Nilifika sehemu ambayo huwa tunafanyia vikao vyetu, ni kazini
kwangu , lakini kuna sehemu maalumu imejengwa kwa ajili ya vikao, na siku hiyo
sehemu hiyo ilipangwa mahsusi, kwa ajili ya hicho kikao cha familia yangu.
Nilipofika kwenye chumba cha mkutano nilimkuta baba keshafika, yeye
alifika mapema tu baadae akafika mama,
baba ni mtu anayejali sana muda.
Nilipofika tu nilimkuta akipitia makabrasha yake, na lapotop yake
ikiwa pembeni, akionyesha kuwa anakwenda na wakati, na mar simu yake ikawa inaita, hapo akawa na
wakati huo alikuwa anataka kuongea na mimi.
‘Tafadhali bint, karibu, ngoja niongee na hii simu…’akasema na
mimi nikawa nimekaa kwenye kiti nikisubiria amalize kuongea na
simu,…alipomaliza tu, akaanza kunilaumu akisema;
‘Nilitarajia watu watafika kwa muda, lakini naona dakika tano
zimepita, siwaoni watu, ..’akaanza kulalamika
‘Foleni na hulka zetu baba, lakini nina uhakika wote watafika,
ambao ni muhimu kwa kikao hiki,....’nikasema
‘Sawa hebu kaa kwenye kiti tuanze kuongea yetu, ya baba na
binti yake, wewe mama unaweza kukaa kimia kwanza, usiingilie….’akasema
‘Sawa mimi siunaniona sina maana kwako…’akalalamika mama
‘Hapana unakaribishwa nilikuwa natania tu…’akasema baba
‘Umafanikiwa ulichokwenda kununua…?’ baba akamuuliza mama kwanza
‘Ndio…japokuwa sio vyote,…’akasema mama
Mama alisema alipitia kumfanyia manunuzi binti yake, nguo na
vifaa, vya safari ya huyo bint.
‘Ni binti gani huyo?’
nikamuuliza.
‘Utamuona tu , na yeye atakuwepo kwenye kikao, ....’akasema na
sikutaka kumuuliza zaidi, kuhusu huyo bint.
Nilipotulia kwenye kiti, baba akaniangalia kwa makini kama
ananisoma kwenye ubongo wangu, halafu akasema;
‘Nilitaka kufahamu maamuzi yako, nataka nijue ni nini msimamo wako
baada ya haya yote, nataka nikushauri kama baba yako, kama mzazi wako, japokuwa
mimi na mama yako tumeshaongea na kufikia uamuzi wetu, ambao sio tofauti na ule
wa awali, kwa nia njema tu lakini yote inategemea nyie wenyewe,....’akasema
‘Baba maamuzi yangu yatatolewa mbele ya wahusika, ninawahitajia
wenyewe waje wathibitishe waliyoyafanya, ninataka kusikia kauli zao kwanza, je
wamesimamia wapi, kwenye ukweli au kuficha ukweli..’nikasema
‘Sio rahisi mtu kukubali kosa kwanza, hasa akijua madhara
yake..’akasema baba
‘Sasa kwa vile watakuwepo, ngoja tuwasikie kwanza , yote
yaliyotokea tutayamaliza kwa amani na salama, kutegemeana na wao wenyewe, vinginevyo, kama ndivyo walivyo, na
watang’ang’ania kuwa waongo, basi baba mimi nitanawa mikono..’nikasema
‘Hebu niambie wewe ulishafikia wapi, maana uliniambia kuwa
unafanya uchunguzi, na utakuja kutoa maamuzi yako mbele ya kikao, ..nataka
kuona mtoto wangu anaongea kama mimi, au zaidi ya mimi, unanielewa, nataka
niione kazi yangu kwako, kama huwezi uniambie, nitajua ni nini cha
kufanya...’akasema
‘Hivi baba hujaniamini, baada ya yote hayo niliyoyafanya, baba
mimi sio mtoto tena, ni mtu mzima nafahamu ni nini ninachokifanya, nimeweza
kuisimamia kampuni yangu bia kutetereka, na ikawa kubwa, kama unavvyoiona,
nimetulia kidogo baada ya matatizo na mume wangu, lakini kuna msaidizi wangu
ambaye anaifanya hiyo kazi vizuri tu, japokuwa sasa naona mume wangu kaamua
kuingilia kati, lakini ni kwa muda tu, baada ya hiki kikao nitarejea tena kwenye
ulingo wangu..’nikasema
‘Binti yangu, sio kwamba nakushusha chini katika utendaji wako wa
kazi, hapana, kiukweli unajitahidi sana, hata mimi najisifia mbele ya wenzangu,
lakini hili lililotokea, ....mmh, limekushusa, haya yaliyotokea kati yako na mumeo
wako, imeharibu kila kitu. Unafahamu kupanda juu, kunachukua muda, akini
kushuka, ni mara moja tu...’akarudisha kichwa na kuegemea kiti, haafu akasema;
‘Baba mimi sijashindwa kabisa kuiongoza familia yangu, na
unapozungumza hivyo, unasahahu kuwa mimi ni mke wa mtu, ambaye nina mipaka yangu,
...lakini hata hivyo, sio kwamba nimeshindwa kuiongoza familia yangu kama
mke...nimejitahidi kufanya yale ya mpaka wangu, kwa kadri ya uwezo wangu,
yaliyotokea yamekuwa changamoto kwangu..na sizani kwamba nitafanya hayo makosa
tena,..kamwe, baba niamini, ....’nikasema
‘Binti yangu, Usije ukaharibu, .mimi hilo sitakubali, kwasababu
tabia ya kizalia haina dawa, hayo waliyokufanyia ni mwanzo tu, ujue chini kwa
chini kuna dhambi za damu ya mtu, unafikiri hiyo damu itafukiwa kwa mchanga tu
hivi hivi, hata kama tutayamaliza kienyeji, lakini sio sahihi, kuna mtu
kauwawa, hakuna haki iliyotendeka, hata kama alikuwa na madhambi yake, watu
wanasema aheri kafa, lakini ni wapi sheria ilisema auliwe hivyo,hilo uliangalie
kwa makini..’akasema
‘Baba mimi naomba unipe nafasi hiyo, kama nitakuwa nimekosea
mtanisahihisha, lakini nina imani kila mmoja atajihukumu mwenyewe muda ukifika,
uwongo na hadaa una mwisho wake, ...wewe subiria, tu, tusichukue maamuzi kabla
wenyewe hawajajitetea tukaona ukweli upo wapi..’nikasema.
‘Na muda mfupi uliopita nilikuwa nawasiliana na mkuu wa upelelezi
wa kituo chenu, na yule aliyefuatilia kesi ya mauaji ya Makabrasha, wameniambia
mengi ambayo wameyagundua wao kama wao,…’akasema na kabla hajaendelea watu
wakaanza kuingie, ikabidi tukatize mazungumzo;
**********
‘Hivi mama huyo bint yupo wapi…?’ nikamuuliza mama
‘Ataingia tu usiwe na wasiwasi, hatutaki watu wamuone sana, na iwe
ni maswali mengi, ataingia kwa muda muafaka akihitajika, baba yako kasema kuna
muda atamuita, lakini sio kwasasa ..’akasema mama
‘Ni muhimu kulifahamu hilo, maana hayupo kwenye orodha ya wajumbe
wanaohitajika kuwepo, kikao hiki kipo kisheria…’nikasema
‘Usijali, mimi nimemuita kama mwenyekiti…nitamlinda, na
kumdhamini,…’akasema baba.
Muda wote tuliokuwa tukiongea mawakili walikuwa upande mwingine
wakiongea yao , hawakutaka kuingia mambo ya kifamilia hasa pale tulipokuwa
tunaongea na baba, lakini kwa hivi sasa wakasogea karibu, kwenye meza kubwa
‘Nyie mawakili wetu mtakaa kimia, ila mkihitajika kuongea au
kuelezea jambo, tutawafahamisha, au sio, haya ni mazungumzo ya kifamilia zaidi,
lakini kuna muda mtahitajika…’akasema baba, na mimi nikakubaliana na hilo.
Tulitaka kuanza kikao, lakini kuna wajumbe muhimu walikuwa bado
hawajafika na wao ni muhimu sana, kikao kisingeliweza kuendeshwa bila kuwepo
kwao, nikataka kupiga simu , lakin kabla sijafanya hivyo mara wakaanza kuingia
wajumbe wengine.
Aliyefika sasa hivi alikuwa rafiki wa mume wangu akiwa na mkewe,
na baadaye akaingia mume wangu, alipofika kwanza akajibaragua kidogo, kama
ujuavyo, waliokuwepo hapo ni wazazi wangu tu, ni wakwe zake, kwahiyo alionyesha
ile adabu ya ukwe, akawasalimia na baadaye akaja kukaa karibu yangu,
‘Samahani sana nimechelewa najua mimi ndiye mwenyeji, lakini kuna
mambo yalinitinga,…’akasema
‘Hamna shida…’akasema mzee
‘Ni lazime niwajibike, hata mkataba wetu unasema hivyo…’akasema
akijitutumua, na mimi nikamuelewa anaelekea wapi.
‘Mkataba upi unaouzungumzia hayo, wa zamani au mpya?’ nikamuuliza
kumchokoza huku nikitabasamu, hapo akasita na baadaye akasema;
‘Hakuna mkataba mpya na wa zamani, hiyo kauli yako tu mke wangu
usiwachanganye wajumbe...’akasema na hapo nikajua hajafahamu kuwa nimeshaupata
ule mkataba wetu wa asili.
‘Tutaona..muda ukifika hilo litasahihishwa, ...fungua kikao, au
nifungue mimi maana ndiye niliyekiitisha,…?’nikasema na kuuliza
‘Hapana, tunafuata mkataba wetu, nataka kikao hiki kitambue kuwa
kuna mkataba wetu wa kifamilia…’akasema
Mume wangu kwanza akamuangalia baba, akainama kiheshima na
kufungua kikao kwa kumkaribisha mwenyekiti wa kikao, ambaye ni baba, kikawaida
kwenye familia yetu, kukiwepo kikao kama hicho mwenyekiti ni baba.
Baba kwanza alianza kufungua makabrasha yake, na kabla hajasema
neno, mlango ukagongwa, na kwa vile wote tulijua kuwa tumekamilika,
hatukutarajia mtu mwingine mpya, kujitokeza tena, kwahiyo hiyo hali ikatufanya,
sote tugeuke na kuangalia mlangoni, kuona ni nani huyo anayetaka kuingia
***********,
Mara akatokea mtu akiwa kavaa kofia la waendesha pikipiki,
akasimama pale mlangoni akisita kuingia…
Huyu mtu, alikuwa kavalia jaketi la kuzuia upepo mwilini, na
kumfanya aonekane bonge, alisimama pale mlangoni kofia likiwa bado kichwani,
inaonekana hakutaka kulivua huko nje, labda kwa vile aliona keshachelewa, kama
ni mjumbe wa kikao hiki, ambaye mimi sikuwa na habari na yeye,au alifanya hivyo
kwasababu zake nyingine.
Kila mmoja ndani ya kikao alimwangalia yeye, na yeye alipoona watu
wote wanamtizama, akafanya mambo mawili kwa haraka, kwanza akainama, kama
vile anasalimia au kutoa heshima na pili, akageuka kuangalia mlangoni, kuhakikisha
kuwa amefunga mlango, akalivua lile
kofia lake na kuvua koti , halafu taratibu akageukia watu, na kusema;
‘Samahani sana wakubwa zangu, na baba na mama pale..mimi
nimechelewa, nilikuwa naweka mambo yangu sawa, maana kiukweli...jamaa
wananifuatilia kila kona...’ akasema huku akiangalia pale alipokaa mwenyekiti,
lakini alikuwa hamuangalii moja kwa moja usoni, na mwenyekiti akasema;
‘Huyu mtu amefuata nini kwenye hiki kikao...?’ mwenyekiti
akaniuliza mimi na kabla sijamjibu akamgeukia huyo mtu na kusema;
‘Kikao hiki hakikuhusu, hiki ni kikao cha watu maalumu, sizani
kama wewe ni mmoja wa waalikwa…sina uhakika na hilo, ‘ akasema sasa akikagua
majina ya wajumbe..,
‘Mhh, sioni jina lako hapa…kama unavyoona hawa ni wanafamilia, na
watu maalumu...walioalikwa..’akasema mwenyekiti.
‘Lakini mimi nimealikwa pia....’akajitetea huyo mtu akigeuka
kuniangalia mimi.
‘Ni nani aliyekualika, majina yote ninayo hapa, sijaona jina
lako,..., kwanza wewe unatafutwa na polisi, kweli si kweli…?’ akauliza
‘Ni kweli…lakini…’akasema lakini kabla hajajitetea, mwenyekiti
akaendelea kuongea
‘Na kwhiyo ukionakena hapa tutaambiwa kuwa tunamficha muhalifu, tafadhali, ondoka, usituharibie mipangilio
yetu, sisi sio wavunja sheria, kumficha muhalifu ni kuvunja sheria za nchi,
unalifahamu hilo...’akasema baba, na mimi nikaona niingilie kati nakusema;
‘Baba , oh mwenyekiti, mimi ndiye niliyemualika huyu mtu,
nilimualika wakati nimeshakupa hayo majina ya wajumbe, kwani sikuwa na uhakika
naye, kwa vile alikuwa haonekani, lakini ni mmoja wa watu muhimu kwenye hiki
kikao..’nikasema
‘Binti, hilo haliwezekani, huyu ni mshukiwa wa uhalifu, anatafutwa
na polis, mbona unafanya mambo yasikubalika…’akasema mwenyewekiti
‘Baba uwepo wake ni muhimu sana kwenye hiki kikao, ili aweze kutoa
ushahidi, kutokana na mambo tutakayoyaongelea leo hii hapa, hatuwezi kumkosa
mtu kama huyu, na nilikuwa naombea sana awepo...’nikasema na mume wangu
akadakia na kusema;
‘Unasema anakuja kutoa ushahidi…!!’ akasema sasa akimuangalia
mdogo wake kwa mashaka
‘Ndio…’nikasema
‘Ushahidi gani atautoa mdogo wangu, kwanza niulize kwa kauli yako
hiyo , kwani hapa kuna kesi ya nani, sijaelewa hapo mke wangu, ninani
kashitakiwa, eeh..anyway, vyovyote iwavyo, lakini kitu kinachomuhusu mdogo
wangu nilitakiwa mimi nikifahamu kwanza..’akasema akikunja uso, kuonyesha
kukerekwa.
‘Utayafahamu yote hayo baadaye, kikao hiki nimekiitisha mimi, kuna
mambo mengi ambayo yatajitokeza ndani y afamilia, ambayo yanaweza kuvunja
usalama na umoja wa kifamilia,.., na yeye anayafahamu zaidi yako, kwa vile wewe
ulikuwa mgonjwa,....’nikasema
‘Sio kweli,… mdogo wangu hawezi kufahamu jambo, mimi nisiwe
nalifahamu, mimi na yeye muda wote nikiwa mgonjwa tulikuwa tunawasiliana, je kuna
kitu gani anakifahamu mimi nisikijue…?’ akauliza
‘Subiria sasa kikao kipo kwa ajili ya hili na mengine..’nikasema
‘Hapana…wewe una nia mbaya na mdogo wangu, mdogo wangu kwanini,
wewe hujui umejileta kwenye mtego,…’akasema akimuangalia mdogo wake, halafu
akaniangalia mimi na kusema
‘Hivi kwanini mke wangu unataka kumuingiza mdogo wangu kwenye
matatizo, ni kwa vile sio damu yako, au sio.. huyu ni mdogo wangu, mimi ndiye
mwenye dhamana naye, ...kama alivyosema mwenyekiti ni bora mdogo wangu uondoke
hapa hahusiki kwenye hiki kikao..’akasema
‘Kwanini aondoke unaogopa nini wewe, una mashaka gani…?’ nikauliza
‘Sio swala la kuogopa, ni swala la usalama wake, mimi nafahamu,
polis wakimuona hapa watakimbilia kumkamata, kabla hatujaweka mambo sawa, wao
hawajafahamu ukweli ulivyo..’akasema ndugu mtu akionyesha wasiwasi.
‘Hilo nimelifanyia kazi, wewe subiria kwanza…’nikasema
‘Hakuna swala la kusubiria haoa,..nafahamu lengo lako, ni ili
mdogo wangu ajitokeze polis wamkamate, ndio hivyo tu…mimi naomba aondoke tu,
nitaongea naye baada ya kikao, kwanini kila mara unapenda kumuingiza mdogo
wangu kwenye matatizo......’akasema mume wangu.
Muda wote huo mwenyekiti alikaa kimia, akiandika mambo yake ni
kama vile hajali hayo yanayoendelea.
‘Asiondoke, hiki kikao nimekiitisha mimi, na huyu ni mmoja wapo wa
shahid wyangu muhimu sana na ajenda zote za kikao ninazo hapa kama katibu, na
kwa bahati mbaya sikuwawagaia ajenda za kikao hiki mapema, kwasababu maalumu..’nikasema
‘Najua wewe hujali hilo…’akasema
‘Sio kweli …, mimi sijawahi kumuingiza mdogo wako kwenye matatizo,
ni wewe ndiye uliyemuingiza ndugu yako kwenye matatizo, kama tutakavyokuja
kuona huko mbele… hayo yote tutayabainisha kwenye hiki kikao, na ndipo
itajulikana wazi ni nani anayemjali mdogo wako..mimi au wewe…’nikasema
‘Unasema nini, mimi ndiye niliyemuingiza mdogo wangu kwenye
matatizo gani, usilete hoja za kuharibu hiki kikao, kama hakinifai mimi
nitaondoka zangu…’akasema sasa akiniangali a kwa mashaka
‘Huyu ni mmoja wa wajumbe muhimu kwenye hiki kikao, na kuwepo
kwake hapa ni kwa ajili ya kusema ukweli, ulitokana na wewe, yeye hawezi
kuondoka mpaka huo ukweli uthibitishe, na ukweli ukiwa bayana, kama ni mtu wa
kwenda polisi atakwenda tu...’nikasema
‘Hapana hawezi kwenda polisi, labda mimi niende huko kama lengo
lako ndio hilo, hilo halitaweza kutokea nikiwemo hapa, na kwa hili nitachukua
jukumu la kumuondoa, kwani mimi ndiye mwenye mamlaka ya familia na ndugu zangu,
hata mkataba wetu,wa kifamilia, unaliongelea hilo ....’akasema na kuushika
mkataba mkononi, utafikiri ndio mtetezi wake.
Hapo sasa mwenyekiti
akaingilia kati na kusema; ‘Hebu tusikilizane kwanza… mimi ndiye mwenye
mamlaka ya hiki kikao, au sio..kwahiyo mimi ndiye nitasikilizwa…’akasema na
sisi tukatulia,
‘Kwanza , mimi kama mwenyekiti sijakubaliana na kuwepo kwa huyu
mtu hapa, kwani anatafutwa na polisi, mnafahamu kuwepo kwake hapa ni kuvunja
sheria za nchi, na mimi ni mmojawapo wa watu wanaosimamia hilo bungeni…,na mimi
sio mvunjaji wa sheria, kama mwenyekiti ninaamuru huyu mtu atoke kwenye hiki
kikao...’akasema mwenyekiti.
‘Hata mimi nakuunga mkono mwenyekiti, sawa kabisa...’akasema mume
wangu.
‘Mwenyekiti, naomba huyu mtu awepo, na kama ni swala la uvunjifu
wa sheria, hilo tutakuja kuliona hapa, kuwepo kwake, hapa kutasaidia kuyaweka haya
mambo yote sawa, na huenda tukaisaidia hata hiyo polisi kwa hayo
wanayoyatafuta..’nikasema na baba akaniangalia kwa makini, na akageuka
kumwangalia huyo mtu,
‘Mimi bado sijaafiki kwasababu muda uliopita niliongea na mkuu wa
upelelezi wa eneo lenu nikamkatalia kabisa kuwa huyu mtu sijawahi kumuona, na
nikimuona moja kwa moja nitamfikisha kwao, au nitawaita waje wamchukue, na sasa
hivi napiga simu waje wamchukue...’akasema
‘Usifanye hivyo baba tafadhali, huyu ni mdogo wangu, na mimi ndiye
nabeba dhamana naye, kama polisi wanamuhitaji kwanza waje kuonana na
mimi,...mdogo wangu hana hatia, kama wanavyodai wao, wanamuhisi tu..mimi ndiye
niliyesababisha aonekane hivyo...’akasema.
‘Umekumbuka hayo eeh…’nikasema na hapo akatikisa kichwa kama
kuchanganyikiwa halafu akasema, akiniangalia mimi kwa hasira
‘Wewe ndiye uliyesababisha yote haya hdi mdogo wangu kushukiwa
uhalafu ambao hajawahi kuufanya,..basi polisi wakija utawaambai hivyo, lakini
kuwepo kwake hapa ni ukiukwaji wa sheria....’akasema baba.
‘Baba usijali tuendelee na kikao, mwenyewe utakuja kuona umuhimu
wake, kama nilivyokuambia, niamini, nisingemuita hapa kama asingelikuwa ni mtu
muhimu sana kwenye hiki kikao, je hutaki kujua jinsi gani vitu vyangu
vilipotea, hutaki huo ushahidi uwe bayana ...’nikasema na baba akasema;
‘Sawa mimi naendelea na kikao, lakini msimamo wangu ni huo huo,
huyu mtu atoke nje, mimi kama mwenyekiti wa kikao sikumruhusu awemo kwenye hiki
kikao...na kwa vile nimemuona, nitawapigia polisi waje wamchukue..siwezi kwenda
kinyume na sheria...’akasema
Mdogo mtu akawa bado kasimama akishindwa kuondoka, na mwenyekiti
akasema;
‘Kwanza mume wako kasema kuwa nyie katika familia yenu mna katiba,
na Katiba hiyo ndiyo inayowaongoza,..naona katika ajenda zako katibu, hilo
swala la katiba umeliweka kuwa la kwanza, na mume wako keshalianza, naona
tuanze na hicho kipengele, tusipoteze muda…’akasema sasa akindika kitu kwenye
simu yake.
‘Sawa lakini….’akasema mume wangu na kabla hajamaliza mwenyekiti
akaendelea kuongea kwa kusema;
‘Hebu niambieni kwanini mliamua kuanzisha katiba kama hiyo, hata
mimi mwenyewe sina kitu kama hicho, labda itatusaidia na sisi …? Akauliza
mwenyekiti, na mume wangu akasema;
‘Nafahamu kuwa swali hilo limemlenga mke wangu,kwa vile ndiye
mwenye hiki kikao, na ndiye alitakiwa ataje ajenda zake, na bahati mbaya ,
kikao kimeanza juu kwa juu, kutokana na hili lilitokea, ...ni kweli ndugu
mwenyekiti, katika familia yangu, nikiwa na maana mimi na mke wangu na watoto,
tuna katiba yetu inayotuongoza....’akatulia kidogo akiishika ile katiba.
‘Kwanini tuliamau kuwa na katiba, ….kiukweli ni wazo la mke wangu
, hata mimi nikalipenda sana….kwanza tulitaka familia yetu iongozwe kitaalamu
zaidi, ...’ akageuka kuniangalia mimi
‘Lakini sababu kubwa ya kimsingi ni kuwa tulijiona kuwa tuna mambo
mengi, mimi nikiwa nashughulika kwenye kampuni yangu, na mke wangu kwenye
kampuni yake,lakini vyote hivyo ni vyetu, japokuwa kitaalamu kutokana na hisa
kila mmoja alikuwa na mamlaka na kampuni yake...’akatulia
‘Kwa vyovyote iwavyo, mnapo-oana, hata kama mke alikuwa na vitu
vyake, kampuni yake, mali yake, lakini akishakuwa mke wa mtu, basi kila kitu
chake kinakuwa kwenye mikono ya mume kama kiongozi wa familia au sio....na hili
tumelibainisha kwenye katiba yetu, ili kuondoa migongano, tukaona jambo nzuri
ni kuwa na katiba....’akasema akitaka kufungua hiyo katiba.
Mwenyekiti akasema;
‘Mhh, usifungue hiyo katiba kwanza, nilichotaka mimi ni kufahamu
ni kwanini mliamua kuanzisha hiyo katiba, na kwa ufupi tumeelewa hilo...swali
langu la pili, je katiba hiyo imesajiliwa kisheria au ni katiba yenu tu kwa
ajili ya mambo yenu ya ndani?’ akauliza
‘Sisi baba, eeh, ndugu
mwenyekiti, kila kitu tumekipeleka kitaalamu, katiba yetu hii imesajiliwa, na
aliyeiandika ni mwanasheria, kwahiyo katiba yetu ni kisheria, imetimiza
matwakwa yote ya kisheria, ..hatuna matatizo na hilo....’akasema
‘Kwahiyo unataka kusema kila kitu chenu, taratibu zenu za kila
siku mlidhamiria ikiwezekana, kifuate taratibu kama mlivyoanisha kwenye katiba
yenu hiyo…, na likitokea tatizo, mnahukumiana kutokana na katiba yenu hiyo au
sio?’ akaulizwa
‘Ndio mwenyekiti, ndio maana nashangaa kikao hiki, kuitishwa na
mke wangu, nilitakiwa mimi ndiye nikiitishe, lakini kuna dharura kama hizo, siwezi
kuktaa, au sio mke wangu…’akasema akinigeukia na mimi nikabakia kimia tu
‘Kama ikitokea dharura,basi mmojawapo anaweza kuitisha kikao,
lakini ilitakiwa mimi niambiwe kila kitu kwanza…, kwanini kikao kiwepo, lakini
mmh, kwa bahati mbaya kwa hili, silaumu, lakini halikufuata utaratibu...nimeshitukiziwa
tu, kuwa kuna kikao, cha nini na kwanini, sijaambiwa, huo ni ukiukwaji wa
katiba, ila tuliache tu hivyo, tupo pamoja...’akasema
‘Sawa kama imeshtukizwa tu ni makosa, na katibu wako atawajibika
kuelezea ni kwanini…’akasema akiniangalia mimi, na mimi nikatikisa kichwa
kukubaliana na hilo,…Na mume wangu akadakia kwa kusema;
‘Ndugu mwenyekiti naomba niongee kidogo kuhusu hii katiba,
samahani sana, kwani mimi ndio mwenye mamlaka, na kiongozi wa familia yangu, na
kwahiyo nina mamlaka ya kuona kila kitu kinaenda sawa...na hilo lipo kwenye
katiba…’akasema na mwenyekiti akageuka kuniangalia, mimi nikamuashiria amuache
mume wangu aendelee
‘Watu wanapofunga ndoa, wanakuwa na taratibu zao, kama mke
na mume, na wanakuwa wameshajitoa kwenye mamlaka ya baba na mama zao,
hawalindwi au kuchungwa tena na familia za baba na mama zao, kikeni au kiumeni,
wao ni watu huru, na wanakuwa na utaratibu wao kama familia inayojitegemea, au sio …’akasema kama anauliza
‘Na ndivyo tulivyofanya sisi, na kwa ajili ya kurahisisha
mambo yetu tukaona tuwe na katiba, ni wachache sana wanakuwa na utaratibu kama
huo, ni tendo la ajabu lakini sis imetusaidia sana, ningeshauri kila familia
iwe nayo....’akasema mume wangu.
‘Hii katiba imesajiliwa kisheria, kwasababu imeandikwa na
mwanasheri a wa familia, yetu, na sote tukaweka sahihi zetu, mimi na mke wangu,
na wakili wetu. Sio katiba ya mitaani , ni Katiba iliyokubalika kisheria,
ukiangalia hapa ina kila sifa zote za kisheria, ...mimi kama kiongozi wa
familia kwa kupitia hii katiba ninaweza kumshitaki yoyote atakayeingilia au
kuingilia mambo yetu ya ndani....’akasema.
Aliposema hivyo akamuangalia mwenyekiti na mwenyekiti akawa naye
kamkazia macho, halafu akageuka kuniangalia mimi….
‘Kwahiyo itakuwa ni ajabu kama mtu atakuja na kuingilia familia
yangu,wakati yeye ana familia yake, ni ajabu kabisa, labda kuwe na jambo, na
jambo hilo liwe wazi kwa kiongozi wa familia ambaye ni mume wa familia, au sio,
huo ndio utaratibu, na ndivyo ilivyo kwenye hii katiba .....’akasema na
mwenyekiti kwanza akatabasamu, maana aliona hizo shutuma zinaelekezwa kwake, akauliza
‘Hiyo Katiba yenu iliandikwa lini?’ akauliza mwenyekiti
‘Muda mrefu sana, kipindi wakati watoto wetu ni wachanga tu…,
imeshafanya kazi zaidi ya miaka tisa, au sio mke wangu, kwahiyo sio kitu
kigeni ndani ya familia yangu...’akasema
‘Naomba niione hiyo katiba..’akasema mwenyekiti, na mume wangu
akasimama huku akiwa kashika ile katiba na kwa madaha, akaelekea pale alipokaa
mwenyekiti kumkabidhi hiyo katiba, na wakati huo shemeji yangu alikuwa bado
kasimama, alikuwa hajafahamu kuwa akae au aondoke, na mimi nikamuonyeshea
ishara kuwa akae kwenye kiti. Na mwenyekiti akamuona , na haraka mwenyekiti
akasema;
‘Mimi sijakuruhusu ukae, mimi bado sijakukubalia na uwepo wako
kwenye hiki kikao, kama mwenyekiti siwezi kukaa kwenye kikao kinachovunja
sheria, nimeshasema huyu mtu anatafutwa na polisi, kuwepo kwake hapa ni
uvunjifu wa sheria....’akasema mwenyekiti sasa akiangalia kitu kwenye simu
yake, na mimi nikasema;
‘Mwenyekiti nakuomba uniamini, huyu mtu ni mtu muhimu sana kwenye hiki
kikao nakuomba umruhusu awepo, na kama ni uvunjifu wa sheria mimi nitalijibu
hilo, ...’nikasema.
‘Mimi nakubaliana na mwenyekiti, ndugu yangu huyu atoke nje,
kwanini mke wangu unamkaidi mwenyekiti, unaona ilivyo vigumu kwenye
familia yangu, silaumu lakini hili halikubaliki, kiongozi ni kiongozi lazima
aheshimiwe bila kujali ni nani, sasa na mimi ni kaka yake nipo hapa,
nitawakilisha mawazo yake, kwanini ung’an’ganie awepo apa, au unataka polisi
waje wamkamate...’akasema na kuongeza kusema;
‘Nina maana muhimu sana, …na ni muhimu sana kuwepo hapa, najua ni
kwanini hutaki awepo hapa…’nikasema
‘Mke wangu umekuwa ukimuandama sana mdogo wangu, sijui
kwanini,kama kuna lolote dhidi yangu niambie mimi mwenyewe…, na sio kumtumia
mdogo wangu kinyemela,mimi sipendi, kama kaka yake ninaamuru atoke kwenye hiki
kikao, mimi nitawakilisha mawazo yake kama kuna umuhimu huo, ni kwa usalama
wake kwa sasa, mengine aniachie mimi ...’akasema mume wangu.
‘Hata mimi sioni umuhimu wake hapa, maana anatafutwa na polisi
akionekana hapa itaonekana kuwa tunamficha sisi, au ngoja tulimalize hili,
ngoja ofiswa wa upelelezi aje amchukue,...’baba akasema huku akinua simu yake
kumpigia huyo mtu wa usalama
‘Baba tafadhali utaharibu kila kitu, nilishakuomba kuwa unipe
nafasi nifanye nionavyo mimi ni sawa… , kama utamuita huyo ofisa wa polisi
utaharibu kila kitu, naomba tafadhali endelea na kikao chako, muda utafika ,
utaona ni kwanini nimeamua awepo hapa kwenye kikao hiki...’nikasema,
‘Wewe unataka tufanye kikao kisicho fuata taratibu, unanielewa
sheria za nchi zilivyo, unaelewa mamlaka niliyo nayo..unataka wapinzani wangu
wapate cha kuongea..’mwenyekiti akasema;
Mdogo wa mume wangu, alipoona malumbano dhidi yake yanapamba moto,
akaona aingilie kati mwenyewe, akasema;
‘Tafadhali mzee wetu, na wajumbe wote wa kikao hiki,mimi
naomba mnipe muda, niongee kilichonileta hapa, na baadaye kama unaona nimevunja
sheria, basi utampigia huyo mtu wa usalama, aje anichukue, mimi siogopi
kukamatwa kwa hivi sasa, ..kwa vile nimeshathibitisha kile nilichokuwa
nikikichunguza, na kumgundua muuaji wa Makabrasha,...
‘Nini…wewe unasema nini, acha kuongea haya hapa,…utaharibu!!’
ayetamka hivyo na hata kusimama alikuwa mume wangu.
‘Mimi kuja kwangu hapa,ni kusema ukweli…’akasema na kiukweli hapo
kila mtu akabakia kimia, kumsikiliza yeye hasa hapo aliposema keshampata muuaji
wa Makabrasha.
‘Pamoja na mengine, nafahamu kuwa askari polis wananitafuta mimi
kuthibitisha kuwa kweli kaka ndiye muuaji,..’akasema
‘Hapana sio kweli…kaka yangu sio muuaji..’akasema
‘Mimi sijaua…ni uwongo wao tu..’akasema mume wangu
‘Ndio hivyo kaka,..ndio maana mimi nataka nilithibitishe hilo
mbele ya hiki kikao, kuwa wewe hujamuua Makabrasha…’aliposema hivyo, kaka mtu
akakaa kwenye kiti sasa akipumua kidogo.
‘Lengo langu hadi kufika hii leo hapa, ni kumtetea kaka yangu,
kwani kuna mipango ilipangwa dhidi yake, yeye hafahamu tu…, kuwa kuna watu
walioshirikiana kumuua Makabrasha, na kwa vile wanataka wasikamatwe, wameona
kosa hilo wambambikie yeye, kaka yangu, bila ya hata yeye kufahamu, ...’akasema
na kaka yake akabakia kuduwaa,
‘Mimi nina ushaidi kuwa kaka hajamuua Makabrasha, na wala hajui ni
kitu gani kilitokea siku ile, yeye kwanza alikuwa mgonjwa, na pili, aliyemuua,
alikuja bila ya kaka kufahamu kinachoendelea, alitokea kwa nyuma wakati yeye kaka akiongea
na marehemu na huyo mtu alikimbia..kwahiyo kaka hafahamu lolote kuhus huyo mtu,
na kwanini ilitokea hivyo..’akasema na
kaka mtu akataka kumzuia mdogo wake asiendelee kuongea.
‘Inatosha, usiseme kilakitu,…’akasema kaka mtu
‘Kaka nakuomba utulie , nataka kuongea haya kwa masilahi yako, na
masilahi ya wote waliohusika, kwasababu nimeona huk o tunapokwenda ni kubaya
kuliko mnavyofikiria nyie…, na hayo yaliyopangwa dhidi yako, au yenu, yatakutia
matatani kaka, yataharibu familia yako, na kashfa itasambazwa kila mahali..’akasema
na kaka yake akamsogelea na kumshika mkono na kusema;
‘Mdogo wangu hayo sio ya kuongea hapa, tutakuja kuyaongea tukiwa
wawili, wewe toka nje ya kikao,...’akasema huku akimshika mdogo wake mkono, ili
watoke naye nje...mwenyekiti alipooa hivyo akasema;
‘Naomba mtulie mimi ndiye mwenyekiti wa kikao, nimeshamfahamisha
mkuu wa upelelezi, amesema tuendelee na kikao, lakini kikao kikisha, huyu mtu
tunatakiwa tumkabidhi kwake, kwahiyo kuanzia sasa upo mikononi mwa polisi mimi
siwezi kuvunja sheria kwa ajili ya kumfurahisha mtu yoyote, hata akiwa
mwanangu,mimi nafuata sheria na taratibu zilikubalika ....’akasema
‘Kwahiyo mimi sihitajiki tena kusema ukweli ambao nilitarajia
kuusema?’ akauliza shemeji yangu.
‘Ukitaka kuusema sawa, sasa hivi upo huru kusema, maana wenyewe
wameshatambua kuwa upo hapa, na ukweli gani ulio nao ambao ni tofauti na ukweli
ninaoufahamu mimi, hayo unayotaka kuyasema , na jinsi ulivyoelezea hapo, ni
mbinu tu ya kuficha ukweli halisi…ni jinsi nyingine ya kumtetea kaka yako
kiujanja unjana, na mimi sikubaliani na hilo....maana ushahidi wote ninao
hapa...’akasema baba.
‘Baba labda tufuate utaratibu wa kikao chetu, wewe endelea
na kikao, ukifika muda wake wa kuongea ataongea, na ukweli utajionyesha, labda
tuanze na ajenda zetu kama zilivyojipanga, kama tulivyoanza awali, tulikuwa
tukiongelea kuhusu katiba,,...au sio mwenyekiti…’nikasema.
‘Utaratibu kama huu siutaki, mnasikia, … sawa tuendelee na kikao, na kijana upo chini ya ulinzi,
kuanzia sasa, ...’akasema mwenyekiti kwa hasira.
Kikao kikaendelea kwa namna hiyo…Karibuni kikaoni..
WAZO LA LEO: Taratibu na sheria zilizowekwa zina umuhimu wake kwenye
jamii husika, na jamii hiyo inatakiwa
kuzifuata hizi sheria na taratibu zilikubalika, ili kuzuia uvunjufu wa amani.
Watu wakianza kutafuta uchochoro wa kuzikweka sheria hizo kwa visingizio mbali
mbali, malengo na dhamira ya kweli hupotea, na matokea yake ni fujo … Sheria au
taratibu zinatakiwe ziwe kwa masilahi ya jamii, na sio kwa ajili ya
kuwakandamiza wanyonge.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment