labda nikuulize wewe, kuna tatizo lolote? ‘akauliza
‘Mume wangu, leo ni siku ya mwisho, sitakaa tuongee hivi
tena, na nataka leo uniambie ukweli, tukimaliza hapa tujue ni nini cha kufanya,
maana mimi nimeshachoka,vitendo vyako vimenichosha, kwanza umekiuka makubaliano
yetu, umevunja mkataba wa ndoa, na hata sikuelewi, na hutaki kuniambia ukweli, ....’nikasema na yeye akanitupia jicho, halafu
akafungua ule mkataba wake, akawa kama anasoma jambo, mimi sikutaka hata
kumsogelea na kuangalia anasoma kitu gani.
‘Kwanini unasema leo
ni siku ya mwisho,hapana usiseme hivyo, tupo wote, na kila siku tutaongea,
maana wewe ni mke wangu, na mimi ni mume wako, ....’akasema na kutulia, na
aliponiona nipo kimiya akasema;
‘Kwani mke wangu situlishaelewana, na ndio maana nilikuwa
nataka niutafute ile nakala yangu ya zamani,ya mkataba huu, nilikuwa nayo,
naikumbuka sana,, na wewe unaihitajia, sijui kwanini unapenda nakala zile za
zaamni uliweka alama zako nini, sehemu muhimu, au....hauna tofauti kabisa na
huu, ni ganda tu, limekuwa jipya, lakini ndani kila kitu kipo sawasawa,
vilevile....’akasema.
‘Hebu angalia, mwenyewe, ....’akasema huku akinipa ule
mkataba, na mimi sikuugusa na wala sikuinua mkono wangu, nikawa namwangalai
usoni nikasema.
‘Kwanza hebu niambia kwanini mlichukua hatua ya kuubadili
huo mkataba bila makaubaliano na mimi?’ nikamuuliza
‘Mke wangu, mimi nakumbuka , hilo swali nilishakujibu,
hakuna aliyebadili huo mkataba,mbona huniamini mke wangu,...hebu niambie ni
wapi huo mkataba umebadilishwa, na kama ulibadilishwa kwanini sahihi yako, ipo
....unaona eeh, mke wangu hakuna kitu kimefanyika bila ya rizaa yako na wakili
wetu wa familia, ...sahihi zenu zipo vile vile’akasema.
‘Kwahiyo kumbe bado upo na msimamo wako ule ule,....hutaki
kusema ukweli, hutaki kuniambia ni nini kinachoendelea, na ni ni kusudio lako,au
kusudio lenu, na washirika wako....’nikasema huku nimemkazia macho, yeye
akaniangalia mara moja halafu akatabsamu, na kusema;
‘Kwani mke wangu kuna nini, mbona sikuelewi, kuna tatizo
gani...hebu niambie , tusaidiane, huenda mimi nipo dunia nyingine, huenda kuna
kitu umekigundua kwangu na unaogopa kuniambia, au nimebadilika, baada ya
kuumwa, nimekuwa toauti, ...’akasema na mimi nikamwangalia mume wangu, na
nikawa kama simuelewi, hivi huyu mtu yupo sawa, au ana matatizo, mbona sio yule
mume ninayemfahamu,..maana namuuliza kitu na yeye kwanza hajali, na pili
anakuwa kama hajui ninachomuuliza, haoni kuwa kafanya makosa.Anaigiza au ni
kweli, hapana huu ni ujanja ujanja wake tu.
‘Mume wangu , pengine, hujanifahamu , pengine unafikiria
kuwa nakutania, pengine, nahitajika kuchukua hatua nyingine ndio
utanielewa,....hivi unajidanganya nini, hivi wewe hufahamu kuwa hilo
unalolifanya linaweza likavunja ndoa yetu...’nikamwambia na yeye hapo akashituka.
‘Unasema nini..kuvunja ndoa yetu, hapana mke wangu, hilo
halipo, na halitatokea, albda niwe nimekufa....kwanini unasema hivyo?’
akaniuliza na safari hii akawa ananiangalai usoni,akionyesha wasiwasi.
'Kutokana na makubaliano yetu ya awali, hata kama mumeugushi
huo mkataba wetu, mkaweka mambo ya kukulinda, hata kama unajifanya mjanja
sana,lakini ukumbuke kuwa makubaliano yetu ya awali yapo pale pale, na moja ya
makubaliano yetu ni kuwa mmoja akivunja miiko ya ndoa, na akafanya tendo ovu,
kama la kuzini nje, ...na kukawa na ushahidi wa kutosha, basi ....’akanikatisha.
‘Mke wangu unasema nini,....sijawahi kufanya hivyo,.....ni
nani akakuambia nimezini, ....na na...mbona sikuelewi..nimezini na nani ,
umedanganywa mke wangu, temea mate chini, sijawahi, ..nakupenda wewe tu mke
wangu, kweli kabisa....sikumbuki, zamani eeh, hapana ile ilikuwa ni ndoto tu,
sio kweli.....’akawa kama anahangaika akigeuza kichwa huku na huku, huku usoni
akionyesha kuchanganyikiwa.
‘Sikiliza, usijifanye kuigiza mambo hapa, hebu niambie
ukweli, wewe huna mtoto nje ya ndoa?’ nikamuuliza
‘Mtoto, nje ya ndoa....sikumbuki, nakumbuka kuota hivyo....na
nikiwa kwenye ndoto, nikajiona nina mtoto , tena mtoto wa kiume...lakini mama
yake akakimbia naye...nikashituak kwenye usingizi,..ilikuwa ni ndoto tu, sio
kweli, japokuwa mke wangu, nilitamani sana kuwa na mtoto wa kiume, alkini basi
tena, ...basi tena, inauma sana, basi tena, ajali imeharibu kila kitu....’akasema
huku akishika shavu kama mkiwa.mimi sikujali nilihisi kuwa auanigiza tu.
‘Nasikia kwenye mkataba wenu, mumeandika kuwa watoto wote
watakuwa na haki sawa, wa kike na wa kiume,...lakini hapo hapo kwenye hicho kipengele,
mkasema mtoto wa kiume atapewa mamlaka ya kusimamia mali , kama wazazi watakuwa
hawapo, huo ndio usawa, .....huyo wakili wako alikuwa akiangalia mambo kwa
kujipendelea,.je kipengele hicho kilitoka wapi na kwenye mkataba wetu wa awali
hilo halikuwepo, sisi tulikubaliana kuwa watoto wote ni watoto wetu, na wana
nafasi ya kumiliki mali yetu, kutokana na urithi tutakao
utayarisha....unakumbuka hilo?’ nikamuuliza
‘Unaonaeeh, sehemu hiyo inasema hivyo, eeh hebu ngoja na
mimi niisome, kwani kuna tatizo gani kwenye maelezo hayo, kama unaona kuna
matatizo, basi tuone jinsi gani ya kubadili, ili ilete maana unayotaka wewe, na
kama kuna sehemu nyingine huzipendi, basi tuziangalia, tuzibadili, unasemaje
mke wangu...na maelezo hayo nafikiri ni kwa mtizamo wa ujumla, leo tuna watoto
wa kike, lakini sio mwisho wa kuzaa, ....ingawaje...’akasita
‘Ingawaje, nini,...kuwa hutaweza kuzaa tena, kama hutaweza
kuzaa tena kwasababu ya matatizo yaliyokupata kwanini mkaongeza hicho
kipengele, kinachomgusa mtoto wa kiume, wewe unafahamu fika kuwa una watoto wa
kike tu, huyo wa kiume mliyemtaja hapo ni nani?’ nikamuuliza.
‘Mke wangu, ...kwanza tuanze moja, halafu huko
tutafahamishana, kama kuna makosa tutaparekebisha, mmh, kwanza hebu kaa,
tuusome wote wawili, naona sasa
tunakwenda pamoja, kuwa mkataba huu ni ule ule, au sio, ....?’ akaniuliza
‘Mkataba ninaoufahamu mimi ni ule ule wa mwanzo, ambao
haukuwahi kufanyiwa mabadiliko, na hilo tuliliongelea kuwa kama kutatokea baadaye
tukaona kuwa kuna umuhimu wa kufanya mabadiliko, ..mabadiliko hayo yatatakiwa kukubaliana
kwa pande zote mbili, mimi na wewe..je hayo mabadiliko mliyoyafanya mlinishirikisha?’
nikamuuliza
‘Mabadiliko gani hayo mke wangu, ...mbona sikuelewei mke
wangu,...leo hii mimi nilitaka nikuulize kuwa kama unaona kuna jambo halipo
sawa, basi tukae tuangalie , maana naona kama wewe hukubaliani na mambo fulani
fulani kwenye huu mkataba...niambie ni mambo gani huyakubali, unataka
tuyabadili, ili tumuite wakili wetu, tuone tutafanya nini..hilo ni la msingi
sana,...’akasema huku akiufungua fungua huo mkataba.
‘Naona hujanielewa, nataka unipe majibu kwa haya maswali
haya nitakayokuuliza,kama usiponijibu nachukulia kuwa umenipuuza, na kwahiyo
nichukue hatua nyingine ambayo hatima yake ni kuvunja ndoa yetu, siwezi tena
kukuvumilia,kwahiyo nataak unijibu haya maswali , na unielewe, .....’nikatulia
kidogo
‘Nakusikiliza mke wangu uliza tu hayo maswali, lakini hilo
la kuvunja ndoa sikubaliani nalo na halipo, na halitakuwepo.....’akasema
‘Kwanza kwanini mliamua kubadili huo mkatana bila ya
kunishirikisha?’ nikamuuliza
‘Jibu nimeshakupa au unataka nirudie, ...mimi sijui kama kuna
mabadiliko yoyote, na ndio maana naona leo tukae kama yapo basi tukayafanye,
ukikubaliana na hilo,. Mimi sina shida,, mimi nafahamu kuwa huu ndio mkataba
wetu, kama kuna mkataba mwingine zaidi ya huu nionyeshe...’akasema akionyesha
kujiamini.
‘Swali la pili...’nikasema
‘Aaah, umerizika na jibu langu kwanza?’ akaniuliza
‘Hujanijibu swali langu, sijarizika,...na naona umenipuuza,
tuendelee na swali jingine’nikasema
‘Unataka niseme nini mke wangu uone sijakupuuza, kama
nimekuambia ukweli, na unaukana huo ukweli, wewe ulitaka niseme nini, hebu
nifafanulie...’akasema
‘Swali la pili, je una mtoto nje,....?’ nikamuuliza
‘Hilo swali ...nimeshakaumbia, sina uhakika na hilo,
nakumbuka nili-ilikuwa ni ndoto ..niliota hivyo, ...na najaribu kufuatailia, nione
ukweli wake, maana kuna muda ninakuwa kama sio mimi, unafahamu mke wangu nahisi
nina tatizo, ...sina uhakika,nakumbuka hata docta aliwahi kuniambia kuwa kuna wakat
hali kama hiyo inaweza kunitokea,....’akashika kichwa chake kwa mikono yote
miwili.
‘Lakini , inawezekana kweli eeh, nina mtoto nje, ...yupo
wapi....hapana, mke wangu huenda tuna mtoto wa kiume, tushukuru sana,..lakini
yupo wapi...!’akawa kama anajiuliza na uso ulionyesha kutafakari,
..ukimwangalia inonyesha picha kabisa, kuwa anahangaika kutafuata ukweli
‘Usijifanye mjanja wa kujizulia ugonjwa wa kuchanganyikiwa,
usinifanye mimi mtoto mdogo, wewe
ulishapona, huo ni ujanja ujanja wako tu, wa kutaka kunighilibu, nijibu swali
langu, je wewe una mtoto nje, na ulizaa nani?’ nikamuuliza.
‘Nina mtoto nje na nilizaa na nani.?’ akawa ananiuliza mimi,
na aliponiangalia na kuniona nimemkazia macho akasema;.
‘Mke wangu naomba unipe muda, nikafanyie uchunguzi,
sikumbuki hilo kabisa, sina uhakika siwezi kukudanganya,..ina maana kweli mimi
nina mtoto nje, ....mbona simjui, au ile ndoto ni ya kweli....mke wangu una
uhakika na hilo , kuwa huenda nina mtoto nje, na mtoto mwenyewe ni wa kiume,...mke
wangu, kumbe tuna mtoto mwingine,...hata kama sitaweza kuzaa tena, lakini tuna
mtoto wetu, tena wa kiume...’akawa anaonyesha uso wa furaha, na kuniangalia,
halafu akaangalia chini.
‘Swali la tatu, ni nani mwanamke mliyezaa naye?’ nikamuuliza
‘Mwanamke niliyezaa naye..!?, wewe ndiye mke wangu, niliyezaa
na wewe....yule aliyemchukua mtoto sio mke wangu, mke wngu ni wewe.....unasikia,mke
wangu ni wewe na watoto wote ni wetu, ....’akasema na akawa kama anahangaika
kufikiria halafu akasema;
‘Kwanza hebu tumalizane na hilo la mkataba umeshaukubali
kuwa ni ule ule , au la...?’ akawa kama anapoteza malengo.
`Swali la nne, je ni wewe uliyechukua mikataba kwenye kabati
langu, la hapa na kule ofisini ?’ nikauliza
‘Mimi....ofisini kwako, lini,..?’ akawa anajishika kuonyesha
ni yeye, halafu akaonyesha mkono kushangaa, halafu akasema;
‘Mke wangu mbona sikumbuki kufika huko ofisini kwako, tangu
nianze kuumwa, sijawahi kukanyaga ofisini kwako’akasema
‘Swali jingine, Je siku makabrasha alipouliwa ulikwenda
kwake kufanya nini?’ swali hili likamfanya ashituke na kugeuka kuniangalia,
alitulia hivyo kwa muda, na akawa kama anakumbuka jambo, halafu akashika
kichwa, na alitulia hivyo kwa muda, halafu akasema;
‘Ma-mamamaah...ina maana ni kweli....ooh, jamani rafiki yangu,
...haiwezekani, kwanini wamemuua, tena mbele yangu...’akasimama,
‘Mke wangu hivi mazishi yake ni lini, nataka kwenda kumuona
nimuulize kwanini, ameondoka kabla hatujamalizana, ..kwanini..ooh, kichwa
kichwa..ooh, ...’akawa anahangaika, na mara akageuka akaanza kutembea kwa
mwendo wa haraka, kuelekea mlangoni.
‘Unakwenda wapi, haujamalizana, nimeshakuambia nikitoka hapa
mimi naelekea kwa wali wetu, nafuata hatua nyingine, tutakutana mahakamani...’nikasema
lakini mwenzangu alikuwa anaondoka, haangalii nyuma akasema;
‘Nawahi mazishi....’akatoka, mimi nilicheka kidogo na kusema
‘Janja yako...nafikiri wewe hunifahamu eehe...’nikatoka nje,
nikamuona akiingia kwenye gari lake, na mara simu yangu ikaita, nikaipokea
kabla sijaangalia mpigaji ni nani. Huyo mtu akasema;
‘Mimi ni docta .....’akasema kumbe alikuwa yule docta
aliyemtibia mume wangu, nikashukuru maana nilikuwa na mpango wa kumpigia,
kuhakiki haya anayoyafanya mume wangu ni ya ukweli au anaigiza tu.
‘Hali yako docta tena nilikuwa nataka kuongea na wewe..’nikasema
‘Ndio ...ndio maana hata mimi nilitaka kujua hali ya mume
wako, anaendeleaje kwani kipindi kile cha matibabu, kulikuwa na docta mwenzangu,
ambaye alikuwa akimwangalia kwa upande wa kumbukumbu, na alitaka kujua kama
kuna hali yoyote inayojitokea kwake..yupo hapa leo ndio karudi toka safari’akasema
‘Kama hali ipi?’ nikauliza nikionyesha kushangaa.
‘Sijui kama aliwahi kukugusia ila hilo hatukuwa tumelitila
maanani sana, maana kipindi chote alichokuwa kwenye uchunguzi, haikuwahi
kutokea...kuna hali ya kusahausahau, hilo linaweza kumtokea mara kwa mara, na
anaweza pia akafanya mambo ambayo hakuwa akiyafanya zamani, anaweza akawa na
mabadiliko mabadiliko, unaweza hata kumuona ni mtu tofauti kabisa, sasa hali
kama hiyo ukiiona imetokea, tafadhali tujulishe....’akasema
‘Unasema nini docta mbona hamkuwahi kuniambia kitu kama
hichoo’nikasema kwa hasira.
‘Baada ya uchunguzi, ...kipindi kile tulipokuwa naye,
alionyesha dalili, kuwa kapona, na mwenzangu akawa kaondoka, ...tulimwambia
yule docta mnayeishi naye, maana wakati huo wewe ulikuwa na matatizo , ulikuwa
jela,..sasa kwa vile mwenzangu karudi leo na tukawa tunafuatilia jarida la mume
wako, na sijui kwanini, kwani mume wako
alitakiwa kufika mara kwa mara hapa hospitali kwa kliniki yake,hajafika kama
tulivyomuagiza, ndio maana tukaamua tukupigie’akasema.
‘Docta mimi ninaweza kuwashitaki, ..hilo ni kosa kubwa sana,
maana sasa hivi nimemuona mume wangu kama kachanganyikiwa, na mimi nilifikiria
kuwa anajifanya..kwasababu nimekuwa nikimuuliza maswali., anajibu kama
anaigiza, kuwa hajui, mara anasema kasahau, mara aliota,..katoka sasa hivi na
gari, yupo kama ...’nikasema.
‘Mfuatilieni haraka,...na mleteni hapa. ....’akasema docta,
na mimi nikakata simu yake na kuingia kwenye gari langu, nikijaribu
kumfuatilia, sikujua kabisa kaelekea wapi.....oh, ina maana mume wangu
akchanganyikiwa kweli....
NB: Kwa leo ndio hivyo,
WAZO LA LEO: Kwa wandoa mmoja anapoumwa, ni vyema mkajaliana kwanza, hata kama kulikuwa na
sintofahamu, migongano, na mitihani ya hapa na pale, hayo yote myasahau na
muangalia afya zenu kwanza, kwani afya ni bora kuliko mali.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment