‘Ahsante mungu…mume wangu ndio wewe, ooh,.., mume wangu sasa
umepona, nashukuru sana…’nilisema hivyo, na mume wangu, hakuchelewa kunijibu
akasema;
‘Yah, nimepona, lakini sasa naogopa hata huko kupona, ...’akasema
‘Kwanini unasema hivyo mume wangu. Usikufuru jamani…?’ nikauliza
nikimuangalia kwa mashaka..
Taratibu akajigeuza na kuniangalia…lakini kwa namna ya aibu …
Tuendelee na kisa chetu…
**************
‘Nina maana yangu kubwa sana kusema hivyo mke wangu…’akasema, na
mimi nikabakia kimia nikimuangalia tu, mume wangu alikuwa kadhoofu sana, uso
umekunjamana, sio mwili wako, maana alishanenepeana sana.
‘Mhh.., ni kweli, nimeponea tundu la sindano, ni wajibu wangu
kumshukuru sana mungu…’akatulia kama anawaza jambo.
‘Ni kweli nimeteseka sana, sio mchezo, hadi kufikia hapa ni kudra
za mungu,…nilijua sitaweza kutembea tena, nilijua mimi ndio basi tena,..bado,
kuna vitu havijawa sawa, siju…ila nimepona…’akatulia kidogo.
‘Kiukweli najua nimekutesa sana mke wangu, nimewatesa sana watu
wengi, nawashukuruni sana, na hasa wewe na docta rafiki yangu, siwataji madocta
wanaoniuguza maana ninaweza kusema ni kazii yao..’akahema kwa kiraafu, halafu
akasema;
‘Lakini kwa madhaifu yetu sisi wanadamu..tunawazia ya mbeleni,
maisha na tamaa zetu za kila siku, ..hapa nilipo, nawazia itakuwaje, ndio maana
naishia kusema, najua nakufuru lakini nitasemaje sasa, ndio hivyo…, kupona
kwangu ni kubaya zaidi, naona ni heri ningeendelee kuumwa tu...’akasema
‘Mume wangu sasa unanichosha….’nikasema
‘Najua …najua sana mke kuwa nakuchosha, lakini haya nitayasema kwa
nani…nisamahe tu mke wangu.., nisamehe, nisamehe, nisa-mehe....hata hivyo
najiuliza ni kwanini niufiche ukweli, wa kutoka moyoni mwangu, hata docta
kasema nisipende kuficha ficha mambo moyoni mwangu, nikawa na duku duku,
nikateseka ndani kwa ndani, sasa nimeamua nijitoe, niwe muwazi..’akatulia
‘Haya fanya utakavyo, ila sipendi kuja kulaumiwa…’nikasema na yeye
huku anaongea kama vile hanijali.
‘Kwahiyo, ni bora niwe natoa dukuduku langu…ili mlisikie, kuliko
nikae nalo moyoni, ni bora niwe na sema ukweli kwenu hata kama hamtaupenda,
lakini uwe ni kwa manufaa yetu sote, sipendi kugabua,...., ndio maana naanza
kuusema ukweli huu leo kwako, ila unielewe, kama kweli wewe ni mke wangu…, japo
unaumia…’akasema
‘Sitaki kukaa kimia alafu uje kusikia kwa wengine kunihusu mimi,
au nije kusemwa na watu kuwa nipo hivyo siwezi kuendesha familia yangu,
mimi…namtegemea mwanamke…nina machungu mengi moyoni, ..ni lazima
niyaseme…nitayasema, nitachukiwa, lakini nitayasema…’akashika kichwa
‘Mume wangu, najua akili yako bado haijawa sana, hujapona bado..na
mimi ..sitaweza kufanya yale ninayojua yatakuumiza, nafahamu sana
hilo,…ninachokuomba mume wangu usijiwekee vikwaza visivyo na msingi, usijitwike mzigo kabla haujatua kichwani
mwako, tafadhali nakuomba…’nikasema
‘Ahahahaha mke wangu huyo,..oh, oh, oh… unajua hivi sasa, kwa vile
naumwa, kwa vile…eeh…utajifanya hunielewi, lakini kwa sirini, ndani ya moyo
wako unafahamu nina maana gani, na ushajipanga kwa hilo, najua..haina haja ya
usbishi kwa hilo…’akasema
‘Haya niambie ni kwanini
kupona kwako kuwe kubaya.. maana sasa inabidi nifanye utakavyo wewe, ninaweza
kukuuliza maswali ya kakuwaza, ukadondoka hapa, ni nani atalaumiwa kama sio
mimi,..hata hivyo, wewe ni mume wangu lazima nikujali, ina maana hayo
ninayofanya nafanya vibaya..?’ nikauliza na hapo hapo nikahis nimefanya kosa,
nikageuka kuangalia kule mlangoni.
‘Usiogope mke wangu, nipo sawa, sitadondoa, na nikidondoka si nipo
hospitalini, una wasiwasi gani…mke wangu nimejipima kabla hujaingia humu ndani,
mimi sasa…nipo sawa kabisa, nimejiandaa kwa lolote lile, leo najisikia nina
nguvu,…na najua nkianza kusema ukweli utakasirika, utakuja juu, lakini kwanini
nifiche eeh…’akajiinua kidogo, kama anataka kukaa, halafu akalala vile vile.
‘Mume wangu, kwanini unakuwa mbishi, sisi tunahangaika kwasababu
ya afya yako, afya yako ni muhimu kuliko hayo unayoyafikiria wewe…, au hutuonei
hata sisi huruma, wewe hujui ni kiasi gani tunaumia tukikuona kwenye hiyo hali,
wewe unajifikiria wewe mwenyewe tu..’nikasema.
‘Ni kweli mke wangu, unasema kweli kabisa, wala hujakosea,...nashukuru
sana kwa kunijali, na eeh, na…eeh, siku
nilipokuomba msamaha na ukasema umenisamehe, nilijua nimemaliza kazi, …kuwa
sasa nipo salama, …lakini nikaja kukumbuka jambo,nilisahau kabisa…mmh, mungu
mkubwa...’hapo akatulia kidogo.
‘Ulikumbuka….! Ulikumbuka nini, mungu wangu sasa unanifanya nianze
kukuuliza maswali, hata docta akija hapa atanikaripia mimi…’nikasema
‘Usijali, wewe uliza tu…ni hivi, nashukuru ulisamehe au sio,
sizani msamaha wako ulikuwa wa kugeresha, mimi nakufahamu sana…lakini kuna kitu
tulisahaua, labda mimi, maana ndiye muathirika ….nlipokumbuka hilo, nikajua,
msamaha wako hauna maana, hata ukitamka mara kumi,..hata ukisema umenisamahe…,
ha-i-ta-sa-i-d-i-a kitu, huo ndio ukweli,…’akasema
‘Kwahiyo unataka kusema nini, au wewe ulitakaje, ulitaka …nikatae kimia…au,
maana unataka na mimi nianze kukueleleza, nifanya jambo, ili nionekana mimi
mbaya, ili hayo uliyopanga yaonekane ni kweli kuwa mimi sikujali au
sio…nakuomba tena, tafadhali, jail afya yako kwanza, umenisikia..’nikasema
‘Siliza bwana…ni hivi, nimesema nin vile, eeeh, kuwa msamaha wako
hautasaidia kitu, kwani kuna jambo zito ambalo haliwezi kutatuliwa kwa msamaha
wako wa maneno, hata kama unatokea moyoni, na kwanini utokee moyoni wakati
unajua ni nini unachokifanya, ulijua haya yanaweza kutokea, na hapa ndio
namuona baba yako kuwa ni mtu mwerevu sana …ni wazee wanaoona mbali, wazee sio
mchezo…’akasema
‘Ok, haya niambie ni jambo gani hilo zito mume wangu, ambalo
halijali msamaha wangu..?’ nikauliza
‘M-ka-ta-ba …’akayatamka hayo maneno kwa uzito..na kuniangalia
machoni, na mimi nilikuwa namuangalia lakini sio machoni,
‘Naona hata hushtuki, hushtuki, kwa maana kuwa wewe unalifahamu
hilo, …ndio maana ukaniaga kwenda kazini, hahaha mke wangu bwana,…lakini ni
wajibu wako kufanya hivyo au sio, kufuatilia kuwa kila kitu kinakwenda sawa
sawa....’akasema
‘Mkataba gani huo, na wa nini mume wangu,…’nikasema
‘Mkataba…mkataba ule uliobuni wewe mwenyewe, siongelei kitu kigeni
hapa, na unafahamu fika nazungumzia kuhusu mkataba gani…wewe ulijua kama
alivyojua baba yako, kuwa kwangu, …ni kunguru hafugiki, au sio, lakini sio
kweli haya yangeliweza kutokea kwa yoyote yule....’akasema.
‘Mume wangu sasa unanilazimisha nifanye unavyotaka wewe, nikuulize
wewe una wasiwasi gani na hilo, unaogopa nini, kwenye huo mkataba, eeh, maana
huo mkataba siku nyingi hautumiki…na mimi ndiye muhusika mkuu pamoja na wewe,
kauli ykao na yangu inaweza ikabadili …na nikuulize umafanya kitu gani kibaya,
eeh, umenilazimisha mwenyewe nikuulize hayo, sio ndio hivyo,…?’ sasa nikawa
siogopi tena kumuuliza
‘Sawa kabisa, nataka hivyo, uniiulize, na mimi nitakujibu, nipo
tayari kwa hilo, sitaki uwe unazunguka zunguka, mara mdogo, mara kwa docta,
niulize mimi mwenyewe…’akajiiunua na kukaa vyema.
‘Una lako jambo, sio bure…’nikasema
‘Mke wangu, kiukweli, nikuambie kutoka moyoni mwangu, mimi nina
wasiwasi sana, wasiwasi ambao sijawahi kuupata awali, na nikiendelea hivi,
nitawehuka, ndio maana sasa ni lazima niamue, la sivyo, …natumai utanielewa…’akasema
‘Sasa hayo ni yako, na kama nia yako ni kunitesa mimi, itafikia
sehemu nitashindwa, ngoja nimuite docta, ili asikie unachokitaka wewe, ili
likitokea la kutokea nisije kulaumiwa mimi…’nikasema
‘Utashindwa! Unasema nini, kuwa utashindwa, …hapana mke wangu,…usifikie
huko, ni lazima tuwe pamoja, kama utanielewa, na docta nimeshaongea naye,
kasema naweza kuendelea tu, usijali…’akatulia na mimi nikatulia, na yeye ndio
akaanza kuongea;
‘Unajua mke wangu, ni lazima ulijiuliza sana ni kwanini nikafikia mimi
mume wako unaniyenifahamu, kuja kukuomba msamaha…kweli si kweli…usinijibu’akahema
tena, nikawa namuangalia kwa mashaka, nilitamani docta aingie akatize haya
mazungumzo, lakini moyoni pia nataka aongee auseme ukweli nijue moja tu.
‘Nafahamu sana wewe mke wangu, umehangaika sana kuutafuta ukweli,
ukazunguka huku na kule, ..lakini, hata ingelikuwa ni mimi, au sio…lakini
nakupongeza sana mke wangu, kwa kitu kimoja, wewe huna haraka ya kumshuku
mtu…’akasema
‘Ndio maana baada ya kusubiria sana, baada ya matukio mengi, nahis
na baada ya kuambiwa na watu wengi , kunihusu mimi, ..hapa naongelea yangu,
eeh, wewe hukuchukulia pupa, unajua ni kwanini, kwasababu una kitu cha
kukulinda, nacho si kingine, bali ni mkataba…’akasema .
‘Lakini mke wangu…mengine, eeh, hayavumiliki au sio, hata
ukikubali, hata ukinisamehe, hata hapa yapo au sio, lakini tulisahau jambo
moja, kuwa kuna udhaifu wa kibinadamu, au sio, mimi yaliyotendeka sio kwa
makusudi yangu…’akatulia, na mimi nikakaa kimia
‘Unajua nafahamu baada ya leo, huenda ukanichukia sana, …lakini ni
lazima nifanye hivyo, kwa vile mimi nakupenda, mimi naipenda familia yangu,
nawapenda watoto wangu wote bila kubagua, sijali umasikini au utajiri…’akasema
nakutilia mpaka nikaingilia kati na kusema;
‘Unajua mume wangu mpaka sasa sijakuelewa, ni nini unachokitaka
maana sikuelewi, ni nini shida yako, una tatizo gani, haya niambie hayo nijue
mapema…’nikasema
‘Najua kwanini unaniuliza hayo, najua lengo lako ni nini, wewe hutaki
kuharibu, kuvunja mkataba au sio..mkataba unasema mtu akiumwa, mwenzake
amuhudumia blab bla aa, eeh…..na mmoja akiumwa, mwingine eeh, asifanye kadha wa
kadhaa, kama kuna tatizo, mpaka mwingine apone, kwa kufanya hivyo eeeh, utakuwa
umevunja mkataba..au sio..sijui kama nimepatia…’akasema
‘Mume wangu mimi sifanyi hayo kwa sababu ya mkataba, mimi ni mke
wako natakiwa kuwajibika, kama ungeliwajibika wewe kwangu kam ningelikuwa
naumwa kama unavyoumwa wewe..na uwepo mkataba au usiwepo, hiyo ni haki ya
wanandoa…’nikasema
`Ok,..ok,…labda nisipoteze muda, maana najua muda umefika, saa
ngapi vile, mmh, naona kuna kuchelewa hapa, lakini itafanikiwatu..hili zoezi
eeh, ni lazima lifanyike tu,..mke wangu, kabla sijasahau, naomba ile nakala ya
mkataba....’akasema na mimi nikajikuta nikishikwa na kigugumizi nikasema;
‘Mume wangu achana na mambo hayo ya mkataba, huu sio muda wa mambo ya mkataba, hapa
tupo hopsitalini,..nataka wewe upone kwanza, kama huo mkataba ndio unakuumiza
na kufannya hayo yote basi, tuachane nao kabisa, kwangu mimi afya yako ni zaidi
ya huo mkataba...’nikasema.
‘Mke wangu naomba ule mkataba ile ni nakala yangu.....’akasisitiza
‘Una uhakika kuwa hiyo ni nakala yako, sema ukweli mume wangu…’nikasema
sasa kwa sauti ya kutokujali.
‘Nimesema naomba ule mkataba…’akasema sasa akinikazia macho, nikaona
isije ikawa taabu yakazuka mengine, nikafungua mkoba wangu na kumkabidhi huo
mkataba, na yeye akaupokea na kuuweka kifuani, akageuka na kulala kama ilivyo
kuwa awali, huku ule mkataba upo kifuani mwake.
‘Kwahiyo unaendeleaje…’nikasema, nilisogea na kukaa karibu naye na
akashtuka nahsi alijua nataka kuuchukua huo mkataba, akaushika na kuuweka
pembeni upende wa pili ambao siwezi kuuchukua kwa kirahisi, na , akawa kimia
akiwa kaangalia juu, kama vile hataki kuniangalia tena machoni, sikumuelewa, na
mimi sikuwa na haraka naye, hapo nilitaka nifanya atakavyo halafu nitoke humu
hospitalini.
Hali ya ukimia ilitanda kwa muda, kimia kingi kina mshindo moyoni,
lakini sikutaka kumghasi, labda alikuwa akiwaza jambo, na ..baadae akauvunja
ukimia, kawa kusema;
‘Mke wangu unisamehe sana kwa hayo yaliyopita na huenda na-yajayo,
nafahamu na kukwaza sana, wewe moyoni utahisi sikujali,...lakini mengine
nayafanya kwa nia njema tu...wewe hujui tu, …lakini siwezi kukufanya wewe unielewe
kwa haraka hivyo, najua hilo…’akasema na mimi nikaa kimia
‘Mke wangu kwa vyovyote itakavyokuwa ujue nakupenda sana, kama
itafikia sehemu ya kulazimishana jambo, tukawa hatuelewani, na huenda haya
yakifika kwa baba yanaweza kuleta maana nyingine na huenda ikafikia, …mimi na
wewe kulazimishwa tuachane..najua hilo,, hasa kutokana na huu mikataba, lakini sitakubali kwa hilo…’akasema.
‘Mume wangu kiukweli sikuelewi, hivi unataka nini, niambie ukweli
wako, ni kitu gani unakitaka kutoka kwangu ..ni mali au….niambie ukweli…ili
usipate taabu sana, niambie hapa hapa, mimi nitakupatia hicho unachokitaka, ili
tu uwe na amani, ni nini inachohangaika nacho, niambie?’ nikauliza sasa sijali,
na yeye akabakia kimia tu.
‘Utaelewa tu….’akasema hivyo
‘Kiukweli mimi nimechoka…’nikasema.
‘Mke wangu mimi sio mtoto mdogo, ...nilijua tu, siku nilipokubali
haya maswala ya mkataba ndipo nilipokubali kuwa mtumwa, na mfungwa wa maisha
yangu mwenyewe, mkataba huu ulilenga wengine, lakini hauku lenga usawa, utakuja
kulifahamu hilo baadae..’akasema
‘Mkataba , mkataba mkataba..mume wangu ni hicho, lete niuchane
mbele yako, si ndio unakufanya uwe hivyo, mkataba unaweza kubatilishwa, lakini
maisha yetu je, watoto wetu je,..hivi unafikiri dunia hii ni yetu tu mume
wangu, ..’nikasema
‘Hapo hapo…eeh, natumai sasa tunaanza kuelewana….’akasema sasa
akikaa vizuri
‘Kama ulifahamu hilo, ni kwanini ukaleta haya maswala ya mkataba,
mimi nilikubali tu, kwa vile nakupenda, na nilijua haya yatakuwa kwa masilahi
yetu yote, sikujuwa kuwa kuna kuteleza...sawa yametokea yaliyotokea, eeh, si
hivyo,...sasa nifanye nini....nikae kimiya, na hata wasiohusika wapate taabu
kwa makosa yangu.....hapana..’akatulia kidogo
‘Mke wangu, nilifikia sehemu nikaona bora nife tu, mitihani
ilikuwa mingi kichwani mwangu..lakini nikakumbuka kuwa mimi ni mume wa familia,
nina watoto, ..nina dhima mbele ya mungu, hapo nika…eeh, nikamuomba mungu anisaidie
nipone ili nibebe majukumu yangu mwenyewe...’akasema.
Ikapita muda, nikaona kama anahangaika, nikaangalia mlangoni,
nikitaka docta atokee, na baadae nikasema;
‘Unajua mume wangu nimeliwazia hili sana, nakuona haupo vizuri,
akili yako haijatulia, bado unaumwa, kwa ajili ya afya yako,. Itabidi ukalazwe
sehemu ukae mpaka upone, maana kukutana mimi na wewe inakuwa ni taabu, unakuwa
huna amani, sijui kwanini na....unanipa shida sana ya kukuhudumia....’nikasema.
‘Hilo halitawezekana kabisa…, nitakaa na wewe hadi hatua ya
mwisho, kwanza nimeshapona, unaona ...’akasema na kujiinua , akateremka
kitandani,…akasimama na kuruka ruka, kiukweli hata mimi sikuamini hilo, mtu
alikuwa hawezi kujiinua leo hii yupo hivyo, kweli mungu mkubwa….hapo nikasema;
‘Nashukuru sana kukuona umepona, lakini bado,...docta kasema hatua
uliyofikia ni hatari zaidi kama hutafuata masharti, ukipata mshtuko kidogo tu,
uka…inaweza ikawa mbaya zaidi....’nikasema
‘Masharti gani, masharti ya kutesana, hahaha eti masharti, …sawa. ni
sawa , lakini wanajua kilichopo moyoni mwangu, kilichopo moyoni mwangu kama
kisipowekwa sawa, haitasaidia kitu, na hiyo, ya mshtuko, ni kutokana na hilo…sasa
kwa vile nimeweza kuuinua huu mwili, basi, ni lazima nipambane…’akasema
‘Na nani..upambane na nani
mume wangu?’ nikamuuliza hapo akanitizama, na mimi nikamtizama, tukatizamana,
yeye akawa wa kwanza kuangalia pembeni.
‘Ni hivi mke wangu, mimi si ndio mume wako au sio, kichwa cha
familia, haijalishi hali , haijalishi kuwa wewe ndiye mwenye uwezo wa kifedha,
hiyo ni kweli au sio..hata kama baba mkwe ndiye anatufadhili hiyo haina maana
kwenye ndoa yetu au sio…lakini vyovyote iwavyo, mimi ni lazima niwajibike kama
mume, siwezi kujipweteka, unaona eeh,..dunia itanicheka…’akatulia
Na mimi nikabakia kimia tu…
‘Sasa ni hivi, namshukuru mungu kuwa nimepona, ...siwezi kuendelea
kukutesa tena mke wangu, ....ninachotaka ni ijulikane moja,...nataka nikitoka
hapa tukae, tujue moja, nafahamu wewe utasimamia kwenye mkataba…sijui…lakini
hata ikiwa hivyo, sio mbaya, mimi nipo tayari kwa lolote lile, japokuwa
nafahamu ni nini kitatokea,ila kuna masilahi ya watu wengine ni lazima
niyapiganie kwa nguvu zangu zote..’akasema.
‘Hao watu wengine unaowataja sana , ni akina nani,na kiukweli mimi
sio mtoto mdogo…hata hivyo mume wangu waonaje haya tuje kuyaongelea nyumbani,
au,,,>; nikauliza, nikijaribu kujishusha japokuwa moyoni haikuw ahivyo.
‘Kupona kwangu mimi ni pamoja na kufahamu hatima yangu,...nilipokumbuka
kuhusu huu mkataba, nikajau kuwa kupona kwangu ni hatua tu, nina kazi kubwa
mbele yangu
‘Nikuambie ukweli mke wangu nimekuja kugundua kuwa kumbe huo
mkataba ulikuwa ni mtego kwangu, ...sasa siwezi kulala hapa, kwa vile naumwa,….aah,
nimejipima, ..nikatembea…nikaruka, nikaona sasa nipo safi, bado kuna udhaifu
fulani, lakini sio hoja, sasa ni lazima nipiganie haki zangu, na za hao wengine....’akasema
na mimi nikabaki kushangaa.
‘Kama uonavyo ni sawa, haya, maana mimi sijui unataka kupigana na
nani, na hizi haki za nani, kutoka kwa nani,…mimi sikuelewi kabisa, lakini
upendavyo, siwezi kusema zaidi....’nikasema.
‘Sawa kabisa hapo umenielewa na kunisikia....kwa vile huu mkataba
ulikuwa mtego kwangu, utakuwa wa kwanza kuufanyia kazi…’akasema
‘Sawa uonavyo,…’nikasema
‘Kifupi mke wangu ni hivi, kwa vile mimi ni mume wako, natakiwa
kuanzia sasa nianze kusimamia mambo yetu kama kichwa cha familia, kwahiyo kama
kulikuwa na jambo jingine ambalo
linanifanya niwe mume bwege, kuanzia sasa nitaliondoa kwa mikono yangu
mwenyewe…’akasema
‘Unasema nini, mume bwege, hiyo kauli imetoka wapi…?’ nikauliza
kwa mshangao
‘Usijali, utakuja kunielewa ni na maana gani, kwanza tutaanza na
huu mikataba , tuangalia vipengele vyote vya mitego mitego…ikibidi tuuharibu
tuanzishe mwingine kwa masilahi ya familia yetu sote, sio kwa masilahi ya
familia yangu ndani ya familia nyingine..’akasema
‘Mhh..’nikaguna tu
‘Utakuja kunielewa tu, akija muhusika …’akasema
‘Muhusika gani. Ni nani anakuja huku hospiali…?’ nikauliza kwa
mshangao
‘Ndio… atakuja muhusika na
tutaweza kuyaongea yote vizuri tu, mambo yote, ya familia, yaliyotokea na
hatima yake, lakini muhimu ni mambo yetu, sitaki tena kuishi kwa mashaka,
nimeamua, na wewe utanisaidia ukishirikiana na huyo naye....’akasema.
‘Mume wangu, ni nani huyo..?’ nikauliza
‘Unajua mke wangu huu mmkataba una madhaifu mengi, ndio tutakaa
pamoja watu watatu, baada ya kuhakikisha ule mkataba wa awali umefutwa,
tuandika kitu kincahogusa watu wote, sisi , watoto na mali zetu,, uwe mkataba
unajali familia yetu, na mambo yetu , na sio kwa kuegemea familia
nyingine..’akasema
‘Kuegemea familia gani…?’ nikauliza
‘Hivi nikuulize mke wangu, mimi si ndio nimekuoa, kama mimi ndiye nimekuoa
kwanini tuendelee kutegemea familia ya kwako,…hapo natoa mfano tu…’akasema
‘Tunategemea ndio kwasababu ndio wafadhili wetu, kama isingelikuwa
hivyo, hiyo kampuni ungeliweza kuianzisha, haya maisha tunayoishi sasa
yangelikuwa hivyo, hebu jiulize hilo wewe mwenyewe hilo hatuwezi kulikwepa
bwana unajidanganya tu, madeni kibao, ndio unataka hivyo…’nikasema
‘Ni sawa, lakini kuanzia sasa tuanweza kuishi wenyewe au sio, kama
kuna mapungufu, eeh hayo madeni nk… tutayakabili wenyewe, ndivyo nimejipanga
hivyo, tutapambana wenyewe kufa na kupona, bila kutegemea familia
nyingine…’akasema
‘Hbu kwanza nikuulize maana umeyataka mwenyewe, kuna muda ulisema hata ukiwa na mtoto nje,
ulikuwa na maana gani, ya kuwa unaye
mtoto nje au, niambie ukweli…?’ nikauliza,sikutaka kuongea naye kihasira,
nikiwa na maana yangu tu.
‘Hayo sasa tutakuja
kuyaongea mbele akija muhusika, huyo atayaweka
kila kitu sawa….nataka kila kitu sasa kiwe kwa namna ambayo, hakuna mtu
ataumia,..sio mimi wala wewe au yoyote ..nataka nitende haki, kama mume wa
familia na tutakuja kuyaongea tukiwa watatu tu…’akasema
‘Hujanijibu swali langu, nataka kufahamu maana haya umeyataka wewe
mwenyewe, je kweli una mtoto nje…na ni nani huyo…?’ nikauliza na kabla
hajanijibu,
‘Mtoto sio, ngoja nikuambie….’akatulia maana mlango uligongwa na
kufunguliwa
Mimi pale akili yangu
ilishaanza kubadilika, mume hajaweza kunijibu, inaonekana kuna kitu kama hicho,
inawezekana mume wangu ana mtoto nje ya ndoa, je ni nani, je ni kweli
wanayozungumza watu, kama ni kweli, itakuwaje…nikawa nawaza mambo mengi kwa
muda mfupi, lakini mawazo yangu hayo yalikatizwa na hao walioingia pale mlangoni
Kwanza aliingia docta anayemuuguza mume wangu, akafuatia nesi
wake, halafu docta rafiki wa mume wagu…usioni hakuonekana na furaha, nikahisi
kuna jambo, .., lakini zaidi ya hao, kuna mmoja ambaye alinifanya moyo wake
udunde, nijawe na hasira, ni kama vile kuwepo kwake huyu ndio kumetibua ile
hasira niliyokuwa nayo, nikajikuta nikhema kwa shida, na uso ukabadilika kwa
ghadhabu.....
NB: Naishia hapa kwa leo, nikiwatakia maulidi mema....
WAZO LA LEO: Tabia njema ndicho kiigizo chema katika jamii,
tujipambe kwa tabia njema hata wale wanaokuiga wakuongezee fadhila zako katika
maisha yako hapa duniani na kesho ahera.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment