Mwenyekiti, akauliza tena;
‘Huyu mtu wenu ameenda wapi, mnakumbuka nyie ndio mliotaka
awepo hapa kwenye hiki kikao mkifahamu kuwa anatafutwa kwa uhalifu, na mimi
nikamthibitishia mkuu wa kituo, wa upelelezo kuwa, huyo kijana atakuwepo hapa
hadi mwisho wa kikao, na mimi nitamkabidhi kwake, sasa kaondoka, mnataka mimi
nieleweke vipi, kuwa namlinda kwasababu ni mkwe wangu, mdogo wa mkwe wangu,
niambieni huyu mtu kaenda wapi...?’ akauliza mwenyekiti
‘Mwenyekiti, huyu mtu alitoka kipindi tunaangalia hiyo lap-top
yako, na hakuna aliyefikiria kuwa huyu mtu ataondoka, kwa vile alifika hapa kwa
hiari yake mwenyewe, mimi sikumuona wakati anatoka, lakini hata mtu angemuona angelifikiria labda anakwenda kujisaidia...’akasema rafiki wa mume wangu.
‘Haiwezekani mtu atoke humu ndani bila ya mtu yoyote humu, kumuona, docta , wewe na mke wako mlikuwa huku nyuma,
wakati tunaendelea na hilo zoezi, hususani mke wako ambaye kwa muda mwingi
alikuwa amekaa huku nyuma, alikuwa wa mwisho kuja kuangalia tunachokifanya,
kwahiyo nina uhakika, kuwa atakuwa alimuona huyo kijana akitoka, kwanini tusiwe
wakweli, ...’akasema mwenyekiti.
‘Hapana mimi sijamuona akitoka, kiukweli mimi muda mwingi
nilikuwa nimegubikwa na mawazo yangu, sikuwa nikimtizama mtu, na hata
ningelimuona akitoka ningelijuaje kuwa anatoroka, sikumuona kabisa...sikuwa na
haja ya kumuangalia yeye, nina mambo yangu mengi kichwani ya kuangalia,
kwanini nihangaike kumchunga yeye, ....’akasema huyo mke wa rafiki ya mume
wangu, na mwenyekiti akamwangalia kwa mashaka, na kumuuliza
‘Unavyozungumza hivyo hueleweki, ina maana haupo pamoja na
sisi hapa kwenye kikao, sasa umefuata nini, ni kweli unaonekana kabisa kama
vile haupo ndani ya kikao, upo kimwili lakini kiakili unaonekana haupo kabisa,
kuna tatizo gani linalokukabili?’ akauliza mwenyekiti.
‘Haya ni ya kwangu, niachieni mwenyewe, kama ikibidi Itafika
muda wake, mtayafahamu, ....naona tuendelee na kikao....’akasema huyo mke, na
mimi nikaona niingilie kati nikasema;
‘Baba , hilo la kutoroka kwa shemeji yangu, tuwaachie polisi
wakiuliza tutawaambia ukweli, sisi sio walinzi wa huyo mtu na sisi
hatutawaficha ukweli,ni kuwa huyu mtu alikuja kwenye hiki kikao na baadaye akatoroka,sisi tungelifanyaje...’nikasema
‘Hilo unalitamka tu kirahisi kama mtu siyekwenda shule, hivi
kweli kuna mtu atakuamini ukisema hivyo, wakati mimi nilishachukua dhamana juu
yake, hivi nyie taifa la leo mna nini akilini mwenu, msipende kuchukulia mambo
kirahisi tu, kitendo kama hiki kinatutia dosari, uamanifu wetu unapungua,..'akafoka mzee
'Kiukweli mimi sipendi
kabisa tabia ya namna hiyo...unapoahidi kitu, unatakiwa ukitimize, ...mimi sio
tabia yangu ya kukubali dhamana halafu ninakuja kuihini,mnaniharibia mwenendo
na tabia yangu..’akasema mwenyekiti na kuanza kumpigia simu huyo mkuu, sikutaka
kumzuia tena, yeye akaongea na huyo mkuu akamweleza ilivyokuwa na alipomaliza
kuongea naye akasema
‘Sawa tuendelee, wanamfuatilia wenyewe, keshajiharibia
kabisa, ...’akasema
‘Kwanini mnamfanya hivyo mdogo wangu,kwani ungekaa kimiya
unafikiri wangekuja kukuuliza, nyie mnajipendekeza kwa hao watu, lakini
hawatawasaidia lolote, siku yako ikifika wanakusweka ndani kama hawakujui’ akasema
mume wangu, na hapo nikakumbuka jinsi alivyomnong'oneza kitu muda uliopita
‘Hiyo ndio tabia ambayo siitaki, na hilo nimekuwa
nikiwakanya, ....kama umezoea tabia hiyo ya uwongo, mimi kwangu haipo, na
kwanini unasema tumemfanya nini mdogo wako, hakuna aliyemfanya kitu mdogo wako,
sisi tunatimiza wajibu wetu kama raia wema, ukiishi kwa kufuata sheria, muda
wote unakuwa na amani, lakini kama unaishi kiujanjajaja,ukawa mkiukaji wa
sheria, ukawalinda wahalfu muda wote utaishi kwa mashakamashaka....’akasema
mwenyekiti.
‘Mdogo wangu hana hatia,yeye sio mhalafu...polisi
wanamshuku bure,wamshindwa kazi yao sasa wanapapatika...na huenda kaondoka hapa
kutokana na vitisho vyenu, kama litamkuta baya nyie ndio mtawajibika...’akasema
mume wangu.
‘Tuendelee na kikao chetu, atawajibika mwenyewe, yeye
anajiona ni mtoto wa mjini, haya ngoja tuone ujanja wake utaishia wapi. Na
wewe, nakuonya, sasa sitaki utani,tuambie, imekuwaje, ukawa na mkataba tofauti
na ule mliokubaliana na mke wako, na ukijua kuwa huo ni ukiukwaji wa sheria,umekiuka
kiapo chako ulichokiweka kisheria wewe na mke wako, ndivyo unavyoishi hivyo,...?’
akauliza mwenyekiti.
‘Mimi sijui kama huo mkataba ni tofauti na ule tuliokubalina
na mke wangu, kwangu mimi nauona ni ule ule,na kama nilivyowataka, japokuwa
msajili kasema hivyo, nahisi nay eye kaongea tu bila ya kuuangalia mkataba huu
nilio nao, angeliona angeligundua kuwa hata wao wamefanya makosa, kwanini hawa
watu wakubali jambo, bila kunihusisha mimi, mimi ndiye mume, niye ninayefahamu
ukweli wa huo mkataba, kwani ni wao waliubuni,....kama nyie mnadai kuwa uligushiwa
mimi sijui...na ninani kaugushi?’ akauliza mume wangu.
‘Unauliza ni nani, hilo swali tunakuuliza wewe, kama sio
wewe, na kama hujui wakati wewe umekiri hapa kuwa wewe ni mume na wewe ndiye
unayebeba dhamana za familia, haya tuambie ni nani aliyeugushi huo mkataba,
kwanini kunapatikana mikataba miwili, huu mkataba ulio nao unatoka wapi, hayo
ni maswali yako ya kujibu...’akasema mwenyekiti.
‘Hayo nimeshawajibu, sijui...ninachojua ni kuwa huu mkataba ndio halali.....na kama sio halali mimi sijui, kwangu mimi hadi sasa bado sijaamini...’akasema na watu wakamwangalia kwa mashaka, na alipoona watu
wanamwangalia yeye, akasema;
‘Kama ni hivyo, ili niwaamini, mnao huo mkataba mnaosema ni
halali?’ akauliza
‘Umeshaonyeshwa na msajili wataka upi tena, eeh, usitusumbue .....’akasema mwenyekiti
‘Ili niwaamini naomba utolewe hiyo nakala nyingine mliyo nayo, nyie,..., ili tuone kweli kuwa upo
tofauti na huu....’akasema
‘Mimi naona lengo lako ni kutupotezea muda, hebu mke wa
familia mtolee huo mkataba, anaoutaka yeye, na kwa amri ya kikao hiki, halali,
tunataka ujibue maswali yetu, kwani kila ulichokitaka umekipata, kwahiyo timiza
wajibu wako, sisi tumeshatimiza wajibu wetu....’akasema mwenyekiti.
Mume wangu akanigeukia, huku akionyesha kushangaa, pale
aliponiona nikitoa mkataba kwenye mkoba wangu, nikauinua juu, na kusema;
‘Mkataba halali ndio huu hapa, mkataba uambao umeuulizia
ndio huu hapa...’nikasema na yeye akabakia mdomo wazi, akiwa katoa macho ya
kutokuamini.
‘Mpe wakili wenu wa familia authibitishe kuwa ndio
wenyewe,..’akasema mwenyekiti, na mimi nikainuka na kwenda kumkabidhi wakili wa
familia ambaye aliufunua akaanza kuukagua na kufanya kama alivyofanya kwenye
mkataba aliokuwa na mume wangu, halafu akatabasamu na kuuliza;
‘Umeipatia wapi hi nakala, ndio wenyewe kabisa, sasa mambo
yamekwisha, tumemaliza kazi...’akasema kwa furaha.
‘Siamini ina maana mke wangu umeamua kunifanyia hivyo,
...ina maana ..haiwezekani, kumbe,..hapana,....umaupata wapi huo mkataba,
uli...uli...oh, huyu mdogo wangu yupo wapi’akasema huku akiwa kashika kichwa.
‘Haya mume wa familia, sasa kazi inaanza, natumai sasa upo
tayari, hatuna muda wa poteza,kama wenzako wamekusaliti, utakwenda kuwauliza
baadaye, sasa hivi ni kazi ...jibu swali letu, kama ningelikuwa mimi ndio wewe
ningekiri makosa na kukubali yaishe, maana mwisho wa hadaa ni fedheha, kwanini
unataka ufedheheke’akasema mwenyekiti.
‘Swali gani,...sikumbuki kama uliniuliza swali...’akasema
‘Nilikuuliza kuwa kwanini huo mkataba uliokuwa nao ni
tofauti na mkataba halali, tunahitaji kulitambua hilo, kama wanafamilia, kama
wajumbe wa kikao hiki, na ikibidi pia sheria inatakuhitajia uilezee kwani wao
bado wanatafuta kiini cha hilo tatizo, ilikuwaje kuwepo na mikataba miwili,..’akasema
mwenyekiti.
‘Ndugu mwenyekiti, mimi muda mwingi nilikuwa naumwa, na
siwezi kujua jinsi gani huo mkataba ulivyobadilika, mimi hadi sasa sioni
tofauti yake, sijaona hayo mabadiliko ni yapi...’akajitetea hivyo.
‘Kwahiyo bado hutaki kukiri kuwa kuna hujuma mlipanga, kuwa
mlifanya kosa, kwahiyo kama wanafamilia, kama kikao tukufikirieje, unaonekana
unatujaribu, unatuona sisi hatuna akili?’ akauliza mwenyekiti.
‘Sijasema hamna akili, lakini siwezi kusema mimi nimefanya
hujuma, nikiri kosa ambalo sijalifanya, hilo halipo,kwani kama ni hujuma iliyofanywa mimi siijui, huenda kuna
watu walifanya hivyo, bila ya mimi kujua, hasa kipindi kile nilichokuwa naumwa,
nilipopata ajali, ndio maana nimekuwa niking’ang’ania kuwa hiyo katiba ndiyo
ile katiba niliyo kuwa awali na ndiyo iliyokuwa sahihi, mimi sikumbuki kuwa na
katiba nyingine tofauti..mnakumbuka kuwa ajali hiyo ilinifanya niwe
nasahau...’akajitetea
‘Lakini kama sikosei, katiba hiyo iligundulika kuwa
imebadilishwa kabla hujapata ajali, ina maana mipango hiyo mliipanga mapema, na
mlikuwa mkiifanyia kazi hatua kwa hatua,, na ajali hiyo ilipotokea mkapata sababu
nyingine, na hiyo ajali ilitokea mkiwa kwenye michakato yenu ya kukamilisha
hiyo hujuma....’akasema mwenyekiti.
‘Mimi hayo siyajui, nayasikia kutoka kwenu, na kwa jinsi
inavyokwena hapa, mimi naona nitafute wakili wangu, kwanini naona mnataka
kunitia hatiani, na mimi sitaweza kujitetea kwa hali kama hii...’akasema
‘Kwahiyo unarudi kule kule, kuwa hili swala kwa vile ni la
kisheria zaidi, na linaonekana ni kuvunjwa kwa sheria ilitambulikana kisheria,
twende ngazi za juu, tulipeleke hili swala mahakamani...’akaulizwa
‘Sijasema twende mahakamani, ...sio lazima twende mhakamani,
hapa tuna mawakili, lakini hatupo mahakamani, wakili atanisaidia kunitetea na mimi,
...mimi hapa sina mtetezi wote mnanisakama mimi, na inafika mahali siwezi
kujitetea kisheria.....’akasema.
‘Hakuna anayekusakama wewe, wewe ndiye uneyeweka mazingira
ya kuonekana, hivyo, kama ungelikubali kusema ukweli, haya yote yasingelitokea,
kwanini usikubali kuwa kuna shetani aliwapitia, mkaamua kupanga hayo
mliyoyafanya, lakini kwa vile dhamira mbaya haijengi, basi imefika
kikomo,kubali, tuangalie jinsi gani tutalimaliza hili tatizo...’nikasema.
‘Wewe mke wangu hujui tu, mimi hapa nafanya kila iwezavyo
kuulinda ndoa yangu, wenzako wanataka ivunjike, hili lipo siku nyingi, kama
kweli unanipenda, ulitakiwa uwe pamoja na mimi....huoni kuwa wamenitega,...kama
hupo na mimi bado wewe ni mke wangu,...’akasema.
‘Sikuelewei ukitaja neno kupenda,....’nikasema.
‘Unaona, nilijua kabisa mnanitega, wewe na familai yenu,
mumelipanga hili makusudi,na kwa vile umeshaona mumefanikiwa mipango yako, sasa
unatafuta njia za kuniharibu kabisa maisha yangu, mimi sikubali....na kwa hilo
la kukubali kuwa nimefanya kosa, mimi hadi hapo sioni kosa langu kabisa, mimi
kauli yangu ni hiyo kuwa sijui kama hiyo katiba iligushiwa, na hiyo mipango
mnayosema nyie siijui, ni nani walifanya mnajua nyie, mimi sijui,....kwanini
nikubali jambo ambalo silijui...mnataka niseme uwongo.’akasema.
‘Kwahiyo unataka tulitolee ushahidi kama hilo la hiyo katiba
kuwa sio katiba halali, ujue kila tutakavyofanya hivyo ndivyo na sisi
tunashindwa kukuamini tena, na hapo ina maana kuwa wewe haupo nasi..unajiweka
mbali na sisi, unaikimbia ndoa yako kiujanja, huku unajifanya upo nayo’akasema
mwenyekiti.
‘Tangu hapo naona mumeshaniweka pembeni, sizani kwenye nafsi
zenu kuwa mimi nipo na nyie, mumeshaniweka kwenye kundi la wahalaifu, unaona
mdogo wangu ambaye hana kosa mumeshamuitia polisi, na nahisi hata mimi
mtanifanyia hivyo hivyo,niwaulize kama angelikuwa ndugu yenu wa damu awe
anatafutwa na polisi, mngelimfanyia hivyo mnavyomfanyia ndugu yangu,au kwa vile
sio ndugu yenu?’ akauliza
‘Huo ni unyonge unaojitakia, nimeshakuambia, wewe kama mume
wa familia unatakiwa upambane kiume, lakini katika misingi ya ukweli na haki,
hiyo kauli yako uliyoongea sasa hivi kuwa tunakuonea wewe na ndugu yako, ni
kauli ya kujizalilisha, kujishusha, ...ongea ukweli, toa hoja zenye mshiko,
tuoni ukweli upo wapi,...’akasema mwenyekiti.
‘Ukwelii gani nitakaouongea sasa hivi mniamini, mimi
sijajizalilisha, ndio maana ninaendelea kukataa hayo mnayonishinikiza nayo,
haya nipeni huo ushahidi kuwa mimi nilikuwepo kwenye huo mpango wa kufanya hayo
yaliyotokea...maana ndivyo mnavyotaka nyie, mimi nimeshawambia ukweli wangu,
hamunikubalii, sasa kwa vile mnaona nasema uwongo, nikosoeni uwongo wangu...’akasema
kwa kujiamini.
‘Kwa hali hiyo ni kuwa hutaki kusema ukweli, unataka sisi
tuutafute kwa nguvu za ushahidi, ..kama unataka iwe hivyo, sisi tutafanya,
lakini kwa mtaji huo ni kuwa wewe hutaki kushirikiana nasi, hutaki kuwa mwenzetu,
ukatusaidia tukalimaliza hili tatizo kama wanandugu....na kwa hali hiyo
ikibainika na ndivyo ilivyo, tukatoa ushahidi, basi hatuna jinsi nyingine,
hukumu itafuatia kitanzi chenu wenyewe kitakuhukumu.’akasema mwenyekiti.
‘Kwahiyo nyie mnataka mimi niseme nini?’ akauliza
‘Sema yote yaliyotokea, jinsi gani mlivyoibadili hiyo
katiba, na kwanini ,lifanya hivyo. Na mlikuwa na nani na nani, haafu unaomba
msamaha yamekwisha,...sisi kama kikao tutakaa na kuangalia jinsi gani ya
kulimaliza... huo ndio uadilifu na utawala bora, kwanini mnataka msutane
kwanza, mshikane mashati, hata ifikie damu kumwagika, ...hiyo ni tabia ya watu
wasio waungwana’akasema mwenyekiti.
‘Mimi sio mtoto mdogo, wa kudanganywa kihivyo, nawafahamu
sana, hapo mnataka kunitega tena, kama mlivyonitega hapo mwanzo, ...ukweli
niliouongea ni huo huo, kama kuna ukweli mwingine niambieni nyie, na
mnithibitishie na mimi kama nitaona kuna ukwel ambao niliusahau ,au nilikuwa
siujui, maana mengi yametokea nikiwa mgonjwa, sikumbuki, nikumbusheni nyie,....’akasema
‘Na ikiwa ni hivyo, tukakuthibitishia kuwa ni mpango ilipangwa
na wewe ukiwemo ukiwa na akili zako timamu, ukishirikiana na wenzako, kwa ajili
ya masilahi fulani, .. upo tayari
kuwajibika?’ akaulizwa
‘Hiyo ni juu yenu...lakini mimi sijui kama kulikuwa na mipango
huyo, mimi sikumbuki....’akasema.
‘Unakumbuka sana, unalifahmu sana, ndugu mwenyekiti naona
tunapoteza muda, huyo mtu nimeshamuelewa, ...anachotaka ni kuona je tunafaamu
hiyo mipango yao, je tunafahamu hayo aliyoyafanya yanajulikana,...hataweza
kukubali na kusema ukweli...mimi naona tuendelee na kikao, na hatima ijulikane,
mkataba upo utafanya kazi yake...’nikasema.
‘Kutokana na uchungzi uliofanyika, inabainisha wazi kuwa
mipango hiyo ilikuwepo kabla yaw ewe hujapata ajali, ...wao waligundua kuwa
kuna mikataba miwili, mapema kabisa, wakawa wanafanya uchunguzi na walipombana
mtu wao, mtu wao kwa vile ni muadilifu akakubali kusema ukweli, kuwa kuna
shinikizo lililomfanya abadili mkataba ule halali na mkataba huo mpya
alioletewa, na
mtandao....’akasema mwenyekiti.
‘Mimi hayo sijui....sikumbuki, kama nilivyowaambia
ninachojua mimi , hii ndio katiba, niliwahi kuwekeana na mke wangu,kama
kulitokea kubadilishwa, basi labda kuna mtu alifanya hivyo, akanitumia mimi
kama chambo, kwa vila anafahamu kuwa kumbukumbu zangu hazikiwa sawa...’akasema
‘Alikutumia kwa msilahi ya nani, yake au ya kwako, hebu
tuangalia hiyo katiba, inamgusa nani, na kwa masilahi ya nani,
...usitudanganye, na kama unahisi hivyo kuwa labda kulikuwa na mtu kafanya
hivyo kukutumia wewe, basi tuambie ni nani...’nikasema.
‘Ni kwa masilahi ya familia yangu, mimi na wewe, ukiangalia,
katiba inatuhusu mimi na wewe, na ya kwamba hakuna mtu mwingine wa kuingilia
masilahi yetu, zaidi ni mimi na wewe....’akasema
‘Ni ile ya mwanzoni ilikuwa haifanyi hivyo?’ nikamuuliza
‘Mimi sijui hiyo katiba ya mwanzoni ilikuwa inasemaje,
sikumbuki, kwani ninachofahamu mimi ni haya kwenye katiba hii, labda nyie
mnikumbushe ..’akasema.
Mwenyekiti akamtizama binti yake, na kutikisa kichwa, na
wajumbe wengine kwenye kikao wakaonekana kuchoka, na hapo mwenyekiti akasema;
‘Naona tupate mapumziko kidogo, tukirudi tunaingia ajenda
nyingine, tukitumia katiba halali, mliyojiwekea wenyewe, huu ujanja
wanaoendelea hapa, tumeshaufahamu,tunafahamu kuwa baada ya ajli ulipoteza
kumbkumbu, na mengi yalifanyika kipindi hicho, ...huenda ilichukuliwa hivyo
kama mwanya wa kukamlisha huo mpango, ...’akasema mwenyekiti
‘Kwahiyo unamaanisha kuwa kwenye huo mpango tulipanga mimi
nipate ajali, ili baadaye nisingizie kupotewa na fahamu,yafanyike kama
yalivyotokea ...hivi kweli kuna mtu mwenye akili zake anaweza kufanya jambo kama hilo la hatari, ina
maana hata hawo madakitari walionihudumia wanahusika na huo mnaouita mpango, maana wao
wanajua fika kuwa nilipotewa na fahamu , na kupoteza kumbukumbu kwasababu ya
hiyo ajali.....?’akasema mume wangu.
‘Hatukatai kuwa kutokana na hiyo ajali ulipoteza kumbukumbu
na hali hiyo akasabbisha wewe kutokukumbuka mambo ya nyuma, lakini hiyo kwa
mtizamo wenu,na uchunguzi wetu hali hiyo ilikuwa imetokea kwa muda fulani tu, ambao kitalamu
inajulikana, ...wewe ukauendeelza ule muda, na kuendelea kujifanya kuwa bado
unaumwa, ili kutimiliza malengo yenu....’nikasema.
‘Hivi kweli mke wangu unaweza kusema maneno kama hayo, naona
kweli umenichoka, sikujua kama utafiki hatua hiyo, ....kuna nini kibaya
nilichokufanyia ambacho kimeweza kukugeuza na kunichukia kiasi hicho, mke wangu,
mimi sio kama wanavyonifikiria hwazazi wako,kwanini nikudanganye mke wangu,
kuwa naumwa na uzidi kuteseka, ili iweje, hapana, siwezi kukufanyia hivyo, hizo
ni hisia umepandikiziwa, usiwasikilize watu wasioitakia ndoa yetu
mema....’akasema.
‘Dunia ya sasa imejaa hadaa, mkwe wangu mimi nakufahamu
sana, usijifanye kuwa hayo yaliyotokea huyafahamu, nakufahamu na washirika wako
wote,mimi niltaka kuona kuwa kweli labda umebadilika kama alivyokuwa akidai mke
wako, lakini kwa haya uliyoyaonyesha leo, sioni ajabu ....kuna watu siku hizi,
wameamua kutumia udhaifu wa wenzao kwa jili ya kufanikisha malengo yao, ..kauli
yako utakayoitoa mbele za watu , wao wanaitumia kwa malengo yao....tukio dogo,
ambalo nyie mtaliona ni la kawaida tu, wenzenu wanalifanyia kazi kwa masilahi
yao...’akasema mwenyekiti.
‘Ajali iliyokupata, ilichukuliwa kama nafasi nzuri ya
kufanikisha malengo yenu, na huenda kulikuwa na hujuma kwenye gari
lako,...ilipangwa makusudi, ili itokee, ....lakini hilo halikuweza
kuthibitishwa, nia ilikuwa nife , kwani siku hiyo nilipanga kulitumia hilo gari
lako,....lakini kwa bahati , ukalichukua mwenyewe, sijui ni kwa kusahahu au....’nikasema
‘Huo uwongo wa hali ya juu...’akasema mume wangu.
‘Hiyo ajali ilipotokea, ikawa imefanikisha baaadhi ya mambo
yenu,hata kama utakataa kuwa hiyo ajali ilipangwa, kwa nia ya kumuua binti
yangu, lakini ilichukuliwa kama sehemu ya kuwezesha mambo mengi,mengi
yalifanyofanyika yalifanyika baada ya
hiyo ajali, ili usiwepo nyumbani, li isionekane kuwa wewe unahusika, ...’akasema
mwenyekiti na mume wangu akatikisa kichwa kukataa.
‘Kwa vile tumeongea sana na huu ni muda wa kupumzika, ...hiki
kikao kinakupa nafasi ya mwisho, ya kufikiria kwa makini..., tukirudi uje na
ukweli, kama utaendelea kutuficha huo ukweli ambao sisi tumeshaujua, kikao,
kitakuchukulia wewe kama mhalifu ambaye kafanya kosa, lakini hataki kukiri kosa,
na hivyo, unatuweka katika nafasi ya kutengeneza kesi, ya kifamilia,na hukumu
tutaitoa wenyewe, kama inatosha kuishia kifamilia, tutaimaliza kifamilia, kama
itabidi, na kwa mujibu wa sheria, kuna mambo ambayo hatuyawezi kuyahukumu, hayo
tutawaachia wenyewe, lakini cha muhimu, ni ukweli....’akasema mwenyekiti.
‘Sasa tukapumzike kidogo, nafahamu bado kuna ajenda nyingi,
zenye maswali mengi yanayohitajai majibu, na yote ni dhidi yako, na moja
wapo,ni kutuambia kwanini ulimuacha wakili wenu wa kawaida ukaamua kumtumia
Makabrasha, hivi wewe kweli ulikosa mawakili, mpaka uamue kumchukua Marehemu...hilo
nakufungua akili tu, kuwa sisi tunafahamu mengi zaidi ya unavyofikiria!’
Akasema mwenyekiti na kumfanya mume wangu amuangalie mwenyekiti kwa mshangao.
‘Makabrasha ndiye aliyekuwa kichwa chenu, mbinufu wa hayo
yote, ni nani asiyemfahamu Marehemu kwa mambo yake, yeye anatambulikana kwa mbinu
zake, za kugeuza sheria, kwa masilahi yake binafsi,haat wewe mwenyewe,unamfahamu
hivyo, hii ni kuonyesha kuwa ulimchukua
kwa lengo maalumu ili mfanikiwe kwa kile
mlichokipanga, na mliona kuwa mkataba ndio njia sahihi ya kuyafanikisha hayo
malengo yenu...mkaona muutumie huo huo,..’akasema mwenyekiti.
‘Kwahiyo hatua ya kwanza ni kuubadili huo mkataba, kwa
masilahi yako, ambayo baadaye wewe bila kujua kuwa mwenzako alikutega, ni kuwa
masilahi hayo yanakuja kuhamie kwake, ndio maana akakushawishi tena kutengeneza
mkataba mwingine wa makabidhiani, kati yako wewe na yeye, maana huo mkataba
wako na mke wako mlioutengeenza ulishakupa amdaraak ya kufanay upendavyo...yote
hayo tunayafahamu...’akasema mwenyekiti na mume wangu akawa kainama chini.
‘Marehemu anatambulikana kwa uhalifu wake wa milungula,
wenzetu huko majuu, wanaita blackmail.
Yeye kwasababu lisoma soma huko, akaona kwa wabongo, hawana ufahamu sana na
mambo hayo, basia anaweza kuutumia njia hiyo kujitajirisha,...baba, mkwe wangu,
ilikuwaje wewe umtumie Makabrasha kwa jambo la kifamilia kama hilo ambalo ni very sensitive,...usitudanganye,
inaonyesha kabisa yeye alishakuingiza kwenye mitego yake, ukawa huna jinsi,
sasa kwanini suituambie ukweli,ili tuweze kuliweka hili jambo sawa,...tutahitajai
majibu yako, ...tukirudi,...’akasema mwenyekiti, na mume wangu akasema;
‘Makabrasha ni rafiki yangu wa siku nyingi, kumtumia mimi
sio jambo la ajabu sana, na mengi anasingiziwa, tu, mimi sipendi kumuongelea
marehemu, lakini nitajitetea kwa nafasi yangu, na kumtetea yeye ikibidi,lakini
mimi sitapenda kumuongelea yeye sana, maana hayupo duniani, kama kuna lolote
dhidi yangu,nitajitetea mimi kama mimi kadri ya uwezo wangu, kwasababu sina
hatia, nilikuwa natimiza majukumu yangu kama mume wa familia, na kuyafanya yale
niliyoona ni sahihi, kama kuna niliyotelekeza ni katika kuhakikisha naweka
mambo sawa, mengi mnayonisakama nayo hapa ni ya kupangwa tu, ili ndoa yangu
ivunjike..mimi nitaipigania ndoa yangu na sitakubali ivunjike.........’akasema
‘Tutaona tukirudi, kama nikuivunja ndoa yako utakuwa umeivunja
ndoa yako wewe mwenyewe, kwani wanasema mume au mke mjinga huivunja ndoa yake
kwa mikono yake mwenyewe,...na wewe huna tofauti na watu hawo,..kama sivyo,
thibitisha kwa kusema ukweli, vinginevyo baba, ...lakin tusipoteze muda
tukapumzike, tusiwachoshe watu, au mnasemaje.?’akasema mwenyekiti, na kabla
watu hawajajibu mume wangu akasema;.
‘Mimi sijaivunja ndoa yangu, niliyokuwa nayafanya ni katika
kuijenga ndoa yangu kwa njia iliyosahihi,ili na mimi nionekane mume, kwa hivyo,
mimi nasema hivi ndoa haivunjiki,
hilo nawahakikishia kwasababu hakuna kosa la ajabu hapo la kuvunja ndoa yangu, katiba
niliyokuwa naitambua mimi ilinipa mamlaka kama mume, kama muoaji, nifanye yale
niliyoona ni sahihi kwa masilahi ya familia yangu,....’akasema halafu akageuka
kuniangalia mimi na kusema;
‘Mimi sijakwenda kuingilia ndoa za watu, mbona nyie mnakuja
kuingilia ndoa yangu...mimi nimeoa, sijaolewa, kwanini hamnipi uhuru ndani ya
ndoa yangu, nilikuja kuoa, sikusema kuwa niwe na watu wa kunisaidia,...baba na
mama yangu wapo kijijini, hata siku moja hawajawahi kuja kuniingilia kwenye
ndoa yangu , nawashangaa nyie, ...ni kwa vile mlikuwa hamtaki nimuoe binti yenu
au....niacheni niijenge ndoa yangu mwenyewe, mimi sitakubali mtu aniingilie,
mimi ni mume wa familia na nitabakia kuwa hivyo, ...’akasema na mimi nikacheka na kusema;
‘Unasema nini, eti kuwa ndoa bado ipo, wewe kwa vitendo ulivyovifanya,
bado unashikilia kuwa ndoa bado ipo, ..vitendo vyako vimeshaivunja ndoa yako tayari,
ina maana gani kung’ang’ania kuwa ndoa ipo na nani,...hujisuti moyoni, hujuti
moyoni, ukakiri kuwa umefanya kosa...nimeshakutambua unachokitaka nini,,
unachotaka kwangu ni kufanikisha malengo yako tu, yenye mlengo wa kutwaa mali, na
ili uje kunizalilisha baaaye, hapana, hilo skubali, leo tutajua moja...’nikasema
na yeye akaniangalia kwa jicho baya, akisema;
‘Na wewe mke wangu, usiseme neno, mengo umeyasababisha wewe
mwenyewe, ...ukitaka niyasema nitayasema, ndio maana nasema ndoa ipo, na
haitavunjika..na kama umeamua wewe kuwa ndoa haipo mimi sikubali, nitaisimamia
kwa nguvu zangu zote...’akasema huku akipiga meza kwa ngumi , na watu ambao
walishaanza kutoka nje, kwa ajili ya mapumziko
wakawa wanamuangalia na mwenyekiti akarudi na kuuliza
‘Jamani kuna tatizo lolote...?’ akauliza mwenyekiti na mume
wangu akasema
‘Hakuna tatizo tunaongea tu na mke wangu...’akasema huku
akijaribu kukunjua uso wake.
‘Mimi, nimesema huu ni muda wa mapumziko, tutakutana baada
ya nusu saa, mimi natoka, nimeitwa na mkuu wa polisi wa kituo chenu, nitarudi,
kabla ya muda huo, nikirudi nataka tuyamalize yote, na haki itendeke,....’akasema
na m ume wangu akamwangalia kwa mashaka, na kusema;
‘Unaona, baba yako anakwenda wapi,....ndio zenu hizo,
anakwenda kuwaweka sawa hao watu wake, nakuambia ukweli mimi siogopi, najua
anachotaka ni kumfunga mdogo wangu, akija na mimi ananitafutia sababu za
kunifunga, kwa hali hiyo, mimi napinga kuendelea na hiki kikao, mpaka aje
wakili wangu...tukiahirishe hiki kikao’akasema huku akiwa kashika kichwa, baadya akalivaa koti lake huku akiendela kushika kichwa, kama vile kinamuuma, akaanza kuondoka.
‘Eti nini...unakwenda wapi wewe...?’ nikamuuliza.
NB : Haya tutaona tukirudi mapumziko kama kikao kitaendelea.
WAZO LA LEO: Kuna
matendo tunayotenda kila siku hasa kwa wanandoa, matendo ambayo kiimani, kimila, na kiutaratibu
yanakuwa moja kwa moja yameshavunja miiko, na mikataba ya yale tuliyokubalina, hata kabla
hautajoa kauli zetu. Kila kitu kina makubaliano na masharti yake, ndoa ina
masharti na makubaliano yake, ndio maana ikaitwa ndoa. Je tunafahamu nini maana
ya ndoa! Je kama ndoa ni kuhalalisha mahusioano kati ya wawili hao, iweje mtu
umsaliti mwenzako. Mtu anayeisaliti ndoa yake ni sawa na yule mtu anayeacha nyama yake safi nyumbani na kwenda
kula nyuma iliyooza maporini, huyo keshavunja ndoa yake kivitendo,...Tuweni
makini na ndoa zetu.
Ni mimi:
emu-three
1 comment :
Story imefika patamu kweli, ngoja tuone jinsi mume wa familia anavyoumbuka
Post a Comment