Mwenyekiti alituliza kikao baada ya kuona kuna majibishano makali
kati ya rafiki yangu na mume wangu, kiasi kwamba kama asingeliingilia kati yangelizungumzwa
mengi ambayo hata hayakustili kuzungumzwa kwenye hicho kikao bila mpangilio
maalumu..
Tuendelee na kisa chetu…
************.
Rafiki yangu alipewa kibali cha kuongea na mwenyekiti, akawa
anatoa maelezo yake, japokuwa mimi akili yangu ilikuwa mbali sana, lakini
niliweza kumsikiliza, rafiki yangu alisema;
‘Nitatoa maelezo yangu katika sehemu kuu mbili, ya kwanza ni
ukweli kabla sijapata mtoto na sehemu ya pili yenye ushahidi mnzito, ni ukweli
baada ya mimi kujifungua, naomba muwe watulivu, ili niweze kuyasema yote
niliyoyakusudia kuyaongea leo hii...niliahidi na sasa natimiza’akasema na
kuniangalia mimi.
‘Mimi ninaamini kwamba kila jambo huja kwa minajili fulani, na
hili la kupata mtoto huenda na kweli limetokea ili iwe fundisho sio kwangu tu,
na hata kwa wale wote lililowagusa kwa namna moja au nyingine. Ni changamoto,
ambayo sitaweza kuisahau katika maisha yangu, ....’akasema
‘Hii ni changamoto iliyonipa fundisho moja kubwa, kuwa kutaka
kupata kitu kwa njia zisizo halali, zina mateso baadae, usijione umepata
ukadhani umefanikiwa, mitihani yake ya hicho ulichokipata kwa njia isiyo halali
huja baadae, na huko ndipo kwenye majuto…’akatulia
‘Kiukweli mimi nimechelewa kuzaa, na sababu kubwa, naweza kukiri
kuwa ni madhaifu yangu ya kupenda kuchagua…nisipoteze muda huko, ni kwanini
ilikuwa hivyo, lakini kitu kilichokuja kunigusa baadae ni kuwa, nilikuwa nataka
kupata mtoto, sasa swali likaja nimpateje..’akatulia
‘Madhaifi yangu yapo pale pale, nikitaka kitu nakichanganua sana,
haya nataka mtoto aweje, na ..afananeje..hilo likawa ni changamoto pia kwangu,
kiukweli sio siri, kuna watu niliowapenda, bahati mbaya wengi niliowapenda
walikuwa waume za watu, siwezi kulificha hili..hata hivyo sikupenda kuvunja
ndoa za watu, nikiwa na maana sikutaka kabisa mahusiano na mume wa mtu.
‘Mimi nilifikia kuhini ahadi yangu ya kuzaa ndani ya ndoa, na pili
kwa mume asiye kuwa mume wa mtu, na ilipotokea nilitaka iwe siri kubwa..na pia
nikata mtoto huyo asiwe na baba, japokuwa huwezi kuzaa mtoto bila baba, haya nitayaeleze
kinamna, kwa jainsi tunavyokwenda..’akasema
Japokuwa nilipanga iwe hivyo, kuwa mtoto ni wangu, na hana baba,
lakini mume wa familia alipogundua kuwa nimejifungua, akawa wa kwanza kufika
hospitalini, na alipomuona tu huyo mtoto, aligundua kuwa ni wake...haijifichi.
'Kiukweli mume huyu alipagawa hasa pale alipojua kuwa mtoto huyu
ni wa kiume maana ndoto yake kubwa ilikuwa kupata mtoto wa kiume,na hapo hapo
akasema huyo ni mtoto wake, hakuna ubishi,...
‘Siku ile nilipojifungua nilijaribu kila njia ili huyo mume asijue
lolote, lakini ilishindikana, na kama nilivyosema kila kitu huja kwa sababu
fulani, nahisi hata kufanana kwa mtoto huyu na huyu mwanaume ni sababu maalumu
ya kuliweka hili jambo liwe bayana.
‘Siku ile ile nikajua sasa mambo yatakwenda kinyume na
matarajio yangu, kinyume na makubaliano yangu na mshauri wangu mkuu, kuwa
nikizaa, hata kama nimezaa na mume wa mtu , hiyo iwe iri yangu mimi mwenyewe
asije kufahamu mtu yoyote.
‘Mimi ninahisi kilichomfanya mume wa familia ang’ang’anie sana ni
kwa vile nimepata mtoto wa kiume, na yeye kwa kauli yake mwenyewe, alikuwa
akitaka mtoto wa kiume, maana watoto alio nao hadi sasa na mke wake , ni watoto
ni wa kike...'akarudia sehemu hiyo.
'Kiukweli mimi sikuyajali hayo kwani mipangilio wangu ulikuwa
nizae mtoto, na huyo mtoto awe ni wangu wote hata nikiandikisha jina lake
kwenye cheti chake, lisomeke jina lake,na ubini wa baba yake, liwe ni jina
langu kwa herufi yangu ya mwanzo, halafu jina la tatu liwe la baba yangu mzazi
ndio nilivyotaka iwe hivyo...'akatulia
Lakini baadaye tulipokutana mimi na mwanasheria wao na mume wa
familia, mume wa familia akasema hilo halikubali, mtoto huyo ni wake, kwani
yeye ndiye mume aliyeweka mbegu, naye pia ana haki zake na anawajibika kwa
mtoto,na hata kisheria za nchi, inabdii iwe hivyo.
Kwahiyo akanisihi kuwa mtoto huyo aandikwe kwa ubini wa baba yake,
nilikataa, na huyo wakili akarudi kwa mume na wakaongea walichoongea, na
aliporudi kwangu, akasema mume huyo kasema huyo mtoto ni lazima atambulikane
kuwa yeye ni baba yake, na hili atalifaya nipende au nisipende.
'Sasa hiyo upende au usipende ina maana gani, ndio hapo utaona
mbinu walizokuja kutumia baada ya kuona mimi nimekaidi maagizo yao, nitayaeleza
hayo kwenye ushahidi wangu wa pili,..ambao una mambo magumu zaidi…
Kabla ya hiki kikao tulikutana mimi na yeye, moja ya ajenda yake
ni hiyo ya mtoto kutambulikana kuwa huyo ni mtoto wake kisheria, ...maana mimi
nilishakataa...pamoja na mengine mengi aliyoyataka, mimi nikawa kinyume
chake...'akatulia
Kwahiyo yeye akaja huku kwenye kikao, akisema akifika huku
kwenye kikao atahakikisha kuwa huyo mtoto anatambulikana, kwa vile anao uwezo
wote kikatiba yao ya kifamilia,
'Kwa vipi ...?' akaulizwa
'Alisema mkataba alionao yeye unampa hiyo nafasi, alinionyesha huo
mkataba, lakini niliuona una utofauti mkubwa na ule mkataba ambao niliwahi
kuusikia kutoka kwa rafiki yangu , sikuwahi kuusoma huo mkataba wao wote kiundani
maana ni mambo yao ya kifamilia, lakini kwa kauli ya rafiki yangu, mkataba wao,
ulikuwa hauruhusu mume au mke, kujitwalia madaraka bila kumshirikisha mwenzake.
Ndivyo nilivyokuwa nafahamu hivyo.
Na nakumbuka rafiki angu huyo aliniambia kuwa kama mmoja
akimsaliti mwenzake, na ukapatikana ushahidi bayana, na ushahidi bayana unaweza
ukawa wa kuona tendo likitendeka, au ushahidi wa vielelezi kama hivyo mtoto wa
nje..basi mtenda kosa kavunja mkataba, na hapo atawajibika, ..kama mkataba wao
unavyosema
'Kwahiyo mpaka hapo nilijua kabisa hili jambo likija kugundulikana
ndoa hiyo haipo tena,..na ukumbuke kufahamu kuhusu mkataba wa kifamilia
nimekuja kulifahamu hilo baada ya mimi kupata mtoto, mkataba wao huo ulikuwa siri
yao, wanafamilia haou….mnielewe hapo,….'akatulia
'Na nilikuja kumwambia wazi huyo mume wa ndoa siku kadhaa
alipokuwa akizidi kung’ang’ania kuwa huyo mtoto ni wake, ilibidi nimkumbushe
hilo, baada ya kugundua kuwa kumbe wana mkataba mkali kama huo...'
‘Wewe unataka huyu mtoto hujui kutambulikana kwake ndio utakuwa ushahid
wa kuvunja ndoa yenu? Nilimuuliza hivyo, sasa uone alivyonijibu…’akasema
‘Hilo nimeshalifanyia kazi,
kila kitu kitakwenda sawa, mimi ndiye mumiliki wa kila kitu,na nina
madaraka yote, kuna mambo macheche tu hayajakamilika, lakini yapo mbioni
kukamilika,..'akasema
'Kwa vipi..?' nikamuuliza
'Wewe utayaona tu, haya yalishapangwa, na yatafanyika tu, usicheze
na watu na fani zao, kuna mtu mkali analifanyia kazi, hutaamini..'akasema
'Kwahiyo unataka mimi nifanye nini..?nikamuuliza baada ya kuona
ananitishia maisha’
'Wewe ninavyotaka mimi, hii
hatua ya kwanza ikipita, utaona, kuna ujanja ujanja mwingine unatakiwa utumiwe,
mke wangu akikubali baadhi ya mambo, na ukapatikana ushahid basi mkataba huo
utakuwa umeshafanyiwa kazi,...kila kitu kitakuwa mali yangu, na hapo nitajua
jinsi gani ya kukuingiza wewe.
‘Kuniingiza mimi kwa vipi..?’ nikamuuliza
‘Kama mshirika mwenza, wa kila hali, na huenda tukajaliwa kupata
watoto wengine zaidi...'akasema
‘Kwanini unataka upate watoto na mimi, kwani mke wako hatoshi..?’
nikamuuliza
‘Hataki, mke wangu hataki, yeye anasema kazi kwanza, tuej kuzaa kwa
malengo, mimi sioni ubaya wa kuzaa, maana mali tunayo, na watoto ndio wa
kuzitumia, na sasa hivi tuna mabinti, wataolewa ni nani wa kuendeleza mali zetu…’akaniambia
hivyo
Hapo mume wa familia hakuweza kuvumilia akasimama na kusema;
'Mwongo wewe, hivi kwanini unataka kusema huo uwongo, usiseme
lolote kuhusu watoto wangu, mimi nawapenda sana watoto wangu, sikiliza tunga
uwongo wako wote lakini usiguse watoto wangu, …mke wangu usimsikilize huyu
lengo lake ni kuniharibia ndoa yangu…na wewe,..' mume wa familia akaingilia
kati kumkatisha mzungumzaji huyu.
'Hahaha, unataka nitoe ushahidi,…?’ akauliza
‘Ndio toa, una ushahidi gani wewe acha uwongo wako..?’ akasema
‘Una uhakika na unachokitaka, unauhakika unataka nitoe ushahidi au unasema tu kujihami?’ akuliza mzungumzaji
na mume wafamilia alitaka kuongea kitu, lakini wakili wake akamzuia. Wakawa
wanateta kwa chini chini…
‘Kama unataka niyathibitishe haya kwa ushahidi mimi nipo tayari,
ushahidi upo, nikipata kibali kutoka kwa mwenyekiti nitafanya hivyo…’akasema
mzungumzaji
‘Ushahidi gani ulio nao wewe…?’ akauliza wakili wa mume wangu
‘Muhimu ni ushahidi, ..siwezi kukuambia kwa hivi nina ushahidi
gani, lakini ushahidi upo, nikipata kibali nitauotoa hadharani, ..’akasema
akimgeukia mwenyekiti
‘Je naweza kuutoa huo ushahidi…?’ akauliza, na mwenyekiti akageuka
kuniangalia mimi, halafu akageuka kumuangalia wakili wake, halafu akasema;
‘Kama kikao, kwa hivi sasa tunahitajia maelezo tu, nia yetu ni kuwaptia
nafasi waliokosea wajirudi, wawe wakweli kwetu, tulimalize hili kwa amani, na
kama kuna makosa mengine ya kisheria, hayo sio juu yetu,…sasa mpaka tunafikia
hatua hii ni kwamba watu hawataki kujisalimisha na kuomba msamaha, lakini sasa
wataendelea hivyo haitakuwa na budi, kila kitu kitawekwa hadharani..’akasema
mwenyekiti
‘Kwahiyo mwenyekiti unasemaje..?’ akauliza mzungumzaji.
‘Labda utupe maelezo yako tu, kuwa una ushahid wa namna gani,
mengine yatafuata baadae…’akasema mwenyekiti.
‘Tulipokuwa na kikao hicho mimi na yeye tulikuwa wawili tu, lakini
mimi nilikuwa na kitu cha kurekodi mazungumzo yetu, na kipo tayari hapa kama
ushahidi je nitoe hayo mazungumzo yetu yasikike na kila mtu, na tusije
kulaumiana baadae..?’ akauliza mzungumzaji
‘Ndio toa…’akasema mume wa familia, baadae wakili wake akawa
anamzuia, wakawa wanateta, jambo, mzungumzaji akawa anasubiria wamalize, na
alipoona wanaendelea kuongea kupoteza muda, yeye akasema;
‘Nilishajiandaa kwa haya yote na usahidi kila hatua ni muhimu
sana, kama itabidi, nitautoa huo ushahidi na watasikia yote na yale ambayo mume
wa familia hatapenda yasikike hapa kikaoni, …’akasema
‘Sawa tumekuelewa…’aliyesema hivyo sasa ni wakili wa mume.
‘Ni kweli maana mume wa mtu alikuwa akinibembeleza, akasahau kuwa
ana mke, sasa hayo yakisikika, sio vizuri, au sio, au niyasema hapa ulivyokuwa
unanitongoza,..’akasema na watu wakaguna
‘Ni kweli haya ninayoyaongea, ameongea mengi sana na ya aiabu,…wakati
mwingine nahisi huyu jamaa yetu hayupo sawa, namuheshimu sana, lakini kavuka
mpaka,..na jamani kwa hali kama hii aliyo nayo bado huogopi,.. lakini ndio
hivyo, mimi nahisi marehemu alimteka sana akili yake maana yule shemeji
ninayemfahamu sio huyu wa sasa,…na pengine, ila mimi sina uhakika na hilo,
nasema pengine, hiyo ajali yaweza kuchangia..’akasema.
‘Wakati mnaongea naye, kwa kugusia tu mliongea maswala yapi na
yapi, ambayo ni muhimu kama kikao wakayafahamu…?’ akaulizwa
‘Kuna mengi, aliyaongea, mimi kama binadamu siwezi kuyasema au
hayafai kusikilizwa hapa mbele za watu, ..maana huenda hakunifahamu kuwa mimi
ni nani, wakati namchota akili, na akaingia kwenye anga zangu, akajikuta
anaongea kila kitu, hahaha, wewe mtu, uwe makini, hajui kwa hivi sasa kila
kauli yake inachukuliwa kwa uzito mkubwa sana, chunga ulimi wako wewe mtu..kwa
kuhusu seehmu hii kwa tuliyoyaongea ni hayo, labda kwenye shemu ya pili...'akasema
na hapo mume wangu akanywea.
‘Endelea,…kama ushahidi tutauhitajia tutakuambia baadae … ila nina
swali..’akasema wakili mtetezi
‘Kuhusu nini…?’ akuliza mzungumzaji
‘Wewe, unaposema kuwa hayo uliyoyafanya uliyafanya kwa kushinikizwa,
sio kwamba ulifanya baada ya kuona kuwa mkataba wa familia utakuja kukunufaisha,
na sasa unajifanya kujikosha ili uonekane wewe ni mwema..?’ akulizwa na wakili.
‘Kuhusu huo mkataba wao, sikuwa naufahamu kabla, kwani pia unaweza
kusema kuwa nilifanya makusudi ili nipate mtoto na huyo mume, ili ndoa yao
ivunjike, ili mimi nije kuchukua nafasi ya mke wa mume wa familia, na mali iwe
imeshaandikiswha kwa mtoto wangu,..ndio mawazo yak ohayo sio…, au sio..?’ akawa
kama anauliza. Na wakili akabakia kimia tu!
‘Hiyo sio kweli, mimi tokea awali nilishawaambia sitaki lolote
kuhus mtoto wangu, na pia sina tamaa ya mali, hasa mali hizo za kitapeli,
niliwaambia hilo mapema sana wakanishangaa…, na hata kwenye kikao chetu cha
hivi karibuni, kama mtataka kuyasikiliza haya mazungumzo utasikia nikilisisitizia
hilo, naombeni sana mniamini kwa hilo.
Hapa nazungumzo ukweli kutoka moyoni mwangu...'akasema.
‘Kwani kuwepo kwa huo mkataba wao, ulifahamu lini…?’ akaulizwa
Mimi huo mkataba wao wa familia, niliufahamu kutoka kwa maelezo y
abosi wangu maana alikuw ani rafiki yangu, hakunificha hilo, lakini sio kwa
undani wake, na wala hakuwahi kunionyesha …lakini huo mwingine uliokuja
kutengenezwa baadae, nilikuja kuelezewa tu , juu, kwa juu, hawakutaka uonekane.
Nilioweza kuuona, ni huo wa kuhamisha hisa..ili nione kuwa hata
mimi nipo, na huo niliuona baada ya kuchukuliwa na wao hado ifisini kwao, niliporudi
kwa dharura..’akasema
‘Ulirudi kwa dharura, au ulirudi kwa vile umehakikishiwa mafao…usitake
kudaganga watu hapa, hilo jambo la kibali ungeliweza kulimalizia huko huko…’akaambiwa
‘Ushahid upo, huko chuoni, na sehemu za vibali za kwenda kusoma
nje, nenda kafuatilie, hapa nina ushahidi wa barua niliyoandikiwa, kuwa kuna
tatizo la kibali changu natakiwa kurudi nchini kukamilisha baadhi ya taratibu, ‘kurudi
nchini’ ipo wazi inasomeka, mimi nisingelipoteza muda wangu wa masomo kwa hayo
mambo yao ya kitapeli..’akasema
‘Je wewe unahisi, hiyo kurejeshwa nchini ni mbinu au ni taratibu za kawaida za vibali…?’
akaulizwa sasa na mwenyekiti.
‘Mpaka sasa kwa uhakika sijalithibitisha hilo, kuwa labda kuna
watu wapo nyuma ya hilo tukio, ila kikao
kikitaka mimi naweza kuifanya hiyo kazi na nitaweza kuwatolea maelezo yenye
uhakika..’akasema
‘Haya endelea na maelezo yako..’akaambiwa na mwenyekiti, japokuwa
wakili mtetezi bado alikuwa na maswali anataka kuuliza.
*************.
‘Siku nilipofika uwanja wa
ndege nikiwa najiuliza kuna nini kimetokea kuhus kibali changu, kiukweli, moyoni
nilikuwa nimemuhisi mdhamini wangu, yaani rafiki yangu kuwa huenda kayafanya
hayo kwa makusudi, lakini nimjuavyo yeye, asingelifanya hivyo, angeliniambia
moja kwa moja..’akasema
‘Na mpaka nafika uwanja wa ndege bado nilikuwa najiuliza. Na
ujuavyo kazi zangu huwa zinanifanya niwe na akili ya ziada, nikawa najiuliza je
kama ni kuhusu tatizo la mtoto labda,…ili kumpata baba wa mtoto,basi mtoto
wangu anaweza kuwa hatarini.
Nilipojiwa na wazo hilo, kuna mtu nilikuja naye namfahamu na
anaifahamu familia yangu, nikaongea naye, ni wazo la haraka lilinijia na bila
kusubiria, nikalifanyia kazi..kwahiyo nikamelekeza huyo jamaa yangu , ni nini cha
kufanya, tukifika hapo Dar, hakuwa na kipingamizi, akasema atafanya hivyo huyo
jamaa yangu.
‘Kama nilivyohisi nilipofika tu, nikavamiwa uwanja wa ndege, walisubiria
wakati nimeshaingia kwenye taksii, kumbe hata huyo mtu wa taksi, alikuwa mtu
wao, wakasema mimi nipo chini ya ulinzi, nikawauliza kwa kosa gani, wakasema
nitaambiwa nikifika kituo cha polis, nikawaomba vitambulisho, wakanionyesha,
sikutia shaka
‘Walikuwa ni polisi kweli…?’ akulizwa
‘Mhh…vitambulisho vilikuwa vinaelezea hivyo, sikuwa na muda wa
kuhakiki zaidi, na kiukweli sikuwa na muda sana wa kupoteza,…’akasema
‘Sasa wakati tupo njiani, nikasikia wakipigiana simu,, wakaulizwa
kuwa mtoto ninaye, wakasema sina mtoto, wakaambiwa waniulize mimi
nikawadanganya kuwa sijarudi na mtoto, nimemuacha huko nilipotoka, huyo
aliyewapigia akawaambia mimi ni muongo, lakini baadae wakasema;
‘Mkuu kasema, atakuhitajia kuongea na wewe baadae sasa hivi uende
nyumbani kwako, na usiwe na wasiwasi,
nia ni kukuonyesha kuwa ujio wako una manufaa makubwa, ila usipoleta
ushirikiano, kusoma kwako ndio basi tena, hutasoma tena, na mtoto hutampata…’wakasema
na hapo nikawa na mashaka, mtoto sitampata tena, ina maana labda walishamteka
mtoto wangu..nikasubiria mpaka waliponiachia, ndio nikampigia simu jamaa yangu
‘Mtoto keshafika hapo kwako…?’ nikamuuliza
‘Ndio, mbona…?’ akataka kuniuliza maswali mengi, nikamkatiza kwa
kusema
‘Usijali, gharama zote nitakutumia, hakikisha huyo mtoto anabakia
hivyo hivyo, ukimaliza kumuogesha, unamvalisha hivyo hivyo…na usimtoe nje, kuna
wabaya wanataka kumchukua mtoto wangu…’nikawaambia na kwa vile huyo ndugu yangu
ni jamaa yangu anafahamu mambo yangu
kidogo, akanielewa.
‘Kwahiyo hadi hapo nikafahamu kuwa mtoto wangu yupo salama, na
maelezo mengine kama nilivyotoa kwa rafiki yangu, aliponiuliza kuhusu mtoto
wangu, mengi yalikuwa ni namna tu ya kuhakikisha mtoto wangu yupo salama, na
kipindi hicho sikuwa nafahamu ni nani wa kumuamini,…nilijitahidi hakuna
anayefahamu wapi mtoto wangu yupo, hadi pale niliporudi chuoni…’akasema
‘Hata hivyo, wao hawakujali hilo la mimi kutokuwa na mtoto, hawakulijali
sana, walifuatilia wakajua kuwa moto nilikuja naye, sasa kaenda wapi, hapo hawakuweza kupata jibu, wakaona
wasipoteze muda na hilo, walichotaka ni mimi kukubali huo mpango wao,
‘Kwanza alitumwa mtu, akiwa na hiyo mikataba nikatakiwa nisome na
nielewe, baadae nikapigiwa simu isiyo na namba ya mpigaji, akaniulize kama
nimesoma na kama nimesema nasemaje, nikawaambia, mimi siwezi kuongea mambo hayo
kwenye simu, na ndio maana baadae nilikuja kuchukuliwa na hao watu hadi ofisi
moja, huko uwanja wa ndege, kwa wakili marehemu’akasema
‘Hapo ...nikaonyeshwa tena huo mkataba maalumu, nikaambiwa kuwa,
kila kitu kipo kisheria, kilichobakia ni sahihi yangu tu, na nikikubaliana nao,
basi nitapata mafanikio mengi, na haki za mtoto wangu, ila nikikataa, mtoto
atachukuliwa na mimi nitakipata cha moto, kiukweli sikujali hayo, lakini mtu
akinigusia mtoto wangu nahisi kuchanganyikiwa.
‘Hapo nikapima vipi nifanye hilo, kwanza kwa ajili ya usalama wa mtoto wangu,
nikaona bora nikubaliane nao tu, halafu mengine yatakuja kufauta baadae,..naona
hayo na mengine yaliyofuata baadae nitayaelezea kwenye sehemu ya pili, maana
ndani yake kuna mambo ya kisheria, na usalama , kama ni lazima itabidi nitete
na mwenyekiti kwanza..’akasema na kutulia kidogo
‘Swali…’ilikuwa sauti ya wakili mtetezi, na hakusubiria kupewa
kibali akauliza
‘Wewe umesema uliwahi kusikia mambo kuhusu mkataba wa familia
kupitia kwa rafiki yako, na ina maana kuwa wewe ulikuwa unafahamu vipengele
vyake, na ulifahamu kuwa ukifanya lolot baya, inakuwa ni tatizo kwa mume wa
familia, huoni hapo unatudanganya,..kuwa wewe ulijua hatari yake na bado
ukatumia mbinu ili umpate mume wa familia, ukijua masilahi yake…?’ akauliza
wakili
‘Kwanza futa maneno yako,..vipengele vipi nilikuwa navifahamu,
maana unavyouliza ni kama unafahamu ufahamu wangu wa vipengele ninavyovifahamu
kwenye huo mkataba,…lakini pili futa kauli yako kuwa, mimi ndiye nilitumia
mbinu kumpata mume wa familia, sio kweli, ngoja nije kuelezea ukweli hasa kwa jinsi
gani ilitokea…..’akasema
‘Elezea sasa..mimi siwezi kufuta kauli yangu, wewe ndiye wa
kuifuta hiyo kauli kama unaona sio sahihi,..kwa maelezo yako, yenye ushahidi
sio unatutungia hadithi hapa…’akasema wakili kukawa na malumbano kidogo na
mwenyekiti akaingilia kati na kusema
‘Endelea na maelezo yako, mzungumzaji…’akasema mwenyekiti
NB: Bado kuna muendelezo wa maelezo haya kabla ya sehemu hii ya kwanza, najaribu kupitia pitia, maelezo yake n marefu sana, huenda mengine ni kupoteza muda, kwahiyo ili siku isiende bure, tusome hayo maelezo ..ni muhimu sana, kwani ndio hitimisho ya mambo mengi yaliyotokea kwenye hiki kisa..
WAZO LA LEO: Tusiongee uwongo ili kuhalalisha ubaya
wetu, tusisingizie uwongo ili tuonekana sisi ni wema, tusitafute kashfa mbaya
kwa wengine ili sisi tuonekane wema, kwa ajili ya masilahi tu ya kidunia.
Uwongo, kashfa na fitina kwa wengine kwa ajili ya masilahi kidogo ya hapa
duniani, kama kupata cheo, mali, nk.., ni mzigo mkubwa wa madhambi tunayoyabeba mbele ya mola wetu.
Tukumbuke kuwa hayo yote tutakuja kuulizwa siku hiyo ya hukumu.
Jiulize swali, je unataka kuyafanya hayo kwa manufaa ya nani, na je una uhakika
gani kuwa utapata muda wa kutubia hayo madhambi, na je huyo uliyemtendea kaumia kiasi
gani, na je maumivu yake utaweza kuyafidia vipi kwa huyo uliyemtendea...
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment