‘Ndugu mwenyekiti, sio kwamba nakataa kusema ukweli, unanifahami
fika kuwa mimi sio mtu wa kusema uwongo, hujanialea hivyo, lakini ninachotaka
kukifanya hapa ni kumpa mwenzetu muda wa kutafakari…’nikasema nikimuangalia
mume wangu
‘Muda gani anahitajia yeye…na hilo sio jukumu lako….’akasema
mwenyekiti.
‘Mwenyekiti nazungumza hilo,..kwa nia njema, ikurejea hali halisi aliyokuwa nayo
awali,…nap engine kuna kitu anakiogopa, mimi ninamuhakikishia kuwa akisema
ukweli, sisi tutamlinda, sisi hapa tupo kama familia, tunachohitajia ni
kusawazisha haya mambo ili tuwe na msimamo wa kifamilia, .....’nikasema.
Mungu wangu aliniangalia huku akiwa keshakunja uso wa
kukasirika,…hakusema kitu na mwenyekiti akasema;
‘Mimi kama mwenyekiti ndiye ninayefahamu ni kitu gani kinakiwa
kifanyike, sioni kwanini uingiwe na kigugumizi kusema ukweli, sisi tumeshampa
muda wa kutosha huyo mume wako,na hata ukimpa siku nzima, inavyoonekana, ni
kuwa hatageuza kauli yake,…’akasema mwenyekiti na kumuangalia mume wangu ambaye
bado alikuwa kimia tu.
‘Kwa jins ninavyomfahamu tutakesha hapa, sasa kama na wewe
unaogopa kusema ukweli kwasababu ni mume wako, basi wote labda enu ni moja,
lakini sisi kama kikao bado tunahitaji jibu lako, ...umenisikia swali langu au
nirudie...?’ akauliza mwenyekiti.
‘Nimelisikia swali lako mwenyekiti, ukweli upo wazi, hii katiba
sio katiba halali, hii katiba imetengezwa upya kwa ku-...’nikaanza kusema na
mume wangu akanikatisha, na kusema;
‘Ina maana hata wewe mke wangu unanisaliti, siamini hilo kabisa,
huoni kuwa umekiuka katiba….’hapo akasita kidogo.
‘Eti jamani, ni wapi ulisikia mke anakuwa kinyume na mume wake,
....hujui ni kosa kubwa, kumkana mume wako, tena mbele ya watu..na kwanini
uukane ukweli,.., hapo umetenda kinyume na maadili ya ndoa,umenikana mimi
mume wako…’akasema huku akitikisa kichwa.
‘Yaani mke wangu unataka mimi nionekanae muongo, hebu angalia hii
katiba, ina makosa gani, hii katiba ni ile ile, kama kuna makosa yamejitokeza,
nilishakuambia tutayaangalia na kuyamaliza kama familia, kwakweli umenivunja
nguvu...’akasema
‘Mume wangu, katiba ipi, unayozungumzia wewe, maana hii sio katiba
yetu halali, sisi tunaitafuta katiba halali, ambayo mimi na wewe tulikubaliana,
na wakili wetu akaipeleka kuisajili,...hadi hapa tulipofikia inaonyesha hii
katiba sio halali, na sisi tunajaribu kukupa muda, ili useme ukweli, na wewe
hutaki kusema ukweli, unaogopa nini kusema ukweli...’nikasema.
‘Mimi sijaogopa kusema ukweli, ukweli ndio huo niliousema na
katiba ninayoitambua mimi ni hii hapa, haya, kama kuna katiba nyingine
unayoifahamu wewe nionyeshe, na iwe imetimia, kisheria,iko wapi hebu
nionyesheni, mbona tunabishana kitu kidogo tu..’akasema.
‘Hilo tu, usiwe na shaka.....’nikasema huku nikitaka kuichukua kwenye
mkoba wangu, ile nakala ya katiba yangu niliyokuwa nayo, lakini kabla sijafanya
lolote mwenyekiti akasema;
‘Mim ndiye mwenyekiti wa hiki kikao, heshimuni taratibu za kikao,
.., na wewe mke wa familia , huwezi kufanya anavyotaka mume wako, mpaka
nikuamuru mimi ufanye hivyo, na ningelipenda kutoa angalizo tena, sitarudia
hilo tena, kama mnataka nitaondoka hapa mtafute mwenyekiti wenu mwingine,
...’akasema mwenyekiti.
‘Sitaki tena kurudia, hili, nataka mfuate taratibu, mimi ndiye
ninyeongoza hki kikao, na ninasema hivi, hili swala huko linapokwenda ni
kubaya, maana kama muhusika mkuu anasema katiba halali ni hiyo ambayo
mwanasheria kasema ni batili, na mwenza wake, ambaye ni mke wake
waliyeshirikiana naye pia kasema katiba hiyo sio halali...yeye bado anaendelea
kusema ndiyo katiba halali, mnataka sisi tufanye nini, nawauliza nyie wajumbe
mliopo hapa, ...’akasema mwenyekiti, wajumbe wakakaa kimia
‘Ndugu mume wa familia, unafahamu hatima ya haya yote, kuwa
sasa hivi tutashindwa kufanya lolote kwasababu kile tunachokitaka kituongoze,
kama ulivyotaka, kinaonekana kina mashaka, eeh, unataka tuongozwe na katiba
batili, tuambie sasa…’akasema mwenyekiti
‘Ulituzia kwa mbwembwe kuwa katiba yenu ni kila kitu, katiba
yenyewe ndio hiyo, je bado unataka ituongoze, hebu tuambie wewe tufanye nini,
tunakuuliza maana muda unakwenda?’ akauliza mwenyekiti.
‘Ndugu mwenyekiti, nikuulize swali tu,..mimi ni nani?’
akauliza swali na watu wakacheka,
'Msicheke jamani, kauliza akiwa na maana yake kubwa,....'akasema
mwenyekiti
'Nataka nijibiwe...'akasema, akiwaangalia wajumbe.
‘Wewe ni mmoja wa wajumbe kwenye kikao hiki, au unauliza kuwa wewe
ni nani kisifa ya ndoa, kama ni hivyo wewe ni mume, wa mkeo....’akasema
mwenyekiti, na wajumbe wakacheka.
‘Au ni mkwe wangu, kwa sifa wanayoitambua hata watu wa magazeti….hasa
ya udaku…’akasema
‘Mimi ni mume wa familia tunayoizungumzia hii leo, na wote
wamjumuika hapa kwa ajili ya hii familia, na kikao hiki kinagusa mambo makubwa
ya familia, sijui kama ndivyo ilivyo maana mke wangu hakuwahi kuniambia…’akasema
‘Sasa mmi kama mume ninaheshima zangu, na moja ya heshima, ni kuwa
mimi ni kiongozi wa hii familia, na kama ni kiongozi, mimi ndiye ninayebeba
majukumu yote ya familia, na kwahiyo mimi ndiye ninayetakiwa kuaminiwa...na
ninachosema ndio msingi, wa familia,....kama hamuniamini mimi, mtamuaminini
nani....’akasema.
‘Sikiliza mume wa familia, ...hapa ni kwenye kikao, na mnapoitisha
kikao, kuna viongozi wanaokiongoza, wewe kama ni mume wa familia, ni kwako
kwenye familia yako, hapa unakuwa mjumbe wa kikao, na unatakiwa kufuata
taratibu za kikao,....kikao kinakutaka useme ukweli, ukisema kinyume chake,
kikao kitakuhoji, ili kijue ni kwanini, na hicho ndicho tulichokifanya…sasa
tuspoteze muda,…, tutahitajai kujua ni kwanini, mkafanya hivyo, ni kwanini
kukawa na katiba mbili tofauti, hii na hiyo ambayo ni sahihi…?’ akauliza
mwenyekiti.
‘Kwahiyo mnataka nisema mnayotaka nyie, kuwa hii sio katiba halali
kuna katiba nyingine halali…maana mimi nimeshausema ukweli wangu, kama mume wa
familia kuwa katiba ni hii hapa, kama kuna katiba nyingine, ya kwenu
mnayoitambua nyie, basi itoeni,...mbona
hiyo katiba nyingine haitolewi,....’akasema.
‘Kabla hatujafanya hivyo, unavyotaka wewe, tunarudia maswali yetu
kwako, ili tuwekane sawa, je kama ikitolewa hiyo katiba ambayo ndiyo halali,
ikathibitishwa hivyo, kuwa ndio katiba halali, upo tayari kuwajibika nayo…?’
akaulizwa
‘Mwenyekiti ni nini maana ya kuhitajia hiyo katiba, usiniulize
maswali ambayo majibu yapo wazi…’akasema
‘Hiki kikao kinataka kauli yako,…maana kwani kwanza utakuwa
umesema uwongo, pili umevunja sheria, tatu, umekaidi kikao ,hapo hatujaingia
kwenye makosa yaliyosababisha kukiitisha hiki kikao, mke wako ana mashitaka, .....je
upo tayari kuwajibika?’akauliza mwenyekiti.
‘Hiyo katiba nyingine ipo wapi, ..hilo ndilo la msingi, kwanini
mnapoteza muda, kama ipo,...’akasema
‘Mhh, mimi ndiye nakuuliza swali, upo tayari kuwajibika..?’
akaulizwa
‘Kuwajibika nipo tayari , lakini kwa katiba ninayoitambua mimi,
katiba iliyosajiliwa kihalali, sio hiyo ya kwenu, …mimi nitaisimamia hii maana
ipo kihalali…’akasema
‘Mhh..jamani huyu mtu tumsaidieje…bodo anadai hii Katiba yake ndio
halali…’akasema mwenyekiti
‘Sio swala la kunisaidia mimi, nasema hivi mimi nipo tayari kuwajibika
kwa katiba yetu halali, inayotambulikana, hata kwa msajili ipo, hiyo yenu
kwanza haipo pili haijasajiliwa, mumeitoa wapi, kama ipo na imesajiliwa mimi
naapa nipo tayari kuwajibika nayo, na nyie mfanye hivyo, kama hii ndiyo
inayotambulikana kwa msajili..’akasema na mdogo wake aliyekuwa kainama akainua
kichwa na kumuangalia kaka yake kwa macho ya mshangao, nahisi kama angelikuwa
karibu angemtuliza kaka yake asiendelee kuongea.
‘Unaona eeh, dalili za watu kama hawo zilivyo, wanaweza hata
kuapa, inasikitisha sana...mke wa familia, umesikia mwenyewe,..sasa usisite
kujibu maswali yetu ukimtegemea mume wako, jibu ukijitegemea wewe mwenyewe,
mwenzako yupo kivyake,....’akasema mwenyekiti.
‘Ndugu mwenyekiti, mimi naona tuendelee, kwani nahisi kuna tatizo,
sizani kama mume yupo sawa, huyu sie yule mume niliyemfahamu mimi, mimi naona
kuna tatizo....mimi nilitarajia mume wangu ungekiri kosa, ili tuweze kuyaweka
haya mambo sawa, lakini naona ana ajenda ya siri, simuelewi tena…’nikasema.
‘Kuna tatizo !!! kwanini mke wangu unasema hivyo… wewe mwenyewe
umekimbilia kwa wazazi wako kuitisha hiki kikao, ni mimi mwenye tatizo au ni
wewe, na kikao kimefikia kunishutumu mimi, kwa vile nipo peke yangu, wako wapi
wazazi wangu, yupo wapi wakili wangu, unahisi ni nani atakuwa upande wangu hapa…’akasema.
‘Swali umeulizwa, upo tayari katiba halali ifanye kazi yake?’
nikamuuliza.
‘Katiba halali ipi, una maana gani ukisema katiba halali, katiba
halali ni ile ipo kwa msajili, nendeni mkawaulize,..mimi nipo tayari,...katiba halali
ifanye kazi yake...mimi siitambui katiba nyingine na kama ipo nyingine ipo
wapi, sasa...’akasema
‘Ndugu mwenyekiti, mume wangu, keshakubali kuwa katiba halali
ifanye kazi yake, mimi ninaomba tuendelee, yeye hataki kuwa mkweli, na kutubu
makosa yake, basi iliyobakia, kikao ndio kitaamua, na sio kikao, katiba hiyo
halali ije ihukumu, basi mimi nimenawa mikono yangu....’nikasema.
‘Namuuliza tena muhusika, kiupendeleo zaidi, je umekiri mwenyewe
kuwa katiba halali ikipatikana, ndiyo itakayoongoza yote hayo
yatakayofuata,ndivyo hivyo ....?’ akauliza mwenyekiti
‘Msinitege,..ndugu mwenyekiti mimi naona hapo mnanitega, katiba
halali ninayoitambua mimi ni hii hapa, kisheria,… sio nyingineyo, kwanza nyie
muikubali hii katiba, kwasababu inatambulikana kisheria, halafu hayo mengine
yatafuata...’akasema
‘Ni nani ataweza kuikubali katiba iliyogushiwa wewe...’nikasema
kwa ukali
‘Ni nani kagushi hii katiba, ina maana serikali wao, hawajui
kulinda mali zao, mnawashutumu hata watu wa..aaha, muheshimiwa mwenyekiti wewe
na wenzako ndio mnatunga sheria, je sheria halali ni ipi, niambie nyie..ni kile
kilichosajiliwa kihalali au ni hicho chenu cha maneno matupu, niambieni jamani....?’
akauliza
‘Kwahiyo wewe unataka kikao hiki kikuthibitishie hilo, kuwa katiba
hii imegushiwa, kuwa Katina hiyo haitambulikani kisheria, na walioitengeneza ni
wakosaji, na sheria ifuate mkondo wake au sio..maana kama unafikia kunishutumu
mimi kuwa kama mtendaji wa serikali sijui wajibu wangu, umefika mbali, sasa
wewe unataka tulifanye hilo..?’ akauliza mwenyekiti
‘Mimi nimeongea kwa nia njema tu, …je mlitaka mimi nisemeje, sawa
thibitisheni, na mimi ndio nitakuwa nimeamini, maana mpaka sasa mimi naamini
hii ndio katiba halali…ikitokea vinginevyo, nipo tayari kuendelea na hiyo
Katiba mnayodai nyie kuwa ndiyo halali...sasa thibitisheni, tusipoteze muda…’akasema
kwa kujiamini, na mimi nikamwangalia kwa mashaka, na kusema;
‘Sawa mwenyekiti endelea na kikao, nipo tayari kwa lolote lile,
nimeamini kuwa mume wangu ana lake jambo, kama hana tatizo kichwani, docta
rafiki yake, hebu tusaidie, kweli huyu mtu yupo sawa, ...’nikasema na
mweneykiti akasema
‘Mjumbe anataka tuthibitishe kuwa katiba hiyo aliyo nayo sio
halali, na kwahiyo tunaingia kwenye kipengele cha kisheria,..hatukutaka tufikie
huko, lakini kwa vile mwenzetu kashikilia msimamo wake, basi inabidi tumpe haki
yake, kabla hatujaangalia ni jinsi gani swala hili tutakavyolipeleka kwenye nyombo
vya sheria ninataka kumuuliza tena mume wa familia...’akasema mwenyekiti.
Mume wangu pale akashtuka na kusema;
‘Kwanini unasema hivyo, ni nani kasema tulipekele hili swala
kwenye vyombo vya sheria, ...wakati katiba ipo hapa,...mimi sijasema
tushitakiane,mimi nimetaka ushahidi, na kuonyeshwa hiyo katiba nyingine
mnayoikubali nyie...hiki ni kikao cha familia, sio kushitakiana hapa..’akasema
mume wangu.
‘Umesema kuwa hiyo katiba uliyo nayo ni halali, na hutambui katiba
nyingine, mke wako anasema hiyo katiba uliyo nayo sio halali, imetengenezwa,
wakili wenu kabainisha wazi kuwa hiyo katiba siyo ile aliyoisajili yeye, ina
maana hapo unagusa sheria,, ...hivyo vyote vipo kisheria, na vimesajiliwa, je
tutajuaje kipi ni kipi,kama hatutakwenda kwenye vyombo vya sheria,
wakathibitisha hilo..’akasema mwenyekiti.
‘Vyombo vipi vya sheria zaidi yangu mimi na mke wangu ambao ndio
tulioitengeneza hiyo katiba...hii katiba ipo kwa msajili, ndiyo sheria, mimi na
mke wangu, ndio wahusika, tupo hapa, mnachotaka zaidi ni nini, najua lengo lenu
ni nini....’akasema
‘Lengo letu ni nini…?’ akauliza mwenyekiti
‘Ni kuvunja ndoa yangu, na mimi sitakubaliana na hilo…katiba
halali ni hii nah ii ndio ipo kwa msajili, mpende msipende ndio hivyo…na mimi
ni mume wa familia hii, mpende msipende ndio hivyo…’akasema
‘Kwahiyo hiyo katiba unayodai wewe ndiyo iliyopo kwa msajili.si
ndio hivyo..?’ akaulizwa
‘Ndio hivyo mwenyekiti, ukitaka kulithibitisha hilo, twendeni huko…’akasema
‘Kumbe tusipoteze muda, ngoja tumuulize huyo mdhamini wa serikali,
swali ni kuwa je tukimuuliza akisema kuwa katiba hiyo sio halali, ipo katiba
nyingine utasemaje?’ akaulizwa
‘Labda muwe mume-mnunua..maana nitasemaje sasa, maana nina uhakika
katiba iliyo huko ni hii…mimi na wakili wangu tulikwenda kulihakikisha hilo,
sasa nitaona ajabu ikiwa tofauti,....’akasema
‘Unasema nini, labda tuwe tume-mnunua, una maana gani hapo, hizo
kauli zako sio nzuri, lakini sawa, kama umefikia huko, ngoja tuone ubabe
wako..upo tayari sio?’ akauliza mwenyekiti kwa hamaki
‘Nasema hivi huko kwa msajili ipo nakala hii, huo ndio ukweli,
hakuna katiba nyingine zaidi ya hii, kaulizeni vinginevyo, mnapoteza muda wenu
tu, kwanini lakini kwani nyie hamna ndoa zenu..’akasema kwa kujiamini.
‘Jambo gani hebu liweke wazi, maana uunatamka maneno sasa ya
zarau, kauli za dharau, mimi mwenyekiti sitaweza kuzivumilia , nataka maelezo
kuhusu hiyo kauli uliyoitoa, kumnunua nani… vinginveyo uifute hiyo kauli
yako,...’akasema mwenyekiti.
‘Samahani mwenyekiti, kauli hiyo ilinitoka kwa bahati mbaya, sio
dhamira yangu, nimeifuta,unafahamu hapa nimechanganyikiwa, najiona kama nipo
peke yangu wote mnanisakama mimi...’akasema kwa kusikitika.
‘Hakuna anayekusakama hapa, acha kauli za kienyeji, hapa tupo watu
wazima waliosoma, wanaojua sheria, usiseme kauli za kizalili, jitetee kisheria
kama mume wa familia, kama unashindwa kujitetea kama mume wa familia, utakuwa
hujui majukumu yako kama mume, wewe kila mara unatamba kwa neno hilo, `mimi
mume, mimi mume,..’sasa thibitisha uume wako, kwa hoja, zenye mshiko na hapa
tupo kwenye sheria..’akasema mwenyekiti.
‘Sijashindwa mwenyekiti , mimi ni mume wa familia,nipo tayari kwa
lolote lile, tuendelee na kikao..’akasema
‘Haya tuendeee, mumemsikia mwenyewe akisema, kuwa yupo tayari
kuwajibika kama katiba halali,itapatikana, kama katiba aliyo nayo
itathibitishwa kuwa ni batili, ...sasa mimi naanza kazi yangu, ya kutaka
uthibitisho, kwani katiba zote hizi kama ni halali, zitakuwa zimesajiliwa kwa
msajili, na kama wao watakuwa na hii katiba, basi kisheria itabidi tuifuate..au
sio...'akasema na wajumbe wakasema
'Ndio, ila mume wa familia akasema 'hapana'
‘Kwanini unasema ‘hapana’ ?’ akaulizwa
‘Lugha za vitisho mwenyekiti,…na pia, hiyo ya kusema kuifuta,
huwezi kufuta hii katiba kwa mdomo tu, kwanza muikubali, na mkishaikubali ndipo
tukae tuanze kuangalia ni wapi tubadilishe, ..na ndipo, tusajili hiyo ambayo
mnaiona ni halali…’akasema
‘Leo wewe unatifundisha sheria…lakini hilo tuliache, sisi kwanza
tunataka kukuthibitshia kuwa katiba yako sio halali, ..kama ulivyotaka, kuwa
tuhakikishe huko kwa masajili…’akasema mwenyekiti
‘Sawa…’akasema
'Na huko kwa msajili kama wana katiba nyingine, itathibitisha kuwa
hio katiba yako ni batili, na kwahiyo kuna udanganyifu umefanyika, kama kuna
udanganyifu umefanyika, tunahitaji maelezo ya kina, kabla sheria haijachukua
mkondo wake....watuambie na wao huko imekuwaje,...kuna nini, na n nani
anahusika na yote hayo...’akasema mwenyekiti na mume wangu akatulia
akimwangalai mwenyekiti.
‘Sasa mume wa familia,…subiri, ..’mwenyekiti akageuka kuniangalia
mimi,
‘Nikuulize kwanza mke wa familia, je wewe umethibitisha kuwa
katiba hiyo aliyoshika mume wako ni batili, sio katiba halali, mliyoitengeneza
nyie na kusajiliwa kihalali ?’ akauliza mwenyekiti
‘Ndio mwenyekiti, nimethibitisha hilo...’nikasema
‘Kwa vigezo gani?’ akauliza mume wangu
‘Kwanza, kuna hizo alama zangu nilizokuwa nimeweka, kwenye hii
katiba hazipo, ina maana hii ni katiba iliyotengezwa kivingine, pili kwa
kupitia mwanasheria wetu kathibitisha kuwa hii katiba sio ile tuliyompa yeye
kwenda kuisajili, na tatu yale yaliyoandikwa ndani yamebadilishwa, hayafanani
kabisa na ile katiba halali, yamebadilishwa kiujanja ili kuleta maana nyingine
tofauti na ile tuliyokubaliana,...’nikasema
‘Ahsante, sasa naomba mnipe muda kidogo niweke mambo sawa, sio
lazima twende kwa msajili, uzuri wenzetu nao wamejipanga, sasa hivi
wamerahisisha mambo, wana vyombo vya kisasa…’akasema akifungua laptop yake.
‘Siku hizi kuna vyombo vya kisasa, vitaturahisishia kazi,.. ila
ikibidi tufanye hivyo,tutakwenda. Kwanza nataka kumpa nafasi ndugu yetu, kwa
ushahidi mwingine, ...kama atazidi kukaidi basi hili tatizo tutalipeleka kwenye
vyombo vya sheria ili wathibitishe wao …’akasema mwenyekiti huku
akifungua komputa yake aina ya lap top, akafungua sehemu
anayoitaka, halafu akachukua simu, na kupiga namba....
‘Siku hizi mambo ya mitandao yapo mbele, dunia sasa imekuwa ni
kijiji kimoja, tunaweza kuwashirikisha wajumbe wengine japokuwa hawapo kwenye
hiki kikao, ..sasa hivi tunakwenda chumba cha msajili wa katiba, yeye atakuwa
nasi, ...’akasema na mara simu yake ikawa hewani.
‘Mimi ni muheshimiwa Malimoto, mkongwe wa siasa…hahaha kumbe namba
yangu unayo, sawa sasa nimekupigia kwanza, kama mlivyosema siku hizi mpo ‘online..’
tunaweza kuwapata mbashara, au sio…naombe nikualike kwenye kikao chetu cha
familia, kwa kukuweka mbashara, je una nafasi hiyo…?’ akauliza.
‘Sawa muheshimiwa, nipo na nafasi, hamna shida tupo kwa ajili ya
wnanchi, nikusaidie nini…’akasema sasa akimuweka huyo muhusika hewani, akawa
anaonekana moja kwa moja kwenye laptop ya mwenyekiti.
‘Hapo tupo na wajumbe kwenye kikao cha familia, ni kikao halali
cha kifamilia, kikao hiki kinawajumuisha wanafamilia ambao kwa nia moja walikukabidhi
mkataba wao, ambao ni katiba yao halali, ya kifamilia katika mambo yao
waliyokubaliaan nayo ya kifamilia na makampuni yao,..natambua kuwa hilo ni
jambo la siri la familia hiyo ...'akasema
'Ndio muheshimiwa japokuwa hiyo sio njia halali ya kuuliza jambo
kama hilo, nafikiria ingelikuwa vyema wahusika wakafika ofisini...'akasema
'Nafahamu hilo , lakini si umenifahamu mimi ni nani..nisingeliweza
kulifanya hili kama sio muhimu sana, na wahusika wapo hapa wameridhia hilo
lifanyike, na hawa hapa...'akasema mwenyekiti, akielekeza kule kwa mume wa
familia na mkewe na wakili wao
'Sawa endelea muheshimiwa...'akasema huyo mtendaji wa masijala ya
mikataba.
'Sasa ni hivi kutokana na kutokuelewana kwa wanafamilia hawa
waliopo kwenye kikao hiki, nakuonyesha, uwaone tena, na wao wajithibitishe..’akasema mwenyekiti na
kuisogeza hiyo laptop, kuelekeza kwetu, halafu akawa anaionyesha kwa mtu mmoja
mmoja, mimi na mume wangu na wakili wetu, tukatakiwa kujithibitisha kuwa
tumekubali hilo lifanyike
Tukajithibitisha kuwa tupo tayari kwa hilo....na mwenyekiti
akaendelea kusema;
‘Kutokana na matatizo hayo wanahitajia kutumia katiba yao halali
kuhukumiana, kisheria, na sisi tupo kama wanafamilia kuhakikisha kuwa haki
inatendeka, tunahitaji swala hilo limalizwe kifamilia, na kama kutakuwa na
kutokuelewana zaidi tutalifikisha hilo swala mahakamani...’akasema mwenyekiti.
‘Lakini, samahani muheshimiwa, kama unasema kuna tatizo la
kutokuelewana, hilo sasa ni swala la kisheria, kwa vile mkataba wao umesajiliwa
kisheria, ningeliwashauri wakalifikisha mahakamani kwanza, kuliko kulifanya
hivyo...’akasema huyo msajili.
‘Hilo litafuata baadaye, kama hatutaelewana, tunachotaka ni kuthibitisha
tu jambo moja ambalo limeleta utata, ni kuhusu katiba uliyo nayo kwenye ofisi yako,
tunahitajia kuithibitisha hiyo katiba yao kwenye kikao kuwa ipo kwako na
imesajiliwa kihalali,...’akasema mwenyekiti
‘Ni kwanini imefikia hapo, tafadhali…?’ akauliza
‘Tatizo lipo kidogo, lakini kama wanafamilia tunaweza
kulisahihisha, ni tatizo kuwa kuna kutokuamini kuhusu nakala ya katiba tuliyo
nayo sisi, na hiyo iliyopp huko kwa msajili, ,,...’akasema mwenyekiti na huyo
msajili akasema
‘Mhh, nimekumbuka, unajua kuwa muda walifika mawakili , tukaongea
nao, kukawa na maelekezo kwao, niliwaagiza wafanye hivyo, lakini hakuna
aliyefika tena hapa, kwani kuna utata ulijitokeza hapa kwetu....’akasema
'Sasa hayo ni mambo ya ndani ya kiofisi,..lakini kwa vile yapo tayari
kisheria, na hukumu imeshapitishwa, na hiyo ni baada ya baadhi ya watu
kulalamika, kuwa kuna ubadhirifu wa taarifa huku kwenye ofisi yetu, na sisi
tulifanya uchunguzi na kugundulikana kuwa kweli kulikuwa ma mapungufu ya hapa
na pale,...na ndio maana kupitia kwa mawakili wote waliowahi kuleta mikataba
yao, katiba zao, tuliwaomba waje hapa kuthibitisha mikataba yao tena, kama kuna
mashaka...’akasema
‘Ndio kusema kuwa wakili wenu analitambua hilo, ila tulishangaa,
siku ambayo tuliwaita mawakili wote wenye mikataba yao hapa,kwa familia hiyo
walifika mawakili wawili, kinyume na ilivyokuwa awali..’akasema
‘Na wakili huyo alitumwa na mume wa familia akimwakilisha
yeye,kitu ambacho awali hakikuwepo, awali alikuwepo hakikuwepo awali,...huyo
wakili,akasema katumwa kuthibitisha, kuwa mkataba uliopo ni huo huo,, cha ajabu
zaidi, yeye alikuja na nakala tofauti na tuliyokuwa nayo sisi, ....
‘Nakala aliyokuwa nayo sio ambayo imesajiliwa hapa, nakala zote
zikiletwa hapa , tulikuwa kwanza tunaziscan, yaani tunachukua nakala hiyo
kwenye mtandao, na kuziweka kwenye huo
mitandao, kwahiyo hata kama mtu atafanya mbinu na kuiba nakala, zilizopo hapa
masijala, lazima tutakuja kuligundua hilo baadae,...’akasema
‘Sawa wakili aliyetumwa na mume wa familia hiyo, alikuja na
nakala, ambayo ilikuwa sawa na nakala iliyokuwa kwenye kabati letu awali,
lakini tulikuja kugundua kuwa hiyo nakala sio ile nakala halisi tuliyoiscani,
na kuiweka wenye mtandao
‘Yawezekana wawili hao walifanya marekebisho baadae, lakini hilo
halikuwahi kuletwa kwetu, ndio maana tukawaambia mawakili hawo kama kuna
marekebisho yamefanyika, basi waende wakaelewane, na walete maombi upya, lakini
mwenzetu hao hawajarudi tena. Sijui kwanini, na sisi hatuwezi kuondoa ile
nakala halisi ya awali kwa nakala nyingine bila utaratibu wa kisheria
.....’akasema
‘Sasa niwaambie hivi, kwa ajili ya kuweka mambo sawa, na kwa vile
ule mikataba sahihi, umeshatengenezewa nakala yake, wanaweza kuja na barua ya
kuwa hiyo nakala iliyopo sasa hawaitaki, wanataka hiyo nyingine mpya,.
‘Samahani kidogo, je kwenye makitaba yenu kulikuwa na nakala gani,
kabla ya hilo zoezi la kupitia nakala mlizoziscan…?’ akaulizwa
‘Kama nilivyosema kulikuwa na mazaifu ya utendaji, na muhusika
mwenzetu akafikishwa kwenye utawala , baada ya uchunguzi, na akakiri kuhusika
kwa namna moja au nyingine, kwa shinikizo la mtu aliyemfanyia mlungula
(blackmail),..hilo kwetu halina msingi, kwahiyo sheria imefuata mkondo,
kwafukuzwa kazi,..kwahiyo msiwe na wasiwasi kwa hivi sasa kwani kila kitu
kimewekwa sawa, na katiba halali nakala yake tunayo hapa, ....’akasema
‘Una maana gani kusema nakala halali?’ akauliza mwenyekiti
‘Kama nilivyosema awali, hilo ni swala la ndani ...kwenye kabati
kulionekana nakala ambayo ina marekebisho, kinyume na nakala iliyopo kwenye
kwenye mtandao..na sisi tunatambua wazi, hayo yametokana na mapungufu ya
kiofisi au labda, ni wenyewe wahusika walitaka kufanya marekebisho, sasa waje
wathibitishe hilo, na mawakili wao,...’akasema.
‘Samahani unaweza kutuonyesha nakala hilo hapa, mbashara, ili
tuhakikishe kuwa inafanana nah ii tuliyo nayo hapa..’akasema mwenyekit’, na
mata muhusika akasimama na kutoweka kidogo baadae akarudi na nakala, akaiweka
hewani..halafu akasema
‘Nakala hiyo ipo kwenye mtandao, lakini nyie hamuwezi kuingia huko…’akasema
‘Sawa tufungulie kidogo kidogo…ili tuhakiki…’akasema mwenyekiti
‘Hii hapa ndio nakala halisi,....’akasema huku akiifungua ukurasa
mmoja mmoja kwa taratibu...na wakili wa familia hiyo akawa ana hakiki na kupiga
picha kwenye simu yake, mpaka ikaisha…na wote waliporizika, mwenyekiti akasema;
‘Je hiyo nakala iliyokuwepo kwenye kabati ambayo haifanani na
nakala huyo halisi mnayo hapo..?’ akaulizwa
‘Haipo hapa ipo kwenye vyombo vya sheria kama ushahidi…’akasema
‘Tunashukuru sana, maana sasa tunaweza kuhakiki hili kwenye hiki
kikao…’akasema na baadae mwenyekiti akazima laptop, na kumgeukia wakili wa
familia, akamuuliza
‘Unasemaje, umehakiki vyema, na kila mmoja kaiona au sio…?’
akulizwa
‘Hiyo ndiyo yenyewe, ...umeona huo muhuri wangu ndio huu hapa…’akasema
wakili akionyesha huo muhuri, na huku akifungua ukurusa mmoja baada ya
mwingine, sasa kitumia simu yake.
Wakati hayo yakiendelea
mume wangu alikuwa anasogea huku akiwa kashikilia ile nakala yake kama vile
anataka kumuonyesha huyo msajili, lakini rafiki yake-docta, akamuona na
kumsogelea, na kumvuta pembeni na kumnong’oneza , mimi nilikuwa karibu nao,
nilimsikia akimwambia rafiki yake;
‘Usionyeshe kabisa hiyo nakala yako, utafungwa, hiyo nakala yako
imeonekana ni bandia, kwahiyo kuna ukiuwaji wa sheria, na wote waliohusika,
wataweza kushitakiwa, ...achana na hiyo nakala yako, ikibidi uiharibu kabisa,
huo ushahidi... kilichobakia sasa ni kukubali kuwa kuna makosa
yalifanyika, na ukubali mkataba wenu wa awali ufanye kazi yake, huna jinsi,
...’akambia rafiki yake, na mume wangu akatikisa kichwa kama
kuukataa....alionekana hajakubali.
Mimi nikawa bado nipo naangalia yale yanayoendelea kati ya mawakili
na wajumbe kuhakikisa uhalali wa mikataba hiyo yote miwili, na baadaye
mwenyekiti akasema;
‘Haya zoezi hili limekamilika,na ushahidi alioutaka mwenzetu
umekamilika, sasa turejee kwenye viti vyetu, tuingie sehemu inayofuata, na huku
tukijiweka sawa, nataka mume wa familia atueleze ukweli, kikao kinahitaji
maelezo yake ya ukweli, kwa jinsi ilivyotokea, hadi kupatikana hiyo katiba
iliyogushiwa ‘akasema mwenyekiti
Mume wangu akawa kimia sasa
‘Hii sasa ni amri, tunataka ukweli, wenye mshiko,
vinginevyo, baba, itabidi swala hili liende mbali zaidi,...’akasema
mwenyekiti, akiweka vitu vyake sawa tayari kwa kuendelea na kikao.
Mume wangu alikuwa ameshafika kwenye kiti chake, na kukaa, alitulia
akiwa hana raha, na baadaye akageuka kuangalia kulia na kushoto kwake, na sisi
tukawa tunamuangalia kwa mashaka, kwa jinsi anavyo angalia huku na kule, halaf
akauliza;
‘Mdogo wangu yupo wapi?’ akauliza na sisi ndio tukagundua kuwa kumbe
mdogo wake hayupo, haonekani ndani ya chumba cha kikao, na hakuna aliyemuona
wakati natoka kwani kila mmoja alikuwa akishangaa katoka muda gani.
‘Huyu mtu wenu kaenda wapi,..au kaenda kujisaidia mara moja, hebu
hakikisheni hili maana huyo mtu yupo hapa kwa dhamana yetu…? akauliza
mwenyekiti na yeye akiangalia huku na kule
Watu walitafuta huku na kule na baadae ikathibitishwa kuwa mtu
huyo hayupo katoweka, katoroka…
'Ngoja niwaite watu wa usalama, ...hili haliwezi kuishia hivi,
siwezi kuingia matatani kwa uzembe wa watu wengine...'akasema mwenyekiti, sasa akitaka kupiga simu.
NB: Haya tunaishia hapo kwa leo, sehemu ijayo tutaingia sehemu
nyingine ya kikao hicho, cha kifamilia, je ni nini kitafuata.
WAZO LA LEO: Uwongo
ni tabia chafu, ukiwa na tabia hiyo utambue kuwa wewe ni mwovu, na hutawahi
kuwa na amani maishani mwako…kwani kila muda utakuwa na mashaka, mwenye tabia
hiyo ni mtu mchafu , ananuka japokuwa hatoi harufu, ni heri mara mia ya mchafu
wa mwili kuliko mchafu wa nafsi mwenye tabia ya urongo, Mtu mwenye tabia hiyo MNAFIKI.
Tuepuke tabia hiyo, ili tuwe na maisha ya amani na raha.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment