Baada ya mapumziko mwenyekiti alirudi, na kutuambia tuingie
ndani, ili yuendelee na kikao chetu, na wakati huo mume wangu alikuwa keshaondoka
na haijulikani kama atarudi tena,au ndio keshakimbia kikao, nikataka kwenda
kutoa taarifa kwa mwenyekiti, lakini kabla sijainuka kwenye kiti , mara mume
wangu akaingia akiongozana, na jamaa mmoja na moja kwa moja wote wawili
wakaenda kuonana na mwenyekiti.
‘Mwenyekiti nimeona nimchukue wakili wangu, ili aweze kunijibia
maswali, kwani naona nimelemewa, ...’akamwambia mwenyekiti.
‘Kwani tulikubaliana vipi, na kwanini umtafute wakili, kuna kosa
gani kubwa umeliona ambalo linahitajia wakili?’ akamuuliza mwenyekiti.
‘Lakini nyie mna mawakili wenu, ..mbona mimi sijalalamika
hilo..’akasema
‘Hawa wapo kwasababu ni watendaji wetu wa kila siku wakili wangu
ni mtendaji wangu wa kila siku, huyo wakili wenu, ni mtendaji wenu, anahitajika
kutoa ushahidi wa huo mkataba,..haya ni mambo yetu hayahitaji mtu mwingine
ambaye sie mtendaji wetu wa kila siku, na kama umeamua kuleta wakili, basi
tulipeke hilo swala mahakamani...’akasema mwenyekiti.
‘Hapana nia ya kumleta huyu wakili ni kunisaidia tu, kwa saabbu
kuna mambo mengine yanahitajia sheria, na natambua kabisa tukimaliza hapa,
watakuja maaskari, kama sio mimi ni kwa ajili ya mdogo wangu, ndio maana
nimeamua kumleta huyu wakili...’akasema
‘Ili afanye nini....?’ akauliza mwenyekiti.
‘Ili aone kama kweli ninatendewa haki,..’akasema
************
Ni katika kipindi kingine baada ya mapumziko, wajumbe
wakaingia ukumbini, na mwenyekiti kama kawaida yake alishafika kwenye kiti
chake, na walikuwa wakiteta,na mume wangu, baadae mwenyekiti akasema
'Kuna mjumbe kaongezeka, ...na taarifa hii nimepewa hapa na
mjumbe mwenzenu, mume wa mtayarishaji wa hiki kikao;
'Huyo mnayemuona kakaa karibu na mawakili wengine ni wakili wa
kujitegemea, yeye ni wakili anayemuwakilisha mume wa binti yangu...siwezi
kulipinga hilo, maana huenda mwenzetu ana dhamira yake...' akasema mwenyekiti
'Lakini ndugu zanguni, je kulikuwa na haja gani ya kumleta wakili
mwingine,...kulikuwa na haja gani ya kujihami kiasi hicho, sisi kama kikao,
..na ilivyo mujibu wa vikao kama hivi vya kifamilia, ni kutatua matatizo yale
yaliyopo ndani ya kifamilia...'akasema mwenyekiti.
'Sasa ikizidi, au tatizo likivuka mpaka, ndio tunaweza kusema sasa
tunakwenda mbele ya sheria, lakini kwa historia ya vikao vyetu haijawahi
kutokea hivyo, labda hiki ndio kiwe cha kwanza..'akasema mwenyekiti.
'Karibu sana wakili, na huenda umeshaambiwa ni kitu gani
kinachoendelea, sisi hatuna pingamizi, nia na lengo letu ni kuweka haya mambo
sawa sawa...'akasema mwenyekiti na kunigeukia mimi
'Nikuulize wewe mume mtu, je upo hiari, na ujio wa wakili huyu ,
maana siwaelezi, kuwa na mawakili wakili, kila mtu na wake kwa jambo hilo
hilo,...'akasema mwenyekiti akiniangalia mimi
‘Kama kaamua hivyo, ni vyema tu, ila nilitaka kumwambia huyo
wakili atambue kuwepo kwa mkataba huo halali, na ule aliowahi kuonyeshwa awali
autambue kuwa ni batili,..sasa kama yeye kaja na ajenda ya kuusimamia mkataba
huo, wa awali ajue kuwa atahitajika kuwasiliana na mahakama au na watu
wanaodhamini mikataba hiyo,..’nikasema
Wakili huo akanyosha mkono na mwenyekiti akageuka kutuangalia sisi
wajumbe na kusema
'Hili jambo litatupotezea muda, lakini sawa, hebu tuambie
muheshimiwa wakili,...'
‘Mimi nimeletwa hapa na huyu mteja wangu, alishanisimulai yote
siku nyingi, na nilichukua nafasi ya marehemu, wakili wake wa awali,.., kwahiyo
yote nayafahamu, sio mtu mgeni kwa hili linaloendelea hapa...’akasema.
‘Kwahiyo wewe unafahamu undani wa kila jambo la kifamilie, ikiwemo
mikataba ya kifamilia, na kikazo..ya kuwa wawili hawa waliamua kutengeneza
mkataba, ambao umekuwa ukiongoza familia na taratibu zao za kila siku ikiwemo
makampuni yake?’ akaulizwa
‘Nafahamu,..’akajibu
‘Kuna uhakika kuwa mkataba huo wa awali uligushiwa, na mteja wako,
akishirikiana na marehemu, kwa matilai fulani, je unalifahamu hilo?’
akaulizwa
‘Hilo ndilo limanifanya nifike hapa, kwani mteja wangu anashukiwa
kufanya jambo ambalo, halitambui,...'akasema
'Kwa vipi asilifahamu maana yeye ndiye muhusika wa kuandaa
mikataba yote miwili, wa awali ambo ndio sahihi, na huo mwingine wa
kugushiwa...?' akaulizwa
'Kwa maelezo ya mteja wangu, yeye alikuwa akimtegemea wakili wake,
na alifanya hivyo ili kupunguza mambo mengi aliyokuwa nayo, kwahiyo akampa na
jukumu hilo la mkataba, kwahiyo likitokea jambo la kisheria kuhusiana na
mkataba, yeye alikuwa akimuhusisha wakili wake huyo...'akasema wakili
'Ok...endelea...'akasema mwenyekiti.
'Kwahiyo alipopatwa na ajali, mambo yote ya kisheria yalikuwa
mkononi kwa wakili wake huyo,na bahati mabaya akafariki,ikabidi sasa achukue
ule mkataba aliomkabidhi wakili wake wa zamani awe anausimamia yeye kwa muda,
huku akitafuta wakili mwingine ambaye likuja kunipata mimi.
'Kifupi yeye, hadi leo, ambao mumekuja kugundua kuwa mkataba huo
una matatizo, alijua kabisa kwua mkataba ni ule ule, na mkumbuke jamani, kuwa
mteja wangu alipatwa na ajali na kipindi kingi alikuwa kwenye matibabu, na huo
mkataba, kama ulibadilishwa basi ulibadilishwa kipindi hicho akiwa
mgonjwa,...’akasema wakili.
‘Una uhakika na hilo muheshimiwa wakili?’ akauliza mwenyekiti
‘Kwa taaifa za kutoka kwa mteja, wangu ndio nina
uhakika..muheshimiwa mwenyekiti.’akasema huyo wakili.
Mwenyekiti akachukua simu na kumpigia msajili wa mikataba,na
akaweka sauti a kusikika watu wote, na kumuuliza msajili,
'Samahani muheshimiwa kama nilivyokuomba awali, tutakwua
tukikusumbua mara kwa mara, sasa kumetokea tatizo, kidogo, tulitaka kufahamu
tu, ni lini tatizo la mapungufu ya kiofisi, lilitokea, nikiwa na maana ni lini
iliogundulikana kuwa mkataba wa kifamilia wa hii familia ulibadilishwa
Huyo msajili akataja tarehe , na ikaonekana kuwa tarehe hiyo ni ya
kipindi cha nyuma hata kabla mume wangu hajapata ajali,...
‘Umesikia tarehe iliyotajwa hapo, ilikuwa hata kabla mteja wako
hajapatwa na hiyo ajali, mkataba huo uligundulikana kuwa umebadilishwa,je
unawezaje kusema hiyo michakato ilifanyika akiwa yeye hajui! Kiukweli yeye
alikuwa na ufahamu wake, na alishiriki, na alifahamu ni nini kinechoendelea na
ndio maana ugonjwa ukaendelezwa mbele au sio ...’akasema mwenyekiti.
‘Mkataba huo uligundulikana kuwa umebadilishwa, kipindi mteja wangu
akiwa hajapata ajali, inawezekana ikawa hivyo, hatukatai, lakini yeye alikuwa
hajui kuwa mabadiliko hayo yameshafanyika, hana ufahamu huo kabisa,,...'akasema.
na kabla hajatulia akaongezea kusema;
'Na kama waligundua hivyo, hawakumfahamisha mteja wangu,
walimfahamisha wakili wake, ambaye na yeye kipindi hicho pengine, nasemea
hivyo pengine, alitingwa na shughli nyingi, na alikuwa akisubiri muda muafaka
wa kumfahamisha mteja wake,, na wakati anajiandaa kuja kuonana naye ndipo
ikatokea hiyo ajali, ni ajali haina kinga, haina taarifa....’akasema wakili
huyo
‘Uwongo una mwisho wake, sisi tunataka kuwaonyesha kuwa hayo
yalifanyika kipindi ambacho mume wa familia hii akiwa mzima na fahamu zake na
alipanga yeye na wezake hiyo katiba ibadilishwe, si ndio mnataka kila kitu
kithibistishwe hii leo, hamtaki kusema ukweli, sasa mimi namsimamisha wakili wa familia
anayetambulikana kisheria,atuelezee ilivyokuwa;…
Wakili wetu wa familia akasimama na kuanza kuelezea mchakatao
mzima wa katiba ulivyoanza, hadi kukamilika, na mangapi yemeshafanyika na
kumalizwa kikatiba, na mafanikio yake, na alipofika kwenye changamoto zake,
akasema,;
‘Pamoja na nia njema ya katiba hiyo, bado kulikuwa na changamoto
zake, lakini zaidi ni hizo zilizofanywa kwa makusudi kwa nia ya kuharibu lile
lengo jema la kuanzisha hiyo katiba.
‘Kiukweli katiba au makubaliano kama hayo yangelitumika kwenye
ndoa zetu, nahisi ndoa nyingi zingaliimarika zaidi, na hakuna ambaye
angelidiriki kuvunja ndoa yake kwa matendo yake. Lakini sasa…’hapo akatulia
kidogo akifungua makabrasha yake..
'Ilikuwa tarehe mmh,....’akaangalia kwenye mkabrasha yake na
kutaja tarehe,’
'Siku hiyo alinijia mume wa familia ofisini kwangu..’akasema
‘Ina maana huyo hapo au sio..?’ akauliza mwenyekiti
‘Ndio mwenyekiti, ndio huyo hapo, ..alinijia ofisini kwangu,
akasema amekuja na ombo la kutaka huo mkataba ubadilishwe baadhi ya vipengele nikamuuliza kwa vipi maana huo mkataba upo
kisheria, na ukitaka kubadili chochote kwenye huo mkataba kuna taratibu
zake,kwanza inabidi wakae yeye na mke wake wakubaliane, na baada ya hapo,
inabidi tuandike barua yenye maelezo ni
kwanini tunataka kufanya hivyo.. ...?’nikamwambia hivyo.
'‘Mimi nafahamu jinsi ya kuubadili, hata bila kupitia hiyo
milolongo yrnu isiyo na maana, kwani mkataba ni wa nani, ni wa kwangu mimi na
mke wangu, kwanini niwahusishe tena watu wengine, kama nataka kubadili sihitaji
kumuomba mtu, wewe sema kama hauwezi nimtafute mtu mwingine atakayefanya hiyo
kazi...'’akaniambia hivyo mume wa familia..'
‘Sio swala la kuweza, ni swala la utaratibu, yoyote anayefahamu
sheria, ni lazima azifuate taratibu hizo,mimi nakushauri kwanza nenda mkaongee
wewe na mke wako, muone kama kuna sehemu za kubadili,mkubaliane,ili tukienda
kuomba, tufanye kazi ya kujitosheleza, sio leo hiki kesho kile, hatutakubalika
kisheria…’nikwambia hivyo
‘Kama huwezi sema..bwana…’akasema
‘Hapana sijasema siwezi..wewe nenda mkaongee na mke wako kwanza,
na kama mtanihitajia mimi niwepo kwenye hicho kikao, mimi nitakuja, ili tufuate
utaratibu..’'nikamwambia hivyo'
Yeye akasema hivi....
‘Sikiliza wewe nimeshakuona hutufai, nimeshatafuta wakili mwingine
ambaye atashughulikia maswala hayo yote, kwani kama jambo dogo kama hili linakushinda
huoni utatukwaza, kuna mambo mengi yanahitajika, na hili dogo ni mojawapo, wewe
umeshindwa, mimi kuanzia leo nakufuta awakili wa familia, nimeshapata wakili
mwingine....’akasema hivyo kuniambia mimi.
‘Mambo hayaendi hivyo bro, kuna taratibu zake bosi, hata kama mimi
mnaona sifai, ujue tumeshaandikishana mkataba , na kama mnataka kuukatisha huo
mkataba wangu na nyie pia kuna taratibu zake, huwezi kuamua mara moja kuwa wewe
sio wakili tena,....ngoja mimi nitongea na mke wako tukutane, tuone jinsi gani
ya kulifanya hili jambo kisheria,...’nikamwambia hivyo
Na yeye akasema hivi....
‘Nimekuambia mimi kama mume wa familia, sijakuambia umwambia mke
wangu, mke wangu ana shughuli nyingi za kampuni, hili la uwakili kaniachia
mimi, kwahiyo haina haja ya kuongea na mke wangu na hata ukiongea naye
haitasaidia kitu, maana nimeshapata wakili wetu mwingine..anayejua
kazi...’akasema.
Mimi niliwasiliana na mke wa familia naye akaonekana kushangaa na
taarifa hiyo, akasema nimpe muda kidogo yeye, ataongea na mume wake, na baada
ya siku mbili, nikiwa ofisini kwangu nikafikiwa na ugeni..
'Mgeni huyo alikuwa ni marehemu Makabrasha...akiwa na ajenda ile
ile kuwa amekuja kuchukua nafasi yangu, kwahiyo nimkabidhi shughuli zote,
...nikamwambia hilo halipo, na ili ahakikishe nikampigia simu mke wa familia,
na mke wa familia akaniambia hakuna kitu kama hicho, na nisitoe chchote kwa
huyu mtu, yaani Makabrasha...’
Makabrasha akaniambaia kuwa hilo lipo na litafanyika, kwani hayo
ni mambo ya kifamilia, mume anaweza kuamau kubadili chochote kwenye mkataba,
kama anaona kuna ulazima, kwa masilahi ya familia, ..akaongeza kusema kuwa
mambo mengine yanaweza kusimamiwa na mume wa familia bila mkewe kufahamu,...
‘Na kwa jinsi ilivyo, kwa vile kuna mambo kama hayo ya mke
kutingwa na kazi nyingi, na mume anatakiwa kuhakikisha kila jambo linatendeka
vyema basi kuna haja, ya kurekebisha baadhi ya vipengele kwenye mkataba huo,
umeona eeh, hilo halipo wazi kwenye huo mktaba, ndio maana nataka kufanyiwe
marekebisho..’akasema.
'Sikiliza nikuambie jambo, ili wewe undelee kuwepo, fanya kama
nitakavyo, ni kitu kidogo tu, hata ukirekebisha mke wangu hatafahamu, au sio…lakini
kama hutaki sawa, kazi zote hizo itabidi nizifanye mimi, na wewe utakuwa na
kazi,gani, eeh..hebu lifikirie hilo...'akaniamba hivyo.
Mimi nikamwambia;-
‘Wewe ni mwanasheria, unafahamu taratibu zilivyo... haiwezekani
hayo mambo kufanyika kwa haraka hivyo, kwasabbu huo mkataba umeshasajiliwa,
kuna michakato inatakiwa kupitiwa, kwahiyo ni bora hilo swala tukawauliza
wahusika wenyewe kwanza na ni vyema tukalifanya wakiwemo wote wawili,
hata hivyo, mke wa familia anasema hakutambui wewe kama wakili wa familia...’nikamwambia.
‘Na mume wa familia hakutambui wewe,a kama wakili wa familia,
umenielewa hapo, ni nani mwenye nguvu ya kifamilia, mke au mume....’akaniambia
huyo makabrasha.
Sikutaka kubishana na yeye, niliwasiliana na mke wa familia, na
mke wa familia akazidi kunisisitiza kuwa huyo mtu hamtambui na kama akizidi
kunisumbua,a basi hatua za kisheria zifuatwe,.
Baada ya kikao hicho huyo mtu sikumuona tena kuja kwangu, ila siku
moja nilikwenda kwa msajili kwa nia ya kufuatilia mambo aliyonituma mke wa
familia, nikiwa pale, nikajiwa na wazo la kupitia mkataba wa familia, nikaenda
kuonana na huyo anayesimamia hiyo mikataba,
‘Cha ajabu kabisa huyo jamaa wa masijala ya mikataba akaniambia
kwasasa hanitambui mimi,...anamtambua wakili mwingine, aliyeletwa na wahusika,
kwahiyo sistahili kuchukua chochote, ikabidi nimpigie simu mke wa familia, na
mke wa familia, akaniambia nifuatilie kwa msajili mkuu, na nilipokwenda huko,
wenyewe waliona ajabu, wakaniambia niwape muda watalifuatilia hilo swala..
Wakati wao wanalifuatilia huko, mimi nikaona kuwa hilo sasa ni
tatizo, hata kama ni ajira,unatafuta kipato, lakini kama kuna sintofahamu ya
namna hiyo ni bora uwaachie wenyewe, lakini kwanza nikaona, nionane na wahusika
wote wawili.
Nikaongea na mke wa familia dhumuni langu hilo, yeye alinikatali
na kuniomba niachane nalo kwa hivi sasa, yeye ataona ni nini cha kufanya, hata
hivyo mimi nikamshauri kuwa ni bora tukae kikao yeye na mume wake, na ikibidi
tumkaribishe na huyo Makabrasha tuliongee kwa mapana, ili tupate muafaka,
lakini mke wa familia alipinga kabisa kumkaribisha huyo Makabrasha akisema
anamfahamu sana huyo mtu yeye hawezi kumruhusu mtu kama huyo kuingiza
kwenye shughuli zake.
‘Basi tukakubaliana kuwa tukae yeye na mume wake, akakubali
na tukakubaliana tufanye hicho kikao mwisho wa wiki hiyo, lakini kabla
hicho kikao hakijafanyika ndio hiyo ajali ikatokea...’akasema huyo wakili.
Mwenyekiti akamuangalia wakili wa mume wangu na kumuuliza;
‘Je una swali lolote kwa wakili mwenzako, maana huo ndio ukweli
wenyewe,sasa kama ulidanganywa, basi ujue umeingia choo cha kike...’akasema
mwenyekiti na watu wakacheka.
‘Mimi hapo sioni tatizo, ..katiba sio msahafu, kuwa hauwezi
kubadilishwa, wazo kama hilo la kufanya mrekebisho kumbe lilikuwepo, na alikuwa
nalo mteja wangu, kipindi hicho hajapatwa na ajali, na alikuwa katika harakati
za kulifuatilia hilo jambo kisheria kwa kupitia kwa huyo marehemu...hilo
hatulipingi, ni jambo la kawaida...’akasema huyo wakili na akainama
kunong’onezana na mteja wake, halafu akasema;
‘Ni kweli mteja wangu akiwa na nia hiyo alimtumia wakili
Makabrasha, ambaye ndiye aliyeanza mchakato wa kufuatilia jinsi gani ya kufanya
hayo marekebisho ya hiyo katiba, na wakati anaendelea na mchakato huo, bahati
mbaya mteja wangu akapatwa na ajali, ya nyuma yakafutika kwenye ubongo wake, na
alipopata nafuu, akaikumbuka katiba yake, na aliyoiona ndio hiyo aliyokuwa
akiwaonyesha nyie, hakuwa na kumbkumbu zingine za nyuma, hata mkienda hospitali
mtapata taarifa zake...kwahiyo michakato mingine ilifanyika yeye akiwa
mgonjwa...’akasema wakili.
