Niifuata maelekezo kama walivyotaka wao, walichokuwa
wakifanya ni kuniamuru, kwa kunielekeza kuwa nielekee wapi, nikate kushoto au
kulia, hadi tukafika maeneo yasiyokuwa na umeme, eneo hilo ilikuwa na majengo
mapya mapya, na nikaambiwa nisimamisha gari.
‘Simamisha gari..’nikaamriwa
Nikafanya kama walivyoniamurisha na nilipotaka kugeuka kuwaangalia
ni akina nani, maana nilishahisi kuwa wapo wawili, kiyoo cha kuangalia nyuma
walikuwa wameshakigeuza kwa juu ili nisiweze kuwaona kwa nyuma.
Wakati nataka kugeuza kichwa, mkono wenye kitambaa ukapitishwa
puani kwangu na aliyefanya hivyo, akanishika shingoni kama mtu anayenikaba, na
mwenzake akasema;
‘Mbona unamkaba, hukusikia bosi alivyosema, bosi alisema
tusimdhuru sehemu yoyote, atajua mwenyewe ni nini cha kufanya
tukimfikisha..’akasema mwenzake
Niliposikia hivyo mawazo yakanipeleka mbali kuwa huenda ni yale
yale niliyotaka kumfanyia rafiki yangu, ndio yamenigeukia mimi, sikuweza kujitetea
maana kile kitambaa walichoniwekea puani, kilinivunja nguvu zote, viungo vyote
vikalegea, japokuwa kwa mbali niliweza kusikia wanachokiongea.
‘Sasa ningewezeje kumweka hii dawa...kwanza haijaingia vyema huoni
bado yupo macho...’akasema na wakanishikisha kile kitambaa puani, na nilipoivuta
pumzi, nikahisi nikizama kwenye giza, sikujitambua tena.
Sijui ilipita muda gani, lakini nahisi ni karibu ya saa moja au
nyuma kidogo, ..nilihisi kitu kikipita puani, na hapo nikapiga chafya
mfulululizo, hadi nikashikwa na kikohozi, na hapo hapo nikawa kama mtu
aliyekuwa kwenye ndoto ya majinamizi, napaigana kushindana na hiyo hali, lakini
viungo havina nguvu, nikawa kwenye hiyo na hali na baadae nikaanza kurejewa na
fahamu.
Ikapita muda, na taratibu akili yangu ikaanza kunirejea kama mtu
anayetoka usingizini, bado wakati huo mwili mzima ulikuwa umelegea, nikajaribu
kuinua mkono, mkono ulikuwa kama haupo kwenye mwili wangu mara nikasikia sauti
kwa mbali;
‘Bosi anasema kila kipo tayari,..ngoja azindukane tu…’sauti ikasema
Nikajitikisa kidogo, kujaribu mkono kama unaweza kuinuka…
‘Naona kama keshaanza kuzindukana....mnaweza kumrejesha kwenye
gari lake, lakini hakikisheni, anazindukana kabisa ndio muondoke, mlindeni
asije akaumizwa na watu wengine, tukaja kupata lawama, kazi tuliyomuhitajia
imekamilika, kila kitu chake kirudisheni kama kilivyokuwa....’sauti ikasema
‘Bosi ina maana tumuache hivi hivi tu....’nikasikia sauti ikisema
‘Wewe ulitaka kumfanya nini, acha na tama mbaya, hapa ni kazi tu,
kama tulivyoagizwa, kazi yetu ni kufuata maagizo, tunachohitajia sisi ni pesa
si vinginevyo, hatutafuti mengine, hayo unayoyataka wewe sio utaratibu wetu, na
ole wenu mumuguse, huyo ni hatari kuliko ,mnavyofikiria, ...’sauti ikasema
‘Kama ni hatari huko mbele akizindukana itakuwaje...?’ akauliza
mmojawapo
‘Ndio maana nawataka mumurudishe kwenye gari lake, na hakikisha
mnamkalisha kwenye kiti chake aonekane kalala kwenye gari lake, akizindukana,
atajijua mwenyewe, sisi kazi tumeshamaliza, tunakwenda kuchukua mshiko wetu,
...’ sauti ikasema
‘Sawa bosi…’sauti nyingine ikasema
‘Na muhimu hakikisheni kuwa yupo salama, na mkiona kuwa
kazindukana, poteeni mbali kabisa, ukibakia hapo yatakayokupata sisi hatupo, na
hakuna kutajana hapa, kila mtu afe kivyake,…nawaambia tena, ukishikwa ukafunua
mdomo wako, utakuwa mgeni wa mchwa..’sauti ikasema
‘Sawa bosi tumekuelewa...’nikahisi mmoja akisema wakanibeba, na
mmoja akawa anasema kichichini.
