‘Baada ya uchunguzi,
...kipindi kile tulipokuwa naye, alionyesha dalili, kuwa kapona, na mwenzangu
akawa kaondoka, ..’Hii ilikuwa kauli wa dakitari aliyekuwa akimtibia mume
wangu, na muda mwingi, wakati mume wangu alipokuwa kwenye matibabu ya mwisho
nilikuwa jela...kumbe kuna mengi yalifanyika, na waliokuwepo hawakukumbuka
kuniambia, mume wangu alionekana kuwa kapona..
Sasa haya yanayotokea
sasa, yalinifanya niona kama mchezo wa kuigiza, ina maana kweli mume wangu
kachanganyikiwa...
‘Docta mimi ninaweza
kuwashitaki, ..hilo ni kosa kubwa sana, maana sasa hivi nimemuona mume wangu
kama kachanganyikiwa, na mimi nilifikiria kuwa anajifanya..kwasababu nimekuwa
nikimuuliza maswali., anajibu kama anaigiza, kuwa hajui, mara anasema kasahau,
mara aliota,..katoka sasa hivi na gari, yupo kama ...’nikasema
‘Mfuatilieni
haraka,...na mleteni hapa. ....’akasema docta, na mimi nikakata simu yake na
kuingia kwenye gari langu, nikijaribu kumfuatilia, sikujua kabisa kaelekea
wapi.....oh, ina maana mume wangu akchanganyikiwa kweli....
Endelea na kisa
chetu....
***********
Ina maana mume wangu kachanganyikiwa, na kuchanganyikiwa
huko ni kwa muda gani, je huko kuchanganyikiwa hakutakuwa na madhara yoyote
kwake, na pengine kwangu, maana anaweza kufanya jambo la kuhatarisha maisha yake
au yangu,au ya watoto....’nikawa nawaza huku nikiendesha gari nikimfuatilia mume wangu,ambaye sijui atakuwa
kaelekea wapi.
Nikiwa naendesha wazo likanijia kuwa nielekee njia ambayo
mara nyingi hupita akielekea kazini kwake, sikuwa na uhakika, ila hisia zangu
zilinituma hivyo, na nilipofika kwenye barabara inayoelekea maeneo anayoishi
rafiki yangu, nikajikuta nikielekea huko, hisia zilinituma nifanye hivyo.
Nilipofika kwenye nyumba aliyokuwa akiishi rafiki yangu,
niliona gari la mume wangu limesimama nje ya hiyo nyumba, haraka nikasimamisha
gari langu na kutoka nje, nilisogea hadi kwenye lile gari lake, nikihisi bado
yupo ndani ya hilo gari, lakini hakuwemo ndani ya hilo gari, nikageuka,
kuangalia kwenye ile nyumba, nilimuona mume wangu akiwa kasimama pale mlangoni na
mkono ukionekana kugonga ule mlango.
Kukaonekana mtu akifungua mlango, yule mtu alijitokeza sehemu
ya juu, yaani kichwa na sehemu ya ndogo ya kiwiliwili, wakawa wanaongea na mume
wangu, na yule mtu alionekana kama kushangaa, halafu akaongea jambo, kwa umbali
ule sikuweza kufahamu wanaongea nini, lakini baadaye nilimuona mume wangu akigeuka,
na kuanza kuja muelekeo wa gari lake.
Nilikuwa nimesimama pembeni ya gari lake, ina maana jinsi
anavyokuja angeliniona lakini cha ajabu hakuniangalia wala hakuonyesha dalili
ya kushituka, na inavyoonekana hakunitambua kabisa, akafika kwenye gari lake
akaingia na kuliwasha, akasogeza nyumba kidogo, akageuza gari na kuelekea bara
bara kuu.
Mimi kwa haraka nikakimbilia gari langu na kuliwasha, na
hapo nikaanza kumfuatilia kwa nyuma, na wazo likanijia, kuwa nijaribu kumpigia
rafiki yake niongee naye, huenda akanipa ushauri ;
‘Unasema mume wako anaonekana kuchanagnyikiwa kwa vipi?’
akaniuliza, nikamuelezea ilivyokuwa kwa kifupi , na yeye akasema;
‘Ndio madakitari wake, waliniambia niwe nikifuatilia nyendo
na afya yake, kama kuna mabadiliko kama hayo, mwanzoni nilifatulia sana, na
nikajaribu kuwa naye karibu, na sikuweza kuona dalili kama hizo, kwangu mimi
nikaona huenda hali kama hiyo haitaweza kutokea, na ....sikuona hata umuhimu wa
kukuambia hilo,...’akasema
‘Kwahiyo nifanyeje sasa?’ nikamuuliza, sikutaka kumlaumu
‘Cha muhimu ni kumfuatilia, kuna mambo kayapanga kichwani
mwake, kuyafanya, akiyamaliza atarudi nyumbani, lakini asije akawa kapanga
kufanya jambo baya....’akasema
‘Una maana gani kusema hivyo?’ nikamuuliza
‘Hapo alipo yupo kama vile mtu aliyelala, na anakuwa kama anaota,
...sasa anaweza akapanga kufanya jambo kutokana na fikira zake
zilizopita,anaweza akawa kajenga kisasi moyoni, na akataka kufanya lolote kwa
mtu anayemuhisi ni mbaya wake, hiyo inaweza ikatokea, sio lazima itokee hivyo,.....’akasema
‘Mbona unanitisha..’nikasema
‘Unatakiwa uwe muangalifu kwa sasa, maana anaweza akafanyamatendo
hata akiwa usingizini..’akasema
‘Kwa vipi , mbona sikulewi’nikasema
‘Hujawahi kusikia watu wanafanya matendo wakiwa usingizini , inaitwa `disambiguation, or somnambulism' mtu mwenye matatizo kama hayo anaweza akaamuka kabisa kitandani, akatoka hata nje, akaenda kufanya kazi kama
mtu anayeota,..lakini anafanya kiukweli, ..’akasema
‘Mungu wangu...!’ nikasema
‘Wasi wasi wangu kwa jini mnavyoishi kwasasa, mnaweza mkawa
mumekwaruzana, na ikawa imemkwaza, na akili za kwenye ndoto zikamtuma kufanya
jambo baya kwako, kwahiyo, hakikisha mkilala, vitu kama visu, mapanga,...na...oh,
na ile bastola yako umesharudishiwa?’
akauliza
‘Ndio ninayo...’nikasema
‘Oh, sasa inabidi uiondoe hapo unapoweka, uiweke sehemu
ambayo hataweza kuiona, vinginevyo kwa hali kama hiyo anaweza kufanya lolote
baya, sio kwako tu, hata kwa mtu mwingine kwa jinsi akili yake
itakavyomtuma....’akasema
‘Kwa namna hiyo unaweza kusema mume wangu keshaharibikiwa
akili?’ nikauliza
‘Hapana..sio kihivyo sana kuwa kapungukiwa..., hiyo itakuja
kuisha, au kurejea kwa kipindi fulanifulani, na walichoshauri wataalamu ni kuwa
kama hali kama hiyo itatokea, ni vyema, akarudishwa na kuwa kwenye mikono
yao....wamachunguze tena...kwani kuna hali ya mkwaruzano ulitokea baina yenu?’akasema
na kuuliza
‘Hatujakwaruzana, ilikuwa mazungumzo ya kawaida, ...na hata
hivyo, ni lazima ifike mahali tuyamalize haya, na ndivyo nilivyotaka, iwe,
sikujua kuwa kuna tatizo kama hilo...’nikasema.
‘Pole sana, ....’akasema na kutulia.
‘Kwahiyo sasa nifanye nini, nimwambieje kuwa anatakiwa
hospitalini?’ nikauliza
‘Kwasasa mfuatilie kwanza , uone anataka kufanya nini, na
huenda huko anapokwenda kukaweza kukupa majibu ya mambo mengine, japokuwa
nakushauri usichukulie kuwa ndio ukweli wenyewe, maana hapo anavutika na hisia
za akili yake tu, ....kuna mambo keshayapanga kichwani mwake anayafuatilia,
hakikisha unakuwa naye karibu..’akasema
‘Kwanini nisiwaambie polisi, wakamkamata,...?’ nikasema
‘Hapana, usije ukawaambia polisi, hatujui mume wako
alikumbwa na nini huko nyuma, ....inaweza kuja kumletea matatizo baadaye,
huenda aliwahi kufanya jambo, ambalo polisi wanalifuatilia, na kama ujuanvyo
wenzetu hao, wakimuona au kumuhisi, hawatajali kuwa huyo mtu ana matatizo,
watakamkata na kumweka, ndani, na hapo tutakuwa tumemaliza...’akasema.
‘Ok, nimekuelewa, ....’nikasema na kabla sijakata simu,
akasema
‘Je unaweza kuyafanya hayo peke yako, au nije kukusaidia?’
akauliza
‘Ninaweza, usijali....’nikasema na wakati huo niliona mume wangu akielekea
barabara ya kuelekea uwanja wa ndege, na akilini mwangu nikahisi atakuwa
anaelekea kule kwa marehemu, maana hata alipotoka nyumbani alisema anakwenda
kwenye mazishi, sasa sijui mazishi ya nani, kwani Makabrasha alishazikwa
zamani..
Nilimfuatilia kwa karibu, nikiogopa asije akafanya jambo la
hatari, alikuwa akiendesha kama kawaida, na hakukuonekana kukosea kama kuyumbayumba
hivi , au kwenda kinyume na utaratibu wa bara bara, na hapo sikumuelewa alivyosema
kuwa mume wangu anaweza kuwa kama yupo usingizini.
Tukafika maeneo karibu na uwanja wa ndege, na kama
nilivyohisi, nilimuona akigeuza gari kulia kwake, na kuingia eneo lililopo lile
jengo, alipokuwa akifanyia kazi Makabrasha, alifika kwenye eneo la kuegesha
magari, akasimamisha,
Na mimi nikafika na kugesha gari langu pembeni yake,
nikatoka, na kumfuatilia, nilimuona akiongea na muhudumu mmoja, na baadaye
akasogea pale alipokaa mlinzi wakawa wanaongea, ilionekana kama hawaelewani, na
yule mlinzi akawa kama anafoka, na kumzuia mume wangu, kuna kitu mume wangu
alikuwa anataka kukifanya , lakini mlinzi akawa anamzuia, na baadaye
wakaongezeka walinzi wengine, na mlinzi mmoja akamshika mkono mume wangu na
kumvuta pembeni, wakawa wanaongea halafu mume wangu akaonekana kutikisa kichwa..
Ilionekana kama kuna kutokuelewana, lakini baadaye niliona
mume wangu akasalimu amri, akageuka na akawa anarudi kwenye gari lake, alifika
kwenye gari lake, akakaa kwenye kiambaza cha hilo jengo,huku kainamisha kichwa
chini, alikaa vile kwa muda, na mimi kwa haraka nikaenda kuongea na wale
walinzi.
‘Yule ni mume wangu kuna nini kinaendelea?’ nikawauliza
‘Yule jamaa sijui kachanagnyikiwa, anakuja anamuulizia
Marehemu Makabrasha, sisi tumemwambia huyo mtu hayupo tena duniani, keshafariki,
lakini hatuelewi, yeye anadai wameahidiana kukutana ofisini kwake....’akasema
‘Oh, ...’nikasema hivyo tu, na huyo jamaa akahisi sijaelewa,
akesema;
‘Tukamwambia huyo mtu hayupo duniani tena, lakini cha ajabu,
huyo jamaa unayesema ni mume wako, yeye kakataa kata kata, akasema yeye ana
uhakika Makabrasha yupo ofisini kwake, waliongea naye kwenye simu....’akasema
‘Hamna shida, ....muachenia atulie, nahisi bado hajaamini
kuwa rafiki yake hayupo duniani.., alikuwa rafiki yake mkubwa...’nikasema
‘Unasema huyo jamaa ni mume wako,...mmh, huwezi amini
alivyovalia kama bosi fulani, lakini mbona anaonekana kama hazipo sawa, na anaendesha gari mwenyewe,
ni hatari, uwe makini naye....’akasema huyo mlinzi na mimi nikageuka
kumwangalia mume wangu, ambaye kwa muda huo alikuwa kasimama, na mara akaingia
kwenye gari lake na kuanza kuondoka, na mimi kwa haraka nikachukua gari langu
na kuanza kumfuatilia nyuma....
**********
Kutokana na hali hii, nikaona mtu anayeweza kunisaidia hili
ni mdogo wake, ...hasa kipindi cha usiku, kama alivyoeleza rafiki yake kuwa
anaweza kufanay lolote baya, basi usiku nitakuwa na wakati mgumu sana, kwahiyo
nikampigia simu mdogo wake.
‘Shemeji kuna tatizo?’ akaniuliza
‘Nakuomba uje nyumbani, ...’nikasema
‘Kuna nini shemeji?’ akauliza kwa mashaka
‘Kuna kitu nataka unisaidie kuhusu kaka yako,....’nikasema,
sikutaka kumwambia ni nini kinaendelea kwa wakati ule, lakini nilifahamu nikimwambia
kuwa ni mambo ya kaka yake, atakuja haraka.
‘Sawa nakuja shemji, lakini haumwi sana?’ akauliza
‘Haumwi, ni jambo dogo tu nitakuambia ukifika’nikasema
Niliona mume wangu anaelekea ofisini kwangu, alifika eneo la
ofisini kwangu akasimamisha gari, akapiga honi, na mlinzi akatoka, na nikasikia
akimuuliza;
‘Mke wangu yupo ofisini kwake?’ akauliza
Mlinzi alimwambia hapana, na wakati huo nilikuwa
nimeshasimamisha gari langu, mbali kidogo, na pale aliposimamisha gari lake,
yule mlinzi hakuliona gari langu, nikatoka kwa haraka na kusogea, nikasimama
seehmu ambayo hawo wawili walikuwa hawawezi kuniona, nikawasikia wanachoongea, haraka nikachukua simu yangu na
kutuma ujumbe kwa yule mlinzi.
‘Mwambia mimi nipo nyumbani namsubiri...’nikatuma kwa yule
mlinzi, ambaye kwa vile gari la mume wangu limemzuia, hakuweza kuliona gari
langu, akasikia sauti ya ujumbe kwenye simu yake, akawa anausoma, halafu
akamwambia mume wangu.
‘Mke wako yupo nyumbani anasema anakusubiri...’akamwambia
‘Hapana mimi nina uhakika yupo ofisini kwake, nina uhakika
huo, ..nataka kwenda kuonana naye...’akasema
‘Ofisi kwasasa imefungwa, huoni kabisa kuwa huu sio muda wa
kazi, hakuna mtu ndani...’yule mlinzi akasema
‘Mh, oh, ina maana muda wa kazi umekwisha,..oh, samahani,
....’akasema na kulirudisha gari lake
nyuma na kuligeuza, nikajua kwasasa atakuwa akielekea nyumbani.
Nilimfuatilia hadi tukafika nyumbani , na niliona gari la
mdogo wake limeshafika, na yeye wala hakuangalia pembeni, akatoka kwenye gari
lake na kwa haraka akakimbilia ndani, na mimi nikatoka kwenye gari langu na
kuingia ndani.
Nilipofika ndani nilimuona mdogo wake, akiwa kakaa kwenye
sofa, lakini mume wangu hakuwepo, nikamuuliza
‘Umemuona kaka yako akiingia?’ nikamuuliza
‘Ndio kaingia, lakini hakunisemesha, alionekana kama
hanioni, kanipita kwa haraka akakimbilia chumbani kwenu kwani kuna nini?’
akaniuliza
‘Nitakuambia, ila nataka ulale hapa leo, kesho inabidi tumpeleke
kaka yako hospitalini, kaka yako
anaonekana kuchanganyikiwa kidogo....’nikasema.
‘Ina maana hiyo hali imejitokeza?’ akauliza
‘Ina maana ulikuwa unafahamu kuwa hali kama hiyo
itajitokeza?’ nikamuuliza
‘Ndio kipindi akiwa kule hospitali kwenye uchunguzi walisema
hivyo, lakini jinsi alivyokuwa alipotoka huko, tuliona kuwa haitaweza kutokea
tatizo kama hilo, hata docta, rafiki yake, alisema huenda hiyo hali haitajitokeza
tena, baada ya yeye kumfuatilia kwa muda.....’akasema
‘Sasa ndio hivyo imejitokeza, na kwa hali kama hiyo,
kunahitajika mtu wa kuwa naye karibu wakati wote, naogopa usiku nisije nikashindwa,
nikapitiwa na usingizi, ....kama kuna lolote la kufuatilia huko kazini kwako
nenda , au wapigie simu, ...kuwa kuna dharura, hutarudi huko...’nikasema
‘Hakuna shinda nimeshaaga tayari,...’akasema na mara mume
wangu akatoka na kuniangalia alionekana
kama kunishangaa, halafu akasema;
‘Mke wangu, sijui kuna nini kinaendelea kwenye kichwa changu...’akasema
‘Kwani unajisikiaje?’ nikamuuliza
‘Hivi lini tulikuwa tunaongea kuhusu mtoto, ukaniuliza kuwa
nina mtoto nje, mtoto wa kiume?’ akaniuliza
‘Mchana, tuliongea mchana, kwani vipi?’ nikamuuliza
‘Nimekwenda kumfuatilia huyo mtoto, hayupo,... hayupo , hata
mama yake hayupo.....nahisi watakuwa wameamua kutukimbia na mtoto, huenda
wameamua kunisaliti, una uhakika, kuwa nina mtoto ....tuna mtoto wa kiume, una
uhakika?’ akawa ananiuliza
‘Hamna kitu kama hicho mume wangu, nilikuwa nakutania tu ...’nikasema
‘Sio utani huo, nikweli nina mtoto...ni lazima tumchukue
mtoto wetu, mama yake hawezi kunikatalia, anasema mtoto ni wa kwake, sio wa
kwangu na sina haki naye,...sikubali, nilimwambia Makabrasha alifuatilie hilo ,
na alisema kila kitu kipo sawa sawa.....kwahiyo usijali mke wangu, mtoto yule
ni wa kwetu, kwahiyo tuna watoto hawa....’akasema akionyesha vidole vitatu.
‘Hapana mume wangu sisi tuna watoto wawili,....’nikasema
‘Usinibishie mimi, ...., mimi ndio najua, mimi ndio mume
wako,...tuna watoto wanne, ...na ...’mara akamuona mdogo wake, akatabasamu na
kumsogelea, kama vile anataka kumkumbatia, lakini mdogo wake akanyosha mkono
wakashikana kusalimiana.
‘Jembe, umekuja, sasa mambo safi, utanisaidia kazi moja..kuna
kazi moja usiku, sio sasa, hiyo ni siri yetu,..unasikia, sitaki mke wangu afahamu,...unasikia jembe....’akasema na
hayo maneno kuwa hataki mimi nifahamu akawa kama anamnong’oneza, .
Mdogo wake akawa anamwangalia kaka yake kwa mashaka.Nilimuonyeshea
ishara akubali tu, na mdogo wake, akamsogelea kaka yake na wakawa kama
wanakumbatiana, nilimuona mdogo wake akijizuia kutoa machozi.
Niligeuka na kuangalia pembeni, maana kwa hali kama ile hata
mimi hali ilinishinda, karibu nitoe machozi, sikuamini, mimi nilishafahamu kuwa
mume wangu keshapona, na tunatakiwa kuganag mengine, sasa ahli hiyo
imerudi,..na haijulikani kuwa ni ya muda tu au ndio keshaanza kuchanganyikiwa
kabisa...lakini anavyoongea inaonyesha kuna mengi kayatenda, ina maana kuna
mengi kayaafanya, ina maana kweli ana mtoto nje...ina maana...haiwezekani
‘Sasa mke wangu nataka kutoka na mdogo wangu, tutaonana
baadaye...’akasema na kunishitua kwenye lindi la mawazo, nikamwangalia, yeye
akamshiak mdogo wake mkono
‘Lakini mume wangu unatakiwa kupumzika...’nikasema
‘Hatutakawia, nipo na jembe, huyu ndiye mimi, ukimuona huyu
umeniona mimi, hata nikifa leo, usije ukamtupa mdogo wangu,....usije
ukamnyanyasa mdogo wangu, nitafufuka na kuja kumtetea, nampenda sana mdogo
wangu.....hili ndilo jembe langu...’akasema na kumshika mdogo wake mkono, wakatoka
naye.
Nilibakia mle ndani nikiwa sijui nifanye nini, na mara simu
ikaita, ilikuwa ni namba ya nje, na nilifahamu atakuwa ni rafiki yangu.
‘Habari za huko?’ nikauliza
‘Nzuri tu, bosi, tumemaliza mitihani mmoja kesho tunafanya
mwingine, na huenda nikaja huko siku za karibuni...’akasema
‘Itakuwa vizuri sana, maana kuna mambo nataka tuyamalize...’nikasema
‘Yale yale..au?’ akauliza
‘Ndio,..yale yale, na hapa tunapozungumza mume wangu
anaonekana hayupo sawa’nikasema
‘Mhh, hiyo hali imeshajitokeza ehe..?’ akawa kama anauliza
‘Ina maana unafahamu?’ nikamuuliza
‘Wewe hukuwa makini na mume wako, ooh, kumbe kipindi hicho
ulikuwa jela, ..ok, samaahni nimesahau, nimekumbuka, nilipofika hapo , kwa
dharura, nilimtembelea mume wako hospitalini, na docta alisema mume wako
kapona, lakini kuna mambo yanaweza kujitokeza, kama vile kupoteza kumbukumbu, na
kitabia anaweza akabadilika badilika, asiwe kama alivyokuwa mwanzoni, na pia
anaweza kufanya mambo kama yupo kwenye ndoto...’akasema
‘Kwanini docta alikuambia hivyo, wakati hayo nilitakiwa
kuambiwa mimi ?’ nikauliza
‘Wewe siulikuwa haupo, ..ulikuwa Segerea, na mimi yule docta
ananitambua sana kuwa ni ndugu yako wa karibu, ...’akasema
‘Ni ndugu yangu wa karibu,ehe, ...kweli wewe ni ndugu yangu
wa karibu, kama ungelikuwa ni ndugu yangu wa karibu ungelinifanyia hayo
uliyonifanyia’nikasema
‘Yapi tena bosi, mbona kila siku unakuja na hoja mpya, ...?’
akauliza.
‘Unayafahamu sana.....’nikasema.
‘Bosi nakuomba bosi, usichukulie hayo mambo kwa hasira,
nikirudi tutaongea, nina imani hakitaharibika kitu..’akasema
‘Kama ni kweli, ninavosikia, kama ni kweli, wewe umezaa na
mume wangu...sizani kama tutakaa kwenye meza moja tuongee, hilo sahau, na
nilishakuambia, kama kuna mtu anataka ubaya na mimi ...basi atembee na mume
wangu, sitajali kama ni nani, hata kama ni ndugu yangu wa tumbo moja, nitafanya
yale yale niliyowahi kukuambia...’nikasema.
‘Lakini...’akaanza kujitetea.
‘Sasa hivi mume wangu anaumwa, na hali aliyo nayo siwezi
kufanya lolote, lakini akipona tu,...kama ni kweli, basi, ...mkataba utafanya
kazi yake, na mengine yatafuta baadaye....’nikasema.
‘Mkataba upi bosi ...maana kama nilivyoona, kwenye mkataba
hakuna tatizo, ...mume wako ana uhuru wa kufanya lolote, huoni kwamba ukitumia
huo mkataba utakuwa umejimaliza mwenyewe..’akasema
‘Ndivyo unavyojidanganya ehe, ndivyo mlivyopanga, au sio?’
nikauliza
‘Mimi sijapanga lolote, mimi niliitwa kuja huko kwa dharura,
na nilipofika hapo, nikajikuta naingizwa kwenye mambo ambayo hata siyajui,....walipanga
wao wenyewe, ..kama ningelifahamu hivyo nisingelikuja huko, hadi nimalize
mitihani,...unaona ilivyotokea,nimefika tu wakamshikilia mtoto wangu ,
nikalazimishwa kufanya mambo ambayo sikuwa na hiari nayo, na ndio nikauona huo
mkataba, sijui lolote jingine, ....’akasema
‘Msijidanganye kwa hilo,yaani yote niliyowatendea fadhila
zangu zote ndio malipo yake ni hayo...msijiona nyie ni wajanja sana, ....’nikasema
‘Jamani dada, ...bosi, usinifikirie hivyo kabisa, sipo
kabisa kwenye hayo mambo yao, ndio maana wakatumia mbinu hizo walizotumia, ...hebu
niambia mimi ningelifanya nini kwa hali kama hiyo,...Bosi, nakuhakikishia
nikirudi tutayamaliza...’akasema
‘Ndivyo unavyofikiria kwa vile utakuwa mke mwenza, au mshirika, au nani ?’
nikamuuliza
‘Mimi sielewi una maana gani kusema hivyo’akasema
‘Unaelewa sana....’nikasema.
‘Basi subiri nirudi, naona hapa kwenye simu hatutaelewana, ila nakuhakikishia kuwa sijui
lolote kwenye mambo yao, na mimi siwezi kufanya jambo baya dhidi yako, na
ukiona nimefanya jambo, ujue ni kutokana na ushauri wako,....’akasema
‘Niliwahi kukushauri uje ufanya ufusuka na mume wangu?’
nikamuuliza
‘Bosi,...naona hatutalewana,...kwasasa, naomba uniache ili
nimalize masomo kwanza, hayo na mengine mengi tutayamaliza, hakuna tatizo
kabisa....mimi sijawahi kufanya jambo kinyume na matakwa yako, hilo
nakuthibitishia, ...mengi nimeyafanya kutokana na kinywa chako
mwenyewe.....nitakuja kukuthibitishia hilo..’akasema na kukata simu.
NB: Kisa kinarudi kuleee...na kuashiria kuwa mambo yanawekwa
hadharani
WAZO LA LEO: Tuwe
makini na kauli zetu , ulimi unaweza ukasababisha mema na mabaya,ukiutumie
vyema ulimi wako unaweza ukapata faida kubwa, lakini ulimi huo huo, unaweza ukawa ni
silaha yenye sumu,ukapandikiza chuki nafitina, urafki ukageuka kuwa uadui, Tuweni
makini sana, na ulimi.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment