Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, November 28, 2017

MKUKI KWA NGURUWE-31





‘Hakikisha umeharibu kila kitu…kila kitu, hasa mikataba, mengine nitayamaliza nikija…’Ni meseji pekee iliyokuwa imebakia kwenye simu, na imetumwa kutoka namba za nje...mume wangu alihakikisha kafuta kila kitu, hadi picha.

Hasa mikataba, mikataba gani hiyo ya kazi, na ni nani huyu kamwandikia mume wangu, …’ nikajikuta nikisema, nikirejesha simu ya mume wangu sehemu nilipoichukulia, mume wangu alikuwa kalala kwa amani kabisa.

Ujumbe huo ulinifanya niwazie kwenda ofisini, kuhakikisha kama kila kitu kipo sawa, na kuhakikisha mikataba ya kazi, na mingineyo ipo sawa sawa,…niliweza kuondoka, maana hali ya mume wangu ilikuwa sasa inaendelea vyema, na ningeliweza kumuagiza mfanyakazi wa ndani akaendelea na huduma nyingine bila shaka, muhimu ni mume wangu mwenyewe akubali,

‘Mume wangu naona hali inaimarika sasa namshukuru mungu kwa hilo…’nikasema

‘Kweli mke wangu nakushukuru sana…’akasema

‘Sasa nilikuwa na ombi moja, nataka kesho asubuhi na mapema nifike ofisini kwangu mara moja, unaweza kuniruhusu…?’ nikamuuliza

‘Ofisini eeh, …ooh, hivi kweli, samahani sana mke wangu,ina maana siku zote ulikuwa huendi kazini kwa ajili yangu, mimi nilijua upo likizo…’akasema

‘Nilichukua likizo kwa ajili yako…’nikasema

‘Nashkuru sana mke wangu,  sasa…, wewe nenda tu, si umeona mwenyewe siku hizi najitahidi, yaani sijui kwanini wiki hii nimeingiwa na kitu kikanifanya mwili uwe na nguvu za ajabu, nikaweza kusimama, na sasa natembea japo kwa shida…mmh, nahisi hizi ni nguvu za ajabu…’akasema

‘Hongera, tumshukuru mungu…’nikasema

‘Haya wewe kesho nenda tu..

Basi kesho yake asubuhi nikafika ofisini.

                 *****

Kesho yake nilipofika ofisini, kwanza nilihangaika na maswala ya kikazi, ambayo yalinihitajia mimi kama mkurugenzi mkuu, na nilipomaliza, nikawa natatafakari kitu gani kingine nifanye kabla sijaondoka.

‘Lakini usichelewe…’ nilikumbuka kauli ya mume wangu.

Hata hivyo, muda ulikuwa bado, nikapiga simu nyumbani, na mfanyakazi akasema kila kitu kipo sawa, mume wangu anachukua mazoezi mwenyewe ya kutembea, ..

‘Sawa naona nitachelewa kidogo…mwambie nilimpigia sikumpata sawa..’nikasema

Siku hiyo nilijiona sina raha kabisa, na ilitakiwa niwe na raha, maana mume wangu hali yake inaimarika, keshaanza kutembea kidogo kidogo....nilishangaa kumuona akiwa furaha kuliko siku za nyuma, ni kama vile amesikia jambo kubwa ambalo limefurahisaha sana

 Kiukweli niliombea iwe hivyo, ili apone haraka na maisha yaendelee, ila sikutaka kumdadisi sana, kujua kuna nini kimetokea, nilijitahidi kujizuia sana , kwa kutokumuongelesha au kumuuliza maswali ya kumpa mawazo, japokuwa sio kazi rahisi, kichwa changu kilikuwa na maswali mengi yasiyo na majibu na mwenye majibu ni yeye.

 Wakati nipo mezani nikifanya hiki na kile akili bado ilikuwa inafanya kazi, inawaza, na sasa nikakumbuka kauli ya mume wangu:

Nakupenda sana mke wangu, niache nikuambie ukweli, nimekukosea sana, na ninachoogopa ni kuwa huenda kosa langu likaenda kuwaathiri wengine,  sasa umemuingilia mdogo wangu, sijui kakukosea nini, haya…kesho atakuwa mwingine, unaona eehe, ni vyema tukayamaliza haya sisi wenyewe…kama ni dhambi zangu nibebe mimi mwenyewe… achana na mambo  ya baba yako…au .

 Inaonekana kuna kitu kwa mume wangu…sasa ni kitu gani hicho

‘Hakikisha umeharibu kila kitu…kila kitu, hasa mikataba, mengine nitayamaliza nikija…’

‘Hasa mikataba….’ Nikasema hilo neno na lulirejea mara nyingi, na sijui ni kwanini kuna kitu kikanikumbusha jambo…. nikakumbuka…

‘Mkataba wa ndoa…’

Nilipokumbuka hivyo, nikasimama,

‘Hivi kweli eeh, ule mkataba wetu wa ndoa,…ooh, afadhali, nimekumbuka, …sasa mambo yatakwisha kwa amani…sasa kama ni kweli, …mkataba ule utafanya kazi yake,...’nikasimama na kujinyosha,

‘Mkataba wa ndoa…’nikasema nikichezesha mikono kuonyesha kuwa nimekumbuka jambo la muhimu sana.

**********

Nilipokumbuka hili nikataka kujirizisha , nilitaka nikausome tena ule mkataba…najua mume wangu atakuwa keshalisahau hilo, lakini ulikuwa ni muhimu sana kwenye maisha yetu,…na ndio ulionifanya nimuamini sana mume wangu, kwani mkataba huo ulikuwa umetufunga tusifanye makosa..

‘Lakini kwa hili…wanalosema kuwa mume wangu kafanya,..ina maana kweli hakumbuki huo mkataba, hapana, watu wengelijua wasingelisema hilo, mume wangu aliuthamini sana huo mkataba, aliahidi na akawa wa kwanza kuutekeleza huo mkataba,…sasa iweje,..siamini,….’nikasema

`Yah,..hili sasa litakuwa ndilo suluhisho la hili tatizo, na sizani kama mume wangu kalisahau hilo, kama kasahau, basi kakusudia kweli, na kama kakusidia kweli, basi sheria itachukua mkondo wake, maana ahadi ni deni…’nikasema kwa sauti.

 Hapo nikapata nguvu ya ajabu,….niliinuka kwa haraka kwenye kiti, nikasimama kwanza nikajinyosha tena na tena,…, sikuwa na haraka, sikuwa na jambo jingine muhimu kwa muda huo la kufanya, ...

‘Kwenye ule mkataba ushahidi ni muhimu sana, hasa likitokea kosa, hilo lilisisistizwa sana, …’nikawaza hapo nikakuna kichwa

‘Sasa mimi nina ushahidi gani, kuwa hayo waliyosema watu ni kweli, kuwa huenda , mume wangu kafanya kosa, na kosa lenyewe ni lipi, mmh…kazini, huko sina uhakika, lakini hili kosa kubwa la kuvunja masharti ya ndoa, je kweli kafanya hivyo, ushahidi upo wapi…?’ nikajiuliza

‘Ok, ngoja kwanza,…nikausome vyema ule mkataba, mambo ya ushahid ni mengine, je nitauweza kuutumia muda ukifika, je …haaa, sizani, mume wangu hawezi kufany ahivyo, ina maana kasahau, haaaah, mungu wangu....’nikasema.

Nikatembea hadi kwenye kabati langu maalumu, kabati hilo, huwa naweka kumbukumbu zangu muhimu, na hakuna mtu mwingine mwenye mamlaka ya kufungua hilo kabati, ….Kwanza nikafungua sehemu ya  ukutani, kuna kabati maalumu za nyaraka za ofisini, lipo ndani ya ukuta, na humo kuna sehemu maalumu, ina ufunguo wake, na kuna sehemu imejificha sana hapo ndio niliweka ufungua wa kabati…

 Nikafungua kabati, na ndani ya kabati kuna sehemu maalumu, humo nimeficha ufungua wa sehemu ambapo nimeweka hizo nyaraka, hakuna anayeweza kuuona huo ufunguo,… ni muda mrefu sijalifungua hilo kabati, maana vyote vilivyopo humo ndani, sio mambo ya kila siku ya kikazi. Na humo niliweka nakala zangu nyingine za mikataba ya kazi , jengo nk, pia kuna nakala za vyeti vya ndoa, na nakala za vyeti vya watoto…


            ********

 Wakati nimeshauchukua huo ufunguo, ndio nikakumbuka jisi gani tulifikia hadi kuamua kuwa na mkataba wa ndoa,… ilikuwa kama masihara tu, ilikuwa kama fikira zilizokuwepo kabla ya kuolewa , na baada ya kuolewa nikasahau, sikuona umuhimu wake tena.

Nakumbuka ilikuwa kipindi nakaribia kujifungua, hilo wazo likanijia akilini, ikawa naliwazia sana, mpaka nikashindwa kuvumilia, ndio nikampigia simu wakili wa kazini, nikamuelezea hilo wazo.

‘Muheshimiwa, kuna kitu kinanisumbua sana akilini, ni wazo tu, lakini nimefikiria sana, nikaona lina umuhimu wake,..mimi napendelea kuwa na kitu kama mkataba wa ndoa kati yangu na mume wangu....’nikasema

‘ Wazo zuri sana,…basi kama mtakubaliana wewe na mume wako.., mimi nipo tayari, na nitawatengenezea mkataba mnzuri sana, na wenyewe mtaona jinsi gani utakavyowasaidia, ...ongea kwanza na mume wako mkubaliane, maana hilo ni swala la nyie wawili, kukubaliana kwanza...’akasema.

Nikahamasika,na jambo hilo , niliona uwe mkataba mkubwa zaidi, ambao utagusia kila kitu,  mambo yote ya familia, kuanzia ya kifamilia hadi ya mali zetu,  na hili nililifanya makusudi, ili hata nisipokuwepo mimi, au mume wangu basi kusije kukatokea mambo mengine ya kuja kuidhulumu watoto wetu. 

Basi siku hiyo nilikaa nikiliwazia hilo, na jioni alipokuja mume wangu, nikaona nimwambie…ilikuwa siku ya kumbukumbu sana, na tarehe hiyo ilikuwa muhimu kwenye familia yetu.


‘Mume wangu kuna kitu nataka nikuambie...’nilimwambia,  na yeye akanisogelea na kushika shika tumbo langu, huku akitabsamu , akasema;

‘Usiniambia siku zinakaribia, maana nina hamu sana ya kumuona mtoto wetu huyu’akasema huku akinishika shika tumbo langu..kiukweli siku za awali, hakuna mtu angeniambia kitu dhidi ya mume wangu nikakisikiliza, nilimpenda sana mume wangu na nilikuwa namuamini sana.

‘Usiwe na shaka mume wangu, siku yoyote kuanzia leo tunaweza tukaitwa baba au mama fulani, lakini sio hicho nilichotaka kukuambia.....’nikasema

‘Mhh, ok…kuna nini,  niambie tu...mama watoto wangu …mama kijacho…’akasema huku akiendelea kushika shika tumbo langu.

‘Kuna kitu siku nyingi nilikiwaza..awali nilichukulia kama mambo ya kishule tu, lakini jana , juzi nikaliwazia hilo, nikaona kumbe lina umuhimu wake,..na nilipoona  wazazi wetu wameanza kutkubali,  nikaingiwa na hamasa, ila sitaki wazazi wangu walifahamu hilo ni mimi na wewe tu…’nikasema

‘Ehe, niambie…unazidi kunipa hamasa…’akasema

‘Lakini unielewe mume wangu, ...sina nia mbaya na wazazi wangu, au jamaa zangu, au jamaa zako, lakini haya hutokea sana katika  dunia hii, na sisi kama wazazi inabidi tuwe makini kwa hili...’nikaanzia mbali.

‘Kwani kuna tatizo kutoka kwa wazazi wako tena?’ akauliza akionyesha mashaka

‘Hapana, hili ni kati yangu mimi na wewe, na familia yetu inayokuja, hatujui tutapata watoto wangapi, na hatujui watakuwa wakike au wakiume wangapi, ....hilo ni mimi na wewe lakini linalenga maisha ya mbeleni…’nikasema.

‘Hahaha mke wangu bwana, una wasiwasi,..’akasema akiwa bado hajafahamu nataka kuongea nini.

‘Mume wangu sipo huko kwenye kuzaa kwangu, nipo kwenye baada ya kuzaa, maisha yetu , mali zetu, na mipangilio yetu ya kila siku, maana hilo ndilo muhimu sana....’nikamwambia.

‘Mhhh, mhh, kwahiyo watakaje labda....’akasema huku akikaa vizuri na kuniangalia machoni.

‘Nataka tuwe na mkataba wa kifamilia...’nikasema na yeye akawa kama anashituka halafu akapepesa pepesa macho.

‘Mkataba wa kifamilia, wa nini tena,..si sis tuna ndoa yetu tayari ndoa ni mkataba tosha au sio,… unahitajia mkataba gani tena, huniamini au kuna nini umekigundua dhidi yangu, au familia yangu au yako?’ akaniuliza kwa mashaka.

‘Niliongea na wakili wetu wa kampuni,.....ambaye kama unavyojua, anashughulika kwenye kampuni zote mbili yangu na ya kwako pia, mimi sina lengo la kuingilia kampuni yako saana, lakini hili la mkataba ni kwa ajili ya mali zetu zote, zikiwemo kampuni zetu,  ili kusije kukatokea sintofahamu baadaye....’nikasema.

‘Mhhh, okey, niambie maana mpaka sasa sijakupata vyema, na hata hivyo huyo wakili hajaongea na mimi... kwahiyo sijui unachotaka kusema ni nini hasa…’akasema.

‘Ni hivi, katika maswala yote ya mali, kama hakuna matatizo, hakuna shida, lakini kukija kutokea matatizo, watu , binadamu tulivyo, cha kwanza kukimbilia ni mali, hutaamini, watu mlikuwa mnapendana, mnasaidiana, ni marafiki, lakini kukitokea mfarakano kidogo tu, wote akili na macho yao ni kwenye mali...’nikasema

‘Ni kweli, lakini sio mimi….’akasema

‘Najua, sote tutasema hivyo…lakini sio kwetu tu, na wengine wa nje, umeona visa vingapi vinatokea, baba au mama, au baba na mama wakiondoka, kunatokea nini,, watu ambao hata wahajui mali imetokea wapi ndio wa kwanza kuja kuvamia mali za mayatima,  wakitamani kila kitu..’nikasema

‘Ni kweli…’akasema

‘Sasa mimi nimesoma sheria kidogo, na nilitaka kile nilichokisomea angalau kije kufanya kazi kimatendo kwenye familia yetu, unaonaje hapo kwanza,…’nikasema.

‘Mke wangu mbona unanitia wasiwasi, ina maana unaogopa kuwa ukienda kujifungua ....unaweza usirudi, hapana bwana,…mke wangu kuzaa ni kawaida tu, hutapata lolote baya...hutakufa bwana, usinitishe…usinitie wasiwasi na majonzi, hakuna shida, huna matatizo yoyote, docta kasema huna tatizo lolote…utajifungua salama…’akasema.

‘Mimi siongei hili kwa vile nakwenda kujifungua, hapana, naliongelea hili kwa ujumla wake, ni jambo la maisha yetu,...na ukumbuke mume wangu, sisi kama wandamu, hatuna mamlaka na mungu, kuwa nitaishi muda gani au nitakufa lini,...’nikasema.

‘Ni kweli…’akasema bado akiniangalia kwa mashaka.

'Lakini hata hivyo ni vyema tukawa na utaratibu mzuri tu, tukajiandaa kwa lolote lile, hata kama tupo hai, bado mkataba unaweza kutusaidia katika maisha yetu, tukawa na utaratibu mnzuri tu kwa nia njema,...’nikasema

‘Ni sawa, nana kukuelewa…’akasema

‘Na hatuombei mabaya…, maana sisi ni wanadamu,kama kutatokea mfarakano wowote, makataba huo utakuja kutusaidia...hamna haja ya kushikana mashati, wakili yupo na mkataba upo..’nikamwambia.

‘Sawa, sawa kabisa....kwahiyo ulikuwa unataka kusema nini, ..tuwe na mkataba, kuhusu nini hasa mali, au…maana ndoa ina masharti yake, kidini kisheria, imebainishwa kila kity au..sijakuelewa zaidi, ?’ akauliza akishika kichwa, nahisi alikuwa akiwazia mbali, na mimi nikamwambia;

‘Eheeeh, sasa tulia nikuambia, mimi niliongea na wakili wangu, akanishauri kuwa sisi ni wanandoa na pia mungu katujalia tujaliwa kuwa na watoto, tuna kampuni, na bahati nzuri tuna kampuni mbili, yako ya ya kwangu..na baba yupo ana hisa kwetu japokuwa ni kidogo, nia ni kuhakikisha anatulinda, tulifanya hivyo kwa nia njema tu..sio kwamba kila mtu ana maisha yake, hapana, ni katika kujijenga zaidi….’nikasema.

‘Sawa kabisa, na huo ulikuwa ni ushauri wako, japokuwa mimi nilitaka tuwe na hisa nusu kwa nusu kwenye kampuni yangu, hata kama sio ya kwako, maana mtaji karibu wote unatoka kwako na kwa wazazi wako...’akasema.

‘Hapana hilo halikufanyika kwa nia mbaya...sote ni wazazi wetu, na uchungu wa familia ulio nao wewe ni sawa na nilio nao mimi, ndio maana hakuna aliyefikiria kuwa ukipata hisa zote hizo, utadhulumu, au utakimbia nazo, ..hilo halipo, na utambue kuwa mimi nakuamini moja kwa moja...amini hivyo...’nikamwambia.

‘Sawa kabisa hata mimi nakuamini sana,...’akasema.

‘Sasa ni hivi, niliongea na wakili wetu, nikamwambia atayarishie mkataba, mkataba ambao, utagusa kila kitu chetu, kuanzia, mali, watoto na hata ndoa yetu,...hii itasaidia sana, ili tuwe makini na si kwenye mali tu, bali pia na kwenye ndoa yetu, mkataba huo uainishe kuwa kama mmoja wetu atakiuka maswala ya ndoa, basi ...amevunja mkataba na mali na kila kitu chake, kinachukuliwa,..’nikasema

‘Mke wangu, unajifunga wewe mwenyewe…’akasema kwa kujiamini

‘Nikuulize wewe je upo tayari na kitu kama hicho , maana mimi sina shida....’hapo nikatulia.

‘Una maana mtu akikiuka hata kwenye maswala ya ndoa…kama, usaliti au sio..ok, inakwenda hadi kwenye mali, mtu anakuwa hana haki na mali tena, kuachia kuchana nak….ok, …mimi sina shida na hilo,..ni sawa kabisa, lakini wewe huoni kuwa wewe ndio utadhulumiwa…’akasema

‘Usijali…’nikasema

‘Unajua nina maana gani, mali ni zako, mtaji umetoka kwa wazazi wako, leo umevunja mkataba mali inakuja kwangu, je wazazi wako watakubali hivyo, hapana hapo kuna walakini...’akasema.

‘Ndio hivyo, kwani wewe unatarajia kukiuka masharti ya ndoa, mimi naliona kwangu ni kinga, sitaweza kukiuka, na sheria ni msimeno, nikikiuka sheria ipo una haki ya kudai haki yako..au sio..?’ nikamuuliza.

‘Kwangu mimi mke wangu sina shida, mimi  nakupenda sana mke wangu, sizani kama kuna mtu anaweza kuja kunivuruga akili…, hakuna..kwahiyo mimi naunga mkono huo mkataba, tena bila wasiwasi....lakini ni wewe tu, kama ikatokea, haya utapoteza kila kitu, ila siwezi kukuacha....’akasema na mimi nikamkatisha na kusema;

‘Sawa mimi nilitaka nikuweke wazi kwa hilo,na nilimwambia wakili autayarishe, halafu tutakutana sote kwa pamoja tuusome, tuone kama kuna chochote cha kubadili, au kuongeza,..na ningelipendelea ikiwezekana iwe kama katiba yetu ya familia, na nina imani kuwa hakuna atayekiuka huo mkataba, mimi sina shaka kwangu...’nikasema na kumwangalia.

‘Hata mimi..mimi sina shaka na hilo, ..wewe niamini mia kwa mia...’akasema.

‘Mimi nina uzoefu , mimi naheshimu sana hayo mambo ya mkataba, kwani nimeona jinsi gani unavyosaidia maswala ya kikazi, ndio maana nikaona  kwanini mkataba kama hiyo tusiitumie kwenye familia zetu, ili kukwepa makatizo mbeleni..kaa ufikiria kwanza…’nikasema.

‘Hakuna shida kabisa, mimi nipo pamoja na wewe, na nipo tayari kwa hilo...naliunga mkono kwa nguvu moja.’akasema.

‘Sawa kama umekubali basi, tuombe mungu, ...na ni vyema wewe ukakaa ni kuliwazia hilo kwanza, ili uone ni vitu gani muhimu vinahitajika kwenye mkataba huo, isiwe ni mawazo yangu tu, ....au  isiwe ni mawazo ya wakili wetu tu,...mkataba huo uwe kama katiba yetu..unaonaje..?’ nikasema.

‘Ni sawa kabisa mke wangu

‘Basi ni vyema, basi kaa ufikirie zaidi….’nikasema nikipumua, sikutarajia kuwa mume wangu atakubaliana na hilo.

‘Mimi sina cha kufikiria zaidi, cha muhimu tukutane na huyo wakili tuone jinsi gani alivyoandaa, na kama kuna nyongeza mimi nitasema, na wewe pia utasema, ili mwisho wa siku tuwe na kitu kimoja cha watu wote, hilo naona lisichukue muda, hata leo, kama wakili keshaandaa, tunaweza kumuita...’akasema.

‘Sawa tutamuita wakili wetu kesho,kama yupo tayari, na kama keshaandaa, nilimuambia akasema ataandaa ,lakini kwanza mimi na wewe tukubaliane....’nikasema

 ‘Sawa mke wangu, mimi sina shida kabisa mke wangu nakuunga mkono kwa wazo hilo la hekima, nipo tayari  kwa wakati wowote...’akasema.

Na baada ya siku mbili mkataba ukatayarishwa, baada ya kukutana na kupitia kila kipengele, na tukaongezea na mengine mengi, ilimradi uwe mkataba unaogusa kila kitu kwenye maisha yetu, na tukaupitisha , ukapelekwa mbele kisheria, na mwisho wa siku ukawa ndio katiba yetu.


Mwanzoni tulikuwa tukifuatilia sana, na ikawa kila mmoja ana hamasa na utaratibu wote, hadi tukawa tumeweza kushika kila jambo, na kila mmoja akawa na tahadhari , asije akavunja mkataba, na kila mara tunakumbusha,kama jambo limafanyika, sivyo ndivyo, utasikia `mkataba unasemaje...’

Siku zikaenda, mambo yakwa mengi, watu tukajisahau,ikafikia hatua hakuna aliyejali kangalia mkataba unasemaje,ila kuna yale mambo ya msingi, kama ya ndoa, masilahi, na uwajibikaji,...mengine madogo madogo yakawa yanakiukwa hapa na pale, hakuna aliyejali,...ilimrdi tunaaminiana...tukajisahau lakini maisha yakaenda mbele, maana kulikuwa hakuna matatizo.


`Ngoja nikausome tena ule mkataba wa familia...’ nikasema sasa nikifungua kabati, hiyo ni nakala niliificha sehemu maalumu,  hakuna mtu anayeweza kuupata.

Ufunguo ulikuwepo pale pale,....nikauchukua, na kusogea kwenye kabati, nikahakikisha nimefunga mlango wa ofisini, kabla sijafungua hilo kabati, maana sikutaka mtu aingie na kuja kunisumbua. Nikasogea kwenye lile kabati, na kuchuchumaa, maana sehemu nilipoweka hizo nyaraka ni sehemu ya chini ya hilo kabati, ...

Nikafungua kidroo hicho, kilikuwa na namna ya kukifungua, sio kwa haraka, ni kama unafuatilia namba, nikafuatilia kwa makini mpaka mlango wake ukafunguka...., nakumbuka kabisa wapi niliuweka ile nakala ilikuwa pembeni,..sehemu yake maalumu, niliisimamisha  maana ni mkataba mrefu, sikutaka ijikunje…

Nikavuta kidroo chake, kilikuwa kitupu hakuna kitu…

‘Haiwezekani…’nikasema

Nikavuta sehemu yote, kulikuwa na nyaraka nyingine tu ambazo kwa muda huo sikuwa na umuhimu nazo...

Hapo sasa, nikahisi moyo ukinienda mbio,....nikatulia kidogo, labda nimesahau, labda niliwahi kuuchukua huo mkataba, hapana, sijawahi, ni muda sijautumia, sasa upo wapi.

‘Haiwezekani, nakumbuka kabisa huo mkataba niliuweka hapo, kwenye sehemu yake maalumu…’nikawa naongea peke yangu sasa. Na mimi ni hodari sana wa kuweka vitu vyangu kwenye mpangilio wake, na nahakikisha kila nikitoka ofisini kwenda popote, kila kitu nakiweka katika mahali pake kwa mapangilio wake, hilo sikosei hata mara moja.

Nikatuliza kichwa na kutafakari, lakini hakuna dalili yoyote kichwani ya kuniambia kuwa labda niliwahi kuutoa hapo. Nikaingiza mkono ndani na kusogeza kwa ndani kabisa, kama umegandia kwa ndani, hakukuwa na kitu kama hicho, nikaanza kuhisi vibaya. Sasa nikatoa kila kitu, na kupanga upya, ili kuhakikisha, , lakini sikuona cha mkataba wala nini….

Mkataba haupo, ….

‘Ni nani huyu mwenye nia mbaya,kaweza kuugundua huo ufungua, na akautoa, na kufungua hili kabati, halafu akalifunga na kuhakikisha kuwa hajagusa kitu kingine chochote, ni nani huyu…’nikawaza

Kiukweli ufungua wa hapo ni huo huo, hakuna  akiba...na hakuna anayefahamu kuwa ufunguo huo upo wapi zaidi ya mimi mwenyewe,….na ni nani anayefahamu kuhusu huo mkataba, zaidi ya mume wangu na wakili…,nikajaribu kuangalia tena kwa makini, lakini mkataba ulikuwa haupo....

Mkataba haukuwepo....!

‘Hakikisha umeharibu kila kitu…kila kitu, hasa mikataba, mengine nitayamaliza nikija…’


NB:  Sehemu hii ni muhimu sana, ndio maana nimeandika kwa taraibu na msisitizo, msichoke kusoma sehemu hii, itatusaidia sana kwenye maisha yetu


WAZO LA LEO: Kama tutakuwa na taratibu za mikataba kwenye ndoa zetu, kwenye familia zetu, kwenye vikundi vyetu, kwenye maisha yetu,kwenye sehemu zetu za kazi, nk, tungeliepuka migongano na mfarakano, maana mambo mengi yangelitatuliwa kisheria. Familia nyingi zinajikuta kwenye matatizo,pale anapofariki mmojawapo, au pale kunapotokea tatizo, na kutokuelewana. Na mwisho wa mifarakano hiyo, au matatizo hayo, wahanga wa haya yote ni watoto na akina mama, ambao wanakuja kudhulumiwa haki zao. Je hatuoni kuwa ili kukwepa hayo yote, ni bora kukawa na mikataba katika maisha yetu? Tuliwazie hili na wanasheria watusaidie...

Ni mimi: emu-three

No comments :