`Je unamuafiki huyo shahidi aanze?’ akaniuliza mwenyekiti, na
mimi kwa vile sikuwa namfahamu huyo shahidi ni nani hasa, nikajikuta nimeshikwa
na kigugumizi cha kujibu, na mwenyekiti akaligundua hilo, akasema;
‘Aitwe huyo shahidi, tumalize mambo haraka, ...’akasema
Kila mmoja alikuwa na hamu ya kumuona huyo shahidi, na
wengine walipumua, kwani hakuna aliyejua ni nani ataitwa kama shahidi, na hadi
aple mlango unagongwa, wengi bado walikuwa kwenye kutafakari, na kuwazia ni
nani huyo binti na atazungumza nini, au kilimtokea nin hadi aitwe kama shahidi.
Mlango ukafunguliwa, na akaingia binti, akiwa kavalia
kiheshima na mkononi alikuwa kashika bahasha, na , hakuwa na kitu kingine, kwanza kwa aibu
alipoingia pale mlangoni, hakujua afanye nini, alishikwa na butwaa hasa
alipoona watu wote wamegeuza kichwa kumuangalia yeye,...
‘Sogea huku mbele...’ilikuwa sauti ya mwenyekiti, ndiyo
iliyompa nguvu na sauti hiyo ilimshitua mume wangu aliyekuwa kainama, sijui
alikuwa akiomba au alikuwa akifanya nini, maana tangu azozane na wakili wake,
yeye alimua kuinama, na kukaa kimiya, ...
‘Wewe umefuata nini huku...’sauti iliyowafanya watu wageuka,
na kuangalia muongeaji ni nani, hakuwa mwingine bali alikuwa ni mume wangu,
ambaye alikuwa kasimama nusu, huku akiyatoa macho yasiyooamini kile
anachokiona, na mwenyekiti akawa anaangalia hili tukio kwa hamasa ya aina yeka,
na mimi kwanza nikatabsamu kuwa shahidi aliyeletwa anastahili, lakini
nikajikuta nikiingiwa na huzuni.
‘Haya huyo hapo shahidi wako wa kwaza, unataka uendelee naye
mwenyewe, au nishike usukani..?’ akauliza mwenyekiti, lakini mimi niliishiwa
nguvu, nilibakia nikiwa nimwangalia yule binti, sijui ilikuwa ni huruma,
hasira, au nini sikuweza kuongea, kilichotokea ni mimi kuangusha chozi..
Mwenyekiti akaiona ile hali, akaamua kuendelea mwenyewe,
akasema;
‘Kweli inauma, hii isikie kwa mwenzako tu, lakini ukitendewa
wewe utaona uchungu wake, na hasa utendewe na mtu unayemwamini, hukutgemea
kabisa,...lakini ndio ilivyo, tuweni makini sana, ..hasa nyie wanawake, nawaasa
muwe makini sana, na wafanyakzi wenu wa ndani, msipende kuwaacha na waume zenu
kwa muda mrefu, au kuwapa kazi ambazo sio stahiki zao...hata hivyo, sio kwamba
nasema wanaume wote wana tabia hiyoo chafu, ..hapana, muulizeni mke
wangu...’akasema mwenyekiti na watu wakacheka.
‘Huyu hapa mbele yenu ni shahidi, anayezihirisha, urijali wa
mume wa familia, hachezi mbali, yeye aliamua kucheza na humo humo ndani,
...jamni huyu sio sawa na binti yake, labda niseme, huyu sio sawa na mdogo
wake,....yeye aliamua kula kuku na mayai yake....sitaki kupoteza muda, ngoja
tuanze na huyu shahidi wetu...’akasema mwenyekiti.
‘Hebu tuambia jina lako,....na usiogope, hata tunachotafuta
ni haki yako,ukiogopa haki yako yote iatpotea, na waliokuharibia masiha yako
wataendelea kuyafanya haya kwa watu wengine, ...sisi tunataak haya yakomeshwe,
na hili tunaweza kulianzia majumbani kwetu, kama hivi,..likitokea jambo,
mkosaji aitwe, aadhibiwe, ikishindana, apelekwe kunakostahiki,...’aaksema
mwenyekiti.
‘Haya jitambulishe mpendwa,...’akasema mwenyekiti.
‘Mimi naitwa Tabia...’akasema kwa sauti ya kinyonge
‘Tabia,..tabia yako ni ya upole, au sio, mchapakazi, au sio,
...sasa nasikia kuna kitu kilitokea, wakati unafanya kazi kwenye nyumba moja,
kilipotokea ukakimbia jiji, ni kwanini ulikimbia jiji...?’ akamuuliza
mwenyekiti.
‘Sikukimbia jiji, niliambiwa niondoke, la sivyo yatanikuta
makubwa, na...na...’akasita kuongea
‘Hebu sasa tuanze, maana nilikuwa nakuweka sawa, hebu
niambie, wewe ulikuwa ukifanya akzi wapi , na kwa nani/’ akaulizwa
‘Mimi nilikuwa mfanyakazi wa ndani wa nyumba, ya
ya...’akageuka kuniangalia mimi
‘Ya mke na mume wa familia tunayoiongelea ..ngoja
nimsaidie...’akasema mwenyekiti.
‘Ulifanya kwenye hiyo nyumba kwa muda gani?’ akaulizwa
‘Kwa zaidi ya mwaka mmoja...’akasema
‘Hebu niambie, wakati upo hapo, kulitokea nini,
kilichokufanya uondoke, uliamua kuacha kazi , kwa vile umepata mume huko kwenu
au ilikuwaje?’ akauliza mwenyekiti.
‘Niliondoka baada ya kugundua kuwa nina uja uzito...’akasema
na watu wakaguna
‘Jamani msigune, ndio hali halisi, na tunapoongea hapa watu
wanafikiria tunamuonea mlalamikiwa, sasa ngojeni masikie wenywe, haya tuambie,
unasema ulipata uja uzito, kumbe wewe badala ya kufanya kazi za ndani ulikuwa
ukifanya uhuni na wavulana wa mitaani eehe...’ aaksema mwenyekiti kwa sauti ya
nzito, kama kumtisha huyo binti.
‘Hapana mimi sio muhuni, sijawahi kufanya uhuni na mvulana
yoyote, ...’akasema
‘Unasema hujawahi kufanya uhuni na mvulana yoyote, sasa hiyo
mimba uliipaat kutoka mbinguni, hebu sema ukweli, ...’akasema mwenyekiti
‘Mimi nilikuwa smjui mwanaume, yoyote, nilikuwa nafanya kazi
zangu na sikupena haya yaotokee, ..niliapa kwa mama yangu kuwa sitakuwa muhuni,
na nilipochukuliwa na ....wazazi wangu hawo, nilijua kuwa nimefika mahali
salama....sikutarajia kuwa hayo yangelitokea,....akaanza kusimulia;
***********
Mama yangu ni mjane, baada ya kufariki baba, kwa ghfla,sisi
tulibakia na mama kwenye kiban kibovu tu,tukiwa watoto watano, na alituacha
tukiwa masikini sana, mama akawa anaangaika sana kututafutia riziki, na sisi
japokuwa tulikuwa wadogo, lakini tulijijua kuwa hatuna mtu atakayetusaidia,
kwani baada ya msiba, vitu vilivyokuwepo vichache viligawanywa, na wanandugu
wakachukua kile walichoona kinawafaa, tukabakia mikono mitupu.
Mimi nilikuwa mkubwa ukilinganisha na wadogo zangu,kwani
mimi nilikuwa mtoto wa kwanza nna kwa vile ni mwanamke , nilionekana mkubwa
kidogo, basi ikawa kazi kubwa ni kumsaidia, kila tukitoka shule tunajipanga,
huyu afanye hiki na yule afanye kile, ili tu tuweze kumpunmguzia mama kazi za
nyumbani..
‘Kazi kubwa ya mama ilikuwa kutengeneza vyungu, kwa kutumia udongo
wa mfinyazi, alikuwa akienda huko mlimani kuutafuta na akileta anatengeneza
vyungu vya kupikia, mama alikuwa mtaalamu sana wa kazi hiyo, lakini hata hivyo
kazi hiyo ilikuwa hailipi, kwani akijitahidi sana anakuwa katengeneza vyungu,
hata kumi havifiki, na bei za kijijini ni ndogo, ni kazi nzito, lakini
tungefanyeje...kuna kipindi tunakuwa hatuna hata senti moja, nyumbani, inabidi
mama aende kwa majirani kuomba hata kazi ya kulima, au kuosha vyombo ili
angalau tupate pesa ya kula, ndio maisha niliyokulia hayo.
Wingi wetu, ulikuwa mzigo sana kwa mama, na ukumbuke baba
alifariki akatuacha tukiwa tunasoma shule ya msingi, mimi nilikuwa darasa la
saba, na wenzangu, la sita, la tano la nne, na la tatu, na wamiwsho alikuwa
darasa la pili,tulipishana mwaka mmoja mmoja wa shule, japo kimuri tulipishana
kidogo. Ilibidi tusome kwa shida, haat nguo za shule, zilichakaa, ikawa
tunaweka viraka, na wengi walianza hata kututania, kuwa sisi ni
viraka.....’akasema
Darasa la saba nilimaliza kwa shida sana, kwa vile mimi
ndiye mkubwa, basi ilikuwa kama mimi ndiye msaidizi mkubwa wa mama, nilitakiwa
kuamuka asubuhi sana, kumsaidia mama, ili aweze kukusanya, vile vyungu
vilivyokuwa tayari, maana tulikuwa tukivichoma usiku,na asubuhi, tunavitoa ili
vipoe, vingine vinavunjika, ndio hivyo tena...’akatulia.
Nilipomaliza darasa la saba tu, watu wengi wakaja kunitaka,
niende nikafanye kazi kwao, kama mfanayakazi wa ndani, kutokana na jinsi
walivyoniona, kuwa ni mchapakazi, sikupena kabisa niondoke nimuache mama yangu,
lakini pia tulihitajia pesa kwa ajili ya kuwasomesha wadogo zangu, basi mtihani
ukaanzia hapo, niende kwa nani..
Kabla hatujaamua ndio lsiku moja likaja gari, na wakaja hawa
wazazi wangu , ambao mama alikubali niondoke nao,mama alisema anawafahamu
vyema, na aliona kuwa watatusaidia kujikwamua kimaisha, angalau wadogo zangu
waweze kusoma na kufika mbali sio kama mimi niliyeishia darasa la saba
...’akatulia.
‘Wageni hawo, waliongea na mama wakakubaliana, na kesho yake
nikachukuliwa na kuja huku Dar, na kama ujuavyo, kila mmoja kule kijijini
anatamani sana kuja huku, kwahiyo hata mimi nilifurahi sana, na nilishukuru
kuwa nimapata kazi kwa watu wenye uwezo. Nikaiga familia yangu na wadogo zangu
na mama alizidi kuniusia kuwa nifanye kazi kwa bidii nizije nikandanganyika na
kuingiwa na tamaa, na kujiunga na wahuni, mimi nikamuahidi kuwa sitafanya
lolote baya.
Mshahara wangu wa kwanza wote niliutuma kijiji kwa mama, na
mama yangu mpya alikuwa akinijali sana, alinisaidia mambo mengi, na kuanza
kunisomesha msomo ya jioni, nikaanza kuelewa maisha na jinsi gani ya kuishi
kisasa, sio kama nilivyokuwa huko kijijini, na alikuwa akinisaidia kunipa peza
za kuwasomesha wadogo zangu kila nilipomweleza matatizo ya nyumbani kwetu...’akatulia
kidogo.
Kwakweli mimi darasani sielewi, ninachojua ni kufanya kazi,
nikamwambia mama asipoteze pesa zake bure, kwania litaka kunisomesha sekondari,
kiujumla kichwa changu ni kizito sana darasani, akaniuliza kitu gani rahisi
ninaweza kukisomea au kukifanya, nikamwambai ufundi, na nikachagua ufundi wa
kushona, na kweli huo nikauwezea sana...akaninunulia cherehani, nikawa nashona
nguo hapo nyumbani, na alikuwa na mpango wa kunifungulia duka langu...lakini oh
bahati haikuwa yangu....’akaanza kulia.
‘Aaah, tulishakuambia, ujikaze, mambo ya kulia hapa
hatuyataki...yote ni mitihani ya maisha, unachotakiwa ni kumkabidhi mungu,
..usilie mwanangu ongea...’mama yangu akamwambia na kumpa moyo.
‘Ndoto zangu za kuwa mtu maarufu zikazimwa kama taa ya
kibatili,maana nilikuwa na ndoto za kuwa mwanamitindo, nishone nguo za kila
aina,lakini ndio hivyo tena yakanikuta makubwa ambayo sikuyatarajia...kwasababu
ya ...ya...’akasita kusema huku akigeuka kumwangalia mume wangu ambaye kwa muda
huo alikuwa kainamisha kichwa chini.
‘Hebu tuambie ndoto yako hiyo ilizimikaje, kwa maana ulikuwa
unaishi na watu wenye uwezo wangeliweza kukusaidia sana tu, na nakumbuka mwanzoni nilipowatembelea ulionekana mwenye
furaha,ukasema kuwa umewapata wazazi wazuri wanaokujali...?’ mwenyekiti
akauliza
‘Ndio mwanzoni mambo yalikuwa mazuri sana, sikuwa na shida,
na niliwaona wazazi wangu ninaoishi nao ni kama baba na mama yangu, na kwa
ujumla wao walikuwa wachapakazi kweli, hawakutaka mchezo, na wakanikuta na mimi
ni mchapakazi kama wao, japokuwa ni za nyumbani, kwahiyo kila mmoja alikuwa akiamuka
asubuhi anakimbilia kwenye kazi yake, hakuna muda wa kuongea, na mimi nilikuwa
nafanya kazi yangu vyema, bila ya kusimamiwa,...ghafla nikahisi mabadiliko,
maabdiliko hayo niliyaona kwa baba, akawa analewa sana....’akasita kidogo pale
mume wangua lipoinua uso kumwangalia.
‘Usimwangalie, wewe ongea ,hana lolote kwa sasa, hawezi
kukufanya lolote....’akamwambia mama, ambaye alionekana kama muongozaji wake.
‘Kabla hata ya hapo, nilipokuwa nimekaa hapo kwa mwezi mmoja
tu, nilikuwa nimeshabadilika sana, mwili wangu ukawa mkubwa, nikawa naonekana
msichana,m, mmmh....’akatulia na mwenyekiti akasema;
‘Msichana mrembo...eeh’akamalizia mwenyekiti
‘Ndio ndivyo walivyokuwa wakiniambia watu, lakini mimi
sikujali, maana nilikuwa nafahamu ni kitu gani kimenileta hapa Dar, nikawa
nawajibika ipasavyo, sikuwa na muda na watu wa mitaani hasa wavula, ambao
walikuwa wakinisumbua kile nilipokuwa nikitoka, kwenda dukani au sokoni,
...huko nje niliweza kabisa kuwashinda, sikuwapa muda wa kuongea name, lakini tatizo
likawa ndani,....’akatulia kidogo.
‘Ulikuwa unanyanyaswa, au hayo mabadiliko yalikuwa yapi,
mpaka nyumbani kuwe ni mtihani kwako?’ akauliza mwenyekiti.
‘Baba, nilimuona baba
akinitizama kwa macho yaliyonitisha..sivyo kama ilivyokuwa mwanzoni’akasema
‘Kwa vipi hebu fafanua..na ulihisje hivyo, kwani mama yeye
alikuwa hakuangalii, kama anavyofanya baba ?’ akaulizwa na mwenyekiti.
‘Ni kama ..ya tamaa, maana anakutizama mpaka unaona aibu,
kuna siku nilimuuliza mama mbona baba ananitizama hivyo,mama akasema hajawahi
kumuona baba akifanya hivyo, akaniambia nifanye kazi zangu, nisiwe namwangalia
baba, kwani utajuaje kuwa mtu anakutizama, kama wewe humwangalii, nikaona aibu
kwanini nilimwambia mama hivyo, hata siku moja nilipomuona baba ananitizama
nikaona ngoja nimuulize kama baba yangu, yeye, akasema siku hizi nimekuwa mrembo sana...’akasema
‘Kauli hiyo ikanikwanza, nikaona nimwambia mama tena, kesho
yake, nilimuona baba kanikasirikia, na hakutaka hata kuitikia salamu yangu, nikahisi
huenda waliongea na mama kuhusu hayo niliyomwambia, na hali ikatulia kidogo,
lakini baadaye, nikaona ile hali inarudi tena, baba akawa ananifuata hata
sehemu ninyofanya kazi na kuanza kunitania, mimi kwa vile niliona ni baba
yangu, nafurahi,naongea naye tu, ila kwa tahadhari, kwani mama alishaniambia
kuwa nisipoteze muda kwa kuongea ongea...’akasema.
`Ikazidi, kwani nilishawahi kumfuma baba akinichungulia,....’akasema
na watu wakaguna
‘Akikuchungulia kwa vipi?’ akaulizwa
‘Kama nimetoka kuoga, nikiingia chumbani kwangu,kama mama
hayupo, baba anaweza kuingia chumbani kwangu ghafla na kujifanya kauliza kitu,
na wakati huo huenda nilikuwa nipo uchi, kwani .....’akatulia
‘Tunaelewa endelea..’akasema mama.
‘Kuna kipindi alikuwa akija usiku nimelala, na kuanza
kunifunua nguo...nikishituka, anasema alikuwa akinifunika vizuri,....’akasema
‘Oh, muongo mkubwa wewe, unawadanganya watu , mimi niliwahi
kukufanyia hivyo, nitakukomesha kwa uwongo wako...’mume wangu akasema kwa
hasira na wakili wake akamtuliza.
‘Je alikuwa akifanya hivyo, akiwa amelewa?’ akaulizwa
‘Hapana hiyo ilikuwa mwanzoni kabla hajaanza kulewa, na
alipooanza kulewa, ndio akaanza visa vyake...’akasema.
‘Haya tuambie hivyo visa vyake vilikuwaje...’ akasema
mwenyekiti
‘Alianza kunitongoza...’akasema na watu wakaguna
‘Eehe, alikuambiaje, na ulijuaje kuwa anakutongoza, na wewe
ulimjibuje vipi?’akaulizwa
‘Aliniambia kuwa ananipenda sana, na anataka...anataka tuwe
wapenzi wa siri...’akatulia kidogo.
‘Akasema atanifundisha jinsi ya kupata raha ya mapenzi,...’akatulia
kiogo.
‘Kwa kipindi kile mimi sikuwa namuelewa ana maana gani, ila
akilini mwangu ikanituma kuwa huyu anataka nifanye naye kiteno kibaya, ..’.nikamwambia.
‘Wewe nakuheshimu kama baba yangu, kwanini unaniambia mambo
kama hayo, yeye akasema hajanizaa, na mimi ninaweza kuwa hata mke wake, na yupo
tayari kuninunulia chochote hata kunijengea nyumba ya kifahari huko
kijijini,...mimi nikamwambia mimi nawaheshimu wao kama wazazi wangu siwezi kufanya
jambo kama hilo, na mama yangu alinikataza kabisa kufanya huo uchafu, kwani
mimi bado mdogo, na natakiwa kufanya hayo mambo nikiolewa...’akasema
‘Ulimwambia hivyo huyo baba yako, na ulijuaje kuwa anataka
mfanye mambo machafu, ?’ akaulizwa
‘Ndio nilimwambia hivyo, yeye aliniambia kuwa anataka
tufanye mapenzi, ...mapenzi alikuwa na maana gani, nilifahamu kuwa ananitaka
kwa mambo machafu , mama alishaniambia hayo kuwa mwanaume akisema anataka
kufanya mapenzi na wewe anamaana gani, ....’akasema.
‘Baba hakuchoka kunibembeleza na aliniambia nikumwambia mama
hayo anayoniomba, atahakikisha narudi kijijini na kuwa masikini wa
kutupwa,...nikaaogopa sana, kwani kule kijijini kweli baba yangu huyo
wanamuogopa sana....’akasema
‘Kwanini wanamuogopa?’ akaulizwa
‘Wanasema baba huyu ni tajiri na anaweza kukufanya lolote
asifungwe, kwa vile ana kampuni yake kubwa, na anajuana sana na polisi...na pia
anajuana sana na yule mwanasheria aliyekufa,...’akasema
‘Huyo mwanasheria aliyekufa naye alikuwa akiogopewa sana,
kuliko hata baba, kwasababu wanasema anafahamu
uchawi wa kisasa, anaweza akakuangalia hivi akakuambia yoye unayofikiria
kichwani mwako,anaweza kujua kitu gani ulikuwa ukifanya nyumbani kwako,,...anaogopewa
sana kule kijijini, na huyo alikuwa rafiki mkubwa wa baba yangu huyu
...’akasema
‘Kwahiyo alipokutongoza alikuambia kuwa usipomkubalia
atakuloga au atakufanya nini?’ akaulizwa
‘Hakusema kuwa ataniloga,yeye alisema atahakikisha mimi na familia yangu
tunasota, tutakikimbia kijiji,na kuwa omba omba...na mama yangu atakufa kwa
kihoro...mimi niliogopa sana alipofikia kusema mama yangu atakufa kwa
kihoro..hata hivyo sikumkubalia alivyotaka yeye...’akasema
‘Siku moja alikuja nyumbani, huwa ana kawaida ya kuja
akifahamu kuwa mama hayupo, na ananiambia niache kazi zote tongee, na siku hiyo
akanituma pombe, akanywa na kunilazimisha mimi ninywe, nilikataa kabisa,...kuna
muda akanituma maji ya kunywa nikaenda kumletea, akanywa, na mimi nikaondoka
kufanya kazi zangu , baadaye akaniita, nikashangaa ananimiminia maji ya kunywa
na kuniambia ninywe, kweli nilikuwa na kiu, lakini niliingiwa na wasiwasi
nikijua huenda kaweka kitu.
Akanishika kwa nguvu mpaka nikayanywa yale maji..yalikuwa
hayana ladha nzuri, sijui ilikuwaje, maana niliona macho yote mazito, ...nikawa
sina nguvu tena, akanibeba, hadi chumba cha akiba, akanilaza kitandani...hapo
akaanza kulia ...
‘Niliumia sana siku hiyo, aliniumiza..alinishika kwa nguvu,
na sikuwa an nguvu za kujitetea mwili wangu wote ulikuwa umelegea, lakini
niliweka kuhangaika, na.....akaniumiza....sikuamini yaani baba yangu
niliyemuamini kama baba yangu mzazi, alifikia hatua ya kunifanyia hivyo,mungu
ndiye anayejua, ...nikakumbuka mama alivyoniusia, nikajitahidi kutimiza wajibu,
nikawa namuogopa mungu, lakini baba akayaharibu yote hayo,..ningefanya nini,
..ina maana sisi kwa vile ni masikini wetu ndio watufanyie wanavyotaka,
niliumia sana siku hiyo...’akawa anaongea huku akiwa analia.
‘Endelea, usilie, ongea ili watu wasikie, unyama wa mtu
anayejiona mwema usoni kwa watu kumbe kavaa ngozi ya kondoo..’akasema mama.
‘Alipomaliza shughuli zake, akaondoka, huku akisema
nikimwambia mtu ataniua, atamuua na mama yangu...sikuweza kumwambia mama, wiki
nzima nikawa kama mgonjwa, nikawa nalia,hadi mama akaja kunifuma nikilia,
sikuweza kumwambia, kwa vile niliogopa kuvunja ndoa ya watu, na pia kwa vile baba
alinitishia kuwa nikimwambia mama atamuua mama yangu. Nilimwambia kuwa
nimemkumbuka marehemu baba yangu alivyokuwa akinipenda.
‘Tatizo mama kipindi hicho alikuwa na kazi nyingi, na kila
unachomuambia anakuamini, hakupenda kunidadisi sana, akanipa pole, na
kunishauri kuwa nisikumbuke sana kwani hayo ni mapenzi ya mungu, halafu
akaniuliza kuwa baba ananisumbau tena,...kwa kuogopa nikamwambia hanisumbui...
‘Ikapita hiyo siku, na wiki nikijua hilo limekwisha, siku
moja akiwa amelewa akanijia chumbani, ilikuwa usiku akanishika kwa nguvu,....na
karibu aniue, alinikaba nikafikiria kuwa huenda alikuwa anataak kuniua, nilipigana
naye sana, lakini akanizidi nguvu, baadaye akaanza kunizalilisha tena, ...yaani
karibu nimtapikie akwa jinsi nilivyo kuwa najisikia, harufu ya pombe na matendo
yake, ...nilijua nafanyia yote hayo kwa vile mimi ni masikini, nitasema nini
nieleweke kwa jamii, akafanya alichotaka akaondoka...kesho yake nikataka
kumwambia mama, lakini ikashindikana, kila nilipotaka kumwambia mama, baba anakuwa
karibu, na siku ikapita., Siku ikipiata unajikuta umesahahu, ukikumbuka inaishia
kulia.
Basi nikaona niache tu iwe kama iwavyo, akawa akifika, usiku
anajifanya halali na mama, anakuja kulala chumba chaakiba, akiona kupo kimiya
anakuja kwangu..nikawa najitahidi hivyo hivyo, ila sikuwa na raha, nikawa nalia
sana, na kuanza kukonda, na baadaye ndio nikagundua kuwa nina miimba..sikujua
kuwa ni mimba, siku hiyo nilikwenda kupima malaria, nilikuwa najisikia vibaya
sana, mama akaniambia nikapime malaria, ndio docta akaniambia nina mimba...
Nilipotoka pale nikapitia duka la dawa za mifugo nikanunua sumu
ya kuulia wadudu, baada ya kuuliza na kuambiwa hiyo dawa binadamu akinywa
anakufa mara moja,..akilini , nilishazamiria kujiua tu, sikujiona binadamu
mwenye thamani kwenye hii dunia, kwani sikuweza kuvumilia tena,nilishaona kuwa
nimefanya makosa makubwa, kwanini sikumwambia mama yangu huyo wa kufikia mapema...nilijiona
mzembe, ...mkosaji asiye na maana .
Akilini mwangu, nilijua hata nikimwambia mama kwa sasa hataweza
kuniamini tena, ataona mimi nilikubali kirahisi , na atanichukulia mimi ni
mzinzi, Malaya. Na pia sitaweza kumwambia mama, yangu mzazi, nitamuumiza sana,
mama ambaye siku zote alikuwa akinionya,nisije kujiingiza kwenye uchafu wa
zinaa, je nitmwambieje mama yangu, nikaona bora nikajiue tu....niondoke kwenye
hii dunia, wabakie wenye pesa zao.
Nilipofika nyumbani nikaikoroga ile sumu kwenye kikombe cha
plastiki, ilikuwa haiwezi kuonekana maji hayakubadilika rangi, nikaweka kwenye
meza karibu na kitanda changu, nikachukua karatasi na kuandika ujumbe
nikielezea kila kitu ilivyotokea...
Nilipomaliza hiyo kazi ya kuandika,... sikutaka nife kabla
sijatimiza wajibu wangu, kwahiyo nikahakikisha nimefanya kazi zangu zote za
nyumbani,...nilipomaliza nikaoga, nikamuomba mungu, nikaingia chumbani
kwangu,nikaichukua kile kikombe, ambacho kilikuwa na maji niliyochanganya na ile sumu ....
Wazo likanijia, kuwa nisifie chumbani kwangu, nikaona sehemu
nzuri ya kufia ni kule kule nilipozalilishwa , nikavua nguo zangu za kawaida,
nikachukua gauni kubwa jeupe, refu, lenye mikono mirefu, nikalivaa, halafu moja
kwa moja nikaenda chumba ambacho baba huwa analala, nikamuomba mungu tena, na
kulia, nikisononeka, na kila uchungu ulivyonizidi, ndivyo tamaa ya kujimaliza
ilivyozidi kunijia, kuna muda nilikuwa nasita kufanya hivyo, nikimkumbuka mama
yangu, lakini baadaye nikaona jambo jema, ni kuondoka hapa duniani, bila
kupoteza muda nikanywa yale maji niliyokuwa nimechanganya na sumu...
NB: Tuendelee na huyo binti, au ..tukutane sehemu ijayo.
WAZO LA SIKU:
Tuweni na ubinadamu kwa wafanyakazi wetu wa ndani, visa vingi vinaelezewa jinsi
gani wafanyakazi hawa majumbani wanavyonyanyaswa au kuzalilishwa, lakini wengi
wanaofanyiwa hivyo wanashindwa kuongea ukweli kwa wazazi wao kwa kuogopa , na
wengi wanaofanyiwa hivyo ni watoto wa kike,wasichana.
Akina mama mnaoishi na wafanyakazi wa ndani, mliowachukua
mabinti wadogo, tujaribu sana kuwa karibu na hawa wasichana, tukumbuke kuwa
hawa ni watoto wa wenzetu, mama zao ni kama wewe, tukiona mabadiliko yoyote, yasiyo ya kawaida, tutumie
busara kuwahoji hawa mabinti,, huenda kuna jambo linaloendelea kwa huyo binti,
mchukulie huyo kama ni mtoto wako, ujue litakalofanyika kwake ni sawa na
lingelifanyika kwa watoto wako mwenyewe. Hakupenda awe hivyo, na wewe umepewa
dhamana kutoka kwa mzazi wake, tusije tukaona kuwa kwa vile huyu sio mtoto wangu haijalishi sana, ...hiyo ni sawa na kusema mkuki ni kwa nguruwe tu, huwezi jua,maisha ni kupanda na kushuka,.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment