‘Mimi naomba aje Binti yangu wa kufikia, ..aje yeye kwanza maana
anahitajika kwenda kujiandaa kesho anasafiri....’akasema mama
Na mwenyeketi akageuka kumuangalia mwenyeji wa kikao ambaye ndiye
alikuwa muongeaji , na yeye ndiye alistahiki kuita mashahidi wake,…
‘Unajuaje kuwa huyo ni shahidi wake, usiharibu utaratibu,
au..’akasema mwenyekiti
‘Sawa ila…’nikasema nikiwa sijui lolote kuhusu huyo bint
‘Mimi nina uhakika ni shahidi wake..’akasema mama.
‘Haya, kama muhusika umemkubali kuwa ni mmoja wa shahidi zako,
aitwe, au unasemaje mwenyeji wa kikao..?’ mwenyekiti akauliza na mume wangu
akawa kabakia kimia, akiwa kashika kichwa…
Tuendelee na kisa chetu
**************
Kila mmoja alikuwa na hamu ya kumuona huyo shahidi, na wengine
walipumua, kwani hakuna aliyejua ni nani ataitwa kama shahidi, na hadi pale mlango
unagongwa, wengi bado walikuwa kwenye kutafakari, na kuwazia ni nani huyo binti
wa kufikia wa huyo mama, ambaye hajulikani, ni nani huyo binti ambaye anaweza
kutoa uahshidi na alifanyiwa nini...
Mlango ukafunguliwa, na akaingia binti, akiwa kavalia kiheshima na
mkononi alikuwa kashika bahasha, na , hakuwa na kitu kingine, kwanza kwa
aibu alipoingia pale mlangoni, hakujua afanye nini, alishikwa na butwaa hasa
alipoona watu wote wamegeuza kichwa kumuangalia yeye,...
‘Sogea huku mbele...’ilikuwa sauti ya mwenyekiti, ndiyo iliyompa
nguvu huyo binti, na taratibu akawa anasogea kuja upande ule watu walipokaa,
kulikuwa na kiti kipo wazi.
‘Wewe umefuata nini
huku...’
Sauti iliyowafanya watu wageuka, na kuangalia muongeaji ni nani,
Kumbe mume wangu wakati
watu wanahamasa ya kumuona huyo shahidi yeye bado alikuwa kainamisha kichwa, na
hata sauti ya mwenyekiti, ya kumkaribisha huyo shahidi ilikuwa bado haijamshtua
vyema, akawa kama katokea usingizi, akainua kichwa na kumuona huyo shahidi.
Hakuamini macho yake,, macho yakamtoka pima, mdomo ukabakia wazi,
na alichosema ndio hicho…
‘Wewe umfuata nini huku……….’.
Binti yule kusikia hivyo, akawa anaonyesha hali ya kuogopa, …akawa
kashikwa na butwaa, akawa sasa hajui afanye nini..
Kwa wakati huo watu wote sasa wamemtupia macho mume wangu, ambaye
kwa muda huo alikuwa kasimama nusu, na
mwenyekiti akawa anaangalia hili tukio kwa hamasa ya aina yeka, huku tabasamu
tele mdomoni, alikuwa akisubiria hiyo hali kwa hamu kubwa sana,..
Na mimi nilipogundua kuwa ni huyo binti, moyoni nikasema, ‘huyu ni
shahid wa kweli,..hata hivyo mimi sikuamini, maana sikuwa nimelifahamu hilo,
kwahiyo kwangu moyoni nilitamani kusikia atakachokizungumza huyo binti…nilimuangalia
yule binti wa watu kwa moyo wa huruma….
‘Haya huyo hapo shahidi wako wa kwaza, unataka uendelee naye
mwenyewe, au nishike usukani mimi, maana wewe ndiye mzungumzaji..?’ akauliza
mwenyekiti, lakini mimi niliishiwa nguvu, nilibakia kimia, nikiwa nimwangalia
yule binti, sijui ilikuwa ni huruma, hasira, au nini sikuweza kuongea,
kilichotokea ni mimi kuangusha chozi..chozi la nguvu, nikikumbuka huyo binti
alikuwa kwenye dhamana yangu, nikikumbuka kuwa huyo ni sawa na watoto wangu,
mtoto wa mwenzio ni sawa na mtoto wako, umtendeayo mtoto wako ukumbuke na wewe
utakuja kutendewa.
Mwenyekiti akaiona ile hali, akaamua kuendelea mwenyewe, akasema;
‘Kweli inauma, hii isikie kwa mwenzako tu, lakini ukitendewa wewe
utaona uchungu wake, na hasa utendewe na mtu unayemwamini, huwezi kuamini …huwezi
kuamini mpaka likufike, tujiulize hivi sisi hatuwezi kuwa na watoto…’akasema
mwenyekiti.
Hatukupenda aibu kam hizi ziwekwe hadharani hivi, ila naamini kuwa
nyie ni wanafamilia, na hili kwa hivi sasa libakia humu humu, hadi hapo,
tutakapoona sasa ni wakati muafaka wa jamii kufahamu…’akasema mwenyekiti.
‘Nawausia ndugu zanguni, mimi hapa ni mzazi, na ni mkubwa wenu
wote hapa, tuweni makini sana, ..tena
sana na wafanyakzi wenu wa ndani, msipende kuwaacha na waume zenu kwa muda
mrefu, au kuwapa kazi ambazo sio stahiki zao, kila kitu mfanyakazi wa ndani,
hata kutandika kitanda chenu..jamani, ..’akasema na watu kidogo wakacheka.
‘Binti wengine ni mtihani…yeye aje kukutandikia kitanda, afagie,
ainame wewe dume upo humo..mnawatia majaribu waume zenu..’hapo watu wakacheka,
‘Lakini sahamanini,..lakini ..hahaha, msicheke jamani, sio kwamba nasema
wanaume wote wana tabia hiyoo chafu, ..hapana, wapo wanaume wanajikubali,
wanahulka ya utu wema, ..muulizeni mke wangu...mimi aah, maana na umri huu nao…’akasema
mwenyekiti na watu wakacheka.
Ilibidi watu waachwe kwanza
watulie maana baada ya kicheko, ilifuatia watu kuteta, kwa kunong’ona na mnong’ono
wa wengi ni ngurumo, mwenyekiti akaacha hali hiyo ipite kidogo.
‘Huyu hapa mbele yenu ni shahidi,…kama mjumbe alivyotaka upatikane
ushahid wa madhambi yake,..hajataka kukubali mpaka ushahidi, haya ushahidi ndio
huo hapa, ambao, utadhihirisha urijali wa mume wa familia…’aliposema hivyo watu
wakacheka.
‘Tusicheke jamani, hebu muangalieni huyu binti, afadhali sasa
kakua, ..anaonekana mdada, kumbuka umri aliokuwa nao, kipindi hicho wanaishi nah
ii familia, ndio ni kweli umbo lake lilikuwa kubwa la kuvutia, lakini kumbuka
kiumri…na kumbuka huyu ni binti sawa na binti yako wa umri huo…napenda kurudia
sana haya maneno ili nyote muwe ni mashahid kuwa nililisema hili…’akasema
mwenyekiti.
‘Huyo ni sawa na binti yako mume wa familia, japokuwa binti zako
hawajafikia umri wake, lakini watafikia umri huo, huyo ni sawa na dada yako,
kama una madada…wewe ukaamua kula kuku na mayai yake..bado hutaki kukiri kume
umekosa, una makosa, utubu mbele ya jamii…haya ngoja tuanze na huyu shahidi
wetu...’akasema mwenyekiti.
‘Binti usiwe na hofu, wala usimuogope huyo mtu, kauli yake ya
kukutisha haina maana mbele ya jamii…kama kakosa kakosa, ..na wewe uliyekosewa
ni haki yako kusema ulichotendewa, sisi hapa tutakulinda, …’akasema mwenyekiti
‘Hebu tuambie jina lako,....?’ akaulizwa na akabakia kimia, halafu
akainama, halafu akaanza kulia
‘Binti, ..ule ushujaa umekwenda wapi, kwanini unalia, sikia binti usiogope,
hata tunachotafuta hapa ni haki yako,ukiogopa haki yako yote itapotea, na waliokuharibia
maisha yako wataendelea kuyafanya haya kwa watu wengine, ...’akasema mwenyekitu
‘Sisi hapa tunataka ukitoka hapa, uondoke na tumaini, na haya
yaliyotokea kwako, yakomeshwe, na ili
hili lifanikiwe tunatakiwa tuanzie huku majumbani kwetu, kama hivi,..likitokea jambo,
mkosaji aitwe, aadhibiwe, ikishindikana, apelekwe kunakostahiki,...’aksema
mwenyekiti.
‘Haya jitambulishe mpendwa,...’akasema mwenyekiti.
‘Mimi naitwa Tabia...’akasema kwa sauti ya kinyonge
‘Tabia,..tabia yako ni ya upole, au sio, mchapakazi, au sio,
...sasa nasikia kuna kitu kilitokea, wakati unafanya kazi kwenye nyumba moja,
kilipotokea ukakimbia jiji, ni kwanini ulikimbia jiji, wakati wenzako wanasema
tutabanana hapa hapa...?’ akamuuliza mwenyekiti.
‘Sikukimbia jiji, niliambiwa niondoke, la sivyo yatanikuta
makubwa, na...na...’akasita kuongea
‘Hebu sasa tuanze, maana nilikuwa nakuweka sawa, hebu niambie,
wewe ulikuwa ukifanya kazi wapi , na kwa nani…?’ akaulizwa
‘Mimi nilikuwa mfanyakazi wa ndani wa nyumba, ya ya...’akageuka
kuniangalia mimi
‘Ya mke na mume wa familia hao hapo au sio, hapa tunawatambua kama
mke na mume wa familia, ambayo ndio tunayoiongelea hapa hii leo ..ngoja
nimsaidie...’akasema mwenyekiti.
‘Ulifanya kwenye hiyo nyumba kwa muda gani?’ akaulizwa
‘Kwa zaidi ya mwaka mmoja...’akasema
‘Hebu niambie, wakati upo hapo, kulitokea nini, kilichokufanya
uondoke, uliamua kuacha kazi , kwa vile umepata mume huko kwenu au ilikuwaje?’
akauliza mwenyekiti.
‘Niliondoka baada ya kugundua kuwa nina uja uzito...’akasema na
watu wakaguna
‘Wakili wa mume wa familia, unalisikia hilo…sitaki uweke pingamizi
najua ndio zenu kuwalinda wahalifu..’akasema mwenyekiti alipoona huyo wakili
wakitaka kunyosha mkono.
‘Jamani msigune, ndio hali halisi, na tunapoongea hapa watu
wanafikiria tunamuonea mlalamikiwa, yeye anafikia kusema mimi nataka kuvunja
ndoa yake tu , kwa vile… ngojeni sasa myasikie na nyie kwa masikio yenu…’akasema
mweneykiti.
‘Haya tuambie, unasema ulipata uja uzito, kumbe wewe badala ya
kufanya kazi za ndani ulikuwa ukifanya uhuni na wavulana wa mitaani eehe...’ aksema
mwenyekiti kwa sauti ya nzito, kama kumtisha huyo binti.
‘Hapana mimi sio muhuni, sijawahi kufanya uhuni na mvulana yoyote,
tangia nifike hapa mjini , kazi yangu ilikuwa …...’akasema na hapo akaanza
kulia
‘Unasema hujawahi kufanya uhuni na mvulana yoyote, sasa hiyo mimba
uliipata kutoka mbinguni, hebu sema ukweli, ...’akasema mwenyekiti
‘Mimi nilikuwa simjui mwanaume yoyote, nilikuwa nafanya kazi zangu
na sikupenda haya yanitokee, ..niliapa kwa mama yangu kuwa sitakuwa muhuni, na
nilipochukuliwa na ....wazazi wangu hawo, nilijua kuwa nimefika mahali
salama....sikutarajia kuwa hayo yangelitokea,....’akawa analia
‘Usilie, …ongea yaliyokukuta sasa, ilikuwaje tuanataka kusikia
kuhusu maisha yako…wapi ulipotokea wazazi wako, ulifikaje hapa kwa hiyo familia
ili muone ni dhambi gani huyo mtu aliibeba, na kama bado anakataa kutubu basi
huyu sio mwanadamu..hebu tuambie kisa cha maisha yako;
***********
Mama yangu ni mjane, baada ya kufariki baba, kwa ghfla,sisi
tulibakia na mama kwenye kibanda kibovu tu,tukiwa watoto watano, na alituacha
tukiwa masikini sana, mama akawa anaangaika sana kututafutia riziki, na sisi
japokuwa tulikuwa wadogo, lakini tulijijua kuwa hatuna mtu atakayetusaidia,
kwani baada ya msiba, vitu vilivyokuwepo vichache viligawanywa, na wanandugu
wakachukua kile walichoona kinawafaa, tukabakia mikono mitupu.
Mimi nilikuwa mkubwa ukilinganisha na wadogo zangu,kwani mimi
nilikuwa mtoto wa kwanza nna kwa vile ni mwanamke , nilionekana mkubwa kidogo,
basi ikawa kazi kubwa ni kumsaidia, kila tukitoka shule tunajipanga, huyu
afanye hiki na yule afanye kile, ili tu tuweze kumpunmguzia mama kazi za
nyumbani..
‘Kazi kubwa ya mama ilikuwa kutengeneza vyungu, kwa kutumia udongo
wa mfinyazi, alikuwa akienda huko mlimani kuutafuta udongo wa mfinyanzi, na
akileta anatengeneza vyungu vya kupikia, …
‘Kiukweli mama alikuwa mtaalamu sana wa kazi hiyo, lakini hata
hivyo kazi hiyo ilikuwa hailipi, kwani akijitahidi sana anakuwa katengeneza
vyungu, hata kumi havifiki, na bei za kijijini ni ndogo, ni kazi nzito, lakini
tungefanyeje...kuna kipindi tunakuwa hatuna hata senti moja, nyumbani, inabidi
mama aende kwa majirani kuomba hata kazi ya kulima, au kuosha vyombo ili
angalau tupate pesa ya kula, ndio maisha niliyokulia hayo.
Wingi wetu, ulikuwa mzigo sana kwa mama, na ukumbuke baba
alifariki akatuacha tukiwa tunasoma shule ya msingi, mimi nilikuwa darasa la
saba, na wenzangu, la sita, la tano la nne, na la tatu, na wamiwsho alikuwa
darasa la pili,tulipishana mwaka mmoja mmoja wa shule, japo kimuri tulipishana
kidogo. Ilibidi tusome kwa shida, hata nguo za shule, zilichakaa, ikawa
tunaweka viraka, na wengi walianza hata kututania, kuwa sisi ni
viraka.....’akasema
Darasa la saba nilimaliza kwa shida sana, kwa vile mimi ndiye
mkubwa, basi ilikuwa kama mimi ndiye msaidizi mkubwa wa mama, nilitakiwa
kuamuka asubuhi sana, kumsaidia mama, ili aweze kukusanya, vile vyungu
vilivyokuwa tayari, maana tulikuwa tukivichoma usiku,na asubuhi, tunavitoa ili
vipoe, vingine vinavunjika, ndio hivyo tena...’akatulia.
Nilipomaliza darasa la saba tu, watu wengi wakaja kunitaka, niende
nikafanye kazi kwao, kama mfanyakazi wa ndani, kutokana na jinsi walivyoniona,
kuwa ni mchapakazi, sikupena kabisa niondoke nimuache mama yangu, lakini pia
tulihitajia pesa kwa ajili ya kuwasomesha wadogo zangu, basi mtihani ukaanzia
hapo, niende kwa nani..
Kabla hatujaamua ndio siku moja likaja gari, na wakaja hawa wazazi
wangu , ambao mama alikubali niondoke nao,mama alisema anawafahamu vyema, na
aliona kuwa watatusaidia kujikwamua kimaisha, angalau wadogo zangu waweze
kusoma na kufika mbali sio kama mimi niliyeishia darasa la saba ...’akatulia.
‘Wageni hawo, waliongea na mama wakakubaliana, na kesho yake
nikachukuliwa na kuja huku Dar, na kama ujuavyo, kila mmoja kule kijijini
anatamani sana kuja huku, kwahiyo hata mimi nilifurahi sana, na nilishukuru
kuwa nimapata kazi kwa watu wenye uwezo. Nikawaga wanafamilia, yaani mama na
wadogo zangu. Mama alizidi kuniusia kuwa nifanye kazi kwa bidii nisije
nikandanganyika na kuingiwa na tamaa, na kujiunga na wahuni, mimi nikamuahidi mama
sitafanya lolote baya.
Mshahara wangu wa kwanza wote niliutuma kijiji kwa mama, na mama
yangu mpya, yaani bosi wangu, alikuwa akinijali sana, alinisaidia mambo mengi,
na kuanza kunisomesha msomo ya jioni, nikaanza kuelewa maisha na jinsi gani ya
kuishi kisasa, sio kama nilivyokuwa huko kijijini, na alikuwa akinisaidia
kunipa peza za kuwasomesha wadogo zangu kila nilipomweleza matatizo ya nyumbani
kwetu...’akatulia kidogo.
Kwakweli mimi darasani sielewi, ninachojua ni kufanya kazi,
nikamwambia mama asipoteze pesa zake bure, kunisomesha, kwania yeye alitaka kunisomesha sekondari,
kiujumla kichwa changu ni kizito sana darasani, akaniuliza kitu gani rahisi
ninaweza kukisomea au kukifanya, nikamwambai ufundi, na nikachagua ufundi wa
kushona, na kweli huo nikauwezea sana...akaninunulia cherehani, nikawa nashona
nguo hapo nyumbani, na alikuwa na mpango wa kunifungulia duka langu...lakini oh
bahati haikuwa yangu....’akaanza kulia.
‘Aaah, tulishakuambia, ujikaze, mambo ya kulia hapa
hatuyataki...yote ni mitihani ya maisha, unachotakiwa ni kumkabidhi mungu,
..usilie mwanangu ongea...’mama yangu akamwambia na kumpa moyo.
‘Ndoto zangu za kuwa mtu maarufu zikazimwa kama taa ya
kibatili,maana nilikuwa na ndoto za kuwa mwanamitindo, nishone nguo za kila
aina,lakini ndio hivyo tena yakanikuta makubwa ambayo sikuyatarajia...kwasababu
ya ...ya...’akasita kusema huku akigeuka kumwangalia mume wangu ambaye kwa muda
huo alikuwa kainamisha kichwa chini.
‘Hebu tuambie ndoto yako hiyo ilizimikaje, kwa maana ulikuwa
unaishi na watu wenye uwezo wangeliweza kukusaidia sana tu, na nakumbuka
mwanzoni nilipowatembelea ulionekana mwenye furaha,ukasema kuwa umewapata
wazazi wazuri wanaokujali...?’ mwenyekiti akauliza
‘Ndio mwanzoni mambo yalikuwa mazuri sana, sikuwa na shida, na
niliwaona wazazi wangu ninaoishi nao ni kama baba na mama yangu, na kwa ujumla
wao walikuwa wachapakazi kweli, hawakutaka mchezo, na wakanikuta na mimi ni
mchapakazi kama wao, japokuwa ni za nyumbani, kwahiyo kila mmoja alikuwa
akiamuka asubuhi anakimbilia kwenye kazi yake…
‘Na mimi nikawa naendana nao,.. hakuna muda wa kuongea, na mimi
nilikuwa nafanya kazi yangu vyema, bila ya kusimamiwa,...ghafla nikahisi
mabadiliko, maabdiliko hayo niliyaona kwa baba, akawa analewa sana....’akasita
kidogo pale mume wangua lipoinua uso kumwangalia.
‘Usimwangalie, wewe ongea ,hana lolote kwa sasa, hawezi kukufanya
lolote....’akamwambia mama, ambaye alionekana kama muongozaji wake.
‘Kabla hata ya hapo, nilipokuwa nimekaa hapo kwa mwezi mmoja tu,
nilikuwa nimeshabadilika sana, mwili wangu ukawa mkubwa, nikawa naonekana
msichana,mkubwa kuliko umri wangu, mmmh....’akatulia na mwenyekiti akasema;
‘Msichana mrembo...eeh’akamalizia mwenyekiti, na watu wakacheka
kidogo
‘Ndio ndivyo walivyokuwa wakiniambia watu, lakini mimi sikujali,
maana nilikuwa nafahamu ni kitu gani kimenileta hapa Dar, nikawa nawajibika
ipasavyo, sikuwa na muda na watu wa mitaani hasa wanaume…, ambao walikuwa
wakinisumbua kila nilipokuwa nikitoka, kwenda dukani au sokoni, ...huko nje
niliweza kabisa kuwashinda, sikuwapa muda wa kuongea nami, lakini tatizo likawa
ndani,....’akatulia kidogo.
‘Ulikuwa unanyanyaswa, au hayo mabadiliko yalikuwa yapi, mpaka
nyumbani kuwe ni mtihani kwako?’ akauliza mwenyekiti.
‘Baba….a-a-ah…, nilimuona baba akinitizama kwa macho
yaliyonitisha..sivyo kama ilivyokuwa mwanzoni’akasema
‘Kwa vipi hebu fafanua..na ulihisje hivyo, kwani mama yeye alikuwa
hakuangalii, kama anavyofanya baba ?’ akaulizwa na mwenyekiti.
‘Ni kama ..ya tamaa, maana anakutizama mpaka unaona aibu, kuna
siku nilimuuliza mama mbona baba ananitizama hivyo,mama akasema hajawahi
kumuona baba akifanya hivyo, akaniambia nifanye kazi zangu, nisiwe namwangalia
baba, kwani utajuaje kuwa mtu anakutizama, kama wewe hujamuangalia, nikaona
aibu kwanini nilimwambia mama hivyo
‘Siku moja nikashindwa kuvumilia, nilipomuona baba ananitizama
nikaona ngoja nimuulize kama baba yangu, yeye, akasema siku hizi nimekuwa
mrembo sana...’akasema.
‘Unaona eeh…haya endelea…’akasema mwenyekiti
‘Kauli hiyo ikanikwanza, nikaona nimwambia mama tena, kesho yake,
nilimuona baba kanikasirikia, na hakutaka hata kuitikia salamu yangu, nikahisi
huenda waliongea na mama kuhusu hayo niliyomwambia, na hali ikatulia kidogo,
lakini baadaye, nikaona ile hali inarudi tena, baba akawa ananifuata hata
sehemu ninyofanya kazi na kuanza kunitania, mimi kwa vile niliona ni baba
yangu, nafurahi,naongea naye tu, ila kwa tahadhari, kwani mama alishaniambia
kuwa nisipoteze muda kwa kuongea ongea...’akasema.
`Ikazidi, kwani nilishawahi kumfuma baba
akinichungulia,....’akasema na watu wakaguna
‘Akikuchungulia kwa vipi?’ akaulizwa
‘Kama nimetoka kuoga, nikiingia chumbani kwangu,kama mama hayupo,
baba anaweza kuingia chumbani kwangu ghafla na kujifanya kauliza kitu, na
wakati huo huenda nilikuwa nipo uchi, kwani .....’akatulia
‘Tunaelewa endelea..’akasema mama.
‘Kuna kipindi alikuwa akija usiku nimelala, na kuanza kunifunua
nguo...nikishituka, anasema alikuwa akinifunika vizuri,....’akasema
‘Oh, muongo mkubwa wewe, unawadanganya watu , mimi niliwahi
kukufanyia hivyo, nitakukomesha kwa uwongo wako...’mume wangu akasema kwa
hasira na wakili wake akamtuliza.
‘Je alikuwa akifanya hivyo, akiwa amelewa?’ akaulizwa
‘Hapana hiyo ilikuwa mwanzoni kabla hajaanza kulewa, na alipooanza
kulewa, ndio akaanza visa vyake...’akasema.
‘Haya tuambie hivyo visa vyake vilikuwaje...’ akasema mwenyekiti
‘Alianza kunitongoza...’akasema na watu wakaguna
‘Hahaha, anamtongoza binti yake,…jamani…’akasema mama
‘Eehe, alikuambiaje, na ulijuaje kuwa anakutongoza, na wewe
ulimjibuje vipi?’akaulizwa
‘Aliniambia kuwa ananipenda sana, na anataka...anataka tuwe
wapenzi wa siri...’akatulia kidogo.
‘Akasema atanifundisha jinsi ya kupata raha ya
mapenzi,...’akatulia kiogo.
‘Mungu wangu…’mimi nikasema hivyo nitaka kumwambia huyo binti
asiendelee maana nilikuwa naumia ndani kwa ndani, kila hatu ilikuwa ni mateso
kwangu.
‘Kwa kipindi kile mimi sikuwa namuelewa ana maana gani, ila
akilini mwangu ikanituma kuwa huyu anataka nifanye naye kitendo kibaya, ..’.akasema.
Basi aliponitongoza tena, mimi nikamwambia;.
‘Wewe nakuheshimu kama baba yangu, kwanini unaniambia mambo kama
hayo, yeye akasema hajanizaa, na mimi ninaweza kuwa hata mke wake, na yupo
tayari kuninunulia chochote hata kunijengea nyumba ya kifahari huko
kijijini,...’akasema
‘Mwongo sana huyo binti msimsikilize ni mfitinashaji huyo ndio
maana nilimfukuza..’akasema mume wangu lakini hakuna aliyemsikiliza
‘Wewe endelea, cahana na huyo…’akasema mama
‘Mimi nikamwambia mimi nawaheshimu wao kama wazazi wangu siwezi
kufanya jambo kama hilo, na mama yangu alinikataza kabisa kufanya huo uchafu,
kwani mimi bado mdogo, na natakiwa kufanya hayo mambo nikiolewa...’akasema
‘Ulimwambia hivyo huyo baba yako, na ulijuaje kuwa anataka mfanye
mambo machafu, ?’ akaulizwa
‘Ndio nilimwambia hivyo, yeye aliniambia kuwa anataka tufanye
mapenzi, ...’akasema
‘Wewe mapenzi uliyajuaje..?’ akaulizwa
‘Mimi nilifahamu mapenzi ni kitu kichafu, lakini ni kizuri kwa
wandoa, ..shuleni tuliwahi kufundishwa vitu kama hivyo…kwahiyo mimi hapo
nilifahamu kuwa ananitaka kwa mambo machafu , mama alishaniambia hayo kuwa
mwanaume akisema anataka kufanya mapenzi na wewe ujue anataka kufanya mambo
mabaya ya kukuharibu usichana wako, ....’akasema.
‘Baba hakuchoka kunibembeleza na aliniambia nikumwambia mama
hayo anayoniomba, atahakikisha narudi kijijini na kuwa masikini wa
kutupwa,...nikaaogopa sana, kwani kule kijijini kweli baba yangu huyo
wanamuogopa sana....’akasema
‘Kwanini wanamuogopa?’ akaulizwa
‘Wanasema baba huyu ni tajiri na anaweza kukufanya lolote
asifungwe, kwa vile ana kampuni yake kubwa, na anajuana sana na polisi...na pia
anajuana sana na yule mwanasheria aliyekufa, ...’akasema
‘Kwanini huyo mwanasheria aliogopewa…samahani kidogo japokuwa
tunamteta marehemu lakini hapo kuna ushahid pia tunauhitajia,…’akasema
mwenyekiti
‘Huyo mwanasheria aliyekufa naye alikuwa akiogopewa sana, kuliko
hata baba, kwasababu wanasema anafahamu uchawi wa kisasa, anaweza
akakuangalia hivi akakuambia yoye unayofikiria kichwani mwako,anaweza kujua
kitu gani ulikuwa ukifanya nyumbani kwako, wanamsema kwa mambo mengi tu,...anaogopewa
sana kule kijijini, na huyo alikuwa rafiki mkubwa wa baba yangu huyu
...’akasema
‘Kwahiyo alipokutongoza alikuambia kuwa usipomkubalia atakuloga au
atakufanya nini?’ akaulizwa
‘Hakusema kuwa ataniloga,yeye alisema atahakikisha mimi na
familia yangu tunasota, tutakikimbia kijiji,na kuwa omba omba...na mama yangu
atakufa kwa kihoro...mimi niliogopa sana alipofikia kusema mama yangu atakufa
kwa kihoro..hata hivyo sikumkubalia alivyotaka yeye...’akasema
‘Siku moja alikuja nyumbani, huwa ana kawaida ya kuja akifahamu
kuwa mama hayupo, na ananiambia niache kazi zote tongee, na siku hiyo akanituma
pombe, akanywa na kunilazimisha mimi ninywe, nilikataa kabisa,...kuna muda
akanituma maji ya kunywa nikaenda kumletea, akanywa, na mimi nikaondoka kufanya
kazi zangu , baadaye akaniita, nikashangaa ananimiminia maji ya kunywa na
kuniambia ninywe, kweli nilikuwa na kiu, lakini niliingiwa na wasiwasi nikijua
huenda kaweka kitu.
Akanishika kwa nguvu mpaka nikayanywa yale maji..yalikuwa hayana
ladha nzuri, sijui ilikuwaje, maana niliona macho yote mazito, ...nikawa sina
nguvu tena, akanibeba, hadi chumba cha akiba, akanilaza kitandani...hapo
akaanza kulia ...’ hapo hakuweza kuendelea akaangua kilio..
Kulitulia kwa muda..mimi niligeuka kumuangalia mume wangu…unajua
chuki, uso uliomwangalia ulikuwa sio wangu…lakini niliwastahi wazazi wangu
nikabakia kutikisa kichwa tu
‘Niliumia sana siku hiyo, aliniumiza..alinishika kwa nguvu, na
sikuwa an nguvu za kujitetea mwili wangu wote ulikuwa umelegea, lakini niliweka
kuhangaika, na.....akaniumiza....sikuamini yaani baba yangu niliyemuamini kama
baba yangu mzazi, alifikia hatua ya kunifanyia hivyo,mungu ndiye anayejua, ...’akatulia
akilia
‘Hapo nikamkumbuka mama alivyoniusia, nikajitahidi kutimiza
wajibu, nikawa namuogopa mungu, lakini baba akayaharibu yote hayo,..ningefanya
nini hapo jamani, ..ina maana sisi kwa vile ni masikini wetu ndio watufanyie
wanavyotaka, niliumia sana siku hiyo...nililia sana mpaka macho yakavimba…’akawa
anaongea huku akiwa analia.
‘Endelea, usilie, ongea ili watu wasikie, unyama wa mtu anayejiona
mwema usoni kwa watu kumbe kavaa ngozi ya kondoo..’akasema mama.
‘Alipomaliza shughuli zake, akaondoka, huku akisema nikimwambia
mtu ataniua, atamuua na mama yangu...sikuweza kumwambia mama, wiki nzima nikawa
kama mgonjwa, nikawa nalia,hadi mama akaja kunifuma nikilia, sikuweza
kumwambia, kwa vile niliogopa kuvunja ndoa ya watu, na pia kwa vile baba
alinitishia kuwa nikimwambia mama atamuua mama yangu. Nilimwambia kuwa
nimemkumbuka marehemu baba yangu alivyokuwa akinipenda.
‘Tatizo mama kipindi hicho alikuwa na kazi nyingi, na kila
unachomuambia anakuamini, hakupenda kunidadisi sana, akanipa pole, na
kunishauri kuwa nisikumbuke sana kwani hayo ni mapenzi ya mungu, halafu
akaniuliza kuwa baba ananisumbau tena,...kwa kuogopa nikamwambia hanisumbui...
‘Ikapita hiyo siku, na wiki nikijua hilo limekwisha, siku moja
akiwa amelewa akanijia chumbani, ilikuwa usiku akanishika kwa nguvu,....na
karibu aniue, alinikaba nikafikiria kuwa huenda alikuwa anataka kuniua,
nilipigana naye sana, lakini akanizidi nguvu, baadaye akaanza kunizalilisha
tena, ...’akasema
‘Kwahiyo kumbe ilikuja kwua ni tabia yake…?’ akauliza mama
‘Ndio…yaani karibu nimtapikie akwa jinsi nilivyo kuwa najisikia,
harufu ya pombe na matendo yake, ...nilijua nafanyia yote hayo kwa vile mimi ni
masikini, nitasema nini nieleweke kwa jamii, akafanya alichotaka
akaondoka...kesho yake nikataka kumwambia mama, lakini ikashindikana, kila
nilipotaka kumwambia mama, baba anakuwa karibu, na siku ikapita., Siku ikipita
unajikuta umesahahu, ukikumbuka inaishia kulia.
Basi nikaona niache tu iwe kama iwavyo, akawa akifika, usiku
anajifanya halali na mama, anakuja kulala chumba cha akiba, akiona kupo kimiya
anakuja kwangu..nikawa najitahidi hivyo hivyo, ila sikuwa na raha, nikawa nalia
sana, na kuanza kukonda, na baadaye ndio nikagundua kuwa nina miimba..sikujua
kuwa ni mimba, siku hiyo nilikwenda kupima malaria, nilikuwa najisikia vibaya
sana, mama akaniambia nikapime malaria, ndio docta akaniambia nina mimba...
Nilipotoka pale nikapitia duka la dawa za mifugo nikanunua sumu ya
kuulia wadudu, baada ya kuuliza na kuambiwa hiyo dawa binadamu akinywa anakufa
mara moja,..akilini , nilishazamiria kujiua tu, sikujiona binadamu mwenye
thamani kwenye hii dunia, kwani sikuweza kuvumilia tena,nilishaona kuwa
nimefanya makosa makubwa, kwanini sikumwambia mama yangu huyo wa kufikia
mapema...nilijiona mzembe, ...mkosaji asiye na maana .
Akilini mwangu, nilijua hata nikimwambia mama kwa sasa hataweza
kuniamini tena, ataona mimi nilikubali kirahisi , na atanichukulia mimi ni
mzinzi, Malaya. Na pia sitaweza kumwambia mama, yangu mzazi, nitamuumiza sana,
mama ambaye siku zote alikuwa akinionya,nisije kujiingiza kwenye uchafu wa
zinaa, je nitmwambieje mama yangu, nikaona bora nikajiue tu....niondoke
kwenye hii dunia, wabakie wenye pesa zao.
Nilipofika nyumbani nikaikoroga ile sumu kwenye kikombe cha
plastiki, ilikuwa haiwezi kuonekana maji hayakubadilika rangi, nikaweka kwenye
meza karibu na kitanda changu, nikachukua karatasi na kuandika ujumbe
nikielezea kila kitu ilivyotokea...
Nilipomaliza hiyo kazi ya kuandika,... sikutaka nife kabla
sijatimiza wajibu wangu, kwahiyo nikahakikisha nimefanya kazi zangu zote za
nyumbani,...nilipomaliza nikaoga, nikamuomba mungu, nikaingia chumbani
kwangu,nikaichukua kile kikombe, ambacho kilikuwa na maji niliyochanganya
na ile sumu ....
Wazo likanijia, kuwa nisifie chumbani kwangu, nikaona sehemu nzuri
ya kufia ni kule kule nilipozalilishwa , nikavua nguo zangu za kawaida,
nikachukua gauni kubwa jeupe, refu, lenye mikono mirefu, nikalivaa, halafu moja
kwa moja nikaenda chumba ambacho baba alianzia kunizalilisha
‘Pale nikamuomba mungu tena, na kulia, nikisononeka, na kila
uchungu ulivyonizidi, ndivyo tamaa ya kujimaliza ilivyozidi kunijia, kuna muda
nilikuwa nasita kufanya hivyo, nikimkumbuka mama yangu, lakini baadaye nikaona
jambo jema, ni kuondoka hapa duniani, bila kupoteza muda nikanywa yale maji
niliyokuwa nimechanganya na sumu...
NB: Tuendelee na huyo binti, au ..tukutane sehemu ijayo.
WAZO LA SIKU: Tuweni
na ubinadamu kwa wafanyakazi wetu wa ndani, visa vingi vinaelezewa jinsi gani
wafanyakazi hawa majumbani wanavyonyanyaswa au kuzalilishwa, lakini wengi
wanaofanyiwa hivyo wanashindwa kuongea ukweli kwa wazazi wao kwa kuogopa , na
wengi wanaofanyiwa hivyo ni watoto wa kike,wasichana….je wewe uliwahi kumuuliza
mfanyakazi wako wa ndani kuhusu shida zake, je yupo salama na baba….tuwaulize
kama mabinti zetu wa kuzaa.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment