Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, November 29, 2017

MKUKI KWA NGURUWE-32


Nilipohakikisha kuwa kweli ule mkataba haupo kwenye sehemu yake, nikamuita mmoja wa wafanyazi wangu wanaofanya usafi na kujaribu kumdadisi kama aliwahi kumuona mtu mwingine akiingia ofisini kwangu wakati nipo mapumzikoni.

‘Hakuna bosi aliyewahi kuingia bila ya ridhaa yangu…’akasema

‘Lakini kuna mtu aliwahi kuingia, ukiwemo

‘Hakuna bosi…mtu akija namuekeleza kwa msaidizi wako…’akasema,  

 ‘Kwani kuna kitu kimepotea bosi?’ akauliza kwa mashaka.

‘Bado sijahakikisha, kama kuna kitu kimepotea, ila kama kipo nitakuambia, na uwe na uhakika ..jaribu kukumbuka vyema kama kuna mtu ulimuona akiingia humo, au alikuomba ufunguo, ...ndicho ninachotaka kusikia kutoka kwako, nakuamini sana...? ‘nikauliza

‘Hakuna kabisa mtu aliyeingia humo,,...hilo nina uhakika nalo...’akasema na kwa vile mimi namwamini sana huyu mfanyakazi wangu sikutaka kumshinikiza zaidi.

‘Hamna shida,....’nikasema

Niliona hakuna haja ya kuendelea kuuliza uliza watu wengine, na sikuwa na hamu tena ya kuendelea kufanya kazi kwa siku hiyo, haraka nikaondoka zangu kurudi nyumbani maana bado nilikuwa likizo.

 Wakati nikiwa ndani ya gari, nilijaribu kuwaza, nifanye nini,...na sikutaka mambo haya ya ndani ya familia yangu yatoke, nje, na mtu pekee angeweza kunisaidia kwa hili ni rafiki yangu, ambaye hayupo.

‘Lakini nasikia anarudi…’nikajikuta nikisema hivyo

‘Hata hivyo maswala ya mkataba wangu na mume wangu hastahiki kuhusika kabisazaidi ya wakili wangu..’nikasema.

Hata hivyo sikuwa na shaka sana, maana ipo nakala nyingine nyumbani , nikifika nitaisoma, ila kiukweli kupotea na nakala hiyo kulipa ni shida sana, ni nani kaichukua na kwa nini. Akili yangu ilivyo, sikuwa na dalili yoyote ya kumshuku mtu yoyote, na kila niliyemuwazia, nilijikuta nikimuondoa kwenye ushukiwa.

Nafasi kubwa ilikuwa kwa mume wangu, lakini alikuwa mgonjwa,...na kabla hajaumwa, nakumbuka ipo siku niliwahi kuuchukua huo mkataba na kuusoma, na kuurejesha nilikuwa natafuta mkataba wa kampuni ya mume wangu, nilikuwa na nakala , na siku mbili baadae ndio akapatwa na hiyo ajali.

‘Haiwezekani akawa ni mume wangu,, yeye ana nakala yake,

Nilijaribu kumuwazia mtu mwingine, lakini sikuweza kumpata, kwani sikuona umuhimu wake na huo mkataba wetu.

‘Sasa atakuwa ni nani?’ nikajiuliza bila kupata jibu.

Nilifika nyumbani, nikaliendesha gari langu mbele kidogo, kuna duka langu la vipodozi, na vifaa vingine vya namna hiyo,, nikamwambia mlinzi wa pale, aniangalizie hilo gari, nitalipitia baadae, nikarudi nyumbani  kwa miguu, ni hatua chache, kwani ukuta wa sehemu hizo za duka zimeshikana na ukuta wa nyumbani kwangu.

Kwa haraka nikaingia ndani, na moja kwa moja nikakimbilia chumbani kwangu, nikafungua mlango taratibu maana sikutaka kumsumbua mume wangu kwani akiwa amelala haitakiwi kusumbuliwa.

‘Kwa vile kalala nitafungua kabati na kuchukua huo mkataba, nikasome huko mbele kwa mbele..’nikasema na huku nikihakikisha kama kweli mume wangu kalala. Alikuwa kalala, dawa zilikuwa bado zinafanya kazi,...nikageuka na kuelekea chumba chetu cha maktaba,  humo ndipo kwenye kabati, sehemu hiyo ni kama ofisi yetu ndogo.

Nikajifungua, kuhakikisha kuwa hakuna mtu atakayekuja kunisumbua, haraka nikaliendea kabati tunapoweka nyaraka za kifamilia, huwa kila mmoja ana ufungua wa hilo kabati, lakini mimi nilikuwa na sehemu yangu nyingine, ambayo mume wangu hana ufunguo nalo, ninaweka vitu vyangu vya kike, lakini nilitengeneza sehemu ya kuhifadhia kumbukumbu zangu binafsi ambavyo .

Nikafungua ile kabati, ...niliona kila kitu kipo kama nilivyokuwa nimeacha, hapo huwa napatumia mara kwa mara, nikihitajia vitu vyangu , nikasogeza vitu vingine na kuinua sehemu ambapo niliweka huo mkataba, ..sikuamini macho yangu

Kweupe...hakuna kitu...nikashikwa na butwaa, haiwezekani , haiwezekani, sasa hili ni tatizo, ...

‘Kwa hali ilivyo, sasa naanza kumuhisi mume wangu, hakuna mwingine anayeweza kuhangaika na huu mkataba,..huyu atakuwa ni mume wangu tu..’hapo nikasema kwa sauti

‘Hata hivyo kaupatia wapi ufungua wa hapa, uungua bado ninao mwenyewe na akiba yake....’nikawaza mwa kwa sauti, nikafunga kama ilivyokuwa na sikutaka kuchukulia pupa…nilipohakikisha nimefunga kama kawaida nikageuka kuondoka.

Ni wakati nataka kutoka nikakumbuka kitu, sijui kwanini niliwazia hivyo, nikarudi sehemu ile tena, nikafungua, upande wa pili yake.., na kuangalai hicho nilichotaka kukiangalia...nikakuta kipo pale pale...sijui kwanini nilitaka kufanya hivyo, lakini moyo ulitaka kuhakiki, kuwa silaha yangu binafsi bado ipo, ..huwa nina kibali cha kumiliki bastola, na tangu niinunue, ni muda sasa sijawahi kuigusa. 

Mwanzoni nilikuwa na tabia ya kwenda kulenga shabaha hata kuwindia, lakini kutokana na majukumu, nikawa sina muda huo tena. Kwahiyo ni muda sasa sijaitumia hiyo silaha

‘Hata hivyo silaha ya nini....?’ nikajiuliza, niliikagua na kuhakikisha ipo salama, baada ya kumaliza kuikagua nikafuta alama za vidole, kama kawaida yangu,..na kurudisha sehemu yake.nikahakikisha nimefunga kabati vyema, nikafungua mlango wa hicho chumbani , na kutoka, hapo akili ilikuwa kama sio yangu, hasira..lakini

Nikaingia chumbani, nikajikuta nashikwa na butwaa, kitanda kilikuwa kitupu, mume wangu alikuwa hayupo kitandani,…kaamuka muda gani na kaenda wapi…nikajiuliza kwa haraka nikajua katoka nje.

‘Huyu mume wangu kaamuka saa ngapi?’ nikajiuliza maana nilihakikisha kuwa alikuwa kalala, kabla sijaenda huko maktaba yetu, na kuamuka huko ni kama vile huyu mtu alikuwa macho, maana sikukaa muda mrefu pale ndani.

Na mimi kwa haraka nikatoka kule chumbani na kwenda sebuleni, sehemu ya mapumziko, …lakini kwa kunyata kimia kimia…na pale sebuleni.., nikamkuta mume wangu kakaa kwenye sofa.Alikuwa hajaniona, na mkononi kashika kitu.

Taratibu nikamsogelea, hadi nikamkaribia,….nahisi alihisi kuna mtu nyuma yake, kwani aligeuka,… akaniona, alishituka, mpaka nikaogopa, maana kwa hali yake, hakutakiwa kushituka kiasi hicho,....

‘Oh, mke wangu umerudi saa ngapi..si ulisema hutarudi mapema?’ akaniuliza huku akiwa ananishangaa, na mkononi alikuwa kashika mkataba.

Ule mkataba wa kifamilia…!!

Kwanza nilijifanya kama hakuna kitu, lakini yeye aligundua kuwa macho yangu yalikuwa yameangalia ule mkataba aliokuwa nao mkononi, na nilivyomshitukizia, hakuweza hata kuuficha, akawa kaushika vile vile mkononi, na mimi nikawa namsogelea kuhakikisha kuwa ni huo mkataba wetu, yeye ana nakala yake, na mimi ya kwangu, ila mimi kuna alama niliweka kwenye nakala zangu.

‘Nilikuona umelala, wakati naingia na sikutaka kukusumbua, kuna kitu nimekifuatilia huku nyumbani, na huenda nikarudi tena ofisini, ila na mimi nashangaa maana muda huu ulitakiwa ulale, kwani hujanywa dawa zako sawa sawa nini?’ nikamuuliza.

‘Dawa nimekunywa, lakini sasa hivi hata nikinywa, sipati usingizi kama ule wa mwanzo...’akajitetea.

‘Sawa mimi naona nisikusumbue,,..’nikasema kama vile nataka kuondoka, lakini nikamsogeela na kuangalia kile alichokuwa kashika mkononi nikasema;

‘Naona unasoma mkataba vipi tena, unajikumbushia zile enzi zetu za kuishi kwa kufuata mkataba, hahaha mume wangu bwana, au unaangalia nini, na peni, kama unasahihisha jambo, kuna nini kimekukwanza mume wangu ...?’ nikamuuliza na yeye akajibaragua kama vile anataka kuuweka chini, kama vile sio kitu muhumi sana kwake, akasema;

‘Aaah unajua tena ukikosa la kufanya, niliona nisome some tu kupoteza muda.....lakini ....’akasita.

‘Hakuna wasiwasi mume wangu, ...hiyo naona kama ni nakala yangu au , niliiweka wapi, sijui, uliipatia wapi...?’ nikamuuliza nilipoona ile alama yangu, nakutambua kuwa ilikuwa ni nakala yangu.

‘Hapana hii ni nakala yangu, sio ya kwa-kwako…kwani nakala yako haipo?’ akaniuliza akionyesha ishara ya kushangaa.

‘Unavyouliza ni kama vile unafahamu kuwa nakala yangu haipo, au?’ nikamuuliza huku nikitabasamu, nilikuwa nimejisahau sasa, maswali kama hayo sikutakiwa kumuuliza.

‘Ndio maana nakuuliza, maana kila mmoja ana nakala yake, au sio,...mmh, halafu mke wangu nilataka tuongee kitu muhimu, nilikuwa najaribu kupitia baadhi ya vipengele mbali mbali kwenye huu mkataba eeh, na sijui utakuwa na nafasi tukae tuongee, kwasababu mengi yamepita, na hatujawahi kuongea haya yaliyotokea...’akaanza kusema.

‘Mume wangu achana kabisa na mambo hayo, wewe hujafikia muda wa kuongelea hayo mambo, hujaruhusiwa na docta kabisa…subiria kwanza upone, na hata hivyo, sioni kwanini ukimbilie kusoma katiba kwa sasa, huoni utajitakia matatizo, unakumbuka tulivyokubaliana, hata kwenye mkataba hilo lipo kuwa mtu akiumwa, mambo ya mkataba yanawekwa pembeni kwanza,mengine yote yanasahaulika mpaka anayeumwa apone..sioni umuhimu wa mkataba ukiwa kwenye hiyo hali.’nikasema.

‘Swali linalonisumbua ni kuwa nikipona, itakuwaje…inanipa shida sana hiyo, na akili yangu haiwezi kutulia kama tusipolitatuia hilo, unanielewa hapo..itakuwaje sasa…?’ akauliza huku akifungua fungua ukurasa kwenye ule mkataba.

‘Kwani una wasiwasi gani mume wangu,...mimi sioni tatizo, kwani ulishaniomba msamaha, nikakukubalia kuwa nimekusamehe, hayo yanatoka wapi tena?’ nikamuuliza .

‘Kusamehe kwa maneno ni kitu kingine, lakini yapo mambo ya kisheria…na haya ni kati yangu mimi na wewe…sasa….’kabla hajamaliza mlango ukagongwa, nikageuka kuangalia mlangoni, na mara ukafunguliwa akaingia docta, rafiki wa mume wangu, ambaye aliponiona kwanza alijifanya kama vile hajashituka. Lakini nilimuona na dalili ya kushtuka, hakutarajia kunikuta hapo


‘Nilisikia umekwenda kazini au…mbona umerudi mapema hivi,.....?’ akaniuliza docta

‘Kwani tuliongea na wewe leo, kuwa nimeenda kazini na sitarudi mapema, mbona unaingilia mambo yasiyokuhusu, unakuwa kama unafahamu ratiba yangu kuwa nitarudi nyumbani kwangu saa ngapi, kwanza ukumbuke kuwa nipo likizo, kwa ajili ya kumuuguza mume wangu!’ nikasema nikimwangalia kwa makini machoni.

‘Nilipiga simu kwa mumeo akasema haupo, ....nikajua upo kazini, na kama upo kazini, sizani ungelifika tu na kuondoka…’akasema na akawa sasa anamuangalia mume wangu kwa makini, nahisi kuna ishara aliona kutoka kwa mume wangu ndio akakatiza maneno, sikutaka kuongea sana au kufanya lolote litakalo wakwanza, nikasema;

‘Mume wangu naazima hii nakala …mara moja…’nikasema nikiwa nimeinama kuichukua hiyo nakala, ni kitendo cha haraka, maana nilipotamka hivyo, nay eye alikuwa keshafikisha mkono kama kuishika hiyo nakala ya mkataba, lakini mimi nilihsiwahi

‘Hapana nina kazi nayo…si una ya kwako…’akasema

‘Ni kitu kitu kidogo, nakurudishia sasa hivi, nyie si mnaongea wewe na rafiki yako, au sio…’nikasema nikimuangalia docta, na docta akawa anaonyesha uso wa tahadhari, akimuangalia sana mume wangu

‘Mhh, hapana hiyo nakala yangu ...ina mambo yangu binafsi nimeandika,....unaonaje ukaenda kuchukua nakala yako, kama hutojali mke wangu...’akasema akionyesha wasiwasi fulani.

‘Usijali mume wangu, nitakurudishia tu, ....endeleeni kuongea...’nikasema huku nikiwa nimeshauchukua na kuanza kufungua sehemu za ndani za mkataba ule, niliona mistari imechorwa chorwa, kama kukata kata kata sehemu, na maneno mengine yameandikwa kwa mkono, kama vile ni rafu.

Kiukweli hii ilikuwa nakala yangu , pamoja na sahihi, kuna sehemu niliandika mambo yangu, na sahihi,  lakini kwa hivi sasa naona mume wangu naye kaandika mambo yake..akifuta yale yangu…, nikageuza kuangalia juu, nikaona sahihi yangu na sehemu niliyokuwa alama ipo, kuashiria sijakosea hiyo ilikuwa ni nakala yangu...’

‘Mke wangu, ...nauomba huo mkataba, tafadhali....’akasema huku akisimama kuja kuuchukua mkononi mwangu, na mimi nikasogea pembeni nikiendelea kufungua fungua, na yeye akawa hana jinsi, akatulia huku kanikazia, macho akionyesha wasiwasi,

Mimi kwa muda huo  sikujali tena kuwa nitamkwaza, nikawa sasa natembea kutoka nje nikiwa bado nimeushikilia huo mkataba huku nikiendelea kufungua sehemu nyingine, na hakukua na maandishi ya kuhakikiwa kwenye sehemu nyingine zaidi ni kwenye vipengele vya ndoa.

Nikafika mlangoni bila kugeuka nyuma, na huyo nikatoka nje bila ya kugeuka nyuma, nikawa sasa naelekea kule kwenye bustani, ili nikae, nitulie nipate muda wa kuangalia ile sehemu,…kwa haraka nikachukua simu yangu na kutaka kupiga picha ili niwe na kumbukumbu, lakini kabla sijafanya hivyo nikasikia sauti toka ndani;

`Shemeji,...njoo haraka...’ ilikuwa sauti ya hatari kutoka kwa docta, rafiki wa mume wangu. Simu ililia mlioa wa kuchukua picha, lakini sizani kama itakuwa imelenga sawa sawa maana nilisthuka…

 Kwa haraka nikajizoa zoa na ule mkataba haukubanduka mkononi, nikakimbilia ndani, nilipofika nikakuta mume wangu kalala sakafuni..na docta kamuinamia akimfungua shati, na mimi nikamsogelea na kuuliza;

‘Kuna nini tena jamani..?’ nikauliza, na docta akaniangalia kwa macho, yaliyoonyesha kukerwa, na kusema;

‘Umefanya nini sasa...nilishakukanya, unaona sasa....’akaanza kunilaumu mimi na sikujau ananilaumu kwa lipi….

**************

Hali ya mume wangu ilibadilika na kuwa mbaya,na juhudi za docta hazikufua dafu, alimpa huduma ya kwanza lakini haikusaidia,  ikabidi akimbizwe hospitalini na docta huyo huyu na alipofika docta wake akamkagua, na kusema haraka aingizwe kwenye chumba cha wagonjwa mahututi.

‘Kuna jambo gani limemshitua?’ akauliza huyo docta baada ya kumhudumia na kurudi pale nilipokuwepo, na hadi muda huo tulikuwa hatujaongea lolote na docta rafiki.

‘Kwakweli mimi siwezi kujua, labda tumuulize rafiki yake, maana mimi nilimuacha wakiwa naye, akiwa mzima kabisa, na niliwaacha hata dakika mbili hazikupita, nikasikia sauti ya huyo rafiki wa mume wangu akiniita kuwa mume wangu hali yake sio nzuri...’nikasema.

‘Mhh, inaonyesha kuwa kuna kitu kimemshutua, na wewe unakifahamu ni kitu gani,...hukutakiwa kulazimisha kufanya kitu ambacho hakitaki, au alipata mshtuko fulani, mshituko kwake ni tatizo…lakini….’akasema huyo docta, na docta rafiki akamkatiza na kusema;

‘Nahisi ni ule mkataba…’akasema

‘Lakini mbona ni mkataba wetu mimi na yeye, na anaufahamu siku zote kuwa tunao , na haikuwa na ubaya mimi kuuchukua, na hata hivyo wewe unajuje kuwa ni kuhusu huo mkataba…?’ nikauuliza kwa mshangao.

‘Kwasababu nilimuona na dalili mbaya, wakati huo mnaongea na uliuchukua mkataba akawa hataki, ile hali ikawa inazidi kumsukuma kwenye hatari…’akasema

‘Usinitupie lawama kabisa…’nikasema.

‘Kwani ni mkataba gani huo, inawezekena kuna kitu hakipendi kwenye huo mkataba…?’ akauliza docta anayemtibia

‘Hakuna cha maana vitu vilivyopo humo ni kati yangu na mume wangu hakuna la zaidi, na sioni ni kwanini liwe ni tatizo hilo…..’nikasema.

‘Una uhakika kuwa hakuna jambo linalomkwanza mume wako kwenye huo mkataba, nahisi inawezekana kuna kitu ambacho anakihofia..?’ akaniuliza huyo docta, na mimi nikasema;

‘Lakini sizani hata kama kuna kitu…kipo kipo…nahisi ana lake jingine, hata sielewi, kwanini iwe hivyo, unajua nimejitahidi sana, sasa nachoka jamani…aah, basi nifanyeje jamani?’ nikasema huku nikuliza kwa mshangao.

‘Muhimu, ni kumuhakikishia kuwa kama kuna lolote humo, halitafanya kazi, au kama hataki wewe uwe nao, mrejeshee, haraka iwezekanavyo…’akasema docta rafiki.

‘Hivi kwanini unaongea hivyo, unajua lolote kuhusu huo mkataba maana, maana moja ya makubaliano yetu mimi na yeye ni kuwa mkataba huo ni baina yangu mimi  na yeye tu, wewe umayefahamu vipi hayo…?’ nikamuuliza docta rafiki kwa ukali, mpaka docta anayemtibia mume wangu akatuangalia kwa mshangao

‘Off course, …mimi sijui lolote zaidi ya kuwakuta pale mkiwa kwenye kubiashana..eeeh, nahisi , mimi nahisi huenda mwenzako kinachompa shida kwa sasa ni kuhusu mliyoandika kwenye huo mkataba…sasa sisi hatujui ni nini kilichomo humo ndani,...je huna uhakika kuwa huenda kafanya kitu kinyume na huo mkataba wenu..?’ akaniuliza docta rafiki.

‘Mimi sijui, na hakuna kitu kama hicho, huo ni mkataba wetu tu wa kikazi, hakuna tatizo, …’nikasema kuvunga ili isije kuleta maana kamili ya kilichomo kwenye huo mkataba.

‘Haya, kama unaona hivyo, sawa,...ila jitahidi sana, kuwa mvumilivu, huko mnapokwenda, ni kubaya, na mwenzako yupo mahali pabaya, hajijui...na usije ukafanya mambo kwa pupa, ukaanza kujijutia, ....itakuathiri sana kwenye maisha yako...’akasema.

‘Hamna shida, hilo niachie mimi,..., cha muhimu ni kutafuta njia za kumponyesha huyo mtu, na sijui nifanye nini, maana kila ninachotaka kukifanya, kwa masilahi yetu, kinakuwa na utata, nitawezaje kuishi maisha ya nama hii, ina maana mimi nakuwa kama mfungwa...’nikalalamika.

‘Ni swala la muda tu...vumilia, hadi mume wako apone, na mengine yatakuja baadaye, usije ukafanya mambo, ambayo yatakuharibia, na hata ukienda kisheria ukaonekana wewe huna haki...’akasema huyo rafiki wa mume wangu na wakati huo docta alikuwa akitusikiliza tu baadae yeye akaondoka zake na kutuachia nafasi ya kuongea.

Aliposema hivyo, nikaingiwa na shaka, kwani anavyoongea ni kama vile anafahamu kitu kwenye huo mkataba wetu, kuna kipengele, kuwa kama mmoja akiumwa, mambo mengine yote yasimame, hadi hadi huyo anayeumwa apone....na isitokee shinikizo la mmoja kuchukua nafasi hiyo kwa masilahi yake binafsi...

‘Kwahiyo wewe unasemaje...unataka mimi nifanye nini?’ nikamuuliza, kwanza alitabasamu, kama kunidhihaki kuwa sasa naanza kumtegemea yeye, lakini hakufahamu mantiki ya swali langu.

‘Kwa taarifa yako, tu, licha ya kuwa ni hatari, lakini docta kasema tukio hilo limesaidia kitu fulani, limashitua ile mishipa iliyokuwa haijashituka, na sasa hivi kila sehemu ya mwili imerejea kwenye hali yake ya kawaida, lakini kuna angalizo kubwa, tena hilo ni hatari zaidi, kuwa kama hali hiyo ikiendelea inaweza kuleta matatizo mengine makubwa zaidi...’akasema

‘Kama yapi?’ nikauliza kwa hamaki

Stroke....anaweza akapata na kiharusi,ni hiyo ikamfanya apooze kabisa...’akasema

‘Mungu wangu....’nikasema

‘Lakini yote yanategemea nyie wawili, kama kuna kitu unaona kinaweza kumkwanza mume wako, ni vyema ujaribu kukiwepa, jaribu kujizuia,....kwanini usiwe na subira…achana na mambo mengine yote..’akasema na mara docta akafika, na mimi nikawa na shauku ya kusikia mume wangu anaendeleaje. Na kabla hajaongea kitu rafiki wa mume wangu akasema;

‘Docta mimi nilikuwa na wazo, je huyo mgonjwa hatuwezi kumpeleka mahali ambapo atakuwa hakutani na mkewe...maana naona wakiwa pamoja matatizo kama haya yataendelea kutokea na kama ulivyosema kuwa ni hatari kama akipatwa na stroke? Akauliza rafiki yangu.

‘Hiyo ni mbaya zaidi, maana mume wake, hataki kuwa mbali na mkewe, niliwahi kumwambia hilo kabla, lakini alipinga kabisa,.., na kufanya kitu ambacho hakipendi kitamfanya ajisikie vibaya, cha muhimu ni mke wake, kukwepa yale yote yanayoweza kumfanya mume wake ashituke,au ahisi vibaya, ndio hivyo....’akasema docta.

‘Unasikia, ....nilikuambia, uwe makini, mimi nakushangaa  una haraka gani, kuna kitu gani unakihitajia kwasasa, sasa uchague mwenyewe, mume au hayo unayoyataka wewe....’akaanza kunilaumu rafiki wa mume wangu

‘Wewe hujui kinachoendelea ina maana nikae kimiya wakati naona kuna mambo yanaharibika, kuna vitu muhimu vinapotea, kwanini vipotee, kuna nani yupo nyuma ya hayo yote, unataka mimi nikae kimiya, hivi kweli mimi unaniona kuwa sina uchungu na mume wangu....’hapo nikawa nasema kwa ukali.

‘Hujanielewa …’akasema docta

‘Nimekuelewa sana,…nikuulize kama kuna vitu vinapotea, ambavyo vitakuja kuitahiri familia, akiwemo huyo mume wangu… , nikae kimiya tu..nisifuatilie, na hata huko kufuatilia, sijamuhusisha yeye, ila yeye anajiingiza kwenye mambo yasiyomuhusu kwasasa…ni lazima nifanye yote, nimhudumie mume wangu na wakati huo huo nilinde masilahi ya familia..’nikasema.


Na mara kukatokea suti ndani ikumuita huyo docta, na docta akakimbilia ndani, na sisi tukabakia tukiwa na wasiwasi, lakini baadaye huyo docta akarudi na kusema;

‘Mgonjwa anaendelea vizuri, lakini anamuhitaji mke wake..’akasema docta

‘Itabidi nifuatane naye maana mimi nawajulia hawa watu…’akasema docta rafiki

‘Hapana, mgonjwa kasema anataka kuongea yeye na mke wake tu...’ aliposema hivyo docta, mimi sikupoteza muda nikakimbilia huko ndani alipolazwa mume wangu…, na nilipofika ndani nilimuona mume wangu akiwa kalala huku kaweka mikono yote miwili kichwani kama vile hakuna mto, huku kaangalia juu.

‘Oh, mume wangu umepona...’nikasema na yeye akajitahidi kucheka huku bado akiwa kaangalia juu, kama hataki kuniangalia machoni,na kwa sauti ya huzini, akasema;

‘Yah, nimepona, lakini sasa naogopa kupona, ...’akasema

‘Kwanini unasema hivyo mume wangu?’ nikauliza

NB: HAYA KWA LEO NIISHIA HAPA

WAZO LA LEO: Dunia nzima, inaingia kwenye matatizo kwasababu kubwa ya mali na masilahi,. Watu wanakosana, kunakuwa na vita, migongano makazini, familia hazipatani, ukichunguza sana ni kwasababu ya mali na masilahi.Ubinadamu, utu, udugu, unasaba, ndoa vyote hivyo vinaharibika, na kuingia kwenye matatizo kwasababu ya mali, na masilahi. 


Tukumbuke kuwa vyote hivyo, mali na masilahi ni vitu vya kupita tu...vilikuwepo, na vitaendelea kuwepo, wewe kama binadamu mali na masilahi yako ni matendo yako mema.Matendo yako mema ndio mali na masilahi yako, itakayoweza kukusaidia hata baada ya kufa..
Ni mimi: emu-three

No comments :