‘Je kweli wewe una uhakika kuwa hii ndio katiba halali,
mliyoitengeneza wewe na mke wako, ikasainiwa na wakili wa familia yenu…
‘Je ninaweza kujibu mwenyekiti swali lako…maana, mimi sina
wasiwasi na hilo..’akasema mume wangu
Tuendelee na kisa chetu…
**************
‘Ndugu mwenyekiti mimi hapa ni mkweo, ni mume wa binti yako, ndiye
ninayefahamu ukweli wa mambo ndani ya familia yangu, na kwahiyo hicho
ninachokuambia ndio ukweli wenyewe,....’akasema
‘Hujajibu swali langu, je hii ndio katiba halali mliyokubaliana
wewe na mkeo,?’ akauliza tena mwenyekiti, na mume wangu akasema
‘Ndio, hiyo ndio katiba halali tuliyokubaliana mimi na mke wangu,
na ukiangalia humo utaona sahihi zetu wote ikiwemo ya wakili wetu,...’akasema.
‘Sawa nilitaka kusikia kauli yako tena ili wajumbe wote waisikie,
na sasa nataka kuthibitisha ukweli wa kauli yako…’akasema mwenyekiti
‘Kuthibitisha…kuthibitisha nini…?’ akauliza mume wangu kwa uso wa
kushangaa
‘Kuna malalamiko kuwa katiba iliyokuwa halali imebadilishwa ,
imegushiwa kiujanja ujanja na kutengenezwa katiba nyingine kwa minajili ya
kujitwalia mali, na kuhalalisha mambo kwa manufaa ya mtu, au watu wake, bila ya
mmoja wa wahusika kwenye mkataba huo kuhusishwa, na bila wakili wa familia hiyo
kuhusishwa pia, .....’akasema mwenyekiti
‘Hiyo sio kweli mwenyekiti, muulize mke wangu, kama kweli hii sio
katiba halali, na wakili yupo hapa, apinge kuwa hiyo sio sahihi yake, na sahihi
ndio ushahidi muhimu kwenye vitu kama hivi....’akasema mume wangu kwa
kujiamini.
‘Hiyo sio kazi yako, mimi kama mwenyekiti nafahamu jinsi gani ya
kuhakiki uhalali wa hilo,… na kama kweli ndiyo katiba yenu, ambayo
mlikubaliana, tutathibitisha hilo, bila shaka, na kama kuna ubabaishaji wa hilo
ni kosa kubwa, na ni kosa linalostahiki kufikishwa mbele ya sheria..’akasema
mwenyekiti.
‘Ni…hi, sio kweli mwenyekiti…’akasema mume
‘Unajua ..mimi sikutaka sana kuingilia kwenye mambo yenu ya katiba
, kwasababu kikao chetu kilikuwa na utaratibu wake, huenda hilo ni moja ya
mambo ambayo alitaka kuyaongelea mwenyeji wa hiki kikao, mimi sijui..’akasema
mwenyekiti.
‘Lakini imenibidi niingilie hili kati,kwa vile wewe mwenyewe
umekuwa ukisisitizia kuhusu hiyo katiba, na ya kuwa katiba kwenu ni kila kitu… na
hata kikao hiki ni ukiukwaji wa katiba,…na zaidi ya hilo, nyie hamtaki watu
wengine wawaingilie , kwasababu mna muongoz wenu, sio ndio hivyo mume wa
familia?’ akauliza mwenyekiti
‘Ndio hivyo mwenyekiti, kila kitu kipo kwenye hiyo katiba..naona
ajabu watu kutuingilia kwenye mambo yetu ya ndani,…hiyo ni kweli mwenyekiti,
samahani kwa hilo…’akasema huku akitabasamu.
‘Kuna malalamiko,kuwa hii katiba uliyonipa , hii hapa...itakuwa ni
hii au sio…maana sijajua kuwa kuna katiba nyingine nyie ndio mtanithibitishia,
hilo…’akaiinua juu mwenyekiti,..
Mume wangu akataka kuongea lakini mwenyekiti hakumpatia nafasi
hiyo
‘Mimi sijui, maana hii hayo mliyatengeneza nyie wawili, na
kilichomo humu, mnakifahamu nyie wawili, lakini katiba hiyo imesajiliwa
kisheria, kwahiyo yaliyomo humo ni sheria yenu wawili,na yupo shahidi wenu mkuu
kisheria, wakili wenu, ..’akatulia akimuangalia wakili
‘Sasa kwa minajili hiyo kila mmoja wenu ana haki nayo, na kama
mmoja atafanya ujanja na kuibadili, kavunja sheria, na nazidi kusisitiza,
kuhariri, kubadilisha kitu kama hiki mlichokubaliana kisheria, bila ya ridhaa
ya mwingine ni kosa kubwa, …’akasema mwenyekiti
‘Nimeamua kuacha utaratibu wetu, ili kuliweka hili sawa, ni
kutokana na wewe mume wa familia, … kuna kauli kuwa katiba mliyotengeneza awali
imegushiwa, imekarabatiwa kiujanja ujanaja…,je wewe kama mume wa familia,
unasemaje kuhusu hilo, ?’ akaulizwa.
‘Mimi nalipinga kabisa, hakuna kitu kama hicho, na huyo aliyesema,
hivyo hafahamu ukweli wa mambo yetu ndani ya familia, hao ndio wavurugaji wa
ndoa za watu, wanastahiki kukemewa…’akasema
‘Una uhakika na hilo..?’ akaulizwa
‘Ndio mwenyekiti...mimi kama mume wa familia, nina majukumu ya
kulinda familia yangu, na ni pamoja na kuilinda hii katiba yetu halali, kwani
imebeba mambo yetu yote,....sitakubali mtu aibadili, bila kumshirikisha
mwenzagu, na haijabadilishwa, ni nani kaongea hilo....’akasema
‘Ndugu mume wa familia, hili ni muhimu sana, uwe na uhakika na
majibu yako, usije ukajiweka kwenye hatia,…Ina maana kweli hakuna katiba mbili,
hii ya sasa na nyingine ya awali?, je hamjawahi kuikarabati kwa pamoja
kutengeneza katiba nyingine mpya..?’ akauliza mwenyekiti
‘Ndio mwenyekiti, hakuna katiba nyingine, kama ipo tofauti na hii
ambayo kweli imesajiliwa watuonyeshe hawo watu wanasema hivyo, kwasababu kila
kitu kipo kisheria, hata ukienda kwa msajili, utaiona nakala kama hiyo hapo,..’akasema
‘Na je kama itathibitishwa kuwa hii sio katiba halali, na ya kuwa
hii imetengezwa kwa kugushiwa kwa malengo maalumu, utasemaje?’ akauliza
‘Nitasema nini,…hahaha ndugu mwenyekiti kauli hiyo inatoka wapi,
..ni kwamba hakuna katiba nyingine, katiba ndio hii, kwanini mwenyekiti
huniamini..kwanini
unang’ang’ania kuwa kuna katiba nyingine, mimi ndiye mume wa
familia na unatakiwa uniamini mimi, kwani nasema hili kwa masilahi ya familia
yangu’akasema kwa kupaza sauti kidogo.
Mwenyekiti akageuka kidogo kuniangalia mimi pale nilipokaa, na
kutikisa kichwa akionyesha kusikitika, akasema;
‘Nawaasa sana nyie wanandoa, sawa mume ni mume, ana mamlaka yake
makubwa tu, lakini niwaambia jambo moja, hakuna kitu muhimu katika ndoa kama
uaminifu, hakuna kitu muhimu katika ndoa kama kutii yale mliyokubalina nyie
wawili kama wanandoa…’akatulia akimuangalia mume wangu.
‘Na zaidi ya hayo,kama wanandoa mtakuwa na ajenda za siri kwa nia
ya kuumizana, basi ndoa hiyo haina usalama tena, ndoa hiyo sio ndoa tena bali
ni ndoana. Mimi nilishatoa angalizo kuwa kuna mambo yanayosamehewa kama watu
watatenda kwa bahati mbaya...’akasema
‘Ni kweli…’akasema mume wangu
‘Lakini kuna mambo ambayo unayaona kuwa kweli ni makusudi, na yana
nia mbaya, na ukiyaachia yanaweza kukiharibu kizazi, uwongo, utapeli, kugushi,
ni dhambi, unajenga taifa la watu wasio waaminifu..sasa mimi sitaki kuwa
mchochezi, nimeletewa mashitaka hayo, kuwa kuna ukiukwaji wa sheria, tena wa
hali ya juu, kwani kama mtu anaweza kubadilisha kitu kilichosajiliwa kisheria,
akatengeneza kingine, kikiwa na sahihi za wahusika, basi huyo ni mkiukaji wa
sheria wa hali ya juu..'akasema mwenyekiti
Mume wangu akawa anaonyesha ishara ya kushangaa, kuwa ni nini mwenyekiti anaongea, ni kama kudharau hivi.
‘Hii hapa ni katiba, ambayo inawahusu watu wawili, na sijui kama
ndio yenyewe au la, wanahusika wataithibitisha wao wenyewe.., sasa mume wa familia anasema
hii ndio katiba halali, ...maana wewe mwenyewe ndio umelitaka hili, ...kabla sijamuuliza mkeo ,ambaye ni kiungo muhimu, ambaye
walikaa pamoja yeye na mume wake, wakaitengeneza,…’akatulia kidogo huku akigeuza kichwa taratibu kuelekea sehemu nyingine,
‘Mimi naona ni bora nimuulize mtengenezaji wa hii katiba kisheria
na ambaye alihusika kwenye kuisajili ambaye ni shahidi wa hiki kitu, maana
nikikimbilia kumuuliza mke wa familia, nitaionekana nimeweka shinikizo kwa vile ni binti
yangu, mnielewe hapo,japokuwa hapa wote ni wajumbe...’akasema mwenyekiti na kutulia kidogo, akamuangalia mume wangu, na mume wangu akawa anatikisa kichwa tu.
‘Mume wa familia, nakuomba wewe mwenyewe, uchukue hii katiba
ukamuonyeshe wakili wenu ili athibitishe kwenye kikao hiki kuwa hiyo ndio
katiba halali mliyoiandika wewe na mke wako, kwa msaada wa huyo wakili
wenu ...'akatulia kidogo
'Sasa yeye akithibitisha kuwa ndio yenyewe, mbona jambo limekwisha, mimi sitakuwa na haja ya kumuuliza binti yangu, nimuulize wa nini tena..eeh ..’akasema
akiishika ile katiba kumkabidhi mume wangu.
‘Nitamuuliza tu kwa vile yeye ni kiungo muhimu, na kama yeye atakuwa na pingamizi, kama na yeye hana pingamizi, basi, tufanyeje sasa..
'Au sio wajumbe...?' akauliza wajumbe na wajumbe wakatikia kwa kauli
'Sawa kabisa mwenyekiti..
'Basi, tunataka zoezi hilo lifanyike kwa haraka ili twende na muda,..baada ya hapo, tutaingia kwenye kipengele kingine ama cha kusikiliza malalamiko ya muitisha kikao, au kuzidi kuthibitisha uhalali wa hiyo katiba,...na kama itakuwa tofauti, kukaonekana kuna utata wa hiyo katiba,...mmh, mimi sitasema mengi...'akasema na wajumbe wakacheka
'Msicheke, hili ni tatizo jamani,...kama haya yanatokea ndani ya familia ya mke na mume, watu walio kitu kimoja, mnatarajia wakipewa madaraka nchi itakuwaje,...mimi nipo kwenye siasa, naliangalia hili kwa umbali zaidi,..matatizi mengi huanzia huku kwenye familia, chagueni viongozi kwa kuwachunguza huku wanapotokea...'akasema na mke wake akapiga makofi.
'Kama alivyo dai mume wa
familia kuwa tusiingilie mambo yenu , maana katiba yako ndio kila kitu, sasa tuone uhalali wake, na baadae hiyo katiba halali ifanye kazi yake, mkuki kwa nani ni mchungu, sasa mkuki huo utamgeukia, nani..matajaza wenyewe...’akasema
mwenyekiti.
'Haya zoezi lianze...'akamalizia hivyo.
‘Sawa kabisa mwenyekiti....’akasema mume wangu, huku akisogea
mbele, na kuelekea pale alipokaa mwenyekiti, wakati anapita akapita pale
alipokaa mdogo wake, akamnong’oneza kitu, na mdogo wake, akamwangalia kaka
yake, kwa macho ya kushangaa, lakini huyo mdogo mtu hakusema neno. Mwenyekiti hakuliona hilo tendo, alikuwa akiteta na mkewe.
Mume wangu akaichukua ile katiba kwa mwenyekiti , akaikagua kwa
kiufungua, akatikisa kichwa kama kukubali kuwa ndio yenyewe,huku akiwa
anatabasamu akatembea hadi pale alipokaa wakili wa familia yangu na kumuonyesha
wakili ile katiba huku akisema;
‘Ndugu muheshimiwa wakili, hii ndio Katiba ambayo tuliitengeneza
tukishirikiana na wewe, na kama unavyoona kuna sahihi yako, hii hapa, ...na hii
hapa ni sahihi yangu na hii hapa ni ya mke wangu, nataka wewe uthibitishe
kwenye kikao hiki kuwa hii ndio katiba halali, ili tuondoe hiki kiwingu cha
kutoakuaminiana ...ukumbuke wewe ni wakili wa familia, na mimi ni mume wa
familia, mwenye mamlaka yote a familia....’akasema
Kwanza wakili alisita kuipokea ile katiba, akamwangalia
mwenyekiti, na mwenyekiti akasema;
‘Labda tufanye hivi, mimi nina wakili wangu, kabla wakili wenu
hajathibitisha hilo hebu muonyeshe wakili wangu, ili yeye aione hiyo katiba,
ili awe ni mmoja wa mashahidi walioyoiona hiyo katiba, ili baadaye tusije
tukarukana, kuwa haikuwa hiyo, pia wajumbe wengine, kuna docta pale, kisheria
anatambulikana anaweza naye kuthibitisha hilo, sio mbaya na wajumbe wengine
wakaiona maana kwasasa haina siri tena,...’akasema
Mume wangu akatembea hadi pale alipokaa wakili wa wazee wangu
akamuonyesha ile katiba, wakili wa mzee, akaichukua na kuifungua, akasoma
kidogo, halafu kwa haraka akapitia ukurasa mmoja baada ya mwingine, akachukua
simu yake, akawa anaipiga picha sehemu muhimu, halafu akasema
‘Je una nakala nyingine ya hii katiba yenu?’ akauliza wakili huyo
‘Ndio ninayo, nina nakala tatu, unaweza kubakia na nakala hii,
kama unahitaji, zipo nyingine, hakuna shida,....’akasema na kwenda kwenye mkoba
wake, akatoa nakala nyingine, na kusema;
‘Hiizi hapa nakala nyingine,zote ni sawa sawa,....’akasema
‘Haya kamuonyeshe wakili wenu, ili athibitishe kuwa Katiba hiyo
ndio Katiba sahihi ambayo yeye aliitengeneza, na kuipeleka kuisajili kwa
msajili wa katiba,...yeye ndiye mtu wenu wa sheria, kwani kwa jinsi ilivyo,
hatua itakayofuatia, kama kweli kuna uvunjaji wa sheria kiasi hicho, basi yeye
ndiye muwajibikaji mkubwa’akasema mwenyekiti.
Wakili wetu, aliichukua ile katiba, akafungua ukurasa wa kwanza,
akawa anangalia kwenye ganda la juu, kwa ndani, akawa kama anashangaa, hakusem
neno, akafungua ukurasa wa kwanza na kuangalia kwa ndani, akainua ukurasa wa
kwanza ni kufanya kama vile ananinginiza, kama vile mtu anayeangalia pesa kuwa
ni halali,.....’akatikisa kichwa na kusema;
‘Hii sio ile katiba halali…’akasema
‘Rudia tena…’akasema mwenyekiti
‘Hii sio ile katiba halali niliyoisajili mimi…’akasema
Watu kimia…sasa wakigeuka kumuangalia mume wa familia, aliyekuwa
kashikwa na butwa,
Kwa haraka mume wa familia, akasogea pale alipokaa huyo wakili,akichukua
ile katiba kutoka mikononi mwa huyo wakili na kusema;
‘Hii ni katiba halali, unaona sahihi yako hii hapa, na hii hapa ni
ya mke wangu, unataka kusema nini, mbona unatupinga sisi wateja wako...wakili
gani anayewapinga wateja wake…hapana hufai..’akasema akimuonyesha huyo wakili,
lakini huyo wakili hakutaka hata kuiangalia,akasema;
‘Ndugu mwenyekiti, kila fani ina watendaji wake, na wanao jinsi
gani ya kulinda mambo yao, sisi, kama mawakili tunafahamu haya yote kuwa
yanaweza kutokea, kwa hiyo kila mmoja ana namna yake ya kuweka mambo yake
katika usalama, ili mtu mwingine asije akabatilisha kazi yake..hii kazi ni ya
hatari na ina dhamana kubwa, ukizingatia kuwa unacheza na maisha ya familia za
watu....’akasema.
‘Mimi na wengine tuna mihuri ya siri, ni wachache sana wasio na
mihuri hiyo ya siri, inayothibitisha kuwa hii kazi ni ya mtu fulani, hii kazi
ni yangu, hasa kwenye kazi kama hizi ambazo zina usiri wa kifamilia. ..’akasema
na mume wangu akawa kaduwaa tu.
‘Kiukweli mimi sikutarajia kuwa katiba hii aliyoitoa mume wa
familia, ingeliweza kuwa sio yenyewe ambayo niliitengeneza mimi..maana
ukiiangalia juu juu, utaona haina tofauti na ile katiba niliotengeneza mimi
lakini kuna kitu kinakosekana, hakuna hiyo alama yangu…’akasema na mume wangu
akawa anaichunguza ile katiba.
‘Labda nimuulize mteja wangu huyu…je ni kwanini huo muhuri wangu
haupo, je ulitoa nakala nyingine, na kama ulitoa nakala nyingine, bado ule
muhuri wangu ungelionekana kwa kufifia…, ningelitambua kuwa hiyo ni nakala tu....’akatulia.
‘Kwahiyo huo ndio mtego, hii katiba haina kitambulisho changu, kwa
kuiangalia tu bila kusoma kilichopo ndani…’akasema
‘’Huo muhuri, unakaa wapi,lakini mimi ninachojua ni kuwa hii ndio
katiba halali, na wewe unachotakiwa ni kusimama kwa ajili yetu, kama unanipinga
mimi basi wewe sio wakili wetu...’akasema
‘Mimi ni wakili wenu kisheria… nasimamia taratibu zenu ki- sheria,
siwezi kusema uwongo, hii sio katiba niliyoitengeneza mimi, ...na kwa haraka
nimeshaipitia ndani, na niliwahi kuipata kabla, kuna mambo mengi yamebadilishwa...’akasema
huyo wakili, na mume wangu akabakia kimia.
‘Ndugu mwenyekiti, Wakati mume wa familia anaongea kwa kujiamini,
nilijua kabisa huenda huyo aliyewatengeneza atakuwa anafahamu muhuri wangu,
kwani kama aliweza kugushi sahihi, zetu, asingelishindwa kugushi muhuri wangu
wa kificho, unaowakilisha kazi zangu...ndugu mwenyekiti, kiukweli hii sio
katiba halali niliyotengeneza mimi....’akasem wakili.
Mwenyekiti, akakunja uso, akamwangalia mume wangu, na kusema;
‘Mkwe,...nimeamua kukuita hivyo mkwe, ili nikupe heshima, yako,
nataka unijibu hayo, ninayokuuliza kama mkwe, mkwe wa kweli hasemi uwongo,
useme ukweli wako, kama mkwe, mkwe ana heshima yake, hawezi kumdanganya baba
mkwe wake,...eti jamani uliona wapi mkwe anamdanganya baba mkwe wake, ...kwahiyo
nakuomba, unjibu haya maswali kwa ukweli wako,, nakuuliza tena;
‘Hiyo katiba ni katiba halali mliyotengeneza wewe na binti yangu?’
akauliza baba.
‘Baba mkwe, mimi ninamshangaa wakili wetu, yeye ndiye
anayewakilisha mawazo yetu na kutuwakilisha sisi, nashangaa, leo anapina kazi
yake mwenyewe, mimi sijali huo muhuri wake anaosema, ninachojali ni hiyo
sahihi, yake, je akiri mbele ya kikao hiki kuwa hiyo sio sahihi yake, je hii
sio sahihi ya mke wangu...?’ akauliza
‘Inaweza ikawa ni sahihi yangu,..lakini sahihi hii imechukuliwa
kitaalamu na mihuri, kuna mihuri siku hizi, inabandikwa kwenye maandishi, na
yale maandishi yanabakia kwenye ule muhuri, na unaweza kwenda kuyabandika
sehemu nyingine, kama vile unavyoweza kufanya kwenye komputa kukopi na kupesti,
..’akasema wakili
‘Una ushahidi kuwa ilifanyika hivyo?’ akauliza mwenyekiti
‘Ukiangalia kwa makini, utaona sahihi hizi ni kama zina kivuli,
angalia kwa makini, kuna kivuli, na hii kwa wataalamu wa maandishi wanaweza
kulithibitisha hili....mimi nilikuwa nashauri kwa vile jambo hilo limefanyika
kitaalamu zaidi, ni bora tukawahusisha wataalamu wa maandishi,…’akasema
wakili na mume wangu akataka kusema neno lakini akatulia kwanza.
‘Na kwa vile tendo hili limefanyika likisaidiwa na wakili, nina
uhakika, kuna wakili yupo nyuma ya hili, kashiriki kulifanya hili, kwani sehemu
zilizobadilishwa zimebadilishwa kwa utaalamu wa hali ya juu wa
kisheria.....basi hili swala naona liende kisheria, lichunguzwe kisheria,
..’akasema
‘Nikuulize tena kuna kitu gani kingine unachokiona ni tofauti na
mkataba halali ulioutengeneza wewe?’ akaulizwa
‘Kuna maandishi yamebananishwa, ukiangalia utaona kama mistari
ilikuwa iantaka kupandana, sivyo ilivyokuwa kwenye mkataba halisi,… nahisi ni
ili kusije kukaongezeka ukurasa, na kuleta tofauti kati ya mkataba ule halali
wa mwanzo na huu wa kugushi...’akasema
‘Inatosha…’akasema mwenyekiti, na hakumuangalia mume wangu ambaye
alikuwa bado kaduwaa, akizidi kuikagua ile katiba, kama haamini..
‘Kabla hatujaingia ndani tukaona ni nini kimebadilishwa na
kwanini,…maana kama kuna mabadiliko, yatakuwa na maana fulani au sio, narudi kwako mume wa familia, je bado
unashikilia msimamo wako huo kuwa hiyo ndio katiba halali ya familia, ambayo
uliitengeneza wewe na mke wako?’ akaulizwa.
Mume wangu akabakia kimia kidogo, halafu kwa haraka akasema;
‘Kauli yangu ni ile ile mwenyekiti, mimi nawashangaa, maana mimi
ndiye ninayefahamu katiba ipi ni halali, kwanza kwanini niseme katiba ipi,
hakuna mbadala wa hii, au sio mke wangu…?’ akasema akiniuliza mimi na mimi
nilikaa kimia tu.
‘Ndugu mwenyekiti mimi ndiye ninayewakilisha familia yangu,
nashangaa watu wa nje, mnakuja kuipinga katiba yetu, kwani mlikuwepo wakati
tunaitengeneza,...hii hapa ndio katiba halali, kama ipo nyingine, nataka
niione, ili hii ionekane sio yenyewe...’akasema
Mwenyekiti akatabasamu kidogo, na kutikisa kichwa kama kusikitika,
halafu akasema;
‘Kabla hatujathibitisha hilo,kabla hatujafanya unavyotaka wewe,
nataka sasa nimgeukie mke wa familia, nataka na yeye, atuthibitishie kuwa hiyo
katiba aliyo nayo mume wake, ndio katiba halali mliyokubaliana kati yenu
wawili, ..’akasema
Kwa haraka mume wangu akaichukua ile katiba kutoka kwenye mikono
ya wakili wetu akaniletea na kunikabidhi mimi, huku akifungua sehemu zile
tulizoweka sahihi zetu, ....kiukweli huwezi kuona tofauti kati ya katiba hiyo
na ile ya kwetu ya awali, kwani kila kitu kilionekana sawasawa kwa juu-juu,
ukiangalia kwa haraka haraka inafanana kabisa na katiba ile ya awali,
Huyo aliyebadilisha alikuwa mtalaamu kweli wa kazi hiyo,..na
kwa mtu asiyejua, hutaweza kugundua utofauti wowote mpaka usome ndani,na
usome kwa makini kweli, kwani kuna lugha ya kisheria, ukibadili neno moja
unaleta maana nyingine na kuna mambo yameongezeka, na mengine kupungua, lakini
bila kuongeza ukurasa, au kuhamisha maneno mengine kwenye ukurasa mwingine,
Nilimuangalia mwenyekiti kabla ya kuipokea, na mwenyekiti akasema;
‘Ikague uhakikishe kama kweli ndio yenyewe…’akasema mwenyekiti na
mimi ndio nikaichukua na kuanza kuikagua..
Niliingalia kwa makini, na huku mume wangu akinitizama kwa macho
yaliyojaa shauku, na aliponiona nasita kutoa majibu, akasema;
‘Mke wangu hii ndio katiba yetu, kila kitu kipo kwa ajili ya
masilahi yetu, hakuna kilichobadilika, ukiangalia hapo kuna sahihi zetu, na
sahihi ya wakili, mimi sioni kama ni katiba tofauti, ....hii ni kwa ajili yetu
na watoto wetu, lifikirie sana hilo akilini mwako, ....’akasema akionyesha
sauti ya huzuni, mimi nikamwangalia na kusema;
‘Una uhakika na hayo maneno yako, una uhakika kuwa unalolisema
ndio ukweli, mume wangu..?’ nikamuuliza na mume wangu akaniangalia kwa mashaka,
na kusema
‘Mke wangu na wewe vipi, unanigeuka tena..’akasema
‘Mume wangu nakuuliza hivi, una uhakika kuwa hii ndio katiba yetu
tuliyoitengeneza mimi na wewe siku ile...naomba mume wangu uwe mkweli, na huu
ndio mtihani wako, ukweli wako ndio utakaodhirisha kuwa kweli upo na
mimi...’nikasema na mume wangu akageuka kumwangalia mwenyekiti.
‘Mwenyekiti unaona hata mke wangu hawezi kulithibitisha hilo maana
yeye anafahamu katiba ni moja tu, hio kauli ni yako tu …’akasema mume wangu
‘Nimekuuliza swali mke wa familia, je hiyo katiba ndiyo
mliyoitengeneza nyie wawili, ...jibu swali, sitaki umuulize swali mume wako,
nataka kauli yako wewe, kwasababu wewe unaifahamu vyema,...?’ akauliza
mwenyekiti.
Kiukweli sijui kiliniingia kitu gani,..ule ujasiri wa kujibu kwa
haraka ulinitoka, nikamwangalia mume wangu ambaye alikuwa akiniangalia kwa
macho ya huruma, na machoni, nikawa nawaona watoto wangu wawili, na sijui
kwanini, ilitokea hivyo kuona taswira ya watoto wangu,na mwingine akiwa kwa
mbali, na ikaja hisia kama ya watoto wangu wakilia, na kuita baba,baba yupo
wapi....,
Nikageuka kumwangalia mwenyekiti, nikasema,;
‘Ndugu mwenyekiti, katiba hii, inafanana sana na katiba ya
awali...ni vigumu sana kuitofautisha na katiba..ya....’nikaanza kuongea na mume
wangu akatabasamu na kupiga makofi kushangilia, huku akisema;
‘Unaona mwenyekiti, mimi na mke wangu ndio tuliotengeneza hii
katiba kwahiyo tunaifahamu sana, namshangaa sana wakili wetu kutegeuka hii leo,
sijui ana masilahi gani...’akasema mume wangu, na alipomaliza nikaendelea
kuongea
‘Lakini ndugu mwenyekiti, wakati katiba hii inatengenezwa, sijui
ni hisia au sijui ni kwanini nilijiwa na kitu kama hicho kuwa huenda ikatokea
kubadilishwa badilishwa hii katiba, basi nikajiwa na wazo,..ilinijia tu mungu
mwenyewe ndiye anayejua..’nikasema
‘Sawa kabisa waambie..’akasema mume wangu.
‘Kwa vile, shemeji yangu, yaani mdogo wa mume wangu ni mtaalamu wa
komputa, na mambo yake, nilimuomba anisaidie kutengeneza maneno ya siri ambayo
ninaweza kuyaweka kwenye kumbukumbu zangu, kiasi kwamba mtu mwingine asiweze
kugundua hilo....’nikasema
‘Na kiukweli, sikuwahi kumwambia hata wakili wetu kuwa kwenye hiyo
katiba kuna maneno nimeyaweka ya siri, kwahiyo hata yeye hajui hilo, niliyaweka
wakati wakili wetu aliponiletea katiba hii kwenye mtandao ili mimi niupitie,
ndipo hapo nikayaweka hayo maneno, na kila ukitoa nakala,halisi utayaona hayo
maneno, yanakuwa huku pembeni, na ukitoa nakala, isiyo halisi maneno hayo
hugeuka, yakawa kinyume chake....’nikasema na kumwangalia shemeji yangu ambaye
alikuwa kabakia mdomo wazi.
‘Je shemeji hayo ninayozungumza ni kweli ...hukunitengenezea hayo
maneno,...’ na akilini nikajiuliza kwanini shemeji yangu hakuweza kuwaambia
wenzake kuhusu hayo maneno, wakati wanatengeneza hii katiba mpya, ili wayaweke
hayo maneno, huenda hakuwepo, na huenda hakushirikishwa, na huenda hakujua kuwa
lengo langu ni kuayaweka kwenye huo mkataba, Mume wangu aliposikia nikimtaja
mdogo wangu akasema.
‘Mdogo wangu hahusiki na haya mambo, hii katiba ni kati yangu mimi
na wewe, sema ukweli wako kama alivyokuuliza mwenyekiti, mimi ni mume
wako,unahitajika kuwa na mimi, na hii katiba ni kwa ajili yangu mimi na wewe,
na watoto wetu, wengine hawana masilahi nayo, usikatae ukweli....’akasema kwa
huruma, na mdogo wake, akanyosha mkono, akitaka apewe nafasi aongee, mwenyekiti
akasema;
‘Unataka kusema nini wewe uliyeingilia vikao vya watu,, ....wewe
ni mualikwa tu, ....na muda wako ukifika utaongea,…’akasema na shemeji yangu
bado akaendelea knyosha mkono kutaka kuongea
‘Haya hebu niambie wewe unataka kusema nini?’akasema mwenyekiti,
na shemeji yangu huyo akasema;
‘Nakubali kuwa kweli nilimtengenezea shemeji hayo maneno, lakini
sikujua kuwa alikuwa na nia ya kuyaweka kwenye hiyo katiba,...na pia mimi sijui
lolote kuhusu hiyo katiba, kuwa ilibadilishwa, na kama kuna ya zamani na
mpya,naomba kwa hilo niliweke bayana kwenu…mnisamehe kwa hilo ndugu zangu...’akasema
‘Nimewaambia mdogo wangu hajui lolote, haya mambo ni kati yangu mimi
na mke wangu, hii katiba tuliitengeneza tukiwa wawili, naomba msimuhusishe mdogo
wangu kwenye swala la hii katiba, ...’akasema kaka yake.
‘Lakini wewe unafahamu kuwa kuna katiba mbili,au nikuulize hivi je
wewe uliwahi kuziona katiba mbili tofauti?’ mimi nikamuuliza shemeji yangu.
‘Siwezi kujibu hilo swali kwasasa, kwa hali niliyo nayo, ila
ninachoweza kusema ni kuwa niliwahi kuona katiba sasa sijui utofauti wake maana
zote zinafanana, kama zipo mbili tofauti au la...’akasema.
‘Mke wa familia, hujajibu swali langu, naona unaniingilia majukumu
yangu ya kuuliza maswali,…, je hiyo katiba ndiyo katiba mliyoitengeneza
wewe
na mume wako, jibu swali ili tuendelee,..?’ akauliza mwenyekiti
Hapo wajumbe wote wakawa wananiangalia mimi, na mimi nikamwangalia mume wangu, na nilimuona
sasa akionyesha uso wa kukata tamaa, na mimi kawaida yangu sipendi kusema
uwongo, hasa mbele ya wazazi wangu, lakini kuna kitu kilikuwa kikiniuma,..ni
kwanini mume wangu bado anaendelea kusema hiyo ndio katiba halali.
Akilini nikawaza, huyu ni mume wangu nimezaa naye watoto, na
hatima ya hilo, ni kuharibika kwa ndoa, hakuna ujanja hapo, na ikitoka katiba
halali, na kwa matendo mengine aliyoyafanya basi, ndio hitimisho maana kila
kitu kipo wazi, lakini hata hivyo, mimi nilitaka mume wangu awe mkweli, akiri
kosa, na mimi ningelijua jinsi gani ya kufanya,...
Kwa hali ya mume wangu kutokutaka kusema ukweli, ilinipa shida
sana, na nikahisi huenda hana ufahamu wa kweli kuhusu kubadilishwa kwa hiyo katiba,
huenda maadui zake walihakikisha hilo haligundui, kama sio ujanja wake...,..
Mimi nikasema;
‘Ndugu mwenyekiti, naomba jibu langu lisubiri kidogo kwani kwanza,
kwa sababu kuna mambo nahitajia yakamlike, kuhusu uaminifu na ukweli wa mume wangu,
unajua yeye ametokea kwenye matatizo ya akili, sasa huenda ni kweli hana
ufahamu huo, kuwa katiba hii imebadilishwa, sasa mimi nilitaka mume wangu atoe
kauli yake ukweli,kwangu, ....’nikasema.
‘Mwanangu, mimi ndiye mwenyekiti wa hiki kikao, na ukweli, ni kwa
wote, na hapa yupo docta, anaweza kuthibitisha kuwa kweli huyu mtu hana akili
timamu…’akasema mwenyekiti akimuangalia docta
Docta akashtuka, maana anaona kama ataingizwa kwenye mtihani
mnzito.
‘Mimi kama mwenyekiti kwa niaba ya kikao hiki, tunachohitajia ni
ukweli wako wewe, usizunguke, ukweli ni ukweli, usije ukaharibu ukweli wako kwa
kungalia sura ya mtu, ukigeuza ukweli, ukawa uwongo, kwasababu ya dhamira
fulani, hata kama wewe unaiona ni kwa masilahi ya huyo mlengwa, lakini ukasema
uwongo, ukweli, ukaugeuza ukawa uwongo, wewe sio mkweli tena, wewe sio
mwaminifu tena…’akasema mwenyekiti
‘Oh…na..na..’nikasita kusema na mwenyekiti akasema;
‘Mtu mkweli na mwaminifu husema, ukweli bila kujali huyu ni mume
wangu au huyu ni mtoto wangu, au huyu ni mzazi wangu, ukweli utasimama kuwa
kweli, kwahiyo ninachotaka hapo ni ukweli wako wewe,...je hiyo katiba, kama
ulivyoiona ndio katiba halali mliyoitengeneza wewe na mume wako, usijali kauli
ya wakili, au ya mume wako, hapo ni wewe....?’akaniuliza mwenyekiti
Na mimi nikamwangalia wakili wetu, nikaiangalia ile katiba, na
sijui kwanini nilikuwa nasita kutoa kauli yangu,kuna hali fulani ilivunja
ujasiri niliokuwa nao, kuna hali ya huruma iliniingia, sijui ni kwanini,na hali
hiyo ilinijia pale tu nilipomuangalia mume wangu machoni, na kuona zile taswira
za watoto wangu .
Pale pale…nikageuka kumwangalia rafiki wa mume wangu, ambaye muda
mwingi alikuwa kimiya, alikuwa kakunja uso kama anatafakari jambo, na macho
yetu yalipokutana, nilihisi kama ananiambia, 'msaidie mume wako, japo kwa hilo tu,
unaweza ukampoteza mume wako ' na alipoona namtizama akatabasamu, na mimi kwa
haraka nikageuka kumwangalia mwenyekiti tayari kutoa jibu........
NB: Haya sehemu hii inaishia hapo kwasababu maalumu, tusichoke,
nia ni ujumbe ndani ya kisa, kwa wanaofahamu wataona ni kwanini siendi moja kwa
moja kwenye kukimaliza kisa, someni na kati kati ya mistari mtanielewa...tukutane
sehemu ijayo.
WAZO LA LEO: Ukweli utabakia kuwa ukweli, huwezi ukahalalisha ukweli kwa
kusema uwongo , kwa ajili ya kumsaidia mtu, hata kama ni mtu wako wa karibu,
ukisema uwongo, ukaukana ukweli, ili kusadidisha jambo, kwa huruma, basi
unavunja uaminifu wako, tujifunze kuwa wa kweli popote pale, ili tuwe
waaminifu.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment