Kikao kiliendelea, na mwenyekiti akawa mkali kidogo, kabla ya
kusoma dondoo nyingine za kikao, akasema;
‘Ninataka hili niliweke hili wazi, siku nyingine mkiniita kwenye
vikao vyenu, sitaki kuona kitu kama hiki, kwanza mumechelewa kufika, mimi kama
mwenyekiti natoa onyo, sipendi tabia hiyo itokee tena, mkiniita kwenye kikao
chenu mjipange vyema, muda ni mali, sina muda wa kupoteza…’akasema baba
‘Samahani kwa hilo mwenyekiti…’nikasema
‘Sijatoa nafasi ya mtu kuongea…’akasema na mimi nikabakia kimia
‘Pili sitaki mambo kama haya ya watu kujitokeza katikati ya kikao
bila mipangilio, na tatu kikao kama hiki mkinichagua mimi kama mwenyekiti wenu,
sitaki mtu kujiona yeye yupo juu yangu, mimi ndiye mwenye mamlaka ya kikao
hiki, mambo ya familia zenu mnayaweka pembeni...mnanielewa …’akasema.
‘Sawa, lakini mzee, naweza kujitetea kwa hilo…’akasema mume wangu
‘Sijataka mtu kujitetea…’akasema na mume wangu akabakia kimia
‘Naona wewe mjumbe unataka kuongea sana, au nikupishe wewe uje
hapa,..siolazima mimi niwe mwenyekiti..na kujitetea, unajitetea nini, kwani
mimi nimesema nataka kutoa adhabu leo, ninachotaka kukiweka wazi ndio hicho,
unasikia mkwe…na hapa sio mkwe, wewe ni mjumbe wa hiki kikao, au sio…’akasema
mwenyekiti
‘Ndio nimekuelewa baba mkwe…, nilitaka tu, nikuelekeze kitu kwenye
hiyo katiba…’akasema na mwenyekiti akaiangalia ile katiba halafu akaisogeza
pembeni na kusema;
‘Hapa hatuongozwi na hii katiba yako,…maana sisi hatuijui, au
nimekosea wajumbe, au niwaulize wajumbe je mnaifahamu hii katiba..?’ akauliza
na wajumbe wakakaa kimia, na ndipo akaanza kuuliza mtu mmoja mmoja…
‘Docta na mkewe, mnaiafahamu hii katiba…?’ akauliza mwenyekiti
‘Hatuifahamu ndugu mwenyekiti…’akasema docta, na mkewe akabakia
kimia.
‘Na…nimuulize na nani, haya wewe uliyetuingilia kwenye hiki kikao,
nikuulize wewe unaifahamu hii katiba…?’ akaulizwa shemeji mtu
‘Mhh..naifahamu kwa mantiki…’akatulia
‘Ongea, usiwe na wasiwasi, nimekuuliza … kwa hivi sasa unaweza
kuongea tu…haya kwa mantiki gani..?’akaambiwa na kuulizwa.
‘Naifahamu kwa vile nimemuona kaka akiwa nayo…’akasema
‘Ukajua kuwa ni katiba , au kwa vile imendikwa hapa juu, …Je yaliyoandikwa
ndani unayafahamu, yanakuhusu wewe..umeshawahi kuyasoma..?’ akaulizwa
‘Hayanihusu, siku-ya-yasoma kwa sababu hayanihusu…’akasema
‘Kabla ya kaka yako kuionyesha hii katiba hapa, uliwahi kuiona
wapi kabla…?’ akaulizwa
‘Mhh…niliwahi kutumwa na kaka, …kuichukua nyumbani na kumpelekea
hospitalini…’akasema
‘Kwanini alikutuma wewe…?’ akaulizwa na kukaa kimia
‘Nduguzanguni, ninachotaka kukielezea hapa, ni jinsi gani katiba
hii isivyowahusu watu wengine, zaidi ya familia husika,… haya ya
kwanini…kukuhusu wewe bwana mdogo yatakuja baadae maana mpaka hapo nimegundua
jambo….wewe ndiye unayetumwa kila kitu na kaka yako, au sio…?’ akaulizwa
‘Sio kila kitu mwenyekiti,..ila mara nyingi ananituma…’akasema
‘Kwahiyo wewe umeifahamu hii katiba kwa kutumwa, na sio kuwa
inakuhusu au sio..?’ akaulizwa
‘Ndio mzee, …hainihusu…’akasema
‘Je kwenye kikao hiki inastahiki kutumiwa..kuongoza hiki kikao,
..?’ akaulizwa
‘Hapana mzee, nionavyo mimi, hiyo ni katiba ya wanafamilia, na
sisi wengine haituhusu, natumai hilo ni jibu la wote, au sio …’akasema na
wajumbe wakatikisa kichwa kukubaliana na hilo
‘Sawa kabisa, kumbe kweli unaifahamu kuwa ni ya wanafamilia, na
huenda unaifahamu zaidi ya hilo…mmh, mawakili, nyie kwanza siwaulizi hili, hata
mke wangu hapa simuulize maana yeye yupo na mimi, au nikuulize mke wangu,…’akasema
akimgeukia mama
‘Hapana endelea tu mwenyekiti, tujali muda…’akasema mama, na baba
hapo akanigeukia mimi akitaka kuniuliza lakini akaghairi na kugeukia kikao,
akasema;
‘Tujali muda, msaidizi wangu wa nyumbani kaniasa hilo, haya tuliache
hilo kwanza, ..nilitaka ndugu mjumbe, mume wa familia kuliweka hili sawa, kuwa
kuna mambo ya kurejea katiba yako ni sawa…, na kuna mambo ambayo hayastahiki,
na hili la kuongoza hiki kikao, halihitaji katiba yenu, katiba ya hapa ni
dondoo za kikao na mimi mwenyekiti ndiye ninayeziongoza hizo, au sio…’akasema
mwenyekiti
‘Sawa mwenyekiti nimekuelewa…’akasema mume wangu na alitaka
kuongeza neno, lakini mwenyekiti hakumpatia nafasi,…
‘Kingine kuna mambo nataka kuyaweka wazi, ndio mna katiba mna
utaratibu wenu wa kimaisha kama familia ni sawa pia…, mimi sikatai, na
nimefurahi kama mlifikia hatua hiyo,lakini ninataka niwarejeshe nyuma kidogo,
niwakumbushe, nyie wanandoa….’akasema na kumgeukia mume wangu
‘Nilishasema kwenye familia yetu hatutaki mambo ya kashifa,
ikiwemo kuvunja sheria za ndoa na za nchi, na kuvunja sheria ni swala pana
zaidi, ni pamoja na uwongo, kusalitiana, na kugushi, na mambo kama hayo,
..mambo ambayo yanatuharibia jina letu,achilia mbali kuua, ambalo ni kosa la
jinai ....hilo niliwakanya tangu mapema, na nilisema hata kama ni mtoto wangu
kafanya hayo, sitasita kumfikisha kunakostahili..
Nilifanya hilo kwa binti yangu, niliposika kakamatwa, sikukimbilia
kumtoa, nilifanya uachunguzi wangu ili niupate ukweli, sijamlea binti yangu awe
mvunjifu wa sheria,..hilo najisifu…sasa kama akitaka kunisaliti na mimi
nitawajibika kwa hilo..hakuua, na ndioa maana nilimsaidia…’akatulia,
‘Sasa kwako wewe mume wa familia,…’akasema
‘Ndio mwenyekiti, nakusikia….’akasema mume wangu
‘Ni kwanini hayo, ni kwanini niliwaasa mapema hilo jambo…’akasema
halafu akatoa gezeti, na kulikabidhi kwa mume wangu
‘Hebu soma hicho kichwa cha habari hapo juu…’ akaambiwa mume wangu
na akawa anasita kulipokea, halafu akalipokea, na kusoma
‘Mkwe wa familia ya mzeemkongwe wa siasa,(akataja jina) anashukiwa
kwa mauaji ya wakili wake…’akaliachia lile gazeti kama kashika kitu kichafu
‘Sio kweli mzee, waongo hawa, watu wa udaku hawa…’akasema
‘Hebu soma na hili…’kampa gezeti jingine
‘Mkwe wa…’akasoma hivyo tu na kuliweka pembeni, akasema
‘Ina maana mzee unaamini haya magazeti, haya hayakufai
mzee…;akasema
‘Hebu nikuulize mimi ni baba yako…?’ akauliza mwenyekiti
‘Ni baba mkwe, mwenyekiti..’akasema
‘Kwanini hao watu wa magazeti hawajaandika, jina lako na baba
yako, wakaandika mkwe wa…unaelewa mantiki yake..?’ akauliza
‘Ni magazeti ya udaku hayo tu mzee…’akasema
‘Hujanijibu, hata kama ni ya udaku lakini yanasoma na watu wengi
kuliko hayo magazeti mengine,…nimekupati hayo magazeti kama mfano…kukuonyesha
ni kwanini, ..nilikuasa mapema kabla hujaoa kwangu..’akatulia
‘Ni kwasababu mimi nipo kwenye ulingo wa kisiasa…silifichi hili,
kuwa katika siasa kuna upinzani, na kila mmoja anajaribu kutafuta kashfa za
mwenzake..ili afanikiwe kwenye ulingo wa siasa, hilo linakubalika, kisiasa,
ndio maana najihami, na wenye lengo jema na mimi watanisaidia kwa hilo,
mumenielewa jamani, mimi naongea sana …’akatulia
‘Lakini baba hayo ni maswala yako, na sisi hatuwezi kuyaingilia…au
sio jamani..’akasema mume wangu.
‘Ndio maana ulipokuja kuoa kwangu nilikuambia hilo mapema tu, kuwa
mimi nipo hivyo, na maisha yenu yawe vipi..na hayo maisha yenu, kuwa vipi sio
kwamba nawataka muwe kama mimi, hapana, niliwatahdaharisha kuwa ningelipenda
maisha yenu yawe mfani wa mume na mke bora…kweli si kweli…?’ akaulizwa
‘Ni kweli mzee…’akasema
‘Sasa tatizo lipo wapi, nimekosea nini hapo, kuyakemea hayo
yanayokwenda kinyume na maadili ya mke na mume bora, nimekosea nin kuyakemea
maovu, ..sitaki kashfa, na nilisema kama mtu hataliweza hilo, asioe kwangu,
hata binti yangu nilimuwambia kama mume wako ..hana maadili mema, usikubali
akuoe, akasema , atahakikisha mume wake yupo kwenye njia sahihi, kweli si kweli…’akasema
na kuniuliza mimi, na kabla sijajibu mimi, mume wangu akasema;
‘Ni kweli mzee, mke wangu kanisaidia sana, na tunaishi vyema tu…mengine
ni udhaifu tu wa kibinadamu…’akasema.
‘Sasa mimi nisingelikaa kimia tu, mfanye mtakavyo, na baadae mje
kunisema kwanini mimi sikuwahi kuwaambia hilo, je sikukuambia hilo mapema,
wakati unakuja kuoa kwangu…?’ akauliza mwenyekiti kumuuliza mume wangu
‘Uliniambia mzee…lakini..’akasema mume wangu
‘Sitaki lakini, huko kujitetea kuwa ni udhaifu wa kibinadamu, sio
utetezi, ufanye makusudi halafu usingizie ubinadamu, hakuna hilo..unasikia
‘Sasa…kama kuna kujitetea utakuja kujitetea sana…au kama unataka
kujitetea, basi nikuuliza ni kwanini umeyapinga hayo maagizo yangu, Ulidharau
sio …kwa vile sasa una mamlaka kama ulivyoanza kunialati ..kuwa mna katiba
inayokulinda…?’ akauliza
‘Hatujayapinga maagizo yako mzee, labda ni katika kuwekana sawa tu,
au kuwajibika kama limetokea hilo ni kwa bahati mbaya tu mzee, na kashafa gani
kubwa tumefanya sisi, kwangu mimi sijaiona, ni mambo ya uzushi tu..’akasema
‘Kufikia hadi kuua, sio kashfa…?’ akaulizwa
‘Mzee nani kaua, hakuna mtu aliyeua hapa,..huo ni uzushi, na
polisi wanafanya hivyo kikamata watu katika kuhangaika kumpata muhalifu, lakini
sio kweli…’akasema
‘Kutoka nje ya ndoa na kuzaa ovyo sio kashfa…?’ akauliza mzee
‘Aaah, huko mzee umeenda mbali, ..hapana mzee, ni maneno ya watu tu, waongo hao…’akasema
‘Una uhakika na hilo jibu lako..?’ akauliza mzee
‘Kwanini mzee unauliza hivyo, mke wangu hajafanya hilo, walimfunga
kimakosa, wakimshuku kuwa ameua, na sio kweli, hata wewe mwenyewe
umelithibitisha hilo…’akasema
‘Sijamuulize mke wako, nimekuuliza wewe, uliyekuja kuoa kwangu,
umesema hujafanya kashafa kubwa, au sio,…na unavyoonekana kuzaa nje kwako sio
kashfa, anyway…mimi najaribu kukuweka sawa hapo, au wewe kashafa kwako ni ipi,
ya wizi, ya kuhujumu au nini kashafa kwako…?’ akauliza
‘Mzee mimi sijafanya kashafa kubwa kihivyo, ya kukuharibia mambo
yako kisiasa ndio utetezi wangu huo…’akasema
‘Haya mume wa familia, ngoja tutakuja kuliona hilo…,’akasema
mwenyekiti
‘Sawa mzee nitajitetea kwa shutuma zote, nina imani utakuja
kunielewa…’akasema
‘Ngoja tusipoteze muda, twende kwa mujibu wa utaratibu wa kikao,
dondoo zinasema sasa ni wakati wa kumkaribisha mwenyeji wa kikao, mtu
aliyetuita hapa kwenye kikao, kuelezea duku duku lake, lakini kabla
sijamkaribisha, nataka yeye anipe maelezo sahihi, maana yeye amekuwa muda wote
akitetea ndoa yake, mume wake nk..sasa nataka haya uyaweke wazi, pamoja na hayo
uliyotuitia…’akatulia kwanza akiniangalia mimi, halafu mume wangu
‘Ni kwanini sisi wazazi wenu tusiingilie familia yenu, wakati
mumeshaingilia familia kuu, kwa matendo yenu yenye kashfa, ushahidi mmojawapo
ni hayo magazeti, ina maana mumefanya mambo ambayo yamekiuka yale makubaliano yetu
ya awali…ni kwanini sisi kama wanafamilia kuu tusichukue maamuzi, tuliyoona ni
sahihi, kwa masilahi ya familia na vizazi vijavyo,…hili ni muhimu.’akasema
mwenyekiti na mume wangu akawa anataka kuongea
‘Tulia…’mwenyekiti akasema na mume wangu akatulia.
‘Ni kwanini nyie watoto mnatengeneza katiba ya kutuzuia sisi
wazazi wenu tusiwaingilie hata kama mumeshindwa kutimiza wajibu wenu ndani ya
familia zenu, sitaki kusema yapi ni yapi mumeyakiuka, lakini kwa ujumla wake,
mumetia doa familia yetu, haijawahi kutokea hivyo kabla, je ni kwanini, na kuna
nini...’akasema na kuniangalia mimi, kabla sijasema kitu, mume wangu akanyosha
mkono na hata kabla hajaruhusiwa akasema;
‘Mimi kama mume wa familia inayoshutumiwa kwa kukiuka hayo
aliyosema baba, nataka kuelezea ni kwanini hayo yalitokea, naomba niongee mimi
kwanza kabla hajaanza kuongea mke wangu japokuwa ni yeye aliyeitisha hiki
kikao,....’akasema na baba, akataka kumkatiza lakini mimi nikasema;
‘Mwenyekiti, hebu muache kwanza aongee amalize yote…na akimaliza mimi
nitaongea tu...’nikasema
‘Kikao ni lazima kiwe na mpangilio, sio kwamba mimi sifahamu hilo,
kuwa wewe ni mume wako familia, hata mimi ni mume wa familia, tena ni baba mkwe
wako, au wewe ni familia special,..mmh, …’akasema mwenyekiti kwa ukali
‘Hapana mzee…nilitaka kujibu shutuma zako mzee…’akasema
‘Hiki kikao sio wewe
uliyekiitisha, tumeitwa na mke wako, na hii ipo kwenye ajenda ...na kama
nilitaka wewe uongee, ningelikupa hiyo nafasi, sipendi kabisa huo utaratibu
wako…’akasema mwenyekiti
‘Na nikuambie kitu,.., heshima ni muhimu sana,..sawa kwa vile mke
wako kakuruhusu uongee, sijui labda ni heshima au ni kwa mujibu wa katiba yenu
kuwa hawezi kuongea mke mpaka wewe umnyoshee njia, …haya ongea kama ulivyotaka
wewe, maana kila hatua mnazidi kunionyesha jinsi gani mlivyo....’akasema baba
na mume wangu bila kujali akasema;
‘Nakubali kuwa kuna udhaifu ulitokea, na hilo linaweza kutokea kwa
yoyote yule, hasa mnapokuwa katika harakati za kutafuta maisha, kuna changamoto
za hapa na pale,..huenda katika kuyafanikisha hayo tulijaribu njia ambayo sio
stahiki, ...ni katika kujaribu, ndio tukajikuta tumeteleza,..naomba tusamehewe
kwa hilo...’akasema.
‘Lakini, pamoja na hayo, mimi nimeshaitoa katiba yetu, ambayo inanilinda
mimi jamani, sifanyi haya kwa vile..hapana ni kwa mujibu , ndio maana nikaitoa
hiyo katiba hataka kama haiwahusu wote, lakini kikao hiki kinahusu familia
husika …samahani kwa hilo mwenyekiti maana mimi nitakuwa narejea mara kwa mara
hiyo katiba, kwa mantiki ya kulinda familia yangu…’akasema
‘Endelea…’akasema mwenyekiti
‘Kama kuna kitu kinaitwa makosa,au kashfa imefanyika, ..kama
nilifanya mimi, basi ujue nilifanya kwa nia njema tu, na kama nilitenda jambo
fulani, kama mume, nina haki zangu, kisheria...na nilifanya mengine kwa
minajili ya msilahi ya familia, hatujui kama linakizana na wewe kisiasa, sijui
mimi kama hayo ni kashfa..’akatulia
‘Endelea…’mwenyekiti akasema alipoona mjumbe yupo kimia kidogo
‘Na ningelipenda kuliweka hili wazi kwa nia njema tu kuwa, sisi
kama familia tuna sheria na taratibu zetu, kwa vile ni familia inayojitegemea,
kama mtaona tumekwenda kombo, ni swala la kutushauri tu, na sio kutuingilia
kiasi cha kutoa hata adhabu,...’akasema
‘Endelea…’akasema mwenyekiti
‘Mwenyekiti, katiba yetu ipo wazi, inatulinda, inanilinda mimi
kama mume wa familia, naomba hilo liwekwe bayana, hakuna familia nyingine yenye
mamlaka ya kutuingilia, au kutuadhibu sisi kinyume na hiyo katiba,
hakuna…sheria hiyo, hivi mimi kweli naweza kuja kuingilia familia yako mzee,
hakuna kitu kama hicho..nachukulia mfano huo sio kwa kukosa adabu naomba
nieleweke hivyo...’akasema na kukaa kimia
‘Umemaliza...?’ akauliza mwenyekiti
‘Ndio mwenyekiti, nilitaka kuliweka hilo wazi tu, maana nimeona
ukitoa vitisho kwenye utangulizi wako..’akasema
‘Sio vitisho mjumbe…, hayo niliyoongea ni kweli na yatafanyika
hivyo…’akasema mwenyekiti
‘Itabidi nimuite wakili wangu kwa hilo…’akasema mume wangu
‘Wa nini..?’ akauliza mwenyekit
‘Unavunja katiba yangu na familia yangu…’akasema
‘Wapi nimevunja katiba yako..?’ akaulizwa
‘Unatoa lugha za vitisho, kuwa nyie kama familia kuu mnaweza
kutuwajibisha, ..na vitu kama hivyo, hilo halikubaliki…’akasema
‘Usitupotezee muda, na katiba yako, hii ambayo bado sijaimini,
…’akasema
‘Ukisema hivyo mzee utakuwa unatuingilia, na kuvunja kanuni na
sheria za nchi, katiba hiyo, inatambulikana maana tumeisajili …au unaniona mimi
sifai kuwa mume wa familia…?’ akauliza
‘Sikiliza mume wa familia, ni matendo yako.. , kama ulikubali kuoa
kwangu, ujue una wajibu wa kutunza heshima yangu, sio kwamba nakuingilia, ...na
sina haja ya kukuingilia, ila kama umevuka mipaka sitasita kukuwajibisha, kama
umefanya mambo yenye kuleta kashfa kwenye familia hilo sitalivumilia kamwe,
umenisikia, ilibidi mliweke hilo kwenye katiba yenu, maana ndio katiba ya awali
wakati unaoa kwangu..’akasema mwenyekiti.
‘Katiba ya familia yangu inanilinda ndugu mwenyekiti samahani sana
kwa hilo, mtaniona napoteza muda kwa hilo, lakini ni lazima hilo lieleweke
maana nafahamu ni nini kinachofuatia,..mimi sitakubali jambo lolote liende
kinyume na katiba yetu ya familia, lije livuruge ndoa yangu, sitakubaliana na
hilo..’akasema mume wangu, na mwenyekiti akaichukau ile katiba na kuinua juu na
kuuliza
‘Hii ndio Katiba unayosema inakulinda?’ akauliza mwenyekiti
‘Ndio mwenyekiti, hebu
gauze huku, ehee, ndio hiyo hiyo...’akasema mume wangu.
‘Katika katiba yenu halali,…sijui kama ni hii, mlikubaliana kuwa kila kilichoandikwa
kitasimamiwa, kitatekelezwa, na sheria itafuata mkondo wake, si ndio hivyo,
kama mmoja akikosea, kutokana na mlivyokubalia atawajibishwa kisheria, hata
kama ni kuvunjika kwa ndoa..., au sio?’ akauliza mwenyekiti
‘Ndio…hahaha, kumbe uliwahi kuisoma, …ndio hivyo
mwenyekiti…’akasema
‘Sijaisoma hii, maana mimi bado sijaihakiki, kisheria,…nakuuliza
tu kama kipengele hicho kipo…’akaambiwa
‘Ndio tumekubaliana hivyo, na kila mmoja analifahamu hilo, ndio
maana tukaisajili hiyo katiba, na mimi nipo tayari kuwajibka kwayo, hiyo hapo
isome,utaona kila kitu kipo wazi, hakuna nilichokosea hapo,..’akasema ni
kunigeukia mimi. Sikusema kitu
‘Lakini unaposema kuvunjika kwa ndoa una maana gani mzee?’
akauliza alipohisi kuna kitu kategwa.
‘Unaniuliza tena mimi, si kipengele hicho kipo kwenye katiba yenu
halali au sio, si umakubali kuwa kipengele hicho kipo, au..…’akasema mwenyekiti
‘Nahisi hukusoma sehemu yote kwa ukamilifu wake, ukisoma vyema
hiyo katiba utaona kuwa mimi ndiye mwenye usemi wa mwisho kuhusu ndoa, na
ndivyo ilivyo hata kwenye dini…au sio,..na mimi kama mume, siwezi kukubali ndoa
yangu ivunjike, nitailinda kidini na kikatiba yetu hii ya
familia,tuliyokubaliana nayo..’akasema
‘Nauliza tena, upo tayari kuwajibika kutokana na katiba yenu
halali,ambayo inatambulikana na msajili wa katiba,… ?’ akauliza mwenyekiti
‘Ndio nimeshakuambia hilo, yote yapo wazi kwenye hiyo katiba,
sioni kwanini uniulize swali hilo, wakati katiba unayo hapo, isome tu mzee, ili
kila mjumbe asikie hilo,.. na mimi nimekubali na sahihi yangu ipo na ya mke
wangu ipo na ya wakili wa familia pia…wakili ambaye anayetambulikana na mke
wangu, au sio mke wangu..?’ akauliza mume wangu.
‘Unajua kuongea sana siku hizi..’akasema mwenyekiti
‘Hapana ni lazima nionyeshe uhalisia, mimi kama mume wa familia,
uliniozesha mimi, niwe mume wa binti yako, kwanini nisiongee kutetea ndoa
yangu, hata wee utanishangaa nikikaa kimia, au sio..’akasema
‘Huyo wakili aliyesimamia huo mkataba wenu ni nani..?’ akauliza
mzee, kabla mimi sijasema neno, na mume wangu kwa haraka akasema;
‘Ni wakili wa familia, yule pale,….akatae kama sio yeye
aliyetayarisha hiyo katiba, sahihi yake ipo, hawezi kuikana, au…muulizeni yeye mwenyewe…’akasema
‘Nakumbuka awali ulilalamika kuwa mbona wakili wako hayupo, ina
maana wewe una wakili mwingine zaidi ya huyo…?’ akaulizwa
‘Ndio yupo..’akasema
‘Ni kwanini sasa ukatafuta wakili mwingine kama huyu ndiye
aliyewawekea sawa hiyo katiba yenu halali, inayosimamia kila kitu kwenye
familia yenu mpaka hapa unatulizimisha na sisi tuifuate,…?’ akaulizwa kabla
hajajibu mzee akaendelea hapo hapo kwa kusema;
‘Huyo si ndiye wakili wa familia sio, na katiba hiyo halali,
ameiweka yeye sawa kisheria, maana nyie ndio mlitayarisha mawazo yenu, mkajadiliana
kila mmoja akatoa mawazo yake kipengele kwa kipengele, wakili yeye, alichofanya
nikuweka sawa hivyo vipengele kimoja baada ya kingine ili vikae sawa kisheria,
kweli si kweli...?’ akaulizwa
‘Ndio mzee,… ni wakili wa familia, lakini kiutendaji, mimi kama
mume wa familia niliona kuna haja ya kuwa na wakili mwingine,, ukiangalia
kwenye hiyo katiba inanipa mamlaka hayo ya kufanya mambo nikiona ni sahihi kwa
masilahi ya familia,…mimi niliona kuna umuhimu wa kuwa na wakili mwingie, sio
mbaya wangapi wana wakili zaidi ya mmoja..’akasema
Mwenyekiti akaangalia saa, halafu akaangalia pale walipokaa
mawakili, halafu akasema;
‘Kabla sijamuuliza wakili kulithibitisha hilo, nakuuliza maswali
haya muhimu napenda uyajibu ukiwa na uhakika nayo …’akasema mwenyekiti
‘Uliza tu mzee, sina wasiwasi kabisa, mimi nipo hapa kwa ajili ya
familia yangu ,na ndoa yangu…’akataka kuendelea na mzee akauliza
‘Kwahiyo kwa jinsi ilivyo, nyie maisha yenu , majukumu yenu, na
kila kitu, siwezi kusema kila kitu, ila mambo yote muhimu yanategemea huo
mkataba halali…?’ akaulizwa
‘Ndio mzee, unatusaidia sana…’akasema
‘Na je mtu akikosea, kuna vipengele vya hukumu,..?’ akaulizwa
‘Ndio vipi, hatukubakiza kitu…’akasema
‘Kwahiyo wewe kama umekosea,au mke wako kakosea, haihitajii kwenda
mahakmani, hukumu zipo wazi, na hukumu hizo zinaweza kusimama kama ushahidi
unajiotosheleza..?’ akaulizwa
‘Ndio kabisa…’akasema
‘Na wewe hapo ulipo, upo tayari kuhukumiwa kwa mujibu wa katiba
yenu halali…?’ akaulizwa na hapo kidogo akasita
‘Kwa mujibu wa katiba yetu ndio…kama inavyosema ..ndio…kila kitu kipo
wazi, na nashangaa kwanini mke wangu akaamua kuitisha kikao kama hiki, labda
kama anaona yaliyopo kwenye hio katiba, hayafai, tubadilishe, labda, iwe hivyo,
vinginevyo, sisi hatukuwa na haja ya vikao kama hivi..’akasema
‘Sasa nakuuliza swali, hili swali ni muhimu sana, nataka ujibu
ukiwa na uhakika, maana baada ya hapa, sisi kama kikao, mimi kama mwenyekiti
sitarudi nyuma tena, maana sikutaka iwe hivi, ila wewe mwenyewe umenilazimisha
nifanye hili, kila mara katiba katiba, haya …ngoja tufuate katiba yenu, pamoja
na mengine ambayo ni muhimu kwenye hiki kikao…
Sasa hili nahitajia jibu lako kutoka moyoni, uwe na uhakika nalo..’akasema
na mume wangu akasubiria,…
‘Je una uhakika kuwa hii ndio katiba halali mliyokubaliana wewe na
mke wako,...?’
Alipoulizwa swali hili akatulia kwanza akionyesha uso wa
kushangaa…, halafu akageuka na kuniangalia mimi, mimi nikawa natoa tabasamu tu,
lakini sikusema neno, yeye akasema;
‘Kwanini unaniuliza swali kama hilo mzee, kwani wewe ulikuwepo
wakati tunaitengeneza hiyo katiba mpaka utoe kauli hiyo ya shaka,…, kuwa labda
unaifahamu katiba nyingine zaidi ya hii…’akasema
Mwenyekiti akamuangalia tu, na yeye akaendelea kuongea kwa kusema
‘Ndugu mwenyekiti, wewe usisikilize maneno aliyonitania mke wangu
awali, hakuna katiba mbili, na mimi ndiye ninayeifahamu hiyo katiba kwa vile
mimi ndiye mume wa familia yangu, katiba ndio hiyo hakuna katiba nyingine…’akasema
‘Sikutaka maelezo mengi kihivyo, …nataka jibu la uhakika, …nakupa
dakika moja ya kulifikiria hilo jibu lako vyema, ni muhimu sana kwangu na kikao
hiki kilisikie hilo jibu kama ushahidi…, ‘ akasema
‘Kama ushahidi…!!’ akauliza mume wangu
‘Ndio…nataka kupima uadilifu wako wa ndoa…nataka katiba yako
yenyewe ifanye kazi, si wewe umelisisitiza hilo, au unaanza kuogopa…?’
akaulizwa
‘Hapana..siogopi, maana naifahamu vyema katiba yangu, wewe uliza
swali lako tu..’akasema
‘Wewe unatamba kuwa wewe ni mume mwema wa familia,,kama kweli wewe
ni kiongozi muadilifu wa familia, nirudia
swali langu, kumbuka uwongo, kugushi, wizi..kuua, ni moja ya mambo yanayokiuka
sheria, sijui kwenye katiba yenu mumeyawekaje hayo, na kuna mambo ukiyafanya,
unavunja ndoa,.., sasa nataka uwe muwazi kwa hilo, kama huna uhakika useme...’akasema
mwenyekiti
Mume wangu hapo akakaa kimia kidogo, na mwenyekiti akauliza tena….;
‘Je kweli wewe una uhakika kuwa hii ndio katiba halali,
mliyoitengeneza wewe na mke wako, ikasainiwa na wakili wa familia yenu..nasisitiz
hapo, tena, je una uhakika nataka unijibu, na nataka uchukue muda kuliwazia
hilo jibu lako…’akasema mwenyekiti akiangalia saa yake.
Nilimuona mdogo wake aliyekuwa pembeni, akiinamisha kichwa chini,
kama anaomba, halafu akainua mikono na kujishika kichwani, akainua kichwa na
kumuangali kaka yake,…
Rafiki wa mume wangu docta, alikuwa makini kweli akifuatilia hatua
kwa hatua, na alipoona mdogo mtu anahangaika, kutaka kuongea, akamuangalia na
nahisi alikuwa anataka kumuashiria huyo mdogo mtu atulie…
Sasa nikamuona mdogo mtu kama anataka kunyosha mkono aongee,
lakini akarudisha, alipokutanisha macho yake nay a docta, kiukweli hata mimi
pale nilipokaa, ..nilitamani huyu shemeji mtu aongee huenda ana jambo muhimu la
kumsaida kaka yake, lakini sikuwa na jinsi ya kuingilia hilo
Nikageuka sasa kumuangalia mume wangu, alikuwa akitabasamu tu hana
wasiwasi, akasema;
‘Naweza kujibu mwenyekiti, mimi sina wasiwasi…’akasema na
mwenyekiti, kabla hajamjibu akaangalia saa yake
NB: Mambo yamenza, ushaidi wa kwanza wa kupima ‘uaminifu kwenye
ndoa’.
WAZO LA LEO: Uongozi
ni wito, uongozi ni kubeba dhamana za watu, na ukiwa kiongozi mwadilifu, watu
wako ni kwanza, na wewe unakuja baadaye, kwahiyo kimasilahi, utahakikisha
kuwa watu wako wametosheka kwanza, kabla ya kujali tumbo lako, huo ndio uongozi
bora.
Je kiongozi kama huyo yupo
katika hii dunia ya sasa,...
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment