‘Hebu mleteni huyo mtoto...’akasema mwenyekiti, na mama yangu
akatoka nje, na aliporudi akawa kambeba mtoto, kila mmoja akawa na shauku ya
kumwangalia huyo mtoto.
Kila mtu alitaka kumuona huyo mtoto kwa sura, na huku wakijiuliza
ni kwanini mume wa familia akang’ang’ania mtoto aletwe…
Tuendelee na kisa chetu
********
Mtoto akaletwa na mama hadi kwenye kiti kilichowekwa maalumu kwa
mtoa ushahidi, na mama akakaa naye hapo, huku akiwa kambeba yule mtoto,
hakutaka kumpa yule binti, mama wa huyo mtoto, sasa akawa anamfunua ili kila
mtu amuone kwa uwazi mkubwa, na wa kwanza kusema alikuwa rafiki yake mume
wangu, yani docta akasema;
‘Bro, wewe kweli damu yako ni kali, huwezi kukataa hapo,
utafikiri ni pacha mwenzako...’akasema docta.
Mume wa familia, alikuwa katulia kimiya, hakuinuka, wala kusema
neno, aliyeinuka alikuwa ni wakili wake, ambaye alikwenda hadi pale alipokaa
mama, na kumwangalia yule mtu, akatabasamu, na kugeuka, akarudi pale alipokaa,
mteja wake, akamnong’oneza kitu.
Mume wangu akamwangalia kwa macho ya kuonyesha mshangao, lakini
hakusema kitu, akabakia kimiya, na mwenyekiti alipohakikisha kila mtu kafika
kumuona yule mtoto, na ambaye hakuweza kufika alikuwa mume wangu, mume wangu
hakuinuka, alibakia pale pale akiwa kainamisha kichwa chini, na mwenyekiti
akasema;
‘Mume wa familia ni zamu yako kumuona mtoto, usikatae, maana hilo
tumelifanya kutokana na ombi lako, ulifahamu kuwa una mtoto, lakini ukajifanya
hujui, ukifikiria kuwa huyo binti kaja peke yake, hana ushahidi, sasa mtoto
ndiye huyo hapo, nenda kamuona, je ni mtoto wako, je ni damu yako, sasa uikane
damu yako mwenyewe,...’akasema mwenyekiti.
Hata hivyo mume wa familia hakuinuka, mimi nikainuka na kwenda
kumchukua yule mtoto kutoka kwa mama, nikaenda naye hadi alipokaa mume wangu
nikamuonyesha mume wangu.
‘Huyu hapa, muone anavyofanana na watoto wangu, utafikiri mapacha,
muone anavyokuangalia, katambua kabisa kuwa wewe ni baba yake..humdanganyi mtu
hapa, sura yake haijifichi, anafanana kabisa na wewe...kwa kila kitu, haya
niambie, ..’nikamwambia
Mume wangu badala ya kumwangalia mtoto akawa ananiangalia mimi
usoni, na macho ya kutahayari, nilipoona hamuangalii mtoto, ananiangalai mimi
tu, nikamuweka yule mtoto mapajani kwake, hakusogeza mikono yake, wala kusem a
neno, moyoni nikasema ;ujumbe umefika. Nikamchukua na kumrudisha kwa
mama, ambaye alimwangalia mwenyekiti kujua ni nini kinachofuata
‘Haya naona zoezi hilo limekamilika,...’akasema mwenyekiti na mama
akamchukua yule mtoto na kwenda kukaa sehemu yake, pale alipokuwa amekaa awali.
‘Bado mwenyekiti, mimi nataka mume wa familia akubali kuwa huyu ni
mtoto wake au sio mtoto wake, na kauli yake, ichukuliwe hapa rasmi ndani ya kikao hiki, kama akimkana, basi
kwa vile wapo wanasheria hapa, wataandika, mkataba rasmi wa huyo mtoto
kuchukuliwa na mtu mwingine, maana hatakuwa hana baba...’mimi nikasema.
‘Sawa, ni wazo zuri, na sisi tupo tayari kumchukua huyo mtoto kama
baba yake atamkana kuwa sio mtoto wake,..’akasema mwenyekiti.
Wakili wa mume wangu akawa anaongea na mume wangu, na niliona mume
wangu akisita kusema neno, na baadaye akasema neno kwa wakili, na wakili
akasema;
‘Mteja wangu kasema hilo ni jambo lake binafsi,
asingelipenda mtu kumuingilia, kwasababu kila kitu kipo wazi, anaona hilo la
mtoto liachwe kama lilivyo, ataongea na mimi na ni jinsi gani ya kufanya..’akasema
wakili wake.
‘Swali lwetu lipo pale pale, je huyo ni mtoto wake, au sio mtoto
wake, kikao kinataka majibu?’ akaulizwa
‘Ni mtoto wake kwa mtizamo wa haraka, lakini kuna maswala ya
kuthibisha kitaalamu, maana kufanana sio tija….yeye anafanana na wadogo zake,
je haiwezekani akawa mtoto wa wadogo zake, kwahiyo mteja wangu kaomba apewe
muda,…tuhakiki hakiki hilo kitaalamu zaidi...’akasema wakili na watu wakaguna,
maana hapo hakuna cha kuhakiki, kila kitu kipo wazi.
‘Pamoja na hayo kuna swali la ziada, namuuliza mume wa familia, je
anakubali sasa kuwa alimbaka mfanyakazi wa ndani…?’ akauliza mwenyekiti
‘Ndugu mwenyekiti, kama mteja wangu alivyosema awali, hawezi kuwa
na uhakika na matukio hayo ya nyuma, kuna mengine mpaka sasa hayakumbuki,
kwahiyo kwa hivi sasa hana jibu la swali hilo mpaka kupatikane vipimo vya
kitaalamu.
‘Je vipimo vya kitaalamu vikisema huyo sio mtoto wake atafanya
nini..?’ akaulizwa
‘Basi yawezekana akawa mtoto wa ndugu zake wengine..’akasema
wakili
‘Na je ikithibitishwa kuwa ni mtoto wake, yeye ana kauli gani ,
rejea mkataba wao ulivyokuwa unasema..?’ akaulizwa
‘Mpaka sasa hatuwezi kusema lolote kwa hilo ..kwanza tupate
uhakika, mfahamu alivyo mteja wangu yeye anathamini sana ushahidi, maana mambo
mengine ya nyuma ameyasahau, na ikitokea ni kweli, basi hapo atakuja kutoa
tamko lake..’akasema wakili wake.
************
'Huo ushahidi umakamilika, iliyobakia ni je katiba inasema nini,.
Asileta ujanja ujanja wa kusahau hapa…tumekuwa tukienda na yeye kiuungwana ili
tuone na yeye ni muungwa na kiasi gani..hana hiyo hulka…’akasema mweneykiti
‘Sasa tuspoteze muda, tuone kosa kaam hilo mkataba wao unasema
nini, na je ni nini mkataba wao, unasema
kwa watoto wa nje au hilo halipo, maana hata kama baba yake kakubali kwa shingo
upande,lakini sisi kama familia ni lazima tujue hatima ya huyu mtoto kifamilia,
kwani kazaliwa ndani ya familia,na hatuwezi kuliachia hivi hivi, zaidi
alifanyiwa kitendo hicho kwa nguvu...’akasema mwenyekiti.
Mwenyekiti akakaa kimia akisubiria mawazo ya watu, na docta
akasema;
‘Hatuwezi kukimbilia kwenye hukumu kwanza maana bado sheria,
haijabaini kuwa mlengwa ni mkosaji, sisi bado tupo kwenye ushahidi au sio, mimi
naona ukianza kuangalia katiba inasema nini utakuwa umeshahitimisha kila
kitu..’akasema docta
‘Nafahamu hilo, kama nilivyosema awali, binti anastahiki kuondoka kwenye kikao hiki mapema ili akaweze kujiandaa, kwani yeye ana safari, kwahiyo tunahitajia aondoke hapa akiwa na ufahamu kamili
ni nini hatima ya mtoto wake…’akasema mwenyekiti
‘Kwa hali kama hii, mimi ningelishauri huyo binti asisafiri, aahirishe hiyo safari yake, ili muafaka ufikiwe kwanza, ni muhimu sana aondoke akiwa na uhakika, kuliko kusubiria au kutumia njia zisizo faa…tunafahamu baba wa mtoto wake anastahiki kuwajibika kwa hilo, lakini je ni kweli, huyo baba wa mtoto ni nani..ni huyu au yupo mwingine..’akasema docta
‘Mimi sijawahi kutembea na mwanaume yoyote mwingine zaidi ya yeye, yeye
ndiye alinibaka, na sikuwa hiyari kwa hilo tendo, aliniumiza, alishika kwa nguvu kama nilivyokwisha kusema awali…’akasema binti.
‘Bado nahitajia mawazo, …maana ni lazima huyo mtoto ahakikishiwe
anapewa haki zake zote ikiwemo mama yake,..na kwa ushahidi wake imedhihirisha hali halisi, ni ipi tabia ya
mume wa familia, na inavyoonekana ni kama vile bado ana watoto wengine
nje, hilo nalo litakuja kutolewa ushahidi, sina shaka, …’akasema mwenyekiti na mume wa familia akainua uso kumuangalia mwenyekiti.
‘Kama nasema uwongo, nataka mume wa familia anikane…nina ushahidi
wa hilo..’akasema mwenyekiti. na mume wa familia akawa anateta na wakili wake.
‘Haya mimi namuachia mke wa familia atoe kauli yake kwanza, maana
tumempa muda wa kutosha wa kutuliza akili yake , haya mambo yasikieni kwa
wengine, yanagusa mioyo ya watu…’akasema mwenyekiti
‘Lakini kabla sijalirejesha hilo jukumu kwa mke wa familia hii, nataka
nisisitize wazo langu, kuwa kwa huyu mtoto, kwa vile imeshathibitika hivyo,
tunataka kikao hiki, leo hii , kitoe tamko rasmi, tena kisheria, ili mtoto huyu atambulike rasmi kuwa ni mtoto
wa nani, je ni mume wa familia, au ni wa nani,...'akasema mwenyekiti akimuangalia mume wa familia
'Ushahidi upo kuwa huyo mtoto ni wa mume wa familia,..huo utaalamu anaouhitajia yeye, upo, hautahitajia, kusubiria yeye, kuwa eti anahitajia utaalamu wa zaidi , hiyo ni namna ya kupoteza muda,..au sio jamani, lakini huko tutafika kama bado atazidi kuwa mkaidi, au sio jamani...?' akauliza
mwenyekiti, na kabla watu hawajajibu mimi nikasema;
'Kama wao wanahitaji kuthibitisha kitaalamu, kivyao.. sisi hatulipingi hilo, lakini akumbuke kuwa kuna matendo kayafanya na huyo binti, na iwe isiwe kuwa huyo mtoto ni wake, au si wake, bado yeye ana madhambi, ya kavunja sheria za ndoa yake yeye mwenyewe, na pili kavunja sheria na haki za huyo binti,..huo ushahidi upo dhahiri...labda aulizwe hata ushahidi huo wa kumzalilisha huyo binti, anahitajia vipimovya kitaalamu…?’ akauliza mama
‘Wakili unasemaje..?’ mwenyekiti akauliza, na wakili akawa anateta
na mteja wake
‘Mteja wangu anasema hayo ya ushahid ni kuzalilishana, hayana
umuhimu kuonyeshwa, lakini hilo la mtoto lina umuhimu wake, maana baada ya
hapo, ndio ataweza kutoakauli yake..mengine kama alivyosema hakumbuki..’akasema
wakili.
‘Akionyeshwa huo ushahidi alivyokuwa akizalilisha mtoto wa wezake
atakumbuka tu…’akasema mama
‘Mimi naona ushahidi dhahiri upo hapa hapa,..kama alivyosema mke
wangu, na ushahidi huo unaonyesha dhamira ya kweli ya mtendaji, ..aisje
kusingizia ulevi, maana humo humo kuna sehemu kabisa hajalewa…’akasema
mwenyekiti
‘Kiukweli nimeuangali huo ushahidi wote, ilibidi nifanye hivyo ili
kujirizisha, sio kwamba nilifurahia kuuona uchafu huo, kiukweli inakera, na
ukiangalia hiyo video, unaweza ukafanya jambo baya sana,..mliona kipindi fulani
nilikuwa na hasira sana na huyu mtu..ni sababu hiyo..’akasema mwenyekiti.
‘Sasa kwangu mimi, nataka sheria ichukue mkondo wake, sio haki
kulifumbia macho hilo, sisemi hivi kwa vile namchukia huyo mkwe wangu, hapana,
ila namuangalia huyu binti, …alichotendewa sio halali, na kama mtasema liachwa
hivyo hivyo, jiulize ni ni haki ya huyu binti..hilo mimi nitawaachia wana kikao
hili muamue wenyewe..’akasema mwenyekiti,na kuniangalia mimi, na mimi nikasema;
‘Huo ulikuwa ushahidi mmoja katika madhambi yake mengi, kuna mtoto
mwingine ambaye hajajulikana, naona sasa ni zamu ya mume wangu kuongea
mwenyewe, kwasababu anafahamu hilo, na anafahamu huyo mwingine kazaa na nani,
mimi naona ni muda wa yeye kujirudi, ili tusipoteze muda....’nikasema
‘Haya mume wa familia, unasikia sasa wewe mwenyewe unaitwa kama
shahidi, usema ukweli wako, na ninafasi nyingine ya kutoa lako la moyoni,
hatuwezi kukulazimisha kutubu, lakini unatakiwa sasa useme neno, ..maana kumbe
wewe ni dume la mbegu..’akasema mwenyekiti na watu wakacheka
Na hapo wakili tena akawa akiteta na mteja wake, na wakawa kama
wanasigishana, na baadaye wakili akasema;
‘Mteja wangu anasema hayo ni mambo yake binafsi hataki kuyaongea
hapa,..na hata hivyo, yeye hana mtoto yoyote mwingine kama mnavyo dai nyie, hayo
yote yanayoletwa kwa hivi sasa ni shinikizo, na inabidi akubali tu,...lakini
huo sio utaratibu mzuri, ....kwahiyo kwa swala la watoto, analiomba lisitishwe,
tuongee mengine, yeye anahitaji muda wa kulifanyia kazi...’akasema wakili.
‘Kikao hiki kinatoa madhambi ya mume wa familia, ambayo yeye
aliyakana tokea awali, kama yeye angekubali kuwa kuna madhambi kayafanya,
akayasema japo kwa uchache, sisi kama waungwana tungemuelewa, tukatafuta jinsi
ya kumsafisha, lakini kwa ujeuri wake, akaona sisi hatujui lolote..yeye ni
mjanja, aliju yeye anaweza kutuvunga akafanya apendavyo, sasa hatutayaacha madhambi
yake yapite hivi hivi, yatatajwa yote, ...’mimi nikasema.
Na hapo mume wa familia akafunua mdomo na kusema;
‘Hivi wewe unaposema nina madhambi, wewe ni mungu, unafahamuje
kuwa nina madhambi, huwezi kunihukumu kihivyo, hayo ni makosa tu, yoyote
anaweza kuyafanya, na kwanini unasema kuwa na mtoto ni dhambi..huyo mtoto
alipangwa patkane hivyo, sio kusudio langu..?.’akasema mume wangu kama
ananiuliza huku kakunja uso kwa hasira.
‘Swala hapo ni je huyo mtoto umempataje,mtoto hana kosa..ndio..,
ila taratibu za kumpata huyo mtoto ni zipi,....hebu tuambie, huyo aliyeletwa
hapo umempata kwa njia gani, sio kwa njia ya kumbaka, hiyo sio dhambi, .?’
akauliza mama sasa kwa ukali.
‘Nimesema hilo sikumbuki mimi…’akasema mume wa familia
‘Aaah, unaulizwa kubaka sio dhambi, au wewe dhambi unaielewaje, kutembea
nje ya ndoa sio dhambi au ulikuwa umefunga ndoa ya muda na huyo binti..?’
aakulizwa
‘Mnielewe jamani…sikumbuki hayo madhambi kama kweli mimi
nilifanya, sikumbuki…’akasema
‘Je na huyo mtoto mwingine, hatujui umempataje huenda ni kwa
kubaka hivyo hivyo, huenda hiyo ndio tabia yako ya kubaka, na ujue, uliyafanya
hayo ukiwa wewe ni mume wa mtu, ukaikana ndoa yako kivitendo, ukaisaliti ndoa
yako, je hiyo sio zambi?’ akaulizwa na mama.
‘Kwahiyo nyie mnataka mimi nisema nini, kama mumeamua kama
familia, baba, mama mke mniandamu mimi sawa, semeni mnavyopenda, ..mimi kwa
sasa nasubiria maamuzi yenu, ila nasema hivi, ndoa yangu haitavunjiki, na haki
zangu zipo pale pale...kama mumelipanga hili liwe hivyo, na nyie ni waungu wa
kuhuku kuwa mimi nina dhambi…sawa, lakini mkumbuke kuna mimi nina nafsi, hamjui
nilivyomlilia mola wangu...’akasema kwa sauti ya kukerwa.
‘Hayo yatafuata baadaye kama unavyodai kuwa ndoa haivunjiki, na
haki zako zipo pale pale. Ni sawa tutaliona hilo, hapa tumekamilika, sheria
itasema, na hatutako hapa mpaka kieleweke, ...sawa si sawa…?’ akauliza
mwenyekiti akimuangalia docta
‘Tupo pamoja…hata mimi ningelipenda haya matatizo yafikie muafaka,
lakini pia, nisingelipenda kuwe na maamuzi ya haraka kihivyo, kama ni hukumu au
maamuzi inafaa tupate muda, muhimu leo tujadilianeni tu..’akasema docta.
‘Leo kila kitu kitabainika, na maamuzi hayatasubiria,… sisi
tulitaka tushirikiane na yeye kama ndugu, tukamuomba na kum-bembeleza, ili hili
tatizo tulimalize kindugu, lakini yeye amasaidia vipi kulitatua hili, na
umesikia kauli zake za sasa hivi, kwahiyo wakili wake ana kazi kubwa ya
kufanya, kama ana ubavu huo wa kugeuza hayo makubaliano yao kimkataba, lakini
pia makubaliano yetu kama ndugu,.....’akasema mwenyekiti.
‘Makubaliano gani mnayoyasema, ya huo mkataba wenu, hapana mimi hayo makubaliano siyatambui, nilishasema
toka awali kuwa ninachokitambua mimi ni huo mkataba niliokuwa nao mimi, huo
mwingine sijui umetoka wapi...mnanichangany tu, mara huu mara ule, kwanini iwe
mikataba miwili mimi sijui…’akasema kwa hasira
‘Naona wewe hujui sheria, kwa kukusaidia tu, wewe kaa uongee na
wakili wako vizuri, atakushauri vyema kuhusu sheria, maana hapo unavyoongea,
unaongea kama mtu asiyesoma, mkwe, usiniangushe...’akasema mwenyekiti, na
kumfanya mume wangu amuangalie mkwe wake kwa macho yaliyojaa hasira.
**********
‘Tunaendelea na jingine, mke wa familia ulisema dhambi
alizokufanyia mume wako ni nyingi, na tunaona kuwa yeye sio mtu wa kukubali na
kukiri kosa, sasa ili tusipoteze muda, labda tukuulize, kuna dhambi gani
nyingine, ambazo, amekiuka, na anahitajika kuwajiba nazo, au tumuulize tena mwenyewe
muhusika, kuwa yupo tayari kukiri makosa yaliyobakia, ili tusipoteze muda?’
akauliza mwenyekiti.
‘Mimi sipendi kuyaongelea machafu yake,lakini yeye ananilazimisha
nifanye hivyo, kama nilivyosema awali mume wangu ni mzinzi, ana tabia chafu,
ambayo haivumiliki, inasadikiwa kuwa ana mtoto mwingine nje ya ndoa zaidi ya
huyo aliyempata kwa kubaka…’nikasema
‘Ndio maana ningelipenda akiri yeye mwenyewe hilo, ili nimuone
kuwa kweli sasa kawa ni muungwana, na yupo tayari kuwa raia mwema, kwa jamii,
kwani yote tuliyomshukutumu nayo yamethibitika kuwa ni kweli, je na hili
la kuwa na mtoto mwingine nje, atalikataa...nataka nisikie kauli yake yeye mwenyewe?’
nikauliza, na mwenyekiti akamwangalia mume wangu.
Mume wangu alipoona watu wapo kimya wanamuangalia yeye, kwanza
akamuangalia wakili wake, na wakali wake akamuonyesha ishara kuwa aongee, na
hapo mume wangu kwa hasira akasema;
‘Sina mtoto mwingine, kama unavyodai wewe, mimi nimeona lengo lenu
ni kunizalilisha, sasa mimi nasema sina
mtoto mwingine, kam yupo huyo mtoto mwingine mleteni nimuone, ili nijaribu
kuvuta kumbukumbu zangu kama ni kweli….’akasema mume wangu kwa hasira
‘Una uhakika na hilo, maana sasa tukianza kutoa ushahidi mwingine,
hakuna kurudi nyuma sisi tutachukulia kuwa wewe ni jeuri, hututhamini, na
kwahiyo kama wanafamilia, tutahukumu, bila msamaha...’akasema mwenyekiti.
‘Nimeshawaaambia kuwa sina mtoto mwingine, kama yupo Malaya
anayedai hivyo aje kama livyofanya huyo,wote kwangu hao ni wahuni tu walaghai,
walifanya hivyo ili labda kunitega, ili wapate pesa, hakuna kingine ...’akasema
na kila mtu akawa kimiya kwa kauli yake hiyo chafu.
‘Kwanini unazungumza hivyo, huoni kuwa hiyo ni lugha chafu kwa
walengwa, na wakati wewe uliwabaka…?’ mwenyekiti akamuuliza
‘Nimechukia sana, kwani kinachoendelea hapa ni kunizalilisha na
mimi, hilo hamlioni au mimi sio binadamu,..nia yenu ni kunichafua , ili
nionekane mbaya, na mwisho wa siku mfanye mnavyotaka, mimi nimechoka, na labda
niseme hivyo, maana hamtaki ombi langu, nyie fanyeni maamuzi yenu muonavyo ni
sahihi…’akasema
Na watu wakabakia kimia, hawaamini anachokiongea huyo mume wa
familia.
‘Na narudia hivi, kauli
yangu ni ile ile, mimi sikubali kuvunja ndoa yangu,na wala sikubali kuachia
chochote kilicho changu, kwa ajili ya
hawo wajanja wajanja, hao ni wahuni tu ,…na sitasita kuwaita Malaya,..’akasema
na wakili wake akamzuia kuongea hivyo.
‘Ni Malaya tu,..kama wameamua kutumia ujanja wa mwili wao kupata
pesa kutoka kwangu, na kudai eti watoto wangu, kama yupo malaya mwingine kama
huyu aje athibitishe hayo, kuwa ana mtoto wangu, mimi sina mtoto na Malaya yoyote
zaidi ya mke wangu huyu hapa...’akasema na kauli yake ilikatishwa, kwani kuna
mtu aligonga mlangoni, na sote tukageuka kuangalia mlangoni.
Haikupita muda, huyo mtu akagonga tena , na kufungua mlango, ….
Kiukweli pale nilipokuwa nimekaa nilijikuta nikishikwa na
mshangao, .na niliona hali hiyo pia ilitokea kwa wengine…!
Hakuna aliyetegemea…..
Rafiki yangu alikuwa kasimama kati kati ya mlango, akiwa na mtoto
wake mkononi..
‘Hiyo kauli chafu imenikera, ...unafikiaje kutuita sisi Malaya,
wewe ambaye uliyetembea na wanawake wengi tutakuitaje, au unataka tuseme kila
kitu, sasa mimi nimefika, nasema hivi huyu hapa ni mtoto wako niliyezaa nawewewe,....’akasema
rafiki yangu, ...’
Watu wote walijikuta wakishikwa na mshangao, hakuna aliyesema neno
kwa muda huo hata mwenyekiti alikuwa kimia, akimuangalia huyo aliyeingia, na
mimi hapo nikapata nafasi ya kugeuka na kumuangalia mume wangu, alikuwa kwenye mshangao wa aina yake..ni kama
haamini.
Mwenyekiti alipoona hiyo hali, akasema;
‘Hebu kidogo,..naona haya mambo yanajirudia , nilichokikataa
kinajirudia tena, hii maana yake ni nini…huyu mtu alistahiki kuwepo kwenye hiki
kikao.., na ni ustaraabu gani huu…’akasema mwenyekiti.
‘Samahani mwenyekiti, nilipewa taarifa ya kuwepo kwenye hiki
kikao, lakini kutokana na yaliyotokea, sikupenda kufika kabisa…hata hivyo,
ikafika muda, nikaona ni kwanini nisiwepo, ni kwanini isiwe nafasi ya kuja
kuusema ukweli..’akasema.
‘Na kwa bahati, …ila sikutarajia hili, ..nilikuwepo hapo nje muda
mrefu tu, nikisita kuingia ndani, na kauli hizo chafu za kutuzalilisha sisi
wanawake ndizo zimenifanya niingie, nije ..nipambane na huyu mtu
anayetuzalilisha wanawake..’akasema
‘Lakini sio ustaarabu ulioufanya..’akasema mwenyekiti
‘Samahani sana,…ila mwenyekiti, mimi naona mnapoteza muda wenu na
huyu mtu , hatutaweza kukaa kimiya tukisubiri huyu mtu aseme ukweli, ambao hataweza
kuusema, huyu mtu ni mwongo,mzalilishaji mbakali na pia anahusika na uuwaji,..’akasema
Mume wangu akataka kusema ..lakini wakili wake akamzuia..
‘Kama mtu huyo ana tabia hizo, unategemea nini, nawaambia ukweli,
mnapoteza muda wenu bure, je hamna mambo yenu mengien ya kufanya, mpaka
mumbembeleze mtu kama huyu,, imeniuma sana, …anafikia kutuita sisi malaya...’akasema
rafiki yangu kwa sauti .
‘Mimi nataka anijibu swali langu kuwa ni nani Malaya, yeye
aliyetembea na wanawake wengi huku ana ndoa yake halali au sisi ambao kwa hadaa
zake alituzalilisha, ..ni nani Malaya?’ akauliza rafiki ynagu kwa hasira.
‘Kwani nilikuja nikakushika kwa nguvu,....wewe ulijileta mwenyewe
kwangu, ukidai unataka mtoto, au umesahau, usitake nikakuumbua bure
hapa...’akasema mume wangu kwa hasira.
‘Wewe mwanaume, mimi nilikuja kwako nikakuambia nataka mtoto,..?’
akauliza kwa mshangao.
‘Umesahau eeh…’akasema na kutulia, baada ya kuhis wakili wake
akimzuia.
‘Sio kwamba mipombe yako ilikutuma na kunitilia dawa ya kulevya
kwenye kinywaji kwa siri, nikazidiwa, ukanifanya ulichonifanya huko sio kubaka,
wewe ni mbakaji, na sio mara moja, kama wewe ni mwanaume kweli kwanini utumie
mbinu hiyo,…’akasema
‘Sema sasa kama wewe ni mwanaume kweli kwanini ulishindwa
kuongea.....na ole wako, chunga sana kauli yako, na ninakuambia hivi yale yote
uliyoyaandikisha kwa ajili ya huyo mtoto ninayataka yote, nimeshayawakilisha
hayo maombi kwa wakili wangu, sikutaka kufanya hivyo lakini sasa utawajibika,…unasikia
utawajibika...’akasema rafiki yangu kwa hasira.
‘Kama una wakili wako na mimi nina wakili wangu, usinibabaishe,
...hukutaka kukubali matakwa yangu toka awali, sasa unakuja kwa nyodo, hupati
kitu hapa, nimeshakuambia,..wewe si umekataa na mtoto wako, haya kaa naye sasa,
umtafute baba yake, sio mimi...’akasema na wakili wake akamkatisha na
kumtuliza.
‘Jamani hebu kwanza…’akasema mwenyekiti, lakini mama akamzuia,
amueche huyo mdada aendelee kuongea;
‘Ndugu mwenyekiti samahani sana, sikutaka kuyasema haya yote kama
hivi, ilitakiwa niyasema ili kuondoa hii sintofahamu lakini sio kwa utaratibu
huu, ila hatua iliyofikia inabidi niseme kila kitu, ili mumuone huyu mtu jinsi alivyo,
nakiri kuwa kweli nilimkosea rafiki yangu, lakini ni lazima mwisho wa siku
tumtambue mbaya wetu ni nani...’akasema rafiki yangu.
‘Mimi nimekuwa hapo nje nikisiliza yote , awali nilikuja na ajenda
nyingine kabisa ya kutaka kumsaidia huyu mtu, kumbe ni mtu mbaya sana ,
sikumuelewa kabisa,..sasa wakati umefika wa kusema ukweli wote, na nasema
ukweli wote sitaficha kitu ili haki itendeke, hata kama mimi ni mkosaji, basi
niwajibike kwa madhambi yangu…’akasema rafiki yangu
‘Najua rafiki yangu hatanielewa kwa hivi sasa…, lakini univumilie
kwa hili..na yale uliyokuwa ukiniuliza leo utayapata majibu yake hapa hapa,
kuwa huyo mume wako sio mtu mnzuri, ni Malaya, mbakaji, muongo, mwizi, ..na
sifa zote mbaya, anazo, hakustahili kabisa kuwa mume wako…’akasema akimnyoshea
kidogole mume wa familia
‘Usininyoshee kidole wewe mwanamke, ..usitake kikao hiki kikaharibika,.kama
umekuja na yako, fanya yaliyokuleta, si unataka upate mali, haya,…endelea na
tabia hiyo kama utazipata…ndio zenu.’akasema mume wa familia na wakili waka
akawa anamsihi.
‘Nitakunyoshea sana maana, muda wa kukueshimu umepita,
nilikuheshimu sana kipindi cha nyuma, lakini sio sasa, umejivunjia heshima yako
wewe mwenyewe, umajitoa kwenye ubaba, ulezi, ..ushemeji na kujitwika
yasiyostahiki…na ..’akajizuia kulia
‘Ongea tu, hiyo ndio shukurani yako…na toka humu ndani maana
hujaalikuwa, umekuja na mihasira zako, ulitaka nikumbembeleze, sasa sikiliza
hupati kitu , Malaya mkubwa wewe..’akasema mume wangu na wakili wake akamzuia.
‘Shukurani gani wewe upewe, ..utufanyie unyanyasaji, utuzalilishe,
ututukane , halafu utegemee shukurani, ..nakuambia hivi mimi sikuogopi,
usinione hivi, mimi ninaweza zaidi ya hili, mimi sio mwanamke kama wanawake
wengine, kama ni kupigana nipo tayari, na wewe wala hunishindi, nitakuzalilisha
mbele ya watu hawa, umeniuzi sana mimi…’akasema.
‘Kwahiyo unataka nikuonyeshe mimi ni nani, sio…ukweli umekuuma
eeh..’akasema mume wangu.
‘Ukweli gani, ..sasa, ulikuwa hujaniafahamu mimi upande wa pili
wangu,s asa utanifahamu…umemtoa nyoka pangoni, sasa atakuuma, mimi nitawaambia watu
wote hawa kila kitu ...bila kuficha, nilishaahidi kuwa nitasema kila kitu siku
ikifika, naona sasa muda umefika...’akasema rafiki yangu sasa akimsogelea mume
wangu.
‘Aah, usimsogelee, kaa pale kwenye kiti kile cha ushahidi…’akasema
mwenyekiti wake..
‘Ndugu mwenyekiti, huyu mtu hajaalikwa hapa, mnamkaribisha, huyu
kaja na yake kwa vile kakosa alichokitaka, huyu mtu ni muongo mkubwa, hana
jipya hiyo ndio tabia yake,…amekuwa akimtimua mke wangu, kujinufaisha, na
baadae kaja kumsaliti rafiki yake mwenyewe, ..hapa, sasa a jifanya
kujikosha..nakuambia hivi, wewe mwanamke kwa sasa hupati kitu kwangu na kwa
rafiki yako umeharibu,umalaya wako umekuponza ....’akasema mume wa familia, bila kujali
Na hapo mwenyekiti akaingilia kati na kusema;
‘Hebu tutulizane kwanza, na nawaombe nyie wajumbe wawili mrekebishe
hizo kauli zenu, tusija kukifanya hiki kikao cha watu wasio wastaarabu, .na kwa
hizo kauli tutahitaji uhalali wake,
huwezi kutamka tusi,au nen la kashifa kwenye kikao kama hiki lipite bure,
utastahiki kulitolea ushahidi, vinginevyo, wewe mtamkaji utashitakwia kwa kutoa
maneno machafu mbele ya kikao halali..’akasema mwenyekiti
‘Mimi nitathibitisha kauli yangu mwenyekiti, hayo maneno
niliyotamka dhidi ya huyu mtu ni kweli na nina ushahid nayo…’akasema rafiki
yangu
‘Hata mimi nitathibitisha hayo ya kwango dhidi yako, ya kuwa wewe
umekuja hapa kwa nia ya kujikosha tu, na ni kutokana umekosa ulichokitaka
kutoka kwangu, mimi sio mtu wa kuchezewa...’akasema mume wangu.
‘Subirini tutakwenda hatua kwa hatua,.., tutakuhitaji nyote kuyathibitisha
hayo maneno yenu la sivyo kikao kitawajibika kuwachukulia hatua…. kwanza nataka
tutulie, maana naona mambo yanajileta yenyewe, tunakuomba ndugu uliyeingia,
utulie kwanza, ili tufuate utaratibu wetum huwezi kutuingilia na kuharibu
ajenda zetu...’akasema mwenyekiti.
‘Ndugu mwenyekiti, naomba mnipe hii nafasi , niongee, nafahamu mna
utaratibu wenu, lakini naona kuna mengi yalitokea, na imefikia mimi kuonekana mbaya, hata kwa rafiki yangu, na
ubaya zaidi ukaka kupandikizwa juu yangu,…’akasema
‘Ubaya huo ni wa mauaji ya Makabrasha, nakuja kushangaa, naambiwa
mimi nilihusika, wakati huyo mnayemuita mume wa familai siku hiyo alikuwepo,
wakati marehemu anauliwa, yeye anafahamu kila kitu,.. hebu muulizeni vizuri
siku hiyo kule kwa Makabrasha alifuata nini, na wakati alistahiki kuwa
hospitalini,…je aliwezaje kufika huko..huyu ndiye muuaji, anafahamu kila kitu...’akasema
na watu wakawa wametulia kimiya.
‘Hayo ni yako…mimi sijui kutumia silaha, wewe ni mtaalamu wa
silaha, je sio wewe uliyefanya hayo mauaji, ili kunibambikia mimi, unejileta
mwenyewe…’akasema mume wangu
Mwenyekiti hapo akatulia kwa makusudi…
‘Unataka nielezee siku ile ilivyotokea au sio, maana wewe huamini
kitu mpaka uambiwe ukweli, wakati ni kweli ulikifanya, ndio tabia yako, sio…sasa
‘akatulia akimgeukia mwenyekiti.
‘Naomba kibali chako, ndugu mwenyekiti ili nisema kila kitu kwa
ukweli wake na ushahidi, sitako niongee kama yeye, umeniuma sana, maana
nimefika kutoka masomoni na kukamatishwa watoto wa kihuni wanifanyie unyama,…mimi,
wakati mbaya mwenyewe yupo, kwanini yeye asifanyiwe hivyo, leo ni lazima niseme…’akasema
‘Sawa utasema lakini ngoja tufuate utaratibu..’akasema mwenyekiti
‘Samahani mwenyekiti ninaona kabla huu mukari haujashuka, uniache
mimi niendelee kwanza, sitaweza kuvumilia, mkizunguka zunguka, wakati muhalfu
yupo nanyi, na ninavyomfahamu hatakubali ukweli, mtazungushana naye tu, tafadhali
mwenyekiti, mimi nafahamu kila kitu mnachokihitajia…’akasema
Mwenyekiti akageuka kuniangalia mimi, halafu wakili wa mume wangu,
kabla hajasema neno, rafiki yangu huyo akasema;
‘Mimi sijawahi kutukanwa hivyo, eti mimi ni malaya… eti kwa vile
nimetembea na mume wa mtu, yeye huyo mume wa mtu ataitwa nani, mbakaji mkubwa
huyo, yeye ndio Malaya, tena wa hali ya juu, mbakaji ana sifa gani..ni nani
mwenye dhambi kubwa, kati ya mtu mwenye ndoa na asiye na ndoa, kwenye maswala
ya uzinzi, aniambie yeye,..’akasema na alipoona mwenyekiti anamuangalia yeye,
akasema
‘Samahani sana mwenyekiti,..naomba nikae hapo kwenye hiki kiti
maalumu, ili niweze kuwaelezea kila kitu kiushahidi na mwisho wake, tutaona
ukweli upo wapi, kuwa mimi ni Malaya au ni yeye...’akasema na kwenda kukaa
kwenye kiti cha mashahidi.
**********
‘Mke wa familia unasemaje, tuendee naye au una shahidi mwingine?’
akaniuliza mimi na wakati huo nilikuwa nimeshikwa na hasira, sijui kwanini
nikimuona huyo rafiki yangu, ninakuwa hivyo, nilitamani wale wahuni waje,
wamfanyie ubaya mbele ya watu wote hawo, nikamwangalia huyo rafiki yangu kwa
macho ya hasira, maana nilishampatia dhabu yake na haikuwahi kufanyika,…hapo nikamwambia
mwenyekiti.
‘Nataka huyu mtu asema ukweli wote, na haki itendeke, kwani wote
lao ni moja, mume wangu, na huyo rafiki
yangu, alikuwa rafiki yangu, kwasasa hivi sio rafiki yangu tena, nawaona wote
lao ni moja, kwangu mimi ni wasaliti, sina msamaha na hawa watu wawili,
....’nikasema
‘Mke wangu…’akataka kuingilia mume wangu na mwenyekiti akamzuia
kwa ishara ya mkono, na rafiki yangu akachukua nafsi hiyo kwa kusema;
‘Hata wewe usijitetee, na kujiona msafi sana nakuheshimu sana, na
nitaendelea kufanya hivyo…ila na wewe una mapungufu yako.., kwani isingelikuwa
wewe kunishauri haya, unafikiri mimi ningeliyafanya …nisingeliingia kwanye
ubaya na mume wako,..’akasema
‘Lakini hayo kwangu nimeyasahau, ..najua hata nifanye nini, ubaya
wangu hauwezi kuzidi haya niliyokufanyia, lakini…kuna mbaya wetu zaidi, ambaye
anastahiki kuzibeba lawama zote hizo,..huyo mume wako,…, uneyemuita mume wako,
nataka leo akitoka hapa, anaelekea jela, kwani hastahili kuishi kwenye maeneo
ya raia wema, nina ushahidi wa kutosha, kwa hilo wa kumweka, ndani...’akasema
rafiki yangu.
Mume wangu akajifanya kucheka na kutikisa kichwa, huku
akimuangalia wakili wake, na wakili wake akamuashiria atulie kwanza..lakini
mume wangu hakuweza kutulia akasema;
‘Usinitishe wewe, ....toa huo ushaidi wako, na mimi nitakuja kutoa
ushahidi wangu kuwa wewe ni Malaya, pili mlaghai, na tatu, msaliti, na pia wewe
unahusika na mauaji ya Makabrsha,..utasema ukweli ulikuwa wapi siku ile…nilikuja
kuyafahamu hayo, wewe siku ile tokea muda mrefu ulikuwa na marehemu, ukajifanya
kujificha uwanja wa ndege…’akasema mume wangu
‘Haya sawa, ngoja tuone mimi na wewe ni nani zaidi, si ndio hivyo,
kikao kitatusikiliza, kila mtu atoe ushahidi wake, na uwe wa ukweli, na hapo
ndio tutaona ni nani malaya, ni mimi au wewe, ninani ana sifa hizo mbaya,
usaliti, wizi, ubakaji, umalaya na uuaji, tuanza kazi mwenyeki....’akauliza
akimgeukia mwenyekiti, na mwenyekiti akageuka kuniangalia mimi.
Na mimi nikaguka kumuangalia wakili wangu…
NB: Haya mambo yamekwenda haraka kihivyo, tumerahisishiwa kazi…,
lakini ndivyo ilivyotokea, tuwepo kwenye sehemu ijayo,
WAZO LA LEO: Tuchunge
sana kauli zetu tunapoongea, kuna maneno yakitamkwa mbele za watu, yanakuwa na
picha mbaya, lakini kuna watu ni wepesi kuyamtamka hayo maneno kama vile
ni maneno ya kawaida, kwa lugha sahihi, yanaitwa ‘lugha za matusi’ .
Kuna baadhi ya watu
wanayatuma haya maneno bila kujali anayamtaka wapi, na kwa nani, na anamlenga
nani, baya zaidi, wengi wanaozalilishwa kwa maneno hayo ni akina mama, ...iweje
ugombane na mtu mwingine baki, wewe unakimbilia tusi linalomlenga mama, mzazi
wa mwenzako, unamtusi yule mtu mwenyezi aliyekuzaa, je huyo mama kakukosea
nini, ...tuchunge sana ndimi zetu, kwani tunajilaani sisi wenyewe kwa kauli zetu chafu.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment