Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Saturday, January 27, 2018

MKUKI KWA NGURUWE-68


Nilimfikisha rafiki yangu nyumbani kwao, na akapokelewa na shoga yake, na sikutaka kuongea nao zaidi nikaondoka, kwani ilikuwa ni usiku, na nilikuwa na hasira kweli kweli...na wakati natoka hapo, mara, akakatiza mtu mbele ya gari, nikafunga breki

'Wewe vipi...?' nikafoka

Na mara huyo mtu akasogea kwenye kiyoo cha gari, akaashiria nishushe kiyoo, kwanza nilihofia, sikusha,..akasogea karibu kiasi cha suti kusikika;

‘Usije ukatutosa tena bosi, kesho tunakuja kuchukua pesa zetu....tutakuwa tumeshamaliza kazi...tunasubiria muda muafaka, kama umebadili nia utuambie haraka, maana muda ukifika hakuna kurudi nyuma...na ukighairi bado kuna gharama zetu ni lazima utulipe..’akasema

Mimi pale sikusema kitu!

Tuendelee na kisa chetu

**************

Wakati naendesha gari, kurudi nyumbani kwangu, nilianza kuwaza hicho niichokusudia kifanyike, hapo hapo huruma ikaanza kunijia, nikikumbuka jinsi gani nilivyohadithiwa na mmoja wa watu waliowahi kushuhudia ndugu yao aliyewahi kufanyiwa hivyo, ni ukatili wa hali ya juu, alisema ndugu yao alishindwa kuvumilia, haikupita muda ndugu yao huyo akajiua. 

‘Ina maana mimi nimekuwa na roho mbaya kiasi hicho, japokuwa rafiki yangu amenifanyia huo ubaya, lakini sio vyema, kumtendea hayo, huo utakuwa ni ukatili wa hali ya juu, mbona nimechukua mambo kihasira zaidi, ina maana ubaya nalipiza kwa ubaya wa kiasi hicho, ..kwanza huyo ni mama mtoto , analea, je hicho kitoto kitalelewa nani...’nikajiuliza

‘Ndio labda, nitamchukua mimi, na kumlea kama mtoto wangu,....lakini kila nitakapomuona huyo mtoto nitakumbuka huo ukatili...mmh, hapana...lazima nifikiriz zaidi hili...’nikawa nawaza kichwani huku naelekea kwangu na muda unazidi kwenda.

Kabla sijafika nyumbani ndio nikakumbuka mazungumzo yangu na rafiki yangu huyo tukiwa ndani ya gari;

'Vipi khali ya mtoto, mbona amekuwa mzungu, umemfanya nini mtoto...?' nikamuuliza nilipotupia jicho kwa mtoto, na haraka akamfunika

'Ni fasheni tu, na kuogopa vijicho cya watu...'akasema

'Siku hizi umekuwa mshirikina..?' nikauliza

'Sio wa kikwetu, huo ni wa kitaalamu, ...sitaki watu wamfahamu mtoto wangu alivyo, najua fitina ni nyingi sana, ambazo hazina ukweli...'akasema

'Zina ukweli, ila unauogopa huo ukweli, au sio, kwa vile umevuka mpaka..'nikasema

'Sawa...nitasema nini tena..ila kwa vile nimerudi tutamalizana na wote wanye kutaka ukweli, na sina shaka juu ya hilo...'akasema

'Haya, ila jiandae pia kuachana na huyo mtoto..'nikasema

'Kwanini...?' akauliza

'Unajua ni kwanini, ahadi ni deni, nilishawahi kukuambia kabla, kuwa dhamira yangu ni ile ile..'nikasema

'Sijakuelewa...'akasema

'Utaelewa tu muda ukifika, sizani kama wewe ni jasiri kiasi hicho, wapo mjasiri lakini walishindwa, ogopa sana macho ya watu, ogopa sana watu wakikunyoshea vidole kwa kashafa ya udalilishwaji..'nikasema

‘Huyu mtoto ndiye jicho langu, sitakubali kuachana naye hata siku moja, na hao watakaotaka kufanya hilo, wajiandae pia, maana mimi sio yule wa jana...’alisema kwa kujiamini

'Hahaha, ina maana unajiamini kiasi hicho,..hata baada ya hayo madhambi, badala ya kutubu, ..'nikasema

'Sawa nilitenda madhambi, lakini kwa misingi ya kukubaliana, sikujipeleka mwenyewe, sikulazimisha, na huenda yaliyotokea yalikuwa sio lengo langu, ..lakini ufanyeje na imeshatokea, muhimu ni huyu kiumbe asiye na hatia, nitampigania hadi tone la mwisho..'akasema

‘Hivi hata kama baba yake akimtaka, akaishi naye, kwani labda utakwua kwenye hali mbaya, utamkatalia?’ nikamuuliza.

‘Kwa misingi ipi, kwani mimi nimekufa, au sina uwezi wa kumlea..na hali mbaya gani hiyo ya kunifanya nishindwe kumlea mtoto wangu...hapana hilo halipo..’akasema.

‘Baba yake ana haki na mtoto wake pia au sio...’nikasema.

‘Hata mimi nina haki na mtoto wangu, hilo sikubaliani nalo hata siku moja, kwasabbu mimi mwenyewe nina uwezo wa kumlea, kwanini huyo anayejiita baba aje kumdai mtoto wangu, kwani tuliahidiana hivyo, sikuahidiana na mtu kuwa tuzae halafu mtoto awe wetu sote, hali halipo...’akasema.

‘Lakini wakija na hoja kuwa wanamtaka huyo mtoto, wamlee, ikizingatiwa kuwa huyo baba mtoto ana mke wake, na mke wake yupo tayari kuishi na huyo mtoto, utakataa?’ nikamuuliza.

‘Kwanini lakini...sijasema siwezi kumlea mtoto wangu,...aah, hebu kwanza maana nina mengi ya kufikiria, nimesharudi nahitajia muda wa kutafakari mengi kabla sijaanza kupambana na uhalisia, najua hata wewe unanihitajia sana ...lakini naomba muda kidogo...'akasema

'Muda utaupata tu...na huenda ukiwa umelala kitandani, hujiwezi,...'nikasema

'Mhh...maneno yako yananitisha sana...'akasema

'Dada yangu, bosi wangu...mimi sina cha kuongea kwa leo, sikujiandaa kwa hilo,.ila kwa hilo la mtoto na huyo anayejiita baba yake, kauli yangu ipo wazi, kuwa huyu mtoto sitaachana naye kamwe,labda mimi niwe maiti...’akasema.

‘Hujaniambia kwa kauli yako ni nani baba wa huyo mtoto  ni nani,...?' nikamuuliza

'Kifupi hana baba...'akasema

'Au unaogopa kwa vile ni mume wangu kama inavyojulikana na wengi, maana nimeshayafahamu yoye hayo, na wapi mlipokuwa mkikitania?’ nikamuuliza

‘Waache watu waseme wapendavyo, lakini anayefahamu ukweli wa yote ni mimi mwenyewe, na ukweli huo hautabadilika kwa maneno ya watu..kwa vile hata mimi nina ushahidi wa kitaaamu, nina kila namna ya kujilinda..'akasema

'Ushahidi gani zaidi ya DNA, au umegushi hata hiyo, hata ukigushi tutapima tena na tena..'nikasema

'Kwanini tufanye hivyo, nikitaka nini sasa....?' akauliza

'Mume wangu anamuhitajia mtoto wake, ..hapo alipo hana amani, na ikizingatiwa ni mtoto wa kiume, anamuota na kuchanganyikiwa kwa ajili hiyo, hujui jinsi ani mume wangu aliposikia una mtoto wake wa kiume alivyofurahia...'nikasema

'Huyo shemeji, akiwa hivyo basi hana akili...'akasema

'Kwanini...?' nikauliza

'Wewe hujui jinsi gani niivyotaabika na huyo mume wako, hujui tu, vinginevyo angeliishia kutembea na changudoa, lakini nilimsitiri, na kumlinda ili aendelee kuitunza ndoa yake, lakini hayo hutanielewa kwa sasa nitakuja kukusimulia yote, nipe muda nipumzish kichwa, na kukusanya ushahidi wote..’akasema

‘Hahaha, yaani unajisifia kuwa uliweza kuhangaika naye, kuzini na mume wa mtu huoni ni kosa kubwa, au ulimsitirije...?' nikauliza

'Nitakuja kukuelezea...'akasema

'Vyovyote iwavyo, zinaa, na kutembea na mume wa mtu ni dhambi kweli si kweli..?' nikauliza

'Uliyajua hayo sio..sasa hivi unayajua hayo, umesahau eeh...kuwa wewe ndiye uliyenishauri nikazini, nitembee na hata mume wa mtu...'akasema kwa hasira.

'Hahaha...kwahiyo ukataka kunikomoa, au sio...na hata wakati nakushauri hivyo mlishakuwa na mahusioano wewe ulitaka upate mwanya tu wa kuyafanikisha hayo, mimi sikujua lengo lako ni nini,..na ushahidi upo...'nikasema

'Mhh..kichwa kimechoka jamani..'akasema

'Utapumzika tu..japo sijui., sasa kwa kumbukumbu maana huenda huko tunapokwenda tunaweza tusipate muda wa kuongea hivi tena, hebu niambie huo mkataba wa bandia mlioutengeneza, na Marehemu, lengo lenu ilikuwa ni nini, kulinda haki za mtoto, au kutaka mali, angalia mwenzko alikuwa na tamaa hiyo sasa yupo wapi..?’ nikamuuliza

‘Mimi sijui lolote kuhusu huo mkataba, hayo ni ya kwao, mimi nina maisha yangu ya kujitegemea mimi mwenyewe sijawa kilema,..ni wao tu walinilazimsha kuweka sahihi, na wakati kaam ule sikuwa na jinsi,na sijakaa na kuliwazia hio...'akasema

'Sasa unavyosema kuwa una kila namna ya kujilinda una maana gani..?' nikauliza

'Mimi nazungumza maswala ya kitaalamu, kuhusu mtoto wangu,...kuwa hana baba,kama wanavyodai watu, na nitalithibistiha hilo hata mbele ya mahakama, huyu ni mtoto wangu mwenyewe....’akasema

‘Kwa vipi,...huwezi kuzaa mwenyewe, hukupandikizwa mbegu, wewe ulizini na waume za watu, ndio ukazaa, na huyo mwanaume ni mume wangu, hata kama ulizini na wengine, lakini aliyewezesha wewe kupata mimba ni mume wangu, kwei si kweli...?’ nikamuuiza.

‘Kuzini ni kitu kingine, wangapi wanazini na hawapati mimba,...sitaki kuyaongelea hayo zaidi maana hutanielewa, maana kwa hivi sasa huwezi hata kukumbuka kuwa wewe ndiye uliyekuwa mshauri wangu mkuu, mimi sikuwa na wazo hilo kabla, sikuwa na tabia ya kutembea na waume za watu kabla,..'akasema

'Hahaha, hiyo ni kauli ya kujitetea, wakati mlikuwa mkikutana kwa rafiki yako, ndio ilikuwa makao makuu yenu, mkisingizia mnaongea mambo ya kikazi, au umesahau,...'nikasema

'Haina ukweli kabisa hiyo,..mimi nilianza kutembea na waume za watu baada ya wewe kunishauri, nafahamu hutanielewa, na sina njia nyingine ya kukuelewesha, kwasasa,...sina zaidi, naomba tusiongee, tutakuja kuyaongea siku nyingine....’akasema

‘Hamna shida...lakini kiukwei, sitakuja kukuelewa kamwe, mimi siwezi nikawa mjinga kiasi hicho, eti nikushauri ukazini na mume wangu halafu, halafu kitendo hicho hujafanya mara moja, ungelisingizia kuwa ni bahati mbaye, mlikuwa mumelewa, kumbe kila siku ndio ilikuwa kazi yenu...’nikasema.

‘Wewe hujui tu, ...usilolijua ni sawa na usiku wa giza, ...’akasema.

‘Ndio siwezi kukuelewa, hakuna sababu ya msingi ya kuzini na mume wa mtu, tena mume wa rafiki yako, rafiki yako unayemtambua kama dada yako, anayekuamini..mpaka sasa akili yangu inashindwa  kuamini kama kweli wewe ulifanya hivyo,huna sababu ya kusamehewa,  ..’nikasema na kumwangalia, alikuwa kakunja uso na kushika kichwa kuonyesha kukerwa na hayo ninayoongea.

‘Naomba tuyaache hayo mazungumzo dada maana hayana ukweli..yananitesa sana moyo wangu, na kwa vile, nimesharudi ngoja nipate muda, nitakuambia ukweli ulivyokuwa,..lakini kwa sasa naomba uniache, sina cha kuongea zaidi...’akasema

‘Haya mimi naisubiri hiyo siku kwa hamu, maana umeshaniahidi mara nyingi kuwa utaniambia, sasa umerudi, sasa utausema hata ukiwa hao kitandani,...nataka kusikia huo utumbo wako, wa kujiidhinishia madhambi yenu, mimi nilichotaka ni kauli yako tu, kuwa kweli ulizini na mume wangu, ungeisema hapa, ningeshamalizana na wewe,...'unasikia

'Sawa nimesikia, na siwezi kusema uwongo..'akasema

'Ilimradi umekubali kuwa ulizini na mume wangu, hiyo inatosha... inatosha kabisa...asante sana.’nikasema 

'Sijakubaliana na hilo..lakini subiria...'akasema na mimi nikaka kimiya,kwani hata mimi niikuwa na mawazo yangu kichwani, na hasira nilizokuwa nazo zilikuwa kubwa sana, kwahiyo tukawa tupo kimiya hadi tunafika.



*******

 ‘Je ni haki kumufanyia huyo mama wa mtoto hayo ninayotaka kuyafanya, akili yangu hakukubaliana na huo uamuzi,  niliingiwa na wasiwasi, nikawa na mawazo mengine kuwa niwazuie wasiendelee na hilo zoezi, kwani kama walivyosema, vitendo watakavyomfanyia vinaweza kumuua, na hata kama hatakufa hapo, lakini anaweza kuja kujiua mwenyewe

Nikaamua kuwapigia simu ili wasitishe hilo zoezi, lakini simu zao zikawa hazipatikani, nikaamua kumpigia simu huyo rafiki yangu, ambaye alipokea simu yangu halafu aliposikia sauti yangu, akakata simu.

Muda ukawa unakwenda na na sikujua kabisa nifanye nini, maana muda huo ni usiku, na nisingeliweza kurudi kule kwa rafiki yangu, mara simu ikalia, nilipoangalia mpigaji nikaona ni baba yangu;

‘Baba mbona simu usiku-usiku..?’ nikauliza baada ya kusalimia

‘Je kikao cha kesho kipo , kama ulivyotaka?’ akaniuliza

‘Ndio baba nimeamua iwe hivyo, ..’nikasema, maana nilipanga kuwa , tuwe na kikao cha pamoja, kikiwahusisha wazazi wangu. Niitaka kikao hicho kiwe cha hitimisho ya hayo yote, ili hukumu itolewe na kila aliyehusika awajibike.

‘Basi itakuwa vizuri, na uwe na ushaidi wote, kwani sisi hatutaweza kuvumilia hayo yanayotokea kwenye familia yako, nilishakuambia kuwa mimi sitaki kashifa, sasa hicho kinachoendelea hapo kwenu kinaniharibia jina langu...unalifahamu hilo, na mpinzani wangu wa kisiasa anazidi kuwa juu yangu,..nikikosa kuchaguliwa safari hii, sitawasamehe..je una kila kitu?’akaniuliza

‘Kwanini unasema hivyo baba, kwani kuna nini kimetokea huko kwako…kwasabau hayo yote hayana ukweli, zaidi ya kashfa za kupandikiziwa?’ nikamuuliza

‘Jana Askari walifika hapa kwangu na kunihoji, ...wanahisi kuna uwezekano mkubwa kuwa mume wako kahusika kwenye mauaji ya Makabrasha, na wanayo ushahid wa kutosha, na kwanini waje kwangu badala ya kumkabili mume wako, unaona jinsi wanavyopanga mambo..’akasema

‘Na hapo najiuliza kwanini waje kwako, ungewauliza na kuwaambia utalichukulia kisheria zaidi ili waogope..?’ nikauliza

‘Kwasababu wanatumiwa na mpinzani wangu, sio kwa kuwatuma lakini mpinzani wangu anapandikiza fitina na askari kadi yao ni kuhakika ukweli,..na zaidi wameniuliza  mahusiano ya kampuni zangu za zako, na kwanini kulionekana mikataba miwili..’akasema

‘Mikataba gani baba, hayo yanakuhusu vipi..?’ nikauliza

‘Yananihusu kwa vile nina hisa kwenye kampuni zenu, na kuna mikataba kama hiyo ya kuuza hisa kwa watu wengine mimi nina maoni gani kama mmoja wa wenye hisa..ni aswali ya mitego…’akasema

‘Kwahiyo umewarizisha kwa majibu..?’ nikauliza

‘Kuwarizisha kisiasa sio tatizo kwangu, tatizo ni huo mtego wa mpinzani wangu alikuwa na malengo gani,..na muhimu kwetu ni kuhakiksha tupo safi, familia ipo na mashirikiano manzuri, na isitokee kashafa nyingine tena…umenielewa..’akasema

Baba aliposema hivyo nikakumbuka hilo nililopanga litokee kwa rafiki yangu, linaweza kuleta kashfa mbaya kwenye familia na inaweza ikawa ni chanzo cha waandidhi kudadisi…oh, sasa nimefanya nini, nilitamani nikate simu, nianende kufuatilia hilo.

‘Swali jingine ambalo linawatia shaka, ni kwanini mume wako akamchuku amakabrasha kama wakili wake na ilihali tunatambua tabia ya huyo wakili, na kwanini kuna mikataba miwili ya familia yenu,  je huo mkataba mpya ulitayarishwa lini na kwanini mkampa hiyo kazi Makabrasha, wakati mnamfahamu tabia yake?’ akauliza

‘Baba hilo ni moja ya jambo tutakaloliongea kesho, kuna mengi yamefanyika, nakubali hilo, na nimeamua kesho niyaweka yote wazi,, ili kijulikane kimoja, mume wangu hajambo, na anaweza kujieleza, na lolote linaweza kutokea, sijaamua ni nini cha kufanya baada ya hapo, ukizingatia kuwa mume wangu hajawa na afya ya kutosha, inabidi nitimize wajibu wangu kama mke wake..’nikasema

‘Hujaamua la kufanya hadi sasa, wakati unaishi na mtu anayeweza ku-kuua, kwa ajili ya mali zako, wewe hulioni hilo, kama wamefikia hatua ya kubadili mikataba ya halali...na katika harakati zao, inaonekana walishindwana,  wakauana. Huoni kuwa mkono ukionja damu, inakuwa kama muonja asali, hajali tena kufanya maasi,....hilo sisi hatutalikubali, kama wazazi tutachukua hatua ...’akasema.

‘Baba nafahamu, mnavyojisikia ...lakini...’nikataka kujitetea lakini baba hakukubai kunipa nafasi , akasema;

‘Sitaki kusikia jambo jingine la kupinga maamuzi yangu, kama unanikubali mimi kuwa ni baba yako, kama unamkubali mama yako, basi itabidi ukubaliane na sisi, ....wewe huoni, wameamua kumuua,mtu wao wanayemuamini, na kumtambua kama sehemu ya famiia yao, kwa ajili ya kuficha ukweli, unafikiri watakuwa na huruma na wewe, binti yangu nilishakuambia huyo mume hakufai, mbona unatuweka roho juu...’akasema

‘Baba nilishawaambia mambo yangu nitajua jinsi gani ya kuyatatua, mwenyewe...niachieni,kwanza, nifanye nijuavyo mimi, ...msikimbilie kuchukua maamuzi yenu kwanza,kesho nimewaomba ili muweze kusikia maamuzi yangu, ambayo yatakuwa ni maamuzi yenye muafaka wa kudumu, nimesema sijafikia uamuazi bado, lakini mpaka kesho nitakuwa nimeshaamua ni nini cha kufanya, kwani kuna mambo ambayo nilikuwa nayamalizia...’nikasema.

‘Ulikuwa unamsubiria mpelelezi wako, ambaye keshakusaliti,...usimwamini huyo binti, kesharubuniwa, na kwasababu ya mali ..kwasababu ya tamaa, na kwa vile ana mahusiano na mume wako hatajali lolote itakao tokea kwako....anakufahamu udhaifu wako, anafahamu siri za kwako za nje na ndani, kwahiyo hatasita kukufanyia lolote baya....’akasema.

‘Baba huyo nimeshamweka sawa, hana lolote kwangu, nimeshamfahamu,...’nikasema

‘Sisi kama wazazi, tumeshafikia uamuzi,  sisi kama wazazi, kesho tutatoa maamuzi yetu,kwa masilahi ya familia kuu, hili siwezi kulivumilia tena, na tuijaribu kuongea na mume wako, tuone lipi jema kwa hayo yote, asing’ang’anie ndoa tu wakati haiwezi, hivi karibu nikiongea naye ananijibu kama sio yule mkwe ninayemfahamu tena, kwanini kabadilika hivyo, wameshajua kuwa wamekuweka mkononi mwao, ....’akasema.

‘Baba kwanini mnaongea na huyo mtu wakati yupo kwenye matibabu,...hamuoni kuwa mtakiuka makubaiano yangu na yeye.....’nikasema.

‘Mume wako alishapona, na hayo yaliyotokea baada ya yeye kupona, ni moja ya mbinu zao, sisi hilo tulishaiona, na tumeshaongea na dakitari wake, na ingawaje dakitari wake anamtetea, lakini tuna uhakika kuwa mume wako anafanya hivyo makusudi, ili kufanikisha maengo yake na sio malengo yake, yeye anatumiwana mpinzani wangu bila hata ya yeye kulifahamu hilo...’akasema

‘Baba naombeni mniachie nifanye jinsi nionavyo mimi,...nisingelipenda nyie muingilie kati kwenye maamuzi, kwani mimi sijashindwa bado..’nikasema nikiangalia saa yangu

‘Ushindwe mara ngapi, kama umekubali, mume wako awe na nyumba ndogo, umekubai mume wako, azae nje, hujashindwa hapo. Hilo lilikuwa ni jukumu lako kubwa sana kuhakikisha kuwa mume wako anakuwa na utulivu wa ndani, ....hukuweza kulifanya hilo, na huo unaonyesha udhaifu, niambie kuhusu watoto wa mume wako ....au unafikiri sisi hatufahamu hilo?’ akaniuliza

‘Watoto!! Watoto….?? watoto gani wa mume wangu,?!’ nikauliza kwa mshangao

‘Unaniuliza, wakati sasa hivi umesema kuwa mambo yako utayaongoza mwenyewe, ..hufahamu kuwa mume wako ana watoto nje..huoni athari zake, wewe unalichukulia kawaida tu, hiyo ndio adabu tuliyokufundisha, huoni hiyo ni aibu kwenye familia yetu,…’akasema

‘Baba mimi nimesikia tetesi za mtoto lakini sio watoto..’nikasema

‘Mhh,. Halafu unajifanya kuwa unaweza kujimudu mwenyewe, hivi unatuweka wapi sisi,..hebu angalia maisha ya mbele, hao watoto, watakuja kujitokeza na madai yasiyoeleweka, watakuja kugombana na wenzao, ...maana kwa hivi sasa hamuwatambui, mpaka mmoja wenu afariki,..ndivyo ilivyo, ni heri wangejitokeza muda huu, mkiwa hai, ili mjue ni nini cha kufanya, haya tulikukanya, tunaifahamu sana hiyo familia...’akasema

‘Baba hili nimeligundua, lakini nijuavyo mimi , mtoto wa nje ni mmoja tu, huyo wa pili sio kweli’ nikasema.

‘Huyo wa pili sio kweli, ni yupi wa kweli na yupi sio wa kweli?’ akaniuliza na mimi hapo sikuwa na uhakika wa kumuelezea nikasema.

‘Baba yupo mtoto namfahamu,...japokuwa mume wangu hajanikubalia, na hata huyo mzazi mwenzake hajakubali lakini ushahidi wake kwa hivi sasa upo wazi, hawezi kuliping ahilo tena...’nikasema

‘Mimi nina ushahidi, ana watoto wawili,...unamkumbuka yule mfanyakazi wenu wa ndani aliyeondoka hapo bila kuaga,ulifuatilia ukajua ni kwanini aliondoka bila kuaga,...hujui kuwa aliondoka kwa shinikizo la mume wako…?’ akauliza

‘Mhh…mbona sina habari hizo..’nikasema

‘Ndio sasa tunakuambia..mume wako anaweza hata kutembea na mdogo wako kama mtaishi naye hapo nyumbani,…, ilikuwa siri yao wawili, huyo binti  aliondoka akiwa mja mzito, na mume wako anafahamu, akawa anamtumia pesa za matumizi huko huko kwa siri, alijifungua, mtoto wa kiume, wanafanana na mume wako kama mapacha...’akasema

‘Mhh, hilo kwangu ni jipya, sikuwahi kulisikia, nitamuuliza mume wangu na ikibidi nitamtafuta huyo binti ii niweze kuhakikisha ...na kesho hayo yote yatajulikana, na ingekuwa vyema huyo msichana awepo kwenye hicho kikao, ..nyie mlipata wapi hiyo taarifa?’ nikamuuliza

‘Sio kwamba tumesikia, huyo msichana yupo hapa kwangu, alikuja kulalamika, kwasababu tangu mume wako aanze kuumwa hajatumiwa pesa za matumizi, na ilikuwa bahati tu kumpata, na sisi ikabidi tumchukue aje hapa kwetu, alikuwa mbioni kuja hapo kwako, tumelifanya hilo ili kuepusha kashifa zaidi…, sasa hili halina siri tena, unafikiri wewe utachukua hatua gani, ili hii hali isifike kwa hawa wadaku...’akasema

‘Oh,..baba naona unipe muda niweze kulfikiria hilo,,imekuwa ni mshtuko kwangu,…kiukweli siwezi kuvumilia tena....’nikasema nikiwa nimeingiwa na wasiwasi, kumbe namuhukumu mtu mmoja, na huyo je atahukumiwa na nani, na je ni hawo wawii peke yao....

‘Huna haja ya kuumiza kichwa, nashukuru kusikia kuwa umeshaupata huo mkataba wenu wa hiari, kati yako na mume wako,...nimeupenda, na ni vyema sasa ukachukua hatua kama mivyokubaliana, na kama utashindwa kuchukua hatua, ujue wewe huwezi kujiendesha wewe mwenyewe...huo ndio mtihani wako, sisi tumeshachukua maamuzi yetu,....’akasema

‘Baba naomba nipumzike, maana akili yangu haipo sawa...’nikasema

‘Haya usiku mwema,..lakini uwe makini, usije ukachukulia hasira, ukatenda mambo kama mtu asiyesoma, ujue kuna sheria,..ujue ni kitu gani unachotakiwa ukifanye kama msomi, unasikia,  usije ukatenda mambo kama watu wengine, ...ukiharibu , sisi hatutakubali...’akasema

‘Sawa baba....’nikasema

Nikachukua simu yangu na kumpigia rafiki yangu, akawa hapatikani, nikajaribu kuwapigia hawo watu niliowapa hiyo kazi, na wao wakawa hawapatikani...sikukubali, nikatoka nje, na kuingia kwenye gari, sikuwa na muda wa kuongea na mlinzi, nikalitoa gari, na wakati nataka kutoka mlinzi akaja kunisalimia

‘Bosi unatoka?’ akaniuliza

‘Ndio kuna kazi nafuatilia, je mambo yapo sawa?’ nikamuuliza

‘Yapo sawa...’akasema lakini nilimuona kama alitoka kulala..

Wakati nimeshafika barabarani, nikahisi kuna mtu nyuma yangu, ndani ya gari, na kabla sijaweka gari sawa, sauti ikasema;

‘Fuata maelekezo yetu, la sivyo, tutakufanya kitu kibaya..’sauti nzito ya kiume ikasema na nikahisi kitu kikali kikigusa ngozi yangu, nikahisi kuwa ni kisu....

NB; Kulikoni...

WAZO LA LEO:Ushauri wa wazazi ni muhimu sana, tunaposhauriwa na wazazi wetu tujaribu kuwasikiliza, hata kama tunajiona tuna uwezo zaidi yao wa kihali na mali, tujue kuwa wao wameona mengi zaidi yako, na wamepitia maisha ambayo wewe hujawahi kuyapitia, hekima zao zinaona mbali zaidi, tuwasikilize, tukae pamoja nao, tuone je mawazo yao na mawazo yetu yanaweza kufikia muafaka wenye manufaa, tusichukulie ubabe kwa vie tunazo, tumesoma sana, nk.


Hata hivyo, na wazazi nao wanahitajika kuwasikiliza watoto wao, wasikie mawazo yao, kwani  huenda kwa elimu yao mpya, na upeo wao wa kuchanganyika na watu wanaweza wakaja na njia mbadala,...hii ni kwa nia njema, kwani  maafa yakitokea ni athari za pande zote.

Ni mimi: emu-three

No comments :