Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, July 20, 2012

Hujafa hujaumbika-71 Hitimisho 29‘Hivi mumeo naye anaendeleaje?’ nikamuuliza mke wa wakili mkuu. Mke wa wakili mkuu aliniangalia kwa macho yake yaliyolowana machozi akasema;

‘Hajazindukana bado, na hali yake ni mbaya, ….ni mbaya sana, ….bado wanamhangaikia na wazo lililotolewa hadi sasa ni kufanyiwa upasuaji,…..nimewasiliana na kaka yake, na yeye kakubali ufanyike tu,….maana hadi sasa sijielewi, naona kama filamu ya kuigiza tu, sijui hawa watu wana nini,….’akasema mke wa wakili mkuu, huku akijizuia kulia.

‘Ni moyo wa kupenda huo, mpaka kupitiliza,….maana mimi nimejifunza kutoka kwa huyo rafiki yako, na nimegundua mengi, kuwa moyo ukipenda, haumabiliki,…. akili inakuwa haina uweze wa kuchuja tena, na hili ni tatizo….’akasema wakili mwanadada.

‘Lakini hata hivyo mimi sioni kuwa huo ni upendo wa dhati, maana kama kweli ungelikuwa ni upendo wa dhati huyo mume wangu angeliniambia mimi ukweli, na tukajadiliana na tungelijua hatima yake, ….lakini huku unapenda na kule unapenda, kweli huo ni upendo au ni tamaa za kimwili tu?’ akauliza mke wa wakili mkuu.

 ‘Lakini je ni kweli mumeo alikubali kunywa hiyo sumu, ili wafe….kama alivyodai nesi, kuwa wanywe wafe, wakaoane huko mbele kwa mbale, mimi hapa naona nesi kadanganya…na hebu angalia hawa watu, huyo ni nesi anaongea hivyo, hilo lingeongelewa na watu wasio na taaluma…’ nikasema.

‘Si ulimsikia livyosema mwenyewe kuwa pale hawezi kudanganya tena, maana anajiona kama ni mtu wa kufa…nahisi mwenzake aliona kama ni uwongo, alipoambiwa kuwa wanakunywa sumu ili wafe ….’akasema wakili mwanadada.

‘Unajua kwa hali ile waliyokuwa nayo, hasa wakili mkuu, walikuwa kama wamechanganyikiwa, ikizingatia kuwa kuna kesi ya mauaji mbele yao, na mambo ,mengi ya kuwazalilisha yameshapita, yale mapicha mbaya, yamewaweka uchi mbele ya jamii, sasa aliona kabda ni heri ya kufa kuliko kuaibika …’nikasema.

‘Siamini mtu kama wakili mkuu,ambaye anajua sheria, na yeye ni kama askari angelichukua hatu kama hiyo. Hatua hiyo ni udhaifu kwa mpiganaji, mara nyingi mtu kama askari, wengi hawapendelei sumu, wao hujiua kwa risasi….’akasema mtu mmoja ambaye likuwa pembeni yetu akitusikiliza.

Mara akaja yule mlinzi na kusema tunaitwa tena huko ndani, na tulipofia tulimkuta nesi akiwa kajiandaa kuongea na sisi…

********
‘Sijafa bado na siamini kuwa bado nipo hai,…., bado napumua, na naomba safari hii niwasimulie kila kitu, msiniulize maswali tena, sikumbuki vyema tuliishia wapi, …sikumbuki vyema niliwaambia kitu gani, ..mmh, …kumbukumbu zinaanza kupotea….’akawa anajaribu kukumbuka.

‘Tulikuuliza je ndio wewe uliyemuua Kimwana…!’ akasema wakili mwanadada.

‘Siku ile ambayo Kimwana aliuliwa, mimi nilibakia hospitalini, na nilijua kabisa kuwa Kimwana siku hiyo hatapona, kwasababu nilijua kuwa mke wa wakili mkuu, na rafiki yake wamekwenda huko kufanya mauaji, na nilipoagana na wakili mkuu kuwa na y eye anakwenda huko nikajua sasa Kimwana kapatikana….lakini…..’akatulia kama vile anatafuta hewa.

‘Niliingiwa na wasiwasi maana wote hawo nawajua, ….namjua wakili mkuu udhaifu wake, nilijua akifika kwa Kimwana na akalegezewa yale macho, hataweza kufanya hicho alichokusudia, na wale akina dada wawili, hawawezi kumuua mtu, zile ni hasira tu, itafikia muda watashindwa kufanya hilo walilolikusudia, hapo hapo nikampigia simu Sokoti, na kumwambia kuwa huko kwa Kimwana kunatakiwa kufanyike jambo la haraka…

‘Jambo gani la haraka, mbona tulishakubaliana kuwa hawo akina dada wawili watamaliza kila kitu…?’akaniambia Sokoti.

‘Sikiliza nina taarifa kuwa wakili mwanadada anamfuatilia Kimwana, na ninavyojua huyo dada akipata mwanya wa kuongea na Kimwana, ataweza kujua kila kitu, na ukumbuke kuwa Kimwana keshasema kuwa atabomoka, atasema kila kitu kuhusu hili kundiletu, na mimi sikubali kwenda jela kwa uzembe huo…heri ya kufa mapema, lakini kabla ya kufikia hatua hiyo, nataka nihakikishe nimemlaiza adui yangu…..’nikamwambia Sokoti.

‘Sasa unataka tufanyeje?’akaniuliza.

‘Wewe nakuachia kazi moja, kuhakiisha kuwa unamziba mdomo huyo wakili mwanadada,….maanahuyo ukimuachia mwanya umeumbuka, mpaka sasa inanokena keshajua mambo mengi,anachotafuta ni ushahidi tu,….huyo hakikisha hakatizi leo,… mimi niachie Kimwana huyo ni mtu wangu….’nikasema.

‘Hiyo haina shida, kuna mtu wetu yupo huko, anaweza kumaliza kila kitu..nikimwambia tu, ….atatekeleza…’akasema.

‘Lakini nahitaji mawasiliano yako baadaye kidogo, uwe hewani…’nikamwambia na wakati huo akili yangu ilishafanya kazi kwa haraka, na nilipoangalia saa nikagundua kuwa kama wakili mkuu keshaondoka kwenda huko kwa Kimwana atakuwa keshakaribia kufika, na mimi nilitaka nihakikishe kuwa najua nini anachokitaka kukifanya…kama sio mbinu yao ya kukutana….’akatulia.

‘Sikujua kuwa kuna mtu mjanja angeligundua hilo, maana nilifanya mambo yote kitaalamu, na siku wakili mwanadada alipokuja kunihadithia haya, na akawa anaelezea jinsi nilivyokuwa nimepanga kama vile alikuwa kichwani mwangu, sikuamini hilo….nikajua sasa sina ujanja,…mmh’ akaguna na kuhema kwa nguvu, halafu akasema;

‘Naomba wakili mwanadada uwaelezee jinsi gani ulivyo gundua maana naona pumzi kama inakwisha….

*******

Wote tulimgeukia wakili mwanadada ambaye alikuwa akimtizama nesi kwa macho ya huruma, akasema kwa sauti ndogo;

‘Nilitaka yote yatoke kinywani mwako, maana huu sasa ni ushahidi waliokuwa wakiuhitaji watu wa sheria, na nitaongea yale muhimu, kama utaona nimesema uwongo naomba unisimamishe haraka…’akasema wakili mwanadada huku akimwangalia hakimu na mkuu, na mwandishi maalumu wa mahakama ambaye alikuwa akiandika taarifa zote.

‘Kama ulivyonielezea, ndivyo hivyo nilivyofanya, …wewe ongea ninakusikiliza, maana hapa kichwa , tumbo vyote vinauma, kama roho ndivyo inavyochomolewa hivi mbona kuna kazi…’akasema na kuhema kwa nguvu.

 Docta alimsogelea na kumuangalia….akahakikisha kuwa kila kitu kipo shwari,akasema wakili mwanadada aendelee tu, mgonjwa yupo macho anawasikiliza…

‘Nawasikiliza, nipo shwari kwa sasa…’akasema nesi.

‘Nesi alipofika hapo hospitalini, alifanya mengi makubwa, na hata ukienda kumuuliza mganga mkuu wa hiyo hospitali, atakuambia kuwa huyo nesi ndiye aliyeifanya hiyo hospitalini iwe na uhai tena maana ilishafikia kubaya…na kitu kimoja kikubwa alichokifanya ni kuhakikisha kuwa hospitali hiyo ina ulinzi thabiti.

‘Yeye kwasababu alipitia uaskari, basi hata katika utendaji wake wa kazi ulikuwa una alama ya uaskari. Kitu kimoja alichokifanya ni kuhusu walinzi kuwa wawe na madafatri mawili. Moja ambalo wanasaini watu wanapoingia, na la pili ni lakuandika kumbukumbu zote za wale watu wanaoingia  au kutoka…nakwasababu fulani hawakuweza kuacha kumbukumbu zao pale getini kwa mlinzi.

Daftari hili la pili anakuwa nalo mlinzi wa juu, maana pale getini walijenga kitu kama kigorofa, na mlinzi wa juu kazi yake ni kuandika kila kitu, anahitajika kuangalia kila mtu anayeingia na kutoka, na kuandika kila tukio,…

Sasa utaratibu huo ndio uliokuja kummaliza nesi mwenyewe, maana nilipopitia hilo daftari la huyo mlinzi wa juu, niligundua kuwa siku hiyo,  kwa maelezo ya mlinzi ndani ya lile daftari, pale getini  alitoka mtu na pikipiki, akiwa kavalia koti refu na nywele za bandia, …..mlinzi huyo aliandika kuwa mtu huyo sio mara ya kwanza kuonekana hivyo, akiwa kavalia hivyo na alipoelezea wasifa wa huyo mtu, nikakumbuka yule mtu aliyewahi kukutana na Msomali kipindi cha nyuma, akiwa na nywele nyingi, ambaye alikuja hata kumkimbia Msomali…

‘Niligudnua kuwa kumbe ulikuwa ni ujanaj fulani wa kuigiza….’akatulia na kumwangalia nesi, ambaye alionekana kuwa macho, akitabasamu kwa kujilazimisha..

Kwahiyo kazi yangu kubwa ilikuwa kumtafuta mtu wa namna hiyo ni nani, maana mtu huyo amekuwa kama jinamizi fulani linalokuja na kufanya jambo halafu linatoweka,…hisia zangu zilinituma kabisa kuwa huyo anaweza akawa mtu muhimu sana katika haya matukio.

Nilipopata hizo kumbukumbu, nikaingia ndani na kutafiti , nilikwenda hapo alipokuwa kalazwa wakili mkuu, nilitaka kujua ukweli kuwa je alikuwa akiumwa kweli, maana kwa kipindi hicho nilishaingiwa na wasiwasi kuwa huenda wakili mkuu ndiye aliyefanya haya yote, kwahiyo nilitaka kujua kuwa yupo nesi mwingine aliyekuwa akishirikiana na nesi huyu na je anaweza akawa anajua lolote.

Hapo ndipo nilipogundua mengi, ….nilipofika pale hospitalini, niliongea na daktari aliyekuwa akimhudumia wakili mkuu, nikamuuliza hali halisi ya mgonjwa, na yeye hakunificha aliniambia kila kitu, kuwa kweli wakili mkuu alikuwa akikabiliwa an shinikiza la damu ..na tatizo hilo, linatokana na msongo wa mawazo, kwahiyo kama atapata muda wa kutuliza kichwa chake haitachukua mudaangelipona kabisa,lakini kama atashindwa kufanya hivyo, anaweza akaishia kubaya…

‘Je docta ni nesi wa ngapi waliokuwa wakimuhudumia huyo mgonjwa?’ nikamuuliza.

‘Wapo nesi wawili ambao nimewapa hiyo kazi, ..yupo nesi ambaye ni rafiki mkubwa wa huyo mgonjwa na mwenzake mmoja ambaye sasa yupo likizo…’akaniambia huyo docta.

‘Anatarajia kurudi lini?’nikamuuliza.

‘Ni baada ay siku kumi tano hivi, lakini nasiki kesharudi kwani alikuwa akifuatilai malipo yake, kwahiyo haajsafiri bado. Kama unahitaji kumuona nenda masijala watakupa taarifa zake….’akaniambia huyo docta, na nilijua hana kubwa la kunisaida kwa muda huo, nikaona cha muhimu ni kumtafuta huyonesi.

Kwanza nikaimbilia masijala, na kwa bahati nzuri, nikamkua huyo nesi akiwa anasubiri taarifa zake humo. Kwani hapo ndipo wanapopatia taarifa zao hasa wanapokuwa wakifuatiliwa mambo yao ya kikazi, na lionekana hapo kama kajificha, hakutaka watu wamuone.

‘Wewe ndiye uliyekuwa ukimhudumia wakili mkuu, na mwenzako,..?’nikamuuliza.

‘Nani kakumbia hivyo…?’ akaniuliza kwa wasiwasi, na ule wasiwasi ukaniambai kuwa kuna jambo fulani analijua huyo nesi,na hakupenda kabisa lijulikane, na hata hiyo likizo inaonekana kama alilazimishiwa, nahisi kwa shinikizo fulani, ambalo nilikuja kugundua kuwa ni kutokana na yaliyotokea siku hiyo.

‘Ni docta wako, kaniambia kila kitu,kuwa wewe ndiye uliyepewa kazi pamoja na nesi wenu mkuu, kumhudumia waklii mkuu, na kuna siku wakili mkuu alitoka nje bila ya taarifa ya docta ….’nikasema na yeye bila kujua akaanza kuhaha na kutetemeka.

‘Mimi ni wakili na lengo langu nikukusaidia wewe na mwenzako, iili misje mkaingia kwenye matatizo maana mwenzako keshaongea kila kitu na kukutupia mzigo wewe,na usipoangalia vyema utajikuta kwenye matatizo, makubwa ….’nikamwambia.

‘Nilijua tu,ndio maana kanilazimisha nichukue hii likizo ili aje anichomee uwongo wake nikiwa huko likizo,sikubali…’ akasema.

‘Uwongo gani wakati ni kweli wewe ulikuwepo siku hiyo?’ nikamuuliza.

‘Ndio nilikuwepo, lakini mshiriki mkuu wa kumhudumia huyo mgonjwa ni yeye, na alishatuambia kuwa sisi tutaelekezwa jinsi ya kufanya tu, hatuna nafasi ya kuwa karibu na huyo mgonjwa,kwasababu ya wivu wake….’akasema huku akiwa na wasi wasiwasi.

‘Sasa iku ile nilikuwa nipo ndani ya wodi nikiwahudumia wagonjwa, nikawa nimepungukiwa na vifaa,…nikaenda kumfuata yeye. Bahati sikumkukuta kwenye ofisi yake, nikakimbilia kule alipolazwa mgonjwa, wakati nafika chumba cha kubadili nguo, nikamuona yeye akiingia humo kwenye hicho chumba,na yeye muda huo hakuniona.…

Nikasubiri nikiwa na wasiwasi naye, maana siku hiyo nzima alionekana kutokuwa na amani, alikuwa hasemi na akiongea huongea kwa hasira, nikajua kuna jambo,….nikatulia kwa muda, na nilipoona kimiya nikasogelea pale chumba cha kubadili, na nikashangaa mlango wa nyuma ambao mara nyingi haufunguliwi, ukawa unafungwa kwa nje, ina maana yeye alitokea mlango huo wa nyuma.

Nikakimbia haraka kwenye dirisha ambalo unaona kwa nje, na nikamuona mtu akiwa kavalia nywele za bandia na koti refu akipanda kwenye pikipiki,..nywele zile zilikuwa zikimfunika uso mzima, kwahiyo usingeliweza kumuona sura yake, lakini viatu alivyokuwa kavalia siku hiyo vyekundu vilimshitaki,nikajau  kuwa ni yeye.

Nikajiuliz a huyu mtu anakwenda wapi saa hizi na nywele za bandia, na jinsi alivyo ni kama hataki mtu amjue ….nikarudi haraka hadi kule kwenye chumba cha kubadili, nikakuta nguo zake alizokuwa kavalia siku hiyo zikiwa zimewekwa mle kwenye kabati lake, nikajua kuwa kuna jambo linaendelea.

Nikakimbilia kule kwenye chumba alicholazwa yule mgonjwa, nikakuta kama kuna mgonjwa kalala pake kitandani, ..lakini ulalaji ule ukanitia mashaka, kama ni mgonjwa, basi atakuwa maiti, nikatka kujiridhisha , nikaingia ndani, na nilipofunua kitanda, nilikuta ni mito imewekwa mithili ya mtu aliyelala…nikashituka ajabu….nikajua kuwa huenda hawa watu wamepanga kwenda kufanya mambo yao…

‘Mambo gani….’nikamuuliza.

‘Mapenzi yao labda..sikuwa na uhakika zaidi ….’akasema huyo nesi

‘Je uvaaji wa hizo nguo ulishawahi kumuona mara nyingine, huyo nesi akiwa kavalia hivyo?’nikamuuliza.

‘Ndio sio mara ya kwanza,….na huvaa jioni wkati anatoka, sijui huwa anakwenda wapi, na mra nyingi akivaa hivyo haagi mtu, anafanya kama siri fulani. Na kwa jinsi ninavyomuogopa sijawahi kumuuliza, ila nilihisI huyu nesi ana lake jambo ….’akasema.

‘Ikawaje?’ nikamuuliza.

‘Nilirudishia vile vile na kutoka nje,haraka nikiwa na wasiwasi asije akanikuta humo ndani,…’akasema.

‘Ina maana ulikuta mlango upo wazi, au ulikuwa na ufunguo wa hicho chumba?’ akaulizwa.

‘Mlango ulikuwa haujafungwa, ….lakini mara nyingi hicho chumba hakuna anayeingia, na kuingia humo mpaka umuone yeye au dakitari,na dakitari siku hiyo aliaga mapema kwani alikuwa na mkutano . Na huyo mgonjwa alikuwa kwenye mamlaka ya nesi, …

‘Baadaye sana, akarudi ….na alirudia njia ile ile,…aliingia na pikipiki lake,pikipiki hilo ni la huyo mgonjwa,lililetwa hapo kipindi huyo mgonjwa alipoletwa kulazwa, na mara nyingi linakuwa hapo nje. Na pikipiki la huyu nesi lilikuwa hakipo, sijui lilikuwa na nani kwa muda huo, lakini baadaye lilionekana…

Aliporudi mimi nilikuwa pale dirishani,maana nilikuwa mara kwa mara nafika hapo kuangalia je huyo nesi atarudi saa ngapi na akirudii atarudi na huyo mgonjwa….na kama bahati nilipofika hapo dirishani nikamuona akifika na pikipiki lake, akashuka kwa haraka na nyuma yake alikuwa kabeba kitu…’akasema huyo nesi.

‘Kabeba kitu gani?’ nikamuuliza.

‘Kabeba kitu kirefu, inawezekana ni gitaa, ndivyo nilivyowaza kwa muda ule, nikacheka kimoyomoyo, ina maana huyu nesi ni mwanamziki pia, na sikuhanagaika tena nikarudi wodini, lakini baadaye moyo ukawa haujatulia, nikatoka kwenda kumuona huyo nesi, sikumkuta ofisini kwake, nikaondoka kwa haraka hadi kule wodini, sikumkukuta…nikaamua kuingia pale alipolazwa mgonjwa.

‘Najuta kwanini nilifanya hivyo, maana nilipoingia pale ndani, nilikuta mgonjwa kweli kalala, na katundukiwa ile mipira kama kawaida, nikajua labda huyo nesi yupo kwenye sehemu ya kubadili nguo, nikaenda mle ndani, na nikakuta hayupo pia, nikaingiwa na tamaa ya kuangalia kwenye kabati lake, na hamadi nikaona yale manywele ya bandia aliyokuwa kavalia, na lile koti…

Nikawa na hamasa ya kuchunguza ule mzigo aliokuwa kabeba, nikafungua vyema na kweli kwa ndani 
nikakuta umeegemezwa, na kwa ujinga wangu, nikautoa, na kuufungua maana ulifungwa kwa zipu, nilipofungua nafasi ya kutosha, nikakuta ni chuma kimetokeza,….ooh,na akili yangu ikawaza, hiki sio chuma kama cha bubduki kweli,…. nikafungua kwa mapana…oh,mungu wangu ilikuwa ni bunduki,…nikaanza kutetemeka,…nikafunga ule mfuko kwa haraka na kulirudishia pale nilipoikuta, na wakati nageuka kutoka mara nikasikia sauti ikisema kwa hasira.

‘Wewe unafanya nini huku muda kama huu..?’ nilishituka, karibu nidondoke chini, nikatoka hapo mbio,kwani alikuwa ni huyo nesi,na wakati natoka aliniangalia kwa jicho la kiuaji kabisa.....
Nikasema ,`Kuna vifaa vimeniishia nakuhitaji boharini….’

‘Nakuona unachokonoa moto…chunga sana nyendo zako…’akaniambia na mimi nikawa natetemeka,….

NB: Haya kwa leo tuishie hapa.

WAZO LA LEO: Kufunga sio kufunga tu kula chakula, kufunga ni pamoja na kufunga matendo yote mabaya, ni kujikurubisha kwa mungu zaidi kwa kufanya ibada zaidi,…kama vile ndio siku ya mwisho wa uhai wako hapa duniani. Omba sana, tubu sana madhambi yako, na uwe na huruma sana kwa wenzako, hasa masikini na wsiojiweza...

TWAWATAKIA WOTE RAMADHANI NJEMA NA WAAJIRI MUWASAIDIE WAFANYAKAZI WENU KUTOKA MAPEMA ILI WAWAHI KUFUTURU MAKWAO!


Ni mimi: emu-three

1 comment :

Anonymous said...

dah, siamini kama natakiwa kusubiri hadi jumatatu kisa hiki kiendelee! kimefika patamu sana