‘Huu mwili, laini, laini hivi, tutaishia kuubeba tu...hawa watu
hawana akili kweli, ...’akasema
‘Unajua wewe utakufa kwa ukimwi, wewe unapenda mambo hayo sana,
kama umelaaniwa nayo, mwili tu unakusumbua,..tunachokitafuta hapa ni
pesa, tufanye kazi yetu tulipwe, ..ukishapata pesa, watu kama hawa utawapata
wengi, ....’sauti nyingine ikasema.
‘Sawa bwana,...pesa yenyewe , shilingi ngapi kwanza, ...aheri ile
ya wenzetu, wabakaji, wanaopewa kazi ya kudhalilisha wanawake,..wanaifanya
hivyo na bado wanalipwa...’akasema.
‘Kubaka nako kazi, ..ile sio kazi ya kufanya, ni hatari tupu, na
umewasikia wenzako, kilichowatokea,...sasa hivi wanatafutwa na polisi, safari
hii wameshindwa, nasikia wamepewa kazi, kabla hawajaifanya wakafumwa, ngoja
wafukuzwe na polisi,karibu wakamatwe..nilikutana na yule jirani yako, akikimbia
utafikiri yupo kwenye mbio za dunia, na akaniomba nauli, anataka kupotea hapa
jijini.’mmoja akasema
‘Kwani na nani na kwanani?’ mmoja akauliza
‘Nasikia ni kwa binti mmoja , aliyetoka ulaya hivi karibuni…’akasema
‘Sasa huyo ana kosa gani , maana nasikiwa wakijiita kundi la
kurekebisha tabia..’akasema
‘Anajua huyo aliyewatuma kuwa ana kosa gani…’akasema
‘Ikawaje sasa
‘Basi bwana,..walifanya kama kawaida yao, na hizi dawa za kupoteza
fahamu, kwanza walipambana, maana huyo binti sio mchezo, kilichowasaidia ni
hiyo dawa ya nusu kaputi, walifanikiwa kumnusisha, hapo ndio wakamuweza,
wakambeba, sasa walisahau kuwa nyumba hiyo kuna mtu mwingine,alikuwa chumba cha
pili, huyo ndiye aliyewaharibia, akawapigia simu polisi..
‘Ehe, ikawaje..?’ akauliza na wakati huo, wameshanifikisha kwenye
gari langu , wakawa kwenye harakati za kuniweka kwenye kiti, nilikuwa bado
nimelegea lakini akili ilishaanza kufanya kazi,sikutaka kuwashitua ili nisikie
ni nini wanakiongea, nikaendelea kufumba macho.
‘Basi bwana kama kawaida yao, maana wanapofanya hiyo shughuli, huku
wakirekodi tukio nzima, kwahiyo walipomfikisha huyo binti kwenye kichochoro,
walichoona kina usalama, wakaanza kuweka vyombo vyao vya kuchukua hilo tukio,
ili wakamuonyeshe tajiri wao, wakati wanajiandaa, wapo tayari, kufanya mambo
yao, mara king’ora cha polisi kikasikika, na hawo polisi walifanya hivyo
makusudi, maana hawakujua hawa jamaa wamejificha wapi...’akasema
‘Oh, kwahiyo kazi ikavurugika...wakakamatwa...?’ akauliza mwenzake
‘Wakamatwe wapi, ...tatizo lao waliposikia king’ora cha polisi
hakuna aliyemwangalia mwenzake kila mmoja akajua njia yake, wakaacha kila kitu
hapo, polisi wakafika na kumuokoa huyo mwanadada...na vitu vyote vikachukuliwa
kama ushahidi, na mijamaa hiyo inatafutwa kama alimasi...kwasababu
wanajulikana, na huyo dada anawafahamu, ...’akasema
‘Mhh, hapo kazi ipo....’akasema
‘Nafahamu kukamatwa sio rahisi, watakuwa wameshavuka milima na
mabonde, hawataonekana hapa hadi mwaka upite, tatizo, hawana pesa, maana kazi
hawakufanya, watalipwaje sasa...je wataweza kuvumilia kuishi bila pesa, ...huko
walipokwenda labda wakavunje nyumba za watu na kuiba, na hiyo sio fani
yao....’sauti ikasema.
‘Mhh, imenitisha, kwahiyo polisi wamecharuka kwa hivi sasa, mmh,
hapo sasa mimi naanza kuogopa, tuondoke zetu, kama ni hivyo polisi watakuwa
kwenye patroo zao, hebu mwangalie, nimemuona kama anajitingisha, keshaamuka
yule, funga mlango wa gari tuondoke zetu bwana...’sauti ikasema
‘Una uhakika..?.’akauliza mwenzake.
‘Nenda wewe ukahakikishe, unasikia ulivyo ambiwa, huyo dada sio
mchezo, kwa vyote, ana pesa na pia anazijua ngumi,,...mimi sitaki jela, naondoka
zangu...’sauti ikasema na mara baadae kukawa kimiya
Hapo nilipo nikahisi wameshaondoka, na mimi nikajaribu kuinua
mkono, na huku nikijikagua, sikuhisi maumivu sehemu yoyote, nikajinyosha na
kukaa vyema, nikafungua viyoo kupata hewa, nikataka kutoka nje ya gari, mara
nikaona gari likija mbele yangu.
Mimi nikawasha gari langu, lakini kabla sijaanza kuendesha, gari
hilo likiwa limeshafika, walikuwa ni polisi, wakasimamisha gari lao karibu na
gari langu, na silaha zao mikononi, mmoja akasogea kwenye gari langu na kugonga
kwenye kiyoo, mimi nikashusha kiyoo, akaniangalia kwa makini akaniomba
kitambulisho, nikamuonyesha leseni yangu, akaikagua halafu akasema;
‘Madamu huku umefuata nini, kuna tatizo lolote..?’ akauliza
‘Nahisi hakuna tatizo, gari lilinizimikia , lakini naona lipo
sawa...’nikasema, na sauti kavu ya kulazimisha ikanitoka, ilikuwa kama sio ya
kwangu, nilihitajika kupata kitu cha kulainisha koo, na yule askari aliposikia
hiyo sauti akaniangalia na kusema;
‘Unahis ulikuwa kwenye tatizo,…nyie zunguka kila mahali…’akatoa amri.
‘Madam tuambie ukweli maana hizi
sehemu hizi sio nzuri, kuna watu wabaya huku, kuna kesi nyingi za
wahuni, wavuta bangi na wabakaji, kama kuna tatizo lolote, tuambie, vinginevyo,
ni bora uondoke kabisa eneo hili..’akasema na mimi sikutaka kumsikiliza tena
zaidi, nikaondoa gari langu na sasa nikawa na kazi ya kutafuta njia ya kurudi
nyumbani.
*************
Ilikuwa ni kama saa sita na nusu hivi za usiku nilipofika
nyumbani, na mlinzi wangu alikuwa keshaanza kuingiwa na wasiwasi, aliponiona
akanijia na kuanza kuongea kwa haraka haraka;
‘Bosi, nilishaingiwa na wasiwasi, hapa tu nilitaka kuwapigia simu
polisi, lakini kwanza nilitaka kuwasiliana na wakubwa zangu wa kazi, sio
kawaida yako kutoka usiku, na kuchelewa kurudi kama leo, kuna tatizo lolote
bosi?’ akaniuliza
‘Hakuna tatizo..’nikasema na sikutaka kuongea na mtu nikakimbilia
ndani, na cha kwanza ni kunywa dawa , ni dawa maalumu za kuvunja nguvu za
madawa kama hayo waliyonunusisha puani.
Ninafahamu jinsi gani ya kuyavunja nguvu, na nafahamu ni aina gani
ya dawa hizo, nilifanya juhudi ya kuyaondoa hayo madawa kabla sijala kitu,
ilikuwa usiku sana kwakweli, na baadaye nikaoga, huku nikijikagua kuhakikisha
kuwa nipo salama, na kilichofuata hapo ni kutafuta usingizi, nililala hadi saa
tatu, asubuhi.
Niliamushwa na kelele za mlangoni, nikatoka na kukutana na
msaidizi wangu wa kazini amfika nyumbani, akasema kapiga simu yangu haipatikani
ndio maana akaamua kuja nyumbani…, nikamwambia sijisikii vyema, na akanikumbusha
kuwa leo nina kikao cha kukutana na familia yangu, saa nne, nikamwambia kitafanyika
kama kilivyopangwa.....
‘Na pia kutoka msajili wa mikataba, alikuwa anataka kuongea na
wewe..’akasema
‘Kwanini aongee na mimi , anatakiwa kuongea na wakili wangu au sio…’nikasema
‘Hata mimi nimemwambia hivyo hivyo, lakini akasema ni muhimu
angeongea na wewe …kasema atakupigia tena…’akasema
‘Ok akipiga niunganishie kwenye namba yangu nitakayokuwa hewani,
kuna jingine …?’ nikauliza
‘Hakuna bosi mengine ni ya kawaida,…matumizi ya ofisi…kanipatia
muhasibu, na hundi ya kuweka sahihi..’akasema
‘Ok, nipatie….’akanipa nikapitia kwa haraka, nikaweka sahihi, na
mambo ya kiofisi yakaishia hivyo.
*********
Nilijiandaa kutoka, na nilipokuwa tayari nikaenda kuchukua laptop
yangu, sehemu nilipoiweka, nikaumbuka sikuirudisha kabatini, ikawa ni kosa, haikuwepo...sikuamini,
maana hapo nilipokuwa nimeiweka sio rahisi mtu kuigundua, lakini
imeshachukuliwa
‘Ni nani huyu…?’ nikajiuliza na kwa haraka ,...nikajua huenda
waliochukua ni hawo watu walionikamata jana...nikatoka na kwenda maktaba,huko
niliona kila kitu kipo kama kilivyokuwa japokuwa kuna dalili za kutaka
kuvunjwa...
Hawa watakuwa hawo watu wa jana, na kwanini wachukue laptop yangu
tu...?’ nikajiuliza, na mara nikakumbuka,.
‘Ina wezekana ni shemeji yangu, huenda alitaka kuhakikisha kuwa
sina zile kumbukumbu zake za diary yake, amejidanganya...’nikasema kimoyomoyo
Wakati nataka kuondoka, nilipotoka nje, niliona boksi limewekwa
mlangoni, sikulishika kwanza, nikamuita mlinzi, kwani msaidizi wangu wa mambo
ya ndani, alikuwa kaelekea sokoni kununua mahitaji ya nyumbani, Mume wangu
alishatoka hospitalini, lakini tulikuwa hatukai naye hapo nyumbani, alikuwa
akikaa kwenye nyumba yetu nyingine, tulikubaliana iwe hivyo.
‘Hili boksi kaweka nani hapa?’ nikamuuliza mlinzi, akasema yeye
hafahamu
‘Hufahamu ina maana huu mzigo umeingia wenyewe humu, kuna mtu
kaingiza, wewe hukuwepo getini?’ nikauliza kwa ukali, kiukweli hata mlinzi
akiliniangalia kwa mashaka, sina kawaida ya kuongea na wafanyakazi wangu kwa
ukali hivyo.
‘Bosi nilikimbia kidogo kujisaidia, nilipokuja , sikuangalia huko
, hata hivyo, ...mmh, ndio, niliona mtu akitoka wakati wakati natoka chooni,
nikajua ni wafanyakazi wako, ....kwani sio boksi lako bosi,..?’akasema
‘Haya lifungue mwenyewe, kama ni bomu utajua mwenyewe jinsi
gani ya kulitegua...’nikasema na huyo mlinzi akiwa na wasiwasi akalifungua, ...
‘Oh, ni laptop yangu...’nikasema huku nikiitoa, nikaikagua,
ilikuwa haina tatizo lolote, nikaingia nayo ndani cha kwanza ilikuwa kuangalia
ni ile diary ya shemeji,...kila nilipojaribu kuiifungua inasema haifunguki,
haifanyi kazi, na mwisho ikasema haipo kabisa...nikajua kuwa ni huyo shemeji
yangu
Kabla sijaifunga hiyo laptop yangu, nikaona ujumbe kwenye komputa
ulikuwa umeandikwa kama barua pepe, nikaufungua na kuusoma
Ujumbe;
‘Samahani sana shemeji imenibidi nitumie njia hii, ili kuzipata
kumbukumbu zangu, ambazo nyingi ni mambo yangu binafsi, na si vyema watu
wengine wakayafahamu, natumai ulifika salama, hakuna lolote lililotokea dhidi
yako, na kila kitu chako kipo salama, japokuwa kuna vitu nilishindwa kuvichukua
kwenye kabati la kaka, kaka aliniagiza, lakini hakijaharibika kitu, mtamalizana
na yeye, ninachokuomba ni kumsaidia kaka, na mimi unisamehe sana kwa
kutokukukutimizia yale uliyoyataka....’
‘Huna adabu kabisa,unafikiri hilo ulilolifanya litasaidia kitu,
tatizo huyu kijana hanielewi mimi, yeye hujui kuwa mimi ni mjanja zaidi
yako...’nikasema, nikachukua kidude cha mtandao (moderm), nikaweka mawasiliano,
nikaingia kwenye mtandao, nikatafuta kumbukumbu zangu, nikaona ninachokitafuta,
nikafungua, nikaiona kumbukumbu iliyoandikiwa diary ya shemeji,
ipo kama ilivyokuwa...nikatabasamu, nikainakili tena kwenye laptop yangu.
Nilipohakikisha kuwa kila kitu kipo sawa, nikampigia simu, rafiki
ya mume wangu, ili kuhakikisha kuwa na yeye atakuwepo kwenye kikao, kwani bado
alikuwa akihangaika na mke wake,...
‘Vipi upo, maana siku hizi wewe hukai nyumbani kwako, sijui bado
unatafuta mtoto wa kiume au..?’nikamuuliza
‘Ni kawaida tu, ...nipo kwenye kikao, na ikao cha familia nitafika
pia, na mke wangu keshafika, alifika jana usiku, na amekubali kuwepo kwenye
hicho kikao, anasema ana yake ya kuongea, baada ya hapo anarudi huko kijijini alipokuwa,
sijamuelewa huyu mwanamke mpaka sasa, nimechoka...’akasema.
‘Vyema kabisa, nimefurahi kusikia hivyo, je uliwahi kuongea naye
lolote na akaweza kukuambia chochote.... ?’ nikamuuliza
‘Hataki kuongea lolote, anasema yote atayaweka wazi hapo kwenye
kikao, alikuwa anatafuta nafasi kama hiyo, ...nahisi kuna jambo kubwa
linamkera, maana hata wazazi wake, wanasema kawa kama mtu aliyepagawa,
hana raha,...sijui ana tatizo gani...’akasema
‘Pole zake, ndivyo ilivyo, majuto mara nyingi huja baada ya
kitendo, tunapofanya mambo bila kuangalia mbele,mwisho wake unakuwa mgumu,
...natumai atakuwa mkweli, na ukweli wake ndio utakaoweza kumsaidia, sio
vinginevyo...’nikasema.
‘Mhh,..kwanini unasema hivyo nahisi wewe kuna jambo unalifahamu
kumuhusu yeye, na ameamua kuwa msiri sana, na hilo ndilo litakalomuangamiza, ni
jambo gani hilo jamani..?’akasema na kuuliza
‘Kila jambo lina mwisho wake, nina uhakika yote yatajulikana
kwenye kikao, ujiandae kwa lolote lile, na mimi siwezi kukuambia chochote, yote
yataanikwa kwenye hicho kikao...’nikasema.
‘Kwanini lakini, hamjui mnavyonitesa?’ akaniuliza
‘Wewe ulijifanya unafahamu yangu mengi tiu…, mbona hukuniambia,
hukujua jinsi gani nilivyokuwa nateseka,..sasa ni zamu yako, lakini usijali,
yote yatajulikana kikaoni, natumai wote watafika, wasiwasi wangu ni kuwa
shemeji yangu anaweza asifike, na yeye ni mtu muhimu sana....’nikasema
‘Kwani kaenda wapi, maana hata mimi namtafuta kwenye simu
hapatikani..?’akaniuliza
‘Unamtafuta wa nini..au ndio kupanga njama za kuharibu ushahidi,
safari hakiharibiki kitu,…’nikasema
‘Kijana amekuwa mtoto wa mjini, anayoyafanya anayafahamu yeye mwenyewe,
na hata mke wake analalamika sana,..na zaidi hata kaka yake ananipigia simu
mimi kuniuliza wapi alipo mdogo wake…’akasema
‘Waongo hao…jana tu walikuwa pamoja, walichokifanya mungu mwenyewe
anajua, lakini ama zao, ama zangu…’nikasema
‘Mhh, haya bwana, lakini namlaumu sana mume wako, yeye ndio
anamuharibu mdogo wake, ...nasikitika sana, kwani juhudi zangu zote zimekuwa
hazina manufaa, kwa huyo mdogo wetu...’akasema.
‘Je mie niliyemgharamia masomo na kila kitu, hadi kuoa, nitasemaje…ni
kweli shutuma zote ni kwa kaka yake, mimi sizani kama nitakuja kumsamehe…’nikasema.
‘Unajua sema ni kwa vile mambo yangu yamekuwa mengi nimeshindwa kuyafuatilia
maisha yao, na yenu kwa ujumla,mnisamehe sana, hata wazazi wako nimewaambia
hivyo, mambo yemeniwia mengi sana, ila kwenye kikao nitajitahidi niwepo tu, japokuwa
…sijui..nitakuwepo, ngoja niweke mambo yangu sawa....’akasema.
‘Ni muhimu sana uwepo, kama mkeo yupo, basi hatima ya yote haya
itajulikana kwenye hicho kikao, na wasiwasi wangu ni kuwa baada ya hicho kikao
huenda kusiwe na urafiki tena, lakini sio kitu, bora nusu shari kuliko shari
kamili ....’nikasema
‘Kwanini kusiwepo na urafiki, mimi nilijua ni kikao cha usuluhishi?’
akauliza
‘Kwasababu ukweli ni mzuri sana, lakini unauma, na utahukumu
yanayostahiki kuhukumiwa, ili haki itendeke,...’nikasema.
‘Sawa hamna shida, mimi sina tatizo,...kama kuna ukweli
ninaoufahamu nitausema, kama utasaidia, ...’akasema.
‘Na hasa uwe wa kumsaidia mke wako, ...’nikasema.
‘Yah, mke wangu na wewe pia,....nikuambe ukweli, hapa nilipo
nakuwaza wewe, namuomba sana mungu, itokee miujuza, ile hali ya zamani
irejee,sina raha kabisa, najuta kwanini haya yametokea, inafikia hatua natamani
ndoa yangu ifike mwisho tu, ili nijue moja...’akasema.
‘Nini…ndivyo unavyoombea ili iweje sasa, muhimu ni wewe na mwenzako,
...kila mtu ana shida zake, hilo nilowahi kukuambia kuwa usione mimi napata
taabu na mume wangu, wapo watu wanapata shida sana na ndoa zao, sio mchezo,
lakini mwisho wa yote ni nyie wenyewe, kila mmoja anatakiwa kuwa na maamuzi
yake, unasikia, kila mtu aubebe mzigo wake yeye mwenyewe..’nikasema.
‘Haya nakuja , ngoja nimpitie mke wangu, ,....’akasema
‘Sawa na mimi ndio naondoka nyumbani hivyo, uwe makini na mkeo..’nikasema
‘Na wewe pia…’akasema
Nikaanza safari ya kuelekea kikaoni na wakati nipo njiani nikahisi
kuna pikipiki, ilionekana ikinifuata kwa karibu sana, sikusimamisha gari hadi ninafika,
na yule mtu mwenye pikipiki, akanipita, na kunipungia mkono, sikujua ni nani,
kwani alikuwa kavaa helimeti ...mimi nikafika kwenye eneo tulilopangia kufanya
kikao.
Wazazi wangu na mawakili walikuwa wameshafika…,
WAZO LA LEO: Migogoro
mingi huishia pabaya, wengine husihia hata kupigana, au kukosana kabisa, ni
kwanini tukimbilie vita, kukosana, na hata kutalikiana, kwanini kwanza tusikae
tukaongea tukatafuta chanzo cha tatizo ni nini, huenda ni shetani, tu, huenda
ni wenzenu wanataka muharibikiwe tu…mzungumzo ya heri, ya kujadili tatizo yana
tija zaidi ya uhasama wenyewe.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment