Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Thursday, February 8, 2018

MKUKI KWA NGURUWE-77



‘Bila kupoteza muda nikanywa yale maji yaliyochanganywa na sumu , sumu ambayo ukiinywa kutokana na maelezo ya muuza dawa za mifugo:

‘Hii sumu ni hatari sana kwa watu, usije kuiweka sehemu ya ovyo, ..tafadhali, kama unataka kuua, panya,..na wanyama wakubwa wakubwa, weka kidogo kwenye maji, watakufa hapo hapo..unasikia…’alisema muuza madawa.

Tuendelee na kisa chetu

*********

Wakati binti wa kijijini, anaendelea kutoa ushahidi wake huo mimi nilikuwa napigana na dhamira yangu, maana, nilihisi chuki, hasira, na kutaka kufanya jambo, sijui hali hiyo ilikuwa ikielekezwa kwanani, kwani mimi nilishaapa kuwa yoyote atayeingilia ndoa yangu, nikimgundua, sitajali ni nani, sitasubiria polisi au kwenda kumshitaki, nitachukua hatua mimi mwenyewe, na nilishabuni njia ya kuwaadhibu watu wa namna hiyo.

Sasa huyu binti wa watu wa watu, ndio kaingilia ndoa yangu lakini sio kwa kupenda, je na yeye anastahiki adhabu hiyo…hapana

Hapa mkosaji ni mume wangu, yeye ndiye atabeba madmabi yote hayo, na sijui nitampatia adhabu gani ili nafsi yangu iridhike..Kilichoniuma zaidi ni kuwa mambo hayo yalifanyika ndani ya nyumba yangu, mimi nikiwepo, mimi ambaye nilibeba dhamana ya huyo binti, … japokuwa sikufahamu hilo..ila kwa namna nyingine nalaumiwa mimi

‘Nilimualezea mama lakini alionekana hakujali, yeye alijali kazi zake, ..’ nikauli ya kunishitakia.

Yule binti mtoa ushahidi akawa anaendelea kutoa maelezo yake;

 ‘Nilikunywa yale maji ambayo nilikuwa nafahamu kuwa yana sumu, kwanza nikapiga fundo moja, nikaona yananyweka, nikaweka la pili, na baadaye nikayanywa yote hadi tone la mwisho halafu nikaweka kile kikombe, juu ya karatasi niliyokwisha iandika, na mimi taratibu nikapanda juu ya kile kitanda, kilichonitesa, nikalala nikiangalia juu, nikisubiri kufa, dakika tano zikapita, kumi zikapita, robo saa,sikuoni hata dalili zozote za kufa, sikusikia maumivu ya tumbo, tofauti na maelezo ya muuza duka..

‘Ina maana hii dawa ime-ekisipaya nini, ‘nikajiuliza,akilini nikapanga nichukue ile dawa iliyobakia, ambayo niliicha chumbani kwangu,nikataka niinuke nienda kule lipo, niikoroge ninywe hata nikizidi kipimo, haijalishi..ninachotaka mimi ni kufa tu..

Nikawa sasa nataka kuinuka, mara mlango ukagongwa,...nikashituka,

‘Labda ni malaika wa mauti anakuja kihivyo…’nikajisema moyoni, huku bado nimelala pale pale..kukawa kimia, nikainua kichwa, na wakati huo mlango ukawa umegongwa tena.

Hapo sasa nikajua ile dawa ni ya uwongo, huenda muuza duka, aliafahamu dhamira yangu akanipa dawa ambayo sio…nikajiinua kidogo, mwili ulikuwa hauna nguvu, mawazo,…nikawaza huenda ndio hiyo dawa inafanya kazi,mimi nikatulia..

‘Mlango ulivyoendelea kugongwa tena, nikahisi ni baba wa nyumbani kaja,...lakini yeye hana tabia ya kugonga mlango, huwa akija anaingia moja kwa moja hajali kuwa mimi nipo katika hali gani,...

‘Huyo atakuwa ni mtu mwingine , …atakuwa nani muda kama huu..’nikajiuliza
Hata hivyo sikutaka kusimama kusimama, nilikuwa bado nina imani kuwa hiyo dawa itafanya kazi, labda inachukua muda, na nilitaka mimi nifie hapo hapo kitandani

‘Hodi hapa…’ilikuwa sauti ngeni…lakini dio ngeni sana,…hata hivyo akili yangu ilishakwenda kwa wafu, sikutaka kuifikiria dunia, kwahiyo nikawa kama nimedharau, ili huyomgongaji, akate tamaa aondoke zake, na mimi niendelee na zoezi langu.

Nikawa nimefumba macho nikiwaza kuwa huenda dawa ndivyo inafanya kazi taratibu kwahiyo sasa naelekea kukata roho, lakini kwanini tumbo haliumu, mara nikahsi  mlango umefunguliwa..sikfumbua macho kwa haraka

Na mara nikahisi mtu akikaribia pale kitandani nilipolala, nikaanza kufungua macho taratibu,, na sura niliyoiona mbele yangu, ikanifanya nifungue macho kwa haraka, na kujikunyata , nikiogopa, na kuuliza kwa haraka;

‘Wewe umefuata nini huku chumbani?’ nikauliza na yule mtu akasema kwa sauti ya pole pole, kama mwalimu anayefundisha watoto wadogo;

‘Unafahamu nilikuwa nakuamini sana,kuwa wewe ni binti jasiri...’yule mtu akaniambia

‘Toka humu ndani..’nikasema

‘Umenisikitisha sana,, ....’akasema

Hapo, nilikuwa nimejikunyata kama mtu anayejikinga asipatwe na baya, nikainuka kwa haraka pale kitandani na kukaa, nikanyosha lile gauni vizuri, na kumwangalia huyo mtu aliyeingia, alikuwa mkononi kashikilia kikombe, kinachofanana na kile kile nilichokuwa nimeweka sumu. Vikombe kama hivyo vipo vingi hapo nyumbani. Nikamuuliza

‘Unataka kunifanya nini, kwanini unanifuata huku chumbani?’ nikamuuliza nikiwa nimeshamuweka kwenye kundi hilo hilo la watu wabaya, ....

‘Hahaha, unafikiri nitakufanya nini, mimi sina tabia hiyo, tabia yangu ni nyingine kabisa, pesa…hiyo ndiotabia yangu…’akasema

‘Sasa umefuata nini huku ndani…?’ nikauliza

‘Nilikuona ukitaka kujiua..’akasema

‘Uliniona…!!?’ nikauliza kwa mshangao
‘Ndio nilikuona..nikiwa ofisini kwangu ikanibidi nichukue pikipiki kwa haraka kuja hapa kukuokoa,...’akasema

‘Kwanini umefanya hivyo…?’ nikamuuliza

‘Kwasababu sitaki wewe ufe, unahitajika sana ..kwenye mipango yangu, na nikuambie kitu, wewe hutakiwi kujiua, nafahamu yote yaliyotokea dhidi yako, na nilikuwa natafuta njia za kukusaidia, lakini imekuwa vigumu kukupata, na kila nikija hapa unanikwepa, unaniogopa...kama vile mimi ni mtu mbaya, mimi sio mtu mbaya, nakujali sana’akasema huyo mtu

‘Umejuaje hayo wakati sijamwambia mtu dhamira yangu?’ nikamuuliza

‘Mimi macho yangu yanaona mbali, kila wanachokifanya watu kwenye hii nyumba mimi nawaona, mimi nakupenda sana, na nilishakuambia awali kuwa mimi nakupenda sana, unakumbuka…’akasema

‘Sikumbuki mimi, wanaosema hivyo wote nawaogopa, hawana ukweli..’nikasema

‘Mimi sikupendi kwa nia hiyo unayoifikiria wewe, …mimi nakupenda kwa moyo, na kukujali, .. na unakumbuka nilikuambia mimi ningeliweza kukusaidia kwa kila hali, nilikuomba uwe rafiki yangu wa karibu, ukawa unamjali sana huyo unayemuita baba yako, sasa kipo wapi...’akasema

‘Uliingije humu ndani na hicho kikombe kina nini,?’ nikamuuliza

‘Hilo sio muhimu sana, ila usijaribu tena kutumia hii sumu, usijaribu tena kujiua,kwanini ujiue wakati aliyekufanya hivyo, yupo hai, anastarehe, na hata ukifa yeye, hatapata shida, utazika na wote watakusahau…’akasema

‘Mimi sijali,..i bora nife tu….’nikasema

‘Sikiliza nikufumbue macho na masikio, kwanini unajipa shida wakati keshakutengenezea njia ya kuondokana na huo umasikini ulio nao.’akasema na mimi hapo nikashituka, japokuwa bado sijamuelewa.

‘Nielewe vyema…mimi nataka kukusaidia jambo, … mimi nitakufundisha kila kitu, cha kuweza kukusaidia na kusahau umasikini wako…na kuanzia leo jihesabu kuwa wewe sasa ni tajiri..kama utakubaliana na mimi.’akaniambia huku akinusa ile dawa kwenye kile kikombe.

‘Hii ni sumu mbaya sana, kama ungekunywa, ungeharibika matumbo yote, na ungekufa kwa machungu makali, sana, kwanini unataka kujitesa kiasi hicho?’ akaniuliza

‘Kuna haja gani ya kuishi baada ya haya yote..’nikasema

‘Hayo yote uliyoyaandika kwenye hiyo karatasi, niliyasoma, ni ujumbe tu usio na maana na ambao wangeusoma, wangelikuona wewe ni mjinga tu, wangekuzika, wakakusahau, usiwe mjinga kiasi hicho…’akasema

Hapo ndio nikagundua kuwa kumbe ni yeye alibadili kikombe nilichokuwa nimeweka sumu na kuweka kingine kisichokuwa na sumu, moyoni nikajiuliza huyu mtu anadhamira gani kwangu.

‘Ujue,...mimi nilishaanza kuwafuatilia wote kwenye hii nyumba, nayafahamu yote yaliyotokea, ...hebu angalai hii hapa...’akatoa kitu kama simu, lakini kubwa, kama komputa ndogo, akaiwasha, halafu akawa anafanya kitu kwenye hicho kidude, akainama kunionyesha

‘Unaona yote yaliyotendeka hapa ndani nayafahamu, ...’akasema huku akinionyesha, tukio mojawapo wakati baba huyo hapo akinibaka kwa nguvu, na akaonyesha na jingine …sikutaka hata kuangalia.

‘Wewe ni mchawi, umeyapataje hayo..’nikasema.

‘Hahaha, lakini mimi sio mchawi wa kiafrika ni kisasa, wa kidhungu,…hahaha..’akacheka huku akizima kile kidude chake kama simu.

‘Sasa sikiliza fuata yote nitakayokuambia, ili upate haki zako, ...sasa ninakupa mbinu za kuwa tajiri, kama kweli utayafuata hayo nitakayokuambia,... kwa hivi sasa, akija baba yako mwambie una mimba yake, usimfiche kabisa, kama ulivyoeleza kwenye huo ujumbe kuwa una mimba yake, umweleze hivyo hivyo, na baada ya hapo ..’akatulia

‘Sitaki kumuambia…ataniua…’nikasema

‘Hwezi kukuua, sikiliza kwa makini maagizo yangu, sasa hivi usiogope kabisa, jenga ujasiri,..sasa ni muda wa kutengeneza pesa, …ni lazima unamdai pesa, tena pesa nyingi...’akasema na mimi nikamtolea macho ya kushangaa.

‘Usishangae, hawa watu wana pesa nyingi sana, ndio zinawapa kiburi cha kufanya hayo waliyokuanyia…’akasema

‘Kwa vipi…?’ nikauliza

‘Kwa vipi ni hivyo nitakavyokuelekeza…’.akasema na ndio akaanza kunielezea kwa kirefu jinsi gani niongee na baba wa hiyo nyumba akija...aliyoniambai niliona kama ni mambo yasiyowezekana, lakini yeye akanipa moyo kuwa hayo yanawezekana, maana baba wa hiyo nyumba, anamfahamu vyema na udhaifu wake, akiambiwa hivyo ni lazima ataogopa...’akaniambia

‘Mhh,..’nikaguna tu hivyo, sikumuamini

‘Baba yako huyo udhaifu wake upo kwa mkewe, fanya kama nilivyokuagiza…’akasema

Mimi sikuwa na chohote cha kusema au kukataa, maana yale niliyoyaona kwenye hiyo simu yake,yalinifanya nimuogope zaidi huyo mtu, na nilifahamu nisipofanya hayo anayoyataka, huenda ataweza kunifanyia lolote, na kuzionyesha kwa watu, hizo picha chafu na mimi nitazalilika zaidi, na watu huenda hawataniamini, kwangu mimi hayo yalikuwa ni aibu tupu, nikawa sina jinsi nikamkubalia hayo aliyonielekeza, na mwishoni akaniambia.

‘Kwanza kabisa unamdai shilingi Milioni kumi..’akasem

‘Mungu wangu…’nikasema hivyo

‘Hahaha, milioni kuwa kwa hawa watu ni kitu kidogo tu, hasa akiona hatari kaam hiyo, …unaona eeh, hebu fikiria ukiwa na pesa kama hizo utafanyia nini, utakuwa tajiri, kwa dhambi zake…’akasema

‘Na huo utakuwa ni mwanzo tu,...maana kwa sasa una ushahidi wa kumfanya lolote unalolitaka, ukizipata hizo pesa, nusu yangu na nusu yako..unanielewa...baada ya hapo nitakuelekeza namna nyingine ya kuzipata hizo pesa nyingine kila mwezi,..na atazitoa tu hana ujanja, vinginevyo….’akaniambia na mimi nikamuitikia kwa kicha kukubali,na hakukaa sana akaondoka zake...

********a
‘Milioni kumi…’nikajikuta nikisema hivyo, maana ni kitu ambacho sijawahi kukifikiria kichwani, kupata pesa nyingi kiasi hicho, hapo hapo ibilisi la pesa likaanza kuningiia,
‘Milioni kumi…kweli..’nikawa nasema hivyo tu

Mimi nikatoka pale chumbani na kwenda kuendelea na shughuli nyingine nikimsubiria baba mwenye nyumba aje.., nilifahamu kuwa muda kama huo atakuwa anarudi, na kweli kabla sijatulia, mlango ukafungulia na mwenye nyumba akaingia, akiimba nyimbo zake za kilevi...

***********

Kama kawaida yake, alikuwa kalewa, na siku hizi alikuwa kazidisha kweli kweli, utafikiri sio yeye, niliyemfahamu kipindi cha mwanzoni,  alikuwa kalewa, anapepesuka, na moja kwa moja akaingia kwenye chumba hicho anachopumzikia, na nilijua baada ya muda ataniita,  mimi nilikuwa nimeshatoka nipo nje, na nikasikia akiniita,

Nikajivunga kidogo, akaniita sasa kwa ukali, na hapo ndio taratibu nikaenda huko chumbani, nikijua ni nini kitafuata, …nikaingia ndani na kumkuta kavua nguo kabakia na chupi tu, yaani hana hata aibu mbele yangu, akaniambia niende tulale naye, nikakataa..

‘Unaleta kiburi eeeh, kwanza leo sikutaki, nilikuwa nakujaribu tu, nimechoka, nimeshastarehe huko nilipotoka, na watu wanaofahamu mapenzi, sio wewe mpaka tushikane miereka, mmh, ni shida tu, japokuwa kuna raha yake…’akasema

‘Lakini..eeh, ,..lakini-kumbuka kuwa nikikuambia kitu, ukanikatalia ujue kuwa mama yako nitam-maliza,.yule mama yako masikini masikini, eeh, nita-mu-maliza,…kwanza nilishampigia simu kuwa wewe siku hizi una kiburi, ..akalia sana..anasema hajakufundisha hivyo….’akasema kilevi

Sikutaka aendele kuninyanyasa kwa kupitia kwa mama yangu, nikasema kwa kiburi;

‘Fanya unalota, sasa hivi siogopi, maana mimi sina maana tena kwenye hii dunia..ulichonifanyia, kinatosha, umenizalilisha vya kutosha..kunizalilisha huku ni sawa na kuizalilisha familia yangu…’nikasema

 Kwanza akashangaa…hakutegemea mimi kuongea vile, akanikodolea macho, na mimi sikumjalia nikaendelea kusema

‘Na nafahamu unatufanyia hivyo kwa vile sisi hatuna maana kwenu…ni masikini, lakini kumbuka na wewe ulipotoka…na sisi hatukuomba tuwe hivyo, mungu anayaona haya yote…’nikasema na yeye akasimama, na kutaka kuja kunishika kwa nguvu kama kawaida yake, mimi nikamsukumiza kwa nguvu zote, akadondoka chini, alikuwa kalewa, hakuwa na balansi, ila akikukamata ana nguvu za ajabu, sikupenda aniwahi kunikamata, nikamwambia;

‘Mimi nina mimba yako..’nikasema hivyo

Hiyo kauli ilimfanya ashtuke,..na haraka akasimama juu, na ikawa kama pombe zote zimemuishia, akatikisa kichwa na kupangusa macho akaniuliza

‘Unasema nini wewe...?’ akaniuliza

‘Nina mimba yako,..umenibaka na sasa umenipa mimba…je  ulivyokuwa ukinibaka , ulitegemea nini, sasa nina mimba yako, nilikwenda kupima leo mchana, nikaambiwa nina mimba, na mimi simjui mwanaume mwingine zaidi yako wewe, ..wewe ndiye uliyenianza, na sasa nina mimba yako, nitamwambia mama akija..’nikamwambia.

‘Nitakuua,..unasema nini wewe Malaya, , kwanza toka kwenye hiinyumba haraka, sitaki hata kukuona, toka kimbia na potelea mbali Malaya mkubwa wewe....’akasema

‘Mimi nitaondoka tu, sina haja ya kukaa hapa, ...’nikasema

‘Sawa, sasa hivi fungasha, ..ondoka, ..vinginevyo nitakuua…’akasema

‘Nitaondoka …lakini kwa masharti, nataka pesa za kujenga nyumba kama ulivyoniahidi, pesa za kutosha, nyumba nzuri kule kijijini, kwa sasa utanipa kiasi cha kuanzia, nataka pesa za kunitosha kuilea hii mimba yako, unawajibika nayo, , ...’nikasema

‘Nini…! ‘akasema hivyo kwanza

‘Ndio hivyo, ukifanya hivyo ndio nitaondoka humu ndani, mbali kabisa na nyie, la sivyo…’nikasema

‘Wewe Malaya mkubwa, ina maana unanisingizia kuwa nimekupa mimba ili nikupe pesa, pesa hupati, na humu ndani utaondoka...’akaniambia huku akinitolea jicho.

Nikachukua ile karatasi niliyopima hospitalini, na kuna picha aliniachia huyo jamaa ambaye alikuwa na kumbukumbu zote za hapo nyumbani, na matendo aliyonifanyia, nikampa
‘Ni nini hiki…?’ akauliza

‘Angalia mwenyewe ushahidi wa madhambi yako…’nikasema

 Akawa anaisoma ile karatasi ya docta, na alipofikia kuziangalia zile picha akatupa chini, kwa hasira,  akisema;

‘Nitakuua, unasikia, ninaapa nitakuua,...ni nani kakusaidia kuyafanya haya, ..’akasema akiangalia ile picha pale chini, ilikuwa imekaa vyema inaonyesha lichokuwa akinifanyia.

Akaipiga teke lakini hakigeuka, akasema

‘Kwa hili mimi,, ...nitakuua, usipoondoka kwenye hii nyumba, usiku wa leo nitahakikisha unakuwa maiti..’akaniambia huku akitaka kuinama kuchukua ile picha na ile karatasi ya vipimo nilivyompa, sasa akawa anaviangalia huku katoa macho, kama kaona kitu cha kutisha, mimi nikamwambia;

‘Mimi siogopi kufa, nilishajiandaa kufa, lakini bahati nzuri kuna mtu kaja kaniokoa, na yupo tayari kunisaidia hili jambo, ikibidi tutalipeleka mahakamani, lakini kwanza ni lazima nimfahamishe mama..’nikamwambia

‘Ni nani huyo aliyekusaidia?’ akaniuliza kwa hasira, sasa akionyesha wasiwasi.

‘Haina haja ya kumfahamu kwa sasa…, ninachotaka ni hizo pesa kwa haraka, ili niondoke hapa kabla mama hajarudi,na ikitokea akaja na kunikuta hapa nyumbani nitamwambia yote na ushahidi wote nitamuonyesha...’nikamwambia

‘Ohoooo, kumbee, …sikujua, wewe ndio janja yako, ndio tabia yako, eeh,..kwanza ni nani huyu..aliyekusaidia kufanya huu uchafu.’akasema kwa hasira, akijua labda nitatishika, hakujua kuwa sasa nimepata ujasiri niliokuwa sina kabisa.

‘Unapoteza muda, nataka kuondoka...sikuwa na tabia chafu, kama unavyosema wewe, uchafu huu, ulinianzishia mimi, na sikuwa na wazo kama hilo kabisa, ila kutakana na haya sina jinsi, na sitarudi nyuma, ….’nikamwambia

‘Wewe ondoka, nitakutumia hizo pesa,kwasasa sina pesa za kukupa ...’akasema sasa akiwa anaongea sauti ya kawaida sio kama ile ya ulevi, naona alishahisi hatari.

‘Mimi sitoi mguu wangu humu ndani, nizipate hizo pesa bila kupungu ahata senti moja,…kama nilivyokuambia sipo peke yangu kwa hili, huyo aliyenisaidia ana kila kitu zaidi ya hiki, ana picha ya video ukinibaka,..kila kitu kipo wazi, ukinua mimi yeye atakuja kwakokama mbogo aliyejeruhiwa..’nikasema

‘Shilingi ngapi, unataka wewe Malaya tu, nia yako si pesa nitakupa uondoke humu ndani kwangu...?’ akauniuliza huku akinitolea macho ya kunitisha, lakini niliona ajabu, sikuwa naogopa tena, utafikiri kuna nguvu za ajabu ziliniingia.

‘Milioni kumi...’nikasema, na aliposikia hicho kiasi akashituka, karibu adondoke, na kuniangalia kwa macho ya chuki, akasema;

‘Ni nani huyo kakufundisha uchafu huo, milioni kumi, wewe unaota, pesa zote zote hizo unazitaka wewe za nini wewe masikini?’ akaniuliza

‘Ni mtu wa usalama wa taifa, nilimwambia akanifundisha jinsi gani ya kuwakomoa watu kama nyie..hata kama ni masikini , lakini ni bora ya uamsikini wangu kuliko utajiri wenu wa kinyama, wenye tabia chafu ya unyanyasaji, ubakaji,....wizi na dhuluma..’nikamwambia

‘Unasema usalama wa taifa...ni nani huyo?’ akauliza sasa akinywea.

‘Utanipa hizo pesa au niendelee na shughuli zangu nimsubiri mama, aje, nimwambia hivyo, na sasa nikamuona hana jinsi, akabadilika akawa mnyonge, akawa yule baba niliyemfahamu awali

‘Hebu subiri nifikirie...’akasema na pombe zote zikaisha, na mara akachukua simu na kuanza kuongea na watu wake kama watatu, kila mmoja alikuwa akimuomba pesa, milioni tatu tatu, na wa mwisho milioni moja, akawaambia wampe mdogo wake, atazileta hapo nyumba

**********


Mdogo wake namfahamu sana, huwa yeye hakai sana hapo nyumbani, na akija huwa na chumba chake nje ya nyumba kubwa, kwahiyo mara nyingi hafahamu kinachoendelea humo ndani, lakini mara nyingi ndiye anayemtuma mambo yake..na wakati mwingine wanakwenda kulewa pamoja, akizidiwa ni kazi ya mdogo wake kumrudisha nyumbani.

Nikaenda chumbani kwangu nikajiandaa, na huku nikiwa na tahadhari, kama nilivyoambiwa na huyo mtu aliyenifundisha hayo yote, maana niliambiwa kuwa nikimwambia hivyo huyo baba anaweza akaniua, kwahiyo nikawa nina kisu kikali tayari kwa kujihami, hakupita muda nikasikia pikipiki nje,...

Nikachungulia nje, nikamuona mdogo wa huyo  baba akiwa na pikipiki, akaingia ndani nikasikia wakiongea na kaka yake kwa muda, baadaye nikasikia mlango wa chumbani kwangu ukigongwa, alikuwa huyo mdogo wa baba mbakaji, akaniita nitoke pale chumbani, nikatoka , akaniambia kuwa kaka yake kasema nichukue kila kitu changu , yeye atanichukue na pikipiki, na kunipeleka sehemu nitakapolala hadi kesho,..

‘Yeye yupo wapi?’ nikamuuliza

‘Yupo ndani kalala, kasema kila kitu kipo kwenye huu mfuko, akanipa mfuko, nikaangalia ndani na kukuta mabulungutu ya pesa, nikayahesabu moja moja, hadi yakatimia idadi , kwa yalivyofungwa, sikuweza kuhesabu moja moja, lakini kwa bunda moja moja, ambalo liliandikwa juu, milioni moja, nilifahamu kuwa zimefika milioni kumi, nikazichukua na kuziweka kwenye mkoba wangu wa safari, nilizifunga vizuru sana.

‘Twende, kaka kasema hana haja ya kuonana na wewe...’akaniambia,na mimi nikafanya kama alivyosema huyo mdogo wake, tukaondoka naye kwa pikipiki , hadi sehemu aliyoniambia kuwa nitalala hapo hadi kesho.

‘Mimi nakwenda kukata tiketi, kaka kaniambia unaondoka kesho asubuhi na mapema, sijui kuna nini kinachoendelea kati yenu, sitaki kufahamu, ila nakuonya ,kama kuna mtu anayekudanganya ujue umajipalia mkaa, hizo pesa unaweza usionje hata utamu wake, ni pesa haramu hizo,..na  kaka kakasirika kweli, kwa jinsi ninavyomuona anaweza hata kukua,...’akaniambia

‘Mimi sijali kukasirika kwake, alichonifanyia mimi ni dhaidi ya hizo pesa,..., nimeshamuambia kwa hivi sasa sijali kufa, ameshaniua moyoni, kilichobakia hapa ni kiwiliwili tu,...’nikamwambia, na huyo ndugu yake akaonyesha kushituka kidogo, baadae akaondoka zake baada ya kuhakikisha nimekula, na pesa za matumizi.

‘Mimi sitakuja leo, tutaonana asubuhi sana usitoke nje,...’akaniambia

‘Mimi sitoki nje niende wapi sasa nsubiria aje kunai…na kama nikitaka kutoka nje, sitakaa sana, nitarudi humu humu,..na zaidi kama nikiona vipi nitarudi kule kule nionane na mama, mwenye nyumba’nikamwambia.

‘Wewe..usirudi tena kule kuonana na shemji yangu,  kaka kasema usirudi huko kabisa, wala usije kuonana na huyo mama mwenye nyumba, mimi nakuamini, ndio maana nakuacha peke yako, la sivyo, niliambiwa nikuchunge hadi hapo utakapoondoka kesho, niahidi kuwa hutatoka nje, mpaka kesho’akaniambia.

‘Niende wapi, siendi mahali, ..nakusubiri wewe na mkileta ujanja nimeshampigia huyo mtu wa usalama wa taifa, ananifuatilia kila ninapokwenda...’nikamwambia

‘Usalama wa taifa..ni nani huyo !! ..ooh kumbe ndio maana eeh,  kuna mtu nimemuona akitufuatilia nyuma, toka tunatoka kule nyumbani, na nahisi yupo hapo nje,..’akasema

‘Habari ndio hiyo...’nikamwambia na hapo hapo akachukua simu na kumpigia simu kaka yake,akimwambia kweli kuna mtu ametufuatilia kwa pikipiki, na huenda ni usalama wa taifa. Mimi sikujua kuwa kuna mtu alikuwa akitufuatilia, na siwezi kujua ni nani, labda ni yule jamaa aliyenipa hizo mbinu, ambaye kwenye zile pesa, alitaka nimpe nusu.

Moyoni nikasema huyu mtu simpi hata senti moja, kwa kazi gani aliyonifanyia...na mimi tamaa za pesa zikawa zimeniingia.

Alipoondoka huyo mdogo mtu, nikatoka pale ndani na kuangalia huku na kule, sikuona mtu, haraka nikachukua begi langu, kwa kupitia mlango wa nyuma, nikatoka,...na kuingia mitaani, nikachukua boda boda hadi sehemu nyingine, nikatafuta nyumba ya wageni nikalipia kwa siku moja, nikalala huko, na hiyo ilikuwa salama yangu. Nilikuja kupata taarifa kwa mtu anayenifahamu, ambaye aliniona nikifika pale, mtu huyo aliniambia kuwa kwenye ile nyumba, usiku kulitokea ujambazi,

Aliniambia kuwa kuna kundi la watu walifika wakinitafuta mimi,lakini waliponikosa, ikabidi wawapore watu pesa zao, ...aliniambia huyo jamaa ambaye nilikuja kukutana naye huko kijijini, baada ya siku nyingi.

Asubuni ya siku ile, niliwahi kituo cha Ubungo, nikampigia simu huyo mdogo wa baba..alishangaa kunisikia nikiongea

‘Ulijua nimekufa sio…’nikasema

‘Ha-hapana, ni kwa vile umenipigia simu, nitakuja kukukatia tiketi…’akasema

‘Kwahiyo kumbe ulikuwa hujakata tiketi…’akasema

‘Niliwauliza hapo ubungo wakasema tiketi inakatwa siku hiyo hiyo…’akasema

‘Sawa, sasa mim nitakata tiketi mwenyewe haina haja yaw ewe kufika huku tena, nitaondoka usiwe na wasiwasi na mimi, mwambie kaka yako, kuwa nikifika nitawasiliana naye…’nikasema

‘Usikate wewe mwenyewe nitakuja kukukatia tiketi mimi, kaka alisema nihakikishe kuwa umeondoka…’akasema

‘Uhakikishe nimeondoka wakati alitaka kuniua..au una njama nyingine tena za kuja kunimalizia, ukija safari nitakuitia mwizi, unasikia usije kabisa hapa kituoni..’nikamwambia, na kukata simu

************



Ni kweli, nilinuna tiketi, ya usafiri wa kwenda huko kwetu, na mara kwa mara huyo mdogo wa baba, akawa ananipigia simu, lakini nikawa sipokei, hadi tunaondoka, sikuonana naye...’

Alipofika hapo akatulia na kusubiri, kama ataulizwa swali na mwenyekiti akamuuliza.

‘Huyo mtu aliyeweza kuchukua picha za tukio la hapo ndani, ulikuwa na mazoea naye kabla?’ akauliza mwenyekiti

‘Alikuwa mara kwa mara akija hapo nyumbani kabla, lakini hakuwa akionana na mama wala baba, na kila mara akija alikuwa akiniuliza mambo ya hapo nyumbani, nilifahamu kuwa ni rafiki wa baba wa hiyo nyumba, kwani kuna siku nyingine walikuwa wakija wote,

Alijaribu kunizoea sana, akisema yeye ni ndugu yake baba, kwa baba mwingine, na anamsaidia baba kwenye shughuli zake za biashara, nilishangaa ni kwanini baadae alikuja kumfanyia hivyo..mimi sikutaka hata kufahamu zaidi

‘Ila  nakumbuka  kuna siku moja alikuja, akanituma kumchukulia maji, na niliporudi akawa hayupo pale nilipomuacha, baadaye akatokea, nilimuona kabisa akitokea  chumba anacholala, huyo baba aliyenitenda hayo machafu. Chumba cha wageni, nilitaka nimsemee kwa mama, lakini nikasahau

‘Unafikiri alikwenda kufanya nini?’ akaulizwa

‘Kwa kipindi kile sikujua alichokwenda kufanya, lakini alikuja kuniambia kuwa kwenye ile nyumba,a likuwa kaweka vyombo vya kunasa matukio yote ya humo ndani, kwahiyo alikuwa akifahamu kila kitu kinachoendelea humo ndani..na aliniambia hayo alipokuja huko kijijini, kumbe ni mtu wa huko huko kijijini,..na anafahamika sana, mimi sikuwa namfahamu kabla...’akasema.

‘Kwahiyo mkajenga urafiki wa karibu kutokana na hilo tukio…?’ akaulizwa

‘Sikujenga urafiki naye kihivyo, ni urafiki tu wa hilo tukio, na ilibidi anielekeze jinsi gani ya kuzipata hizo pesa za kila mwezi,…na akija hapo kijijini anakuja kudai pesa zake, nikawa simpi kama anavyotaka yeye, na ilifikia kipindi alitishia kuwa atanifanyia kitu kibaya, kweli namuogopa, lakini moyo wangu ukajaa usugu fulani, sikujali kufa tena.

Baada ya kuondoka na zile milioni kumi, alinifundisha kuwa kila mara nitakuwa nadai milioni mbili mbili, moja yake, kuna muda alikuwa  anapandisha kiwango kuwa nimwambie huyo baba aitumie milioni tatu, hata tano,.akijua huyo baba ana pesa, kama hana anasema tudi milioni mbili zisishuke hapo

‘Nikawa namuuliza yeye anataka pesa za nini, wakati hana baya lolote alilofanyiwa, akasema ni gharama ya vyombo vya kunasa matukio yote kwenye hiyo nyumba.

‘Vyombo hivyo vinauzwa pesa nyingi, nataka nipate hizo pesa kuwalipa watu walioniazima hivyo vyombo, kwasababu asingeliweza kuvinunua, kwani vinauzwa pesa nyingi, kwahiyo alikuwa akiazima kwa muda fulani...’akasema

‘Je ulipofika huko kijijini ilikuwaje?’ akaulizwa

‘Sikuenda moja kwa moja kwa mama, nilikwenda kijiji cha jirani, huko nikanunu shamba na kujenga nyumba yangu nzuri, na ilipokamilika ndio nikaenda kumchukua mama...’akasema

‘Ehe, endelea…’akaambiwa

‘Kiukweli mama hakuamini, na sikutaka kabisa kumwambia mimi kilichotokea, alisikitika tu kuwa nimezaa bila kuwa na mume..nilikaa na mama yangu mpaka nikajifungua, nikamlea mtoto wangu huku nikiendelea kudai pesa mwanzoni alikuwa akinitumia,..’hapo akatulia kidogo

‘Lakini baadaye akawa hafanyi hivyo, na siku zikawa zinakwenda, nikaona maisha yanakuwa magumu, kuhangaika na mtoto mgongoni, maji, kulima, na biashara, nikaona ni bora nije nimuone...aliyenifanya hivi,  nijue ni nini hatima ya mtoto wangu, kwani yule mtu aliyekuwa akinisaidia alikuja kufariki.....’akasema huyo binti huku akimwangalia mume wangu kwa jicho baya, na mume wangu alikuwa kainama tu hainui kichwa.

‘Naona umeongea vya kutosha, ushahidi tulioutaka tumeupata je wakili mtetezi una swali dhidi ya huyo shahidi, ?’ akaulizwa.

********

‘Mteja wangu anakana yote aliyoyaongea huyo binti, je kama alifanyiwa hivyo, kwanini hakushitaki, hii inaonyesha kuwa huyo binti ana michezo yake ya namna hiyo, kuwarubuni wanaume ili aje kuwadai pesa, kwasababu mtu hivi hivi, asingeliweza kufanya jambo kubwa kama hilo, adai shilingi milioni kumi, mtoto wa kijijini...!’akasema wakili kwa mshangao.

‘Ushahidi ninao, kuna kanda alinipa huyo jamaa aliyenisaidia kama mnataka ninaweza kuwaonyesha..’akasema huyo binti, na wakili akanong’onezana na mteja wake, na wakili akasema;

‘Unasema ulipewa mimba, huyo mtoto yupo wapi?’ akaulizwa

‘Hilo lingelifuata baadaye, kwanza tulitaka kauli ya mlalamikiwa je, ni kweli hayo anayoyaongea huyo binti, kama si kweli, tutaonyesha hiyo kanda, inavyoosha anavyombaka huyu binti, ....ionyeshe tukio zima, ni ya aibu, lakini kwa ushaidi tutaionyesha,...kama anataka,..’akasema mwenyekiti.

‘Tunataka kumuona mtoto kwanza...’akasema wakili.

‘Haaah, ina maana bado tu mume wa familia hujaona umefanya kosa ukatubu, sawa, sisi tutafanya utakavyo, lakini hatutasita kuonyesha hiyo video, baada ya hapo…’akasema mama.

‘Sawa…’akasema wakili, mume wangu hakutaka hata kuinua uso wake, alikuwa kainama tu.

‘Sasa kabla ya kuonyeshwa huyo mtoto, kama anavyotaka …’samahani kidogo mzungumzaji, mimi nataka hili jambo tuliendeshe kisheria zaidi, kama mahakamani,..kuonyesha mtoto tutafanya, lakini mimi ningelipenda shahidi mmojawapo aje hapo..’akasema mwenyekiti

‘Sawa mwenyekiti,uonavyo maana mimi hapa akili haipo sawa..’nikasema

‘Mimi ningependa kumuita shahidi mtaalamu anayekubalika kisheria, yeye aje kutoa ushahidi wa kitaalamu zaidi, ili kumuonyesha mume wako kuwa sisi tunamfahamu zaidi anavyojifahamu yaye, na sisi sio lengo letu kuvunja ndoa yenu,lakini tunamfahamu kuwa hataweza kuishi na watu wastaarabu, kazoe vya kunyonga,,lakini siwezi kuhukumu hapa, hilo ni juu ya kikao baadae...’akasema mwenyekiti.

‘Shahidi huyo ni docta…’akasema mwenyekiti

Rafiki wa mume wangu alikuwa kama kashitukiziwa, na alionekana kubabaika, pale alipotajwa yeye kuwa anahitajika kutoa ushahidi.

**********

‘Ndugu docta samahani kidogo, nafahamu hukutarajia hili, lakini inabidi uwajibike, wewe ni docta, na huyo binti unamfahamu kwasababu alikuwa jirani yako, tunataka ukweli wako, utuambie je wakati unafika hapo nyumbani kwao kwa jirani yako, uliyaonaje maisha ya hapo ?’ akaulizwa

‘Mh,h, yalikuwa ya kawaida, tu, sikuona tofauti yoyote...’akasema

‘Huyo mlalamikiwa hakuwahi kukuambia lolote kuhusu huyo binti?’ akaulizwa

‘Mhh, kama lipi, ..ndio kuna ya hapa na pale, kuwa huyo binti ana adabu mchapakazi, na mambo kama hayo, baadaye akasema ametoroka, lakini sio mambo kama alivyoyaongea huyo binti..’akasema

‘Hukuweza kuhisi lolote katika tabia za rafiki yako dhidi ya huyo binti?’ akaulizwa

‘Kwakweli hapana, kama yalikuwepo basi hayo aliyoyaelezea huyo binti yalifanyika kwa siri sana, mimi sikuwahi kuyashuhudia...’akasema

‘Huyu binti alikuwa anatibiwa kwenye hospitali yako mara kwa mara, kama sikosei, je aliwahi kuja kwako ukampima na kumwambia ana mimba?’ akaulizwa

Wakili wa mtetezi akalipinga hilo swali, na kusema doctari analazimishwa kusema jambo, hakupewa nafasi ya kuelezea yeye mwenyewe...’akasema

‘Niambie docta huyo binti aliwahi kuja kwako kutibiwa kabla hajatoweka hapa Dar?’ akaulizwa

‘Ni kweli kwa mara ya mwisho kuja kwangu, alifika akisema anajisikia vibaya, na alitaka kupima malaria, na alivyojielezea, kama docta nikahisi mbali zaidi, nikamwambia inabidi tumpime mkojo, damu na choo, na hakupinga, tukachukua vipimo vyake, na majibu yake, yakaonyesha kuwa ni mja mzito...’akasema.

Hapo kila mtu akamgeukia mume wangu kuona atasema lolote, lakini alikuwa kainama chini tu

‘Ulimwambia moja kwa moja, kuwa ana mimba...?’ akaulizwa

‘Mimi naifahamu hiyo familia, na sikutaka kuingilia ndani sana, nilipogundua kuwa ana mimba, nilitaka kuongea na mama, yaani mke wa hiyo familia, lakini nikaona nitakuwa nimeliingilia hili jambo kwa ndani sana, nikaamua kumhoji huyo binti kwa kadri ya kujua kama anafahamu ni nani aliyempa hiyo mimba..’akasema docta

‘Alikuwa kachanganyikiwa kwa siku ile hakuweza kusema kitu, na aliniomba sana, nisimwambia yoyote, mpaka atakapoweza kuliweka sawa,...nilimuelewa, hata hivyo, nilitaka niongee na rafiki yangu kuhusu hilo, na shughuli zikawa nyingi, kiukweli sikuweza kuongea naye kwa muda wa karibu

‘Nilikuja kulikumbuka hilo baada ya siku kandaa mbele, nikamuuliza rafikii yangu kuhusu binti wao wa kazi, na rafiki yangu akaniambia kuwa huyo binti ni muhuni, katoroka, nikamuuliza kwanini katoroka yeye akasema, ni uhuni tu, hana lolote.
‘Hakuna lolote lilitokea ambalo limemfanya kutoroka, baada ya kupimwa, kuhusu afya yake, ?’ nikamuuliza

‘Achana naye, sitaki hata kumsikia, hata mke wangu hataki kusikia habari zake, usiongee lolote kumuhusu yeye kwa mke wangu,maana kakasirika sana, mtu anaondoka bila kuaga, kaniibia pesa zangu, tapeli mkubwa yule...’akaniambia

Mimi sikutaka kuliongea hilo la ujauzito, maana kama docta, unastahiki kuficha siri za mgonjwa,nikawa kimiya kuhusu hilo, lakini nilihisi kuna kitu zaidi ya hicho,lakini sikupenda kuyachimba sana mambo yao, kwani, nilikuwa na mambo yangu yanayonisumbua, na aliposema kuwa ni muhini, na kaondoka na hata mama wa familia hajataka kuliongelea hilo nikayaacha kama yalivyo..’akasema

‘Ina maana hukuongea na mke wa familia kabisa…?’ akaulizwa

‘Kuna kipindi nilitaka kuongea na mke wa hiyo familia, nikaona na yeye hanipokei kama tulivyokuwa awali, baadaye nikaona hilo jambo halina nguvu sana, kwasababu huyo binti keshaondoka, na wenyewe waliokuwa nao hawalalamiki au kuulizia ulizia, nikaona yamekwisha, huenda wenyewe wameyamaliza hayo mambo kifamilia, sikuwahi kuliulizia tena...’akasema

‘Mnaona, ...huyo ni docta, ndiye aliyethibitisha kuwa huyo binti ana mimba..sasa niambie bado mteja wako anapinga,kuwa huyo binti hakuwa na mimba yake, au anataka ushahidi gani mwingine?’ akaulizwa

‘Inawezekana alipewa mimba na mtu mwingine akaona sehemu ya kupatia pesa ni kwa mume wa familia, .ndio maana tunataka tumuone huyo mtoto wake.’akasema wakili.

‘Halafu mkisha muona mtathibitishaje kuwa ni kweli..?’ akaulizwa wakili

‘Kwanza tumuone, mteja wangu anasema akimuona atathibitisha na atakuwa tayari kusema lolote…’akaswa wakili

‘Sisi tutafanya kila kitu akitakacho,lakini na sisi hatutarudi nyuma, maana hatua iliyofikia, sio ya kuaminiana tena, unasikia..’akasema mwenyekiti

‘Mteja wangu anazidi kusisitiza kuwa anataka kumuona huyo mtoto, maana hakumbuki hayo aliyoongea huyo binti, hana uhakika na maneno yake..’akasema wakili na watu wakacheka kidogo

‘Hebu mleteni huyo mtoto...’akasema mwenyekiti, na mama yangu akatoka nje, na aliporudi akawa kambeba mtoto, kila mmoja akawa na shauku ya kumwangalia huyo mtoto.

NB: Njia za muongo ni nini..kila ushahidi utatoka lakini imani ya mtu, ni ngumu sana, hasa ikiwa na malengo fulani...


WAZO LA LEO: Usimtendee mtoto wa mwenzako ubaya, eti kwa vile sio mtoto wako, hiyo ni dhambi ambayo malipo yake ni hapa hapa duniani, ulivyomtenda mtoto wa mwenzako ujue na wewe watoto wako atakuja kutendewa hivyo hivyo. Ukitaka kufanya lolote baya kwa mtoto wa mwenzako kwanza jiulize na mimi nikitendewa hivyo, au mtoto wangu akitendewa hivyo nitajisikiaje. Isije kuwa mkuki ni kwa nguruwe tu.
Ni mimi: emu-three

No comments :