Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Saturday, February 3, 2018

MKUKI KWA NGURUWE-74


Mwenyekiti, akauliza tena;

‘Huyu mtu ameenda wapi, mnakumbuka nyie ndio mliotaka awepo hapa kwenye hiki kikao mkifahamu kuwa anatafutwa na polisi kwa uhalifu, na mimi nikamthibitishia ofisa wa polisi kuwa, huyo kijana atakuwepo hapa hadi mwisho wa kikao…?’ akauliza mwenyekiti na watu wote wakawa kimia.

‘Hakuna wa kujibu .. mnataka mimi nieleweke vipi kwa hao watu wa usalama, kuwa nilikuwa namuhadaa, au sio,…sasa niambieni huyu mtu kaenda wapi...?’ akauliza mwenyekiti kwa ukali, lakini wote walibakia kimia kuashiria kuwa hakuna aliyemuona akitoka.

‘Mwenyekiti, inawezekana huyu mtu alitoka kipindi tunaangalia hiyo lap-top yako, na kwa kipindi hicho hakuna aliyefikiria kuwa huyu mtu ataondoka…’akasema docta, na wakili naye akasema hivyo hivyo.

‘Haiwezekani mtu atoke humu ndani bila ya mtu yoyote humu, kumuona,  docta , wewe na mke wako mlikuwa huku nyuma, karibu na yeye, nakumbuka hata wakati tunaendelea na hilo zoezi, hususani mke wako ambaye kwa muda mwingi alikuwa amekaa huku nyuma, alikuwa wa mwisho kuja kuangalia tunachokifanya, kwahiyo nina uhakika, yeye atakuwa kamuona huyo kijana akitoka, kwanini tusiwe wakweli, ...’akasema mwenyekiti.

‘Hapana mimi sijamuona akitoka, kiukweli mimi muda mwingi nilikuwa nimegubikwa na mawazo yangu, sikuwa nikimtizama mtu, na hata ningelimuona akitoka ningelijuaje kuwa anatoroka, sikumuona kabisa...sikuwa na haja ya kumuangalia yeye, nina mambo yangu mengi kichwani ya kuangalia, kwanini nihangaike kumchunga yeye, ....akili yangu haipo hapa jamani’akasema huyo mke wa rafiki ya mume wangu, na mwenyekiti akamwangalia kwa mashaka, na kumuuliza

‘Unavyozungumza hivyo hueleweki, ina maana haupo pamoja na sisi hapa kwenye kikao, sasa umefuata nini, ni kweli unaonekana kabisa kama vile haupo ndani ya kikao, upo kimwili lakini kiakili unaonekana haupo kabisa, kuna tatizo gani linalokukabili?’ akauliza mwenyekiti.

‘Haya ni ya kwangu, niachieni mimi mwenyewe, kama ikibidi Itafika muda wake, mtayafahamu, ....mimi naona tuendelee na kikao, huyo muachieni polisi hao ndio kazi yao....’akasema huyo mke, na mimi nikaona niingilie kati nikasema;

‘Baba , hilo la kutoroka kwa shemeji yangu, tuwaachie polisi wakiuliza tutawaambia ukweli, sisi sio walinzi wa huyo mtu na sisi hatutawaficha ukweli,ni kuwa huyu mtu alikuja kwenye hiki kikao  na baadaye akatoroka,sisi tungelifanyaje...’nikasema

‘Hilo unalitamka tu kirahisi bila kujali kuwa mimi ndiye niliyemdhamini,  hivi kweli kuna mtu atakuamini ukisema hivyo, hivi nyie taifa la leo mna nini akilini mwenu, msipende kuchukulia mambo kirahisi tu, kitendo kama hiki kinatutia dosari, uamanifu wetu unapungua,..'akafoka mzee.

‘Ni kweli baba, lakini imeshatokea swala ni tufanye nini…’nikasema

'Kiukweli mimi sipendi kabisa tabia ya namna hiyo...unapoahidi kitu, unatakiwa ukitimize, ...mimi sio tabia yangu ya kukubali dhamana halafu ninakuja kuihini,mnaniharibia mwenendo na tabia yangu..’akasema mwenyekiti na kuanza kupigia simu, alikuwa akiwapigia watu wa usalama, akaongea na huyo mtu wa usalama, na kumuelezea ilivyokuwa na alipomaliza kuongea naye akasema

‘Sawa tuendelee, wanamfuatilia wao wenyewe kwasasa, ila imewakwaza sana, kwani hatukutimiza wajibu wetu,…sasa wewe kaka mtu, mdogo wako keshaharibu, hata kama tulitaka kumsaidia, sasa haitawezekana tena,.., keshajiharibia yeye mwenyewe kabisa, ...’akasema

*********

‘Kwanini mnamfanyia hivyo mdogo wangu,kwani ungekaa kimiya unafikiri hao polisi wangekuja kukuuliza, nyie mnajipendekeza tu kwa hao watu, lakini hawatawasaidia lolote, siku yako ikifika wanakusweka ndani kama hawakujui…’ akasema  mume wangu, na hapo nikakumbuka jinsi alivyomnong'oneza kitu muda uliopita

‘Hiyo ndio tabia ambayo siitaki, na hilo nimekuwa nikiwakanya, ....kama umezoea tabia hiyo ya uwongo, mimi kwangu haipo, na kwanini unasema tumemfanya nini mdogo wako, hakuna aliyemfanya kitu mdogo wako, unajua mimi nilipanga nini akilini mwangu…’akasema mwenyekiti

‘Nilishakuwa na malengo ya kumsaidia, nilitaka tukitoka hapa mimi na yeye mguu kwa mguu hadi kwa hao watu kuona yeye ana hatia gani,....sasa sisi tushatimiza wajibu wetu kama raia wema, ....’akasema mwenyekiti.

‘Mdogo wangu hana hatia yoyote…,yeye sio mhalafu...polisi wanamshuku bure,wameshindwa kazi yao sasa wanapapatika...na huenda kaondoka hapa kutokana na vitisho vyenu, sasa mimi nasema hivi, kama litamkuta baya nyie ndio mtawajibika...’akasema mume wangu.

‘Tuendelee na kikao chetu, atawajibika yeye mwenyewe. Na wewe mkwe…, nakuonya, sasa sitaki utani,tuambie, imekuwaje, ukawa na mkataba tofauti na ule mliokubaliana na mke wako, na ukijua kuwa huo ni ukiukwaji wa sheria,umekiuka kiapo chako ulichokiweka kisheria wewe na mke wako, ndivyo unavyoishi hivyo,...?’ akauliza mwenyekiti.

‘Mimi sijui kama huo mkataba ni tofauti na ule tuliokubalina na mke wangu, kwangu mimi nauona ni ule ule,na kama nilivyowataka, japokuwa msajili kasema hivyo, nahisi na yeye kaongea tu bila ya kuuangalia mkataba huu nilio nao…’akasema akiwa sasa kaushika huko mkataba.

‘Mkataba huo ni ushahidi tosha kuonyesha jinsi ulivyo…’akasema mwenyekiti.

‘Ni ushahid wa nini, mimi sijui kama upo tofauti na huo wanaosema ni halali, kama wlaiona kuna tofauto hiyo kwanini hawakuniita mimi, mimi ndiye mume, niye ninayefahamu ukweli wa huo mkataba, sasa kama kuna tofauti mimi kiukweli  sijui...na hiyo tofauti imetoka wapi?’ akauliza mume wangu.

‘Unamuuliza nani hilo swali, hilo swali tunakuuliza wewe, kama sio wewe, na kama hujui wakati wewe umekiri hapa kuwa wewe ni mume na wewe ndiye unayebeba dhamana za familia, haya tuambie ni nani aliyeugushi huo mkataba, kwanini kunapatikana mikataba miwili, huu mkataba ulio nao unatoka wapi, hayo ni maswali yako ya kujibu...’akasema mwenyekiti.

‘Hayo nimeshawajibu, sijui...ninachojua ni kuwa huu mkataba ndio halali.....na kama sio halali mimi sijui, kwangu mimi hadi sasa bado sijaamini kuwa kuna mikataba miwili, mimi sijui..’akasema na watu wakamwangalia kwa mashaka, na alipoona watu wanamwangalia yeye, akasema;

‘Kama ni hivyo, hebu tuuone huo mkataba mnaosema ni halali?’ akauliza

‘Umeshaonyeshwa na msajili wataka upi tena, eeh, usitusumbue  .....’akasema mwenyekiti

‘Mke wangu kasema anao mkataba anayo nakala halali ya huo mkataba, kama anavyodai yeye,…nataka anionyeshe tofauti iliyopo kati ya mkataba huo na nakala hii niliyo nayo hapa....’akasema

‘Mimi naona lengo lako ni kutupotezea muda, hebu mke wa familia mtolee huo mkataba, anaoutaka yeye, na kwa amri ya kikao hiki, halali, tunataka ujibue maswali yetu, kwani kila ulichokitaka umekipata, kwahiyo timiza wajibu wako, sisi tumeshatimiza wajibu wetu....’akasema mwenyekiti.

Mume wangu akanigeukia, huku akionyesha kushangaa, pale aliponiona nikitoa mkataba kwenye mkoba wangu, nikauinua juu, na kusema;

‘Mkataba halali ndio huu hapa, mkataba ambao umeuulizia ndio huu hapa, hii ni nakala yangu...’nikasema na yeye akabakia mdomo wazi, akiwa katoa macho ya kutokuamini.

‘U-ulipatia wapi …haiwezekani…’akasema kwa kigugumizi

‘Mpe wakili wenu wa familia authibitishe kuwa ndio wenyewe,..’akasema mwenyekiti, na mimi nikainuka na kwenda kumkabidhi wakili wa familia ambaye aliufunua akaanza kuukagua na kufanya kama alivyofanya kwenye mkataba aliokuwa na mume wangu, halafu akatabasamu na kuuliza;

‘Umeipatia wapi hi nakala, ndio wenyewe kabisa, sasa mambo yamekwisha, tumemaliza kazi...’akasema kwa furaha.

‘Siamini ina maana mke wangu umeamua kunifanyia hivyo, ...ina maana ..haiwezekani, kumbe,..hapana,....umaupata wapi huo mkataba, uli...uli...oh, huyu mdogo wangu yupo wapi’akasema huku akiwa kashika kichwa.

‘Haya mume wa familia, sasa kazi inaanza, natumai sasa upo tayari, kuwajibika kama ulivyoahidi wewe mwenyewe,…hatuna muda wa kupoteza tena..,kama wenzako wamekusaliti, utakwenda kuwauliza baadaye, sasa hivi ni kazi ...jibu swali letu, kama ningelikuwa mimi ndio wewe ningekiri makosa na kukubali yaishe, maana mwisho wa hadaa ni fedheha, kwanini unataka ufedheheke’akasema mwenyekiti.

‘Swali gani,...sikumbuki kama uliniuliza swali...’akasema

‘Nilikuuliza kuwa kwanini huo mkataba uliokuwa nao ni tofauti na mkataba halali, tunahitaji kulitambua hilo, kama wanafamilia, kama wajumbe wa kikao hiki, na ikibidi pia sheria inatakuhitajia uilezee kwani wao bado wanatafuta kiini cha hilo tatizo, ilikuwaje kuwepo na mikataba miwili,..’akasema mwenyekiti.

‘Ndugu mwenyekiti, mimi muda mwingi nilikuwa naumwa, na siwezi kujua jinsi gani huo mkataba ulivyobadilika, mimi hadi sasa sioni tofauti yake, sijaona hayo mabadiliko ni yapi...’akajitetea hivyo.

‘Kwahiyo bado hutaki kukiri kuwa kuna hujuma mlipanga, kuwa mlifanya kosa, kwahiyo kama wanafamilia, kama kikao tukufikirieje, unaonekana unatujaribu, unatuona sisi hatuna akili?’ akauliza mwenyekiti.

‘Sijasema hamna akili, lakini siwezi kusema mimi nimefanya hujuma, nikiri kosa ambalo sijalifanya, hilo halipo,kwani kama ni  hujuma iliyofanywa mimi siijui, huenda kuna watu walifanya hivyo, bila ya mimi kufahamu….’akasema

Ni nani zaidi yako wewe ambaaye ni muhusika, na wewe ulianza kutimiza yaliyoandikwa kwenye hiyo katiba tofauti na ile ya kwanza, unafikiri sisi ni watoto wadogo au…’akaambiwa

‘Ninachoongea hapa ndio ukweli, kuwa kipindi hicho nilikuwa mgonjwa, yote haya yamefanyika, nilipopata ajali, ndio maana nimekuwa niking’ang’ania kuwa hiyo katiba ndiyo ile katiba niliyo kuwa awali na ndiyo iliyokuwa sahihi, mimi sikumbuki kuwa na katiba nyingine tofauti..mnakumbuka kuwa ajali hiyo ilinifanya niwe nasahau...’akajitetea.

Kukawa na ukimia kidogo

***********

‘Lakini kama sikosei, katiba hiyo inavyoonyesha ilibalidilishwa kipindi wewe hujapata ajali, ina maana mipango hiyo mliipanga mapema, na mlikuwa mkiifanyia kazi hatua kwa hatua,, na ajali hiyo ilipotokea mkapata sababu nyingine, na hiyo ajali ilitokea mkiwa kwenye michakato yenu ya kukamilisha hiyo hujuma....’akasema mwenyekiti.

‘Ulikuwa unawahi kufanya jambo, bahati mbaya ajali ikakukuta njiani…’akaambiwa

‘Mimi hayo siyajui, nayasikia kutoka kwenu, na kwa jinsi inavyokwenda hapa sasa, mimi naona nimuite wakili wangu, kwasababu mnataka kunitia hatiani, na mimi sitaweza kujitetea kwa hali kama hii, ni lazima mwanasheria wangu awepo...’akasema

‘Hatujafika huko, ikifika huko ikibid tutakupa nafasi hiyo, lakini bado tunakuhitajia wewe uwe mkweli kwetu, unasikia,…’akaambiwa

‘Hata nikisema ukweli ni nani ananiamini kwasasa..hakuna nyote mumeshaniona mimi ni mkosaji..nimekosa nini,…eeh, sasa ili na mimi niwe na amani, nataka hili swala liende kisheria, awepo hakimu wangu hapa…’akasema

‘Kwahiyo wewe, sasa unarudi kule kule, kuwa hili swala kwa vile ni la kisheria zaidi, na linaonekana ni kuvunjwa kwa sheria, kama alivyopendekeza awali wakili, tulipeleke kisheria zaidi, ikibid twende ngazi za juu, tulipeleke hili swala mahakamani, si ndivyo unavyotaka wewe..’akaulizwa

‘Sijasema twende mahakamani, ...sio lazima twende mhakamani, hapa tuna mawakili wenu, lakini hatupo mahakamani, hawa mawakili hawanitetei mimi, wanatetea nafsi zenu , matakwa yenu, mkinisakama mimi wao wataangalia jinsi gani y akunibana mimi kisheria wajuavyo wao,.. basi ngoja ni mimi nimuite wakili wangu ili naye aangalie upande wangu.....’akasema.

‘Hakuna anayekusakama wewe, wewe ndiye uneyeweka kwenye mazingira ya kuonekana hivyo, kama ungelikubali kusema ukweli, haya yote yasingelitokea, kwanini usikubali kuwa kuna shetani aliwapitia, mkaamua kupanga hayo mliyoyafanya, lakini kwa vile dhamira mbaya haijengi, basi imefika kikomo,kubali, tuangalie jinsi gani tutalimaliza hili tatizo...’nikasema.

‘Wewe mke wangu hujui tu, mimi nayafanya haya kwa masilahi ya familia yetu, hapa nafanya kila iwezavyo kuulinda ndoa yangu, wenzako wanataka ivunjike, hili lipo siku nyingi, kama kweli unanipenda, ulitakiwa uwe pamoja na mimi....huoni kuwa wamenitega,...lakini nawaambia hivi hata kama mke wangu haupo na mimi bado wewe ni mke wangu,...’akasema.

‘Sikuelewei ukitaja neno kupenda,....’nikasema.

‘Unaona, nilijua kabisa mnanitega, wewe na familai yenu, mumelipanga hili makusudi,na kwa vile umeshaona mumefanikiwa mipango yako, sasa unatafuta njia za kuniharibu kabisa maisha yangu, mimi sikubali....na kwa hilo la kukubali kuwa nimefanya kosa, mimi hadi hapo sioni kosa langu kabisa, mimi kauli yangu ni hiyo kuwa sijui kama hiyo katiba iligushiwa, na hiyo mipango mnayosema nyie mimi siifahamu, ni nani walifanya hayo nyie ndio mnaofahamu, sio mimi, kwanini mnanilazimisha niseme uwongo.’akasema.

‘Kwahiyo unataka tulitolee ushahidi kama hilo la hiyo katiba kuwa sio katiba halali, ujue kila tutakavyofanya hivyo ndivyo na sisi tunashindwa kukuamini tena, na hapo ina maana kuwa wewe haupo nasi..unajiweka mbali na sisi, unaikimbia ndoa yako kiujanja, huku unajifanya upo nayo’akasema mwenyekiti.

‘Tangu hapo naona mumeshaniweka pembeni, sizani kwenye nafsini mwenu mpo na mimi tena, mumeshaniweka kwenye kundi la wahalaifu, unaona mdogo wangu ambaye hana kosa mumeshamuitia polisi, na nahisi hata mimi mtanifanyia hivyo hivyo,niwaulize kama angelikuwa ndugu yenu wa damu awe anatafutwa na polisi, mngelimfanyia hivyo mnavyomfanyia ndugu yangu,au kwa vile sio ndugu yenu?’ akauliza

‘Huo ni unyonge unaojitakia, nimeshakuambia, wewe kama mume wa familia unatakiwa upambane kiume, lakini katika misingi ya ukweli na haki, hiyo kauli yako uliyoongea sasa hivi kuwa tunakuonea wewe na ndugu yako, ni kauli ya kujizalilisha, kujishusha, ni unyonge wako mwenyewe,  ...ongea ukweli, toa hoja zenye mshiko, tuoni ukweli upo wapi,...’akasema mwenyekiti.

‘Ukwelii gani nitakaouongea sasa hivi mniamini, mimi sijajizalilisha, ndio maana ninaendelea kukataa hayo mnayonishinikiza nayo, haya nipeni huo ushahidi kuwa mimi nilikuwepo kwenye huo mpango wa kufanya hayo yaliyotokea...maana ndivyo mnavyotaka nyie, mimi nimeshawambia ukweli wangu, hamunikubalii, sasa kwa vile mnaona nasema uwongo, nikosoeni kwa kulibainisha hilo...’akasema kwa kujiamini.

‘Kwa hali hiyo ni kuwa hutaki kusema ukweli, unataka sisi tuutafute kwa nguvu za ushahidi, ..kama unataka iwe hivyo, sisi tutafanya, lakini kwa mtaji huo ni kuwa wewe hutaki kushirikiana nasi, hutaki kuwa mwenzetu, ukatusaidia tukalimaliza hili tatizo kama wanandugu....na kwa hali hiyo ikibainika na ndivyo ilivyo, tukatoa ushahidi, basi hatuna jinsi nyingine, hukumu itafuatia kitanzi chenu wenyewe kitakuhukumu.’akasema mwenyekiti.

‘Kwahiyo nyie mnataka mimi niseme nini?’ akauliza

‘Sema yote yaliyotokea, jinsi gani mlivyoibadili hiyo katiba, na kwanini ,lifanya hivyo. Na mlikuwa na nani na nani, halafu unaomba msamaha yamekwisha,...sisi kama kikao tutakaa na kuangalia jinsi gani ya kulimaliza... huo ndio uadilifu na utawala bora, kwanini mnataka msutane kwanza, mshikane mashati, hata ifikie damu kumwagika, ...hiyo ni tabia ya watu wasio waungwana’akasema mwenyekiti.

‘Mimi sio mtoto mdogo, wa kudanganywa kihivyo, nawafahamu sana, hapo mnataka kunitega tena, kama mlivyonitega hapo mwanzo, ...ukweli niliouongea ni huo huo, kama kuna ukweli mwingine niambieni nyie, na mnithibitishie na mimi kama nitaona kuna ukwel ambao niliusahau ,au nilikuwa siujui, maana mengi yametokea nikiwa mgonjwa, sikumbuki, nikumbusheni nyie,....’akasema

‘Na ikiwa ni hivyo, tukakuthibitishia kuwa ni mpango ilipangwa na wewe ukiwemo ukiwa na akili zako timamu, ukishirikiana na wenzako, kwa ajili ya masilahi fulani, ..  upo tayari kuwajibika?’ akaulizwa

‘Hiyo ni juu yenu...lakini mimi sijui kama kulikuwa na mipango huyo, mimi sikumbuki....’akasema.

‘Unakumbuka sana, unalifahmu sana, ndugu mwenyekiti naona tunapoteza muda, huyo mtu nimeshamuelewa, ...anachotaka ni kuona je tunafaamu hiyo mipango yao, je tunafahamu hayo aliyoyafanya yanajulikana,...hataweza kukubali na kusema ukweli...mimi naona tuendelee na kikao, na hatima ijulikane, mkataba upo utafanya kazi yake...’nikasema.

‘Kutokana na uchungzi uliofanyika, inabainisha wazi kuwa mipango hiyo ilikuwepo kabla ya wewe hujapata ajali, ...watu wanaohifadhi hiyo mikataba, wamelibainisha hilo, na hata huyo mtu mliyeingia naye kwenye hilo kosa, baada ya kubanwa, na baada ya uchunguzi alikuja kusema kila kitu. Hata kama kulikuwa na shinikizo lakini ndani yake kulikuwa na mbinu zenu....’akasema mwenyekiti.

‘Mimi hayo sijui....sikumbuki, kama nilivyowaambia ninachojua mimi , hii ndio katiba, niliwahi kuwekeana na mke wangu,kama kulitokea kubadilishwa, basi labda kuna mtu alifanya hivyo, akanitumia mimi kama chambo, kwa vile anafahamu kuwa kumbukumbu zangu hazikiwa sawa...’akasema

‘Alikutumia kwa msilahi ya nani, yake au ya kwako, hebu tuangalie hiyo katiba, tutakuja kuiangali vipengele mlivyobadilisha, vilikuwa vinamgusa nani, na kwa masilahi ya nani, na hapo mengi yatagundilikana,  kwahiyo ndugu yangu,...usitudanganye hapa, na kama unahisi hivyo kuwa labda kulikuwa na mtu kafanya hivyo kukutumia wewe, basi tuambie ni nani huyo mtu...’nikasema.

‘Ni kwa masilahi ya familia yangu, mimi na wewe na watoto wetu…, ukiangalia hiyo katiba eeh , nilivyoisoma mimi,  inatuhusu mimi na wewe mkwe wangu, na ya kwamba hakuna mtu mwingine wa kuingilia masilahi yetu, zaidi ni mimi na wewe, kuilinda ndoa yetu , watoto wetu na familia yetu kwa ujumla....’akasema

‘Ni ile ya mwanzoni ilikuwa haifanyi hivyo?’ nikamuuliza

‘Mimi sijui hiyo katiba ya mwanzoni ilikuwa inasemaje, sikumbuki, kwani ninachofahamu mimi ni jinsi nilivyosoma kwenye katiba hii, labda nyie mnikumbushe ..’akasema.

Mwenyekiti akamtizama binti yake, na kutikisa kichwa, kama kusikitika, na wajumbe wengine kwenye kikao wakaonekana kuchoka, na hapo mwenyekiti akasema;

‘Naona tupate mapumziko kidogo, tukirudi tunaingia ajenda nyingine, sasa tukitumia katiba halali, mliyojiwekea nyie wenyewe, si ndivyo uliahidi mjumbe, mume wa familia, hakuna kurudi nyuma kwa hilo…’akasema mwenyekiti

Mume wa familia akabakia kimia

‘Tulishajua mbinu zenu, na huu ujanja wenu sijui mlifikiri hamtapatikana, na hapakwenye kikao, limeshafahamika, kuwa baada ya ajali, kuna muendelezo wa mambo mengi, ajali hiyo ilitumiwa kufanikisha mambo mengi, ni kama ilipangwa…’akasema mwenyekiti

‘Ilipangwa…!!’ akasema mume wangu kwa kushangaa.

‘Ni kweli baada ya hiyo ajali, wewe ulipoteza kumbukumbu, na mengi yalifanyika kipindi hicho, ...huenda ilichukuliwa hivyo kama mwanya wa kukamlisha huo mpango, mpango ulikuwa umepangwa kabla ya hiyo ajali, ...’akasema mwenyekiti

‘Kwahiyo unamaanisha kuwa kwenye huo mpango tulipanga mimi nipate ajali, ili baadaye nisingizie kupotewa na fahamu,yafanyike kama yalivyotokea ...hivi kweli kuna mtu mwenye akili zake  anaweza kufanya jambo kama hilo la hatari, ina maana hata hawo madakitari walionihudumia  wanahusika na huo mnao-uita mpango, maana wao wanajua fika kuwa nilipotewa na fahamu , na kupoteza kumbukumbu kwasababu ya hiyo ajali.....?’akasema mume wangu.

‘Hatukatai kuwa kutokana na hiyo ajali ulipoteza kumbukumbu na hali hiyo akasababisha wewe kutokukumbuka mambo ya nyuma, lakini hiyo kwa mtizamo wenu,na uchunguzi wetu hali hiyo ilikuwa imetokea  kwa muda fulani tu, ambao kitalamu inajulikana, ...wewe ukauendeelza ule muda, na kuendelea kujifanya kuwa bado unaumwa, ili kutimiliza malengo yenu....’nikasema.

‘Hivi kweli mke wangu unaweza kusema maneno kama hayo, naona kweli umenichoka, sikujua kama utafiki hatua hiyo, ....kuna nini kibaya nilichokufanyia ambacho kimeweza kukugeuza na kunichukia kiasi hicho…?’ akauliza mume mtu.

‘Hakuna aliyekuchukia ni matendo yako yanatufanye tuwe hivyo, na kwanini hutaki kukiri kosa…’nikasema

‘Nikiri kosa , kosa lipi,..huo ni mtego wenu,..mtego ambao wazazi wako wanausubiria,…kwanini  mimi nisingizie ugonjwa, mke wangu, kuwa naumwa na uzidi kuteseka, ili iweje, hapana, siwezi kukufanyia hivyo, hizo ni hisia umepandikiziwa, usiwasikilize watu wasioitakia mema ndoa yetu....’akasema.

‘Mjumbe, usitusingizie sisi wazazi, hilo ni lenu wawili,…mimi huwezi kunidanganya kitu,nakufahamu sana, usijifanye kuwa hayo yaliyotokea huyafahamu, nakufahamu na washirika wako wote nawafahamu…,mimi nilitaka kuona kuwa kweli labda umebadilika kama alivyokuwa akidai mke wako, lakini kwa haya uliyoyaonyesha leo, sioni ajabu ....lakini haya bado tuendelee kukupatia nafasi nyingine ya mwisho..ila kwangu mimi nataka kusikia ulivyofanya hayo, na kwanini…ukiyaeleza kiunaga ubaga, nitajua kweli umekiri kosa na hukumu itabakia kwa wajumbe….’akasema mwenyekiti.

‘Mimi sielewi hapo…ina maana baba mimi nijifanyize ajali, nijifanyize ugonjwa, hapana , hiyo sio kauli nzuri kutoka kwa wazazi…’akasema

‘Ajali iliyokupata, ilichukuliwa kama nafasi nzuri ya kufanikisha malengo yenu, na huenda kulikuwa na hujuma kwenye gari lako, hicho kitu utakuja kupambana nacho kwenye taarifa ya polisi ambayo haijawekwa wazi,..ajali hiyo...ilipangwa makusudi, ili itokee, ....’akasema mwenyekiti na mume wangu akamuangalia mwenyekiti kwa jicho la kushangaa…

‘Lakini hilo halikuweza kuthibitishwa,…kuna kitu kilitakiwa kifanyike, muulize mke wako aseme ukweli…atakuja kuyaelezea hayo yote kama kweli anataka kuelezea ilivyokuwa, hatujasikia alichopanga kuelezea,..wewe ndio umevuruga utaratibu…’akasema mwenyekiti

‘Unasema nilipanga ajali, baba ni kweli uanongea jambo kama hilo…na mke wangu unabakia kimia, ndivyo mlivyoongea hivyo..’akauliza

‘Inavyoonekana ndivyo..hata polis waliliona hilo, japokuwa halina nguvu, na mimi nikawaoba wasiliongelee maana ni hisia labda ..labda..na vielelezo, inavyoonekana ilitakiwa mimi ndio nije kupata ajali na hiyo gari,… nia ni mimi nife , kwani siku hiyo kama unakumbuka vyema nilikuomba gari lako, nilitumie mimi,....lakini kwa bahati , ukalichukua wewe mwenyewe, sijui ni kwa kusahahu au ilikuwaje, mimi hapo ndio sijui, ndio maana nikawaomba polis waliache hilo kama lilivyo....’nikasema

‘Huo ni uwongo wa hali ya juu, mimi nipange kukua wewe halafu unakubali huo uzushi, kwanini nifanye hivyo...’akasema mume wangu.

‘Hiyo ajali ilipotokea, ikawa imefanikisha baaadhi ya mambo yenu,hata kama utakataa kuwa hiyo ajali ilipangwa, kwa nia ya kumuua binti yangu, na iliposhindikana lengo lake hilo, ikageuzwa, ikachukuliwa kuwezesha mambo mengi,mengi yalifanyofanyika yalifanyika  baada ya hiyo ajali, ili usiwepo nyumbani, ili isionekane kuwa wewe unahusika, ...’akasema mwenyekiti na mume wangu akatikisa kichwa kukataa.

‘Kiukweli hii ni kashfa ..mnanikashfu..na sitaweza kuvumilia hili..hiyo kauli yenu inanisikitisha sana…kiukweli siwafichi, imeniuma..na sijui kama nitaweza kuwaamini tena, sawa…ila nitataka hili mlithibitishe,la sivyo..hata sijui..’akasema

‘Kwa vile tumeongea sana na huu ni muda wa kupumzika, ...hiki kikao kinakupa nafasi ya mwisho, ya kufikiria kwa makini..., tukirudi uje na ukweli, kama utaendelea kutuficha huo ukweli ambao sisi tumeshaujua, kikao, kitakuchukulia wewe kama mhalifu ambaye kafanya kosa, lakini hataki kukiri kosa, na hivyo, unatuweka katika nafasi ya kutengeneza kesi, na yote mengine yatabainishwa, na hapo hatutakuwa na kurudi nyuma tena…’akaambiwa

‘Kesi ya nani,..ni nani mhalafu hapa..kuwa nilipanga kumuua mke wangu au…?’ akauliza

‘Ni kesi dhidi yako ndio…kudanganya , kugushi…na mengineo, yatakuja kujitokeza kama hutakubali kusema ukweli tukamaliza na mengine yakamezwa, sisi ni wanadamu, tutaangalia utu,…sasa kaam wewe hutujali, tufanyeje, kama hujijali familia yako, tufanyeje....’akasema mwenyekiti.

‘Hata siwaelezi…mimi nimeshasema yote haya,…ni kwa ajili ya familia, yangu, ndoa yangu, na watoto wangu, hata hiyo katiba imenipa mamlaka hayo,…sasa jaman kichwa kinauma…’akasema mume wangu, akishika mkataba wake mkononi, kama anataka kuondoka.

‘Sasa tukapumzike kidogo, nafahamu bado kuna ajenda nyingi, zenye maswali mengi yanayohitajai majibu mengi, wajumbe hapa wana yao mengi tu…, na yote ni dhidi yako wewe…au nyie wanandoa wawili.., na moja wapo jingine ni kuhusu kifo cha makabrasha,..hili linaanzia ni kwanini ulimuacha wakili wenu wa kawaida ukaamua kumtumia Makabrasha, kifo chake kimeanzia hapo, sasa jipange na hilo…’akaambiwa

‘Hahaha mnataka kusema mimi ndiye nilipanga hili pia, ili auwawe, hapo sasa mumevuka mpaka, hilo, nipo tayari, hata makamani…’akasema

‘Ni katika kuweka haya mambo sawa, kabla hatujaenda kumpumzika, hebu kwanza niambie ulikosa mawakili wa maana, mpaka uamue kumchukua Marehemu, eeh, kila mtu anajiuliza hilo…’akasema mwenyekiti

‘Yeye ni wakili mbona anatambulikana kisheria, mimi sijui kosa lake…’akasema

‘Nasikia , sio nasikia , ndivyo ilivyokuwa, kumbe marehemu ndiye alikuwa kichwa chenu akisemacho ni lazima mkifuate..na uliamua kumchukua kabisa sasa awe wakili wako ili kubadilisha hiyo katiba, lakini baada ya hilo, yeye naye akakugeuka, na ndipo kifo chake kikatengenezwa,…hahaha, mjumbe hili unalo, sisi tutamalizana na wewe lakini una kesi ya kujibu, haya hilo tutakuja kuliongea badae!’ Akasema mwenyekiti na kumfanya mume wangu amuangalie mwenyekiti kwa uso uliokunjamana kwa hasira

‘Sio kweli mwenyekiti, ninapinga hizo shutuma zote…’akasema mume wangu kwa sauti kubwa.

‘Tumeshachunguza na kuligundua hilo, …baada ya kugundua wewe umefanya makosa makubwa ya kukufanya uvunje ndoa ukose kila kitu,  maana dhamira yako ni mali, hakuna zaidi…vingine ni visingizio…ukaona njia ya kulikwepa hilo ni katiba…mikakati ikapangwa jinsi gani ya kubadili katiba, marehemu akakuambia hiyo ni kazi rahisi kwake...’akasema mwenyekiti na mume wangu akawa kainama chini.

‘Marehemu anatambulikana kwa uhalifu wake wa milungula, wenzetu huko majuu, wanaita blackmail. Yeye kwasababu alisoma soma huko nje, akaona kwa wabongo, hawana ufahamu sana na mambo hayo, basi anaweza kuutumia njia hiyo kujitajirisha, hapa kwetu...’akasema mwenyekiti

‘Kosa kubwa linalobainsiha mipango yako, ni huko kumtumia Makabrasha, ni kwanini umchukue yeye,… lakini hukujua kuwa unamfuga nyoka, ili akulinde, wakati yeye ana sumu,, sasakwanini usituambie ukweli,ili tuweze kuliweka hili jambo sawa,...tutahitajai majibu yako, ili tukusaidie, kama hutaki, haya tutaona mbio za sakafuni huishia wapi..hilo...tukirudi,...usikimbie kama mdogo wako..’akasema mwenyekiti, na mume wangu akasema;

‘Makabrasha ni rafiki yangu wa siku nyingi, kumtumia yeye, kwangu sio jambo la ajabu sana, hilo naweza kulithibitisha popote pale, waulizeni hata familia yake,.. na mengi anasingiziwa tu, mimi sipendi kumuongelea marehemu, lakini nitajitetea kwa nafasi yangu, na kumtetea yeye ikibidi,lakini mimi sitapenda kumuongelea yeye sana, maana hayupo duniani,…’akasema

‘Sawa tutaliongea hilo baadae…kila kitu kipo tayari, ushahidi wote upo, ukikana huo ushahidi tunauwakilisha polisi, wao watajua jinsi gani ya kukufanya, hapo hatutakuwa na lawama tena ..’akasema mwenyekiti

‘Vyovyote iwavyo, mimi sikubali kuivunja ndoa yangu…’akasema

‘Tutaona hilo tukirudi, kama nikuivunja ndoa yako utakuwa umeivunja ndoa yako wewe mwenyewe,…muda umekwenda jamani…mnasemaje, tukapumzike kidogo halafu tutarejea, au vipi docta… ’akasema mwenyekiti,..na watu wakasimama na kunza kutoka nje

************.

 Mume wangu badala ya kutoka nje akanizonga,

‘Wewe mke wangu haya umeyasababisha wewe, sasa nakuambia hivi hata ufanye nini, ndoa haivunjiki…si ndioengo lenu hilo…sasa ndoa itabakia hivyo hivyo, ili tuone mwisho wake…’akasema

‘Kwanini hutaki kusema ukweli tukayamaliza haya mambo..?’ nikamuuliza

‘Tungeyamaliza tukiwa sisi wawili kulikuwa na kosa gani, kulikuwa na haja gani ya kuita watu hapam kuanza kuumbuana na kunitwika makosa ambayo sio ya kweli..?’ akauliza

‘Hilo la kuita watu bado kabisa, sijaliongelea,…huo ni mwanzo tu…maana umesaidia kuweka mambo mengine sawa, kushinikiza kwako kwanza tuongelee mkataba umenisaidia sana, sasa tutaingia kwenye kadhia yenye, ni kwanini nikaitisha hiki kikao, jiandae kwa hilo, mume wangu nimekupa muda wa kutosha umeshindwa kuutumia, nimeshajua lengo lako, sasa kabla hujaniwahi, naona kila mtu alifahamu hilo…’nikasema

‘Hahaha, mke wangu, unafikiri mimi naogopa, utaona..hata kama hilo mumepanga wewe na baba yako, au sio mimi halinitishi kwani wewe unajua mangapi yako ninayafahamu tu,...wewe na rafiki yako mlijadili nini..hilo hutaki lisikiwe na watu, eeh,…na na hapo nakupa angalizo tu,…na jingine nikuambia ukweli, hakuna mwenye uwezo wa kuvunja ndoa yangu, hakuna..…wanasahau kuwa ndona inavunjwa na mume…’akasema.

‘Kwanini unatetea kitu ambacho hakipo, au hulijui hilo..kiimani, kisheria..wewe kwa vitendo vyako ulivyovifanya, ulishaivunja ndoa yako wewe mwenyewe, bado unashikilia kuwa ndoa ipo ndoa ipo,  hebu niambie,  ina maana gani kung’ang’ania kuwa ndoa ipo na wakati matendo yako yanaikana, una watoto wangapi nje,..eh, kauli zako za kuikana ndoa, umeziongea mara ngapo kwa hao mahawara wako, eeh,....’nikasema

‘Haya ongea tu..utaongea mengi,lakini na mimi utanipa nafasi ya kuongea mengi, nasubiria hio nafasi,…na kuvunja ndoa ni kutoa talaka, ni nani alitoa talaka …wapi nilikutolea tamko kuwa nimekupa talaka,..wapi kwa maandishi gani, acha wewe…huo mkataba uliubuni wewe, haya kama uliubuni wewe ndio mimi nimetoa talaka, humpati mtu hapa…ndoa haivunjiki …hata wafanye nini..’akasema kwa kujiamini kabisa.

‘Ndio ni mkataba…ulishatamka kama ukifanya hili na lile basi ndoa haipo, hukutamka kwenye kile kikao, mbele ya wakili, au hilo umelisahau,…hujazaa nje,…au hilo utalikana, utamkana mtoto wako, huo sio ushahidi yote haya yameandikwa waziwazi, hata ukisema ni mimi nimeubuni huo mkataba, lakini kauli zako je…mume wangu tuliza kichwa, kuwa mkweli, ongea ukweli tuyamalize haya…’nikasema

‘Hahaha..mke wangu, tatizo wewe hujui kuwa mimi nina mambo yako mengi tu, mimi sitaki kusema sana maana wewe ni mkwe wangu nitakulinda wewe na familia yangu…hilo nimeahidi…’akasema

Mara baba akaingia, yeye alishatonga nje akiwa anaongea na simu, na alipotuona tunazozana na mume wangu akasema;

‘Jamani kuna tatizo lolote...?’ akauliza mwenyekiti

‘Hakuna tatizo tunaongea tu na mke wangu...’akasema mume wangu huku akijaribu kukunjua uso wake.

‘Mimi, nimesema huu ni muda wa mapumziko, tutakutana baada ya nusu saa, mimi natoka, nimeitwa na ofisa upelelezi kituoni , nitarudi, kabla ya muda huo wa kikao, nikirudi nataka tuyamalize haya yote leo, nataka haki itendeke, na kashfa iliyotuama kwenye familia yangu isafishike, kwa amani, na vinginevyo, mimi sitakuwa na lawama tena....’akasema mwenyekiti

Na pale muume wangu akamwangalia baba mkwe wake kwa mashaka, na kusema;

‘Unaona, baba yako anakwenda wapi,....ndio zenu hizo, anakwenda kuwaweka sawa hao watu wake, ..kama mlivyowaweka sawa watu wa kusajili mikataba, lakini hayo hayanitishi mimi…’akasema kwa sauti ndoto ili baba asisikie.

‘Eti baba unasema unakwenda kituoni ni kuhusu shemeji, au kuna nini huko kuonana na mtu wa usalama ..?’ nikauliza

‘Ni kuhusu kesi ya mauaji ya Makabrasha kuna mambo wameyagundulikana zaidi na ni muhimu nifike nionane nao mimi mwenyewe kuhusu pia kutoroka kwa huyu mtu, maana mimi ndiye nilimdhamini, ..ni muhimu..’akasema mwenyekiti

‘Ina maana mdogo wa mume wangu wamempata..?’ nikauliza

‘Sijui, nitalifahamu huko mbele, ila walitaka kuja kumkamata na mume wako, wanahisi anahusika na kutoroka kwake..’akasema

‘Kwanini mimi nihusike…?’ akauliza mume wangu.

‘Kuna kitu umemtuma akakifanye, au …?’akasema mwenyekiti na mume wangu akabakia kimia, na mwenyekiti akaondoka zake.

 Haya tutaona tukirudi mapumziko kama kikao kitaendelea.


WAZO LA LEO: Kuna matendo tunayotenda kila siku hasa kwa wanandoa,  matendo ambayo kiimani, kimila, na kiutaratibu yanakuwa moja kwa moja yameshavunja miiko ya ndoa,…tunavunja mikataba ya yale tuliyokubalina siku ya kufunga harusi,, hata kabla hautajoa kauli zetu.

Kila kitu kina makubaliano na masharti yake, ndoa ina masharti na makubaliano yake, ndio maana ikaitwa ndoa. Je tunafahamu nini maana ya ndoa! Je kama ndoa ni kuhalalisha mahusiano mema kati ya wawili hao, iweje mtu amsaliti mwenzake kwa siri. Mtu anayeisaliti ndoa yake ni sawa na yule mtu  anayeacha nyama yake safi nyumbani na kwenda kula nyuma iliyooza maporini, huyo keshavunja ndoa yake kivitendo,...Tuweni makini  na ndoa zetu.


Ni mimi: emu-three

No comments :