Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, November 27, 2017

MKUKI KWA NGURUWE-30


Nilipomaliza kuongea na mdogo wa mume wangu, akili yangu ilikuwa kama imefunguka, japokuwa kwa jinsi nilivyomuona huyu shemeji yangu, nahisi kama anahusika kwa amna moja au fulani, anaweza akawa ndiye baba wa mtoto wa rafiki yangu au anajua lolote kuhusu hilo..na kwa hali hiyo, nikajikuta naanza kutawaliwa na hasira, hasira kwa watu wangu niliowapenda sana…

Kuna muda nikawa natamani niongee kwa hasira… , nifoke, kama vile nipo ofisini na wafanyakazi wangu, lakini haikuwa rahisi , kwani nilikuwa kwenye kifungo maalumu,..kifungo cha kuwajibika kwa mume. 

Tuendelee na kisa chetu…

*****************

Mume wangu siku hiyo hakutaka kuongea kabisa, na nikaona nisimsumbue zaidi, nikajitahidi kutimiza kila kinachostahki, na akaja kulala…


 Yakapita masiku kadhaa, na siku hiyo nilikuwa nimetoka nje kidogo, nikiangalia taratibu za usafi, ni baada ya kuhakikisha kuwa mume wangu bado amelala, Nilikaa nje kama nusu saa au karibu saa nzima, baadae nikarudi ndani kuona kama mume wangu amesha-amuka ili nimpatie kifungua kinywa...

Wakati naingia ndani nikamkuta kashikilia simu,...simu kuashiria kuwa anaongea na mtu, na aliponiona naingia  kwa haraka  akakata hiyo simu , na kujifanya kama ndio anataka kupiga...

‘Ulikuwa unaongea na nani, …mume wangu, kwanini unaharibu,  ulishaambiwa usijisumbue na simu, au huyo mtu kakupigia wewe ndio maana sitaki ubakai na simu…?’ nikauliza, na alitulia kidogo , baadae akaniangalia na kusema

‘Mdogo wangu kakukosea nini..?’ aliuliza hivyo na kunifanya nishtuke, swala la mdogo wake nilishamalizana naye, iweje tena aulizie hivyo.

‘Mdogo wako…!?’ nikauliza kwa mshangao

‘Ndio…’akasema hivyo na kutulia


 ‘Kama ni ile siku tuliongea naye mambo ya kawaida tu, kwani ndiye umempigia simu au yeye ndio kakupigia simu kwani.. kasema nini…?’ nikauliza.

‘Nimekuuliza swali na unakwepa kunijibu, hufahamu jinsi gani ninavyojisikia vibaya familia yangu kuonekana tegemezi, kuwa kama omba mba, au huko kumsaidia imekuwa ni tatizo...’akasema

‘Mume wangu kwani shemeji kasemaje, niambie ukweli, ..unajua mume wangu hutakiwi kuwa na mawazo mengine ya kifamilia, utashindwa kupona haraka…’nikasema.

‘Inaonekana unamshuku vibaya, na kama ni mambo yangu mimi, kwanini umuulize yeyem niulize mimi mwenyewe…’akasema

‘Nilimuuliza kwa nia ya kutaka kukusaidia wewe, sikuwa na nia mbaya mume wangu…’nikasema

‘Ok…sasa unahitajia nini, nikuambie mimi mwenyewe..?’ akauliza

‘Hakuna kitu nahitajia kutoka kwako…’nikasema

‘Kama ni kuhusu kazini, ndio nina madeni mengi tu..na inatokana na biashara kuwa mbaya…ilibidi nikope nikitafuta masoko, ilibid nikope kuweka vifaa vya kisasa, lakini bishara haikutikia, ni hali ilivyo, nikajikuta naongeza madeni juu ya madeni, na hilo litakuja kulimaliza mimi mwenyewe…’akasema

‘Nimekuelewa mume wangu, lakini hukuwahi kuniambia hayo au sio, lakini sio shida, na wala lisikuumize kichwa… nashukuru sasa nimekuelewa, tutaangalia jinsi gani ya kufanya, kama itabidi tutakopa pesa kwa baba ili tulipe hayo madeni..’nikasema

‘Hahaha, ukope pesa kwa baba yako…labda awes io yeye,…kwa kauli yako hiyo naona wewe na baba yako kitu kimoja, ndio maana aliniwekea mitego, hataki mimi niwe mume wako, hili lipo wazi, lakini mimi sitakubali, hataweza nakuhakikishia,…’akasema

‘Mume wangu haya yote hayana maana kwa sasa, hebu achana nayo uangalie kwanza afya yako, kwanini unanipa wakati mgumu, ...?’ nikamuuliza na kabla hajajibu nikasema;

‘Jitahidi kusahau kila kitu ili upone haraka , tuendelee na maisha mengine..’nikasema

‘Pole sana mke wangu, najua nakupa wakati mgumu, lakini mimi sijapenda hilo, hivi kuna mtu anajitakia ajali…?’ akauliza

‘Ni ajali haina kinga nafahamu..’nikasema

‘Muhimu kwangu,..ni msamaha wako…na kiukweli sasa naanza kufahamu kuwa nakuumiza, nakuweka kwenye wakati mgumu sana, utanisamehe tu mke wangu, lakini haya yanahusuje  mdogo wangu,…’akasema

‘Mdogo wako hana tatizo, nilikuwa naongea naye tu….mambo ya kawaida, kumuulizia maendeleo yake , kama kuna sehemu kakwama niweze kuona kama tutaweza kumsaidia…’nikasema

‘Mhh…ndio hapo sitaki,…yeye anajiweza, kwanini asaidiwe, kwanini azidi kuongeza mzigo kwako, baba yako akisikia hivyo atakuja juu, na kutusimanga, mimi sipendi hilo kabisa,  na kama kuna adhabu ya madhambi yangu, basi nipeni mimi....’akasema.

‘Mume wangu, ukumbuke shemeji kwangu namuona kama mdogo wangu, kama ulivyooona tumekuwa tukijitahidi kwa pamoja kumjenga katika njia njema,ya kumbadili kutoka kwenye tabia ya utegemezi kwenda kwenye tabia ya kuweza kuishi mwenyewe, na hilo tumefanikiwa, kwahiyo kila hatua pia tunahitajika kumuuliza, wewe sasa unaumwa, ni lazima mimi niwajibike naye...’nikasema.

‘Ni kweli mke wangu, na inabidi nikushukuru sana kwa wema wako huo, kama ingelikuwa ni mimi mwenyewe ningelishakata tamaa, maana bwana mdogo alikuwa keshadekezwa na mama,maana yeye ni kipenzi cha mama, na wao walifikiria kwa kmfanyia hivyo ndio wanampenda,wakawa wanamdekeza, kumbe wanamharibu tusingelimwahi mapema, angeshajiunga na hayo makundi ya kuuza madawa ya kulevya....’akasema.

‘Ni kweli mume wangu, hilo ni kosa wanalofanya wazazi wengi, ambao kwa kuwadekeza watoto wao ndio wanafikiria kuwa ndio mapenzi kwa mtoto, kumbe ni kinyume chake…’nikasema nikibadili mada.

 ‘Nashukuru sana mke wangu najua sasa naingiwa na moyo kuwa umenisamehe kabisa, kama una lolote unataa kufahamu niulize mimi mwenyewe, najuta sana kwa hayo yaliyotokea...na kama hutanisamehe, ukaamua kumsikiliza baba yako hewala, lakini mimi sizani kama nitaishi ikitokea hivyo,ni..heri ya kufa tu...’akasema

‘Mume wangu usijali,..nimeshakusamehe, cha muhimu ni wewe kupona, hilo ndilo unatakiwa uliwazie jinsi gani unatakiwa kufanya mazoezi na kuondoa mawazo....’nikamwambia

‘Nikipona mke wangu, nitakuwa mimi na wewe bega kwa bega, ...unajua mke wangu, wakati mwingine kama binadamu, tunajisahau…mimi nimeliona hilo kivitendo..na eeh,..na wakati mwingine inatokea kwa vile tunakuwa mbali mbali kimawazo, nawaza hivi mwenzangu vile, lakini hayo yamepita au sio mke wangu…?’ akauliza

‘Ni kweli…hayo yasahau…’nikasema

‘Sasa mke wangu, nakuahisi kuwa mimi mume wako, ...nitajitahidi sana tuwe pamoja tuiondoe hiyo hali, au unasemaje mke wangu..?’akasema, nikakumbuka kuwa mtu huyu hatakiwi kuongea kwa muda mrefu, kwahiyo natakiwa kukubali tu, japokuwa nilikuwa sijamuelewa bado , hapo nikasema.

‘Usijali mume wangu, cha muhimu kwa sasa, ni kuhakikisha yale tuliyo anza nayo yanafankiwa,…kampuni eeh, hiyo nitapambana nayo, na hili la huyo mdogo wetu  achana naye, lisikuumize kichwa, au kuna nini zaidi,..hakuna achana naye, jingine ni kuhusu watoto wetu , najua familia inakua, sasa, hapa kuna kitu nataka tukiongee....’akasema

‘Tutakuja kuongea tu mume wangu usijali…’nikasema lakini hapo nahis kuna jambo anatakak kulisema, naogopa anaweza kusema jambo, nikaingiwa na hasira, na haitakiwi,..hapo nikasema.

‘Lakini mume wangu…’akanikatiza na kusema;

‘Huyu mdogo wangu kwa sasa hana tatizo, keshajiweka mahali ambapo hatuna haja ya kuhangaika naye tena,....na kwa watoto wetu bado wadogo, hatuna shaka nao, tutawajenga kimaadili, na umeshafanikiwa kwa hilo, kama wanaweza kuamuka asubuhi na kuwajibika hata bila kuelekezwa, tunataka nini tena mke wangu..au sio….’akasema.

‘Ni kweli…’nikasema

‘Sasa mke wangu kuna kitu kingine nilitaka tuongee…’akasema

‘Mume wangu unakumbuka docta alisemaje…’nikasema

‘Ndio nakumbuka alisema nisiwaze sana, na nisiongee sana…’akasema

‘Sasa hapa umeongea vya kutosha, unahitajika kumpumzika..’nikasema

‘Lakini niliyo nayo kichwani yananifanya niwaze sana , ndio maana nataka tuyaongee, tuyaweke sawa, yananifanya niwaze sana, na baba yako, yupo nyuma ya hili, akiona nimepona tu, atanivaa, sitaki, nataka tuyaweke sawa sisi wawili kwanza…’akasema

‘Tutaongea tu mume wangu usijali, sasa hivi wewe unahitajika kupumzika kwanza…unajua mume wangu nimekukosa sana, nataka upone haraka, au wewe hulioni hili, …’nikasema

‘Kweli mke wangu nafahamu..hata mimi naona nakutesa sana, nawazia sana hilo pia, utaishi hivi mpka lini, ndio maana naingiwa na wivu, nahisi  kama naibiwa…’akasema

‘Hahaha mume wangu….wivu gani huo, kwa umri huu usiwe na wasiwasi kabisa, si unanifahamu mimi sina mwili wa tamaa tamaa za ajabu ajabu, mimi najimudu mwenyewe kabisa…’nikasema

‘Mhh, ..ni kweli, hata hivyo wivu hauachi kuwepo,…ila kiukweli mungu alikujalia , lakini tatizo ni mimi mume wako, tamaa ni nyingi sana, ndio maana mungu kaona aniadhibu….’akasema

‘Oh,…. pole sana, sasa mume wangu tulia , dawa zifanye kazi, ulale sasa…’nikasema

‘Ngoja nikuambie ukweli kwanza kabla sijalala,…mke wangu, nataka tufurahi pamoja, tuongee pamoja,… nilishaanza kuwazia vibaya sana, hii ajali ndio imeniokoa, sasa nataka kusiwepo na uadui, kati yangu mimi na wewe na …marafiki zako pia..kama ni langu liwe langu…’akasema

‘Usijali mume wangu nimekuelewa tu…’nikasema

‘Hapana, wewe hujui tu…nilishaanza kufikia kubaya, na….isingelikuwa hayo mambo ya baba yako, ningelishajiandaa kufanya mabaya tu, tamaa zilishaanza kuitawala nafasi yangu,…wakati mwingine mungu anajua tu nilikuwa naelekea wapi…’akasema

‘Mume wangu sasa lala…’nikasema

‘Nakupenda sana mke wangu, niache nikuambie ukweli, nimekukosea sana, na kosa langu linakwenda kuathiri wengine ndio maana naogopa, sasa mdogo wangu kesho atakuwa mwingine, unaona eehe, ni vyema tukayamaliza haya sisi wenyewe achana na mipango ya baba yako, hebu sogea hapa mke wangu, nahisi sauti inakwisha, dawa hizo…’akasema hapo nilitaka kuanza kukasirika, maana ni kama unaongea na mtoto ambaye unamkanya kitu hasikii, lakini sikuwa na jinsi, nikasogea na kukaa karibu yake

‘Kaa hapa kwenye miguu yangu…’akasema

‘Mume wangu lala basi…’nikasema

‘Ni amri ya mume wako…’akasema na mimi nikaenda na kujiegesha kwenye miguu yake, na akawa ananishika ili kunifanya nikae, huku namuonea huruma, ..kitendo hicho kikamfanya acheke..na mimi nikajikuta nacheka tu

‘mke wangu kweli unanipenda, wanionea huruma sana, lakini huruma hiyo isiishie hapa,..unihurumie kabisa kabisa..usimsikilize baba yako, kila kitu alichpanga tukisahau, unanielewa, hayo niachie mimi, au sio…akanishika kama ananitekenya,......’

‘Aah, mumu wangu, nini tena lala, utajiuliza…’nikasema na kucheka na yeye akacheka,   na mara nikasikia sauti ya mtu akipiga hodi, na kabla sijasema karibu mlango ukafunguliwa, ..., alikuwa ni docta.

‘Kumbe ni wewe jirani…’nikasema na kujiinua haraka miguuni mwa mume wangu.

‘Oh, naona leo mpo na raha, maana nimesikia kicheko, ..kicheko cha raha, ...’akasema  na mimi nikashukuru kuwa hatmaye mgonjwa atakubali kulala.

‘Kwanini nisiwe na raha na mimi nipo na mume wangu..’nikasema.

‘Ni kweli hayo ndio maisha,...inatakiwa  mfanye hivyo kila siku,, au mara kwa mara, au sio rafiki yangu?’ akamuuliza mume wangu huku akimsogelea na kushikilia kile kigari,..na mume akasema;

‘Na wewe bwana, unakuwa dakitari wa kila kitu....’akasema

‘Ni kweli natamani iwe hivyo, na nimekuja na mtu wa mazoezi, leo tunataka kumfanyisha mume wako mazoezi maalumu, na kama hutajali naomba nimchukue mume wako’akasema

‘Unataka kumpeleka wapi?’ nikauliza nikimwangalia kwa uso uliotahayari.

‘Ndani ofcourse, tunahitajia tuyafanyie ndani,  sehemu yenye nafasi, hasa kule maktaba au sio…docta kaja na vifaa maalumu, yupo nje,…docta ingia...’akasema, na mara akaingia docta akiwa kavalia kikazi zaidi.

Mimi hapo sikuwa na jinsi…nikawaacha wao wakielekea kwenye chumba cha maktaba, na wakati wanaondoka kuingia  mume wangu akageuza kichwa na kuniangalia kwa nyuma, akasema;

‘Mke wangu nakupenda sana....’akaniambia mimi sikujibu kitu, muda huo akili ilikuwa imezama kwenye mawazo, nawaza hayo mume wangu aliyoongea, inaonekana kiukweli mume wangu kakosea, na huenda, ..kuna ukweli wa hayo yanayosemwa, na …na huenda baba yangu ameshaligundua hilo…sasa itakuwaje…

*************

 Baadae docta akarudi, naona alimuacha mwenzake akiendelea na mazoezi na mume wangu.

‘Nimekuona ukimuhoji sana mume wako, ...huu sio wakati muafaka, wa hayo maongezi yako...’akasema

‘Mbona sijamuhoji kitu chochote cha kumfanya awaze sana, yeye ndio anaongea mambo mengi tu…’nikasema

‘Kwanini una haraka na hayo mambo, uwe na subira  na hicho unachotaka kukijua, utakifahamu na…utakuja kuniamini niliyokuwa nikikuambia.., lakini kwa hivi sasa yasubirishe hayo..wasiwasi wangu ni kuwa, unaweza ukafanya jambo ambalo utakuja kujijutia. Ukiwa umeshachelewa….unanielewa hapo…’ Akasema na mimi nikawa namsikiliza tu..

‘Japokuwa namuona mume wao leo ana furaha sijui kwanini…lakini ndivyo itakwavyo, awali alikuwa akionyesha kuwa ana jambo linamkera, hata hivyo hayo ysikupe mawazo kuwazia kuna nini, hayo yaweke pembeni kwanza, mengine nakusaidia, niamini mimi…’akasema

‘Kwani wewe unafikiri mimi nimemuuliza nini mume wangu kibaya,..tulikuwa tunaongea tu, ila mimi najiuliza kwanini wewe unayejua ukweli hutaki kuniambia,..’nikasema

‘Kukuambia nini sasa, wakati mimi nimeshakuambia kila kitu au…?’ akauliza

‘Hapana,..hujaniambia…’nikasema

‘Tatizo  ..wewe unataka nikutafunie kila kitu, mimi siwezi kuvunja ndoa ya mtu, na sitaki hilo litokee, …unasikia, snitajuta sana ndoa yenu ikivunjika…’akasema

‘Unajua mimi sikuelewi, wewe unajifanya kuwa unanijali, kumbe kuna mengi makubwa unanificha, hukutaka kuniambia mapema, na huenda yote yasingelitokea kama ungelikuja kuniambia mapema..’nikasema.

‘Ina maana unanilaumu mimi kwa hilo, ...unanichekesha kweli, wa kujilaumu ni wewe mwenyewe, wewe umeshindwa kuihudumia ndoa yako halafu na hatimaye hayo yakatokea,mengine yameanzia huko…, umesahau eeh, ni mara ngapi ninakuja kuongea na wewe na kujaribu kukuelekeza…’akasema.

‘Usijitetee bwana…, wewe ulikuwa na mume wangu wakati anafanya yasiyofaa, kama alishaanza kujihusisha na umalaya, kama alivyosema leo hii , ina maana wewe ulikuwa unafahamu,, je hukuwahi kumuona na wanawake wewe huniambii, ni nini maana ya kunijali...’nikasema.

‘Na wanawake, kakumbia hivyo…hapana ….’akasema

‘Kasema tamaa zilimzidi, akaanza na kutamani kufanya mabaya, hayo yana maana gani…?’ nikauliza

‘Sizani kama alikuwa na maana hiyo…’akasema

‘Lakini kuna kipindi nilikuambia hilo, unakumbuka kuna siku nilikuja nikakuambia kuwa mume wako naona kama ana…kuwa kuwa karibu na wanawake, kitu ambacho sio kawaida yake, lakini sio kwa ubaya, sikuona huo ubaya wa ndani …’akasema

‘Anakwua nao kwa vipi,…?’ nikauliza

‘Lakini nilikuambia, ukasema mimi naleta fitina, umeshasahau eeh, usinione kuwa mimi ni mjinga, nafanya haya mambo kihekima, nisingelikuja na kukuambia moja kwa moja, nilikuambia kwa namna ya wewe kulielewa, ukaniona mimi ni mbaya...’akasema.

‘Swali je kuwa nao karibu ni kwa nia mbaya, kuvunja ahdi ya ndoa , au kwa vipi, nataka unijibu hapo…’nikasema

‘Hilo kwa utashi wangu sijaliona, wanakunywa pamoja, kuongea inaishia hapo ila mimi niliona hilo lina muelekeo mbaya…’akasema

‘Kwahiyo wewe umesahau ile ahadi yako,?’ nikamuuliza

‘Ahadi gani?’ akaniuliza

‘Kuwa kamwe hutakubali mtu aniumize...’nikasema.

‘Na ndicho ninachokifanya...wewe mwenyewe utaona, si unajifanya mpelelezi, endelea,...lakini mimi nitajitahidi kuhakikisha kuwa hakuna mtu atakayekuumiza,ahadi yangu ipo pale pale, hata kama hunitaki niwe karibu na wewe....ila nakukanya uwe mwangalifu, usichukulie mambo kwa pupa..’akasema huku akitabasamu na kushika kidevu

‘Halafu kuna ujumbe, nimeupata, kutoka eeh, kwa rafiki yako, anasema kuna mambo yameshindikana anahitajika arudi kwanza huku, ...sijui ni mambo gani, kwani hamjawasiliana naye ?’akaniuliza


‘Rafiki yangu yupi tena, ooh, kwahiyo mnawasiliana naye wewe, mimi ananiona sina maana tena kwake…’ nikasema.

‘Una marafiki mangapi bwana, huyo huyo,..unayemwamini kupidukia,...nahisi akija sasa mtamalizana naye na ukweli utagundulikana, ila bado nakukanya, uwe makini, hasa akija huyo rafiki yako,...’akasema

‘Mimi hajaniambia, kwanza kaondoka bila kuniaga kwahiyo hata akija sizani kama nitakwua na muda wa kuongea naye…’nikasema

‘Hutataka kuujua ukweli…?’ akaniuliza

‘Ukweli upi…?’ nikauliza

‘Kuhusu mtoto…?’ akaniuliza na ikawa kama kanitonyesha jeraha, nikakunja uso, nikabakia nimeduwaa, halafu nikasema;

‘Nimeongea na mdogo wa mume wangu, anavyojikanyaga inawezekana akawa ndio yeye, au anaufahamu ukweli wote, nataka nije kuongea naye kabla huyo shetani hajarudi…’nikasema

‘Leo hii inamuita shetani…’akasema

‘Kutokana na wewe..ila mimi sijaamini, kama nimekosea mungu atanisamehe, ila kama ni kweli…sizani kama tutaelewana…’nikasama

‘Utamzuia asirudi kusoma, wewe si ndio umemfadhili…?’ akauliza

‘Hilo ni jambo jingine halihusiani kabisa na hili, siwezi kukosa fadhila za utu wema kwa ajili ya ubaya wa mtu…kama ataniambia ukweli, na ikawa hivyo ni kweli, kila kitu kipo wazi,…’nikasema

‘Kwa vipi…?’ akauliza

‘Mume wangu anafahamu…’nikasema

 Mara tukasikia docta akija na alipotufikia akasema;

‘Oh mume wako kajitahidi sana leo, naona anafuraha fulani, mpaka kaweza kuinua miguu ni hatua nzuri sana, sasa jitahidini, awe na furaha kama hivyo, atapona haraka, ila mwishowe kaonekana mnyonge, …’akasema

‘Kwanini docta…?’ akauliza docta rafiki

‘Nahisi kuna kitu akikikumbuka kina mtesa, kuna kitu kasema, kapokea ujumbe unaompa shida sana, ujume wa simu kitu kama hicho…’akasema

‘Oh, labda ni huyo mshenzi, kamtumia ujumbe kuwa anarudi..’nikasema kwa hasira

‘Haiwezekani….’akasema docta rafiki.

‘Huyo mtu hana jema…ikibidi hata simu msiwe mnamruhusu atumie, lakinikwa hekima zaidi…’akasema docta.

‘Ni kazi, hataki kabisa kuchana na simu yake…’nikasema

‘Basi lakini kwa hatua aliyofikia, ni maendeleo mazuri tu…’akasema

Na baadae huyo docta akaaga kuondoka, na mimi nikaona niende kumuona mume wangu kama kalaa…niliingia na kumkuta anachat kweye simu.

‘Mume wangu hujalala..?’ nikamuuliza

‘Kuna kitu nakifuta kwenye simu yangu lakini hakitaki…’akasema

‘Kitu gani nikusaidie…’nikasema

‘Hapana…ni ujumbe, ..haina shida, umeshafutika…’akasema na sasa akazima simu yake, na kiukweli mimi sina muda na simu yake hata sijui anatumia neno gani la siri, lakini nikawa na hamasa sana ya kujua kaandikiwa ujumbe gani.

Nilipohakikisha mume wangu kalala, nikaichukua simu yake na kutoka nayo nje, nikampigia mtu wangu mmoja mtaalamu wa simu, anisaidie kuwasha simu iliyowekewa kifungo..ni mtaalamu sana, na akasema anakuja.

NB:  Samahanini sana kwa kutokuwa hewani kwa kipindi cha siku tatu hivi, ni matatizo ya umeme na mtandano, na mitihani ya hapa na pale..



WAZO LA LEO: Ndoa nyingi zina matatizo yake, na huenda yakawa ni matatizo madogo tu, lakini kwa wanandoa wakashindwa kuyatatua, kwa vile, hakuna anayekubali kushuka chini, kila mmoja anajiona anafahamu zaidi ya mwingine...au mmoja anaogopa kumuelezea mwenzake ukweli.....wewe kama rafikji tumia hekima kuwashauri, usitumie mwanya huo kuharibu badala ya kujenga. Hekima ya ushauri ni muhimu sana kwa watu kama hawo.

Ni mimi: emu-three

No comments :