‘Nikuulize swali, hayo mabadiliko yaliyofanyika kwenye hiyo katiba
mpya ndivyo alivyopendekeza mteja wako kabla hajapatwa na hiyo ajali au kuna
mengine yaliongezwa yeye hakuwa hana ufaham nayo?’ akaulizwa
‘Hilo yeye hakumbuki, kwasababu hana kumbukumbu sana za nini
kilitakiwa kibadilishwe, na mlipomshinikiza zaidi, ndio kumbukumbu ikaanza
kumrejea kuwa hilo jambo lilikuewepo akilini mwake, kipindi cha nyuma, na
bahati mbaya akapatwa na hiyo ajali, sasa huenda kweli hayo yaliyopo humo
kwenye katiba ndiyo aliyokuwa amependekeza au kuna mengine yaliongezwa kwa
ushauri wa wakili wake..yote yawezekana, tatizo lililopo hapa ni Makarasha
hayupo, ndiye angeliweza kutupatia majibu ya hayo yote, na mbaya zaidi kazi zake
zilikuja kuibiwa zote na watu, sasa sikuweza kujua wapi aliishia...’akasema
huyo wakili.
‘Naona tusipoteze muda kwa hio, hapa tumeshaona kuwa kweli,
kulikuwa na mbinu za kuibadili hiyo katiba bila ya mke wa familia kuhusishwa,
lakini hazikufanikiwa,..vyovyote tutakavyoliweka, litasomeka kuwa kulikuwa na
hujuma za hadaa, baada ya kukataliwa na mke wa familia, na wakati mke wa
familia anajitahidi waliongee yeye na mume wake, akitafuta ni kwanini
mwenzake anataka kuwe na mabadiliko katika hiyo katiba, mwenzake akawa
anajaribu kupoteza muda ili wafanikiwe katika mbinu yao hiyo, na kwa haraka
wakakimbilia kufanya hicho walichokifanya...’akasema mwenyekiti.
‘Kwahiyo basi katiba hiyo aliyokuwa nayo mteja wako ni batili,
haipo, na haitambulikani kisheria, sisi tunaendelea kutumia katiba
halali, na hiyo ndiyo tunayotaka ifanye kazi yake hii leo,...sawa muheshimiwa
wakili?’ akaulizwa, na kabla huyo muheshimiwa wakili hajajibu, mume wangu
akamnong’oneza kitu wakili wake, na wakili wake akawa kama anasita kuongea, na
kukawa na kama ubishi , na wakili wake, akasikika akisema;
‘Hayo ni mambo ya kisheria huwezi kuyakwepa, acha iwe kama ilivyo,
nitajua jinsi gani ya kupambana nao hawaniwezi hawa...’akasema na mume wangu
akaonekana kutokurizika na maamuzi ya huyo wakili, na baadaye kidogo baada ya
wao kuongea kidogo huyo wakili akamgeukia mwenyekiti na kusema;
‘Samahani kwa kuwapotezea muda, unafahamu mteja wangu anakuwa na
wakati mgumu, kwani hiyo katiba inayotambulikana kisheria, yeye, haikumbuki
sana, ...sasa inamuwia vigumu kwake kukubali moja kwa moja...naomba hilo
mliweke akilini, ila anahisi hadi kufikia hatua ya yeye kuomba kuwe na
mabadiliko, marekebisho, anahisi kulikuwa na vipengele vilivokuwa
vikimkandamiza na kutokumpa nafasi ya kutumiza wajibu wake kama mume wa
familia...’akasema huyo wakili.
‘Kwahiyo..?’ akawa kama anauliza mwenyekiti.
‘Kwahiyo mteja wangu anasema, tukiendelea kuitumia katiba hiyo ya
zamani, yeye anaweza akadhulumia na kutendewa isivyo haki, na ndio maana
aliamua hiyo katiba ifanyiwe ukarabati,..anaomba itumike katiba hiyo mpya kwa
masilahi ya familia, kwani yeye ameipitia na kuiona ina faa sana kwenye familia
yake..’akasema wakili.
‘Wewe kama wakili unaifahamu vyema sheria, hilo kweli ni sahihi,
maana ukumbuke huo mkataba, ilishatumika huko nyuma, na hakukuwa na matatizo,
matatizo yamejitokeza baada ya mteja wako kufanya mambo kinyume na
makubaliano,....’akasema mwenyekiti, na kabla wakili hajasema neno mwenyekiti
akaendelea kusema;
‘Hoja kama hiyo alitakiwa mteja wako aisema kabla,hajafanya hayo
aliyoyafanya, kama tutakuwa tunabadili mkataba kila tukifanya makosa, au
tukitaka kukidhia haja zetu, unafikiri huo mkataba utakuwa na maana kweli, je
ni mkataba wa masilah binafsi au ni mkataba wa kukidhi haja za wote, na kwanini
alipoona hivyo, hakuongea na mke wake kwanza, ..hizo ni njama za makusudi, hayo
yanajulikana , hoja yake kwa sasa haina mshiko, hata wewe wakili unaliona hilo,
kama unafahamu vyema kazi yako..mimi ninaona tusipoteze muda tuendelee na kikao
chetu au sio muheshimiwa wakili,...?’ akauliza mwenyekiti.
'Mwenyekiti akanigeukia mimi, na kuniuliza
'Au wewe mke wa familia, unasemaje kwa hilo...maana wewe umekuwa
mstari wa mbele kumtetea mume wako...haya tukusikilize na wewe...'akasema
mwenyekiti.
‘Ndugu mwenyekiti, mimi naomba tuendelee na ajenda
nyingine,...katiba yetu ni hiyo hiyo, tumashaona kuwa kulikuwa na njama za
kuibadili, kwa vile mume wangu alishaona kuwa kafanya madhambi, tena madhambi
makubwa, na akafahamu kuwa kutokana na hiyo katiba, ataingia matatani, akaamua
kumshiriksiha makabrasha ,akimfahamu fika kuwa ni mtaalamu wa hadaa, wa kucheza
an sheria kibatili, ....’nikasema.
‘Madhambi gani niliyafanya wewe mke, usitie mafuta kwenye moto,
..sisi tunataka kulimaliza hili kwa masilahi a familia, wewe unaleta mambo
mengine,mimi ninaangalia mbali kwa ajili ya vizazi vyetu, na sio kwa ajili ya
kuwafurahisha watu wengine, wewe hujui kuwa wenzako hapa, nikiwa na maana watu
wasioitakia mema ndoa yetu iwepo, wana malengo mengine kabisa, kiuvunja ndoa
yetu halali,….akasema mume wangu kwa hasira.
‘Kulimaliza hili kwa vipi ukumbuke hizo ajenda nyingine
zinahusiana na huo mkataba, na tumeshindwa kuingia kwenye ajenda hizo kwasababu
ya huo mkataba wenu wa bandia..., ‘nikasema na mume wangu akataka kusema kitu
na mimi sikumpa nafasi.
‘Ujue fika, …ajenda nyingine, nikuhusu madhambi yako, yale uliyoyafanya
ambayo ni kinyume cha katiba hiyo. Tumepoteza muda mwingi kwasababu ya uwongo
wako, na sasa uwongo wako umebainika, na madhambi mwenyewe yatakuja kukusuta…’nikasema
‘Madhambi gani wewe…’akasema kwa karaha
‘Ina maana wewe hujafanya madambi, huna makosa…?’ nikauliza
‘Sema ukweli ..kama kwel huna madhambi,...mbona unaogop ahapo
kutoa kauli…’nikasema na mume wangu akabakia kimia.
‘Tuendelee na kikao ndugu mwenyekiti…’nikasema, na kabla
mwenyekiti hajaanza kuongea mume wangu mara akaanza kuongea kwa kusema;.
‘Sijafanya madhambi yoyote mimi, na wala siogopi, ninachotaka ni
kuitetea ndoa yangu ambayo naona wenzako wanataka kuivunja kwa nguvu, kwa
kigezo hiki cha kutumia huo mkataba, mkataba ambao uliipendekeza wewe, ukiwa
umeshaongea na wazazi wako, mimi hilo nilishalifahamu, lakini kwa muda ule
sikuwa na la kufanya...’akasema mume wangu, na mwenyekiti hapo akaingilia kati
na kusema;
'Kwahiyo hilo unalikumbuka, kuwa mkataba huo ulipendekezwa na mke
wako, wewe hukuhusika, au ...?' akaulizwa
'Sio swala la kukumbuka , ndivyo ilivyo,kila kitu hapa
kinajionyesha, mnataka mimi niseme nini zaidi ...'akasema
*************
‘Kwa vile tumeshaona kuwa katiba ya kugushi haina mamlaka tena
hapa, sasa tunaingia kwenye sehemu ya nyingine ya ajenda zetu, na ajenda hii,
ni kumuacha mke wa familia, aongee ni nini kusudio lake la kuitisha hiki kikao,
...’akasema mwenyekiti. Na pale nikaona mume wangu akiandika kitu kwenye
karatasi na kuisogeza hadi kwa wakili …wakili huyo hakuwa amekaa mbali na
alipokuwa mume wangu.
Mara wakili wa mume wangu akaonyesha mkono na kusema;
'Mteja wangu anasema hataweza kuingia kwenye ajenda nyingine mpaka
swala hili la katiba ya kifamilia litatuliwe, kwani mkataba wao ndio msingi wa
mambo mengine yote...'akasema wakili huyo
‘Hatuwezi kupoteza muda zaidi,..tafadhali mkumbuke hapa kuna watu
wanataka kusafiri, kuna watu wameacha shughuli zao, kama docta pale, kwa ajili
ya hili jambo, kiukweli tutakuwa hatuwatendei haki…’akasema mwenyekiti, na mimi
nikaongea hata bila ya kibali.
‘Ndugu muheshimiwa wakili, mteja wako anafahamu fika kuwa kafanya
madhambi mengi tu, na aliyafanya hayo akiwa na akili zake timamu, makosa ambayo
kikatiba yetu ya kifamilia, ..nikiwa na maana mkataba…madhambi hayo yanatambulikana
kama makosa makubwa, ambayo ukiyafanya, kama mkataba unavyojieleza, adhabu yake
ni kubwa sana, na haina msamaha..kipengele hicho kwenye katiba ya kugushi
kimeondolewa kinamna, ...'nikasema.
'Lakini huwezi kuyaita makosa makubwa , mpaka ibainike wazi kuwa
ni makosa au sio na ikiwa na maana ni lazima kuwe na ushahid wenye mshiko, uliothabiti, au sio...'akasema wakili
'Na ndio maana tunahitajia tuendelee na ajenda nyingine ili
kuyabainisha hayo makosa,...'nikasema
'Lakini mteja wangu hajakubaliana na hiyo katiba iliyojitokeza
kwasasa, huwezi kumshikinikiza kwa kitu ambacho hakitambui unielewe hapo maana
baada ya kutaja hayo madhambi ni nini kitafuta, si adhabu au, na je adhabu hizi
zitatumia kigezo gani...'akasema wakili
'Ndugu muheshimiwa wakili, ukumbuke hii katiba tumeshaitumia zaidi
ya miaka tisa, na haikuwahi kuwa a utata, kwahiyo tuna udhoefu nayo, tatizo ni
hivi sasa, utajiuliza ni kwanini, ..jibu ni rahisi hapo,ni kwa vile kumetokea
matatizo makubwa, matatizo ambayo mteja wako anafahamu fika kuwa ni madhambi
makubwa, na hajataka kuyakiri hayo makosa,anajua ni kwanini...'nikasema.
'Sawa,...tumesikia hayo, lakini huwezi kuyaita madhambi
makubwa, kwa mteja wangu, mpaka yathibitishwe, kuwa ni madhambi makubwa, na kwa
ushahidi, ..na ushahidi bayana uwepo, hiyo ushahidi bayana ina maana
kubwa sana hapo..’akasema wakili
‘Tutaonyesha hilo, halina shaka…’nikasema
‘Hata hivyo, hatuwezi kukimbilia kuhukumu kwenye katiba ambayo
imeshatiliwa mashaka, na pande zote mbili, kwanza haikuwepo, imekuja baada ya
hiki kikao, pili mteja wangu haiamini, ndio maana mteja wangu anaona kuwa kuna
umuhimu kwanza wa kuhakikisha tatizo la mkataba limekwisha, na kila mmoja akawa
karizika,…kwanini tukimbilie kwenye makosa kwanza....''akasema wakili.
‘Nimeshakuelezea hilo, kuwa mkataba huu, na matuzimizi yake
haukuanza jana au leo, una miaka mingi, kwanini anaogopa hivi sasa, ni kwa vile
kafanya madhambi, ndio maana anajihami…’nikasema
‘Mdhambi gani hayo, na kwenye mkataba yana msimamo gani..?’
akauliza wakili na hapo mume wangu akamuangalia wakili huyo kwa hasira, kama
kumuonyesha hapo kuwa katoa swali sio mahali pake. Na mimi kwa haraka nikaamua
kuitumia nafsi hiyo kuelezea …
‘Kwenye katiba yetu kuna makosa tuliyaanisha kama makosa makubwa,
kama zinaa, uzinzi, kuua, kuiba, ushirikina ....hayo ni baadhi ya makosa
makubwa, na humu kwenye katiba tulianisha kuwa, mke au mume akigundulikana
kutenda hayo makosa,...hukumu yake..’nikatulia nikijaribu kufungua ule
mkataba..
‘Haina haja ya kusoma, ile inasema makosa kama hayo, yanaruhusu
talaka moja kwa moja, na mwenye makosa, hatapata haki yoyote, tunatambua kuwa
mtoaji talaka ni mume, lakini hata mke anaweza kuiomba hiyo talaka, na hilo
limebainishwa hapo, kuwa kama ni mume kafanya hivyo, talaka ipo wazi, sio swala
kuomba tena, na mume hana haki y akudai chochote….’nikasema
‘Na maelezo hayo hayakubakia kwa mke au mume peke yake, kila mmoja
limagusa,..na hata nini haki mtu anazikosa, zote zimeelezewa kwenye kipengele
kinachofuata,..sasa ni kwanini kwa hivi sasa aogope mkataba usifanye kazi yake,
...yeye si anadai hana makosa, ..basi tuache ukweli useme...'nikasema na hapo
mwenyekiti akaingilia kati, na kusema
‘Mimi sitaki kuingia undani wa huo mkataba kwani wakili wao yupo
hapa, yeye ndiye mtaalamu wa huo mkataba ambo kwao waliuita katiba ya familia,
kwani yeye ndiye aliyeikamilisha hiyo kazi kisheria, kama ni muhimu
atasimama na kubainisha au kufafanua kila kipengele, lakini kwa sasa
tunataka kuyafahamu hayo madhambi makubwa aliyoyafanya mume wa familia...au sio
wakili..?’ akauliza mwenyekiti
‘Sawa ni vyema tukayaona hayo makosa, ili yabainishwe kama kweli
mteja wangu kayafanya,…vinginevyo hatuwezi kuyatambua kama makosa..kwa
kipengele gani….na...’akasema wakili na kabla hajamaliza, mume wangu akasema.
‘Hilo haliwezekani, huo ni mtego wakili, nimekuambia kuwa, uhakikishe
swala la mkataba linamalizika kwanza, mimi siukubali huo mkataba, kwanini
unataka uanze kufanye kazi,…wakili fanya kazi yako,…’akasema mume wangu
‘Ndio naifanya hivyo, usiwe na wasiwasi..bosi…’akasema wakili
‘Lazima niwe na wasiwasi, wewe huwajui hao watu, ni wanjana ndio
maana nikakuita upambane nao kisheria,, sio ukubaliane na huo utumbo wao na
mbinu zao za ujanja ujanja za kunitega, lengo lao ni ili kunichimbia kaburi,
kama huwezi kazi sema, nikatafute mtu mwingine....’akasema mume wangu kwa
hasira.
‘Ina maana huu tunaoongea hivi sasa hapa ni utumbo, wakili mwambie
mteja wako achunge kauli zake…hiyo sio kauli ya mtu muungwana, au sio?’
akauliza mwenyekiti aliposikia mume wa familia akilalamika.
‘Samahani ndugu mwenyekiti, hayo yamemtoka mteja wangu, akionyesha
wasiwasi tu, ninamuhakikishia mteja wangu kuwa hilo la hiyo katiba
lisimtie shaka, cha muhimu ni kuangalia hayo madhambi yanatotajwa, ni madhambi
gani, kwani kama yalivyoanza kuelezewa, hayajafafanuliwa na ushahidi ulio
dhahiri , kwahiyo hayana msingi, mimi kama wakili nitakutetea kisheria, na haki
yako italindwa, una wasiwasi gani, usijali...’akasema huyo wakili kwa
kujiamini.
‘Wewe umeharibu kila kitu… huo mkataba ndio msingi wa kila kitu
hapa,…haukubaliki, unasikia, haukubaliki…’akasema mume wangu akimtolea macho
wakili wake na mwenyekiti akaona asipoteze muda, akaendelea na kikao akisema;
‘Kwanza kabisa kama kawaida ya mambo ya kifamilia huwa tunampa
nafasi mtetezi, atoe kauli ya kukiri kosa, kwani jambo hili ni la kifamilia,
mtetezi, anaweza akakiri kosa na kuelezea udhaifu wake, na makosa yake, kwanini
alifanya hivyo, kwa kupitiwa, au kwa makusudi, na sisi kama familia
tutamsikiliza,...mnaonaje jamani tukampa huyu mtu nafasi ya mwisho…'akasema
mwenyekiti
'Ujanja huo…swala hapa ni huo mkataba, mimi sina imani nao…'akasema
mume wa familia
'Cha muhimu ni kwako ndugu, mtetezi, ni wewe kuongea ukweli,
ukweli ni silaha kubwa kwa mtu yoyote, ukikiri kosa ukatubu, watu wanakusikiliza,
kwasababu kila mtu ni mkosaji, sasa tunakupa nafasi hiyo mume wa familia, hapo
hatuhitaji wakili wako, tunahitaji kauli yako wewe, kauli yako kwetu ni muhimu
sana, ....’akasema mwenyekiti.
‘Mimi sijafanya hayo madhambi makubwa mnayonisingizia, yote ni
uwongo na ni mbinu za kuniharibia ndoa yangu...’akasema mume wangu kabla
hajaruhusiwa.
‘Je uliposema madhambi makubwa, ina maana unayafahamu hayo
madhambi makubwa ni yapi, kikatiba?’ akaulizwa na akakaa kimiya na wakili wake
akasema;
‘Mteja wangu anasema kuwa hayo madhambi mnayomshutumu nayo
hajawahi kuyafanya, kibinadamu kuna kuteleza, yeye kama aliteleza hakupewa muda
wa kujitetea, kama kuna jambo lilitokea akalifanya ni yale ya kibinadamu tu,
yoyote anaweza kupitiwa, ndio maana alitaka katiba hiyo ifanyiwe marekebisho,
maana inahukumu moja kwa moja bila kujali ubinadamu, bila ya kumpa nafasi
mkosaji,...’akasema wakili.
‘Sisi tutatoa ushahidi kuwa hayo aliyoyafanya sio kwa bahati
mbaya, kama ni kwa bahati mbaya mbona hataki kuyakiri hayo makosa, kukataa
kwake, kuwa hajafanya kunaonyesha usugu, na uthubutu wa mteja wako, na
tusipoteze muda, .kama hataki kukiri makosa basi sisi kama wanafamilia tunataka
kuyaweka makosa yake hadharani, na wanafamilia watayaangalia, kwa mizania, je
alifanya hayo madhambi kwa bahati mbaya au alikusudia,...’akasema mwenyekiti.
‘Kwanini anaogoa kama kweli hajayatenda,hajiamini! …muulize mteja wako,kwanini anaogopa hata
kuyataja hayo madhambi…’nikasema na hapo mume wangu akaniangali na kusema kwa
hasira
‘Ni nani anaogopa…siogopi kabisa, ila nawafahamu nyie, mambo yenu
mnayapeleka kimtego, mtego…sasa mimi nawaambia hivi, mimi nitapigania haki yangu mpaka mwisho..ndoa
haivunjiki kirahisi hivyo, nimeshalisema hilo, na ndio kauli yangu mpaka
mwisho...’akasema na wakili wake, akamwendea na kumnong’oneza jambo, na mume
wangu akasema;
‘Sawa fanya unavyoweza wewe, lakini…huo ni mtego, ..kwa hali kama
hii, mimi..aah, umeshanikatisha tamaa,...haya endelea, uonavyo wewe...’akasema
kwa hasira
Mwenyekiti hakuwasubiria akasema;
‘Mke wa familia uwanja ni wako…na tunataka usiongee maneno mengi,
lenga moja kwa moja kwenye makosa, kama ni makosa, na mkataba wenu ndio
utakaofanya kazi, kwani tokea mwanzo,mume wako ndiye alisema mkataba wenu ndio
kila kitu, basi, sisi hatuna kazi tena, kazi yetu ni kupima uzito wa hayo
makosa, kama yapo,..’akasema mwenyekiti, na mimi sasa nikaamua kusimama kabisa,
na safari hii, nikiwa sitaki kabisa kumwangalia mume wangu, nikasema;
‘Mume wangu ana makosa makubwa, nikisema makosa makubwa
itaeleweka, na hata kwenye mkataba wetu, hayo makosa makubwa yana nafasi yake,
na ni mhimu kama tutakubaliana, niweze kuyataja hayo makosa yake kwa kifupi tu,
na nitakuja kuyafafanua, au mkataba wenyewe utafafanua…’nikasema
‘Mume wangu kafanya makosa
ya uzinzi, na zaidu ya hayo yeye
ni mnafiki....’nikasema na mume wangu akasimama na kuniangalia kwa hasira
‘Unaleta matusi hapa..mimi ni mzinzi, una ushahid na hilo…’akasema
mume wangu kwa hasira na wakili wake akamkalisha chini na kumnong’oneza kitu,
na mimi sikumjali nikaendelea na maelezo yangu.
‘Kwanini nasema kuwa mume wangu ni mzinzi na mnafiki, angalia
katika katiba yetu, kosa linalotambulikana kama huyo mtu ni mzinzi na au huyo
mtu ni mnafiki..'nikasema
'Maneno haya ni kauli yake yeye mwenyewe siku ya kutunga huo
mkataba alitaka hayo maneno yawekwe kama yalivyo, kuonyesha madhambi hayo
makubwa, na akataka yawekwe hivyo kama
yalivyo,kwahiyo mimi, sijakutukana kama unavyodai wewe, ila umejitukana wewe
mwenyewe kwa matendo yako, kauli yangu inashuhudia tu hayo…ila wewwe ulikwisha
kuyafanya hayo kwa vitendo vyako mwenyewe, ashakumsi matusi, kuwa wewe ni
mzinzi kwa jina jingine wewe ni muhuni na sitasita kukuita malaya....’nikasema
na watu wakaniangalia kwa mshangao.
‘Mumesikia wenyewe jamani…’akasema mume wangu akilalamika, lakini
wakili wake alikaa kimia.
‘Sitamki haya meneno kwa nia mbaya, hapa wapo wazazi wangu
nawaheshimu sana, naomba wakili wetu atusomee kwenye katiba yetu; mzinzi ni mtu
gani, au Malaya ni mtu gani:..nikasema na mwenyekiti akatabasamu huku akitikisa
kichwa kama kunikubali, na mwenyekiti akanyosha mkono kumruhusu wakili asome
maana ya maneno hayo, wakili akasema;
‘Mzinzi ni tabia ya mwandoaa u mtu yoyote ambaye katenda tendo la
ndoa kwa asiyekuwa mke wake au mume wake au yoyote akifanya bila kuingia kwenye
ndoa..’akasema wakili.
`Na mnafiki ni yule asiyetunza ahadi, mwongo mdanganyifu,
mzandiki, aliyeahidi akashindwa kutimiza ahadi yake, aliyeongea uwongo huku
akijua anaongea uwongo, aliyeaminiwa akashindwa kutimiza imani yake kwa
watu...na ...’akasema wakili. na mwenyekiti akakatisha na kusema
'Endelea na maana ya hilo neno jingine, tusipoteze muda, mtu
akitaka kusoma ufafanuzi zaidi mkataba huo sasa upo huru...'akasema mwenyekiti
‘Na Malaya...hebu kidogo hapo..’ akasema mwenyekiti
‘Mwenyekiti mimi naona inatosha....’ nilitaka watu wasikie maana
ya hayo maneno mawili ya awali kwanza…’nikasema
‘Mume wangu nimegundua kuwa wewe ni mzinzi, na tabia hiyo ipo
kwenye damu,...na wewe ni mnafiki wa hali ya juu, kwa vile umehini ndoa yetu,
umezini na wanawake zaidi ya mmoja, ukijua kabisa kuwa hilo ni kosa, na mungu
akatoa ushahidi usiokwepeka, ...’nikasema na yeye akajifanya kutabasamu kwa
dharau
‘Mume wangu wewe ni mnafiki, kwa vile umeyakana makubaliano yetu,
ukadanganya, ukashindwa kutimiza yale uliyoyaahidi, na ukatafuta njia ya
kuhadaa, tena kwa kuwaribuni watu waliopewa dhamana hiyo kwa kuwaonga, hilo ni
kosa jingine kubwa...’nikasema kwa
huzuni.
‘Hayo yote ni makosa makubwa, sio kwa mkataba wetu , lakini
kifamilia, umejiabisha,… na uliyafanya hayo ukiwa na akili zako timamu na sio
mara moja, ingelikuwa mara moja tungelisema,..ooh, ni bahati mbaya, uliteleza,
lakini imekuwa ni tabia yako, hadi ukaumbuliwa ....na mungu hakukufichia
madhambi yako, ....’mara mume wangu akasimama na kusema;
‘Sio kweli, wewe umeamua kunitukana tu na kunizalilisha tu, hayo
unayoyasema yote ni uwongo, wewe nakuona sasa umeungana na wazazi wako, ili
mnisaliti, hayo uliyosema nimeyafanya wapi, ni nani shahidi yako,
..nimeshutikia,lengo lenu, nia yenu ni kunizalilisha tu, wakili wangu yanukuu
hayo matusi, kwasababu ninaweza kumchukula hatua huyu mwanamke, hanijui tu
mimi..’akasema mume wangu.
‘Hujatukanwa, Katiba yenu inaelezea hivyo, ila wewe ulitakiwa
umwambia mke wako athibitishe kauli yake, kama ni ya uwngo basi tutayachukulia
kama ni matusi na wewe una hiari ya kumuadhibu mkeo, na hata kumshitaki
kikatiba,lakini kama ni kweli, wewe una tabia hiyo, basi usikasirike kuitwa kwa
sifa hizo..’akasema mwenyekiti.
‘Sio kweli , mimi sina hiyo tabia, yeye ni mtaalamu wa kuongea tu,
anaona sifa sana kumharibia mume wake heshima yake, na hajui hilo kindoa ni
makosa, unatakiwa ufiche siri za mwanandoa mwenzako, wewe unazianika hadharani,
hiyo ni tabia gani, na wazazi wako wanakuunga mkono, siwaelewi kabisa
mimi...’akasema mume wangu kwa hasira.
‘Ndugu mwenyekiti, sio kwamba napenda kutaja siri za mume wangu
hadharani, lakini kwa hali kama hii alitegemea mimi nifanye nini, inabidi
tufanye hivyo, kwasababu hukutaka kukiri makosa yake, na nilimuomba afanye
hivyo, tukiwa sisi wawili, hukutaka kusema ukweli,,ni kweli si kweli...?'
nikamuuliza mume wangu akasema
'Si kweli...'akasema kwa sauti kama ya kunishushua..na mimi
sikujali, niksema;
'Wewe, uliendelea kufanya jinsi ulivyotaka wewe mwenyewe kwa
masilahi yako binafsi, na hawo waliokudanganya, hata kwa kile cha makubaliano
ya watu wawili...na mbele ya hiki kikao hukutaka kukiri ukweli, japokuwa kusema
tu, kweli nilifanya nisameheni, hutukutaka ataje kila kitu, ...kukiri kosa
kashindwa, je mtu kama huyu alitaka mimi nifanye nini, mimi nikae tu kimiya
huku ukiendelea kuvunja amri za ndoa, hapana, hilo halipo...’nikasema na kutulia
‘Unanisingizia tu, hayo yote ni uzushi, na wewe nashangaa siku
hizi unaukubal uzushi, sijui una malengo gani na mimi, lakini kumbuka mimi ni
baba wa watoto, watoto wanajua jinsi gani ninavyowajali…’akasema
‘Mimi hayo yote ninayoyasema hapa sijakusingizia,kama
itaonekana ni uwongo, mimi nipo tayari kuwajibika, na kwahiyo, ni bora ukakiri
makosa, ili tusipoteze muda hapa,..ongea ukweli, tuone kikao kitasemaje, je upo tayari kukiri
kosa,?’ nikamuuliza na yeye akatikisa kichwa kukataa, na baadae akasema.
‘Usinifanye mimi mjinga, nafahamu malengo yenu ni kunitega, nikiri
kosa, ili muanze kuhukumu kwa ….mkataba huo…sasa mimi nasema hivi, wewe si
unajifanya unayafahamu makosa yangu na una ushidi, utoe huo ushahii, na nasema hivi kama huna
ushahidi na lengo lako ni kuniharibia, kibao kitakugeukia wewe,
...nitahakikisha naitumia hiyo hiyo katiba kukufunza adabu...’akasema kwa
hasira.
'Subirini kwanza, naona mumekwenda haraka kidogo...'akasema
mwenyekiti, huku akimgeukia mume wangu, akamtizama kwa makini halafu akageuka
kumtizama wakili wake.
'Ndugu muheshimiwa wakili, mtu unayetaka kubeba dhamana yake
ndivyo huyo na ndivyo hivyo alivyo,..pamoja na yote, pamoja na kupewa nafasi ya
kukiri kosa, bado kabakia na msimamo wake, je ni wewe ulimshauri hivyo...?'
akauliza mwenyekiti
'Mwenyekiti..mimi kama wakili wake, kwanza nilipenda kuyasikia
hayo makosa, ili niweze kumtetea mteja wangu, je ndio imanipatia hiyo nafasi,
...?' akauliza wakili huyo.
'Hapana nafasi hiyo utaipata tu,..ila kwa vile uwanja ni wa
mwenyeji wa kikao hiki nataka yeye mwenyewe ayathibitishe hayo madai yake,
maana kama ni uwongo, basi hata mimi nitachukua jukumu hilo la kumuadhibu,
maana hayo ni makosa makubwa, ...je msemaji una ushahid gani wa hayo
makosa...?' akauliza mwenyekiti.
‘Ushahidi upo mwingi tu…’nikasema
************
‘Nimeongea kwa kifupi ili kutokupoteza muda, na sasa namuomba
shahidi wangu wa kwanza kuthibitisha kauli hizo nilizozitoa, sio matusi, bali
ndio ukweli halisi. Wapo wengi wakuthibitisha maneno yangu, ila kwa sasa
namuomba....’nikageuka kuwaangalia washiriki,nikamwangalia rafiki yake docta…
Docta akainamisha kichwa, nikajua ni kwanini, nikamwangalia mke wake, mke wake alikuwa kama
hayupo, alionekana ana mawazo mengi, na kabla sijatamka neno ...’ mama ambaye muda
mwingi alikuwa kimiya akasema;
‘Mimi naomba aje Binti yangu wa kufikia, ..aje yeye kwanza maana
anahitajika kwenda kujiandaa kesho anasafiri....’akasema mama na mwenyekiti
akauliza
‘Unajuaje kuwa huyo ni shahidi wake, usiharibu utaratibu, au..’akasema
mwenyekiti
‘Sawa ila…’nikasema nikiwa sijui lolote kuhusu huyo bint
‘Mimi nina uhakika ni shahidi wake..’akasema mama.
‘Haya, kama muhusika umemkubali kuwa ni mmoja wa shahidi zako,
aitwe, au unasemaje mwenyeji wa kikao..?’ mwenyekiti akauliza na mume wangu
akawa kabakia kimia, akiwa kashika kichwa.
'Sawa maana shida hapa ni kuthibitisha kauli zangu ambazo mume
wangu kasema namkashfu, nimemtukana na sio kweli kuwa ana watoto nje ya ndoa, ...sasa huyo shahidi atathibitisha hayo
niliyoyaongea, ili tusipoteze muda..'nikasema.
‘Hahaha…’akacheka mume wangu akionyesha dharau, kuwa labda
nahangaika bure
'Na sio huyo tu, hapa ninao, na wengine hawajafika, ...sio kusudio
langu kuyaweka haya hadharani, lakini nitafanya nini,..eeh,..basi aitwe huyo
binti, akimaliza nitamsimamisha shahidi wangu mwingine,...'nikasema.
‘Sawa…’akasema hivyo mume wangu, lakini sasa akionyesha wasiwasi
kidogo.
'Kama nilivyosema awali kikao hiki nimekirejesha kwa mwenyeji
wetu, sitapenda mimi kuingilia, haya sasa akaitwe huyo binti,...'akasema
mwenyekiti
Na aliposema hivyo, watu wote wakawa na hamu ya kumfahamu huyo
binti ni nani, ambaye ataweza kutoa huo ushahidi wa jambo nzito
kama hilo, nilimuona hata mume wangu akiwa na hamu ya kumuona huyo binti,
hamjui ni bint gani huyo...
Watu wote mle ndani wakakageuza kichwa kuangalia mlangoni,
waliposikia mlango ukigongwa, na mara ukafunguliwa, na mwenyekiti akasema;
‘Ingia na njoo huku mbele,...utoe ushahidi wako, tuambie
ilikuwaje, na ni nani alikupachika mimba, usiogope, sema kila kitu….’
NB, Ni binti wa kufikia huyo anakuja kutoa ushahidi , je atasema
nini
WAZO LA LEO:Kukosa
ni kawaida ya binadamu, hakuna anayeweza kujithibitishia kuwa hatendi kosa,
yapo ya bahati mbaya na yapo makosa ya kudhamiria, vyovyote iwavyo, unapokosea
unastahiki kukiri na kutubu kosa lako, na kumuomba msamaha yule uliyemkosea,
unapokosa ukabainika, au hata kama hujabainika, wewe ukalikana lile kosa, unakuwa
umetenda kosa jingine. Tujifunze kuwa wa kweli, na tukikosea tujute, tutubu,
tuwaombe msamaha tulio wakosea, na
tudhamirie moyoni kuwa hatutarudia tena kutenda hayo makosa.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment